Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Jerry William Silaa (5 total)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati kutusaidia kutatua migogoro iliyopo ndani Kata ya Kapele kwa kuwafuatilia watu wote ambao wamehodhi na kupora maeneo ya wananchi kinyume na utaratibu bila kuwa hati na wengine kuwa na hati za uwongo kwa kigezo na kusingizia wametumwa na wakubwa huko juu? Ni lini Wizara ya Ardhi mtatusaidia kutatua jambo hili?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nina nyongeza ndogo kwenye majibu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kuzungumza, naomba dakika moja kutoa shukrani. Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambae amenipa kibali kuhudumu kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuhudumu na kumsaidia kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ninachoweza kumuahidi ni utumishi uliotukuka wa uadilifu. Nitatumikia kwa nguvu zangu na akili zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliomba Bunge lako tukufu ushirikiano na wakati wote nitakuwa tayari kwa ajili ya kufanya kazi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa nyongeza ndogo ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Serikali imejipanga na lipo suala la migogoro ya ardhi. Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane ilishafanya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa 26 yote ya nchi nzima, kuendelea na utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge ambao wengi tumekutana na wameelezea kero zao akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Momba, Mheshimiwa Condester. Baada tu ya Bunge hili kuna mkutano wa Kimataifa Arusha na unaisha Alhamisi, tutajipanga kuanza ziara nchi nzima kutekeleza maagizo ya Baraza la Mawaziri kwenye vijiji 975. Vilevile, kutatua migogoro yote ambayo inajitokeza kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushirikiano. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa tena nafasi niulize swali la nyongeza, kwanza nitoe shukurani nyingi kwa majibu mazuri ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Jerry Silaa ambaye alikuwa Mwenyekiti wangu Kamati ya PIC, nimpongeze kwa kuwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu majibu yake yapo sawasawa lakini watendaji wakati wa kutekeleza huwa hawaweki bayana sheria inasemaje badala yake wanakuja wanakuambia jamani hili eneo linachukuliwa kwa ajili yakazi hii na hii ya Serikali ninyi mnatakiwa muondoke, mtapata fidia kwa maendelezo ambayo mlikuwa mmefanya.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni muhimu wakati wa kuhamisha wananchi kwenye maeneo yao watoe maelekezo kwamba watapata nini na nini kulingana na eneo ambalo linachukuliwa either kwa uhifadhi au utekelezaji wa miradi?

Pili, swali langu ni je, Waziri utakuwa tayari kuambatana na mimi tuende tukafanye mkutano uwaeleze wananchi maeneo ya Momela pamoja na KIA ambao wanatakiwa wahame?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa majibu kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John Danielson Pallangyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, naomba kutumia Bunge lako tukufu kuagiza Wathamini wote na Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali kuhakikisha inatoa elimu stahiki kwa wananchi pindi ambapo maeneo yao yanatwaliwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Wananchi waelezwe wazi takwa la sheria kwa wale wanaotaka kuchukua fedha taslimu kwa niaba ya ardhi yao na kwa wale ambao wanataka kutafutiwa ardhi mbadala.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, pamoja na kwamba niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Dkt. John Pallangyo lakini eneo la KIA na eneo la Momela ni maeneo ambayo yanaangukia kwenye vile vijiji 975 ambapo wananchi walikuwa wameingia kwenye maeneo ya hifadhi na wengine wameingia kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa KIA. Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona ni busara kuwafidia kwa yale maendelezo waliyoyafanya, maeneo haya fidia yao wanayolipwa haihusishi ardhi ambayo wamekuwa wakiikalia. Baada ya Bunge hili Mheshimiwa Dkt. Palangyo tutaongozana pamoja kwenda kutoa elimu kwa wananchi wa Jimbo lako, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba ni sikivu sana, kwa sababu niliuliza hili swali la imelitekeleza. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuyaelimisha Mabaraza ya Kata ili yasitoe hukumu kwenye mashauri ya ardhi?
Swali langu la pili, katika Wilaya ya Chunya hakuna kabisa Baraza la Ardhi, ukizingatia wananchi wa Chunya wanatoka Kambikatoto, Kipambawe, Mafieko, Bintimanyanga, Matwiga, Luhanga, Ifumbo na Shoga wanakwenda kushtaki mashauri yao kwenye Jiji la Mbeya.

Je, ni lini Serikali itawaepushia shida hiyo wananchi wa Wilaya ya Chunya?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi ya Kata yameanzishwa chini ya Sheria Sura ya 206 na kupitia Bunge lako Tukufu kwenye Marekebisho ya Sheria Namba 3 ya Mwaka 2021 Mabaraza haya yalipunguziwa nguvu ya kimaamuzi na yanapaswa kufanya usuluhishi ndani ya siku 30 baada ya shauri kufikishwa.

Mheshimiwa Spika, tuliongea na Waandishi wa Habari lakini naomba kutumia Bunge lako Tukufu kuwatangazia wananchi wote kwamba Mabaraza ya Ardhi ya Kata nguvu yake ya kisheria ni kufanya usuluhishi ndani ya siku 30 tokea shauri lifikishwe mbele yake. Baada ya hapo kama usuluhishi utashindwa kufanyika mashauri yawasilishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Ninaomba tena kupitia Bunge lako, Wakurugenzi wa Halmashauri maana Mabaraza ya Ardhi ya Kata yanasimamiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wakurugenzi wa Halmashauri wanasimamia kwa niaba yake, Waendelee kusimamia mabaraza haya ili wananchi waendelee kupata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kati ya Mabaraza ya Wilaya zote 139 ni Mabaraza 94 tu ndiyo yenye Wenyeviti wa Baraza la Wilaya. Tayari ofisi yangu imeendelea kufanya mawasiliano ya kuomba vibali vya ajiri kwa ajili ya kupata ajira ya kuajiri Wenyeviti wengine 45, lakini kwenye maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Chunya kwenye maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge ikiwemo Maeneo ya Bintimanyanga na maeneo ya Shoga tunaendelea kutoa maelezo kwa Msajaili wa Baraza la Ardhi la Wilaya kutumia Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ya jirani kwenda kwenye mabaraza haya kwenda kusikilza mashauri mpaka pale Serikali itakapokamilisha Wenyeviti kwenye Mabaraza ya Wilaya zote, ninakushukuru. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata aliuliza swali juu ya mgogoro huu na ulitoa maelekezo kwamba Waziri afanye utaratibu wa kuja kuangalia mgogoro huu na umalizike. Hata hivyo, nashukuru Naibu Waziri alikuja, jambo lililofanyika ni kutoa maelekezo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wahakikishe wanashughulikia tatizo hili. Mheshimiwa Naibu Waziri hakupata fursa ya kwenda field kuona tatizo na uhalisia wake.

Mheshimiwa Spika, naomba tena nirudie, naomba tena kupitia Bunge lako, niombe Waziri aje Mkoa wa Rukwa, aende akafuatilie aone uhalisia wa tatizo hili kwa sababu suala la kumuachia Mkuu wa Mkoa limekuwepo tangu miaka 13 iliyopita ambapo Mkuu wa Mkoa, mama yangu Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya analijua vizuri. Ninataka Waziri aje na timu ya wataalam wajifunze vizuri kuliko haya majibu ambayo yanaweza yakachochea hasira na mgogoro zaidi, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini niungane na Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake ya kupambania wananchi wake.

Naomba nimuahidi tarehe 17 Novemba, baada tu ya Bunge hili nitafika jimboni kwake, nikiambatana na timu ambayo tumeunda task force ya wataalam kwa ajili ya kutatua migogoro mikubwa kama hii, kwenda uwandani kuona hali halisi na kutatua tatizo hili mara moja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, uhalisia uliopo ni kwamba, kuna mkanganyiko mkubwa sana kwenye halmashauri za miji ambazo zina vijiji. Sasa, Waziri atakubaliana nami kwamba, ni wakati sasa wa kutoa maelekezo kwa sababu sheria inataka utayari wa eneo kabla halijawa declared planning area. Maeneo mengi yamekwenda kuwa declared planning area kabla hayajawa tayari na ni maeneo ya vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yuko tayari kutoa maelekezo ili kufanyike marekebisho ya kutangaza upya maeneo ya vijiji yasitawaliwe na Sheria za Miji? Ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, kwa kuendelea kufuatilia maslahi ya wananchi wake wa Jimbo la Njombe Mjini. Ni kweli Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355 kifungu cha 77(1)(b) kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, kutoa Kanuni zinazoongoza upangaji wa miji (Planning Space Standard). Vilevile mwaka 2018 Kanuni hiyo ilitolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilithibitishie Bunge lako kwamba Kanuni hii tumeisimamisha na tumetoa maelekezo kwa wataalam wa ardhi wa Wizara ya Ardhi, kuipitia upya na kutoa Kanuni ambayo itaendana na hali halisi ya maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni hii ndiyo inayohusika kwenye ujenzi wa vituo vya mafuta vile vyenye ardhi ndogo, inahusika kwenye mashamba ya mijini ya ekari tatu na ukiangalia hali halisi ya Mji wa Njombe kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mji wa kilimo. Pia kilimo kinacholimwa pale ni kilimo cha parachichi na sisi Wizara ya Ardhi hatuwezi kuwa kikwazo cha kuendeleza zao la parachichi ambalo linalimwa kwenye Wilaya ya Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuirejea Kanuni hiyo na tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge wa Njombe na Wabunge wengine wenye maeneo ya vijiji ambayo na sura ya kijiji, ili Kanuni itakayotoka iweze kuendana na mazingira ya wananchi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.