Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Asya Sharif Omar (9 total)

MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya usafiri katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022 Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba umepatiwa magari matatu yaliyonunuliwa na Serikali ili kupunguza uhaba wa magari katika Mkoa huo. Serikali itaendelea kununua magari na pikipiki kila mwaka na kuzigawa katika Mikoa na Wilaya zenye uhitaji mkubwa ikiwemo Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba. Nashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati katika Kituo cha Polisi Matangatuani Wilayani ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Matangatuani kilichopo Wilaya ya Micheweni ni kituo kilichojengwa siku nyingi na jengo lake ni chakavu. Katika tathmini iliyofanyika jengo hilo halifai kufanyiwa ukarabati kutokana na udhaifu wa kuta za jengo hilo. Serikali ina mpango wa kujenga Kituo kipya cha Polisi cha daraja "C". Michoro na makadirio yameshafanyika na kiasi cha Shilingi 427,604,929 kinahitajika kwa ajili ya kujenga Jengo la Kituo pamoja na nyumba mbili za makazi ya Askari. Fedha za ujenzi zinatarajiwa kuombwa kwenye Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kutegemea na upatikanaji wa fedha.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuongeza viwanda vya kusindika ngozi za mbuzi na ng’ombe?

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa uwekezaji katika sekta ya ngozi unaongezeka. Mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi lakini Vilevile, Serikali katika kuhakikisha inavutia na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya ngozi, imehakikisha viwanda vya ngozi vya ndani vinapata malighafi za kutosha hapa nchini kwa kuongeza ushuru kwa ngozi zinazouzwa nje ya nchi. Mfano, asilimia 80 kwa ngozi ghafi na asilimia 10 kwa ngozi iliyoongezwa thamani hadi kufikia kuwa ya “wet blue”. Aidha, Serikali imekuwa ikitoa vivutio mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuvutia uwekezaji kama vile kusamehe kodi kwa mitambo inayoingizwa kutoka nje ya nchi kwa lengo la kusindika na kuzalisha ngozi na bidhaa za ngozi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya ngozi kwa kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini kupitia MKUMBI. Ninakushukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza nyumba za makazi kwa Askari Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba moja ya kuishi familia nne za askari katika eneo la Finya, Wilaya ya Wete. Mradi unaoendelea sasa ni ujenzi wa hanga la kuishi familia 18 za askari kwenye Kituo cha Polisi Micheweni. Ujenzi huo umefikia hatua ya kumalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh.270,121,580 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za kuishi familia nne za askari Polisi eneo la Konde Wilaya ya Micheweni. Utaratibu wa kujenga nyumba za makazi ya askari ni endelevu na utakuwa ukifanyika kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kutoa mafunzo ya kuogelea kwa wakulima wa Mwani Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa zao la mwani katika kuongeza kipato, ajira na kukuza uchumi katika ukanda wa pwani na Taifa kwa ujumla. Vilevile, inatambua kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wakulima wa mwani ni wanawake. Ili kuwa na kilimo endelevu na kulinda usalama wa wakulima wa mwani wawapo katika shughuli zao, ni muhimu wakulima hawa kuwa na ujuzi wa kuogelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa na mikakati mbalimbali kuhakikisha wakulima wa mwani wanapatiwa nyenzo bora za kuhakikisha usalama mahali pa kazi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitatoa mafunzo ya kuogelea kwa wakulima wa mwani pamoja na kununua na kusambaza vifaa vya kulinda usalama wakiwa kwenye maji wakishughulika na kilimo cha mwani.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa huduma ya kifungua kinywa kwa wanafunzi wa shule za msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma ya chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni wakati wa masomo katika kupunguza utoro, kuongeza usikivu na kuboresha afya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa wanafunzi Elimumsingi unaoelezea taratibu za mifumo ya uchangiaji wa huduma ya chakula shuleni. Aidha, Serikali iliwaelekeza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri kusimamia mwongozo wa Lishe wa Mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii, kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuona namna bora ya utekelezaji wa mwongozo wa lishe na kuwawezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati nyumba za makazi ya Polisi zilizopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 100,000,000 kutoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa ajili ya kufanya ukarabati nyumba ya makazi ya Askari Polisi ya familia 12. Aidha, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba nane za makazi ya kuishi familia 32 za askari Polisi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 416,000,000 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ukarabati zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali na Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati nyumba za makazi ya Polisi zilizopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 100,000,000 kutoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa ajili ya kufanya ukarabati nyumba ya makazi ya Askari Polisi ya familia 12. Aidha, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba nane za makazi ya kuishi familia 32 za askari Polisi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 416,000,000 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ukarabati zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali na Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru vyanzo vya maji dhidi ya shughuli za kibinadamu?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea na Programu Maalum ya Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji iliyoanza mwaka 2021 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2035. Utekelezaji wa programu hiyo unashirikisha sekta zinazohusiana na maji pamoja na taasisi zake ambapo utekelezaji wake unafanyika kupitia Timu ya Kisekta ya Kitaifa iliyoundwa kwa kujumuisha sekta za maji, kilimo, mifugo, maliasili na mazingira.

Mheshimiwa Spika, kupitia programu hiyo, kazi mbalimbali za uhifadhi wa vyanzo vya maji zinatekelezwa ikiwemo kutambua vyanzo vya maji, kuweka mipaka na kuvitangaza vyanzo hivyo kwenye Gazeti la Serikali, kupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji na kufanya kilimo na ufugaji rafiki wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya vyanzo 3,285 vimetambuliwa ambapo kati ya hivyo, 317 vimewekewa mipaka na vyanzo 61 vimetangazwa katika Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu. Aidha, jumla ya miti rafiki 5,381,548 imepandwa katika vyanzo vya maji mbalimbali nchini.