Primary Questions from Hon. Amina Ali Mzee (7 total)
MHE. AMINA ALI MZEE Aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhamasisha vijana nchini kujiunga na biashara mtandao?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbali mbali katika kuweka mazingira wezeshi nchini ya kuvutia wananchi wengi kujiunga na biashara mtandao hususan vijana. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala ya kielektroniki inayofanyika kimtandao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inapitia Sheria na tozo mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa vijana, wabunifu wa TEHAMA na wale wanaochipukia (start-ups) ili kuweka mazingira wezeshi ya vijana kushiriki kwenye biashara mtandao. Hii hatua inakwenda sambamba na maboresho yanayoendelea ya kupunguza tozo za leseni za maudhui mtandaoni, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania imeanzisha jukwaa la kutangaza na kuuza bidhaa na huduma kwa njia ya mtandao ambapo maduka 270 ya kuuza na kununua bidhaa yamesajiliwa na jukwaa hili ambalo linapatikana kupitia tovuti https://www.postashoptz.post. Jukwaa hili limeunganishwa na mtandao wa vituo 670,000 duniani. Jukwaa hili linatoa fursa kwa wafanyabishara ikiwemo vijana kutumia mtandao huo kufanya biashara mtandao kwa kuunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma ulimwenguni. Ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -
Je, Serikali inatumiaje Chuo cha Bahari cha DMI kuendeleza vijana wa Kitanzania ili kukabiliana na changamoto za ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P. KATAMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ni Chuo cha Serikali ambacho kimeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 1991 Chuo kinatoa elimu na mafunzo katika sekta ya usafiri wa njia ya maji na hivyo kina mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za ajira, Chuo cha DMI kina kitengo maalum cha uwakala wa ajira za mabaharia (DMI Crewing Agency). Kitengo hiki kilianza kazi mwaka 2018. Kina usajili Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ajili ya kutafuta ajira na mafunzo melini kwa vijana wa Tanzania kwa meli za ndani na nje ya nchi yetu hususan kwenye mashirika mbalimbali ya meli ikiwemo Azam Maritime, Zan Fast Ferry, TPA Kyera, Greece Marine Company na Verba Shipping Company.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wahitimu wa Chuo cha DMI na mabaharia wa Tanzania kupata ajira katika meli za Kimataifa, Serikali inaendelea na taratibu za kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kusimamia masuala ya Bahari duniani (IMO Convention
– Maritime Labour Convention). Kuridhiwa kwa mkataba huu, kutawezesha kutoa mafunzo na ajira kwa mabaharia takriban 150 ambao ni sawa na 25% ya wahitimu kwa mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASYA SHARIF OMAR K.n.y. MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa madarasa na mabweni ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) Mabibo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP), mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, imeanza ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500. Ujenzi wa mabweni hayo umefikia asilimia 28. Aidha, kupitia mradi huo Serikali inajenga jengo lenye Madarasa ya wanafunzi 1,500 pamoja na maabara na karakana yenye kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 30.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Rasilimali Mafunzo (maktaba) chenye madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,653 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo kwa sasa upo kwenye asilimia 85.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Chuo, itaanza ujenzi wa Jengo la Kitaaluma la ghorofa tano litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,700 kwa siku, mara litakapokamilika.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-
Je, ni lini Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa utapelekwa katika Wilaya 14 ikiwemo za Mjini Magharibi na Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar imefikisha huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar. Mjini Magharibi inapata huduma kupitia vituo vilivyopo maeneo ya Jamhuri Garden, Fumba na Ofisi za Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) na Kusini Unguja inapata huduma kupitia kituo kilichopo Paje.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya Wilaya 43 nchini zimefikiwa na Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya Wilaya mpya 23 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 66 nchini zenye huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuwa Wilaya zote nchini zitafikiwa na huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ifikapo mwaka 2025. Mwaka wa fedha 2022/2023 Wilaya zingine mpya 15 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 81. Wilaya zinazobaki zitafikishiwa huduma za Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kwa kipindi kinachobaki kufikia 2025 kama ilivyopangwa. Ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuliwezesha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kujiendesha kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatekeleza majukumu yake kikamilifu kama chombo cha utangazaji cha umma. Serikali ipo katika mkakati wa kukamilisha utungaji wa Sheria ya TBC ya mwaka 2023, itakayowezesha kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato. Aidha, TBC inazo chaneli za kimkakati kwa ajili ya kuongeza mapato ikiwemo TBC2, TBC Online, TBC FM na Radio za Jamii Dodoma na Arusha, ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia ajira ya kudumu vijana ambao wanatumika kama vibarua kwenye ujenzi wa Reli nchini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu inaonyesha kuwa, toka kuanza kwa ujenzi wa mradi wa Standard Gauge mwaka 2017 hadi kufikia Desemba 2023 jumla ya vijana wa Kitanzania 51,153 wameshiriki katika ujenzi wa mradi wa SGR.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998, ajira katika Utumishi wa Umma uzingatia sifa na weledi (merits) na hutolewa kwa ushindani wa wazi. Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa vijana wanaoshiriki katika mradi wa ujenzi wa SGR wanapata ujuzi mahsusi katika teknolojia ya reli ya kisasa ambayo itahitajika katika kuhakikisha uendelevu wa reli tunayoijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumtaarifu Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge, kuwa kwa kuzingatia mahitaji ya uendeshaji wa reli, vijana hawa watapewa kipaumbele kwa kuwa na sifa za ziada (added advantage) zinazohusiana na ujuzi waliopata kwa kushiriki katika ujenzi wa reli pindi ajira hizo zitakapotangazwa.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza wimbi la vijana wanaomaliza masomo na kukosa kazi kutokana na sharti la vigezo vya uzoefu wa miaka miwili na zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwezesha vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuwa na uzoefu wa kazi pamoja na sifa nyingine za kujiajiri ndani na nje ya nchi, Serikali inaendelea na programu mbalimbali za mafunzo ya uzoefu wa kazi ikiwemo internship na maboresho ya Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo inahimiza uwepo wa mfumo endelevu wa kuwajengea vijana ujuzi na stadi mbalimbali ili waweze kuajirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninaomba kutoa wito kwa wahitimu kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia programu za elimu, mafunzo na uwezeshaji wa kiuchumi kwa kutoa mikopo na mitaji, fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi katika miradi ya Serikali inayopatikana katika Wizara za Kisekta na Sekta Binafsi.