Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asya Sharif Omar (7 total)

MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza na kwanza naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Lakini nataka kuuliza, je, kuna mkakati gani mahususi la kuongeza suala hili la usafiri katika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa sababu bado changamoto ni kubwa na hasa ukizingatia na vituo vidogo ambavyo vina mahitaji makubwa ya usafiri ikiwemo Kituo cha Mchangamdogo, lakini pia Kituo cha Mapana Kifuani ambacho nimekuzungumzia juzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Asya Sharif Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, hivi sasa wamegaiwa magari matatu, tutaendelea kuwapatia magari ili wamudu kutekeleza majukumu ya ulinzi, usalama wa raia mali zao kadri tutakavyopata bajeti na kama anavyofahamu Mheshimiwa mwaka huu tumepitishiwa bajeti ya shilingi bilioni 15, yakanunuliwa magari, miongoni mwa maeneo yatakayopata magari ni pamoja na mikoa ya Pemba. Nashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini bado naona iko haja ya Mheshimiwa Naibu Waziri kulipa kipaumbele suala la kwenda kukiona kituo kile kwa sababu Askari wale wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda katika eneo hilo la Kituo cha Polisi cha Matangatuani ili kuweza kutoa msukumo zaidi katika bajeti hiyo 2023/2024 kufanikisha ujenzi huo wa kituo kipya lakini pia na nyumba za makazi ya Askari Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ambayo kwa kweli yanakaribia kufanana ya Mheshimiwa Asya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba eneo hilo halina Kituo cha Polisi lakini jambo kutia moyo wananchi hawa tayari wametenga eneo la kutosha kujenga kituo na nyumba za watumishi upande wa Polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaahidi kwamba niko tayari kukitembelea ili kuona kiasi gani kinahitajika na pia kuweka msukumo ili jengo hilo likamilishwe kwa haraka baada ya kutolewa kwa fedha hizi. Kwa hiyo, kuongozana naye wala halina tatizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini pia nina swali la nyongeza kwamba, wana mkakati gani wa kuwachukulia hatua wale wananchi ambao wanaharibu kwa makusudi miundombinu ya maji tukizingatia mahitaji ni makubwa ya wananchi mjini na vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tauhida ambalo limeulizwa kwa niaba yake: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee pongezi lakini mkakati ambao tunaendelea nao ni kuchukua sheria. Sheria ziko bayana, kwa hiyo yoyote ambaye atakutwa sheria itafuata mkondo wake.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bado mahitaji ni makubwa ya wananchi hao wajasiriamali ambao wanajishughulisha na biashara ya ngozi ya mbuzi na ng’ombe, hasa tukizingatia kwamba wananchi wengi wana mahitaji makubwa lakini tunanunua nje. Kwa mfano, mikoba ya kike ambayo ni hand bag, viatu pia mikanda ya akina Baba.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza nguvu ya viwanda ili vifaa hivi sasa viwe vina ubora katika nchi yetu?

Swali la pili, pamoja na kuwa umesema mnatafuta uwekezaji labda mtuambie Serikali viwanda vingapi ambavyo kwa sasa vipo, katika nchi yetu vinavyojishughulisha na usindikaji wa ngozi ya mbuzi na ng’ombe?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asya Sharif, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mahitaji ya ngozi ambazo zipo katika hatua ya mwisho kwa maana finished leather kwa ajili ya bidhaa za ngozi ikiwemo mikoba na viatu bado ni changamoto katika viwanda vyetu vya ndani. Moja ya mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunawahamasisha kwanza wafugaji kuzalisha ngozi zinazokidhi mahitahji, ikiwa ni pamoja na kuchunga mifugo yetu katika hali nzuri, ikiwa ni pamoja na kutokupiga chapa kuharibu ngozi, pia kupiga fimbo au viboko, mbuzi na kondoo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili tunahamasisha uwekezaji katika viwanda hivi ambavyo vitatumia malighafi yetu kuzalisha bidhaa za ngozi kwa maana ya ngozi hadi mwisho (finished leather) kwa hiyo ni moja ya mikakati ambayo Seriakli inaendelea kufanya, katika kuhakikisha tunakuwa na ngozi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na takwimu, tutamletea takwimu sahihi ya viwanda kwa sababu bado tunaendelea kuhamasisha na kuna viwanda vingi vidogo ambavyo vinaendelea kuzalisha bidhaa za ngozi katika nchi yetu, vikitumia ngozi kutoka ndani ya nchi lakini nyingine kutoka nje ya nchi. Ninakushukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na maelezo yake nataka kujua ni lini ujenzi huo utaanza katika maeneo hayo ya Finya, Micheweni na Konde? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; naomba kujua Serikali imejipangaje kuhusu kuchimba visima katika maeneo hayo ambayo yatajenga hizo nyumba kwa sababu kama tunavyofahamu maeneo hayo yana uhaba wa maji. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini ujenzi utaanza kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ujenzi unaendelea kwenye maeneo tofauti. Kwa mfano, eneo la Finya kuna nyumba nne zinaendelea kujengwa na ziko kwenye hatua ya umaliziaji. Kuhusu uhaba wa maji tutashirikiana na mamlaka ya utoaji wa huduma za maji katika Wilaya ya Micheweni ili ishiriki kwa sababu si kazi ya polisi ku-supply maji, lakini pale tunapokuwa na uwezesho wa kifedha tunachimba visima vya maji, lakini kwa sasa bajeti tuliyotenga ni kwa ajili ya ujenzi wa vituo na makazi ya askari, nashukuru. (Makofi)
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Serikali nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa chuo hichi cha usafirishaji kuongeza wanafunzi wa kigeni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Usafirishaji ambacho kiko pale Dar es Salaam kina wanafunzi 14,464 na katika wanafunzi hao asilimia 99.2 ni wanafunzi wa Kitanzania na asilimia 0.8 ni wanafunzi wa nje.

Mheshimiwa Spika, chuo kimeendelea na programu mbalimbali za kuhakikisha kinaongeza wanafunzi wengi kama ambavyo imeulizwa na Mheshimiwa Mbunge ikiwa ni kwa ajili ya kuhakikisha tunaongeza forex, lakini pia kwa ajili ya kuongeza experience kwa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Spika, programu mbalimbali zimefanyika katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Balozi zetu za nje kukitangaza chuo chetu kimataifa. Vile vile tumeshiriki katika mikutano mbalimbali mingine imefanyika Nchini Rwanda kwa ajili ya kuongeza na kutangaza chuo chetu.

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi, chuo chetu kwa sasa kinaandaa mkutano mkubwa tarehe 18 mpaka tarehe 20 mwezi ujao ambao ni First International Conference on Transport and Logistics and Management ili kuleta wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kwamba pengine tunaweza kujitangaza zaidi na kupata wanafunzi wengi zaidi, ahsante.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri lakini bado kuna mahitaji makubwa ya kupata makazi ya kudumu katika maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ili kuondosha usumbufu. Swali la kwanza; ningependa kujua, je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuandaa makazi kwa askari wetu hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza maeneo ya makazi katika Wilaya ya Wete ili kuondosha askari wetu kupanga nyumba za mitaani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asya Sharif, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, kwamba kuna mahitaji makubwa ya makazi, ni kweli na sisi kama Serikali tunatambua kuwa kuna mahitaji makubwa ya makazi ya askari wetu. Tunatenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga makazi ya askari wetu ili wafanye kazi ya kulinda wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la maeneo ya makazi, Serikali itafanya tathmini katika maeneo yote ya Pemba na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari yatatengewa bajeti katika miaka inayokuja ya fedha, 2025/2026 na miaka inayoendelea. Ahsante.