Contributions by Hon. Jerry William Silaa (28 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa Bungeni akifungua Bunge letu hili la Kumi na Mbili.
Kwanza na mimi kwa sababu ni mara ya kwanza, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa mimi kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge lako hili tukufu. (Makofi)
La pili, nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi, chama ambacho nimekitumikia kwa zaidi ya nusu ya uhai wangu, kwa kunipa fursa, namshukuru sana Mwenyekiti, navishukuru vikao vya uteuzi na wanachama wenzangu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuungana na wenzangu kuunga mkono hoja, lakini vilevile naomba sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba hii iliyobeba dira na maelekeo ya nchi yetu kwa miaka mitano. Hotuba hii ukiisoma na ile ya Bunge la Kumi na Moja, ukisoma utekelezaji wa Ilani, ukisoma machapisho mbalimbali ya taarifa ya uchumi, utaona jinsi gani Rais wetu amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo ya uchumi, uchumi wa nchi yetu umekua, Pato la Taifa limekuwa, mfumuko wa bei umekuwa uko katika hali nzuri, haujazidi asilimia 4.4, akiba ya fedha za kigeni kwa mara ya kwanza iko juu na inaendelea kuongezeka, thamani ya shilingi imeimarika sana, pongezi kubwa kwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika huduma za jamii, kazi kubwa imefanyika, vituo vya afya, zahanati zimejengwa nchi nzima na tumeona kwenye hotuba hii tunayoijadili.
Mheshimiwa Spika, lakini labda kwa kifupi sana ni kuomba Bunge lako tukufu kwamba tuna kazi kubwa baada ya kumpongeza Rais kumsaidia ili malengo aliyoyaweka kwenye miaka hii mitano yatimie na katika kumsaidia wote tuna wajibu wa kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wa kwanza ni wasaidizi wake, na bahati nzuri tunaye Waziri Mkuu mchapakazi, mpenda watu, anafikika na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa ni mashahidi. Lakini wako wasaidizi wake wengine, watendaji wa Serikali nao wanafanya kazi nzuri, tumeanza vizuri. Sisi kule Dar es Salaam katika Jimbo langu la Ukonga, Mkurugenzi wetu Jumanne Shauri na watendaji wenzake wanatupa ushirikiano. Ingawa hatuwezi kuacaha kusema wako watendaji ambao inabidi wabadilike kuendana na kasi ya Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, binafsi sina taabu na wewe na ninaamini Wabunge wenzangu hawana shida na wewe, tunafahamu kasi yako. Tumeona juzi hapa Mawaziri walivyokuwa wanajibu maswali ukisimamia Serikali kutoa majibu yanayoendana na shida za wananchi. Niwaombe Wabunge wenzangu, sisi tuna kazi kubwa ya kusaidia Mheshimiwa Rais kufikia malengo haya ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge hawa wamefanya kazi kubwa ya kampeni. Ukiingia hapa asubuhi Wabunge wengi wakiweka sura zao zile mashine zinakataa, siyo kwamba mashine ni mbovu ila sura walizokuja nazo hapa Novemba siyo sura walizonazo leo. (Makofi/Kicheko)
Tumefanya kazi kubwa, Waheshimiwa Wabunge wengine hapa wameosha vyombo, wengine wamepaka rangi kucha, tunayoyasema hapa ndiyo reflection ya matatizo ya wananchi wetu kule tunakotoka, tunaomba tusikilizwe na Waheshimiwa Wabunge, niwaombe tuseme, na wasiposikia tuwafokee. Tufoke kwa niaba ya wananchi tunaowawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi niliwahi kuwa mmoja wa watu tuliokuwa tunaishauri Serikali kuanzisha TARURA. TARURA imekuja kuondoa matatizo ya urasimu ule wa kihalmashauri wa ujenzi wa barabara, ilikuja kuleta tija kwenye utendaji wa kihandisi, lakini matokeo yake, tulianza vizuri na mameneja wa TARURA wa wilaya, akawa kuna coordinator wa mkoa, leo kumetengenezwa Meneja wa Mkoa, Mhandisi wa TARURA yule Meneja wa Wilaya amegeuka kuwa karani. Hana fedha, hatafuti zabuni, hamlipi mkandarasi, nimshukuru Mheshimiwa Jafo ameanza kulifanyia kazi. (Makofi)
Tulileta jambo lile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jerry Silaa.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano na wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali,k hotuba ya Waziri ameonesha kazi kubwa iliyofanyika kwa miaka mitano. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma rasimu hii ya Mpango wa Miaka Mitano, naomba kuchangia kwenye Sura ya Tano; 5.4.10 ukurasa wa 102 kwenye miundombinu ya barabara. Kwenye miaka mitano iliyopita kazi kubwa sana imefanyika kwenye miundombinu ya barabara. Nchi nzima barabara zimejengwa, madaraja yamejengwa na sisi wa Dar es Salaam tumeona ujenzi mkubwa wa miundombinu kwenye Daraja la Mfugale, Ubungo interchange na interchange zingine zinaendelea kujengwa pale Chang’ombe na ujenzi unakaribia kuanza pale Morocco na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Rasimu hii ya Mpango inaonesha jinsi gani Serikali imejipanga kwa miaka mitano hii inayokuja kukamilisha ujenzi wa barabara za lami lakini vilevile kuondoa msongamano wa magari katika majiji. Mimi naamini Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba unapoongelea mafanikio haya makubwa ya miudnombinu mikubwa ya barabara lazima uoanishe na barabara za ndani ambazo ndiyo zinamhudumia mwananchi katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia barabara hizi za mijini na vijijini, unaizungumzia TARURA. Naomba sana kuishauri Serikali kwamba lazima kwenye mpango huu kuwe na mipango inayotekelezeka ya kuisaidia TARURA iweze kutatua changamoto ya miundombinu kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wakazi wa Jimbo la Ukonga tunamshukuru Rais, ile foleni ya TAZARA pale haipo tena. Hata hivyo, leo wakazi wangu akiwemo Mheshimiwa Waitara, akishavuka TAZARA kutoka pale Banana kuitafuta Kivule ama Kitunda kuna kazi kubwa sana. Ukienda TARURA mfumo mbovu lakini na fedha hazitoshi. Leo Dkt. Ndumbaro na wakazi wenzake wa Majohe atavuka vizuri TAZARA lakini nyumbani hapafikiki. Simu zetu hizi ukiona simu yoyote inatoka maeneo hayo unaanza kuomba dua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi yako mambo mawili ambayo Serikali ikijipanga vizuri itafikia malengo haya yaliyowekwa kwenye Rasimu ya Mpango. La kwanza, ni muundo wa TARURA. Tulianza vizuri, tulikuwa na Regional Coordinator na na Meneja wa Wilaya. Kazi ya Meneja wa Wilaya ilikuwa ni kutekeleza miradi ya barabara kule kwenye Wilaya na Majimbo yetu. Hata hivyo, mfumo umebadilika, tumemgeuza yule Regional Coordinator amekuwa Regional Manager na yule Manager wa Wilaya sasa hata ile kazi aliyokuwa anafanya ya kulipa wakandarasi wanaofanya kazi kwenye maeneo yake imehamishiwa mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kumpata mkandarasi wa kufanya kazi Nachingwea anatafutwa Lindi Mjini, mazingira haya ni tofauti sana. Huwezi ukampata mtu kufanya kazi Ngara kwa kumtafutia pale Bukoba Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri ameliona hili kwenye ziara zake, ameahidi kuanza kulifanyia kazi na mimi naomba kuishauri Serikali. Ili Mpango huu uweze kutekelezeka lazima tuwe na muundo wa uhakika wa TARURA. Yule Meneja wa Wilaya awezeshwe, aweze kupata wakandarasi, fedha zifike, aweze kusimamia miradi yake na aepuke kuwa karani wa kutujibu sisi maswali yetu Waheshimiwa Wabunge ambayo hana utendaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakii la pili, ni fedha. Ipo dhana na naendelea kuliomba Bunge lako na Serikali ijenge dhana ya kusikiliza michango ya Wabunge kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hawa wanayoyasema hapa siyo mawazo yao ni mawazo ya wananchi wanaowaongoza. Ipo dhana kwamba ukiongeza tozo ya barabara kwa mfano, leo Bunge likashauri kuongeza tozo ya barabara za mjini na vijijini kwenye mafuta, iko dhana kwamba gharama ya usafirishaji itaongeza. Leo kwa miundombinu isiyopitika kwenye maeneo yote ya pembezoni ya mijini na vijijini ya nchi yetu gharama za usafirishaji ziko juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mwananchi wa kule Majohe Bomba Mbili kuitafuta Mombasa analipa nauli Sh.700 mpaka Sh.1,000. Naamini barabara ya uhakika ingejengwa leo kungekuwa na daladala zinatoka kuanzia Bomba Mbili mpaka Kariakoo na gharama ya usafirishaji itashuka badala ya kuongezeka kwa kuongeza tozo kwenye mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapokuja ku-wind up Mpango na wewe mwenyewe umesema kwamba Mpango huu ni Rasimu, basi mawazo haya tunayoyatoa yaweze kuchukuliwa kwa uzito na yahusishwe kwenye Mpango huu wa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi ya TASAC, miradi ya DMDP Phase II, kule kwetu ni kizungumkuti, inasemekana imekwama kwenye maamuzi kwenye meza za watendaji wa Serikali lakini matatizo kule chini ni makubwa sana. Ni vyema tunavyotengeneza Mpango ukaongeza na kasi ya utendaji kwa watendaji wetu hasa kwenye miradi hii inayowagusa wananchi wa hali ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika dhana hii hii ya kusikilizwa na leo wewe nikupongeze kwenye swali lile la Mheshimiwa Gambo asubuhi lazima Serikali ijifunze kusikiliza yale yanayosemwa na Waheshimiwa Wabunge. Ukiingia sasa hivi kwenye mitandao comments za wananchi wa Arusha wanaoathirika na utalii wanasikitishwa sana na majibu yale yaliyotolewa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kuiomba Serikali hii sikivu kwa sababu tunafahamu jinsi gani Rais wetu alivyokuwa msikivu, tunaona anavyotatua matatizo ya wananchi kule anakopita, tuombe na Mpango huu na wenyewe ujipange katika kutatua matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naskuhukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kufungua dimba katika uchangiaji wa hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Naomba kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Waziri, Mheshimiwa William Vangimembe Mwalukuvi. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt Angelina Mabula na wataalam wao wa Wizara. Nimpongeze pia Katibu Mkuu wa Wizara hii, dada yetu Mary Makondo, ambaye pamoja na sifa za kiutendaji lakini ana sifa ya unyenyekevu ambayo ni sifa muhimu sana kwa utendaji wa kazi za Serikali. Vile vile nimpongeze Naibu Katibu Mkuu Nico Mkapa na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwenye maeneo matatu, eneo la kwanza ardhi ni rasilimali ambayo kama itapangwa na kutumika vizuri ina uwezo mkubwa wa kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwenye Taifa letu. Utaona kwenye mwaka wa fedha uliopita Wizara ilikadiria kukusanya bilioni 200 na mpaka hivi tunavyozungumza zaidi ya shilingi bilioni 110 zimekusanywa kwenye halmashauri zote za nchi nzima, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa hapa ni fedha hizi zinavyokusanywa, uwekezaji wake unaorudi kwenye Wizara kuwekeza katika upimaji wa ardhi ni mdogo sana. Ukisoma bajeti ya mwaka wa fedha uliopita pamoja na fedha za nje, kwenye fedha za ndani Wizara ilitengewa shilingi bilioni 16 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hata hivyo, mpaka Waziri anawasilisha hotuba yake ya bajeti ni shilingi bilioni tano tu ndiyo zimepelekwa kwenye Wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 30.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni Mwalimu na moja kati ya wanafunzi wako umemtambulisha hapa asubuhi asilimia 30.9 kule shuleni ukiipata kwenye mtihani nadhani tutakubaliana supplementary. Ninachoomba kusema, lazima Serikali itenge fedha za kutosha kwenye Wizara hii ili Wizara iweze kutekeleza wajibu wake wa kupanga matumizi ya ardhi na kupima ardhi. Mpango huu na upimaji huu utakuja baadaye kuwa mapato makubwa kwa Serikali kwa mapato ya land rent. Kwenye Jiji la Dar es Salaam mpaka hivi tunavyozungumza tayari bilioni 5.6 zimekusanywa kati ya malengo ya bilioni, 11 ni kazi kubwa, lakini zitakusanywa zaidi kama maeneo mengi zaidi yatapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, mimi nilikuwa Meya pale Ilala kabla halijawa Jiji la Dar es Salaam. Nilikaa miaka mitano nakaimu Mkuu wa Idara Mipango Miji. Nimeondoka miaka mitano kuna Kaimu Mkuu wa Idara hivi nimerudi kwenye Ubunge bado kuna Kaimu Mkuu wa Idara. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu am-confirm mtendaji yule aweze kufanya kazi hizi akiwa tayari amethibitishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ninalotaka kuchangia, ni eneo la urasimishaji. Kutokana na bajeti finyu na uwezo unaofanya Wizara iwe na uwezo mdogo wa kupima, Serikali mwaka 2015 ilianzisha zoezi la urasimishaji kwenye maeneo mengi ya mijini kwenye Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye Jiji la Dar es Salaam, kwenye Jimbo la Ukonga inafanyika kazi ya urasimishaji. Pale Jimbo la Ukonga yako makampuni 24 kwenye mitaa 64 kwenye Kata zote 13 za Jimbo la Ukonga, kuanzia Kitunda, Mzinga, Kivule, Kipunguni, Ukonga, Gongolamboto, Pugu, Pugu Station, Buyuni, Zingiziwa, Chanika na mpaka Kata ya Msongola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, zoezi hili linasuasua. Ukisikiliza hotuba ya Waziri ziko hatua wameanza kuzifanya. Nimpongeze Waziri, Waziri wetu wa Ardhi ni mtu mwepesi na anajituma sana katika kazi ya ardhi, maana kazi yenyewe hii haitaki sana kukaa ofisini. Tulipata tatizo pale Kata ya Kivule na upimaji wa kile Chuo cha Ardhi Morogoro nilimwambia Waziri na alifika kutatua tatizo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile juzi Naibu Waziri amekwenda Chanika kutatua matatizo haya ya urasimishaji. Nimeona kwenye hotuba ya Waziri wanachukua hatua, lakini tukumbuke kampuni hizi zimechukua pesa za watu, hatua za kuzisimamisha, hatua ya kuzifungia upimaji, hazitasaidia Mtanzania aliyechanga fedha zake kwenye Jimbo la Ukonga na maeneo mengine kupata upimaji wa eneo lake. Nimwombe Mheshimiwa Waziri katika kuhitimisha aje atueleze nini mpango sasa wa kusimamia kampuni hizi ili Watanzania waweze kupimiwa ardhi zao, wapate hati milki, waweze kumiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ninaloomba kuchangia ni migogoro ya ardhi; migogoro ya mipaka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Naomba nijikite kwenye eneo moja tu la migogoro ya mipaka baina ya hifadhi mbalimbali na vijiji na maeneo yetu tunayotoka. Kule Ukonga uko mgogoro wa kudumu baina ya Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Jimbo la Ukonga wa Kata za Buyuni, Chanika na Zingiziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, maana leo nilikuwa nimeshapanga kabisa jioni hapa, siyo kwa kuwa jana alisikia wachangiaji wachache angedhani bajeti ingepita kirahisi. Nilipanga leo jioni niwaombe Wabunge tushike shilingi kwenye eneo hili, lakini nimpongeze Waziri kwenye hotuba yake ameelezea vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, The Land Survey Act, Sura ya 324, inampa Mkurugenzi wa upimaji na Ramani mamlaka ya kusimamia upimaji na kutatua migogoro yote ya mipaka. Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 68 ameeleza vizuri na kwenye ukurasa wa 69, naona amelimaliza tatizo hili na naomba nimnukuu Waziri anasema:
“Ni marufuku kwa Idara au Taasisi yenye migogoro kwenda yenyewe uwandani kutafsiri GN zao bila uwepo wa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani ambaye ndiye mhusika mkuu. Aidha Viongozi wa Mikoa, Wilaya lazima washirikishwe wakati wote mipaka inapohakikiwa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni marufuku kwa idara yoyote ama taasisi kwenda kunyanyasa wananchi na kujitafsiria GN zao wenyewe. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Ndumbaro marufuku, Mheshimiwa Naibu Waziri Mary Masanja marufuku, siyo maneno yangu, maneno ya Waziri mwenye dhamana ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maelezo yake Waziri ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, maana wengine ni mabingwa kuweka watu ndani, sasa hawa ndiyo wa kuwaweka ndani, hawa wanaokuja kutafsiri GN zao wenyewe na migogoro ya mipaka na kunyanyasa wananchi wetu.
T A A R I F A
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Charles Mwijage
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa mzungumzaji MCC mstaafu kwamba unapotoa taarifa, wale unaowapa taarifa hawapo, tatizo la maliasili hifadhi ndilo tatizo la mifugo ninalolipata kwangu kule, lakini unaowaambia hawapo hawawezi kuelewa unavyopata uchungu, hawapo hapa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge nimeshasisitiza mara kadhaa, Serikali ipo Bungeni na ndiyo maana mnazungumza na mimi, yaani kama kuna mtu yeyote wa Serikali ambaye jambo linamhusu limezungumzwa hajaelewa vizuri hata kama yupo humu ndani ataelezwa vizuri, ni jambo gani limezungumzwa kuhusu yeye. Kwa hiyo msiwe na wasiwasi na michango yenu mnayoitoa, Serikali iko Bungeni.
Mheshimiwa Jerry Silaa, malizia mchango wako.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, kaka yangu, mtaalam wa propaganda, sisi wataalam wa sheria hapa tuna address the chair, tunaongea na kiti na ujumbe utafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ni eneo la uthamini. Niseme tu kwamba, Wizara ya Ardhi inafanya kazi yake ya uthamini vizuri sana chini ya Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, mama yetu Evelyn Mugasha. Nafasi hizi zenye mambo ya hela hela ama za uadilifu uadilifu, wanapokaa akinamama wanazifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kitu kimoja, naiomba Wizara ambayo ndiyo wataalam wa masuala haya, waishauri vizuri Serikali. Kulikuwa kuna wakati tunatumia sport valuation kuweza kupata bajeti ili idara ama taasisi inayotaka kufanyiwa uthamini iweze kutenga fedha, lakini tumeona mara nyingi uthamini unafanyika lakini kumbe hata hiyo taasisi inayoagiza uthamini hata fedha kwenye bajeti haijatengewa. Matokeo yake uthamini unafanyika, fidia zinachelewa na wananchi wetu wanapata shida sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iweke utaratibu mzuri wa kufanya uthamini na kulipa wananchi kwa wakati. Ili hili lifanikiwe lazima wakati uthamini unafanyika tayari bajeti iwepo na fedha ziwe zimeshatengwa. Maeneo mengine wawe wanaaminiana, hawawezi wakafanya uthamini ukaidhinishwa, wakaanza uhakiki, ukakamilika, ukaja uhakiki mwingine wakati wananchi wanasubiri fidia zao, ile miezi sita ya kisheria inapita, hela za riba hazipo, tunaanza tena kurudi nyuma na wananchi wanapata shida kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nirudie tena kuipongeza Wizara, inafanya kazi nzuri hasa katika kujikita kuingia kwenye mifumo ya TEHAMA. Tukienda hivi nchi yetu itapata tija kubwa kwenye sekta ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. JERRY W. SILAA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wenzangu kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa kutoa muda wa kutosha wa ripoti za Kamati hizi tatu, kujadiliwa na Bunge kwa kipindi cha siku nne, tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, niwashukuru sana Wabunge kwa michango yao. Tumepata michango ya jumla ya Wabunge 83. Katika hao Wabunge 19 wamechangia hoja mahususi ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma tokea Novemba mpaka leo. ukiondoa waliochangia Taarifa ya Hesabu za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pekee, wachangiaji Taarifa ya PAC waliyagusa mashirika ya umma.
Mheshimiwa Spika, wakati nawasilisha Taarifa ya Kamati, Kamati ilikuwa na mapendekezo nane, baada ya majadiliano Kamati imeboresha mapendekezo kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge jumla ya mapendekezo matano hivyo kupelekea jumla ya mapendekezo kufika 13.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu ya Kamati yetu ya PIC ya kuangalia ufanisi na tija ya uwekezaji na pamoja kwamba ripoti za ukaguzi zinawasilishwa ila tunazitumia tu kwa ajili ya kukokotoa vigezo vya uwekezaji. Wenzetu wa PAC wana majukumu ya hoja za ukaguzi wa mashirika ya umma.
Mheshimiwa Spika, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, mashirika yafuatayo ambayo tunayasimamia uwekezaji wake, yametajwa na yameonekana yana hoja za ukaguzi wa mabilioni ya shilingi. Mashirika hayo ni pamoja na NHIF, TRA, DART, KADCO, TANROADS, MSD, TPA, TRC, TAMESA, GPSA, Bodi ya Mikopo, Ngorongoro Conservation, REA, DUWASA na TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri hoja za ukaguzi kwenye ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 ndio yamepelekea kutofikia lengo la makusanyo ya Msajili wa Hazina kwa maana katika lengo la kukusanya gawio la shilingi bilioni 308.82 sawa na asilimia 75 ya lengo ilikusanywa. Katika michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, ni jumla ya shilingi bilioni 202.2 tu sawa na asilimia 51 ya lengo ilikusanywa. Kama mashirika haya yangesimamia fedha vizuri, basi wangeokoa fedha za walipakodi, faida ingeongezeka na mchango kwenye Mfuko Mkuu wa Taifa ungeongezeka.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kusoma maoni na mapendekezo ya maazimio ya Kamati, naomba kuzungumzia mambo mawili ambayo yamechangiwa sana na Waheshimiwa Wabunge, ili kama yataboreshwa inawezekana ile mianya ya uvujaji wa mapato, katika hela za umma na matumizi yasiyo ya lazima yanaweza kufikiwa. Maeneo hayo mawili la kwanza ni la mifumo. Wachangiaji wengi wamechangia mifumo mbalimbali na kwenye mifumo nimeona kuna maeneo mawili. Kwanza mifumo mingi ni dhaifu, utasikia POS inaongezwa muda fedha zinafutwa, labda GPSA wanakuwa hawana mifumo mizuri ya uwagizaji, TANePS haijibu majibu ya manunuzi. Kwa hiyo mifumo mingi iliyopo kwenye nchi yetu ni dhaifu.
Mheshimiwa Spika, mifumo inakuwa dhaifu kwa mambo mawili tu, moja, aidha, inapewa udhaifu kwa makusudi katika kutengeneza mianya ya upigaji wa fedha za umma. Kwa sababu mfumo unapokuwa madhubuti kama ilivyo mifumo yetu ya miamala ya simu, sijawahi kumsikia hata Mheshimiwa mmoja huku anasema hela zake zilizopo kwenye miamala ya simu zimepotea, zimevuja, zimefutwa au salio halionekani. Kwa hiyo mifumo inapokuwa dhaifu inawezekana ni kwa makusudi katika kutengeneza utaratibu wa uvujifu wa mapato na matumizi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, tuliwahi kulizungumza hapa Bungeni, ni Serikali kushindwa kufika mwisho wa mambo mawili. Moja, ni ujengaji wa mfumo wa public infrastructure kwa maana ya PKI ambao ndio mfumo unaweza kusaidia authentication ya transactions zote za kieletroniki kwenye mifumo hii ya mapato na matumizi.
Mheshimiwa Spika, la pili, kutokuwa na centralize ledger, kwa sababu ukisikia hapa kuna mtumishi ana malimbikizo ya mshahara na kuna mtumishi amestaafu amelipwa na kuna mapato yamekusanywa ghafi yameliwa, maana yake hakuna sehemu ya pamoja ambapo Taifa la Tanzania, nchi yetu, tunakuwa na centralized system ambayo inaweza kuona, vitendo kama hivi havifikiwi na kama vinafikiwa vinaweza kuonekana ni nani kafanya nini na lini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimesema niyaseme haya kwa utangulizi kwenye mifumo na tutakuwa na maazimio mahususi. La pili, ni Bodi za Wakurugenzi. Nadhani nilichangia pale nyuma siyo vyema kwa kuokoa muda, lakini Kamati inaomba kidhati kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa nia yake na vitendo vyake ambavyo anaonyesha wazi, anaunga mkono si tu uwekezaji kwenye mashirika ya umma lakini sekta nzima ya uwekezaji kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pale awali nilieleza kwamba kwenye uteuzi wa bodi Mheshimiwa Rais amewahi kunukuliwa hadharani akieleza ni jinsi gani anatimiza wajibu wake pale tu anapopelekewa uteuzi wa bodi. Kama nilivyoeleza pale awali jumla ya mashirika 23 kufikia Octoba 31, yalikuwa yana bodi zilizomaliza muda wake na hazijateuliwa. Kwa kudhibitisha kauli ile ya Mheshimiwa Rais, yako mashirika 12 yaliyopo kwenye Wizara tisa (9) ambayo tayari Mheshimiwa Rais ameshateua Wenyeviti wa Bodi na Wajumbe ambao ni mamlaka ya uteuzi wa Wizara kuteua, hawajateuliwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa mapendekezo 13 na kati ya hayo kama nilivyosema pale awali nane yalipendekezwa na Kamati na matano yametokana na michango ya Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, moja, Taasisi kutokuwa na bodi za wakurugenzi kwa muda mrefu kutokana na kuchelewa kuteuliwa kwa Wajumbe wa Bodi:-
KWA KUWA mashirika mengi yanayotumia mitaji ya umma yameendeshwa bila kuwa na Bodi za Wakurugenzi kutokana na bodi zilizokuwepo kumaliza muda wake;
NA KWA KUWA hadi sasa kuna taasisi na mashirika 12 ambayo yana Wenyeviti wa Bodi na bila wajumbe na taasisi za mashirika 23 ambayo hayana kabisa Wenyeviti wala Wajumbe wa Bodi, jambo ambalo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika uwekezaji wa mitaji ya umma na kwamba ni jambo linalokwamisha upatikanaji wa tija uwekezaji unaofanywa na Serikali;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba: -
(a) Serikali ikamilishe uteuzi wa wajumbe wa Bodi 12 kwenye Wizara tisa ambazo Mheshimiwa Rais ameshateua Wenyeviti ndani ya miezi 3. (Makofi)
(b) Serikali ikamilishe uteuzi wa Wajumbe wa Bodi 23 kwenye Wizara 12 ambazo hazina bodi ndani ya miezi sita.
(c) Serikali ihakikishe inatimiza utaratibu wa kuanza maandalizi ya uteuzi wa bodi miezi tisa kabla bodi hazijamaliza muda wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbili, changamoto ya kupata vibali vya kuajiri: -
KWA KUWA mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi katika kujiendesha kwake kutokana na kutegemea mchakato wa ajira unaoendeshwa na Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma katika kupata watumishi;
NA KWA KUWA changamoto hiyo inaathiri tija ya uwekezaji na manufaa yaliyotarajiwa kupatikana kutokana na kukosa watumishi wanaostahili kwa wakati, hata pale ambapo Shirika la Umma linakuwa na uwezo wa mapato wa kuwalipa mishahara;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba Serikali iweke utaratibu maalum wa kutoa vibali kwa taasisi zinazojiendesha kibiashara ili ziweze kuajiri zenyewe ajira ya moja kwa moja na kuweza kuendana na soko la ushindani kibiashara.
Mheshimiwa Spika, tatu, uwezo wa SGR kuzidi uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam: -
KWA KUWA Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo mdogo wa kupokea mizigo kulinganisha na uwezo wa SGR iliyoigharimu Serikali kwa uwekezaji mkubwa ilihali bandari hiyo ndio chanzo kikuu cha mizigo. Hii itachangia SGR isipate mzigo wa kutosha kwa ajili ya kusafirishwa pindi itakapokamilika;
NA KWA KUWA changamoto ya SGR kutopata mzigo wa kutosha kusafirishwa ni jambo linalokwamisha kupatikana kwa tija ya uwekezaji uliofanyika na kwamba mkwamo huo unaweza kutatuliwa kwa kuongeza Bandari ya Dar es Salaam na kujenga Bandari ya Bagamoyo;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba: -
(a) Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
(b) Serikali iharakishe zoezi la kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kuongeza gati za kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam na zoezi hilo likamilike kabla ya ujenzi wa reli ya SGR kukamilika. Hatua hii itasaidia SGR kupata mzigo wa kusafirisha na hivyo tija iliyokusudiwa kufikiwa.
Mheshimiwa Spika, nne, umuhimu wa Shirika la Maendeleo (NDC): -
KWA KUWA manufaa ya mradi wowote wa uwekezaji yanategemea kuanza kwa mradi lakini Mradi wa Mchuchuma na Liganga umechukua muda mrefu katika hatua za majadiliano ambayo kwa sasa yanaratibiwa na Kamati ya Majadiliano ya Serikalini (GNT);
NA KWA KUWA kutokukamilika kwa majadiliano hayo yanayoendelea kwa muda mrefu tangu kuanza kwake ni jambo linalochelewesha upatikanaji wa manufaa ya mradi huo;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe kuwa mazungumzo yanayoendelea katika Kamati ya Majadiliano ya Serikali (GNT), yanafika mwisho ndani ya miezi mitatu au yapelekwe NDC, lengo ikiwa kuyamaliza na kupata tija inayokusudiwa katika miradi, kwa sababu Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika taasisi hii ikiwemo kuipatia Bodi mpya ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti.
Mheshimiwa Spika, tano, mikopo chechefu (non- performing loans): -
KWA KUWA imebainika kuwa baadhi ya taasisi kama vile Benki ya Maendeleo (TIB) na Benki ya Biashara (TCB) zinakabiliwa na changamoto ya kuwa na kiasi kikubwa cha mikopo chechefu (non-performing loans);
NA KWA KUWA hali hiyo inaathiri mizania ya vitabu vya taasisi hizo jambo ambalo ni hatari kwa misingi ya kibiashara na uendeshaji wa taasisi zinazotumia mitaji ya umma;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba: -
(a) Serikali ifanye tathmini ya madeni hayo na kuhakikisha wanayaondoa kwenye vitabu vya benki hizo bila kuathiri ulipaji wa mikopo inayolipika (performing loans). Hatua hiyo itasaidia benki hizo kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija inayokusudiwa.
(b) Serikali itengeneze mfumo fungamanishi kati ya Bodi ya Uhasibu (NBAA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Taasisi za Fedha na wafanyabiashara ili chanzo cha hesabu zote zinazotumiwa na wafanyabiashara kiwe kimoja. Hii itasaidia kukadiria kiwango halisi cha mkopo kinachoweza kulipika na mkopaji ili kupunguza mikopo chechefu.
Mheshimiwa Spika, sita, upungufu wa mtaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL):-
KWA KUWA Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inakabiliwa na changamoto ya mtaji hasi na changamoto ya uendeshaji wa biashara kutokana na utaratibu wa kukodisha ndege kutoka Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA);
NA KWA KUWA utaratibu huo unaongeza madeni wanayodai yaani payables katika vitabu vya TGFA.
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba, Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania (TGFA) ikamilishe taratibu za kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alipokuwa anapokea Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tarehe 30 Machi, 2022 la kurudisha umiliki wa ndege kwa ATCL kwani ukiondoa tatizo hili ATCL ina uwezo wa kujiendesha kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, saba, kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB): -
KWA KUWA TADB ambayo ndio benki pekee inayohusika moja kwa moja na shughuli za kilimo, lakini haijapatiwa mtaji wa kutosha na kuendana na nia ya Serikali ya kuongeza tija kwenye kilimo, kuleta mageuzi ya kilimo na kulisaidia Taifa kufikia usalama wa chakula;
NA KWA KUWA pamoja na jitihada za Serikali kuipatia TADB kiasi cha shilingi milioni 208 mwaka 2021, bado kuna ahadi ya Serikali ambayo kama ingetekelezwa benki hii ingekuwa na mtaji wa jumla ya shilingi bilioni 760. Kutofikiwa kwa mtaji huu kunaathiri ufanisi na tija katika sekta ya kilimo;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba, Serikali itekeleze ahadi yake (commitment) waliyoitoa kwa TADB ya kuiongezea mtaji kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa kila mwaka wa fedha, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, nane, kuathirika kwa kilimo cha pamba kutokana na maelekezo ya Serikali ya mwaka 2019 ya kuuza pamba kwa bei ya juu zaidi ya soko la dunia:-
KWA KUWA agizo la Serikali inayoitaka pamba kununuliwa kwa bei ya juu zaidi ya soko la dunia imeathiri uwezo wa wanunuzi wa pamba kwa kiasi cha shilingi bilioni 21.8, kiasi ambacho Serikali iliahidi kufidia deni hilo;
NA KWA KUWA deni hilo limeathiri taswira ya Bodi ya Pamba kwa wakulima na kuongeza changamoto katika biashara ya kilimo cha pamba;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba, Serikali iharakishe utekelezaji wa ahadi yake ya kulipa deni la pamba. Hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa sekta hiyo na kurudisha taswira chanya ya Bodi ya Pamba.
Mheshimiwa Spika, tisa, mwingiliano wa majukumu kwa baadhi ya taasisi za umma:-
KWA KUWA mwaka 2017 Serikali iliamua majukumu ya Tanzania Air Port Authority ya kujenga viwanja vya ndege yahamie TANROADS;
NA KWA KUWA jambo hili ni kinyume cha viwango vya kimataifa na ni kinyume cha matakwa ya International Civil Aviation Organization (ICAO) ambayo Tanzania Air Port Authority ni mwanachama wake na ICAO inazitaka Mamlaka za Viwanja vya Ndege kusimamia shughuli zote za viwanja vya ndege ikiwemo ujenzi wa viwanja vyao;
KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze haraka agizo la kurejesha jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) pamoja na rasilimali zake zote ikiwemo watumishi waliohama mwaka 2017. Hii ni muhimu kwa ajili ya kukidhi viwango vya kimataifa katika uendeshaji wa viwanja vya ndege. (Makofi)
(10) Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
KWA KUWA, katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, Serikali inatekeleza mageuzi ya kidigitali yanayojumuisha teknolojia ya TEHAMA, kuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi kwenye mifumo ya uzalishaji huduma na utawala;
NA KWA KUWA, mashirika mengi ya umma hayazingatii matumizi sahihi ya TEHAMA hali inayopelekea upotevu wa mapato na udanganyifu katika utoaji huduma zake;
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba: -
(a) Serikali ikamilishe mchakato wa public infrastructure (PKI)
(b) Serikali iunde mfumo wa taarifa ya pamoja (centralized ledger) kuondoa udanganyifu wa mifumo ya taasisi.
(c) Serikali ihakikishe inasimamia kikamilifu taasisi na mashirika ya umma kuimarisha mifumo ya TEHAMA. Hatua hizi zitasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kudhibiti udanganyifu kwa lengo la kupata tija inayokusudiwa.
(11) Changamoto ya uendeshaji wa Kampuni ya Meli (Marine Services Company).
KWA KUWA, Kampuni ya Meli (MSC) iliyokuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari kwa sasa imekuwa Kampuni huru inayojitegemea;
NA KWA KUWA, kitendo cha Mamlaka ya Bandari kuendelea kumiliki baadhi ya mali za (MSC) kunaathiri utendaji wa (MSC) ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa mtaji wa umma uliowekwa (MSC);
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iharakishe mali zote za (MSC) zilizopo Tanzania Port Authority zirejeshwe haraka sana (MSC) zikiwemo chelezo, karakana na nyinginezo.
(12) Matumizi ya TEHAMA katika Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF).
KWA KUWA, Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) umeonesha udhaifu katika utoaji wa huduma zake jambo ambalo limepelekea Mfuko kupata hasara;
NA KWA KUWA, changamoto zilizojitokeza katika uendeshaji wa (NHIF) kwa kiasi kikubwa imetokana na kutokakuwa na mfumo thabiti wa TEHAMA inayotoa mianya ya kufanya udanganyifu kwa urahisi;
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ihakikishe (NHIF) inaandaa mfumo madhubuti wa TEHAMA na kuanza kuutumia haraka iwezekanavyo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma wa mfuko na kuziba mianya ya udanganyifu. (Makofi)
(13) Matumizi makubwa ya gharama za bima za Ndege kwa Shirika la Ndege la Taifa - ATCL.
KWA KUWA, Shirika la Taifa la ATCL linalazimika kununua Bima kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambapo NIC ananunua Bima hizo kutoka kwa Wakala wa Nje ya Nchi kwa mfumo wa moja kwa moja single source;
NA KWA KUWA, changamoto zilizojitokeza ni kwa Shirika la Ndege kujikuta linanunua bima hizo kwa gharama kubwa hali inayopelekea kupunguza faida na tija kwa Shirika;
KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ielekeze ATCL na NIC kufanya zabuni shindanishi ili kupata wakala mwenye bei nafuu, huduma bora na ambaye atazingatia uwiano wa ndege, shirika anazomiliki, hii italeta ufanisi, tija na kupunguzia shirika gharama za matumizi.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kupata fursa ya kuchangia kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano. Nakushukuru zaidi kwa sababu pamoja na kupongeza Mpango huu mzuri, nitaanza kuchangia si mbali sana na alipomalizia mchangiaji aliyepita.
Mheshimiwa Spika, kwanza, niipongeze sana Serikali kwa kuja na Mpango huu ambao ukiusoma umezingatia sana michango ya Wabunge waliyotoa wakati Mpango huu umewasilishwa. Pia ukiusoma Mpango huu unakuja kuendeleza pale Mpango wa Miaka Mitano iliyopita; Mpango wa mwaka 2015-2020 ambao tumeona Serikali ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaenda kulifanya Taifa letu kuwa na uchumi unaojitegemea.
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika kwenye Bwawa la Stigler’s Gorge. Kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika kwenye Reli ya Standard Gauge. Kazi kubwa imeendelea kufanyika katika miradi ya kufufua Mashirika ya Umma ikiwepo Shirika letu la Ndege la ATCL. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine na mimi kidogo ni Mwanasheria. Ukisikiliza mchango wa Mwanasheria mmoja hapa dada yangu nauona kabisa umepungua sana knowledge ya kimkakati kwenye miradi ya kimaendeleo na fedha. Unapoongelea Shirika la ATCL…
SPIKA:Mheshimiwa Halima usikilize vizuri unasomeshwa shule hapa. Hii ni shule unasomeshwa, kwa hiyo tulia. Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, kule kwenye sheria tunafundishwa purposive approach ya legal interpretation, kwamba unasoma sheria kama ilivyoandikwa, kwenye fedha hatufanyi hivyo. Unapoongelea Shirika la Ndege, kwanza lazima utambue ni Shirika ambalo lilikuwa lina-operate kwa ndege moja. Katika miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya kazi kubwa ya kufufua Shirika hili. Ndege ya kwanza imepokelewa mwishoni mwa mwaka 2017, zimekuwa zikipokelewa ndege mpaka tunavyozungumza zimepokelewa ndege nane (8) na ndege tatu (3) zitakuja kwenye Shirika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa wale wenye kufanya biashara wanafahamu, huwezi ukawa unafufua Shirika at the same time ukawa unatengeneza faida, haijawahi kutokea. Ziko aina ya biashara ambazo mpaka sheria zetu za kodi zinaruhusu hasara miaka mitatu mpaka miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wako Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema, Shirika la Ndege si biashara bali ni huduma inayoenda kuchochea maeneo mengine ya biashara. Ukisoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, maana Financial Statement hazisomwi kwenye purposive approach, husomi tu ile hasara ukabeba ukaleta hapa Bungeni kuja kupotosha umma wa Watanzania, unasoma uwanda mpana wa ripoti ile.
Mheshimiwa Spika, yapo madeni ya kurithi kwenye Shirika hili, lakini ningetegemea maana na majina tunaitwa wengine Njuka ningetegemea maneno hayo yasemwe labda na Njuka, mzoefu alitakiwa kufahamu kwamba hata ndege hizi zilivyonunuliwa zinamilikiwa na TGFA, ATC inazikodisha. Kwenye Ripoti ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ukiisoma inasema kabisa kwamba kuna deni limetokana na kipindi ambapo TGFA inakodisha ndege ATC lakini wote tunafahamu, si ATC peke yake au hamtembei jamani, dunia nzima ndege zimepaki kwa sababu ya COVID- 19! Hili siyo Shirika pekee lililoathirika! (Makofi)
T A A R I F A
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Elibariki.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe msemaji taarifa kwamba dunia kwa ujumla, kwa mwaka huu peke yake ime-accumulate loss ya dola bilioni 118 katika Mashirika ya Ndege. Kwa hivyo, hii haiwezi kutu- discourage sisi tuone kwamba ATC haina faida kwa Watanzania. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Jerry endelea.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa. Unaponunua ndege kwenye mizania ya kampuni ni capital expenditure. Kumbuka manunuzi haya yatakuja na mafunzo ya wataalam, marubani, wahandisi, kuboresha karakana; zote hizo huwezi ukaanza kuona faida kwenye miaka hii ya mwanzo. Pia ndege hizi, maana msemaji anasema ndege zimepaki, ndege haziruki kama kunguru zinaruka kwa mpango. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa bado dakika tano zako. (Makofi/Kicheko)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, sisi wengine tumekulia kwenye familia za aviation. Tumenunua ndege za Bombadier Q4100 kwa sababu ya safari za ndani. Tumenunua Airbus, jamani hata mitandao hamuangalii? Ukiona Mheshimiwa Rais Mama Samia anasafiri ndani anasafiri na Q4100; jana ameenda Uganda na Airbus kwa sababu ndege zile zimenunuliwa kwa sababu ya Regional Flights. Zile Dreamliner, kila siku mnatangaziwa kwamba zilinunuliwa kwa sababu ya safari za masafa, trip za Guangzhou, London, India, ndege ya moja kwa moja toka nchini kwetu. Ukitoka zako ulikotoka ukaja Jijini Dar es Salaam ukakuta zimepaki, usishangae, mashirika haya yameathiriwa na magonjwa ya COVID-19 ambayo imeathiri sana usafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, tunapofanya capital expenditure yoyote huwezi kuepuka kukopa. Swali huwa unakopa ufanyie nini? Kama tunakopa kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimkakati, miradi hii ina tija kubwa kwenye uchumi wa nchi yetu, ni jambo la kupongezwa wala si jambo la kubezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa sisi tuliopewa dhamana na wananchi wa Tanzania, bila kujali umeingilia mlango gani, maana wako Wabunge hapa Vyama vyao wenyewe vinawakana…(Kicheko)
Mheshimiwa Spika, lakini sisi tunawaheshimu kama Wabunge wenzetu, tukisimama hapa kuchangia tuweke maslahi mapana ya nchi yetu.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, tuweke maslahi mapana ya legacy aliyotuachia Rais wetu na tuisaidie Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mezani ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Nampongeza kaka yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Mbunge kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuiongoza Wizara hii na Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange na Mheshimiwa David Silinde kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwa karibu na Wabunge kwa kutusikiliza na kuwa wanyenyekevu katika kutumikia Taifa letu. Binafsi niwaahidi ushirikiano, vijana wenzetu tupo tutawalinda, tutawatetea katika kutekeleza majukumu yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo kupitia kwenye Wizara hii. Tumesikia kwenye Hotuba ya Waziri, fedha zilizokuja za barabara kupitia TARURA kila Jimbo tumepata fedha hizi, tunaishukuru na kumpongeza sana Rais. Tumepata pesa za tozo kujenga vituo vya afya, Jimbo la Ukonga tumepata bilioni 1.5, Kituo cha Afya Kipunguni kinajengwa, Kituo cha Afya Majohe na Kituo cha Afya cha Zingiziwa tunaishukuru na kuipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuleta fedha za elimu bila malipo, shilingi bilioni 1.2 kwenye elimu ya msingi na shilingi bilioni 3.84 kwenye elimu ya sekondari kwenye Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zimepokelewa, tunaishukuru na kuipongeza Serikali. Ujenzi wa zile shule za kimkakati kwenye Mradi wa SEQUIP fedha zimeanza kupokelewa na kule Jimbo la Ukonga shule itajengwa kwenye Kata ya Mbondole na kuna mpango mwingine wa shule nyingine kwenye Kata ya Kitunda, tunaishukuru sana Serikali.
Naomba Serikali, niiombe sana tuendelee kutenga fedha hasa za barabara kwenye majimbo yote lakini kwenye Jimbo la Ukonga tunaomba sana Serikali, uendelezaji wa mradi wa DMDP awamu ya pili ambacho ndiyo kilio kikubwa cha wananchi wengi wa Jimbo la Ukonga na Mkoa wa Dar es Salaam kama wenzetu tulivyosikia hapa kwenye hotuba ya Waziri, mradi wa TACTIC ambao ni uendelezaji wa mradi wa Tanzania Strategic City Project ambao umeanza, tunaiombe Serikali ijitahidi kuongeza kasi ya mazungumzo na Benki ya Dunia ili Mradi wa DMDP awamu ya pili na wenyewe uweze kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Dar es Salaam na kule Jimbo la Ukonga pamoja na fedha hizi za TARURA zilizoletwa na Mheshimiwa Rais, Wabunge wengi hapa alivyotambulishwa Engineer Seif wamepiga makofi kutokana na fedha zile kupokelewa kwenye majimbo karibia yote nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe sana Serikali barabara nyingi za Dar es Salaam kile kigezo cha traffic density, cha wingi wa magari yanayotumia barabara kimezidi yale magari 400 ya kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe na kiukubwa ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami. Barabara za Pugu - Majohe, barabara za Banana - Kitunda - Kivule tunategemea kwenye mradi huu wa DMDP tukipata fedha zitajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la barabara niombe mambo mawili; jambo la kwanza niiombe sana Serikali inapogawa fedha hizi basi vigezo vya kitaalam vya wenzetu vya TARURA vizingatiwe. Majimbo mengi yanatofautiana urefu wa kilometa za barabara, majimbo mengi yanatofautiana changamoto za ujenzi wa vivuko na madaraja. Nikuombe radhi hata humu Bungeni kwako ikitokea unagawa huduma yoyote ya mpango ya uzazi salama hauwezi Bi. Asha Mshua ukamuweka kundi moja na Ng’wasi Kamani, lazima utaweka kwa vigezo vyao na umri wao kutokana na hali halisi ya mazingira ya uzazi salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana kwenye mgao wa fedha hizi ombi la pili na wenzetu wa Zanzibar kwa mahusiano mazuri ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnapogawa fedha hizi za barabara, basi kama tulivyofanya kwenye fedha za UVIKO na wenzetu wa majimbo ya Zanzibar nao muangalie jinsi ya kuweza kuwafikishia fedha za barabara ili kuwe na usawa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nizungumzie system za structures za Serikali za Mitaa, leo hapa tumeombwa zaidi ya trilioni 4.6 kama mishahara kwenye Serikali za Mitaa kwa jumla ya watumishi zaidi 319,000, tumeombwa fedha za maendeleo zaidi ya shilingi trilioni 3.26 ambazo zinaenda kutekelezwa kwenye Serikali za Mitaa. Lakini Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Katiba, zinapata mamlaka yake kwenye Ibara ya sita, Ibara ya nane, Ibara ya 145 na Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wananchi wa Tanzania wenyewe ndiyo wameamua kwenda kutengeneza Serikali za kusimamia maendeleo yao. Fedha hizi zinaenda kule chini kuna Wenyeviti wa Vijiji, kuna Wenyeviti wa Mitaa, kuna Waheshimiwa Madiwani, tujiulize swali moja la msingi je, mifumo na miundo ya Halmashauri hizi inawapa mamlaka ya kutosha ya kusimamia uwezo wa miradi hii ya maendeleo? Halmashauri hizi zinawezeshwa na watendaji hawa kwenda kusimamia watumishi hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inapaswa kufanyika, kazi ya kwanza kwenye miundo. Muundo wa Halmashauri zetu tukitoka hapo nje getini ukamtafuta Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kama ana ufahamu wa bajeti hii inayosomwa na Waziri, nadhani majibu yake utayapata. Kuna kazi kubwa ya kurekebisha muundo wa Halmashauri, ili Waheshimiwa Madiwani wapate fursa ya kujadili bajeti hizi kwa kina kabla hazijafika hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwenye Halmashauri imekuwa ni desturi ya bajeti hizi kupita kwa kasi na kuwa na haraka ya kupita yale malengo ya Regional Secretariat na kuleta Bungeni.
Mhshimiwa Naibu Spika, lakini la pili; je, Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji; je, Waheshimiwa Madiwani wanapata mafunzo ya kutosha ya kuweza kusimamia rasilimali fedha na rasilimali watu kule kwenye Halmashauri zetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la tatu niipongeze Serikali toka mwaka fedha uliopita imeanza kulipa posho za Madiwani. Lakini je, posho hizi zinatosha? Je, posho za Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji zinatosha? Hivi kweli Mwenyekiti wa Mtaa analipwa posho ya shilingi 100,000 kwa mwezi, ataacha kuwa- charge wananchi gharama za kuandika barua ofisini? Ataweza kweli kusimamia maendeleo kwenye eneo lake?
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme ifike wakati Serikali itengeneze muundo mzuri wa kuwawezesha kimuundo, kimafunzo, lakini kimaslahi viongozi wetu hawa wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji na Waheshimiwa Madiwani waweze kusimamia majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni Halmshauri zenyewe Serikali kuzitendea haki. Mwaka 2019/2020 kodi ya majengo (property tax) ilikuwa inakusanywa na Halmashauri zetu; na pale Halmashauri nyingi za Dar es Salaam tulikusanya shilingi bilioni tisa, lakini mwaka 2021zilipelekwa TRA. Fedha hizi hazikukusanywa wala hazikuletwa kwenye Halmashauri kuja kutekeleza majukumu yetu. Mwaka 2021/2022 zimepelekwa kwenye LUKU, sijui hii mwaka 2022/2023 mtazileta wapi? Niiombe sana Serikali tuziwezeshe Halmashauri zetu, tuzipe mamlaka ya kukusanya mapato yake, zitengenezewe malengo na zisimamiwe kuweza kutekeleza majukumu kwa wananchi wake. Hata hao Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji, Waheshimiwa Madiwani, wawekewe malengo ya kukusanya mapato, kuwe na sera ya retention ili waweze kuendesha shughuli zao kwenye ofisi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mtaa inapokuwa na retention ya kodi ya majengo haitam-charge mwananchi barua ya dhamana kulipia kwenda kumtoa ndugu yake aliyekuwa na matatizo mahakamani. Watakuwa na uwezo wa kujiendesha, kutoa mafunzo kwa wananchi wao, hata kusimamia vikundi vya kina mama na vijana na walemavu wanaopata mikopo ya Halmashauri hata kuwaandikia katiba, kuwasajilia vikundi; na huu uwezeshaji wa wananchi utafika kwenye maeneo ya mitaa, vijiji na vitongoji na Waheshimiwa Madiwani leo watakuwa na uwezo wa kusimamia halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuheshimi muda na kwa wachangiaji waliopo leo, naomba niseme naunga mkono hoja iliyowekwa mezani na Waziri wa Nchi, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. JERRY W. SILAA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuja kuhitimisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza sana wachangiaji wote waliochangia hoja zote tatu mezani. Tumetambua wachangiaji 24 ambao waamechangia kwenye maeneo mbalimbali ya hoja hizi tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii ni mtambuka. Katika wachangiaji waliochangia zipo taaisi zimetajwa ambazo zinasimamiwa na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Viwanja vya ndege (TAA), Mamlaka ya barabara kwa maana ya TANROADS, TANAPA, TAMESA, Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Kiwanda cha Ngozi Kilimanjaro (KLICL), Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wachangiaji wamezungumzia suala la uhamishaji wa Mamlaka ya Ujenzi wa Viwanja vya Ndege toka TANROAD kwenda TAA. Naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba katika kikao chake cha tarehe 4 Novemba, 2022, katika Mkutano wake wa Tisa, Bunge lilikuwa na Azimio mbalo lilitokana na Mapendekezo ya Kamati yetu Na. 9, kwamba Serikali ihamishie Mamlaka ya Ujenzi wa Viwanja vya Ndege kutoka TANROAD Kwenda TAA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuthibitishie, kama alivyosema Naibu Waziri wa Ujenzi, tayari Serikali imeanza mchakato wa kuhamishia na wameleta utekelezaji wa azimio hili kwenye kamati na utekelezaji wake unaridhisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kwa kifupi maeneo Matano. Eneo la kwanza ni Mfuko Maalum wa Uwekezaji (Investment Fund). Kamati imeleta pendekezo la kuiomba Serikali ianzishe mfuko huu ili kusaidia mashirika na taasisi yenye kuhitaji fedha za uwekezaji kuweza kupata fedha kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya, ipo Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) chini ya Wizara ya Kilimo. Bodi hii ikiwezeshwa fedha za kutosha ina uwezo wa kununua mazao, kwa maana ya mazao ya nafaka na inaweza ikasaidia huko mbele ya safari hata hili tatizo ambalo Waheshimiwa Wabunge leo wamesema la mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaamini kama Bunge lako litapitisha azimio hili, basi Investment Fund hii itasaidia siyo tu taasisi za kiuwekezaji za biashara, bali hata taasisi kama CBP ambayo inaweza ikasaidia kwenye mifumuko ya bei ya chakula nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la Mifumo ya TEHAMA. Namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene, amemnukuu Mheshimiwa Rais katika kikao chake cha tarehe 28 Machi, 2021 akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hata hivyo, pale alipoishia kunukuu, yapo maneno ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasema, “kama mifumo imewashinda, basi ombeni misaada kwa wataalamu.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la mifumo limesemwa hapa na Wabunge wengi, na maelezo yake ukitoa majibu yake hapa, hakuna anayeelewa. Ipo mifumo mingi ambayo haieleweki. Leo wafanyabiashara ikifika muda wanaweka return zao TRA, mfumo uko down. Yaani mtu anataka kulipa kodi, anaambiwa mfumo uko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia Mamlaka ya Bandari (TPA). Pale TRA wana mfumo wao wa TANCIS wa kulipa custom duty; huku bandarini nao wana mfumo wao wa cargo system. Ukishalipa kodi, uende bandarini na wakati mwingine kodi mfumo uko chini. Ukienda bandarini wanaku- charge storage. Kule bandarini nako, ingawa wanaweza kuingia kwenye TANCIS na kwenyewe kuna matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Rais anasema, siyo lazima kila jambo ujidai wewe Masoud Mwamba unaliweza. Kama limewashinda, tafuteni wataalamu waliobobea kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tukizungumzia mifumo, tunatoa mifano. Sisi wote hapa tuna simu za mikononi, na wote hapa tukifanya miamala ya simu za mikononi, hakuna siku muamala unazidiwa, hakuna siku unatuma pesa ambayo hauna; hakuna siku unadhulumu muamala unaenda kushughulikia mahali unaambiwa jambo limeshindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mifumo ya kitaalamu ikijengwa vizuri; ndiyo maana Kamati inashauri Bunge kwamba uanzishwe mfumo wa single integrated information management system and network ambao utajumuisha mambo yote haya. Ukisikia mtu ana NIDA basi itambulike maeneo yote. Sio mtu wa Halmashauri hii anakopa, halafu anaenda Halmashauri nyingine; au unasikia kuna POS Halmashauri, mtu anaingiza anachokitaka yeye. Leo kuna Halmashauri fedha hazionekani, nyingine zinakusanywa haziendi Benki halafu unaambiwa huo ni mfumo. Hakuna mfumo wenye tabia kama hizo. Hicho ni kitu kingine, labda kitafutiwe jina lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali na Mheshimiwa Simbachawene kwa kauli hiyo aliyoisema ya Mheshimiwa Rais. Tunaiomba Serikali iende ikawe serious kwenye mifumo ili Watanzania hawa, watu wanaotumia bandari yetu waweze ku-clear mIzigo yao wakiwa Congo. Unaweza ku-trace mzigo kuanzia Congo mpaka unafika Bandari ya Dar es Salaam, lakini ukifika pale ni nenda rudi, mfumo uko chini, baadaye unachelewa kulipa kodi, ukilipa kodi, unakuwa charged kwenye storage, mwisho wa siku bandari inakosa wateja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni la utalii. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana kwenye eneo hili. Filamu yake ya Royal Tour imeongeza watalii kwa kiasi kikubwa. Leo Ngorongoro mpaka kufikia Desemba wamekusanya zaidi ya shilingi bilioni 98. Leo TANAPA mpaka kufikia Januari 23, wamekuja kwenye Kamati wamekusanya shilingi bilioni 233. Tunategemea hawa kufikia mwezi Juni mwaka huu 2023 watakuwa wamevunja rekodi ya ukusanyaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nenda huko Ngorongoro, pita hiyo barabara, ukienda likizo Serengeti kupumzika na mkeo, zile rasta utakazopiga njia nzima mpaka ufike hotelini, hata hiyo sababu yenyewe ya kwenda kufanya na mkeo inaweza ikakushinda kwenye kufanya huko. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ngorongoro waliomba Shilingi bilioni 160 tu kujenga barabara inayoendana na mazingira, na walipata kibali UNESCO, mpaka leo hawajapewa fedha hizo. TANAPA walikuwa na hifadhi 16 zenye jumla ya Kilomita za mraba 57,000, wameongezewa hifadhi sita zenye jumla ya Kilomita za mraba 47,000, karibia mara mbili ya eneo lao. Fedha za maendeleo ni hizo hizo, fedha za matumizi ya kawaida ni hizo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea hivyo, alisema mchangiaji mmoja hapa, fedha za utalii ni Non-Tax Revenue. Ni pesa ambazo tunazipata kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu alitujalia kama Rasilimali zetu. Tukiwekeza vizuri TANAPA, Ngorongoro na TAWA, tutapata mapato makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watalii 1,500,000 tunaozungumzia ni wale tu wenye kiu ya kwenda kuona The Eighth Wonder of the World, Serengeti. Akifika pale, zile rasta atakazopiga saa ya kwenda na kurudi, harudi tena. Kwa hiyo, tunaomba sana Bunge lako Tukufu lipitishe azimio na TANAPA itengewe fedha za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, ule utaratibu wa kukusanya fedha kupitia TRA siyo mbaya, lakini utengenezwe utaratibu mzuri wa Revenue Disbursement Automated System wa kurejesha fedha kwa wakati. Wanakusanya fedha nyingi, wanaomba pesa za maendeleo, mtu akae Hazina apeleke kwa muda anaotaka yeye. Kuhusu mifumo ameleezea vizuri sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwamba wakati mwingine inakuwa na first track na mambo mengine mengi ya miradi mikubwa ambayo yanafanya fedha zisiende kwa wakati. Kwa hiyo, tunaliomba sana Bunge lako liazimie fedha ziende kwa wakati. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nne, ni deni la Pamba. Tunaishukuru Serikali imeonesha jitihada kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tano na la mwisho, ni sheria ambazo zimepitwa na wakati, alisema Mheshimiwa Dkt. Kikoyo kuhusu Sheria ya TR, Sheria ya TBS, Sheria ya TRA ya Stamp Duty, tunaiomba Serikali iharakishe mchakato ilete sheria hizi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kutoa hoja.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mezani.
Mheshimiwa Mwneyekiti, kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Wizara hii ya Ujenzi inafanya kazi kubwa sana. Sisi tumefanya ziara na Kamati, iko miradi mikubwa inayosimamiwa na TANROADS. Daraja la Kigongo – Busisi shilingi bilioni 716 fedha za ndani, kazi inaendelea vizuri sana. Iko barabara kubwa ya Kabingo – Kasulu – Manyovu kilometa 260.6 wakandarasi wako site na itafungua sana Mkoa wa Kigoma. Pongezi nyingi Wizara, Dkt. Samia Suluhu Hassan na wenzetu wa TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kule Jimbo la Ukonga na Dar es Salaam, barabara ya BRT Awamu ya Tatu, kuanzia Gongo la Mboto mpaka Kariakoo, mkandarasi yuko site na kazi kubwa ya mradi huu inafanyika, ni kazi ya kupongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia maeneo matatu; eneo la kwanza ni reli katika ukurasa wa 74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali, wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani kulikuwa na vipande viwili vya reli ya SGR vinajengwa; Dar es salaam - Morogoro na Morogoro – Makutupora, lakini bajeti hii inavyowasilishwa hivi sasa tayari vipande vyote vitano vya kuanzia Dar es Salaam mpaka Mwanza kilometa 1219 vina wakandarasi, kilometa 506 Tabora – Kigoma ina mkandarasi yuko site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niseme jambo moja, Tanzania ndio nchi inayojenga reli ya SGR kwa gharama nafuu zaidi kuliko nchi zote Afrika. Wakati Tanzania iko kwenye dola milioni 4.3 kwa kilometa anayefuatia ana dola milioni 5.9 kwa kilometa, ni kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba hii haina eneo la ongezeko la bei, whether kuna inflation hakuna variation, bei iliyosainiwa kwenye mkataba ndio bei atalipwa mkandarasi mpaka mwisho. Hili linatufundisha nini? Linatufundisha kwamba suala kubwa kwenye miradi mikubwa ya ujenzi ni uadilifu na sio njia ya kumpata mkandarasi. Hizi nchi ambazo zinajenga kwa milioni sita, saba zilifanya competitive bidding, lakini Serikali ya Awamu ya Sita kwa njia yao ya single source bado ndio nchi ya Afrika ambayo inajenga reli kwa gharama ya chini zaidi. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.
TAARIFA
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba anachokisema hata ukiangalia BOQ zilizotumika katika kujenga standard gauge bado mkandarasi ameshinda tender chini ya kiwango cha BOQ zilizopitishwa. Kwa hiyo, ninaungana naye kwamba gharama tulizozitumia Tanzania kujenga SGR ni gharama za chini ukilinganisha na mataifa mengi duniani. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, unaipokea taarifa?
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea, Mheshimiwa Kingu una akili nyingi, utafika mbali, una kitu ndani yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme tu amesema vizuri engineers estimate ziko juu kuliko gharama ya reli inayojengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ni eneo la bandari. Nchi yetu imepata kudra ya Mwenyezi Mungu ya kuwa strategically geographically located, kuwa nchi ambayo inahudumia nchi zaidi ya saba ambazo ziko land locked. Bandari yetu imekuwa na miradi mingi ya uboreshaji, Serikali imefanya lazi kubwa, lakini bado kuna suala la efficiency.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo bandari yetu wale wageni wa Dar es Salaam wakifika pale Coco beach usiku wanaona taa kule baharini wanadhani ni majengo, kumbe ni meli zinazosubiri kutia nanga kutokana na masuala madogo tu kiutendaji ya efficiency. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishauri Serikali, yako mambo ambayo kuna watu wamebobea kuliko sisi. Tunapo invest kwenye miradi mikubwa masuala ya operations ni vema tukawaacha watu wenye tija kubwa ya operation, tija kubwa ya investment ili bandari iwe efficient. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisemea reli ya SGR; reli ya SGR ikikamilika itahitaji mzigo mkubwa sana wa kupeleka Mwanza, Kigoma na nchi za Jirani na itahitaji mzigo mkubwa sana wa kuja bandarini na bila kuwa na efficient port tutatkuwa tumefanya kazi bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo matatu; jambo la kwanza ambalo linatutatiza sana Watanzania ni ujuaji, yaani tunakuwa wataalamu kuliko wataalamu wenyewe kwenye baadhi ya mambo ya maamuzi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni hofu; yaani mtu anakuwa na hofu ya jambo ambalo hajawahi kuliona na jambo la tatu ni imani. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuwe na imani na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, itupeleke kwenye uendeshaji wa bandari ambayo tija yake ndiyo itakuja kujenga shule, barabara, elimu na afya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kudra ya biashara Mwenyezi Mungu hajaijalia. Tufanye yale ambayo tunaweza kuyafanya kwa ubora zaidi lakini yale mengine ambayo yanafanywa na private sector, tuwaachie private sector.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Catherine Magige.
TAARIFA
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mchangiaji anechangia kuwa bandari kubwa duniani ya Singapore inaendeshwa na sekta binafsi pamoja na Serikali na ndio tegemeo la nchi hiyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, taarifa unapokea?
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea mwanangu Catherine, hii ndio inaitwa beauty of brains, mwanangu uko vizuri. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni ATCL; Shirika la Ndege la ATCL lilipotoka na lilipo sasa ni kazi kubwa sana ambayo Serikali imefanya. Shirika limetoka kwenye ndege moja leo tuna ndege 11. Shirika limetoka kwenye mapato ya bilioni 23 leo tuna mapato ya bilioni 254; Shirika hili linafaida nyingi. Leo Babu Tale enzi hizo yuko Tiptop Connection tunakuja na ndege hapa Dodoma nauli shilingi milioni moja. Leo kuna flight tatu zinakuja Dodoma, leo kuna flight inakwenda Mpanda, watalii waliokuwa wanakwenda Mbunga ya Katavi walikuwa wanalazimika kukodi ndge leo wanakwenda kwa commercial flight. Shirika hili lina faida ya biashara, faida ya utalii, limeifungua nchi, linaitangaza nchi. Leo wapo Watanzania na wageni wanaokwenda kupata matibabu India, watu wanakwenda China wanapata direct flight kutoka nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisoma vitabu vyake vya hesabu, sasa hapa ni eneo la kuwa makini, utasoma vitabu vya hesabu utaambiwa kuna hasara. Ni kweli? Ndio kuna hasara, hasara ni nini? Hasara ni revenue ukiondoa expenditure ndio unapata hasara. Kwa nini kuna hasara? Kuna hasara kwa sababu shirika hili linazo changamoto nyingi. Moja kati ya changamoto ni kukodisha ndege kutoka TGFA ambalo Serikali imeliona, Rais amelitolea maelekezo, Kamati yetu sisi tumekwishatoa mapendekezo hapa Bungeni na tukaazimia na Serikali inalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua zile lease expenses za ATCL ukaweka na zile maintenance reserve na interest za yale madeni, yuko Mbunge mmoja hapa jana ameomba Serikali iendelee kulipa yale madeni. Kwa gharama ya mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya bilioni 89 zimetumika kwenye maeneo haya. Ukisema uondoshe zile gharama maana yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022 unaona hasara ya bilioni 35 kuna faida ya bilioni 54 kwenye Shirika hilo, tuwatie moyo. Mwenyekiti, wa Bodi Profesa Neema Mori anafanya kazi kubwa mwanamama huyu na wamesema hapa kwenye swali leo asubuhi wakina mama wakipewa nafasi hizi wanafanya kazi nzuri. Engineer Matindi na wenzake jana wametuletea hapa marubani. Shirika hili ni moja kati ya mashirika Afrika yenye watumishi ambao ni wazawa wa nchi zao. Tunao marubani wanawake, wako ma-cabin crew wazuri walikuja hapa ningewataja majina, lakini nitapata tabu nyumbani, lakini wanafanya kazi nzuri, tuwapongeze na tuwatie moyo shirika hili linakwenda kuifungua nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya ya kibiashara ni vema tunavyoyafanyia analysis, tuyafanyie analysis kwenye uwanda mpana zaidi kuliko kuangalia items chache kwenye financial statements ambazo zinaweza zikakatisha tamaa watu wanaolitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini Serikali kwenye bajeti hii imesema inanunua ndege nne mpya. Ndege hizi zikija na hizi zilizopo na matatizo haya yakitatuliwa, matatizo ya Covid yamekwisha, shirika hili linakwenda kuingiza faida na kuwa shirika kubwa sana hapa nchini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, ahsante sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nusu dakika niseme tu kwamba hata hiyo mikataba ya kukodisha ndege ni mikataba ile ambayo inakwenda kwa style ile ya Mandonga. Ndege ikiruka inalipa, ndege isiporuka inalipa. Kwa hiyo, kipindi cha Covid wakati ndege ziko chini, zilikuwa zinaingiza hasara kwa matumizi makubwa ya lease wakati mapato ya tiketi na usafiri yalikuwa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana naunga mkono hoja, naipongeza Wizara hii, niwatie moyo waende wakatekeleze majukumu yao. Nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hoja iliyoko mezani.
Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa kuomba kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye mambo mawili; jambo la kwanza, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uongozi wake anafanya mambo kwa uwazi na kushirikisha Watanzania wote na Bunge lako hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bandari Sura ya 166 ya mwaka 2004 kifungu cha 12(1)(b) na kifungu cha 5(e) kinaipa mamlaka Mamlaka ya Bandari kuingia kwenye mikataba ya upangishaji na uendeshaji. Kama Serikali ingeamua kufanya matakwa ya kisheria leo azimio hili lisingekuja Bungeni, lakini Mheshimiwa Rais kwa busara yake na kwa uongozi wake wa uwazi ameamua kuchukua njia ambayo inaonekana ni ndefu, lakini ni njia shirikishi leo tuko hapa tunajadali mkataba ama makubaliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya uwekezaji wa bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili amesema Mheshimiwa Reuben Kwagilwa ni uhuru wa kujieleza kwenye Taifa letu. Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa uhuru mpana sana wa kujieleza. Watu wanasema mpaka wanavuka mipaka, lakini nikuthibitishie wanayosema maneno hayo ni wananchi wetu na sisi ni viongozi wa watu lazima tuwasikilize katika kuelekea kwenye maamuzi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya azimio hili kuletwa Bungeni na wewe kuilete kwenye Kamati ya Pamoja inayoundwa na Kamati zetu mbili, mijadala imekuwa ni mingi. Mijadala ni afya kwa Taifa letu lakini lazima tuseme, wako watu ambao walikuwa wana nia njema ya kutaka kuelemishwa, lakini lazima tuseme vilevile wako watu wanaopotosha jitihada nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuleta maendeleo ya uchumi katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze wanasiasa wakubwa wa nchi hii wakiwemo wa upinzani ambao walitoa maoni yao ya haki na hawakutumia fursa ya kupotosha umma juu ya azimio la makubaliano haya yalioko Bungeni. Maneno mengi yaliyosemwa amesema hapa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kakoso, ambao sisi kwenye Kamati yetu ya Pamoja tumepokea maoni ya wananchi wengi, pamoja na yale maoni yalitoka kwenye maeneo ya mitandao ya kijamii yalionyesha kuna hofu kubwa baina ya Watanzania. Hofu yao iko kwenye maeneo mengi, yakiwemo watu wana hofu ya ajira za Watanzania, wananchi wana hofu ya ardhi yetu, wananchi wana hofu ya mapato, wananchi wana hofu ya ukomo, wananchi wana hofu ya usalama wa bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu, azimio lililoko mezani mbele yetu ni makubaliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai na si mkataba wa aina yoyote wa uwekezaji, uendeshaji wala ubia wa bandari. Naomba niseme hili na kaka yangu Kitila Mkumbo naomba na yeye vilevile nimshauri, ni ngumu sana na kwa nia njema kabisa kwa mtu asiyekuwa na taaluma ya sheria kutofautisha baina ya a contract and an agreement. Kwa lugha ya Kiingereza cha kawaida inaonekana ni nyaraka zinazofanana, lakini kilichopo mbele yetu ni makubaliano yanayojenga msingi wa Serikali kwenda kutengeneza mikataba ambayo ndio itakuwa na utaratibu wa uwekezaji baina ya Host Government Agreement na concession agreement za project moja moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wengine elimu zetu za kwanza hazikuwa sheria, mimi nilisoma Electronic Science and Communication, nilienda kuongeza ujuzi huo tu katika nia ya kujaribu kufahamu nyaraka hizi unapozisoma kwa lugha ya kawaida inawezekana ikakupotosha ama mtu akakupotosha kwa makusudi. Zipo clip zinatembea za mwanasheria mmoja ukisikiliza lafudhi yake utajua nchi anayotokea, nchi ambayo tunashindana nayo kwenye shughuli hizi za bandari na ukisikiliza kwa makini hata usomaji wake anasoma kipengele kwa kukikatisha kipande ambacho anajua anaweza akapotosha umma kwa wale ambao hawajui legal interpretation ya kifungu kile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini naomba niseme Kamati imetoa maoni na Wabunge wengi waliochangia wametoa maoni; Serikali inapoenda kutengeneza Host Government Agreements na inakwenda kutengeneza mikataba ya mradi mmoja mmoja itazingatia maeneo yote ya hofu za wananchi mliyoyataja pale juu kama Kamati ilivyopendekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, liko eneo naomba niseme na niwathibitishie Watanzania katika kipindi Bunge lina Spika mbobevu wa sheria ni kipindi hiki. Spika Dkt. Tulia Ackson Mwansasu ni Mwanasheria mbobevu. Wale wasiofuata historia amewahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndiyo kipindi pekee usingeweza kuleta jambo lenye matatizo likaingia kwenye floor ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini naliomba Bunge kazi iliyoko mbele yetu ya azimio la makubaliano haya, ni kazi uliyoitaja kwa mujibu wa kanuni fasili ya 107 na fasili ya 111 kama inavyotohoa ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia makubaliano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai ili kutengeneza msingi wa Serikali kwenda kutengeneza mikataba ya Host Government Agreements na Concession Agreements ambazo ndiyo zitajenga msingi mzima wa aina ya uwekezaji. Hapa hatuna ubia, hapa hatuna partnership, hapa hatuna uendeshaji, yote hayo yataelekezwa kwenye mikataba ile ambayo Serikali itaenda kuandika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ambalo nataka kulisema kwenye sheria niwaombe Waheshimiwa Wabunge na utatuongoza. Bunge linafanya kazi yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tusijiingize kwenye kazi ya Serikali ya kuwa waandishi wa mikataba tutajiondolea wajibu wetu wa kuisimamia Serikali pale ambapo Serikali itakuwa imekosea. Najua ni matamanio na ni mihemko ya kuona kwamba Bunge hili kila kinachofanywa na Serikali, kila mkataba uletwe, siyo utaratibu wa kikatiba na wewe utatuongoza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwaambia umma wa Watanzania maana matatizo yote ya bandari yameelezwa na wengi, wapo wanaochangia ambao hawalitakii mema Taifa letu. Mchakato wa maendeleo siyo mchakato rahisi, amesema Mheshimiwa Tauhida hata maendeleo yako binafsi ametaja marafiki, ametaja majirani hata ndugu zako wenyewe wanaweza wakawa wanapinga maendeleo yako binafsi, lakini wako washindani wetu wa kiuchumi, wako washindani wa wenzetu tunaoingia nao kwenye makubaliano haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini wako wengine ni clout chasers tu kwenye mitandao; clout chasers ni mtu anayetaka kupata na umaarufu, yuko mtu mmoja anaheshimika sana anaandika maandiko mengi juzi ameandika haiwezekani ukampa mtu bandari zote hiyo ni sole proprietorship. Hivi jamani hata ku-google tunashindwa? Maana ya sole proprietorship ni kumpa mtu bandari zote? Lakini ni mtu anaandika kwa kutafuta fame na watu wanamfuata wakimsikiliza. Lazima Bunge hili litoe uongozi na litoe ufafanuzi wa maeneo haya ili wananchi wetu wafahamu kabisa tuko hapa kwa ridhaa ya Watanzania. Tunaanza vikao vyetu kwa dua, tumeapa hapa kwa imani za dini zetu. Tunayoyafanya hapa yanahesabu kwa wananchi, lakini yanahesabu kwa Mungu wetu huko mbele ya haki. Tunafanya kwa uadilifu wa hali ya juu na wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nina maombi matatu; ombil la kwanza,...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30 malizia kengele imeshalia.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, ombi la kwanza niliombe Bunge lako liendelee kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mipango yake mema ya kujenga uchumi imara wa nchi yetu. (Makofi)
Ombi la pili, kuwaomba wananchi kuendelea kutuamini kwamba Wabunge wao wataendelea kusimamia maslahi yao kwenye maeneo yote katika kuishauri na kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi la tatu Serikali iendelee kutoa elimu kwa umma ili kuondoa hofu na izingatie maoni ya Kamati na maoni ya Wabunge katika kutengeneza mikataba mizuri yenye tija kwa Taifa letu na kulinda maslahi ya Taifa hili na wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana dada yetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu na wenzake wote kwa nafasi na fursa waliyoipata kutumikia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitauelekeza kwenye maeneo matatu lakini kwanza ni kwenye Jiji la Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam lina historia ndefu kuanzia mwaka 1920 lililopata hadhi ya kuwa mji mpaka lilipokuwa Manispaa ya Dar es Salaam mwaka 1949 na lilipopata hadhi ya kuwa Jiji tarehe 10 Desemba 1961. Mafunzo tuliyoyapata kutoka mwaka 1972 mpaka mwaka 1978 kwenye Madaraka Mikoani na mafunzo tuliyoyapata kuanzia mwaka 1996 mpaka 2000 kwenye Tume ya Jiji, naamini tunaweza kuyatumia kwa upana wake katika kuhakikisha tunatengeneza mbinu bora zaidi ya kutengeneza mazingira ya uongozi na utawala kwenye Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuishukuru Serikali kwa kuanzisha ama kwa kuipandisha hadhi Manispaa ya Ilala kuwa Jiji la Dar es Salaam. Tunapozungumzia masuala ya majiji, tunazungumzia maisha ya watu na makazi kwa maana ya urbanization, lakini niseme tu kwamba Dar es Salaam kwa kipindi kirefu imekuwa ikiendeshwa bila master plan. Master plan ya mwisho iliandikwa mwaka 1979 na kwa bahati mbaya hizi master plan huwa zinatakiwa kuhuishwa kila baada ya miaka mitano. Hata hivyo, master plan hii ilikuja kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali mwaka 1984 miaka mitano muda ambao ulitakiwa master plan hii ihuishwe lakini tokea wakati huo jiji hili limekosa master plan. Naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwamba mwezi Juni, 2020 katika Gazeti la Serikali tumetangaziwa master plan ya Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumzia master plan ya Jiji la Dar es Salaam tunazungumzia Mkoa mzima wa Dar es salaam, lakini tunazungumzia wilaya za jirani ambazo kutokana na ongezeko la makazi, sasa zimeungana na Jiji la Dar es Salaam. Wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga, zote sasa zimeungana na Jiji la Dar es Salaam. Sasa tumepata Jiji pale kwenye Manispaa ya Ilala imekuwa Jiji la Dar es Salaa lakini juzi tumeona Manispaa ya Temeke nayo imeomba na ina vigezo vya kuwa jiji naamini Kinondoni nayo itafika wataomba jiji na naamini kuna siku Ubungo nao wataomba jiji, tutakuwa na majiji mengi. Dhana hasa ya kuwa na jiji ni ya kupata mamlaka yenye uwezo wa kusimamia master plan hii ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, yuko Mheshimiwa Mbunge hapa alichangia kwenye mpango wenzetu kwenye majiji mengine wamewahi kutafuta namna bora zaidi ya kuhakikisha majiji haya yanakuwa na miundombinu ya uhakika na uongozi ambao unaweza kusaidia maisha ya wakazi wa jiji lile kuwa maisha yanayoendana na maeneo mengine. Ziko nchi zimetengeneza Wizara za masuala ya jiji, ziko nchi zimetengeneza mamlaka ya kusimamia jiji. Niombe Serikali iiangalie Dar es Salaam na maeneo yanayozunguka maana jiji hili ndiyo linazalisha zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya nchi yetu iweze kutengeneza mfumo ambao utasaidia kuboresha makazi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zungu hapa amesema, leo Dar es Salaam tunavyozungumza mvua zimenyesha, Dar es Salaam haipitiki, maisha ya wananchi yamekuwa ya tabu. Leo mtu kutoka kule Mzinga Magore, Bomba Mbili Majohe, Mpemba Majohe, Mkolemba anatumia zaidi ya shilingi 1,000 kupanda bajaji imfikishe kwenye eneo la kupata usafiri kwenda mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitaungana na wenzangu kuendelea kuisii Serikali iangalie umuhimu wa Mradi wa Dar es Salaam wa Metropolitan Development Project (DMDP II). Nami niseme tu pamoja na kuungana na wenzangu kwamba tunapozungumza kwenye bajeti ya TAMISEMI, dada yetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu ni mchapakazi, hilo hatuna shaka na ana Manaibu Waziri wazuri lakini wenzetu hawa ni watumiaji wa bajeti kama sisi wengine tujipange vizuri kwenye kuishauri Serikali jinsi ya kupata fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha na bajeti kuu ya Taifa ili miundombinu ya Dar es Salaam iweze kuboreka, wananchi wale waendelee kuzalisha uchumi na mapato ya Taifa hili yazidi kuboreka kupitia miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge katika kipindi cha kampeni na katika michango yetu mingi humu ndani tunasema kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya afya, elimu na sekta nyingine zinazosimamiwa na Wizara ya TAMISEMI. Zimejengwa zahanati nyingi, vituo vya afya vingi, hospitali za wilaya, shule Kongwe zimekarabatiwa na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya inaendelea. Naomba kusema jambo moja hasa katika nyakati hizi ambapo miradi yetu mingi hii inatekelezwa kwa force account, kazi hizi zimefanywa na Wakurugenzi na watendaji wa halmashauri zetu nchi nzima. Sikatai, yawezekana wako watendaji wachache wenye upungufu lakini wako watendaji wengi wanaofanya kazi nzuri ya ujenzi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge na Serikali, nawaomba; Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe wa Kamati za Fedha na Utawala kwenye Halmashauri zetu; na kamati hizi ndiyo Mamlaka ya Nidhamu kwa watumishi wote ndani ya Halmashauri. Nawaomba sana, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Wale watumishi wenye upungufu tuwachukulie hatua kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma na Sheria ya Utumishi wa Umma; na wale wanaofanya vizuri tuwapongeze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusimbebeshe Waziri wa TAMISEMI mzigo wa kuwa disciplinary authoriry ya mpaka Mtendaji wa Kata majukumu ambayo ni ya kwetu kule Halmashauri. Tusigueze Bunge hili ikawa ni sehemu ya kuja kusulubu watu ambao bahati mbaya wengine hawana uwezo wa kuja kujitetea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iendelee kusimamia nidhamu ya watumishi, lakini na sisi tuwaangalie tuwaangalie wenzetu amabo ni wadau wenzetu…
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
T A A R I F A
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa msemaji, lakini kwanza nampongeza kwa alivyoanza. Ila naomba amalizie kwa kusema Dar es Salaam isiwe mamlaka, iwe na Wizara ya kuiendesha Dar es Salaam. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Sasa unaipokea hiyo taarifa ambayo imekuja kwa namna ya wazo jipya! (Kicheko)
MHE. JERRY W. SILAA Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili; na ametujenga, ndiyo maana nikasema iko Miji ilichukua mbinu tofauti hili Serikali iangalie maeneo haya, kwa maana ya Wizara, kama ni Dar es Salaam Metropolitan Authority ili tupate mamlaka nzuri ya kusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hoja iliyopo mezani ya bajeti ya Serikali ya trilioni 44.38. Kwanza nianze kwa pongezi kwa bajeti hii ambayo imeenda kutoa majibu kwenye maeneo mengi. Vilevile naomba niungane na wenzangu kuipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa ya uchumi. Uchumi wa nchi yetu umepanda kutoka dola bilioni 69.9 mpaka dola bilioni 85.4. Mapato ya Serikali yamezidi kukua na hii imepelekea nchi yetu kupata rating za juu kwa kampuni zinazoheshimika duniani za Fitch Writing na Moody’s Investors Service.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu, kampuni kama hizi ni sawa na timu zetu zinavyopata faraja, zinapopata rating ya FIFA ama rating ya CAF. Huku duniani huwezi kufanya mwenyewe ukajipa viwango mwenyewe, kwa hiyo kwa rating hizi za kampuni hizi yanayoheshimika duniani nchi yetu imeongezeka viwango vya kukopesheka nani pongeze kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, uwezo mkubwa wa Serikali katika ukusanyaji wa mapato umeiwezesha Serikali kuwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi ya kimkakati na miradi mikubwa. Kwa mfano Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere tumeoneshwa hapa inatekelezwa kwa asilimia 86 na inakaribia kukamilika, ujenzi wa SGR unaendelea bila kukoma vipande vyote vina wakandarasi, Daraja la Kigongo – Busisi liko katika hatua nzuri na litakamilika kwa muda uliopangwa, grid za umeme zinaendelea kusambazwa nchi nzima. Ni kazi kubwa kwenye miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya kati pia. Sisi kule Dar es Salaam kuna Bwawa la Kidunda ambalo litasambaza maji Dar es Salaam ambao inaenda ku-complement ile miradi ya maji usambazaji wa maji ambayo hata kwenye Jimbo la Ukonga ipo. Upo mradi wa mwendokasi awamu ya tatu Gongo la Mboto - Kariakoo. Jimbo la Ukonga ni wanufaika na unajengwa kwa kasi kubwa. Serikali pia haijasimamisha hata mradi mmoja ile miradi midogo, madarasa yanajengwa, vituo vya afya vinajengwa, zahanati zinajengwa na hii ni pongezi kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niongelee maeneo machache. Kwanza nikuendelea kuishauri Serikali kuongeza wigo mpana wa ukusanyaji wa kodi. Tumeoneshwa hapa kwenye hotuba, nchi hii watu wenye TIN ni watu milioi 4.45, na hizi ni TIN zinazo-include zile leseni na wale wanaolipa PAYE kwenye mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TIN za biashara zimekomea milioni 1.641 na tumeambiwa hapa katika hizi TIN za biashara asilimia 80 ya makusanyo inatoka kwenye TIN asilimia 20; yaani watu kama laki nne ndio wanatuendeshea nchi kwenye makusanyo haya ya takribani trilioni 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Serikali iendelee kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na mifumo hii, nimemsikia Mbunge mmoja hapa nadhani kwenye mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha, aliongelea mfano wa Estonia. Estonia ni nchi ambayo imeweza kuwa na central ledger ambayo shughuli zote za kiuchumi na kijamii ziko kwenye eneo moja. Hii inasaidia Serikali kuweza ku-monitor shughuli za wananchi ili kuweza kuwa na utaratibu mzuri zaidi wa ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlimsikia hapa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, leo mtu ana-export mahindi lakini hasomeki sehemu yoyote. Lakini leo mfanyakazi mwenye threshold inayozidi 270,000 na kwenye mapendekezo yao 370,000 analipa PAYE kwenye mshahara wake. Leo kuna mtu anasafirisha mahindi tani kwa tani halipi kodi. Leo kuna mtu ana mifugo maelfu kwa maelfu halipi kodi. Mimi nadhani Serikali iendelee kuboresha mifumo lakini iendelee kwenye kulenga kuwa na central ledger, maana kila mtu anaandika mfumo wake; na ndiyo inakuja hoja ya mifumo ya kusomana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Bashe amekuwa na mfumo wake anagawa pembejeo, lakini mfumo ule hauwezi kwenda kumsoma ni mkulima yupi amepata pembejeo kiasi gani na leo mahindi yake ameuza wapi na anaingiza kiasi gani kwenye Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ipo mifumo mingine kwa mfano Mfumo wa ETS. Kila mtu anakubaliana na mimi na takwimu zipo, kwamba tangu ufungwe ETS makusanyo ya kodi yameongezeka, zile exercise duty zinazotozwa kwenye biashara zinazozalishwa nchini zimeongezeka. Na SICPA ni moja ya kampuni reputable duniani ambayo si tu inafanya mifumo ya kodi lakini pia imeaminika kwenye printing hasa ya vitu kama noti au fedha kwenye nchi mbalimbali na inafanya kazi kwenye nchi nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutakapokuwa na mifumo ya kisasa, na maeneo mengine Wizara ya Fedha ama Serikali isione tabu; Mheshimiwa Rais alishawahi kusema, nadhani alipokuwa akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mwaka jana, kwenye maeneo ambayo tunakwama sisi ndani tusipate tabu kutafuta utaalam wa nje kwa sababu yako maeneo yanahitaji ubobezi. Mimi naamini tukiwa na mifumo bora zaidi makusanyo yataongezeka kama tulivyoona kwa mfano wa ETS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo ambalo mimi nitaomba kutoa ushauri kwa Serikali, na ninadhani kama sitopata majibu ya msingi tutakutana kwenye Finance Bill. Serikali inapendekeza kufuta kodi ya VAT kwenye gaming odds na gaming software. Iliwahi kuwekwa huko nyuma kwenye Section 64 ya Value Added Tax Act Cap.149 ya 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia gaming odds maana yake ni unazungumzia michezo yote ya kubahatisha. Bidhaa pekee inauzwa ni gaming odds. Serikali inapotaka kuchukua gaming odds ikaisamehe VAT, na ukizingatia gaming odds ina michezo mingi ya kubahatisha ni kampuni za kimataifa ambayo Serikali na Bunge hili liliweka ile Section 64 ili kampuni zile zipate representative hapa nchini waende wakalipe VAT; na ndiyo kodi pekee inakusanywa kwenye eneo hili. Ukisha iondoa, ukachukua gaming odds ukaipeleka kwenye jedwali la kusamehewa, ambao kule kumejaa kilimo, mifugo na maeneo mengine ya uzalishaji, maana yake unaenda kujikuta kwenye shughuli hii ya michezo ya kubahatisha kwenye kampuni za nje hatutakusanya hata shilingi moja kwa sababu wale wanaofanya michezo hiyo ya kimataifa ni non-resident kwenye tax base yetu. Kwa hiyo, mimi ningependa kusema wazi kabisa siliungi mkono na ninadhani nitapata majibu ama tutakutana kwenye finance bill.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa uchache kabisa, siku ya jumamosi tarehe 17 tulikuwa pale Mlimani City, Mheshimiwa Rais alipokea Hundi ya shilingi bilioni 45.5 kutoka benki ya NMB. Huwezi kuzungumzia benki ya NMB bila kuzungumzia walipa kodi wakubwa, benki hii kwa mwaka wa fedha huu walitoa gawio, wamelipa kodi shilingi bilioni 453.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukaizungumzia benki ya NMB bila kuzungumzia mkakati wa Serikali ulioanza kwenye awamu ya tatu ya ubinafsishaji. Tuliwahi kuuza hisa zetu Label bank mwaka 2004. Jambo hili lilikuwa na kelele kubwa; bodi ya NMB iligoma, ilipelekea Serikali kuvunja bodi hiyo ya Wakurugenzi ya NMB. Lakini tangu uwekezaji ule ufanyike benki imezidi kuboreka, mifumo imeimarika na gawio limeongezeka. Tangu gawio la shilingi bilioni nne mwaka 2009 mpaka gawio la shilingi bilioni 45.9. Maana yake nini; Serikali hailipi mishahara NMB, Serikali hailipi umeme NMB, Serikali imeenda kupata gawio la bilioni 45.5 na kodi ya bilioni 453.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuendeleza nchi hii bila kushirikiana na sekta binafsi, na mimi niombe Serikali, tulipitisha hapa Azimio la IGA ya bandari yetu ya Tanzania, kelele zimekuwa ni nyingi. Nishukuru Serikali imeendelea kutoa elimu, na elimu kubwa ni kwamba IGA sio mkataba wa utekelezaji na yeyote anayeenda nje ya hapo ana nia yake ovu maana wa kuelewa ameshaanza kuelewa. IGA ni makubaliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya uwekezaji utakaoenda kufanyika kwenye bandari zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba ya kwenda kutekeleza miradi (Host Government Agreement) na zile concession agreement bado hazijaingiwa na concern zote za wananchi Serikali iliahidi hapa Bungeni na inaendelea kuahidi, na juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema, watazi-consider kwenye kuingia mikataba yenye maslahi na Taifa. Mimi naamini kabisa ufanisi wa bandari ukiongezeka na takwimu zipo uchumi wa Taifa utakua, forodha itaongezeka, kilimo kitachachuka, sekta zote za uchumi zitaenda kuboreka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaiomba Serikali, kama vile Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa alivyokubali kupigiwa kelele mwaka ule 2004, leo tunapokea Hundi pale Mlimani City jina lake halikutajwa hata mara tatu. Niombe Serikali ikubali ushauri, isikilize wananchi lakini wakati mwingine isikubali kuyumbishwa na watu wenye nia zao za kuitaka nchi yetu isiendelee kiuchumi; ikubaliane na hizo hoja za msingi za kuendeleza Taifa tuwe na uwekezaji na kushirikisha sekta binafsi kwenye maeneo ambayo wenzetu wamebobea tupate uendeshaji mzuri wa bandari. Miaka ijayo tutakuja hapa kupongeza na wakati wote nawajua binadamu hata wale walioshiriki jambo hilo hawatatajwa, sifa zitakwenda kwa wale watakaokuwepo wakati huo lakini ndiyo kazi ya viongozi kuweza kusimamia uongozi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda mwisho, niombe Serikali iendelee kushirikiana na sekta binafsi, lakini kama nilivyosema iendelee kuboresha mifumo ya nchi yetu. Mifumo hii ikiwa bora kero zote tunazozisikia hata zikiwemo hizi za mahindi zilizotajwa hapa Bungeni na Mheshimiwa Mwenisongole na kupata majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo zitafika wakati zitakwisha na kila mtu atachangia katika uchumi wa Taifa lake kwa kadri anavyochochea kwenye uchumi wa Taifa lake. Isiwezekane kukuta mfanyakazi analipa kodi kwenye mshara wake kwenye threshold ndogo ya laki mbili na elfu sabini analipa kodi lakini kuna mtu mwingine anafanya biashara kubwa zaidi na hasomeki kwenye uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia katika hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu, kwanza kipekee kuipongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso; Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi na watendaji wote wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu, Eng. Sanga na mwanamama machachari Naibu Katibu Mkuu, Eng. Nadhifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuseme kwenye Wizara hii kazi kubwa imefanyika. Serikali imefanya kazi kubwa ya kufanya utambazaji wa maji kwenye nchi yetu. Na wote mmesikia kwenye hotuba kwamba malengo ya kusambaza maji vijijini kwa asilimia 85 kufikia 2025 mpaka kufikia mwezi Machi tayari asilimia 72.3 maji yamesambazwa. Lakini malengo ya kusambaza maji mijini tumefikia asilimia 84; tunaipongeza sana Wizara ya Maji kwa kazi kubwa waliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niipongeze Serikali, zaidi ya shilingi bilioni 200 zimewekezwa katika kazi ya kusambaza maji safi na salama kwenye Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini iko miradi mingi mikubwa; upo ule mradi wa Arusha, zaidi ya shilingi bilioni 520; upo Mradi mkubwa wa Tabora – Igunga – Nzega, zaidi ya bilioni 600; lakini iko miradi ile ya miji 28 ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 500, kazi kubwa sana imefanyika kwenye sekta ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye wanufaikaji wa miradi hii na Jimbo la Ukonga ni wanufaikaji. Sisi kwa miaka yote tulikuwa tukipata maji toka Ruvu chini, maji ambayo yalikuwa mpaka yapite katikati ya Jiji la Dar es Salaam yapandishe Mlima wa Magereza – pale Magereza kulikuwa na mashine ya maji – yaje mpaka Gongo la Mboto – pale Gongo la Mboto kulikuwa na mashine ya maji, na mtafahamu Jimbo la Ukonga lina asili ya Milima ya Pugu mpaka Milima ya Kisarawe kwa kaka yangu, Mheshimiwa Selemani Jafo. Na kwa kipindi kirefu tokea miaka tisini hatukuwahi kupata maji safi na salama ya bomba. Katika uwekezaji huu wa Serikali, Mradi wa Maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini imeboreshwa na uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maji haya yalipofika Kibamba ukabuniwa mradi mwingine ukatoa maji Kibamba mpaka Kisarawe na Kisarawe imejengwa njia ya maji mpaka Pugu limejengwa tanki kubwa la lita milioni mbili na tayari mradi ule umezinduliwa, na hivi ninavyozungumza Jimbo la Ukonga linapata maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Ukonga, Mheshimiwa Waziri alifika, alikuja na Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais kuzindua mradi ule; tunawashukuru sana. Na DAWASA kupitia Mhandisi Cyprian Lwemeja, wanafanya kazi kubwa ya kuendelea kusambaza maji yale kwa uwezo wao wa ndani. Tayari kazi ya transmission imekamilika na hivi wmaeshapata fedha wanaanza kazi ya distribution. Sisi tunaamini katika malengo ya 2025 tutakuwa wa kwanza kuyafikia kabla ya wakati na maji yatasambaa kwenye Jimbo la Ukonga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, mpaka kufikia mwezi huu Aprili, fedha za maendeleo zilizopokelewa ni asilimia 54.1. Katika fedha zilizopangwa za Mwaka wa Fedha 2020/2021 mpaka kufikia mwezi huu wa Aprili ni asilimia 54.1 tu ndiyo zimepokelewa na Wizara. Imebaki miezi miwili, siamini kwamba kufikia mwisho wa bajeti hii Wizara ya Maji itakuwa imepata fedha zote za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na Wizara hii isipopata fedha maana yake maombi yote uliyoyasikia hapa Waheshimiwa Wabunge wakiyaomba, miradi yote ambayo umeisikia inaendelea kwenye majimbo yote ndani ya Bunge hili haitakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu wa Wizara ya Maji ni waombaji kama sisi tunavyoomba, inapokuja hapa bajeti kuu ya Serikali naomba tusimame tuseme Wizara hii ipatiwe fedha za kutosha. Pia isipatiwe tu fedha kwa maana ya kuzitenga kwenye bajeti lakini na fedha zenyewe zipelekwe tena kwa wakati ili miradi ya kuwasambazia maji Watanzania iweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie pia ama kuongezea pale alipochangia Mheshimiwa Anne Kilango Malechela, miradi ya maji hasa vijijini ukiondoa hii ya mijini ambayo inasimamiwa na Mamlaka ni kweli inagharimu fedha nyingi. Niungane na mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango, Wizara ya Maji, RUWASA, Menejimenti ya RUWASA na DG yupo hapa nadhani anasikia, Clement anafanya kazi nzuri kujenga taasisi hii mpya na changa iliyoanzishwa muda mfupi uliopita, mjitahidi mtengeneze mfumo utakaofanya wale akina Ali Mabomba waliokuwa Same waweze kupatikana kusimamia miradi hii nchi nzima. Itakuwa ni kichekesho kutengeneza miradi ya thamani kubwa ya mabilioni ya shilingi lakini kuiacha kwenye mikono ya watu ambao hawana utaalamu, lakini hawana usimamizi wa kitaalamu chini ya taasisi yetu hii ya RUWASA.Ni vyema tukajipange na hili litawezekana kama Wizara hii itakuwa na fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kusisitiza RUWASA kutengeneza utaratibu wa kuwa na wataalam wa kutosha kusimamia miradi lakini nitaendelea kuliomba Bunge lako na tutakutana tena hapa kwenye bajeti kuu ya Serikali kuendelea kuitaka na kuishauri Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maji ili utendaji huu uliotukuka tunaouona wa Waziri wetu Mheshimiwa Jumaa Aweso uweze kwenda kwa vitendo akiwa na fedha za kulipa makandarasi wanaofanya kazi kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja mezani ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba niipongeze sana Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wa Wizara. Lakini kipekee nimpongeze sana Katibu Mkuu wa Wizara hii Mhandisi Balozi Aisha Amour, mama huyu ni msikivu na anafikika na nimpe pole kwa mitihani aliyoipata, Mwenyezi Mungu ampe nguvu aendelee na utendaji wake wa kazi. Wizara hii inafanya kazi nzuri, kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza kidhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa miradi ya miundombinu. Miradi yote mikubwa haijawahi kusimama hata siku moja anatenga fedha za ndani na kwenye safari zake anatafuta fedha za nje, nampongeza sana na tumeambiwa hapa maana wakati mwingine ukipongeza wako watu wanapenda kuhoji. (Makofi)
Tumeambiwa tarehe 25 Mei kule Accra, Ghana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anakwenda kupata tuzo ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank) ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli, tunampongeza sana wanaotaka kujibu wajiandae kujibu kwa kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye hotuba ya Waziri ameeleza kazi kubwa Serikali inayoifanya kwenye upanuzi wa bandari zetu nchini na kule bandari kazi kubwa inafanyika. Tunaipongeza Serikali, tunampongeza Mkurugenzi wa Bandari Ndugu Eric Hamisi, niwaombe tuendelee kuiunga Serikali mkono.
Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Machi wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2021 alitoa agizo muhimu sana ambalo Kamati zako ya Public Accounts Committee na Public Investment Committee imekuwa ikiishauri Serikali kuomba kuisaidia Air Tanzania Corporation Limited. Mheshimiwa Rais aliagiza zile ndege zote zinazomilikiwa na Tanzania Government Flight Agency (TGFA) umiliki wake urejeshwe kwenye Shirika la Ndege la ATC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, agizo hili linakwenda kuwa na mchango chanya kwenye mizania ya Shirika hili, mizania ambayo kwa vipindi vichache vya miaka ya fedha imekuwa ikipata negative equity ambapo ukienda kwenye notes zake kule kwenye plan tern equipment’s walikuwa na plans and equipment’s zenye thamani yenye shilingi bilioni 119 tu. Ndege hizi 11 zina thamani ya shilingi trilioni 1,473.2 na ndege hizi zikihamishiwa ATC mizania yake sasa inakwenda kuwa chanya. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais tunaamini sasa Serikali itakwenda kusaidia yale madeni hasa ya kurithi ya Aerovista na mengine, madeni yale ya kukodi ndege toka TGFA ambayo ni kampuni dada ama kampuni kaka zote zinamilikiwa na Watanzania na tunategemea, kuanzia mwaka wa fedha unaofuata ambao Audit yake itakuja mwaka 2024 vitabu hivi vitakaa vizuri sana; Engineer Matindi, Mwenyekiti wa Bodi Profesa Morick tunawatakia kila la kheri tutaendelea kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa imekuwa ikifanyika kwenye Shirika la Reli Tanzania, tumekwenda juzi kuzindua Lot III ya awamu ya kwanza kutoka Makutupora kwenda Tabora, tunaomba tuendelee kuwaunga mkono na Masanja Kadogosa ama almaarufu Engineer Masanja Kadogosa aendelee kufanya kazi hii na sisi kazi yetu kubwa ni kuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili sitoacha kulisema nililisema na ninasema tena nitaendelea kulisema, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, Watanzania hata viongozi wa Serikali, haya mashirika yanayofanya biashara yakipata faida yanatoa gawio kwa Serikali na gawio hili linakwenda kufanya maendeleo kwa wananchi wetu. Kama yana mapungufu unazo Kamati zako, ni uwanda mzuri zaidi wa kuyakosoa, tukiyakosoa kwenye uwanda wa wazi clip hizi tunazozisema hapa zinatumiwa na competitor wa mashirika haya kwenda kuwachafua kibiashara halafu tunaanza kujiuliza kwa nini Mashirika hayafanyi vizuri.
Mheshimiwa Spika, pale Dar es Salaam tuipongeze Serikali inatekeleza mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili ambayo ina kilometa 19.3 kutoka Mbagala kwa Mheshimiwa Chaurembo inakuja mpaka Kariakoo kwa Mheshimiwa Zungu kutoka pale Kurasini kwa Mheshimiwa Kilave inakwenda mpaka Magomeni kwa Mheshimiwa Tarimba. Mradi ule una mkandarasi wa Lot I na Lot II mwezi Disemba wakati Mheshimiwa Rais amealikwa kuzindua Lot II kuna maneno aliyasema naomba kuyanukuu na ulishatuelekeza jinsi ya kunukuu kauli za viongozi na nimezingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Rais alisema: “Mwezi Juni nadhani nilifanya ziara ndani ya Wilaya ya Temeke, lakini nikapita pia barabara ya BRT na nikakuta ubovu ambao Waziri umeutaja na nikaeleza hatua zichukuliwe na ubovu ule kama viongozi wasingesimama na kusema hapa ni pabovu mkandarasi angeendelea na kutujengea ubovu ule ule. Kwa hiyo, niombe sana viongozi wa Wilaya, Halmashauri mlioko huko muwe macho lakini wakati mwingine nao labda na sisi Serikali tuna tatizo kwa sababu unaweza kukuta mkandarasi mmoja ana kazi nne, tano kwa wakati mmoja. Sinohydro utaikuta kwenye hydropower kule Nyerere, Sinohydro utaikuta kwenye BRT, Sinohydro iko Msalato, Sinohydro iko Maji, Sinohydro iko kule kwenye umeme sasa mkandarasi mmoja maeneo yote hayo lazima atavuruga. Kwa hiyo, mnaotoa tender hizi nanyi muwe makini kuangalia nani yuko tayari kujenga miradi tunayowapa.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri alikuwepo, TANROADS walikuwepo na Sinohydro walikuwepo. Wakati Mheshimiwa Rais anasema nadhani wenzetu mioyoni walikuwa wanasema mama sema haraka umalize kwa sababu sio kazi nne, tano tunakwenda kumpa kazi ya sita.
Mheshimiwa Spika, Sinohydro amepewa mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu toka Gongolamboto mpaka Kariakoo. Mkandarasi huyu ambaye tayari kilometa 2.5 zimetinduka zimeweka ufa kule Mbagala ,mkandarasi huyu asiyelipa wafanyakazi, mkandarasi huyu asiyelipa wazabuni amekwenda kuongezewa kazi nyingine. Kazi hii ya kilometa 23.6 inapatikana ukurasa wa 69 wa Ilani hii ya Uchaguzi, wala haikusema tutajenga mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu na tutampa Sinohydro; ilisema tutakwenda kutatua kero kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ndio Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, amesema hadharani, ameonya, mmekwenda kutoa kazi ile. Mheshimiwa Rais kule Mbagala alisema alikwenda mwezi Juni, akaenda Disemba, hii Nyerere ndio anapita kila siku kwenda kwenye safari zake kwenda kutafuta fedha kwa ajili ya miradi kama hii. Mnakwenda kufanya vitendo vya namna hii.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako hili na wewe ukiwa Spika ndio litakuwa Bunge ambalo limesimamia bajeti hii ambayo inakwenda kututengenezea kero ambayo leo iko Mbagala, iko Temeke inakwenda kurejeshwa tena kwa Gongolamboto na maeneo mengine tutakuwa ni Bunge la namna gani? Mkuu wa Wilaya pale Temeke Jokate Mwegelo alikwenda kusimamia haki za wale wananchi wanaonyanyaswa na wale Wachina, TANROADS wakamuandikia barua usiingilie mikataba hii ya ujenzi inayosimamiwa na TANROADS. Kuna mkataba unaosema mtu asilipe watu? Ndio TANROADS hii, halafu ukisema unaonekana una jambo lako binafsi, jambo gani binafsi? Hatuwezi kuacha watu hawa wakaendelea kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo nilisema hapa na kuna watu walinifikiria vibaya haya mambo ya single source. Single source sio mbaya competitive tender sio mbaya ubaya ni uadilifu wa wale wanaosimamia kazi hizi. Mradi wa mwendokasi awamu ya kwanza kutoka Kimara mpaka Posta umejengwa na STRABAG leo mwaka wa sita, wa saba hata shimo moja halijatokea. Hivi wangempa DRT Phase III Single Source STRABAG kuna mtu angelalamika? Kwa nini wanafanya hivi? Leo nenda pale Arusha mradi wa shilingi bilioni 520 una Lot 13; Lot 12 zimekamilika, Lot moja ya Sinohydro mpaka leo haujakamilika wananchi hawapati maji kwa sababu ya Sinohydro. Vyanzo vya maji vimekamilika matenki yamekamilika ila mtu mmoja anafanyakazi kwa utaratibu anaoona yeye unafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na nimuombe Waziri akija hapa kujibu mimi nitashika shilingi ya mshahara wake, nitashika shilingi ya Fungu la TANROADS ukiwauliza, wanakujibu eti World Bank walitoa letter of no objection, msituletee habari za namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Manunuzi Sura ya 410 ya mwaka 2011 TANROADS ndio procurement entity ndio anaandaa nyaraka za zabuni, ndio anaandaa sifa za mwombaji. Mmetunga mtihani wenyewe, mmempa majibu wenyewe, mmehakikisha ameshinda, Rais ametoa kauli bado mnakwenda kumpa kazi mnataka nchi iende namna gani? Sisi tunakwenda kwenye uchaguzi 2025… (Makofi)
(Hapa Mhe. Jerry W. Silaa alilia)
SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwenye hii Bajeti Kuu na nianze mchango wangu kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa bajeti nzuri. Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Fedha, bajeti hii imeenda kujibu vilio vingi vya Watanzania na niseme naipongeza sana.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kuondosha ada ya kidato cha tano na cha sita kimeenda kujibu vilio vya wananchi wengi. Mimi mwenyewe binafsi yuko kijana mmoja, mjukuu wa mama mmoja maarufu kule tulikokulia, marehemu Kibibi ilikuwa nimlipie ada wiki hii, kwamba kauli hii na mimi mwenyewe hela yangu imepona, naipongeza sana Serikali. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi kwenye kilimo, mifugo na uvuvi inaenda kuwatengenezea Watanzania maeneo mengi zaidi ya kujishughulisha kwenye shughuli zao na sasa tunaenda kupata matokeo chanya kwenye Sekta ya Kilimo, kwenye Sekta ya Mifugo na Sekta ya Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza nitakalolisemea ni eneo la kodi na mimi nimpongeze kidhati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kauli yake aliyoitoa pale Bukoba kwenye ziara yake ya Mkoa wa Kagera. Kauli ile imepokelewa vizuri sana na wafanyabiashara wa nchi hii. Kumekuwa na dhana na tumekuwa tukisema hapa kwamba Serikali kwa kukusanya kodi anajikuta ni mbia asiyechangia mtaji kwenye biashara ya Mtanzania. Kwa hiyo tumekuwa tukiishauri sana Serikali ukusanyaji wao wa kodi, taratibu zao za makusanyo ziwe rafiki na elimu itolewe kwa wafanyabiashara na wasitengeneze dhana ya kugombana na wafanyabishara na kufunga biashara zao. Kauli ile ya Mheshimiwa Rais yuko rafiki yangu mmoja ambaye najua kabisa hata mimi hakunipigia kura mwaka 2020 alinitumia speech ile na akaniandikia Mama Samia Suluhu Hassan amepata kura yangu 2025.
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali, niwaombe sana TRA waende wakatekeleze maagizo yale. Tuliongea hapa, wako wafanyabiashara wadogo hawa presumptive tax regime ambapo naona sasa hapa tena wamewekewa asilimia 3.5 ya turn over. Asilimia 3.5 ya turn over siyo hela ndogo, lakini hawa ndiyo wenye mitaji ya Sh.1,000,0000 au Sh.500,000, unapomwambia aende akanunue mashine ya Sh.500,000 ni ngumu kuweza kutekelezeka. Sasa kama Serikali ni mbia wa kodi ni lini Serikali itaona ni wajibu wake kumpa mtu mashine ya EFD bure ili mashine ile sasa iweze kuweka rekodi za kodi Serikali iweze kupata kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako marekebisho mengi ya kodi ambayo Serikali imeelekeza yafanyike. Nitachangia kwa uchache na nadhani nitachangia vizuri kwenye Finance Bill. Unapoweka withdrawing tax ya asilimia mbili kwenye small scale miners, maana yake unaongeza pale ilipokuwa loyalty na ile inspection charge ya asilimia sita na moja sasa unaenda kwenye asilimia tisa.
Mheshimiwa Spika, as we speak right now dhahabu nyingi inayochimbwa na wale wachimbaji wadogo wale wa kushika na mercury inatoroshwa nchini. Unapoongeza kodi Serikali hamuendi kuongeza mapato mnakwenda kuongeza utoroshaji wa dhahabu na ziko nchi zinanufaika na utoroshaji huo. Mwaka jana hapa iliwekwa withholding tax kama hii kama kwa wakulima, Bunge la mwezi wa Agosti liliiondosha. Sasa niwaombe sana Serikali tusingoje tufanye jambo tupate kilio, tuje tena kubadilisha sheria wakati jambo tunaliona halitatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, muda ni mchache lakini ukichukua turn over za corporates kubwa Tanzania Breweries Limited, Vodacom Tanzania, TIGO ukaangalia na corporates tax wanayolipa ni chini ya hiyo asilimia 3.5. Mwaka huu wa fedha Vodacom ime-declare loss, TIGO wame-declare loss, kwa hiyo hawajalipa corporate tax, unapotaka hawa presumptive tax measure walipe 3.5 percent ya gross huendi kuwatendea haki na nadhani utekelezaji wake utakuwa ni mgumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda niseme tu Serikali niiombe na niishauri iongeze nguvu kwenye communication. Tulikwenda kule Amani Muheza kwa Mheshimiwa MwanaFA tulikuta wale wasafirishaji wa vipepeo wanaathirika na lile katazo la Serikali la kusafirisha wanyama hai nje as if wanyama simba wanafanana na vipepeo. Juzi Serikali ikatoa kauli hapa kauli, nilivyoielewa ni kusaidia wale wa vipepeo na wale wanaoshika mijusi na wanyama wengine wadogo wadogo, lakini kwa sababu haikuwa communicated vizuri ikatengeneza taharuki, Waziri naye alivyopata taharuki akajaa upepo, akafuta lile agizo. Kwa hiyo, wale waliokuwa wanasherehekea maskini wa Mungu wale Conservators wa misitu wa kule Amani ambao wanasaidia kutunza misitu kwa ajili ya vipepeo na wao wamerudi tena kwenye back to square one 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hili la TIN Number, kwa tabia za TRA za ukusanyaji wake wa kodi ukimwambia mwananchi naye apewe TIN Number lazima ataruka kimanga, anajua tunarudi kule kule wanakofanyiwa wafanyabiashara, sasa tutafanyiwa Watanzania wote. Naomba Serikali ifanye communication, ielimishe wananchi na ndio maana Mheshimiwa Twaha amesema ziko nchi zinaita Insurance Number, ziko nchi zinaita Social Security Number, kikubwa Mtanzania leo tunavyozungumza hapa alipo mwenyewe ni mlipakodi. Anaponunua pembejeo ile transaction inatakiwa ilipiwe kodi, anapolipa nauli kwenye daladala, anapopanga chumba, anaponunua chakula zote zile ni transaction za kibiashara ambazo huyu mwananchi angekuwa na namba yake zingeingia kwenye taarifa zake. Tunapoongelea universal worthy insurance ndio atajikuta ametumia kiasi gani kwa mwaka apate bima ya maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa wanaiweka TIN Number limebutuka huko la kwao hilo, kazi yao kwenda kuelimisha wananchi kwamba namba hii ya NIDA ikitumika kuweka miamala yako inakusaidia wewe mwenyewe, kama tunagawa pembejeo za ruzuku tunajua wewe ni mnunuaji mzuri na matumizi yako na kilimo chako upate pembejeo. Sasa naamini Serikali italifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kifupi, niombe mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, niombe na niipongeze Serikali imemwongezea fedha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kukagua matumizi ya Serikali. Imepokea ushauri wa Kamati ya Bunge, imeongeza meno kwa Internal Auditors kusimamia matumizi. Sasa niiombe iendelee kupokea ushauri wa kuweka mifumo ya TEHAMA. Mifumo ya TEHAMA ndio itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali na mifumo hii ya uangalizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nia yangu ni nini? Let the Government be the Government, let corporate be corporate and let the Parliament be Parliament. Huwezi ukaendesha Serikali kama shirika la kibiashara this is not a profit-making organization, yaani leo Kamishna wa Ardhi akopeshwe Prado akitaka kwenda kukagua mgogoro wa ardhi anajiendesha mwenyewe, haitakaa itokee. Tusipende kutengeneza vitu ambavyo vitatengeneza mkwamo kwenye utendaji wa Serikali. Serikali ijiendeshe, matumizi yabanwe, controls ziwepo, mifumo iwepo, lakini uendeshaji wa Serikali ni ngumu kulinganisha na sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kifupi kwenye custom duty, matairi ya bodaboda yameongezwa toka asilimia 10 mpaka asilimia 25. Kule juu wakulima tumewaangalia, wafugaji tumewaangalia, wavuvi tumewaangalia, hebu tuwatambue na hawa bodaboda na wenyewe kama Watanzania na tupunguze kodi kwenye matairi ya bodaboda kwa sababu uendeshaji wa bodaboda sio anasa bali na yenyewe ni ajira kama eneo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, liko eneo Serikali ina-propose kupunguza mikopo ya halmashauri ya asilimia 10, ambayo ni mikopo inayokopesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, eti ibaki asilimia tano. Tunawathamini sana Wamachinga na sisi ni wapiga kura wetu kule mijini, Serikali itafute mahali kwingine fedha ya kujenga miundombinu lakini sio kwa Wamachinga. Mikopo hii asilimia 10 ibaki, hapo ilipo yenyewe haitoshi, kama mnavyogawa pembejeo bure kwa wakulima na sisi wa mjini mikopo hii inasaidia wapiga kura wetu. Hili naomba kushauri na hatutokubali lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naona hotel levy ilikuwa asilimia 20 imekuja asilimia 10 inakwenda asilimia tano. Hotel levy ilikuwa ni suluhu ya wale wanaokimbia VAT asilimia 18, wanakuja kwenye hotel levy na ndio maana ika-balance kwenye asilimia 20, haya ni mapato ya Local Government, naomba tuyaangalie.
Mheshimiwa Spika, vile vile niombe jambo moja property tax ilichukuliwa ikapelekwa TRA haikukusanywa na taarifa ziletwe hapa, haikuwahi kukusanywa effective kama mamlaka za Serikali za Mitaa zinavyokusanya. Mwaka jana wakachukua wakapeleka kwenye LUKU, nyumba ya Masaki inalipa Sh.1,000 kwa mwezi Sh. 12,000 kwa mwaka. Niombe kwenye bajeti hii kodi ya majengo irudishwe kwenye halmashauri, ikirudishwa kwenye halmashauri itengenezwe retention scheme asilimia tano ibaki kwenye mtaa, asilimia tano ibaki kwenye kata, isaidie uendeshaji, isaidie mafunzo, ujenzi wa ofisi, posho za Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji na za Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusitengenezeane fitina ya kisiasa kwa jambo ambalo linawezekana kwa kudhani mishahara ya Madiwani inatakiwa kutoka Serikali Kuu; na kama Serikali haina uwezo basi isijibu suala hilo wakati maeneo mengine wanafanya. Fedha hazikusanywi, hawa viongozi wanatakiwa kuwa ni chachu ya ukusanyaji wa mapato ukisoma Local Government Authority Act na Kanuni za Kudumu za Halmashauri, Madiwani wanapaswa kuwa ni watu wa kuchochea maendeleo na kusimamia shughuli za kijamii kwenye maeneo yao. Waturejeshee kodi ya majengo, watuwekee malengo, mifumo ya kukusanya ipo watuwekee retention scheme. Kuna kata zitanunua magari, zitajenga ofisi za magorofa, zitalipana posho, kuna Kata na Mitaa wananchi wataacha kutozwa Sh.1,000 za barua kwa fedha itakayobaki kwenye maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda la mwisho na sio kwa umuhimu hizi kodi ndogo ndogo mara kwa king’amuzi, mtu kashachoka kashatumika siku nzima, karudi nyumbani anataka kuangalia mpira wake wa Yanga anaambiwa king’amuzi tena kilipiwe na tozo. Niombe sana tutengeneze mifumo ya kodi ambayo ni rafiki inayoweza kukusanyika kirahisi ambayo itasaidia Watanzania wapende kodi na wapende Taifa lao.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuja hapa kuhitimisha hoja yangu, lakini niruhusu niwashukuru kidhati Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 45 wamechangia, Wabunge 40 wamechangia hapa Bungeni na Wabunge watano kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba uniruhusu nitumie fursa hii kumshukuru kidhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini nimsaidie kazi. Ninamwahidi nitafanya kazi kwa uaminifu na kwa moyo na kwa nguvu zangu zote na nitaishi kiapo changu wakati wote kumshauri kwa hekima na uaminifu. Ninamshukuru kwa maagizo na maelekezo na miongozo anayotupatia Wizara ya Ardhi, hasa falsafa yake ya 4Rs na sisi tumejikita zaidi kwenye zile R mbili za mwisho za Reforms and Rebuilding. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niruhusu nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa miongozo yake anayoendelea kutupatia na usimamizi. Ninaomba tena unipe fursa nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa miongozo na usimamizi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Timotheo Mnzava (Mbunge), Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga na Wajumbe wote. Tunawashukuru sana kwa usimamizi wao, ushauri na maelekezo yao. Ninahakika tutazingatia katika utendaji wa kazi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bunge lako mwaka 1995 lilitunga Sheria, Sura Na. 398, Sheria hii imeainisha, kiongozi ni kiongozi mwenyewe, mke au mume wake na watoto chini ya miaka 18. Niruhusu nitumie fursa hii kuishukuru sana familia yangu hasa mke wangu Bi. Mariam Bakar Silaa kwa matunzo yake. Kazi hii inachukua muda mrefu, kule nyumbani hatuonekani, bibi huyu wa Kitanga hodari. Malezi ya mtoto simba yako vizuri, utulivu wa Waziri uko vizuri, mambo ya huduma zote yako sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi ya ardhi ni ngumu, utoke kwenye mgogoro wa ardhi usiku saa tano ukutane na mgogoro wa mwanamke nyumbani, utatembea unaongea mwenyewe kama chizi. Ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru sana na Mwenyezi Mungu amjalie na aendelee kuniombea dua njema. (kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakishukuru Chama changu Cha Mapinduzi, kwani kimenilea toka ngazi ya tawi, Jumuiya ya Umoja wa Vijana, leo nimesimama hapa kama zao la chama hiki. Ninaomba nitumie fursa hii niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Ukonga na leo baadhi yao wako hapa, kwa kunivumilia katika kipindi ambacho ninatumikia Serikali na kuendelea kuniunga mkono kule jimboni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Katibu wangu Ndugu Ayubu Msalika na wenzake pale kwenye ofisi ya jimbo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, kipekee ninaomba nikupongeze wewe binafsi, kwanza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge ya IPU. Uchaguzi wako mimi sikupata shaka, sisi tunaofahamu sifa zako tulijua unastahili na unafanya vizuri, Mwenyezi Mungu akubariki sana. Aidha, ninaendelea kukupongeza wewe pamoja na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuongoza na kusimamia kwa umahiri shughuli za Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, ninawapongeza Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama na Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, kwa kuteuliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge. Tunawaombea Mungu aendelee kuwasimamia katika kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi waliochangia wamenipongeza. Upo msemo wa Kiswahili unasema; “Usimsifie mwenye mbio, msifie anayemkimbiza.” Kazi tunazofanya Wizarani sifanyi peke yangu, ipo timu pale Wizarani, ninaomba nitumie fursa hii, kwanza kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Ardhi na Mbunge wa Kavuu. Ninatumia fursa hii vivevile kumpa pole kwa kupoteza wananchi wake saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unaweza ukamwona Mheshimiwa Pinda ni mkimya, kwanza amepita jeshini na wewe unafahamu ndiyo Mjeshi wa Bunge hili, lakini la pili, ana uzoefu mkubwa wa utumishi wa umma. Pale Wizarani anatusaidia sana hasa sisi katika kuona jinsi gani ya kuenenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Engineer Anthony Sanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Pale Wizarani tunamwita Baba Paroko, Mtendaji huyu ana sifa zote za utendaji wa umma. Ni mtu mpole, msikivu na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa ni mashahidi jinsi anavyoendesha Wizara yetu ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukurui Bi. Lucy Kabyemela, Naibu Katibu Mkuu ambaye pale kwetu kwenye Uongozi wa Wizara ndiyo practitioner wa Wizara. Amekuwa akitushauri na kutusaidia vizuri na amekuwa kiungo kizuri baina yetu sisi viongozi wakuu wa Wizara na watumishi wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ndugu Nathaniel M. Nhonge, Kamishna; Evelyne Mugasha, Chief Valuer; Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani na watendaji wote wa Menejimenti, lakini watumishi wote wa Ardhi ngazi za mikoa na wilaya ambao wanatekeleza majukumu yao ya kila siku, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi wa dini hasa kiongozi wangu wa kiroho Baba Askofu Alex Gehaz Malasusa kwa malezi ya kiroho. Ninawashukuru pia viongozi jimboni, Ijumaa walikuja hapa Mashekhe na leo amekuja Prophet Nicholaus Suguye, yuko hapa katikati yetu, wameendelea kutuombea na kutusaidia kiroho. Tunaendelea kuwaomba waombee Taifa letu, wamwombee Rais wetu na waendelee kutuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimejifunza mengi kwa marehemu baba yangu Captain William John Silaa lakini nitasema mambo mawili. Baba yangu alinifundisha mambo mengi, lakini makubwa mawili; la kwanza ni kuheshimu kazi. Wale waliowahi kufanya kazi na mzee yule Mheshimiwa Tabasamu anafahamu, alikuwa ni mtu mwenye kuheshimu kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, alinifundisha ukiamka asubuhi lazima uandike to-do list, uandike orodha ya shughuli utakazozifanya na jioni ufanye tathmini ya yale uliyoyafanya, ni yapi umefanikiwa na ni yapi hujafanikiwa ili uyahamishie siku nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mafunzo hayo yamenifanya na mimi nije na miongozo mitano ambayo nimewapa watendaji wa Wizara wawe wanayazingatia katika utendaji wao wa kazi. La kwanza ni sense of urgency, lazima tunavyofanya kazi ya umma tuweke seriousness na kuwa na uharaka wakati wote kwa sababu wananchi tunaowahudumia wanahitaji matokeo ya kwenda kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, msingi wa pili ni sense of care, lazima tuwajali Watanzania, lazima tuwahudumie kwa upendo, lazima tuwajibu kama sisi tukijibiwa hivyo tutajisikiaje ndani ya mioyo yetu. Ndiyo maana pale Wizarani nimekataza kuacha kusaidia Watanzania na tuanze kuwahudumia kwa sababu ni haki yao kupata huduma kwenye Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la tatu ni discipline (nidhamu), lazima tukisema saa mbili ni saa mbili, lazima tukisema saa nne ni saa nne, lazima tuheshimu watu na lazima tuheshimiane. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la nne ni attentiveness, lazima tuwe tunasikiliza na kuelewa, siyo unaambiwa kitu leo unamwambia mwananchi akija kesho hukumbuki alikwambia nini. Lazima uzingatie; pale Wizarani tuna wataalamu, sisi ni viongozi, ukimsikiliza mwananchi msikilize kwa makini, umwelewe ili uweze kumtatulia shida yake.
Mheshimiwa Spika, la tano ni result orientation, lazima tuwe na majawabu ya matatizo ya Watanzania. Hatuwezi kuwa watu ambao tumekaa na majibu, aliniambia Mheshimiwa Yahya Nawanda, ninafikiri Mkuu wa Mkoa wa Simiyu rafiki yangu; tuwe na majawabu, majibu ni njoo kesho, majibu nashughulikia, majawabu Mheshimiwa Janejelly ni shahidi, tumeweka kliniki pale ya Bunge, amepata hati zake tano, nyingine alikuwa anashughulikia kuanzia 2010, amezipata hapa leo, alikosa tu muda wa kuchangia. Lazima tuwe na majawabu, ndiyo ile to do list aliyonifundisha baba yangu, uweke malengo yako, uweke matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya matano yanatumika kwenye corporate world, humu kwenye Serikali tumeongeza la sita la integrity, lazima tufanye kazi yetu kwa uadilifu. Maneno matakatifu ya Mungu, kutoka kitabu cha Kutoka, mlango wa 23, mstari wa nane, neno la Mungu linasema: “Kwani hiyo rushwa hupofusha macho hao waonao na kuyapotoa maneno ya wenye haki.” Ukifanya kazi hii hasa ya ardhi, sina nia ya ku-discourage sector nyingine, ukifanya bila integrity utapofuka macho na ukipofuka macho maneno ya wenye haki utayapotoa, utajikuta unayoyasikia wewe huwezi kupata tena ule uwezo wa kusikia kwani macho yako yamepofushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilithibitishie Bunge lako, tumedhamiria kufanya kazi. Wizara ya Ardhi tumedhamiria kufanya kazi, Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema wengi kwamba ardhi ni rasilimali muhimu sana, kilimo kinafanyika kwenye ardhi, mifugo kwenye ardhi, maliasili ni ardhi, maji na vyanzo vyake ni ardhi, mazingira ni ardhi, madini ni ardhi, miundombinu na nishati zote zinapita kwenye ardhi. Waheshimiwa Wabunge wameshauri sana kwamba Wizara hii ni sekta mtambuka na tufanye kazi kwa kushirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilithibitishie Bunge lako Tukufu tunashirikiana sana ndani ya Serikali, Wizara zote zinazohusiana na ardhi tunashirikiana na kama mlisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Bashe hapa, ndani ya bajeti ya Kilimo ametenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya upimaji wa ardhi za mashamba na tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Mheshimiwa Abdallah Ulega, Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Antony Mavunde, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mawaziri wengine wote tukiratibiwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa Majaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, ametukumbusha maneno ya msingi sana ambayo Baba wa Taifa aliyasema mwaka 1958 ni maneno marefu sina haja yakuyarudia lakini yapo kwenye Hansard. Baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere aliamua kidhati kabisa kuondosha umiliki wa ardhi kwa utaratibu wa free hold, akaleta umiliki wa ardhi kwa utaratibu wa lease hold mwaka 1963 lakini kama haitoshi mwaka 1969 akaweka utaratibu wa rights of occupancy. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako bado misingi aliyotuwekea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ipo pale pale. Ardhi yetu yote nchi hii kilometa za mraba 948,132 zinamilikiwa kwa pamoja na umma wote wa Watanzania milioni 61.7 na wale wenzangu na mimi tunapata haki ya ku-occupy rights of occupancy. Tunapata haki ya ku-occupy ardhi ambayo inamilikiwa na Watanzania wote na mdhamini wa ardhi hii ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ardhi yetu imegawanyika kwenye makundi matatu, alisema Mheshimiwa Olelekaita akichangia, ipo ardhi ya jumla kwa sasa ni 10%, ipo ardhi ya vijiji kwa sasa ni 57% na ipo ardhi ya hifadhi na sasa ni 33%. Bunge hili limetunga sheria 13 ambazo zinasimamia sekta ya ardhi. Kwa kuwa wote tunaotumia ardhi, tunatumia ardhi ya Watanzania ndiyo maana tunapaswa kulipia Kodi ya Pango la Ardhi. Kodi hii tunawalipa Watanzania, kodi hii tunawalipa wamiliki wa ardhi kwa sisi kutupangisha kuitumia.
Mheshimiwa Spika, nilisema kwenye hotuba yangu, tumeanzisha kampeni ya ulipaji wa Kodi ya Ardhi. Yupo Mbunge amechangia leo aliomba sana tukianza oparesheni tuanze na watu wakubwa wakubwa tusianze na watu wadogo. Kampeni hii imeitikiwa vizuri sana, wakati nakuja ku wind up hoja yangu hapa nimeletewa orodha ya viongozi.
Mheshimiwa Spika, nikupongeze umelipia kodi ya pango la ardhi, ungeniweka katika wakati mgumu sana tunapoanza zoezi. Nikuthibitishie Wabunge wa Bunge lako mpaka leo ninavyozungumza na muda bado upo, 96% wamelipia Kodi ya Pango la Ardhi. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao hawajalipa, walipie Kodi ya Pango la Ardhi, hawanilipi mimi wala hawalipi Wizara ya Ardhi, wanawalipa Watanzania ambao ndiyo wamiliki wa kodi ya ardhi na fedha hii wataitumia kwenye huduma zao za jamii ambazo zipo majimboni mwenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mdogo wangu Diamond Platnumz alikuwa amesafiri na alijua nimepania kuanza na yeye, leo ameenda kulipa kodi zake za pango la ardhi. Maana niliwaelekeza wataalamu wangu tukianza tuanze kama Bunge lilivyoshauri, tuanze na wale watu ambao jamii inawaangalia ili watu wajue kwamba sheria ni msumeno. Nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba wananchi wa Tanzania kulipa Kodi ya Pango la Ardhi, kuwalipa Watanzania ambao ndiyo wamiliki wa ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwenye maeneo mengi na yote ni muhimu, nitaanza na yale ya jumla na baadaye nitaenda kwenye yale maeneo moja moja. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupa maelekezo twende tukatende haki ya Watanzania kwenye ardhi. Naomba nimnukuu Mheshimiwa Rais, alituelekeza; “Simamieni haki za watu kwenye ardhi ndiyo msingi wa kila kitu, ardhi ndiyo utajiri wa wananchi na kila kitu ni ardhi.” Hayo ni maneno ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la haki ni jambo la Mwenyezi Mungu, maandiko matakatifu kutoka Kitabu cha Yeremia, mlango wa 22, mstari wa tatu, neno la Mungu linatueleza; “Bwana asema hivi, fanyeni hukumu na haki, mwokoeni mkononi mwa mdhulumu yeye aliyeibiwa.” Kitabu cha Isaya, mlango wa 32, mstari wa 17 kinasema; “Matunda ya haki yatakuwa amani na matokeo ya haki yatakuwa utulivu na matumaini milele.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kwenda kuwatendea Watanzania haki yanalenga kuingiza matumaini kwenye mioyo ya Watanzania, yanalenga kudumisha amani na utulivu kwenye Taifa letu hasa kwenye rasilimali hii muhimu ya haki. Kila siku asubuhi tukiingia hapa Bungeni tunaomba dua kwa Mwenyezi Mungu na kwenye dua lile yapo maneno yanasema; “Ee Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumba wa Mbingu na Dunia, umeweka katika dunia Serikali za wanadamu na Mabunge ya Mataifa ili haki yako itendeke.” Suala la haki ni suala la Kimungu na Serikali inapaswa kusimamia haki za watu na Bunge hili linapaswa kusimamia haki za watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, wote wamezungumza haki ya wananchi wao, haki za mipaka, haki za vijiji, haki za wakulima, haki za wafugaji na haki za mijini. Niahidi katika kipindi chote nitakachotumika kwenye Wizara hii nitasimamia haki bila kumwonea mtu yeyote na tutafanya hivyo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini kwa maelekezo ya Mwenyezi Mungu ambaye si tu tutaishi hapa duniani lakini mbele za haki tutaenda kukuta hesabu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya ardhi, Serikali imefanya kazi kubwa, nimeeleza hatua mbalimbali toka kipindi cha uhuru wa nchi yetu, hatua za Baba wa Taifa, Serikali ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nimeeleza hatua na wengi hapa wamechangia. Serikali za Hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi ambaye ndiyo baba wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa nchini kwetu. Yeye ndiyo aliyeleta Sera ya Ardhi na imechangiwa vizuri hapa leo. Serikali ya Mzee Benjamini William Mkapa, ndiyo iliyokuja na Sheria ya Ardhi Namba Nne na Namba Tano. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli na sasa Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bado kuna matatizo lazima tukiri. Ipo migogoro, migogoro ya mipaka, migogoro ya mirathi, migogoro ya dhuluma, migogoro ya uvamizi, wapo watu wenye nguvu wanavamia wanyonge, lakini wakati mwingine wapo hata wananchi na wenyewe wanavamia maeneo mbalimbali yaliyopimwa. Ipo migogoro inayosababishwa na viongozi, Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na viongozi wengine wa kisiasa. Limezungumzwa hapa suala la double allocation, ipo migogoro inayosababishwa na watumishi wa sekta ya ardhi. Wapo watumishi wengi sana waadilifu, wengi sana waadilifu lakini lazima tukiri wapo watumishi wachache ambao nao wanasababisha migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Conchesta alieleza vizuri hapa na Mheshimiwa Chumi ameelezea historia ya hapa Dodoma. Zipo historia za utawala wa ardhi hapa Dodoma toka enzi ya CDA na sasa halmashauri ya Jiji. Mheshimiwa Rwamlaza amezungumza hapa, lakini naomba kusema, matatizo aliyoyapata yeye na Mheshimiwa Agnesta, hapa Halmashauri ya Jiji la Dodoma amewasemea wengi humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huwezi kuamini, sasa umekaa kwenye kiti, wewe mwenyewe ni mhanga wa vitendo vya baadhi ya watumishi wa Jiji la Dodoma kwenye sekta ya ardhi. Yupo Mheshimiwa Waziri mmoja hapa na yeye ni muhanga, wapo Manaibu Waziri sita nao ni wahanga, wapo Wabunge zaidi ya 30 nina taarifa na wenyewe wamepata madhara. Mheshimiwa Waziri Mkuu aliunda Tume, Tume ya kuchunguza utendaji wa sekta ya ardhi na Mheshimiwa Waziri Mkuu alitupa maagizo Wizara ya Ardhi, twende tukatafute njia bora zaidi ya kufanya land administration kwenye Jiji la Dodoma ambalo ndiyo Makao Makuu ya Nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu inatosha, wananchi wengi wanapata madhara, mtu anapewa kiwanja leo anaanza kulipia akija mtu akikipenda anapewa invoice ya siku za nyuma, analipishwa hicho kiwanja, yule mwananchi akija anakuta mwingine ametengenezewa hati. Tumeamua rasmi ndani ya Wizara kufunga masjala ya ardhi pale kwenye Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mheshimiwa Spika, pale Dar es Salaam tulichelewa, vitendo vya double allocation vilitokea sana Dar es Salaam na mpaka leo tunaishi navyo, lakini mwaka 2018 Waziri wa Ardhi Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, ambaye bado ni Mwalimu wetu sisi alifunga pale Masjala ya Halmashauri ya Jiji. Leo tunafanya administration ya ardhi pale Ofisi ya Kamishna Msaidizi na shida zote zimepungua. Waheshimiwa Wabunge wameona mfumo tulioufunga Dar es Salaam, leo wapo hapa Dodoma na wamepata hati zenu hapa kwenye Viwanja vya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kesho asubuhi saa moja Katibu Mkuu namwelekeza, tutaamkia pale Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma na watumishi wote wanaohudumu kwenye Wizara hii ya Ardhi pale Halmashauri ya Jiji kufikia saa moja na nusu muwe mmeripoti kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma. Hapa Dodoma tutakuwa na Masijala moja, Halmashauri ya Jiji kwa mujibu wa Sheria za Mipango Miji itabaki na mamlaka yake kama planning authority na sisi Wizara tutaisaidia kutekeleza majukumu yake lakini land administration itafanywa kwenye Masjala moja na tutaanzisha uchunguzi wa kuhakikisha wale wote waliyoathirika wanapata nafuu ya athari zao ili kero hii iweze kwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumejipanga Wizarani, tunayo mikakati ya muda mfupi, tunayo mikakati ya muda wa kati na tunayo mikakati ya muda mrefu. Mikakati ya muda mfupi ndiyo kliniki za ardhi tunazozifanya maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Dkt. Mollel angesimama hapa angesema na nyinyi ni mashahidi, kliniki za afya zinafanyika kwenye magonjwa ambayo yamezidi, magonjwa madogo madogo kama homa na nini unaenda kwenye hospitali ya kawaida, lakini magonjwa ya moyo, magonjwa ya sukari yanawekewa kliniki maalum. Sasa kazi ya migogoro ya ardhi imekithiri na ndiyo maana tumekuja na kliniki za ardhi. Kwa hiyo tutaendelea na kliniki hizi kama mikakati ya muda mfupi.
Mheshimiwa Spika, dhuluma na matapeli kwenye ardhi wamekithiri na lazima twende tukawasikilize wananchi wetu, lazima twende tukawasikilize tuwatatulie matatizo yao. Alichangia hapa Mheshimiwa Kunambi na akaelezea Mhimili wa Mahakama, Katiba inavyotaka kufanya kazi ya kusimamia haki. Nikuthibitishie Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaheshimu Katiba na inaheshimu Mahakama. Serikali hii, Bunge hili la kwako na Mahakama kote kuna binadamu na hakuna binadamu aliyekamilika. Hata mimi Waziri wa Ardhi kuna wakati nitafanya maamuzi mtu mwingine ana haki ya kuyaangalia akasema maamuzi haya Mheshimiwa Waziri, hayakuwa sahihi. Mahakama yetu inafanya kazi nzuri sana, sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Kariakoo, Mtaa wa Kongo kuna kesi maarufu ya familia ya Pazi imekwisha na wamepata haki yao na mliona tumeenda kuwakabidhi jengo lao lakini kesi ile imechukua miaka 26. Miaka 26 familia ile inapambana kupata haki yake ambayo hata Waheshimiwa Wabunge hapa ambao hawajasoma sheria ukiwaonesha shauri lile watakwambia haki yao wangeiona miaka 26 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe ni daktari wa sheria, civil procedure code inatuelekeza kwenye order forty-three rule namba mbili, kwamba maombi yote Mahakamani yatawasilishwa kwa chamber summons na affidavit. Haya hapa Mheshimiwa Mbunge umsimamishe akuandikie chamber summons na affidavit, hivi ile familia ya Mwananyamala waliyoiona kwenye kipindi cha Maimartha cha ICU kuna mtu pale wa kuandika chamber summons na affidavit? Inabidi atafute wakili. Mawakili nao ni binadamu, wapo Mawakili wenzetu wengi waadilifu wanaofanya kazi nzuri ya kutetea wateja wao, lakini wapo mawakili wanaoingiza wateja wao kwenye matatizo na kukosa haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, there is a legal maxim inasema; “those who come into justice, should come with clean hands.” Leo Mheshimiwa Kanyasu amesema hapa, sheria inataka watu wanaokwenda Mahakamani kutafuta haki waende na mikono misafi, lakini wapo matapeli wanaoghushi nyaraka, wanafungua mashauri. Amesema hapa Mheshimiwa Kanyasu yupo mtu anachukua ramani ya kughushi anapeleka Mahakamani na anaipelekea Mahakama hii inayotenda haki impe haki kwa kutegemea nyaraka zile ambazo siyo sahihi na yule mwananchi mnyonge anayeenda kumpora haki yake hana taarifa kuna kesi, hana uwezo wa kujitetea. Tutasimamia haki za wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Civil Procedure Code Order 37 inaelezea vigezo vya kutoa interlocutory orders na inaelezea vizuri kabisa, Waheshimiwa Wabunge wanapata fursa ya kwenda kusoma lakini tumeona watu wenye nguvu wanaenda na ile interlocutory orders inasababu zake kubwa kupunguza hasara mtu asivunjiwe nyumba, mnada usifanyike na imesema pale kwamba Serikali haitazuiwa kutekeleza majukumu yake lakini watu wenye nguvu, wenye ufundi wa kisheria wakati mwingine wanakwenda Mahakamani kuzuia haki ya mwananchi mwenye nyaraka halali kabisa za umiliki wa ardhi ili asipate haki yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutasimamia haki na tupo tayari wakati mwingine kutofautiana na baadhi ya maamuzi kwa sababu tunasimamia haki bila kumwonea mtu yeyote. Kuna kesi moja imefanyika pale Dar es Salaam, yupo tapeli mmoja wa ardhi alichukua hati ya Mzee mmoja anaitwa Mwinyimvua pale Mbezi Beach, amekaa na ile hati zaidi ya miaka 10, yule mzee amepambania hati yake mpaka amefariki dunia. Wamebaki warithi wake (wanaye) wanapambania hati yao, akaja kwetu, tukampatia notice yule tapeli hakurejesha hati. Tukawapatia wale warithi duplicate title wakaendelea wakapata wateja wao wakawauzia, yule tapeli akaenda Mahakamani kufungua shauri.
Mheshimiwa Spika, Jaji aliyesikiliza kesi ile mwaka 2015, ndiyo aliyekuwa Wakili ali-attest document za Mzee Mwinyimvua kwenda kuvunja nguvu ya Kisheria Power of Attorney ya tapeli yule aliyefanya kwa forgery na akakutwa na forensic ya Jeshi la Polisi kwamba ame-forge na akapelekwa Mahakamani na huyo huyo tapeli akashinda na ame-forge nyaraka. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, Jaji aliyekuwa Wakili aliye-attest nyaraka za Mzee Mwinyimvua kwenda kuondoa utapeli ule, kaja kuwa Jaji anasikiliza kesi ya tapeli anataka kwenda kuwaonea wale yatima, wale warithi wa yule mzee marehemu wa watu. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, tumeshafungua mimi binafsi maana mwisho ameanza kuwaita watumishi wa ardhi ambao Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo hapa, inataka mtumiShi wa Serikali akifanya kazi, afanye kazi kwa kuitetea Serikali na atatetewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Jaji anaita watumishi kwa majina yao anawa-harass wale watumishi.
Mheshimiwa Spika, hii vita nimeinunua mimi mwenyewe, nimeandika barua kwa Waziri wa Katiba na Sheria, hakuna mtu nchi hii yupo juu ya Sheria. Majaji nao wanayo kanuni zao za maadili tunataka tuone kama kilichofanyika ndiyo maadili ya utaratibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, alikuja kutufungulia kliniki ya ardhi na alitoa maelekezo kupitia Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwamba masuala ya utapeli wa ardhi una jinai ndani yake. Ambacho tumefanya marekebisho kwenye Sera ya Ardhi ni pale tu kuongeza ile trespass of land kuja kuwa criminal.
Mheshimiwa Spika, Penal Code, Sura ya 60, ukisoma Kifungu cha 333 forgery (kughushi nyaraka) ni kosa la jinai. Ukisoma Kifungu cha 302 kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu false pretense ni kosa la jinai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa maelekezo yake, lakini tunamshukuru sana Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura, anaunga mkono jitihada hizi, mmeona matapeli papa pale Dar es Salaam, wameanza kwenda mbele ya vyombo vya sheria, hatutachoka mpaka haki za wananchi zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bunge hili limetunga Sheria Sura 113, moja ya njia za kupata ardhi haikuorodheshwa kwenye Sheria ile ambayo Bunge hili Tukufu limetunga kwamba, unaweza kupata ardhi kwa kupata ex-parte judgment ya nyaraka za kughushi eti ukaleta kwa Msajili wa Hati ukapata ardhi, tutaendelea kufanya kazi ndani ya Serikali na kushirikiana na wenzetu wa Mhimili wa Mahakama kuhakikisha wananchi wanapata haki zao, nilitaarifu Bunge lako kwamba tutaendelea na kliniki hizi mpaka ugonjwa huu wa migogoro ya ardhi utapopungua na kwisha kabisa kwa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, tunaendelea kuwaomba waendelee kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais, waendelee kushirikiana na Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa Mikoa yote ya Tanzania Bara na waendelee kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Ardhi wa Wilaya zote kufanya kliniki.
Mheshimiwa Spika, Wizara wa Ardhi, tutaendelea na ile kliniki kubwa ambayo sisi Viongozi wa Wizara wenyewe tunahudhuria, safari hii tulikuwa tumefanya kidogo yale waliyokuwa wanayaona Mheshimiwa Cosato, itabidi aongeze bundle ile ilikuwa ni 10% tu anayoiona, tulikuwa tunaogopa kidogo tunaweza kuja hapa kwa Wawakilishi wa Watanzania labda wamelipokea vibaya. Pongezi zao zimetuongezea nguvu kwamba, wanayoyasema ni pongezi za Watanzania, tunaenda kuongeza kasi na sasa kliniki hii itaenda kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kliniki hii sasa itakuwa ni kliniki rasmi na itajulikana kama Samia Ardhi Clinic, tutakwenda, Waziri atakwenda, Naibu Waziri atakwenda, tutakwenda kusikiliza Watanzania na tutakwenda kuwafuta machozi Watanzania wote waliodhulumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wito wangu ni kwa Mtanzania yeyote ambaye anajua amemdhulumu mtu ardhi, mtu ana hati yake wewe umeingia tu kwa sababu una nguvu, arejeshe mapema kabla hatujaja. Tutakuja na niwathibitishie kampeni hii ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tutakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo tukiri tumekosea wapo watu tumefanya kazi hii in camera hamjayaona na wapo watu tumewaagiza kistaarabu wengi wao wametoka wametusema, wameona kama hatujawatendea haki, safari hii tutaenda kufanya kama yale mengine wanayoyaona. Tutaenda na kipira wa mung’anda wataenda mung’anda hatua za kisheria zitachukuliwa kila mtu atapata haki yake, wale wote wenye jinai Sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, alisema hapa Mheshimiwa Kanyasu, kliniki hii vilevile ni elimu, ni darasa kwa watumishi wetu wa ngazi za Mikoa na ngazi za Wilaya ili yale tunayoyafanya Viongozi Wakuu wa Wizara, tukiondoka na wao waendelee kuyafanya ili kazi hii iwe endelevu. Katika hatua za muda mfupi tumeunda Mikoa Maalum ya Ardhi. Pale Dar es Salaam tumeunda Mkoa Maalum wa Ardhi Kinondoni, Ilala, Ubungo, Temeke na Kigamboni, kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za uwekezaji tumeunda Mkoa wa Uwekezaji. Kwenye Majiji makubwa Mbeya, Mwanza, kote tumeunda Mikoa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Muharami, amesimama hapa Pwani ya Kaskazini tumeunda Mkoa Maalum na Pwani ya Kusini, pia tumeendelea kufanya kazi ya kuboresha utendaji na kama nilivyosema hapa Dodoma na pale Dar es Salaam, tunaongeza uwezo wa Ofisi ya Waziri ya kufanya kazi ili kuwapunguzia wananchi mzigo.
Mheshimiwa Spika, mwananchi wa Dar es Salaam anapomfuata Waziri Dodoma na wataalamu amewaacha Dar es Salaam hawezi kupata suluhu ya tatizo lake. Kwa pale Dar es Salaam wananchi wapata huduma wakati wote na hapa Dodoma wapata wakati wowote na maeneo mengine tumeendelea kuwasihi wananchi watumie Ofisi za Makamishna Wasaidizi wa Mikoa kama maeneo ya kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, tuliagiza tarehe 13 Aprili, kwamba watumishi wote Mikoani watekeleze majukumu yao. Hatuwezi kuwa na Maafisa Ardhi, Maafisa Mipango Miji na Wapima, wamerudikana Ofisini na Miji yetu inaendelea kuharibika lazima watoke. Tumeelekeza wakae Ofisini siku ya Jumatatu na Ijumaa lakini siku ya Jumanne, Jumatano na Alhamisi waende wakafanye kazi zao za kitaalam, nimeelekeza kwenye ziara zetu viongozi tutakagua log books zao watuambie wamefanya kazi gani katika kipindi ambacho tumetoa maelekezo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo masuala ya migogoro ya mipaka yamechangiwa na Mheshimiwa Makoa, Mheshimiwa Olelekaita, Mheshimiwa Kakunda, Mheshimiwa Francis Isack na Mheshimiwa Genzabuke. Tutaendelea kushirikiana na mamlaka zingine ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuondoa migogoro hii ya mipaka ya kiutawala. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vipo vijiji vingi vina migogoro ya mipaka, zipo Wilaya nyingi zina migogoro ya mipaka, lazima tukiri kwamba, vipo vijiji vimesajiliwa ndani ya hifadhi, vipo vijiji vimesajiliwa na vime-overlap upimaji wake. Tutaendelea kushirikiana na kwa kuwa tutafanya ziara nchi nzima, tutafanya kazi ya kujitahidi kutatua matatizo hayo. Naliahidi Bunge lako tutafanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanya marejeo ya Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, Toleo la mwaka 2023. Natumia fursa hii kumtoa hofu Mheshimiwa Simai, hatujafuta Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, tumeifanyia maboresho. Wakati anazungumza nilimwona Daktari wa Falsafa Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akipiga makofi, nimejua alikuwa na shaka ya mchakato wa maboresho ya Sera hii. Sera ya Ardhi ipo palepale tumeongeza matamko toka matamko 46, mpaka matamko 67, tumeongeza malengo makuu toka malengo makuu nane mpaka malengo makuu 16. Misingi ya Sera ile ikiwemo lile tulilolisema hapa la ardhi yetu kumilikiwa na umma wa Watanzania bado ipo palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuliambia Bunge lako katika Sera hii ambayo imepitishwa mwaka 2023 na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, haki za wanawake zimeenda kulindwa. Sera ya Ardhi ya mwaka 1995, ilitambua haki za wanawake hasa kwenye mirathi, lakini iliongeza maneno mila na desturi zitazingatiwa. Watu wanapotaka kumdhulumu mwanamke nchi hii, watu wanapotaka kumdhulumu mjane mirathi yake ndiyo mila na desturi zao watazikumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa naongea na Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, ana Shahada ya Uzamivu, ana watoto sita mwenye elimu ya chini ana Degree ya Uzamili. Mmoja kaoa Mhehe, unaenda kumiliki ardhi Mikocheni, Dar es Salaam, unamiliki ardhi Kisasa halafu unataka mirathi yako ifuate mila na desturi. Ukitaka mila na desturi ungebaki kule Kibosho ukae na kiamba chako uishi maisha ya kijijini na maisha ya kimila ili ukitaka mambo ya mila na desturi tukuelewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, Sera ya Ardhi Mapitio ya 2023, inaenda kulinda maslahi na haki za wanawake ambao wamekuwa wakidhulumiwa kwenye mirathi kwa kisingizio cha mila na desturi wakati ni dhahiri maisha tunayoishi si maisha ya mila na desturi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi hii ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mimi ninaomba Waheshimiwa Wabunge, muendelee kutuunga mkono. Tumetoa maelekezo wasimamizi wa mirathi ni marufuku kuuza mali za warithi. Nimeelekeza Wasajili wote wa Ardhi nchi nzima, kazi ya msimamizi wa mirathi ni kupeleka majina ya warithi ili Msajili awaingize kwenye usajili wa ardhi ili wakitaka kuuza wauze ardhi yao wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukisoma hati ya jina la msimamizi wa mirathi imeandikwa kabisa as legal representative wa marehemu, lakini imekuwa ni desturi ya watu kuuza mali za marehemu kwa kisingizio cha usimamizi wa mirathi. Ipo hukumu moja ya Mahakama ya Rufaa pale Tabora imeondosha kile kilichokuwa kinaitwa beneficiary consent maana ilikuwa msimamizi akiuza lazima warithi waridhie. Hukumu ya Mahakama ya Rufaa, imewaondoa warithi kutoa ridhaa ya kuuza, tukienda hivi yatima watadhulumiwa kwenye nchi hii na watu waliopewa kazi ya kusimamia mirathi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu uvamizi, tutaendelea kulinda haki za ardhi na haki halali za ardhi, kila mwenye hati yake tutailinda na tutahakikisha tunaendelea kupiga vita uvamizi ili kila mtu apate haki ya ardhi. Mheshimiwa Mkenge, nitakuja Bagamoyo na Waheshimiwa wote waliomba hapa kufanya ziara kote tutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafanya marekebisho ya Tangazo la Serikali Namba Saba la Mwaka 2021, kwa zile nyaraka za mauziano ya ardhi. Nilipiga marufuku Wenyeviti wa Mitaa, kushiriki mauzo ya ardhi. Maana Wenyeviti wa Mitaa wamejigeuza Makamishna wa Viapo, wanafanya kazi ya Mawakili. Mawakili wana utaratibu wao wa kazi, Wakili akishuhudia utiaji saini anashuhudia biashara ya watu wawili, Mwenyekiti wa Mtaa siyo Wakili. Tunaenda kurekebisha nyaraka za mauzo ya ardhi mitaani ili Mwenyekiti wa Mtaa akishuhudia yale mauzo ashuhudie kwamba, anamfahamu muuzaji na anathibitisha ardhi ile ni ya muuzaji ili siku yule mnunuzi akiona ametapeliwa na Mwenyekiti wa Mtaa huyu awe ni mmoja atakayeshirikiana na muuzaji katika kwenda kupata mkono wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tuokoe Watanzania wetu wanyonge wanaotafuta riziki yao kwa taabu wanaishia kwenda kuuziwa ardhi. Hii double allocation ya Dodoma inayofanyika na kwenye mitaa inafanyika. Hili litaenda pamoja na Wenyeviti wa Vijiji, Sheria namba tano Kifungu cha 8(5) kinatoa mamlaka ya ardhi ya vijiji kwa Mkutano Mkuu wa Kijiji na si kwa Mwenyekiti wa Kijiji. Mwenyekiti wa Kijiji hana mamlaka ya kuuza ardhi, kama kuna mtu kanunua ardhi kwa Mwenyekiti wa Kijiji tukimkuta atakuwa ametapeliwa. Tunaenda kufanya marekebisho ya Sheria, Sera ya Ardhi ilishakamilika kwenda kuingiza Kamishna ili aangalie maslahi ya wananchi wa Tanzania kwenye ardhi ya Kijiji na kuepusha Wenyeviti wa Vijiji ambao wanauza ardhi ya wanakijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ile hoja ya Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, ya wanakijiji ama Viongozi wa Vijiji kuuza ardhi na wananchi Watanzania. Kwa hotuba ile ya Mwalimu Nyerere tusipokuwa serious tutatengeneza Taifa la watu ambao watawatumikia wengine wenye ardhi kubwa na wao kukosa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa haraka haraka mambo ya muda wa kati, cha kwanza, ni mfumo wa TEHAMA. Mheshimiwa Kunambi, alichangia hapa na alisema Mfumo wa ILMIS. Mheshimiwa Kunambi, ni Mwanasheria mwenzangu ila mimi degree ya kwanza inaitwa Bachelor of Science and Electronic Science and Communication, ndiyo Shahada pekee ya mifumo ambayo computer inashughulikiwa kwa mbele kwenye software, inashughulikiwa kwa nyuma kwenye hardware na kwenye mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anavyosema Mheshimiwa Kunambi, ILMIS ni kama kusema Toyota ni aina ya gari. Tunaenda kuunda mfumo wa kisasa kabisa utaofanya management ya ardhi nchi hii na tayari timu ya vijana ipo pale Arusha na ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni maelekeo yake kuhakikisha Sekta ya Ardhi inatawaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupanga, kupima na kumilikisha (KKK) yamesemwa vizuri sana hapa na Naibu Waziri amesema, kupanga matumizi bora ya ardhi vijijini, kupanga maeneo wataalamu wetu wafanye kazi pa kupanga wapange, pa kupima wapime na pa demarcation wafanye demarcation. Kuna upimaji mwingine hauhitaji hata vifaa wafanye kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Bashe ametenga fedha, lakini tumefanya marekebisho ya Kanuni GN. No. 91, kwa kufanya mabadiliko ya maeneo ya wazi Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa. Tumeongeza mchakato mkutano wa mtaa utahusika na Kamati za Usalama za Wilaya zitahusika, tunataka maeneo ya wazi yalindwe, tunataka mabadiliko ya matumizi yasimamiwe, hatuwezi kuwa na Taifa ambalo kila mtu akiamka akitaka kubadilisha matumzi anabadilisha matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, aliwahi kuuliza swali hapa Bungeni na Mheshimiwa Bashe nimesema tunashirikiana tunafanya marekebisho ya GN. No. 93 ili wananchi wanaolima kwenye maeneo ya Miji waweze kulima kwa furaha na kile kikomo cha eka tatu tumekiondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepokea hoja ya Jiji la Mbeya, nikuahidi Jiji lile tutalifanyia kazi kupitia Mradi wa LTIP Mheshimiwa Suma amesema vizuri. Tutahakikisha na nikuahidi, bajeti hii ikimaliza kupita eneo tutaanza nalo tutaanza na Jiji la Mbeya. Tutaanza na Jiji la Mbeya kwa heshima kubwa ambayo dunia imekupa wewe pia kwa heshima kubwa ambayo Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili wanayo kwako. Tunataka tutengeneze sura nzuri ya Jiji lile maeneo yote ring road yapangwe, yapimwe tuwe na Jiji la kisasa, ubaki na legacy katika miaka yako 20, 30, 40, 50 utayokuwa Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Mjini, uache Jiji la kisasa na kazi hii tunaahidi tutaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya mashamba. Pamoja tutaendelea kulinda haki za kumiliki lakini hatutaruhusu Watanzania wazawa na wageni kumiliki maeneo makubwa ya ardhi kwa kisingizio cha umiliki na wasiyatumie na waishie kuwakodisha Watanzania na kuwageuza wao feudalism ndani ya ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunashirikiana na Wizara ya Kilimo, tutakagua mashamba mwenye haki yake atapata haki yake na pale ambapo hakuna uzalishaji hatutasita kubatilisha matumizi na kuwapa wenye uwezo ili ardhi ile iweze kuzalisha na wananchi waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inaenda sambamba na hoja ya dada yangu Mheshimiwa Halima James Mdee, Mheshimiwa Halima amezungumzia Shamba la DDC, Mheshimiwa Halima tutakwenda kuwasikiliza wananchi wale. Hatuwezi kuwa Serikali ambayo tunakubali kuna haki ya karatasi, lakini lazima tusikilize na haki nyingine tutumie busara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Halima amezungumzia hekima, Mheshimiwa Tauhida, ameniomba nimwombe Mwenyezi Mungu hekima na Mheshimiwa Hokororo, ameelezea suala la hekima, lazima tunapofanya kazi za kutenda haki hasa ya watu wengi Mheshimiwa Rais, ametuelekeza wananchi wasipate taharuki tutumie hekima na busara kutafsiri Sheria. Tusitumie busara kuvunja Sheria bali tutafsiri sheria kwa hekima na busara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ni nyingi kuna hoja ya uthamini tumetoa waraka namba moja wa mwaka 2024, tutakuwa wakali Wizara ya Ardhi, kwa mtu yeyote ndani ya Serikali anayetaka kuwa na mradi ahakikishe kabla ya kutwaa maeneo ya wananchi anazo fedha za kulipa fidia. Unakuta kule mkoani au wilayani, Afisa tu wa Serikali ameamua kuwe na mradi anatwaa maeneo ya watu. Hata Mkoani hawajui, Wizara yake haijui mpaka ije kujua ni miaka mitatu, minne, waje kuomba fedha hapa mpaka zitengewe miaka mitano, sita wananchi wanateseka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumetoa Waraka Na.1 wa Mwaka 2024 kulinda wananchi wetu, Katiba yetu Ibara ya 24(2) inataka wananchi wamiliki mali na tulinde umiliki wao, hoja hiyo amezungumzia Mheshimiwa ya Magessa, ya surface right versus mining right, tunafanya kazi na Mheshimiwa Mavunde, kuweza kuhakikisha jambo hili na lenyewe linafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikikaribia kumalizia naomba niliambie Bunge lako, sifa na pongezi mlizotupa niwaahidi hazitotulevya wala hatuwezi kuzichukulia poa. Sifa na pongezi tulizopewa na Waheshimiwa Wabunge tumezichukua kama deni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naahidi dawa ya deni ni kulipa na usiku wa deni haukawii kukucha. Tutahakikisha tunalipa sifa hizi kwa kuwafanyia kazi Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Kanyasu tutakwenda kwenye jimbo lake, Mheshimiwa Agnesta amesema kule Mkoa wa Pwani tutakwenda kwa wale wananchi wa Segerea, Mheshimiwa Condester kwenye lile shamba tutakwenda na maeneo mengine yote. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge hizi suti tutavaa hapa Bungeni, tukimaliza bajeti tutavaa buti na jeans tutakwenda kule wananchi wanakopata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii Mheshimiwa Rais sio Wizara ya kwenda Nje ya Nchi. Kwenda Nje ya Nchi ni kazi ya Wizara ya Mambo ya Nje, sisi Wizara yetu tutakwenda kule wananchi walipo. HIi ndiyo dhamana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa Wizara ya Ardhi na wala hatutochoka. Tutakuja na itakuwa ndiyo malipo ya deni hili ambalo wametukopesha kwa kutupa sifa hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kushukuru vyombo vyote vya Serikali na Serikali nzima. Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote wamekuwa wakitupa support. Nimeeleza hapa Mheshimiwa IGP amekuwa akitu-support. Niwathibitishie tutafanya kazi hii.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lusinde aliongelea suala la ulinzi. Zaburi ya 127:1-2 neno la Mungu linasema, “Bwana asipoulinda mji, yeye aulindae akesha bure.” Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotuombea Baraka za Mungu, niwahakikishie vilio na machozi ya Watanzania tunayoyafuta ndiyo ulinzi mkubwa kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikuthibitishie yuko mtu mmoja aliandika kwenye mtandao hii nchi sio ya kuchukuliana poa. Msituone Kariakoo tunazurura, siyo kila mtu pale ni machinga wengine wako kazini, jichanganye utaona nguvu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pale napo vijana wa Kizimkazi wapo na hapa ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikuthibitishie kazi tuliyoifanya lakini naomba niwaahidi Wabunge wote waliochangia, hoja zote tutazijibu kwa maandishi. Waheshimiwa Wabunge niwaombe sana zile hoja ambazo hatujazijibu tumeziheshimu sana, tutatoa majibu kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuomba fedha. Jumla ya fedha zinazoombwa kuidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa mafungu yote mawili (Fungu la 48 na Fungu Na. 3) ni jumla ya shilingi 169,628,415,000. Fedha hizo kwa Fungu 48 ni shilingi 157,455,085,000 na kwa Fungu Na. 3 ni shilingi 12,173,330,000.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Finance Bill ya Mwaka 2021. Kama muda utaruhusu nitachangia kwenye maeneo manne; Part VIII, The Amendment of Income Tax Act, Chapter 332 ambayo nitachangia kwa pamoja na Part XXI, Amendment of the Tax Administration Act.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Income Tax ndiyo inakusanya kodi na Tax Administration Act ndiyo inatoa utaratibu wa kukusanya kodi pamoja na adhabu. Ukisoma bajeti, ukurasa wa 52 kuna maneno ya kufanya marekebisho kwenye Regulation ama the Transfer Pricing Regulation za Mwaka 2014 kuondoa adhabu ya asilimia 100 kwa wale watakaobainika kufanya vitendo hivi vya Transfer Pricing. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo makubwa yanayopoteza kodi ya nchi yetu hasa kwenye makampuni makubwa ni Transfer Pricing. Ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Audit on Transfer Pricing, kwenye Executive Summary Part XVI, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ametoa mapendekezo kwa Wizara kui-support Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza nguvu kwenye suala la kusimamia Kitengo cha International Tax Unit katika kuhakikisha tunaondosha utoroshwaji wa fedha nchini kupitia Transfer Pricing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, naamini taarifa hii tutaijadili Bunge linalofuata, Wizara ya Fedha badala ya kutengeneza utaratibu wa kutoa support inaleta mabadiliko ya kwenda kuondoa adhabu kwenye jambo ambalo ni kosa kisheria. Ukurasa wa 23 wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali inaonyesha Kitengo hiki cha ITU kwa miaka zaidi ya mitatu kimefanya ukaguzi kwenye asilimia 33 tu ya makampuni ambayo yameainishwa kama the most risk companies kwenye Transfer Pricing. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe na niliombe Bunge hili na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa lugha ya mjini tunasema hii umechomekewa, usisaini kanuni hii, ukisaini unaenda kuipa Serikali hasara kubwa ambapo siku za nyuma tulikuwa tumeshaondoka. Niseme tu na Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakuwa anafahamu, ipo kesi, The Civil Appeal Case No. 144 ya Mwaka 2018 ambayo imetolewa hukumu tarehe 20 Agosti, 2020 na panel ya Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ikiongozwa na Jaji Mkuu Ibrahimu Juma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hii imeenda kutoa hukumu ya kodi ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 900 kwa kampuni ya African Barrick ambayo kwa miaka mitatu mfululizo ili-declare loss hapa Tanzania, lakini iligawa dividends kwa wanahisa wake kule Uingereza. Kampuni ile haina mali yoyote duniani zaidi ya ile migodi mitatu na ukitaka kujua fedha hizi ziliondokaje nchini ziliondoka kwa Transfer Pricing. Sasa mnapoenda kusema mnataka kufuta kanuni hii ya adhabu kwa kigezo cha kusema eti unaenda kuhamasisha uwekezaji, aliyeandika hili Mungu anamuona, ameandika akijua wazi haendi kukuza uwekezaji.
T A A R I F A
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwenye kesi hiyo ambayo anaizungumzia hapa ni kwamba pia hawa Barrick wali-declare kwenye kesi ile kwamba walitumia kiasi cha asilimia 2 kama fedha za CSR katika ujenzi wa miradi mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala, Kata ya Bulyankulu. Hata hivyo, mpaka hivi tunavyozungumza zile asilimia 2 ambazo walizi-declare kule mahakamani zile nyumba ambazo walijenga kwa fedha hizohizo za CSR walienda kuziuza tena kwa wafanyakazi na sasa hatujui hizo fedha ziko wapi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Jerry.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu kwamba masuala haya ya Transfer Pricing siyo mambo ya kujifungia sisi wenyewe. Kuna mkutano ulifanyika Addis Ababa unaitwa The Addis Ababa Action Agenda ulifanyika tarehe 15 Julai, 2015. Mkutano huu labda kwa sababu muda tu ni mfupi ulieleza mambo mengi sana kuhusiana na Transfer Pricing, ilieleza ni jinsi gani fedha nyingi zinatoka Africa kila mwaka katika utaratibu huu. Niliombe Bunge hili lakini nimuombe Waziri kwamba jambo hili likienda kufanyika tunaenda kutengeneza hasara kubwa sana kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, ile ni adhabu kwa yule anayebainika amekwepa kodi ile siyo kodi. Tumetoa hapa ada ya faini za barabarani kwa bodaboda toka shilingi 30,000 mpaka shilingi 10,000, lakini adhabu bado ipo, unaenda kuondosha adhabu maana yake unaenda kuhalalisha kosa, unaenda kumfanya mtu sasa afanye kosa kwa amani kwamba hata akikamatwa hakuna adhabu. Ningetegemea labda adhabu hii itoke asilimia 100 iende zaidi ya hapo ili kutengeneza uwoga kwa makampuni haya makubwa ambayo kwa miaka mingi yanalipa kodi ndogo kuliko Watanzania wazawa wanaofanya biashara hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wafanyabishara wa Tanzania wa kawaida kabisa wana adhabu ukichelewesha returns una adhabu…
MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa
MWENYEKITI: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, msemaji anazungumza point nzuri sana, muhimu sana, tuna vijana takribani asilimia 50 ya idadi ya watu wa Tanzania. Nampa taarifa kwamba tunavyopunguza adhabu ya pikipiki na kufanya shlingi 10,000 ni lazima tujue taarifa ni ajali ngapi zilikuwepo wakati faini ni shilingi 30,000 na faini ikiwa shilingi 10,000 kutakuwa na ajali ngapi? Hii ni taarifa sisi kama Bunge na msemaji lazima aizingatie wakati anachangia ili kuokoa watu wasikatwe miguu kwenye ajali za pikipiki, nampa taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry, taarifa.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naamini dakika zangu unazilinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilikuwa na mengi sana ya kuchangia hata dakika zikiniishia kwenye hili la Transfer Pricing nitasimamia na nimuombe Waziri asijaribu kuingia kwenye historia hiyo. Kama hilo litafanyika na wewe utaingia kwenye historia kwamba uli-chair kikao ambacho kimeenda kufanya jambo hilo la kuweza kudhulumu haki za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili nataka kuchangia ni Part IX ya Amendment ya Local Government Authorities (Rating) Act, Chapter 289. Kodi ya Majengo ina historia yake, inapata historia kwenye karne ya 17. Kule Uigereza Malkia Elizabeth I mwaka 1601 walipitisha sheria inayoitwa The Poor Relief Act iliyokuwa inatoa mamlaka kwa mamlaka za Local Government kukusanya kodi kwenye majengo ili kuwatengenezea huduma wakazi wakazi wa maeneo yale, The Property Tax. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii Part IX, Serikali imeleta mabadiliko inataka kuongeza section 31A inayotaka fedha hizi na wewe uko pale Ilala unafahamu majengo pale wapiga kura wako wanavyotaka huduma kupitia Property Tax zao, kifungu hiki cha 31A kinakwenda kupeleka pesa hizi kwenye Consolidated Fund na inarudishwa asilimia 15 si kwenye mamlaka husika zinarudi TAMISEMI zigawiwe nchi nzima. Labda watafute jina lingine la kodi hii na mimi nitaunga mkono kama ni Kodi ya Maendeleo au Kodi ya Miradi, naomba nilindie dakika zangu, hizo ni kumi zile za mwanzo bila taarifa. Kama tunataka kuipa jina lingine tuipe kodi jina lingine, lakini kama itaitwa The Property Tax msingi wake ni Kodi ya Majengo na wenye majengo yao kwenye mamlaka zile za Serikali za Mitaa wanasubiri huduma, wanasubiri barabara na mitaro, niiombe Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho kwa dakika moja naomba nichangie Part XIII. Serikali inataka kurekebisha The Non-Citizen Employment Regulation na kutengeneza faini ya shilingi laki tano kwa wafanyakazi wageni. Tarehe 6 Aprili, mmemsikia Mheshimiwa Rais akitoa wito kwa wenzetu wa vibali vya kazi kutaka kuondoa urasimu kuwasaidia wawekezaji kupata vibali vya kazi. Kibali Class A ni dola 3,050, kibali Class B ni dola 2,050 bado Labour wanachukua dola 1,000 na unreturn fees ya application, halafu unataka umdai mwekezaji huyu shilingi laki tano eti hajaleta return ya watumishi wake. Tunaenda kukwamisha uwekezaji kwenye nchi hii, kila mwezi mnaenda kuwagongea milango yao. Hatuwezi tukawa tuna nchi ambayo mtu anakuja serious investor anaomba serious permit analipa three thousand dollars halafu kuna mtu anataka kwenda kumgongea mlango wake kila mwezi amdai laki tano kwa sababu hajaleta return ya watumishi wake, mnaenda kukwamisha uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huku kwenye Transfer Pricing mnaenda kupoteza mabilioni mnasema mnakuza uwekezaji mnakuja huku mnachukua shilingi laki tano kwa mwezi. Naomba Waziri wa Fedha hii Amendment ya Part XIII aiondoshe, hatuwezi kuwa na nchi ya aina hii ya kwenda kusumbua watu wanaokuja na mitaji yao. Tutakuwa ni nchi ya kipekee duniani ambayo tuna tamaa na fedha za watu na tutakwamisha uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kugundua mchango wa sekta ya TEKNOHAMA katika uchumi wa Taifa letu. Kwa kuunda Wizara hii, ni matumaini yetu sasa kwamba Serikali itatengeneza utaratibu mzuri ili sekta hii iweze kutoa mchango chanya kwenye uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Waziri ameainisha takwimu za watumiaji ambao mpaka hivi tunavyozungumza wanatumia line za simu. Mpaka kufikia anasoma hotuba hapa leo wapo watumiaji 53,063,000 wanaotumia line za simu. Kuna Watanzania 29,071,000 wanaotumia mtandao wa internet lakini zaidi ya Watanzania 32,000,000 wanatumia miamala ya fedha kwa maana ya fedha za kwenye simu. Ukiangalia takwimu zote hizi za mamilioni utagundua kwamba tayari Tanzania ipo na wenzetu wa duniani, kwamba sasa tumehama toka kwenye mifumo tuliyoizoea (traditional systems) kwenda kwenye mifumo ya kimtandao kwa maana ya online systems, tutakutana kwenye bajeti kuu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi tunavyozungumza wenzetu wa Mamlaka ya Mapato wanao Watanzania wenye Tax Identification Number kwa maana ya TIN Number milioni mbili na laki tano. Ukiangalia takwimu hizi za online na takwimu zetu zile tulizozizoea za makaratasi, utakubaliana na mimi kwamba tayari dunia imehama na ni wajibu wetu kama Watanzania kuwekeza nguvu kubwa zaidi ya kutumia advancement hii ya teknolojia kuendesha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kwenye maeneo matatu. Eneo la kwanza, tumeona kwenye Finance Act nyingi kwamba wenzetu wa Serikali wanatumia takwimu hizi za wingi wa watumiaji wa simu, internet, mitandao ya fedha kwenye simu kama ndiyo mtaji na kuweka makodi mengi ambayo yanawaumiza watanzania. Wanasahau kwamba takwimu hizi zinapaswa kutumika kama platform ya kutengeneza system nzuri zaidi ya kuwa kwanza na tija kwenye matumizi yenyewe ya mitandao, lakini pili kama kuna ukusanyaji wa mapato, kukusanya mapato stahiki kwa wale ambao wamebeba ama wale ambao ndiyo online platform prayers kwa maana wale ambao ndiyo hasa wamiliki wa mitandao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Ufaransa ndiyo walikuwa wa kwanza (pioneers) wa kuanzisha Kodi ya Mitandao, kwa maana ya Digital Service Tax (DST). Waliseti asilimia tatu, kwa mtu yeyote anayefanya biashara ya mtandao lakini biashara hiyo inafanyika na wananchi wa Ufaransa. Tukisema watu hawa ni watu kama YouTube, Facebook, Instagram, Amazon na watu wote wale ambao ndiyo wenye biashara zao za mtandao. Wenzetu wakenya kwenye Finance Act ya mwaka 2019 wame-introduce Digital Service Tax.. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nayasema haya kwa sababu tutakuja kukutana kwenye Bajeti Kuu ya Taifa kuiomba na kuishauri Serikali kuanza kuondoa fikra kwenye kumbana Mtanzania wa kawaida anayetumia mtandao na kupeleka fikra kwenda kuwabana wale wanaopata pesa kupitia mtandao. Tukitumia takwimu hizi vizuri na tukiweza kutengeneza mifumo mizuri ya kuhakikisha biashara zinazofanyika duniani kupitia mitandao ambazo wateja na watumiaji wake ni wananchi wetu wa Tanzania hawa tunaowataja milioni 53, milioni 29, milioni 32 tuna uwezo kwanza kumsaidia Mtanzania kupata mawasiliano mazuri zaidi lakini kuiongezea Serikali mapato bila kumuumiza Mtanzania wa kawaida anayetumia mtandao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza content nyingi za habari zinapita kupitia mitandao. Hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani michango wanayoitoa, kazi wanazozifanya asilimia 90 zinapita kwenye mitandao na siyo kwenye traditional media systems. Hapa tunapozungumza TCRA waje watuambie wakati tunahitimisha hotuba hii ya bajeti, hatuna aggregator wa YouTube ndani ya nchi yetu, wote hawa unaowasikia wanaotusaidia na sisi, ukisikia Millard Ayo YouTube Channel wanafanya aggregation yao ya content wanayoi-air kwenye online platforms kupitia nchi nyingine. Wapo wanaofanya Kenya, Afrika ya Kusini na wapo wengine vijana wa Kitanzania wanaofanya Marekani na hata kulipwa inabidi walipwe kwa accounts za Marekani. Hii si tu inatupunguzia mapato lakini inatengeneza urasimu mkubwa kwa vijana wetu ambao wangeweza kupata tija kubwa zaidi kwenye sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo la pili, nizungumzie maeneo ya Pay TV. Zipo leseni TCRA wanazitoa za Pay TV ambapo moja kati ya TV hizi ni kama Wasafi. Moja kati ya masharti wanayopewa kwanza hawaruhusiwi kutoa any live coverage including coverage za matamasha yao ya muziki wanayoifanya. Leo tuna vijana wasanii wanafanya kazi kubwa, wametoa ajira kwa vijana wengi, lakini matamasha hata ya kwao yenyewe wanashindwa kuyaonyesha live kwa masharti wanayopewa na TCRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu pekee kinachoruhusiwa kuonyeshwa live ni mpira wa miguu. Sasa wakati tunaendelea kuuenzi mpira kama ajira kwa vijana tukumbuke vilevile na tasnia ya sanaa ya muziki na yenyewe ni ajira kwa vijana wetu. Inapoonyeshwa live Pay TV zinazoonekana kwenye mitandao ya DSTV zinaonekana Afrika na dunia nzima, wataitangaza nchi yetu na tija tutaiona hata kwenye utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotengeneza masharti haya tuangalie Wizara hii kwa suala mtambuka kwa maana inagusa maeneo yote ya uchumi wa Taifa hili. Tunapokuwa na mifumo ambayo utekelezaji wake unabana fursa badala ya kutanua fursa tunawaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho niungane na wewe na wachangiaji waliotangulia na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ni shirika letu la TTCL, kama kweli Serikali inataka kufanya biashara ifanye biashara. Hatuwezi kuwa na Shirika ambalo fedha haziendi, tumechukua deni la Mkongo tumepelekea Shirika kulipa tabu, sisi wenyewe Serikali ni wateja wa Shirika hatulipi madeni yetu, naomba tuweze kutengeneza seriousness katika kusaidia Shirika letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine itafika wakati tutalichukulia hili suala hili kidogo personal kwa sababu tushukuru Serikali tunaye Mkurugenzi kijana na masuala ya TEKNOHAMA haya huwezi kuyatofautisha sana na vijana hata mtaalam wangu Mheshimiwa Getere angekuwepo angesema, ni masuala ambayo yanaendana na vijana. Sasa tumuunge mkono, tusiwe sisi wenyewe Serikali tunataka tufanye biashara, lakini sisi wenyewe tukidaiwa madeni hatulipi, sisi wenyewe hatuwekezi na ndiyo wa kwanza kuwasema kwamba hawatekelezi majukumu yao ipasavyo. Kwa hiyo, Waziri utusaidie na useme humu Bungeni maana mengine inawezekana na wewe yapo nje ya uwezo wako kwa maana ya Wizara yako inatakiwa iwezeshwe, Wabunge tulisaidie Shirika letu la TTCL liweze kupewa uwekezaji wa kutosha liweze kushindana kwenye ushindani wa kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kurudia tena kwamba tunavyotengeneza masharti yanayosimamia tasnia hii ya mitandao, basi tutengeneze masharti ambayo yanaendana na masuala mengine ya kidunia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Balozi Libelata Rutageruka Mulamula kwa uteuzi wake wa kuwa Waziri wa Wizara hii, lakini na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii vilevile kuwapongeza Watendaji Wakuu wa wizara, kaka yangu na rafiki yangu Balozi Joseph Edward Sokoine na Mheshimiwa Balozi Fatma Mohammed Rajabu kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Mambo ya Nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuteua wanadiplomasia wabobezi kwenye Wizara hii, lakini kwa kuzingatia si tu mgawanyiko wa Muungano wa nchi yetu lakini vilevile na jinsia kwenye teuzi zake. (Makofi)
Mimi naamini kama wachangiaji wengine kwamba ubobezi wa wana diplomasia hawa kwenye Wizara hii utaleta matokeo chanya kwenye utendaji wa kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kazi yetu sisi ni kuwaunga mkono, kuwatia moyo na kuendelea kuwasadia kuhimiza Serikali kutenga fedha za kutosha kama walivyoomba kwenye bajeti yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeisikiliza kwa makini hotuba ya Mheshimiwa Waziri na mimi niungane na wenzangu kupongeza kazi kubwa Wizara hii inayofanya kwenye eneo la economic diplomacy, wamefanya kazi kubwa, miradi mingi inatekelezwa na Wizara hii inaratibu na yapo mambo mengi baadhi ya Wabunge walioanza kuchangia wametoa wito, namie nitoe wito kwa Wizara hii kuongeza nguvu kwa kuisemea na kuitangaza nchi yetu. Na mimi naamini kama Serikali itachukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge Balozi Pindi Hazara Chana na kufungua Balozi nyingi zaidi, lakini si tu kufungua Balozi na kuziweka strategic, umetolewa mfano mzuri sana hapa, leo watanzania wengi wanakwenda China kufanya biashara, lakini ukimuuliza mtanzania wa kawaida kama amewahi kufika ubalozini Beijing hata hafahamu ni eneo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Watanzania wangi wanafanya biashara kweye Miji ya Guangzhou, Shenzhen, Yuan na hata kama tutashindwa kupata Balozi mdogo basi hata ukipata Honorary Consular maslahi ya Watanzania kibiashara yatalindwa kwenye maeneo yale. (makofi)
Mheshimiwa Spika, ningeomba Wizara imefanya kazi kubwa kwenye utalii, lakini iongeze kazi kubwa ya kutangaza utalii kwenye balozi zetu kwa sababu utalii ni moja ya kati ya sekta ambazo inategemewa sana kwenye uchumi wetu kutuingizia pato la kigeni.
Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu ningeomba kuchangia kwenye eneo la itifaki, ukurasa wa 87 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Na ningemuomba Waziri pamoja na ubobezi wao wa diplomasia nimrudishe kwenye sheria, kwenye Katiba ambayo ndio sheria mama ya nchi yetu. Nimuombe Waziri nimrejeshe kwenye Ibara ya 4(2) ya Katiba yetu ambayo inaeleza utawala wa nchi yetu ulivyogawanyika katika mihimili yake mitatu; kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakama. (Makofi)
Lakini nimrudishe kwenye Ibara ya 62 ya Katiba yetu ambayo inalitaja Bunge na kuelezea kazi na mamlaka ya Bunge letu. Lakini Ibara ya 66 inayowaelezea Waheshimiwa Wabunge, Ibara ya 84 inayomwelezea Spika wa Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini na Ibara ya 85 inayomwelezea Naibu Spika na Ibara ya 105 inayoelezea Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini naeleza ibara hizi? Kumekuwa na dhana na wenzetu wanaosimama itifaki ya shughuli zetu za kitaifa. Unakwenda kwenye shughuli ambayo Mheshimiwa Spika amehudhuria, unafanyika utambulisho Mheshimiwa Spika hatambulishwi. Si tu kutokumtambulisha ni fedheha kwake yeye binafsi, maana inawezekana Spika wetu Job Ndugai wote mnafahamu ni mtu rahim na mtu ambaye hana makuu. Lakini usipomtambulisha Spika maana yake umeamua wewe mwenyewe kuandika Katiba yako mpya na kuondoa Bunge ambalo linawakiwalisha wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini haiishii kwa Spika, zipo shughuli nyingi wanakwenda Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Wabunge wakienda vilevile tusiangalie wao kwa majina yao, wanakwenda kuwawakilisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye shughuli zile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ziko shughuli anakwenda Mheshimiwa Naibu Spika, ziko shughuli wanakwenda Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Ziko baadhi ya shughuli ambazo uratibu wa itifaki una-fail na Waheshimiwa Wabunge wanakuwa kama ma-gate crasher kwenye shughuli zile. Kuingia tabu mpaka watu waulizane wee mtu asimame pale mlangoni kila anayepita anakushangaa, bwana vipi! Tupo tumekuja kwenye shughuli. Kila anayepita anakuonea imani, wamekuona? Enhee wameniona wanashughulikia. Mpaka itokee hisani ama kiongozi wa itifaki afike aseme basi andika jina lako uingie. Lakini ndani ya shughuli ile utambulisho utatambulishwa sisemi kwa sababu Babu Tale hapa hayupo mpaka wasanii watatambulishwa, Mheshimiwa Mbunge hajatambulishwa.
Sasa hatusemi haya kwa maana tu ya kusema labda Wabunge wanataka makuu, hapana. Nayasema haya kwa kuwa Katiba inatambua nafasi hizi. Shughuli inapoandaliwa, viongozi wanapoalikwa, wanapofika wapate heshima na stahiki inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiri Mheshimiwa Waziri ameliona, Mheshimiwa Naibu Waziri ameliona na Mheshimiwa katibu Mkuu ameanza kulifanyia kazi, ni Mabalozi wazuri wanafanya kazi vizuri sana. Nalisema kuweka kumbukumbu sahihi kwa kuwa nawaamini sana viongozi hawa niliowapongeza mwanzo wa mchango wangu. Kulikuwa na dhana kwamba shughuli hii inaandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, shughuli hii inaandaliwa na TPDC, shughuli hii inaandaliwa na TANESCO, ukisoma vizuri utaratibu wa shughuli za Kitaifa na za Kimataifa huwezo ukaondoa majukumu ya Idara ya Itifaki ya Wizara ya Mambo ya Nje katika kusimamia itifaki ya shughuli zile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe Waziri bahati nzuri umekuja na mzee na nilidhani atatoka baada ya kutambulishwa, lakini amebaki. Kwa heshima yake, twende kwa utaratibu wa kushauri, naamini ukija kuhitimisha hotuba yako utahitimisha vizuri na kunyoosha itifaki ya shughuli zetu.
Mheshimiwa Spika, na nikuambie kwa dhati ya moyo wangu, ikitokea tena Spika wangu wa Bunge hili aidha kwa makusudi ama kwa bahati mbaya kwenye shughuli yoyote hakutambulishwa au hakupewa itifaki inayostahili Mheshimiwa Waziri utakutana na jambo linaitwa Azimio la Bunge na wala usitafute mchawi, mimi nimeamua kununua hiyo kesi. Lakini sina shaka na wewe, sina shaka na Naibu Waziri wako na watendaji wako, naamini mtajipanga vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako hayo na mengine madogo madogo tu, hata Rais wetu anaenda kwenye shughuli haijulikani gari linasimama wapi, anashuka watu wamejipanga upande huu anashukia upande mwingine. Ni majukumu yenu, chukueni role yenu ya itifaki na msikubali mtu yeyote akachukua majukumu ambayo sio ya kwake kwa kuwa majukumu ya itifaki ni majukumu yenu chini ya Wizara yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naamini haya yakifanyiwa kazi na yale ambayo wachangiaji wenzangu wamechangia, Wizara hii ikawezeshwa kwa fedha sit u kutengewa fedha lakini kuhakikisha fedha zinapelekwa hasa katika uwekezaji wa majengo ya ubalozi kwenye nchi ambazo tuna uwakilishi na kufungua Balozi nyingine za ziada. Wizara hii ikija hapa mwakani itakuja na mafanikio makubwa kuliko ilivyofanya hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kunipa nafasi kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza, niungane na Wabunge wengine kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya katika usambazaji wa umeme wa REA. Sisi Wabunge wa majimbo ya mijini tunanufaika na usambazaji wa umeme wa Mradi wa Peri- Urban kwenye kata zote za Jimbo la Ukonga na kazi inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu napenda kujikita kwenye maeneo mawili. La kwanza ni ujenzi wa LNG Plant kule Lindi.
Niipongeze Serikali na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ukurasa wa 68 ameelezea hatua zilizofikiwa na mipango ya Serikali ya kuhakikisha ujenzi huu unakwenda kwa kasi ama mazungumzo baina ya Serikali na wawekezaji yanakamilika kwa wakati kama vile Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa kutumia timu ile iliyopata uzoefu kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta la Uganda ama East Africa Crude Oil Pipeline kuitumia katika negotiation ya mradi huu. Niiombe Serikali ifanye kila liwezekanalo kuhakikisha mazungumzo haya yanafanyika kwa wakati, lakini katika kuzungumza huko Serikali ijitahidi sana kutotumia haraka lakini kuweka mbele maslahi mapana ya Taifa. Kwenye hotuba ya Waziri ameelezea kwamba tayari fidia ya eneo imeshafanyika sasa zile hatua zilizobaki za pre- FEDD decision, FEDD decision yenyewe lakini final investment decision na mpaka mradi uanze zifanyike kwa utaratibu mzuri ili Taifa liweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba kuishauri Serikali wakati negotiation zinaendelea ifanye micro and macroeconomic study ili kuweza kuona mradi ule pamoja na faida zile za kifedha zitazopatikana kwenye mradi lakini faida nyingine mtambuka kwenye maeneo yale ya Lindi na Mtwara na maeneo mengine ya Taifa letu. Faida hizo ni muhimu ziweze kufahamika na kujulikana ili Serikali inapoingia kwenye mradi ule iingie kwenye jambo ambalo ukiangalia mtazamo mzima wa negotiation kwenye open book economic model haziangaliwi basi ziweze kuwa covered kwenye micro and macroeconomic study.
Mheshimiwa Spika, lakini tujifunze kwa Mozambique, wenzetu wameanza wako katika hatua nzuri sana na hivi tunavyozungumza mnafahamu vinafanyika vikao vya SADC katika kuangalia hali ya usalama ya Msumbiji. Niiombe Serikali itumie vikao hivi hivi kuweza kujifunza kwa wenzetu ili na sisi tufahamu hivi tunavyo-negotiate hatuhitaji msaada wa utaalamu maeneo mengine, hatuhitaji ushauri wa majirani zetu ili mradi huu uweze kufikiwa na Tanzania iweze kupata mapato.
Mheshimiwa Spika, kwenye huu ukurasa wa 68 mradi huu utagharimu siyo chini ya dola bilioni 30 sawa na trilioni 70 za kitanzania. Mradi huu ukianza kuzalisha mapato yanakadiriwa kuwa siyo chini ya dola bilioni 3 kama trilioni 7 kwa taifa letu. Niombe kuungana na wachangiaji wa jana akiwemo Mheshimiwa Getere kama itaipendeza Serikali akina Mheshimiwa Kalemani hawa wakipatikana wawili mmoja akahangaika na huu umeme wa REA akapatikana Kalemani mwingine kuhangaika tu na mradi huu wa gesi asilia itasaidia taifa kuweza kuongeza kasi na ufanisi katika kutekeleza mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kuchangia kama walivyosema wachangiaji wenzangu, niipongeze Waziri, Naibu Waziri na uongozi wa Wizara kwa kushirikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kufanya kazi adhimu ya kulinda kodi na mafuta ya nchi yetu. Ziko dhana nyingi wakati mwingine sisi wenyewe Watanzania tunapenda kujidharau na kuthamini vitu vya nje. Naomba Serikali katika jambo hili ilitilie mkazo na ilifanye kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme Waziri wa Viwanda na Biashara ama Serikali kwa ujumla TBS iwezeshwe iweze kufanya kazi hii kwa ufanisi. Nasema hivyo maana hivi tunavyozungumza vifaa vidogo tu vya detection ya vinasaba bado TBS hawajapeleka EWURA. Wizara ya Viwanda na Biashara iko hapa, Serikali iko hapa iweze kuongeza nguvu, jukumu walilopewa ni kubwa iongeze nguvu TBS ifanye kazi hii kwa ufanisi kwanza kwa usalama wa Mtanzania lakini pili kwa usalama wa Taifa letu lakini tatu tunaamini Shirika hili ni la kizalendo na ni la Tanzania ambapo manufaa yoyote yatayopatikana yatakuwa kwa Watanzania. Serikali ifungue macho zaidi maana inawezekana Shirika hili likakwamisha mradi huu ili kuonekana tumefeli kuweza kujenga hoja maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 iliyowasilishwa hapa Bungeni na Waziri wa Fedha tarehe 10, Juni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kidhati kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuja na bajeti iliyobeba matumaini mapya kwa Watanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee maeneo mawili makubwa ambayo bajeti hii imekuja na matumaini mapya. Mosi; bajeti hii imekuja kujibu lile swali ambalo Watanzania wamekuwa wakijiuliza kuhusiana na uendelezaji wa miradi yetu ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma bajeti hii – naomba kunukuu – inasema hakuna mradi hata mmoja utakaokwama bila kusimama hata kwa mwezi mmoja. Na maneno haya yanachukua uhalali wake kwenye maneno aliyoyasema Rais wetu tarehe 06, Aprili, pale Ikulu, Dar es Salaam akiapisha Makatibu Wakuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema, naomba kunukuu;
“Tuna urithi aliyotuachia marehemu Rais wetu; miradi mikubwa miwili” – akimaanisha Mradi wa Bwawa la Nyerere na Mradi wa Standard Gauge – “na miradi mingine midogomidogo.”(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anaendelea kusema; wanasema ukifanya vibaya kwenye urithi, Mungu anakulaani. Aliyekuachia urithi hana radhi na wewe, na Mungu atakulaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa siyo maneno ya Mheshimiwa Rais, lakini naamini neno urithi unaweza ukaliondoa ukaweka neno wosia. Kwa maana yako maneno aliwahi kuyasema mwendazake. Naomba kunukuu;
Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliwahi kusema, akizungumzia miradi hii mikubwa ya kimkakati, alisema;
“Mimi ni dereva tu, lakini pia najiuliza, ikiwa siku moja Mungu atanichukua hawa wanaokuja watakuja kuyamaliza kweli?”(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu tarehe 06, April wakati Mheshimiwa Rais anaelezea ule urithi, alikuwa anazungumzia kauli hii. Na ukisoma sentensi hizi, maneno aliyoyasema Hayati Magufuli, liko neno ikiwa siku Mungu atanichukua. Hakuelezea kwamba ikiwa atafika mwisho wa ukomo wa utawala wake kwa mujibu wa Katiba; ni maneno mazito sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema bajeti hii imekuja kujibu kiu ya Watanzania, imekuja kujibu wosia aliotuachia Hayati Magufuli na imekuja kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inakwenda kutekelezwa na kukamilika kwa asilimia 100. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili; bajeti hii imekwenda kutoa majibu ya kero zilizosemwa hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge. Ukiangalia mijadala yote, kuanzia tunajadili Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, mjadala wa bajeti mbalimbali, siamini kuna Mbunge yeyote alisimama hapa hakuzungumzia barabara zetu zinazotekelezwa kwa kusimamiwa na TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hapa waliongea kwa hisia kubwa. Na mimi nilikuwa mmoja wao na nilikuwa nasubiri bajeti hii niangalie Serikali imejipangaje kuongeza fedha kwa TARURA. Ukurasa wa 72 zimetengwa shilingi bilioni 322,158,000,000 kwa ajili ya barabara zetu za TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku hapa hakukosi swali la Wizara ya Maji. Na hisia za Wabunge zilijionesha sana kwenye bajeti ya Wizara ya Maji. Bajeti hii imekuja kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya; kwenye majimbo yetu wananchi wamejenga maboma, Serikali imeshindwa kumalizia. Pamoja na ujenzi mkubwa wa miundombinu ya afya, vituo vya afya, vifaatiba, wataalam, dawa; bajeti hii imekuja na mwarobaini wa kutatua kero hizi za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi ambayo bajeti hii imeyagusa. Lakini naomba niseme; ili kufadhili miradi ya maendeleo – wataalam wa uchumi wanafahamu na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni mtaalam wa uchumi – ziko njia nne. Njia ya kwanza ni mikopo, ya pili ni misaada, ya tatu ni fedha zetu za ndani, na ya nne ni venture capital ama PPP ama miradi inayosajiliwa na sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii tunayoikopa tukisema tutatekeleza miradi yetu kwa mikopo tunabebesha Taifa letu mzigo wa uchumi wa sasa, watoto wetu na wajukuu zetu. Leo kwenye bajeti hii deni la Taifa ni himilivu kwa mujibu wa international standards ambazo zinataka deni la nje lisizidi asilimia 50; deni la Taifa letu ni asilimia 17. Deni la nje na ndani ukichanganya kwa pamoja kwa vigezo vya kimataifa halipaswi kuvuka asilimia 70; leo sisi tuko asilimia 27, tunafanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ziko nchi za majirani zetu, takwimu hizi zipo, zimekopa mpaka sasa ziko nje ya vigezo hivi. Lakini maeneo mawili salama, ukiacha eneo la misaada ambalo wote mnafahamu misaada hii inakuja na masharti, na masharti mengine ni magumu, hatuwezi hata kuyataja humu kwenye Bunge hili, tunabaki na maeneo mawili salama zaidi ya ku-finance miradi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kwanza ni kodi zetu sisi wenyewe. Naomba ninukuu maneno ya Hayati Dkt. Magufuli aliyoyasema kule Kyela; alisema tunajenga vituo vya afya, barabara kwa fedha zetu. Alisema Tanzania inatakiwa iwe mfano kiuchumi katika dunia, yale mawazo ya kufikiri kuna mtu ataleta misaada tuyapoteze kichwani, ule ni ugonjwa mkubwa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema; Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali ya wala rushwa. Lakini pamoja na TRA na Serikali kupambana kuongeza wigo wa kodi, mpaka sasa walipa kodi walioko kwenye tax base ya TRA ni watu milioni mbili na laki saba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini? Kwa sababu tulikuwa kwenye semina pale Ijumaa; sekta kubwa ya Watanzania iko kwenye sekta isiyo rasmi. Kwa hiyo, ukisema unapanua wigo wa kodi utabaki palepale kwa watumishi, palepale kwa walimu wetu, palepale kwa wafanyakazi wetu, palepale kwa kuwaumiza wafanyakazi kwa kodi za mishahara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upande wa pili…
NAIBU SPIKA: Sekunde 30.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upande wa pili, tunao mtandao mkubwa wa watumiaji wa simu za mkononi kwa laini zisizopungua milioni 52; hawa ndi Watanzania wanaoteseka kukosa dawa. Tunayo miamala ya fedha kwa Januari mpaka Desemba, 2020 ya jumla ya trilioni 201; hapa wako wanaotuma miamala tukiwemo wale tunaotuma na ya kutolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Watanzania tukubaliane kugharamia bajeti yetu sisi wenyewe. Waziri wa Fedha ameupiga mwingi sana tarehe 10, ametoa hotuba nzito sana, ameupiga kama Bernard Morrison, siyo Morrion huyu, Morrison yule aliyekuwa Dar Young Africans. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi/Vigelegele)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. JERRY W. SILAA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwashukuru wote, tumepata wachangiaji 20 ambao wamechangia hoja zote mbili lakini katika hoja ya Kamati ya Bajeti wametaja mashirika ambayo na sisi tunasimamia kwa haraka haraka Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mheshimiwa Christine Mnzava, Mheshimiwa Subira Mgalu, Mheshimiwa Hyuma, Mheshimiwa Esther Bulaya, Mheshimiwa Joseph Kandege, Mheshimiwa George Malima, Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mheshimiwa Dkt. Oscar Kikoyo, Mheshimiwa ShallyRaymond, Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Kwagilwa Reuben, Mheshimiwa Stansalaus Mabula, Mheshimiwa Luhanga Mpina, DKT. John Pallangyo, Mheshimiwa Ally Hassan King, Mheshimiwa Abbas Tarimba na Naibu Mawaziri wawili; Naibu wa Viwanda na Biashara - Mheshimiwa Kigahe na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango - Mheshimiwa Chande. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na maoni na mapendekezo yaliyoko kwenye taarifa ya kamati naomba kama walivyosema wachangiaji wengi niseme mambo machache yafuatayo; niombe tuipongeze sana Serikali na tumpongeze kipekee Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuweka mtaji mkubwa kwenye benki yetu ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa yetu tumeelezea mwezi disemba Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 208 kama mtaji kwa benki hii na juzi tumeona ufaransa benki hii imesaini euro milioni 80 sawa na shililingi bilioni 210 tunaamini fedha hizi zitaenda kuleta tija kubwa kwenye sekta ya kilimo kupitia benki yetu ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe binafsi kwa mwongozo wako kwenye kikao cha leo lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Acskon, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumshukuru Katibu wetu ndugu Nenelwa Mwihambi, Mkurugenzi wa Idara ndugu Athumani Hussein, Kaimu Mkurugenzi msaidizi ndugu Bisile, makatibu wa kamati yetu wakiongozwa na Zainabu Mkamba, washauri wetu wa mambo ya sheria na wataalamu wengine kwa ushirikiano mzuri wanaotupa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kamati yetu inafanya kazi na Msajili wa Hazina ndugu Mgonya Benedict, tunamshukuru sana kwa kazi kubwa anayotusaidia na wataalamu wake ambao anafanya nao kazi, tuwataje ndugu Lightness Mauki, Mkurugenzi wekezaji wa umma, na Linus Kwakesigabo, Mhasibu Msaidizi wambao wamekuwa wakitusaidia sana kwenye kazi zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamezungumza mambo yale tuliyoyatoa kwenye maoni na mapendekezo itoshekusema tu maeneo yote mlioyataja ya APZA, NHIF, MSB, TARURA, NHC, TPA, kwenye maeneo ya TICTS
na kule kwenye uyejushaji wa mafuta, RUWASA, yote tutayafanyia kazi kwa mashirika yale tunayoyasimamia na tunaamini Msajili wa Hazina atatengeneza utaratibu mzuri wa kamati yetu kuweza kufanya kazi ya kusimamia uwekezaji wa mitaji ya umma na mashirika haya yaweze kuleta tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwenye taarifa yetu kwamba gawiwo la mashirika haya ni moja kati ya chanzo kikubwa cha mapato kwenye mfuko wa Taifa, Kamati yetu itaendelea kufanya kazi kwa moyo na uwadilifu wa hali ya juu katika kuishauri Serikali kuweza kuwezesha mashirika haya yaweze kufanya kazi vyema katika kuleta tija na ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho siyo kwa umuhimu niwashukuru sana wajumbe wa kamati Makamu mwenyekiti, Mheshimiwa George Malima na wajumbe wote kwa ufinyu wa muda naomba majina yao yaliyokwenye kamati yaingie kwenye Kumbu kumbu za Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kutoa hoja.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi katika kuchangia na kuliomba Bunge lako pamoja na kuunga mkono hoja ya kuridhia kuiongezea The East African Court jurisdiction ili iweze kufanya kazi ya kutoa tafsiri na kutatua migogoro itakayotokana na zile protocol ambazo wachangiaji wengi wamezitaja nami nitazitaja hapo baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wenzangu kumpongeza kwa dhati Dkt. Damas Ndumbalo, Waziri wa Sheria na Katiba kwa uwasilishaji wake mzuri wa hoja ambayo imetupa uelewa mpana wa Itifaki hii ambayo tunaenda kuiridhia. Vilevile nimpongeze mdogo wangu Keisha kwa uwasilishaji wenye ueledi mkubwa alioutoa hapa kwa niaba ya Kamati ya Bunge na Sheria ya Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza; nimpongeze sana ndugu yangu Abdullah Mwinyi, maana yeye leo hakuchangia ametoa lecture na nimemwomba aandae notisi kina Kingu wangependa kuzisoma, zilete uelewa mpana zaidi na ametueleza na tumepata fursa ya kuona Wabunge wa Afrika Mashariki wenye sifa tunaowapeleka kule wanapokuja kuleta tija kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nchi yetu ni Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa the East African Treaty tuliyotia saini mwaka 1999 na ilivyoanza rasmi mwaka 2001 kama walivyoeleza wachangiaji wengine. Article 9 ya Treaty hiyo ndiyo inayoanzisha vyombo mbalimbali vya kiutendaji, The East African Legislative Assembly, The East African Court of Justice na ukisoma article ile inaipa mamlaka mahakama hii kuweza kutafsiri mambo yanayotokana na treaty ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wote wamesema, mwaka 2004 tumeingia kwenye common customs, tumeridhia kuwa na common custom kwa maana ya custom union ya pamoja, rates za forodha na nadhani Mheshimiwa Abdullah ameelezea vizuri zaidi na ndio maana hapa tukiwa tunapitisha bajeti zile custom measures (jitihada) za Serikali za forodha zinakuwa zimeridhiwa na Nchi zote za Afrika Mashariki na sisi kama Nchi Wanachama tunatakiwa tuendane nazo kwa jinsi Mawaziri wa Fedha wa Nchi za Afrika Mashariki walivyokubaliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010 tumeingia kwenye common market na mwaka 2013 tumeenda kwenye single currency ambayo imeelezewa mchakato wake wa kufikia kule kwa kufanya integration ya chumi za nchi zote wanachama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoombwa hapa leo ni nini? Amekisema vizuri Wakili Msomi Zainab Katimba, ni ile article 27(2) ambayo inaipa Nchi Wanachama ya ile East African Treaty tuliyoingia mwaka 1999 uwezo wa ku- extend jurisdiction ya Mahakama hii ili iweze kutoa majibu kwenye hizi protocols nyingine ambazo kabla ya kuomba ridhaa hii, masuala yote yaliyokuwa ya kimgogoro wa protocol hizi yalikuwa yanaamuliwa na Mahakama za partner state na madhara yake ni nini? Madhara yake kila Mahakama ya Nchi Wanachama itatoa tafsiri kwa kadri ya busara ya Mahakama husika kama mhimili unaojitegemea wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala moja linaweza kujitokeza kwenye nchi mbili tofauti kwa item moja ya common customs, lakini ikapata maamuzi mawili tofauti kwa Mahakama ya Nchi Wanachama na ku-set precedent mbili kwa jambo linalofanana kwa protocol moja. Kwa hiyo, kinachoombwa hapa ni nini? Kinachoombwa hapa ni jambo la kisheria ambalo lipo kwenye treaty la kutaka ku-extend jurisdiction ya Mahakama hii ya Afrika Mashariki ili sasa iwe na nguvu ya kufanya tafsiri na maamuzi wa hizi protocol tatu tulizozieleza kwa maana ya common custom, common market na monitory union na hilo nilishawishi Bunge hili lina faida kubwa katika ule uwanda mpana mzima wa ile nguvu ya kiuchumi tunayoitafuta kama Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata leo tulipokaa hapa Babu Tale hajakaa, tumekaa katika safu moja tu ya kutafuta ile mantiki ya kutengeneza jambo hili kwenye uwanda wake wa kisheria na Mheshimiwa Kingu amekiri kwamba kuna kiti kilikuwa wazi lakini ameshindwa kuja kukaa kwa sababu amesema yeye ameona ajikite na Ole-Lekaita kwenye uchangiaji wa mwisho yeye amejitolea kwenye suala la kupiga makofi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashawishi sana Waheshimiwa Wabunge kuweza kuridhia hoja hii iliyopo mezani ili nchi yetu kama wanachama tuliyoridhia ile East African Treaty mwaka 1999, tuweze ku- extend jurisdiction ya Mahakama hii kwa faida pana ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno hayo, naunga mkono hoja na nirejee tena kuomba Bunge lako liliridhie protocol hii. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako hili linafanya kazi kwa mujibu wa Ibara ya (63) (2), (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaipa mamlaka na madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Spika, nimesikiliza kwa makini sana hotuba ya bajeti iliyosomwa hapa Bungeni leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, nimegundua yapo mambo makubwa ambayo Serikali Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwenye utumishi wa umma. Mambo haya yamefanyika katika kipindi hiki cha mwaka mmoja ambapo Serikali Awamu ya Sita imekuwa madarakani.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana naamini si watumishi wa umma pekee lakini Watanzania wote walipata mshtuko kwa msiba wa kuondokewa na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Spika, kazi iliyofanywa na Serikali ya Mheshimiwa Samia kwa mwaka mmoja, naamini imeleta matumaini makubwa kwenye sekta ya Utumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako maandiko kwenye Quran Tukufu iko sura alishushiwa Mtume Muhammad (S.A.W) Mwenyezi Mungu akitaka kumtia moyo na sura hii nitaisema hapa. Sura inasema walaak ahkirut kairulaka minaluula. Bila shaka wakati ujao utakuwa ni bora zaidi kuliko wakati uliotangulia. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa. (Makofi/Vicheko)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa ukae kuna Wabunge wawili wamesimama hapa. Mheshimiwa Mohamed.
T A A R I F A
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hii aya ambayo ameinukuu, ameinukuu vibaya. Sasa kwa mujibu wa Quran Tukufu na kwa mujibu wa dini yetu ya Kiislam ukibadilisha herufi moja, umebadilisha maana. Kwa hiyo naomba kumpa taarifa kwamba aya hii inatamkwa walal- akhiratu khairulaka minal uula. (Makofi)
SPIKA: Haya sasa, Mheshimiwa Jerry Silaa hiyo ilikuwa ni taarifa ambayo nafikiri sasa hili jambo ili likae vizuri chukua yeye alivyoinukuu halafu iseme kwa tafsiri. (Vicheko/Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana mtoa taarifa, Kiiarabu changu kidogo kimechanganyika. Kwa hiyo niombe kumbukumbu sahihi za Bunge zichukue kiarabu cha mtoa taarifa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema wakati huu umekuwa bora kuliko wakati uliotangulia? Ni kwa mambo makubwa ambayo yamefanyika kwenye utumishi wa umma. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumeona watumishi 190,781 wamepandishwa madaraja na Mheshimiwa Waziri ametueleza hapa kwamba watumishi wengine 92,619 watapandishwa madaraja kabla ya mwezi Juni mwaka huu 2022, ni kazi kubwa sana, tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri vile vile kwenye Hotuba yake ameeleza kwamba wako watumishi 13,495 wamepata ajira mpya, maana yake nini? Wako Watanzania 13,495 waliokuwa tegemezi na leo nao wamekuwa wanategemewa kwa kupata mishahara kupitia utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wako watumishi 21,127 wamefanyiwa recategorization kwenye kada zao za utumishi. Sasa maana sahihi ya recategorization nadhani Mheshimiwa Dullo utamtafsiria Babu Talle ili aelewe kazi kubwa iliyofanywa na Serikali hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako mambo Serikali imefanya, siyo kwenye Wizara hii lakini yana impact kwenye Wizara ya Utumishi wa Umma. Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetoa non cash bond ya trilioni mbili kwa Mfuko wa Pensheni wa PSSSF ambayo imefanya Mfuko huu kuweza kulipa pensheni kwa wakati. Jana nimezungumza na Mkurugenzi Mashimba, leo tunavyozungumza hapa wastaafu wa mwezi wa tatu tayari wanalipwa pensheni zao, ni kazi kubwa sana imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa agizo la kuongeza wanufaikaji wa Mfuko wa Bima ya Afya, wale wategemezi toka umri wa miaka 18 mpaka umri wa miaka
21. Hivi tunavyozungumza wako watu 77,345 ambao walikuwa wamevuka miaka 18 na ilimpasa mtumishi kama ni mtoto wake atoe pesa mfukoni kumuhudumia matibabu, leo wanahudumiwa na Mfuko wa Bima ya Afya na yenyewe ni jambo kubwa kwenye utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako mambo mengi kwa sababu ya muda niseme tu, Mheshimiwa Rais kwa kuthibitisha mapenzi yake na watumishi wa umma wa nchi hii amemteua mtu bingwa kabisa, mwanamke aliyehudumu ndani ya Bunge hili kwa muda mrefu kuliko akinamama wengin,e amekuwa Mbunge wa Viti Maalum lakini amekuwa Mbunge mbobezi wa Jimbo la Peramiho. Amepita Wizara ya Elimu anajua matatizo ya watumishi Walimu. Amekuwa Chief Whip hapa Bungeni na tumeona wote kazi yake. Amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, siyo mwingine ni binti wa Katekista wa Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Magigi Mhagama ambaye watu wa namna hii ndiyo wale King Kiba (Ally Kiba) aliwaimba kwenye kibao chake cha utu. Pamoja na upole na uzuri wake lakini amejaliwa utu na utulivu wa hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imetangaza ajira mpya 32,604. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, niiombe Serikali ajira hizi ziende kuajiriwa kwa haki. Ningetamani sana ajira hizi 32,604 kama vile zigawanywe kama zile pesa za TARURA kila Jimbo lingepata. Nafahamu ziko sheria za Utumishi wa Umma, nia yetu ni kuona kwamba ajira hizi zikitoka maana nadhani kila Mheshimiwa Mbunge hapa ana meseji ya ajira hizi za 32,000. Ni ombi langu, ama ni ushauri wangu kwa Serikali ajira hizi zikitoka tuzione zimetapakaa nchi nzima kwa usawa. Tuone kwenye Majimbo yetu kama kweli ajira 32,604 basi kila Jimbo takribani watu 100 wawe wamepata ajira. Ikifanyika hivyo italeta usawa kwa Taifa, italeta uhimilivu kwa Taifa na itaondoa ile kero ya unemployment kwetu sisi sote kwa umoja wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, nilipita Tabora tarehe 12 Aprili nilikutana na mzee Ramadhani Ally Mkwande, yeye ni mstaafu wa TTCL. TTCL ilikuwa na mkataba na NSSF kulipa pensheni za watumishi wake na wao ni moja kati ya wale watumishi ambao bado wanalipwa shilingi 50,000 kwa mwezi, aliniomba nije kusema Bungeni na nimeona nimtendee haki. Tunaiomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ijaribu ku-standardize watumishi wote wafike kile kiwango cha shilingi 100,000 wanachopata pensioners wengine ili na wenyewe waweze kuendesha maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda la mwisho la kusema, niliongea kidogo pale kwenye Mfuko wa PSSSF kwenye ile bond ya two trillion aliyoitoa Mheshimiwa Rais kupitia Serikali yake. Niseme tu Kamati ambayo Bunge lako limekasimia kazi ya uwekezaji inasimamia Mifuko hii, kazi kubwa imefanyika lazima tuseme. Kazi kubwa imefanywa na Serikali kuweza kutengeneza liquidity kwenye Mifuko hii na kazi kubwa inaendelea kufanyika. Nikuombe na niliombe Bunge lako Tukufu, tuendelee kuwatia moyo, tuendelee kuikumbusha Serikali kwa adabu, lakini mwisho wa siku naamini pensioners wa nchi hii wataendelea kupata pensheni zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; naanimi kuna mtu atajitoa huko mbele ya safari utaniongezea muda kwa kuanzia.
Mheshimiwa Spika, naomba kwanza kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa uteuzi wake, Mheshimiwa Kairuki ni mtu muungwana. Tarehe mbili mwezi wa pili aliniahidi hapa kwamba atakuja ukonga nilithibitishie Bunge lako tarehe 23 Februari alikuja na hakuja kufanya kazi ndogo, alifanya kazi kubwa sana, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wakati nachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga mwaka 2020 bajeti ya TARURA Wilaya ya Ilala ilikuwa bilioni 8.3 na iliyokuja Jimbo la Ukonga ilikuwa bilioni 2.2. Hivi tunavyozungumza mwaka wa fedha 2022/2023 bajeti hii ya Wilaya ya ilala imefika bilioni 24, na kwa Jimbo la Ukonga peke yake zimekuja bilioni 11.7 zaidi ya mara sita ya bajeti tuliyoikuta; ni kazi kubwa sana imefanyaka tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Chanika – Umbozi inajengwa kwa kiwango cha lami, Barabara ya Mombasa – Mazizini ile eneo la Mombasa lilioharibika barabara hii tulijenga wengine tukiwa madiwa imerudishwa lami na taa za barabarani.
Mheshimiwa Spika, na barabara nyingine ambazo Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up hapa nitataka anipe maelezo ni zile za mapato ya ndani Majoe, Mwanagati na Kitunda. Nilikueleza kwamba halmashauri haiwezi kujenga barabara, ikainyang’anya TARURA jukumu hili leo ni mwezi wa nne hawajaanza wako kwenye mchakato wa manunuzi.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la ujenzi wa BRT awamu ya tatu ujenzi umeanza na umeanza kwa kwasi sana Gongolamboto – Kariakoo. Ninachoomba Mheshimiwa Waziri miradi hii imeasisiwa mwaka 2004 imeasisiwa kipindi ambacho Gongolamboto ndio mji mkubwa leo mji umeheama, imeasisiwa kipindi ambacho mradi wa SGR haujajengwa leo SGR imechukua eneo. Imeasisiwa kipindi ambacho mwaka 2004 Kilitex kulikuwa na kiwanda, leo kuna kiwqnda cha kioo na kina mkopo wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Spika, Nimuombe Mheshimiwa Waziri hebu acha alama kwenye mradi wa BRT, mradi uende mpaka Pugu ni kilomita nne tu kuongezea pale. Lipo eneo la kutosha la maegesho, lipo eneo la kutosha la kituo, lipo eneo la kutosha watu wa Kisarawe Chanika na Pugu Stesheni, kwenye stesheni mpya ya SGR watatumia mradi huo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali lakini hali ya barabara kwenye Jimbo la Ukonga ni mbaya sana. Pamoja na bilioni hizi 11 bado Barabara za Kitunda, Kivule, Msongola, Mwanagati kuja Kitunda, Magore, Kwa Mperemba, Bombambili, Majohe, Viwege, Pugu Stesheni na Zingiziwa hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Spika, jana Mheshimiwa Bonnah hapa alisema mvua zimeshesha barabara zimekatika. Wananchi wamenituma kuja kuiomba Serikali; tulikuwa tunakaa hapa, Mbunge wa Mbeya mjini anakaa hapa kulilia miradi ya World Bank, Mbunge wa Nyamagana wenzetu TaCTIC imeanza, leo hata tukiwasalimia hamtuitikii. Kuna mradi wa rise upo kwenye majimbo mbalimbali Jimbo la Ruangwa lina rise bilioni 300 zimeenda kule, sijui hata Mbunge wa Ruangwa ni Mheshimiwa nani humu ndani bungeni. Basi! nafuta kauli ya Ruangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sasema hivi kwa sababu ule mradi wa DMDP ule ambao tunaambiwaga utaanza Dar es salaam niseme ukweli hauanzi leo wala kesho. Waheshimiwa Wabunge niwaombe, Waheshimiwa Wabunge wote humu mnakaa majimboni mwenu lakini mnao wananchi wenu wanakaa Dar es salaam hali ya barabara ni mbaya. Niiombe serikali ije na mkakati wa kutatua kero hii kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza matumizi ya mafuta kwa siku kwenye nchi yetu ni lita takribani 10,700,000 katika hizo lita 3,400,000 zinatumika Dar es salaam sawa na silimia 31. Ukisikia hotuba ya Waziri jeuri yote ambayo TARURA wanaitumia sasa ni ile shilingi mia iliyoongezwa kwenye mafuta ambayo Wabunge waliipigia kelele kila wakati hapa na Serikali wakati huo ilikuwa inakaidi. Baada ya shilingi mia ile kuongezwa leo mafuta yanapatikana lakini barabara za TARURA zinajengwa.
Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge wa Dar es salaam tunaomba kwa mafuta haya ya asilimia 31 iongezwe shilingi mia kwa lita tupate angalau bilini 130 za kujenga barabara. Leo bei ya mafuta Ngara ya EWURA ya mwezi huu ni shilingi 3,050, bei ya mafuta kwa Dar es salaam ni shilingi 2,847. Ukiongeza shilingi 100 kwa Dar es salaam bei ya Dar es salaam itafanana na Arusha itafanana na na Chemba ambako nako kuna Watanzania lakini zitapatikana pesa za kujenga barabara.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa tunataja mradi wa DMDP ilhali mradi huo haupo. Naomba sana zitafutwe fedha za ndani ili Watanzania wanaoishi Dar es Salaam waweze kujengewa barabara.
Mheshimiwa Spika, kwa dakika moja naomba unisaidie mambo mawili. Jambo la kwanza naomba unisaidie kuwaambia wananchi wangu wa Jimbo langu la Ukonga kwamba kazi ya Mbunge ni kusema hapa Bungeni; na ndiyo kazi ninayoifanya sasa. Ilifikia wakati nikataka kutengeneza bango niweke picha ya Mheshimiwa Kairuki na namba yake ya simu na ya Injinia Seff wa TARURA. Maana kule ukisema Mbunge una-post salamu za pasaka yesu amefufuka mwananchi anakujibu achana na mambo ya Yesu jenga barabara; unapost post ya Ramadhani Kareem mtu anakuambia unatoa wapi nguvu za kufuturisha wakati barabara ni mbovu kazi hii hapa.
Mheshimiwa Spika, la pili unisaidie kuwaambia wapiga kura wangu kanuni ile ya 170; maana jana nilikuwa jimboni kule Majohe tukaingia kwenye matope mwananchi mmoja akaniamba Mheshimiwa Mbunge ukienda Bungeni hebu nenda na hayo matope wajue unavyopata tabu. Sasa akiniona hapa na suti inawewezekana akaniona siko serious. Kumbe ni aknuni zako ndio zinatupelekea kuja hapa kwa mavazi haya wala haina maana yoyote kwamba sikereki na kero za barabara kwenye jimbo langu.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa dakika hizi sita itoshe, lakini frame ya hiyo shilingi mia ninayo, nitampa Mheshimiwa Waziri, nitampa Waziri wa Fedha. Kwa hiyo sasa kwenye bajeti hii tutafute fedha za ndani tuweze kujenga barabara kwenye jiji la Dar es salaam ili tuwaondolee wananchi hawa kero; ambao wengine ni wapiga kura wenu. Hakuna msiba unao safirishwa kutoka mkoani kuja Dar es salaam, misiba yote inatoka Dar es salaam kwenda mikoani na siasa ya Dar es salaam inaathiri maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nakushukurusana kwa kunipa nafasi hii, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko Mezani ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumpongeza kidhati Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Bwawa la Kidunda shilingi bilioni 329.46 limesainiwa. Bwawa la Kidunda linaenda kuwa Suluhu ya upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye Mkoa wa Dar- es-Salaam. Kazi hii ni kazi kubwa, Mheshimiwa Rais anastahili pongezi kubwa sana. Katika miaka yake miwili moja kati ya mambo makubwa aliyoyafanya ni kuhakikisha tunapata chanzo cha uhakika cha maji kwenye Mkoa wa Dar-es-Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumpongeza kidhati Waziri wa Maji, Mheshimiwa Juma Aweso. Waziri huyu tukianza kutaja sifa zake hapa muda wangu utaniishia, niruhusu nitaje chache. Mheshimiwa Aweso ni mtu mnyenyekevu, Mheshimiwa Aweso ni mtu mpole, Mheshimiwa Aweso anafikika, Mheshimiwa Aweso ni Waziri ambaye ukikutana naye barabarani unaweza ukasema sio Waziri, hajakivaa cheo. Mtu hajapata cheo bali cheo kimempata mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo methali ya Kichina kwamba, kiongozi bora uongozi wake unaanzia nyumbani kwenye familia yake. Mheshimiwa Aweso huyu anaongoza familia mbili vizuri sana na ndio maana Wizara hii haimpi tabu. Sisi hatuna kubwa zaidi ya kumwombea dua; “Rabbana aatiina fii dduniya hassana wafil akhirat hassana.” Mwenyezi Mungu ampe neema yote ya hapa duniani na hata akhera, aendelee kufanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amepata Katibu Mkuu mzuri, Engineer Nadhifa Kemikimba ni mtu aliyekulia kwenye Wizara ya Maji. Kama lile suala la institutional memory hapo ndio mahali pake. Mama mpole, mnyenyekevu ana sifa zote za utumishi wa umma. Tunaona timu hii inaenda kutekeleza ajenda ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kiasi kikubwa na Ilani ya Uchaguzi itatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi pale Dar-es- Salaam tulikuwa na mtu bingwa kabisa, Engineer Cyprian Lwemeja aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa DAWASA. Ingekuwa ni usajili labda sisi tungemkatalia kumsajili huku Wizara ya Maji, mtu bingwa, mtu mzuri, anacheza kama Aziz Ki alivyofanya leo pale Uwanja wa Taifa. Naibu Katibu Mkuu huyu naamini ataisaidia Wizara na Taifa hili katika kutekeleza kazi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji kwenye Mkoa wa Dar-es- Salaam imefika asilimia 95, lakini kwenye Jimbo la Ukonga, jimbo ambalo ndio linaongoza kwa watu kwenye nchi hii, watu 921,957 tuko asilimia 57, lakini Serikali hii ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ziada ya ule mradi uliotoka Ruvu Juu ukapita Kibamba, ukaenda Kisarawe, ukaja pale Pugu, sasa kuna mradi mwingine kule Zingiziwa, Somelo, Ndiole Juu kwenda Msongola, lakini DAWASA wanaenda kutekeleza mradi mkubwa wa thamani ya shilingi bilioni 42, Kata ya Kitunda, Kata ya Kivule, Kata ya Mzinga, Kata ya Kipunguni mpaka kule Chamazi kwa Mheshimiwa Chaurembo na Temeke kwa Mheshimiwa Kilave, wanaenda kupata maji haya na sisi Jimbo la Ukonga tunaenda kufikia hii asilimia 95 ya maji kwenye upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii kule naomba nichukue fursa hii vilevile kumpongeza Engineer Sirila, Mwanamama huyu Mhandisi, Meneja wa Wilaya ya Ukonga ya maji na Engineer Alex Wandu ambaye anahudumia Wilaya ya Kisarawe, lakini anahudumia maeneo ya Jimbo la Ukonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba, kazi hii inayofanywa inaenda kuheshimisha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Serikali hii iliahidi upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 mijini, kazi inayofanyika bilioni 42 hizi za mradi mpya, bilioni saba zile za Mradi wa Pugu - Kisarawe, bilioni 11 za ule Mradi wa Somelo, bilioni 60 zinaenda kuwekezwa kwenye Jimbo la Ukonga ni kazi kubwa sana. Sisi watu wa Ukonga tunasema ahsante sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kweli wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, bilioni 60 hili sasa ni sinia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kubwa, ninachomwomba Mheshimiwa Waziri mwaka 2021, amesoma Pugu kama mimi na amepata shida ya maji, no wonder anafanya kazi ya maji vizuri. Alikuja Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais pale Pugu na alienda pale Pugu Secondary kuona maji yalivyofika kwenye shule ile ya historia ya nchi yetu. Aliahidi mradi ule atakuja kuufungua yeye mwenyewe. Tunaomba Waziri afikishe salamu zetu, tungefurahi kumwona anakuja kuzindua mradi ule wa maji maana ameahidi kufikia Disemba, 2023, Jimbo zima la Ukonga litakuwa limepata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawili madogo ya mwisho, niwapongeze sana. Kama alivyosema Mheshimiwa Mabula, watendaji wote wa Wizara ya Maji, wako wengi, lakini ninaamini watendaji wengi wamepata unyenyekevu na uchapakazi kutoka kwa Waziri wao. Ukienda RUWASA ingawa haihudumii Dar es Salaam, Clement, Kivugalo Mtendaji Mkuu, ni mtu mwema hata alivyotambulishwa asubuhi niliona Wabunge wengi wakipiga makofi, aendelee na moyo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti wangu, Haji Nandule, CEO wa Mfuko wa Maji, amesema pale anafanya kazi nzuri. Ni watu ambao Mheshimiwa Aweso kwa ukaaji wake kwenye Wizara hii ametengeneza timu nzuri na anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe kusema naunga mkono hoja. Naomba sana tupitishe bajeti hii kwa mikono miwili, ili kazi hizi za maji ziende zikamguse Mtanzania na kumtua mama ndoo kichwani, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza. Kwa kuwa muda ni mchache, kwanza nimpongeze kipekee Mheshimiwa Nape Moses Nauye, Waziri; tokea ateuliwe kushika nafasi hii, amerejesha heshima, amani na utulivu kwenye Sekta ya Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye eneo moja tu la TEHAMA na katika hilo nitajikita kwenye kuwa na mfumo mmoja wa kieletroniki katika kuendesha shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kauli nyingi na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye mara tatu akiapisha Makatibu Wakuu, akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu mwaka 2021 na vilevile akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mwaka huu tarehe 30 mwezi Machi, amesisitiza jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hatua kubwa sana iliyofanywa na Serikali katika uwekezaji kwenye Sekta ya TEHAMA. Tunacho kituo cha National Internet Data Center (NIDC) ambacho kina miundombinu mikubwa na ya kisasa kabisa katika suala la TEHAMA, lakini Serikali kupitia sheria Na.10 ya mwaka 2019 imeanzisha wakala e-GA (e-government) ambaye anafanya kazi ya kusimamia mifumo ya TEHAMA kwenye Serikali. Pia asilimia 100 Serikali ina political will katika kuhakikisha Sekta ya TEHAMA ina flourish na kwa kufanya hivyo imeanzisha wizara maalumu kwa ajili ya Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ametueleza kwenye mobile connectivity kwamba sasa tunawatumiaji zaidi ya milioni 55 wa simu na milioni 29 wa mitandao ya internet.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache, upo upungufu. Upungufu wa kwanza, nchi yetu haina central database system ambayo ina taarifa zote za Mtanzania. Kwenye Taifa letu tunayo NIDA wanaandikisha vitambulisho, tunayo RITA wanatoa vyeti vya kuzaliwa, tunayo TRA wanatoa TIN Number; na hii kuipata siyo mchezo, upeleke nyaraka nyingine toka taasisi nyingine; Tunaye humu ndani Seif Gulamali anatoa Kadi za Yanga; tunao CRDB nao wanatoa kadi zao kwa wateja wao; tunayo Tume ya Uchaguzi na yenyewe inaandikisha Watanzania hao hao; tunao NHIF mmeona wanatibia wanaume mpaka ujazito kwa kutoa vitambulisho vyao na kuandisha watu; una leseni ya udereva; una kadi ya Chama cha Mapinduzi; kwa utaratibu huu hatuwezi kufikia pale tunapotaka kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa kuwa muda ni mdogo, niyaseme machache. Leo Mtanzania akiomba mkopo, ataombwa nyaraka hii, ataombwa nyaraka nyingine kwa sababu hakuna sehemu moja ambapo benki inaweza ikaenda ikakuta taarifa zote za Mtanzania huyu za kuweza kumsaidia. Hata huo mkopo ukiwa approved; juzi nilienda ofisini kwa mtu mmoja nikakuta anasaini nyaraka za mikopo, alikuwa na nyaraka siyo chini ya 40 amesaini signature 219, kitu ambacho tungekuwa na mfumo wa kieletroniki, angesaini tu pale kieletroniki agreed, angepata mkopo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, e-GA ipo chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi. Leo Waziri anawasilisha hapa TEHAMA, yupo Wizara nyingine na hilo nalo ni tatizo kwenye mfumo wa kisheria wa nchi yetu. Nimeenda e-GA vijana wale wanafanya kazi nzuri, nawapongeza sana, lakini wakati naondoka nikashangaa, nikapewa nyaraka hizi. Wewe una mamlaka ya kieletroniki, una-print nyaraka za nini? Kama kweli tuna nia ya kwenda kietroniki, leo hapa nani amewahi kuprintiwa nyaraka na face book? Nani kaprintiwa nyaraka na Instagram? Nani amewahi kuprintiwa nyaraka yoyote na simu yake ya mkononi au anamjua hata meneja wa kampuni ya simu anayoitumia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme mifumo ifuatayo kwa ufupi wake. Tunao mfumo wa TANePS. Huu siyo mfumo, ni kitu kimetengenezwa cha kumsaidia tu Mtanzania, mzabuni asi-print nyaraka za PDF ofisini kwake, bali azi-upload ziende kule zikafanyiwe kazi. Ingekuwa ni mfumo, ulitakiwa kieletroniki umtambue mzabuni, utangaze zabuni, ufanye evaluation, uandae mkataba, ukafanye vetting mkataba uliozidi Shilingi bilioni moja, uende ukafanye maombi ya msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ufanye contractor management, uandae certificate, umlipe mkandarasi, tusipate zile hasara alizozionesha CAG za ucheleweshaji wa malipo kwa kuwa kazi zinafanyika kwenye manual system. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi nitaje hasara zinazopatikana nchi katika mifumo ya kieletroniki. Ukisoma ripoti ya CAG ukurasa wa 348 TANROAD peke yake wamelipa Shilingi bilioni 224 kwa ukosefu wa mifumo ya kulipa hii, wanalipa kwa manual system. Leo Bodi ya Mikopo inao wadaiwa 155,722 wanaodaiwa Shilingi bilioni 422 hawajui wako wapi? Yaani kuna Watanzania wamesoma degree, halafu Bodi ya Mikopo haijui itawapata wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukisema Bima ya Afya kwa watu wote bila kuwa na mfumo wa kieletroniki ambapo Watanzania wote wanapatikana, itakuwa ni ndoto. Kama tu hii NHIF inashindwa kutibia watu na inajiendesha kwa harasa, hatuwezi kufika. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika tano ni chache, nitachangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, senior anasema uniongeze kidogo Mwenyekiti ukiridhia.
MWENYEKITI: Nilishakuongeza sekunde karibu 40 mpaka sasa. Kwa hiyo, nikushukuru kwa mchango wako.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Kwanza nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, nimefuatilia hotuba ya Waziri na yapo maeneo matano, kama muda utaniruhusu nitaomba kuchangia.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kwenye bajeti hii tumeona Ofisi ya Msajili wa Hazina ikichangia shilingi bilioni 629 kutokana na magawio ya mashirika ya umma ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina inayasimamia, na nitumie fursa hii kumpongeza binafsi Msajili wa Hazina, Bwana Mgonja, na timu yake yote.
Mheshimiwa Spika, lakini niombe sana Serikali, tulisema hapa kwenye taarifa ya Kamati na ninaomba niseme hapa, mpaka ninapozungumza hapa yako mashirika 30 yasiyokuwa na Bodi za Wakurugenzi. Sasa kwenye mashirika haya, kwenye cooperates, Bodi ya wakurugenzi ndiyo kama Bunge lako hili.
Mheshimiwa Spika, unapokuwa na shirika ambalo lina management, halina bodi, hata zile hoja walizokuwa wanazungumza akina Mheshimiwa Subira Mgalu za kiukaguzi, hata zikifikishwa kwa afisa masuuli na bodi hakuna tija inakuwa iko chini sana. Niiombe sana Serikali iongeze kasi na itengeneze mfumo mahususi wa kuhakikisha mashirika haya bodi zinapomaliza muda wake basi kuwe na bodi mpya ili succession plan iweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo ambalo ningeomba niongee kwa msisitizo mkubwa. Ni eneo la kilimo. Kilimo cha nchi yetu kina¬-employ zaidi asilimia 65 ya watu. Ndio sekta inayoajiri watu wengi zaidi, lakini kilimo kina mchango mkubwa kwenye GDP ya nchi yetu takribani 29.1%. Tulipata taarifa hapa kwamba Benki Kuu imetenga shilingi trilioni moja kama stimulus fund ya kusaidia kupata mikopo ya riba nafuu kwenye mabenki.
Mheshimiwa Spika, taarifa nilizonazo mimi mpaka hivi tunavyozungumza hata shilingi moja bado haijatoka Benki Kuu kwenda kwenye benki yoyote ya kibiashara ikiwemo Benki ya Kilimo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up hapa atueleze hii trilioni moja iliyokuwa imetengwa na Benki Kuu kwa ajili ya kusaidia mikopo ya kilimo, maana wote mnafahamu mkulima, hapa ameongea Mheshimiwa Maganga, hizi rfiba anazoziongelea kwenye benki za biashara wanakopeshwa wafanyabiashara, wanakopesha watu wenye security, hakuna sehemu mkulima anaweza kupokelewa akakopeshwa na kama atakopeshwa kwa riba hizi anazoongea Mheshimiwa Maganga hakuna mkulima anaweza kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na ndio maana tuliipongeza sana Serikali ilivyotenga hii trilioni moja tuliamini sasa muarobaini wa mikopo ya kilimo unaenda kupatikana, lakini mpaka sasa pamoja na kwamba masharti yaliyotengenezewa ile shilingi trilioni moja moja kwa moja yali-exclude Benki ya Kilimo kwa sababu inakosa zile sifa zilioainishwa kwenye masharti yale ya Benki Kuu tungetegemea kuona mikopo hii ya kilimo kwenye benki nyingine yanatoka.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa waziei akija ku-wind na sio vyema, kaka yangu, Yanga mwenzangu, kushika shilingi, lakini nitakuwa sina jinsi. Atueleze hii shilingi trilioni moja ni wakulima wangapi wa benki ipi wameshapata mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana sisi watu wa Dar es Salaam hatuna wakulima, lakini tunazungumzia nchi mzina, tunazungumzia Waheshimiwa Wabunge ni wakulima humu ndani, na sisi chakula cha Dar es Salaam kinatokana na kilimo cha nchi nzima. Kwa hiyo, tungependa kuona jambo hili linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, eneo la sensa. Niipongeze Serikali maandalizi yanaenda vizuri, lakini bado kuna kitendawili cha wale watakaotumika kufanya sensa ile ya watu na makazi. Tumeona kwenye postcode, postcode kule kwetu kuna asilimia imetekelezeka kwa utendaji mzuri na kuna asilimia imefeli kutokana na kupata watu, kweli tuna matatizo ya ajira, kweli vijana wetu hawana ajira, lakini unapata mtu ambaye hana weledi wa kiutumishi, anapewa kazi kwa kuwa ina posho ataomba, lakini unakuta mtu anatoka Msasani anakuja kuhesabu watu Gongo la Mboto, tija inakuwa iko chini.
Mheshimiwa Spika, ni ushauri tu kwa Serikali, sensa za miaka ya nyuma zilikuwa zinatumia sana walimu. Walimu si tu kwamba wana weledi, lakini ni watumishi, wanaaminika, wanaishi maeneo yale, wanaheshimika na jamii. Kwani walimu wa nchi hii wamekosa nini? Wamekosa sifa gani kutumika kwenye maeneo haya? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi niseme inawezekana tukachukua jambo hili kama tumetengeneza solution ya ajira ya vijana ambao hawana ajira, kweli tunataka kuwatetea, lakini tuangalie tija ya sensa.
Mheshimiwa Spika, na nitumie fursa hiyohiyo kutoa wito kwa wananachi kujitokeza kwa wingi sana kuweza kushiriki zoezi la sensa kwa sababu sensa hii ndio inaenda kujenga msingi wa maendeleo na utengaji wa fedha za miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, sio kwa umuhimu wake, kumekuwa na kilio kirefu cha wafanyabiashara wanapoenda kutafuta TIN Number. Mamlaka ya Mapato Tanzania inataka kuwe na assessment, kuwe na makadirio ya mapato na akipewa TIN Number ile robo ya kwanza alete marejesho. Anazitoa wapi na hajaanza biashara? Akina Mheshimiwa Katimba wamewahi kuchangia Mabunge ya nyuma, Wabunge wengi wamechangia, hivi kuanza na assessment ya zero tunapata tatizo gani?
Mheshimiwa Spika, ili mtu yule akianza biashara aje a-declare mapato aanze kulipa. Sasa unavyompa mtu TIN Number leo, ndio maskini wa Mungu labda kastaafu ama hana ajhira ama anajiajiri, kapata kiusajili chake, anataka TIN Number unamwambia wewe utaleta shilingi 400,000 kwa mwaka na robo ya kwanza ulete shilingi 100,000 anaitoa wapi? Ni kilio kikubwa, ni kilio kikubwa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa nchi hii ambao tunaomba sana Serikali iliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ni mbia katika biashara hizi, mbia ambaye hatoi mtaji wala haji kufanya biashara kwenye maeneo haya, kwa hiyo, inatakiwa afahamu kwamba, mtu anapojitolea kufanya biashara ndio amejitolea kuwa mbia mpya wampokee vizuri watengeneze mazingira ya kumsaidia kufanya biashara, ili akipata yeye na kodi imepatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mheshimiwa mmoja amechangia hapa kuhusiana na EFD machine. Kule kwangu kuna mfanyabiashara mmoja amenitumia message amefungiwa biashara kule Kigogo Fresh Pugu. Unamfungia mfanyabisahara duka kwa kuwa hana EFD machine, haya, sasa ameshafunga, unapata wapi kodi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo elimu itoke, lakini tuangalie mfumo mzuri wa kuwasaidia wafanyabiashara hawa waweze kufanya biashara vizuri.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. JERRY W. SILAA: Kengele ya pili? (Makofi)
SPIKA: Sekunde 30. Malizia sentensi.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nikushukuru wewe, sio kwa sura ile ya Mheshimiwa Maganga kwa kunipa nafasi ya kusema, maana nafasi zipo na zinapatikana, lakini niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MANDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hizi zilizopo mezani na mimi nichukue fursa hii kuwapongeza sana wenyeviti wa Kamati hizi mbili kwa taarifa zao. Niwapongeze sana wachangiaji waliochangia kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuishauri Serikali kwa niaba ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwenye Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali ukurasa wa 40 kulikuwa na hoja ya Mradi wa Urasimishaji wa Makazi. Serikali mwaka 2013 ilikuja na mpango wa miaka kumi wa kurasimisha makazi holela kwa maana yako maeneo mengi hasa Dar es salaam na miji mingi mikubwa ambayo tayari makazi yalijengwa bila kupangwa na kupimwa.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulikuja kama suluhu ya kuunganisha nguvu, kwa maana ya kutumia kampuni binafsi za upimaji na upangaji kama wataalamu na kuziba lile gap la upungufu wa wataalamu, kutumia wananchi kuchangia zoezi zima la kupanga na kupima, lakini pia Serikali kuratibu. Zoezi hili likikamilika litasaidia kuongeza mapato lakini pia kupunguza migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, ardhi kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge lako zinapaswa kumilikiwa kisheria. Umiliki wa ardhi mijini unasimamiwa na Sheria Na. 4 ya mwaka 1999, na kila mtu anayeishi kwenye eneo lililopangwa na kupimwa atamiliki ardhi yake kwa hati, na ndio umiliki ambao Serikali imekuwa ikihimiza kupitia Mradi wa Urasimishaji, na hii inaondoa migogoro kwa sababu umiliki huu huu wa kienyeji, nimetumia lugha ambayo si sahihi; ni umiliki wa haki ya Mungu, kwamba ili umthibitishie mtu unamiliki ni lazima uapie. Hata hivyo, zoezi la urasimishaji lilienda kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako mpaka kufikia mwezi Januari, 2024 jumla ya vipande vya ardhi 2,400,000 vimetambuliwa na viwanja 2,500,000 vilikuwa vimekwishapangwa kwa maana ya TP Drawings. Kati ya hivyo, viwanja 1,400,000 upimaji wake umekamilika, kwa maana ya survey, na viwanja 1,100,000 sawa na asilimia 42 bado havijakamilika.
Mheshimiwa Spika, niombe pia kupitia Bunge lako niseme kwamba katika pesa ambazo zilikadiriwa kukusanywa ili zoezi hili likamilike, shilingi bilioni 331 ni bilioni 72 tu ndizo zimechangwa na wananchi, na ndiyo maana zoezi hili limekuwa linakwenda kukwama.
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini suluhu? Suluhu namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekwishatoa maelekezo, na kupitia Mradi wa LTIP zimetengwa jumla ya dola milioni 62; zile dola milioni 21 alizosema Mheshimiwa Mtemvu ni kiasi cha fedha hizo na mradi huu unakwenda kukwamuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maeneo yote na tumeanza na Dar es salaam, hapa Dodoma tumekwishafanya pilot, jimbo la Mtemvu yeye ni shahidi litakuwa la kwanza pale Dar es salaam na kazi kubwa inafanyika.
Mheshimiwa Spika, zoezi hilo la ukwamuaji linakwenda pamoja na kliniki za ardhi ambazo ukiangalia kwenye viwanja hivi 1,400,000 vilivyopimwa, ni ankara 623,000 tu ndizo zimeanza kufanyiwa process za kupata hati na ni hati 230,000 tu zimemilikishwa. Sasa kutoka viwanja 1,400,000 mpaka hati 230,000 ni namba ndogo lakini kliniki hizi zinamsogezea mwananchi huduma karibu zaidi na zinampunguzia urasimu wa kufuatilia hati. Hivi ninavyozungumza kliniki iko pale Kibo – Tegeta; na kuanzia Jumatatu tarehe 29 mpaka tarehe 25 kliniki ya ardhi itakuwa pale Bunju kwenye Wilaya ya Kinondoni. Hiyo wiki moja ni ile wiki ambayo na Wizara ya Ardhi kwa maana ya Waziri na watendaji wa makao makuu watakuwa pale Bunju kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi pamoja na kuendelea kukwamua zoezi hili la urasimishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilithibitishe Bunge lako kwamba Wizara imejipanga, uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, umekwishatupatia maelekezo na pesa zipo. Ninaamini kwenye ripoti zijazo za CAG na ripoti zijazo za Kamati, zoezi la urasimishaji litakuwa limefika mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kulishukuru Bunge lako kwa miongozo na maelekezo mnayotupatia na wakati wote Serikali iko tayari kwa maelekezo, ushauri wa Bunge na wakati wote tunachukulia very serious ripoti hizi za Kamati na michango ya Wabunge wote waliochangia tumechukua na tutaifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kadri ya ratiba ya Bunge kwenye vikao vinavyokuja, tutakuwa tukitoa taarifa ya zoezi la urasimishaji na mazoezi mengine ya ardhi ili kuweza kuhakikisha kwamba kero za ardhi zinafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena na ninaunga mkono hoja. (Makofi)