Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Jerry William Silaa (8 total)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -

Je, upi mkakati wa kuwapa Wananchi ardhi mbadala wanapoondolewa kwenye maeneo yao kupisha uhifadhi na miradi ya mkakati?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri, kunakuwepo na ulazima wa wananchi kuachia ardhi pale ardhi inapohitajika kwa matumizi ya umma. Mahitaji hayo ni pamoja na ardhi ya uhifadhi na ardhi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa sheria nchini, umeweka wazi juu ya takwa na haki ya wamiliki wa ardhi kulipwa fidia ya ardhi na maendelezo pale ardhi inapotwaliwa kwa matumizi ya umma. Aidha, sheria inaruhusu fidia hiyo kulipwa kwa fedha taslimu au kupatiwa ardhi mbadala. Pamoja na sheria kuruhusu wananchi kupewa ardhi mbadala pindi ardhi yao inapotwaliwa, wananchi wamekuwa wakipendelea fidia ya fedha badala ya ardhi mbadala ili kuwawezesha kutafuta maeneo mengine wanayoyahitaji. Ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Wilaya ya Rungwe italetewa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuajiri Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ili kuongeza kasi ya kusikiliza na kuamua mashauri ya ardhi. Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Rungwe ameteuliwa na kupangiwa kituo tarehe 18 Septemba, 2023 na tayari ameanza kazi. Nakushukuru.
MHE. DEODATAUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, kwa nini Sheria za Ardhi zinazokusudiwa kutumika kwenye miji zinatumika maeneo ya vijijini?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa kisheria wa usimamizi wa ardhi nchini umegawa ardhi katika makundi matatu ambayo ni Ardhi ya Kijiji, Ardhi ya Hifadhi na Ardhi ya Jumla. Kwa kuzingatia mgawanyo huo, Ardhi ya Vijiji inasimamiwa na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114 na maeneo ya miji yanasimamiwa na Sheria ya Ardhi, Sura 113. Hata hivyo, yapo baadhi ya maeneo ndani ya mipaka ya vijiji yanayosimamiwa na Sheria ya Ardhi, Sura 113 kutokana na kumilikishwa kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114 au kuhawilishwa. Aidha, baadhi ya maeneo ya vijiji yametangazwa kuwa ya kuendelezwa kimji (Planning Area) na kuandaliwa Mpango Kabambe (Master Plan) na hivyo kuyafanya yasimamiwe na Sheria ya Ardhi, Sura 113.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la ekari 1,000 lililotengwa kwa matumizi ya viwanda Kata ya Pembamnazi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, eneo la Pembamnazi lipo Manispaa ya Kigamboni na lina ukubwa wa ekari 1,000. Eneo hilo limetengwa kama hazina ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali inaendelea kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwekeza katika eneo hilo. Hivyo, wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika maeneo hayo wawasilishe maombi yao Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam au kwenye mamlaka za uwekezaji wakiainisha kiasi cha ardhi wanachoomba na uwekezaji tarajiwa. Aidha, Wizara iko tayari kupokea ushauri Mheshimiwa Mbunge kuhusu uwekezaji katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi wa Jimbo la Kilosa kutokana na uwepo wa migogoro ya muda mrefu ya Wakulima na Wafugaji?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Wilaya ya Kilosa umeandaliwa mwaka 2008 na utamaliza muda wake mwaka 2028. Mpango huu ndio mwongozo wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vya wilaya.

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Desemba, 2023 jumla ya vijiji 58 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Kilosa kati ya vijiji 138 vilivyopo sawa na asilimia 42, ambapo kati ya vijiji hivyo, vijiji 23 vipo katika Jimbo la Kilosa na vijiji 35 vipo katika Jimbo la Mikumi. Wizara kupitia Tume itaendelea kuziwezesha mamlaka za upangaji katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji mbalimbali nchini vikiwemo vijiji 10 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika mwaka wa fedha 2024/2025. Natoa rai kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zake kila mwaka kwa ajili ya uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO K.n.y MHE. JULIANA D. MASABURI aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kusimamia sheria kikamilifu na kukomesha utaratibu wa wapangishaji nyumba kutoza pango kwa fedha za kigeni?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna sheria mahsusi inayoelekeza aina ya fedha inayotakiwa kutumika katika kutoza pango kwa wapangishaji wa nyumba. Hata hivyo, Benki Kuu imekuwa ikitoa miongozo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini ambayo pamoja na mambo mengine inakataza matumizi ya fedha za kigeni kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini. Mwongozo unaotumika sasa ulitolewa mwezi Desemba, 2017.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha utendaji wa soko la nyumba nchini, Wizara ipo katika mchakato wa kutunga Sheria ya Milki ambayo pamoja na masuala mengine itaweka utaratibu wa utozaji wa pango hususan kwa raia wa Tanzania. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali imetoa na kukusanya kiasi gani kutokana na mkopo wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kiasi gani kimerudi kuendeleza mpango huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali ilitoa bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK). Fedha hizo zilikopeshwa bila riba kwenda kwenye halmashauri 57 ambacho kilikuwa ni kiasi cha shilingi bilioni 43.6. Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Iringa kiasi cha shilingi milioni 450, Vyuo vya Ardhi vya Tabora vilipata milioni 644, Morogoro vilipata bilioni 1.2 na Chuo Kikuu Ardhi kilipata milioni 892.8 ambazo zimewezesha jumla ya kupanga na kupima viwanja 218,337.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufika Machi, 2024, jumla ya shilingi bilioni 23.5 sawa na asilimia 47 zimekwisharejeshwa. Halmashauri 12 zimekamilisha marejesho yenye kiasi cha shilingi bilioni 11.3, halmashauri 43 zimerejesha sehemu ya fedha yenye jumla ya shilingi bilioni 10.9, Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Iringa imerejesha shilingi milioni 581.3, Chuo cha Ardhi Morogoro milioni 250, Chuo cha Ardhi Tabora milioni 100, Chuo Kikuu Ardhi milioni 100 na halmashauri mbili ambazo ni Shinyanga Manispaa shilingi bilioni 1.055 na Musoma DC shilingi milioni 200 hazijarejesha kabisa. Wizara yetu itaendelea kufuatilia halmashauri ambazo hazijakamilisha kurejesha fedha hizo ili zitekeleze wajibu huo kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Wizara na halmashauri hizo.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itahamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mfumo wa Mahakama?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuboresha mfumo uliopo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa mapendekezo ya kuhamisha shughuli zinazofanywa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda katika mhimili wa Mahakama. Pindi taratibu zitakapokamilika, Serikali italifahamisha Bunge lako Tukufu, nakushukuru. (Makofi)