Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya (14 total)
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-
Je, ni lini uzalishaji wa madini ya niobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium katika Wilaya ya Mbeya unahusisha leseni tatu za uchimbaji wa kati na eneo hili lina jumla ya kilometa za mraba 22.1. Mradi huu unatarajiwa kuwa na uhai wa miaka 30 na unamilikiwa na Kampuni ya Panda Hill Tanzania, ambayo ni kwa ubia wa 50:50 na kampuni za Cradle Resources Limited na Tremont Investments. Mradi huu utahusisha uchimbaji wa madini ya niobium ambayo yataongezwa thamani nchini kwa kuchanganywa na madini ya chuma ili kuwa na mchanganyiko wa madini ya FerroNiobium, zao hili ndilo lenye soko katika nchi za Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, Mwekezaji aliwasilisha Wizarani maombi ya misamaha ya kodi katika uwekezaji wake. Mwekezaji alielekezwa na Wizara kufuata matakwa ya Sheria ya Madini ambayo ndiyo inayotumiwa na wawekezaji wengine wote katika Sekta ya Madini.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa mwekezaji kukamilisha taratibu za kumwezesha kuanza utekelezaji wa mradi ikiwepo pia kupata ridhaa ya maandishi kutoka kwa wamiliki wa maeneo katika leseni zake kama ilivyo Sheria ya Madini. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti ili kubaini uwepo wa aina mbalimbali za madini katika Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Kata za Sasilo, Makuru, Kintinku na Solya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi yetu ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST) kwa nyakati tofauti imefanya utafiti wa awali, nisisitize tu utafiti wa awali katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania zikiwemo Kata za Makuru, Solya, Kintinku na Sasilo ambako ndiko Mheshimiwa Mbunge anatoka.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya tafiti za awali zilizofanyika katika maeneo hayo zinaonesha kuwa kuna viashiria vya uwepo wa madini kama ifuatavyo:-
(a) Katika Kata ya Makuru – kuna dhahabu kidogo pamoja na ulanga (nickel);
(b) Katika Kata ya Solya – Kuna urani, thorium na madini ya ujenzi;
(c) Katika Kata ya Kintinku – kuna Urani; na
(d) Katika Kata ya Sasilo – kwa utafiti uliofanyika hakukuonekana kwamba kuna viashiria vya uwepo wa madini.
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha uchimbaji kufanyika, mara nyingi sana tafiti za kina zinahitajika ili kujiridhisha na kiwango cha mashapo iwapo yanaweza kuchimbwa kwa faida au la.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa matokeo ya tafiti za madini katika lugha nyepesi kwa wachimbaji wadogo ili ziwasaidie katika uchimbaji kwa kuwa Sheria ya Madini inazitaka Kampuni zinazofanya utafiti kwenye madini kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo GST?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) tangu mwaka 2019 imekuwa ikitoa matokeo ya tafiti za madini kwa lugha ya Kiswahili na iliyorahisishwa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuelewa kwa urahisi. Aidha, GST imeandaa kitabu mahususi chenye Kichwa “Kitabu cha Madini Yapatikanayo Tanzania” ambacho nacho kimeandaliwa kwa lugha ya Kiswahili na kinabainisha maeneo yenye viashiria vya madini ya aina mbalimbali yanayopatikana nchini.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, GST imeandaa Kitabu cha Mwongozo wa Uchukuaji wa sampuli za madini na kitabu hicho ni cha mwaka huu huu wa 2021 ambacho pia kimeandaliwa kwa lugha fasaha ya Kiswahili, nyepesi na inayoeleweka, lengo likiwa ni wachimbaji wetu wadogo waweze kufaidika na lugha hiyo iliyorahisishwa. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalinda Akinamama wanaochenjua dhahabu dhidi ya sumu ya zebaki ambayo ina madhara makubwa kiafya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali katika kuwakinga akinamama wanaochenjua dhahabu kwa kutumia kemikali ya zebaki ni kuendelea kutoa elimu ya uchimbaji na uchenjuaji salama wa madini pamoja na madhara ya kemikali hiyo kwa wachimbaji wadogo. Elimu hiyo inatolewa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mpango huu, Serikali kupitia Wizara ya Madini imejenga Vituo vitatu (3) vya Mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika maeneo ya Itumbi (Chunya), Lwamgasa (Geita) na Katente (Bukombe) ambayo yameonekana kuwa na wachimbaji wadogo wengi zaidi. Teknolojia ya uchenjuaji inayotumika katika vituo hivyo ni Carbon–in–Pulp (CIP) ambayo ni mbadala wa matumizi ya kemikali ya zebaki.
Mheshimiwa Spika, zipo kampuni tayari za uchimbaji mdogo ambazo zimeanza kuchenjua dhahabu kwa kutumia teknolojia ya shaking table, meza inakuwa itatikiswa kufuatia gravity ambayo haitumi zebaki wala kemikali yoyote. Teknolojia hii Wizara inaendelea kuifanyia majaribio ili kuona tija yake kabla ya kuanza kuitumia kwa wachimbaji wote hasa wale wachimbaji wadogo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira?
(b) Je, ni lini baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira watalipwa stahiki zao baada ya mgodi huo kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, yenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mgodi wa makaa ya Mawe wa Kiwira ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2013 kwa lengo la kuuendeleza. STAMICO kwa kushirikiana na TANESCO wanaendelea na mpango wa pamoja wa muda mrefu wa kuanzisha mradi wa kuzalisha umeme zaidi ya megawatt 200 utakaotumia makaa ya mawe yatakayozalishwa katika mgodi huo. Makubaliano ya ushirikiano baina ya STAMICO na TANESCO yako hatua za mwisho kabla ya kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha kusainiwa.
Mheshimiwa Spika, tayari timu ya wataalam wa STAMICO na TANESCO imetembelea eneo la mradi kwa lengo la kutambua mahitaji halisi ya uendelezaji wa mradi huo na STAMICO imeanza kufanya ukarabati wa miundombinu ya mgodi wa chini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzalishaji mkubwa kwa ajili ya mahitaji ya mitambo ya kuzalisha umeme. Aidha, kutokana na ukubwa wa mradi, Mashirika haya yanaendelea na jitihada za kutafuta fedha na uwekezaji kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kuihusisha Serikali yenyewe kuona uwezekano wa kutengewa sehemu ya bajeti kwa ajili ya uwekezaji huo.
(b) Mheshimiwa Spika, kipindi ambacho mgodi unakabidhiwa kwa STAMICO kulikuwa na malimbikizo ya madeni yanayofikia shilingi bilioni 1.02 ikiwa ni stahiki na mapunjo ya wafanyakazi takriban 893 waliopunguzwa. Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na shirika tayari imehakiki deni hilo kwa mara nyingine mwezi Juni, 2019 na taratibu za ulipwaji wa madeni hayo zinaratibiwa na Hazina. Nakushukuru.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa Madini ya Nickel unaotarajia kuanza katika eneo la Kabanga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mbunge Mheshimiwa Ndaisaba kwa jinsi ambavyo anafanya ufuatiliaji kuhakikisha kwamba, wananchi wake wa Jimbo la Ngara wananufaika na mradi tarajiwa wa uchimbaji. Serikali imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini kupitia Marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kutungwa kwa sheria mpya za usimamizi wa rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini, Sura 123, imeweka bayana kuwa, makampuni yote ya uchimbaji madini ni lazima yawasilishe mpango wa ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya uchimbaji kwa maana ya local content plan ambao ni lazima ubainishe manufaa yatakayopatikana kwa wananchi kutokana na uanzishwaji wa miradi ya madini. Hivyo, kwa kuzingatia matakwa hayo ya Sheria, Serikali itahakikisha kwamba inachambua kikamilifu mpango utakaowasilishwa na Kampuni ya Tembo Minerals Corporation Limited inayotarajia kuwekeza katika mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nickel katika Jimbo la Ngara na kuusimamia kwa kushirikiana na Mamlaka zingine za Serikali kuhakikisha kuwa unatekelezwa na unaleta manufaa kwa wananchi wa Ngara na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mbali na suala hili la local content, wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi watanufaika kama ambavyo makampuni mengine yote yanafanya kupitia malipo ya ushuru wa Huduma kwa maana ya Service Levy lakini pia na miradi itakayotekelezwa kupitia mpango wa Corporate Social Responsibility kwa maana ya CSR.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Madini itaandaa mpango mahsusi wa uendeshaji wa semina elekezi kwa wananchi wa Halmashauri ya Ngara na halmashauri yenyewe na maeneo jirani ili kuwawezesha kubaini fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na bidhaa na huduma mbalimbali ambazo wataweza kuzitoa katika mradi huo ili waweze kujiongezea kipato. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -
Je, ni kwa kiasi gani Serikali inafahamu madhara yatokanayo na madini ya zebaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma (Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali inatambua madhara makubwa ya kiafya kwa binadamu, mimea na mazingira yanayosababishwa na matumizi ya kemikali ya zebaki na hasa katika shughuli za uchenjuaji wa madini. Na miongoni mwa madhara ya kemikali hiyo kwa binadamu, ni kuathiri mifumo ya fahamu, uzazi, upumuaji na kusababisha magonjwa mbalimbali kama vile ya figo, moyo na saratani. Aidha, kemikali hiyo pia, huathiri viumbe hai vya majini na nchi kavu pindi zebaki inapotiririka na kuingia kwenye vyanzo vya maji ambavyo hutumiwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, na njia zinazopelekea kemikali ya zebaki kuingia mwilini ni kushika, kuvuta hewa na kula vyakula vyenye viambata vya kemikali hiyo. Pamoja na athari hizo kiafya, matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu yameonesha uwezo mdogo wa kutoa dhahabu ambao ni chini ya asilimia 30, hali ambayo imekuwa ikipelekea wachimbaji wadogo kushindwa kuzalisha kiwango cha kutosha na hivyo kupata faida kidogo.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu athari za kemikali hiyo na kutoa njia salama za utumiaji, ikiwa ni pamoja na usakafiaji wa mialo na utumiaji wa retorts kiswahili chake ni (vigida) wakati wa uchomaji. Aidha, Serikali kupitia STAMICO itaendelea kutoa elimu ya matumizi ya njia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kupitia vituo vyetu vya mfano vilivyoko maeneo ya Lwamgasa, Katente pamoja na Itumbi. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-
Je, ni kwa nini Mgodi wa Mwadui Williamson Diamond Limited umesimamisha shughuli za uzalishaji wa almasi kwa muda mrefu na ni lini mgodi huo utaanza uzalishaji tena?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na Kampuni ya Williamson Diamond Limited ulisimamisha shughuli za uzalishaji mwezi Aprili, 2020 na hii ni kutokana na kushindwa kumudu gharama za uzalishaji kufuatia anguko la bei ya madini ya almasi katika masoko ya dunia. Anguko la bei ya almasi katika soko la dunia lilisababishwa na athari za ugonjwa wa COVID-19 mwishoni mwa mwaka 2019. Athari ya kuanguka kwa bei hii ya almasi kulisababisha bei ya wastani ya almasi katika mauzo ya mgodi huo kwa mwezi Machi, 2020 kuanguka hadi kufikia Dola za Kimarekani 131.13 kwa karati, bei ambayo kimsingi haikidhi gharama za uzalishaji wa mgodi huo. Kwa mujibu wa makadirio ya mgodi huo wastani wa bei unapaswa kuwa angalau Dola za Kimarekani 208 kwa karati ili mgodi uweze kukidhi gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi huo utaanza tena uzalishaji baada ya maombi yao ya overdraft funds kukubalika na benki za hapa nchini. Hii ni kwa ajili ya kugharamia shughuli zao za uzalishaji angalau kwa kipindi cha miezi mitatu hadi kufikia awamu nyingine ya mauzo ya almasi. Hali ya bei ya almasi kwenye soko la dunia kwa sasa inatarajiwa kuwa bora zaidi ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2020.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:-
Je, Serikali ina teknolojia gani mbadala ambayo itaepusha kutumia magogo kama matimba kwenye mashimo ya migodi hasa maeneo ya Nyamongo, Tarime, Buhemba na Butiama?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wachimbaji wengi wadogo nchini na katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa dhahabu yakiwemo maeneo ya Nyamongo, Tarime, Buhemba na Butiama wamekuwa wakitumia magogo na kwa lugha yetu ya kichimbaji yanaitwa matimba na yanatumiwa kama mihimili ulalo pamoja na wima kwenye mashimo ya migodi ili kuweka support. Pamoja na teknolojia hiyo kuonekana kuwa ya gharama nafuu, imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira licha ya kuwa si salama na si ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia mbadala inayotumika kwa sasa ni ujenzi wa mashimo ya migodi kwa kutumia zege pamoja na nondo. Teknolojia hii ni salama na haina athari kubwa za kimazingira ukilinganisha na ile inayotumia magogo. Miongoni mwa sababu zinazopelekea wachimbaji wadogo kutotumia teknolojia hii ni ufinyu wa mitaji, lakini pia, kutokuwa na maeneo ya kudumu ya uchimbaji na baadhi yao kutokuwa na leseni za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwarasimisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni za madini ili waweze kutambulika kisheria na kwa jinsi hiyo kuwawezesha kuaminika katika taasisi mbalimbali za fedha. Aidha, Serikali kupitia STAMICO inaendelea kutoa elimu kwao kuhusu uchimbaji wa kitaalam na wenye tija unaozingatia masuala ya afya, usalama na utunzaji mazingira.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nipende kulieleza Bunge lako tukufu kuwa, Mikoa ya kusini mwa Tanzania ikiwemo Lindi na Mtwara imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya madini ya kinywe ambayo kitaalam inaitwa graphite ambayo ni madini ya kimkakati yanayohitajika sana duniani kwa sasa kutokana na matumizi yake kama malighafi za viwandani.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uwepo wa hazina ya madini hayo, yapo makampuni mengi yanayomiliki leseni za utafutaji na uchimbaji madini ya kinywe katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Lindi na Mtwara. Hadi sasa kwa nchi nzima kuna jumla ya leseni 68 za utafutaji, leseni 24 za uchimbaji wa kati na leseni moja ya uchimbaji mkubwa wa madini ya kinywe.
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Chiwata ambayo ipo Jimbo la Ndanda, Wilayani Masasi kuna leseni mbili za uchimbaji wa kati zilizotolewa kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited na leseni hizo zilitolewa mwaka 2018 baada ya kuwa kampuni hiyo imekamilisha shughuli za utafiti. Na kinachosubiriwa ni Kampuni hiyo kuanza uchimbaji na hatimaye uchakataji wa madini ya kinywe katika leseni hizo.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuona kuwa makampuni yanayomiliki leseni za utafutaji madini yanakamilisha shughuli za utafiti na kuomba leseni za uchimbaji mkubwa na wa kati. Kuwepo kwa leseni za uchimbaji wa madini katika maeneo hayo kutasababisha kuanzishwa kwa miradi ya uchimbaji ambayo italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Sekta ya Madini.
Mheshimiwa Spika, aidha, uanzishwaji wa miradi hiyo utaiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi, kutoa fursa za ajira kwa Watanzania hasa wanaoishi katika maeneo yanayozunguka miradi, uhaulishaji wa teknolojia, fedha za kigeni, lakini pia na manufaa mengine kwa jamii kupitia local content pamoja na CSR.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa shughuli za utafiti wa madini ya kinywe katika Kata ya Chiwata ambayo ipo Jimbo la Ndanda, Wilayani Masasi, mpango wa Serikali ni kutoa leseni ambapo hadi sasa leseni mbili za uchimbaji wa kati zimekwishatolewa kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupewa leseni, ni wajibu wa kampuni iliyopewa leseni sasa kuendeleza mradi huo kwa kuanza uchimbaji.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itasimamia ulipaji fidia kwa Wachimbaji Wadogo wa Kata ya Tumuli?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kukusu usimamizi wa Serikali juu ya fidia kwa wachimbaji wadogo wa Kata ya Tumuli, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, jitihada za pamoja baina ya Wizara na ufuatiliaji wa karibu sana wa Mheshimiwa Mbunge, mnamo tarehe 9 Agosti, 2021, malipo ya fidia ya shilingi 90,000,000.00 yalilipwa kwa wachimbaji wote 90 wa Kata ya Tumuli na malipo haya yalifanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ili kupisha uwekezaji wa Kampuni ya PUBO Mining Limited. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro uliopo katika eneo lenye madini ya Jasi kati ya Wananchi wa Kata ya Bendera Mkoani Kilimanjaro na Wananchi wa Kata ya Mkomazi Mkoani Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, imetoa leseni za uchimbaji mdogo katika maeneo hayo ya Kata ya Bendera iliyopo Mkoani Kilimanjaro na Kata ya Mkomazi iliyopo Mkoani Tanga.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo hayo ya kata hizo mbili, hivi tunavyoongea, hakuna mgogoro wowote unaohusiana na leseni za uchimbaji mdogo wa madini ya Jasi na wachimbaji wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawaruhusu wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Sakale, Kata ya Mbomele, Wilayani Muheza kuanza uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyothibitishwa kupatikana katika kijiji hicho?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uchimbaji mdogo katika eneo la Sakale zilikuwepo kati ya mwaka 2004 na mwaka 2016. Baada ya ziara za viongozi wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Muheza, Wizara ya Madini pamoja na NEMC na pia Mheshimiwa Mbunge mwenyewe iligundulika kuwa uchimbaji huo unafanyika katika chanzo cha Mto Zigi ambacho ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Muheza na Jiji la Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya wataalam wa mazingira iliyofanyika mwaka 2018 Oktoba, ilionyesha kuwa athari za kimazingira ni kubwa endapo uchimbaji utaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo na kwa kuhifadhi chanzo cha maji katika bonde la Mto Zigi, uchimbaji mdogo wa dhahabu katika Kijiji cha Sakale, Kata ya Mbomele, Wilayani Muheza hauruhusiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.