Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima (26 total)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hujamsikia swali lake naomba ukae ulisikie tena swali lake. Mheshimiwa Hawa Mchafu nakupa nafasi uulize tena swali lako. Ngoja aulize tena swali ili wamsikie,issue siyo majibu,issue ni kumjibu swali ambalo mtu ameuliza. (Makofi)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi tena. Mheshimiwa Waziri mgao wa fedha wa kununulia madawa kwa mwaka huu wa bajeti tuliokuwa nao, umeenda mara moja tu kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati zetu na isitoshe fedha hizo zinakatwa juu kwa juu kwenda kulipa deni sugu lililopo Bohari ya Madawa.Nataka kujua sasa mkakati wa Serikali juu wa ulipaji wa deni lililopo MSD na dawa ziendelee kuwepo katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, wanampango gani kuhakikisha mgao wa fedha unaopangwa kwenda kununulia madawa haukatwi juu kwa juu kwenda kulipia deni?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu kujibu swali naomba kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuifanya siku ya leo iwepo katika ramani ya mipango yake.

Mheshimiwa Spika, pili naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuona kwamba natosha kuwa sehemu ya chombo hiki tukufu cha kuleta maendeleo katika nchi yetu. Tatu naomba nimshukuru sana familia hususani mume wangu Advocate, wakili msomi Metusela Gwajima Mpenzi wangu sana pamoja na watoto wetu…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sasa majibu ya maswali ya nyongeza.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Evelyn, Mary Mkubwa, Mary Mdogo na Victoria Gwajima.

Sasa Mheshimiwa Naomba nijielekeze kwenye swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu kuhusu dawa.

Mheshimiwa Spika, kweli dawa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha zimekwenda mara moja, lakini katika mfumo huu wa sekta ya afya tunapopeleka dawa kutoka MSD, sheria ni cash na carry kwamba ulipe ndiyo upewe hizo dawa, kwa kipindi kirefu vituo vyetu vimekuwa havitekelezi vizuri usimamizi wa cost sharing ile user fees pamoja na bima ili zirejeshe zile pesa huko. Hata hivyo, Serikali imeendelea kupeleka hizi dawa kule kwao, baada ya kuona kwamba wana madeni tukaweka utaratibu kwamba wao sasa wanaruhusiwa kwenda pale MSD wakasaini contract kwamba hizi pesa zisikatwe kwanza tupeleke kule tukafanye ule mzunguko turejeshe. Wengine wamefanya hivyo wanapelekewa hizo dawa kwa utaratibu huo wa makubaliano watalipaje deni, wengine hawafanyi hivyo. Kwa hiyo, nimelipokea, nimelichukua naomba nikawasiliane huko kwenye halmashauri tukaone tatizo liko wapi wa kutekeleza hiyo offer.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la nyongeza la kwamba tutaendeleaje kuhakikisha kwamba pesa zinaenda na Serikali inaendelea kulipa hilo deni. Serikali inampango na mipango yake ni mipana kuimarisha makusanyo ambayo yamekuwa yakivuja sana kule kwenye hivi vituo, lakini pia kufuatilia matumizi ya zile bidhaa tunazopeleka kule. Hivi sasa ninavyosema kuna timu zetu ziko kule zinafanya ukaguzi. Kwa hiyo, msingi mkubwa hapa ni kwamba tunavitaka vituo viende MSD viingie makubaliano lile deni halitakatwa kiasi cha kuwanyima zile bidhaa zao, watachukua bidhaa tutaendelea kuimarisha ili nao watekeleze sheria ya cash and carry.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Tunajua na tunakumbuka kwamba malezi bora ya mtoto yanaanzia katika umri mdogo na ili mtoto aweze kukua anahitaji malezi rafiki kutoka kwa wazazi na walezi.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba watoto hawa wanalelewa na hawa wazazi na walezi yanapowakuta mazingira mabaya mtoto anapoeleza kwa wazazi au walezi anatishwa na wakati mwingine wanaofanya vitendo hivyo wapo ndani ya familia hiyo hiyo, aidha inaweza ikawa ni mjomba, ndugu wa karibu, dada anaogopa kueleza tatizo matokeo yake mtoto anaumia na anaharibika sana kisaikolojia.

Je, Serikali hapa inatuambia nini? Na sababu kubwa ni mojawapo Tanzania ina utaratibu mzuri sana juu ya mpango wake kuna Jirani, kuna Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kuna Kitongoji kila mtu linapotokea kila mtu analijua. Serikali mnatuambia nini juu ya jambo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mmeeleza kwamba kuna mkakati ambao unamalizika, kuna MTAKUWWA, unaomalizika 2022 lakini kuna program ambayo imeandaliwa na mpaka sasa kuna vituo 30, vituo 10 vipo Dar es Salaam, vituo 20 viko Dodoma. Nini matokeo ya vituo hivi ambavyo ni vituo vya majaribio? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana namshukuru Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kwa maswali yake mazuri ya nyongeza na nashukuru sana ni kama ametoa semina hapa. Ni kweli katika swali lake la kwanza masuala ya walezi yanaanza tangu mtoto akiwa mdogo pia matatizo anayopata mtoto akiwa mdogo yanatokana na ile jamii anayoishi nayo ndani na ndivyo tafiti zinavyoonyesha kwamba athari ya kwanza ni wale ambao wanaomzunguka yule mtoto.

Mheshimiwa Spika, katika kulifanyia kazi hili Serikali tumejipanga kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii yetu na Maendeleo ya Jamii hivi sasa tunakwenda kuanzisha mpango kama tunavyofanya kwenye afya, huduma za mkoba au mobile kuzifikia hizi familia na kuzielimisha kaya kwa kaya kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, mwenyewe juzi nilitoka Mwanza kama mwezi mmoja umepita nilifika mpaka kwenye nyumba ambako mtoto aliketishwa anamuhudumia bibi haendi shule mpaka amefika miaka 9 nikajifunza mambo mengi. Kwa hiyo, tukaona kwamba tunavyowafikia wagonjwa wanaoumwa kwa mobile na kliniki tuanzishe hiyo kwenye maendeleo ya jamii ili tuguse kabisa hizi jamii na kuanza kuwalea wazazi wenyewe ili waje kuwalea watoto wote wakiwa na confidence moja.

Mheshimiwa Spika, katika masuala ya vituo hivi vya Dodoma na Dar es Salaam naomba nilipokee hili tumeshaanza evaluation kwa ajili ya kwenda kuona ile impact tuwasilishe taarifa kwenye kamati yetu na itakuja kufika Bungeni kwa ridhaa ya Spika then tunakwenda kupeleka nchi nzima, faida ni kubwa kuliko kutokuwa na vituo hivyo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza Je, Serikali iko tayari kushughulikia masuala ya bima za afya kwa wauguzi wastaafu wakianzia na Hospitali ya Mkoa wa Iringa ili watibiwe bila usumbufu? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni sahihi kwenye mwelekeo wetu huu wa Bima ya Afya kwa Wote tutachukua makundi yote, hakuna atakayebaki nyuma yakiwepo hayo. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Naibu Waziri, tatizo hili la watoto kutelekezwa limekuwa kubwa sana kuzalisha watoto wa mitaani.

Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kutazama upya sheria za kuzuia uwepo wa watoto wa mitaani kwa ajili ya wale wanaotelekeza watoto? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Issaay kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua kwamba tatizo hili ni kubwa na tunakiri kwamba kuna haja ya kufanya kitu cha ziada hapa kuweza kulidhibiti. Niseme kuelekea tarehe 16 Juni, 2021 tunapokwenda kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika, hili nalo tutaliangalia tuliwekeje. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni sehemu mojawapo ambayo tunapata changamoto sana ya kuwa na idadi kubwa ya watoto waliotelekezwa na mara nyingi watoto hawa waliotelekezwa huwa wanakimbilia Ofisi ya Ustawi wa Jamii. Wanapofikiwa kule, Afisa wa Ustawi wa Jamii anapaswa kuwahudumia kwa huduma zote yule mtoto anazokuwa anahitaji mpaka atakapopata kituo cha kumpeleka. Lakini changamoto wanayoipata ni kwamba hawana fedha za kuwahudumia watoto hawa.

Je, ni lini Serikali itakuja na fungu maalum kwa ajili ya Maafisa wa Ustawi wa Jamii kuweza kuwahudumia watoto wao. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila; ni kweli, Serikali inatambua kwamba bado hatujawekeza vya kutosha kwenye eneo hilo kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii wetu waweze kufanya kazi hizi. Naomba niahidi kwamba tutafanya tathmini tuone ili kwenye kipindi kijacho cha bajeti tuweze kuanzisha namna gani ya kuwawezesha hawa Maafisa Ustawi wa Jamii. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatoa matumaini kwamba hospitali hii sasa itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ili hospitali iweze kuanza kufanyakazi inahitaji matayarisho ya kuwa na vifaa tiba vya kutosha ikiwemo ultrasound, x-ray na vinginevyo vyote.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inapofika Julai vifaa tiba vitakuwa vimeshapatikana ili wananchi wa mkoa huu waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa majengo haya mawili ambayo ameyasema umechukua muda mrefu sana kutokana na mfumo uliokuwa unatumika wa force account ambao haukuleta tija sana kwa sababu ya usimamizi hafifu.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba majengo yaliyobaki sasa wanatumia mkandarasi badala ya force account ili yakamilike kwa viwango vinavyokubalika?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Hasunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba hivi ikiwemo x-ray, ultrasound na vingine vyote kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma zinaanza Julai napenda kumhakikishia kwamba tayari tulishapewa fedha MSD inaendelea na manunuzi na ufuatiliaji unafanyika na x-ray itakayokuja na ultrasound tumelenga kuelekeza kwenye hizi hospitali kubwa ambazo tayari zimeshakamilika kwa ajili ya kuanza huduma.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa sababu swali lingine la pili la nyongeza ni kuhusu mfumo huu wa force account kuchukua muda mrefu ni kwa sababu gani tusihamie kwenye utaratibu wa mkandarasi. Naomba kulichukua hili nikaangalie na kabla ya Bunge hili kwisha nitafika pale mimi mwenyewe nikaone uhalisia wa kasi jinsi unavyoendelea sasa hivi kwa ajili ya kufanya maamuzi hayo ambayo ameyapendekeza, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatoa matumaini kwamba hospitali hii sasa itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ili hospitali iweze kuanza kufanyakazi inahitaji matayarisho ya kuwa na vifaa tiba vya kutosha ikiwemo ultrasound, x-ray na vinginevyo vyote.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inapofika Julai vifaa tiba vitakuwa vimeshapatikana ili wananchi wa mkoa huu waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa majengo haya mawili ambayo ameyasema umechukua muda mrefu sana kutokana na mfumo uliokuwa unatumika wa force account ambao haukuleta tija sana kwa sababu ya usimamizi hafifu.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba majengo yaliyobaki sasa wanatumia mkandarasi badala ya force account ili yakamilike kwa viwango vinavyokubalika?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Hasunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba hivi ikiwemo x-ray, ultrasound na vingine vyote kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma zinaanza Julai napenda kumhakikishia kwamba tayari tulishapewa fedha MSD inaendelea na manunuzi na ufuatiliaji unafanyika na x-ray itakayokuja na ultrasound tumelenga kuelekeza kwenye hizi hospitali kubwa ambazo tayari zimeshakamilika kwa ajili ya kuanza huduma.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa sababu swali lingine la pili la nyongeza ni kuhusu mfumo huu wa force account kuchukua muda mrefu ni kwa sababu gani tusihamie kwenye utaratibu wa mkandarasi. Naomba kulichukua hili nikaangalie na kabla ya Bunge hili kwisha nitafika pale mimi mwenyewe nikaone uhalisia wa kasi jinsi unavyoendelea sasa hivi kwa ajili ya kufanya maamuzi hayo ambayo ameyapendekeza, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Kwa kuwa, azma nzima ya kuondoa malaria siyo kupunguza bali ni kumaliza kabisa na Zanzibar wamefanikiwa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kugawa viuadudu hivyo wakati wa weekend zote za kufanya usafi majumbani kwa watu? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa Kamati ya Bunge ilipotembelea kwenye kiwanda hicho ilikuta bado Halmashauri nyingi hazijalipa mikopo ambayo walichukua. Ni lini sasa Serikali italipa ili kiwanda kile kiweze kuendelea vizuri. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE
NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunaelekea kwenye elimination na ndiyo mkakati wa Serikali na tumejipanga pamoja na wadau wetu kwamba tunapata fedha kwa ajili ya kufanya haya masuala ya kununua hivi viuadudu endelevu kwa ajili ya kuelekea kwenye elimination. Kwa mfano, Serikali ya Uswiss kwenye mpango wake wa Miaka Nne, 2021- 2024 kuna bilioni 4.4 zimetengwa ambapo bilioni 3.7 zitatumika kununua lita 284,810 kwa ajili ya utekelezaji huo. Sasa hivi tunaandika andiko ambalo litagharimu bilioni 294 kwenye Mwaka wa Fedha ujao tutalileta kwa wastani wa bilioni 59 kila mwaka tuweze kuwa na utaratibu wa kuwa tunapuliza haya mazalia mpaka kila kitu kiishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haya masuala ya Halmashauri kutokulipa kama nilivyosema kwenye jibu la msingi zimetengwa bilioni 2.7 tutasimamia walipe yale madeni lakini waendelee kuchukua na kupewa viuadudu vingine vya ziada. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa Mikoa ambayo inaongoza kwa maambukizi ya malaria ni pamoja na Mkoa wa Mtwara. Nataka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha Mkoa ule unaondoka katika janga hilo la ugonjwa wa malaria. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE
NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Mtwara ni kati ya Mikoa ambayo ina maambukizi makubwa ya malaria, tunalitambua hilo, iko Mikoa ya Lindi, Katavi na mingine mingi. Tunaipa kipaumbele kwa hizi rasilimali tulizonazo hatutazitumia tu hivi randomly. Kwa mfano Arusha, Manyara, pamoja na Moshi wenyewe wameshakwenda kwenye elimination. Kwa hiyo tutaongeza nguvu sana ku- adress haya masuala ya Mikoa ambayo bado maambukizi yapo juu. Tutashirikiana pia na Wizara ya Mazingira kwa sababu suala hili ni mtambuka kuhakikisha kwamba tunaifikia hii Mikoa tushushe kama Manyara, Arusha na Moshi. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, kaa hapo hapo. Sasa hivi kuna mtindo watu wanapita majumbani wanamwaga dawa kwa barua za Halmashauri asilimia kubwa ya dawa hizo ni maji. Hilo nalo mlidhibiti.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE
NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimepokea na nawatumia salamu huko walipo. Tunaanza kuwafuatilia leo hii tujue walitumwa na nani na kiwango cha ubora wa hizo dawa wanazomwaga. Nasema waache maana Serikali iko kazini. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kuna uchache ama upungufu mkubwa wa hizi mashine za incubator; na anasema kwamba hakuna utafiti wa kisayansi ambao unaonesha kwamba zinaweza kusaidia maisha ya Watoto; je, yuko tayari kuleta utafiti wa kisayansi kuelezea mahusiano ya vifo vya watoto njiti kwa kukosa huduma hasa kwa kutokuwepo kwa hizi incubators?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kama wametambua kwamba Kangaroo Mother Care imekuwa ni njia mujarabu katika kuokoa maisha ya watoto, ni juhudi gani za Serikali zimechukuliwa kuhakikisha elimu hii inafika vijijini ili kuokoa maisha ya watoto? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Londo kwa maswali yako mawili mazuri kabisa. Napenda kujibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, scientific data au scientific evidence kuhusu eneo hili zipo na sayansi huwa inaendelea kufuatilia mambo mbalimbali kadri muda unavyokwenda na ku-adapt marekebisho ili kuboresha. Hivyo, kwa ridhaa yako, kama tutapata fursa tunaweza tukawasilisha kupitia Kamati ya Huduma za Jamii baadaye ikafika Bungeni, hizi tafiti mbalimbali zilizofikia, tukafanya adjustment siyo tu Tanzania, dunia nzima, kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu kufika vijijini, tayari tulishatoa mwongozo wa maboresho eneo hili, upo; na kupitia Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya tutahakikisha tunasogeza elimu hii kwenye jamii ili waweze kuona umuhimu wa kukaa na mtoto kifuani kwao, hasa anapokuwa amezaliwa na uzito pungufu sana tuendelee kuokoa maisha. Hii imeonesha kwenye data zetu za mwaka 2018 mpaka 2020 vifo vimeendelea kupungua kutoka 11,524 mpaka 8,190. Ni katika mikakati hii ambayo tumeichukua ya kuhakikisha kwamba tunaokoa maisha ya watoto.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza; na nitauliza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mashine ya kupima kiwango cha usikivu kwa watoto mara wanapozaliwa (auditory brainstem response test) ipo Muhimbili peke yake hapa nchini. Hospitali zote za rufaa nchini hazina kifaa hiki, sasa ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuhudumia wanafunzi wenye ububu na uziwi na kuendesha kwa gharama kubwa shule hizo: Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha kwamba mashine hizo zinapatikana na inakuwa ni lazima kwa kila mtoto anayezaliwa kupimwa kiwango chake cha usikivu?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa swali zuri la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha, Mbunge, kuhusu masuala ya kuwapima watoto kiwango cha usikivu pale wanapozaliwa, kwamba ni gharama sana kwa sababu ni hadi uende Muhimbili. Nakubaliana kabisa na ninampongeza kwa kuliona hili.

Mheshimiwa Spika, niweze tu kusema haja ipo na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu ya hospitali za kibingwa, hasa za kanda ili kusogeza siyo tu vifaa, pamoja na hawa wataalam wanaotakiwa kupima. Tuna hospitali yetu ya Mtwara imeshafikia asilimia 95, tuna ya Chato inakamilika, pia tuna Meta Mbeya inakamilika.

Mheshimiwa Spika, ni pendekezo la msingi na ni hoja ya msingi sana. Katika bajeti inayokuja tutaanza kuona kadri tunavyozindua, hata hawa wataalam wanaoshughulika na masuala ya usikivu, tuendelee kuwapa training tuwasogeze kwenye hospitali hizo. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na kutokana na hayo basi swali langu la kwanza litakuwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu zake na kwa jinsi hali halisi ilivyo, zipo Halmashauri ambazo hazijakamilisha zoezi hili na ni kwa madai kwamba hazina mapato ya kutosha. Sasa je, Serikali inatoa tamko gani kwa zile Halmashauri ambazo hazina fedha za kutosha kukamilisha zoezi la utambuzi na la utoaji vitambulisho? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba lipo tatizo wazee wanapofika hospitalini wanaandikiwa dawa na kuambiwa waende kununua katika maduka ya dawa kwa madai kwamba katika kituo husika hakuna dawa: Je, Serikali inatoa maelezo gani pale ambapo wazee wanakuwa wakiambiwa wakanunue dawa ilhali wanastahili kupata matibabu ya bure? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge Anastazia kwa kuendelea kuwatetea na kuwapambania wazee. Naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kweli zipo Halmashauri ambazo zinashindwa kutimiza hili, kati yake zipo ambazo hawatimizi tu mpaka uwafuatilie sana na wapo wengine ambao kwa kweli uwezo wao unakuwa mdogo sana. Niseme kwenye bajeti yetu hii iliyopita, nilishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kupitisha ile bajeti yetu ya shilingi bilioni 149 ambazo tunatarajia kwenye muswada huu wa sheria zitakwenda kuhudumia zile nyumba zote wakiwemo wazee ambao watakuwa wamebainika kwamba hawana uwezo kabisa. Kwa hiyo, tunatarajia kumaliza kabisa hili suala la wazee hawa wasio na uwezo kabisa ili wawe covered kupitia Mpango wetu wa Bima ya Afya Kwa Wote tunaotarajia kwenda kuuchukua.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tumekuwa na vikao vya kwenye mtandao pamoja na Mtandao wa Wazee nchi nzima, kila Jumamosi; tumeanza hiyo sera, “Jumamosi Zungumza na Wazee.” Tunafanya hivi vikao kujadili hizi changamoto. Wiki iliyopita tumekubaliana kwamba; awali iliagizwa asilimia sita ya bajeti tunayopanga lazima dawa zake ziende kwa wazee. Kwa hiyo, hata sasa hivi Serikali imefanya uamuzi wa kurudisha kupitia Hazina ile fedha ya Hospitali kwa mfano za Mikoa iliyokuwa inaenda moja kwa moja MSD, ili dawa zinapokosekana, zinunuliwe huko kwenye hospitali. Asilimia sita ya ile fedha ndiyo itumike kununua hizo dawa za wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Kamati za Maamuzi kwenye Vikao vya Bodi za hizi hospitali zetu, tumeona kwamba tuweke hata mwakilishi wa wazee awe anahakikisha kwamba anatetea ile hoja yake pale. Hii ni mikakati ya kufanya kwamba wazee wawe na sauti katika vikao vya maamuzi vya management za hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tumeanza mkakati wa kila hospitali; mnawaona wale wamevaa nguo za “Mpishe Mzee Apate Huduma Kwanza.” Hawa nao wanachukua takwimu za kujua mzee gani amekwenda kituoni, ameondoka bila dawa ili Medical Officer in Charge ahusike kuhakikisha mzee huyu anapata dawa kwa taratibu hizi za kuweka bajeti ya dawa pembeni yao. Ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nami niungane na Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya sekta ya Asasi za Kiraia, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara hii mpya mahususi ambayo inalenga kusimamia masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, na kwa kuwa tunafahamu sisi waswahili tunasema anayemlipa mpiga zumali ndio anayechagua wimbo, sasa kwa mustakabali huo na kwa kutambua kwamba NGOs nyingi zinapata fedha ambazo zimetengwa na Serikali za nje; je, Serikali haioni ipo haja ya kuona namna gani ambavyo pia itatenga fedha kwa ajili ya NGOs za ndani ili kuepusha baadhi ya NGOs kwenda na kufanya kazi ambazo zinakwenda kinyume na maadili na malengo ya Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa hali ya sasa ipo changamoto kubwa sana kwa upande wa TRA na namna ambavyo inaangalia hizi NGOs. Pale ambapo inatokea NGO inapata rasilimali fedha na inakwenda kutekeleza mpango ule kutoka mwaka mmoja kwenda wa pili, TRA wanatoza kodi ya mapato kwenye hizi NGOs kwenye zile fedha ambazo zinakuwa zimebaki mwisho wa mwaka, lakini zinakwenda kutekeleza mradi mwaka unaofuata. Nwa kwa mantiki hiyo TRA inafanya hivyo kana kwamba NGOs zinafanya biashara wakati hazifanyi biashara, zinatoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni haja ya kuleta hizi sheria, kanuni na haya maelezo mbalimbali ambayo yanatoa fursa kwa TRA kufanya hivyo ili iletwe Bungeni ifanyiwe maboresho ili kuimarisha mazingira wezeshi kwa hizi Asasi za Kiraia ili ziweze kuendelea kufanya kazi kwa tija na kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii ambayo kimsingi ili Wizara hii itekeleze malengo yake ni lazima ifanye kazi kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa nyingine niweze kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Neema Lugangira.

Mheshimwa Mwenyekiti, nianze na sehemu ya kwanza, kwamba Serikali ina mpango wa kutoa fedha kwa ajili ya Mashirika haya Yasiyo ya Kiserikali. Niseme kwamba Serikali imekuwa ikifanya hivyo tangu miaka ya nyuma kwenye baadhi ya taasisi chache ile zile NGOs ziweze kuchangia maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni CCBRT, ile ni hospitali yetu ambayo inawanufaisha akinamama na watoto na watu wengine wenye magonjwa mbalimbali ya ulemavu. Imekuwa ikipeleka fedha kule tangu miaka ya 2000 na
kikubwa katika mwelekeo huo, pamoja na hili andiko tunalolifanyia kazi, bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali inajielekeza kuanza kutekeleza mpango wa ruzuku kwenye baadhi ya hizo NGOs zitakazokuwa zimeonekana zina vigezo na tutawasilisha kwenye kipindi cha bajeti, mtaweza kuona mwelekeo huo wa Serikali.

Mheshimwa Mwenyekiti, aidha, katika kipengele kingine cha pili cha swali, maboresho ya kanuni na sheria ili kuzifanya hizi NGOs zetu ziweze kufanya kazi kwa kujiamini na kuwa na uendelevu baadaye. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu alishaelekeza, andiko limeanza kuandikwa lakini tayari tumeanza kutekeleza kupata maoni kutoka kwenye NGOs mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilifanyika kikao Arusha; Mashirika 200 yalikaa yakatoa maoni na tarehe 5, hapa Dodoma kinafanyika kikao kingine, NGOs nyingine zimealikwa, zitakuja kutoa maoni na baadaye tunakwenda Mwanza Kanda ya Ziwa, tunafunga. Yale maoni ndiyo tutayafanyia kazi na kuyachakata kuona tunaendaje katika suala zima la kuhakikisha sheria na kanuni zote zilizopo zilizopitwa na wakati ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo hatua tuliyonayo. Lengo kubwa la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona NGOs hizi zilizo ndani yetu zinapunguza utegemezi, zinakaa vizuri na kushiriki kuwa wanufaika wa Serikali yao kupitia National Cake. Ahsante. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. kwa kunipa nafasi. Pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri, moja ya changamoto kubwa anayoanza nayo kwenye Wizara hii ni mauaji ambayo yanaendelea katika jamii hasa katika yanayosababishwa na jinsia, ikiwepo wanawake kuwaua wanaume, wanaume kuwaua wanawake, watoto kuwaua wazazi wao kwa ajili ya kupata mali: -

Je, Wizara imejipangaje sasa kabla ya kufikia kwenye vyombo vya usalama kuhakikisha kwamba wanazuia hali hii inayoendelea katika jamii?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kuhusu vitendo vya ukatili vinavyoendelea kwenye jamii yetu. Ni kwamba tunao mkakati wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto mpango wa Taifa uliozinduliwa mwaka 2017/2018 na unakwenda mpaka mwaka 2021/2022, ambao umeandaa Kamati kwenye ngazi ya Kijiji zinazoongozwa na Wenyeviti wa Serikali za Kijiji, Mtaa, Kata, Halmashauri mpaka Taifa na mkoa ukiwemo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hizi tumeshazipelekea maelekezo na leo tunakwenda kuazimisha Siku ya Kupinga Ukeketaji tarehe 6 Februari, 2022. Hii ni Fursa ya kuziamsha hizi Kamati zote zifanye kazi yake. Zikitekeleza majukumu yake yaliyomo kwenye huo mwongozo, tutaweza kudhibiti ukatili huo unaotokea kwenye jamii kwa kuona viashiria husika na kuvitolea taarifa katika vyombo husika vinavyoshughulika na uhalifu.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii ya swali la nyongeza. Licha ya Serikali kuleta Wizara hii maalum kabisa ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, naomba kufahamu ni nini mpango wa Serikali kuajiri Afisa Maendeleo Jamii Kata na Afisa Maendeleo Jamii wa Vijiji ambao ni wachache sana ili wanawake wetu waweze kufikiwa na kuweza kukua kiuchumi? (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Ulenge. Serikali inatambua upungufu wa watumishi hawa, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii. Kadri ya asilimia 96 kwenye Kata zetu hazina hawa watu; na kwenye bajeti ya mwaka huu tutapanga kuanza kupunguza upungufu huo kwa kushirikiana na wadau wetu.
MHE. AMINA DAUDI HASSAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili iweze kupunguza changamoto ya ndoa za siri na za utotoni?(Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amkina Daudi Hassan, kuhusu Sheria ya Ndoa na Marekebisho yake.

Mheshimiwa Spika, wiki ijayo Kamati ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Sheria na Katiba zinaketi kikao kwa ajili ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Hivyo, basi tumepokea hoja yake, tunaenda kuwasilisha tujumuishe ili vijadiliwe pamoja. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria za ndoa, lakini kuna tatizo kubwa sana la malezi kwa watoto wetu. Kuna changamoto kubwa sasa hivi ya wazazi kuwapeleka watoto wadogo kuanzia nursery school mpaka sekondari katika shule za boarding na watoto kukosa malezi ya wazazi. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa mitaala inarudishwa kwa mfano ile ya sayansikimu katika shule zetu ili watoto waweze kupata malezi na kupata elimu za kujitegemea?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimkiwa Dkt. Ritta Kabati la nyongezab kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumepokea hoja yako. Ni kweli, kuna kasi kubwa ya mmomonyoko wa maadili inayoendelea na inasababisha masuala mengi sana ya visa vya ukatili. Kwa sababu marekebisho ya mitaala yanaangukia sekta nyingine tumelipokea tutakwenda kukaa tulijadili kwa pamoja, tujange hoja tuone namna gani tunaweza tukafanya ili kurekebisha hiyo mitaala ikidhi na kuakisi changamoto za sasa kwa ustawi wa Taifa letu la kesho.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa ukatili huo upo nchi nzima, kwa nini vituo hivi vimejengwa katika mikoa miwili tu yaani Dodoma vituo 20, Dar es Salaam vituo 10, ilhali changamoto hii ipo nchi nzima ikiwepo Mkoa wetu wa Iringa?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara hii sasa haioni haja ya kushirikiana a Wizara ya Elimu ili kuwa na shule maalum zitakazotoa msaada kwa watoto walioathirika na ukatili huo kama ilivyofanyika katika programu ya MEMKWA?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Kabati Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu hivi vituo 30 vilivyoanzishwa vilikuwa ni vituo vya awali vya majaribio ili kutuwezesha kuona jinsi mfumo unavyofanya kazi. Kwa sasa tumeshaona na tayaru tuko kwenye maandalizi ya mwongozo wa jinsi ya kuvianzisha na kuviendesha nchi nzima, katika mikoa yote. Tunatarajia mapema mwakani mwongozo ukamilike ili tuende nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu kuufanya mfumo tuwe kama mfumo wa MEMKWA katika suala zima la kuwafundisha hawa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo uliopo unafanya kazi vizuri kiasi kwamba mtoto anapokutwa na matatizo anapata huduma za kisheria, kisaikolojia, kiafya, chakula na tunamrejesha kuendelea na maisha. Ikitokea sasa kuna tatizo lingine linalozuia asiendelee vizuri tunawapeleka kwenye nyumba salama makao ya watoto na hapo tunaungana na Wizara ya Elimu kutafuta aendelee shule gani tofauti na ile ya awali. Hivyo basi, tumepokea maoni kama itabidi iwe hivyo tutajadili na Wizara ya Elimu kwa nyakati zijazo tuone jinsi ya kufanya, lakini sasa hivi mfumo unafanya kazi vizuri.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini hata hivyo swali hili naona halipaswi kujibiwa na Wizara hii. lakini nitauliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa kuna baadhi ya Wizara kama vile Wizara ya Ardhi na Wizara ya Afya imeweza kuhamisha wataalam wa kada zinazoendana na Wizara zile kutoka halmashauri kwenda kwenye Wizara mama zao. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya tathmini ya kina ya Sera hii ya Ugatuaji ili kuendana na mahitaji halisi ya sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu namba mbili; kwa kuwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la upotofu wa maadili nchini, kama vile ukatili wa watoto na wanawake. Je, Serikali haioni haja katika Ofisi ya Sekretarieti ya Mkoa (RAS) kuwepo na RAS Msaidizi kwa ajili ya maendeleo ya jamii? Kwa sababu mpaka sasa hivi ofisi zote za mkoa hakuna RAS Mmsaidizi kwa ajili ya issues za maendeleo ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi kama nilivyosema kwamba Serikali sasa baada ya kuundwa kwa Wizara hii mpya inaendelea kuangalia utaratibu gani mzuri utaweza kuimarisha uratibu au mfumo wa ngazi ya mkoa mpaka kwenda kwenye halmashauri ili Wizara hii ambayo sasa hivi inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii iweze kufanya kazi kwa uharaka na ufanisi kwa kuwatumia wale wataalam wake. Hivyo basi niseme kwamba nimepokea mchango wake na tunapoendelea na majadiliano haya ya kuimarisha hii mifumo tutawasilisha ili Serikali kwa ukubwa wake na upana wake iweze kuangalia.

Lengo letu ni kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa kule na wataalam hawa ziko vizuri wakati wote na za haraka na jamii inabadilishwa fikra zao ili kupokea maelekezo na matakwa ya utekelezaji wa sera zingine zote. Naweza nikaweka hivi kwa ujumla wake.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa katika mikoa 12 iliyotajwa ya hizo nyumba, Mkoa wa Singida siyo miongoni mwa Mikoa iliyo na hiyo huduma. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha nyumba hizo katika Mkoa wa Singida?

Swali la pili, kwa kuwa ukatili kwa watoto bado unaendelea siku hadi siku. Je, Serikali imefikia wapi au ina mpango gani wa kuanzisha Vituo vya Kulelea Watoto (ECD Centers) ili kuhakikisha kwamba wazazi wanakuwa wanawaacha watoto kwenye mikono salama? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nehemia Gwau: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga nyumba salama katika Mkoa wa Singida, ni dhahiri kwamba iko mikoa mingi kweli ambayo haina nyumba salama, hapa ni mitano tu inayo, na wizara inafanya jitihada za kuwasiliana na wadau ambao wamekuja kutusaidia katika mapambano haya ya kutokomeza ukatili. Andiko hilo likipita, tutapeleleka hizi rasilimali katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa ikiwemo huko Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kupitia mwongozo huu, tunaomba mamlaka za Mikoa na Halmashauri na wadau walioko huko waone umuhimu wa kuanza kuanzisha nyumba hizi wakati Wizara inakuja kuongezea nguvu. Vilevile kwenye bajeti zinazokuja; mwaka ujao tutaendelea kutenga fedha kidogo katika ngazi zote kwa ajili ya kuchochea ujenzi wa nyumba Salama hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu maelezi ya Watoto, ni kweli, mpango wa Serikali ni kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri kwa kuwajengea vituo vya kuwalea na kuwakuza katika maeneo ya jamii. Sasa tuna vituo 200 tumeshirikiana na wadau kuvijenga. Formular ni ile ile, tunahamasisha wadau waliopo kwenye Halmashauri zetu waendelee kujitokeza na kuchangia fedha kwa ajili ya vituo hivi, lakini kwenye bajeti zetu tutatenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi sasa Wizarani tuna kikao kinaendelea cha resource mobilization. Hivyo, tukiipata, tutaanza kuwapelekea wale ambao wameshamiliki na wameanza huku tukiwaelimisha wengine ambao bado hawajaona umuhimu huo, kuamka na kujipanga kwenye bajeti za mwaka unaokuja, ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Baadhi ya wahanga wa ukatili wamekuwa wakirushwa picha zao katika mitandao hivyo kutwezwa utu wao; na hivyo kusababisha baadhi ya ambao wanafanyiwa ukatili kutokutoa taarifa: Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na jambo hili?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq kuhusu hao wanaopiga picha mitandaoni, kweli inasikitisha sana. Serikali imekuwa ikitoa maelekezo na maagizo ya kwamba waache kufanya hivyo, na wamekuwa wakiendelea. Sasa kauli ya Serikali ni kwamba, vitendo hivyo ni vibaya katika malezi, makuzi na maadili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo hivyo vinawaharibu watoto wetu ambao ni Taifa la kesho. Kwa sababu wamekuwa hawasikii, sasa hili ni onyo la mwisho, vinginevyo nakwenda kuita kikao cha wadau wote na wote hao waliopiga hizo picha za namna hiyo, nitaongoza kwenda kuwashitaki kwa mujibu wa sheria kwenye Jeshi la Polisi ili sheria zetu tulizozitunga wenyewe zifanye kazi yake, zisikae tu kabatini. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa kuozesha mtoto bila ridhaa yake ni unyanyasaji wa kijinsia; je, ni lini mwangozo huo utamalizika?

Swali la pili, je, kwa nini jambo hili lisiingizwe kwenye sheria? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo huu umeshakamilika na kinachofuata ni kuzindua. Kwa swali lake zuri la leo tutaenda kuzindulia Manyara hukohuko au Arusha na tutamualika na yeye awepo ili awe Balozi kabisa wa kubeba ujumbe huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili kuhusu masuala ya sheria, ni kweli naona umuhimu huo, kwa sababu bado tunaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Mtoto nimelipokea tutaliwasilisha kwenye Kamati waone itifaki ya kisheria kwa sasa kama inaweza kuingizwa au kunahitaji tafiti zaidi kisha tutawasilisha taarifa. Ahsante.(Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kubaini mila zote nzuri ili kurithisha vijana wetu wa sasa waachane na mambo ya kigeni?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nchini Tanzania tunazo mila nyingi sana nzuri ambazo kwa wakati wa sasa zingetusaidia kupambana na mabadiliko ya mmomonyoko wa maadili katika dunia nzima jinsi ambavyo inakumbwa. Hivyo basi, nimepokea hoja hii, tutakwenda kuunda kikosi kazi tukishirikiana na Wizara ya Utamaduni, Michezo na Sanaa pamoja na Wizara nyingine zote tuweze kuja na list ya hizo mila nzuri, kwa pamoja tuweze kuweka mkakati wa kuzielimisha, kuzithibitisha na kuziweka kwenye kumbukumbu sahihi za mila zetu ambazo tutakuwa tunazifanyia kazi Nchini.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hivi karibuni kumeibuka utamaduni mzuri na mila nzuri sana ya kumtetea, kumlinda na kumjengea uwezo mtoto wa kike, lakini tunao utamaduni wetu ambao mtoto wa kiume ni baba au kiongozi wa familia: Je, Serikali ina mpango gani wa kumuimarisha na kumjengea uwezo mtoto wa kiume ili awe kiongozi mzuri wa familia? (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha, Mbunge, swali zuri kabisa, tuna utamaduni gani wa kumjengea uwezo mtoto wa kiume? Ni kweli kabisa tunatambua sasa hivi pia mtoto wa kiume tofauti na awali anakumbwa na changamoto nyingi sana zitokanazo na mmomonyoko wa maadili, anakosa malezi na makuzi bora, kiasi kwamba sasa hata akija kuwa baba atashindwa kuwa baba mzuri wa kupambana na changamoto za familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Serikali inatekeleza mpango wa malezi na makuzi ya watoto kwenye umri wa awali ambapo hii inaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya kulea watoto hawa kwenye ngazi ya jamii, na kule tunakuwa na watoto wa kiume na wa kike. Tuna mpango wa pili wa kuwawezesha na kuwaendeleza vijana balehe, kuanzia miaka 10 mpaka 19. Sasa hapa tutajikita tu kuongezea nguvu zaidi katika uwekezaji, pengine tuje na programu za kimkakati zinazojikita zaidi kwenye masuala ya watoto wa kiume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani watoto walikuwa wanapelekwa jando, lakini sasa hivi tutakuwa tunapeleka jando la kisasa na miongozo yao mizuri mizuri inayosema maana ya kuwa baba pindi wanapokuwa vijana balehe wajue changamoto watakayokutana nayo huko kwenye ndoa kwamba ndoa siyo mchezo, lakini itawezekana kwa sababu tumewaandaa.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa mpango wa malezi na makuzi kwa mtoto ulishazinduliwa: Je, ni lini utekelezaji huu utaanza? Ahsante (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto tulishauzindua tangu mwaka 2021, unakwenda mpaka 2026. Mojawapo ya afua zilizopo mle ni hizi za kujenga vituo hivi vya malezi na makuzi. Tayari vituo 200 vimeshajengwa kwenye maeneo mbalimbali ya jamii na sasa tunatafuta rasilimali na kuhamasisha jamii na wadau tuendelee kujenga kwenye maeneo ambayo yana hali mbaya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpango huu unatekelezwa na tayari kuna watoto wapo humo wanapata hizi huduma na jamii imethibitisha kwamba kweli sasa hivi wazazi wanapata amani ya kwenda kutafuta maendeleo huku watoto wao wakiwa salama. Tutaongeza kasi hii na tutaleta taarifa kupitia Kamati zetu tunavyoendelea. (Makofi)
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini mbali ya watoto ambao wapo katika vituo pia, kuna watoto ambao wapo katika vijiji na mitaa, hasa vijijini. Pamoja na mpango mzuri wa Serikali wa kutoa elimu kupitia Maafisa wa Maendeleo ya Jamii, je, Serikali ina mpango gani au haioni kuwa, sasa ipo haja ya kutafuta wafanyakazi wa kujitolea katika ngazi ya vijiji wakapewa mafunzo ili huduma hii isogee karibu na jamii? Ahsante.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis. Serikali ina mpango wa kufikisha huduma hii ya kuwarekebisha watoto hawa mpaka kwenye ngazi ya familia na jamii na kwamba, inatekeleza mpango wa kuwadahili wahudumu wa ngazi ya jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, wahudumu hawa wataungana na Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa Jamii na kujengewa uwezo kuwa wanafuatilia kuanzia kwenye ngazi ya familia ili kuweza kuwabaini mapema pamoja na kuzuia kwa kuielimisha jamii, wazazi, walezi na wanafamilia jinsi ya kufanya ili kuepuka vitu vinavyoweza kusababisha mtoto mwenye ulemavu kupatikana.