Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Toufiq Salim Turky (8 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kunijalia kufika hapa, lakini pia kumtakia Rehema mzee wangu aliyekwishakutangulia mbele ya haki Mheshimiwa Salim Turky, Mr. White. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue fursa hii nikishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuona ninafaa na kuweza kuwakilisha wananchi wetu wa Jimbo la Mpendae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze na kuunga mkono hoja, kwa kweli Mpango huu ni mpango kazi. Kusema kweli nchi yetu inavyoelekea imetuletea hamasa kubwa mno ndani ya miaka mitano hii. Mheshimiwa Rais wetu kafanya makubwa sana, ile hamasa imekuja mpaka Visiwani. Kwa mara ya kwanza katika historia CCM kushinda kwa asilimia 74 Zanzibar, imeonesha kwa namna gani Awamu ya Tano ilivyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uchumi, nataka kuongelea masuala mawili tu, hatuwezi kuongelea uchumi kama hatuongelei mtaji. Mtaji tukisema inaingia katika masuala ya ajira, lakini muhimu sana namna gani unaweza kuipata ile capital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ajira tunatafuta ajira milioni 8, namna gani tutazipata hizi ajira? Ni kwa kupitia private sector lakini pia watu kuweza kujiajiri wenyewe. Tukitizama mabenki yetu wanawapatia mtaji matajiri zaidi kuliko wanyonge, sasa namna gani wale wanyonge wanaweza kupata mtaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuitazame katika taswira mbili; uchumi wa pande hizi mbili uko tofauti, tukifuata uchumi wa Bara uko tofauti na wa Zanzibar. Zanzibar kitu gani tunaweza tukafanya ambacho kinaweza kusaidia kwa pande zote mbili, kupitia Benki Kuu (Bank of Tanzania), tunaweza tukaongeza wigo wa kuanzisha offshore banking. Hii off shore banking itasaidia vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia visiwa vyote vilivyoendelea duniani, mfano Singapore, Dubai, Hongkong, Mauritius, Panama masuala yote wanayofanya ni offshore banking, wanahakikisha watu wanaleta fedha ndani ya nchi zao. Sasa zikipatikana zile hela ndipo yale mabenki wanakuwa na excess funds za kuweza kuwapatia wajasiriamali wadogowadogo watakuwa na appetite. Sasa kwa kwa nini tusianzishe offshore banking katika kusaidia uchumi wa Zanzibar lakini BoT ikawa ni msimamizi mkuu kupitia Bank of Tanzania branch ya Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu Zanzibar kuendelea katika real estate. Uchumi wa visiwa ni fedha na real estate, hiyo ndiyo ukitizama karibu visiwa vyote vilivyoendelea. Sasa tukitizama katika suala la real estate kuna changamoto moja kubwa nayo ni suala la immigration. Dubai leo ukitaka kununua nyumba zaidi ya milioni 1 Dirham, sawasawa na Dola 270,000 unapatiwa resident permit ya miaka mitatu. Leo kuna nyumba ya Dola 600,000 imejengwa pale na Mzee Bahresa, wako wengine wamejenga hata resident permit ya mwaka mmoja hupati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitizama ule mradi wametumia tayari almost 150 million dollars, lakini hauwezi ku-take off. Miradi ya namna ile iko mingi sana Zanzibar. Zanzibar kuendelea ni suala zima la tourism na real estate, sasa ni namna gani tunaweza kusaidia? Tunaweza kutizama katika wigo huo, namna gani immigration kupitia Zanzibar ikawa na wigo fulani sasa wa kuwawezesha Wazanzibar kule katika uwekezaji wao. Tutaweka cealing, mtu aki-invest dola laki tatu anaweza kupata resident permit, pengine inamruhusu kubakia Zanzibar au akitaka kuja mpaka Bara kuwe na namna fulani ya kuweza kuwekeza watu wasiweze kutumia vibaya ile mianya ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana tufanye hivyo kama kweli tunataka maendeleo yafanyike, hususan kwa uchumi wa Zanzibar. Tukitizama rasilimali zetu sisi zaidi ya uchumi wa blue ambapo tunaongelea bahari ni mdogo mno tofauti na Bara; kuna rasilimali watu, rasilimali nguvu na minerals. Kwa hivyo, naombeni sana tulitizame suala hili na muhimu suala la BoT kwenda offshore na immigration hususan katika masuala ya resident permit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa dakika hizo chache nilizopata. Kusema kweli nilikuwa sipo katika wachangiaji, lakini inabidi tuongee jamani kwenye ukweli. Mnyonge mnyongeni haki yake apewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi kama dunia sasa hivi iko katika changamoto. Sote ni mashahidi kuwa sasa hivi bajeti iko katika constrain, lakini leo mbali baada ya kuisifu Wizara na Serikali ya mama wengi najua kila mmoja kupitia jimboni kwake tuna changamoto nyingi, lakini umepatikana muarobaini wake na muarobaini ni kitu gani? Mheshimiwa Waziri kaongea kama sasa hivi anakuja na EPC Plus Finance. Maana yake nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa leo hata kama bajeti haipo, basi leo tutafute huko nje watu, watakuja. Kuna miradi imewekwa kilometa 900 kwa ajili ya kuleta mkakati wa kusaidia Serikali. Kwa hivyo, niipongeze kwanza Wizara, hususan Waziri na timu yake kwa kuhakikisha wamekuja na wazo zuri zaidi kwa kuhakikisha wanaweza kuzi-finance hizi barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika naomba niongelee suala zima la ATC, ATC jamani karibuni tu nilikuwa na safari ya kibiashara kuelekea Kigoma. Mtu wangu akaniambia ili kufika Kigoma itabidi nimpatie posho ya siku mbili, nimpatie posho ya siku mbili, nimpatie na gari na mafuta kilometa elfu moja na zaidi. Nikamwambia hayo yote unataka bei gani? Akasema milioni tatu na service ya gari? Nikamwambia kwa nini usichukue tiketi ya ndege laki sita ukaenda ukarudi ukamaliza biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ahsante kwa Wizara kwa kuhakikisha leo tunaifungua mikoani. Mikoa tunaifungua kwa kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa juu. Jamani lazima tupige na hesabu, sio kila time tutazame ndege inapata hasara gani, faida gani inapatikana. Tutazame ni biashara gani inapatikana kwa watu kuzunguka kwao na ile mikoa inafunguka vipi kibiashara? Huo ndio uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo nafikiri kuna umuhimu sana wa Wabunge kufanyiwa semina ya kuweza kufahamu hili suala. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, mengine andika.

TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ilibakia dakika moja lakini.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Naomba nitangulize kumshukuru Mwenyezi Subhanahu Wata’ala kwa kutujalia uhai na uzima na kufika siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa juhudi kubwa sana zinazotendeka kupitia Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli dira ya nchi hii inakoelekea na vision iliyokuwepo ndani ya nchi yetu ni ya kupatiwa faraja na fahari kubwa sana siyo ndani ya nchi yetu tu bali ndani ya Bara la Afrika na duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi hii ya kimkakati na nataka niipongeze Serikali hususani katika Mradi wa SGR pamoja na Nyerere. Kupitia miradi hii Tanzania ndani ya Bara hili la Afrika kupitia East Africa tutakuwa kinara. Sasa pamoja Mji wetu huu wa Dodoma leo Mheshimiwa hapa Bibi Mwantumu alikuwa anaongelea kuhusiana na suala la ndege kuja ndani ya capital city yetu hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Sasa hivi ndege inafika shilingi milioni moja mpaka shilingi milioni na nusu kwa sababu ndege zote zinakuwa full. Serikali walitazame suala hili la kuongeza ndege ili sasa Mji huu wa Dodoma uweze kunawiri na uweze kweli kuwa capital city. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akihutubia Bunge letu hapa alituambia katika sababu zinazofanya Deni la Taifa kuongezeka ni kwa sababu sarufi imeshuka thamani. Tujiulize, changamoto hii imeikumba dunia yote, lakini ndani ya Tanzania sababu kuu iliyofanya sarufi yetu kushuka ni kuongezeka kwa import lakini pia kuwepo kwa scarcity ya dola imesababisha scarcity ya dola. Hii scarcity inatokana na kitu gani? Tuna imports ambazo asilimia kubwa ya import zetu ni mafuta na sababu nyingine kwa sababu ya loan repayment zetu zinahitaji forex. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, Mheshimiwa mwenzangu aliyenitangulia, Mheshimiwa Tendega aliaongelea suala zuri tu la CNG. Jamani ilipotokea vita Ukraine mafuta kwetu huku yanapanda, vita vinatokea Israel na Lebanon kwetu sisi vinapanda. Tuna rasilimali zetu Tanzania, hatuna ushawishi wala hamasa wala incentives ya kuongeza masuala ya CNG. CNG gesi tunayo leo tunaelekea kwenye kuzalisha umeme kupitia Nyerere Dam Hydro gesi yetu tutakuwa tunayo kwa wingi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna gani tunatazama hili suala la forex tukiweza ku-save forex tu basi tayari tulishalipa deni kubwa tu la Taifa letu. Kwa nini hatupi kipaumbele suala zima la forex tukasema hapa lazima rasilimali ya nchi yetu tuitumie ili sarufi yetu iwe imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatoka mjasiriamali Kariakoo alikuwa na pesa zake dola 10,000 akaenda zake China akaleta mzigo. Kafika zake Dar es Salaam kalipa kodi anauza bidhaa yake kakopesha kwa wiki mbili, kauza. Mwanzo alikuwa na milioni 25 kawekeza milioni 30 anauza mzigo anasema bwana kapata faida mwenyewe milioni tano, kumi anaenda ku-change ile dola anaambiwa umepata hasara ya milioni mbili, huyo Mtanzania anaelekea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ifike sehemu jamani lazima tuwe na mkakati madhubuti, tumechukua mikopo ambayo ni mizuri kwa sababu ya Taifa letu tumewekeza katika mpango na maendeleo ya nchi yetu, lakini yako mataifa makubwa tu kama Spain, Marekani na duniani kote wana restructure mikopo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumechukua mikopo ambayo tunatakiwa tulipe ndani ya miaka nane hadi 10, kwa nini tusiwarudie tukawaambia mikopo hii tunataka tulipe ndani ya miaka 15? Inawezekana, tukipandisha ule muda automatically ile EMI ya kila muda inapungua. Kwa hiyo, yale mahitaji ya dola yatapungua yataingia kwenye soko letu ndipo tutaweza kui-save forex yetu. Kwa hiyo, naomba sana kupitia Wizara hizi mbili, ya Fedha na Mipango, lazima waje na mkakati maalum wa kuhakikisha kupitia Wizara ya Fedha waje na restructure za loan. Lazima muda wa kulipa hii loan uwe mrefu ili wao wapate pumzi ya kuweza kuhimili kutokulipa dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni lazima tutumie rasilimali zetu. CNG ipo, hamasa ipo, lakini bado Serikali hatujaona kuwapa kipaumbele suala zima la gesi asilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tukiwa tunatembea katika ndege hizi na tukienda safari hizi za mikoani, unaenda sehemu unakuta kwa mbali hakuna nyumba, unapita baada ya mwezi unakuta nyumba mbili, tatu, baada ya miezi sita zinaanza nyumba 10, 20 baada ya mwaka unakuta ni kijiji. Huu mpangilio wa ardhi wa nchi yetu inaonekana bado hatujaupa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna tunavyoendelea tutafika mwisho wa dunia tutasimama hapa itakuwa kilio chetu ni maji, barabara na umeme kwa sababu hatuna mpango wa ardhi, kuna umuhimu sana. Sasa hivi ni lazima ifike sehemu nchi nzima tuwe na mpango wa ardhi. Tujue wapi pa kulima, wapi pa kufuga na wapi kwenye maendeleo ya makazi ya watu kuishi. Haiwezekani leo mtu ajiamulie tu aende porini aweke banda lake, kesho amuite jamaa yake, mjomba wake na shangazi yake, waseme sasa hivi hii ni Kata hatuna maji! Nchi haiendeshwi hivyo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huko Marekani, Uingereza na uende sehemu yoyote iliyoendelea ziko sehemu haziruhusiwi kujengwa nyumba. Ziko sehemu za kujenga makazi na ziko sehemu za kufanyia biashara, lazima kuwe na mpangilio. Kwa hiyo, naiomba Serikali itizame suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujikita sasa katika suala la biashara hususani baina ya Tanzania Visiwani na Tanzania Bara. Wizara ya Fedha kuna changamoto kubwa sana ambayo inafanya Visiwani Zanzibar kutokuwa na advantage ya biashara. Leo hii mfanyabiashara anaponunua bidhaa zake Zanzibar anachukua VAT analipa 15%, anapokuja Bara anatakiwa alipe difference ya three percent, inakuwa 18 percent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina hoteli, nataka ni-claim vitu ninavyonunua Zanzibar ile asilimia ya input ya 15% iweze kunisaidia. Ile haikubali kwenye mifumo yao. Kwa hivyo Sasa mfanyabiashara wa Bara anasema kwa nini ninunue Zanzibar ambapo siwezi ku-claim VAT yangu? Kwa sababu mifumo haioani. Kwa hivyo, namwomba Waziri awaelezee Wizara ya Fedha huko kuhakikisha mifumo yao iendane na ZRA kuhakikisha watu wa Bara waweze ku-claim VAT yao, hilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili katika suala zima hata masuala ya bidhaa, hapa Mheshimiwa Mwantumu pia kaliongelea, suala zima la biashara unapoleta bidhaa zako kutoka Visiwani kuja Bara na Bara kwenda Visiwani. Jamani hakuna easy of doing business kabisa. Unapofanya biashara baina ya Visiwani na Bara ni kama unaenda zako vitani vile. Unajiwekea makombora yote na kadi zote, leo bwana akija huyu niwe na hiki, niwe na hili na niwe na lile maana inakuwa bugudha hata saa nyingine bora usifanye biashara! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba sana kuna umuhimu wa kuwa na kamati maalum ya kupeleka hizo kero, leo kuna kamati maalum za kupeleka kero hapa East Africa Community, kama kuna tatizo baina ya Kenya na Tanzania, ipo, baina ya Rwanda sijui na nani, ipo, kwa nini baina ya Zanzibar haipo na wakati ni nchi moja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nenda TRA hiyo moja, huyu anakwambia hivi, yule vile, huyu lile na huyu lile, haiwezekani! Ifike sehemu lazima kuna sehemu twende. Kuna mambo mengine hayataki hata, kuna tatizo la sheria wala policy, kila kitu kipo. Ni mtu tu na tabia yake siku hiyo kakerwa kaamua na yeye akere kila mtu, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi kuna mifumo ya digitalisation, sasa hivi kuna e-office na kuna kila kitu, hata tunapozungumza committee siyo kama mtu utengeneze jambo lolote kubwa, inatakiwa ile mifumo ioane na kama kuna complains zifanyiwe kazi na siku hizi complains zinaonekana kwa graph tu, ngapi zimechukuliwa na ngapi zimefanyika, hutakiwi ku-address. Huko tunakotaka kuelekea hilo ndiyo Taifa, dunia ndiko inakoelekea katika masuala ya artificial intelligence. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi bado hatu embrace mifumo wala hatutaki kuitumia, bado tunataka Mungu watu. Maana lazima mtu asimame aseme bwana mimi ndiye kibambe, haiwezekani! Leo tuiachie mifumo ifanye kazi, watu wafanye kazi tuende katika easy of doing business tuwajibike. Ndiyo maana katika Sekta ya Elimu nikasema sana, jamani kuna umuhimu sana vizazi vyetu sisi tukiwemo na wajao, kuna umuhimu wa artificial intelligence. Kazi zitakazokuja baadaye siyo kazi za Mungu mtu, siyo kazi ya kuonekana wewe, ni kazi za maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu vijana wetu wawe tayari katika hilo Taifa linalokuja baadaye. Uchumi unaokuja, nilizungumza mara nyingi hapa, tulipoanza dunia hii tuliambiwa landlords ndiyo walikuwa wenye pesa, wakaja industrialists, wakaja watu wenye mifumo (ma-ICT), Sasa hivi tunapoelekea ni artificial intelligence, roboti. Taifa letu limejiwekeza wapi? Katika research and development, bado tuko nyuma sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kupitia Bunge lako hili Tukufu Serikali ijielekeze katika suala zima la artificial intelligence na research and development, kwani Mabara yote yanayoendelea duniani sasa hivi na yaliyotajwa yatakayoendelea duniani yamejiwekeza katika digitalisation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache naomba niunge mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Turky kuna mahali ulitamka sarufi, nadhani ulimaanisha sarafu naomba ufanye marekebishio ili Hansard ikae vizuri.

MHE. TOUFIQ S. TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sarafu (currency), ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan tungali sote salama. Pia tuwatakie rehema waliotutangulia mbele za haki wazee wetu hususan Hayati Rais mpendwa wetu Magufuli.

Mheshimiwa Spika, haijapata kutokea mabadiliko ya Serikali ya namna hii na sisi wananchi na Serikali kwa ujumla, sote tukawa kitu kimoja. Lazima tumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-Waatalah. Pia na Waheshimiwa wengine tukawa tunajiuliza, Hayati Dkt. Magufuli Waziri Mkuu alimtolea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli katika kubarikiwa huku, tumebarikiwa kupata kiongozi aliyekuwa mtumishi mtiifu mno. Katika kubadilika kwa Serikali hii, kiungo kikubwa bado kingalipo. Kwa hiyo, tuendeleeni, ilikuwa Bunge hili hili tukampitisha kwa kura zote kabisa, kwa heshima zote kabisa, kwa hiyo, tuendelee kushikamana na Serikali yetu kuhakikisha uchumi wetu unaendelea kuwa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumwombee sana Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mwenyezi Mungu ampe hekima, busara na maono (maana viongozi huwa wanapata maono) yale ya kuipeleka Tanzania yetu mbele kama waasisi wa nchi hii walivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda sana kuongelea kwa uchache katika suala zima la uwekezaji. Uwekezaji hauwezi kupatikana ndani ya nchi yetu kama elimu hatujaipa kipaumbele. Hivi karibuni nilipata bahati ya kwenda Kenya nikakaa na viongozi wa pale, katika masuala waliyokuwa wanaongelea wakasema Tanzania sisi tunaionea wivu sana, kwa sababu wana rasilimali za kila aina kuliko sisi; lakini sisi tuna rasilimali moja ambayo Afrika nzima hawana, ni rasilimali nguvu watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, literate level ya Kenya ni 93%. Vile vile elimu yao wanasema ni tofauti na elimu ya watu wengi sana. Afrika watu husoma kwa ku-pass, sisi tunasomesha vijana wetu kwa kufahamu. Mara nyingi sana, ndiyo maana utaona Tanzania hapa tuna ma-degree, wengine wana Masters, wengine Ma-professor, lakini inapokuja katika uelewa na katika suala zima la dunia inavyoenda, exposure ni tofauti. Attitude yetu iko mbali. Ndiyo maana katika suala zima la uwekezaji, watu wanatafuta ma-expatriates. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona Wabunge tunavutana sana katika suala la kwa nini tunachukua watu kutoka nje? Hakuna mtu anataka kutoa gharama mara tatu, mara nne, mara tano kuwalipa watu wa nje na wakati Watanzania wapo, lakini bado vijana wetu wako nyuma mno kielimu. Tunafanyaje sasa katika suala hili? Ni lazima turudi tena, tutazame namna gani tunaweza kuwasaidia wanafunzi wetu kuhakikisha wanaendana na matakwa ya dunia ya sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Armania ni Eastern Europe Country, sasa hivi kuanzia Darasa la Sita wanafundisha subject ya coding; masuala ya software. Miradi yote karibu sasa hivi watu wanasema tunataka sisi tuwe na mfumo, lakini mifumo yote inatoka nje ya nchi. Hizo ndio ajira za baadaye. Watu duniani wanakadiria, ndani ya miaka 10 ijayo akili zetu zitakuwa hazifanyi tena kazi, itakuwa ni suala zima la artificial intelligence. Vijana wetu tumewatayarisha vipi kuhakikisha ajira za baadaye hatuzikosi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ajira za mwanzo zilikuwa za viwanda, tunatafuta watu wa kulima. Ajira za pili zikaja kuwa ni masuala mazima ya vibarua kwa ajili ya viwanda. Ajira za tatu zimekuja katika kutengeneza viwanda. Ajira zijazo ni namna gani dunia itaenda ki-ICT only; Artificial intelligence? Vijana wetu tuwatayarisheni katika ajira za baadaye. Hizo milioni nane zitakuwa ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia uzima tukafika katika Bunge hili. Halikadhalika naomba tumwombee dua Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Ghati amepata ajali na yuko mahututi, lakini tumwombe Mungu amjaalie shufaa aweze kurudi katika Bunge hili tuwe nae pamoja. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Turky, ngoja tuelewane vizuri. Taarifa kuhusu wagonjwa na vifo hutolewa na Kiti. Kabla Kiti hakijatoa maelezo usije ukasema hapa mgonjwa yuko mahututi kumbe sio mgonjwa. Kwa hiyo tafadhali, hayo maneno yaondoke, madam Kiti hakijatoa bado Taarifa.

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii tumuombee mzee wetu Hayati Kenneth Kaunda alikuwa katika waasisi wa Bara letu hili la Afrika. Alikuwa pamoja na mzee wetu Mwalimu Nyerere katika kuwakomboa Waafrika wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuja na bajeti ya namna yake. Kwa kweli bajeti hii imewagusa karibu Watanzania wote, tukisema wote pamoja na wa visiwani. Kwa kweli, mwenyewe nimeshaenda kwenye vikao tofauti katika Baraza la Biashara Zanzibar, Baraza la Biashara la Taifa la Bara na katika kilio kikubwa sana kilikuwa ni kilio cha VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Fedha kwa kuona kilio cha Watanzania. Watanzania sisi ni ndugu tuna ushemeji kila mkoa kutokana na kwamba, kuna Wasukuma wako Zanzibar, wako Wagogo Zanzibar, wanakuja kule kutembelea kwetu, wanaona TV, wanaona blender, wakichukua wanalipishwa VAT, wakija zao bara wanalipishwa VAT Bara, lakini hiki kilio cha Watanzania kimeonekana. Hongereni mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika tunafahamu Watanzania wengi waliokuwepo ni wajasirimali na wafanyabiashara wadogo wadogo. Kama hatujabuni miradi tofauti basi Watanzania tutabakia kuwa na vibaka au wakawa waporaji. Leo kwa kupitia punguzo la bodaboda hizi faini peke yake, basi imeleta hamasa ndani ya nchi watu wameweza kufanya kazi zao ipasavyo. Ilikuwa ni juzi wakati inasomwa bajeti nilikuwa na Mheshimiwa Shabiby wakati linaongelewa suala la kupandisha mafuta bei, akasema sasa haya mafuta yameshapandishwa, nikamwambia kwani unadhani zile pesa za TARURA za 500 zingetoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Wizara ya Fedha na Mipango kuja na ubunifu wa kutafuta vyanzo tofauti vya kuleta maendeleo ndani ya Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda sana kuongelea suala zima la forodha ndani ya Afrika Mashariki. Hivi karibuni nilimwona rafiki yangu, Mheshimiwa Bashe akienda zake Namanga kwenda kupigania masuala ya mahindi. Tukajiuliza, kwani hii kazi ya Waziri au ya Wizara? Kulikuwa kuna itifaki ya Forodha ya Afrika Mashariki. Katika itifaki hii ilipaswa kila mwanachama atoe wajumbe watatu. Mjumbe mmoja ni Mwanasheria, anatakiwa Afisa wa Forodha halafu pia anatakiwa na Afisa wa Biashara. Toka 2005 itifaki hii kupitia Ibara ya 24 ya Biashara inatakiwa kuwe na Kamati ya Biashara ambayo inatatua changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya au nzuri wakaongezeka wanachama wawili wengine Burundi na Rwanda, ikabidi ifanyike amendment. Miaka 15 imechukua kubadilisha amendment. Kwa bahati nzuri amendment imekamilika, kinachohitajika sasahivi ni kupitisha katika Mabunge yetu kuhakikisha hii Itifaki ya Forodha inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo naomba sana kupitia Bunge hili la Kumi na Mbili kuweka historia kuwa Itifaki ile ya Forodha tumeweza kuipitisha na tukawa katika mstari wa mbele kidiplomasia kushawishi wanachama wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi kupitia Mabunge yao kuhakikisha ile itifaki inapitishwa. Baada ya hapo tutakuwa na Kamati sasa inayotatua haya masuala ya NTBs. Haiwezekani leo kuona tuna changamoto ya bidhaa fulani mtu anatoka katika Wizara yake anakwenda kutatua, anaenda mipakani na wakati tayari tumeshajipangia inawezekana kuwa na Kamati ya Biashara kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaelekea katika AfCFTA ukanda wa Afrika nzima kuwa na biashara huru wakati East Africa pekee mpaka sasa hivi tunatafuta Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu waende kutatua matatizo haya. Kusema ukweli ile ndoto ya kuwa na Ukanda wa Afrika ya Biashara Huru, basi itakuwa ni ndoto tu. Kwa hivyo, nawaomba sana tuipitishe itifaki hii kuhakikisha Kamati ya Biashara inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nataka niongee kidogo kwenye suala la ufugaji. Tanzania sisi ni wa pili katika kuwa na wanyama (cattle) wengi. Hata hivyo, ukitazama value katika wanyama hao, yetu iko chini mno.

Nimetazama kuna Mabara ya Japan wana steak inaitwa Wagyu, kuna wenzetu kupitia Scotland wanaitwa Angus. Ile nyama kilo moja inaweza kufika mpaka dola 200 sawasawa na ng’ombe mzima tunayeuza sisi. Sasa hebu tuwasaidie wakulima wetu kuhakikisha tunakuwa na prime steak pia. Leo katika hoteli zote za nyota tano nyama zinatoka Afrika Kusini, Argentina, New Zealand na sisi bado nyama zetu haziko katika quality za kuwepo katika five Star properties. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hata siku moja tuwe wa pili katika Bara la Afrika na nyama zitoke nchi nyingine kwa sababu kiwango chake bado hakijafikiwa. Naiomba sana na naishauri Wizara husika kuhakikisha tunaelimisha wafugaji wetu kuweza kuwalea ng’ombe, mbuzi na wanyama wetu kuhakikisha wanakuwa wa kiwango, sio tu kwa kutumika kwenye hoteli zetu lakini kupitia ukanda mzima wa Afrika na dunia kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Sub-hanau Wataallah kutujaalia mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani uwe salama na baraka kwa Taifa zima, pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita tulikuwa tunahojiana sana katika suala la tozo, kila mmoja anapiga kelele tozo lakini sasa hivi toka tumekuja wote wamekaa kimya kwa sababu zile neema za tozo kila kona ya Tanzania zimefika. Hivi tunavyoongelea mpaka mimi kupitia Jimboni kwangu nina Skuli ya Sekondari sasa hivi hapa nina meremera na speed yake kali, kwa hivyo ninaipongeza sana kwa ubunifu na nakiri kuzitumia hizi pesa ipasavyo kwa kila Mtanzania kupata zahanati na skuli kila kona. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka niipongeze Serikali kwa kuja na suala la postcode na suala la sensa, mataifa yaliyoendelea haya masuala mengi pengine watu hawaelewi kwa nini hizi postcode na sensa ina umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, postcode tunapata kujua kama kuna kifaa mtu yeyote unataka kumpelekea unajua njia gani, mtaa gani, nyumba gani, unampelekea unapata ile postcode na kwa kupitia sensa unajua ndani ya nyumba ile kuna watu wangapi, wana mahitaji ya aina gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kupitia hizi mbili ndiyo mataifa mengi yameweza kuendelea. Sasa hoja yangu au mchango wangu uko sehemu moja kwamba tunaweza tukawa na sensa tunaweza tukawa na postcode lakini kama hatuna mfumo wa kuwezesha watu kuitumia hizi postcode tutapata athari kubwa sana. Wenzetu sasa hivi wana database kupitia hii database ndiyo service industries wanapata kodi, leo kila siku tunatafuta tunabuni kodi kwa ajili ya mradi ndiyo maana vifaa bidhaa zinapanda bei, lazima sasa hivi tuondokane kwa mlaji tu tuende katika services.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukitizama kuna mitandao ya booking.com kuna Airbnb, hatuna mfumo wa kuweza direct kupata hizi kodi. Watu wanalipa wanapata pesa zao Serikali inakosa kodi zile kwa kupitia watu kukodishwa.

Hali kadhalika kuna mataifa makubwa ya Google, Facebook wanafanyabiashara na watu wengi sana, sasa hivi tunafanya online purchase lakini kinachofanyika Serikali inakosa kodi zao. Ninachoomba sana tutafute mfumo wa kuhakikisha tunadhibiti kodi zetu kuweza kuzipata na hayo yote haitowezekana kama hatujawekeza katika elimu ya artificially intelligence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongelea Bunge lililopita na safari hii naongea tena, jamani dunia inapoelekea inaenda katika digital hakuna jambo hata moja linalotumika bila artificial intelligence, bado elimu yetu hatujawekeza katika artificial intelligence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Rwanda wameanza kwa kuwa wanataka kuwa ni sehemu ya market ya AI sisi tuko wapi? Leo mpaka unamaliza University somo la coding hatujalianzisha wenzetu kuanzia Darasa la Sita coding inakuwa ni compulsory, lazima watu wafundishwe coding wanajua dunia ijayo haitakuwa na mikono tena itakuwa dunia ya akili lazima tuwekeze elimu yetu katika digitalization ni ombi langu mahsusi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tuna wenzetu walemavu wa kuweza kuzungumza na kusikia, tunafurahi sana kuwa sasa hivi television zote wanakuwa wanaweka sehemu kwa ajili ya watu kufahamu. Lakini ni lazima pia tuanzishe katika madarasa japo zile sign ndogo ndogo za kuweza kuongea nao mtu ana mahitaji yake haiwezekani mtu ana mahitaji leo, mahitaji yake mpaka akufanyishe kwa mkono hivi haipendezi tunawanyanyapaa! Kwa hivyo ninaomba sana kupitia sekta ya elimu tuanzishe at least kuwe na curriculum ya kuwa na masuala ya sign language lakini suala la artificial intelligence siyo tena suala la kulipuuza ni lazima lipewe kipaumbele chake, dunia ndipo inapoelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mhehsimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu subhanahu wa ta’ala kwa kutujalia kufika siku ya leo nikiambatana na familia kwa mara ya kwanza pia nikiwa na mke. Wengi wanasema ametoka Uhindini lakini ni Mturuki, kwa hiyo nimetafuta asili kidogo. Pia naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia mfungo huu wa Ramadhan umefika kwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli katuheshimisha sana ndani ya Tanzania yetu na nje ya Tanzania yetu. Kwa kipindi kifupi mno, na hususan wengi tukiamini akina mama speed zao zinakuwa ndogo, lakini kusema kweli wengi wetu katufunulia macho yetu na kudhihirisha kuwa mama anafanya kazi kubwa mno, katika nyanja zote. Kama tukiongelea kilimo basi kulikuwa kuna mapinduzi ya kilimo nafikiri sote mashahidi; tukijaa katika suala la zahanati, sasa hivi kila Wilaya sasa hivi inaongelea masuala ya zahanati, shule, maji, umeme.

Mhehsimiwa Spika, nilikuwa katika Bunge la Afrika ya kule South Africa, wenzetu wana mgao wa umeme wa masaa sita, hakuna umeme ni bara linasemekana kuwa la kwanza ndani ya Afrika na wapo katika G-20 hawana umeme, South Africa, lakini Tanzania tuna umeme. Sasa ni muhimu sana tukawa watu tunaongelea mengi tu. Najua bado hatujafikia kiwango kikubwa tunachokitaka lakini kazi tunafanya. Kwa hivyo ni muhimu sana linapokuja wakati wa kupongezana ni muhimu kutoa hiyo taarifa. Si umeme tu; lakini nitashangazwa; tulikuwa katika mall fulani kule Johannesburg katika mji mkuu kabisa basi ndani ya lile mall kulikosekana maji. Sidhani kama tumeenda sisi sehemu hapa zetu kuu tukakosa maji, nafikiri tunapaswa pakubwa sana kumpongeza Mama yetu kwa namna kazi namna anavyochapa kazi.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika tumeona katika Bahari, hususan katika maziwa tuna MV Mwanza sahivi, ni meli ya namna yake ambayo imejengwa kwa kuhakikisha katika maziwa yetu masuala ya safari, mizigo yanaenda salama na uchumi unaweza kuimarika. Lakini pia mwenzangu hapa alikuwepo Bw. Tabasamu akaniambia daraja lake la Kigongo limeshakamilika, limebakia nguzo tatu tu na mkandarasi ashalipwa kila kila kitu. Kwa hivyo hapo tunatakiwa tumpongeze mno.

Mheshimiwa Spika, na mimi katika hoja hii ya kumchangia Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nimpongeze sana kwa hotuba yake ya jana. Amegusa sehemu zote, nafikiri Watanzania tuliosikiliza imeigusa kila mwana Tanzania; na tumeona namna gani Serikali ya Mama na hususan kupitia Mhehsimiwa Waziri Mkuu, namna walivyojipanga kuhakikisha umasikini unazidi kupungua na watu wanapata faraja ndani ya Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii nilitaka kuchangia hoja moja tu, na mara nyingi napenda kuichangia hiyo kwa sababu watu wameona kama ipo mbali sana lakini hili suala haliko mbali bali lishafika.

Mheshimiwa Spika, wakati wa zamani uchumi ulivyoanza wakulima walikuwa wanatumia mikono. Zilipokuja mashine wengi wao wakaona kazi inaanza kupungua zinaenda kwenye mashime sasa sisi hatutafanya kazi, ajira. Ikaja wakati sasa wakaona kumbe sio kwamba tutapungukiwa lakini ile work force ikahama ikaenda katika industrialization; kwenye viwanda, kwa kuwasaidia karakana zile mashime ziweze kujengwa. Ikaja wakati wa 80 dunia ikapatwa na janga kubwa, ajira zikashuka kwa sababu yaliingia masuala ya kompyuta na watu wengi sana wakakosa zile ajira kwa sababu watu walikuwa wameshazoea ma-typewriter kuandika barua na nini yote yakachukuliwa katika work force ikaenda katika kompyuta, watu wakaona kazi zitakosekana. Ni kweli zilikosekana zikachukua muda, lakini baada ya hapo watu wakapata kazi na dunia ikaendelea.

Mheshimiwa Spika, nimesoma majarida mbalimbali na imefanyiwa tathmini; kwamba, miaka mitano mpaka kumi ijayo takriban robo ya Europe na Marekani, robo ya work force itakuja kuondoka, inaondoka wapi? Kuna kitu kinaitwa Artificial Intelligence; ambapo kuna wahariri, waandishi wa habari humo ma-journalist waliozoea kuandika vitabu majalada, matoleo mabalimbali na newspaper; hata watu wetu wa hansard hizo kazi zitaenda kwenye a high; ni mfumo, zinaenda kwenye mfumo watu hawahitajiki tena.

Mheshimiwa Spika, kuna kazi za utawala za kupeleka barua sijui za administrative work; zote zile zitapungua. Kazi za sheria, kuandika sijui mabarua ya kupeleka kisheria, kuandika zile code kila kitu nyingi zitapungua; hali kadhalika katika masuala ya ujenzi, mawasiliano na maitnaince. Hili sio kama litakuja tayari limeanza.

Mheshimiwa Spika, jana, kwa bahati, kuna App niliisoma; na naombeni Waheshimiwa Wabunge na nyie mkipata nafasi mnaweza mkai-download inaitwa Chat-GPT. Hii Chat-GPT umei-download unamwambia nataka nimuandikie barua Waziri Mkuu nimuelezee nina changamoto a b c basi, inaandika barua, tena unamwambia niandikie kwa namna ya shakespeare inakuandikia kila kitu na tena kwa namna ya literature unayoitaka wewe. Maana yake nini kama mtu ulikuwa hujui kuandika, hujasoma sijui hujafanya nini, yote inafanya yenyewe. Sasa tujiulize wale watu waliokuwa wanafanya watapata wapi kazi hizo? Hata hivyo, sasa tunatakiwa na sisi tuwe na think tank yetu ambayo sasa humu ndani na naomba tuishauri Serikali kuwa na think tank ambayo itaweza kutathmini na sisi tutaathirika vipi katika hili wimbi jipya lililokuja duniani la artificial intelligence. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mdogo ni suala zima la madereva, kama tunavyokumbuka zamani madereva walikuwa unaenda zako sehemu mbalimbali wanakusimamisha njia, lakini sasa hivi una bolt, bolt ile imesababisha mtu yeyote anaweza kujiajiri, lakini wale madereva wa zamani sasa hivi wamepungukiwa na kazi kwa sababu, sasa hivi hutaki kujua akili yako. Kwa hivyo, naishauri Serikali kuwa na kamati, la kwanza kuwa na semina ya Wabunge humu ndani tufahamu nini artificial intelligence, ili tuweze kuwasaidia wenzetu wengi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mwaka uliopita Rais wa African Development Bank alihutubia akasema kuwa, katika jambo rasilimali ambayo itakuja kuwa ghali basi itakuwa ni chakula. Tumeshafika asilimia, sasa hivi nimetizama dunia inapoelekea inaenda katika exhaustion na ukitizama watu tumeshazidi Milioni Saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kupitia kwa Mama yetu Rais mpendwa kuona uono huo na kuja na mapinduzi makubwa sana ya kilimo Tanzania. Ukitizama katika historia ya Tanzania basi hii tumeupiga tena tumeupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kumshukuru sana Waziri husika kuja na taswira tofauti, kuna kitu kinaitwa agriculture na agro-business. Agriculture tunaenda katika tamaduni, lakini safari hii tukasema hatutaki kilimo cha utamaduni, tunataka kilimo cha biashara. Kwa hivyo, nampongeza sana Waziri Bashe kuja na mfumo mpya. Pia lazima nimshukuru Bwana Mzee wa Mayele kuhakikisha katenga bajeti. Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu pale akasema aah! safari hii nitachumba huku, nitachumba huku, uono wa Mama hii agro-business na tunapoelekea dunia inayohitajika kilimo kuweza kupatikana kwa hivyo, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani jana nilipata fursa ya kuonana na wanafunzi kutoka UDOM, wanamaliza research zao na tulikuwa tunabadilishana mawazo tu, wakawa wanazungumza kuna mmoja kamaliza uchumi, ananiambia Mheshimiwa tunamaliza sisi uchumi tayari, sasa a tunataka kuja huko utusaidie tutafanikiwa vipi? Tutapata fursa gani katika biashara au katika ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikamwambia sasa wewe umekuwa mchumi, sisi kawaida yetu kule watu wenzetu wanapomaliza vyuo wanakuwa wameshakuwa wachumi wanakuja na maarifa. Sasa hebu nikuulize mwenzangu, wewe sasa hivi umeshakuwa mchumi, unaona katika hali halisi sasa hivi ya nchi yetu, kitu gani kinaweza kutusaidia sisi katika nchi yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kanambia mambo mengi tu. Nikamwambia mambo mengi gani, niambie? Akaniambia unajua kama sera zetu. Sera kama zipi? Akasema unajua kuna sera nyingine haziko sawa, lakini ukienda huku, vipi, tunaweza tukaziweka sawa. Kama zipi? Akawa hakamati sehemu. Nikamwambia inawezekana tuambie pengine tuambie Fiscal Policy, Investment Policy au Policy ya aina gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukitizama akawa ameganda. Baada ya hapo tukaitizama sasa tulilokuwa tunaongelea suala zima la hapa tunapozungumzia kabla ya hapa katika michango yangu ya kabla kuwa, wanafunzi wengi tunamaliza University, lakini wanakuwa hawana mchango katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mama juzi karibuni kati hapa alikuja Zanzibar katika organization ya MIF, (Mwanamke Initiative Foundation), akawa anaongelea suala zima la kubadilisha curriculum. Namshukuru sana Mama kwa kuja na uono wa kuona sasa elimu yetu nafikiri umefika wakati wa kuja na mageuzi na hilo ni muhimu sana kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa na vijana wanamaliza, wenzetu mataifa mengine wanatumia fursa hizi wanakuwa wanakaa na makampuni. Wanaenda katika Universities wanafanya interview kwa sababu tunajua umuhimu wao kuwa sasahivi tunawahitaji wao wanakuja na maarifa mapya, lakini wanafunzi wetu bado wanategemea maarifa yaleyale yaliyopita na siyo maarifa mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia huko wakaja pia wakaniambia kabisa sisi bwana Walimu wetu wanatuambia, ukitaka kufaulu au kuendelea kimaisha lazima unatakiwa mtu akukamate mkono uwe nae hivi ndiyo maisha utapiga, lakini siyo kwa elimu yetu tuliyo nayo. Hao ni Maprofesa wetu wanaongea lugha hizo, sasa hawa wanafunzi wetu watakuwa na dira gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani watu wengi sana pengine au mtakuwa mnajua, hamfahamu, lakini tajiri wa dunia wa sasa hivi anaitwa Elon Mask, watu wengi labda wanaweza wakafikiri kuwa huyu ni Mmarekani, lakini huyu ni mwana Afrika, kazaliwa Pretoria, South Africa. Kuna wakati mmoja akaulizwa kwa nini ulitoka zako Afrika unaendazako Marekani? Akasema unanua mimi nilitengeneza instrument ya kulipa inaitwa PayPal, alianzisha yeye na mwenzake, lakini baada ya hapo wakaiuza, baada ya hapo akaenda zake Marakeni. Akaulizwa kwa nini ulienda zako Marekani? Akasema nimeona Afrika hakuna mtu anaewekeza katika ndoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Afrika tunabonyezwa tunabakia huku, nimekuja Marekani nikasema mimi nataka nianzishe gari lisilokuwa na dereva, nitaanzisha battery ambayo haitaki mafuta haitaki chochote itakuwa inafanya kazi. Afrika hakuna mtu kanisikiliza. Nimeenda Marekani watu wamenisikiliza na leo ile kampuni inaitwa Tesla ni namba moja duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukitizama jamani duniani kwetu huku Afrika, imekuwa ni jambo la ajabu sana kwamba hatutaki kuwekeza katika suala zima la ndoto ya research. Katika Bara linaloongoza sasa hivi kwa kukua katika masuala ya teknolojia ni South Korea. Waliulizwa ilikuwaje wewe ghafla umekua kwa haraka katika Bara hili la Asia? Akasema tumetenga asilimia Nne ya GDP yetu katika research and development, na leo wao ni viongozi katika masuala yote ya electronics. Samsung sasa hivi anaendana pamoja na iPhone na kampuni nyingine kubwa, Hyundai, ana kampuni nyingi sana, anashindana na Japan. Leo tujiulize tumewekeza kiwango gani katika research and development? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo watu wanafanya research, Oxford wamefanya research, Universities zinafanya research, Imetoka AstraZeneca ndiyo imekuwa vaccine ya COVID-19. Tujiulize Universities zetu research zao zinasaidia nini katika uchumi wa Taifa? Jibu litakuwa hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Serikali ilitazame suala zima la research and development kwani kama tunataka tuendelee katika dunia hiyo, tusibakie katika ndoto tu, basi lazima tuende na wenzetu katika masuala ya research and development. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, jana walikuja wenye viwanda wanaotengeneza biscuit, biscuit viwanda wazalendo wamezidishiwa 500 shillings kwa kilo as excise duty. Wanasema sisi tuna viwanda sote tunafahamu sasa hivi mfumuko wa bei viwanda vinatumia unga, unga wenyewe kupatikana taabu, bei zimepanda, leo tunakuja tunaambiwa tulipe 500 Shillings per kilo as excise duty na wakati watu wa importation hali iko vilevile, sasa hapa tutaishi vipi? Sasa nilikuwa naomba sana kupitia Waziri, Wizara ya Fedha, walitazame hili suala na nyakati zilivyo. Nafahamu tunatafuta mapato ya tofauti katika sehemu na nyanja tofauti, lakini hii biscuit tuitizame wanakula akina nani? Ni watoto wetu wa shule kwenye vishughuli hivyo vya madarasani na sehemu nyingine, kwa hivyo, nilikuwa naomba sana katika sehemu hizi….

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Turky, mengine andika.

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga hoja kwa asilimia zote. (Makofi)