Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Abubakar Damian Asenga (22 total)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI (K.n.y MHE. ABUBAKAR D. ASENGA) Aliuliza: -

Je, ni lini Ujenzi wa Barabara ya Kidatu hadi Ifakara utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshmiwa Abubakar Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kidatu – Ifakara ni sehemu ya Barabara Kuu ya Mikumi - Kidatu - Ifakara - Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye urefu wa jumla ya kilometa 547. Barabara hii ni miongoni mwa barabara muhimu katika Taifa kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Morogoro na mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ya Njombe, Ruvuma na Lindi kupitia Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara kati ya Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa kilometa. 66.9 pamoja na Daraja la Ruaha Mkuu vinajengwa na Mkandarasi M/S Reynolds Construction Company Limited (Nigeria).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii kwa gharama ya Euro 40,441,890.81 takribani sawa na shilingi bilioni 113.13 bila VAT. Mradi ulitegemea kukamilika tangu tarehe 29 Septemba, 2020. Mradi huu umechelewa kukamilika kwa sababu za kimenejimenti kwa upande wa Mkandarasi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kumsimamia Mkandarasi kwa karibu ili akamilishe mradi kama ilivyopangwa. Mradi huu umepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kilombero ili kunusuru miwa ambayo haijavunwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaona kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa sukari nchini ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa sukari ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara. Kwa msingi huo, hoja ya kuongeza uwekezaji katika Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ni ya msingi sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikisimamia utendaji kazi wa Kiwanda hiki cha Sukari cha Kilombero kwa ukaribu kama inavyosimamia kampuni nyingine ambazo Serikali ina hisa chache kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370. Serikali pamoja na Mbia Mwenza (Kilombero Holding Limited) imekuwa kwenye majadiliano ya kina kuhusu kuongeza uzalishaji wa kiwanda hiki kwa kufanya upanuzi wa kiwanda ambapo imekubaliana kupitia gharama za upanuzi wa kiwanda, kufanya upembuzi yakinifu na namna ya ugharamiaji wa mradi. Mara baada ya zoezi hili kukamilika uwekezaji katika kiwanda hiki utafanyika haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvutia wawekezaji hasa katika kutumia pumba za mpunga ambazo hutumika katika uzalishaji wa uyoga hasa katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza baada ya uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru kwanza Mungu kwa kutuweka hai, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini katika nafasi mpya ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji. Ahadi yangu kwake ni kwamba nitatumikia nafasi niliyopelekwa kwa uadilifu, uaminifu na kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ya mwanzo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, nijibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inavutia uwekezaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo ya uwekezaji ya mikoa ili kubainisha fursa za uwekezaji za mikoa husika, kuandaa makongamano ya uwekezaji ya ndani na nje na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Kilombero wanayo fursa kubwa ya kuingia kwenye kilimo cha uyoga kwa kutumia pumba za mpunga kwa kuwa wilaya hiyo ni kati ya maeneo yanayoongoza kwa kilimo cha mpunga nchini. Kwa mfano, Halmashauri ya Mji wa Ifakara inazalisha tani 11,125 za pumba za mpunga kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uyoga una soko kubwa nchini, Serikali imeanza uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uzalishaji wake. Kwa mfano, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) lilianza utafiti na uhamasishaji wa zao la uyoga mwaka 2001 kwa kutumia masalia ya uzalishaji wa kilimo cha viwanda ambapo jumla ya wajasiriamali 1,823 wamefundishwa uzalishaji uyoga ikiwemo uyoga wa dawa aina ya gonagema na shitake kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TIRDO kwa kushirikiana na taasisi za utafiti inaendelea kufanya tafiti zaidi ambapo mwezi Machi, 2021, imeanza utafiti wa kujua uwezo wa vimeng’enya aina tofauti katika kuongeza uzalishaji wa uyoga na ubora wa uyoga unaozalishwa kilishe (yield and nutritive value).
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kiburubutu katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 nchini ukiwemo Mji wa Ifakara ambao utapata maji kupitia chanzo cha Lumemo. Mradi utahudumia jumla ya Kata tisa na vijiji tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kupatikana kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huu zimeshakamilika na unatarajiwa kuanza wakati wowote katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 na ujenzi wa mradi umepangwa kutekelezwa kwa miezi 24.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuanza uzalishaji katika Kiwanda cha Chuma Mang’ula?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini, pamoja na mambo mengine unalenga kufufua na kuendeleza viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mang’ula Mechanical Workshop ni karakana iliyoanzishwa kwa msaada wa Serikali ya China mwaka 1969. Karakana hiyo ilianzishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa vipuri mbalimbali ya mitambo iliyokuwa inatumika wakati wa ujenzi wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA), pamoja na utengenezaji wa vipuri sehemu ya eneo la karakana hiyo ilitumika kujenga kiwanga cha Pre-Fabricated Concrete Manufacturing kwa ajili ya kutengeneza mataruma ya zege kwa maana ya concrete slippers na nguzo za zege.

Mheshimiwa Naibu Spika, karakana ya Mang’ula Mechanical and Machine Tools Company Limited ilirejeshwa Serikalini mwaka 2019 kutokana na mwekezaji wake kushindwa kuendeleza kiwanda hicho kwa mujibu wa mkataba wa mauziano. Kufuatia urejeshwaji huo Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa utaratibu wa kutafuta wawekezaji wapya watakaoviendesha viwanda hivyo kikiwemo kiwanda cha Mang’ula Machine and Mechanical Tools Limited.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2018 ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa Hospitali za Halmashauri nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali 102 na kuanza ujenzi wa hospitali mpya kwenye halmashauri 28 zikiwemo hospitali zilizoahidiwa na viongozi wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni miongoni mwa halmashauri 28 zisizo na Hospitali za Halmashauri, ambayo imetengewa fedha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo matatu ya awali. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE K.n.y. MHE. ABUBAKARI D. ASENGA) aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapima upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Jimbo la Kilombero na maeneo jirani ya Mlima Udzungwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Damian Assenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imefanya utafiti wa awali na kuchora ramani kwenye maeneo yote yaliyoko katika Jimbo la Kilombero katika mfumo wa Quarter Degree Sheet (QDS). Tafiti hizi za awali zinaonesha kuwa kuna uwepo wa madini ya dhahabu na madini ya vito katika Kata ya Chisano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, GST pia ilifanya utafiti wa awali na kuchora ramani ya eneo la Hifadhi ya Milima ya Udzungwa na maeneo jirani. Hata hivyo, utafiti umeonesha kwamba, hakuna taarifa zozote za uwepo wa madini ya thamani katika milima hiyo. Ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Ifakara watapewa fedha za ujenzi wa Soko la Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambao umesuasua kwa muda sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuwa na Soko la Kisasa ili kuboresha mazingira ya wafanyabishara wa Mji wa Ifakara na kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Mji wa Ifakara iliandaa na kuwasilisha Serikali Kuu andiko la mradi wa kimkakati wa ujenzi wa soko hilo kwa gharama ya shilingi bilioni 14.3 ambalo halikukidhi vigezo. Hivyo, Halmashauri ya Mji wa Ifakara inahimizwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha kwenye bajeti yao ili kukamilisha andiko la mradi huo ambalo litawezesha kutafauta fedha za kutekeleza mradi huo.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Vituo vya Polisi vya Tarafa ya Mang'ula na Kidatu vitakarabatiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa Vituo vya Polisi katika Tarafa za Mang'ula na Kidatu. Jengo la Kituo cha Polisi linalotumika Mang'ula ni mali ya Shirika la Reli Tanzania na Zambia -TAZARA, na jengo la Kituo cha Polisi linalotumika Kidatu ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania -JWTZ. Mnamo tarehe 22 Novemba, 2021 Halmashauri ya Mji wa Ifakara ilitoa eneo la ekari nne kwa ajili kujenga Kituo cha Polisi cha Mang'ula na tarehe 23 Januari, 2023 uongozi wa Kata ya Kidatu ulitoa eneo la ekari mbili kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi. Taratibu za upimaji wa maeneo hayo zinaendelea kwa ajili ya kupata hatimiliki ili kuandaa michoro na hatimaye kuomba fedha kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Daraja C.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mamlaka ya Upimaji (Halmashauri ya Mji wa Ifakara) waharakishe upatikanaji wa hatimiliki hizo ili mipango ya ujenzi wa vituo hivyo iweze kuandaliwa, nashukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia Kibajeti Taasisi za Wenza wa Viongozi Wakuu wa nchi ili ziweze kujiendesha na kupata ufadhili?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ta Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakar Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za nchi, taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi zinasajiliwa na kuendeshwa kwa taratibu zinazotumika kusajili na kuendesha taasisi nyingine binafsi na zisizo za Kiserikali. Hadi sasa Serikali haina mwongozo wa kisheria au kikanuni unaoielekeza kutoa usaidizi wa kibajeti kwa taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Kilombero baada ya wanachi kutenga eneo la hekari 30?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ni azma ya Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2203, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilombero eneo lililotengwa kujengwa chuo cha ufundi stadi ni katika Kijiji cha Nakaguru Kata ya Mchombe. Aidha, tayari kiasi cha shilingi million 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali za ujenzi wa chuo hicho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kufufua Kiwanda cha General Tyre na shamba la mpira Kata ya Mwaya-Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kiwanda cha Matairi Arusha, uko kwenye hatua ya kukamilisha taratibu za kuutangaza ifikapo mwezi Oktoba, 2023 ili kuweza kumpata mwekezaji mahiri mwenye mtaji na teknolojia ya kisasa inayohitajika. Mradi huu unatarajiwa kutangazwa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mashamba ya mpira likiwemo shamba la Kilombero, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) imeendelea kuboresha uzalishaji wa mpira kwa kupanda miche mipya, kujenga miundombinu, kununua mashine za kugemea utomvu, uchakataji na vitendea kazi vingine ili kuongeza upatikanaji wa utomvu na mpira mkavu wenye viwango bora, nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa wanashiriki mafunzo ya JKT ya muda mfupi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa linaendesha mafunzo kwa kundi la lazima (compulsory), kundi la kujitolea (voluntary) na kundi maalum (special). Mafunzo ya kundi maalum hutolewa kulingana na mahitaji yanayowasilishwa na taasisi au Wizara husika na huendeshwa kulingana na maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu kundi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika katika kuendesha mafunzo ya makundi maalum ni kwa Wizara au taasisi kutuma maombi Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kisha Jeshi la Kujenga Taifa huelekezwa kuendesha mafunzo hayo, ambapo taasisi ama Wizara husika huyagharamia. Hivyo, endapo kuna uhitaji wa viongozi wa ngazi za wilaya na mikoa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa kundi maalum, basi Wizara au taasisi inayohusika na viongozi hao iwasilishe maombi hayo ili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iweze kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha mradi wa Umwagiliaji wa Kisawasawa – Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya umwagiliaji Kisawasawa ipo katika Kata ya Kisawasawa, Tarafa ya Mang’ula Wilaya ya Kilombero. Skimu hiyo ipo umbali wa kilometa 43 kutoka Mji wa Ifakara kupitia barabara ya Ifakara - Mikumi. Skimu ya Kisawasawa ina eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu ili kupata gharama halisi za uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hiyo.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha Tawi la Chuo Kikuu Huria katika Halmashauri ya Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali haina mkakati wa kuanzisha Tawi la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania katika Halmashauri ya Ifakara. Aidha, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimefungua matawi yake katika Makao Makuu ya Mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Mkoa wa Morogoro ambapo wananchi wa Halmashauri ya Ifakara wanapata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania pia kina vituo vya mitihani kwenye ngazi ya wilaya kwa pale ambapo idadi ya wanachuo ni 50 na kuendelea. Nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa maji mserereko wa Kiburubutu Ifakara utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa maji wa Mserereko wa Kiburubutu ni miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kupitia mradi wa Miji 28 ikiwemo mji wa Ifakara. Ujenzi wa mradi huo utaanza kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, mpango wa kuugawa Mkoa wa Morogoro umefikia wapi hasa baada ya kuonekana kuwa na sifa ya kugawanywa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa huduma za kiutawala, kiuchumi, kijamii kupitia ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa katika maeneo ya utawala yaliyopo ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata na Vijiji, endapo kuna ulazima wa kuanzisha maeneo mapya, Serikali itatoa maelekezo muda muafaka utakapofika.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi VETA katika Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi pamoja na Chuo cha Mkoa wa Songwe. Aidha, Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa wilaya 64 ambazo zinajengewa vyuo vya ufundi stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imeshapeeka kiasi cha shilingi 324,694,243 pamoja na vifaa vya ujenzi ikiwemo nondo na simenti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kilombero ambacho kitatoa mafunzo kwa vijana wa Wilaya ya Kilombero ikiwemo Mji wa Ifakara. Aidha, ujenzi wa chuo hiki upo katika hatua ya ujenzi wa kuta za boma na ufungaji wa linta pamoja na ukamilishaji wa misingi, nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA aliuliza:-

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa barabara ya Kidatu kwenda Ifakara kilometa 67?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa Barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilomita 67 lilifanyika mwaka 2007 kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007. Jumla ya wananchi 142 waliopisha ujenzi wa barabara hii walilipwa fidia ya jumla ya shilingi 2,576,081,789. Kwa wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara hawakustahili fidia kwa mujibu wa sheria. Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-

Je, kati ya mwaka 2021 – 2022 Serikali ilianzisha miradi mingapi mipya ya umwagiliaji ili kukuza kilimo cha mpunga katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kilombero ni miongoni mwa Majimbo ambayo yana maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hii ikijumuisha bonde la Kilombero lenyewe pamoja na skimu ya Msolwa Ujamaa ambayo imefanyiwa ukarabati na kukamilika mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeingia Mkataba na Mshauri Elekezi Saba Engineering PLC kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika bonde la Kilombero ili kujua gharama halisi za kujenga miundombinu ya umwagiliaji kabla ya kuingizwa katika mpango wa ujenzi.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi VETA katika Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi pamoja na Chuo cha Mkoa wa Songwe. Aidha, Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa wilaya 64 ambazo zinajengewa vyuo vya ufundi stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imeshapeeka kiasi cha shilingi 324,694,243 pamoja na vifaa vya ujenzi ikiwemo nondo na simenti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kilombero ambacho kitatoa mafunzo kwa vijana wa Wilaya ya Kilombero ikiwemo Mji wa Ifakara. Aidha, ujenzi wa chuo hiki upo katika hatua ya ujenzi wa kuta za boma na ufungaji wa linta pamoja na ukamilishaji wa misingi, nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, lini Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools kitafunguliwa baada ya kufungwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa katambua umuhimu wa Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools katika uzalishaji wa mashine na vipuri nchini, Serikali imekusudia kukifufua Kiwanda hicho na kuwezesha kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mitambo, kukarabati badhi ya majengo, uhakiki mali (stocktaking) na uthamini mali wa kiwanda (valuation) ambapo thamani ilibainika kuwa shilingi bilioni 9,571,000,000 kulingana na taarifa ya tarehe 21 Machi 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua itakayofuata ni kutafuta Mbia mwenye uwezo wa kifedha na teknolojia inayohitajika kwa ajili ya kufufua kiwanda hiki. Aidha, kutokana na mpango kazi inatarajiwa mwekezaji apatikane mwishoni mwa Mwezi Februari 2025, ukarabati wa majengo na usimikaji mitambo kukamilika mwezi Disemba, 2025 na hatimaye uzalishaji kuanza Januari, 2026, ahsante!