Supplementary Questions from Hon. Jerry William Silaa (33 total)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mradi huu katika mapendekezo ya awali ulikuwa ufike kwenye eneo la Pugu na kwa kuwa sasa mji umekua kwa kasi na wote mnafahamu Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani vimeungana, je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kutekeleza mradi huu mpaka eneo la Pugu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutumia historia ama matokeo ya mradi wa awamu ya kwanza kutoka Kimara mpaka Kariakoo na Posta wakati miundombinu imejengwa na sasa wafanyabiashara ndogo ndogo wanafanya biashara kwenye miundombinu hii mipya, je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuunganisha miundombinu ya mradi huu wa mabasi yaendayo haraka na masoko yatayoingiza wafanyabiashara kwenye maeneo haya ya vituo mlisho vya Banana, Mombasa na Gongolamboto? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali ndugu yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mawazo ni mazuri na tukifahamu kwamba Jiji la Dar es Salaam linazidi kutanuka, lakini design ya kwanza ilikuwa inatuelekeza tunaishia mahali fulani. Si hivyo tu, tulifikiria hata sehemu ya barabara inayoenda Mbagala, sasa hivi inaishia pale Mbagala Rangi Tatu, tulikuwa tunafikiria jinsi gani tutafanya tufike mpaka pale mbele ya Kongowe.
Kwa hiyo, haya yote ni mawazo mazuri, wataalam wetu wataendelea kuyafanyia kazi, lakini tuna phase one ya design, kama tutakuwa na variation yoyote tunaweza tukaifanya katikati ya kazi yetu lakini lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma vizuri, hasa hii ya mwendokasi.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili la kuhakikisha haya mabasi yanapita katika vituo vya kutoa huduma; ni kweli na hata ukiangalia katika ujenzi wa soko letu la Kisutu pale Dar es Salaam, Ilala moja ya jambo kubwa ni kutengeneza daraja linalounganisha mwendokasi na kutengeneza soko. Wataalam wetu wa TANROADS na wale ambao wanafanya ujenzi walikuwa wanaendelea na kazi hiyo. Kwa hiyo, hilo jambo ni kipaumbele chetu kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, hata kuwa na pack maalum kwamba mtu akiondoka sehemu fulani anaweza akaacha gari lake na kuweza kusafiri. Hayo yote ni mambo ambayo tunayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika awamu hii tutaenda kufanya maboresho makubwa kwa lengo kubwa miundombionu hii na usafiri wetu huu unakuwa safi na salama kwa wasafiri wote wa Jiji la Dar es Salaam.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani kwa Serikali kwa kufungua wilaya ya TANESCO pale Chanika na kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa kufanya ziara kwenye Jimbo la Ukonga, je, Serikali inawaeleza nini wananchi wa Jimbo la Ukonga ambao mpaka sasa miradi yao ya REA haijakamilika kwenye Kata za Chanika, Zingiziwa, Msongola, Majohe na Kivule? Serikali inatoa tarehe gani wananchi wategemee mradi huu kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba miradi ya umeme ya REA awamu ya tatu mzunguko wa pili itaanza mwezi huu wa pili na itakamilika kufikia Septemba, 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa ujumla kwamba miradi yote ya kupeleka umeme vijijini kwa vijiji 2,150 vilivyokuwa vimebakia havijapata umeme, vyote vitapatiwa umeme katika awamu hii ya tatu mzunguko wa pili ya REA. Baada ya hapo hatutarajii kuwa na kijiji chochote ambacho kitakuwa hakina umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwasihi Waheshimiwa Wabunge waendelee kuwa watulivu na wajiandae kupokea mradi mkubwa wa kupeleka umeme vijijini ambao utakuwa unakmilisha vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijapata umeme.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakubaliana na Serikali kwamba kifungu cha 9 (1)(j) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kinaipa mamlaka PPRA kufanya kazi nyingine ikiwemo ya kuandaa mifumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kwamba mfumo huu wa TANePS umeandaliwa na wataalam wa nje kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia; lakini atakubaliana na mimi, kwamba Serikali kupitia wataalam wa ndani kupitia Wizara ya Fedha imeandaa mifumo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ukiwepo huu wa GPG, MUSE na GSPP.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Juzi tumeona Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, ameonesha nia ya kuitaka serikali kuwa na mifumo michache ili kuongeza ufanisi.
(i) Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuwa na mifumo mingi kwenye taasisi nyingi itaendeleza urasimu badala ya ufanisi?
(ii) Kwa kuwa mfumo huu ukiuangalia na kwa language iliyoandikwa na wataalam hao wa nje haikuzingatia business concept ya nchi, yetu na mfumo huu umekuwa na matatizo mengi, hata siku mbili zilizopita mfumo huu ulikuwa chini na kuleta matatizo makubwa kwenye manunuzi.
Je, haoni kwamba ni wakati muafaka sasa kupitia kurugenzi yetu ya taarifa za mifumo ya fedha pale Hazina tutapunguza gharama kwa ku-integrate mfumo huu na mifumo ambayo nimeitaja hapo juu? (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Silaa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfumo wa TANePS tayari umeshaunganishwa na mifumo mingine ya GPS na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya serikali ikiwemo mifumo ya MUSE nakadhalika ili kupunguza gharama za uendeshaji Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Slaa, ni kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya juzi alipokuwa akipokea taarifa za CAG; kuhusu kuunganisha mifumo ya malipo yote ya Serikali ili kubaki na mifumo michache ili kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa hivyo, Mheshimiwa Rais amesema kwamba tuwe na mifumo michache ambayo inaweza kuendesha Serikali na kupunguza gharama za Serikali ili kuondoa usumbufu na upotevu wa fedha za Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa pale Pugu kwenye Jimbo la Ukonga kuna Mnada wa Upili na tulishafanya ziara pale na Naibu Waziri wa Mifugo na ziko ahadi alizitoa; tukiwa tunaelekea kwenye kipindi cha Bajeti, naomba kauli ya Serikali kuhusiana na maboresho ya mnada ule hasa miundombinu ya ukuta, njia za kuingilia na vitendea kazi vya watumishi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba Mnada wa Pugu ni mnada wa kimkakati na ni katika minada ambayo inaingiza fedha nyingi za maduhuli ya Serikali. Katika Bajeti ya Mwaka 2021/ 2022, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumejipanga kuhakikisha kwamba Mnada wa Pugu unaboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara kwa wakati huu tuko tayari kuhakikisha tunatumia mbinu za mapato yetu kuuboresha taratibu wakati tunaendelea kusubiri Bajeti Kuu ya mwaka 2021/2022.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha na kupeleka fedha kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kivule na tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi na shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Afya ya Kinywa na Meno.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha na kupeleka kwenye Kituo cha Afya cha Mama na Mtoto, Chanika ili kiweze kujengewa wodi na kuweza kupanda hadhi kuwa hospitali kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya wananchi wa Kata za Chanika, Zingiziwa, Msongola, Majohe na Buyuni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kusimamia kwa karibu sana miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Ukonga. Kwa kweli Serikali imeendelea kushirikiana sana kwa karibu na wananchi pamoja na Mbunge wa Ukonga kuhakikisha vituo vya afya hivyo alivyovitaja Kivule na pia kuhakikisha fedha zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali zimepelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Chanika kwa sasa kinatoa huduma kwa akina mama wajawazito, lakini Serikali inaona kuna kila sababu ya kutenga fedha ili kuongeza miundombinu ya huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Chanika ili pamoja na huduma za Afya ya Mama na Mtoto kianze kutoa huduma nyingine kwa wagonjwa ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba katika mipango ya Serikali, tutakipa kipaumbele Kituo cha Afya cha Chanika ili kiweze kupata fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu hiyo na kuhakikisha kwamba huduma zote za afya zinasogezwa kwa wananchi.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na salamu za shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Waitara kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na shukurani zetu kwa Mheshimiwa Rais kwa kumpa nafasi hii, tunaamini swali hili angeweza kulijibu bila hata kusoma, kwa nasaba yake na Jimbo la Ukonga. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Jimbo la Ukonga na Jimbo la Mbagala ndiyo majimbo pekee kwenye Mkoa wa Dar es Salaam ambayo hayaunganishwi na barabara ya lami; na barabara hii ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Kata ya Chanika, Msongola kujiunga na Jimbo la Mbagala.
Naomba commitment ya Serikali kipande hiki kidogo kilichobaki cha kilometa 4.95 ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mazingira ya Jimbo la Ukonga yanafafana na Jimbo la Mbeya Mjini, ni lini Serikali itapanua barabara ya TANZAM inayotoka Dar es Salaam kuelekea Tunduma, kipande cha Uyole – Tunduma kilometa 104, na kipande cha Uyole – Igawa kilometa 116. Barabara hii inasomeka ukurasa wa 66 wa Ilani yetu ya Uchaguzi yenye kurasa 303. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili ni swali la kihistoria, Waswahili wanasema mtoto mpe mchawi akulelee. Ni kweli kwamba barabara ya Mbagala – Mbande naifahamu na Mheshimiwa Jerry pamoja na Mheshimiwa Chaurembo Mbunge wa Mbagala, nilipoteuliwa kuwa Naibu Waziri katika eneo hili suala la kwanza, hata hawakunisalimia, walitaja barabara hii na kwa sababu ya umuhimu wake. Barabara hii ikijengwa vizuri kiwango cha lami wananchi wanaweza wakatoka Ukonga wakaenda Mbagala wakaenda Kusini au Kusini anakuja Dodoma haina sababu ya kupitia mjini kuepuka foleni anaweza akapita eneo hili.
Mheshimiwa Spika, nimekwishaongea na Chief wa TANROAD Engineer Mfugale, kwamba walikuwa wametenga fedha vipande vipande vya matengenezo mbalimbali katika eneo hili. Kuanzia mwezi Julai mwaka mpya wa fedha 2021/2022 Mheshimiwa Jerry na Mheshimiwa Chaurembo barabara hii kilometa 4.9 zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili watu waweze kupata huduma katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wiki iliyopita Mheshimiwa Naibu Spika alikalia kiti hapo ulipokaa, akatoa malalamiko kwamba eneo lake daraja lilivunjika tangu 2019 na mpaka leo anapozungumza na asubuhi amenikumbusha mkandarasi hayupo site na nilitoa maelekezo hapa kwamba mkandarasi aende site wafanye kazi ya dharura ili kuwa na uunganisho katika eneo hilo ili watu wapite.
Mheshimiwa Spika, leo nazungumza habari ya barabara. La kwanza, kabla leo jua halijazama nipate maelezo kwa nini mkandarasi hajawa site katika eneo lile, daraja lile halijatengenezwa tangu 2019 mpaka leo. La pili, kwa kibali chako na kibali cha Mheshimiwa Waziri Mkuu weekend ijayo nitaenda Mbeya kutembelea barabara hii pamoja na daraja nione kama kweli mkandarasi hayupo site, baada ya hapo tutaongea vizuri. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa masuala haya ya mipaka baina ya makazi ya watu na maliasili yamekuwa ni ya kudumu lakini nchi hii inaongozwa na sheria, Sheria Sura 324 inampa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani mamlaka ya kuhakiki mipaka pale panapotokea mgogoro. Kule kwenye Jimbo la Ukonga upo mgogoro mkubwa baina ya Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata za Buyuni, Chanika na Zingiziwa. Tayari uhakiki ulifanyika tarehe 24 Februari, 2012 na magazeti yote yalitoa tangazo na lipo linafahamika.
Je, ni lini Waziri atakuwa tayari tuambatane na wataalam wa Wizara ya Ardhi kwenda kuhakiki mpaka huu na kuwaondolea kero ya kupigwa, kubakwa na kuchukuliwa hatua kinyume na sheria wananchi Jimbo la Ukonga?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mbunge Jerry Silaa kwa kuendelea kuwaonyesha wananchi wake kwamba wamemtuma kwa kazi maalum hapa Bungeni. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya bajeti hii tutaongozana naye kwenda kutatua mgogoro huu. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali moja la nyongeza, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali na niruhusu vile vile kumpongeza kidhati Mheshimiwa Jumaa Aweso Waziri wa Maji kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya katika kutekeleza miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi na shukurani hizi vile vile zimfikie Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini kwenye Wizara hii. Ninaamini wale ambao huwa wanapita pita kutoa zile PhD kama za Dkt. Musukuma punde tu watampa Udaktari wa Miradi ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu haya mazuri na kwa ahadi ya Serikali ya kufikia Mwezi Agosti, 2022 miradi hii itakamilika je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana na Mheshimiwa Mnzava kufanya ziara punde tu baada ya Bunge hili?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana kaka yangu Jerry Silaa kwa kazi kubwa ambayo anayoifanya, katika Jimbo lake la Ukonga kwa kweli anafanya kazi kubwa na nzuri sana na yenye kuonekana. Lakini kubwa kuhusu suala la kwenda katika Jimbo la Mkoa wa Shinyanga niko tayari baada ya Bunge hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanya kwenye miundombinu ya barabara. Tarehe 1 Februari Daraja la Tanzanite limeanza kutumika pale Dar es Salaam. Kwa niaba ya watu wa Dar es Salaam tushukuru sana na nikuombe Kamati za mwezi Machi zifanye ziara Dar es Salaam mpate kupiga picha pale kwenye daraja la kisasa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ya barabara kwenye Jimbo la Ukonga inaweza isitofautiane sana na kule Katavi kwa Mheshimiwa Martha aliyeuliza swali la msingi. Iko barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola (kilometa 14.7) ambayo nishukuru sana Serikali imeshajengwa kwa kilometa 3.2 na kwenye Ilani ya Uchaguzi ukurasa wa 78 inaeleza wazi kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kilometa 11.5 kutoka eneo la Kivule Mwembeni – Fremu Kumi –Msongola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inahudumia watu wengi na hali yake ni mbaya mpaka inasababisha…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry swali.
MHE. JERRY W. SILAA: …mpaka inasababisha Mbunge siwezi kufanya ziara Kivule bila kuwa na mabaunsa wa kunilinda kutokana na kero kubwa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali inieleze, haioni inahitajika jitihada ya dharura kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa kilometa hizi 11.5 kama inavyosema kwenye Ilani ya Uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi kwa niaba ya Serikali kutoka kwa Mbunge kwa kazi ambazo Serikali inaendelea kuzifanya, shughuli za miundombinu na ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga kwamba barabara ya Banana – Kitunda –Msongola kama ilivyoainishwa kwenye Ilani, lakini pia iko kwenye mpango wa Wizara kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali ina mpango wa kukamilisha barabara hii na ndiyo tayari kwanza tumeshakamilisha kilimeta 3.2 na hizo kilometa zilizobaki tunahakikisha kwamba tutazikamilisha ili wananchi waweze kupata huduma sahihi. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia jibu la Mheshimiwa Waziri, na ni kweli kwamba kero ya barabara ni kubwa sana kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na Mheshimiwa Waziri ameahidi maandalizi yataanza januari, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni lini hasa ujenzi wa barabara za
DMDP utaanza katika Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na shukrani zangu za dhati kwa Serikali kwa ujenzi wa barabara lami ya Chanika - Womboza inayoanza kujengwa hivi sasa kero ambayo imeliliwa kwa muda mrefu na diwani wa Kata ya Zigiziwa Mheshimiwa Maige Selemani Maganga.
Naomba kuuliza nini kauli ya Serikali juu ya kutenga fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Dar es Salaam kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa fursa lakini nipongeze majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ninaomba nijibu mawili ya Mheshimiwa Jerry Silaa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itakamilisha majadiliano na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutengeneza barabara Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa miradi hii ni wahakikishie Mheshimiwa Jerry pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam tunashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha negotiations zinaenda haraka iwezekanavyo ili Serikali iweze kufikia makubaliano na Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nini mwongozo wa Serikali kuhusu mapato ya ndani? Nilishatoa maelekezo kwa halmashauri ambazo zinatenga asilimia 60 ya mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo kutoa asilimia 10 kwa ajili ya kutengeneza barabara za mitaa, ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwaelekeza wakurugenzi ambao wanahusika na kigezo hiki kuhakikisha asilimia kumi inatengwa na hawatengenezi barabara peke yao wanaungana na TARURA, kuwa na mpango mkakati mmoja ili wanachokitengeneza tuweze kukipima na kupata uhalisia wa matumizi wa fedha. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. Ahsante sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri hapo hapo simama, huu mradi wa bonde la Jangwani, fedha zilishatoka, wananchi wamefanyiwa tathmini ya nyumba zao miezi saba iliyopita, mpaka leo kuna sintofahamu, kuna nini huko kwenu? Nasikia mara mnataka mjenge daraja kutoka Magomeni mpaka Mjini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, negotiations kati ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali na Benki ya Dunia inaendelea. Lakini kwa sababu Serikali hii nishirikishi na Waheshimiwa Wabunge, kesho mimi, Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Fedha na Mipango na pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, tuna kikao saa saba kwa ajili ya kujadili jambo hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Kwakuwa Serikali sasa inaandaa kanuni za ujenzi, kwa maana ya Billing regulation, nini commitment ya Serikali kuhakikisha majengo yote yanayojengwa kwenye nchi yetu yanazingatia mahitaji wa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali, kwa sasa majengo na ujenzi wowote unajengwa wa Serikali lazima uzingatie watu wenye mahitaji maalum. Na kwa suala la hizo regulation nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lipo na linaendelea kufanyiwa kazi. Lakini hadi sasa hivi hakuna ujenzi wowote unaojengwa bila kuzingatia hayo mahitaji maalum. Ahsante (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Airport – Banana, Gongolamboto – Pugu - Chanika ndiyo barabara pekee kwenye Mkoa wa Dar es Salaam ambayo siyo double road. Naomba kujua mpango wa Serikali wa kuipanua barabara hii na kuwa ya njia nne.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya kuazia Airport kwenda Gongolamboto ni sehemu ya barabara ya Nyerere Road. Barabara hii kama nimemwelewa Mheshimiwa Mbunge, ni barabara ambayo ipo kwenye awamu ya tatu ya hizi barabara za kwenda kwa kasi kwa maana ya BRT. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkataba umeshasainiwa tarehe 17 Machi na Mkandarasi atakayejenga pale ni Sinohydro.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunategemea muda wowote kuanzia pale katikati ya mji kwenda Gongolamboto barabara hii itaanza kujengwa kwa maana ya kupunguza msongamano kwa wananchi wa Dar es Salaam, hasa kwenye Jimbo la Mheshimiwa Silaa, Ukonga. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na kwa operesheni inayoendelea maana Dar es Salaam ilikuwa kila ukikaa unasikia koro koro nyuma ya gari yako, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Kifungu cha 54 cha Sheria, Sura ya 168 ya Usalama Barabarani; je, Waziri ameshatoa vibali vingapi mpaka sasa vya utumiaji wa ving’ora ukiondoa magari yaliyoorodheshwa?
Swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho ya sheria hii ambayo ni ya muda mrefu ili kuweza kutoa adhabu stahiki kwa watu wanaovunja sheria hii, vilevile kuweza kuona namna ya kuongeza viongozi wenye kustahili heshima hii na kuweza kuwaondolea taharuki wananchi. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jerry Silaa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tokea nimepewa dhamana hii sijawahi kutoa kibali hata kimoja.
Pili, kuhusu mabadiliko ya sheria tunao mchakato ambao unaendelea wa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani, kwa hiyo kwa kuwa mchakato huu hatma yake ni hapa Bungeni, basi Mheshimiwa Mbunge naomba hoja zake aziandae vizuri ili kuweza kuhakikisha mchakato huu utakapofika Bungeni aweze kusaidia kutoa hoja za kuongeza yale ambayo anahisi yanafaa katika marekebisho hayo ya sheria itakapokuja. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hospitali ya Mama na Mtoto, Chanika ina upungufu wa general wards za wanaume, wanawake na watoto ili kukifanya kituo cha afya kitoke kwenye hadhi ya kituo cha afya kuwa hospitali: Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizi ili kuweza kuwasogezea huduma karibu wananchi wa Kata za Zingiziwa, Chanika, Mkuyuni, Kongola na Pugu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Hospitali ya Mama na Mtoto ya Chanika ni hospitali ambayo inatoa huduma kwa akina mama lakini ina uhitaji wa wodi ya akina mama wajawazito na wodi ya watoto. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya tathmini na pia tunatafuta fedha kwa ajili kwenda kujenga wodi katika hospitali ile ya Chanika ili sasa iweze kuwa na miundombinu yote kwa ajili ya kulaza akina mama na mtoto. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kuwa suala hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara. Je, Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi kwenda kukutana na wafanyakazi hawa ambao wana malalamiko ya muda mrefu ili kuweza kuwapatia majibu waweze kufunga shauri hili mara moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kama nilivyoeleza na kujibu kwenye swali la msingi kwamba sisi tuko tayari kuweza kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mheshimiwa Mbunge ili kwenda kutatua changamoto za wafanyakazi hawa na kuweza kulifanyia uchunguzi wa kina, kama wapo wanaostahili kulipwa basi watalipwa na tutaweza kilifanyia kazi.
MHE. JERRY W. SLAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule - Msongola inayoenda hospitali ya wilaya kilometa 11.7 ina hali mbaya sana.
Je, Waziri na nimemwona Waziri mwenye dhamana yupo atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi kwenda kutoa majibu ya Serikali, lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Slaa kuhusiana na barabara ya kilometa 11 ya kutoka Banana kwenda Msongola na nimhakikishie kwamba mwezi huu wa Februari tutakapomaliza Bunge atakapokuwa tayari tutaongozana naye kwenda kuangalia barabara hiyo na kuitekeleza, ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kituo cha afya cha Nguvukazi - Chanika kinahudumia mama na mtoto na Serikali, ni lini sasa itaona umuhimu wa kujenga majengo wezeshi kama wodi za wanawake, wanaume na chumba cha kuhifadhia maiti ili kituo cha afya hiki kipate hadhi ya kuwa Hospitali na kuwahudumia wananchi wa Kata za Chanika, Buyuni, Zingiziwa na Msongola?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa JImbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Afya hiki cha Chanika kinahudumia wananchi wengi na tulishatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya Manispaa ya Ilala, kutenga fedha kati ya asilimia 60 kwa ajili ya kufanya upanuzi na ujenzi wa wodi katika kituo hiki. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi kwamba hiki ni kipaumbele cha wananchi ahakikishe anatenga fedha kwenye mapato ya ndani ili tuweze kujenga wodi hizo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nishawahi kuuliza swalli hapa Bungeni la Msitu wa Kazimzumbwi na Mheshimiwa Waziri aliniahidi kwamba Kamati ya Mawaziri Nane itafika kwenda kutatua mgogoro baina ya Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata ya Zingiziwa, Chanika, Buyuni na Pugu, lakini mpaka ninapozungumza hapa Mawaziri Nane hawajafika.
Naomba kujua, Je, ni lini Mawaziri hawa nane watafika kwenda kutatua mgogoro huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ziara ya Mawaziri wa Kisekta hivi sasa ninavyoongea wako safarini kuelekea Arusha na nimuahidi tu Mheshimiwa Jerry kwamba, kwa kuwa oparesheni hii imeshaanza na tunaendelea na zoezi hili tutafika katika msitu huo na tutatatua changamoto hiyo. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; Zahanati ya Mongo la Ndege imejengwa kwa kipindi kirefu tokea nikiwa Diwani wa Ukonga.
Je, Serikali haioni sasa kutokana na ongezeko la wakazi kwenye mtaa wa Mongo la Ndege na maeneo jirani ya Jimbo la Segerea ni wakati sasa wa kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Zahanati ya Mongo la Ndege inahitaji kupanuliwa na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya, kwa awamu hii tunaendelea kwanza na ukamilishaji wa zahanati na vituo vya afya ambavyo kazi ya ujenzi imeanza.
Mheshimiwa Spika, ninatoa wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuona uwezekano wa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza kupandisha hadhi kituo hiki cha afya cha Mongo la Ndege. Ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye Jimbo la Ukonga tarehe 23, Februari, alitoa maelekezo ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanza mchakato wa ujenzi wa soko kwenye Kata ya Gongo la Mboto, soko ambalo litatumiwa na wafanyabiashara ambao kwa sasa wanafanya biashara barabarani na kutumiwa na zaidi ya kata tano. Je, Serikali imefikia wapi kwenye utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Waziri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo aliyatoa ni maelekezo ambayo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alishaelekezwa kuyatekeleza. Kwa hiyo, ninarudia tu kumwelekeza mkurugenzi wa manispaa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafsi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola inatajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ukurasa wa 78, kilometa 11.5, na mpaka sasa Serikali imetenga kilometa 2.2 tu. Ni lini Serikali sasa itatenga fedha za kumalizia kilometa 9.3 ili kutekeleza ahadi iliyoko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge ya Msongola ya kilometa 2.2 ambayo ndiyo imetengewa fedha, tayari nilikaa na Mheshimiwa Mbunge, alikuja kulifuatilia na lenyewe na tukakaa na wataalam wa TARURA kuhakikisha kwamba tunaona ni namna gani tunapata fedha hii ya kilometa 9.3 iliyosalia kama ambavyo iliahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa kuangalia tunafanya vipi ili fedha hizi ziweze kupatikana na barabara hii iweze kutengenezwa.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya Msongola – Mbande nilipewa ahadi kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 itakamilishwa yote kilometa 4.95 kwa kiwango cha lami. Naomba commitment ya Serikali kutimiza ahadi hii iliyotolewa mwaka 2022 hapa Bungeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara aliyoitaja ambayo inaanzia Pugu – Mvuti – Msongola – Mbande inaunganisha majimbo mawili; Jimbo la Mheshimiwa Silaa na Jimbo la Mbagala la Mheshimiwa Chaurembo. Tuna kilometa nne point ambazo bado hazijakamilika. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti tunayokwenda kuitekeleza tutakamilisha kwa lami kipande kilichobaki, ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, Barabara ya Msongola – Mbande kilometa 4.95, ujenzi wa kilometa 1.5 una suasua. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi huo pamoja na kilometa 3.45 za kumalizia kwa lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba tu nichukue nafasi hii kumuelekeza Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Dar es Salaam kumsisitiza mkandarasi kwa sababu yuko site ili barabara hiyo iweze kukamilika ili tuondokane na hiyo vumbi ambayo ina kilomita kama 3.2. Hivyo tutakuwa tumeunganisha barabara yote kwa kiwango cha lami. Ni kumsisitiza tu meneja amsimamie mkandarasi kwa ukaribu. Ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Vijana wengi wa Dar es salaam wanaendesha bodaboda za mikataba. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kushirikiana na ma-bank yanayotoa mikopo ya bodaboda bank ya NMB na bank ya CRDB ili wanapofungua sasa dirisha la mikopo hii ya asilimia 4:4:2 za vijana, wanawake waweze kutoa mikopo ya vijana kuwakwamua kwenye unyonyaji wa mikataba hii ya bodaboda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema utaratibu wa ukopeshaji wa asilimia 10 unafanyiwa kazi na utaboreshwa, kwa hivyo tutaona pia uwezekano wakuchukua wazo hili na kuliboresha kuona namna ambavyo utawezesha vijana kupata mikopo kwa urahisi zaidi kwa kadri ambavyo itaonekana inawezekana, ahsante.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya kuona mahitaji ya barabara za lami kwenye Jimbo la Ukonga. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua zinazoendelea kunyesha Jijini Dar-es-Salaam zimeharibu sana miundombinu ya barabara ikiwemo Jimbo la Ukonga, barabara nyingi zimekatika ikiwemo barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola. Nini mpango wa Serikali wa kuzikarabati kwa dharura, hasa kipindi hiki ambacho wananchi wanapata taabu na barabara hizi?
Swali la pili. Barabara ya Mwembe Supu – Kwakupepeteka – Bangulo CCM mpaka Mwembe Kiboko kwenye Kata ya Pugu Station haijawahi kutengenezwa kwa kiwango chochote. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda kuona barabara hii na kuweza kutoa kauli ya Serikali mbele ya wananchi wa Kata ya Pugu Station? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jerry Silaa kwamba, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilifuatilia sana hili suala, hasa la kupata fedha kwa ajili ya emergency kwenye barabara zake Jimboni kule.
Ninalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki amekuwa akifanya vikao mbalimbali na wenzetu wa TARURA na Wizara ya Fedha kuhakikisha TARURA inaongezewa bajeti ya kutoka bilioni 11 ya emergency mpaka bilioni 46, niwatoe mashaka vikao hivyo vinaenda vyema na Wizara ya Fedha imeahidi kutafuta fedha hizo kwa ajitihada za Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Jerry William Silaa kuelekea katika Jimbo lake la Ukonga na kuzikagua barabara zake. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia ratiba hata weekend tutoke hapa tuelekee Jimbo la Ukonga tuweze kukagua barabara hizo na kuona ni kipi Serikali inaweza ikafanya. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Mvua za masika zimekuwa ni ndefu sana kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na miundombinu mingi ya barabara imeharibika. Tarehe 30 Mei Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kwamba Barabara ya Banana-Kitunda-Kivule - Msongola itapitika na hali bado ni mbaya ikiwemo Barabara ya kwa Diwani – Bomba mbili. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na miundombinu hii ya Jimbo la Ukonga ambayo ina hali mbaya kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry William Silaa naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam aweze kutembelea barabara hizi ambazo amezitaja Mheshimiwa Jerry William Silaa na kufanya tathmini ya haraka na pale tunapoanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kuzipa kipaumbele barabara hizi kwa ajili ya kuzitengeneza.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.
Wananchi wa Mtaa wa Bangulo kwenye Kata ya Pugu Station walikuwa na mgogoro na shamba la Kabimita ambao Serikali iliumaliza kupitia Mawaziri wa Ardhi na Mifugo mwaka 2018 lakini mpaka leo wananchi wamefanya urasimishaji na Kabimita kupitia Wizara ya Mifugo haijakabidhi hati ya eneo hilo.
Je, ni lini sasa Serikali itaenda kukabidhi hati hiyo kwa Kamishina wa Ardhi ili wananchi wa Mtaa wa Bungulo Kata ya Pugu Station waweze kukabidhiwa hati yao na kuishi kwa amani?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga ka,a ifuatavyo:-
Ni kweli kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya kutatua migogoro tayari jambo hili tulikwishafika mwisho na Mheshimiwa Jerry kama ambavyo nimemjibu Mheshimiwa Massare katika swali la awali ni kwamba utaratibu wote ulikwisha kufanyika, wananchi wote ambao wanapaswa kupewa haki wanafahamika nani hatua tu za Kiserikali.
Sasa nitamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Kamishina wa Ardhi, jambo hili lifike mwisho na hatimaye hati iweze kuwa surrendered na wale ambao wanapaswa kunufaika, wanufaike na kama kuna malipo ya premiums ambazo wanatakiwa kufanya, wanatakiwa wafanye sawa na Sheria za Ardhi zinavyoelekeza, ahsante sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wakati ule ilijenga Barabara ya Mombasa- Mazini-Moshi Bar na kipindi hiki barabara hii imeharibika sana hasa kipande cha kuanzia pale Mombasa mpaka Transfoma. Je, Serikali haioni ni wakati sasa kufanya ukarabati wa dharura wa kipande kile cha barabara ili kuwapunguzia wananchi kero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba ni kweli barabara ile ilijengwa na sasa hivi kwa kweli imeharibika kutokana na adha za mvua. Nimhakikishie Mbunge tu kwamba, tunawaagiza watu wa TARURA, Mkoa wa Dar es Salaam waende wakafanye tathmini na kutafuta fedha kwa ajili ukarabati wa barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kauli yake kwamba Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi. Pale Mzinga Injinia Cyprian Romeja na wananchi wenzake wamechanga Milioni 108 na Mbunge amechangia Milioni 8.7 kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo kile cha Polisi kwa kutuchangia fedha za ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu juhudi za Mheshimiwa Silaa na mara kadhaa amenishirikisha juhudi wanazozifanya ikiwemo kuchangia ujenzi wa vituo hivi, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wetu wa uboreshaji, ukamilishaji na uendelezaji wa Vituo vya Polisi eneo la Mzinga ni moja ya Kata itakayozingatiwa katika ukamilishaji huo. Nashukuru sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali kwa mradi mkubwa wa maji wa Kibamba, Kisarawe na Pugu ambao tayari umeaanza kusambazwa kwenye kata mbalimbali za Jimbo la Ukonga. Swali langu je, Serikali sasa ina mpango gani wa usambazaji wa Kata ya Kitunda, Mzinga, Kivule na Kipunguni ambazo hazina usambazaji wa maji haya safi na salama ya DAWASA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyokiri Serikali tumeendelea kufanya kazi nzuri kwa Mkoa wa Dar es Salaam na katika maeneo haya aliyoyataja tayari tunafedha zaidi ya shilingi bilioni 25 kwa ajili ya mradi huu na sasa hivi tayari mkandarasi ameshapatikana tunaratajia kufika mwishoni mwa mwaka 2022 haya maeneo yote usambazaji wa maji utakuwa umewafikia.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi; masuala ya uwekezaji wa viwanda si tu yanaleta tija kubwa kwenye ajira na kusaidia upatikanaji wa bidhaa kwenye soko la ndani yakiwemo mafuta ya kupikia na bidhaa nyingine.
Nini mkakati wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuisaidia Benki ya Rasilimali Tanzania (Tanzania Investment Bank Development) kupata mitaji ya uhakika kwa ajili ya viwanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli azma ya Serikali ni kuona namna gani tunawasaidia wawekezaji hasa wa ndani kupitia kuwasaidia kwenye changamoto ya mitaji ya rasilimali fedha. Kwa hiyo, mojawapo ni kupitia mabenki yetu yanayosaidia wawekezaji ikiwemo Benki hii ya Rasilimali na mabenki mengine. Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ikiwemo hiyo ya kuwapa mitaji au kuhakikisha wawekezaji ambao wanataka kuwekeza kwenye viwanda hivi wanapewa huduma hiyo ya kifedha.
Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanyakazi kuona kila namna inayowezekana kuwezesha benki zetu ambazo zinakopesha wafanyabiashara au wawekezaji katika sekta ya viwanda. Nakushukuru sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuwa Jimbo la Temeke linapakana na Jimbo la Ukonga na sisi ni wanufaikaji wa mradi kwenye Kata za Ukonga na Gongolamboto.
Naomba sasa kujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mradi huu kwa awamu ya tatu unazinufaisha Kata za Majoe, Kivule, Kitunda na Chanika katika barabara za Pugu, Majohe – Gwera katika barabara ya Kitunda, Kivule, Msongola…
SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa hilo ni swali la nyongeza unataka kumaliza barabara zote kweli? (Kicheko)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, aondoe shaka, kuhusu utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa ni mradi unaohusu jiji zima la Dar es Saalam ikiwemo katika Jimbolake la Ukonga. Kwa hiyo mara utakapokamilika barabara alizozianisha ziko katika huo mpango, ahsante sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kauli yake kwamba Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi. Pale Mzinga Injinia Cyprian Romeja na wananchi wenzake wamechanga Milioni 108 na Mbunge amechangia Milioni 8.7 kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo kile cha Polisi kwa kutuchangia fedha za ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nafahamu juhudi za Mheshimiwa Silaa na mara kadhaa amenishirikisha juhudi wanazozifanya ikiwemo kuchangia ujenzi wa vituo hivi, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wetu wa uboreshaji, ukamilishaji na uendelezaji wa Vituo vya Polisi eneo la Mzinga ni moja ya Kata itakayozingatiwa katika ukamilishaji huo. Nashukuru sana.