Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Toufiq Salim Turky (10 total)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani juu ya mfumuko wa bei unaoendelea nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2021/2022, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 4.0 ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021. Pamoja na ongezeko hili, mfumuko wa bei umeendelea kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja na upo ndani ya lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki la asilimia 8.0 na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika la kati ya asilimia 3.0 hadi 7.0.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ikiwemo: kuimarisha sekta za uzalisha ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa unaoendana na mahitaji; kutoa ruzuku kwa ajili ya kupunguza bei ya nishati ya mafuta kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa mwezi ambapo shilingi bilioni 500 zimetengwa; kutoa ruzuku ya pembejeo za mbegu na mbolea na kutoa unafuu wa kodi katika uagizaji wa baadhi ya bidhaa muhimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua nyingine katika suala hili ikiwemo: kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu; kuanzisha mfuko wa kuhimili ukali wa bei za mafuta baada ya bei za mafuta kutulia katika soko la dunia; kuanzisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati na kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja. Ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuiwezesha TASAC iweze kuhudumia meli nyingi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuiwezesha TASAC kuhudumia meli nyingi, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi wa ukaguzi wa meli kutoka watumishi 23 hadi watumishi 34. Watumishi walioongezwa wamepelekwa mikoa yote yenye kuungana na bahari na maziwa. Aidha, katika kuboresha uwezo wa wakaguzi, TASAC imepata mkaguzi wa michoro na ujengaji wa meli (naval architect) na imepeleka mkaguzi mmoja kwenda kusomea uchoraji na ujengaji wa meli nchini Uingereza.

Mheshimiwa Spika, TASAC pia imeingia makubaliano na Chuo cha International Maritime Safety, Security and Environment Academy kilichopo Nchini Italia ili kupatiwa mafunzo ya ukaguzi kwa meli za ndani na meli za nje (Flag State Inspection and Port State Inspection). Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kusaidia makampuni ya wazawa yenye mikopo katika taasisi za fedha kutokana na athari za UVIKO-19?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taofiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza hatua za kiutawala na kibajeti kwa kuwa athari zilizojitokeza za UVIKO-19 zilitokana na kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika nchi washirika wa kibiashara ikilinganishwa na soko la ndani. Aidha, uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuwa shughuli zote za kibiashara hapa nchini ziliendelea kama kawaida.

Mheshimiwa Spika, hatua za kiutawala na kibajeti zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na: -

i. Kuiagiza benki na taasisi za fedha kutoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo kwa kuongeza muda wa urejeshwaji wa mikopo.

ii. Kushirikisha sekta binafsi kupitia zabuni za watoa huduma na wakandarasi katika utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Athari za UVIKO-19 kwa lengo la kuiwezesha kutengeneza faida na kurejesha mikopo katika benki na taasisi za fedha.

iii. Kutoa kipaumbele kwa malipo ya malimbikizo ya madeni, madai na marejesho ya kodi yaliyohakikiwa ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi; na

iv. Kutoa unafuu wa kikodi, ikiwemo kodi ya kuendeleza ufundi stadi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia nne na kupandisha kiwango cha chini cha idadi ya waajiriwa wanaostahili kulipiwa kodi kutoka asilimia nne hadi 10 ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa waajiri na hivyo kuwezesha marejesho ya mikopo kwenye benki na taasisi za fedha.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE K.n.y MHE. TOUFIQ S. TURKY aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Saratani nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio na televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama Facebook, Instagram na pia televisheni sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya ugonjwa wa saratani kama ifuatavyo: -

(i) Kuandaa kampeni mbalimbali za uelimishaji wa jamii na uchunguzi wa awali wa saratani nchini ikiwemo huduma Mkoba.

(ii) Kuandaa mtaala wa mafunzo wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa watoa huduma wa ngazi za msingi ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu kwa jamii.

(iii) Kuandaa vipindi mbalimbali na machapisho ya utoaji wa elimu ya afya dhidi ya magonjwa yasisyo ya kuambukiza ikiwemo saratani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga majengo ya viwanda kuwapangishia wawekezaji wazawa ili kuongeza idadi kwani gharama za kuanzisha kiwanda ziko juu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Sera za Serikali katika uwekezaji ni kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maendeleo ya viwanda. Serikali ina jukumu la msingi la kutwaa, kupima na kupanga matumizi ya ardhi, wakati sekta binafsi hukaribishwa na kuhamasishwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya viwanda. Utaratibu huu umeshaanza kuzaa matunda ambapo hadi kufikia Desemba jumla ya kongani kubwa tatu za viwanda zimejengwa kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti matumizi mabaya ya Akili Mnemba, kutumia Akili Mnemba kuchangia ukuaji wa uchumi nchini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya akili mnemba yameendelea kuongezeka siku hadi siku hapa nchini katika kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya akili mnemba, Serikali imechukua jitihada za kutosha kujenga uwezo wa wataalam na kuandaa miongozo ya kisera na kisheria ambayo italinda na kuchochea matumizi sahihi na salama ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili mnemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tayari Serikali imetoa ufadhiri wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watumishi wa umma 500 kwenye maeneo ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo eneo la matumizi ya akili mnemba. Kati ya watumishi 500, watumishi 20 tayari wameanza masomo ya kozi ya muda mrefu na nafasi 480 zilizobaki tayari Serikali imetangaza nafasi hizo na mchakato wa kupokea maombi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeanza taratibu za ujenzi wa chuo mahiri cha TEHAMA kitakachojengwa Nala Dodoma kwa lengo la kuzalisha wataalam watakokidhi mahitaji yaliyopo kwa sasa ikiwemo hitaji la akili mnemba. Ujenzi wa chuo hiki unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya ubunifu vinane kwenye maeneo ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya, Arusha, Lindi pamoja na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Wizara imeboresha sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 kwa kuandaa rasmu mpya ya sera ya mwaka 2024 ambayo itajumuisha maeneo ya akili mnemba. Sambamba na hilo Wizara imekamilisha mkakati wa miaka 10 ya uchumi wa kidigiti unaoainisha maeneo muhimu ya matumizi ya akili mnemba katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidigitali. (Makofi)
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga majengo ya viwanda kuwapangishia wawekezaji wazawa ili kuongeza idadi kwani gharama za kuanzisha kiwanda ziko juu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Sera za Serikali katika uwekezaji ni kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maendeleo ya viwanda. Serikali ina jukumu la msingi la kutwaa, kupima na kupanga matumizi ya ardhi, wakati sekta binafsi hukaribishwa na kuhamasishwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya viwanda. Utaratibu huu umeshaanza kuzaa matunda ambapo hadi kufikia Desemba jumla ya kongani kubwa tatu za viwanda zimejengwa kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -

Je, upi mpango wa kuhakikisha viwanda vya kuchinja, kuchana na kusindika nyama vinavyokidhi vigezo vya kusafirisha nje ya nchi vinajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchinja, kuchakata na kusindika mifugo na mazao yake vinavyokidhi vigezo vya kusafirisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji wa viwanda kupitia eneo maalumu la uwekezaji (EPZ) kwa ajili ya soko la nje ya nchi ambapo wawekezaji wanapata msamaha wa kodi ya mapato, kodi ya mitambo na vifaa vya kuchakata na kusindika nyama. Pia, Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vya kuchakata nyama kwa wadau wanaoomba msamaha huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jitihada hizi za Serikali, viwanda vyenye viwango na ithibati ya kimataifa ya kusafirisha nyama nje ya nchi vimeongezeka kutoka viwanda viwili mwaka 2018/2019 hadi kufikia viwanda sita mwaka 2023/2024.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Watanzania wanashiriki Kongamano la Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji mwaka 2027?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia) litakalofanyika mwaka 2027. Serikali imejipanga kwa njia mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu pamoja na kunufaika na Kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati ya Maandalizi ya Kitaifa ambayo inajumuisha wajumbe kutoka Serikalini na sekta binafsi kwa lengo la kuratibu na kufanya maandalizi ya kutosha ili kufanikisha kongamano hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine inajumuisha uhamasishaji wa wananchi katika ufugaji, uzingatiaji ubora na kufungua masoko mapya ya mazao ya nyuki duniani. Serikali pia kwa kushirikiana na sekta binafsi imekuwa ikiandaa maonesho kama hamasa ya maandalizi. Miongoni mwa maonesho yaliyofanyika ni pamoja na siku ya nyuki duniani iliyofanyika tarehe 17 - 20 Mei, 2024 na Maonesho ya Kitaifa ya Asali Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 19 hadi 22 Juni, 2024.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika kukabiliana na ukuaji wa makazi yasiyopangwa, imeendelea kuchukua hatua mbalilmbali ambazo ni pamoja na kuendelea kuandaa Mipango Kabambe (Masterplan) yenye dira ya kusimamia ukuaji wa miji. Aidha, Wizara imeanzisha miradi na programu mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi hapa nchini.