Supplementary Questions from Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza (26 total)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali wawili ya nyongeza.
La kwanza, nasikitika kwamba swali langu halijajibiwa, suala la Chuo cha VETA Kagera limezungumziwa muda mrefu sana humu ndani na nje ya humu ndani. Mkoa wa Kagera mzima hauna Chuo cha VETA cha hadhi ya Mkoa. Kwa hiyo, vijana wote wanaomaliza kidato cha nne au darasa la saba hawana fursa ya kupata mafunzo ya ufundi kuweza kujisitiri kwenye maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliaminishwa kwamba chuo hiki kingejengwa mwaka jana, tukatoa ardhi na mipango mingine ikaendelea na Waziri amefika pale mara mbili, tatu, ameangalia na kusema kwamba ujenzi unaanza, lakini hadi leo kwenye majibu tuliyopewa hapa hakuna matumaini hata kidogo chuo hiki kuanza kujengwa wakati wowote. Kwa hiyo swali langu halijajibiwa, ningependa kujua ni lini hasa kinakwenda kujengwa? Hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tupo humu ndani kwa ajili ya Bajeti ya mwaka ujao, ningependa kujua ni kiasi gani kimeombwa kwenye Bajeti hii kwa ajili ya chuo hicho, hayo mambo ya barabara , miundombinu, michoro na chuo chenyewe, ni kiasi gani kimeombwa kwenye Bajeti hii kwa ajili ya Chuo hicho? Asante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya juu ya chuo hiki, nami naona umuhimu wa chuo hiki katika Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anaweza kusema kwamba hatujajibu swali lake kwa sababu yeye anataka ni lini, lakini ujenzi wa chuo unaanza baada ya kupitia hatua mbalimbali na baadhi ya hatua zilizopitiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba eneo litakalojengwa chuo hicho limepimwa na ndiyo maana Serikali tayari imeshatoa fedha. Vilevile kushirikisha wadau wengine na baada ya kukamilika jitihada hizo, ndipo sasa tunaweza tukasema tukishakuwa na fedha tuanze kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu uzito juu ya chuo hicho lakini kimsingi niseme tu kwamba kwa sababu tulishapata hali ya mwelekeo ya baadhi ya wadau kutaka kukisaidia chuo hicho ndiyo tumekuwa tukiendelea nao na mazungumzo yeye mwenyewe ni shahidi, walishawahi kutembelea mpaka huko Kagera. Kwa hiyo naomba tu kwa sababu amekuwa na imani nasi atuamini na ajue kwamba muda wowote tutampa taarifa kadri tunavyoendelea na jitihada za ujenzi wa Chuo hicho.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Katika jibu Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Serikali imedhamiria na kodi zinazotozwa zitapitiwa, ina maana kazi hiyo haijaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akiwa kwenye kampeni pale Bukoba, tulimwambia kuhusu kodi hizi na tozo nyingi sana na akasema kwamba atakapokuwa Rais akiteua Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha na Waziri wa Biashara wakishindwa kuondoa kodi hizi atawatumbua. Leo yapata karibu miezi sita tangu wameteuliwa watu hawa na hakuna kodi hata moja ambayo imeondolewa. Je, hawa Mawaziri wako tayari kutumbuliwa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rweikiza Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye kwa nafasi yake ya Ujumbe wa Kamati Kuu naye anaweza akamtumbua Waziri yeyote. Nimhakikishie tu kwamba kwa kuwa kodi hizi zinahusisha taasisi zaidi ya moja, hivi tunavyoongea, tayari timu ya wataalam ambayo inaandaa Muswada wa Sheria ambao utaletwa hapa Bungeni ambao ndiyo unaopanga mapato na kodi zitakazofanyika katika mwaka wa fedha unaokuja, inakamilisha kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine, haya yote ambayo tumekuwa tukiyasema, hasa hili ambalo Mheshimiwa ametoka tu kulisema, sisi Waheshimiwa Mawaziri tumepigia mstari kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Rais. Jambo hili alilolisemea Mheshimiwa Rweikiza, liko ukurasa wa 17 paragraph ya tatu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati analizindua Bunge hapa na tuko kwenye hatua za mwisho za kulitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini tutakapokuwa tunajadiliana Finance Bill baada tu ya bajeti kubwa ya Serikali, mambo haya yanayohusu tozo za kero ambazo kimsingi Mheshimiwa Rais tayari alishayatolea maelekezo wakati anatupa kazi hii, sisi tutakwenda kulikamilisha na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake wanaendelea na kazi ya kutengeneza hiyo Finance Bill.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ni dhahiri kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kuna shule 29 za sekondari ambazo ni nyingi kwa shule moja ya form five na six. Hiyo shule moja ya form five na six sasa hivi haipo tena, baada ya tetemeko la ardhi imeharibika kabisa na imefungwa. Sasa Serikali haioni kwamba umuhimu umeongezeka baada ya shule hii kuharibika kabisa kuharibiwa na tetemeko la ardhi, kwamba juhudi zifanywe za ziada kujenga shule ya form five na six?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile shule ya namna hii ni shule ya Kitaifa kwa nini jambo hili wanaachiwa halmashauri ndio washughulike nalo kutafuta fedha, kujenga wenyewe na isijengwe na Serikali Kuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunajua kwamba, pale hali imekuwa ni mbaya na hasa katika ile shule ambayo imeporomoka zaidi, na hata hii Shule ya Lubale karibu nyumba mbili zimehaibika pamoja na baadhi ya madarasa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali italiwekea hili kipaumbele. Na ndiyo maana katika Mfuko huu wa Maafa ya Mkoa wa Kagera maeneo ya elimu tumeyapa kipaumbele cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ile shule iliyoharibika tutaijenga upya yote, lakini halikadhalika hii shule ya Lubale tutaweka nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba majengo yanarudi katika hali yake nzuri, ili vijana ambao wanasoma wapate elimu. Vile vile juhudi za Serikali kwenye janga hili ambalo limeupata Mkoa wa Kagera zitakuwa ni kupeleka nguvu za kutosha katika taasisi zote zilizopata uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake linalohusu shule hizi kuwa ni shule za kitaifa na kwamba kwa nini inaachiwa Halmashauri? Ni kweli na ndiyo maana tumetoa maelekezo kwamba kila halmashauri ifanye hivyo kwa sababu wote tunaunga mkono nguvu moja nguvu ya Kitaifa na ndiyo maana hata mpango wa Serikali wa uwezeshaji wa shule mbalimbali mwaka huu ni kuhakikisha tunaboresha zile shule za Kitaifa, lakini pia kuongeza nguvu kwenye zile za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo naomba nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Rweikiza kwa juhudi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwa upekee niwapongeze wananchi wa Mkuranga, nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Mbunge wa Mkuranga kwa kuwahamasisha vijana wapatao 53 watengenezaji wa matofali mapya karibu 45,000. Naomba niwasihi Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, mambo haya ni mambo ya kuigwa tufanye hayo kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo nilipenda niongezee kwenye eneo lifuatalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisera kila Kata inakuwa na shule ya sekondari ya kidato cha kwanza mpaka cha nne, lakini kwa kidato cha tano na cha sita, shule hizi zina umaalum wake na ni lazima ziwe na vigezo ambavyo vimeelezwa kwa mujibu wa sheria na si lazima kila eneo kuwa na shule yake ya kidato cha tano na cha sita, Kwa sababu hakuna mtoto aliyefaulu kwenda kidato cha tano ambaye atakosa nafasi kwa shule zetu tulizonazo nchini; kubwa hapa ni ubora wa shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rweikiza kama wao wana mpango wa kujenga shule ya kidato cha tano na cha sita waje tutawapa vigezo vinavyotakiwa ili tusirudi kwenye makosa yaliyopita ili tuweze kujenga shule zenye sifa zinazostahili kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita, kwa sababu hata tulizoanza nazo nyingine bado zina changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wawakilishi wa maeneo yote kuhakikisha kwamba tunapotaka kuanzisha shule ya kidato cha tano na cha sita basi vigezo vyote vile vya msingi vizingatiwe ikiwepo kwanza uwepo wa umeme, uwepo wa maji maeneo husika, majengo yanayostahili lakini na mazingira yanayoweza ku-accommodate masomo ya watoto wa kidato cha tano na cha sita.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba lengo la Serikali ya CCM ni kuwapatia Wananchi wengi maji safi na salama kwa gharama nafuu na ndiyo maana kuna miradi ya vijiji vingi nchi nzima kila Halmashauri ya kupeleka maji kwa wananchi na miradi hii inagharimu takribani kila mradi shilingi milioni 700 au 800. Mradi huu ninaoulizia swali, ulikuwa unahudumia vijiji sita; vijiji hivyo ni Maruku, Butairuka, Bwizanduru, Bulinda, Butayaibega na Buguruka. Mradi huu kama ungekarabatiwa haraka ungegharimu kama shilingi milioni 500 au 400 kwahiyo ni gharama nafuu na maji yangepatikana kwenye vijiji vyote hivi pamoja na Chuo cha Kilimo cha Maruku, shule kadhaa zipo pale za sekondari na za msingi. Sasa Serikali haioni kama ni busara mradi huu ukarabatiwe haraka wananchi wapate maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kwamba kuna umuhimu wa huo mradi kukarabatiwa ili uweze kutoa maji kwa namna jinsi ulivyokuwa umepangwa na kwenye jibu la msingi nimeeleza kwamba nia hiyo ipo na tayari Serikali imetenga fedha shilingi bilioni katika kuetekeleza miradi ya Halmshauri ya Bukoba lakini vipaumbele ni mradi upi wanaanza nao, wanaamua kule kule kwenye Halmshauri na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge ni sehemu ya Baraza la Madiwani katika kuweka vipaumbele na kwa sababu mradi huu tayari umeshakubaliwa na Serikali, kwa hiyo mimi ningeshauri kwamba uupe kipaumbele ili tukarabati na hivyo vijiji anavyosema viweze kupata maji.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuzuia uvuvi wa nyavu ambazo hazistahili, hazifai ni ni zuri na wavuvi hawa wanapokamatwa wanapata taabu sana, nyavu zinaharibiwa, wanakamatwa, wanawekwa ndani, na kadhalika, lakini hawa wavuvi hawajitengenezei nyavu hizi, wanazinunua madukani. Kwa nini wasikamatwe wale wanaoziuza ili ziondolewe? (Makofi)
Swali la pili, kwa jinsi ninavyofahamu, Tanzania hakuna kiwanda cha nyavu, kama kipo hakifanyi kazi. Nyavu hizi zinatoka nje ya nchi, zinaagizwa nje ya nchi, zinaingia Tanzania na Wizara ipo. Kwa nini Wizara isizuie nyavu hizi ambazo haziruhusiwi zisiingie? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo wavuvi pekee wanaolazimika kufuata Sheria ya Uvuvi kulingana aina ya nyavu wanayotakiwa watumie. Mtu yeyote yule ambaye anajihusisha na shughuli ambayo inapelekea kutumia nyavu ambazo hazitakiwi kutumika, anakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake 2009.
Kwa hiyo, mtengenezaji, msafirishaji, dalali, mtumiaji, mtu yeyote yule ambaye anaingia katika mfumo wa kuhakikisha kwamba nyavu hizo zinapatikana vilevile anakuwa ametenda kosa la kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba lengo la Serikali siyo kujaribu kuwabana na kuwaletea matatizo wavuvi, wao hasa ndio wanufaika wa kwanza na jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za uvuvi kwa sababu tusipolinda, baadaye hawatakuwa na cha kuvua. Ndiyo maana tunasisitiza zitumike nyavu ambazo zitafanya uvuvi uwe endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba kwa nini tusizuie nyavu ambazo zinatoka nje, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunazuia hata mwaka 2016 tulikamata nyavu pamoja na vifaa vingi ambavyo vilitoka China vilikamatwa bandarini na Serikali inaendelea kufuatilia mtu yeyote yule ambaye anaingiza nyavu ambazo haziruhusiwi.
Lakini vilevile lazima niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge changamoto iliyopo ni kwamba mara nyingine nyavu nyingine zinasokotwa kienyezi.
Kwa hiyo, watu wananunua nyuzi ambazo zinapatikana kwa ajili ya matumizi mengine halafu wanakwenda kutengeneza nyavu ambazo hazitakiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba tunadhibiti uingizwaji wa nyavu zile lakini vile vile utumiaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza siyo kweli kwamba amelipa madeni hadi Oktoba mwaka jana. Madai ninayo bado yapo mengi yana zaidi ya mwaka mmoja, miaka miwili sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, inakuaje Serikali inampa mtu kiwanda kwa mikataba na kwa utaratibu unaokubalika anashindwa kutimiza wajibu wake ambao ni pamoja na kulipa bei za wakulima na mishahara ya watumishi Serikali
inamuangalia tu mwekezaji huyo, anasema hapa ameahidi ambapo siyo kweli kama nilivyosema na Serikali inamuangalia tu huyu inasema ameahidi halafu inamuachia?
Swali la pili, wakulima hawa ambao hawalipwi hela yao ya chai ndiyo wakulima hawa ambao wanalima kahawa. Tumesema humu mara nyingi kahawa ina bei hafifu. Wizara ni hiyo hiyo ya kilimo imeagizwa na Mheshimiwa Rais iondoe kodi kwenye zao la kahawa, kodi ziko nyingi karibu
30. Kwa nini mpaka leo kodi hazijaondolewa na wakulima hawa wanazidi kuumia, kwenye chai wanaumia na kwenye kahawa wanaumia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama ni kweli au siyo kweli kwamba tayari haya malipo yamefanyika, mimi nipo tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge ili tufananishe taarifa tulizonazo, kwa sababu kwa ripoti ambayo ninayo na ambayo ni ya Serikali inaonesha kwamba kuna malipo yamefanyika lakini niko tayari kukutana nae, tujadili tuone
taarifa sahihi ni ipi.
Mheshimiwa Spika, vilevile mazingira ya kampuni
ambayo anazungumzia ni magumu kidogo kwa sababu wakulima wenyewe ni wamiliki vilevile wa hisa kwenye kampuni ile kwa hiyo ilipobinafsishwa na Serikali wakulima wa chai vilevile nao waliweza kupata asilimia fulani. Pamoja na changamoto ambazo zimekuwepo bado wakulima nao vilevile ni wamiliki wa kiwanda kwa kiasi kikubwa, lakini kama nilivyosema Serikali imekuwa ikiendelea kuwasiliana na kiwanda ili kuondoa hizo changamoto ambazo zimetokea.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kumekuwepo na manung’uniko ya haki kabisa kuhusu tozo na kodi nyingi ambazo zimepitiliza katika zao la kahawa na mazao mengine. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge
kwamba siku tutakaposoma hotuba yetu kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha awepo maana yake tutaziondoa tozo mwaka huu mpaka nyingine mtatuomba tuzirudishe.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ingawa baadhi ya maeneo aliyosema yamekamilika, miradi yake haijakamilika. Nina maswali mawili ya nyongeza:
Swali la kwanza; maeneo niliyoyataja haya ya Kata ya Ruhunga, Kibirizi, Izimbya, Mugajwale, Rukoma, Kikomelo na mengine kama Kaitoke, Kyamuraire yana shida kubwa sana ya maji na swali hili nimeliuliza leo ni mara ya nne. Je, niulize mara ngapi ili hawa wananchi nao wafikiriwe kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile tumeshapata ufumbuzi wa tatizo la maji nchi nzima maana yake siyo kwangu tu ni nchi nzima kuna tatizo la maji nao ufumbuzi huo ni kuunda wakala au Mfuko wa Maji nchi nzima kama ilivyo REA kwenye umeme. Tumelijadili humu mara nyingi na tumekubaliana. Je, kwa nini Mfuko huu hauanzi ili tatizo hili liweze kupata ufumbuzi. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza huo mradi wa maji kwenye eneo lake tulishaujadili na tukaangalia uwezekano wa namna gani tunaweza tukapeleka maji pale kwa kutumia chanzo cha maji cha Ziwa Victoria kutoka kwenye mradi uliokamilika pale Bukoba na tayari tulishaagiza wataalam wanafanyia kazi ili tuweze kufikisha maji katika hayo maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu uanzishaji wa Mamlaka ya Maji Nchini tunalifanyia kazi na tuko katika hatua nzuri kabisa wakati wowote tutaleta tangazo kwamba tayari Wakala wa Maji Nchini utaanzishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji pale tutakapopata ridhaa ya Bunge. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu ya Serikali ambayo yametolewa, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Bukoba wanalima chai pamoja na mazao mengine. Wanajituma, wanaweka bidii kubwa sana kwa lengo la kukuza uchumi wao, uchumi wa familia zao na uchumi wa Taifa. Huyu mwekezaji kama jibu lilivyosema anawadhulumu wakulima hawa, hawalipi fedha zao, hawalipi haki zao; wakulima pamoja na wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na majadiliano hayo ya mwezi Oktoba na mwezi Desemba mwaka jana, jibu linamalizia kwamba Serikali haioni saabu ya kuvunja mkataba. Kweli pamoja na dhuluma hii anayowafanyia mwekezaji huyu Serikali haioni sababu ya kuvunja naye mkataba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli inahimiza uchumi wa viwanda, lengo ni hilo hilo kuboresha ustawi wa Tanzania, kuongeza ajira na uchumi wa Taifa. Huyu anafanya kinyume na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, bado wanasema hawaoni sababu ya kuvunja mkataba, kweli hii ni sawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitakuwa mtu wa mwisho kuona Watanzania wanadhulumiwa na mimi na Waziri wangu tukiwa ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema ameshafanya malipo yote na kwa sasa yuko current kwenye malipo ya wafanyakazi lakini pia malipo ya wakulima, anawalipa kila wanapomaliza kuuza chai yao anaendelea kuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kilichotokea huko nyuma, Kampuni hii ya Spearshield Africa Company Limited ilinunua hisa za asilimia 75 kwenye kiwanda hiki. Asilimia 25 zilitakiwa zinunuliwe na wakulima wenyewe hadi leo hii wakulima wameshindwa kununua hizi hisa asilimia 25 na uzalishaji wao ukawa si wa tija ndiyo maana mwekezaji akawa anazalisha chini ya ufanisi, akawa anashindwa kufanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwekezaji huyu pamoja na kwamba makubaliano ya awali ilikuwa baada ya kuchukua asilimia 25 aweze kuweka uwekezaji wa milioni 99 za Kitanzania, lakini kwa sababu ana nia thabiti mwekezaji huyu mpaka Desemba, 2016, tayari alishawekeza zaidi ya bilioni 3.8 kwenye ununuzi wa mitambo, kwenye kilimo na kuwawezesha wakulima kwenye ukulima bora wa mazao yao, kwa hiyo ana nia thabiti ya kufanya jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa imempa maelekezo kwamba awe anatoa taarifa kila baada ya miezi miwili ya utendaji kazi wake, mahusiano yake na wakulima, lakini mahusiano yake na wafanyakazi, na ameanza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, naomba tumpe nafasi mwekezaji huyu, ameonesha dhamira ya kutosha, amewekeza kutoka milioni 999 zilizopo kwenye mkataba mpaka bilioni 3.8 , tumpe nafasi, ana nia thabiti atawawezesha ndugu zangu, wakwe zangu, shemeji zangu na wifi zangu wa Bukoba, kwa kiwanda hiki naamini watarejesha uchumi wao kama ilivyokuwa miaka ya 1960 na 1970.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naishukuru pia Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa nini Serikali wasifikirie kutafuta wawekezaji ili wajenge viwanda huko Buhigwe au kiwanda huko Buhigwe cha kuongeza thamani kwenye zao la tangawizi ili wananchi waweze kunufaika zaidi kupata ajira na kadhalika badala ya kufikiria soko la kwenda Ulaya na Marekani peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, matatizo ya tangawizi Buhigwe yanafanana na matatizo ambayo yanatukumba kule Bukoba kuhusu vanilla. Vanilla ni zao ambalo liliingia Kagera likawa na mafanikio makubwa sana, likastawi vizuri na lilikuwa na bei nzuri sana, lakini hakukuwa na soko la zao hili kwa hiyo wananchi wameacha kulima zao hili. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wananchi hawa ili zao hili lifufuliwe na liongeze kipato kwa wananchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inashirikiana na wananchi kutafuta wawekezaji, mamlaka ya Mkoa kwa kushirikiana na SIDO na Tantrade inatafuta wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie, wawekezaji wa kiwanda cha tangawizi ni sisi wenyewe, kiwanda cha tangawizi kinahitaji pesa isiyozidi millini 200 au 500, hii watanzania wa kawaida wanaimudu. Kwa hiyo wawekezaji wa viwanda vya tangawizi millioni 200, 300, 400, 800 kiwanda cha kati sisi tunaweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili ambayo inaendana na namba moja, Mheshimiwa daktari kepteni ni kwamba nawasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera kati ya mwezi wa saba mpaka wa nane litaendeshwa kongamano kubwa la wafanyabiashara na wawekezaji. Na mimi ni mdau wa Kagera tutasimama wote nikitoka hapo nakwenda Kigoma nitakayoyasema Kagera nitayasema Kigoma tuchangamke sisi wenyewe tuwekeze.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nchi zinazotuzunguka, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi na Msumbiji wote wameridhia mkataba huu. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye jibu lake ni nchi sita tu duniani ambazo hazijaridhia na sisi Tanzania tukiwemo. Je, Serikali haioni kwamba ni aibu kubwa sana Tanzania kuwa kwenye kundi hili dogo la nchi sita ambazo zina matatizo ya ndani ambao hazikaridhia mkataba huu za kina Haiti na nyingine hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kutoa ratiba (timeframe) ya kupitia kumaliza mchakato huu wa mkataba huu Serikalini na hatimaye kwenye Bunge hili kabla haujakwisha mwezi wa Juni au Septemba angalau mkataba huu uje Bungeni hapa kwa ajili ya kuridhiwa? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, haikuonekana sababu wakati ule kwa sababu bila ya kuwa tumeridhia tuliweza kufanya shughuli zetu zote bila ya matatizo yoyote; lakini kwa sasa hivi sababu ipo. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kutokana na matukio ya kigaidi suala hili sasa limefikia wakati muafaka turidhie ili tuondokane na kuwa katika nchi chache ambazo hazijaridhia kama nilivyosema. Ndiyo maana tumeshatayarisha waraka kwa madhumuni ya kupita katika ngazi za maamuzi ili hatimaye uletwe hapa kwa kuridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la timeframe, ninachoweza kusema ni kwamba, utaratibu ni kwamba waraka ukishakamilika una hatua tatu; ya kwanza ni Cabinet Secretariat ambapo unajadiliwa na baadaye IMTC na hatimaye unapita kwenye Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni matumaini yangu kwamba hatua hizi tatu zitafanyika kwa haraka ili tuweze kukamilisha suala hili na mkataba huu uridhiwe. Ningependa nimwarifu Mheshimiwa Rweikiza kwamba, kwa Bunge hili tutakuwa tumechelewa, lakini huenda Septemba tukaweza kufanya shughuli hii ikakamilika.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa tozo karibu 20 kwenye tasnia ya kahawa. Hata hivyo, pamoja na shukrani hizo sehemu ya jibu inasema kwamba bei ya kahawa inakuwa ndogo kwa sababu ya kutoeleweka vizuri kwa maelekezo ya Serikali kuhusu uuzaji wa kahawa kwenye soko la moja kwa moja (direct exports) kahawa hai organic coffee na kahawa haki (fair trade coffee) miongoni mwa wanunuzi na viongozi wa ushirika, kutoeleweka vizuri kwa maelezo ya Serikali.
Je, Serikali imechukua hatua gani ili hii ieleweke vizuri na wakulima wapate bei nzuri?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, bei ya kahawa ni ndogo kama anavyojua Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia Serikali imeuzia wanunuzi binafsi wote, walikuwepo wengi Olam, Kagira na wengine imewazuia sasa hivi hawaruhusiwi kununua kahawa kwa wakulima. Hawa walikuwa na bei nzuri kidogo na msimu ulikuwa unawahi hauchelewi kama ilivyo sasa na mkulima alikuwa anapata nafuu. Kwa nini Serikali imezuia wanunuzi binafsi na inawatesa wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Spika, ni kweli maelekezo ya Serikali yalikuwa kwamba mnunuzi yoyote mwenye soko la moja kwa moja nje ya nchi kwa kahawa hai na kahawa iliyozalishwa kwa kutumia haki anaruhusiwa kuuza kahawa hiyo ili mradi wakulima wale kwa sababu wanatambulika, wapitie kwenye vyama vyetu vya ushirika. Agizo hilo halikueleweka vizuri kwa wanunuzi wala kwa vyama vya ushirika wakadhani kwamba Serikali tumepiga marufuku kwa ajili ya direct export.
Mheshimiwa Spika, hatua gani Serikali imechukua, kwanza tuliwaita wanunuzi wote walifika pale Wizarani wiki moja iliyopita na wadau wengine kwa ajili ya kuwapa ufafanuzi huo na kwa sasa wanunuzi wote wamelielewa hilo na wameshachukua maelekezo ya Serikali. Mnunuzi yoyote mwenye soko la moja kwa moja ambaye anawafahamu wakulima wake anaruhusiwa kukusanya kahawa hiyo na kutuonesha hicho kibali chake kinachoonesha bei aliyouzia ili kwamba tozo na ushuru mwingine wa Serikali tuupate kama inavyostahili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini kama Serikali tumekataza wanunuzi binafsi wasinunue kahawa kwa wakulima. Kama Serikali hatujakataza wanunuzi binafsi kununua kahawa kutoka kwa wakulima. Tulichoelekeza Serikali kwa ajili ya kulinda ubora wa kahawa, lakini pia kupata takwimu sahihi tulizielekeza Halmashauri zetu Serikali za Mikoa na Wilaya pamoja na Vyama vya Ushirika, lakini hasa Vyama vya Msingi vya ushirika ndio wenye jukumu la kukusanya kahawa ile kutoka kwa wakulima na kuipeleka wenyewe Moshi na wale wanunuzi watakuja kununua kahawa pale Moshi. Hili tumelifanya kwa ajili ya kudhibiti ubora na pia kwa ajili ya kupata takwimu sahihi.
Mheshimiwa Spika, nimueleze Mheshimiwa Rweikiza, uzalishaji wa kahawa mwaka jana ulikuwa ni tani 50,000 tu lakini kwa mfumo huu mpaka sasa tulishafikia, kwa kahawa ya maganda, zaidi ya tani 80,000. Mpaka msimu ukiisha tunatumaini tutafikisha zaidi ya tani 100,000.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo lengo lilikuwa kuwawezesha hawa wakulima wauze wenyewe soko la Moshi; lakini kwenye jibu langu la msingi nimeeleza sababu zilizosababisha bei kushuka. Pia kulikuwa na ukiukaji, maelekezo ya Serikali yalikuwa kwamba vyama vya msingi ndivyo vikusanye kahawa ile, lakini…
… baadae kahawa ile ikachukuliwa na vyama vikuu. Nataka nimuhaidi Mheshimiwa Rweikiza mwakani haitokuwa hivyo hivi vyama vyetu vikuu vya ushirika vyenye madeni ya kutupwa havitoweza kuruhusi wa tena kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima bali ni vyama vyao vya msingi wakulima wenyewe ndio watakusanya kahawa na kuiuza katika masoko yetu. (Makofi)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninapenda kujua, kwa kuwa kilimo ndiyo bado ni uti wa mgongo wa uchumi wetu na vijana ni nguvu kazi safi sana, wana nguvu ya kufanya kazi hawa, wakiwezeshwa wakapewa matrekta, pembejeo, utaalam kidogo kwenye makambi kule watafanya kazi nzuri sana tutapata mazao mengi sana tutauza ndani na nje ya nchi tutapata fedha nyingi sana, vijana watajikomboa na nchi itapata utajiri mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mpango huu haujaanza rasmi ili uweze kujulikana kwaba ni mpango wa vijana makambini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wali la pili, jambo hili lipo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015 baada ya mimi kulisema Bunge lililopita 2010 - 2015, liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, tangu ilani hiyo tumeshafanya bajeti tatu, 2016, 2017 na hii ya juzi, sijaliona kwenye mpango wa Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa nini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kwanza kabisa kumuelezea Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya maeneo ambayo yanasaidia sana kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana ni pamoja na kilimo na hata katika Jarida la mwaka 2016 la The Global Employment Trend, limesema moja kati ya maeneo katika nchi zinazoendelea ambayo yakitumiwa vyema yatatatua changamoto ya ukosefu wa ajira ni kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, kwa swali lake ambalo ameuliza kuhusu pembejeo kwa makundi ya vijana rai yetu ni kwamba tumeendelea kuwahamasisha vijana kwa makundi na mmojammoja wale wote ambao wanafanya shughuli za kilimo waendelee kutumia mifuko yetu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na Benki ya Kilimo kwa ajili ya kupata mitaji na fedha kwa ajili ya pembejeo. Tukiamini kabisa kwamba mifuko hii ipo kwa ajili ya kuwasaidia kuweza kufikia malengo yao. Nitoe rai tu kwa vijana wote, hasa wale ambao wanapenda kushiriki katika shuguli za kilimo, waitumie mifuko yetu hii kwa ajili ya uwezeshaji; na wapo vijana ambao wamefanikiwa kupitia mifuko hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu kwamba mpango huo, pamoja na kwamba upo kwenye ilani lakini haujaonekana katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka kuanzia 2016 mpaka leo. Ukiangalia katika taarifa ya Waziri Mkuu kwa maana ya hotuba, hili jambo limesemwa na ndiyo maana tumekuja na mpango mkakati wa ukuzaji ujuzi nchini moja wapo ikiwa ni kuhakikisha kwamba vijana wetu kwanza tunawabadilisha mtazamo waone kwamba kilimo ni sehemu pia ya kufanya shughuli ya kiuchumi. Lakini la pili, tumeamua sasa kuja na mpango madhubuti wa kuwa na vitalu nyumba kama njia ya kwanza kuhamasisha vijana wafanye shughuli za kilimo, kwa hiyo tumelisema na lipo kwenye mpango na tunaanza utekelezaji.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina kata 29. Kati ya hizo, kata 20 zinahudumiwa na barabara niliyoitaja. Kata hizo ni Katerero, Kemondo, Ibwera, Nakibimbiri, Kasharu, Kisogo, Kaibanja, Katoro, Kyamuraire, Ruhunga, Mugajalwe, Izimbya, Kibirizi, Kaitoke, Kikomero, Rukoma, Rubare, Buterakuzi, Mikoni na Bujugo. Aidha, Bukoba kuna mvua nyingi sana barabara ya udongo inaharibika, mara nyingi inakuwa haipitiki na huko ndiyo kuna mazao mengi kama kahawa na ndiyo uchumi mzima uko kule. Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kujenga lami barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rweikiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua maeneo haya ni muhimu sana katika uzalishaji na pia tunatambua kwamba ziko mvua nyingi na kumekuwa na uharibifu wa mara kwa mara. Nampongeza tu Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu mara nyingi tumezungumza juu ya kuhakikisha kwamba barabara hizi tunazitengeneza na kwa kweli kama alivyosema, hizi ni kata nyingi sana, kata 20 kati ya kata 29.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge ikiwa ni pamoja na wananchi wa maeneo ya Kata hizi ikiwemo Kata za Katerero, Kemondo, Ibwera na kata nyingine kwamba baada ya kukamilisha kuunganisha mkoa na mikoa mingine nguvu kubwa tutailekeza katika maeneo haya ya barabara ambazo zinapita kwenye wilaya zetu ikiwemo maeneo haya aliyoyataja ili sasa tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Bukoba Vijijini kwamba maeneo haya tutayatazama na tutayaweka katika mpango ili siku za usoni tuweze kuitengeneza barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na ni kweli ugonjwa huu umepungua kwa asilimia kubwa, lakini haujaisha. Sasa Serikali kwenye majibu inasema kwamba jitihada zimekoma 2014, lakini ukweli ni kwamba ugonjwa huu bado haujaisha kabisa, bado upo ingawa umepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, napenda kujua ni jitihada gani mahususi ambayo Serikali inayo kutokomeza ugonjwa huu uishe kabisa kwa asilimia 100? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sambamba na ugonjwa huo wa migomba kuna mnyauko pia wa mikahawa, kuna mnyanjano pia wa mihogo unaitwa batobato na yote haya yanalimwa Kagera haya. Napenda kujua ni jitihada gani zinachukuliwa na Serikali kuondoa magonjwa hayo mengine na mazao mengine kama kahawa, migomba, mihogo na mazao mengine?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Jasson Rweikiza kwa jitihada nzuri za kuhakikisha kwamba tunatokomeza ugonjwa wa mnyauko wa ndizi pamoja mnyauko wa kahawa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jasson Rweikiza ni mkulima mzuri wa ndizi, nilishawahi kutembelea shamba lake. Kwa hiyo, nakupongeza kwa kupambana na jitihada hizi huku nawe ukiwa mkulima kwa kuonesha mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya Mheshimiwa Jasson Rweikiza, swali la kwanza angependa kujua mikakati ya Serikali ya kutokomeza mnyauko wa migomba, ni kwamba Serikali kama nilivyosema kwenye swali nililojibu wiki iliyopita, Mheshimiwa Rais wetu ametusaidia kupata mabilioni kutoka IFAD; shilingi bilioni 127.3 kwenda kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI na ASA) kwenye kuzalisha mbegu pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi hasa hasa kwenye magonjwa kama haya ya mnyauko na magonjwa mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Rweikiza kwamba Serikali tayari ina jitihada mahususi za kuhakikisha tunapata fedha za kutosha kupambana na magonjwa haya. Vile vile nikuhakikishie katika bajeti ambayo itaenda TARI na ASA tutahakikisha bajeti kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya mnyauko wa kahawa na ndizi na yenyewe inazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu yanayotia matumaini kutoka Serikalini, lakini ametaja vijiji ambavyo bado havijapata umeme, kuna kimoja hakukisema ambacho kinaitwa Ruhoko. Kijiji hiki kimefungwa waya zote, kimefungwa transfoma, kimewekwa nguzo, kila kitu kimekamilika mwaka wa pili leo umeme haujawashwa kwa nini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; amesema vijiji nane kati ya vijiji 94 ambavyo vimesalia kupata umeme, lakini na vitongoji 515, kati ya vitongoji hivyo vyenye umeme ni 86 tu zaidi ya vijiji 400 havina umeme. Utaratibu ukoje kuhusu vitongoji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Samson Jasson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, na-declare interest kwamba mimi natoka Jimbo la Bukoba Mjini na kabla ya utumishi wa Bunge nilikuwa mtumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba. Kijiji cha Luoko nakifahamu kiko katika Kata ya Katoro na katika ufuatiliaji wetu Kijiji cha Luoko tayari kilishapelekewa umeme, lakini tulipata changamoto ya kutopata wateja wa kuwaunganishia umeme katika kijiji hicho na hivyo miundombinu ile ilikuwa haijaanza kufanya kazi.
Waheshimiwa Wabunge, watakumbuka kuna kipindi Mheshimiwa Waziri wa Nishati alisema kwamba, wale ambao atawapelekea umeme na hawatataka kuunganisha basi itabidi tutumie jitihada za ziada za kuwalazimisha kuunganisha ule umeme. Ningekuwa naweza kufanya hivyo na Kijiji cha Luoko kingekuwa kimojawapo ambapo tungewalazimisha wananchi kuunganisha umeme huo.
Mheshimiwa Spika, lakini tayari tumeshafanya sensitization na wananchi wa Luoko wako tayari kuunganishiwa umeme. Tumemuelekeza mkandarasi aliyekuwa anapeleka umeme katika kijiji hicho anaitwa Nakroi ambaye alipeleka umeme katika Awamu ya Pili ya Mzunguko wa REA na yuko tayari kupeleka umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Kijiji cha Luoko kitapepekewa umeme ndani ya muda mfupi baada ya utaratibu wa kuunganishiwa wananchi kuwa umekamilika.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili kuhusiana na vitongoji vya Jimbo la Bukoba Vijijini; upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ni zoezi endelevu na kama ambavyo nimekuwa nikisema, tunapeleka umeme kwenye vitongoji katika njia tatu; kwanza TANESCO wamekuwa wakiendelea kupeleka umeme katika maeneo ya vitongoji vyetu, lakini njia ya pili ni kupitia hiyo miradi ya REA ambayo tumekuwa tukipeleka umeme kwenye vijiji na tunapeleka kwenye vitongoji, lakini njia ya tatu uko mradi maalum wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaoitwa densification. Na tulianza na Densification Awamu ya Kwanza tulipeleka katika mikoa nane, tukaja na Densification Two (A) tukapeleka katika mikoa tisa na sasa tuko Densification Two (B) inaendelea katika mikoa kumi na tutamalizia na Densification Two (C) ambayo tunatarajia ianze mwezi Julai kupeleka katika mikoa inayobakia.
Mheshimiwa Spika, tukiri kwamba hatuwezi kupeleka katika vitongoji vyote kwa wakati mmoja, lakini kama tunavyosema upatikanaji wa fedha na upelekaji wa umeme ni zoezi endelevu tunaamini ifikapo 2022 vijiji vyote Disemba vitakuwa vina umeme na kwenye vitongoji tutaendelea kupeleka kwa kadiri ya kuhakikisha kwamba, kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme. Serikali Sikivu inapeleka umeme kw wananchi kwa maendeleo yao wenyewe.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, majibu haya ni mazuri kuyasikia kwenye masikio na yanafurahisha, lakini siamini kama kuna ukweli wa kutosha kwasababu kwa mfano hili swali (c) kuhusu Mradi wa Maji Karabagaine nimewahi kuliuliza humu ndani majibu yakawa ni haya haya kwamba mradi huu utaanza, lakini mpaka leo haujaanza. Sasa leo nitaaminije kinachosemwa hapa ni kweli?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante nipende kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Rweikiza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara tupo katika mageuzi makubwa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na mradi kama huu wa Karabagaine ni mradi wa muda mrefu lakini ni katika ile miradi ambayo tayari tupo katika mpango wa kuona kwamba utekelezaji wake unafikia sasa mwisho.
Mheshimiwa Spika, hivyo nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameshafuatilia kwa muda mrefu na jitihada kubwa namna ambavyo tumeweza kushirikiana pamoja nikuhakikishie mradi huu unakwenda kutekelezwa katika mwaka wa fedha huu 2021/ 2022 na itawezekana kwa sababu tumedhamiria kuleta mageuzi makubwa.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, lakini majibu haya vilevile yaliwahi kutolewa huko nyuma kwa swali hilihili ambalo limewahi kuulizwa, lakini tukaambiwa hela imepatikana ya msanifu na msanifu huyo hakuonekana na barabara hiyo mpaka leo haijawahi kujengwa. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, Wizara inafahamu umuhimu wa barabara au inajibu tu ilimradi kujibu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa vile Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka jana imeiweka barabara hii kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami na kwa ville hata Ilani iliyopita ya mwaka 2015 ilikuwa na barabara hii, je, naweza leo kupata commitment ya Serikali kwamba ni lini ujenzi huu wa barabara hii kwa kiwango cha lami unaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jasson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatambua umuhimu wa barabara hii na ndio maana mwenyewe anafahamu kwamba ana vijiji karibu 29, vijiji 18 vipo katika barabara hii kwa hiyo ikijengwa ni wazi kwamba uhakika wa yeye kuendelea kuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini utakuwa umetimizwa.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2020/2021 kuna fedha milioni 557 zilitengwa kwa ajili ya kuendelea kufanya maboresho ili barabara hii iendelee kupitika wakati wote.
Vilevile mwaka wa fedha 2021/2022 zimetengwa fedha zaidi ya milioni 217 kwa ajili ya kuendelea kufanya maboresho. Kwa hiyo, hii inaonesha kwamba Wizara inajua umuhimu wa barabara hii na ndio maana imekuwa ikitenga fedha kutoka mwaka hadi mwaka ili kuendelea kuiboresha ili wananchi wa Bukoba Vijijini waendelee kupata huduma hiyo ya barabara.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; ametaka kujua commitment ya Wizara. Kwenye jibu la msingi nimesema barabara hii tayari kuna mhandisi mshauri ambaye atafanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Na barabara hii kuna wahandisi wawili ambao wamepatikana; Mhandisi consultant ambaye atafaya kazi ya kutoka Kyetema – Kanazi – Katoro – Kyaka yenye urefu wa kilometa 60.7 atafanya kazi hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Spika, mhandisi wa pili Age Consultant yeye atafanya kazi sehemu ya barabara ya Bukoba, Bosimbe na Maluku yenye urefu wa kilometa 19.
Kwa hiuyo, wahandisi hao wawili wakifanya kazi hii ikikamilika sasa tutaanza angalau kilometa chache kufanya kazi ya ujenzi wa lami katika eneo hili ili Mheshimiwa Mbunge Jasson Rweikiza aendelee kuwa na uhakika wa kuendelea kuwa Mbunge wa eneo hili, ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Swali la kwanza; kwa kuwa huko nyuma nimewahi kuuliza swali hili humu ndani la barabara hii na daraja hili na nikapewa majibu yanayofanana hivyo huko nyuma zaidi ya mara mbili.
Je, ni lini nitapewa majibu ambayo yanatia moyo zaidi na matumaini zaidi kuliko hayo majibu niliyopewa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kama alivyosema Mheshimiwa Waziri na kazi hiyo inakaribia kukamilika, na kwa kuwa barabara hii na daraja hili linahudumia kata 18 kati ya kata 29 za Jimbo langu, na kwa kuwa hii pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano.
Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa na kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kwa kufuatilia sana hii barabara. Ametaka Serikali impe maneno ya matumaini, naomba niseme siyo tu maneno ya matumaini lakini atakubaliana nami kwamba Wakandarasi sasa hivi wapo site wakiwa wanafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba daraja alilolisema litatekelezwa kwanza kabla halafu wata- submit document lianze kujengwa halafu ndiyo upembuzi na usanifu wa kina wa barabara uendelee wakati daraja hili linajengwa.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Rweikiza awe na imani kwamba kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ipo kazini na wananchi wawe na matumaini kwamba walichoahidi Marais kinatekelezwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, inaonesha kwamba Serikali huenda haifahamu vizuri barabara hii.
Mheshimiwa Spika, barabara hii inahudumia kata 18 za Bukoba, inahudumia wilaya mbili; Wilaya ya Bukoba na Wilaya ya Misenyi, inahudumia nchi mbili; inaziunganisha Tanzania na Uganda na vita ya mwaka 1978 ya Iddi Amini ilipiganwa kwa kutumia barabara hii.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kwenda Bukoba kuangalia barabara hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara hiyo kuna Daraja la Kalebe, daraja kubwa ambalo ni la zamani sana, ni bovu, linaruhusiwa uzito wa tani saba, lakini kwa vile hakuna ulinzi wala kizuizi wanapita magari ya tani 15 mpaka 20.
Je, tunasubiri watu wafe pale ndio mtengeneze daraja hilo na barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rwekiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri Mheshimiwa Mbunge amekuja mara kadhaa Wizarani akifatilia ujenzi wa barabara hii pamoja na daraja lake. Kwa niaba ya Serikali napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ya kwamba nipo tayari kuongozana naye kwenda jimboni Bukoba Vijijini ili nikashuhudie na kuona barabara hii pamoja na daraja hili mara baada ya vikao hivi vya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili suala la Daraja la Kalebe ni sehemu ya barabara hii ya kutoka Kyatema- Kanazi, Bwela, Katoro – Kyaka; na kwa maana hiyo kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekwishakamilika na mwaka ujao wa fedha tumeweka mapendekezo kwamba barabara hii na daraja hili vijengwe.
Kwa hiyo, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikifika aipitishe ili pia daraja tuweze kulijenga, ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa majibu hayo ingawaje kuhusu Lyamahoro Secondary School limejibiwa hivi zaidi ya miaka miwili, kwamba inaanza mwezi ujao, lakini haijaanza. Sasa swali: -
Je, Serikali inafahamu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba nzima haina shule ya ngazi ya kidato cha tano na sita? Inafahamu hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali inafahamu kwamba tukipata shilingi milioni 80 kila shule, kwa Lyamahoro 80 na Rubale 80, shule hizi zinakamilika kuwa na kidato cha tano na sita, zinaweza zikaanza?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua shauku ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha katika Halmashauri yake ya Bukoba wanapata shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita. Na ndiyo maana katika jibu la msingi Shule ya Sekondari ya Lyamahoro imeshapata sifa. Kwa hiyo, nimhaikishie tu kwamba Julai inapokuwa inaanza maana yake na shule hii itatekelezeka; kwa hiyo tunatambua kwamba hakuna na ndiyo maana utekelezaji wake unakwenda kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu kupeleka hizo shilingi milioni 80 katika hizo shule mbili ni sehemu ya fedha ambayo nafikiri itatosha tu kukamilisha baadhi ya miundombinu kwa sababu ili shule iwe na kidato cha tano na sita inahitaji bweni, bwalo, jengo la utawala pamoja na madarasa ya ziada na vyoo. Kwa hiyo kuna bajeti kidogo ambayo inahitajika kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba Serikali itatafuta fedha ikishirikiana na halmashauri pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Awali napenda niipongeze na kuishukuru Serikali kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa Chuo cha VETA, kizuri, lakini nina swali moja la nyongeza.
Je, mara tutakapoanza kuchukua wanafunzi na kuwaingiza kwenye masomo, wanafunzi hawa wa chuo hiki watapatiwa mikopo ya Serikali ili masomo yaweze kutolewa vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa bado Serikali hatujaanza utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa wa VETA na vyuo vingine vya kati. Kwa hiyo, tunachofanya ni nini sasa kama Serikali? Tunachofanya kama Serikali kwa vyuo hivi vya kati pamoja na VETA, tumejaribu kupeleka ruzuku kwenye maeneo hayo na ndio maana utaona hata ada zake tofauti na vile vyuo vingine vya juu. Ada kwa wanafunzi hawa wa VETA kwa wale wa bweni ni shilingi 120,000 na wale wa kutwa ni shilingi 60,000 ambayo sio thamani halisi ya mafunzo hayo pale, lakini baada ya Serikali kuona umuhimu wa mafunzo haya imeamua kutoa ruzuku.
Kwa hiyo, kwa hivi sasa bado hatujaanza kutoa mikopo. Tunalibeba kama ushauri tuweze kuangalia katika kipindi kijacho kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha kama tunaweza tukatoa mikopo katika maeneo haya. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; lakini swali moja la nyongeza. Kuna hasara gani kwa Serikali yetu au kwa nchi yetu kujiunga na Mkataba wa Budapest ambao upo leo tukisubiri huo wa Umoja wa Mataifa ambao bado na una matatizo makubwa ambao haujakamilika? tujiunge na wa Budapest kusudi ikitokea tatizo hapa kati kati tuwe salama.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ingependa kujiunga na Mikataba ya Kimataifa kama nchi zingine zinavyofanya lakini tunachokiangalia ni kutazama kwa kina huu Mkataba tunapoenda kujiunga nao una tija gani kwa Watanzania. Kwa hasara ambayo inaweza ikapatikana, kwanza kabisa katika Mkataba huu tulitamani kwamba tujiunge lakini Budapest Convention wameongeza itifaki, wanasema additional protocol of disclosure of electronic evidence. Maana yake kwamba inaruhusu mataifa mengine kuingilia mifumo yenu na kupata evidence on real time, hii ni hasara kubwa sana kwa nchi ambazo bado tuko nyuma kiteknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, mkataba huu wakati unaanzishwa umejengwa katika hiyo pin context haukuwa na ushirikishwaji wa mataifa mengine; kwa hiyo ni ngumu sana kama Taifa kwenda kujiunga na Mkataba huu. Lakini tunafanya nini kuhakikisha kwamba hasara kama hizi hatuwezi kuzipata? Ni kweli kabisa kutojiunga nao inawezekana tunapohitaji kupata ushirikiano inapotokea mtu amefanya kosa yupo katika nchi za kwao hatuwezi kupata ushirikiano; na tunafanya nini kama Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaenda kujiunga na Mkataba na Malabo Convention. Mkataba huu umeongelea maudhui ya kuhakikisha kwamba tuwe na electronic transaction act, ambayo tayari Tanzania tunayo, tuwe na cyber security act ambayo Tanzania tunayo, tuwe na personal data protection act, Tanzania tayari tunayo; na sasa tayari tumeishapokea maoni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tukamilishe ili tuweze ku-ratify kama nchi; na huu ni Mkataba ambao umetokana na African Union. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huo sasa, tukishakamilisha kujiunga na Mkataba wa African Union maana yake sasa tutaenda kujiunga na ule mkataba, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, tutajiunga na ule Umoja wa Mataifa. Ambapo maana yake European, African Union wote kwa pamoja tutakuwa tunauwezo wa kupata ushirikiano pale ambapo tunakuwa tunashughulikia makosa ya kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; lakini swali moja la nyongeza. Kuna hasara gani kwa Serikali yetu au kwa nchi yetu kujiunga na Mkataba wa Budapest ambao upo leo tukisubiri huo wa Umoja wa Mataifa ambao bado na una matatizo makubwa ambao haujakamilika? tujiunge na wa Budapest kusudi ikitokea tatizo hapa kati kati tuwe salama.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ingependa kujiunga na Mikataba ya Kimataifa kama nchi zingine zinavyofanya lakini tunachokiangalia ni kutazama kwa kina huu Mkataba tunapoenda kujiunga nao una tija gani kwa Watanzania. Kwa hasara ambayo inaweza ikapatikana, kwanza kabisa katika Mkataba huu tulitamani kwamba tujiunge lakini Budapest Convention wameongeza itifaki, wanasema additional protocol of disclosure of electronic evidence. Maana yake kwamba inaruhusu mataifa mengine kuingilia mifumo yenu na kupata evidence on real time, hii ni hasara kubwa sana kwa nchi ambazo bado tuko nyuma kiteknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, mkataba huu wakati unaanzishwa umejengwa katika hiyo pin context haukuwa na ushirikishwaji wa mataifa mengine; kwa hiyo ni ngumu sana kama Taifa kwenda kujiunga na Mkataba huu. Lakini tunafanya nini kuhakikisha kwamba hasara kama hizi hatuwezi kuzipata? Ni kweli kabisa kutojiunga nao inawezekana tunapohitaji kupata ushirikiano inapotokea mtu amefanya kosa yupo katika nchi za kwao hatuwezi kupata ushirikiano; na tunafanya nini kama Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaenda kujiunga na Mkataba na Malabo Convention. Mkataba huu umeongelea maudhui ya kuhakikisha kwamba tuwe na electronic transaction act, ambayo tayari Tanzania tunayo, tuwe na cyber security act ambayo Tanzania tunayo, tuwe na personal data protection act, Tanzania tayari tunayo; na sasa tayari tumeishapokea maoni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tukamilishe ili tuweze ku-ratify kama nchi; na huu ni Mkataba ambao umetokana na African Union. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huo sasa, tukishakamilisha kujiunga na Mkataba wa African Union maana yake sasa tutaenda kujiunga na ule mkataba, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, tutajiunga na ule Umoja wa Mataifa. Ambapo maana yake European, African Union wote kwa pamoja tutakuwa tunauwezo wa kupata ushirikiano pale ambapo tunakuwa tunashughulikia makosa ya kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali ambayo ni mazuri na nashukuru pia kwamba mradi unaenda vizuri kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa maswali mawili:-
Swali la kwanza ni nini kauli ya Serikali kuhusu bei ya maji maana hata kule ambako miradi imekamilika kuna mahali ambako bei ya maji ni kubwa sana hadi shilingi 5,000 kwa unit ambazo ni lita 1000, kama kule Kyamurairi na sehemu nyingine ambako maeneo mengine ni shilingi 1000 lakini kule ni shilingi 5,000.
Swali la pili, kuna Kata Sita ambazo nako kuna mradi unaosemwa siku nyingi Kata ya Izimbya, Kaitoke, Mugajwale, Ruhunga, Katoro na Kaibanja, ambako Mheshimiwa Naibu Waziri amewahi kufika tukazungumzia jambo hilo na anazifahamu Kata hizo, mradi huo unaanza lini kutekelezwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jasson Rweikiza kama ifuatavyo:-
Awali ya yote ni kweli nilifika na Mheshimiwa Mbunge nakupongeza, tulifanya hii kazi kwa pamoja na tutakuja tena kuona kwamba tunakamilisha miradi hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na bei za maji ninaomba kutoa taarifa ni wiki ya jana tu Mheshimiwa Waziri ametoa bei elekezi kwa miradi yote nchi nzima. Hivyo maeneo ambayo yana bei ambazo kidogo siyo rafiki kwa wananchi kama maeneo yako ya Bukoba Vijijini, hata pale Karatu yote tumeyazingatia na bei elekezi zimetolewa na Mheshimiwa Waziri kwa kuzingatia nguvu inayotumika kusukuma mitambo yetu. Kama ni mafuta, kama ni umeme wa jua kama ni mserereko, kama ni umeme wa TANESCO pamoja na pump za mikono, yote haya Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo na sasa hivi bei zitakwenda kuwa rafiki sana, wiki ijayo kwa maana ya mwaka mpya wa fedha zitaanza kutumika.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na Kata Sita alizozitaja Mheshimiwa Mbunge tumeshirikiana kwa pamoja na tayari usanifu nafahamu unaendelea, kadri tutakavyopata fedha tutaleta Mkandarasi mapema sana ili Kata hizi zote ziweze kupata maji na maeneo haya ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakipata matatizo ya maji tunakuja kuyashughulikia.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na kusema kweli napongeza kwa hatua ambazo zimefikiwa katika mradi huo, tunachosubiri ni utekelezaji hapo mwakani mwanzoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine wa maji pale Kemondo, Mradi wa Maji Kemondo umechukua miaka mitatu, karibia minne bila kukamilika. Kwa nini unachelewa hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza na nipokee pongezi zake, ninakushukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kupokea namna ambavyo taratibu tumeendelea kuzifanya na kwa ushirikiano wako Mheshimiwa Mbunge ninakuhakikishia mradi huu utaenda kuanza mara moja kadri tulivyosema.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa Kemondo umechelewa kwa sababu ya kusubiria pampu ambazo zilikaa muda mrefu pale bandarini kupia michakato mbalimbali ya kiutaratibu, lakini mpaka hivi ninavyoongea tayari zile pampu zimeshachukuliwa, anazo Mkandarasi, kupitia Bunge lako Tukufu naomba nimuagize huyu Mkandarasi mwenye pampu za mradi wa Kemondo mara moja kufika mwisho wa wiki hii lazima pampu hizo ziweze kufika kwenye mradi. (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutuletea Miradi ya Maji Bukoba Vijijini, kwa kweli jitihada zinaonekana lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; miradi ya maji ya Bukoba Vijijini inajengwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA). Je, Wizara ya Maji ina maslahi gani kwa kutaka kuhamisha miradi hii ambayo imekamilika ili iendeshwe na Mamlaka ya Maji ya Bukoba Mjini (BUWASA) kinyume na matakwa ya wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pale Kemondo kuna mradi mkubwa sana wa maji ambao Serikali imejenga kupitia RUWASA hiyo hiyo (Wakala wa Maji Vijijini) wa shilingi bilioni 16 na sasa hivi umekamilika kwa 100% awamu ya kwanza. Ni kwa nini maji hayajaanza kutoka? Ni kweli kwamba kuna figisu za kutaka kuhamishia mradi huu Bukoba Mjini (BUWASA)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa labda niseme hivi, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira na RUWASA kwa upande wa vijijini, vyote viko chini ya Wizara ya Maji. Ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kujikita kwenye utoaji wa huduma bora zaidi pamoja na kuhakikisha kwamba tunatoa maji safi na salama bila kujali kwamba yatatolewa na RUWASA ama yatatolewa na mamlaka yoyote. Lengo ni kwamba, kwanza yawe na bei ambayo haitamuumiza mwananchi; hilo ndilo ambalo tunaliangalia kwa ukubwa wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha kuuchukua mradi mwingine kutoka RUWASA kwenda mamlaka tunaangalia ufanisi, hilo la kwanza. La pili, tunaangalia mahitaji ya wananchi wa eneo husika wanahitaji kuhudumiwa na nani; na la tatu tunaangalia utekelezaji jinsi ambavyo mradi ulianzishwa. Ninaomba kabisa kwamba kwenye hili lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawaletea wananchi huduma iliyo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la Kemondo, ni kweli kabisa nimefika pale Kemondo na nilipofika nilikuta kwamba kulikuwa na mitambo na pump zilikuwa hazijaletwa, nikatoa maelekezo. Tayari sasa hivi pumps zimeshaletwa na kilichobaki tunaongea na wenzetu wa TANESCO. Kuna mita fulani ambayo wanatakiwa kutufungia na baada ya kukamilisha; na mkandarasi wetu alikuwa anatudai pesa Fulani, wiki iliyopita tumemlipa hiyo pesa na anarudi site. Tutahakikisha kwamba mradi huo unakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.