Answers to Primary Questions by Hon. Innocent Lugha Bashungwa (36 total)
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiwapangia wakulima wa pamba bei ndogo wakati wa mavuno bila kuzingatia gharama kubwa walizotumia kipindi cha uzalishaji:-
Je, Serikali haioni sasa wakati umefika kuwaacha wakulima wauze pamba kwa bei kubwa wanayotaka wao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge, kwa ridhaa yako, naomba nitumie nafasi hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu ya kuweza kusimama hapa.
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kipekee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na wasaidizi wake kwa kuniamini na kuniteua katika hii nafasi ya Naibu Waziri wa Kilimo. Namuahidi Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake, nitafanya kazi kwa uadilifu na kwa maarifa yangu yote katika kutekeleza majukumu ambayo wamenikabidhi.
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kukushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa support yenu mpaka nikaweza kufika hapa. Ninawaahidi ushirikiano na naamini mtanipa ushirikiano katika kutimiza majukumu yangu. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu wananchi wa Karagwe.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali haiwapangii wakulima bei ya kuuza pamba bali huratibu upatikanaji wa bei nzuri ya pamba kwa wakulima. Sheria ya Pamba Na.2 ya mwaka 2001 inaipa Serikali kupitia Bodi ya Pamba jukumu la kukaa na wawakilishi wa wakulima na kampuni za kununua pamba kukubaliana bei elekezi ambayo inazingatia gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, kwa wastani gharama za uzalishaji wa ekari ya pamba inakadiriwa kuwa Sh.488,000.
Ekari moja iliyotunzwa vizuri hutoa wastani wa kilo 1,000 sawa na kuzalisha kilo moja kwa Sh.488. Bei iliyopangwa na wadau wa pamba yaani bei elekezi ya msimu wa mwaka 2018/2019 ilikuwa Sh.1,100 ambapo kwa mkulima aliyezalisha kwa tija ya kilo 1,000 kwa ekari na kuuza kwa bei hiyo hakuuza chini ya gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, wakulima wa pamba ni wadau muhimu katika kupanga bei ya pamba kwa kila msimu. Serikali inatambua umuhimu huo, hivyo imefanya maboresho katika mfumo wa uuzaji kwa kufufua na kuimarisha vyama vya ushirika kwa lengo la kuongeza fursa ya wakulima kushiriki katika soko kupitia ushirika wao. Upangaji wa bei ya pamba huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo bei ya pamba nyuzi katika soko la dunia, kiwango cha kubadilishia fedha, bei ya mbegu za pamba, gharama za usafirishaji, uchambuaji na uwiano kati ya nyuzi na mbegu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika mwezi Septemba, 2018, baadhi ya wakulima wa Mkoa wa Simiyu waliuza pamba kwa Sh.1,200 kwa kilo juu ya bei elekezi kutokana na mabadiliko ya bei ya pamba katika soko la dunia.
Mheshimiwa Spika, fursa ya wakulima wa pamba kuuza bei wanayotaka itaongezeka kwa kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya pamba hasa kuongeza viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini. Aidha, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa wakulima ili kuongeza tija katika zao la pamba na hatimaye kuongeza uzalishaji na pato la mkulima mmoja mmoja.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Kwa kuwa msimu wa pamba wa mwaka 2018/2019 ulikuwa na bei elekezi ndogo ya Sh.1,100 na kwa kuwa mara nyingi bei hizo elekezi zinapendekezwa kwa msukumo wa bei ya pamba duniani:-
(a) Je, Serikali katika msimu wa mwaka 2019/2020 ina mkakati gani wa kuinua bei ya wakulima kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500?
(b) Kwa kuwa kuna Vyama vya Ushirika na Benki ya Wakulima, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la usambazaji wa mbegu za pamba katika Wilaya ya Bunda na hasa Jimbo la Bunda ambapo kila mwaka kunakuwa na uhaba wa mbegu na kutofika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, bei za mazao na bidhaa mbalimbali hutegemea nguvu ya soko kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji (supply), mahitaji (demand), ubora na viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na nje na ushindani uliopo katika masoko husika.
Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa bei ya pamba kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500 katika msimu wa ununuzi wa 2019/2020 kutategemea nguvu za soko hususani kupanda kwa bei ya pamba katika soko la dunia. Aidha, pamoja na kutegemea nguvu ya soko la dunia, Serikali inatekeleza mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo ili kuimarisha soko la ndani na ushindani.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za pamba nchini, ambapo katika msimu wa mwaka 2018/2019 jumla ya tani 27,851 zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima ikilinganishwa na tani 20,496 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 36. Aidha, kati ya mbegu zilizozalishwa mwaka 2018/2019, tani 1,075 zimesambazwa katika Wilaya ya Bunda ikilinganishwa na tani 688 zilizotumika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 56.
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inahudumia sekta ya kilimo kwa ujumla wake kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ukilinganisha na benki zingine. Aidha, Benki ya Kilimo inatarajia kushiriki katika ununuzi wa pamba sambaba na benki nyingine zilizopo nchini kwa kutoa mikopo kwa kampuni zitakazoshiriki katika ununuzi wa pamba kama ilivyofanyika msimu wa ununuzi wa mwaka 2018/2019.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:-
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Olenasha alitembelea Wilaya ya Siha kufuatilia ubadhirifu kwenye Shamba la Ganrangua na SACCOS ya Sanya Juu wa shilingi milioni 337 na Siha Kiyeyu shilingi milioni 840 ambapo aliiagiza TAKUKURU kuchunguza ubadhirifu huo:-
(a) Je, Serikali iko tayari kufanya upembuzi na kutambua mashamba ya umma, yasiyotumika vizuri na kurejesha kwa wananchi kwa kutumia vijiji na ushirika wao kama wazo la kwanza la Baba wa Taifa J. K. Nyerere, mfano wa baadhi ya mashamba hayo ni Kafoi Farm (Mifugo), Leoni(Ushirika-Mfilisi), Msingi (Ushirika-Mfilisi), Pirita (Ushirika- Mfilisi), Pongo (Ushirika-Mfilisi) na mengine mengi?
(b) Pamoja na juhudi nzuri zilizofanywa na Waziri Mkuu kuhusu ubadhirifu KNCU, je, Serikali ina taarifa kuwa ubadhirifu kwenye mali za KNCU na Vyama vya Ushirika ni mkubwa na unaendelea kulindwa na wahusika hawagusiki na bei ya zao la kahawa linaendelea kuathirika?
(c) Je, Serikali inaweza kuwaeleza nini wananchi wa Siha kuhusu Shamba la Gararagua lililouzwa na KNCU mwaka 2014 na makabidhiano kufanyika mwaka 2016, likitoka mkononi mwa Ocean Link lakini Kampuni hii mpya imepata EPZ Exemption mwaka 2012 na je, Serikali haioni kuna harufu ya ufisadi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, lenye sehemu (a),(b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upembuzi na utambuzi wa mashamba umekuwa ukifanywa na Serikali kila inapohitajika ili kufanya maamuzi sahihi ya matumizi ya mashamba. Mashamba ya Leoni, Msingi, Pirita na Pongo yanamilikiwa na Vyama vya Ushirika isipokuwa Shamba la Kafoi ambalo linamilikiwa na mtu binafsi. Mashamba haya yalikuwa na migogoro kwa muda mrefu kati ya vyama na wawekezaji ambao kwa sasa migogoro hiyo imekwishatatuliwa. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inasimamia kwa karibu vyama husika ili kupata wawekezaji wapya kwa maendeleo ya wanachama wa Vyama vya Ushirika na wananchi wa Vijiji vya Wilaya ya Siha.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imechukua hatua kwa viongozi na watendaji waliobainika kujihusisha na ubadhirifu wa mali za KNCU kwa kuwafikisha Mahakamani kwa kesi ya uhujumu uchumi. Aidha, Serikali kwa kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kutekeleza jukumu lake la ukaguzi wa mara kwa mara kwa Vyama vya Ushirika, itaendelea kufanya ukaguzi kwa Vyama vya Ushirika, ikiwemo KNCU na pale itakapobainika kuwa kuna ubadhirifu wa mali za vyama, Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika bila kujali nyadhifa au uwezo wa aina yoyote walionao.
Mheshimiwa Spika, Shamba la Gararagua limeuzwa na KNCU mwaka 2014 kwa kuzingatia taratibu za manunuzi. Aidha, msamaha wa kodi yaani exemption uliotolewa kwa mwekezaji huyo mwaka 2012 unahusiana na uwekezaji wa Shamba la Kifufu na siyo Gararagua.
Mheshimiwa Spika, kuhusu tuhuma za ufisadi, Wizara itafuatilia suala hilo na itakapobainika kuna viashiria hivyo, Serikali itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR aliuliza:-
Kilimo cha mazao ya viungo vya chakula ni biashara yenye tija kubwa duniani kwa sasa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha kilimo hicho hapa nchini?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nassor Suleiman Omar, Mbunge wa Jimbo la Ziwani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mazao ya viungo kutokana na mchango wake katika kipato cha mkulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya viungo (Spice Sub Sector Strategy twenty fourteen) ambao unalenga kuongeza uzalishaji na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mahususi katika mkakati huo ni utoaj mafunzo ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji kwa wataalam na wakulima, uanzishwaji wa vituo vya kukusanyia mazao na kupanga madaraja na kuunda masoko ya pamoja ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengine mahsusi yanayofanyiwa kazi ni kuhamasisha na kusimamia uanzishwaji wa vitalu vya kuzalisha miche na mashamba ya miti mama kwa ajili ya kuzalisha miche bora ya aina za mazao hayo. Mkakati huo unatekelezwa kwa pamoja na wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi zisizo za Kiserikali na Vyama vya Wakulima ambazo ni pamoja na Sustainable Agriculture Tanzania, Chama cha Wakulima wa Viungo, Amani (CHAWAVIA) na Jumuiya ya Wakulima wa Viungo Wilaya ya Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeandaa mwongozo wa uzalishaji wa mazao ambao umeainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya viungo. Mwongozo huo unalenga kuonesha fursa za uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya viungo. Wizara ndani ya miezi sita ijayo itakamilisha zoezi la usajili wa wakulima wa mazao mbalimbali nchini ikiwemo mazao ya viungo kwa kubaini idadi yao, ukubwa wa mashamba na mahali alipo ili kuwahudumia kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea:
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret S. Sitta, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2008, Serikali imeboresha mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za zao la tumbaku kwa wakulima kupata pembejeo kupitia vyama vya ushirika tofauti na ilivyokuwa kabla ya mwaka 2008 ambapo pembejeo za tumbaku zilitolewa kupitia kampuni zinazonunua tumbaku kwa kuwakopesha wakulima na kuwakata wakati wa mauzo. Utaratibu huo ulikuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na riba kubwa isiyo na tija kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondokana na madeni yatokanayo na riba za mkopo wa pembejeo, Serikali imewahamasisha wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kuainisha mahitaji ya pembejeo mapema na wamekubali kukatwa kiasi cha fedha kutokana na mauzo ya tumbaku ili kuagiza pembejeo hizo kwa wakati. Mfano Chama cha Msingi cha Kahama (KACU) wamekubaliana kukatwa Sh.60 kwa kila kilo kwa lengo la kukusanya takribani shilingi bilioni 3 zitakazotosheleza kuagiza asilimia 75 ya mahitaji ya pembejeo. Utaratibu huo unafanyika kwa vyama vyote ambapo wakulima watanufaika kwa kupata bei ndogo kuliko ile ya kukopa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa uagizaji Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) ulianzishwa kwa lengo la kupunguza gharama au kodi kwa wakulima. Hata hivyo, mfumo huo unategemea bei ya mbolea iliyopo katika soko la dunia kwa wakati huo. Kutokana na changamoto za ongezeko la bei ya mbolea katika soko la dunia, Serikali inasimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wakulima wakiwemo wa zao la tumbaku wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaunga mkono tamko la Kilimo ndiyo Uti wa Mgongo wa Taifa kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Jimbo la Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu Serikali inatambua na inaunga mkono tamko la Kilimo ni Uti wa Mgongo kwa Taifa. Umuhimu wa sekta ya kilimo unajidhihirisha katika viashiria mbalimbali vya kiuchumi na kijamii kama vile mchango wa kilimo katika ajira, pato la Taifa, usalama wa chakula na malighafi za viwandani. Takribani asilimia 65.5 ya wananchi wameajiriwa katika sekta ya kilimo, asilimia 28.7 ya pato la Taifa hutokana na sekta ya kilimo, mazao ya chakula huchangia kiasi cha asilimia 65 ya pato la Taifa litokanalo na kilimo. Zao la mahindi huchangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la Taifa litokanalo na kilimo, mazao ya chakula na biashara yanachangia asilimia 70 ya kipato katika maeneo ya vijijini. Aidha, sekta ya kilimo ni muhimu katika mikakati ya kuendeleza sekta ya viwanda nchini kwa kuchangia takribani asilimia 65 ya malighafi za viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo mikakati na mipango inayolenga kuimarisha sektya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na kuwapatia wakulima masoko ya uhakika. Sera, mikakati na mipango inayotekelezwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya II (ASDP II) pamoja na sera, mikakati na mipango mingineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jitihada madhubuti ya kutambua Kilimo ndiyo Uti wa Mgongo ni kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambayo inatoa mikopo ya riba nafuu ya asilimia 8 tu. Aidha, Serikali imeendelea kupunguza ada, tozo na kodi katika kilimo, kuimarisha huduma za utafiti ikiwa ni pamoja na kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na kuimarisha ushirika ili uweze kuwezesha na kusimamia masoko ya mazao ya kimkakati.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Je, Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya peke yake?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015, uzalishaji wa tumbaku ya moshi (Dark Fire Cured Tobacco- DFC) ulisimama Mkoani Ruvuma kutokana na kukosa soko. Jitihada za Serikali zikawezesha kampuni ya Premium Active Tanzania Limited kuonesha nia ya kununua tumbaku hiyo ya DFC ambayo hapa nchini huzalishwa Namtumbo na Songea Vijijini, Mkoani Ruvuma. Kampuni hii ilieleza kuwa lipo soko kubwa la tumbaku aina ya DFC nchini Misri na Algeria, lakini tumbaku ya Tanzania inauzwa kwa bei ya juu kutokana na kodi inayotozwa ikilinganishwa na aina hiyo ya tumbaku kutoka nchi za Uganda na Kenya kwa kuwa nchi hizo Uganda, Kenya, Algeria na Misri ni wanachama wa Jumuiya ya COMESA na kwa hiyo kodi za kuingiza tumbaku, chai na bidhaa nchini Algeria na Misri kutoka Uganda na Kenya ni za chini ukilinganisha na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo, Wizara ya Kilimo inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuanzisha mazungumzo na Nchi Wanachama wa COMESA na nchi kama Misri na Algeria kupitia Balozi zetu ili kuandaa makubaliano maalum yaani bilateral agreement yatakayowezesha nchi yetu kupeleka tumbaku katika nchi hizo kwa kodi nafuu. Mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kufungua milango ya soko hilo na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, makubaliano hayo yakikamilika Tanzania inaweza pia kuuza chai nchini Misri na Algeria kwa faida kuliko ilivyo hivi sasa au badala ya kuuza chai kupitia mnada wa Mombasa nchini Kenya.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali italeta mbegu bora ya tumbaku kama inayolimwa katika nchi nyingine Kusini mwa Jangwa la Sahara?
(b) “Produce cess” ilishushwa kutoka asilimia tano mpaka asilimia tatu ili mkulima afaidike kwenye bei ya kuuza lakini hakuna utekelezaji kwa Makampuni ya Kununua Tumbaku na kwenye Halmashauri mapato yameshuka. Je, Serikali inaweza kupitia upya Sheria hiyo na kurudisha kama awali?
(c) Je, ni lini Serikali itakaribisha Kampuni nyingine za kununua Tumbaku ili kuongeza ushindani na kuondoa hofu kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa aina ya tumbaku hutofautiana kati ya mteja na mteja. Tumbaku inayozalishwa nchini kwa sasa inatokana na mbegu zinazopendwa na wanunuzi waliopo. Wizara imepokea maombi kutoka Nchi ya China ya kuuziwa aina ya tumbaku inayotokana na mbegu zinazolimwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Utaratibu wa kupate mbegu za tumbaku aina za PVH 2254 na KRK 26 kutoka Malawi na aina ya MHW 86 kutoka Zambia umeanza ili mbegu hizo ziweze kuzalisha tumbaku inayokidhi soko la China kuanzia msimu wa 2020/2021.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipunguza ushuru wa mazao ya biashara katika mwaka wa fedha 2017/2018, kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu ili kuongeza kipato cha wakulima. Utekelezaji wa Sheria hiyo umefanyika kwa mwaka mmoja tu wa fedha wa 2018/2019, hivyo Serikali itafanya tathmini ya utekelezaji wa sheria hiyo na kama itabainika utekelezaji wake katika tasnia ya tumbaku hauna tija kwenye mapato ya Halmashauri na kipato cha mkulima, Serikali haitasita kuchukua hatua na kupitia upya sheria hiyo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza ukiritimba wa Kampuni zinazonunua Tumbaku nchini, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuzivutia kampuni nyingine zaidi na kuleta ushindani. Kufuatia jitihada hizo, Serikali imefanikiwa kupata kampuni zingine za kununua tumbaku ikiwemo Kampuni ya British-American Tobacco (BAT) ambayo imeonesha nia ya kununua tumbaku yetu moja kwa moja kutoa kwa wakulima. Taratibu za kufanikisha mpango huo zinafanyika ili Kampuni hiyo iweze kununua tumbaku ya wakulima kwa msimu wa Mwaka 2019/2020. Aidha, katika hatua nyingine, Serikali inakamilisha taratibu za kulipata soko la China kwa kutumia mbegu za tumbaku zinazozalishwa katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Wananchi wa Kata za Mpombo, Kandete, Isange na Luteba pamoja na Kata za Kabula, Lwanga na Lupata wanalima zao la chai kwa wingi lakini bei ya zao hilo ipo chini:-
Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la Chai ambalo litasababisha kupanda kwa bei kuliko bei ya sasa ya Shilingi 315 kwa kilo?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Chai Tanzania iliitisha kikao cha wadau wa chai kilichofanyika Aprili, 2019 kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za wakulima ikiwa ni pamoja na kupanga bei elekezi ya chai kwa mwaka 2019 kwa kuwashirikisha wadau wote. Mkutano huo wa Wadau wa zao la chai ulifanyika tarehe 3 Aprili, mwaka 2019 Mufindi Mkoani Iringa na Wajumbe walipitisha bei elekezi ya majani mabichi ya chai kwa mwaka 2019 kuwa ni shilingi 315 kwa kilo.
Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali kutafuta masoko ya mazao ya kilimo nchini ni jukumu endelevu. Kwa upande wa zao la chai, jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kuwa chai inayozalishwa inauzwa hapa nchini bila kuwalazimu Wakulima kusafirisha chai yao kwenda kwenye mnada wa Mombasa. Katika kutekeleza hilo, Serikali inakamilisha mkakati wa kuanzisha soko la chai Tanzania kwa kuanzisha mnada wa Kimataifa wa Chai Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza uanzishwaji wa mnada wa chai nchini Tanzania kikosi kazi kiliundwa ambacho kinajumuisha Bodi ya Chai (TBT), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi wa Ghala, Chama cha Wakulima wa Chai Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) pamoja na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai Tanzania yaani (TSHTDA). Maandalizi ya mnada huo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 ili tuwe na mnada wetu utakaosaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa chai nje ya nchi na faida inayopatikana iongeze bei ya mkulima.
Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa soko la Makambako ulianza baada ya Serikali kuona umuhimu wa kujenga masoko ya kimkakati (Strategic Markets) kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya Wakulima. Soko hilo lilibuniwa, ili kufanikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya kilimo hususan nafaka za mahindi na mchele ambazo huzalishwa kwa wingi katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mbeya.
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka 2018 Serikali ililipa kiasi cha shilingi 3,026,341,089.58 ikiwa ni fidia kwa wananchi 209 wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko hilo. Aidha, wakati wa ulipaji fidia, walijitokeza wananchi 15 ambao wakati wa uhakiki wa mwisho hawakupatikana na wananchi 20 ambao hawakuwepo kwenye daftari wala taarifa ya uhakiki. Kwa muktadha huo, Serikali imeamua kufanya tathmini tena kwa wananchi ambao hawajalipwa fidia zao ili waweze kulipwa kama wanastahili.
Mheshimiwa Spika, ninaupongeza uongozi wa Mkoa wa Njombe na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa huo kwa ushirikiano walioutoa katika zoezi zima la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa soko la Kimataifa la Makambako. Zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wote litakapokamilika litawezesha mradi husika kutekelezwa bila kuwa na vikwazo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-
Serikali iliondoa kodi kwenye mbegu za mahindi mwaka 2017 – 2018:-
Je, ni lini Serikali itasimamia upunguzwaji wa bei kubwa ya mbegu za mahindi na pembejeo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua ambazo zinzsaidia kupunguza bei za pembejeo ikiwa ni pamoja na kufuta ada na tozo zilizokuwa zinatozwa na taasisi za udhibiti wa pembejeo za kilimo. Katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018 Serikali imefuta ada na tozo 12 katika tasnia ya mbegu kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na bei ya mbegu.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Februari, 2019 Serikali imekutana na wadau wa pembejeo za kilimo kwa lengo la kujadili maendeleo ya pembejeo za kilimo, ikiwemo kujadili suala la bei ya mbegu. Katika kikao hicho wadau walikubaliana kufanya utafiti wa kuhusisha taasisi ya udhibiti wa mbegu Tanzania (TOSCI) na Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu (TASTA) ili kutathmini gharama za uzalishaji na usambazaji. Jitihada zinazoendelea ni kutafuta vyanzo vya fedha ili kumuwezesha mshauri elekezi kufanya tathmini hiyo. Matokeo ya tathmini hiyo yatawezesha upangaji wa bei ya mbegu ambayo itamnufaisha mkulima na mzalishaji. Ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Ugonjwa wa Mnyauko wa Migomba umekuwa tatizo kubwa na la muda mrefu na limewaathiri Wakulima wa Migomba Mkoani Kagera:-
Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua za makusudi za kupambana na ugonjwa huo na kuutokomeza kabisa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mnyauko wa migomba kitaalamu unaitwa unyanjano wa migomba. Husababishwa na vimelea aina ya bacteria ambao hushambulia aina zote za migomba na jamii yake. Ugonjwa huu unasambazwa na ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; miche iliyoathirika; vifaa vya shambani vilivyotumika kwenye migomba iliyoathirika na vifungashio vya kusafirisha ndizi.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2006 - 2014, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kagera tumekuwa tukitoa mafunzo ya kutokomeza ugonjwa huo kwa wakulima na Maafisa Ugani kwenye Wilaya zote zilizoathirika. Serikali imekuwa ikiendesha kampeni ya kung’oa migomba yote iliyoathirika, kukata Ua Dume na kuitekeleza. Halmashauri zote za Wilaya ya Mkoa wa Kagera ziliweka sheria ndogo ndogo za kuwataka wakulima kung’oa na kuchoma au kuzika migomba yote ailiyoathirika. Zoezi hilo lilipunguza ueneaji wa ugonjwa huo kwa asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya tafiti za kuzalisha miche bora ambayo haina vimelea vya ugonjwa wa unyanjano kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ikishirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation. Hadi sasa miche bora milioni sita imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Kagera na Kigoma.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia mbegu bora za migomba aina ya Shia 17, Shia 23, Nshakara, Nyoya na Kinohasha zinazozalishwa katika Taasisi za Utafiti Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Mikocheni, Uyole, Kibaha, Maruku na Tengeru ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutosafirisha ndizi zilizofungashwa na majani ya migomba kutoka mashamba yaliyoathirika.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-
Mkoa wa Ruvuma umepata mnunuzi wa tumbaku ambaye amekubali kuwawezesha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchambua tumbaku na kugeuza green leaf kuwa dry leaf. Aidha, kutokana na changamoto za kodi na soko mnunuzi huyo hajaweza kutekeleza azma yake.
Je, Serikali inasaidiaje kutatua changamoto zinazomkabili mnunuzi huyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Edward Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Spika, kufuatia kuondoka kwa kampuni mbili za ununuzi wa tumbaku Mkoani Ruvuma msimu wa 2014/ 2015, wakulima walikosa soko la uhakika. Kutokana na hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Mheshimiwa Mbunge Ngonyani walifanya juhudi za kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, jitihada hizo zilisaidia kupatikana kwa mnunuzi wa tumbaku ambaye ni Kampuni ya Premium Active Tanzania Limited ambayo ilianza kununua kilo 250,000 na sasa imeongeza hadi kilo 1,000,000. Serikali pia inapongeza nia ya kampuni hiyo ya kutaka kukiwezesha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa huo cha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchakata tumbaku.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na mwekezaji huyo kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mnunuzi huyo ili kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inatimiza azma hiyo njema kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla, ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Wananchi wengi katika Kata za Fukayosi na Kiwangwa Bagamoyo wanalima mananasi kwa wingi sana.
Je, nini mkakati wa Serikali kuhusu kuwajengea viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuboresha kipato cha wakulima hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Wilaya ya Bagamoyo ni moja kati ya Wilaya zinazolima mananasi kwa wingi Mkoani Pwani. Kwa kutambua uwepo wa malighafi hiyo kwa wingi, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kusindika matunda ikiwa ni pamoja na mananasi yanayolimwa katika Wilaya ya Bagamoyo. Hii inaendana na matashi ya dira yetu ya Taifa ambayo inatambua kuwa sekta binafsi ndiyo engine ya ukuzaji uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za Serikali za kuhamasisha uwekezaji viwandani zimezaa matunda ambapo kwa sasa kuna viwanda viwili vikubwa vya kusindika matunda katika Wilaya ya Bagamoyo vya Elven Agri Co. Ltd. na Sayona Fruits Co. Ltd. vyenye uwezo wa kusindika tani 28 za matunda kwa siku na kuajiri jumla ya wafanyakazi 755.
Aidha, ili kuwa na uhakika wa malighafi za kutosha kwa mwaka mzima, tunashauri Mheshimiwa Mbunge kuendelea kushirikiana na Serikali kuhamasisha uzalishaji wa aina nyingine za matunda yatakayotumika baada ya msimu wa mananasi kupita ili kuwezesha viwanda kuzalisha kwa kipindi kirefu kwa mwaka. (Makofi)
MHE. RUKIA K. AHMED aliuliza:-
Mazingira ya kufanya biashara nchini ni magumu na hii ni kwa wafanyabiashara wa ndani na wa nje:-
Je, ni lini Serikali itaondoa urasimu ili wananchi waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA (k.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikibuni na kutekeleza mikakati na mipango mbalimbali kwa kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini. Kwa mwaka 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta binafsi ilifanya uchambuzi wa kina wa mazingira ya biashara nchini kwa sekta zote na kubaini changamoto mbalimbali zikiwemo mwingiliano wa sheria. Kufuatia changamoto hizo, Serikali iliandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Mazingira ya Biashara Nchini (Blue Print for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania) ambao umeridhiwa na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huo utasaidia kuondoa mwingiliano wa sheria na kupunguza urasimu kwa wafanyabiashara wakati wa kupata huduma katika Taasisi mbalimbali za Serikali. Mpango wa Utekelezaji wa Blue Print umekamilika. Sambamba na hilo, Serikali tayari imetekeleza baadhi ya mapendekezo ambayo ni ya kiutawala na yasiyohitaji mabadiliko ya sheria. Mfano, katika Sekta ya Kilimo na Mifugo, jumla ya tozo 114 na tano za OSHA zimeondolewa na mapendekezo ya kuondolewa tozo nyingine kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 yameshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mafanikio ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara ni kwa Tanzania kuendelea kuongoza kwa uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje (Foreign Direct Investment) katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2012.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) inayotolewa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) ya mwaka 2018, Tanzania imeongoza katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuvutia mitaji ya jumla ya Dola za Marekani 1,180 ikifuatiwa na nchi ya Uganda kwa Dola za Marekani 700. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha maboresho yanayofanyika yanadumishwa na kuendelea kubuni mikakati ya kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara nchini. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kutoa kipaumbele cha ajira kwa Majeshi yote nchini kwa Vijana waliohitimu JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2013 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maelekezo kwa Wizara zote pamoja na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Utaratibu huo umekuwa ukitekelezwa na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kuanzia mwaka 2013 yalipotolewa maelekezo hayo. Aidha, inakumbushwa kuwa lengo la mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwapatia vijana wa Tanzania elimu ya uzalendo, ujasiriamali na kujifunza stadi za kazi ili waweze kujiajiri mara wamalizapo mkataba. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatangaza kumbukizi za Vita vya Majimaji vilivyoanzia Kijiji cha Nandete katika Gazeti la Serikali?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vita ya Maji Maji ilipiganwa kuanzia Mwaka 1905 hadi 1907, kusini mwa nchi yetu katika baadhi ya Mikoa ya Lindi, Iringa, Morogoro na Ruvuma, ikiwa
na lengo la kupinga utawala na ukandamizaji wa ukoloni wa Mjerumani. Mwaka 2006, Makumbusho ya Taifa ilianza kuadhimisha kumbukizi ya miaka 100 ya Vita ya Maji Maji na inaendelea kuadhimishwa tarehe 26 Februari kila mwaka, katika Manispaa ya Songea kwenye eneo la Makumbusho ya Vita vya Maji Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, huadhimisha siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai kila mwaka, ili kuwaenzi mashujaa wetu waliopoteza maisha katika vita na operesheni mbalimbali za ukombozi wa nchi yetu na Bara la Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya kutangaza eneo lolote au lengo la kihistoria iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale, chini ya Kifungu cha Sheria ya Mambo ya Kale, Sura ya 333 ya Mwaka 2002, kifungu cha 3(1) na (2). Sheria hiyo inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Malikale kutangaza eneo lenye sifa ya Urithi wa Taifa kwenye Gazeti la Serikali. Endapo Mheshimiwa Mbunge ana nia ya Kijiji cha Nandete kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya Kumbikizi ya Vita vya Maji Maji, basi namshauri awasilishe ombi hilo Wizara husika ili liweze kufanyiwa kazi, ahsante sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga upya na kufanyia ukarabati nyumba zilizo katika Makambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na kuboresha miundombinu mbalimbali kwenye vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ikiwemo ukarabati wa makambi na nyumba za makazi kwa Maafisa na Askari. Ukarabati wa makambi ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2020, na unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na vipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya ukarabati inahusu nyumba zilizonunuliwa kimakundi nje ya makambi ya Jeshi, ikiwemo magorofa ya Mwenge, Keko, Nyumba za makazi za Masaki, Kitangili, Nyegezi, Nyamanolo, Tabora, Tanga, Shinyanga na Mtwara. Aidha, ukarabati huu umeanza kutekelezwa katika magorofa ya Mwenge Dar es Salaam na Tanga. Inategemewa ifikapo Desemba, 2023, ukarabati wa awamu hii utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati awamu ya pili utahusisha nyumba zilizopo makambini kwa kuzingatia kanda mbalimbali kwa kuanza na Kanda ya Mashariki, Zanzibar, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Ziwa na kumalizia ukarabati Kanda ya Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza toka Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameniteua kumsaidia katika jukumu la Waziri wa Ujenzi, kwa kibali chako naomba kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini. Namwahidi Mheshimiwa Rais sitomwangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Mhandisi Godfrey Kasekenya, kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais. Namwahidi Mheshimiwa Rais, tutafanya kazi kwa bidii tutapambana na kudhibiti rushwa hasa kwenye maeneo ya mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi ili dhamira ya Mheshimiwa Rais na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi uende vyema kama tulivyowaahidi Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 210 unatekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa kilomita 50 umekamilika kwa kutumia fedha za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sehemu ya Mnivata – Newala - Masasi yenye urefu wa kilomita 160, mikataba miwili ya ujenzi chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesainiwa tarehe 21 Juni, 2023, kwa sehemu za Mnivata – Mitesa yenye urefu wa kilomita 100 na Mitesa – Masasi yenye urefu wa kilomita 60 pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwiti. Kwa sasa Makandarasi wa sehemu zote mbili wapo katika hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi, ahsante sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Simbo hadi Ilagala?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Simbo – Ilagala – Kalya yenye urefu wa kilometa 234 imeanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Lower Malagarasi ambalo lipo katika barabara hii na kazi zinatarajiwa kukamilika Disemba, 2023. Kuhusu usanifu wa barabara hiyo, Serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Mheshimiwa Mbunge tumemtengea shilingi milioni 100 ili kufanya kazi hiyo.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Nangomba – Nanyumbu yenye urefu wa kilometa 28.32 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-
Je, kuna mpango gani kujenga mifereji Barabara ya Kigamboni – Kongowe, Mtaa wa Mikwambe, Kata ya Toangoma - Mbagala?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam ipo kwenye hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi wa kufanya ukarabati wa mabega ya Barabara ya Kongowe – Kibada, yenye urefu wa kilometa moja. Ukarabati huo pia utahusisha Ujenzi wa mitaro kwenye baadhi ya maeneo, ikiwemo eneo la Mikwambe yenye urefu wa kilometa mbili, ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa wanashiriki mafunzo ya JKT ya muda mfupi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa linaendesha mafunzo kwa kundi la lazima (compulsory), kundi la kujitolea (voluntary) na kundi maalum (special). Mafunzo ya kundi maalum hutolewa kulingana na mahitaji yanayowasilishwa na taasisi au Wizara husika na huendeshwa kulingana na maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu kundi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika katika kuendesha mafunzo ya makundi maalum ni kwa Wizara au taasisi kutuma maombi Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kisha Jeshi la Kujenga Taifa huelekezwa kuendesha mafunzo hayo, ambapo taasisi ama Wizara husika huyagharamia. Hivyo, endapo kuna uhitaji wa viongozi wa ngazi za wilaya na mikoa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa kundi maalum, basi Wizara au taasisi inayohusika na viongozi hao iwasilishe maombi hayo ili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iweze kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wa Kata ya Tambukareli na Jeshi la Wananchi wa Tanzania?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linalozungumziwa lipo katika Kambi ya Jeshi Usule katika Manispaa ya Tabora. Eneo hilo la Jeshi lilipimwa na ramani yake kusajiliwa Mwezi Septemba, 2004 na kupewa nambari 41,574. Mwezi Februari, 2023 Wizara imepeleka fedha kiasi cha shilingi 194,029,643 kwa Manispaa ya Tabora kwa ajili ya kugharamia fidia kwa wananchi wa maeneo ya Usule na Itaga waliopo katika eneo la Jeshi na tayari wahusika wameshalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua zipo changamoto za mipaka katika eneo la buffer zone katika Kata ya Tambukareli. Naelekeza Idara ya Miliki na Ushauri Majenzi katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kufika eneo hili na kuainisha changamoto hizi na kuzipatia ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kusisitiza wananchi kutovamia maeneo ya Jeshi, kwani ni hatari kwao na mali zao, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO K.n.y. MHE. SHANIF M. JAMAL aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza Barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Mansoor Jamal, Mbunge wa Kwimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu yenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha lami kwa awamu; ambapo mkataba wa ujenzi wa kilomita tatu kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, mwaka huu wa 2024. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -
Je, lini miundombinu ya mipaka ya nchi yetu itaboreshwa ili kukuza diplomasia ya uchumi na nchi zenye fursa za kibiashara kama DR – Congo?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS inaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha nchi yetu na nchi zote jirani ikiwemo nchi ya DRC kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Bandari ya Kasanga yenye urefu wa kilometa 107 Mkoani Rukwa na tayari Serikali imesaini mkataba wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kigwira – Karema yenye urefu wa kilometa 112 kwenda bandari ya Karema mkoani Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha barabara ya kuanzia Igawa – Mbeya - Tunduru kuwa njia nne, mkandarasi yupo site. Serikali inaendelea kuboresha viwanja vya ndege vya Songwe, Sumbawanga na Kigoma ambavyo vipo mpakani na DRC. Kwa hiyo, yote hii ni katika kuiunganisha nchi yetu pamoja na DRC, ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO K.n.y. MHE. SHANIF M. JAMAL aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza Barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Mansoor Jamal, Mbunge wa Kwimba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu yenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha lami kwa awamu; ambapo mkataba wa ujenzi wa kilomita tatu kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, mwaka huu wa 2024. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -
Je, lini miundombinu ya mipaka ya nchi yetu itaboreshwa ili kukuza diplomasia ya uchumi na nchi zenye fursa za kibiashara kama DR – Congo?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS inaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha nchi yetu na nchi zote jirani ikiwemo nchi ya DRC kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Bandari ya Kasanga yenye urefu wa kilometa 107 Mkoani Rukwa na tayari Serikali imesaini mkataba wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kigwira – Karema yenye urefu wa kilometa 112 kwenda bandari ya Karema mkoani Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha barabara ya kuanzia Igawa – Mbeya - Tunduru kuwa njia nne, mkandarasi yupo site. Serikali inaendelea kuboresha viwanja vya ndege vya Songwe, Sumbawanga na Kigoma ambavyo vipo mpakani na DRC. Kwa hiyo, yote hii ni katika kuiunganisha nchi yetu pamoja na DRC, ahsante sana.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Je, lini barabara ya Gomvu - Kimbiji – Pembamnazi itajengwa kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Gomvu – Kimbiji – Pembamnazi ni sehemu ya barabara ya Mjimwema – Kimbiji - Pembamnazi yenye urefu wa kilometa 49 ambayo inajengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sehemu ya Cheka – Avic yenye urefu wa kilometa mbili tayari ujenzi umekamilika. Kwa sehemu ya Avic – Kimbiji kilometa 10 taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi zinaendelea. Ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya Kimbiji hadi Pembamnazi itajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Daraja kuanzia Magomeni - Jangwani - Fire ili kuondoa adha wanayopata Wananchi wakati wa mvua?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANROADS imepanga kujenga daraja katika eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita 15. Ujenzi wa daraja hili utatumia fedha za mkopo nafuu wa Benki ya Dunia. Taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na unatarajiwa kuwa umesainiwa ndani ya mwezi Septemba, 2024, ahsante sana.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa barabara ya Kidatu kwenda Ifakara kilometa 67?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa Barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilomita 67 lilifanyika mwaka 2007 kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007. Jumla ya wananchi 142 waliopisha ujenzi wa barabara hii walilipwa fidia ya jumla ya shilingi 2,576,081,789. Kwa wananchi ambao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara hawakustahili fidia kwa mujibu wa sheria. Ahsante sana.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Je, lini Serikali itafanya upanuzi wa Barabara ya Mombo hadi Lushoto kwa kuwa ni nyembamba kiasi cha magari makubwa kushindwa kupita?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami na upanuzi wa Barabara ya Mombo hadi Lushoto yenye urefu wa kilometa 31.36. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hiyo. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Muhambwe waliopisha ujenzi wa Barabara ya Kibondo – Mabamba?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha tathmini ya mali za wananchi zitakazoathiriwa na Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Kibondo - Mabamba yenye urefu wa kilometa 47.925. Katika tathmini hiyo jumla ya wananchi 724 wakiwemo wananchi wa Muhambwe wanastahili kulipwa fidia yenye jumla ya shilingi bilioni 1.29. Kwa sasa Serikali inakamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi hao. Mara baada ya zoezi hilo kukamilika wananchi hao watalipwa fidia. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa One Stop Center Makambako?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi huu, kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili ujenzi wa mradi huu uweze kuanza. Ahsante sana.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -
Je, lini barabara ya Bashnet – Luqmanda – Bosedesh hadi Zinga itapandishwa hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji hadhi wa barabara unafanywa kwa kuzingatia taratibu na vigezo vilivyoainishwa katika Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge anashauriwa kuwasilisha maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Bashnet – Luqmanda – Bosedesh hadi Zinga kupitia Bodi ya Barabara ya Mkoa. Wizara itapitia maombi hayo na endapo barabara hii itakidhi vigezo itapandishwa hadhi, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali kupanua na kuboresha barabara ya Nangurukuru hadi Kilwa Masoko?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS, tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nangurukuru – Kilwa Masoko yenye urefu wa kilometa 30. Kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati utakaohusisha upanuzi wa barabara hiyo, ahsante sana.