Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Innocent Lugha Bashungwa (14 total)

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji ni tatizo kubwa tuseme nchi nzima, lakini hata Karagwe tuna shida sana ya maji. Wakati wana-Karagwe wanasubiri mradi wa Rwakajunju, Serikali ina miradi ya Benki ya Dunia, lakini kote Jimboni hii miradi haijakamilika. Napenda kuiomba Serikali ieleze wananchi wa Karagwe hii miradi itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi ya Benki ya Dunia, tulikuwa na hiyo awamu ya kwanza ya program ambayo imekwisha Disemba tarehe 30. Sasa tunaingia awamu ya pili ya program ya miaka mitano katika kutekeleza vijiji vile ambavyo havikupata awamu ya kwanza na ile miradi ambayo iko inaendelea. Sasa hivi Serikali imeshapata fedha za kuweza kusukuma miradi ya kwanza ile iliyokuwa imeanza ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, azma ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vilivyokuwa ndani ya program tunakamilisha ili wananchi wetu waweze kupata maji.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, lakini kwa upande wa kahawa, Jimbo la Karagwe tunalima kahawa sana na zao la kahawa bado lina fursa kubwa sana kuwainua kiuchumi wakulima wa kahawa na uchumi wa nchi kwa ujumla lakini mikopo ya TIB imekuwa ni kidogo mno kwenda kwenye kukopesha walimaji wa kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu ni kama ifuatavyo: Kwa vile miche ya kahawa ni ya zamani sana, imepandwa toka enzi za wakoloni na mababu zetu, je, Benki ya Kilimo ina mpango gani wa kuwakopesha wakulima wa kahawa pesa ile waweze kununua miche wakiwemo vijana ambao wana tatizo la ajira na kama miche ikipatikana wanaweza wakajikita kwenye kilimo cha kahawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile kabla ya kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo, TIB ilikuwa ikitoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kupitia Dirisha la Kilimo, kwa nini hii portfolio isitoke TIB ikaenda Benki ya Kilimo ili hii fedha shilingi bilioni 58.8 itumiwe na Benki ya Kilimo kukopesha wakulima wa Tanzania?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Innocent Bashungwa kwa kufuatilia suala la miche ya kahawa na kusema kuwa imechakaa na kwenye hotuba yangu nilisema katika Wilaya na Mikoa inayolima miche ya kahawa wajitahidi kupanda miche 5,000 kwa kila hekari ili kuweza kurejesha heshima ya zao hilo la kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ombi lake hili la kuangalia uwezekano wa vijana kukopeshwa fedha kwa ajili ya kupanda miche mipya, niseme tu nitaielekeza Benki ya Kilimo wawasiliane na Mheshimiwa Mbunge na wapangilie safari ya kuweza kufika huko ili wakaangalie mazingira sambamba na vile ambavyo tulishakubaliana watafika pia Kitulo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kukopesha uzalishaji wa mitamba ili wananchi waweze kupata mbegu za mazao haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge na naelekeza uwasiliane na Benki ya Kilimo ili waweze kuwakopesha vijana wapande miche mipya ili kurejesha heshima ya zao hilo la kahawa. Zao la kahawa litaendelea tu kama tutalipokea kutoka kwa wazee wetu na sisi vijana tukaona ni zao la fursa kwa ajira na kwa ajili ya biashara.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Karagwe tuna kituo cha ufundi stadi cha KVTC Kayanga. Serikali iliandaa mchoro wa kupanua hiki chuo kwa muda mrefu sasa miaka mingi. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kupanua hiki chuo cha KVTC Kayanga.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali imetenga fedha za kufanya ukarabati wa vyuo viwili. Chuo cha Ufundi Stadi cha Korogwe pamoja na Karagwe kwa hiyo fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wananchi wa Karagwe tunamkumbuka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa push-up za kihistoria alizozipiga pale Kayanga. Je, Serikali mnaonaje kama mkitusaidia kujenga uwanja wa Wilaya pale Kayanga ili tuweze kumuenzi Rais wetu kwa ule ukakamavu alioonyesha kwa vijana wa Karagwe? Nashukuru sana
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba push-up kwa mara ya kwanza zilipigwa kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge anasema, hii ilithibitisha uwezo wa Rais John Pombe Magufuli wa afya yake, lakini pia ulionyesha kwamba Serikali atakayoiunda ni Serikali ya Hapa Kazi Tu tofauti na wenzetu mgombea wao nadhani hiyo kazi ilikuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara kwa kushirikana na Halmashauri anakotoka Mbunge tunaweze kuzungumza kuona namna ya kushauriana kuweka kumbukumbu hii muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanywa. Kwa hiyo, Wizara na Halmashauri ambapo anatoka Mbunge tutakaa pamoja tuzungumze tuone namna ya kuweka hii kumbukumbu muhimu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Jimbo la Mkuranga zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Naishukuru Serikali kwa kutuunganisha Jimbo la Karagwe na Jimbo la Kyerwa kwa kuweka mpango wa kujenga kwa lami barabara ya Mugakolongo kwenda Mulongo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri akisaidie Kijiji cha Rwambaizi, barabara imekwepa kijiji na kama mnavyojua barabara huchochea maendeleo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie barabara ya Mgakolongo kwenda Mulongo, ipite kwenye kijiji cha Rwambaizi, ili wananchi wangu wa hicho kijiji waweze kupata maendeleo yatakayokuja na ujenzi wa barabara hiyo la lami, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri barabara anayoitaja ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwa mwaka 2016/2017 anafahamu kwamba imetengewa fedha. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Bashungwa, Wizara yetu dhamana yake ni kutekeleza ahadi za ilani ya Chama cha Mapinduzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha barabara hii katika miaka hii mitano, inakamilika kujengwa kwa lami.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kata za Igulwa, Kanoni, Kituntu, Ihanda na Chonyonyo, zina shida kubwa sana ya maji. Kutokana na shida hii, Serikali iliahidi kuchimba mabwawa katika hizi Kata ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya maji. Je, Serikali itachimba lini haya mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashungwa ameuliza kwamba, ni lini Serikali; kuna Kata za Igulwa pamoja na Kata zingine ambazo zina uhaba wa maji, lakini anapenda kujua ni lini basi, Serikali itachimba mabwawa au kufanya utafiti wa kupata ni chanzo kipi cha maji, ambacho kinaweza kikatosheleza Kata hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tumeagiza kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri wafanye utafiti wa mabwawa, ambayo wanafikiri yanaweza yakachimbwa katika maeneo yao ili tafiti hizo ziwasilishwe Wizara ya Maji ili Wizara ya Maji iangalie uwezekano wa kutenga fedha katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 kutegemea na jinsi watakavyokamilisha hizo study. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bashungwa nikuhakikishie na naomba na wewe kama Diwani, basi ushirikiane na Madiwani wenzako katika Halmashauri yako ya Karagwe ili hatua hii, muwafahamishe watalaam waweze kuifanya.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto za Morogoro Kusini zinafanana na Changamoto za Jimbo la Karagwe. Katika Hospitali ya DDH Nyakahanga tuna tatizo kubwa la upungufu wa madawa, vifaa tiba na Wauguzi.
Mheshimiwa Naibu Spka, swali langu ni je, Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo kaka yangu, anaweza kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda kusaidiana nami kutatua changamoto za Hospitali ya DDH ya Nyakahanga
pamoja na kuanza mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya ukizingatia DDH ya Nyakahanga inahudumia Wilaya mbili; Karagwe na Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba miongoni mwa Wabunge ambao walikuwa wakinisumbua sana katika Sekta ya Afya ni Mbunge huyu wa Karagwe. Ni kweli kabisa, naomba niseme kuwa, pale ana Daktari wake anaitwa Dkt. Sobo ambaye ni kijana mwenzake; naamini kwamba watashirikiana vya kutosha kuhakikisha mchakato wa Jimbo lile unakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, commitment yetu ni kwamba, katika kipindi hiki nitakuwa na ziara katika Mikoa yetu mitano nikianzia Mkoa wa Tanga, Lindi, Pwani Morogoro pamoja na Mtwara, lakini nitapita Ruvuma. Vile vile Mkoa wa Kagera niliupa kipaumbele kwa zoezi maalum katika kutembelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani kwamba kabla ya Bunge lijalo, basi nitajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo tufike eneo lile kubaini changamoto za wananchi wa eneo lile la Jimbo la Karagwe ili mwisho wa siku wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni commitment ya Serikali, tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo, hasa nikijua nawe ni mpiganaji mkubwa katika Sekta ya Afya katika eneo lako, tutasukuma kwa kadiri iwezekanavyo wananchi pale wapate huduma bora.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa Serikali wa kuhamisha nyumba zilizokuwa chini ya Halmashauri kwenda Serikali Kuu umeacha watumishi katika Halmashauri ya Karagwe bila makazi, takribani kaya za Watumishi 60 hivi sasa hazina makazi kwa sababu Serikali Kuu imechukua nyumba ambazo zilikuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Je, Wizara haioni kwamba inabidi iwasaidie watumishi hawa kwa kuiomba NHC ishirikiane na
Halmashauri, Halmashauri tunaweza tukawapa eneo la kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watumishi hawa? Nashukuru
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nyumba zilizokuwa awali za Wizara ya TAMISEMI baadae zikaenda NHC sasa zimerudishwa Serikali Kuu. Hivi sasa wataalam wangu na Wataalam wa Wizara ya Ujenzi wanapima maeneo hayo ili yamilikishwe kwa Serikali Kuu. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba mpya ili ziweze kuboresha mandhari ya Miji, kwa sababu nyumba hizi tangu zimemilikiwa na Serikali za Mitaa na NHC ingawa maeneo yale ni mijini lakini nyumba zimekuwa chakavu na hivyo
zinaleta mandhari mbaya katika miji. Hivyo, lengo la Serikali ni kuzijenga upya.
Pili, kuchukua zile nyumba kuziweka Serikali Kuu hakumaanishi kwamba wale wanaokaa katika nyumba zile sasa wafukuzwe. Mheshimiwa Rais ameagiza kwamba zoezi hili linakoendelea kupima mpaka itakapofikia zamu ya kujenga nyumba mpya katika maeneo hayo, waliomo wanaopanga sasa wabaki katika nyumba hizo wasibughudhiwe na wasifukuzwe. Whether ni watumishi wa leo au watumishi wa zamani wenye mikataba ya kukaa kwenye nyumba hizo wabaki wale wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale wa Karagwe hao hawapaswi kutoka, wakae humo humo whether ni watumishi au wananchi wa kawaida. Nyumba hizi ingawa si lazima wakae watumishi tu lakini kuna sehemu nyingine watumishi wa Serikali wanakaa na wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, waliomo kwenye nyumba hizo wasifukuzwe. Huko Karagwe kama wananisikia wanafikiri kwamba hao wafanyakazi wanatakiwa kufukuzwa hapana. Tunahaulisha tu utaratibu wa umiliki wa Serikali lakini hatuwaondoi wapangaji.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Hata Wilaya ya Karagwe tuna vivutio vingi vya malikale likiwemo eneo ambalo Chief Rumanyika alikaa. Je, Wizara imeweka vivutio vya malikale hizi kwenye orodha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kivutio kinachohusu makazi ya Chifu Rumanyika ni moja tu kati ya vivutio vinavyohusu Machifu wetu wote nchi nzima kila eneo na kila Wilaya. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kama nilivyoeleza hapo awali kwamba ni kuviorodhesha, kuvisajili, kuvikagua na kuona ubora wake na hatimae kuviuza kwa kuangalia sifa zake.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Nina swali kuhusu mradi wa Rwakajunju namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri awaambie akinamama wa Karagwe ni lini mradi wa Rwakajunju utatekelezwa ili kuwatua ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwatulize wananchi wa jimbo la Mheshimiwa Mbunge kwamba Mradi wa Maji wa Rwakajunju unatekelezwa. Mradi wa maji wa Rwakajunju una finacing ya uhakikika kutoka Serikali ya India na tunasubiri sasa hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha asaini mkataba wa fedha. Tayari Wizara tumeshaanza kutafuta Wahandisi Washauri ambao wanahakikisha wanaweka document vizuri. Yule Mhandisi anayefanya usanifu wa mradi huu anakaribia kukamilisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana, nina imani katika mwaka huu fedha tuliouanza juzi 2017/2018 tutaanza utekelezaji wa Mradi wa Rwakajunju ili tuweze kuwatua wananchi ndoo kichwani.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana ambao wanaajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kuzungushwa pale wanapoenda kwenye Mifuko ya Pensheni kudai mafao yao ili waweze kuyatumia kama mitaji ya kujiajiri. Kwa mfano, kule Karagwe Kampuni ya Ujenzi ya Chico iliajiri vijana kwa utaratibu wa mikataba ya vibarua, mpaka hivi sasa wanazungushwa vijana hawa.
Je, Serikali inawasaidiaje vijana hawa kudai mafao
yao ili waweze kutumia hela hii kama mitaji ya kujiajiri?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi ya pekee sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu amekuwa mstari wa mbele sana kufuatilia haki za wananchi katika Jimbo lake na hilo ni jambo jema.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tumekuwa na malalamiko ya namna moja ama nyingine ya wafanyakazi wa namna hiyo ambao wamekuwa wakiajiriwa kwa mikataba, mikataba yao inapoisha walizoea kuwa na fao ambalo si fao sahihi lakini lililokuwa linaitwa fao la kujitoa. Baada ya kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 11, lakini kupitia Sera ya Hifadhi ya Jamii katika nchi yetu na sheria tulizonazo, Serikali pamoja na wafanyakazi wenyewe na vyama vya wafanyakazi, tumekubaliana sasa kuna haja ya kuangalia namna nzuri ya kuwasaidia wafanyakazi wote ambao wamekuwa wakikumbwa na jambo hilo kwa kuanzisha fao lingine ambalo litaitwa ni Bima ya kukosa ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo tumeshaanza kuifanya vizuri kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, niwaombe wafanyakazi wote nchini ambao walikuwa wanaelekea katika fao hilo wavute subira ili matakwa ya kisheria yafanyiwe kazi na ndipo fao hilo litaanza kutolewa kwa mujibu wa sheria ambayo itakuwa imetungwa na Bunge.
Pia ni maagizo ya Mheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi alipokuwa pale Moshi ameendelea kusisitiza kwamba sasa tushughulikie suala hilo na liweze kufungwa kisheria na Wafanyakazi waweze kupata haki zao. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mpango wa kupandisha watumishi madaraja wale wanaostahili lakini kuna changamoto ya wale watumishi ambao wanapandishwa madaraja mishahara huwa inachelewa ku-reflect lile daraja ambalo amepandishwa. Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba ni kweli wako baadhi ya Maafisa Utumishi ambao wamekuwa hawatekelezi wajibu wao kama inavyopaswa na wamekuwa wakichelewesha kurekebisha mishahara katika mfumo wetu wa ulipaji wa malipo ya mshahara wa LAWSON. Nipende kutoa tamko hapa na maelekezo kwa mara nyingine tena, tulishachukua hatua katika Halmashauri ya Bagamoyo, Kilombero, Temeke na nyingine nyingi, hatutamvumilia Afisa Utumishi yeyote au mhusika yeyote katika mamlaka ya ajira ambaye atachelewesha kurekebisha malipo ya mshahara baada ya mtumishi kupandishwa daraja.
Nipende kusema sasa hivi tumeenda mbali itafika wakati tutaanza kuwafungia hata Wakurugenzi wa Halmashauri mishahara yao ili na wenyewe waweze kuona uchungu wa kuchelewesha upandishwaji wa madaraja wa watumishi hao.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Pia katika Wilaya ya Karagwe kuna wahanga ambao wameathirika na wanyama waharibifu hasa tembo na viboko katika kata za Kihanga, Rugu, Nyakasimbi, Nyakabanga, Nyakakika na Bwelanyange, lakini pamoja na kushindwa kuwapa kifuta machozi wananchi hawa, pia vijiji katika hizi kata vinapakana na Pori la Akiba la Kimisi na Burigi na kuna asilimia ambayo inatakiwa kutoka kwenye mapato ya hifadhi kwenda kwenye vijiji ili kuwasaidia katika shughuli za maendeleo. Tumetuma madai katika Wizara kwa muda mrefu, lakini hatujawahi kupata hii fidia ili wananchi hawa nao wafaidike.
Je, ni lini Serikali itatoa kifuta machozi hicho pamoja na yale mapato? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nilisema katika maombi ambayo yameifikia Wizara kwa ajili ya uhakiki, kiwango cha jumla ya fedha takribani shilingi milioni 500 pekee ndicho ambacho kimebaki bila kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuangalia kwenye orodha ile ya wale ambao wanafanya jumla ya madai yawe shilingi milioni 500 nione kama wananchi wanaolizungumzia ni sehemu ya madai hayo. Kwa hiyo, ikiwa hivyo ndivyo, tumesema fedha hizi zinalipwa ndani ya mwaka wa fedha huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa siyo miongoni mwa wale ambao jumla ya fedha shilingi milioni 500 zinadaiwa, basi itakuwa wako katika mchakato; wale ambao bado taratibu hazijakamilika kwenye ngazi za Halmashauri na Mikoa, kwa hiyo, tutakwenda kuhimiza tu ifanyike haraka ili madai hayo yaweze kuifikia Wizara yawekwe kwenye orodha halafu tuweke utaratibu wa ratiba ya kuweza kuyalipa.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kwenye taarifa ya habari ITV kulikuwa kuna kauli kwamba kuna uingizaji wa mbegu fake nchini. Kama kauli hii ina ukweli ni hatari sana kwani inamdhulumu mkulima ananunua mbegu akidhani ni mbegu yenye ubora lakini mbegu hii inakuwa ni feki matokeo yake anapanda havuni anachokitegemea.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kauli hii ambayo ilitoka ITV jana usiku kwenye taarifa ya habari? Nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nimeiona hiyo kauli au statement iliyotolewa na kituo cha televisheni cha ITV kwamba nilikiri nchini hapa mbegu inayotumika kwa wakulima ni mbegu fake. Naomba nitoe ufafanuzi wa hilo jambo kwamba sikusema hivyo na jambo hilo lililotangazwa halina ukweli wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokisema ni kwamba wakulima wengi nchini bado wanatumia mbegu hafifu na kwa hivyo uzalishaji wao bado uko duni kwa sababu ya matumizi ya mbegu hizo na si kusema kwamba wanatumia mbegu feki. Kwa hivyo, niwaombe tu wenzetu wa kituo hicho cha televisheni wafanye hayo marekebisho ya kauli yangu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema kwamba Serikali inachokisema ni kwamba bado yako matumizi ya mbegu hafifu kwa wingi hapa nchini na hiyo inatusababishia uzalishaji hafifu na si vinginevyo.