Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Edward Olelekaita Kisau (12 total)

MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa ajira za upendeleo kwa vijana na fursa nyingine za kibiashara kwa wananchi wa Jimbo la Kiteto kupitia mradi mkubwa wa kimkakati wa Bomba la Mafuta (Hoima – Tanga) ambalo linapita katika Wilaya ya Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Kabaale/Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Mkoani Tanga nchini Tanzania. Kwa upande wa Tanzania, bomba litapita katika Mikoa 8 na Wilaya 24 ambapo Wilaya ya Kiteto itapitiwa na bomba kwa urefu wa kilomita 117.1 pamoja na ujenzi wa kambi ya kuhifadhi mabomba katika kijiji cha Ndaleta na kambi ya wafanyakazi katika Kijiji cha Njoro.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Bomba hilo kupita katika Wilaya ya Kiteto, wananchi wa Kiteto watanufaika na ujenzi wa mradi huu kwa kufanya biashara, ajira na fursa nyingine za kiuchumi na kijamii. Utekelezaji wa kazi za mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2021 na kukamilika mwezi Julai, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutoa hamasa ili wananchi wanufaike na shughuli za ujenzi na uendeshaji wa mradi.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango wa kupunguza bei na kuongeza muda wa mkopo wa Matrekta waliokopeshwa Wakulima wa Jimbo la Kiteto na Shirika la NDC?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Matrekta wa URSUS unatokana na mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Poland, uliosainiwa tarehe 28 Septemba, 2015. Serikali ya Jamhuri ya Poland iliiteua kampuni ya URSUS na Serikali ya Tanzania iliiteua SUMA JKT kama watekelezaji na baadaye mradi huu ukahamishiwa Shirika la la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkataba huo, Serikali ya Poland ilitoa mkopo nafuu wa dola za Kimarekani milioni 110 kwa riba nafuu ya asilimia 0.3 kwa mwaka, ukiwa na kipindi cha mpito cha miaka mitano na utarudishwa katika kipindi cha miaka 30. Lengo la mkopo huo ilikuwa ni kugharamia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kupanga bei ya matrekta, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ilifanya uchambuzi wa gharama na kupanga bei kulingana na uchambuzi huo. Bei hizi zilipangwa kwa kuzingatia gharama za uagizaji, kutolea bandarini, kuunganisha na gharama nyingine za usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipanga bei nafuu ambapo wakulima wengi wanaweza kununua na kukopa matrekta hayo kutokana na mchango wake katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, biashara na kuzalisha malighafi za viwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kurahisisha uuzaji wa matrekta hayo, mkopo uliotolewa haukuwa na riba. Lengo kuu la Serikali siyo kupata faida, bali kuwawezesha wakulima kujikwamua kutoka kwenye matumizi ya jembe la mkono na kuongeza tija zaidi. Hivyo bei ya matrekta hayo kwa sasa inarejesha gharama tu za matrekta hayo pekee bila kupata faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kurahisisha ulipaji wa mkopo kwa wakulima, kuanzia mwaka 2020, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) iliongeza muda wa kulipa mikopo kwa wakopaji ambao muda wa mikataba yao umeisha. Utaratibu unaofanyika ni kuwapa mikataba ya nyongeza wakopaji wote wa matrekta ya URSUS nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba ya nyongeza inahusisha bakaa ya deni na haitozwi riba. Utaratibu wa kupewa mikataba ya nyongeza unahusisha mkulima na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kukaa pamoja na kufanya majadiliano ya namna mkulima atakavyolipa deni lililobaki. Zoezi hili limeshaanza kwa wakulima wa Kiteto katika kipindi hiki na linaendelea ili kuwafikia wale wote ambao muda wa mikataba yao umepita.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa Wananchi wa Jimbo la Kiteto wananufaika na Miradi ya Maji safi na salama ili waweze kufikia azma ya asilimia 85 na asilimia 95 Vijijini na Mijini ifikapo Mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa maeneo kame nchini ambayo chanzo kikuu cha maji ni maji chini ya ardhi. Huduma ya maji ya uhakika katika Wilaya Kiteto kwa upande wa vijijini inapatikana vijiji 35 kati ya 63, sawa na asilimia 53 kwa mjini ni asilimia 44.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vijijini, Serikali imepanga kutekeleza miradi mitano au zaidi kila mwaka ili huduma ya maji ifike katika vijiji vyote 63 na kufikia lengo la asilimia 85 au zaidi. Kwa upande wa Mji wa Kibaya kwa mwaka 2021/2022, Serikali imepanga kutekeleza mradi ambao utahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ambapo huduma ya maji itakayopatikana itakidhi mahitaji ya wananchi wa Kibaya kwa asilimia 95 au zaidi ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha huduma ya maji katika maeneo kame, Serikali itatekeleza mpango wa ujenzi wa mabwawa madogo na makubwa na ukubwa wa kati kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule za Sekondari za Lesoit, Dosidosi, Ndedo na Dongo kuwa Kidato cha Tano na Sita kutokana na uhitaji mkubwa wa Shule za Kidato cha Tano na Sita Kiteto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa shule za kidato cha tano na sita katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto. Shule tatu ni za bweni na moja ni ya kutwa ambazo zilianzishwa makusudi kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu wafugaji wanaohamahama ili wasome bila kukatisha masomo. Shule hizo zinashindwa kupandishwa hadhi kutokana na upungufu wa miundombinu ya mabweni, mabwalo na madarasa ya kutosha kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi cha nne na kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto akishirikiana na wananachi wajenge mabweni, madarasa na mabwalo kwenye shule hizo ili yatosheleze mahitaji ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kuongeza mengine ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kidato cha tano na sita ili tuweze kuzipandisha hadhi shule hizo.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, ni lini ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni za Urais ya ujenzi wa mabwawa mawili ya maji katika Wilaya ya Kiteto itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Wilaya ya Kiteto kwa sasa ni asilimia
52.58. Katika kuboresha huduma ya majisafi na salama katika Wilaya ya Kiteto, Serikali katika mwaka fedha 2021/2022, inatekeleza miradi katika Vijiji 21 vya Nchinila, Engusero, Ngipa, Nasetani, Ngarenaro, Mafichoni, Kibaya Kati, Kanisani Bomani, Magubike na Msakasaka. Vijiji vingine ni Jangwani, Magungu, Kaloleni, Majengo Mapya, Msikitini, Vumilia, Esuguta na Kiperesa.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi hiyo unahusisha ujenzi wa matangi 11 yenye jumla ya ujazo wa lita 1,325,000, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 99.49 na ujenzi wa vituo 69 vya kuchotea maji. Utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 10 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa muda mrefu, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022, imefanya mapitio ya usanifu wa Bwawa la Maji la Dongo na usanifu wa ukarabati wa Mabwawa ya Dosidosi na Kijungu na taratibu za kupata wakandarasi zitakamilika kabla ya mwezi Juni, 2022. Ujenzi wa Bwawa la Dongo pamoja na ukarabati wa Mabwawa ya Dosidosi na Kijungu unatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Arusha – Simanjiro – Kiteto hadi Kongwa kilometa 430 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi (CCM) 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mnamo tarehe 27 Juni, 2022 ilitangaza zabuni kwa ajili ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa Makampuni ya Ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Arusha – Simanjiro – Kiteto – Njiapanda ya Kongwa yenye urefu wa kilometa 453.42 kwa utaratibu wa EPC + Jumla ya Makampuni kumi na moja (11) yalikidhi vigezo na tarehe 22 Novemba, Zabuni hizi zitafunguliwa.
MHE ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kusajili na kuboresha miundombinu ya Shule Shikizi zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Jimbo la Kiteto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vituo shikizi ni vituo vilivyojengwa kwenye maeneo ambayo hayana shule au shule ziko umbali mrefu kutoka kwenye maeneo wanayoishi wananchi. Vituo hivi kabla ya kusajiliwa kuwa shule kamili hufanyiwa ukaguzi na ufuatiliaji na Wathibiti Ubora wa Shule kwa kushirikiana na Maafisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kama hakuna mapungufu taarifa ya ukaguzi pamoja na barua ya kuomba usajili hutumwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili Shule husika ipate usajili.

Mheshimiwa Spika, ili vituo shikizi viweze kusajiliwa na kuwa shule halmashauri pamoja na wananchi wa vijiji husika wayafanyie kazi maelekezo ya wathibiti ubora wa shule ili shule hizo ziweze kupata usajili.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaajiri walimu wanaojitolea katika Jimbo la Kiteto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ina jumla ya walimu 752 wa shule za msingi na walimu wa kujitolea 86. Aidha, kwa shule za sekondari kuna jumla ya walimu 298 na walimu wa kujitolea 34.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa Walimu wa kujitolea katika shule za msingi na sekondari na kwa kuwa Serikali huajiri kulingana na upatikanaji wa fedha. Hivyo nafasi za ajira zikitangazwa, tunawashauri Walimu hawa wanaojitolea waombe nafasi hizo ili wale wanaokidhi vigezo waweze kuajiriwa kwa kupewa kipaumbele, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ajira ya Utumishi wa Umma kuongeza kigezo cha kujitolea ili kutoa fursa kwa wanaojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura Na. 298, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 na Miongozo inayohusu masuala mbalimbali likiwemo suala la ajira.

Mheshimiwa Spika, endapo itabainika bayana kigezo cha kujitolea kitatakiwa kuingizwa katika marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Serikali italeta Marekebisho ya Muswada wa Sheria Bungeni kwako. Kwa sasa Serikali imeandaa mwongozo unaoweka mazingira wezeshi kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia uzoefu utakaomuwezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali zitakapotangazwa.

Mheshimiwa Spika, mwongozo huu unalenga kuziba ombwe lililopo kutokana na kutokuwa na utaratibu mmoja ndani ya Taasisi za Umma kuhusu kujitolea.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Mnara wa TBC – Kiteto?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kujenga mnara wa redio Wilayani Kiteto katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2024, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga fedha kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Kijiji cha Magungu – Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisua, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Magungu Kiteto ulianza mwaka 2015 kwa kutumia michango na nguvu za wananchi. Ujenzi huo ulisimama ukiwa kwenye hatua ya lenta kutokana na kukosa fedha. Wakati ujenzi unasimama kiasi cha shilingi 20,000,000 zilikuwa zimetumika. Tathmini ya kumaliza ili kuunga mkono nguvu za wananchi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 33,985,000 kinahitajika. Fedha hizo zitatengwa kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la maji Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Jimbo ka Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kiteto ni wastani wa 64%. Katika kuboresha huduma ya maji Wilayani Kiteto na kufikia malengo ya 85%. Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi 11 ya Kibaya, Bwagamoyo, Majengo Mapya-Kaloleni, Sunya, Ndirgish, Mdunku, Wezamtima-Bwawani, Matui, Engongungare, Magungu-Nhati na Ostet. Vilevile utekelezaji wa miradi tisa unaendelea katika vijijini 14 vya Nchinila – Engusero, Njiapanda, Chang’ombe-Njoro, Orkine, Ilera-Esekii, Laiseri – Dongo, Kimana, Ngipa, Nasetani, Lembapuri, Esuguta, Kiperesa, Ndotoi na Enguserosidani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2025 na kunufaisha wananchi wapatao 69,825 waishio kwenye vijiji hivyo na kufanya jumla ya vijiji 60 kufikiwa na huduma ya majina salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuwezesha vijiji vilivyobaki kufikiwa na huduma ya maji safi na salama.