Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza (29 total)

MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera hauna Chuo cha VETA chenye hadhi ya Chuo cha Mkoa na kwa sababu hiyo wananchi wa Mkoa huo hawapati elimu inayostahili. Hivyo, Serikali iliamua kujenga Chuo cha aina hiyo Bukoba kwenye Kata ya Nyakato ambako kiwanja kilipatikana na mipango yote ilifanywa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutembelea mara kwa mara eneo hilo, lakini ni muda mrefu sasa umepita hakuna chochote kinachoendelea:-
Je, ni lini ujenzi huo utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera unategemea kuanza baada ya hatua za maandalizi ya msingi zitakapokamilika. Serikali kwa sasa imeshalipa kiasi cha shilingi 4,779,896 kwa ajili ya kupata Hati miliki kwa eneo lenye hekta 40.9 lililopo katika Kijiji cha Burugo, Kata ya Nyakato ambapo chuo kitajengwa. Aidha, uchambuzi wa stadi zitakazofundishwa katika Chuo hicho umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuandaa michoro kwa ajili ya majengo na miundombinu ya chuo, kuandaa mitaala kulingana na stadi zilizotambuliwa, kuandaa mipango ya ukarabati wa miundombinu hasa kiliometa nne mpaka tano za barabara kutoka barabara kuu na kuhakikisha maji na umeme yanapatikana katika eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Watu wa China kuhusiana na ufadhili wa ujenzi wa Chuo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inategemea kukamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera kutegemeana na upatikanaji wa Fedha na juhudi mbalimbali ikiwemo ushirikishwaji wa Wafadhili wa ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kuchangia juhudi za Serikali.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kuna kodi zinazofikia 26 katika kilimo cha kahawa ambazo zimefanya bei wanayopata wakulima wa zao hilo kuwa kidogo sana ikilinganishwa na gharama za kulima hivyo kuwafanya baadhi ya wakulima kupeleka kahawa yao nchi jirani ambako bei yake ni nzuri na kwa kufanya hivyo nchi inakosa mapato na kudhoofisha zao hilo hapa nchini; na hata Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alilikemea jambo hilo kwenye hotuba yake ya kulifungua Bunge Jipya aliyoitoa Bungeni Novemba, 2015.
Je, ni kwa nini Serikali isiingilie kati na kufuta kodi hizo kandamizi kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kuna changamoto ya kuwepo kwa kodi nyingi siyo tu kwenye zao la kahawa, lakini pia kwa mazao mengine ya chakula na biashara hapa nchini. Kwa mfano, kwa kahawa inayozalishwa Mkoani Kagera ambayo ni aina ya Robusta inapouzwa nje kwa kupitia Vyama Vikuu au Vyama vya Msingi, vyama hivyo hutozwa kodi na tozo mbalimbali zipatazo 26, sawa na makampuni mengine binafsi. Kwa kuwa vyama hivi ni vyama vya wakulima, gharama hizi za kodi na tozo mbalimbali kwa njia moja ama nyingine huenda kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua ukubwa wa changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imedhamiria kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika Sekta ya Kilimo kwa kupitia upya taratibu, vibali, tozo, kodi, ushuru na ada mbalimbali zinazotozwa ili kupunguza gharama za kufanya biashara. Tozo, ada na kodi zote zitakazotozwa na Bodi za Mazao na Mamlaka nyingine zitapitiwa upya na kuchambuliwa ili kutoa nafuu kwa wakulima wote ikiwa ni pamoja na wakulima wa zao la kahawa. Kodi zitakazogundulika kurudisha nyuma tasnia ya kahawa zitaondolewa mara moja.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Bukoba Vijijini kuna Shule za Sekondari za Serikali na za Wananchi zipatazo 29 ambazo zinaishia Kidato cha nne na moja kati ya hizo ina Kidato cha tano na sita hali, inayosababisha wahitimu wengi wanaomaliza Kidato cha nne wakiwa na sifa za kuingia Kidato cha tano kukosa nafasi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madarasa na miundombinu inayofaa kwa Kidato cha tano na sita kwenye baadhi ya shule zilizopo ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba inaendelea na upanuzi wa miundombinu ya shule mbili za Lubale na Lyamahoro ili ziweze kuwa na sifa na vigezo kuwa Shule za Kidato cha tano na sita ifikapo Juni, 2017. Serikali imepanga kutumia fedha za Performance for Results (P4R) kukamilisha miundombinu katika shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na angalau shule moja ya kidato cha tano na sita. Vileile kila Tarafa iwe na shule moja ya kidato cha tano na sita. Shule hizi ni za Kitaifa ambazo huchukua wanafunzi waliohitimu na kufaulu kidato cha nne katika mikoa yote.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA Aliuliza:-
Kampuni ya Chai ya Maruku imekuwa sugu kwa kutowalipa wakulima wanaoiuzia chai pamoja na kutowalipa wafanyakazi wake wenyewe.
Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua ya kuwasaidia wakulima na wafanyakazi hao ili kupata haki yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ucheleweshwaji wa malipo ya wakulima na wafanyakazi katika kiwanda cha Chai cha Maruku yalianza Septemba, 2011. Hali hiyo ilitokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Kagera Tea Company Limited iliyowekwa na Spearshield Africa Company Limited inayomiliki Kiwanda cha Chai cha Maruku kwa asilimia 75 kusimamia uendeshaji wake ikiwemo ununuzi majani mabichi ya chai kutoka kwa wakulima wadogo. Wakulima hawa wanamiliki asilimia 25 walizopewa na Serikali kufuatia kiwanda hicho kubinafsishwa kwa Spearshield Africa Company Limited kutoka kwa Mamlaka ya Chai Tanzania waliokuwa wanamiliki kiwanda hicho. Mkataba wa mauziano ulisainiwa terehe 25 Septemba, 2001. Sababu nyingine ni tija ndogo ya majani ya chai ikilinganishwa na gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, ili kunusuru wakulima na wafanyakazi wa kiwanda hicho, Serikali kupitia uongozi wa Mkoa wa Kagera, Bodi ya Chai ya Tanzania na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania, kwa nyakati tofauti wamekutana na mwekezaji huyo kumuelekeza atekeleze
wajibu wake wa kulipa wakulima na wafanyakazi. Kufuatia hiyo mikutano, mwekezaji ametafuta fedha na kulipa madeni mbalimbali ikiwemo malipo ya wakulima na wafanyakazi. Mpaka sasa ameshalipa wakulima wadogo malimbikizo yote ya nyuma hadi mwezi Oktoba, 2016 na ameahidi kulipa madeni ya Novemba na Disemba, 2016 ndani ya mwezi Januari, 2017.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kuna mradi mkubwa wa maji wa siku nyingi pale Maruku (Kyolelo) ambao miundombinu yake mikubwa kama matanki, mabomba chini ya ardhi na vyanzo vyake ni vizuri lakini kutokana na uchakavu mradi huo hautoi maji; mradi huo ulikuwa ukihudumia vijiji vitano katika Kata za Kanyangeneko na Maruku; kukarabati miundombinu iliyochakaa inaweza kugharimu kiasi kidogo cha fedha kama shilingi milioni 500 kwa kuhudumia vijiji vitano wakati mradi mmoja kwa kijiji kimoja wa miradi inayoendelea unagharimu zaidi ya shilingi milioni 800.
Je, Serikali haioni ni busara kuukarabati mradi huu haraka?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa Maji wa Maruku- Kanyangereko ni miongoni mwa miradi iliyoanza kujengwa baada ya Tanzania Bara kupata Uhuru mwaka 1961. Mradi ulijengwa na ulikamilika mwaka 1977 na kuanza kutoa huduma. Mradi huu ulikuwa ukiendeshwa na Serikali chini ya usimamizi wa Idara ya Maji ngazi ya Mkoa. Hadi kufikia mwaka 1983, mradi ulikuwa unafanya kazi lakini ulisimama kwasababu ya wananchi kutochangia fedha za uendeshaji na matengenezo ikiwa ni pamoja na kuhujumiwa kwa miundomibu ya mradi. Aidha, wananchi hawakupewa elimu ya kutosha ya kutambua kuwa mradi huo ni wa kwao na wanatakiwa kuutunza.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri imewasilisha maombi Wizarani ya kukarabati mradi huu kupitia miradi ya maji iliyoko kando kando ya Ziwa Victoria itakayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la maendeleo ya JICA.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imepanga kutekeleza mradi huu kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) na inatarajiwa kuwa mradi huu utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.278 kimetengwa kwa ajili ya Halmashauri ya Bukoba. Ukarabati wa mradi huo utatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Serikali inazuia wavuvi kuvua samaki wadogo na hivyo nyavu zenye matundu madogo haziruhusiwi; katika Ziwa Victoria kuna samaki ambao kwa maumbile yao hawawezi kuwa wakubwa kama vile dagaa, furu na hata sato.
Je, Serikali haioni kuwa kwa kuzuia tu nyavu ndogo samaki hawa hawatavuliwa kamwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 katika kulinda na kusimamia rasilimali za uvuvi ili ziwe endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinavunwa katika njia endelevu bila ya kuathiri vizazi vyao, Serikali imepiga marufuku matumizi ya nyavu (dagaa net) zenye macho madogo chini ya milimita nane kwa uvuvi wa dagaa, badala yake nyavu zinazoruhusiwa kwa uvuvi wa dagaa ni kuanzia milimita nane hadi milimita 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi wa sato na sangara, Serikali imekataza wavuvi kutumia nyavu za makila zenye ukubwa wa macho chini ya inchi sita ili kuvua samaki wakubwa tu. Aidha, samaki hao wanaweza kuvuliwa kwa kutumia mishipi au nyavu za makila kuanzia inchi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kuu la Serikali la kupiga marufuku matumizi ya nyavu zenye macho madogo ni kunusuru kizazi cha samaki kisipotee kwa kuepusha uvuvi wa samaki wachanga kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kizazi kijacho. Hata hivyo, kulingana na sheria na kanuni hizo, samaki wa aina zote huvuliwa kwa kutumia nyavu zilizoruhusiwa kisheria na ndiyo maana samaki wa aina zote wanapatikana sokoni.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Maeneo mengi ya Bukoba Vijijini kama vile Kata za Ruhunga, Kibirizi, Izimbya, Mugajwale, Rukoma, Kikomelo na nyingine yana tabu kubwa sana ya upatikanaji wa maji na kilio hiki kimekuwa cha muda mrefu sana:- Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua ya kuwasaidia wananchi hao.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hali ya upatikanaji wa huduma za maji kwenye maeneo aliyoyataja bado ni changamoto. Hata hivyo, kwa uhalisia hali hiyo ni tofauti na maeneo mengi ya Halmashauri ya Bukoba Vijijini ambako Serikali imekamilisha hivi karibuni miradi 18 ya maji kwenye Kata za Nyakibimbili, miradi mitatu (3); Kyamulaile, miradi mitatu (3); Kemondo, miradi mitatu (3); Buteragunzi, miradi minne (4); Rubole, mradi mmoja (1); Karabagaine, mradi mmoja (1); Rubafu (mradi mmoja (1); na Mikoni, miradi miwili (2) iliyogharimu shilingi 3,552,117,690 inayohudumia wakazi 61,279; hali hiyo imeinua upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 64 ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wote wa Bukoba Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji itapanda zaidi hadi kufikia asilimia 75 ifikapo mwezi Juni, 2018 kutokana na kukamilika kwa miradi ya Rukoma, Ubwera, Katoma na Kibirizi inayogharimu Sh.2,235,274,135 na itakayohudumia wakazi 18,449.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kuna visima 75 vinavyofanya kazi kwenye Kata ya Rukoma, Ruhunga, Butulage, Mgajwale, Izimbya, Katoro, Rubale, Kaibanja, Kishogo, Kasharu, Maruku na Kikomero; na vyanzo vingine 90 vya maji kwenye Kata za Nyakato, Buhendagabo, Katerero na Bujugo. Serikali itatekeleza miradi ya maji kwenye Kata za Ruhunga, Mugajwale, Izimbya na Kikombero ambako kwa sasa wakazi wake wanahudumiwa na visima 23 vyenye uwezo wa kuhudumia watu 7,500 kati ya wakazi 11,794 waliopo katika Kata hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia awamu ya pili ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa Mwaka 2018/2019 imetenga shilingi bilioni 2.5 endapo Bunge litaridhia ili kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za maji Bukoba Vijijini ikiwemo maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Kampuni ya Chai Maruku ilibinafsishwa kwa wawekezaji ili kuendeleza uzalishaji. Tangu kampuni hiyo imebinafsishwa, wakulima hawalipwi fedha za mauzo ya chai kwa wakati na wafanyakazi hawalipwi mishahara na stahiki zao ipasavyo.
Je, katika hali hiyo, kwa nini Serikali isivunje mkataba na mwekezaji na kurejesha umiliki Serikalini au kwa mwekezaji mwingine atakayejali maslahi ya wakulima na wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2016 Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa utendaji na uendeshaji wa Kampuni ya Chai Maruku.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inafanya vikao kwa nyakati tofauti kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai kwa lengo la kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya mwekezaji, wakulima pamoja na wafanyakazi wa kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vikao hivyo haki ya kila upande ilizingatiwa ikiwemo suala muhimu la haki za wafanyakazi pamoja na madai ya wakulima. Katika vikao vya mwezi Oktoba na Desemba, 2017 mwekezaji alikubali kulipa madai ya wakulima ya kiasi cha shilingi milioni 12. Aidha, majadiliano yanaendelea ili kutatua mgogoro wa madai ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sehemu kubwa ya mgogoro inaelekea kutatuliwa, Serikali haioni sababu ya kuvunja mkataba na mwekezaji kwa sasa. Hata hivyo, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili ili kuhakikisha kuwa haki za wakulima na wafanyakazi hazipotei.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Tanzania haijaidhinisha na kujiunga rasmi na mkataba wa kupambana na silaha za sumu (Biological Weapons Convention):-
(i) Je, kwa nini Tanzania haijajiunga na mkataba huo?
(ii) Je, Serikali inafahamu madhara ya kutoidhinisha rasmi mkataba huo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ilisaini Mkataba wa Kupambana na Silaha za Baiolojia na Sumu tarehe 1 Agosti, 1972, lakini mpaka sasa haijaridhia mkataba huo. Kutoridhiwa kwa mkataba huo kulitokana na kutoonekana athari zake za moja kwa moja kwa wakati huo ambapo matumizi salama ya mkataba ikiwemo utafiti wa magojwa ya binadamu, wanyama na mimea yameendelea kufanyika nje ya mkataba huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinatokana na matishio mbalimbali ikiwemo ugaidi, zimesababisha hitajio la kuridhiwa kwa mkataba huo na kutekelezwa kwa vitendo baada ya kutungiwa sheria. Kutokana na umuhimu wa suala hili, Rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya kuridhia mkataba huo imeandaliwa na baada ya kupitia ngazi mbalimbali za maamuzi, azimio litaandaliwa kwa kuwasilishwa katika Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuridhiwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu madhara yaliyopo hivi sasa ya kutoridhiwa kwa mkataba huo. Baadhi ya madhara hayo ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, Tanzania kuwa katika kundi dogo la nchi ambazo hazijaridhia mkataba huo kama vile Haiti, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Somalia na Syria. Tanzania kuwepo katika kundi hili hakutoi taswira nzuri kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani kati ya nchi hizo nyingi zina migogoro ya muda mrefu ya ndani.
Pili, kunanyima fursa kwa wataalam wetu kupata mafunzo mbalimbali yanayotolewa katika kujenga uwezo na kukabiliana na athari za mashambulizi ya silaha sumu na kibaiolojia.
Tatu, kunanyima fursa kwa wataalam na viongozi wa Kitanzania kushiriki kwenye uongozi wa taasisi mbalimbali za kimataifa zinasimamia sheria za silaha za kibaiolojia na sumu.
Nne, kunakosesha Serikali kutoa haki za msingi kupitia mahakama kwa makosa mbalimbali yanayoweza kufanywa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Serikali ilifuta tozo na kodi kadhaa katika kilimo na biashara ya kahawa, lakini bado bei anayopata mkulima ni ndogo.
Je, ni kwa nini tangu kufutwa kwa tozo na kodi hizo bei kwa mkulima haijapanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Rweikiza. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei ya kahawa duniani inapangwa kwa kuzingatia masoko mawili makuu ya rejea duniani ambayo ni Soko la Bidhaa la New York, Marekani (New York Commodity Market) kwa kahawa za arabika na Soko la London, Uingereza (LIFE) kahawa ya aina ya Robusta. Mwenendo wa bei katika masoko hayo una athari za moja kwa moja kwenye soko la kahawa na bei anayopata mkulima. Aidha, bei ya kahawa katika masoko hayo pia huathiriwa na ugavi na mahitaji (demand and supply) ya kiasi cha kahawa kinachozalishwa duniani kwa wakati husika ambapo uzalishaji wa kahawa nchini ni wastani wa tani 50,000 za kahawa safi sawa na asilimia 0.6 ya kahawa yote duniani na hivyo kutokuwa na ushawishi katika bei ya kahawa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kufuta tozo na kodi katika zao la kahawa, bei ya mkulima imeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mzalishaji mkuu wa kahawa duniani, nchi ya Brazil kushusha thamani ya fedha yake (devaluation of currecy) na hivyo kahawa yao kuuzwa kwa bei ndogo ili kuvutia wanununuzi wengi. Pia kuongezeka kwa uzalishaji ambapo msimu wa 2018/2019 nchi ya Brazil na nchi nyingine duniani zimeongeza uzalishaji na kua na ziada ya tani 420,000 na kutoeleweka vizuri kwa maelekezo ya Serikali kuhusu uuzaji wa kahawa kwenye soko la moja kwa moja (direct exports), kwa kahawa hai (organic coffee) na kahawa haki (tair trade coffee) miongoni mwa wanunuzi na viongozi wa ushirika.
Mheshimiwa Spika, pamoja na bei ya kahawa katika soko la dunia kushuka kutoka USD 87.4/50kg za kahawa mwaka 2016/2017 hadi dola 79.8 kwa gunia la kilo 50 la kahawa safi mwaka 2017/2018 bei ya kahawa ya mkulima wa kahawa imeimarika kwa kahawa ya robusta kutoka shilingi 1,400 kwa kilo mwaka 2016/2017 hadi shilingi 1,600 kwa kilo mwaka 2017/2018; na bei ya arabika kupungua kwa kiasi kidogo kutoka shilingi 4,000 kwa kilo mwaka 2016/2017 hadi shilingi 3,800 kwa kilo mwaka 2017/2018. Aidha, bei ya arabika kwa mkulima ingeweza kupungua zaidi kama Serikali isingeondoa tozo katika tasnia ya kahawa.
Mheshimiwa Spika, katika mwa 2017/2018 Serikali ilifuta jumla ya tozo 17 na tozo mbili mwaka 2018/2019 katika tasnia ya kahawa ambazo zimesaidia kuimarisha bei ya mkulima. Aidha, kupungua kwa kodi na tozo hizo kumesaidia bei ya kahawa kuwa nzuri ambapo kwa mara ya kwanza katika msimu wa 2017/2018 kahawa ilitoka nchi ya Uganda na kuletwa Tanzania kutokana na wakulima wa Uganda kuvutiwa na bei iliyokuwa inapatikana Tanzania. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Katika Bunge la Kumi kulikuwepo na mjadala kuhusu kuanzishwa kwa kilimo cha makambi ambapo vijana wengi wangepelekwa makambini, wangepewa mikopo ya pembejeo na kuzalisha mazao kwa wingi. Mazao hayo yangeuzwa nje ya nchi na vijana wengi wangejiajiri. Aidha, mpango huo uliingizwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Je, ni lini makambi hayo yataanzishwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika kilimo kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuongeza ajira. Katika kufanikisha azma hii Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kutumia Makambi ya Vijana ya Kilimo na Mkakati wa Ushirikishaji Vijana katika Kilimo (The National Strategy for Youth Involvement in Agriculture 2016-2021) unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo. Katika kutekeleza mkakati huu Serikali inafanya yafuatayo:-
(a) Kutumia vituo vya maendeleo ya vijana vilivyopo Ilonga - Kilosa, Morogoro na Sasanda – Mbozi, Songwe kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kutumia mashamba yaliyopo vituoni hapo kwa ajili ya shughuli za kilimo ambapo vijana hunufaika kwa kujipatia kipato kupitia mazao yanayozalishwa shambani.
(b) Kushirikisha vikundi vya vijana katika miradi mikubwa ya kilimo kama wakulima wadogo wadogo katika kilimo cha miwa eneo la Mbigiri na Mkulazi, Mkoani Morogoro.
(c) Kutekeleza Programu ya Ukuzaji Ujuzi nchini ambapo vijana wameanza kupatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kufundishwa ujuzi wa kutengeneza vitalu nyumba na kupatiwa vitalu nyumba kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaagiza halmashauri zote zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo ya kilimo. Agizo hilo limeendelea kutekelezwa ambapo hekta 217882.4 zimetengwa katika halmashauri 48 mwaka 2017. Serikali inasisitiza kila halmashauri ihakikishe inatenga maeneo hayo ili vijana wayatumie kwa shughuli za kilimo.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Barabara ya kuanzia Kanazi, Kata ya Kemondo kupitia Ibwera kwenda Katoro, Rubale na Izimbya ipo chini ya TANROADS, na ni muhimu kwa wakazi wa Bukoba na kwa uchumi wa Taifa:-
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara tajwa inaitwa Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 yenye urefu wa kilometa 42.37 na inapita katika vijiji vya Ibwera na Katoro. Barabara nyingine ni Rutenge – Rubale – Kishoju yenye urefu wa kilometa 74 ambayo inapita katika Vijiji vya Izimbya na Rubale. Barabara zote hizo ni barabara za Mkoa na zinahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Barabara hizi ni kiunganishi muhimu cha barabara kuu za lami ambazo ni barabara ya Mutukula – Bukoba – Kagoma – Lusahunga na barabara ya Kyaka – Bugene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa baraba hizi, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, barabara ya Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 imetengewa shilingi milioni 598.13 na barabara ya Rutenge – Rubale – Kishoju imetengewa shilingi milioni 333.20. Aidha, Serikali imejenga kwa kiwango cha lami maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 4.8 sehemu ya Kyetema hadi hadi Kanazi kwenye barabara ya Kyetema – Kanazi – Kyaka 2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za kuunganisha makao makuu ya mikoa, pamoja na barabara za kuunganisha Tanzania na nchi jirani. Hivyo, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za mikoa zikiwemo barabara za Kyetema – Kanazi – Kyaka 2 na Rutenge – Rubale – Kishoju utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Ugonjwa wa Mnyauko wa Migomba umekuwa tatizo kubwa na la muda mrefu na limewaathiri Wakulima wa Migomba Mkoani Kagera:-

Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua za makusudi za kupambana na ugonjwa huo na kuutokomeza kabisa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mnyauko wa migomba kitaalamu unaitwa unyanjano wa migomba. Husababishwa na vimelea aina ya bacteria ambao hushambulia aina zote za migomba na jamii yake. Ugonjwa huu unasambazwa na ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; miche iliyoathirika; vifaa vya shambani vilivyotumika kwenye migomba iliyoathirika na vifungashio vya kusafirisha ndizi.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2006 - 2014, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kagera tumekuwa tukitoa mafunzo ya kutokomeza ugonjwa huo kwa wakulima na Maafisa Ugani kwenye Wilaya zote zilizoathirika. Serikali imekuwa ikiendesha kampeni ya kung’oa migomba yote iliyoathirika, kukata Ua Dume na kuitekeleza. Halmashauri zote za Wilaya ya Mkoa wa Kagera ziliweka sheria ndogo ndogo za kuwataka wakulima kung’oa na kuchoma au kuzika migomba yote ailiyoathirika. Zoezi hilo lilipunguza ueneaji wa ugonjwa huo kwa asilimia 70.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya tafiti za kuzalisha miche bora ambayo haina vimelea vya ugonjwa wa unyanjano kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ikishirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation. Hadi sasa miche bora milioni sita imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Kagera na Kigoma.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia mbegu bora za migomba aina ya Shia 17, Shia 23, Nshakara, Nyoya na Kinohasha zinazozalishwa katika Taasisi za Utafiti Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Mikocheni, Uyole, Kibaha, Maruku na Tengeru ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutosafirisha ndizi zilizofungashwa na majani ya migomba kutoka mashamba yaliyoathirika.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Serikali ilishasema kwamba itatoa fedha ili maji yanayozalishwa na Mradi wa Maji BUWASA (Bukoba Water Supply and Sanitation Authority) yaweze kufika vijijini katika Kata za Maruku, Kanyangero, Kabaragaine, Katoma na Nyakato:-

Je, ni lini mradi huu utaanza kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Manispaa ya Mji wa Bukoba wanapata huduma ya majisafi na salama, mwaka 2016, Serikali ilikamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji. Aidha, baada ya kukamilisha mradi huo, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa maji ili wananchi wa maeneo ya Kata za Kibeta, Kagondo, Ijuganyundo na baadhi ya maeneo ya kata za Kahororo, Kashai, Nshambya na Nyaga waweze kunufaika kupitia mradi huo. Kwa sasa upanuzi huo umefikia asilimia 95. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka maji katika Kata za Maruku, Kanyangereko na Karabagaine.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Katoma, Wizara kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imefanya usanifu ili kutumia Mto Kyeiringisa kama chanzo cha maji katika eneo hilo na Kata ya Nyakato itanufaika kupitia upanuzi wa awamu ya pili ya mtandao wa maji wa mradi mkubwa wa Manispaa ya Bukoba.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, ni lini umeme utapelekwa katika Vijiji vya Buzi, Buguruka, Musina, Nsheshe na vingine ambavyo havijafikiwa na umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme na kufikisha katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo Desemba, 2022. Vijiji vinane kati ya vijiji 94 vya Bukoba Vijijini ambavyo ni Kijiji cha Buzi, Buguruka, Musira, Nsheshe, Ngarama, Omubweya, Kagarama na Rukoma vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ulianza kutekelezwa Mwezi Machi, 2021 na unatarajia kukamilika Mwezi Desemba, 2022 na gharama ya mradi huu kwa Jimbo la Bukoba Vijijini ni shilingi bilioni 2.04.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

(i) Je, ni lini ujenzi wa mradi wa katika Kata za Izimbya, Kyaitoke, Ruhunga, Mugajwale, Katoro na Kaibanja utaanza na kukamilika?

(ii) Je, ni lini mradi wa maji wa Kata za Kemondo, Katerero na Bujugo utaanza na kukamilika?

(iii) Je, ni lini mradi wa maji wa Kata za Karabagaine, Maruku na Kanyangereko utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuanza utekelezaji wa miradi ya maji ambayo itahudumia Kata za Izimbya, Kyaitoke, Ruhunga, Mugajwale, Katoro na Kaibanja katika mwaka wa fedha 2021/2022 na muda wa utekelezaji ni miezi 12 na mradi utakamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Kemondo – Maruku umeanza kutekelezwa ambapo kwa sasa upo katika awamu ya kwanza iliyoanza mwezi Januari, 2021. Utekelezaji wa mradi huu utatumia miezi 18 hivyo utakamilika mwezi Julai, 2022. Kupitia mradi wa Maji Kemondo – Maruku; Kata za Kemondo, Katerero, Bujugo, Maruku, Kanyangereko na Karabagaine zitanufaika.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kyetema – Katoro – Kyaka utaanza na kukamilika kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kyaka 2 – Kanazi – Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 amepatikana na anatarajiwa kusaini mkataba mwishoni mwa mwezi Juni, 2021. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamlika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Daraja la Kalebe utaanza na kukamilika kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Daraja la Kalebe lenye urefu wa mita 32.56 lipo katika barabara ya Kyaka II – Kanazi – Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.65. Barabara hii ni ya Mkoa na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Kalebe umejumuishwa katika mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kyaka II – Kanazi – Kyetema ambao unatekelezwa chini ya Mhandisi Mshauri Luptan Consult Ltd. kwa kushirikiana na Mhandisi Consultancy kwa gharama ya shilingi milioni 340.035. Kazi hii imeanza tarehe 31 Disemba, 2021 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara hiyo. Ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kyatema – Kanazi – Ibwela – Katoro – Kyaka kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kyatema – Kanazi – Ibwela – Katoro – Kyaka yenye urefu wa kilometa 60.6 umekamilika mwezi Oktoba, 2022. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, lini Shule za Sekondari za Lyamahoro na Rubale zitaanza kutoa elimu ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza shule za kidato cha tano na sita katika halmashauri zote nchini kwa kuongeza miundombinu ya mabweni, madarasa na bwalo. Kupitia jitihada hizo, Shule ya Sekondari Lyamahoro imepata sifa ya kuwa Shule ya Kidato cha Tano na Sita na inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano kwa Mchepuo wa CBG Julai, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Rubale bado haina miundombinu ya kutosha kuiwezesha kuwa ya kidato cha tano na sita. Nitumie nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na wananchi kuanza kujenga miundombinu mingine na Serikali itatekeleza kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA Burugo – Nyakato katika Jimbo la Bukoba Vijijini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera ambacho ujenzi wake ulianza mwaka 2019. Utekelezaji wa mradi huo unafanywa kupitia ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wenye thamani ya shilingi bilioni 22.4 na mradi umefikia asilimia 96 na unategemea kukamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa ya utoaji wa mafunzo kwa wananchi wa Jimbo la Bukoba Vijijini na Mkoa wa Kagera kwa ujumla. Nakushukuru.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, lini Tanzania itajiunga na Mkataba wa Budapest ili kujiimarisha na mapambano dhidi ya makosa ya kimtandao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa Budapest ni Mkataba ulioandaliwa mwaka 2001 na Baraza la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Makosa ya Mtandao. Mkataba huu ulianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 2004 na hadi sasa ni nchi 66 kutoka maeneo tofauti duniani ambazo zimejiunga na Mkataba huo, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni kutoka Bara la Afrika. Tanzania si miongoni mwa nchi ambazo zimejiunga na Mkataba huo. Aidha, katika hatua ya kutunga Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kwa sehemu kubwa maudhui ya Mkataba wa Budapest yametumika, kwa kuwa yanaakisi kwa mapana na usahihi mazingira ya kisheria dhidi ya uhalifu wa kimtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kuna jitihada za kuandaliwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya makosa ya mtandao ambao unahusisha nchi zote duniani na una mawanda mapana kuliko Mkataba wa Budapest. Hivyo, baada ya kufanya tathmini tumebaini kuwa hakuna haja ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Budapest na badala yake tutajiunga na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Makosa ya Mtandao utakaokuwa tayari kuanzia mwaka 2025.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, lini Tanzania itajiunga na Mkataba wa Budapest ili kujiimarisha na mapambano dhidi ya makosa ya kimtandao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa Budapest ni Mkataba ulioandaliwa mwaka 2001 na Baraza la Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Makosa ya Mtandao. Mkataba huu ulianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 2004 na hadi sasa ni nchi 66 kutoka maeneo tofauti duniani ambazo zimejiunga na Mkataba huo, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni kutoka Bara la Afrika. Tanzania si miongoni mwa nchi ambazo zimejiunga na Mkataba huo. Aidha, katika hatua ya kutunga Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kwa sehemu kubwa maudhui ya Mkataba wa Budapest yametumika, kwa kuwa yanaakisi kwa mapana na usahihi mazingira ya kisheria dhidi ya uhalifu wa kimtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kuna jitihada za kuandaliwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya makosa ya mtandao ambao unahusisha nchi zote duniani na una mawanda mapana kuliko Mkataba wa Budapest. Hivyo, baada ya kufanya tathmini tumebaini kuwa hakuna haja ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Budapest na badala yake tutajiunga na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Makosa ya Mtandao utakaokuwa tayari kuanzia mwaka 2025.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Maji Kemondo - Maruku katika Jimbo la Bukoba Vijijini utakamilika.
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaendelea na utekelezaji wa awamu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa chanzo cha maji na ulazaji wa bomba kuu kilometa nne na tenki la ujazo wa lita 3,000,000. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 utekelezaji wa mradi utaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, mradi huo utanufaisha Kata Tano za Bukoba Vijijini ambazo ni Kemondo, Bujogo, Katerero, Maruku na Kanyangereko.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, lini mradi wa kupeleka maji katika Kata Sita za Izimbya, Kyaitoke, Mugajwale, Ruhunga, Katoro na Kaibanja kutoka Ziwa Ikimba utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa mradi wa maji wa Ziwa Ikimba uliopangwa kunufaisha Kata Sita za Izimbya, Kyaitoke, Mugajwale, Ruhunga, Katoro na Kaibanja zenye jumla ya Vijiji 17. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Machi, 2024. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 inaendelea na uchimbaji wa visima katika Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo uchimbaji wa visima virefu Sita utafanyika katika Kata za Ruhunga, Kaibanja, Mgajwale, Izimbya, Katoro na Kyaitoke. Kwa ujumla uchimbaji huo umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Novemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali inatarajia kutekeleza mradi wa maji mwingine katika Kata ya Katoro utakaohusisha, ukarabati wa tanki la lita 150,000, Ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 35, ulazaji wa miundombinu ya kusambaza maji kilometa 37, kujenga nyumba ya pampu, kufunga umeme na Kununua na kufunga pampu ya kusukuma maji. Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo anatarajiwa kupatikana mwezi Januari, 2024.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Miradi ya Maji maeneo ya Omubweya, Rugaze, Amani, Kamukole na Kitwe kwani kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Vijiji vya Omubweya, Rugaze, Kitwe pamoja na Vitongoji vya Amani na Kamukole, Serikali imekamilisha utafiti wa maji chini ya ardhi, kwa ajili ya kuchimba visima virefu katika Vijiji vya Omubweya na Rugaze kupitia programu maalum ya uchimbaji wa visima 900. Aidha, kazi za uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu rahisi ya kutolea huduma (point source) katika vijiji hivyo itakamilika Desemba, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Serikali kupitia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, itafanya upanuzi wa Skimu ya Maji ya Karabagaine kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji katika vitongoji ambavyo havijafikiwa na mtandao wa maji katika Kijiji cha Kitwe ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2024 na Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 4,002 wa maeneo hayo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upanuzi wa Skimu ya Maji ya Kibirizi kupeleka huduma ya maji Vitongoji vya Amani na Kamukole.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka umeme vitongoji visivyokuwa na umeme Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuunganisha vitongoji ambavyo havina umeme ambapo vitongoji 258 kati ya 515 vya Jimbo la Bukoba Vijijjini vimefikishiwa umeme. Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 27 ambavyo havina umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini inaendelea kupitia Miradi ya Ujazilizi 2B na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA). Serikali itaendelea kupeleka umeme katika vitongoji vya Jimbo la Bukoba Vijijini kupitia miradi inayotarajiwa kufanyika mbeleni, ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, ni kwa nini Mradi wa Maji wa Kemondo, Maruku, umechukua muda mrefu kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mradi wa Maji Kemondo, Maruku, unaotekelezwa kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza imefikia wastani wa 95% na inatarajiwa kukamilika Mwezi Juni, 2024 na kunufaisha vijiji vitano vya Rwagati, Kanazi, Katoju, Buganguzi na Minazi. Aidha, awamu ya pili ya mradi huo imeanza utekelezaji ambapo umefikia wastani wa 67% na inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2024 na kunufaisha Vijiji vya Butayabega, Bulinda, Mulahya na Maruku.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu ambayo itahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji katika vijiji vya Kata mbili za Muhutwe na Kanyengereko itaanza baada ya awamu ya pili kukamilika. Kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kulisababishwa na kuchelewa kupokelewa kwa pampu za kusukuma maji zilizoagizwa kutoka Nchini Uturuki ambapo kwa sasa zimepokelewa na kazi ya ufungaji inaendelea.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, lini Miradi ya Maji katika Maeneo ya Ombweya, Rugaze, Nsheshe, Amani na Rukoma - Bukoba Vijijini itatekelezwa?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Bukoba. Utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Vijiji vya Ombweya, Rugaze, Nsheshe, Amani na Rukoma umepangwa kufanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza inahusisha uchimbaji wa visima virefu vinne katika Vijiji vya Nsheshe, Rukoma, Ombweya na Rugaze. Uchimbaji wa kisima kirefu katika Kijiji cha Nsheshe umekamilika ambapo kina uwezo wa kuzalisha maji lita 7,600 kwa saa. Aidha, utafiti wa maji chini ya ardhi unaendelea katika Vijiji vya Rukoma, Ombweya na Rugaze.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itahusisha usanifu na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika Vijiji vya Nsheshe, Rukoma, Ombweya na Rugaze pamoja na upanuzi wa Mradi wa Maji Kibirizi kwenda Kitongoji cha Amani ambapo umepangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2024/2025.