Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Assa Nelson Makanika (7 total)

MHE. ASSA N. MAKANIKA Aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwekeza yenyewe katika zao la Mchikichi badala ya kuziachia Halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa mafuta nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makanika, Mbunge wa Jimbo Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2020/2021, Serikali imewekeza Jumla ya Sh.5,820,361,798 kwa ajili ya kuendeleza zao la mchikichi ambapo hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2021 jumla ya miche bora ya michikichi 2,244,935 imezalishwa na jumla ya miche 1,456,111 imesambazwa kwa wakulima katika Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kigoma na miche 788,824 inatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa 2020/2021. Aidha, katika mwaka 2021/2022, Serikali imetenga jumla ya Sh.3,158,200,000 kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza mbegu na miche ya zao la michikichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya mafuta ya kula yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka ambapo hupelekea kama nchi kutumia wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa mazao mengine, Serikali hwekeza katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, udhibiti wa visumbufu vya mazao na utafutaji wa masoko. Aidha, katika utekelezaji wa mikakati hiyo Serikali imekuwa ikishirikiana wdau mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama sehemu ya mkakati wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula, mwaka 2018, Serikali iliamua kuanzisha Kituo Maalum cha Utafiti wa Zao la Michikichi cha TARI Kihinga, Mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi zaidi. TARI Kihinga ikishirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), halmashauri na sekta binafsi katika utafiti, uzalishaji wa miche bora ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kuendeleza zao la mchikichi na mazao mengine ya mbegu za ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinashauriwa kuwekeza katika mazao ya kilimo kutokana na mapato yanayotokana na ushuru wa mazao (produce cess) likiwemo zao la michikichi.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA K.n.y. MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Kigoma ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa kuitwa wakimbizi nchini mwao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupita Idara ya Uhamiaji imepewa jukumu la kudhibiti, kusimamia na kufuatilia uingiaji, ukaaji na utokaji wa wageni hapa nchini kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 rejeo la mwaka 2016.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza jukumu hilo, Idara ya Uhamiaji imekuwa ikifanya operesheni, doria na misako mbalimbali kwa lengo la kuwabaini wageni wanaoingia na kuishi nchini kinyume cha sheria na taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya mahojiano na uchunguzi wa kina ili kujiridhisha juu ya uraia wa watuhumiwa wanaokamatwa wakati wa operesheni husika na kwamba Idara ya Uhamiaji katika kushughulikia masuala ya uraia huzingatia matakwa ya Sheria ya Uraia Sura ya 357 rejeo la mwaka 2002. Operesheni, doria na misako hufanyika kwa mikoa yote na siyo Mkoa wa Kigoma pekee. Nakushukuru.
MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kurekebisha vifungashio vya mafuta ya mawese kwa kuwa wananchi wanaumizwa na kunyonywa kupitia vifungashio vinavyotumika sasa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo, Mkoa wa Kigoma limeshatengeneza sampuli za vifungashio vya mafuta ya mawese vitakavyotumiwa na wakulima. Kwa kuanzia SIDO imetengeneza sampuli za vifungashio hivyo vya lita tano na lita ishirini. Vifungashio hivyo viko katika mfumo wa ndoo ya chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua inayofuata ni sampuli hizo za vifungashio kuwasilishwa kwa Wakala wa Vipimo kwa ajili ya uhakiki wa ujazo huo. Aidha, baada ya Wakala wa Vipimo kuhakiki vifungashio hivyo, itawasilisha sampuli hizo za vifungashio kwa SIDO ili viweze kuzalishwa kwa wingi kwa maana ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshatoa maagizo kwa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Wakala wa Vipimo kuharakisha zoezi hilo la urekebishaji wa vifungashio hivyo ili wakulima wa mawese Kigoma wasiendelee kunyonywa. Aidha, SIDO wataanza kuzalisha kwa wingi vifungashio hivyo na kuviuza kwa bei nafuu kwa wazalishaji wa mafuta ya mawese nchini ili kutekeleza kwa vitendo agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alilolitoa wakati alipokuwa katika ziara yake Mkoani Kigoma mwezi Februari, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y. MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mwandiga – Chankele – Mwamgongo hadi Kagunga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mwandinga – Chankele- Mwamgongo hadi Kagunga yenye urefu wa kilometa 65 ni barabara ya wilaya. TANROADS wanaendelea kuifungua kutoka njia panda ya Chankele hadi Kagunga kilometa 47 na tayari kilometa nane zimeshafunguliwa.

Mheshimshiwa Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 1.85 kuendelea kuifungua barabara hii kwa kiwango cha changarawe. Baada ya kuifungua barabara yote, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Manyovu Mkoani Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwandiga – Manyovu yenye urefu wa kilometa 53 ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami mwezi Agosti, 2008 na kukamilika mwezi Oktoba, 2010. Wakati wa ujenzi wa barabara hii Wananchi wote waliostahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria kutokana na mali zao kuathirika na ujenzi huo walilipwa fidia. Ahsante.
MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Kigoma vijijini katika kukabiliana na Ugonjwa wa Mnyauko unaoharibu migomba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya utambuzi na udhibiti wa ugonjwa huo kwa maafisa ugani, ambapo hadi Juni, 2022 mafunzo kwa maafisa ugani 76 wa Halmashauri ya Buhigwe yametolewa, ili kuwafundisha wakulima mbinu za udhibiti ikiwemo matumizi ya miche bora ya migomba yenye ukinzani wa ugonjwa huo ambayo nitaliban 1, Taliban 2, Taliban 3, Taliban 4 na FHIA 23, William 5).

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tayari wakulima wamepatiwa miche bora 100 ili kuanza uzalishaji wa miche bora ya kupanda mashambani na kazi hiyo ni endelevu. Vilevile, wakulima wameshauriwa kung’oa migomba yote iliyoathirika na Banana Xanthomonas Wilt. Aidha, tunaendelea kusimamia Sheria ya karantini kwa Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine nchini ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
MHE. KAVEJURU E. FELIX K.n.y. MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -

Je, nini mpango wa fidia kwa wananchi walioguswa na ujenzi wa Barabara ya Kigoma -Kasulu ambao nyumba zao zimewekewa X?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI aljibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009 iliongeza upana wa eneo la hifadhi ya barabara kuu na za mkoa kutoka meta 45 hadi 60 ikiwa na nyongeza ya meta 7.5 kutoka katikati ya barabara kila upande. Kufuatia utekelezaji wa sheria hii, alama ya “X” yenye rangi ya kijani iliwekwa kwenye nyumba zote za wananchi zilizopo katika eneo hii ikiwa na maana kuwa wananchi hao waendelee kuwepo katika eneo hilo hadi watakapolipwa fidia, ahsante.