Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Mohamed Kassinge (71 total)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Umuhimu wa reli ya kutoka Tunduma kwenda Kasanga ni sawa kabisa na umuhimu wa reli ambayo ilishakuwepo kabla ya Tanganyika kupata uhuru ya kutoka Mtwara – Nachingwea kwa Mikoa ya Kusini. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kufufua reli ya Mtwara – Nachingwea mpaka Nyasa kwa manufaa ya kiuchumi na shughuli za kijamii kwa Mikoa ya Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Kasinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge atakubaliana nami kwamba, Serikali ina mpango wa kujenga reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay kwa kiwango cha SGR ambapo tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na usanifu wa awali umeshafanyika. Serikali imeshatafuta tayari transaction adviser kwa ajili ya kuandaa andiko ili kutafuta mbia ambapo reli hiyo tunategemea itajengwa kwa mfumo wa PPP. Kwa hiyo, itategemea na kama mbia huyo atapatikana haraka, basi hiyo reli itajengwa. Reli hiyo itahudumia corridor ya Mtwara kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, lakini pia itakuwa na branch kwenda Liganga na Mchuchuma kwa ajili ya kusafirisha madini ambayo tunategemea yatazalishwa katika migodi hiyo. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, gesi asilia ninayozungumzia kwenye swali langu la msingi ni ile gesi ya Songosongo na eneo mahsusi ambalo nimeulizia ujenzi wa kiwanda ni katika Mji wa Kilwa Masoko, ambapo kimsingi tayari eneo la kutosha lipatalo ekari 400 lilishatengwa tangu mwaka 1989, lakini pia TPDC ilishalipa fidia ya eneo hili na ni eneo ambalo lipo huru na lina hati. Je, Serikali inathibitisha kupitia Bunge lako Tukufu kwamba kiwanda hiki cha mbolea kitajengwa mahsusi Kilwa Masoko na si kwingineko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwa ridhaa yako kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda Kilwa ili akajionee maendeleo na maandalizi ya eneo la kutosha la kiwanda hiki? Ikiwa ni pamoja na uwepo wa bandari, uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya upanuzi wa bandari, lakini pia uwepo wa eneo la kutosha kwa ajili ya kutolewa malighafi hii, lakini pia atapata fursa ya kujionea Kiwanda cha Maji cha Swahili Water pale Nangurukuru. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nipo tayari.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba tunataka kuona tunatumia malighafi iliyopo ya gesi asilia na kimsingi kama alivyosema TPDC tayari walishakuwa na eneo na hata wawekezaji hawa tunaojadiliana nao wengi tunataka waeleke kujenga katika Mji huu wa Kilwa Masoko ambapo ndipo malighafi inatoka.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili na kama nilivyosema mwanzoni nitaambatana naye katika maombi yake ili tuweze kupitia kuona namna gani tunajionea, lakini pia kuona na viwanda vingine ambavyo vimewekeza katika Mkoa wa Lindi hususani Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Umuhimu wa barabara ya Kenyatta katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ni sawa kabisa na umuhimu wa barabara ya kutoka Kiranjeranje - Nanjilinji mpaka Ruangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Jimbo la Kilwa Kusini. Lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii ni kati ya barabara ambazo zimeainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ni barabara ambayo pia imeahidiwa na viongozi wa Kitaifa. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakapopatikana barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mara baada ya kukamilisha usanifu wa kina wa barabara hii. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na ufuatiliaji na usimamizi madhubuti wa mradi huu, lakini nina swali la nyongeza. Mosi, kwa kuwa mradi huu utachukua miezi 24 tangu kuanza kwa utekelezaji wake maana yake ni miaka miwili, lakini pia utakuwa ni mradi wa kutoka katika chanzo cha maji kuelekea katika miji hii miwili niliyoitaja ya Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje, lakini viko vijiji ambavyo vitakuwa mbali na mradi huu. Je, Serikali itakuwa tayari kwa upendeleo wa kipekee kutenga bajeti kwa mwaka huu kwa ajili ya vijiji angalau vitatu vya Nainokwe, Limalyao pamoja na Mandawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mohammed Kassinge kutoka Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunapoongelea miezi 24 wakati fulani kwa sababu ya changamoto kubwa ya maji ni muda mrefu, lakini naendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameendelea kuwa karibu na sisi na kwa hakika namna ambavyo anafuatilia tutahakikisha tunakamilisha vile vijiji sio vitatu, ila kwa sasa hivi kwa mwaka huu wa fedha tutajitahidi tumchimbie kisima kimoja cha maji, lakini hivi vingine vitaingia kwenye Mpango wa Mwaka ujao wa Fedha. Haya maeneo ya vijiji vyake vitatu ambavyo viko mbali na mtandao wetu wa mabomba tutahakikisha tunakuja kuwahudumia wananchi kwa mtandao wa visima.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu haya ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale. Swali la kwanza, je, Serikali inatuahidi nini katika bajeti ijayo?

Lakini swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda kuona juhudi za wananchi Liwale lakini wakati wa kwenda au wa kurudi apitie Kilwa Masoko kwa ajili ya kuona changamoto zilizopo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassinge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ijayo kwasababu tuna ujenzi wa vyuo hivi 29 katika Wilaya 29 nchini. Katika bajeti ijayo tumepanga kununua vifaa ambavyo vitakavyowezesha sasa vyuo hivi ifikapo Januari, 2022 viweze kuanza kutoa huduma kwa maana kwamba vianze kutoa huduma ya kufundisha wanafunzi katika maeneo hayo. Hilo ndio lengo letu katika bajeti ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili suala la pili la kuweza kwenda kuona maeneo haya nipo tayari, baada ya Bunge hili la Bajeti tutapanga ziara na hata jana tulikuwa na uwekeaji wa jiwe la msingi katika chuo chetu cha VETA pale katika Wilaya ya Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pamoja na maeneo mengine na dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba nafika Liwale, lakini nitafika Ruangwa, lakini vilevile nitafika kwa ndugu yangu Kassinge pale Kilwa Kusini kuweza kuona changamoto zilizopo na kwa namna gani ya kuweza kuzitatua. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nikushuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Tatu wa Bunge lako hili niliulizia kuhusiana na Barabara ya kutoka Kiranjeranje, Nanjilinji mpaka Ruangwa kujengwa kwa kiwango cha lami na majibu ya Serikali ilikuwa kwamba itajengwa mara tu fedha zitakapopatikana.

Mheshimiwa Spika, sasa je, Serikali iko tayari kwa mwaka ujao wa 2022/2023 kutenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ambayo iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kiranjeranje hadi Ruangwa ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema, ni kweli ipo kwenye Ilani. Hata hivyo, kama nilivyosema, ni kipindi hiki tunachoendelea na bajeti, barabara hii pengine mwaka huu itakuwepo kwenye mpango kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya usanifu wa kina. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia kwa utekelezaji wa changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Likawage.

Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya nyongeza; moja, kwa kuwa changamoto ya mawasiliano Kata ya Likawage imedumu kwa muda mrefu na hivyo wana Likawage wanayo furaha sana kwa ambacho Serikali imewafanyia.

Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kufuatana nami baada ya Bunge hili, ili kwenda kuzindua mnara huo?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, changamoto hiyo iliyopo katika Kata ya Likawage bado pia ipo katika Kata ya Kikole. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto ya mawasiliano katika Kata ya Kikole? Ahsante.
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza cha swali lake ni ombi la uzinduzi wa minara hiyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na sisi tuko tayari kuambatananae na kuhakikisha kwamba, mnara huo unazinduliwa ili wananchi wa eneo husika waendelee kupata huduma ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili ni kuhusu kata ambayo inachangamoto ya mawasiliano. Ni jukumu la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 61(j) ambapo inatakiwa kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa wananchi wote, lakini kabla ya kufanya hivyo lazima tufanye tathmini na kujiridhisha ukubwa wa tatizo na baada ya hapo tutachukua hatua ili kutatua changamoto hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Hospitali ya Wilaya ya Kilwa maarufu kama Kinyonga iliyopo Kilwa Kivinje ni chakavu, lakini imeidhinishiwa fedha shilingi milioni 900: Lini Serikali itapeleka fedha hizo ili ukarabati ufanyike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali chakavu kama hospitali ya Wilaya ya Kilwa maarufu “Kinyonga”, imetengewa Shilingi milioni 900 na katika mwaka huu wa fedha Serikali inaendelea kutafuta fedha ili tupeleke katika hospitali hiyo kwa ajili ya ukarabati. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na umbali wa Kituo cha Afya Nanjilinji kutoka Makao Makuu ya Wilaya, lakini pia kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga; je, Serikali itakubaliana nami kwamba upo umuhimu wa kupeleka gari la wagonjwa kwa umuhimu wake na upekee wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikweli Kituo cha Afya Nanjilinji kiko mbali lakini kinahudumia wananchi wengi na Mheshimiwa Mbunge amekifuatilia na tumekubaliana kwamba katika vituo ambavyo vitapewa magari ni pamoja na Kituo cha Afya cha Nanjilinji.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, shilingi 93,476,190 ni fedha za wakulima wangu wa ufuta 89: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda kulipwa kwa wakulima hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na changamoto zilizopo katika uendeshaji wa bodi zetu pamoja na vyama vyetu vya msingi na changamoto wanazozipata wakulima kwa uongozi usiokuwa madhubuti, Waziri atakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda Nanjirinji kuzungumza na wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza la kuhusu malipo kwa wakulima, namwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushirika Tanzania kuhakikisha anafuatilia na mwisho wa siku wakulima hawa waweze kulipwa madai yao haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kuongozana na Mheshimiwa Mbunge, nimwahidi kwamba niko tayari, baada ya vikao hivi vya Bunge tuongozane mimi na yeye kwenda Kilwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na uvuvi wa mita 50 yanaenda kinyume kabisa na uhalisia katika maeneo yote ya ukanda wa pwani. Wavuvi wetu wa Mtwara, Lindi, Pwani, Kilwa, Tanga ni wavuvi wa kawaida ambao hawana uwezo wa kuvua kina cha mita 50 ambayo ni bahari kuu. Katika mabadiliko ya kanuni yanayokuja, Serikali iko tayari kuondoa kikwazo hiki cha uvuvi wa mita 50?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tulipokee wazo lake na tutalifikisha kwa wataalamu, watalichakata na majibu yatatoka katika Bunge lako tukufu.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Abubakar Assenga, Mbunge wa Kilombero, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kutokana na utafiti uliofanywa na GST na kubaini kwamba, katika maeneo husika madini yapo. Je, Serikali iko tayari sasa kuendelea na utafiti katika maeneo mengine jirani ambapo madini hayakupatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda Jimboni Kilombero katika maeneo ambayo madini hayo yanapatikana au kumekuwa na dalili za uwepo wa madini ili kwenda kujenga uelewa zaidi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda kufanya utafiti katika maeneo mengine, jibu ni ndio. Wizara inaendelea kupitia taasisi yake ya GST kufanya utafiti katika maeneo yote ya nchi yetu kubaini maeneo yenye madini ya aina mbalimbali, ili tuweze kuyafahamu na kuweza kuwagawia wachimbaji wadogo na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali katika dunia kwa sababu, Rais wetu naye alitusaidia sana kupitia Royal Tour kuyatangaza na wawekezaji wanazidi kumiminika nchini kwa hiyo, zoezi la utafiti linaendelea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la mimi kwenda Kilombero na kuendelea kuangalia maeneo yaliyopatikana kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ndio, niko niko tayari kutembelea katika maeneo hayo. Nipende tu kumjulisha kwamba, hata sasa katika maeneo ambayo madini yameshabainika tuna zaidi ya leseni 22 za wachimbaji wadogo ambao wanaendelea na tafiti na uchimbaji wa madini ya vito pamoja na madini ya dhahabu.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya kutoka Nangurukuru mpaka Liwale inayopitia katika Majimbo ya Kilwa Kusini, Kilwa Kaskazini pamoja na Jimbo la Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale ipo kwenye mpango kuijenga kwa kiwango cha lami na tayari usanifu ulishakamilika. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo kwa kuwa usanifu umeshakamilika, Serikali ipewe nafasi na fedha ikipatikana barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Kata ya Nanjilinji katika Jimbo la Kilwa Kusini, wamekamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi wakishirikiana nami Mbunge wao. Je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kupitia Bunge hili kwa Uongozi wa Polisi Mkoa wa Lindi ili wakakague kituo hicho na hatimae kupeleka Askari Polisi pale Nanjilinji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze kwa kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, hivyo ni wajibu wetu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hususan Jeshi la Polisi, kupeleka Askari. Kupitia Bunge lako naomba kuelekeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi wafanye ukaguzi kama kinakidhi wa wapangie Askari ili waweze kutoa huduma za usalama wa raia kwenye eneo hili la Nanjilinji. Nashukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kufuatia ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, wananchi wa Kilwa Masoko tumeandaa eneo la kutosha kwa ajili ya sekta mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kuhakikisha kwamba sekta rafiki au taasisi rafiki na bandari ya uvuvi kama vile Chuo cha Uvuvi, viwanda vya kuchakata samaki pamoja na soko la samaki vinajengwa Kilwa Masoko?

Swali la pili, wapo wananchi wapiga kura wangu ambao wamefanyiwa tathmini ili kupisha ujenzi wa Bandari ya Uvuvi wakiwemo Ndugu Mwanawetu Zarafi, Ndugu Fatima Mjaka, Ndugu Fadhila Sudi pamoja na Ndugu Suleiman Bungara (Bwege) na wenzao 50.

Je, ni lini Serikali itakwenda kulipa fidia kwa wapiga kura wangu hawa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza naomba nimhakikishie kuwa ujenzi wa bandari hii kubwa ya mfano na ya kielelezo katika Taifa letu inaendana na yote aliyoyasema ya uwepo wa miundombinu wezeshi. Kwa hivyo, nataka nikuhakikishie ya kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeliona jambo hili na nikipaumbele chake. Kutakuwepo na soko, patakuwepo na maghala ya kuhifadhia bidhaa za chakula, kutakuwepo na miundombinu mingine yote inayoendana na hadhi ya bandari ya uvuvi ya kisasa na ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni hili la tathmini naomba nilichukue jambo hili kwa kuwa jambo hili tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kwa maana ya Mamlaka yetu ya Bandari (TPA), kwa hiyo nataka niwahakikishe nalichukua hili jambo nakwenda kulisimamia kuhakikisha kwamba wananchi hawa waweze kupata haki yao.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Kiranjeranje – Nanjirinji mpaka Ruangwa imefanyiwa upembuzi wa kina na upembuzi yakinifu kwa lengo ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Wakati Wana-Nanjirinji tukisubiri lami, hali ya barabara hii si nzuri, hususan maeneo kutoka Mangaja – Nakiu – Nanjirinji mpaka Ruangwa, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi ili wakakagua barabara hii na wafanye utaratibu wa dharura?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilifanyiwa usanifu wa awali, na mwaka huu tunakamilisha usanifu wa kina. Kwa hali aliyoelezea nataka tu nitumie fursa hii kumuagiza meneja wa TANROADS aende aiangalie hiyo barabara na kama kutakuwa na changamoto kubwa inayohitaji msaada wa Wizara basi tuweze kuwasiliana; lakini tunavyoongea leo aende aitembelee hiyo barabara ili aweze kurekebisha na wananchi waendelee na shughuli zao za kawaida. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili kwa bajeti inayoendelea inayoishia Juni, 2022, ilipitisha kwamba kiwanja cha ndege cha Kilwa Masoko kifanyiwe ukarabati na maboresho, mpaka tunazungumza kazi iliyofanyika ni ya kilometa moja kwa kiwango cha changarawe bado mita 950.

Nini maelezo ya Serikali kuhusiana na mita 950 zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge Mbunge wa Kilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali ilivyoahidi tumeshakamilisha kilometa moja na tutaendelea kuzikamilisha hizo kilomita 900 zilizobaki kwa kiwango cha changarawe ili tuweze kutimiza ile ahadi ambayo tuliahidi kuifanya, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji kutoka mto Mavuje, kuelekea katika miji ya Kilwa Masoko na Kilwa Kivinje, ni lini utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mbunge wa Jimbo la Kilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni mradi muhimu sana kwa Jimbo la Kilwa na tunafahamu namna ambavyo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia kwa karibu sana. Mheshimiwa Mbunge mradi huu tunakwenda kuutekeleza mwaka ujao wa fedha.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza.

Kwanza nishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia kwa kutupatia shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa majengo katika Hospitali yetu ya Wilaya pale Kinyonga, Kilwa Kivinje. Hata hivyo bado hali ya wodi zetu ni mbaya. Serikali ina mpango gani wa kuipatia fedha Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa ajili ya kujenga na kukarabati wodi pale Hospitali ya Wilaya Kivinje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mmheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imekwishakupeleka shilingi milioni 900 ili kiufanya upanuzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa almaarufu Kinyonga; na zoezi hili linakwenda kwa awamu. Baada ya shilingi milioni 900 kutumika na kukamilisha majengo ya awamu ya kwanza Serikali itaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo mengine. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Katika Jimbo la Kilwa Kusini Kata za Kikole, Kata za Kiranjeranje hususani Kijiji cha Makangaga, Kata ya Nanjilinji hususani Kijiji cha Nakiu na Kata ya Lihimalyao hususani Kijji cha Mangisani na Kisongo hakuna kabisa mawasiliano. Je, ni nini mpango wa Serikali kwenda kujenga minara kwa ajili ya mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali dhamira yake ni kuhakikisha kwamba inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025. Sisi kama Serikali maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja naomba niyapokee ili twende tukayatazame kwa upana, tutume Timu Maalum ikafanye utafiti na tathmini ili tujiridhishe kwamba tatizo kubwa ni mawasiliano hafifu au hakuna kabisa ili tuweze kuona kwamba ni njia ipi itaenda kutatua tatizo hili, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Kiranjeranje - Makangaga – Nakiu - Nanjilinji na hatimaye Ruangwa imefikia hatua gani ili ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imeshafanyiwa usanifu na Serikali inatafuta fedha kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Kiranjeranje hadi Ruangwa, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante na naipongeza Serikali kwa majadiliano yanayoendelea kati yake na wawekezaji, japo nasikitika kwamba ni karibu mwaka sasa tangu mazungumzo hayo yameanza. Kwa hiyo, kwa umuhimu wa mahitaji ya mbolea nchini, naomba basi mchakato huu ufanyike kwa haraka ili tutatue tatizo kubwa la wakulima ambao wanakosa pembejeo za mbolea msimu mpaka msimu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mwaka 2021 kupitia Bunge hili aliahidi kuja Kilwa ili kuona mchakato wa uanzishwaji wa kiwanda hiki, lakini nadhani kutokana na majukumu alishindwa kupata nafasi hiyo. Sasa je, yupo tayari baada au ndani ya Bunge hili wakati mchakato wa majadiliano unaendelea, kufuatana nami kwenda Kilwa Masoko ili kuona maendeleo ya maandalizi ya kiwanda cha mbolea?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naamini Serikali yetu ni sikivu chini ya Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, tutaharakisha majadiliano haya ili tuweze kufanikisha uwekezaji huu muhimu mapema.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la pili, naomba nimwahidi, kwa kweli tangu mwaka 2021 hatujapata nafasi, lakini naamini mwaka huu nitakwenda. Nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya kutoka Kiranjeranje – Nanjilinji mpaka Ruangwa ni barabara ambayo Serikali imeahidi kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 mpaka 2025 lakini pia upembuzi wa kina umeshafanyika. Lini Serikali inakwenda kujenga barabara hii kwa manufaa ya wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii tumeshakamilisha usanifu wa kina, na haya ni maandalizi kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hii hatua ya kukamilisha usanifu wa kina Serikali inaendelea kutafuta fedha ili iweze kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya swali la nyongeza. Niipongeze sana Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa mpango wake huu wa kununua magari ya wagonjwa katika halmashauri zetu zote nchini, hongera Serikali. Nikiamini pia kwamba Hospitali yangu ya Wilaya ya Kinyonga, pale Kilwa Kivinje tutapata gari hili. Lakini tuna changamoto kubwa ya vituo vyetu vya afya ambavyo havina magari haya ikiwemo Kituo cha Afya Nanjilinji. Je, kwa upendelea wa pekee Ofisi ya Rais- TAMISEMI itapeleka gari ya wagonjwa Nanjilinji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Comrade Ally Kassinge Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ally Kasinge, kwa kweli anapambana sana kuwasemea wananchi wa Jimbo lake la Kilwa, na sisi tunamhakikishia tutaendelea kuhakikisha tunampa ushirikiano ili wananchi wa Kilwa wapate matunda ya Serikali yao ya Awamu ya Sita. Nimhakikishie, kwamba tunafahamu kwamba Kilwa, nayo itapata gari la wagonjwa, itapata gari la usimamizi, lakini kituo cha Nanjili nakifahamu kiko mbali lakini kinahudumia wananchi wengi. Na katika magari 195 tuna halmashauri 184. Kwa hiyo, tutafanya tathmini na kuona uwezekano wa kuongeza gari Kituo cha Afya Nanjilinji. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), imefanya maboresho makubwa Kilwa Kisiwani ambao ni mji wa kitalii na Kilwa Kisiwani imetangazwa kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia, lakini makubaliano yalikuwa kwamba wananchi wa Kilwa Kisiwani wapate CSR kupitia kujengewa shule pamoja na zahanati, lakini mpaka sasa hawajajengewa shule wala zahanati.

Mheshimiwa Spika, swali langu, je, Waziri yuko tayari kufuatilia kuona kwamba shule na zahanati inajengwa Kilwa Kisiwani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuliona hili, lakini kama ambavyo nimeeleza mwanzo kwamba kabla ya UVIKO-19 tulikuwa tunatekeleza kupeleka haya maeneo CSR, lakini hii changamoto ya UVIKO-19 ndio iliyoturudisha nyuma lakini kwa sasa hivi tumeshaanza kuimarika vizuri. Hivyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge katika eneo lake nitaenda pia nitaenda kuongea na wananchi wa jimbo hilo ili kuwaambia umuhimu wa kupata CSR pia umuhimu wa utunzaji wa maeneo ya hifadhi. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona kwa nafasi ya swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Hoteli tatu mpaka Pande na hatimaye Limalyao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imeshafanyiwa mapendekezo ya kupandishwa hadhi ili iwe ya TANROADS na vikao husika. Lini Serikali itapandisha hadhi barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoa majibu ya awali kwa Mheshimiwa Mulugo na Mheshimiwa Chaya, ili kupandisha hadhi barabara hizi, baada ya mchakato wote kuwa umeshapitiwa, sasa ni mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya barabara ni Waziri wa Ujenzi. Sasa wakati tunafuatilia suala la Mheshimiwa Mulugo tutahakikisha na hili la Mheshimiwa Kassinge nalo tunaliangalia.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Narabara ya kutoka Nagurukuru, Njenje mpaka Liwale ipo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Je ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami ambayo inaunganisha Jimbo la Kilwa Kusini, Kilwa Kaskazini pamoja na Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabra hii Mheshimiwa Waziri alishaahidi. Aliahidi kwenye kamati lakini pia alimuahidi Mbunge, si tu Ally Kassinge lakini hata Mheshimiwa Kuchauka najua anahitaji sana hii barabara; na jana nimekusikia pia ukiichangia hiyo barabara. Naomba tusubiri bajeti tunayokwenda kuijadili sasa hivi, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Wananchi wa Kata ya Nanjirinji wakishirikiana na mimi Mbunge wao wamejenga na kukamilisha kituo cha polisi ili kupunguza uhalifu mkubwa katika eneo la Nanjirinji. Je, Serikali iko tayari sasa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kuelekeza uongozi wa polisi Mkoa wa Lindi wakakague kituo hiki wafanye tathmini na hatimaye kupanga askari wakafanye kazi pale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kassinge kwa kujumuika na wananchi wake wakajenga na wakakamilisha kituo cha polisi kama ilivyoelezwa hapa Bungeni. Ni maelekezo yangu kwa IGP kupitia Kamanda wake wa Polisi wa Mkoa wafanye ukaguzi wa kituo hiki ili kama kina kidhi haja kiweze kupangiwa askari na kuanza kuwahudumia wananchi wa eneo hilo, nashukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, la kwanza. Kilwa Kisiwani kwa sababu ni kisiwa utaratibu wake ni wa kipekee. Je, na yenyewe nayo imo katika mpango huu na awamu hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kata za Nanjirinji, Narikalage pamoja na vijiji vyake vya Nainokwe, Liwiti pamoja na Narikilage yenyewe inapitiwa na msitu wa hifadhi na kulikuwa na mgogoro kati ya REA na TFS: Je, mgogoro huo umekwisha na Serikali sasa iko tayari kusambaza umeme katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza, tunafahamu kwamba kuna vijiji katika Jimbo la Kilwa Kusini ambavyo vipo katika visiwa na upo mradi unaitwa RBF (Result Based Financing) awamu ya pili ambao utafikisha umeme katika visiwa hivyo pamoja na visiwa vingine Tanzania Bara 36 katika awamu hii. Kwa hiyo, pamoja na visiwa hivyo viwili, viko visiwa vya maeneo mengine vya maeneo mengine ambavyo pia vitafikishiwa umeme katika miradi hii ambapo tunatafuta sasa wakandarasi wa kupeleka mradi wa umeme katika maeneo hayo. Kwa upane wa Kilwa amepatikana Mkandarasi anaitwa Greenl Leaf ambaye anakamilisha taratibu za kupeleka umeme katika maeneo hayo ya visiwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, ni kweli tulikuwa na changamoto ya mawasiliano katika ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitisha miundombinu ya umeme katika mapori ya TFS, lakini tatizo hilo sasa limekuwa solved, na sasa tunazungumza lugha moja. Kwa hiyo, sasa kunapokuwa na mradi unaohitaji kupita katika maeneo hayo, vibali vinatolewa na mradi unaweza kupitishwa kwa wakati.

Kwa hiyo, kwa sasa tatizo hilo limetafutiwa ufumbuzi na halina tatizo.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa upembuzi na usanifu wa barabara ya kutoka Kiranjeranje – Makangaga – Nakiu – Nanjirinji mpaka Ruangwa umekamilika, lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshafanya kama alivyosema upembuzi yakinifu, na yote hayo ni maandalizi ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna mpango wa kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Kiranjeranje hadi Ruangwa kwa kadri fedha itakavyopatikana.
MHE ALLY M. KASINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Nanjilinji ambayo ina umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka sehemu ya kutolea huduma ya afya kwa maana ya Hospitali ya Wilaya pale Kinyonga haina gari la wagonjwa.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Nanjirinji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Nanjirinji na nimhakikishie kwamba kwenye magari ambayo tayari yameanza kununuliwa, tayari magari 117 yameingia kati ya 316 na kituo hiki kitapewa kipaumbele kupewa gari la wagonjwa, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Barabara ya kutoka Hoteli Tatu – Pande – Lihimalyao iko chini ya TARURA, lakini Bodi ya Barabara pamoja na Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Lindi ilipendekeza barabara hii iapandishwe hadhi, ichukuliwe na TANROADS; ni lini TANROADS itaichukua barabara hii? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge aweze kuleta swali mahususi, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza katika Jimbo la Kilwa Kusini, Kata za Nanjilinji, Kikole na Kiranjeranje bado migogoro ya wakulima na wafugaji inaendelea. Je, ni nini jukumu la Jeshi la Polisi kuzuia na kukomesha kabisa migogoro hii badala ya kuendelea na kesi ambazo hatima yake inakuwa si nzuri sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa migogoro katika eneo la Kilwa alilotaja Mheshimiwa Mbunge ni kweli tunafahamu na kuna maelekezo yalitolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Wakuu wote wa Mikoa ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Usalama na wadogo zao kwa maana ya Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Kamati za Usalama ngazi ya Wilaya kuwa na mipango ya usimamizi wa matumizi bora ya ardhi pamoja na kuwapanga wakulima na wafugaji kuepuka mwingiliano unaosababisha migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa Jimbo la Kilwa na hizo kata tatu alizozitaja Mheshimiwa Mbunge nishauri tutumie infrastructure kwa maana ya miundombinu iliyopo ya upatanisho, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii wanaendelea kuelimisha wananchi juu ya kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima kama hii. Hata hivyo, tuwaombe wataalam wetu wa ngazi za Serikali za Mitaa ambao hufanya uthamini wa uharibifu wa mazao kabla Polisi hawajachukua hatua za kurejesta kesi Mahakamani ili watimize wajibu wao ipasavyo, kwa sababu wakati mwingine wanaona inachelewa kumbe ni kutokana na kuchelewa kwa zile tathmini za wenzetu. Vinginevyo tuendelee kuwaelimisha wakulima na wafugaji, wote ni Watanzania, waishi kwa maelewano kila mmoja akitimiza wajibu wake, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Jimbo la Kilwa kusini halina chuo cha VETA na hakuna mpango wowowte wa Serikali kujenga chuo hicho isipokuwa tuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi pale Kilwa Masoko ambapo miundo mbinu yake ni ya muda mrefu na imechakaa. Sasa hivi kipaumbele chetu ni kujenga bwalo na tulishaomba.

Je, lini Serikali italeta fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa bwalo pale chuo cha wananchi Kilwamasoko?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyokwisha eleza kwamba mpango wa Serikali ni ujenzi wa vyuo 64 katika wilaya ambazo hazina, miongoni mwa Wilaya hizo ni pamoja na Wilaya ya Kilwa. Sasa utaratibu gani wa eneo gani linakwenda kujengwa, aidha ni Kilwa Kusini au ni Kilwa Kaskazini ni maamuzi ya Wilaya au Mkoa wa Lindi kuamua chuo hicho kinakwenda kujengwa wapi. Tunatambua uwepo wa Chuo cha FDC pale kulwa Kusini na mimi nakifahamu chuo hiki na tunajua kwamba tunauhitaji wa bwalo pamoja na baadhi ya mabweni. Kama nilivyosema kwa upande wa Korogwe katika mwaka ujao wa fedha tutatenga fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vyuo vile, kuongeza miundombinu ya mabweni pamoja na mabwalo, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi katika bajeti ijayo mambo mazuri yanakuja.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Barabara ya Nangulukulu - Liwale, inayopita katika majimbo ya Kilwa Kusini, Kilwa Kaskazini na Liwale, imeharibika vibaya kutokana na mvua za hivi karibuni. Nini maelekezo ya Wizara, kuelekeza TANROADS Mkoa wa Lindi kufanya marekebisho katika maeneo ya Nangulukulu - Migelegele – Mbate, Naiwanga – Njinjo – Miguluwe mpaka Kimambe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kama tulivyosema huko nyuma na tulikwishatoa maelekezo na ninatoa sasa maelekezo mahususi kwa Meneja wa Mkoa wa Lindi, kuhakikisha kwamba anakwenda maeneo yote ya barabara ya Nangulukulu – Liwale kurekebisha maeneo yote ambayo hayapitiki kwa sasa na kama kutakauwa na changamoto ya kibajeti basi aweze kuwasiliana na TANROADS Makao Mkauu kwa msaada zaidi ili kuhakikisha kwamba anarejesha mawailiano.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kufuatia ujenzi wa bandari ya uvuvi unaoendelea pale Kilwa Masoko. Nini mpango wa Serikali kupanua barabara ya kutoka Kilwa Masoko mpaka Nangurukuru ili iweze kukidhi haja ya wakati wa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Kilwa Masoko tunajenga bandari ya kisasa ya uvuvi na katika mipango yetu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TANROADS, tutaboresha pia barabara hii kutoka eneo la bandari ri kwenda katika eneo la pale mjini na kwa maana hiyo Mheshimiwa Mbunge katika mwaka wa fedha ujao barabara hii tumeitengea fedha kwa ajili ya kuboresha katika ujenzi wa kiwango cha lami. Ni sehemu ya mradi huu wa uijenzi wa hii Bandari ya Kilwa Masoko, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Usimikaji wa nguzo katika Kata ya Likawage na Vijiji vyake vya Nainoku, Liwiti na Likawage yenyewe katika Jimbo la Kilwa Kusini umekwama kutokana na changamoto ya TFS kuzuia kupitisha nguzo katika eneo la hifadhi. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kushirikiana kati ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii kuondoa utata huu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, awali kulikuwa kuna changamoto kubwa ya Sheria ya TFS ambayo ilikuwa inatutaka sisi Wizara ya Nishati au watumiaji wengine wa maeneo yao kulipia gharama fulani lakini baada ya majadiliano tumekubaliana kwamba, kwa sababu tunafanya miradi ya Serikali kwa pamoja basi tupeane hizi leeway kwa ajili ya kupitisha hii miundombinu. Kwa hiyo, case by case zikitokea tunazi-solve kulingana na maeneo husika. Nitawasiliana na Mheshimiwa Mbunge ili tuone wapi tulipokwama na tuweze kutatua tatizo hili kwa sababu maeneo mengine tayari tumelimaliza.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kijiji cha Makangaga, Kata ya Kiranjeranje Jimbo la Kilwa Kusini, kuna skimu ya umwagiliaji ambayo imetelekezwa kwa muda mrefu: Je, Serikali ipo tayari kupeleka wataalamu pale Makangaga ili wakafanye upembuzi yakinifu na hatimaye skimu hii iweze kufufuliwa mara moja?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Serikali itapeleka wataalam waweze kutathmini hiyo skimu na kuona gharama na mahitaji halisi ili iweze kuboreshwa na iweze kutoa tija kwa wakulima wanaotumia skimu hiyo, nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kutokana na changamoto ambayo imeendelea kujitokeza kwa Askari wetu wanapostaafu kucheleweshewa mafao yao, kwanini Serikali sasa isije na mpango wa kufanya uhakiki angalau mwaka mmoja kabla ili mtumishi au askari anapostaafu apate mafao yake pamoja na fedha za usafiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Sisi tunalichukua hili na ni maeneo ambayo tunayafanyia kazi kama nilivyosema kuhakiki mapema. Mosi, madeni na Pili, mahitaji ya mwaka husika ili kupunguza ucheleweshaji huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunalifanyia kazi hili kama ambavyo wamesema na tunahakikisha tunafanya hivyo ili kupunguza adha kwa wastaafu hawa katika maeneo yote. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru, Halmashauri ya Wilaya wa Kilwa inaendelea na ujenzi wa Stendi ya Mabasi pale Nangurukuru, lakini uwezeshaji wake wa kimapato ni mdogo. Je, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, iko tayari sasa kuipa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili ikamilishe ujenzi wa stendi pale Nangurukuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi ya mabasi Nangurukuru, ni kweli umeanza kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Naomba nitumie fursa hii kusisitiza kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, kuhakikisha kwamba anaweka kipaumbele kwenye bajeti ya mapato ya ndani kuongeza kasi ya ujenzi wa stendi ile, lakini na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafanya tathmini kuona kama wanashindwa, kwa maana ya uwezo wa mapato kukamilisha kwa wakati ili tuone uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya kuwa-support ili kuikamilisha kwa wakati, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kata ya Lihimalyao na Vijiji vyake vya Mangesani pamoja na Kisongo katika Jimbo la Kilwa Kusini, hakuna kabisa mawasiliano ya simu na katika awamu hii ya ujenzi wa minara 758 haijafikiriwa au haijapata nafasi. Nini mpango wa Serikali kwenda kujenga minara katika Kata ya Lihimalyao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaongea na inawezekana kuna maeneo mengine ndani ya nchi yetu bado hayajapa mawasiliano. Serikali inaendelea kutekeleza miradi hii kwa awamu. Awamu ya kwanza tumemaliza minara 758, kuna awamu inayokuja ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kwa ajili ya kuleta minara 600.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, tukitoka hapa tukutane ili niweze kuchukua taarifa za uhakika kuhusu maeneo hayo ili tuwatume wataalam wetu, wakajiridhishe ili tuweze kuchukua hatua za kufikisha mawasiliano ndani ya kata hizo. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Serikali iliahidi kutuma wataalam kwenda kufanya tathmini na uchambuzi ili kijengwe kituo cha afya Kata ya Likawage Jimbo la Kilwa Kusini.

Je, ni lini wataalam hawa watakwenda kufanya tathmini hii ili kituo hicho kijengwe mara moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Suala hili lipo ndani ya uwezo wa wataalam wa Mkoa wa Lindi. Tuna Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi na tuna Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilwa. Natoa maelekezo, ndani ya siku 14 wawe wamefanya tathmini ya vigezo kama tunahitaji kujenga kituo cha afya hapo lakini wawasilishe Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tufanye maamuzi kwa ajili ya kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Nashukuru.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kufufua skimu ya umwagiliaji iliyoko Kijiji cha Makangaga, Kata ya Kiranjeranje, Jimbo la Kilwa Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema pale awali ni dhamiravya Serikali kuhakikisha skimu zote za umwagiliaji zinafanya kazi. Nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuangalia kama katika jedwali letu skimu hiyo haipo katika mwaka huu wa fedha, basi tutaitengea fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, inafanya kazi na wakulima wanatumia skimu hiyo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu hayo ya Serikali ambayo yamenipa mashaka katika mawanda ya ushirikishwaji wa wadau, niseme tu kwamba, katika sehemu ambayo Serikali inatakiwa kuwa makini ni katika kutunga sera hii kwa sababu, ndiyo inakwenda kujibu Ibara ya 146 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Swali la kwanza; Ni kwa kiwango gani wadau katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri na kwa upekee wake Waheshimiwa Madiwani wameshirikishwa katika utungaji wa sera hii?

Swali la pili; Je, Serikali iko tayari kutoa commitment hapa Bungeni kwamba, katika mchakato huu kabla ya maamuzi sera hii ipitiwe na Wabunge, kama tulivyopitia Sera ya Elimu, kwa lengo la kutoa input zaidi na kuboresha utungaji wa sera hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ally Kassinge, swali lake la kwanza anasema ana mashaka, nimtoe mashaka haya kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ina imani kubwa na Sera nzima ya D by D na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, chini ya uongozi wake Mheshimiwa Angellah Kairuki itaendelea kusimamia sera hii ya D by D ambayo ni ugatuaji wa madaraka kwenye Halmashauri. Halmashauri hizi ziweze kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe kwa kushirikiana na wataalam ambao wanapelekwa na Serikali katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye Sali lake la pili ambalo anataka commitment, commitment kama nilivyosema hapo nikimjibu swali lake la nyongeza la kwamba, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaamini katika D-by-D. Baada ya mwongozo huu kufanyiwa mapitio tutaileta kwenye Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ili nao waweze kupitishwa kwenye mwongozo ule ambao upo, lakini tutabaki katika D by D Mheshimiwa Mbunge na hatutatoka katika hilo kwa ajili ya kuwapa nguvu Waheshimiwa Madiwani kufanya maamuzi yao katika Halmashauri zao.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Serikali mwaka jana ilipandisha vyeo au madaraja watumishi katika sekta ya umma baada ya kushindwa kupandishwa kwa takribani miaka mitano. Upandishwaji huu umesababisha changamoto ya walioajiriwa mwanzo na walioajiriwa baadaye wote kujikuta wapo katika kundi moja au daraja moja. Nini tamko la Serikali kutoa maelekezo kwa mamlaka za ajira nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili ifanye uchambuzi na hatimaye walioajiriwa wakiwa daraja moja waweze kuwekwa katika madaraja stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Kassinge Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kuwapandisha vyeo watumishi ni sehemu ya kuwapa motisha ili waendelee kufanya kazi vizuri pia ni eneo la kuendelea kusimamia usimamizi wa watumishi wa umma katika nchi yetu. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hapo mapungufu yaliyojitokeza katika utumishi ambayo yanahitaji watu wapandishwe vyeo yote tunayafanyia kazi na tutaendelea kutoa taarifa kadiri tunavyoendelea kupata nafasi ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa za watumishi wako zote ambao wana malalamiko kama hayo kupitia wewe tungependa tuzipate Serikali ili tuweze kuzifanyia kazi na kuweza kuwapatia haki yao wafanyakazi hao.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha afya katika Kata ya Likawage, Jimbo la Kilwa Kusini, kata ambayo iko mbali kutoka sehemu ambayo huduma ya afya inapatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutatuma timu kwenda katika Kata ya Likawage kufanya tathmini na kuona kama vile vigezo vya idadi ya watu na kadhalika vimefikiwa eneo walilolitenga wao katika maeneo hayo na kama vigezo vile vimefikiwa, basi tutaweka katika mipango yetu ya kutafuta fedha.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza na nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa hatua hiyo, lakini niombe mchakato wa malipo sasa uharakishwe kwa sababu uthamini huu umefanyika kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kumekuwa na changamoto katika umakini wa uhakiki hususani uliofanyika katika kipindi hiki cha pili ambapo wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wanapunjwa, kucheleweshwa kwa malipo haya na malalamiko mengine mengi. Je, Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili atakuwa tayari kuambatana nami kwenda Kilwa Masoko kukaa na wananchi hawa kuwasikiliza kero zao na hatimaye kuwapatia majawabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mradi na Mpango huu ni wa muda mrefu, je, ni lini sasa upanuzi na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa jambo hili la fidia kwa wananchi wake na Serikali imeendelea kulifanyia kazi. suala la kuambatana naye nimhakikishie nitaambatana naye mara baada ya vikao vya Bunge. Vile vile, nitakuwa na ziara katika Mkoa wa Lindi (Kilwa) Morogoro, Ruvuma pamoja na Iringa. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge hata huko Kilwa nitafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini hasa upanuzi wa kiwanja utaanza. Ni kwamba tayari tumekuwa na awamu mbili za upanuzi wa kiwanja hiki ambapo awamu ya kwanza ilikuwa kwa ajili ya kutanua ile run way kuweka moramu na sasa hivi tumejenga jengo la abiria lililogharimu takribani milioni 137. Awamu ya pili itafadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo iko katika mpango wa Serikali wa mwaka wa fedha ujao. Kwa hiyo, baada ya hapo kiwanja hiki kitakuwa kimekamilika, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, Serikali imefikia hatua gani kutafuta mkandarasi kwa ajili ya Visiwa vya Kilwa Kisiwani pamoja na Songo Mnara kupeleka umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, wenzetu wa REA wanakamilisha mradi wa kupeleka umeme katika visiwa ambao unajitegema tofauti na wa REA kwa sababu REA inaunganisha kwenye gridi, lakini maeneo ya visiwani bado hatujaweza kufikisha gridi lakini tunakamilisha kwenye visiwa takribani kama 358 vya kupelekea umeme. Mradi huo utakapokamilika Mheshimiwa Kassinge ataona tukiutekeleza.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka jana wakati akijibu swali langu la msingi kwenye swali la nyongeza aliniahidi kunipatia fedha kwa ajili ya kuchimba kisima kimoja cha maji katika Kijiji cha Nainokwe.

Je, lini fedha hizi zitakwenda ili wana Nainokwe wakafarijike kutokana na adha ya maji wanayoipata?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifika tulifanya pamoja ziara na kisima hiki ni lazima kichimbwe. Mheshimiwa Mbunge tafadhali baada ya session hii ya leo tukutane ili tuweze kufuatilia pamoja hii fedha itoke. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Awali ya yote niishukuru Wizara hii kwa kuwezesha mawasiliano katika Kata ya Likawage, Jimbo la Kilwa Kusini. Swali langu, ni nini mpango wa Serikali kupitia Wizara hii kuhakikisha kwamba, Kata za Nanjilinji, Kikole pamoja na Limalyao na zenyewe zinapata mawasiliano ya uhakika?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kata alizozitaja na ni kweli katika Wilaya na majimbo ambayo hali yake ya mawasiliano ni ngumu ni pamoja na Jimbo la Kilwa Kusini. Baadhi ya minara ambayo imejengwa ipo, lakini haijakamilika, ikikamilika itapunguza tatizo tulilonalo, lakini bila shaka Mheshimiwa Mbunge atakumbuka kwenye bajeti ya mwaka huu tumeweka zaidi ya minara mipya 700 nchi nzima, kwa hiyo, naamini kwamba, baadhi ya kata zake zitakuwemo. Kata zitakazobaki, nimhakikishie kwamba, tutakwenda kuzimalizia kwa ule utaratibu wa maeneo maalum.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kiranjeranje – Nanjilinji mpaka Ruangwa ni barabara ambayo imenadiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 mpaka 2025, lakini pia imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Je, lini Serikali itatenga fedha au kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba, azma ya Serikali ni kuzijenga barabara zote kwa kiwango cha lami na ndio maana tumeshaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa tayari tumeshaanza hiyo ni hatua na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, ahsante.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Kwa muda mrefu Serikali kupitia TPDC imetenga eneo la kujenga Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko itakayotokana na malighafi ya gesi asilia; na kwa mara ya mwisho tumepewa taarifa kwamba Serikali iko katika mazungumzo na mwekezaji.

Swali; mazungumzo kati ya Serikali na mwekezaji yamefikia hatua gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ally kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli adhma ya Serikali ni kuona tunajitosheleza katika uzalishaji au mahitaji ya mbolea nchini ambayo ni takribani ya tani 700,000. Uzalishaji tulionao sasa si zaidi ya tani 100,000. Lakini mipango hiyo pamoja na mingine ni kuona gesi asilia katika Mkoa wa Mtwara inatumika kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema na TPDC kweli kuna eneo limetengwa na kwa kweli kama nilivyosema swali hapa Bungeni kuna wawekezaji wameshajitokeza ambao watakuja kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha mbolea kwa kutumia gesi asilia.

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mbunge kwamba Serikali inafuatilia sana jambo hili ili kuhakikisha majadiliano hayo yanakamilika mara moja na kwa kweli tunafanya majadiliano kwa ajili ya kuona namna ya kuwavutia. Kwa sababu kilichopo hapa ni namna ya kuwavutia ili waweze kuwekeza katika kutumia gesi hiyo ikiwemo pamoja na mambo ya bei na mambo mengine/vivutio maalum ambavyo wanahitaji wawekezaji hao. Kwa hiyo, tutakamilisha na kuanza kuzalisha mbolea kupitia gesi asilia, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Nishukuru commitment ya Wizara kuja kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilwa ambayo ina Majimbo mawili ya Kaskazini na Kusini. Pale Kilwa Kusini tuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ambacho ni chakavu, kuna baadhi ya miundombinu inahitaji maboresho. Nini kauli ya Serikali katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka huu wa fedha unaoendelea kwenye vyuo hivi vya FDC Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa zaidi ya bilioni 6.8. Lakini vilevile katika mwaka uliyopita wa fedha tumeweza kufanya ukarabati pamoja na ujenzi wa miundombinu.

Kwa hiyo, nikuondoe wasiwasi mchakato huu au taratibu hizi bado zinaendelea, tunaamini kabisa vifaa hivi vitafika Kilwa. Lakini tunaamini katika mwaka ujao wa fedha kwa vile programu ya kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika vyuo vya FDC navyo vilevile tunaendelea kufanyia kazi tunaweza kufika eneo lile na kuweza kufanya kazi vizuri. Nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Niipongeze na niishukuru Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi kwa hatua ambayo imefikia, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; wakati Wizara inaendelea kurekebisha Kanuni hizi au inakwenda kufanya marekebisho ya Kanuni hizi, ilituma timu ya wataalam kwa ajili ya kufanya utafiti katika maeneo ambamo shughuli za uvuvi zinafanywa na wataalam hawa waliwasilisha ripoti ambayo nadhani Wizara ndiyo inafanyia kazi ikiwa ni kama msingi wa kutengeneza kanuni hizi. Swali la kwanza; je, maoni ya wataalam yatazingatiwa katika marekebisho ya kanuni hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wizara imeshirikisha wadau mbalimbali katika kufanya marekebisho ya kanuni hizi ikiwa ni pamoja na Kamati ya Bunge inayohusiana na Sekta ya Mifugo. Je, Wizara ipo tayari wakati inaendelea kufanya marekebisho kanuni hizi kuwashirikisha pia Wabunge wanaotoka kanda za uvuvi ili kuongeza maoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, maoni ya wataalam yatazingatiwa nataka nimhakikishie yeye na Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla, wataalam maoni yao tutayazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, je, Wabunge ambao walishiriki katika kuibua hoja hii wale wanaotoka katika maeneo ya uvuvi watashirikishwa? Hili pia tutahakikisha tunawashirikisha ili kusudi kuweza kutoka na Kanuni za pamoja. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Lini Serikali itaanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Likawage, Jimbo la Kilwa Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kata ya Likawage katika Wilaya ya Kilwa inahitaji Kituo cha Afya na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia mara kwa mara. Tulishaelekeza wataalamu kwa maana Mganga Mkuu wa Wilaya na Mganga Mkuu wa Mkoa, wafanye tathmini ya vigezo na kuwasilisha maombi Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nasisitiza tupate taarifa hiyo ndani ya wiki mbili ili Mheshimiwa Waziri wa Nchi aweze kuona uwezekano wa kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Ni muda mrefu sasa tangu serikali itoe ahadi ya kupeleka wataalam ili wakafanye upembuzi na usanifu kwa ajili ya Skimu ya Umwagiliaji ya Makangaga Kata ya Kiranjeranje katika Jimbo la Kilwa Kusini kazi hiyo bado haijafanyika mpaka sasa; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kwenda kufanya usanifu huo?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Mradi wa Makangaga uko katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanyiwa usanifu, kwa hiyo unatekelezeka katika mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kata ya Likawage katika Jimbo la Kilwa Kusini haina kituo cha afya na ipo mbali kutoka katika maeneo ya kutolea huduma, na Mheshimiwa Naibu Waziri alishatoa maelekezo kwa Mkurugenzi aandike andiko ili litumwe Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Andiko hilo tayari limekamilika, sasa tunataka kupata commitment ya Serikali, lini Kituo cha Afya Likawage kitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge. Ni kweli alishafuatilia mara kadhaa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusiana na ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo na tayari Mkurugenzi alishawasilisha andiko ambalo tuna makadirio ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie, kwa sababu tayari ameshaleta kama kipaumbele na katika mwaka ujao wa fedha Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatupa idhini ya kutenga bajeti ya vituo vya afya kila jimbo na katika Jimbo lake la Kilwa Kusini tutahakikisha tunapeleka fedha kwa ajili ya kituo hiki cha afya, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, usambazaji wa umeme wa REA katika Kata ya Nanjirinji na Kata ya Likawage, umekwama kwa sababu ya mgogoro kati ya TFS pamoja na mkandarasi. Nini Kauli ya Serikali katika kutatua mgogoro huu ili wananchi wapate umeme huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge nikuahidi, nitafuatilia suala hili ili kuhakikisha linatatuliwa kwa wakati na wananchi waweze kupata umeme katika maeneo yao, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Naibu Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Sagini kwa kufuatilia kwa ukaribu sana harakati za ujenzi na ufunguzi wa Kituo cha Polisi Nanjirinji, alikwenda mwenyewe na ninashukuru sasa Kituo cha Polisi Nanjirinji kimeanza kazi. Pamoja na hayo, bado kuna changamoto za vitendea kazi ambavyo ndani yake ni too professional.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutoa maelekezo kwa uongozi wa Polisi wa Mkoa wa Lindi ili waende wakazungumze na Maafisa au Askari pale Nanjirinji kwa lengo la kujua changamoto zao za kazi ili hatimaye usalama uendelee kuimarishwa pale Nanjilinji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Ally Kassinge kwa namna alivyofuatilia kituo hicho hadi ikanilazimu Naibu Waziri kukitembelea kwa madhumuni ya kukianzisha. Changamoto ya ucheleweshaji wa kuanzisha tuliimaliza siku ile na baada ya wiki mbili kikaanza kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, kwa vile tayari Serikali kupitia Jeshi la Polisi imesharidhia kituo kile kianze kutoa kazi, nitoe maelekezo kwa Mkuu wa Polisi nchini afuatilie kuona kwamba kituo kile kinapata vitendea kazi muhimu kuwezesha majukumu ya ulinzi wa raia na mali zao yaweze kufanyika kwa ufanisi, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nina maswali mawili ya nyongeza. Mchakato wa uboreshaji na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko ni wa muda mrefu sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; nataka Mheshimiwa Naibu Waziri, awahakikishie Watanzania, Wanakilwa na Bunge hili, je, mpango wa Serikali wa uboreshaji na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko bado uko pale pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Kilwa Masoko mara kadhaa. Alifika mwezi Juni akiwa Mwenyekiti wa Kamati na akafika mwezi Agosti akiwa Naibu Waziri katika Sekta hii ya Uchukuzi na alikuja mahususi kwa ajili ya masuala haya ya kiwanja cha ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kuna changamoto kadhaa, kwa wananchi wangu hawa 438 mpaka sasa bado hawajalipwa fidia. Je, yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kwenda Kilwa Masoko akiambatana nami ili kwenda kusikiliza kero za hawa wananchi wangu 438?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. DAVID M. KIHENZILE): Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kusini kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inayo dhamira ya dhati ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko. Pia, hiyo inakwenda sambamba na uwekezaji mkubwa unaofanyika pale wa kujenga bandari kubwa kwa ajili ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia kwamba mpango wa Serikali uko pale pale, mara baada ya wenzetu wa Wizara ya Fedha kukamilisha taratibu za ndani, fidia hiyo kwa wananchi hao itaanza kulipwa. Hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anauliza je, niko tayari kuambatana naye baada ya kumaliza Bunge hili. Amekiri mwenyewe nilikwenda pale pamoja na wenzangu nikiwa Mwenyekiti wa Kamati Kilimo na Mifugo. Vile vile, nimekwenda hapo juzi kukagua bandari hiyo na uwanja huo. Niko tayari kwenda pamoja naye ili tukawape uhakika wananchi hao ambao wanamwamini Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili waendelee kujenga imani naye.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa swali la nyongeza. Kumekuwa na mpango wa muda mrefu wa Serikali kujenga kiwanda cha mbolea kinachotokana na gesi asilia ya Songosongo pale Mjini Kilwa Masoko. Kauli ya mwisho ya Serikali ni kwamba iko kwenye mazungumzo na mwekezaji. Nataka kufahamu na wana-Kilwa pia wanataka kufahamu;

Je, mpango wa kujenga kiwanda cha mbolea Kilwa-Masoko bado uko pale pale au umesitishwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni sahihi kabisa moja ya mipango ya Serikali ni kuhakikisha tunajenga viwanda vingi vya kutosheleza mahitaji ya mbolea nchini. Ninyi ni mashahidi, tumeshaanza kujenga hicho cha Intracom hapa Dodoma lakini pia tunacho kile cha Minjingu ambacho kinaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki cha Kilwa-Masoko ni mahsusi kwa sababu hawa watatumia gesi asilia ambayo nayo ni muhimu sana kwa ajili ya kuzalisha mbolea ambazo zinahitajika hapa nchini. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kutafuta wawekezaji na kukamilisha mipango hiyo. Ujenzi wa kiwanda hiki cha mbolea katika eneo hili la Kilwa-Masoko utatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nipate faraja kidogo kwa majibu ya Serikali kwamba hatua iliyofikiwa sasa hivi ni kwamba tayari daftari lipo kwa Mthamini Mkuu Hazina kwa maana ya Wizara ya Fedha. Wananchi hawa wamekuwa wakiathirika kwa muda mrefu tangu 2013 walikuwa ni 144, ukafanyika tena uthamini 2023 wakafikia wananchi 438. Hivi tunavyozungumza wananchi wangu hawa 438, hawana makazi kutokana na kushindwa kuziendeleza nyumba zao kwa kusubiri taratibu za Serikali. Hali ni tete kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kutokana na ukweli kwamba tumeshakaa na Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Fedha na kukubaliana kwamba, wananchi hao walipwe haraka iwezekanavyo. Je, ni nini kauli ya Serikali kulipa wananchi hawa fidia ndani ya kipindi kifupi kijacho kabla hawajaendelea kuathirika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko ni moingoni mwa viwanja 12 ambavyo tuliviingiza katika mpango wa miaka mitano wa kuboresha na kupanua. Faraja tuliyonayo pale Kilwa Masoko tunajenga Bandari ya Uvuvi. Kufuatia ujenzi wa Bandari ya Uvuvi, umuhimu mkubwa wa kuimarisha kiwanja hiki upo na uhitaji mkubwa utahitajika huko mbele ya safari. Je, ni lini sasa Serikali baada ya kulipa wananchi wangu ndani ya muda mfupi, itaanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ally Kassinge kwa ufuatiliaji makini wa Kiwanja hiki cha Ndege. Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko. Moja, ameeleza vizuri sana, Serikali imewekeza bilioni 268 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kubwa katika Ukanda wetu wa East Africa, Bandari ya Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunao Mradi mkubwa sana wa Gesi wa Mkoa wa Lindi. Hivyo, kiwanja hiki ni muhimu sana siyo tu kwa wananchi wa Lindi na ukanda huo, lakini kwa Taifa letu. Hivyo nimhakikishie Mbunge kwamba, Serikali kauli yake imeshafanya uthamini hatua ya kwanza na ya pili na mpaka wamefika wananchi karibu 454 ambao tunategemea kuwalipa karibu 6,200,000,000. Naomba Mbunge apokee kauli ya Serikali ninayoenda kuitamka sasa. Serikali italipa fidia wananchi hao, mara tu itakapokamilisha hatua za ndani na itaanza hatua za ujenzi mara moja.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri mwenye pesa kasimama.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu kwa majibu yake mazuri, pia nimpongeze sana muuliza swali. Muuliza swali amehusisha Wizara ya Fedha. Ni kweli suala hili tunalitambua na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kule Kilwa, wawe na amani kabisa fedha hiyo italipwa kwa wakati. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Jimbo la Kilwa Kusini halina Chuo cha VETA na hakuna mpango wa Serikali kujenga Chuo cha VETA badala yake tuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, lakini miundombinu yake ni chakavu na haitoshelezi. Tuna upungufu wa bwalo, viwanja vya michezo pamoja na maabara ya kompyuta. Nini mpango wa Serikali wa kukiimarisha Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli anachozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba pale katika Jimbo la Kilwa Kusini tuna Chuo chetu cha FDC, tulifanya ukarabati kidogo, lakini bado kuna upungufu wa majengo haya aliyoyataja ikiwemo pamoja na bwalo. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Kassinge, katika mwaka ujao wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuongeza miundombinu au upanuzi wa vyuo hivi kikiwemo hiki chuo chako, lakini vilevile na chuo cha pale Kisarawe ambacho sasa hivi kinaendelea na ujenzi, pamoja na kule Kigamboni kwa Mheshimiwa Dkt. wa Kigamboni kule tunakwenda kuviongezea miundombinu hii ya majengo ili kuweza kudahili wanafunzi wengi, lakini kutengeneza mazingira mazuri na salama ya watoto wetu kuweza kusoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kutoa maji katika Mji wa Kilwa Masoko kupeleka Kilwa Kisiwani ambao ulitengewa shilingi bilioni 1.6, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa umekwama. Nini maelezo ya Serikali kuhakikisha kwamba wanatatua tatizo la mradi huu na hatimaye wananchi wa Kilwa Kisiwani wanapata maji kama ilivyotarajiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri, jana tulikuwa wote na Mheshimiwa Mbunge na tulijadili sana kuhusu huu mradi. Baada ya kukaa naye na kujadili kwa kina kuhusu mradi huu, nikachukua hatua ya kuwashirikisha wataalam, na hivi tunavyoongea, tayari RM ameshaanza kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi ambaye bado hajatekeleza mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunajiridhisha kama anadai ili tuone kama ameshaleta hati ya madai ili aweze kulipwa na mradi uweze kuendelea bila kuwa na changamoto yoyote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ni lini Mheshimiwa Waziri atatembelea Wilaya ya Kilwa kujionea barabara za TANROADS ambazo zimeharibika na mvua na hatimaye kuzipatia ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kutembelea barabara zote. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama tutapata nafasi muda wowote twende tukazitembelee hizo barabara, aidha mimi au Mheshimiwa Waziri mwenyewe, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Lihilimaliyao katika Jimbo la Kilwa Kusini ndiyo kata yenye changamoto ya ukosefu wa maji iliyokithiri zaidi. Hapa Bungeni uliahidi kwamba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali lako.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nauliza swali, lini Mheshimiwa Naibu Waziri atatekeleza ahadi ya kwenda Lihilimaliyao, Kilwa Kusini ili tukatatue changamoto ya maji katika kata hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea wito wa Mheshimiwa Mbunge na baada ya Bunge lako Tukufu kuahirishwa tutapanga ratiba kwa ajili ya kufika katika eneo hilo na kujionea hali halisi.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, suala hili nimelizungumza hapa Bungeni hii ni mara ya saba, ikiwa maswali ya msingi matatu, ya nyongeza mawili na nimechangia mara moja. Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anahitimisha Mpango na Bajeti wa mwaka 2024/2025 alizungumza masuala ya fidia kuwa yatakuwa kipaumbele. Mwaka wa fedha umeanza na hii ni robo ya kwanza: -

(a) Je, ni lini wananchi wangu hawa watalipwa fedha hizi kiasi cha shilingi bilioni 6.2?

(b) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili aambatane na mimi kwenda Kilwa Masoko ili tukakutane na wananchi wangu hawa tukawape majibu ya Serikali yenye matumaini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, mara tu baada ya Bunge niko tayari niongozane na Mheshimiwa Mbunge twende huko.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, kwamba ni lini; ni mwaka huu wa fedha 2024/2025.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, je, nini mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa haraka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili wakajenge Kituo cha Afya katika Kata ya Likawage?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya katika kata mbalimbali zikiwemo kata katika Jimbo na Wilaya ya Kilwa, lakini nafahamu kwamba, kuna uhitaji wa vituo vya afya katika kata ambazo pia, Mheshimiwa Mbunge amezitaja. Namhakikishia tu kwamba, Serikali inaendelea kujenga vituo hivi kwa awamu na mara fedha zikipatikana tutahakikisha pia, tunapeleka katika Kata hiyo ya Likawage ili tuweze kujenga hicho kituo cha afya. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotupa matarajio sisi Wanakilwa. Hata hivyo, kutokana na ukweli kwamba Kilwa Masoko ndipo ambapo Serikali yetu pendwa inajenga bandari ya uvuvi na kwa maana hiyo, barabara hii ya Nangurukuru – Kilwa Masoko imekuwa ikielemewa sana na uzito wa mzigo wa magari yanayopeleka material bandarini, je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya haraka kupata hizi fedha ili barabara hii iweze kutengenezwa na kuboreshwa kama ambavyo tuliomba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji hususan kipande cha Kiranjeranje – Makangaga tuliomba kujengewa kwa kiwango cha lami, lakini kwa hatua za awali angalau kujenga kwa kiwango cha changarawe ili magari yanayotoka Kiranjeranje kwenda Makangaga kufuata material ya gypsum yaweze kupita angalau kwa mazingira yaliyo mazuri. Je, Serikali imefikia hatua gani kuboresha barabara hii ya Kiranjeranje – Makangaga?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kassinge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Kilwa Masoko kuelekea bandarini, kama alivyosema Serikali inaendelea na ujenzi wa bandari pale Kilwa Masoko na ili bandari iweze kuwa na tija. lazima barabara hii iweze kutengenezwa. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati Serikali inaenda kukamilisha bandari, sambamba na hilo Serikali imeweka kwenye kipaumbele barabara hii ili iweze kuboreshwa kwa kujengwa upya ili iweze kuendana na uwekezaji mkubwa ambao umewekwa pale. Ujenzi wa bandari utaenda sambamba na kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa kadri tutakavyopata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kuhusu Kiranjeranje – Nanjilinji, natumia nafasi hii kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa ambayo ilipata madhara makubwa ya mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya, lakini kwa kazi nzuri ambayo Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Lindi na ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia, na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ameshatupatia shilingi bilioni 140 kwa ajili ya kwenda kurudisha miundombinu ya barabara ambayo iliharibiwa ndani ya Mkoa wa Lindi na barabara hii ikiwemo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uwezeshaji huo. Waheshimiwa Wabunge kutoka mkoa huu mnafahamu tayari nimeshakabidhi wakandarasi ndani ya Mkoa wa Lindi ili kazi iweze kuanza. Natumia nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi kutembelea hii Barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji kuhakikisha inatengenezwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika misimu yote kama Mheshimiwa Mbunge alivyoomba, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukweli kwamba Watumishi wa Umma Kada ya Ualimu ndiyo kada pekee ambayo hainufaiki na aina yoyote ya allowance. Hawana extra duty allowance, hawana sitting allowance, hawana acting allowance na aina nyingine ya allowance. Kwa dhamira hiyo njema ya Serikali; je, Serikali ipo tayari sasa kufikiria kukaa ili kutoa teaching allowance kwa walimu? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo mazuri yanayotolewa na Mheshimiwa Mbunge kwetu sisi Serikali ni kupokea, kuchukua na kwenda kuangalia kwa sababu unapozungumzia allowance yoyote ile jambo kubwa au kigezo kikubwa ni uwezo wa kipato wa kibajeti ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tutaendelea kuangalia haya mawazo mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge. Kama uwezo wa kuweka allowance hizi utakuwepo tutaendelea kuangalia. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na hasa kundi kubwa analolisemea la walimu, Serikali imeendelea kuwaangalia walimu katika maslahi mengi sana yakiwemo maslahi ya kuhakikisha walimu wanaendelea kupunguziwa mzigo wa masomo kwa kuongeza namba kubwa ya walimu ambapo katika mwaka huu wa bajeti watakuja kueleza hapa wenzetu jinsi ambavyo Serikali inaendelea kuongeza namba ya walimu. Pia, kuendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kuwapa motisha nzuri ili waendelee kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kulihakikishia Bunge lako na Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo. Tutalichukua na tutaendelea kufanyia kazi kwa uwezo wa kibajeti.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali yanayoleta matarajio kwamba, barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami huku Serikali ikitafuta fedha, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ya kilometa 120 Kiranjeranje mpaka Ruangwa, Jimboni kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, inapitiwa na mito mitatu na Madaraja matatu ya Kigombo, Nakiu pamoja na Mto Mbwemkuru. Mito hii imeharibika na kwa hivyo, hakuna mawasiliano kati ya Kilwa na Ruangwa, jirani zetu. Ni nini mpango wa haraka wa Serikali kurudisha mawasiliano kwa kujenga Daraja la Mto Mbwemkuru ili tuweze kupata mawasiliano hayo pamoja na huduma za kijamii na za kiuchumi ziendelee? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kilometa 17 kutoka Kiranjeranje mpaka Makangaga ni sehemu ambayo ina tija sana ya kiuchumi kwani ndio sehemu ambayo yanapatikana mawe ya gypsum kwa kiwango kikubwa sana hapa nchini. Ujenzi wa barabara hii ni wa kokoto zisizokuwa rafiki kwa magari yanayokwenda kuchukua madini haya ya gypsum. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba, kilometa 17 hizi tunafanya maandalizi ya awali ya kujenga kwa kiwango cha lami, lakini tunaweka kifusi ambacho ni rafiki kwa wapitaji wa maeneo haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kweli tunatambua eneo hilo ni muhimu sana sasa hivi katika biashara ya viwanda na hasa cement, ambapo gypsum inatoka eneo hilo. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumekusikia na naamini Mtendaji Mkuu wa TANROADS pamoja na Manager wa Mkoa wa Lindi, hizi kilomita saba waende wakaone namna ya kufanya kuweka kifusi rafiki wakati Serikali inatafuta fedha ya kujenga eneo hilo aidha, kwa zege ama kwa kiwango cha lami, ili kutokukwamisha biashara kubwa ambayo najua tunatoa material ya muhimu sana katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, natambua kwamba, hakuna mawasiliano kati ya Kilwa na Ruangwa kwa sababu ya hiyo mito mitatu na ninajua kwamba, mpaka mto ambao wanapakana Mbunge na Jimbo la Mheshimiwa Waziri Mkuu hawawezi wakawasiliana. Mpango uliopo wa Serikali, moja ni kwamba, tayari tumeshatafuta fedha, kwa ajili ya kujenga Mto wa Mbwemkuru ambao hauwezi ukajengwa kirahisi kutokana na mvua iliyonyesha. Tayari fedha inatafutwa na Serikali kwa sababu, bado maji yapo mengi na hawawezi kuvuka, tunalitambua hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fedha ambayo Serikali inatafuta, kwa ajili ya kurejesha miundombinu ni pamoja na hayo madaraja matatu ambayo Mkoa wa Lindi ndio ulioathirika kuliko Mikoa mingine yote katika Tanzania. Kwa hiyo, macho ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, inatafuta fedha na ninakuhakikishia yapo maelekezo mahususi kwa TANROADS, kwa maana ya Wizara, kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba, madaraja yote kwanza yatakuwa ni kipaumbele kuyajenga yawe ya kudumu ili tuweze kurejesha mawasiliano. Ahsante. (Makofi)