Answers to supplementary Questions by Hon. Innocent Lugha Bashungwa (99 total)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali yasiyokuwa na afya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wananchi wamekuwa wakilalamikia kuhusu suala la dawa zinazoua wadudu. Mwaka huu Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba tunapata dawa ambazo zinaua wadudu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kumekuwa na changamoto kipindi cha kugawa dawa za kuua wadudu kwamba mkulima ambaye amelima na akatupia mahindi kidogo hapewi dawa badala yake anaambiwa alipie dawa hizo wakati mMkulima ambaye hajachanganya na zao lolote anapewa dawa bure. Ni kwa nini Serikali imekuwa ikianza na adhabu kwa wananchi badala ya kutoa elimu ndiyo ianze kuwaadhibu wananchi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Gimbi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Gimbi anasema viuatilifu ambavyo wamekuwa wakipewa wakulima haviuwi wadudu. Azma ya Serikali ni kuhakikisha viuatilifu vinavyoingizwa nchini vinaua wadudu kama inavyotakiwa. Tayari Serikali kupitia Taasisi ya Kudhibiti Viuatilifu nchini tumewaelekeza kuhakikisha viuatilifu vinavyoingizwa nchini, Sheria ya Udhibiti Ubora wa Viuatilifu unazingatiwa. Mimi katika ziara zangu nimehakikisha viuatilifu vinavyoingizwa kwa msimu huu wa pamba wa mwaka wa 2018/2019 vinazingatia Sheria ya Udhibiti Ubora wa Viuatilifu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko makini na msimu huu wa pamba tutahakikisha viuatilifu vyote vinavyoingizwa nchini vinafaa kwa ajili ya kuua wadudu. Sambamba na hili, Wizara imeelekeza Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na taasisi nyingine ndani ya Wizara kutoa elimu kwa wakulima ili wakulima wetu wajue namna bora ya kutumia hivi viuatilifu kuweza kupata matarajio ya kuua wadudu kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nimshukuru kwanza Naibu Waziri wa Kilimo, Ndugu yangu Bashungwa kwa uadilifu wako, nadhani Mungu atakusaidia utafika unakoenda. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza la kwanza, na hili niliseme wazi kwa Waziri aliyopo na wewe mwenyewe, na kwa Wabunge wote nadhani unalijua hili, tatizo kubwa la pamba ni mambo mawili tu, la kwanza ni bei ya pamba, la pili ni usambazaji wa pembejeo kwa wakati ambao haufai.
Mheshimiwa Spika, suala la bei, naomba kujua kupata ufafanuzi, ni kwa nini sasa Serikali isitafute masoko ya ndani na masoko ya nje kwa wakati muafaka kwa msimu unaofaa, ili Wakulima wa pamba wapate bei nzuri ya kutosha?
Swali la pili kwa kuwa mwaka jana kwa msimu 2018/ 2019 Serikali ilikuja hapa Bungeni ikatuomba wakate shilingi mia kwa kilo ya pamba kwa wakulima, na lengo lilikuwa kupunguza au kufuta kabisa kero ya usambazaji wa mbegu za pamba au madawa kwa wakati muafaka, nini kimetokea mpaka leo Wakulima wa pamba wanateseka na mbegu hazipatikani kwa wakati na madawa hayapatikani kwa wakati, nini tatizo,? Tatizo ni ubovu wa bodi ya pamba? au ni mikakati mibovu ya Wizara ya Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Boniphace Getere kwa namna anavyohangaikia changamoto za Wakulima Jimboni kwake Bunda hususani zao la pamba.
Mheshimiwa Spika, tatizo la bei na usambazaji tayari Serikali chini ya mfumo wa ushirika tunaendelea kuimarisha ushirika ili ushirika uweze kuwajibika kwa Mkulima kwa kuhakikisha Mkulima anapata pembejeo kwa wakati anazingatia ubora na tayari Wizara yetu kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara tunaendelea kutoa elimu ili wakulima wetu wa pamba wazingatie kupanda kwa kutumia kamba ambayo ina vipimo.
Mheshimiwa Spika, pia, sambasamba na hilo usambazaji wa pembejeo hususani viuatilifu kwa misimu iliyopita vilikuwa vikichelewa lakini tayari Wizara tumeshakaa na kuhakikisha tuna mkakati wa kuhakikisha msimu huu viuatilifu vina wafikia wakulima wetu kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Getere ni kuhusu masoko ya ndani na nje nimuhakikishie Mheshimiwa Getere kwa vile ni mfuatiliaji mzuri tutakaa naye pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mikoa inayolima pamba na kuhakikisha tunakuwa tuna mfumo mzuri ambao utamuhakikishia mkulima kupata bei nzuri lakini na shilingi mia moja ambayo wanakatwa tutaangalia namna ya kuangalia mfumo mzuri ili makato ya mkulima yamsaidie katika kuwa na Kilimo cha tija, ili aweze kupata pato zuri katika msimu wa kuuza pamba, nashukuru.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, vilevile Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo inafanywa kwenye eno hili la ardhi. Najua nia njema ya Waziri aliyejibu swali langu, namfahamu vizuri lakini nimpe taarifa kwamba katika majibu aliyonipa bado umeendelea ule utaratibu wa baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu kupotosha kwenye vitu ambavyo ni vya msingi.
Mheshimiwa Spika, nikianza na baadhi ya majibu yaliyotolewa hapa, mojawapo ya jibu lililotolewa ni jibu ambalo Waziri Mwanjelwa aliwahi kulikataa na kutoa maelekezo tofauti lakini bado jibu hilo hilo limeendelea hapa. Kuhusu exemption tuna barua ya Wizara ya Viwanda ikionesha kwamba mojawapo ya mashamba yaliyopewa exemption, mwaka 2014 Shamba la Gararagua limeuzwa lakini mwaka 2012 tayari mwekezaji aliyenunua mwaka 2014 tuna barua ya Wizara ya Viwanda inayoonyesha kwamba alipewa exemption mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, leo tukiwa hapa hatujui tuna wananchi wetu wa Kata ya Levishi, Kijiji cha Mese mashamba yao ya kahawa yamechukuliwa na TANAPA, Donumoru wananchi sasa hivi wa Kilolepori wanaishi nje, wamebomolewa nyumba zao. Leo hatujui mpaka wa Siha na Wilaya ya Arusha lakini bado huko chini tuna watu ambao wanafanyakazi hiyo. Vilevile kwenye Wizara ya Kilimo tutaona kwamba…
SPIKA: Mheshimiwa Mollel swali sasa.
MHE.DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye swali langu sasa.
SPIKA: Swali moja kwa moja.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Mawaziri wa Wizara husika watakuwa wako tayari kufuatana nami sasa ili twende kwenye maeneo husika kwa sababu tuna Wazungu wanaouza mashamba ya Siha ili wapate mtaji wa kuendeleza maeneo mengine na kuchapa watoto ndani ya Wilaya ya Siha na nitawapa ushahidi hapa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi zitakuwa tayari sasa kukaa chini baada ya Tamko la Rais ili tuone ni namna gani tunaweza tukawapatia wananchi wa Ngarenandume makazi zaidi ya 38,000 wanaoishi kwenye heka 500?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Dkt. Mollel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa namna anavyofuatilia migogoro ya mashamba ya ushirika katika Jimbo lake la Siha.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mollel angependa kusikia commitment ya Serikali kama tuko tayari kuambatana naye kwenda Jimbo la Siha ili kutatua migogoro hii. Jibu ni kwamba tuko tayari na mara tu baada ya Bunge tutaelekea katika Jimbo la Siha ili kuangalia migogoro hii katika mashamba ya ushirika. Pia kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakarabati ushirika kwa manufaa ya wananchi wetu.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa wakulima wa zao hilo hapa nchini kwetu wamekuwa wengi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia soko la uhakika wa bidhaa hizo?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa kuna ongezeko la uzalishaji wa spices hapa nchini na sisi kama Serikali, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, tunayo mikakati ya kusaidia wakulima wetu wa spices kuongeza uzalishaji; sanjari na hilo kuwasaidia kupata masoko ya uhakika. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote ambayo yanatuingia fedha za kigeni tunawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuwasaidia masoko ili waweze kusaidia kwenye pato la Taifa na kuingizia Taifa fedha za kigeni.
MHE. NAJMA M. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile spices yaani viungo vya vyakula mbalimbali ni vinaonesha kwamba vina afya zaidi katika miili ya binadamu. Sasa kwa nini Serikali haitumi wataalam wake wakaja Zanzibar kujifunza faida za viungo hizo ili Watanzania wengine walioko Bara ambao hawajui kama vile Wasukuma, Wamasai na makabila mengine waweze kujua na kutumia na kupata afya njema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake tumeupokea, ni kweli hizi spices zina faida nyingi ikiwemo faida kwa upande afya kwa akinababa na akinamama. Ni ushauri mzuri kwa sababu tunatafuta masoko ya nje, lakini pia masoko ya ndani lazima nayo tuyatumie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wanaume wenzangu, ukiangalia spices kuna faida nyingi sana kwa upande wa wanaume na ni namna mzuri ya kukuza soko la ndani. Kwa hiyo, ushauri wa Mheshimiwa Najma tumeuchukua.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Mkinga, Muheza, Korogwe na Lushoto ni maeneo ambayo yanalima kwa wingi mazao ya spices, lakini kwa muda mrefu maeneo haya yamekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za Ugani, masoko duni ya bidhaa hizi na vilevile mazao haya kuuzwa kwa bei ya chini sana. Je, Waziri yuko tayari na wataalam wake kuja kwenye maeneo haya kujionea hali halisi ili kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwa namna anavyofuatilia masuala ya spices kwa niaba ya wakulima hapa nchini ikiwemo Jimboni kwake. Nimeshamhakikishia kwamba Serikali kwa kutambua kwamba spices hizi zina potential kubwa ya kutuingia fedha za kigeni, niko tayari kwenda Mkoa wa Tanga na kufika maeneo ambayo ameyataja kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia kwenye upande wa kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunawasaidia kwenye mambo ya branding na mikakati ya kimasoko ili kilimo chao kiweze kuwasaidia kuwakwamua kutoka kwenye umaskini, lakini uzalishaji wao usaidie kuchangia kwenye fedha za kigeni za nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa ambazo amechukua kusaidia zao la tumbaku kwa kuja kila wakati katika Mkoa wa Tabora. Pili, naomba nimshukruu pia Naibu Waziri kwa jibu zuri kwamba wataagiza mbolea kwa pamoja yaani bulk procurement ili kusaidia kupunguza bei lakini kufika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, upatikanaji au uagizaji wa mbolea kwa wakati unategemea sana makisio. Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba makisio yanatolewa mapema ili mbolea iweze kuagizwa mapema na imfikie mkulima kabla ya mwezi Agosti?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mkulima anapata moyo wa kulima kutokana na bei anayotegemea kupata. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wanunuzi wengi zaidi ili soko lipatikane kwa wakati na kwa ushindani ili angalau mkulima apate bei inayoweza kumsaidia kumudu maisha na kazi kubwa anayoifanya ya kulima tumbaku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze wananchi wa Urambo kwa kuchagua Mbunge jembe. Mheshimiwa Mama Sitta anawahangaikia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwagiza Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika afike Urambo haraka iwezekanavyo akae na Mkuu wa Wilaya ili waangalie namna bora ya kuratibu utaratibu wa kukusanya madeni kwa wakulima wa tumbaku hasahasa wale wakulima ambao wanadaiwa lakini wanaendelea na kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kufanya makisio mapema. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mama Sitta pamoja na wananchi wake kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha makisio ya wanunuzi yanafanyika mapema ili wakulima waweze kujua ni kiasi gani cha mbolea wanatakiwa kuagiza na mbolea iwafikie kabla ya mwezi Agosti, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu mkakati wa kuongeza wanunuzi. Naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge na wakulima wetu kwamba kwa upande wa zao la tumbaku tayari Serikali tumekaa na wanunuzi waliopo na kuangalia changamoto zao ambazo tukizitatua zitawawezesha kununua tumbaku zaidi lakini tunaendelea kuongea na nchi ambazo zina mahitaji ya tumbaku ikiwemo China na Misri. Kwa hiyo, kwa mikakati hiyo Serikali itaweza kuwasaidia wakulima wa tumbaku kupata soko la uhakika na zaidi na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasiaidia kuhakikisha tumbaku yao inatakiwa na inagombaniwa na wahitaji na kufanya hivyo kutasaidia kuchochea bei kupanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Changamoto za zao la tumbaku zinafanana kabisa na changamoto zinazokabili zao la kahawa. Suala hili la pembejeo hasa mbolea imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu wakulima wa kahama wengi wanashindwa kulima kahawa vizuri, wanashindwa kuhudumia mashamba ya kahawa kwa sababu ya bei kubwa ya mbolea. Licha kwamba Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea wa Pamoja lakini bado haijawa suluhu kwa wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini sasa Serikali itajenga viwanda vya mbolea nchini ili angalau sasa mbolea iweze kushuka bei na wakulima wa kahawa waweze kunufaika na uzalishaji uweze kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumkaribisha Mheshimiwa Haonga pamoja na Wabunge wengine, leo tuna kikao cha wadau wa kahawa kinafanyika hapa Dodoma, kimeanza saa mbili na nusu. Kwa hiyo, baada ya maswali na majibu tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikao hiki na tuweze kupata maoni yenu ili kuboresha mfumo wa ununuzi wa kahawa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Haonga la lini Serikali itajenga viwanda vya mbolea, majibu ya Serikali ni kwamba inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha tunajenga viwanda vya mbolea hapa nchini ikiwemo utumiaji wa gesi asilia ambayo tumeigundua ili kutengeneza mbolea na kusaidia wakulima wetu waweze kupata mbolea hapa hapa nchini na kwa bei nafuu.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusu tumbaku kwa sababu tumbaku Tabora ndio siasa yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vingi vya msingi vimekufa au vimesinzia au havifanyi kazi kutokana na mfumo wa zamani uliokuwepo na hasahasa utoroshaji wa tumbaku, kukwepa madeni kupitia vyama vya IF. Sasa mfumo mzuri umewekwa na kwamba madeni yamedhibitiwa. Je, Serikali kupitia Benki ya Kilimo haiwezi kuwadhamini wanachama hawa wa vyama sinzia ili vilime tumbaku kwa mkakati wa kulipa madeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa ufatiliaji wake wa karibu wakulima wake wa tumbaku. Swali la Mheshimiwa Maige ni kwamba TADB inawasaidiaje wakulima kupitia vyama vya msingi. Jibu ni kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada kwanza ya kufufua vyama vya msingi viweze kuzingatia utawala bora (good governance) kwani kwa kipindi cha nyuma vyama vya msingi baadhi ya viongozi walikuwa siyo waadilifu kwa hiyo fedha nyingi zilikuwa zinapotea kwa njia hiyo kwa sababu walishindwa kuzisimamia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mkakati wa Serikali wa kuboresha ushirika na kuhakikisha vyama vya msingi vinakuwa na viongozi waadilifu basi tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa na TADB na kuangalia ni namna gani tunaweza tukaratibu jambo hili ili wakulima kupitia vyama vya msingi waweze kupata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Bado narudi kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kuhusu tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye kalenda ya Bodi ya Tumbaku ili pembejeo zifike nchini mwezi Agosti na Septemba, makisio hutolewa tarehe 31 Machi, ndiyo deadline. Sasa makisio yametolewa kwa makampuni matatu ambayo yanafanya biashara hapa nchini; kampuni moja haijatoa makisio, hiyo ina maana wakulima wa Tabora, Chunya, Ruvuma, Mpanda watakosa kulima tumbaku msimu ujao. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuitisha kikao cha dhararu kati ya Bodi ya Tumbaku na Wabunge wanaolima tumbaku ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nakubaliana na yeye kwamba kukaa na wanunuzi kufanya makisio mapema iwezekanavyo ikiwezekana mapema mwezi Machi, ni jambo la msingi kwani litasaidia wakulima wetu kujua ni kiasi gani wanahitaji kuagiza kupitia bulk procurement system.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni kwamba tuko tayari kukaa na huyu mnunuzi mmoja ambaye bado hajatoa makisio? Jibu ni kwamba Mheshimiwa Mwambalaswa niko tayari na baada ya hapa nitatafuta namba zao na kuwapigia simu na kuona kwa nini mpaka sasa hawajatoa makisio kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la MKUKUTA na Ilani ya Chama cha Mapinduzi sekta ya kilimo ilikuwa ikue kwa asilimia 8 ndani ya miaka 10 lakini uhalisia kuanzia mwaka 2011 na 2015 sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.4. Ndani ya miaka ya Awamu ya Tano katika miaka yake mitatu ya bajeti sekta ya kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 1.9. Uhalisia unajionesha kwenye bajeti zake, bajeti ya mwaka 2016/ 2017…
MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulitenga shilingi bilioni 101 katika sekta ya kilimo lakini fedha iliyotoka ilikuwa ni shilingi bilioni 3 peke yake. Pia mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi bilioni 150 ikatoka shilingi bilioni 24. Swali, hii ndiyo tafsiri ya Kilimo ni Uti wa Mgongo katika Taifa letu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wote tunajua kwamba Watanzania wengi wanaohitimu vyuo vikuu katika Taifa hili ni 800,000 lakini watu ambao wanaajiriwa kwenye sekta rasmi karibu watu 20,000 tu ambapo 780,000 wanakwenda kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Hata hivyo, sekta ya kilimo kumekuwa na tatizo la uwekezaji, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wahitimu hawa wanapewa mikopo ili wajiajiri na wainue maisha yao pamoja na kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Mwakajoka anasema kwamba sekta ya kilimo imekua ikikua kwa asilimia ndogo kinyume na matarajio. Pamoja na mipango mizuri ya Serikali katika kukuza sekta ya kilimo nchini lakini kuna mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri productivity ya kilimo nchini. Hata hivyo, Serikali inayo mipango madhubuti kupitia Mpango wa Kilimo wa ASDP II kama nilivyotaja kwenye majibu yangu ya msingi, kuhakikisha tunatumia ardhi vizuri kwa kilimo, tunazingatia matumizi mazuri ya utumiaji wa maji ili kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji yaani drip irrigation pamoja na mikakati mingine ambayo tumeiweka ndani ya Serikali kupitia Mpango huu wa Maendeleo ya Kilimo wa ASDP II.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mwakajoka ni kwamba tuna vijana wengi ambao wanahitimu kwenye vyuo vikuu lakini kuna changamoto ya ajira; na wanaoenda kwenye kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo ni wachache, asilimia ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika hili ni kuhakikisha tunaleta mageuzi ya kilimo na kufungamanisha kilimo na viwanda. Kama unavyojua Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge, Serikali inaendelea kufanya jitihada hizi kuangalia kilimo kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, asilimia 65 ya malighafi za viwandani zinategemea mazao yetu ya kilimo. Sasa mkakati wa Serikali ni kuongeza hizi asilimia ili tuweze kufungamanisha uchumi wa viwanda na kilimo.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa. Niipongeze Serikali kwa hatua inazozichukua kuimarisha soko la tumbaku nchini. Njia mojawapo ya kuimarisha soko la tumbaku kwa upande wa sisi Wanaruvuma ni kufufua Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku kilichoko Songea ambacho kinamilikiwa na SONAMKU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, SONAMKU kwa kushirikiana na mnunuzi wanakwamishwa na Serikali kwa kutoilipa VAT return ya jumla ya shilingi bilioni 12 Kampuni hiyo ya Premium Active Tanzania Limited na hivyo kampuni hiyo kushindwa kushirikiana na SONAMKU kuanzisha au kufufua kile kiwanda.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hizi fedha zinalipwa ili sisi Wananamtumbo tuwe na uhakika na soko la tumbaku kwa kufufua hicho kiwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wananamtumbo tunajihusisha vilevile na kilimo cha Korosho na Mazao mchanganyiko ya mahindi mbaazi, ufuta, alizeti na soya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha masoko ya mazao haya ili Wananamatumbo tuendelee kupata nafuu lakini na suala la mbolea au pembejeo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Edwin Ngonyani kwa namna alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kwa kampuni ya Premium Active Tanzania Limited. Nampongeza sana Mheshimiwa Ngonyani na kwa namna anavyohangaikia Wananamtumbo katika kuhakikisha wananufaika na sekta ya kilimo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kufufua viwanda vikiwemo viwanda ambavyo vinachakata mazao yanayotokana na kilimo likiwemo zao la tumbaku. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Kilimo tutakaa na wenzetu upande wa Wizara ya Fedha kuangalia hili suala la VAT ambalo Mheshimiwa Ngonyani ameliuliza kama swali lake la nyongeza namba moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili ni kuhusu mkakati wa Serikali katika uhakikisha tunapata masoko ya uhakika ya mazao mchanganyiko pamoja na zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha tunapata masoko ya uhakika kwa wakulima wetu kwanza tumeanza na mikakati ya kupata institutional buyers na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, walishuhudia Serikali ikisaini mkataba na World Food Programme kwa upande wa zao la mahindi kwa wakulima wetu na tunaendelea kuongea na institutional buyers wengine ambao watasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara kwa kushirikiana na Balozi zetu nje ya nchi tunaendelea kuwasiliana nao na kuangalia mikakati ya kushirikiana ili tuweze kupata masoko zaidi katika mazao mchanganyiko na mazao ya kimkakati. Kwa mfano, mwezi Mei, kuna timu inaenda China hususan kwa ajili ya kutafuta soko la tumbaku pamoja na parachichi, karanga na mazao mengine.
Kwa hiyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Ngonyani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inaendelea kujipanga na tayari tumefanikiwa katika maeneo ya kupata masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waheshimiwa Wabunge kama Mheshimiwa Ngonyani alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kuptia kampuni ya Premium Active Tanzania Limited, basi na wao waendelee kushirikiana na sisi Wizara ya Kilimo kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika. Ahsante.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali juu ya majibu ya tumbaku, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, katika jibu la (b) kuhusiana na tozo (Produce cess) kwa kweli Serikali ilipunguza kutoka asilimia tatu mpaka tano. Ukiangalia discount hii ilikuwa ni karibuni asilimia 40 na mkulima hajafaidika. Kuhusiana na tathmini, binafsi kwenye halmashauri zetu tumekwishafanya tathmini mapato yameshuka. Sasa Je, Serikali iko tayari katika mabadiliko ya sheria yanayoletwa sasa hivi Mwezi Juni kwenye Finance Bill kurudisha hii produce cess kuwa asilimia tano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili dogo; Kampuni ya Premium ambayo inanunua tumbaku nchini ikiwemo Katavi, Chunya pamoja na Ruvuma mpaka sasa haijalipa tozo za halmashauri pamoja na kwenye vyama vya msingi kwa sababu kwamba wana madai yao Serikalini ya marejesho ya kodi la ongezeko la thamani (VAT refund) na tangu mwaka jana tunafuatilia na mpaka sasa Serikali haijailipa hii kampuni na wanadai takribani bilioni 12. Sasa Je, Serikali haioni kwamba kutolipwa kwa wakati fedha hizi inachelewesha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbogo kwa namna anavyofuatilia zao la tumbaku kwa manufaa ya wakulima wa tumbaku nchini.
Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbogo anauliza kama tuko tayari kurudisha produce cess kutoka asilimia tatu kurudi kwenye asilimia tano. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Mbogo ana hoja nzuri lakini kama nilivyojibu ni mapema kwa sababu tuko kwenye fiscal year ya kwanza katika utekelezaji wa hii sheria na Serikali tumesema hatutasita baada ya kufanya tathmini na kuona kuna haja ya kurudisha hiyo produce cess. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira angalau twende kwenye fiscal year kama mbili, tatu halafu baada ya hapo tutafanya tathmini na kuona namna ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbogo, anasema kutolipwa kwa VAT refunds kwa muda kunaathiri malipo kwenda kwenye halmashauri na vyama vya ushirika. Kwa vile suala hili linahusu VAT claims basi nimwahidi Mheshimiwa Mbogo tutakaa na wenzetu Wizara ya Fedha na kuangalia namna ya ku-expedites ili Kamouni hii iweze kulipa madeni ya halmashauri na AMCOS.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Zao hili la tumbaku ina changamoto zinazofanana na zao la vitunguu swaumu. Je, mna mpango gani sasa wa kusaidia zao la vitunguu swaumu kama zao la biashara kama ilivyo tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbogo Flatei kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitunguu swaumu pia ni zao muhimu ambalo linaweza kuwapatia wakulima wetu kipato na liko kwenye fungu la spices, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwa sababu Serikali tuna mkakati wa pamoja wa kuhakikisha tunasaidia wakulima kupata masoko ya spices, basi na suala la vitunguu swaumu tutaliweka katika hilo fungu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tulipitisha azimio humu Bungeni kwamba msimu wa pamba unatakiwa uanze tarehe Mosi Mwezi Mei kila mwaka. Hivi sasa kuna Walanguzi tayari wameshaanza kupitapita na kununua Pamba kwa shilingi mia tano, mia sita, mia saba. Je, ni nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali la Mheshimiwa Ndassa (Senator) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Senator ni taarifa muhimu sana kwa Wizara ya Kilimo kwa sababu tarehe 29 Aprili, tulifanya Mkutano wa 15 wa wadau wa pamba na baada ya hapo jana tulikuwa tuna kikao cha kupitia mwongozo wa msimu wa ununuzi wa pamba na leo hii tunapitia masuala ya bei elekezi ili kuanza msimu tarehe Mosi Mei, 2019 na taratibu hizi zote ziko kisheria, kwa hiyo yoyote yule ambaye ananunua pamba kabla ya uzinduzi wa msimu wa pamba ambao uko kisheria ni ukiukwaji wa sharia. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa baada ya hapa nitawasiliana na Wakuu wa Mikoa na kuhakikisha Serikali tunajipanga kuhakikisha mkulima hanyonywi…
MWENYEKITI: Ahsante, ameshakuelewa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): …kwa sababu shilingi mia sita au mia saba ni hela ndogo sana kwa mkulima.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kampuni ya Alliance One iliyokuwa inanunua tumbaku Serengeti iliondoka wakati ambapo wakulima wako kwenye peak ya kilimo cha tumbaku. Baada ya kuondoka wakulima wakashindwa wapi wauzie tumbaku yao. Kwa kuwa Serikali ina jitihada ya kuwatafutia wananchi wa Serengeti kampuni nyingine ya kununua tumbaku, kwa nini wakulima wanaolima sasa hivi tumbaku wasiruhusiwe kuuza kokote watakako tumbaku yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ryoba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumtoa wasiwasi Mheshimiwa Ryoba pamoja na wakulima wa pamba, Serikali inayo mikakati mizuri ya kuhakikisha tunawasaidia katika kupata masoko ya uhakika na nitumie nafasi hiui kumpongeza Balozi wetu Mheshimiwa Mbelwa Kairuki, Balozi wa China tunawasiliana nae na kuna ujumbe unaondoka mwezi huu mwishoni kwenda China kwa ajili ya kutafuta masoko ya tumbaku. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Ryoba awe na subira, karibuni tutaweza kuwapa uhakika wakulima hawa wa pamba katika Jimbo lake.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Moja ya tatizo kubwa la wakulima wa pamba ni bei ndogo kwa sababu inasimamiwa na soko la dunia. Mwaka 2015/2016 na hata 2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfuko wa Kurekebisaha Bei ya Pamba. Nataka kuiuliza Serikali inasema nini juu ya ahadi hiyo ili wakulima wa pamba sehemu zinazolimwa pamba waweze kupata bei nzuri wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kafumu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge angependa kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha tunasaidia kuinua bei ya pamba nchini. Kama mnavyojua suala la uinuaji wa bei ya pamba unatokana na factor mbalimbali ikiwemo factor ya tija na chini ya SDP II, Serikali tuna mpango mzuri wa kuhakikisha tunawasaidia wakulima wa pamba na mazao mengine nchini kuongeza tija sambamba na ku-plan mapema masuala ya masoko kwa wakulima wetu.
Kwa hiyo, kwa combination ya factor hizo mbili, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba tutaweza kuleta uchochezi wa kuinua bei ya pamba pamoja na mazao mengine nchini. Nimuombe baada ya hapa tukae tuangalie hata hili suala la Mfuko wa kuinua zao hili inaweza ikawa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuinua zao hili.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa zao la tumbaku na pamba, ni lini Serikali itaongeza bei kwenye zao la chai katika Wilaya ya Rungwe na cocoa katika Wilaya ya Kyela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bei linakuwa determined na soko lakini moja ya mkakati wa Serikali kwenye zao la chai ni kuanzisha mnada hapa hapa nchini badala ya kutegemea mnada wa Mombasa. Kuhusu cocoa tunaendelea kuwasiliana na wanunuzi wa cocoa duniani ili kuona kama wanaweza wakanunua cocoa ya Tanzania. Kwa hiyo, mikakati ya Serikali ni mizuri kwa upande wa chai na cocoa na mkakati wa kuwa na mnada wa hapa hapa nchini utasaidia kuwapatia wakulima wa chai bei nzuri. Ahsante.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nipongeze Serikali kwa juhudi pekee ya kuinua bei ya zao la chai kutoka 241 kwa kilo ya majani mabichi chai mpaka kufikia 315, na nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutembelea Jimbo hili la Busokelo na concern yetu ya zao la chai tuliwaambia na kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, Bonde la Mwakaleli tuna Kiwanda cha Chai ambacho kimekuwa kikizalisha chai lakini kwa msimu, kuanzia mwezi wa Disemba mpaka Juni kila mwaka na hivyo miezi Sita mingine huwa hakifanyi kazi; Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kukifanya kiwanda hiki cha chai cha Bonde la Mwakaleli kiweze kufanya kazi mwaka mzima badala ya sasa tunaki- underutilize. (Makofi)
Swali la pili, hivi sasa katika Jimbo langu la Busokelo tunalima viazi mviringo na ni wakati wa msimu wa mavuno lakini bei yake ipo chini sana, kiasi kwamba hata wanunuzi wa viazi hivi wanawaibia zaidi wakulima wana-collude kwa kushirikiana na yale makampuni yanayotengeneza mifuko kwa kufanya kitu kinachoitwa lumbesa. Kwa mfano, mfuko mmoja ambao una debe tano wao wanafanya debe sita na nusu na wananchi hawa wanakuwa wamekopa wamenunua pembejeo, wamelima kwa shida, lakini bei zao ziko chini na kiasi hiki kinafanya mkulima akate tamaa kabisa kuendelea kulima zao hili la viazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani wewe ukiwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuja site ili uone namna mateso ya wananchi wangu wa Bonde la Mwakaleli, Busokelo pamoja na Wilaya nzima ya Rungwe hadi Uyole - Mbeya kwamba wanahitaji masoko ya uhakika katika zao hili la viazi. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete Mbunge wa Busekelo kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwakibete kwa pongezi kwa Serikali kuongezeka kwa bei ya chai kutoka shilingi 241mpaka shilingi 315 lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Mwakibete kwa kweli anawapambania wananchi wa Busekelo tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Fredy Mwakibete Mbunge wa Busekelo ni kuhusu Kiwanda cha Chai kuzalisha miezi Sita peke yake na yeye angetamani pamoja na wananchi wa Busekelo kuona kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba nitatenga muda niweze kwenda nae Jimboni Busekelo tutembelee Kiwanda hiko tuangalie changamoto zilizopo na kuona ni nini Serikali inahitaji kufanya na upande wa Mwekezaji wanahitaji kufanya nini ili kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mwakibete angependa kuujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wa Busekelo tunawapatia soko la uhakika la viazi mviringo.
Mheshimiwa Spika, katika ziara ambayo nitaifanya tutahakikisha tunatoka na mkakati wa kuwapatia masoko ya uhakika wa viazi mviringo tunaujadili na pale inapowezekana tutawaunganisha wakulima hawa kwenye masoko ya viazi mviringo. Suala la lumbesa, halitasubiri ziara Mheshimiwa Mbunge baada ya maswali tutakaa pamoja tuangalie namna ya kushughulikia jambo hili, haliwezi kusubiri ziara, tutafuta namna ya kuliratibu vizuri ili wananchi wako wasiendelee kupunjwa kupitia mfumo wa lumbesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua lini Serikali itamaliza kufanya tathmini hiyo ya pili na kuweza kulipa fidia kwa wananchi hawa wa Halmashauri ya Makambako ambao walikubali kabisa kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Viwanda na Biashara mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba ndani ya Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla kunakuwa na viwanda vingi vidogo vidogo vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ili wanapoenda kuuza kwenye viwanda vikubwa na kwenye soko la Kimataifa tarajiwa wananchi hawa waweze kupata mapato zaidi na kuinua hali zao za kiuchumi, vilevile ili tuweze kufikia azma ya uchumi wa kati. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge Neema Mgaya kwa namna anavyofuatilia changamoto za wananchi wa Mkoa wa Njombe, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mgaya ni kwamba lini tathimini itakamilika. Kwa kuzingatia azma ya Serikali ya kuhakikisha tunawasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika, jambo hili tunalichukulia kwa uzito na tathmini, tutahakikisha inafanyika haraka iwezekanavyoo na kwa vile kupitia Wabunge, wananchi watatupa ushirikiano katika kukamilisha suala la fidia, basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tathmini itakamilika haraka iwezekanavyo, ili kupitia soko la kimataifa la Makambako, wakulima wanaotoka kwenye Nyanda za Juu Kusini waweze kuzalisha kwa wingi na kupata masoko ya uhakika kupitia soko la kimataifa la Makambako.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mgaya angependa kujua nini mkakati wa Wizara yetu katika kuhakikisha tunaongeza viwanda vidogovidogo ili kuchakata mazao ya wakulima. Nimhakikishi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tayari ina mikakati mizuri, bilaterally kwa kuandaa makongamano mbalimbali nchini, ambapo wafanyabiashara kutoka nchi za SADC, wafanyabishara kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakuja hapa Tanzania kukutana na wafanyabiashara na wenye viwanda hapa nchini, lengo hilo na mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kupitia forum hizi tunavutia uwekezaji lakini tunasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ku-network na wenzao ambao wanatafuta fursa za kuwekeza hapa nchini na kwa vile utekelezaji wa blue print unakwenda vizuri, basi nina imani kabisha mikakati hii itaweza kusaidia kuchochea ujenzi wa viwnada nchini.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya dada yangu; kwa sababu ameji-commit kwamba mnafanya utafiti ili kuona gharama halisi ambazo zitasababisha mfufue.
Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Bunda tulikuwa tuna Ginnery tano ambayo ni Kibara, Ushashi, Mara Rint, Bulamba na Olam na zinazofanya kazi ni mbili. Tatu ukiwepo na Ushashi hazifanyi kazi zinafanya kazi Olam na Bulamba lakini Mara Rinti ni nzima na ina kila kitu tatizo lake ni mwekezaji. Sasa ni lini Serikali mtatafuta mwekezaji ili hii Ginerry ya Mara Rinti ifanye kazi na ipo kwenye eneo very strategic na ikifanya kazi itapunguza changamoto ya ajira kwa akina mama na vijana wa Jimbo la Bunda Mjini na Wilaya nzima ya Bunda kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara tuna kiwanda cha nguo, kipo Musoma. Hata hivyo sasa hivi hiki kiwanda hakifanyi kazi kwa ufanisi na ukiuliza changamoto kubwa kwa nini kiwanda hiki hakifanyi kazi; na kuwepo kwa kiwanda hiki ni kutokana na malighafi ile ya pamba iliyopo kwenye Mkoa wetu wa Mara na maeneo jirani. Sasa nimeuliza changamoto ni mtaji, na kama hakifanyi kazi kwa ufanisi ina maana kunapunguza ajira kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua, ni lini Serikali Mtaongeza mtaji ili akina mama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kutokana na kuwepo kwa kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara?
Sasa ningependa kujua ni lini Serikali mtaongeza mtaji ili wamama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kuwepo na kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri swali la msingi. Serikali imeona umuhimu wa kufanya uchambuzi katika kutekeleza Sera ya zao la pamba ya cotton to cloth kwa hiyo, lipo zoezi la kuhakikisha tunachambua na kuangalia namna bora ya kufufua ginnery zote za pamba kwa sababu value chain ya cotton to cloth inaanzia kwenye ginnery kufanya kazi mpaka kwenye textile industries.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bulaya kwamba hata kiwanda cha MUTEX kiko sehemu ya hili zoezi. Nimeshafika kwenye kiwanda hicho na ninakuhakikishia katika zoezi hili tutafia pia kwenye ginnery hizi ulizozitaja na tunashirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha zoezi hili linafanyika haraka sana iwezekanavyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Naibu Waziri kujibu swali. Baada ya kutoa kodi na tozo 12, mategemeo yetu ilikuwa bei ya mbegu kuwa chini au kuteremka kutoka shilingi 9000/10,000 zimepanda bei mpaka 12,500. Je, kuna uhusiano gani sasa tulipiga kelele huku kuondoa tozo na kodi lakini bado bei ya mbegu imeongezeka. Naomba Mheshimiwa Waziri atuambie pamoja na kwamba tathmini haijaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbegu ni suala muhimu sana katika kilimo, sasa yeye amesema mnatafuta fedha na mnategemea kufanya tathmini, hamuoni tumechelewa kufanya hivyo wakati kilimo kinaendelea kila msimu. Naomba uniambie fedha zitapatikana lini na tathmini itafanywa lini ili bei mbegu ithibitiwe na iteremke? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwa namna anavyofuatilia changamoto za wakulima wake katika Wilaya ya Hanang na napenda kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu amesema kwamba pamoja na jitihada za Serikali kuondoa kodi na tozo, bado bei ya mbegu haijashuka na mkakati wa Serikali katika hili ni kwamba tumetambua kwamba mkulima na mzalisha mbegu wamekuwa wote wakitegemea msimu wa mvua, badala ya mzalisha mbegu kuzalisha mbegu za kutosha wakati wa kiangazi ili aweze kumpatia mkulima mvua zinavyoanza mkulima huyu aweze kupanda.
Mheshimiwa Spika, sasa mkakati wa Serikali ni kwamba kwanza nimpongeze Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amesaidia Serikali kuingia makubaliano na EFAD. Tumeingia makubaliano tumepata bilioni 127.3 na fedha hizi asilimia kubwa itaenda kwenye taasisi za uzalishaji wa mbegu. Na nimuhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, Wilaya ya Hanang hatutawasahau katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu alikuwa anazungumzia kuchelewa kufanyika kwa tathmini lakini Serikali haijachelewa kama nilivyosema, tayari Serikali imeshapata dawa fedha zimepatikana, sasa tunaenda kwenye utekelezaji. Ahsante sana.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na ni kweli ugonjwa huu umepungua kwa asilimia kubwa, lakini haujaisha. Sasa Serikali kwenye majibu inasema kwamba jitihada zimekoma 2014, lakini ukweli ni kwamba ugonjwa huu bado haujaisha kabisa, bado upo ingawa umepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, napenda kujua ni jitihada gani mahususi ambayo Serikali inayo kutokomeza ugonjwa huu uishe kabisa kwa asilimia 100? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sambamba na ugonjwa huo wa migomba kuna mnyauko pia wa mikahawa, kuna mnyanjano pia wa mihogo unaitwa batobato na yote haya yanalimwa Kagera haya. Napenda kujua ni jitihada gani zinachukuliwa na Serikali kuondoa magonjwa hayo mengine na mazao mengine kama kahawa, migomba, mihogo na mazao mengine?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Jasson Rweikiza kwa jitihada nzuri za kuhakikisha kwamba tunatokomeza ugonjwa wa mnyauko wa ndizi pamoja mnyauko wa kahawa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jasson Rweikiza ni mkulima mzuri wa ndizi, nilishawahi kutembelea shamba lake. Kwa hiyo, nakupongeza kwa kupambana na jitihada hizi huku nawe ukiwa mkulima kwa kuonesha mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya Mheshimiwa Jasson Rweikiza, swali la kwanza angependa kujua mikakati ya Serikali ya kutokomeza mnyauko wa migomba, ni kwamba Serikali kama nilivyosema kwenye swali nililojibu wiki iliyopita, Mheshimiwa Rais wetu ametusaidia kupata mabilioni kutoka IFAD; shilingi bilioni 127.3 kwenda kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI na ASA) kwenye kuzalisha mbegu pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi hasa hasa kwenye magonjwa kama haya ya mnyauko na magonjwa mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Rweikiza kwamba Serikali tayari ina jitihada mahususi za kuhakikisha tunapata fedha za kutosha kupambana na magonjwa haya. Vile vile nikuhakikishie katika bajeti ambayo itaenda TARI na ASA tutahakikisha bajeti kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya mnyauko wa kahawa na ndizi na yenyewe inazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tatizo la huu ugonjwa wa mnyauko katika migomba, linafanana kabisa kwa miaka mingi na mnyauko au ugonjwa wa manjano kwa kilimo cha mpunga ndani ya Wilaya ya Kilombero na mwaka huu athari hii imekuwa kubwa mno. Kila mara nilikuwa nafuatilia hapa kuuliza maswali Bungeni lakini hatujapata jibu kwamba tunafanyaje sisi wakulima wa mpunga kwani tunapata hasara kubwa?
Je, Serikali ina mpango gani wa kutupa majibu wakulima wa mpunga hususan wa Wilaya ya Kilombero, Ulanga, na Malinyi ambapo ndio walimaji wakubwa wa mpunga ili tuepukane na hizi harasa tunazopata kila mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, Serikali inatambua kwamba kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na moja ya changamoto hizi ni magonjwa ambayo yanashambulia mazao yetu likiwemo zao la mpunga kama Mheshimiwa Susan alivyosema.
Mheshimiwa Spika, Serikali tunatambua mazao haya, ni lazima tuweke jitihada ya kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa wakulima wetu kwa sababu nchi zinazunguka Tanzania zina uhitaji mkubwa wa mchele na mazao mengine. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Susan kwamba Serikali inatambua changamoto zilizopo kwenye mabadiliko ya tabianchi. Kwa kupitia Taasisi zetu za TARI na ASA, tutaenda hata Jimboni kwake kuangalia changamoto alizozitaja ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Serikali yetu kwa ujumla kwa jibu hilo zuri.
Hata hivyo ili tuwe na uelewa wa pamoja kati ya Serikali na wakulima wa tumbuku wa Namtumbo; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuzifafanua changamoto hizo za mnunuzi wa tumbaku zinavyotakiwa kutatuliwa na Serikali kwa ujumla wake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, wakulima wa Namtumbo wanalishukuru sana Bunge lako tukufu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa kwa umahiri mkubwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu kwa kuwawezesha wakulima wa Namtumbo hadi sasa katika minada mitatu tu wamepata shilingi bilioni 5.5 la zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari kuendelea kutatua changamoto za wakulima wa Namtumbo hususan katika mazao ya korosho, soya, mbaazi na mengineyo na hasa katika korosho wale wakulima wachache ambao mpaka sasa hawajalipwa, wameuza korosho zao mwezi wa kumi hususan wa Tarafa wa Sasawala, lini watalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Ngonyani angependa kupata commitment ya Serikali kama tunaweza tukakaa pamoja na Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wakulima wake ili kuweza kutatua changamoto ambazo anakabiliana nazo huyu mwekezaji PATL. Kwa sababu ya muda na kwa vile Mheshimiwa Ngonyani ni mfuatiliaji mzuri, hili ni swali la pili katika kikao hiki basi nimuahidi kwamba nitakaa naye na tutafute muda kuweza kukaa pamoja na kuainisha hizi changamoto ambazo tayari Wizara tunazifahamu na kuzijadili na kuangalia namna bora ya kuzitatua haraka iwezekanavyo ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na uwekezaji, wakulima wetu waweze kupata mahali pa kuchakata tumbaku yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Ngonyani anauliza kama Serikali iko tayari kufanya maboresho na kuongeza jitihada za kuhakikisha mazao ya korosho, soya, mbaazi na mazao mengineyo yanamsadia mkulima Mtanzania na jibu ni ndiyo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote haya na mengine tunaongeza uzalishaji na tunawasaidia wakulima wetu kuwa na kilimo cha tija na sambamba na hilo tunawasaidia wakulima wetu kuwaunganisha na masoko. Suala la malipo ya korosho nimhakikishie Mbunge kuwa Serikali inaendelea kufanya kila iwezekanavyo kuhakikisha waliobaki ambao hawajalipwa na ambao ni wachache waweze kulipwa malipo yao, ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa huyu mwekezaji amefanya jitihada kabisa kuhakikisha kwamba anawekeza katika kile kiwanda na amewekeza anadai zaidi ya dola za Marekani milioni tatu na hivi sasa alikuwa amesimama kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikimkabili. Lakini Serikali tumepanga kabisa kwamba ndani ya wiki mbili hizi tutakaa naye ili tuweze kuzungumza pamoja ikiwa ni pamoja na kuangalia suala lile la madai ya VAT ambayo yalikuwa yamekaa muda mrefu ambayo anasema kwamba yamemuathiri katika kuendeleza hiki kiwanda. Kwa hiyo, tutakaa naye pamoja na makampuni mengine yale ambayo nayo yana changamoto hiyo hiyo ili tuweze kuhakikisha kwamba hili suala linafikia mwisho na kusudi waendelee kununua zao letu la tumbaku. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Nafahamu nchi inatambua kwamba, tarehe 22 kutakuwa na mchezo mkubwa ambao unaweza ukabeba record ya nchi wa Simba Sports Club na Kaiza Chiefs hapa Dar es Salaam. Nataka niulize kwa sababu, mchezo huu unaenda kubeba mafanikio ya timu karibu nne endapo Simba itafuzu, Yanga na timu nyingine. Je, ni mkakati upi wa Serikali wa makusudi kuhakikisha Simba Sports Club tarehe 22 inashinda na mashabiki wanajaa uwanjani?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nikupongeze Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kuchaguliwa na kurudi kwenye Kiti chako, unatosha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumekuwa tukisema timu inaposhinda na kuiwakilisha nchi yetu inakuwa ni timu ya Taifa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuipongeza Simba Sports Club kwa hatua waliyofikia na nitoe wito kwa Watanzania wote kuhakikisha tunaiunga mkono timu ya Simba Sports Club ili match itakayoicheza tarehe 22 waweze kupata ushindi. Ushindi huo utakuwa ni heshima kwa nchi yetu. Kwa hiyo, tunawatakia heri Simba Sports Club na sisi Serikali tuko pamoja nao pamoja na vilabu vyote nchini kwa manufaa ya maendeleo ya michezo nchini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la madaraja katika Jimbo la Mbinga Vijijini ni sawa na tatizo la baadhi ya vijiji katika jimbo la Biharamulo. Kwa mfano; Kijiji cha Nemba kwenye Kata ya Nemba kuna Kijiji cha Kisenga kwenda Nyamazina, kuna makorongo makubwa sana watu hawawezi kupita na ni sehemu yenye mazao mengi Lusahunga, Midaho kwenda njia panda, Nyakahura kuna Kalukwete kwenda Msali B na Nyevyondo kwenda Ngara. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa madaraja ili wananchi hao waweze kuunganishwa na hatimaye waweze kupata huduma wanazostahili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo TARURA inategemewa na Waheshimiwa Wabunge katika kutoa huduma kwenye majimbo yetu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, juzi tuliita wakandarasi wote nchini ambao wanahudumu kupitia TARURA, tuliita Mameneja wa Wilaya ya Mikoa ili kuweza kujipanga vyema kufanya kazi kwa weledi katika kuhudumia barabara za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie tunajenga TARURA mpya. Tumejifunza upande wa TANROADS kwa mfano kwenye masuala ya manunuzi, TANROADS huwa wanaanza mipango yao kuanzia Aprili kwa assumption kwamba haijawahi kutoka Wizara ikapata bajeti pungufu kwa mwaka fedha unaofuata pungufu ya asilimia 60 ya bajeti iliyopita. Kutokana na hilo TANROADS huwa wanafanya mipango ya manunuzi kuanzia Aprili ili inapoanza Julai 1 ya mwaka wa fedha wakandarasi wanakuwa wapo tayari kwenda site kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, utaratibu huo tunauleta ndani ya TARURA na tuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kupitia tozo kwa lita shilingi mia moja tayari TARURA kuna zaidi ya bilioni 322 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye barabara kwenye wilaya zetu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TARURA kuweza kupata Mifuko zaidi ya miwili ambayo tulikuwa nayo, Mfuko wa Tozo tumeona umeanza kutuletea fedha na Waheshimiwa Wabunge tutajipanga vizuri kuhakikisha huduma bora ya barabara za wananchi wetu vijijini na kwenye wilaya zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia kwenye mwaka wa fedha tutakaoleta Bajeti Bungeni hapa, Waheshimiwa Wabunge wataona mabadiliko na tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya upembuzi yakinifu mapema badala ya kusubiri kupata fedha ndiyo TARURA ikafanye usanifu, sasa hivi tutakuwa tunafanya mapema, tunakuwa tuna database, fedha inapopatikana tunakwenda kwenye utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye swali la Mheshimiwa Ndugu yangu Liuka Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, ametaja barabara ambayo inaunganisha mikoa miwili. Dhamira ya TARURA ni kuvipa vipaumbele barabara kama hizo ni kwa sababu ni barabara za kimkakati. Kwa hiyo, tutabainisha hilo kwenye jimbo lake pamoja na majimbo yote ili kuhakikisha tunapotekeleza fedha inavyokwenda basi hiyo barabara inaleta impact za kiuchumi kwa wanachi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Wizara, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza; je, Wizara haioni umuhimu wa kuwawezesha halmashauri kutenga maeneo mahususi kwa wajasiriamali na kuyawekea miundombinu stahiki ili wale wanaopokea mikopo waweze kuanzia miradi yao na shughuli zao kwenye maeneo haya ambayo yatakuwa kama incubation center na pia waweze kupewa ushauri nasaha?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa vile tunafahamu kwamba mikopo inayotolewa na NEDF chini ya SIDO inalipika, inarejeshwa kwa kiwango kikubwa cha zaidi ya aslilimia 90. Je, Wizara haioni umuhimu wa kushirikisha SIDO kwenye kutoa mikopo ya halmashauri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba halmashauri zetu lazima zitenge maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji na maeneo haya pia wanufaika vikundi ambavyo vinakopa asilimia zile 10 wawe ni moja ya wanufaika katika maeneo haya ambayo yanatengwa mahususi kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hili tumeboresha zaidi, tumeshakaa na Wizara ya Kilimo kuangalia hata makundi ya vijana wasomi ambao wanapata asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu, Majiji na Manispaa, kuangalia namna bora ya kuweza kuwasaidia maeneo mahususi kama haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hili tunalifanyia kazi na nitumie nafasi hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini, kuhakikisha maagizo ya Serikali ya kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji yanashughulikiwa. Tunashirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili kuweza kuliratibu hili vyema kwa sababu yapo masuala ya fidia. Halmashauri nyingine zimekuwa na nia ya kutenga maeneo, lakini wanakosa fedha kwa ajili ya fidia. Kwa hiyo, yote haya tunayaangalia ndani ya Serikali ili kuhakikisha tunaratibu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu mikopo ya SIDO na mikopo kupokea, hili ni eneo lingine ambalo Wizara Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara tunaangalia namna ya ku-link pamoja ili zile asilimia 10 ambazo tunazitoa kwenye halmashauri na fedha kupitia Mifuko mengine ndani ya Serikali, tunakaa pamoja na kuangalia namna bora ya kuipeleka kwenye makundi ili iweze kuleta tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili kwenye suala la asilimia 10 mikopo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanya tathmini ya nchi nzima kuangalia namna bora tutakayoweza kutumia fedha hizi kwa sababu tumetathmini ni takriban zaidi bilioni 60 kila mwaka zinapatikana kupitia halmashauri kupitia vikundi.
Kwa hiyo, tungependa kuona mabilioni haya yanapokwenda kwenye vikundi yanaleta tija, yanasaidia vikundi, lakini vikundi hivi vinasaidia nchi katika kujenga uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tathmini hii kufanyika, tutaleta hapa Bungeni uchambuzi huo ili Waheshimiwa Wabunge waweze kushauri ili tuweze kwenda vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nami niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba hizo pesa za 10% katika Halmashauri zote nchini Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo CAG ametoa ripoti ya upotevu wa fedha hizo; haoni sasa ni wakati wa Serikali kusimamia fedha hizo zinazokopeshwa kwa vikundi zinarudi kwenye Halmashauri na zinakopesha tena vikundi vingine vingine?Ahsante kwa kunisikiliza.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba
kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, bondia mwenzangu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Ndugange kwa namna anavyojibu maswali vizuri na kwa ufasaha. Niendelee kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kunipa Naibu Mawaziri ambao tunashirikiana vizuri katika kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanya tathmini nzima ya 10% ambazo zinaenda kwa vijana, akina mama na ndugu zetu, watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, concern ambayo Mheshimiwa Sophia Mwakagenda ameisema, zikiwemo hoja za CAG, ni sehemu ya uchambuzi huu. Kama nilivyosema, baada ya kufanya uchambuzi, tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge ili mwelekeo wa matumizi ya fedha za 10% uweze kuwa na tija na matarajio ambayo wananchi wetu pamoja na Bunge hili tutayapata. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia jibu la Mheshimiwa Waziri, na ni kweli kwamba kero ya barabara ni kubwa sana kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na Mheshimiwa Waziri ameahidi maandalizi yataanza januari, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni lini hasa ujenzi wa barabara za
DMDP utaanza katika Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na shukrani zangu za dhati kwa Serikali kwa ujenzi wa barabara lami ya Chanika - Womboza inayoanza kujengwa hivi sasa kero ambayo imeliliwa kwa muda mrefu na diwani wa Kata ya Zigiziwa Mheshimiwa Maige Selemani Maganga.
Naomba kuuliza nini kauli ya Serikali juu ya kutenga fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Dar es Salaam kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa fursa lakini nipongeze majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ninaomba nijibu mawili ya Mheshimiwa Jerry Silaa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itakamilisha majadiliano na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutengeneza barabara Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa miradi hii ni wahakikishie Mheshimiwa Jerry pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam tunashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha negotiations zinaenda haraka iwezekanavyo ili Serikali iweze kufikia makubaliano na Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nini mwongozo wa Serikali kuhusu mapato ya ndani? Nilishatoa maelekezo kwa halmashauri ambazo zinatenga asilimia 60 ya mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo kutoa asilimia 10 kwa ajili ya kutengeneza barabara za mitaa, ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwaelekeza wakurugenzi ambao wanahusika na kigezo hiki kuhakikisha asilimia kumi inatengwa na hawatengenezi barabara peke yao wanaungana na TARURA, kuwa na mpango mkakati mmoja ili wanachokitengeneza tuweze kukipima na kupata uhalisia wa matumizi wa fedha. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. Ahsante sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri hapo hapo simama, huu mradi wa bonde la Jangwani, fedha zilishatoka, wananchi wamefanyiwa tathmini ya nyumba zao miezi saba iliyopita, mpaka leo kuna sintofahamu, kuna nini huko kwenu? Nasikia mara mnataka mjenge daraja kutoka Magomeni mpaka Mjini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, negotiations kati ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali na Benki ya Dunia inaendelea. Lakini kwa sababu Serikali hii nishirikishi na Waheshimiwa Wabunge, kesho mimi, Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Fedha na Mipango na pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, tuna kikao saa saba kwa ajili ya kujadili jambo hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ya Serikali, majibu ambayo sasa yanaleta matumaini kwa maana mradi huu umekuwa wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina swali la nyongeza, lakini nina maombi kwa Serikali. Mheshimiwa Waziri Innocent Bashungwa alikuja Lindi tarehe 29 Julai, kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Kumpongeza Mheshimiwa Rais. Katika mambo ambayo tulimwomba ni suala zima la utekelezaji wa mradi huu wa TACTIC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Lindi tuna mapokeo ya mradi wa LNG, tunahitaji sasa kuboresha miundombinu mbalimbali. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba wanatuharakishia huo mwezi Januari ambao wameuahidi katika utekelezaji wa mradi huu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa kujibu kwa ufasaha, pia na Mheshimiwa Hamida Abdallah kwa ufuatiliaji wa mradi huu ambao Waheshimiwa Wabunge kutoka miji 45 wamekuwa wakiufuatilia kwa umakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maelekezo ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba baada ya Serikali kusaini na benki ya dunia Juni, 16 mwaka huu 2022, Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alituelekeza kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya TACTIC unaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kwenye tier one, miji 12 kwa maana ya majiji tayari kama nilivyosema, mkataba ulisainiwa na Serikali na Benki ya Dunia Juni 16 na usanifu wa miji 12 umeshakamilika. Sasa hivi kazi ya kutangaza kwa ajili ya kupata wakandarasi itafanyika muda wowote ili kazi zianze Machi, 2023 kwa ile miji 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tunafanya kwenye miji 15 ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema? Tunafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha tier one na tier two zina-overlap katika utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Hamida Abdallah, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwenye miji 45 msiwe na wasiwasi, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan baada ya kusaini Mkataba na Benki ya Dunia mwaka huu 2022, utekelezaji wake wa tier one, tier two na tier three viweze Kwenda kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu tuna group la TACTIC na mnafuatilia kwa karibu sana, tutakuwa tunaandaa vikao ili kuwapa mrejesho wa utekelezaji wa miradi hii utakavyokuwa unaenda. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini na maswali mawili la nyongeza.
Swali la kwanza; agizo la Serikali kwa Wizara nyingine kutoa kipaumbele cha ajira kwa Vijana wa JKT limetekelezeka kwa kiwango gani tangu 2013?
Swali la pili; inafahamika kuwa malengo ya mafunzo ya JKT siyo ajira, bali ni kufundisha ujasiriamali na uzalendo. Je, Serikali haioni haja sasa kuaajiri kutoka JKT kwa kufuata mtiririko ule wa first in first out? Kwa maana operesheni ya mwanzo wawahi kuajiriwa kuliko wale wanaofuata ili kutovunja moyo vijana wetu wazalendo. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Antipas Mgungusi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nianze na suala la first in first out, huu ndiyo utaratibu ambao unatumika, lakini wakati mwingine kunakuwa kuna uhitaji wa utaalam maalum au sifa maalum, kwa hiyo pamoja na kwamba mfumo wa first in first out unatumika, unaweza ukatumia mfumo huu lakini kundi la kwanza usipate watu wenye zile sifa maalum ambavyo Vyombo Vyetu vya Ulinzi na Usalama wanatafuta, kwa hiyo unalazimika kwenda kwenye kundi la pili.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge nimeielewa na ndiyo maana hata Waheshimiwa Wabunge wengine wamepiga makofi wakiashiria kwamba ni swali la msingi. Kwa hiyo, tunachokifanya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, sasa hivi nimeunda Kamati ambayo tunashirikisha Wizara mbalimbali hasa Wizara ambazo ni productive sectors. Wizara ya Kilimo, tayari tunashirikiana nao ninamshukuru Mheshimiwa Bashe, upande wa Kilimo cha kimkakati, tunashirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Spika, tunataka tupanue mawanda au scope ya JKT kwa kushirikisha sekta nyingine. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi ambazo zipo chini ya Wizara hizi. Kwa mfano, SIDO, VETA, TIRDO, TEMDO lakini benki yetu ya TADB. Asilimia 10 za vikundi kwenye Halmashauri tukae pamoja kama Serikali tuwe na mkakati wa pamoja ambao utashirikisha Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara hizi na Taasisi hizi ili kusaidia kutengeneza commitement ya ajira Milioni Nane ambazo tumeahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kupitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa sababu tunaandaa vijana kwenye kujifunza stadi za kazi, basi kwa mawanda hayo tunaweza tuka-absorb vijana wengi zaidi ambao wanamaliza mafunzo ya kujitolea wanarudi nyumbani. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tangu mwanzo wakati Mheshimiwa Waziri, anatoa jibu nimeonyesha masikitiko makubwa sana kwa swali langu kutojibiwa, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri, katika paragraph ya mwisho ya swali lake ameeleza ukweli kwamba swali hili lilipaswa kujibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, tena ametaja mpaka sheria ambayo inaipa Mamlaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kutangaza hizi kumbukumbu za kihistoria kwenye Gazeti la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikiombe kiti chako kwa kuwa swali halikujibiwa. Siku ya Ijumaa tarehe 28, saa tatu asubuhi niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii, iweze kuja kujibu swali hili kwa ufasaha. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu mchango wa Mheshimiwa Francis Ndulane, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunafanya kazi kwa kuwajibika kama Serikali moja na ndiyo maana nimemjibu Mheshimiwa Francis Ndulane kwamba pamoja na swali kuja Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nikaelezea sheria ambayo inatuongoza. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi tutashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuhakikisha tunashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kumwongoza na kupitia utaratibu ambao nimeueleza wa kuangalia hiki Kijiji cha Nandete kama kina sifa ya kuingia kwenye kumbukumbu za nchi yetu za maeneo ambayo yalitumika katika vita vya maji maji, ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa maeneo mengi Mikoa ya Lindi na Mtwara yalihusika katika harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika hasa Kusini mwa Bara la Afrika.
Je, Serikali ina mpango gani kuharakisha maendeleo katika maeneo hayo ambayo yaliathirika? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama yangu Tecla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa mchango wa wapigania uhuru kwa ajili ya nchi yetu kupata Uhuru kutoka kwa Mkoloni fidia yake haipimiki. Kwa sababu mashujaa hawa walijitoa kwa ajili ya nchi yetu kupata uhuru na tunajifunza kutoka kwao kwamba uzalendo huu lazima tuuendeleze na tuwe tayari kupigania nchi yetu bila kutegemea fidia, lakini vile vile nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mama yangu, Mheshimiwa Tecla, Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani inapeleka maendeleo kote nchini ikiwemo maeneo ya Mikoa ya Kusini. Kwa hiyo ningependa kumwondoa wasiwasi Mipango ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko makini katika kuhakikisha maendeleo tunayapeleka kote ikiwemo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa jeshi letu limekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ulinzi wa nchi na mipaka yake; je, ni maeneo gani kwa Zanzibar ambayo yatapewa kipaumbele katika ujenzi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mahanga katika kambi hapa nchini? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maryam Mwinyi kwa kufuatilia mambo haya ya msingi kwa ustawi wa majeshi yetu. Nimhakikishie, kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza kwamba kwenye ukarabati wa makambi ya awamu ya pili, Zanzibar imo katika vipaumbele. Ninapozungumzia Zanzibar, ni Unguja na Pemba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye awamu ya pili upande wa Zanzibar pia ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili kuhusu mahanga, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Wizara itafanya tathmini ya mahitaji ya mahanga kote nchini na kuhakikisha katika utekelezaji wa ujenzi wa mahanga pia upande wa Zanzibar wanapewa kipaumbele, ahsante sana.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefanya uchambuzi yakinifu wa Barabara kutoka Mtama – Mkwiti - Ng’unja – Litehu mpaka Tandahimba miaka mitatu nyuma. Je, lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii ina kipande korofi cha kutoka Ng’unja kuja Mkwiti. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha ya dharura kwa ajili ya kuweka lami kipande kile?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa swali la kwanza, ujenzi utaanza lini. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Katani kwa namna ambavyo amefuatilia mpaka Serikali tukafikia hatua ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mara fedha zitakapopatikana ujenzi wa barabara hii utaanza mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu kipande korofi toka Ng’unja kwenda Mkwiti, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura. Natumia nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wa TANROADS Mikoa yote kuangalia maeneo kama haya, maeneo korofi na kuyabainisha na kufanya assessment na kuleta Wizarani ili tunapokuwa tunaandaa bajeti, maeneo haya kama aliyoyasema Mheshimiwa Katani tuweze kuyaweka kwenye kipaumbele. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mrushaka kwenda mpaka Mrongo ilikuwa isainiwe tarehe 24 Agosti, lakini haikusainiwa ni lini barabara hii itasainiwa kwa umuhimu wa wananchi wa Kyerwa na Karagwe? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, wajina wangu na jirani yangu kule Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mara tu Mheshimiwa Rais, aliponiamini na kunileta Wizara hii, moja ya simu niliyoipata ilikuwa ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate akiulizia barabara hii. Nikamwahidi kwamba naomba awe na subira, niape kwanza halafu nitakapokuja ofisini basi tuangalie cha kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge na kwa vile hii barabara inapita Jimbo la Karagwe, nimegundua kwa Waheshimiwa Wabunge wengi ipo mikataba ambayo inasubiria kusainiwa kama hii ya Mheshimiwa Bilakwate, kwa hiyo, hatutowachelewesha. Nimeshamwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kufanya haraka iwezekanavyo ili mikataba hii isainiwe, Wakandarasi waanze hatua za ujenzi wa barabara hizi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Daraja la Malagarasi Lower litakuwa na kilometa saba za lami. Je, Serikali haioni haja ya kufanya upembuzi yakinifu haraka wa kipande hiki kidogo cha Simbo - Ilagala chenye kilomita 40? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nashon, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge nimeisikia na Mheshimiwa Mbunge naomba unipe muda ili niweze kufuatilia kipande cha barabara hii ili tuweze kuona lile ambalo linawezekana. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mitandao yote ya barababara ambayo ipo chini ya TANROADS, kwanza zile ambazo hatujafanya upembuzi yakinifu, tunafanya upembuzi yakinifu na kuwa na database ili fedha zinapopatikana tu ujenzi wa barabara hizi unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua pia mahitaji ni mengi ya barabara kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini naomba Waheshimiwa Wabunge wanipe muda, nitakaa na timu yangu ya Wizara lakini kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Miundombinu ya Bunge, tuangalie mahitaji haya makubwa na majira haya tunayoingia ambayo Waheshimiwa Wabunge wanafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeahidi vingi kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila aina ya jitihada fedha zinapatikana, kazi inaenda vizuri, lakini hata mahitaji ambayo bado tutaangalia namna ya kujipanga tukisaidiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, kaka yangu Kakoso, Makamu Mwenyekiti Mama Anna Kilango, tuangalie resources ambazo zinapatikana ndani ya Serikali. Tufanyaje kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge ili yale ambayo tuliwaahidi wananchi tuweze kuyatekeleza kwa kiasi kikubwa kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa jitihada inazofanya katika kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa mizuri, lakini naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika barabara hii ninayoitaja ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee wetu Hayati Benjamin William Mkapa, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo hili ambalo mimi nauliza. Sasa ni miaka 25, Serikali bado inatafuta pesa kwa ajili ya kukamilisha barabara hii. Je, Waziri atakuwa tayari katika mwaka huu kuingiza mpango ili mwaka ujao wa fedha, barabara hii ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ningependa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba ahadi za viongozi wetu Waheshimiwa Marais Wastaafu na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinatekelezwa, inaweza ikachelewa lakini haimaanishi kwamba hazitatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameongea kwa hisia kali hapa kwamba ni miaka 25 toka mpendwa wetu Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ameahidi hatujaanza utekelezaji wa barabara hii. Nimhakikishie kwamba, nitafuatilia barabara hii ili hata kama tunaanza kidogo, ilimradi tuanze kutekeleza ahadi za Viongozi wetu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Naomba kuuliza, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuokoa wananchi wa Mikwambe hasa Mtaa wa Zahanati, Rushe, Chambaruba A na B ambao wanaathirika na kutokuwa na mifereji katika barabara hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mkakati wa Serikali wa kujenga mifereji katika barabara zote za lami zilizopo katika Jimbo la Mbagala?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza na la pili Mheshimiwa Chaurembo anaulizia mkakati wa kuhakikisha barabara ambazo tunaweka lami hasa hasa kwenye majiji ni barabara ambazo ni kama barabara za mitaa. Mpango wetu ni upi katika kuhakikisha tunajega mifereji ama mitaro?
Mheshimiwa Spika, Wizara chini ya TANROADS tunayo program ya kuhakikisha barabara ambazo tunaweka lami, tunajenga na mitaro, lakini hata barabara ambazo ni za changarawe pia programu hiyo tunayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mamlaka ya Hali ya Hewa imetabiri mvua kubwa za El-Nino. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa Meneja Mkuu wa TANROADS kushirikiana na TARURA kuhakikisha barabara za TANROADS ambazo maji yanaenda kwenye barabara za TARURA wakae mara moja hasa hasa kwenye maeneo ya majiji na manispaa kujiandaa na kuhakikisha tunajitayarisha vyema kuhakikisha mvua za El-Nino zitakazonyesha basi mifereji na mitaro tutakuwa tumeitengeneza vizuri ili kuwaepushia wananchi maafa ambayo yanaweza yakatokea kwa mvua kubwa na mifereji kutokuwa vizuri.
Mheshimiwa Spika, hili la Mheshimiwa Mbunge tumelichukua, lakini nimeona nitoe maelezo ya jumla hasa kwenye majiji na manispaa Mkurugenzi Mtendaji wa TANROADS ajipange na Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA ili tuweze kulifanya kwa ufasaha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nishukuru Serikali kupitia Jeshi la Wananchi Tanzania kwa malipo ambayo wameshayafanya katika Kata ya Mbugani huko Usule ambako wananchi wote waliokuwa wanahusika wameshapewa malipo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu lilikuwa, huko kwenye buffer zone ambako ni Tambukareli; je, jeshi wana mpango gani wa kuhakikisha wanaonesha kabisa kwamba haya ni maeneo yao na haya ni maeneo ya wananchi ili kuondoa huu mgogoro uliopo? Wao hawana tatizo na eneo la jeshi, tatizo lao ni kujua mipaka ya jeshi iko wapi na wao wanaishia wapi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kwa Jeshi la Wananchi Tanzania na ninaomba kujibu swali lake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bunge hili nimuahidi Mheshimiwa Mbunge nitaambatana naye ili tufike eneo hili pamoja na Idara ya Miliki na Majenzi kutoka Wizarani ili tuweze kuangalia changamoto hii, lakini niwahakikishie wananchi wa maeneo haya tutaweka mipaka bayana ili wananchi wajue wanaishia wapi na jeshi linaishia wapi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wetu lakini bado kuna michango mingi sana ambayo inakera kwa wazazi. Mfano katika shule za kwetu huko vijijini, shule inaambiwa iwe ya bweni, mzazi anahitajika atoe mpaka kitanda, na kuna baadhi mpaka hela ya chakula. Sasa inapotokea mzazi ameshindwa kutoa hizo huduma ambazo anatakiwa achangie mtoto anaadhibiwa.
Je, Serikali ina kauli gani kuhusu hizi shule ambazo zinatoa adhabu kwa wanafunzi, badala ya kwa mzazi ambaye ameshindwa kuhudumia hiyo michango?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake fasaha.
Mheshimiwa Spika, pia niipongeze sana Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, pamoja na sera ya elimu bila malipo, ambayo Serikali tunaendelea kuitekeleza, katika hili nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sera ya elimu bila malipo na kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyosoma hoja yake ya Bajeti Kuu, na sasa hivi tunaenda mpaka Form Five na Form Six tunamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa michango ya wazazi, kwenye masuala ya uendeshaji wa shule za sekondari, upo mwongozo ambapo Bodi au Kamati za Shule zinashirikisha wazazi au walezi. Kwa hiyo, ningependa kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kushirikisha wazazi au walezi kupitia mwongozo ambao Serikali imeutoa namna tunavyoshikirikisha wazazi au walezi kwenye ile michango tunahitaji kushirikisha wazazi au walezi kuendesha shule zetu.
Mheshimiwa Spika, mwongozo upo bayana kwa hivyo maelekezo yangu kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu, ni kuwashirikisha wazazi kupitia vikao ambavyo vimepangwa kwa taratibu zilizopo, bodi za Shule na Kamati za Shule, hayo ndiyo maelekezo yangu. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wetu lakini bado kuna michango mingi sana ambayo inakera kwa wazazi. Mfano katika shule za kwetu huko vijijini, shule inaambiwa iwe ya bweni, mzazi anahitajika atoe mpaka kitanda, na kuna baadhi mpaka hela ya chakula. Sasa inapotokea mzazi ameshindwa kutoa hizo huduma ambazo anatakiwa achangie mtoto anaadhibiwa.
Je, Serikali ina kauli gani kuhusu hizi shule ambazo zinatoa adhabu kwa wanafunzi, badala ya kwa mzazi ambaye ameshindwa kuhudumia hiyo michango?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake fasaha.
Mheshimiwa Spika, pia niipongeze sana Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, pamoja na sera ya elimu bila malipo, ambayo Serikali tunaendelea kuitekeleza, katika hili nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sera ya elimu bila malipo na kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyosoma hoja yake ya Bajeti Kuu, na sasa hivi tunaenda mpaka Form Five na Form Six tunamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa michango ya wazazi, kwenye masuala ya uendeshaji wa shule za sekondari, upo mwongozo ambapo Bodi au Kamati za Shule zinashirikisha wazazi au walezi. Kwa hiyo, ningependa kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kushirikisha wazazi au walezi kupitia mwongozo ambao Serikali imeutoa namna tunavyoshikirikisha wazazi au walezi kwenye ile michango tunahitaji kushirikisha wazazi au walezi kuendesha shule zetu.
Mheshimiwa Spika, mwongozo upo bayana kwa hivyo maelekezo yangu kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu, ni kuwashirikisha wazazi kupitia vikao ambavyo vimepangwa kwa taratibu zilizopo, bodi za Shule na Kamati za Shule, hayo ndiyo maelekezo yangu. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Mwanza ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na Makao Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza, na Wilaya Kwimba ni miongoni ya Wilaya kongwe imeanzishwa toka mwaka 1935. Sasa angalia mpaka muda huu haijawahi kuunganishwa na barabara ya lami.
Je, ni lini Serikali itakamilisha kilomita 25 za kutoka Mwabuki kwenda Ngudu mjini ili Wananchi wa Wilaya ya Kwimba waweze kuungana na Mkoa wa Mwanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili ni kwamba, kwa kuwa barabara yetu ya Mwabuki, inaunganisha pamoja pamoja na Barabara ya Malampaka – Maswa ambayo ni katika Mkoa wa Simiyu na barabara hiyo ni ndefu inakwenda mpaka Singida. Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo? kwa sababu ya kupunguza traffic kubwa kati ya Mwanza na Singida kwa njia ya shortcut ya kupitia Maswa, Meatu pamoja na Singida, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Tabasam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi. Tunajenga hizi kilomita 28 na tumeanza na kilomita tatu, kuanzia Ngudu ambako ndiyo Makao Makuu ya Wilaya lakini vilevile kwa Barabara ya Magu – Ngudu tumeanza kujenga kilomita 10 kutoka Magu kwenda Ngudu. Kwa hiyo mtandao huu utaunganisha Wilaya ya Kwimba na Mwanza kwa maana ya Mwanza mjini, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Tabasam na Mheshimiwa Mansoor kwamba maendeleo ni hatua tumeanza hivyo lakini nia ni kuiunganisha Wilaya ya Kwimba pamoja na Mwanza, kwa maana ya Mwanza mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu swali la pili Mwabuki - Maswa; sasa hivi Serikali ipo kwenye Miradi saba ya EPC+F ipo barabara yenye kilomita 389 ambayo inaanzia Mbulu kuja Manyara, Singida mpaka Maswa. Barabara hii inaenda kuunganisha Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kanda ya Ziwa na ikishafika pale Maswa na mitandao hii ambayo nimeitaja tutakuwa tumeunganisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Singida na Mikoa ya Kaskazini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwaka jana tarehe 16 Juni, tulisaini Mikataba ya Barabara za EPC+F ya Kongwa – Kiteto – Arusha. Naomba kufahamu lini Mradi huu unaanza kwa sababu Wananchi wa Kiteto tunausubiri kwa hamu sana?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nilijibu kwa package yote ya miradi yote ya EPC+F, miradi saba. Kama nilivyosema wakati nachangia kwenye hoja ya Kamati ya Miundombinu, design ya barabara hizi ilifanywa na TANROADS mwaka 2017 miaka mingi imepita. Kwa hiyo Wakandarasi ambao wamepatikana wanafanya mapitio ya design ili kuweza ku-update usanifu wa kina, na baada ya hapo barabara hizi zitaanza kujengwa mara moja. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Olelekaita pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao mnasubiri hii Miradi ya EPC+F tuko tunajipanga usanifu, mapitio yakikamilika basi tutaanza ujenzi wake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa taratibu zote za Ujenzi wa Kipande cha Barabara kati ya Nansio – Lugezi – Kisolya umekamilika lakini Mkandarasi hajafika site. Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya mradi huu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia barabara hii tumepeleka hazina yapo masuala ya VAT lakini nimhakikishie nitakaa na Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ili maombi ambayo tumeyapeleka ya VAT waweze kutukamilishia na ujenzi wa barabara hii uweze kuanza mara moja. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Namtumbo tuna barabara ambayo inatoka Makao Makuu ya Wilaya inapitia katika Kata ya Likuyu, Mgombasi inaunganisha mpaka kwenye Kata ya Kitanda. Kuna daraja ambalo ni la zamani sana lipo katika Mto Uwegu ambalo katika mvua hizi limesukumwa hilo daraja na kufanya kuhatarisha maisha ya Wananchi na vyombo vyao. Je, Serikali iko tayari sasa kuiweka kwa dharura bajeti ya kutengeneza daraja hili la Mto Uwegu ambalo linaunganisha Kata ya Namtumbo, Likuyu na Mgombasi? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kuwa Mheshimiwa Kawawa ameishakuja kuniona kuhusu daraja alilolitaja. Nimeona video na namna ambavyo mawasiliano yamekatika. Nitumie nafasi hii nimuagize Meneja wa TANROAD Mkoa wa Ruvuma kuwasilisha mahitaji ya daraja la dharula katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Kawawa alinionyesha ili tuweze kumpelekea daraja la dharula la chuma, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga – Muyangayanga – Mahenge – Litembo ina urefu wa kilometa 25. Ninaishukuru Serikali imejenga vipande vya lami kwenye maeneo korofi.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema tumeanza kujenga maeneo korofi. Nimhakikishie kwamba kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana tutaendelea kuboresha maeneo ambayo yanahitaji kudhibitiwa, ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati ambako kuna visima na mitambo ya gesi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jambo hili kwenye Ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara mliliulizia na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni barabara hii ni ya muhimu. Kwa hiyo tunaendelea kujipanga kadri fedha zitakapopatikana tutaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tangu mwezi Juni, mwaka jana tumesaini Mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mnivata – Newala – Masasi. Je, ni lini ujenzi huu utaanza? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota ameulizia barabara hii ni sehemu ya ile miradi ya barabara za EPC+F. Kama nilivyoeleza, tuko hatua za mwisho za mapitio ya usanifu wa kina ili ujenzi wa barabara hizi uweze kuanza ikiwemo hii barabara ambayo Mheshimiwa Chikota ameuliza.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Barabara ya Bujera – Masukulu – Matwebe hadi Kyela ni barabara muhimu sana kiuchumi katika Wilaya ya Rungwe. Ni lini Mheshimiwa Waziri utatusaidia ili barabara hii iwe katika kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tutaijenga kama tulivyoipanga kwenye bajeti, kile ambacho tumeweka kwenye bajeti nikuhakikishie tutakizingatia na kama hakipo basi tutajitahidi kujenga barabara hii kadri bajeti itakavyoturuhusu kwenye hizo bajeti zijazo, ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni nini, kauli ya Serikali katika kuipanua barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma kutokana na ufinyu wake na matumizi makubwa ya barabara hii.
Je, Serikali haioni haja ya kuipanua barabara hii na kuifanya njia nne?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa ufatiliaji wake, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na Dar es Salaam ndiyo Commercial City ya nchi yetu, kwa hiyo, ni vizuri tukaviunganisha kwa mawasiliano ya barabara ya uhakika. Bahati nzuri kama nilivyosema juzi, kwenye hoja za Kamati ya Miundombinu, tunapanga kujenga barabara hii ya kutoka Kibaha inapoishia njia nane, Chalinze, Morogoro mpaka Dodoma kutumia utaratibu wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari wapo wabia ambao wamejitokeza tunaendelea na mazungumzo nao, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Tarimba pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote tunahitaji barabara hii kuunganisha Dar es Salaam pamoja na Dodoma, tuko mbioni kuijenga barabara ya Express Way Dar es Salaam – Dodoma kwa njia ya PPP, ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam ndani ya miezi michache itaanza kufanya kazi na kuna uwekezaji mkubwa kwenye kituo cha treni pale Kilosa, wakati huo huo kuna uwekezaji zaidi ya dola milioni 120 kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambayo inaenda kuongeza ndege mpaka 50 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukamilika kwa barabara ya kutoka Kilosa kuja Mikumi kuunganisha miundombinu hii miwili muhimu sana kwa Taifa letu; je, ni amri, taaluma au utaalamu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Londo, nimhakikishie barabara hii ni muhimu na Serikali inafanya kila jitihada lakini yote haya yanategemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie fedha zitakapopatikana tutaweka barabara hii kuijenga kwenye utaratibu aliouomba. Nakushukuru sana.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; ni lini, Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais kujenga barabara ya lami kutoka kipande cha Ngaresero mpaka Engaruka kilomta 39?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Ole-Shangai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara hii na ahadi za Viongozi wetu ni maelekezo, tayari barabara hii tumeiweka kwenye kupaumbele. Kwa hiyo, nimhakikishie tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka miwili sasa bandari ya Kalema ipo tayari lakini hakuna tija iliyopatikana licha ya Serikali kuwekeza zaidi ya bilioni 47. Hii inaleta shida kwa sababu fedha za wananchi zimekaa pale na hakuna pesa inayopatikana kwa sababu tu ya ubovu wa miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali ni lini exactly barabara hii ya kutokea Kigwira kuelekea Karema, itatengenezwa ili kuokoa fedha za walipakodi? (Makofi)
Swali la pili, tuna barabara za kimikakati kuzunguka nchi za SADC. Ni lini, Serikali itaainisha barabara hizi, ili kuweza kuweka soko pamoja lakini kuokoa fedha zinazopotea na kikubwa zaidi kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na la Taifa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi barabara ambayo Mheshimiwa Felista ameitaja ya Kigwira kwenda Karema, tumeshasaini mkataba, kwa hiyo, baada ya kusaini ina maana Mkandarasi anaanza ku-mobilize mitambo ili ujenzi wa kiwango cha lami uweze kuanza. Vilevile Serikali ya Awamu ya Sita hatujaishia hapo, dhamira ya Serikali Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya SADC pia kuna African Union 2063 (The Africa We Want).
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha position ya Tanzania katika mikakati ya kiuchumi kwenye jumuiya hizi nilizozitaja, EAC, SADC na AU - Vision ya 2063 (The Africa we want). Tanzania tunataka tujipange tuwe vinara wa kiuchumi. Kwa hiyo, ujenzi wa barabara hizi na nchi za jirani siyo kwamba tunajenga tu kwa sababu tunawapenda sana, ndiyo ni mahusiano mazuri pia kimkakati lazima tuji-position ili kuweza kujenga uchumi imara, kutengeneza ajira kwa wananchi wetu na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo nikuhakikishie mikakati yote tunayo na tunaendelea kuitekeleza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hii kwa kilomita 27 na sasa bado kilomita 56. Je, ni lini hizi kilomita zilizobaki zinakwenda kusainiwa ukizingatia kwamba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kaka yangu Innocent Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha walitembelea Jimbo la Busokelo tarehe Mosi Oktoba na walifanya mkutano mzuri sana. Tunawashukuru sana kwa kuja, ninyi ni mashuhuda wazuri kwamba barabara hii inahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini itasainiwa? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri pia nampongeza Mheshimiwa Mwakibete kwa kuupiga mwingi kwa ajili ya wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anayoitaja Mheshimiwa Mwakibete ni moja ya barabara 15 ambazo tunasubiri kusaini. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote wa barabara hizi, Mheshimiwa Rais ameshatoa kibali kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema. Tumeona tuandae siku ambayo tutasaini mikataba hii kwa siku moja halafu baada ya hapo mimi pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri tutaambatana na Waheshimiwa Wabunge kwenda kuwakabidhi wakandarasi kwenye Majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuko mbioni katika kuandaa tukio hili ambalo tutaomba Kiongozi Mkuu wa Kitaifa aweze kushuhudia utiaji saini huu. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge, sasa tunaenda kufanya kazi na miradi hii 15 ina thamani ya shilingi 1,034,000,000. Natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge wamefanya kazi kubwa ya ufuatiliaji. Tumefika hatua nzuri na Serikali ya Awamu ya Sita hakika katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi imejipanga vizuri, ahsante. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Mwanza ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na Makao Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza, na Wilaya Kwimba ni miongoni ya Wilaya kongwe imeanzishwa toka mwaka 1935. Sasa angalia mpaka muda huu haijawahi kuunganishwa na barabara ya lami.
Je, ni lini Serikali itakamilisha kilomita 25 za kutoka Mwabuki kwenda Ngudu mjini ili Wananchi wa Wilaya ya Kwimba waweze kuungana na Mkoa wa Mwanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili ni kwamba, kwa kuwa barabara yetu ya Mwabuki, inaunganisha pamoja pamoja na Barabara ya Malampaka – Maswa ambayo ni katika Mkoa wa Simiyu na barabara hiyo ni ndefu inakwenda mpaka Singida. Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo? kwa sababu ya kupunguza traffic kubwa kati ya Mwanza na Singida kwa njia ya shortcut ya kupitia Maswa, Meatu pamoja na Singida, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Tabasam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi. Tunajenga hizi kilomita 28 na tumeanza na kilomita tatu, kuanzia Ngudu ambako ndiyo Makao Makuu ya Wilaya lakini vilevile kwa Barabara ya Magu – Ngudu tumeanza kujenga kilomita 10 kutoka Magu kwenda Ngudu. Kwa hiyo mtandao huu utaunganisha Wilaya ya Kwimba na Mwanza kwa maana ya Mwanza mjini, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Tabasam na Mheshimiwa Mansoor kwamba maendeleo ni hatua tumeanza hivyo lakini nia ni kuiunganisha Wilaya ya Kwimba pamoja na Mwanza, kwa maana ya Mwanza mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu swali la pili Mwabuki - Maswa; sasa hivi Serikali ipo kwenye Miradi saba ya EPC+F ipo barabara yenye kilomita 389 ambayo inaanzia Mbulu kuja Manyara, Singida mpaka Maswa. Barabara hii inaenda kuunganisha Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kanda ya Ziwa na ikishafika pale Maswa na mitandao hii ambayo nimeitaja tutakuwa tumeunganisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Singida na Mikoa ya Kaskazini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mwaka jana tarehe 16 Juni, tulisaini Mikataba ya Barabara za EPC+F ya Kongwa – Kiteto – Arusha. Naomba kufahamu lini Mradi huu unaanza kwa sababu Wananchi wa Kiteto tunausubiri kwa hamu sana?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nilijibu kwa package yote ya miradi yote ya EPC+F, miradi saba. Kama nilivyosema wakati nachangia kwenye hoja ya Kamati ya Miundombinu, design ya barabara hizi ilifanywa na TANROADS mwaka 2017 miaka mingi imepita. Kwa hiyo Wakandarasi ambao wamepatikana wanafanya mapitio ya design ili kuweza ku-update usanifu wa kina, na baada ya hapo barabara hizi zitaanza kujengwa mara moja. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Olelekaita pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao mnasubiri hii Miradi ya EPC+F tuko tunajipanga usanifu, mapitio yakikamilika basi tutaanza ujenzi wake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa taratibu zote za Ujenzi wa Kipande cha Barabara kati ya Nansio – Lugezi – Kisolya umekamilika lakini Mkandarasi hajafika site. Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya mradi huu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia barabara hii tumepeleka hazina yapo masuala ya VAT lakini nimhakikishie nitakaa na Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ili maombi ambayo tumeyapeleka ya VAT waweze kutukamilishia na ujenzi wa barabara hii uweze kuanza mara moja. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Namtumbo tuna barabara ambayo inatoka Makao Makuu ya Wilaya inapitia katika Kata ya Likuyu, Mgombasi inaunganisha mpaka kwenye Kata ya Kitanda. Kuna daraja ambalo ni la zamani sana lipo katika Mto Uwegu ambalo katika mvua hizi limesukumwa hilo daraja na kufanya kuhatarisha maisha ya Wananchi na vyombo vyao. Je, Serikali iko tayari sasa kuiweka kwa dharura bajeti ya kutengeneza daraja hili la Mto Uwegu ambalo linaunganisha Kata ya Namtumbo, Likuyu na Mgombasi? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kuwa Mheshimiwa Kawawa ameishakuja kuniona kuhusu daraja alilolitaja. Nimeona video na namna ambavyo mawasiliano yamekatika. Nitumie nafasi hii nimuagize Meneja wa TANROAD Mkoa wa Ruvuma kuwasilisha mahitaji ya daraja la dharula katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Kawawa alinionyesha ili tuweze kumpelekea daraja la dharula la chuma, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga – Muyangayanga – Mahenge – Litembo ina urefu wa kilometa 25. Ninaishukuru Serikali imejenga vipande vya lami kwenye maeneo korofi.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema tumeanza kujenga maeneo korofi. Nimhakikishie kwamba kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana tutaendelea kuboresha maeneo ambayo yanahitaji kudhibitiwa, ahsante sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati ambako kuna visima na mitambo ya gesi kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jambo hili kwenye Ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara mliliulizia na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni barabara hii ni ya muhimu. Kwa hiyo tunaendelea kujipanga kadri fedha zitakapopatikana tutaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tangu mwezi Juni, mwaka jana tumesaini Mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mnivata – Newala – Masasi. Je, ni lini ujenzi huu utaanza? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota ameulizia barabara hii ni sehemu ya ile miradi ya barabara za EPC+F. Kama nilivyoeleza, tuko hatua za mwisho za mapitio ya usanifu wa kina ili ujenzi wa barabara hizi uweze kuanza ikiwemo hii barabara ambayo Mheshimiwa Chikota ameuliza.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Barabara ya Bujera – Masukulu – Matwebe hadi Kyela ni barabara muhimu sana kiuchumi katika Wilaya ya Rungwe. Ni lini Mheshimiwa Waziri utatusaidia ili barabara hii iwe katika kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tutaijenga kama tulivyoipanga kwenye bajeti, kile ambacho tumeweka kwenye bajeti nikuhakikishie tutakizingatia na kama hakipo basi tutajitahidi kujenga barabara hii kadri bajeti itakavyoturuhusu kwenye hizo bajeti zijazo, ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni nini, kauli ya Serikali katika kuipanua barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma kutokana na ufinyu wake na matumizi makubwa ya barabara hii.
Je, Serikali haioni haja ya kuipanua barabara hii na kuifanya njia nne?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa ufatiliaji wake, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na Dar es Salaam ndiyo Commercial City ya nchi yetu, kwa hiyo, ni vizuri tukaviunganisha kwa mawasiliano ya barabara ya uhakika. Bahati nzuri kama nilivyosema juzi, kwenye hoja za Kamati ya Miundombinu, tunapanga kujenga barabara hii ya kutoka Kibaha inapoishia njia nane, Chalinze, Morogoro mpaka Dodoma kutumia utaratibu wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari wapo wabia ambao wamejitokeza tunaendelea na mazungumzo nao, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Tarimba pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wote tunahitaji barabara hii kuunganisha Dar es Salaam pamoja na Dodoma, tuko mbioni kuijenga barabara ya Express Way Dar es Salaam – Dodoma kwa njia ya PPP, ahsante Sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam ndani ya miezi michache itaanza kufanya kazi na kuna uwekezaji mkubwa kwenye kituo cha treni pale Kilosa, wakati huo huo kuna uwekezaji zaidi ya dola milioni 120 kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambayo inaenda kuongeza ndege mpaka 50 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukamilika kwa barabara ya kutoka Kilosa kuja Mikumi kuunganisha miundombinu hii miwili muhimu sana kwa Taifa letu; je, ni amri, taaluma au utaalamu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Londo, nimhakikishie barabara hii ni muhimu na Serikali inafanya kila jitihada lakini yote haya yanategemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie fedha zitakapopatikana tutaweka barabara hii kuijenga kwenye utaratibu aliouomba. Nakushukuru sana.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; ni lini, Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais kujenga barabara ya lami kutoka kipande cha Ngaresero mpaka Engaruka kilomta 39?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Ole-Shangai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara hii na ahadi za Viongozi wetu ni maelekezo, tayari barabara hii tumeiweka kwenye kupaumbele. Kwa hiyo, nimhakikishie tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka miwili sasa bandari ya Kalema ipo tayari lakini hakuna tija iliyopatikana licha ya Serikali kuwekeza zaidi ya bilioni 47. Hii inaleta shida kwa sababu fedha za wananchi zimekaa pale na hakuna pesa inayopatikana kwa sababu tu ya ubovu wa miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka commitment ya Serikali ni lini exactly barabara hii ya kutokea Kigwira kuelekea Karema, itatengenezwa ili kuokoa fedha za walipakodi? (Makofi)
Swali la pili, tuna barabara za kimikakati kuzunguka nchi za SADC. Ni lini, Serikali itaainisha barabara hizi, ili kuweza kuweka soko pamoja lakini kuokoa fedha zinazopotea na kikubwa zaidi kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na la Taifa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi barabara ambayo Mheshimiwa Felista ameitaja ya Kigwira kwenda Karema, tumeshasaini mkataba, kwa hiyo, baada ya kusaini ina maana Mkandarasi anaanza ku-mobilize mitambo ili ujenzi wa kiwango cha lami uweze kuanza. Vilevile Serikali ya Awamu ya Sita hatujaishia hapo, dhamira ya Serikali Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania ni sehemu ya Jumuiya ya SADC pia kuna African Union 2063 (The Africa We Want).
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha position ya Tanzania katika mikakati ya kiuchumi kwenye jumuiya hizi nilizozitaja, EAC, SADC na AU - Vision ya 2063 (The Africa we want). Tanzania tunataka tujipange tuwe vinara wa kiuchumi. Kwa hiyo, ujenzi wa barabara hizi na nchi za jirani siyo kwamba tunajenga tu kwa sababu tunawapenda sana, ndiyo ni mahusiano mazuri pia kimkakati lazima tuji-position ili kuweza kujenga uchumi imara, kutengeneza ajira kwa wananchi wetu na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo nikuhakikishie mikakati yote tunayo na tunaendelea kuitekeleza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, sawa.
Mheshimiwa Spika, kwenye kikao cha ushauri wa barabara cha mkoa, mwaka 2022 niliambiwa zimeshatoka shilingi milioni 150 na kazi ya upembuzi yakinifu imeanza…
SPIKA: Mheshimiwa Nassor, ngoja. Ili taarifa zetu zikae vizuri kule ulipoambiwa siyo Serikali Kuu inayokuwepo, ni nyinyi watu wa mkoa ule ndiyo mpo kule. Kwa hiyo nilitaka ufafanuzi huu ili taarifa zetu zikae vizuri, kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri amefafanua kwamba kazi zitakazokamilika ni hizi zinazoendelea mpaka sasa.
Sasa kile kikao kule, wewe ulikuwepo ila mimi sikuwepo wala Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa hiyo hawezi kufafanua kuhusu kile ulichoambiwa kule. Kwa hiyo tuanzie hiki cha leo hapa Mheshimiwa, uliza maswali yako mawili ya nyongeza.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, hata kwenye Hansard wakiangalia 2022 ni kwamba imeshatengwa fedha shilingi milioni 150 na kwenye vitabu vya bajeti ilionyesha kabisa kwamba zimeshatengwa na zimetolewa. Sasa hii leo wananiambia ni Msanifu anayeenda kupatikana 2024. Wakati kule tumeambiwa kwamba Msanifu ameshaanza kazi.
SPIKA: Sawa, sasa kwa maelezo yako mwenyewe hapo unasema zimetengwa na zimeshatolewa kwenye bajeti.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Kwenye bajeti, nafikiri huwa tunatenga ama?
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, zilitengwa shilingi milioni 300 kwa 2020/2021 na mwaka 2022 ni kwamba tayari zikawa zimeshatolewa shilingi milioni 150.
SPIKA: Sawa, sasa kwa sababu kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ametaja. Kwa sababu swali lako linasema, je ni lini upembuzi yakinifu utakamilika na kuanza ujenzi wa barabara ya Kahama - Nyang’hwale - Busisi, jibu la msingi linasema utakamilika Februari, 2025. Nilitaka kujiridhisha hapo uliposema, hujaridhika na majibu. Sasa uliza maswali yako ya nyongeza kuhusu hili ambalo umeliuliza kwenye swali lako la msingi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, basi swali la pili; kwa kuwa ahadi hiyo imechukua muda mrefu, mtoto amezaliwa na amefikisha miaka 14 tangu mwaka 2010 ahadi hii imeahidiwa na Viongozi Wakuu wa Nchi, mpaka leo hii tuna miaka 13 tunakaa tunaambiwa maneno haya. Sisi wana Nyang’hwale tunataka majibu ya Serikali. Hivi ni kweli 2024 unavyosema na 2025 namwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya Bunge hili twende akawaambie wananchi dhamira ya Serikali ya kukamilisha ahadi hii. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Amar, naomba hoja yake niichukue. Nimpongeze, juzi tulikuwa tuna kikao, Mheshimiwa Hussein Amar pamoja na Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, tulikaa na Barrick, kuna barabara ya kutoka Kahama kwenda Bulyanhulu kwenda Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Amar, aliomba lami itakapofika kwenye geti la Barrick akaomba kipande cha kwenda Jimboni kwake tukae na Barrick ili kama kutakuwa kuna bakaa tujenge kile kipande. Kwa hiyo kaka yangu Mheshimiwa Amar naomba aendelee kuwa na confidence na Serikali. Hoja yake tumeichukua kwa kadri fedha zitakapopatikana na suala la usanifu tutaweka jitihada, lakini dhamira ya Serikali ni kujenga lami kwenye barabara zote ambazo upembuzi yakinifu umekamilika. Tupo pamoja Mheshimiwa Mbunge na nampongeza kwa namna ambavyo anapambana kwa wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara ambayo ameitoa alipotoka kujibu maswali Mheshimiwa Waziri kutokana na athari za mvua zinazoendelea sasa hivi imekatika na wananchi wanapata shida kubwa sana especially katika maeneo ya kwa Moris na maeneo mengine pale Kimbiji. Je, nini mkakati wa muda mfupi wa ukarabati wa barabara hii ili wananchi wa Pemba Mnazi waweze kufika katika maeneo kwa gharama nafuu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ni Barabara ya Kibada – Mwasonga. Barabara hii yenye urefu wa kilometa 41 na inatumika kwa magari mengi mazito lakini barabara hii mkataba wake umeshasainiwa mwezi Machi, 2024 na sasa hivi imeharibika sana. Wananchi wa Kigamboni wanataka kujua na kupata kauli ya Serikali ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndugulile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuhusu Mvua za El-Nino zinazoendelea na kukatika kwa barabara. Nitumie nafasi hii kuendelea kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wameendelea kutupa ushirikiano kwenye majimbo yao pale mawasiliano yanapokatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za emergency ili tuweze kurekebisha pale ambapo mawasiliano yanakatika. Kwa upande wa Mheshimiwa Dkt. Ndugulile nimwelekeze Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dar es Salaam kufika maeneo haya na kufanya tathmini ili tuweze kujitahidi kwa kadri inavyowezekana kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanaendelea kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kuhusu Barabara ya Kibada – Mwasonga kilometa 47, tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kutupa kibali kwa kusaini baadhi ya barabara ambazo zimefikia hatua ya kusainiwa ili ujenzi uanze. Barabara hii Jimboni kwa Mheshimiwa Ndugulile ni kweli mkandarasi alisaini mkataba huu mwezi Machi na sasa hivi namwelekeza mkandarasi kuendelea na mobilization wakati tukimtafutia taratibu za malipo ya advance. Vilevile, Mkandarasi huyu anawajibika kufanya matengenezo ya barabara kwa sababu tumeshamkabidhi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Barabara ya kutoka Mtama – Kitangali kwenda Newala Jimbo la Newala Vijijini inapitika kwa shida kwa sababu ya ubovu wa barabara ile kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuwanusuru wananchi wa Newala na hali ambayo ipo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Mtama – Newala ni kweli barabara hii Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiomba muda mrefu kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuitengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe. Kwenye vipaumbele vya Wizara ya Ujenzi tutaangalia namna ya kuanza kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana kwa kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Makofia – Mlandizi – Mlandizi Vikumburu imeshafanyiwa tathmini na wananchi wanasubiri kupata fidia. Je, Serikali imefikia hatua gani ya kuwalipa ili barabara hii iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael kuhusu Barabara ya Makofia – Mlandizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kipaumbele kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, lakini naomba yeye pamoja na wananchi waendelee kuwa na Subira, tutaiweka kwenye vipaumbele kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba Barabara ya kutoka Bunju B kwenda Mabwepande mpaka Ubungo ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu, lakini Mheshimiwa Gwajima na Waheshimiwa Wabunge kama wanavyofahamu sasa hivi kuna ukatikaji wa mawasiliano ya barabara na madaraja kote nchini, kipaumbele namba moja ni kuhakikisha tunarudisha mawasiliano haya ili shughuli za uzalishaji kiuchumi na kijamii ziweze kuendelea. Kwa hiyo barabara hizi ikiwemo hii barabara ambayo Mheshimiwa Gwajima amekuwa akiifuatilia kwa karibu tumuahidi yeye pamoja na wananchi kwamba kadri fedha zitakavyopatikana na yenyewe tutaiweka kwenye vipaumbele. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi (Dar es Salaam Metropolitan Development Project Phase Two)?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kuwalipa fidia wananchi wanaoishi katika eneo la mradi wa ujenzi wa Daraja la Jangwani kuanzia Magomeni, Jangwani hadi Fire? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa Daraja la Jangwani tunafanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maana ya ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Suala la fidia linaenda sambamba na jitihada hizi za ujenzi kupitia Mradi wa DMDP.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali tumejipanga, Wizara ya Ujenzi wakati tunajenga Daraja. Pia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia mradi wa DMDP tutashirikiana kuhakikisha ujenzi unaenda sambamba na fidia kwa wananchi, ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Itoni - Lusitu ambayo imesimamisha ujenzi kwa takribani 10, na miezi mitatu ijayo mvua itakuwa imeanza. Kwa hiyo, barabara hii kama haitaanza kujengwa, mwaka mzima mkandarasi yupo offsite hakuna kinachoendelea, Serikali ina mpango gani kuendeleza ujenzi wa barabara hii?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Mwanyika, ameulizia barabara ya Itoni – Lusitu. Habari iliyo njema ni kwamba, Waheshimiwa Wabunge pochi ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imeanza kufunguka. Tumeanza kupokea fedha kwa ajili ya advance payment ikiwemo barabara hii ya Itoni – Lusitu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge, mmefuatilia advance payment kwa muda mrefu. Sasa hivi pochi ya mama imefunguka, tutaanza kutoa advance payment kwenye barabara hii pamoja na barabara nyingine, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Mogabiri – Nyamongo – Serengeti, Mkandarasi ametoa vifaa site na anaidai Serikali shilingi bilioni 7.8. Barabara hii inahudumia Wilaya ya Tarime na Wilaya ya Serengeti. Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa barabara hii kuendelea ili kutoa matumaini kwa watu wa Tarime?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waitara, amekuwa akiifuatilia barabara hii kwa ukaribu sana na habari iliyo njema ni kwamba, zile advance payment tulizozipata, barabara hii pia ni miongoni mwa hizo barabara. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waitara kwa ufuatiliaji.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 2.5 ambayo wameitoa kwa wananchi wetu. Swali langu dogo ni kwamba; je, ni lini wananchi waliobakia bila kulipwa nje ya mita 22.5 watapewa majibu yao baada ya kupitiwa na Kamati ya Mheshimiwa DC na Meneja wa TANROADS mkoa ambayo waliiunda baada ya kuonekana kuna malalamiko ya baadhi ya wananchi hawajalipwa?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asenga kuhusu fidia ya wananchi ambao wako kwenye nje ya mita 22.5. Cha kwanza kabisa naomba niweke rikodi sawa. Mwananchi yeyote ambaye yuko ndani ya mita 22.5 mwenye X nyekundu kwa mujibu wa sheria hastahili kulipwa fidia, lakini wananchi ambao wako kwenye mita 7.5 kila upande wa barabara kwa Sheria Namba 13 ya Mwaka 2007 tuliongeza upana wa barabara kutoka mita 45 kwenda mita 60, 7.5 kila upande wananchi hao huwa tunawawekea alama ya X ya kijani. Maana yake ni kwamba tutakapoanza kujenga barabara wananchi hao wanastahili fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaomba wale ambao wana alama ya X ya kijani tutakapoanza ujenzi, basi tutatoa fidia kwa mujibu wa sheria.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Barabara ya Mianzini – Sambasha – Ngaramtoni tunaishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi kwa kulipa fidia baadhi nya wananchi zaidi ya shilingi bilioni 1.7, lakini kuna wananchi ambao bado hawajakamilishiwa fidia zao katika barabara hiyo. Nataka kujua ni lini Serikali itakamilisha kuwalipa fidia hao wananchi waliobaki ili barabara hiyo iendelee kwa sababu kwa sehemu fulani imesimama?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimwagize Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Arusha kuhakikisha wananchi hawa wanaostahili malipo kwa mujibu wa sheria kama wanastahili basi walete Wizarani mara moja ili tuweze kufikisha Hazina kwa ajili ya mchakato wa malipo. Nakushukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali la kwanza; Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa nini sasa Serikali isiruhusu magari machache kupita ili kupunguza gharama ya vifaa ambayo inasababishwa na gharama ya usafiri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; eneo la Kwai lina kona ambayo ni kali sana na mara nyingi husababisha magari kufeli. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika eneo hilo?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Shabani Shekilindi kuhusu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu magari machache kupita, concern ya Mheshimiwa Mbunge tumeipokea. Nimwagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga kufanya tathmini kwa kushirikiana na vyombo vingine ili kuona kama hili linawezekana kwa sababu concern yetu ni kuhakikisha watumia barabara wanakuwa salama. Kwa hiyo, kama itakuwa salama kwa mujibu wa tathmini tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuweka daraja kwenye kona kali, kama nilivyosema Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia hili na tumefanya usanifu wa kina na tumekamilisha. Kwa hiyo, kwa kadri fedha zitakavyopatikana ujenzi wa daraja hili utakuwa ni kipaumbele. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya njia ya kutatua changamoto ya barabara iliyoulizwa kwenye swali la msingi ni kutumia barabara mbadala ambayo ni ya kutoka Korogwe kupita Dindila – Bumbuli mpaka Soni. Kwenye bajeti Mheshimiwa Waziri aliahidi kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Mpaka leo kuna ukimya, ni ipi kauli ya Serikali juu ya jambo hili?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri Mheshimiwa Mnzava amekuwa akifuatilia barabara hii ambayo ni mbadala kama alivyosema. Ni kweli na kwenye bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mnnzava pamoja na wananchi wake, kwamba kwa vile tumeiweka kwenye bajeti maana yake ni kipaumbele kwa upande wa Serikali na tuko kwenye hatua za kutekeleza bajeti hii. Kwa hiyo, fedha zitakapopatikana tutaijenga barabara hii ili iweze kuwahudumia wananchi lakini pia iwe kama mbadala wa ile barabara ya kwenda Bumbuli kutokea Lushoto. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Ujenzi wa Barabara hii ya lami ya kutoka Kibondo mpaka Mabamba umekwishaanza; na kama ilivyooneshwa kwenye majibu ya msingi, wananchi 724 wa Kata nne za Bitare, Misezero, Bunyanbo na Mabamba hawajalipwa fidia. Je, ni lini Serikali itaharakisha utaratibu huu ili wananchi hawa 724 waweze kupata fidia yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ujenzi wa barabara ya kilomita 25 ya Kibondo Mjini kwa jina la Kibondo Town Link kutoka roundabout ya Iheba mpaka Nduta Junction unasuasua mno kwa madai kwamba mkandarasi hajalipwa pesa na ameshatoa mitambo site, amepumzika anasubiri malipo. Je, ni lini Serikali itamlipa malipo yake ili aweze kurudi site?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Florence kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia ya wananchi 724, kwanza nampongeza Dkt. Florence amekuwa akifuatilia fidia hii pamoja na miradi mingine ya barabara kwenye jimbo lake. Nimhakikishie, kwamba tumeshawasilisha maombi ya fidia Hazina na Wizara ya Ujenzi tutaendelea kufuatilia ili kuhakikisha haraka iwezekanavyo wananchi wanapata malipo hayo ya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kibondo Town Link mkandarasi kucheleweshewa fedha, kwanza nimwagize mkandarasi asisimamishe ujenzi wa barabara hii. Sisi upande wa Wizara ya Ujenzi tumekwishawasilisha mahitaji ya malipo ya mkandarasi huyu Hazina. Kwa hiyo, tutaendelea kuweka jitihada kuhakikisha mkandarasi hasimami. Pia ninamwelekeza aendelee na kazi wakati akisubiri malipo kwa certificates ambazo amewasilisha. Ahsante sana.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Bungu – Nyamisati tathmini imeshafanyika na wananchi wanasubiri kulipwa ili sasa shughuli nyingine za ujenzi wa barabara ile ziweze kuendelea. Je, Serikali ina kauli ipi katika kuweza kuwalipa wananchi wale wa Bungu Nyamisati fidia?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Yahya pamoja na wananchi kwamba natambua barabara hii ya Bungo Nyamisati. Mheshimiwa Yahya amekuwa akiifuatilia sana na hata jana alikuja ofisini kufuatilia fidia hizi za wananchi na tunatambua barabara hii pia ni muhimu kwa wananchi wa Mafia. Kwa hiyo, Serikali inatambua umuhimu huu na tutafanya kila jitihada kuhakikisha fidia inalipwa ili kuweza kuruhusu ujenzi wa barabara hii kwa mujibu wa mipango yetu. Ahsante sana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuna baadhi ya wananchi wa jimbo langu waliopisha ujenzi wa Barabara ya Bunda – Kisorya, bado hawajalipwa. Je, ni lini Serikali itakamilisha malipo yao?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kajege kuhusu fidia ya wananchi wa Barabara ya Bunda – Kisorya. Nimelichukua, tutafanya kila aina ya jitihada ili malipo ambayo tumeya-process kwa ajili ya fidia yaweze kufanyika. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Makambako wanaishukuru Serikali kwa kulipa fidia ya eneo la Idofya, lakini ni lini sasa kituo hiki cha Stop Centre kitajengwa katika eneo la Idofya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri amekuwa ni Waziri wa nne kufika katika Barabara ya Sanzate – Nata na alipofika pale mara ya mwisho alisema hiyo barabara itamalizika mwezi Septemba mwaka huu; mpaka sasa hiyo barabara haijamalizika na ni kero kubwa kwa wananchi wa Bunda. Je, ni lini barabara hii itamalizika?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili yaliyoulizwa na Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tumekamilisha na ni hatua muhimu katika maendeleo ya kuanza kwa ujenzi. Kwa hiyo, nimhakikishie, fedha itakapopatikana kwa vile tumeshajua gharama, basi tutajenga huu mradi pale Makambako.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili; Barabara ya Sanzate – Nata, kwanza nampongeza Mheshimiwa Getere amekuwa akifuatilia, lakini nakiri kulikuwa kuna changamoto za mkandarasi huyu; na miradi yake kwenye mikoa ambayo ana kazi imekuwa ikisuasua. Serikali kwa maana ya Wizara tumechukua hatua, kuna miradi tumemnyang’anya ili aweze ku-concentrate na miradi michache huku tukimweka kwenye uangalizi, ukiwemo huu Mradi wa Sanzate – Nata.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Getere pamoja na wananchi kuwa Serikali tuko kazini tutamsimamia mkandarasi huyu ili barabara hii iweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari (One-stop Inspection Centre). Ujenzi huu ulikuwa umefikia 60%, lakini ulisimama tangu 2016, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanakamilisha ujenzi huu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Chaya amekuwa akifuatilia jambo hili na nakiri Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha tunafanya tathmini ya kuhakikisha miradi hii inakamilika na kulikuwa kuna changamoto ambazo zilisababisha kukwama kwa miradi hii ya One-stop Inspection Centre. Kwa hiyo, namhakikishia Mbunge, Serikali tuko mbioni kuifufua hii miradi ili iweze kukamilika kwa sababu uhitaji wake bado ni muhimu tena ni muhimu zaidi kuliko ilivyokuwa huko mwanzoni. Nashukuru. (Makofi)
MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeuliza ni lini sasa Kituo cha Stop Centre cha Isaka kitaboreshwa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kassim Iddi, Barabara ya Kahama – Kakola kwa kweli amepambana sana. Nafurahi sasa hivi mkandarasi yuko site anaendelea na kazi. Kuhusu swali la pale Isaka naomba Mheshimiwa Iddi nikaangalie kwenye mipango yetu na baada ya hapa nitakaa na yeye ili nihakikishe nampa majibu sahihi ya kituo hiki. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza. Barabara ya Nangwa – Bisambala – Kondoa ilitengewa fedha kwa ajili ya kufanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu. Je, kazi hiyo imefikia hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya Haydom – Mogitu imeshafanyiwa usanifu wa kina na umekamilika. Ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Hhayuma kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Nangwa – Bisambala – Kondoa, kwanza nakiri Mheshimiwa Hhayuma amekuwa akiifuatilia mara kwa mara akishirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Kondoa Mjini na Vijijini kwa sababu zinaunganisha wilaya hizi, nami nimeshawahi kutembelea barabara hii. Namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira, barabara hii hasa kipande cha kuunganisha Kondoa kuna mto mkubwa, lile daraja gharama yake inaweza ikazidi hata gharama ya kuijenga barabara yote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, Serikali tunafahamu, kadri fedha itakavyopatikana tutalipa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Haydom – Mogitu; Mheshimiwa Hhayuma hili vile vile ninamhakikishia kadri tutakavyopata fedha barabara hii tunajua umuhimu wake tutaitenga kwenye bajeti ili iweze kujengwa. Hata hivyo, namhakikishia, kipindi ambacho Serikali inatafuta fedha tutajenga barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ambacho kinapitika misimu yote ya mvua na kiangazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotupa matarajio sisi Wanakilwa. Hata hivyo, kutokana na ukweli kwamba Kilwa Masoko ndipo ambapo Serikali yetu pendwa inajenga bandari ya uvuvi na kwa maana hiyo, barabara hii ya Nangurukuru – Kilwa Masoko imekuwa ikielemewa sana na uzito wa mzigo wa magari yanayopeleka material bandarini, je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya haraka kupata hizi fedha ili barabara hii iweze kutengenezwa na kuboreshwa kama ambavyo tuliomba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji hususan kipande cha Kiranjeranje – Makangaga tuliomba kujengewa kwa kiwango cha lami, lakini kwa hatua za awali angalau kujenga kwa kiwango cha changarawe ili magari yanayotoka Kiranjeranje kwenda Makangaga kufuata material ya gypsum yaweze kupita angalau kwa mazingira yaliyo mazuri. Je, Serikali imefikia hatua gani kuboresha barabara hii ya Kiranjeranje – Makangaga?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kassinge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Kilwa Masoko kuelekea bandarini, kama alivyosema Serikali inaendelea na ujenzi wa bandari pale Kilwa Masoko na ili bandari iweze kuwa na tija. lazima barabara hii iweze kutengenezwa. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati Serikali inaenda kukamilisha bandari, sambamba na hilo Serikali imeweka kwenye kipaumbele barabara hii ili iweze kuboreshwa kwa kujengwa upya ili iweze kuendana na uwekezaji mkubwa ambao umewekwa pale. Ujenzi wa bandari utaenda sambamba na kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa kadri tutakavyopata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kuhusu Kiranjeranje – Nanjilinji, natumia nafasi hii kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa ambayo ilipata madhara makubwa ya mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya, lakini kwa kazi nzuri ambayo Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Lindi na ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia, na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ameshatupatia shilingi bilioni 140 kwa ajili ya kwenda kurudisha miundombinu ya barabara ambayo iliharibiwa ndani ya Mkoa wa Lindi na barabara hii ikiwemo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uwezeshaji huo. Waheshimiwa Wabunge kutoka mkoa huu mnafahamu tayari nimeshakabidhi wakandarasi ndani ya Mkoa wa Lindi ili kazi iweze kuanza. Natumia nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi kutembelea hii Barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji kuhakikisha inatengenezwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika misimu yote kama Mheshimiwa Mbunge alivyoomba, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Ni takribani mwaka mmoja sasa barabara ya Mbulu – Garbabi ya kilometa 25 imetelekezwa na mkandarasi. Je, ni lini mkandarasi atarudi katika kipande cha kilometa 25 katika Barabara ya Mbulu – Garbabi ili iweze kutekelezwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia kuhusu barabara hii ya Mbulu – Garbabi. Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia barabara hii, nampongeza kwa ufuatiliaji. Nawahakikishia wananchi wake kuwa mkandarasi huyu kuna malipo alikuwa anadai na tumeshapeleka fedha Hazina. Fedha itapatikana ili aweze kuendelea na kazi na kurudi site, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Old Shinyanga – Bubiki ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami lakini imefika hapo katikati Busangwa ujenzi umesimama. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi huo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu hitaji la Mheshimiwa Mbunge na namhakikishia kadri fedha itakavyopatikana tutatekeleza ombi lake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini atakumbuka barabara ya Kibiti – Lindi – Mtwara – Masasi ilifungwa mwaka 2023, wakati wa mvua za El-Nino. Ni kweli Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo, lakini sasa hivi mvua zinakaribia na hakuna mkandarasi yeyote aliyeko site pamoja na Serikali kusaini mkataba na wakandarasi hawa. Tunataka kufahamu, kabla ya mvua hizi za El-Nino, lakini pia atuhakikishie wananchi wa Mtwara kwamba barabara hiyo haitafungwa mwaka huu. Ni lini, mkandarasi anayetakiwa kujenga barabara ya Kibiti – Lindi – Mtwara – Masasi atakuwepo site? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cecil Mwambe amekuwa akifuatilia barabara hii na ningependa kujibu swali lake kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuko hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kujenga barabara ya Mtwara – Masasi – Mingoyo, na ni mkakati wa Serikali kujenga upya barabara hii kwa sababu imeharibiwa sana na mvua. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tumejipanga na ninawatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania, kama ambavyo tulifanya mwaka 2023, tulipata mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya lakini Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mvua kubwa ambazo tulizipata tulihakikisha mawasiliano yanakuwepo. Hata msimu huu wa mvua ambao unakaribia kuanza tumejipanga. Kwa hiyo, nawaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania. Kupitia TANROADS ikishirikiana na TARURA tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mawasiliano yanakuwepo muda wote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Machine Tools – Kiaria na barabara ya Kwa Sadala – Mula ni barabara za TANROADS lakini zimejengwa hazikuwekwa taa ilhali barabara ya Makoa Mferejini imejengwa na imewekwa taa, kwa hiyo inaleta tofauti kubwa. Je, ni lini sasa Serikali itaweka taa kwenye barabara hizi?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Saashisha, amekuwa akinifuata kuhusu hitaji hili. Naomba baada ya majibu haya nitakaa naye tuwasiliane na Regional Manager kule Kilimanjaro tuone namna ambavyo tutatekeleza jambo hili, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshajenga kilometa 19.4 za barabara ya Njombe – Iyai yenye kilometa 74 ambayo inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mbeya ndani ya Jimbo la Wanging’ombe kwa kiwango cha lami. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa barabara hii kutokana na umuhimu na uzalishaji mkubwa unaofanywa na wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa barabara hii na namhakikishia Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba tutaipa kipaumbele barabara hii kadiri fedha zitakavyokuwa zinapatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara inayokwenda Kigoma, Kata ya Vumilia kuna wananchi wa maeneo ya Mbaoni na Motomoto ambao wanaidai fidia Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ili wabomoe nyumba zao wapishe nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme katika kituo kipya cha kupozea umeme kinachojengwa eneo la Uhuru. Je, ni lini Serikali italipa ili na sisi umeme ufikishwe katika kituo chetu kinachojengwa? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Margaret Sitta, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia huwa ni sehemu ya gharama ya mradi. Kwa hiyo, naependa kumhakikishia Mheshimiwa Margaret Sitta pamoja na wananchi wake kwamba waendelee kuwa na subira. Mradi husika utakapokuwa unatekelezwa, basi sehemu ya gharama hiyo ni suala la hizi fidia. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la ngongeza. Barabara ya Haydom – Labay imesainiwa na Mheshimiwa Waziri alikuja. Tumesaini barabara ile na akatuahidi ujenzi utaanza. Je, ni lini pochi la Mama linafunguliwa ili fedha zianze kupelekwa kwa mkandarasi na amalize kazi ya kujenga barabara ile? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Flatei kwa namna ambavyo anafuatilia barabara hii na tumeshakaa naye pamoja na Hazina. Mkandarasi anasubiri advance payment. Kwa hiyo, nakuhakikishia yeye pamoja na wananchi wake kuwa barabara hii itaanza kujengwa tutakavyopata tu advance payment. (Makofi)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali, kwamba kuna maendeleo mazuri kwenye barabara hii. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; je, ni lini usanifu na upembuzi yakinifu wa barabara kutoka Busisi, Busolwa, Ijundu kuelekea Kahama utakamilika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa ujenzi wa barabara kutoka Katoro Jimboni Busanda kuelekea Ushirombo Jimboni Bukombe? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tumaini Magessa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwamba ni lini usanifu wa barabara kutoka Busisi, Ijundu kuelekea Kahama utafanyika; kwa kipande hiki cha barabara kutoka Mwanza kuelekea Geita tayari tumekwishampata mkandarasi na usanifu umeanza. Kwa vile barabara hii ina kipande cha kuelekea upande wa Kahama nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya haraka iwezekanavyo ili tupate mkandarasi wa kufanya usanifu wa hiki kipande cha upande wa Geita ambacho kimebaki.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili Barabara ya Katoro – Ushirombo, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge fedha itakapopatikana barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona. Je, Barabara ya Omgakolongo - Kigalama mpaka Mlongo inayounganisha Wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa imefikia wapi kujengwa kwa kiwango cha lami, maana ni ahadi ya muda mrefu? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Semuguruka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Omgakolongo kutoka Karagwe kuelekea Kyerwa mpaka Mlongo ni barabara ambayo hata mimi ninaifahamu, ipo jimboni kwangu pamoja na kwa Mheshimiwa Innocent Bilakwate. Tupo katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi na mara tu baada ya kumpata mkandarasi tutaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali imekwishaanza kutangaza kazi za ujenzi wa kilometa tano kwa ajili ya wakandarasi wanawake na kazi imefanyika Mkoa wa Songwe. Je, anatupa matumaini gani, kwamba jambo hili litakuwa endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Mgalu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kumpongeza kwa namna ambavyo anawapambania wakandarasi wanawake. Nimwondoe wasiwasi, kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambayo nitakayowasilisha kesho kutwa tunayo mikakati kabambe kwa ajili ya wakandarasi wanawake. Si hizi kilometa tano tu, tunazo kilometa nyingi ambazo tumezi-earmark kwa ajili ya kutekelezwa na wakandarasi wanawake. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ningependa kujua; kipande cha barabara itokayo Malagarasi kwenda Uvinza, kilometa 51, kinasuasua kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali watakamilisha kazi hiyo?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii mkandarasi yupo site lakini speed si ya kuridhisha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, changamoto ya mkandarasi huyu tumeiwasilisha Hazina. Mara tu baada kupata malipo tutampa mkandarasi ili aweze kuongeza speed; lakini pia baada ya Bunge la Bajeti tutaenda huko kwa ajili ya kuweka msukumo ili ujenzi uende kwa kasi.