Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya (17 total)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nashukuru vile vile kwa majibu ya Serikali ambayo yanaleta matumaini sasa kwa matumizi ya chuma na matumizi ya niobium na kuwepo kwa kiwanda cha FerroNiobium hapa hapa kwetu nchini. Swali la kwanza, je, sasa kwa vile haya madini inaonesha kuwa ni madini ya viwandani ambayo yatachanganywa pamoja na chuma na ikiwezekena pamoja na aluminium, ni lini sasa Serikali itahakikisha kuwa uzalishaji wa chuma ikiwemo machimbo ya Liganga na Mchuchuma yataanza mara moja ili yaweze kutengenezwa FerroNiobium hapa hapa nchini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa sababu haya madini yanatengeneza FerroNiobium, je, viwanda vya FerroNiobium vinaangukia kwenye Sheria za Uwekezaji za EPZ? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba madini ya Niobium yatachanganywa pamoja na madini ya chuma ili kutengeneza muunganiko huu wa FerroNiobium na ni kweli kwamba Serikali kwa sasa iko katika mazungumzo rasmi na mwekezaji anayewekeza katika Mradi wa Liganga ili hatimaye tuweze kuanza mradi huo kwa sababu umechelewa sana. Kwa hiyo napenda kuamini kwamba maongezi haya yatakapokuwa yamekamilika baina ya mwekezaji wa Liganga na suala likiwa hasa katika mikataba, basi mtanzuko huo utakapokuwa umeondoka tunapenda kuamini kwamba itakuwa ni fursa ya kuendeleza mradi wa Niobium ambayo itachanganywa na chuma chetu cha Liganga.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba madini mengine yana matumizi katika viwanda na pia ndiyo iliyokuwa ni sticking point katika mazungumzo yetu na mwekezaji. Sasa ukiangalia madini ya Niobium katika periodic table ni transition metals, kwa hiyo tunapaswa tuyatambue kwamba ni madini ya metali na ukiyabadilisha yakaonekana kwamba kwa vile yana matumizi katika viwanda tozo inayotozwa ya royalty madini ya viwanda ni asilimia tatu, madini ya metali ni asilimia sita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa napo tulikuwa na mkinzano na mwekezaji kwamba matumizi ya baadaye yasitusababishe tukaanza kuonesha kwamba hayako katika group la metali, kwa sababu hata dhahabu nayo pamoja na kwamba ni metali inaweza ikapata matumizi katika viwanda. Kwa hiyo tukaona kwamba hebu tuendelee kuuangalia upande wa kwamba madini ya niobium ni madini ya metali, royalty yake ibakie kuwa asilimia sita hata kama baada ya hapo itakuja kuchanganywa na kuwa FerroNiobium. Kwa hiyo hayo ni maongezi ambayo tumeongea na mwekezaji na tunaamini kwamba tutafikia muafaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Madini. Nina maswali mawili ya nyongeza. Wewe mwenyewe unatambua kwamba Sekta ya Madini ina mchango mkubwa sana kwenye kukuza ajira kipato na Pato la Taifa. Swali la kwanza, je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na utafiti wa kina ili tuweze kuibua taarifa za kijiolojia zitakayoisaidia Serikali kuwekeza kwenye mambo ya madini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari Naibu Waziri amesema kuna Taarifa za awali kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Kata ya Makuru, katika Kijiji cha Londoni ambako tayari wachimbaji wa madini wadogo wadogo wanachimba. Sasa, je Serikali imejipanga vipi kuwawezesha wananchi katika maeneo ambayo kuna taarifa za awali ili waweze kujikita kwenye uchimbaji wa madini, tukuze ajira na kipato cha nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utafiti wa kina ndilo jawabu la hatimate kuwezesha uchimbaji kufanyika. Sasa mojawapo ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ambayo yanaonesha tumaini na huko mbele ni pamoja na kuziwezesha Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Madini kwa rasilimali ili ziweze kufanya majukumu yake ipasavyo. Ni katika mtindo huo huo kwamba Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Madini - GST imepokea vifaa rasilimali kama wiki mbili zilizopita tulipata magari sita kwa ajili ya kuwawezesha kufanya ugani.
Mheshimiwa Spika, pia STAMICO wamewezeshwa na wao wenyewe kwa pato lao la ndani wamepata mitambo mitatu ya drilling. Sasa hizo ni hatua za kuimarisha Taasisi ili hatimaye ziweze kufanya kazi ya utafiti wa kina na hatimaye kuwasaidia wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu swali lake la pili linauliza ni lini watawezeshwa; ni katika mtindo huo wa kwamba tutakapokuwa tumeendelea zaidi kuimarisha taasisi zetu kwa uwezo wa kifedha kama ambavyo Serikali imeanza kufanya tunapenda kuamini kwamba tunaelekea mahali ambapo Taasisi ya Jiolojia inaweza ikashirikiana na STAMICO na hatimaye wakawa wanafanya utafiti wa kina mahali fulani na kwa utafiti huo sasa wakapewa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa tija. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inafanya utafiti kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo kwa maana ya PMI za wachimbaji wadogo wadogo ili ziweze kuwasaidia waachane na uchimbaji wa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, suala la pili hii Taasisi ya Jiolojia ina ofisi zake hapa Dodoma. Sasa je, kwa mikoa ya nyanda za juu Kusini, ina mkakati gani sasa wa kufungua ofisi kule kwa Mkoa wa Mbeya ili nasi tuweze kupata hii ofisi ili iweze kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Njelu Kasaka Masache, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu utafiti kwa wachimbaji wadogo, taasisi ambayo inapaswa kufanya utafiti ni taasisi yetu ya GST, lakini wao wanaweza kufanya utafiti kwa njia zile za kawaida za awali kwa maana ya jiolojia, jiofizikia na jiokemia. Ili utafiti uweze kuwa wa kufana, unahitajika kidogo uchimbaji (drilling). Sasa taasisi iliyo na vifaa vya drilling ni Shirika letu la Madini la STAMICO.
Mheshimiwa Spika, hii ni habari njema kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wengine wote kwamba wiki iliyopita taasisi yetu ya GST pamoja na STAMICO waliingia makubaliano ya ushirika ili waweze kufanya kazi Pamoja. Kwa maana aliyepewa jukumu la kutafiti, lakini hana vifaa vya drilling na mwingine aliyepewa kulea wachimbaji ana vifaa, basi washirikiane ili kwa pamoja waweze kuwa wa msaada.
Mheshimiwa Spika, sisi tunaamini kama Wizara kwamba ushirika wao huo ambao waliuingia wiki iliyopita, unakuja kuwa msaada mkubwa kwa sababu taasisi mbili chini ya Wizara zimeungana ili mmoja aweze kutafiti akiwa anatumia njia za kawaida, asaidiwe na yule ambaye ana vifaa vinavyoweza ku-drill, lakini itakuwa ni kwa gharama angalau iliyopunguzwa, siyo kama ile kwa wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kwamba ni habari njema, wachimbaji wadogo wajue kwamba tutakapofanya drilling haitakuwa free, badala yake itakuwa kwa gharama iliyopunguzwa tukilinganisha na wale wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; ni kweli kwamba GST Makao yake Makuu yapo Dodoma, lakini maelekezo ya Wizara ni kwamba kazi zake hizi zifanywe pia mikoani. Habari njema ni kwamba mwaka unaokwisha huu tulifungua ofisi Geita na lengo ni kwamba tuendelee kufungua katika kanda ili kurahisisha hasa zile kazi za maabara kwa kutumia ofisi zetu za Tume ya Madini zilizoko mikoani. Kwa hiyo, kwa kuanzia tutazitumi zile na maelekezo yetu ni kwamba shughuli zote zifikishwe kwa ofisi za RMO halafu ziletwe Dodoma na kisha waweze kuhudumiwa kwa jinsi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kadri tutakavyokuwa tunapanua shughuli na kupata watumishi wengi zaidi, tunatamani kwamba tufungue matawi kila kanda katika nchi ya Tanzania ili kurahisisha utendaji kazi wa GST.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Leo ningekuwa CAG kwa majibu haya ningetoa hati hafifu. Haiwezekani leo tunazungumza mambo ya 2013 wakati aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Mizengo Pinda mwaka tarehe 8 Januari, 2015 alisema kwamba sasa wataanza utaratibu wa kupeleka mgodi huu TANESCO na kupeleka kwa STAMICO, lakini kumekuwa na ahadi hizi nyingi zikiendelea. Wananchi wa Wilaya ya Kyela, Wilaya ya Rungwe na Ileje wanachotaka ni kujua tarehe mahsusi ambayo suala hili linaenda kutekelezeka, la kuanza mgodi hiyo ni. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na matamko mengi ya malipo haya. Tarehe 29 Novemba, 2018 walisema STAMICO sasa imesha-save hela ya Serikali, lakini tarehe 12 Septemba aliyekuwa Naibu Waziri Mheshimiwa Nyongo alisema TRA wanawatafuta hawa TAN Power ambao walisema…
SPIKA: Sasa swali!
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ndiyo naomba nipate tarehe ya kulipwa ili na mimi nikienda Jimboni nikawaambie wananchi kwamba Serikali sasa inalipa pesa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba jambo hili limekuwa ni la muda mrefu kama ambavyo tarehe ya kukabidhiwa mgodi kwenda Serikalini imekuwa ya mwaka 2013, lakini pia tujue kwamba uwekezaji katika mgodi ni uwekezaji unaohitaji fedha. Katika kipindi hiki ni kweli kwamba pia Shirika letu la STAMICO limekuwa likipitia maboresho makubwa ya kulipa uwezo wa kuendelea kufanya shughuli zake. Kwa hiyo, ahadi hizi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu, tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa jinsi ambavyo shirika limeboreshwa na kwa jinsi ambavyo Serikali imejitahidi kuwa inalipa mapunjo hasa ya muda mrefu, hatimaye tumewaelekeza Shirika letu la STAMICO pamoja na TANESCO kwamba hata sisi hatuko tayari kuendelea kuchukua fedheha ya kuambiwa tuna hati chafu, badala yake wafanye jitihada zinazowezekana ili waweze kupata mtaji na hatimaye mgodi wa Kyela uweze kufunguliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mustakabali huo, naendelea kuwaagiza STAMICO pamoja na TANESCO kwamba, wakatafute fedha na ndivyo tulivyoongea kwamba sasa ifikie mahali watafute fedha, kama ni kutenga bajeti, kama ni kwa ushirika na partners wafanye hivyo ili hatimaye jambo hili liweze kufikia mwisho. Nakushukuru sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali langu la nyongeza. Tunafahamu kabisa mradi wa STAMICO ni mradi ambao una maslahi kwa wananchi wa Kyela, Rungwe na Ileje. Ileje iko Mkoa wa Songwe. Ningependa kuona mradi huu unafanya kazi mapema sana.
Swali langu liko hapa, majengo yaliyojengwa eneo lile ni majengo mazuri ambayo ni kwa ajili ya ofisi na makazi ya watumishi. Makazi yale, siku hadi siku yameendelea kuharibika. Sasa natamani kujua, je, ni nini dhamira ya Serikali katika kuendeleza haya majengo yasiendelee kuharibika na kufanyika magofu huku wakati tukiendelea kusubiri huo mradi kufanya kazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge, kuhusu ukarabati wa majengo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema STAMICO imeanza ukarabati wa mgodi wa chini kama sehemu ya maandalizi na ili tuweze kuanza mgodi ni pamoja na maandalizi ya nyumba za staff. Kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mbunge tu kwamba jambo hili pia la ukarabati wa nyumba kama maandalizi ya mahali ambapo staff watakaoingia katika mgodi pia litakwenda kutekelezwa na tutawaagiza STAMICO kwamba wafanye mambo haya kwa pamoja ili pia tusiendelee kupata hasara ya nyumba ambazo hatimaye tunaweza tukahitaji kujenga nyumba mpya kumbe tungeweza kuzihifadhi hizi kwa ajili ya mkakati wa baadaye.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa eneo hili la Kabanga Nickel kuna leseni nyingi zimechukuliwa hivi karibuni kuzunguka eneo hili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba leseni hizi zilizochukuliwa hazitazuia uwekezaji wa msingi wa Tembo Nickel?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa vile kuna tathmini ilifanyika hapo awali kwa ajili ya kutoa fidia kwa wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huu na kwa vile tathmini hii ambayo ilishafanyika, ilifanyika kipindi kirefu na hivyo imeshapoteza uhalali; je, Serikali ina mpango gani wa kurudia kufanya tathmini ili wananchi wanaounguka Mgodi huu wa Kabanga ambao kwa sasa unaitwa Tembo Nickel waweze kupata fidia? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uwepo wa leseni zinazozunguka mradi tarajiwa wa uchimbaji wa Tembo Nickel, ni kwamba mtu anapokuwa amepewa leseni ana eneo ambalo lipo katika coordinates na kwa maana hiyo anachimba katika eneo lake na uwepo wa leseni nyingine zozote zinazozunguka eneo la mradi hauna uhusiano wa kuzuia uchimbaji wa mtu aliye na leseni yake. Ni sawa na upangaji tu wa nyumba mtu ana kiwanja chake utaingia nyumbani kwako na mimi nitaingia nyumbani kwangu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishe Mbunge kwamba kuwepo kwa leseni nyingine zozote zilizotolewa siku za karibuni hazitazuia kamwe uchimbaji unao tarajiwa wa mradi wa Nickel.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusu tathmini; ni kweli kwamba tathmini ilishafanyika siku za nyuma na ikipita miezi sita mara nyingi tathmini hiyo kisheria inaonekana kwamba haifai na hivyo inabidi kurudiwa. Katika miradi yote ya uchimbaji mkubwa hakuna mradi ulioanza bila kufanya tathmini na wananchi kulipwa malipo stahiki. Siku zote tunawaelekeza watu hawa wanaofanya miradi mikubwa ya uchimbaji waweze kuwa na social license, kwamba waweze kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.
Kwa hiyo tutawaelekeza Tembo Mineral Corporation kwamba warudie kufanya tathmini na walipe fidia ili hatimaye mradi uweze kuanza. (Makofi) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa Madini ya Nickel unaotarajia kuanza katika eneo la Kabanga.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninalo ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, Serikali inayafahamu kwa kuyataja kabisa madhara yanayotokana na kemikali ya zebaki lakini pia kwa kuwa, kutumia njia hii kuchenjulia dhahabu tunapata asilimia kidogo tu kama ambazo ametaja asilimia 30, ni kwanini sasa Serikali isitumie cyanide kuchenjulia madini hayo ya zebaki na kuachana na kemikali hatari ya zebaki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, kibali cha ku-import kemikali ya zebaki nchini kinatolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali. Wataalam kutoka Wizarani wanatuambia kwamba Mkemia Mkuu wa Serikali hakupokea maombi ya ku-import zebaki nchini. Cha ajabu ni kwamba, kemikali hiyo ipo ya kutosha tu huko mtaani, sasa ni nini kauli ya Serikali juu ya njia hizi za panya zinazoingiza kemikali hii kiholela? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, cyanide pamoja na baadhi ya acids ndio njia sahihi ambayo inafaa kwa ajili ya uchenjuaji dhahabu kwa sasa na ndio teknolojia ambayo aaah! Kama Mheshimiwa Mchafu atakumbuka kwamba, ndio teknolojia mpya ambayo imetumika na ndio imeleta hasa manufaa kwa wachimbaji wadogo. Sema, kwa kutumia cyanide pamoja na vat leaching inakuwa inahitaji kidogo mtaji uwe mkubwa ili mchimbaji mdogo aweze kuitumia. Sasa kitendo cha kuhitaji mtaji mkubwa kidogo ndicho kinachofanya wengine bado wanaendelea kutumia mercury.
Mheshimiwa Spika, lakini ni kweli kwamba, wengi wameshaanza kuhama na ndio msisitizo wa Wizara tunawasisitiza watoke kule kwasababu ya madhara ambayo yanaonekana. Nikweli kwamba, kwa kutumia vat leaching ambayo inatumia cyanide ni kwamba, hata recovery inakuwa ni kubwa na kwa hiyo tumuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama Wizara tutaendelea kufanya jitihada za kutoa elimu. Kwanza, wachimbaji wadogo wajue madhara makubwa yanayotokana na kutumia mercury, lakini pia ikiwezekana hata kama ni kujiunga kwa vikundi waende katika teknolojia ambayo inafanya recovery kubwa lakini pia haina madhara makubwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kweli kwamba mercury inapatikana kwa wachimbaji wadogo wakiitumia na kwasababu, kibali kilipaswa kutoka kwa Mkemia Mkuu kama ambavyo anatoa kuhusu kemikali zingine zozote zile. Lakini Mheshimiwa Mbunge anathibitisha kwamba sio kweli kwamba yeye ametoa vibali. Tulichukue kama Serikali kwasababu tunatamani kulinda mazingira yetu, tunatamani kuwalinda wachimbaji wetu ili tuingie katika mnyororo na ikiwezekana badala ya kutoa elimu kwenye matumizi, basi twende pia kuangalia hata source ya mahali ambapo zebaki inaingilia. Nadhani kwa jinsi hiyo tutaweza kuwasaidia maana yake ni kwamba tuanze udhibiti tangu kwenye source kuliko kule kwenye matumizi yenyewe kwa kujali afya na mazingira yetu. Ahsante (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa majibu ya Serikali yaliyotolewa na Naibu Waziri. Kwanza nipongeze kwa jitihada hizi ambazo zinaendelea, lakini bado lipo tatizo kubwa la hizi benki ambazo Mgodi wa Mwadui umekwenda kwa ajili ya kuomba mkopo huu ilimradi uanze uzalishaji kwa mara nyingine. Jambo kubwa linalohitajika hapa ni hii corporate guarantee ambayo inatakiwa itolewe na Petra ambaye ndiye kimsingi mwekezaji wa Mgodi huo wa Mwadui, lakini jambo ambalo nadhani ni zuri zaidi kwa Serikali ni kuhakikisha inazungumza ama inakaa kwa karibu na Petra, ilimradi suala hili la corporate guarantee liweze kutolewa na Petra na badaye utaratibu wa kutolewa fedha na ili mgodi uweze kuzalisha ufanyike haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, liko tatizo kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Serikali yenyewe, lakini pia na suala zima la Service Levy pamoja na CSR ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Kishapu. Ni lini sasa Serikali itakwenda kusimamia na kushirikiana na hawa ma-banker ilimradi benki hizi ziweze kutoa fedha na kuweza kuzalisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa swali la pili nenda moja kwa moja kwenye swali.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wako watumishi zaidi ya 1,200 pale katika Mgodi wa Mwadui na changamoto kubwa ya hawa watumishi ni mishahara yao kusimama kwa muda mrefu. Sasa ipo sababu ya Serikali kuona umuhimu wa mgodi huu kuhakikisha unaanza uzalishaji, ili adha na matatizo makubwa ya watumishi hawa waliopo katika Mgodi wa Mwadui waondokane na adha hii kubwa. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mbunge pia kwa kutambua kwamba, Wizara inafanya kila linalowezekana kuona kwamba, mgodi huu unarejea katika hali ya uzalishaji. Kwa swali lake la kwanza, lakini pia ni kweli kwamba, natambua Wizara itafanya kila linalowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza uzalishaji wa almasi Tanzania tunaongea habari ya Mgodi wa WDL ndio kiini kikubwa cha uzalishaji wetu wa almasi. Pia, tunatambua adha ambayo watumishi wanapata kwa kushindwa kulipwa mishahara, lakini pia tunatambua kwamba, kama uzalishaji hautafanyika kwa muda mrefu maana yake ni kwamba, hata shimo lile tunapochimba litaanza ku-cave in na kwa hiyo, gharama ya kuja kuanzisha mgodi mara nyingine itakuwa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Madini itafanya kila linalowezekana, iwe ni kuongea na watoa huduma, iwe ni kuendelea kufanya ushawishi wake kwa ajili ya benki za hapa nchini na hata kuongea na Petra, ili ikiwezekana basi turejee katika uzalishaji. Mara tutakapoanza uzalishaji maana yake ni kwamba, matatizo yote aliyoyaainisha Mbunge ya adha ya watumishi kutolipwa pamoja na service levy vyote vitakuwa vinapatiwa suluhisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara itafanya kila njia inayowezekana; yaweza kuwa ni ushawishi kwa benki zetu, hilo moja, au kukaa na watoa huduma ili kwamba, wakubali kufanya hata kwa kukopwa ili baadaye tuzalishe halafu tuuze. Njia zozote ambazo zinaweza zikarejesha uzalishaji katika Mgodi wa WDL tutazi-pursue ili kwamba, tuweze kurejesha hali ya uzalishaji katika Mgodi wetu wa Almasi Tanzania. Ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali machache ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imesema kwenye majibu yake ya msingi kuwa teknolojia mbadala itakayotumika sasa ni ujenzi wa zege kwa kutumia nondo. Je, ni lini teknolojia hii itawafikia wachimbaji wale wadogo wa Nyamongo, Butiama, Tarime na Buhemba ili waweze kufanya uchimbaji wenye tija kwao na kwa Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali imekiri kuwa kinachopelekea kutumia miti, mitimba na magogo kwenye mashimo ni ufinyu wa mitaji waliyonayo wale wachimbaji. Je, ni lini Serikali itawawezesha kwa kuwapa mitaji wachimbaji hao ili waweze kukidhi mahitaji hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niweze kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linazungumza juu ya lini teknolojia hii itafikishwa kwa wachimbaji wadogo. Nimpe taarifa tu, Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mojawapo ya Migodi ya Wachimbaji Wadogo ya Kalende katika eneo la Tarime tayari mgodi mmojawapo wa Mara Mine umekwishaanza kutumia teknolojia hii kuashiria kwamba kumbe teknolojia imefika. Kwa sababu inahitaji kusambazwa kwa wengi nitumie nafasi hii, kumuagiza Afisa Madini Mkaazi wa Mkoa wa Mara, Ofisi yetu ya Musoma, aanzishe mafunzo kwa wachimbaji wote wa maeneo hayo ili waweze kuipokea teknolojia hii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu uwezeshaji. Itakumbukwa hapa kwamba, mwaka jana 2020 Tume ya Madini ilianza kutoa semina kwa mabenki yetu nchini ili kujenga awareness ya kwamba, uchimbaji madini ni biashara inayolipa kama biashara nyingine. Tulipokuwa tukisoma bajeti yetu hapa, tulithibitisha jinsi ambavyo mabenki yamepokea kwamba, biashara ya madini inawezekana na ni kweli kwamba tayari mabenki yameanza kuwezesha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuendelea kutoa elimu hii kwa mabenki ili kwamba, watambue maeneo ambayo yanapata tija katika uchimbaji na kwa jinsi hiyo waweze kuelekeza fedha katika kuwezesha wachimbaji wadogo. Ahsante sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na kutokuanza kwa mradi huu imesababisha kukosekana kwa shughuli za CSR kama ambavyo nilisema wakati uliopita. Kwa hiyo, Mji wa Chiwata na Jimbo la Mtama kwa sababu kuna sehemu inagusa mradi huu, Jimbo la Ruangwa pamoja na Jimbo la Newala DC imesababisha kutokuwepo kwa ajira zaidi ya 1,500 za moja kwa moja na zingine za kwenye mgodi na kukosekana kwa mapato ya Serikali pamoja na Halmashauri hizo nilizozitaja kiwango cha dola milioni 62. Sasa swali langu…
SPIKA: Eehe swali!
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ndiyo iliyosababisha tufike hapa, hawaoni kwamba wanafanya hujuma kwenye uchumi wa maeneo haya niliyoyataja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na Sheria ya Madini iliyobadilishwa mwaka 2018 ndiyo hasa chanzo cha mgogoro huu na kampuni zinazotaka kuwekeza, Serikali sasa haioni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii ili wawekezaji hawa waweze kuja na mitaji yao badala ya kulazimishwa kukopa kwenye benki za ndani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama kuna maeneo ambayo yamefaidika na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ni pamoja na CSR na local content. Yawezekana kweli katika maeneo ambayo miradi haijaanza Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa hawajaona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ila Wabunge walioko katika Mkoa wa Geita katika mikoa ambayo kuna migodi mikubwa tayari watakubaliana na Serikali kwamba ndipo mahali ambapo Serikali imeweza kubainisha sheria pamoja na kanuni za CSR na kuweza kufanya bora zaidi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara mradi utakapokuwa umeanza Serikali itasimamia sheria zake pamoja na kanuni za local content na CSR ili kuona kwamba wananchi wa maeneo husika wanaweza kupata faida.
Mheshimiwa Spika, swali la pili linahusu mabadiliko ya sheria. Mabadiliko haya yalipita katika Bunge lako Tukufu na kwa mahali ambapo sheria hizi zimetekelezwa vizuri tumeona kwamba kuna tija.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aone kwamba wawekezaji wengine wameshindwa kupata mitaji na wawekezaji wake hawa ni watu wa Australia na Australia ni mahali ambapo kulikuwa kuna total lockdown ya COVID kwa hiyo kupata mitaji mahali hapo imekuwa ni shida. Hata hivyo, tunaona kwamba wengine wanaona kwamba Tanzania bado ni mahali pazuri pa kuwekeza na Serikali kwa kweli milango ya Wizara iko wazi kuendelea kujadiliana ili tuone kwamba wawekezaji wanakuja, wanachimba na kama ilivyo sera ya Serikali wao na sisi tuweze kupata. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Serikali ikumbukwe kwamba maeneo haya yalichukuliwa karibu miaka sita iliyopita kwa upande wa Jimbo la Mtama, ikafanyika tathmini wananchi hawakulipwa fidia kwa hiyo maisha yao yamesimama kwa miaka sita. Huu mchakato umeendelea unakwenda unarudi na wananchi hawajui wafanye nini. Serikali iko tayari kutoa fidia pamoja na ile ambayo ilifanyika lakini fidia hii ya miaka sita ambapo maisha ya wananchi hawa yamesimama hawaendelei na maisha yao ya kawaida wakisubiri fidia kwa miaka sita? Serikali iko tayari sasa kutafuta namna ya kuwafidia au vinginevyo tufute wananchi waendelee na maisha yao.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tukubali kwamba mambo haya yalifanyika wakati wa transition ambapo Sheria ya Madini ilikuwa inabadilika. Ni kweli kwamba jambo hili lilionekana kama linaleta hofu na wawekezaji walirudi nyuma. Pia sheria inatoa muda wa kwamba kama fidia imefanyika na ikapita miezi sita basi fidia hiyo inaweza kurudiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu sasa mazingira yanaboreshwa tutawaomba tena tufanye fidia upya ili wananchi hatimaye waweze kulipwa. Nadhani hilo liko katika utaratibu wa sheria na hivyo sisi tutahimiza sheria ifanye sehemu yake ili fidia iweze kurudiwa na hatimaye wananchi waweze kulipwa na mradi uweze kuanza. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mbali tu na tatizo la kemikali ya zebaki, lakini wachimbaji wadogo wamekuwa na tatizo kubwa sana la mitaji wakiwemo wachimbaji la Nyamongo Mkoa wa Mara. Ni lini sasa Serikali watawawezesha wachimbaji wadogo wa Nyamongo hasa vijana na akinamama ili waweze kuchimba vizuri dhahabu zao.
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kuhusiana na kemikali zinazodhuru wananchi, si tu kwa wachimbaji wadogo mbali na kwa wananchi wanaozunguka migodi. Sasa wananchi wa Nyamongo wameathirika sana na mara nyingi Serikali imesema italipa fidia, ni lini sasa itawafidia wananchi ambao wameathirika na kemikali zinazotoka migodini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu mitaji Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya lile linalowezekana kuhusisha benki zetu za ndani ambazo zimehiari kutoa mitaji kwa ajili ya wachimbaji wetu wadogo na kwa taarifa mwezi wa Sita Mheshimiwa Waziri wa Madini alizindua NMB Mining Club ambapo wateja wachimbaji wadogo wanaweza wakaenda pale na wakakopeshwa.
Mheshimiwa Spika, pia benki zetu zingine za ndani zimehiari tayari na tayari tumeona kwamba wanashiriki katika shughuli za kuwakopesha wachimbaji wadogo. Ambacho tumewaasa wachimbaji wadogo ni kwamba kabla ya kwenda benki awe na leseni halali, inayotambulika na Tume ya Madini, lakini pia awe basi na takwimu za kazi anazozifanya ionekane kwamba unaonekana ukizalisha, ukiuza unapata faida benki wamehiari kutoa fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo limefanyiwa kazi kwa namna hiyo na wachimbaji wadogo wameanza kupata matunda. Pia kwa taarifa benki zetu za ndani zimekwenda mbali zaidi hadi kutoa fedha kwa ajili ya miradi mikubwa. Kwa hiyo tunadhani kwamba, hiyo ni hatua na suala la mitaji limeendelea kushughulikiwa halimradi wachimbaji wetu wadogo waweze kutoa ushirikiano kwa jinsi hiyo.
Mheshimiwa Spika, suala la mazingira yanayozunguka migodi. Ni kweli kwamba inapokuja kwenye mgodi ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja, Serikali imeendelea kufanya hatua, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna tena maji yanayotiririshwa katika maeneo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, limeendelea kushughulikiwa na timu yetu ya Wizara ya Madini pamoja na NEMC pamoja na watu wa Wizara ya Maji, wamekuwa wakishirikiana katika kufanya ukaguzi kuhakikisha kwamba hakuna uchafu tena unaoendelea kutiririshwa kutoka katika migodi.
Mheshimiwa Spika, suala la fidia pia limeendelea kufanyiwa kazi na yule Mthaminishaji Mkuu wa Serikali. Ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ambayo yametolewa na Serikali. Pengine niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ningemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii akaambatana nami na kutembelea wananchi wa Jimbo la Serengeti kuona ni namna gani tatizo hili ni kubwa na mikakati iliyowekwa, je inaweza kweli kutekelezeka na kumaliza tatizo? Kwa sababu hivi ninavyozungumza kila mara tunapata ripoti za tembo, simba kuvamia wananchi. Pamoja na majibu haya yanayotolewa lakini bado hatuoni tatizo hili likiisha. Kwa hiyo niombe, kwa maana ya kwamba kwa majibu haya Waziri afike na yeye aona kama kweli haya yanaweza yakatosheleza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ukitoka katika eneo la mpaka wa hifadhi katika vijiji vingi unaingia kijijini moja kwa moja, hili ni tatizo kubwa sana. Serikali iliwahi kutoa mpango kwamba kutaongezwa buffer zone ambayo ni nusu kilomita kuingia ndani ya hifadhi, lakini mpaka leo bado hawajatekeleza. Sasa je, ni lini Serikali itatekeleza uamuzi huu wa kuongeza buffer zone kuingia ndani ya hifadhi ambayo ni moja ya jambo linaloweza likasaidia sana kupunguza mwingiliano huu wa wanyama na makazi ya watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wake wako tayari kutembelea eneo hilo la Serengeti kama Mheshimiwa Mbunge alivyotaka. Na kwa sababu wako tayari kutembelea eneo hilo. Hata yale majibu yanayohusu buffer zone ambayo iliahidiwa napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yatatolewa majibu wakati wa ziara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali ya Mama Samia kupitia Wizara hii, baada ya kilio cha muda mrefu hatimaye wananchi wangu wa Tumuli walilipwa fedha hizo. Pamoja na shukurani hizo naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi wetu wadogo wa Tumuli, ambao walihamishwa pale katika lile eneo na kwenda kuanzisha maeneo mengine hasa kwa kupelekewa umeme na barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili Serikali ina mpango gani pia kwa kuwasaidia hao wachimbaji wadogo vifaa vya uchimbaji kwa mkopo nafuu haswa hao wa Tumuli, Langida na Ibaga ambao ni wachimbaji wadogo wanaokuza uchumi katika nchi yetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji hawa wadogo wa Kata ya Tumuli wanapaswa kuingia katika vikundi, ili watakapokuwa wamekuwa katika vikundi halafu waweze kujisajili na wakishakuwa wamesajiliwa wakatambulika rasmi kama kikundi kilichosajiliwa, basi baada ya hapo taratibu za kuwawekea mazingira bora zinaweza zikaanza ikiwa ni pamoja na kuwapa leseni.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba panapokuwa na uchimbaji wenye tija katika maeneo ya wachimbaji wadogo, tunawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Nishati. Kwamba, kama machimbo hayo yana tija basi waweze pia kupelekewa nishati ya umeme kama ambavyo tumefanya katika machimbo baadhi ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, na hili suala la vifaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo tumekuwa siku za karibuni tukiwasiliana na mabenki yetu ya ndani, kuona kwamba yanaweza yakaanza kukopesha vifaa kuliko hata fedha zenyewe na katika suala hili pia tumefikia mahali pazuri na hivyo nimpe tu tija Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaenda tena kuwaona wachimbaji wake kama wameji-organize katika vikundi tutawasajili na baada ya hapo, tutawaunganisha na mabenki yetu ili kwamba waweze kusaidiwa kama ambavyo wengine pia wanasaidiwa hapa nchini. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, ripoti ya NEMC ya Oktoba, 2018 ambayo Mheshimiwa Waziri anaitaja, ilielezea wazi kwamba kinachokatazwa ni uchimbaji mdogo na inashauriwa ufanyike uchimbaji aidha wa kiwango cha kati ama mkubwa, kwa sababu hizo za kimazingira ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja. Sasa je, Serikali haioni kwamba kwa vile wananchi wa Sakale, Kata ya Mbomole, Wilaya ya Muheza, hawana uwezo wa kufanya uchimbaji wa kiwango cha kati ama mkubwa inafaa sasa iwasaidie kupata mwekezaji mwenye vigezo vinavyotajwa na ripoti hiyo ili uchimbaji ule uweze kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyikiti, la pili; ni ombi kwa Wizara, kwamba tuna maeneo kadhaa mengine katika Wilaya ya Muheza katika Kata ya Pande Darajani katika Kata ya Magila na katika Kata ya Magoroto hasa Kijiji cha Mwembeni ambayo yanaonyesha dalili za kuwa na madini. Je, Serikali inaweza kututumia watalaam wake ili wakafanye tathmini na kuona kama kuna uwezekano wa kuchimba katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge Hamis Mohamed Mwinjuma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kutoa majibu ya Wizara, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mwelewa, kwa sababu tulipofanya ziara hii na kukubaliana kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa za mazingira, mara nyingi watu wasingeweza kuamini kwamba mbona kuna mali, lakini tathmini ya kimazingira ilionyesha kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa ambazo yawezekana zisiwe na faida hata kama uchimbaji unafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kuelewa kwa Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana hata wananchi wote wakaelewa kwamba huenda kama madini haya lazima yachimbwe basi iwe ni kwa uchimbaji wa kati ambao teknolojia yake inakuwa ni ya kuchukua udongo mahali pale na kuchenjulia sehemu nyingine ili kuendelea kulinda vyanzo vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, Wizara itatoa ushirikiano wote ambao wananchi wanauhitaji kwa sababu pale tulikwishatoa leseni za uchimbaji mdogo. Kwa hiyo tutawaomba tu wafuate utaratibu, wao watapata muwekezaji halafu watakuja Wizarani, watafanya amalgamation ya uchimbaji mdogo tutazi-upgrade kuwa za uchimbaji wa kati na tutawapa miongozo yote inayostahili ili waweze kufanya uchimbaji ambao bado utazingatia kutoathiri chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili; GST ndiyo taasisi yetu ambayo inakwenda kufanya utafiti wa awali na huwa tunapenda kuhimiza utafiti wa awali kwa sababu hautakuwa ule ambao unaleta na wingi wa mashapo kwa kule chini. Sasa hilo linawezekana, tutawaagiza waje. Mheshimiwa Mbunge hata baada ya hapa anaweza akaja pale ofisini kwetu tukaongea na watu wa GST na wakapanga namna ya kwenda nawe ili awaelekeze katika maeneo ambayo anataka waweze kufanya utafiti ili huo wa awali uweze kuonyesha kama uchimbaji unaweza kuendelea katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nchi yetu hii imezungukwa sana na wachimbaji wadogo wadogo hasa kwenye maeneo mengi yenye uchimbaji wa madini. Je, ni lini sasa Serikali itarudisha utaratibu uliokuwepo mwanzo wa kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo hawa ili kuweza kuwasaidia waweze kupata vifaa na baadaye waweze kufanya uchimbaji wao uwe mzuri zaidi, tuweze kuwapata walipa kodi wazuri zaidi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Masache, Mbunge wa Chunya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati wa nyuma Serikali ilitoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini nipende kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba utaratibu ule wa ruzuku ama haukueleweka vizuri watu walipokuwa wanachukua na haukuwa na tija yoyote katika kufanikisha malengo yaliyokuwa yamepangwa. Kwa msingi huo Wizara inaendelea kutathimini kuona kama kuna sababu ya kufanya hivyo tena iwe ni wachimbaji wetu wameelewa ili makusudi ya kutoa ruzuku hizo yaweze kufikiwa. Wakati Wizara inafikiria namna ya kufanya hivyo tena tumeona kwamba njia nyingine ambayo inaweza ikawa ni nyepesi ni ya kuyaona mabenki yetu ya ndani, ambapo Mheshimiwa Mbunge ana taarifa kwamba baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo katika Jimbo lake la Chunya wamekwishapokea fedha kutoka kwenye mabenki yetu ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huo ni utaratibu ambao tunadhani kwamba in the interim kabla ya kufikiria kwamba tunaweza tukawa na wakati mwingine wa ruzuku, basi twende na njia hii ambayo nayo imeanza kuonyesha dalili za kufanikiwa katika kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo. Nakushukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naiuliza Serikali, Mgodi wa Kiwira kwa muda mrefu sana umesimama, je, ni lini Serikali itaamua kuleta wawekezaji au Serikali kuweka nguvu ili kusudi Mgodi huu wa Kiwira uweze kutoa ajira, lakini pia kuipatia pato Serikali yetu ya Tanzania. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kiwira ni kweli tunatamani kwamba ndani ya Serikali uweze kuanza na wakati wa nyuma tumekuwa tunatamani kwamba taasisi zetu mbili TANESCO pamoja na STAMICO waweze kukaa pamoja na kukubaliana, kwa sababu mgodi ule pamoja na kwamba unatoa tu makaa ya mawe, lakini pia kinatarajia kuwa chanjo kingine cha kutoa nishati na kwa jinsi hiyo inahusisha taasisi zetu mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema tu kwamba mwezi Julai, TANESCO pamoja na STAMICO waliwekeana makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja na hivi ninavyoongea Shirika letu la STAMICO lipo katika harakati za ku-mobilize mwekezaji ili mgodi ule uweze kuanza. Nakushukuru sana.