Supplementary Questions from Hon. Edward Olelekaita Kisau (42 total)
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Nakushukuru, kwa kuwa swali lililoulizwa linafanana kabisa na matatizo na changamoto tunayopata kama Wilaya ya Kiteto, hususan Hospitali ya Wilaya, tuna upungufu wa mashine ya x-ray, jenereta ni mbovu, majengo, gari la kubeba wagonjwa, vitanda na mashine ya usingizi. Ni lini sasa Serikali itapeleka vifaa hivi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Kiteto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya utoaji wa huduma za afya yakiwemo majengo, vifaatiba, x-ray, ultra sound na vifaa tiba vingine ni vifaa ambavyo vimepewa kipaumbele katika vituo vyetu vya huduma ili kuweza kufikisha huduma bora kwa wananchi na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza jinsi ambavyo Serikali imetenga fedha kiasi cha takribani bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zetu 67 za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vyetu vyote ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Kiteto.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali kwa vijana waliomaliza mafunzo ya JKT na wameshiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nchi yetu lakini sasa wamerudi nyumbani bila ajira?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ni mara kadhaa amekuja tumezungumza juu ya hatma ya vijana na inaonyesha namna anavyowajali vijana wake. Kwa hiyo, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema nafasi hizi za mafunzo ya vijana wetu zina nia nzuri, kwanza ya kuwafanya vijana ambao tunawafundisha kuwaunda ili kuwa na umoja wa kitaifa. Hiyo haipingiki kwa sababu tunavyokuwa tunawafundisha kule hatuna siasa, hatuna maneno mengi, tunawaunda wakae vizuri. Pia tunawaunda kuwa viongozi, wanaweza kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi katika biashara na mambo mbalimbali ya ujasiriamali. Pia tunawafundisha kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na ubunifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa vijana ambao wamepata nafasi ya kupata mafunzo haya pamoja na kupata stadi za kazi, tunawaandaa hawa vijana kwenda kujitegemea. Pia upande wa Serikali ziko fursa kadhaa ambazo Waheshimiwa Wabunge tunazifahamu ni za kuwafanya vijana hawa waweze kuchangamkia fursa ambazo zipo kwa maana ya kupata mitaji na kadhalika. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tukiwaunganisha hawa vijana kwa skill ambazo wamezipata katika mafunzo yetu tutawafanya waweze kujitegemea na kutoa mchango mkubwa sana kwenye taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Wabunge pale ambapo vijana wetu hawana taarifa hizi za fursa ambazo Wabunge tunazifahamu, tutumie nafasi hiyo kuwaunganisha vijana hawa, wawe kwenye makundi au binafsi ili Serikali iweze kuwasaidia vijana hawa na lengo ambalo limewekwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu liweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumejipanga vizuri na Waheshimiwa Wabunge niwakaribishe pale ambapo labda wanaweza wasiwe na uelewa wa kutosha niko tayari kuwaweka vizuri ili tuweze kuwasaidia vijana wetu kadri tutakavyokuwa tumejipanga. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yenye furaha kidogo kwa wananchi wangu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna ajira nyingi sana zinasemwa kuwepo katika mradi huu, je, hawaoni kwamba wananchi wangu wa Kiteto hususan vijiji saba vile; Mwitikira, Ndorokoni, Dareta, Ovoponi, Kimana na Amei wakatengewa kabisa fursa za kibiashara na ajira za upendeleo kwa kuwa wao ndiyo wanabeba burden ya mradi huo kwa kilometa hizo 117?
Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili dogo, je, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa amesema Wizara itaendelea kuhamasisha wananchi wajitokeze kuchukua fursa hizi atakuwa tayari kuongozana na mimi tutembelee vijiji hivi saba ili tutumie wasaa huu kuendelea kuwaandaa wananchi wetu kwa fursa hizo, tena ikizingatiwa kwamba Mheshimiwa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu jana amekwenda kwenye kutiwa saini sasa kwa mkataba huu na kwamba karibu sasa mradi unaanza? Nakushukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nitoe shukrani kwa jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa ya jumla kwa wananchi wa Kiteto pamoja na maeneo mengine kwamba utekelezaji wa mradi huu unaanza mwezi huu Aprili, tulipanga tuanze mwezi Julai kama ambavyo tumeeleza kwenye jibu la msingi lakini tunaanza rasmi mwezi huu wa Aprili kwa muda wa miaka mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania ni kweli mimi nilishiriki nikiwa na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan utiaji saini utekelezaji wa mradi huu jana nchini Uganda. Mradi huu ni mkubwa utapita katika mikoa 8, wilaya 24, vijiji 127, vitongoji 502 vikiwemo vijiji na vitongoji vya Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi utatoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 10,000 katika hatua za awali na hadi ajira za Watanzania 15,000 katika shughuli za ujenzi na shughuli za kawaida. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaomba sana wananchi hasa katika maeneo ambapo mradi utapita wajitokeze kuchukua hizi fursa kwa sababu tumeziweka rasmi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spili, swali la pili la kufuatana naye, tumepanga kuanzia Kyaka nchini Tanzania kule Kagera hadi Tanga Chongoleani, tutaanza kufanya ziara wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa ili kuhamasisha Watanzania kuchukua fursa hiyo. Kwa hiyo, tutafika na katika eneo lake na kutembelea vijiji hivyo saba ambavyo Mheshimiwa amevitaja.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vyangu vya Ndaleta, Ngabolo, Olkoponi, Pori kwa Pori, Mbeli, Amei, Namelok wanasumbuliwa sana na tembo na hivi tunavyozungumza tembo wako mashambani. Nini kauli ya Serikali kwa wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa pole kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo, lakini Serikali kama ambavyo nilisema mwanzo kwamba tumeanza kutoa mafunzo baada ya kuona athari hii inaendelea kuongezeka. Mafunzo haya yatatolewa nchi nzima namna ya kukabiliana na hawa wanyama wakali. Pia tutatoa vifaa maalum kwa ajili ya kudhibiti hawa wanyama wakali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana pale ambapo inatokea watupe taarifa na vikosi kazi ambavyo tumevisambaza nchi nzima vitaendelea kufanya kazi kudhibiti hawa wanyama wakali.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niseme tu kwa majibu pia ya Serikali ambayo ni fifty fifty hivi, wakulima hawa wameanza kusumbuliwa sana na TAKUKURU. Wanakamatwa kila mahali na sijui kwa nini? Kwa sababu ni mkataba; sijui kosa la TAKUKURU linakujaje hapo! Niseme tu Mheshimiwa Rais wetu hapendi sana wakulima waonewe. Kwa kuwa, sasa Serikali imesema ilipata mkopo wa miaka 30, kwa nini wakulima hawa msiwape muda wa miaka 15 ili waweze kurejesha mikopo hii? Kwa sababu naamini ilikuwa ni nia njema sana, nami nimefanya vikao na watu wangu tarehe 10 Januari, 2021 na watu wa URSUS na kuna Wabunge wengi sana hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wizara hii, Waziri na Naibu Waziri ni wapya, kwa nini wasitengeze kikao cha pamoja na Wabunge na watu wote wenye matrekta ili tuanze kujadili namna bora ya kuwasaidia wakulima hawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa ufuatiliaji ambao anafanya ndugu yangu Mheshimiwa Olelekaita kuhusiana na wakulima wa Jimbo la Kiteto. Nachukua maoni yake mazuri, lakini kwanza kuhusu TAKUKURU kuwasumbua hawa wakulima waliokopa, naomba Serikali tuchukue nafasi hii kusema kuwa tutawasiliana kwanza na wenzetu kupitia NDC tuone ni nini kilikuwa kinatokea mpaka TAKUKURU wakaingizwa kwenye utaratibu wa kufuatilia mikopo hii ambayo iliingiwa na wakulima wale waliokopa matrekta na NDC?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ulipaji wa mikopo hii kwa kuongezewa muda, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nalo hili tutalijadili kwa sababu ni mikataba ambayo iliingiwa na wakulima na walitoa wao wenyewe nafasi ya kulipa kulingana na uwezo wao. Kwa sababu ni nia njema ya Serikali kuhakikisha wakulima wanawezeshwa ili tuweze kupata mazao na malighafi za viwandani, basi tutakaa pia kupitia ili tuweze kuona namna gani tunawawezesha walipe kwa unafuu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kikao cha pamoja, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutakuja, tutakaa na ninyi, tutajadiliana na viongozi wote na hasa wakulima ambao wanatakiwa kusaidiwa kwa namna yoyote ile ili waweze kufanya kazi zao kilimo kiwe na tija.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninashukuru sana kwa majibu mazuri sana ya Serikali; na nishukuru juzi tu wakati wa Mbio za Mwenge tulizindua miradi ya Wezamtima na kutembelea miradi mingine ya maji kule Nchinila. Pamoja na haya ninashukuru sana kwa majibu haya ambayo wananchi wangu wa Kibaya pale, na nniafurahi kusema watakuwa wamesikia majibu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini sasa Serikali itajenga Bwawa la Dongo ambalo lipo kwenye mpango wa Mwaka huu wa Fedha 2021/2022. Lakini wakati huo huo pale pale Dongo tuna Mlima Njoge unatiririsha maji; na kwa kuwa tanki ambalo limejengwa ni zamani sana, ni la mwaka 1965, na katika Vijiji vya Dongo na Chang’ombe wananchi wameongeza; ni nini kauli ya Serikali kuhusu kujenga tanki kubwa la maji; pengine la lita laki moja, laki mbili ili wananchi hawa waendelee kunufaika wakati wanasubiria bwawa hili la Dongo ambalo tunasuburia kwa hamu sana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kukushukuru kwa kukiri kazi kubwa ambayo imefanyika na hata Mwenge wetu wa uhuru umeweza kuzindua miradi ile. Lakini vilevile nipende kukujibu swali lako, kwamba ni lini bwawa la Dongo litafanyikwa kazi. Umeshajibu wewe mwenyewe kwamba mwaka ujao wa fedha tayari mpango mkakati umeuona uko pale hivyo tusubiri muda. Na kadri fedha itakavyokuja ndivyo kasi ya ujenzi wa lile bwawa itakuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusiana na hili bwawa lililojengwa miaka ya 1965 tunafahamu ongezeko la wananchi ni kubwa. Tayari tuna mikakati ya kuja kukarabati tanki hilo, lakini vile vile kuongeza matanki mengine kadri fedha tutakavyopata, na mwaka ujao wa fedha naamini tutakuja kufanya hizi zote. Lengo ni kuona wananchi wanapata maji safi na salama ya kutosheleza na wananchi wote wapate maji bombani.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa maelezo haya mazuri, lakini sasa wakati wananchi wanaendelea kusubiri hii kauli ya njema sana ya Mheshimiwa Rais. Nini kauli ya Serikali kwa maafisa hawa wanyamapori ambao wanaendelea kunyanyasa wananchi na kukamata mifugo yao kwa kipindi hiki?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, narudia tena kwamba Mheshimiwa Rais amesema kazi iendelee. Anatambua uamuzi uliotolewa na Awamu ya Tano na yeye amesisitiza kwamba wananchi wote waliopo kwenye maeneo yao wasiondolewe katika vile vijiji 920, uamuzi huo upo vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ametupa kazi ya ziada kwenda kufanya uhakiki wa hali halisi iliopo. Kwa hiyo, ningeomba na wananchi nao wasitumie vibaya uamuzi huu wa Serikali wakafiri kwamba basi wasiondolewe maana yake ni kujipanua wanavyotaka. Tafadhali wakae kama walivyokuwa ili kazi hii ya uhakiki ije iwatendee haki kwa sababu hii pande mbili kuna upande huo wa wananchi, lakini upande wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuna wananchi wengine tulivyotoka na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kule Katavi, baada ya kutoa tamko lile pale watu waliingia kwenye Msitu wa Mbuga ya Katavi. Kwa hiyo, na wananchi nao wasubiri nia njema ya Rais wa Awamu ya Sita ni kutenda haki. Tufanye uhakiki kama alivyoagiza halafu uamuzi utatolewa.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, jambo hilo litatekelezwa, lakini wakati huo huo kazi iendelee maana yake uamuzi ule, ule uliotolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita amerudia maagizo yale yale kwamba nataka wananchi wote waliopo kwenye vile vijiji 920 wasiondolewe. Kwa hiyo, nadhani hakuna mtu wa Serikali anayewaondoa watu katika maeneo yale. (Makofi)
SPIKA: Kwa muda mrefu Wabunge walikuwa wakisubiri taarifa ile ya mawaziri nane, tunajua ni taarifa ya Serikali sijui kama imefikia kiwango cha Wabunge kuweza kujua angalau kilichomo au bado ni...Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana leo asubuhi uliunda kamati mbili twende tukawasilishe ile taarifa, lakini nimewaomba rasmi kwamba jambo hilo ndilo ambalo Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mwezi huu uliopita. Kwa hiyo, nikawaomba radhi kwamba kwa sasa hatuna jipya watusubiri kidogo kazi hii ya kwenda kufanya uhakiki wa kina wa leo kwa sababu maamuzi haya yametolewa miaka mitatu, lakini hali ya leo ni tofauti na yeye ni Rais wa Awamu wa Sita amemetutuma mwezi uliopita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimewaomba radhi kwamba kwa leo hatutatoa hiyo taarifa, lakini itakapokamilika huu uhakiki wa uandani ambao kwa vyovyote vile tukipita mikoani tutawakuta na Waheshimiwa Wabunge huko baada ya kukamilika hiyo kazi na Mheshimiwa Rais akitolea maamuzi tutakuja kuileta taarifa hiyo.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mengine mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa sasa halmashauri na wananchi kwa kweli wamewekeza nguvu kuboresha miundombinu ya mabweni, vyoo, madarasa, mabwalo katika shule hizi za Dosidosi, Dongo, Ndedo na Lesoit, nini commitment ya Serikali sasa kama kuwaongezea nguvu katika jitihada hizi za kuboresha miundombinu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda na mimi Kiteto kwa siku ambazo sio nyingi sana tutembelee shule hizi za Dongo, Lesoitd, Ndedo, Dosidosi na Sunya ili kuona mazingira yalivyo ili tuweze kushauriana? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Olelekaita Mbunge wa Jimbo la Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka tu commitment ya Serikali kutokana na jitihada kubwa iliyofanywa na wananchi wake katika Jimbo la Kiteto. Nikiri tu kwamba moja ya mpango wa Serikali katika Mwaka huu wa Fedha ni kuongeza upanuzi wa shule 100. Katika hizo shule 100 lengo letu ni ili ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, miongoni mwa shule tutakazozingatia ni pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha katika ule mpango wetu wa shule 100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili la kwenda Kiteto, nitakwenda. Nitaongozana na Mheshimiwa Mbunge ili tukajionee hayo maeneo husika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba niulize swali dogo tu la nyongeza. Kuna Mkandarasi anaitwa Giza mlituletea kwenye majimbo yetu, na mlimpa siku za kuja kwa Wabunge, mpaka leo tunamtafuta; nini kauli ya Serikali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli nimepata concerns za baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na Mkandarasi huyu Giza na kama alivyowahi kusema Mheshimiwa Mbunge mmojawapo kwamba jina la mkandarasi halivutii, lakini ni mmoja wa wakandarasi ambao walipata kazi katika Mradi wa REA II, round two katika Mikoa ya Manyara na Mara.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara. Nitoe taarifa kwamba, tumemtafuta na tumempa maelekezo mahususi, nikitoka hapa nitawaeleza Waheshimiwa Wabunge ni namna gani tumechukua hatua ili aweze kufanya kazi yake na kuimaliza, ili inapofika hiyo Desemba 2022 ambayo tumekubaliana naye, tusiwe nje ya muda huo.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na niseme kwa dhati kabisa kwamba nimefurahishwa sana na majibu ya Serikali na wananchi wangu wa Dosidosi, Kijungu na Dongo watakuwa wamesikia haya.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mradi ule wa milioni 400 wa Kaloleni uliotokana na fedha za UVIKO na kwa kweli niishukuru Wizara ya Maji na meneja wa RUWASA aliyeko pale ni mzuri sana, anafanya kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu dogo tu, je, ni lini Wizara ya Maji watakuwa tayari twende Kiteto, hususan pale Dongo, ili tukatembelee mradi mkubwa wa bwawa hili ambalo limewekwa kwenye mpango wa Serikali?Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimepokea pongezi zote na tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu anaendelea kutoa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kufika Kiteto, niko tayari, nitafika Kiteto na tutafanya kazi. Sisi tunasema na kutenda, tutafika Kiteto.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa tulishasema tumalize vituo vya afya kwenye tarafa ambazo hazina: -
Je, ni lini Serikali itajenga Vituo kwa Tarafa za Makame, Dosudosi na Kibaya ambazo bado hazina? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Wakili Olelekaita Mbunge wa Jimbo la Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Jimbo la Kiteto lina Tarafa ambazo bado hazina Vituo Vya Afya, na Mheshimiwa Mbunge amekuwa mara kwa mara akifuatilia hili. Nimhakikishie, kwamba mpango wa Serikali ni kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika tarafa ambazo hazina vituo vya afya, na tutakwenda pia kutoa kipaumbele katika Tarafa za Jimbo la Kiteto ahsante.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Spika, sana, na niseme wazi kabisa kwamba nashukuru sana majibu ya Serikali ni mazuri sana sana. Pamoja na hayo Mheshimiwa Waziri natarajia kwamba hiyo barabara mtaanza kujenga kutoka Kongwa, Kwenda Kiteto mpaka Arusha. Swali la nyongeza, ni lini hasa kwa mipango yenu, baada ya hii process ya kufungua tenda, ninyi mmepanga lini sasa ujenzi huu uanze, ni Novemba, Desemba, Januari? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Edward Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa kuipongeza Serikali kwa hatua ambazo inaendelea kuzichukua. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kwamba taratibu zimeshaanza, na kama makampuni haya mojawapo litakidhi vigezo, litapewa hiyo zabuni, kwa hiyo taratibu za manunuzi zitaanza ili kuanza ujenzi huo kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Naomba tu nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri; tulileta malalamiko kuhusu hii miji midogo ambayo ina sura ya vijiji, mkasema tathmini inafanyika na hiyo timu itakuja kwa Wabunge ili tufahamu kama mnafika maeneo yetu. Sasa ni lini hii timu yenu itafika kwa Wabunge hawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli, tuliahidi kwamba kuna timu itaenda kuwatembelea na kuzungumza na Wabunge ili kuweza kubaini yale maeneo ambayo tunataka kuyafanyia kazi. Timu hii imeanza kufanya kazi ya ndani, ni kama ku-plot maeneo ambayo inatakiwa iende kuyatembelea kwa sababu kuna mengine yanafahamika, hayahitaji kwenda kukaguliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii shughuli ya ndani ya utambuzi itakapokuwa imekamilika kwa taarifa iliyokuwepo, ndiyo sasa itaenda site na Waheshimiwa Wabunge wote wanaohusika wataiona hii timu kwa sababu maelekezo ya Wizara ndivyo yalivyo kwa ajili ya kushirikiana kuweza kutambua maeneo hayo kwa usahihi zaidi. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali dogo tu. Kijiji cha Magungu wamejenga jengo la Kituo cha Polisi tangu mwaka 2016, nini kauli ya Serikali katika kuwasadia kumaliza lile jengo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mhesimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Kijiji hicho cha Magungu, kwa kufanya jitihada na juhudi kujenga Kituo cha Polisi. Tutakachofanya ni kufuatilia kiwango kilichofikia hilo jingo, linahitaji kiasi gani ili liweze kukamilishwa na tuone uwezekano wa kuingiza kwenye mpango wa ujenzi kutegemea upatikanaji wa fedha. Kama tulivyoongea juzi wakati wa ziara yangu nitafikia kwenye kituo hicho ili kuweza kuona hatua iliyofikia.(Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninalo swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mpango huu wa blueprint ulitengeneza changamoto mbalimbali ambazo ziko kwenye Sheria mbalimbali na ucheleweshaji katika kuushughulikia imekuwa ni issue. Wizara ina mpango gani sasa kwamba makosa mapya hayajirudii kwenye sheria zinazotengezezwa mpya?
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli moja ya changamoto katika mambo yaliyokuwa kwenye andiko hili la blueprint ilikuwa ni Sheria na Kanuni zipatazo 88 ambazo zilikuwa na changamoto mbalimbali. Mpaka sasa zaidi ya Sheria na Kanuni 40 zimeshafanyiwa kazi ambayo ni takribani asilimia 45 ya utekelezaji ya mpango huu wa kuboresha mazingira ya wafanya biashara nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaendelea kupitia na kuhakikisha Sheria na Kanuni ambazo bado ni kinzani kwa ajili ya kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini tunaendelea kuzitatua na kupitia Bunge lako Tukufu ninaamini mengi tutaendelea kuyarekebisha kadri ya muda unavyokwenda, kwa sababu pia tunavyotatua baadhi ya changamoto kuna changamoto zingine mpya zinaibuka. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kutatua kadri ambavyo hali halisi itakavyokuwa inajitokeza.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kata ya Sunya katika Kituo cha Afya tulipata ajali mbaya sana mwezi Novemba na tulipoteza watumishi karibu sita, sasa kituo kinataka kufungwa. Je, ni nini commitment ya Serikali kuweza kutuletea watumishi hao kwa haraka sana ili kituo kisifungwe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ilitokea ajali na kupoteza watumishi wetu takribani sita katika Kituo cha Afya hiki cha Sunya. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, lakini shughuli za Serikali lazima ziendelee katika kituo kile cha afya na tulikubaliana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, kuhakikisha anafanya mgawanyo wa ndani wa watumishi waende kwenye kile kituo cha afya waanze kutoa huduma. Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kumkumbusha Katibu Tawala wa Mkoa haraka iwezekanavyo apeleke watumishi kwenye kituo hiki cha afya ili wananchi waendelee kupata huduma za afya, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kumekuwa na baadhi ya wakandarasi ambao wanaacha madeni kwa wananchi kwa kazi za kujitolea na kokoto: Nini kauli ya Serikali kwa wananchi hawa wanaoachwa na madeni na Mameneja wa TARURA kuzuia hili lisitokee siku nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa tukipata hiyo changamoto na tumekuwa tukielezwa na wananchi katika maeneo mbalimbali kwamba wakandarasi wamekuwa wakiacha hayo madeni katika maeneo husika. Moja ya utaratibu wetu sasa hivi, kabla ya kumaliza ule mkataba, hatutalipa fedha zote za mwisho mpaka pale ambapo watakuwa wamemaliza madeni ya watu katika maeneo husika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa majibu ya Serikali.
Swali la kwanza; kwa kuwa Kiteto ina upungufu wa walimu karibu 800 ukichanganya shule za msingi na sekondari. Kwa hivyo kama isingekuwa siyo hawa 120 hali ingelikuwa mbaya; je, ni lini ni lini Serikali italeta Sheria ya Ajira hapa tuweke kigezo cha kujitolea iwe ni sababu ya mtu kuajiriwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja Kiteto akutane na Walimu hawa wazalendo wanaojitolea wanaojitolea ili azungumze nao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edward Kisau Olelekaita, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Kiteto ina upungufu wa walimu, lakini niwapongeze Halmashauri ya Kiteto kwa kuweka bajeti angalau kidogo kwa ajili Walimu wanaojitolea. Nimhakikishie kwamba Serikali imeweka mpango na mwongozo kwa ajili ya kuwawezesha Walimu wanaojitolea kutambulika rasmi, lakini pia kupewa kipaumbele wakati fursa za ajira zinapojitokeza na kwa kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ametangaza jumla ya ajira 21,200 za Kada ya Elimu lakini pia na Kada ya Afya, niwatie shime hawa Walimu wanaojitolea Kiteto na maeneo mengine kuomba ajira hizo ili waweze kupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuhusiana na kukutana na Walimu hawa sisi tuko tayari baada ya shughuli hizi za Bunge, basi tuambatane na Mheshimiwa Mbunge, ili tuweze kuonana na Walimu hao na kuwatia moyo kufanya kazi nzuri, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri kuna tume mliunda ya kupitia vijiji vile vyenye sura ya miji hivi: Lini tume hii itamaliza kazi ili wananchi wajue wako wapi kwenye kuunganishiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa OleleKaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tume iliundwa na ilipita kwenye baadhi ya maeneo kukusanya maoni na tulielekeza ihakikishe inamuona kila Mbunge. Majibu yalipokuja Wizarani tulivyojaribu ku-crosscheck na Waheshimiwa Wabunge tuligundua kuna Wabunge kwa bahati mbaya hawakufikiwa na hawakuonwa na timu hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeiagiza irudie upya zoezi hili kwenye yale maeneo ambayo ilikuwa haikufika na katika miezi miwili inayokuja tunaamini itakuwa imemfikia kila Mbunge na kupata maoni yake kwenye maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa jitihada za kuhakikisha maeneo yenye uso wa mjini lakini ni vijijini yanapatiwa umeme kwa gharama ile nafuu. Kwa hiyo, majibu yatakapofikia mwisho tutaleta taarifa sahihi.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Wilaya ya Kiteto ni ya zamani kidogo na majengo yamechakaa. Kwa jibu la uhakika kabisa, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edward Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa Mahakama, Mahakama ya Wilaya ya Kiteto itajengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri, alipokuja Katibu Mkuu wa CCM, Kiteto alituahidi taa za barabarani pale mji wa Kibaha na tumeleta maombi. Ni lini Serikali itatuletea hizi fedha tuweke taa za barabarani pale mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema ilikuwa ni ahadi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ambae Serikali hii ndio inatekeleza Ilani yake ya uchaguzi, tutakaa na wenzetu wa TARURA ambao ni taasisi iko chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuona wamejipangaje katika kutekeleza uwekaji wa taa hizi kama ambavyo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyotaka.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nilitaka nimuulize tu Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa mtakuja Kiteto kusaini mkataba wa hii barabara ya Kongwa – Kiteto mpaka Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hii ni miongoni mwa barabra ambazo nimezitamka hapa kwamba zitasainiwa kabla ya mwezi wa sita. Barabara ambazo ziko katika EPC+ Financing, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi na nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa kila kazi inayotangazwa tunaambiwa tunataka uzoefu na hakuna mtu anatoka shuleni na uzoefu. Kwa hivyo, walimu wanaojitolea hicho ni kigezo kwamba kujitolea sasa imefika wakati hii sheria iwe ni kigezo namba mbili baada ya meritocracy.
Swali la pili, kwa kuwa Wizara nyingi sasa zimeshatengeneza miongozo ya kujitolea, nilikuwa nasoma moongozo wa Wizara ya Elimu wa kujitolea kwa Walimu wa June na Wizara ya Maendeleo ya Jamii wa 2021, kwa nini sasa ninyi ambao ni wa Utumishi, muendelee kupoteza muda badala ya kuleta mabadiliko ya sheria haraka sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba iko miongozo mbalimbali ambayo inaongoza juu ya jambo zima la kujitolea, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba maagizo yalikwishatolewa na Bunge lako juu ya Serikali kuanza utaratibu wa kuja na sheria na miongozo juu ya jambo la kujitolea kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba, kumekuwa na miongozo mbalimbali lakini hakuna utaratibu maalum unaolenga kuelekeza juu ya jambo zima la kujitolea.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba maagizo uliyoyatoa tunayafanyia kazi, na ndani ya Ofisi ya Rais – Utumishi, tumekwishaanza michakato hiyo na sasa hivi tuko katika document na kama nilivyoeleza kwamba document zitakapokuwa tayari tutazileta mbele ya Bunge lako Mheshimiwa Spika ili Wabunge waweze kutoa mawazo yao, baada ya hapo sasa tuweze kuleta ije kuwa sheria.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba Serikali inayachukua mawazo yote mazuri yaliyotolewa na Wabunge, pamoja na michango yao katika kipindi cha Bunge la Bajeti na kwamba tunayafanyia kazi na kuyaleta mbele ya Bunge lako ikiwa kama miongozo ya Serikali.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa mimi bado natafuta vituo vitatu vya tarafa, lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya vituo vya tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nakushukuru, naomba tu kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto kwamba, pamoja na yeye, bado kuna baadhi ya majimbo pia na wilaya zetu ambazo tarafa nzima haina kituo cha afya. Tunafanya mpango wa kuhakikisha kwamba tarafa zote ambazo zina idadi kubwa ya wananchi na kuwa na umbali mrefu kutoka kituo kingine zinapewa kipaumbele kwenye vituo vya afya vya kimkakati. Kwa hiyo nikuhakikishie kwamba tarafa ulizozitaja zitapewa kipaumbele kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kiteto ilikuwa na vijiji vingi sana, sasa kwa mujibu wa mikataba indication ni lini, walikubaliana watamaliza kwa kipindi gani? Kwa sababu kesho nina mkutano wa hadhara na haya maswali yatakuwa mengi sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Advocate Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye baadhi ya maswali ni kwamba utekelezaji wa miradi hii ya minara 758 kuna hatua kadhaa ambazo zinafanyika na mkataba wetu ukamilishaji wake utaanzia kwenye miezi tisa. Kuna maeneo ndani ya miezi tisa minara itakuwa imeshakamilika na kuna maeneo katika miezi 10, 11 mpaka mwisho wa mkataba wetu itakuwa ni miezi 20 tutakuwa tumehakikisha kwamba minara imeshasimama katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kikubwa sana ili kuhakikisha kwamba Serikali inaendelea ku-monitor utekelezaji, tumehakikisha kwamba tumewapatia utaratibu maalum, kila baada ya miezi mitatu wanatoa taarifa ya utekelezaji walipofikia na mpaka sasa watoa huduma wengi wameshatupatia utekelezaji wao, wengine wameshapata vibali, wengine wameshapata benki guarantee, kuna wengine bado hawajapata benki guarantee.
Kwa hiyo, watoa huduma mbalimbali wako katika hatua mbalimbali, lakini wako ndani ya muda ambao tumekubaliana. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Watanzania kwamba utekelezaji huu utaenda kama ambavyo umepangwa.
MHE EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa wakulima walihamasika sana kuhusu alizeti na bei imeteremka na wakati wanaangalia sheria ili wazuie mafuta yanayotoka nje, kwa nini Serikali isifanye commitment au kununua alizeti yote ambayo wakulima wamelima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumepata changamoto ya bei kuporomoka na ndiyo maana kwenye bajeti yetu Mheshimiwa Waziri alitamka kwenye kitabu chake cha bajeti uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (ADF) Agricultural Development Fund ambayo kazi yake nyingine ni kwa ajili ya price stabilization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema ni kwamba tumeshapata amri kutoka Wizara ya Fedha ya uanzishwaji wa Mfuko huu na Mfuko utaanza kufanya kazi, natumai katika changamoto ambazo zitajitokeza baadaye basi Serikali kupitia Mfuko huu inaweza kufanya kazi hiyo kwa ajili ya kuwa rescue wakulima. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini mtaboresha miundombinu kwa minada ya Kibaya, Dosidosi na Sunya?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu awali, kwa sasa tunatafuta fedha ili tuhakikishe kwamba hiyo minada ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tunaikarabati na kuitengeneza kwa viwango ambavyo vinavyotakiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge waondoe shaka wananchi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itatekeleza kama ilivyoahidi. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa kama wateja tumekuwa tunaripoti hao wanaotutapeli kwa makampuni ya simu, lakini hatupati mrejesho.
Nini kauli ya Serikali kwa Makampuni ya Simu ambayo hayatupi mrejesho wa namna gani wana-deal na matapeli hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii katika Bunge lako tukufu kuwaelekeza TCRA wakae na watoa huduma wote ili waone njia iliyosahihi zaidi ya kuhakikisha kwamba malalamiko yanayofikishwa basi Watanzania wanastahili kupata mrejesho wa malalamiko yao ili iwe rahisi kuweza kupima utekelezaji unakwenda kwa kipimo gani kulingana na malamiko yanayotumwa na mrejesho unaokuja. Hivyo, namwelekeza Mkurugenzi Mkuu na timu yake yote walifanyie kazi na sisi kama Serikali tutaendelea kufuatilia kwa karibu sana, ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri Mji mdogo wa Kibaya na Matui imekuwa ipo kwa muda mrefu sana, sasa imewaacha wale siyo wenyeviti siyo Wenyeviti wa Mitaa wame-hang tu kwa muda mrefu.
Je, ni lini Serikali italeta mpango ili suala hili likae vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali Serikali kwa sasa imeweka kipaumbele katika umaliziaji wa miundombinu na ujenzi wa miundombinu mingine katika maeneo mapya ya kiutawala ambayo yalianzishwa hivi karibuni na yale maeneo ambapo Halmashauri zilihamia kwenye maeneo hayo ya utawala. Pale ambapo zoezi hili litakamilika la ujenzi wa miundombinu hii tutaanza kuangalia namna gani ya kuanza kupandisha hadhi Miji hii, ikiwemo Kibaya na Matui kule Kiteto.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwaka jana tarehe 16 Juni, tulisaini Mikataba ya Barabara za EPC+F ya Kongwa – Kiteto – Arusha. Naomba kufahamu lini Mradi huu unaanza kwa sababu Wananchi wa Kiteto tunausubiri kwa hamu sana?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nilijibu kwa package yote ya miradi yote ya EPC+F, miradi saba. Kama nilivyosema wakati nachangia kwenye hoja ya Kamati ya Miundombinu, design ya barabara hizi ilifanywa na TANROADS mwaka 2017 miaka mingi imepita. Kwa hiyo Wakandarasi ambao wamepatikana wanafanya mapitio ya design ili kuweza ku-update usanifu wa kina, na baada ya hapo barabara hizi zitaanza kujengwa mara moja. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Olelekaita pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao mnasubiri hii Miradi ya EPC+F tuko tunajipanga usanifu, mapitio yakikamilika basi tutaanza ujenzi wake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri mafupi yenye time frame, kwa kweli wananchi wa Kiteto wamesikia na tangu uhuru hawakuwahi kusikia Redio Tanzania. Lakini pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto ni kubwa sana, nataka kujua; Je, mnara huu wa Redio mnaojenga uta-cover eneo kubwa kiasi gani? Swali la pili; mwaka wa fedha 2023/2024 kuna vijiji takriba 20 na zaidi mlikuwa mmepanga kwamba mtajenga minara ya simu kwenye Kata za Dosidosi, Laiseri, Loolera, Magungu, Namelock, Ndirgishi, Njoro, Olboloti, Partimbo na Songambele. Nataka mniambie lini hasa miradi hii itaanza ili wananchi wa kiteto wapate mitandao ya simu.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa mtambo huu utakapokamilika utaweza kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana katika Wilaya nzima ya Kiteto na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mwenyekiti tunamtambo mwingine upo pale Kilindi, ule mtambo utaweza kusaidiana vizuri kabisa na mtambo ambao tutaukamilisha pale Kiteto, na Wilaya nzima ya Kiteto haitokuwa na changamoto yoyote ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ametaja Kata za Dosidosi, Laiseri, Lengatei nafikiri majina kama hayo lakini katika kata zote 12 kata moja ndiyo inaenda kuhudumiwa na Halotel, kata saba zinaenda kuhudumiwa na Airtel, kata tatu zinaenda kuhudumiwa na Tigo na kata moja ambayo ni ya Songambele inaenda kuhudumiwa na Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu uko katika hatua nzuri kabisa kwa sababu nafikiri mmeshaanza kuona wanapita huko kwa ajili ya kutafuta maeneo kwa ajili ya kuingia mikataba ili ujenzi uanze rasmi. Nakuhakikishia Mheshimwa Mbunge tuendelee kushirikiana ili maendeleo kutokana na mawasiliano yaweze kupatikana. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri sana. Hata hivyo, kwa ajili ya kuweka record sawa ni Kituo cha Magungu, siyo Magugu, Magugu ni kwa Mheshimiwa Mwenyekiti pale. Vilevile, jina langu ni Kisau siyo Kisua, Kisua kwa Kichaga ni yule beberu mdogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baada ya kusema hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Ninawapongeza Wananchi wangu wa Kiteto ni waungwana sana, unajua wananchi kujenga Vituo vya Polisi siyo jambo dogo sana. Kwa kuwa Wananchi wa Kijungu nao wamejenga Kituo cha Polisi na imefikia lenta wametumia milioni 15 mpaka 20. Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa nini, msiweke hiyo bajeti ya 2024/2025 ili kumalizia kama mlivyofanya kwa wenzao wa Magungu hapo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa aliyekuwa IGP, 2014/2015 alitoa ahadi ya kujengwa Kituo cha Polisi Kijiji cha Chekanoa, na kwa kuwa Mji Mdogo wa Matui unahitaji kituo chenye hadhi ya polisi. Ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri utatembelea Kiteto ili tukague vituo hivi vya polisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninawapongeza wananchi wa Jimbo la Kiteto, kwa juhudi hizi wanazozifanya kwa ajili ya kuhakikisha uwepo wa usalama wa wananchi na mali zao kwa kujenga vituo hivi vya polisi. Ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge, kwa wito wako na nipo tayari baada ya Bunge hili kuunga nawe kutembelea eneo lako la Kiteto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kata hii ambayo pia wameanza, ni ahadi yetu kwamba wananchi walionesha juhudi za kuanza tutawaunga mkono kwa kutenga fedha za maendeleo na fedha nyingine kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo ili kukamilisha majengo hayo yaweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Kuhusu ahadi ya IGP aliyepita nitamkumbusha IGP aliyepo madamu ilikuwa ni ahadi ya Jeshi la Polisi, ili aweze kusaidiana na wananchi hawa wa Chekanao kujenga kituo hicho kilichoahidiwa, nakushukuru. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, tulisema mpaka mwezi wa 12 mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme na bado kuna vijiji kama Kiteto hatujapata umeme. Nini kauli ya Serikali kwa mpango huu wa mwezi wa 12 vijiji vyote vipate umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edward Olelekaita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Wakandarasi wote ambao tumewapatia mikataba ya kwisha Desemba 30, kupeleka umeme kwenye vijiji vyote, lazima wakamilishe kupeleka umeme kulingana na mikataba yao. Wale ambao walipewa ziada mpaka Juni, 2024 wata-cross kwenda 2024. Niwaelekeze Wakandarasi wote, yeyote ambaye hatahakikisha anamaliza mkataba wake kwa muda, bila sababu za msingi, hatutasita kuchukua hatua na kuweza kutokuendelea na mkataba wake ikifika Desemba, 30 mwaka huu, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwaka jana tarehe 16 Juni, tulisaini Mikataba ya Barabara za EPC+F ya Kongwa – Kiteto – Arusha. Naomba kufahamu lini Mradi huu unaanza kwa sababu Wananchi wa Kiteto tunausubiri kwa hamu sana?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nilijibu kwa package yote ya miradi yote ya EPC+F, miradi saba. Kama nilivyosema wakati nachangia kwenye hoja ya Kamati ya Miundombinu, design ya barabara hizi ilifanywa na TANROADS mwaka 2017 miaka mingi imepita. Kwa hiyo Wakandarasi ambao wamepatikana wanafanya mapitio ya design ili kuweza ku-update usanifu wa kina, na baada ya hapo barabara hizi zitaanza kujengwa mara moja. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Olelekaita pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao mnasubiri hii Miradi ya EPC+F tuko tunajipanga usanifu, mapitio yakikamilika basi tutaanza ujenzi wake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Kiteto tumekosa vyanzo vya uhakika vya maji, ni lini Serikali itatuletea mradi wa Simanjiro ufike Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Olelekaita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Simanjiro kuelekea Jimboni kwake taratibu zinaendelea uhakikisha mara tukipata fedha tutaweka mkakati maalum kuhakikisha tunapeleka kule maji ya uhakika.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro ni lini itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hiyo ni barabara ambayo iko kwenye EPC+F. Kama nilivyosema, tunategemea hizo barabara zianze kujengwa mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kongwa – Kiteto – Simanjiro ni lini itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hiyo ni barabara ambayo iko kwenye EPC+F. Kama nilivyosema, tunategemea hizo barabara zianze kujengwa mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa bei ya madume bora wamekuwa ni ghali sana hasa kwa hawa wa Serikali, kwa nini Serikali isipunguze bei sana ili wafugaji waweze kununua?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli madume hawa bei yake ilikuwa iko juu. Ilikuwa ni shilingi 4,000,000/= mpaka shilingi 6,000,000/=, lakini kwa concern hiyo ya Mheshimiwa Mbunge, pia madume hao wameshashuka bei. Sasa madume hao wanapatikana kwa shilingi 1,000,000/= mpaka shilingi 1,500,000/=. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kupokea ushauri kama bei hiyo pia itakuwa bado inawatatiza wafugaji wetu, tuko tayari kuishusha na kuona namna ambavyo tutawasaidia wafugaji wetu katika maeneo mbalimbali. Ahsante. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ni lini utakuwa tayari kutembelea Jimbo la Arumeru Mashariki kukagua skimu za umwagiliaji alizotaja Mheshimiwa Mbunge hapa?
Swali la pili, katika mwaka wa fedha uliopita Wizara ya Kilimo, Mradi wa Umwagiliaji wa Ngipa, Engusero-Kiteto ulipitishwa, ni lini sasa mtaanza kujenga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, niko tayari kutembelea hizo skimu, katika moja ya weekend tuombe ruhusa tu kwa Mheshimiwa Spika kama nilivyoahidi kwa Mheshimiwa Abubakari Asenga, tukafanye kazi. Nguvu tunayo na uwezo wa kufanya hiyo kazi tunao, Mheshimiwa Dkt. Samia ametuamini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Skimu ya Ngipa ambayo ilikuwepo katika mwaka wa fedha uliopita, nina uhakika Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iko katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi ili iweze kufanyiwa kazi, ahsante. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mradi wa vijiji 14 Nchinila – Engusero umechukua muda mrefu sana: Je, Serikali ina kauli gani ya kusukuma mradi huu ili umalizike na wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kiteto ni kame sana, je, Serikali ina kauli gani kuhusu kutupatia kipaumbele cha mabwawa ili wananchi wa Kiteto wanufaike na maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, nikiri na Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kupigania mradi huu ili uweze kukamilika. Sasa kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu kupitia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nasi sekta ya maji Mheshimiwa Waziri tayari ameshaingiza kwenye mpango wa utekelezaji katika mwaka huu wa fedha, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusoma bajeti tarehe tisa, utaona tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kwenda kusukuma mradi huu ili ukamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tu, siku bajeti ya Wizara ya Maji itakapofika hapa, basi makofi yake yatasaidia kupitisha bajeti hiyo ili wananchi wa eneo lake wakapate huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; ni kweli kabisa kwamba Wilaya ya Kiteto ina changamoto ya ukame. Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali na inaendelea kujiridhisha na vyanzo vya maji ili kuhakikisha kwamba wilaya hii inapata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, kwa kuanzia ni kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri, kwamba kwenda kujenga mabwawa pamoja na malambo, ambapo mpaka sasa kuna malambo ya Dongo, huko tunaendelea na utekelezaji. Kuna Dosidosi, Bwawani, Kijungu pamoja na Lambo la Makame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba tutakapoona maji bado hayajawa toshelezi, tutaendelea kwenda kuongeza miundombinu na kuhakikisha kwamba maji yanatosha katika eneo la Kiteto, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Lengatei, Magungu na Chekanao wameshaanzisha Vituo vya Polisi. Lini Serikali itawasaidia kumalizia vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Lekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa wananchi wameshaanza kazi nzuri ya ujenzi wa Vituo vya Polisi kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Serikali yetu kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inamalizia Vituo vya Polisi ambavyo ni maboma 77 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na ujenzi wa vituo vipya 12. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa vituo vyako pia viko kwenye mpango kwa ajili ya kumaliziwa.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wananchi wa Kiteto, Kata ya Magungu, Kijungu na Lengatei wameshaonesha nia ya kujenga vituo vya polisi. Lini Naibu Waziri utakuwa tayari kutembelea vituo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nipo tayari kwenda Kiteto kutembelea vituo hivyo ambavyo vimeshaanza kujengwa na wananchi, kama nilivyosema maboma yote ambayo wananchi wameshaanzisha, Serikali ipo tayari kumalizia kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Tumetenga shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nitakuja kukutembelea katika eneo lako. (Makofi)