Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jerry William Silaa (11 total)

MHE. JERRY W. SILAA Aliuliza:-

Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Mwendokasi awamu ya tatu toka Gongolamboto mpaka Kariakoo ambao umeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam (DART) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendeayo haraka maarufu kama mwendokasi unaotekelezwa katika awamu sita katika barabara zote kuu Jijini Dar es Salaam zenye urefu wa kilometa 146.2.

Mheshimiwa Spika, awamu ya tatu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka inatekelezwa katika barabara za Nyerere, Bibi Titi, Maktaba, Azikiwe na Uhuru kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto zenye urefu wa kilometa 23.6 ikiunganishwa na awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huu katika vituo vikuu vya mabasi ya Kariakoo, Gerezani na Kivukoni.

Mheshimiwa Spika, kazi inayoendelea sasa ni tathmini ya zabuni zilizowasilishwa ili kumpata mkandarasi atakayeanza kujenga awamu ya kwanza ya mradi, kwa maana ya Lot 1, inayohusisha ujenzi wa barabara, kwa maana ya road works, vituo vidogo vya mabasi pamoja na kituo kikuu cha mabasi cha Gongolamboto.

Mheshimiwa Spika, zabuni ya kazi ya ujenzi awamu ya pili, inayojumuisha ujenzi wa karakana ya Gongolamboto, Kituo Kikuu cha Mabasi cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere pamoja na vituo mlisho vya Jet Club, Banana na Mombasa, zabuni yake haijatangazwa kutokana na mabadiliko ya usanifu wa karakana ya Gongolamboto baada ya eneo la karakana hiyo kubadilishwa kutokana na sehemu kubwa ya eneo la awali kuathiriwa na mradi wa reli ya kisasa.
MHE. JERRY W. SILAA Aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya sasa ya kurejesha mfumo wa TANePS Hazina ili ukatekelezwe na kusimamiwa pamoja na GePG katika kuongeza ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa TANePS umetayarishwa na kukidhi matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma Sura Na. 410 ambayo imeweka misingi na taratibu za ununuzi wa umma inayohimiza uwazi, usawa na haki katika michakato ya ununuzi ili kuipatia Serikali thamani halisi ya fedha zinazotumika katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali. Aidha, kifungu Na. 9(1) cha Sheria kimeipa nguvu mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma kuanzisha na kusimamia mifumo na taratibu zote zinazohusu masuala ya ununuzi wa umma ikiwa ni pamoja na mfumo wa TANePS.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfumo wa TANePS tayari umeunganishwa na mifumo ya GPG na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya Serikali ikiwemo mifumo ya MUSE na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura Na. 410 pamoja na Kanuni zake, Serikali inaendelea kuboresha utendaji na mfumo TANePS ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi, hivyo basi haioni haja ya kuhamishia mfumo huo Hazina kwa sasa. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

Je ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Jimbo la Ukonga na Mbagala kwa mkupuo badala ya kujenga kilometa moja kila mwaka ili kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa Majimbo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, kuanzia mwaka 2000 Serikali imekuwa ikiijenga barabara hii ya Chanika - Mbande inayounganisha Jimbo la Ukonga na Mbagala kwa kiwango cha lami kwa awamu. Hadi sasa jumla ya kilometa 14.34 kati ya kilometa 19.29 sawa na asilimia 74.5 zimejengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami. Aidha, kilometa 4.95 zilizosalia zitaendelea kujengwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

(a) Je, ni taasisi ngapi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango hadi sasa hazina Bodi au Bodi zake zimemaliza muda wake?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha benki ya waliopekuliwa ili muda wowote uteuzi ufanyike haraka kusaidia Taasisi hizo kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais kwani kwa sasa upekuzi imekuwa kisingizio cha kuchelewesha uteuzi?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango ina jumla ya Taasisi 28 ambazo inazisimamia na kati ya hizo Taasisi tisa Bodi zake zimemaliza muda wake na mapendekezo ya majina kwa ajili ya kujaza nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi hizo yamewasilishwa kwenye Mamlaka za Upekuzi.

Mheshimiwa Spika, upekuzi kwa ajili ya kujaza nafasi mbalimbali hufanyika kwa wakati husika kutokana na ukweli kwamba utendaji na mienendo ya maafisa hubadilika kutoka wakati mmoja hadi mwingine. Hivyo, siyo sahihi kuwa na kanzidata ya upekuzi (benki ya waliopekuliwa) ili kurahisisha mchakato wa upekuzi kwa kuwa utendaji na mienendo ya maafisa hubadilika kuendana na wakati husika.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

(a) Je, ni taasisi ngapi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango hadi sasa hazina Bodi au Bodi zake zimemaliza muda wake?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha benki ya waliopekuliwa ili muda wowote uteuzi ufanyike haraka kusaidia Taasisi hizo kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais kwani kwa sasa upekuzi imekuwa kisingizio cha kuchelewesha uteuzi?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Mipango ina jumla ya Taasisi 28 ambazo inazisimamia na kati ya hizo Taasisi tisa Bodi zake zimemaliza muda wake na mapendekezo ya majina kwa ajili ya kujaza nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi hizo yamewasilishwa kwenye Mamlaka za Upekuzi.

Mheshimiwa Spika, upekuzi kwa ajili ya kujaza nafasi mbalimbali hufanyika kwa wakati husika kutokana na ukweli kwamba utendaji na mienendo ya maafisa hubadilika kutoka wakati mmoja hadi mwingine. Hivyo, siyo sahihi kuwa na kanzidata ya upekuzi (benki ya waliopekuliwa) ili kurahisisha mchakato wa upekuzi kwa kuwa utendaji na mienendo ya maafisa hubadilika kuendana na wakati husika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA K.n.y. MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu – Kifuru hadi Mbezi Mwisho kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika barabara ya Pugu – Kifuru – Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilometa 12.7, sehemu ya kutoka Mbezi Mwisho hadi Kifuru (kilometa 6.7) imejengwa lami kwa njia mbili na sehemu ya kutoka Kifuru – Pugu Station (kilometa 6) ni barabara ya vumbi.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya Pugu Station hadi Kifuru (kilometa sita) kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa njia nne na kwa sehemu ya Kifuru - Mbezi Mwisho (kilometa 6.7) kuipanua kutoka njia mbili kuwa njia nne. Zabuni kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri wa kufanya kazi hiyo zimetangazwa na zitafunguliwa tarehe 10 Oktoba, 2022. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, ni Sheria gani inasimamia orodha ya wanaostahili kutumia ving’ora na vimulimuli kwa misafara ya Viongozi na Wananchi wa kawaida?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ndiyo sheria inayosimamia matumizi ya ving’ora na vimulimuli barabarani. Kifungu 39(b) kifungu kidogo cha (1) na (2) cha sheria, kinaelekeza matumizi ya ving’ora na vimulimuli barabarani ambayo ni kutoa ishara kwa watumiaji wengine wa barabara kuchukua tahadhari kuwa kuna dharura. Kifungu cha 54 kifungu kidogo cha (1) hadi cha (5) kinaeleza utaratibu na mazingira ya matumizi ya ving’ora na vimulimuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari yanayostahii kutumia ving’ora na vimulimuli kwa mujibu wa sheria ni magari ya polisi, zimamoto, magari ya wagonjwa (ambulance), magari ya vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na magari yaliyopata kibali maalumu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kutangazwa katika Gazeti la Serikali.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa Wafanyakazi wa Viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongo la Mboto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 1989 Serikali kupitia Mifuko ya NSSF uliokuwa PPF iliwalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongo la Mboto baada ya ukomo wa ajira zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Aprili, 2022 Mfuko wa PSSSF ulipokea malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda Sunguratex wapatao 644 wakidai kuwa hawakulipwa mafao kikamilifu na uliokuwa Mfuko wa PPF. Baada ya Mfuko kufanya uchambuzi wa madai hayo, imeonekana kuwa wafanyakazi hao walishalipwa mafao kikamilifu isipokuwa baadhi yao wanasubiri kufikisha miaka 55 ili waanze kulipwa pensheni ya mwezi. Kuhusu wafanyakazi wa kiwanda cha Kilitex Mfuko haujapokea malalamiko yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kama wafanyakazi hao wapo ili kutatua changamoto ya waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongolamboto. Ahsante.
MHE. ELIBARIKI E. KINGU K.n.y MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuwaingiza Wazee na Wanaume kwenye mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri kwa kuwa kwa sasa wameachwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa Mbunge wa Jimbo la Ukonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria ya mikopo ya asilimia 10 na kanuni zake, mikopo hii inatolewa kwa ajili ya kuwezesha makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo yenye masharti nafuu. Makundi haya kwa kiasi kukubwa hayawezi kupata mikopo katika taasisi nyingine za fedha kwa sababu ya kukosa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utoaji na urejeshaji wa mikopo hii tangu kutungwa kwa sheria. Tathimini hii itawezesha kushauri namna bora ya utoaji wa mikopo pamoja na mapitio ya Sheria. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, Serikali haioni ni busara kuuza nyumba kwa Wapangaji wa kota za Ukonga kwa kuwa wameishi miaka mingi bila kufanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mpango mahsusi wa kukarabati na kuendeleza maeneo yote ya kota nchini ambazo ni nyumba zilizorejeshwa TBA kutoka TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeanza kukarabati nyumba za kota za Ukonga ambapo kwa sasa TBA imekarabati maghorofa mawili yenye uwezo wa kubeba familia Nane. Ukarabati umehusisha maeneo ya paa, dari, mfumo wa umeme, mfumo wa majisafi na majitaka na upakaji wa rangi, ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu - Majohe - Viwege njia nne na Kampala - Bwera - Rada hadi Chuo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikizifanyia matengenezo barabara za Jimbo la Ukonga zikiwemo barabara za njia nne Pugu – Majohe hadi Viwege na Kampala – Bwera – Rada hadi Chuo ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 jumla ya shilingi milioni 701.67 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo yenye urefu wa kilomita 20.7 na kazi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la matumizi katika barabara hizo limesababisha matengenezo yanayofanyika kutokudumu kwa muda mrefu. Hivyo Serikali imeingiza barabara hizi katika mpango wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili, ili barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mradi upo katika hatua za awali za kufanya usanifu.