Supplementary Questions from Hon. Asya Mwadini Mohammed (15 total)
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; bado wavuvi wanalazimika kwenda mbali kwa ajili ya kutafuta samaki kutokana na changamoto mbalimbali za bahari na uhifadhi wa mazalia ya samaki, jambo ambalo linasababisha pia wavuvi hao muda mwingine wanapata ajali za baharini, wanapotea wenyewe pamoja na vyombo vyao.
Je, Serikali ina mkakati gani wa utoaji wa mafunzo kwa wavuvi hasa mafunzo ya uhifadhi wa mazalia ya samaki na hasa kwa wavuvi ambao wanatokea pande za Nungwi, Matemwe na sehemu zingine ambao wanatokea katika ukanda wa Zanzibar? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya Mwadini Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu wa 2021/2022 kwenye mpango wetu tumeweka mkakati maalum, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja tunao mpango madhubuti kwa kutumia mashirika yetu ya Deep Sea Fishing Authority (Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu), lakini vilevile kwa upande wa Tanzania Bara (TAFIRI) na kwa upande wa Zanzibar (ZAFIRI) tumeshafanya partial marine monitoring program ambayo tumeainisha maeneo yetu ya mavuvi.
Mheshimiwa Spika, lengo letu tunataka tuwatoe wavuvi wetu kwenye kufanya uwindaji, sasa tunakwenda katika uvuvi wa kidigitali. Mvuvi kabla hajakwenda kuvua, kupitia vituo vyetu aidha Ofisi za Vijiji au MBU au kwingineko apate taarifa za mavuvi, wapi walipo samaki, umbali anaokwenda; kwa hiyo, tutakuwa na mfumo wa GPS utakaokuwa ukiwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba mfumo huu utawawezesha wavuvi wetu watumie gharama ndogo sana ya mafuta, lakini vilevile wasitumie muda mwingi wa kwenda kuwinda. Tunataka tutoke katika uvuvi wa kuwinda twende katika uvuvi wa uhakika zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Huko nje hasa katika ukanda wa bahari, sisi tunatokea kwenye visiwa, hali ni mbaya sana kuhusu masuala mazima ya mazingira. Wakisema kwamba waanzishe vikundi, kwamba vikundi ndiyo viwe vinasimamia mazingira katika kukusanya taka, bado elimu haijafikiwa. Yaani wananchi walio wengi wanazalisha taka, lakini hawana taaluma ya utunzaji wa hizo taka hasa kwenye upande wa mazingira. Je, nini kauli ya Serikali juu ya usimamizi wa masuala mazima ya utoaji wa elimu ya usimamizi wa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya, ni kweli kabisa anachokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba elimu bado ni ndogo, lakini tumieandaa programu maalumu za kutoa taaluma kwa wanavikundi na wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, jibu langu la pili la nyongeza nilisema kwamba tutaenda mpaka kwa taasisi za dini ili suala la taaluma liwe na wigo mpana. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba taaluma hiyo ya utunzaji wa mazingira itafika nchini kote.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukosefu wa taaluma za kimazingira katika Bonde la Mto Msimbazi ambayo husababisha uchafuzi wa kimazingira kutokea, hali kadhalika ukosefu huu wa elimu unawahusu hasa wavuvi ambapo bahari yetu imechafuka sana na tunakosa samaki wenye afya kutokana na wavuvi kwenda na plastics na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusikia Serikali ina mkakati gani, kwanza kuisimamia rasilimali hii muhimu ya bahari, lakini la pili, kutoa taaluma kwa wavuvi wetu ili rasilimali yetu iwe salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujibu swali lingine la Mheshimiwa Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi kubwa tunayofanya kama Serikali na kama Wizara hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ni kuwapa wananchi elimu; na ni kwa sababu tumefika wakati tumegundua kwamba elimu pekee ndiyo itakayotuokoa sisi kutokana na mazingira machafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wavuvi tumefanya jitihada kubwa. Kaskazini Unguja, kwa sababu kuna bahari tumewapa elimu, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na maeneo yote ya Tanzania yenye visiwa, mito, maziwa pamoja na bahari ambamo shughuli za uvuvi zinafanyika tumejitahidi sana tumewapa taaluma na taaluma inafanya kazi, na tutandelea kufanya hivyo. Nakushukuru.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Changamoto hizi za uchafuzi wa kimazingira ambazo zinatokea katika maziwa mbalimbali vile vile hutokea katika fukwe za bahari yetu. Nataka kujua: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti uchafuzi huu wa kimazingira kwenye fukwe ukizingatia fukwe hizi tunazihitaji zaidi katika vivutio vyetu vya utalii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Asya kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza kama Serikali tumeweza kutoa miongozo na hasa kuona jinsi gani tunafanya uratibu wa kufanya recycling process wa taka zote zinazoingizwa baharini. Hata hivyo, mnakumbuka hivi karibuni tuliweza kutoa baada ya kuona pale kuna changamoto kubwa licha ya kuzuia mifuko ya plastic, lakini imeonekana kwamba katika recycles vile vifuniko vya chupa havirejesheki na hivyo mara nyingi sana vimekuwa vikisababisha changamoto kubwa hasa katika samaki baharini.
Mheshimiwa Spika, hivyo, ndiyo maana tumetoa miongozo mbalimbali ya kuhakikisha tunalinda mazingira. Kubwa zaidi tumesisitiza ajenda ya usafi katika maeneo ya miji yote inayozunguka ufukwe wa bahari. Tulitoa maelekezo tulipokuwa pale Kinondoni kwamba maeneo yote yanayozunguka ufukwe wa bahari, Maafisa Mazingira katika maeneo hayo kuhakikisha kwamba ajenda ya usafi kwa wakazi wote inaendelea kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunakuwa na mazingira rafiki kwa ajili ya utalii. Ahsante.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa mujibu wa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kwamba Tanzania hakuna kiwanda kinachochakata vigae na ukizingatia vigae vingi tunaingiza kwanza chupa za pombe na mengineyo, lakini tunazalisha na hapa nchini maana yake uchafuzi wa kimazingira unaendelea. Nini mkakati wa Serikali kuanzisha kiwanda cha kuchakata vigae nchini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, Serikali haioni sasa kupunguza kodi kwa bidhaa zote zinazochakatwa na taka ngumu ili kuweza kuwavutia wawekezaji waweze kuwekeza nchini lakini pia na kuyalinda mazingira yetu?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asya Mwadini Mohamed Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli bado hatuna viwanda vya kuchakata vigae kwa maana ya mabaki, lakini nia ya Serikali ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji ambao tunaamini wataendelea kuwekeza katika maeneo tofauti ikiwemo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja, kwa hiyo tunaendelea kutafuta na kuweka kuwavutia wawekezaji katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni kweli Serikali tunaendelea kufanya juhudi na kuona namna ya kuweka vivutio maalum katika maeneo mbalimbali ikiwemo hili la kupunguza kodi katika maeneo ya uchakataji au urejeshaji taka ambazo kwa kweli zinaharibu sana mazingira hapa nchini. Kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tunaendelea na juhudi za kuhakikisha tunatunza mazingira kwa kuvutia wawekezaji wanaopunguza taka ambazo zimezagaa mjini nakushukuru.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imefikia wapi katika kuwasaidia wavuvi ili waweze kupata vifaa vya kisasa na waweze kuvua uvuvi wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na zana bora za uvuvi, na kwa mwaka huu wa fedha tayari wavuvi wameshapata taarifa na wameshaanza kufanya maombi na zana hizi watakazopewa zitakuwa hazina riba, watapewa mikopo ambayo haina riba ili kufanya uvuvi uwe ni uvuvi endelevu na wa kisasa, ahsante.
MHE. ASIA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Changamoto hii ambayo inaonekana kwa abiria wetu kwa upande wa Dar es Salaam hali kadhalika changamoto hii imejitokeza sana kwa upande wa Zanzibar. Je, Serikali ina mpango gani wa upanuzi wa Bandari ya Zanzibar ama kuijenga bandari mpya ili kupunguza changamoto hii kwa abira wetu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa suala la Bandari ya Zanzibar ni suala ambalo lipo kwenye Wizara ya Wenzetu kule, tutawasiliana nao ili tuone namna gani ya kupanua ujenzi wa Bandari hii ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mwani unatambulika duniani kwamba ni zao kubwa ambalo linawasaidia akina mama kulima lakini linaweza kutupa bidhaa kama vipodozi, vyakula na vitu vingine.
Je, Serikali haioni sasa kuanzisha kiwanda ama viwanda nchini vya kuchakata mwani ili tuweze kuzalisha bidhaa hizi ndani ya taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya Mwadini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwani hutumika kwa ajili ya kutengeneza kimiminika kizito ambacho hutengenezea vipodozi, na pia vile vile hutumika kama sehemu ya kutengenezea vyakula hususan kama ice cream na vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tunao mpango wa kukutana na wazalishaji wa ndani ya nchi wanaotumia malighafi hii kwa lengo la kuwahamasisha kuingia katika utaratibu ambao utapelekea wakulima wetu waweze kuchakata na kuwauzia wao wanaotumia ndani ya nchi kama vile kampuni za utengenezaji wa vipodozi na kampuni za utengenezaji wa vyakula. Ndiyo maana katika mkakati wetu tumeweka mashine za ukaushaji na hatimaye kutengeneza mpaka katika kufikia hatua ya kuwa kimiminika kizito kitakachokwenda kutengeneza colgates na vipodozi kama vile lotions lakini vile vile kwa ajili ya kutengenezea ice creams.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ajali nyingi za wavuvi zinazotokea baharini husababishwa na utabiri wa hali ya hewa: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia taarifa za dharura wavuvi wetu kabla ya kuingia baharini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwadini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni jema na zuri, tumekwishalianza. Kupitia Taasisi ya yetu ya Utafiti ya TAFIRI tumetengeneza programu maalum ya kuwasaidia wavuvi, inayoweza kuwajulisha juu ya makundi ya samaki mahali yalipo. Pia programu hii itaenda mbele, itawasaidia kwenye kufafanua pia na hali ya hewa. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tunaendelea nalo hivi sasa na tunalieneza ikiwa ni pamoja na elimu yake ili liweze kuwafaidisha wavuvi wetu.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kama tunavyotambua huu mradi wa uvunaji wa hewa ya ukaa ni muhimu sana kwa Taifa letu, inasaidia kupunguza masuala mengi ambayo yanasababishwa na uchafuzi wa kimazingira.
Mheshimiwa Spika, swali langu, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama ambao wamejitolea kwa makusudi kupanda miti ya mikoko Zanzibar katika Vijiji vya Bwimbwini, Bweleo na maeneo mengine na hawa wanawake wanapata changamoto mbalimbali kuhusu kupata miti na mambo mengine ili ile miti kuweza kustawi vizuri. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, asante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Asya amekuwa mmoja wa miongoni mwa vinara ambao wanapambana na suala zima la uhifadhi wa mazingira katika Mkoa wa Kaskazini. Kikubwa tuna mikakati mingi ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia akinamama kwa sababu tumegundua kwamba ni moja ya miongoni mwa vinara wazuri wa uhifadhi wa mazingira na kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuwapa elimu kwa sababu tumegundua kwamba akinamama wengi wana juhudi, wana jitihada na wana hamu ya kuhifadhi mazingira, lakini tumegundua utaalam kidogo umepungua, kwa hiyo tunawapa taaluma.
Mheshimiwa Spika, la pili, tumefikiria pia kuona namna ya kuwasaidia kuweza kupata mitaji ili lengo na madhumuni yaweze kufanya hizo kazi zao za uhifadhi wa mazingira vizuri. Nakushukuru.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa nchini kuna maeneo ya fukwe ambayo yameendelezwa kiutalii, lakini maeneo haya yanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuyahifadhi maeneo haya ili kuweza kuwavutia watalii nchini?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo tunapeleka watalii lazima yawe ni masafi yenye kuvutia ili tuendelee kupata watalii. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye yale maeneo ambayo yanaonekana yana changamoto hizo Serikali itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanavutia na wawekezaji na watalii waendelee kuja.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa maelezo ya Waziri kwamba hakuna changamoto mpya ni kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za zamani bado hazijakamilika. Ikiwemo hasa changamoto ya bandari na hili suala la bandari limekuwa linaleta kelele nyingi kwa wananchi na limekuwa kero kubwa. Kwa nini Serikali haioni haja ya kulichukulia jambo hili kwa udharura wake na kulitatua haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Katika kikao chetu ambacho tulikaa mwezi wa sita tulikubaliana na tulitoa maelekezo. Kwa sababu vikao hivi huwa tunakaa na Wizara za pande zote mbili au pande zote mbili zinagusa Muungano. Tulitoa maelekezo na maelekezo haya yamekwisha anza kufanyiwa kazi kwamba, watu wa TRA na wengine wa Bandari wanaohusika waende wakakae washughulikia hili jambo, tuweze kuambizana zipi zitakuwa zinalipiwa kama sehemu ya changamoto na zipi hazilipiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa kwa kuwa Kamati zinaendelea kukaa, hili jambo tunakwenda kuzimaliza ili kuimarisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nina swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, kuna kero Saba ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi na kuna kero nyingine ambazo wameanza kuzipatia ufumbuzi. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhusiana na utoaji wa taarifa wa kero hizi ili wananchi waweze kujua tathmini na ufuatiliaji wa kero ngapi ambazo zimetatuliwa na ngapi ambazo hazijatatuliwa kwa maslahi mapana ya Taifa? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri la Dada yangu, Mheshimiwa Asya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli safari yetu ya utatuzi wa hoja za muungano kama mnavyokumbuka tulikuwa na hoja 25, katika hoja hizo mwaka 2010 tulitatua hoja Mbili, mwaka 2020 tukatatua hoja Tano. Katika kipindi hichi cha mwaka mmoja chini ya Kiongozi Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi tulitatua hoja 11. Kwa hiyo, tumefanikisha kumaliza kutatua hoja 18 za Muungano kati ya hoja 25, kwa hiyo tumebakiwa na hoja Saba. Utaratibu wetu ni kwamba tarehe 23 Agosti, 2021 jambo kubwa lililofanyika Zanzibar ilikuwa ni kuitisha vyombo vya habari na kuwaeleza wananchi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tumejipanga kupitia vikao mbalimbali ndiyo maana katika bajeti tuliyopitisha mwaka huu tumetoa maelekezo ya kina na kutenga bajeti maalum ya kutoa elimu ya upana kwa suala la muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo jambo hili linaendelea kuwapa wananchi katika taarifa mbalimbali kupitia runinga, vyombo vya habari mbalimbali, magazeti hali kadhalika redio zetu ikiwa ni pamoja na zile local radio zetu.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi; kwa kuwa utunzaji wa misitu iwe ya mikoko ama ya kawaida husaidia sana katika utunzaji wa mazingira.
Swali langu kwa Serikali; je, Serikali ina mpango gani wa kuvitambua vikundi vyote vinavyojitolea kwa maksudi katika utunzaji wa mikoko hasa kwa upande wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Kwanza nipongeze vikundi vyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bara na Visiwani wanajihusisha katika ajenda ya mazingira jambo hilo ni jambo jema sana na sisi kama Serikali jukumu letu kubwa ni kuwatambua. Lakini si kuwatambua peke yake, juzi juzi tulikuwa na mkutano kule Belgium katika miradi maalum inayosemwa miradi ya hewa ukaa na miongoni mwa ajenda kubwa jinsi gani vikundi hivi vidogo vidogo vinavyochipua katika ajenda ya mazingira baadaye vifanyiwe utaratibu maalum wa uwezeshaji kwa ajili ya ajenda ya kulinda mazingira, lakini ajenda ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jambo hilo ni jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais tutaendelea kulifanya na kama mnavyoona bajeti yetu iliyopita imelenga vilevile katika suala zima la capacity building katika makundi na vikundi mbalimbali hilo ni jukumu letu tutaenda kulifanya kwa upana mkubwa zaidi ikiwemo Zanzibar. Ahsante sana.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; je, Serikali haioni haja ya kuleta taarifa ya mchakato mzima wa utatuzi wa kero za Muungano katika vyombo vya kutunga sheria, Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar na Bunge kwa Jamhuri, ili tuweze kupata picha halisi ya mchakato mzima wa utatuzi wa kero za Muungano?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri sana kuhusu masuala ya Muungano. Naomba kumpongeza dada yangu Mheshimiwa Asya kwa swali lake zuri. Katika hili, kupitia Kamati ya Utawala na Sheria ambayo ndiyo ina jukumu la kusimamia Wizara yetu ambayo tunaiongoza, mara nyingi inakuwa ikipata taarifa hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni katika vikao vya Kamati, miongoni mwa jambo kubwa ambalo limeletwa katika Kamati ni suala zima la Hoja zote za Muungano zilizofanyiwa kazi na zile ambazo zimebaki. Naomba nimtaarifu Mheshimwa Mbunge kwamba Wizara yetu inaendelea kufanya hivyo na wakati wa vikao mbalimbali tutaendelea kuleta taarifa hizi katika Bunge letu hili hususani katika kipindi cha bajeti. Mheshimiwa Mbunge asiwe na mashaka katika eneo hilo, ahsante.