Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nishukuru wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru Magharibi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira tuliyonayo ya kuchangia bajeti hii tunaamini kwamba bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2021/2022, ndiyo maana hapa tumeanza mchakato huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea ningependa sana kusema maneno machache kabla sijachangia. Nitumie maneno ya Mungu, wakati ule Yesu alipokuja duniani kwa ajili ya kuokoa dunia alikuwa na wanafunzi wake 12. Katika wale wanafunzi, Yesu alitabiri kwamba kuna wawili watakaomsaliti, alikuwa ni Petro na Yuda Iskariote. Alipokuwa pia akiendelea alijaribiwa na shetani sana akampandisha juu ya mlima mkubwa sana akamwambia ukinisujudu nitakupa dunia hii yote itakuwa ya kwako na miliki zote, lakini Yesu akamwambia rudi zako nyuma shetani kwa sababu miliki yote hii ni ya kwangu.

Mheshimiwa Spika, nayasema hayo, lakini pia alipokuwa akiendelea alikutana na watoza ushuru, wakamuuliza sisi tufanye nini Bwana? Akawaambia na ninyi mtosheke na mishahara yenu. Nimeona nianzie na hapo. Nasikitika sana, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye aliinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa nguvu zake zote na nia yake yote na moyo wake wote, leo tunapata akina Yuda. Leo kina Yuda wamejitokeza kumsaliti Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano. Inasikitisha, mzee wa watu ametangulia mbele ya haki, hawezi kujitetea, lakini ninyi mlioko ndani na nje mnataka kumdhalilisha. Hakika, asilani kabla hamjamdhalilisha Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano, nina hakika Mwenyezi Mungu atawashughulikia usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifanya kazi ya kuwaaminisha Watanzania kwamba kweli ni Rais anayejali maskini, anayejali Taifa hili kama alivyokuwa mtangulizi wake Rais wa Serikali ya Kwanza Nyerere alifuata hizo nyayo na Serikali zote zingine zilizofuata alionesha njia kubwa. Alipokuwa akitunadi, niliumia sana ninapoona kwenye mitandano watu wanachafua hali ya hewa Magufuli hata panya akitoboa gunia kule nyumbani kwa mtu, Magufuli! Kwa sababu yeye hayupo. Kama kuna watu wamefanya ufasadi kwenye Wizara, Bandari na halmashauri watu wanasema Magufuli, kawatuma? Nasikitika sana, lakini Mwenyezi Mungu atawashughulikia kabla ya siku zao si nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akina Yuda hawakosekani, lakini nawaambia ninyi ambao mnadhani mtaishi milele hakuna nafsi, kila nafsi iliyoko hapa kwenye Bunge hili na nje ya Bunge hili itaonja mauti. Hakuna anayedumu milele wala hatuna mji udumuo katika dunia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, mama Samia Suluhu Hassan alikuwa ni msaidizi wa Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Rais wetu wa sasa mama Samia Suluhu Hassan alikuwa mwaminifu na muadilifu na ndiyo maana Mwenyezi Mungu amemuona akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtaona jinsi gani mama yule, Rais wetu mpendwa amehakikisha kwamba wale waliokuwa wanatazamia kwamba atabadilisha Serikali kwa asilimia sijui ngapi, amesema “Kazi Iendelee”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tusifikiri kwamba kwa mwelekeo huo Mheshimiwa Rais aliyeko ataweza kumsaliti Magufuli. Legacy ya Magufuli itaendelea kubaki sasa na hata milele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niendelee kutoa mchango wangu. Najua kabisa Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani ya Mwaka 2020/2021 imefanya kazi kubwa na hakuna mtu asiyejua, hakuna asiyaona. Kwenye dispensary tumefanya vizuri Chama Cha Mapinduzi, kwenye bandari, kwenye reli, kwenye masuala ya hospitali na kadhalika. Barabara nchi hii ni kubwa lakini imetekelezwa Ilani kwa asilimia 90 kuunganisha mikoa yote ya Tanzania. Hakuna ubishi na anayebisha hapa asimame, hii nchi ni kubwa, hata kule Roma, Mji wa Baba Mtakatifu unajengwa mpaka leo wajenzi wapo wanajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2021/2022, sasa ni kazi yetu kuikumbusha Serikali kwamba kuna upungufu ule mdogo mdogo yaliyoko kwenye vijiji, kata, wilaya na kwa ujumla kwenye mikoa. Ni wajibu wa Serikali yetu kwenda kutekeleza kwa kutumia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ahadi ya Waheshimiwa Viongozi wetu Awamu ya Tano, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne. Awamu ya Tano ambayo kwa sasa ndiyo iliyoongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi barabara za lami kwenye majimbo yetu, aliahidi kutengenezwa hospitali, ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye tunamuamini na tunamwona ni mchapakazi, yeye ndiyo anasimamia shughuli za Serikali Bungeni, hebu sasa Serikali ije na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba hizi ahadi ambazo Waheshimiwa Marais wetu wanatoa, Waheshimiwa Mawaziri wahakikishe kwamba wameweka kwenye bundle moja ili iweze kutekelezwa kikamilifu na iweze kuwepo katika reference. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la ahadi linasumbua sana wananchi kwa sababu wanasema Rais ametuahidi kila siku anasema Mbunge wakumbushe, wakumbushe. Sisi ni wajibu wetu kama Wabunge kuikumbusha Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi na imefanya kazi kubwa, imetekeleza ahadi nyingi imepungua hizo ndogo tu, lakini ningeomba ingewekwa kwenye bundle moja ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye jimbo langu Awamu ya Nne iliahidiwa barabara ya Hospitali ya Oturumeti, hospitali ya wilaya kwa lami. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi barabara ya Mianzini – Kimbolo –Ngaramtoni; barabara iliahidiwa na Mheshimiwa Jaffo, barabara ya kwenda Hospitali ya Nduruma, Bwawani na katika majimbo mengine yote Tanzania. Najua hii nchi ni kubwa, lakini ni wajibu wetu kuendelea kuikumbusha Serikali yetu tukufu na sikivu kuhakikisha kwamba imeondoa hizo ahadi za Waheshimiwa Marais wetu.

Mheshimiwa Spika, suala la ajira; kama tunavyojua Serikali inajitahidi, sasa niombe ijitahidi sana kuboresha katika Sekta Binafsi na kwa ajili ya kupata mazingira mazuri ya kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili vijana wetu ambao wanahangaika huku na huku waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kilimo; kuna mashamba makubwa yametelekezwa kama mashamba haya yangeweza kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo wakaunganisha kama wale ma-settler walivyokuwa wanalima kahawa, maharage, mahindi, ingeweza kuleta tija na ajira. Bado naamini kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu itaendelea kuchapa kazi na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanafanya kazi vizuri. Kwa mfano kwenye Jimbo langu, kuna mashamba makubwa kama ya Aga Khan, imechukua mwaka 2006 ikisema itajenga Chuo Kikuu, zaidi ya heka 3,000 hadi leo shamba hilo limesimama, lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500, lakini naamini Wizara ya Ardhi itaekwenda kufuatilia shamba hilo ili kujua hatma yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia katika ardhi na ajira, kuna suala la Mfuko huu wa Akinamama, Vijana na Wenye Ulemavu. Naomba Wizara husika ije na mpango mahsusi wa kuboresha Mfuko ule ukae vizuri kwa sababu, hivi sasa kuna utata mkubwa katika mfuko huo, watu wanaopata mikopo ni 18 – 35, lakini utaona ni jinsi gani bado watu wa age hiyo wako shuleni. Sasa ni vizuri wakaja pia na marekebisho kama itawezekana wakanzia 18 mpaka angalau 40, hapo utapata watu wengi ambao wataongea uchumi na wataanzisha biashara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya…

NAIBU SPIKA: Kila Mbunge anayeitwa anachangia kwa dakika tano.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyenipa fursa hii ya kusimama kwenye Bunge lako hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kwenye suala la ukosefu wa dawa kwenye hospitali zetu. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa. tunajua Serikali imejitahidi sana kwenye masuala ya miundombinu, lakini bado tuna changamoto sana kwenye suala la ukosefu wa dawa. Akina mama wanateseka na watoto, wazee wanateseka. Nilikuwa naomba suala ambalo litamfanya Waziri wa Afya na timu yake nzima wasipate usingizi, wasilale usiku, ni suala la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni suala la ukosefu wa dawa kwa sababu ya hujuma, labda wizi kwenye hospitali zetu, naomba hili suala kwa kweli; akina mama na watoto wanateseka, wazee wanakosa dawa na wagonjwa wengine wanakosa dawa hospitalini. Wale wanaoiba dawa hospitalini, basi mwaangalie na kuwaangazia macho sawa sawa kwa sababu katika jambo hili la ukosefu wa dawa kwenye hospitali, ni sawa sawa na kumsindikiza mgonjwa katika mauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anapokwenda hospitali na akakosa dawa, matumaini ya kuishi duniani tena hakuna. Kwa hiyo, nawaomba sana suala hili tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, suala la ukosefu wa madaktari, hili nalo ni changamoto kubwa. Watu wanapokwenda kwenye hospitali wanakosa madaktari, hii bado ni changamoto kubwa mno. Naomba Serikali kwa sababu imetangaza ajira hizo, iendelee kuongeza kasi kubwa kuhakikisha kwamba tunapata madaktari wa kutosha na manesi wa kutosha kwenye hospitali zetu ili kuokoa akina mama wajawazito na watoto na wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wazee kupewa barua ya kwenda kupata dawa kwenye Dirisha la Wazee bado na yenyewe ni changamoto. Wazee hao wanateseka, hakuna dawa. Nilikuwa naomba Serikali iangalie hiyo Sera ya Wazee na yenyewe kwa sababu bado kuna changamoto kubwa, wale wazee wanateseka. Ni vizuri wakaja na mpango mahususi wa kuhakikisha kwamba wazee hawa badala ya kupewa barua kwa Mtendaji wa Kata na Mtendaji wa Kijiji, ni bora wapewe Bima ya Afya, hata kama ni hii iliyoboreshwa, nao wapate iwe ni sehemu ya kuweza kuhakikisha kwamba wazee hawa wanaangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, tuko hapa lakini tunapata matatizo makubwa kwenye majimbo yetu kwamba wananchi wanalia dawa hakuna, wazee wanateseka, watoto wanateseka, akina mama wanateseka, wajawazito na wagonjwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naomba sana, sana sana Serikali yetu Sikivu ya Chama cha Mapinduzi, katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi chonde chonde; na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan alipokuja hapa Bungeni alituambia yeye ni mama, kwa hiyo, machungu ya mama anayajua vizuri. Kwa hiyo, naendelea kuiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ijitahidi sana katika suala la dawa; na Mheshimiwa Waziri usilale usingizi kwa sababu, wamama hawana dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali kama tuna majengo halafu hatuna dawa ni sawa na hakuna hospitali, lakini tukiwa na dawa; hospitali ndiyo dawa. Kama tukiwa na majengo hata maghorofa, kama hakuna dawa, hospitali hakuna; na unafuu wa maisha haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tena kwamba suala la motisha kwa madaktari na lenyewe ni jambo ambalo Serikali iliangalie kwa makini kwa sababu wale watu wanafanya kazi usiku na mchana, saa 24. Ni sawa na kazi ya jeshi. Wanajeshi wanafanya kazi usiku na mchana kama madaktari. Kwa hiyo, nawaomba pia suala la motisha kwa madaktari na manesi wetu ni suala la msingi na la muhimu sana ili waweze kuwa na moyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado narudia kusema, suala la wizi wa dawa, lazima Waziri asilale usingizi kwa sababu kukosekana kwa dawa ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya dharura kuhusu kuongezwa kwa umri wa waombaji wa ajira za Serikali
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Ninaanza kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Ng’wasi kwamba suala la umri ni suala ambalo hata kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri kwamba ni Jeshi Usu, mimi nadhani pia hawa wataalamu wetu wanaoandaa hivi vigezo wakati mwingine watafakari na kuangalia hali ya Watanzania na vijana tulionao huko mtaani na kiwango cha ajira kinachotolewa; na hiki kigezo cha miaka 25 kurudi 18 mimi nadhani bado hakiko sawa na hakitakuwa sawa. Hakitakuwa sawa kwa sababu Jeshi la Wananchi wa Tanzania na hilo Jeshi Usu mafunzo ni tofauti, hayawezi kuwa makali kuzidi Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nadhani suala hili la umri angalau kutoka miaka 18 mpaka 30 kwa majeshi haya Usu siyo sehemu mbaya. Sasa suala la afya lijulikane wakati wa mafunzo hayo na kupimwa kwao na kuangaliwa kwao. Kuweka miaka 25 ni kuwazuia vijana walio wengi kupata ajira na hasa ukizingatia ajira zenyewe ni chache.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kwamba wakati mwingine Serikali ijitambue na tujitambue sisi sote kwamba umri wa kuajiriwa kwa Mtanzania kuingia kwenye mfumo wa Serikali ni miaka mingapi? Sasa lazima Serikali kila mara inapotoa tangazo lake ijiridhishe kwamba ina Watanzania wangapi ambao kwa sasa umri unapita bila kuajiriwa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kwa kweli naomba tu Bunge hili na kwa busara zako tukahitimishe kwamba na ajira nyingine zote ziangaliwe kuanzia miaka 18 mpaka 30 ni umri sawa. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nichukue nafasi hii pia kukupongeza sana wewe kwa jinsi ambavyo unaongoza Bunge hili, lakini nichukue nafasi hii sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amewasilisha hotuba yake na jinsi ambavyo amehakikisha ametekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hasa kuanzia 2015 hadi 2020.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameonesha umahiri mkubwa sana katika jambo hili. Ukiangalia jinsi ambavyo ameanza katika mwaka 2015 hadi kufikia 2020, watu walikuwa wameanza kusema labda ni nguvu ya soda, lakini kwa kweli, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, amefanya kazi kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na wasaidizi wake kwa kweli, hatuna sababu ya kutokuwapongeza, lakini katika kupongeza huko nakumbuka maneno yako ulikuwa siku moja umesema, Spika wa Bunge la Kenya alisema Mtanzania akisimama, anapongeza halafu anakaa chini, lakini utamaduni wetu Watanzania ni kupongeza. Mtu wa Kenya akienda dukani anasema nataka chumvi hasemi naomba, kama sisi Watanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa pongezi, niende kuchangia kwenye maeneo mawili matatu, kama wenzangu ambavyo wamechangia. Naenda kwenye afya; Wizara ya Afya imefanya kazi kubwa sana. Katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi tunaishukuru Serikali sana kwa kutuletea fedha kwenye vituo vya afya. Kituo cha Afya cha Nduruma kimepata milioni 500, Kituo cha Mbuyuni milioni 400, Kituo cha Musa kimepata milioni 200; hii ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais katika kipindi chake ameboresha afya, amefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Zahanati nyingi tumewahamasisha wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi kwa ajili ya kujenga kwa dhana ile ya kila kata, kila kijiji kujenga zahanati kufikia lenta, kwa maana ya maboma, ili Serikali iweze kumalizia. Naomba kuishauri Serikali, hasa Wizara ya Afya, ni lini sasa itamalizia hayo maboma ambayo wananchi wamejenga katika kuwahamasisha, ili basi lile lengo la kila kijiji kuwa na zahanati, ili hizi zahanati zikamilike?

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu kuna zahanati nyingi sana kama 11 katika Vijiji vya Ilkerin, Bwawani, Kigongoni kule na kadhalika. Hii itasaidia sana kukamilisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kama Mheshimiwa Rais wetu anavyojali katika masuala ya afya.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Wizara ya afya kwamba, badala ya kuwapa wazee kitambulisho, ni kwa nini sasa Serikali isije kwenye sera yake irekebishe wazee wapewe bima ya afya kama watu wengine. Kwa sababu, katika kupewa vitambulisho hawapati huduma ipasavyo. Hilo nalo naomba Wizara hiyo iliangalie.

Mheshimiwa Spika, suala la upungufu wa Madaktari; hili nalo naomba Serikali ijaribu kuangalia kwa sababu, unakuta Nesi katika baadhi ya maeneo, Serikali imejitahidi sana, lakini bado kuna upungufu katika maeneo machache. Ningeomba Serikali irudie tena kuangalia maeneo hayo kwa ajili ya kupatikana kwa Madaktari katika vituo vyetu vya afya.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara. Serikali imejitahidi sana, nchi hii ni kubwa, lakini Serikali imejitahidi kuhakikisha kwamba, imeunganisha wilaya na wilaya, mikoa na mikoa, lakini naomba kuna ahadi ambazo Mheshimkwa Rais pamoja na viongozi wengine wameweza kutoa katika ziara na hasa wakati wa kampeni, basi katika bajeti ijayo barabara hizo zikumbukwe. Kwenye jimbo langu kuna barabara ambayo imefanyiwa tathmini kwa mfano barabara ya Arusha – Mirongoine – Tera kwenda Kongwa. Naomba hii barabara katika bajeti hii isisahaulike.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ambayo tumeahidiwa pia na Mheshimiwa Rais, Barabara ya Mianzini – Timbolo kutokea Sambasha kwenda Ngaramtoni, hiyo ni barabara ya kilometa 18, Mheshimiwa Rais aliahidi kwa kiwango cha lami. Naomba Wizara husika isisahau kwenye bajeti hii; vile vile barabara ya kwenda Hospitali ya Oturumet, Hospitali ya Wilaya, kilometa tatu; na barabara ya kwenda Hospitali ya Seliani, kilometa tatu. Hayo ni maeneo ya huduma ambayo wananchi hawa wanahitaji kwa ajili ya kupata huduma bora. Pamoja na hayo tunaendelea kuipongeza Serikali kwa sababu, kwa kweli inajitahidi kwa kadiri ilivyoweza kuwafikia wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, niingie kwenye suala la ajira; vijana wetu wengi wanakosa ajira, lakini Serikali imejitahidi kuimarisha sekta binafsi na hata ndani ya Serikali katika kuajiri vijana wetu. Ushauri wangu kuna Mfuko ule wa Akinamama na Vijana na watu Wenye Ulemavu; naishauri Serikali iangalie hiyo Sera ya Mfuko huo kwa sababu, utakuta vijana kuanzia miaka 18 mpaka 35 ndio wanaostahili kupata huo mkopo kwenye halmashauri zetu, lakini ukienda mbali zaidi ukiangalia watu wanaoweza kufanya biashara vizuri ni kuanzia miaka 18 mpaka angalau 40 mpaka 45.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali iangalie hiyo sera, ili kwa sababu ya ukosefu wa ajira kuanzia 18 mpaka 45 waweze kuingizwa kwenye sera ili waweze kupata hiyo mikopo. Hata hivyo, tunaendelea kuishukuru Serikali kwa sababu, imeondoa riba kwenye Mfuko huo na sasa wengi wananufaika isipokuwa upande wa vijana kuna changamoto kidogo kwa sababu ya hayo mambo magumu. Naomba pia, kuishauri Serikali kuangalia uanzishwaji wa vokundi kuanzia watu watano mpaka na kuendelea. Kwa sasa hivi ni watu 10, wananchi bado wanaona kidogo inawawia vigumu kuanzisha hivyo vikundi kuanzia watu 10 na kuendelea, lakini wakati ule ilikuwa watu watano angalau wananchi wanapata kujiunga vizuri na kuanzisha vikundi kwa ajili ya ujasiriamali. Nina uhakika eneo hili likiboreshwa suala la upungufu wa ajira ambalo kila siku sisi Wabunge na hasa mimi ninavyozungumzia kwenye jimbo langu, kila siku wananchi wananchi wanasema tutafutie ajira. Eneo hili tukiliboresha vizuri nadhani kwamba, wananchi wetu watapata ajira.

Mheshimiwa Spika, suala la NIDA; Mheshimiwa Rais katika hotuba yake alisema ataboresha vitambulisho vya Wamachinga na baadae viwe kama vya NIDA, lakini naomba watu wanaohusika na NIDA hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa kweli, wananchi wanateseka sana katika maeneo mbalimbali kupata huduma kwa sababu ya ukosefu wa vitambulisho hivyo vya Taifa. Hebu iangaliwe kwamba, kuna nini hasa kinachopelekea mpaka wananchi hawawezi kupata vitambulisho kwa wakati, ili waweze kupata huduma. Hasa ukizingatia kwamba, kitambulisho cha Taifa kwa sasa wananchi walio wengi wanahitajika kuwa nacho kwa ajili ya kupata huduma katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, suala la maji; kwanza niishukuru Serikali kwa kutupatia mradi mkubwa wa maji wa bilioni 500 katika Jiji la Arusha ambao unahudumia hasa katika jimbo langu na maji hayo yametoka kwenye jimbo langu. Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua mradi huo mkubwa kwa kweli, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ameonesha ni kiongozi ambaye watu. Ninachoweza tu kusema hapa naomba sasa niikumbushe Wizara iangalie yale maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameahidi, ili maji yaweze kuwafikia waweze kupata. Kwa mfano maeneo yale ya Floraid, Lemong’o, Lemanda, kule Ngutukoit, Losinoni Juu, Losinoni Kati mpaka huku chini kuja Oldonyosambu. Naamini Wizara itajitahidi kwa jinsi ambavyo inamuunga Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, suala la ulinzi na usalama wa wananchi wetu. Kama tunavyojua Serikali yoyote duniani ni Serikali ambayo inahakikisha wananchi wake wanaishi kwa salama na amani. Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imefanya kazi kubwa sana ukizingatia katika kipindi hiki chote cha miaka mitano uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa mno.

Mheshimiwa Spika, nina tatizo kidogo la kushirikiana. Nimwombe Waziri anayehusika wa Ulinzi, kuna mgogoro mkubwa sana na Waziri wa Maliasili, kuna mgogoro ambao haujakaa vizuri kwenye jimbo langu. Ningemwomba Waziri angefika kule kwenye Msitu wa Meru. Wananchi kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Elimu imekuwa na falsafa nyingi wakati wa miaka nenda rudi. Kulikuwa na suala la Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Elimu ni Bahari, Elimu haina Mwisho. Hayo yote ilikuwa ni kuhakikisha tunahamasisha elimu katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kuhakikisha kwamba elimu katika nchi yetu inasonga mbele. Kama tunavyofahamu elimu ndiyo imefanya Taifa hili likafika mahali hapa. Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema anaitwa J.K. Chesterton alisema: “Education is simply the soul of a society as it passes from one generation to another.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote ni mwelekeo wa kuhakikisha kwamba Taifa letu linakwenda kuwa salama kwa sababu wananchi wetu wanapata elimu. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wametuletea fedha za mabweni, madarasa na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nitajikita katika maeneo manne kuhusu vikwazo vya elimu. Vikwazo vya elimu vipo vingi lakini leo nitajikita katika vinne. Kwanza, suala la lugha, lugha ya kufundishia katika shule za msingi kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiswahili, lakini mtoto huyo anapofundishwa Kiswahili masomo kumi na moja, mara moja anatoka kuingia form one, anafundishwa masomo yote Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa wanateseka kwa sababu hawajui lugha ya Kiingereza wanapoingia form one. Hii inatuleta utata mkubwa, watoto wanachukia shule, hawapendi shule kwa sababu hawaelewi wanapofundishwa darasani form one mpaka form four na wakati huo huo wanapewa mtihani huo kwa Kiingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Wizara ya Elimu hebu suala hili liangaliwe kwa sababu ukiangalia shule za private kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiingereza, lakini mtoto wa shule ya Serikali anakwenda form one akiwa anajua Kiswahili tu, ushindani huu hauko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waziri wa Elimu atakapokuja hapa atuambie utafiti huu unasema nini kuhusu mtoto wa darasa la kwanza wa Serikali mpaka darasa la saba, akaja akaingia form one kwenda four inakuwaje? Hapo kuna usawa au tunawatesa watoto kisaikolojia. Naomba tupate maelezo kwamba Serikali inafikiria nini kuhusu hili jambo, kwa sababu hata ukiangalia ufaulu katika za Serikali watoto wanapata zero nyingi. Tunasema tupunguze zero, tutapunguza zero wakati tunawatesa watoto kwa lugha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia shule za private wanafaulu sana kwa kiwango cha juu, kwa sababu wao wametoka Kiingereza shule za msingi, wameingia shule za sekondari lugha ni ile ile ya Kiingereza. Suala hili naomba baadaye Waziri atakapokuja aweze kutueleza vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kingine ni chakula shuleni. Watoto wanateseka, kule shuleni wanasema, Serikali imetoa elimu bure au elimu bila malipo, wazazi wanasema hatuwezi kuchangia maana Serikali imetoa fedha. Sasa ni vizuri Wizara ya Elimu na TAMISEMI itoe tamko kwamba kila mzazi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata chakula au Serikali itoe chakula mashuleni, kwa sababu tunatengeneza Taifa ambalo tunadhani tuna usawa lakini hatuna usawa. Tutatenga watu walionacho na wasionacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wanaosoma private wanakula chakula kizuri mpaka wanamaliza shule, lakini watoto wanaosoma shule zetu za Serikali wanateseka, wanakataa shule, wanaingia makorongoni, wengine wanapata mimba na kadhalika. Ni kwa nini sehemu hiyo Wizara isitoe tamko, imekaa kimya, naomba atakapokuja pia aweze kutujibu kuhusiana na hiyo suala la chakula shuleni watoto wanateseka na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la upungufu wa walimu. Hili ni tatizo, mtoto anakwenda shuleni lakini katika masomo ya physics, chemistry, biology hakuna Mwalimu, lakini mwisho wa siku anapewa mtihani, kuna usawa gani hapo? Naomba Serikali ijitahidi kwa kadri iwezavyo kuwaajiri Walimu hasa wa sayansi ili kuleta usawa katika shule za Serikali na private, vinginevyo tutatengeneza Taifa la wenye nacho na wasio nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala la Walimu liangaliwe, waajiriwe walimu wa kutosha. Nilikuwa nasoma taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema hadi kufikia 2030 inahitajika Walimu milioni 69 kukidhi. Je, Tanzania sisi tumejiandaaje na suala hilo la kuhakikisha kwamba tumekuwa na Walimu wa kutosha. Pia, naomba Waziri atakapokuja atuambie pamoja na kwamba kuna ajira 6,000 za Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan amesema waajiriwe, lakini bado kuna haja ya kuongeza jitihada za kuhakikisha kwamba Walimu wanatosheleza ili kuleta usawa katika shule zetu za private na shule za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba suala la elimu ujuzi, wenzangu wamezungumza sana. Tuhakikishe kwamba katika Taifa letu mtu akimaliza, sio anazunguka na vyeti kutafuta kazi, anazunguka na vyeti huku na huku, kazi, kazi, lazima Wizara ya Elimu itengeneze Elimu Ujuzi. Iangalie namna gani itatengeza hiyo sera ili iweze kuhakikisha kwamba watu wetu wanakwenda kusoma lakini wawe na ujuzi wa kutosha kujiajiri na hata kuajiriwa ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi. Naomba nianze kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya; na Wizara hii kwa kweli wamejitahidi kuituliza kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri wanayoifanya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kuna changamoto mbalimbali ambayo sitaacha kuendelea kuwaambia ili waweze kuendelea kutatua na kuhakikisha kwamba wanazidi kung’aa. Kwanza kabisa urasimishaji wa makazi. Suala la urasimishaji wa makazi ni changamoto. Mmekuja na mpango wa kuwapa makampuni ili waweze kufanya urasimishaji wa makazi, lakini makampuni haya hayana uwezo, kwa sababu hawana wataalam mahususi wa kuhakikisha kwamba wanapima ardhi kwa manufaa ya wananchi. Wamekuwa kama ni matapeli fulani hivi ambao kule kijijini kwanza hawaeleweki, wakienda wanajifichaficha, hawana ushirikiano na viongozi vya wa vijiji, kata na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Wizara nzima wakaangalia eneo hili la urasimishaji wa makazi ikiwezekana waangalie yale makampuni ambayo hayana uwezo, lakini pia waongezee Halmashauri ili iweze kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wanapimiwa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la wawekezaji kutumia mashamba makubwa kukopa fedha katika Taifa letu na hatimaye kuingia mtini watakapokuwa wamepata hizo fedha. Hili ni suala la kuangalia kwa makini kwa sababu wawekezaji wanakuja wakisema tunawekeza, lakini mwisho wa siku wanakopa fedha kwenye benki zetu na kwenye taasisi zetu za fedha na baadaye wanatoweka na fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano mmoja. Kuna shamba moja kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi Lucy Estate. Mwekezaji huyu alikopa fedha kutoka Benki ya Standard Chartered na baadaye wakakopa NSSF kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni tisa, wametoweka, hakuna uwekezaji wala chochote. Wakati huo huo, baada ya kuona Standard Chartered inataka kuuza hilo shamba na NSSF waliamua kuweka objection mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaona kwamba tunapata hasara kwa sababu ya mali yetu. Shamba ni letu, fedha tumewakopesha, kwa nini tunawaachia hiyo loophole kiasi hicho? Naishauri Serikali kwamba ni vizuri kama mwekezaji anakuja; tuseme umekuja unataka kuwekeza Tanzania kuhusu masuala ya ardhi, basi uwe na asilimia 50 na unachotaka kuwekeza, ndiyo uweze kukopa kwenye Benki zetu na taasisi. Vinginevyo tutaendelea kupoteza ardhi na mwisho wa siku wananchi hawatakuwa na faida na Serikali yetu haitakuwa na faida yoyote. kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja atuambie hili eneo la wawekezaji kutumia loophole hiyo, hatusemi wawekezaji ni watu wabaya, ni wazuri lakini sheria zetu tutaliangalia vipi ili ziwe na manufaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni mashambapori. Kwa mfano, shamba hilo la Lucy sasa ni zaidi ya miaka kama 15, liko, ni shamba zuri, lina rutuba Arusha, hakuna elimu; shamba la Gomba Estate liko pale, ni shamba zuri halilimwi, lakini nazungumzia kilimo. Nitazungumziaje kilimo kama tunaweza kuacha maeneo mazuri kama hayo bila kutumia kwa manufaa ya wananchi wetu ili kuongeza ajira, kukuza uchumi wa nchi yetu? Tunasema kilimo, tunatunza ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri pia maeneo haya ayaangalie kwa sababu inaumiza sana, wananchi hawana ardhi, lakini ardhi inalala miaka 15, 20, 30 hailimwi na ni ardhi ambayo inalimika vizuri, inaingia kila aina ya mazao, inasikitisha na inakera.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Aga Khan ambapo walisema wanajenga Chuo Kikuu tangu mwaka 2006. Wameng’oa kahawa na hilo shamba lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500 mpaka 2,000; wameng’oa kahawa, wamefanya nini, wamesema wanajenga Chuo Kikuu tangu 2006, hawajajenga Chuo Kikuu mpaka leo. Je si ukiukwaji wa Sheria za Ardhi Na. 5 na Na. 4 za Ardhi na sheria nyingine za umiliki? Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri sehemu hii usiiangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili shamba wananchi wanalilalamikia ni zaidi ya ekari 4,000 kasoro limekaa; kwa sababu gani? Ni eneo ambalo linaingia aina ya mazao yote, ilikuwa inalimwa maharage, ilikuwa inalimwa ngano na mazao mengine mengi; maua na kadhalika. Wananchi walikuwa wanapata ajira; na Serikali sasa hivi haipati kodi kutokana na mazao ambayo yangelimwa pale hakuna. Tumeacha, tumenyamaza: Je, Aga Khan tunawaogopa, siamini kama Mheshimiwa Waziri Lukuvi anaweza kuwaogopa Aga Khan, kwa sababu hakuna mtu aliyeko juu ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tuko chini ya sheria, kwa hiyo, naomba eneo hili liangaliwe hasa katika shamba la Aga Khan. Naomba Mheshimiwa Waziri atembelee hilo eneo akague shamba lote aone. Asione tu kwamba sisi tunaongea kwa sababu labda tuna chuki, hapana. Tunataka kueleza namna na azima ya wananchi ambao tunataka Taifa letu liende.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Gomba Estate pia tumewapa JKT sawa, lakini je, wananchi ambao wako maeneo hayo, wao wanapata nini? Hili nalo tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la Mabaraza ya Ardhi. Mabaraza ya Ardhi inaanzia kwenye ngazi ya vijiji kwa maana ya Kushauri Kata na baadaye Wilaya. Mabaraza haya hasa katika ngazi ya wilaya kuna changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa kesi. Kesi inaweza ikakaa mwaka mzima, miaka miwili, miaka mitatu mpaka minne. Hii siyo sawa, ni kuwakosesha wananchi haki. Hili nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa Mabaraza haya wanatakiwa waangalie namna ya kutoa circular kuwapa posho hasa watu wa kwenye ngazi ya Kata, wanateseka. Tunaepukaje rushwa? Tunasema tunaondoa rushwa kwenye mfumo wa Mahakama, kama watu hao hatujawawekea mfumo mzuri, kwa mfano ufunguzi wa kesi kwenye Baraza la Kata, hayo makatarasi wale watu wanapata wapi kama hakuna chochote ambacho wanapewa kwa ajili ya kuweza kufanya hivyo kazi na kuwaangalia pia namna ya kuwapa posho?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi hasa baina ya wananchi na taasisi zetu za Umma imekidhiri. Kwa mfano, kuna mgogoro wa Kata ya Oldonyosambu, wananchi wale waliondolewa kutoka Oldonyosambu Jeshi letu likachukuwa eneo hilo. Ni vizuri sana kwa sababu ni kwa manufaa ya Taifa letu, lakini sheria inasema, mtu unapotaka kuchukuwa ardhi , mmiliki lazima apewe fidia. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inapotaka kuchukuwa eneo, iwape wananchi fidia na wale wananchi wale wananchi wa Odonyosambu wakumbukwe k wa sababu hii ni haki yao ya msingi. Kuwaondoa bila kuwapa haki yao, siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi na Nengun’g Kata ya Musa walishinda kesi Mahakama Kuu toka mwaka 2016, lakini taasisi yetu ya TMA imeng’ang’ania. Ni kwa nini tusiheshimu sheria? Naomba hii migogoro itatuliwe kwa sababu wananchi wanajiona hawana haki na wakati naamini kwamba chini ya Chama cha Mapinduzi, chama chetu, kimetengeneza ilani ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata haki zao kikamilifu. Kwa hiyo, naamini hili litatendewa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba lingine la Mlangalini Kiserya ,nao halikadhalika ni hivyo hivyo. Wananchi wamenyang’anywa kupitia Jeshi lakini bado hawapati haki zao, kutoka kule Kiserya Kata ya Mlangalini. Nayasema haya ili Mheshimiwa Waziri aweze kuona kwamba kuna haja ya kuangalia hayo maeneo kwa kushirikiana na Wizara nyingine kutatua hii migogoro, maana haileti picha nzuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la mabenki kukataa kutoa mikopo kwa kutumia hati miliki ya kimila. Benki nyingi zinakataa hiyo hati kwa sababu wanasema haina value. Sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla tuangalie hati hii, tusije tukawa tunasema tuweke tu hati ya kimila lakini wananchi hawanufaiki. Mtu kuwa na hati ni kwa ajili ya kumsaidia kupata mikopo na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, kama haina value, basi Serikali iseme wazi kwamba hii hati haina value. Kwa hiyo, wananchi wasihangaike kuiweka, lakini naamini kwa sababu Serikali ilikuwa na nia njema, hati hiyo lazima ina value.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba baadaye pia Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind-up, atueleze hiyo hati ni kwa nini mabenki hayapokei na kuna benki nyingine zinasema labda tunaweza tukawapa shilingi milioni tatu tu, mwisho wa hiyo hati. Sababu hakuna. Kwa hiyo, bado kuna changamoto katika hiyo hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangi kwenye bajeti hii ya 2021/2022 katika Bunge lako Tukufu. Na mimi nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru sana Serikali ya mama Samia Suluhu Hassan ya awamu ya sita pamoja na Waziri wa Fedha na Mawaziri wote kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wameshirikiana kutengeneza bajeti hii na kuiwasilisha kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo ninaenda kuchangia katika maeneo kadhaa, nikianzia kwenye eneo la ukusanyaji. Ili tuweze kutekeleza bajeti hii na bajeti hii iwe salama lazima Wizara yetu ya Fedha pamoja na taasisi zake zote, zikiongozwa pia na TRA, kuhakikisha kwamba mapato yakutosha yamekusanywa kulingana na bajeti yetu. Kwa sababu bajeti hii inategemea makusanyo ndipo tuweze kuteleza. Kama makusanyo hayatasimamiwa vizuri kama ambavyo wamejitahidi kusimamia ya 2021 malengo yetu haya yote tuliyoyategemea yatashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, kwa jinsi ambavyo Waziri amewasilisha, na alivyojipanga, ninaamini kazi itaendelea vizuri. Katika bajeti hii kama hatutakusanya vizuri hatutapata maji, barabara zile barabara zetu za kwenye majimbo, ukosefu wa maji, vituo vya afya na zahanati haitatelezwa. Lakini naamini Waziri akisimama vizuri, na Mawaziri wote wa idara zote bajeti itatekelezwa na hatimaye makisio haya ya trioni 36 ambayo tumekadiria kukusanya yatakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri ahakikishe kwamba ameweka mifumo rahisi na itakayowavutia walipa ili kodi walipe kodi kwa utaratibu mzuri kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na masharti yasiwe mengi katika kulipa kodi. Kuna watu ambao wanataka kulipa kodi lakini wanapoona huo mlolongo mrefu na vikwazo mbalimbali basi wanashindwa na wanachoka kwenda kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiweka urahisi katika kulipa kodi, tuweke usawa, kwa mfano mtu anapokwenda kupeleka fedha benki mlolongo unakuwa ni rahisi kwa sababu anaweka fedha benki lakini anapotoa inakuwa ngumu. Sisi katika kulipa kodi tunaweka mlolongo mrefu. Ningeomba milolongo hiyo ipunguzwe ili walipa kodi walipe kodi ili miradi yetu iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kukusanya kuna suala la upelekaji wa fedha kwenye majimbo na halmashauri. Hili nalo Mheshimiwa Waziri tunawapongeza kwa kipindi hiki cha 2020/2021 kwa sababu mmejitahidi kwa kweli. Kwa mfano kwenye jimbo langu mmetuletea bilioni mbili na point juu, mmetupa tena milioni 500 ambayo imetolewa na Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa awamu ya sita kwa kweli mmejitahidi. lakini tunaomba basi tutakapokwenda kukusanya tujitahidi tena mara dufu kwa sababu wananchi wetu wanategemea na wanaamini kwamba pale ambapo tutapeleka fedha za kutosha kwenye miradi tuliyopanga, hiyo ndiyo ahueni na furaha; na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi itatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata tutakapokwenda mbele ya wananchi tutakwenda kifua mbele kwa sababu tumetekeleza ilani ya 2021/2022 bila shida yoyote na watatuelewa vizuri. Kwahiyo naomba hili la upelekaji wa fedha tuhakikishe kwamba tunajitahidi kama tulivyojitahidi 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kupeleka fedha pia nizungumzie suala la uhaminifu na uhadilifu, kwa maana ya nidhamu katika matumizi. Hili suala la nidhamu na uadilifu katika matumizi ni suala muhimu na nyeti kwa sababu kama tutapeleka fedha lakini bila usimamizi tutakwenda kupata panya wanaotoboa magunia, watatoboa miradi yetu mara tutakapopeleka fedha itakuwa hatujatekeleza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tuhakikishe kwamba tumewazuia panya wasiharibu bajeti hii, tumewazua waharibifu, kwa sababu inashangaza sana na inasikitisha pale ambapo watu wanaofanya wizi, ujambazi, ufisadi na ulafi ni wale watu ambao wanalipwa mishahara, wanakaa lakini bado wanatamaa ya kuharibu bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta mtumishi amepewa gari, ofisi, watumishi, wasaidizi, kila kitu lakini bado anaungana na njama za kufanya ufisadi kwenye maeneo ya miradi naomba.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji kaka yangu anayechangia kiukweli anaongea ukweli kabisa, kwamba hii bajeti imekaa vizuri sana. Kama haitapata panya wakazitafuna hizo pesa tunazozipitisha hapa Serikali yetu itakuwa juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilikuwa nataka nimpe taarifa tu mchangiaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema, watu hawa ambao ni waharibifu tukiwaachia wakienda kukondesha bajeti hii, bajeti hii ikakonda kwa sababu panya, hatutaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Mawaziri wote, kwa sababu watatelekeza bajeti hii, wahakikishe kwamba bajeti hii haitakonda, haitakondeshwa, ili hatimaye malengo, nia na madhumuni ya kutelekeza ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika sekta za maji, barabara, elimu, afya na miundombinu vyote kwa ujumla viweze kufikiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo panya hawa tukiwaruhusu; na inashangaza, kama nilivyosema, mtu analipwa mishahara lakini bado ni mwizi na fisadi, yeye ndiye anaanzisha timu ya kufanya uhalifu. Ifike mahali sisi wote kwa ujumla wetu tupige vita rushwa, tutosheke na mishahara yetu. Kwa sababu hata ukikusanya dunia nzima, hata ukikusanya mali ngapi utakufa utaacha lakini huku umewatesa wa akina mama, hawana dawa, umewatesa akina mama wajawazito pamoja na wagonjwa wengine wakakosa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali hata milango yote ya ofisi za Serikali milangoni tuweke acha kupokea rushwa, acha kutoa rushwa. Tukienda kule msalani iwepo acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kwenye magari ya Serikali tuweke acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kila mlango wa Serikali iweke na popote pale panapotolewa huduma; hata mezani pale kama ni kwa Waziri liwekwe bango linalosema acha rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya pili nizungumzie suala la posho ya madiwani. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu imewakumbuka madiwani wetu na kuwaweka kwenye sehemu ya kulipa posho zao kutoka wizarani moja kwa moja. Hilo ni jambo jema sana na ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita. Hata hivyo kwa mshahara huu wa madiwani bado tunaomba Serikali iendelee kuangalia, kwa sababu kimekuwa ni kilio cha muda mrefu. Diwani huyu ndiye anayehangaika na kila kitu katika kata. Vilevile tusiwasahau wenye viti wa vijiji na vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuyaangalie maeneo hayo kwa sababu nao wanateseka sana, wenye viti wa vitongoji na vijiji na hata watendaji wetu wa vijiji ni wachapakazi kule na tunawakabidhi majukumu ya aina mbalimbali. Sehemu hii Serikali yetu imekaa vizuri sana katika masuala ya utawala, lakini naomba basi ikaangalie maeneo hayo kwa kuwa tumetoa fedha hizo za madiwani, na kama zinalipwa na Serikali Kuu naomba Shilingi 250,000 iliyobaki ikawaangalie wenyeviti wetu wa vijiji, watendaji wetu wa vijiji pamoja na wenyeviti wetu wa vitongoji ili nao waweze kuneemeka na Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri atakapokuwa ku-windup wajaribu kutoa waraka maalum wa kuhakikisha kwamba huu utaratibu wa kuwalipa Maafisa Tarafa iko Serikali Kuu lakini hii ya halmashauri itoe waraka unaosema Watendaji wa Kata walipwe kulingana na waraka huu kwenye vituo vya vitongoji kwenye vituo vya vijiji na Watendaji wa Vijiji. Hii itasaidia sana katika kuhakikisha kwamba utaratibu huo uliopangwa kwenye bajeti hii kwa watumishi wetu hawa wa chini inafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la property tax, kwa maana ya kodi ya majengo. Nilikuwa nasema naipongeza Serikali kwa sababu imekuja na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa kodi hii; na muendelee na huo utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba muangalie sana hizi nyumba za tembe, kwa maana ya nyumba za udongo. Unakuta nyumba nyingine ni ya udongo na ina umeme. Je, nayo ni miongoni mwa zinazoolipa proparty tax? Hilo ni suala ambalo Waziri kama ni miongoni au kama si miongoni basi uhakikishe kwamba umeweka utaratibu wa kufanya analysis ya kutosha ili wananchi wetu wasiumie. Ukusanyaji wa kodi ni muhimu ili bajeti hii iweze kufikiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kazi iendelee. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu, lakini nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetupa uzima siku ya leo na hata siku zingine zilizopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kujenga Taifa letu na Serikali yake yote kwa ujumla, Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, Makatibu, Naibu Katibu Mkuu na wote ambao wanamsaidia Mheshimiwa Rais kufikia malengo yake ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia mjadala huu kwa eneo la upimaji wa ardhi. Upimaji wa ardhi katika Taifa letu haiko vizuri na haliko vizuri kwa sababu kwanza wananchi kupata ardhi katika nchi yetu imekuwa ni changamoto. Changamoto yake ni kwamba upimaji wa ardhi bei ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya wananchi wetu katika vijiji na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati Tanzania ni kama kupata lulu, sijajua huwa ni kwa nini Tanzania ukitaka kupata hati inakuwa kama vile sijui una nunua nini? Ile karatasi sijui inapatikana katika misingi gani! Kwa sababu ni kwa nini ardhi haikubaliwi kupimwa kwa urahisi Tanzania na mtu akapewa hati kwa uharaka. Wataalam wanasema sijui wanafanya michoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michoro inachukua muda mrefu, ardhi haipimwi matokeo yake migogoro kwenye vijiji, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya Wilaya na Wilaya, Mkoa na Mkoa hatimaye tunaonekana tunaendelea kukataa kupima ardhi kwa sababu ya kuweka bei kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Wizara imeweka mawakala wa kupima ardhi, yale makampuni yamekwenda kule kwa wananchi wamekusanya fedha hawajarudi kuwapimia wananchi ardhi ili waweze kuwapa ardhi. Wengine wameingia mitini, lakini hii inatokana hivi kwa nini, nadhani ni kwa sababu Wizara mna jambo la kufanya kuhusu eneo hili la upimaji wa ardhi hasa makampuni ambayo mmeyaweka na kuyafanya yakapime ardhi kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaamini kwamba Serikali imetumia makampuni hayo ili iweze kuwachukulia fedha zao. Kila mwananchi ametoa shilingi 150,000 lakini hawajapimiwa ardhi, yale makampuni hayaonekani, sasa hii ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba baadae Mheshimiwa Waziri atoe tamko kuhusu fedha zilizochukuliwa wananchi kwa makampuni haya ambayo yamepima ardhi. Kwa sababu tunakwenda kuwaletea wananchi wetu matatizo kwa kuweka makampuni ambayo sio waaminifu na sio waadilifu. Najua nia ya Serikali ni njema, najua nia ya Wizara ilikuwa ni njema, lakini sasa katika utekelezaji wa jambo hili limeenda kutuletea changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wageni kumiliki ardhi, wakati mwingine hili suala la wageni kumiliki ardhi tunaambiwa sana wageni hawamiliki ardhi, lakini mimi naona ni kinyume sana tukisema hivyo kwa maana hii Derivative Right of Occupancy ambayo anapewa mgeni ni kama amemiliki tu. Unawezaje kumpa mgeni amemiliki ardhi miaka 99 halafu yeye anasema ni mwekezaji, sawa anakuja pale ile ardhi inakuwa ni yake wala hawekezi chochote pale anatumia ile hati aliyopata kwenda kukopa benki. Akikopa benki ule mradi anauacha, anakimbia na fedha, anatelekeza ardhi matokeo yake ile ardhi inakuja inauzwa tena kwa kufidia zile fedha au yule mwekezaji amekaa na ile ardhi yote pale kwa miaka hiyo yote 99 anaamua kuuza ile ardhi kidogo kidogo anauza kidogo kidogo kwa maana anasema ana sublease hii sio sawa. Mimi naona kama hili suala la kusema wageni wamiliki ardhi haliko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima Wizara, Mheshimiwa Waziri mkae muone namna ya kurekebisha hii ya sheria ya wageni kumiliki ardhi kwa sababu kama mtu amekuja na mtaja labda milioni 500 viwekwe vipengele ambavyo mtu haruhusiwi kuuza ardhi, haruhusiwi kutumia ile hati kwa kukopa fedha, anatakiwa aje na mtaji wake kama ile Sheria ya Tanzania Investment Centre inavyosema. Kama hatufanyi hivyo bado tunajidanganya kwamba wageni hawamiliki ardhi. Kama unammilikisha miaka 99 wakati hakuna binadamu ambaye hata kwenye vitabu vya Mungu ni miaka 70, miaka 80 ni ya tabu na huzuni, hiyo miaka 99 nani anajua kwamba atafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa bado kuna changamoto inatakiwa muangalie kwa sababu bado hatuwatendei wananchi haki katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Mabaraza ya Ardhi; Mabaraza ya Ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Land Act No. 113) ya mwaka 1999 na Sheria ya Land Disputes Courts Acts iliyoanzisha mabaraza hayo mwaka 2002 na ikaanza kufanya kazi mwaka 2003, ni miaka 20 sasa imepita nadhani tuna mabaraza 92 Tanzania nzima. Hii sioni kama ni haki kwa sababu ukiangalia hata kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza katika Ibara ya 107(a) kwamba lazima Serikali iweke mazingira ya kutochelewesha haki bila sababu zozote. Sasa katika mabaraza hayo hayana mfumo mzuri wa utoaji haki. Kama baraza linaweza kupiga kesi miezi sita, mwaka mmoja, miaka miwili, mitatu, mitano bila kutoa haki hii sio sawa kwamba wananchi hawa wanapata haki kupitia mabaraza haya. Martin Luther King aliwahi kusema; “A right delayed is a right denied” haki iliyochelewa ni sawa na haki iliyonyimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira hayo ya mabaraza haya hatuwezi kuona kwamba haki inatendeka katika mabaraza ambayo hayana mfumo mzuri wa kimahakama, na kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kwamba mamlaka iliyopewa kutoa haki ni mahakama kwa nini mabaraza haya sasa isifike mahali tuachane na mfumo uliopo ambao udhibiti wake wa namna ya kutoa haki haupo sawa, tukaingiza kwenye mfumo wa mahakama ambayo itakuwa kwenye udhibiti. Mahakama imekaa vizuri sana katika utoaji wa haki kwa sasa. Kwa nini tunaendelea kung’ang’ania mabaraza hayo chini ya Wizara? Hatuoni tunawanyima wananchi haki? Ukizingatia kwamba tumeshindwa kufikia mabaraza yote katika Wilaya nzima. Unakuta katika Mkoa mmoja wenye Wilaya saba mpaka tisa kuna mabaraza mawili tu tena yapo pale Mkoani, hii haki iko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hatutendi haki kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais amefika mahali anawataka wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapate haki mpaka ameenda mbali zaidi ameunda Tume ya Haki Jinai; unafikiri anafikiria nini? Watu walioko magerezani na popote pale wakiteseka waweze kupata haki zao. Je, ni kwa nini sisi kama Wizara au ninyi kama Wizara msione sasa kwamba kuna haja ya ku-handover hayo mabaraza kwenye mfumo wa mahakama? Kuna tatizo gani na shida gani? Kwa sababu ukiangalia kwa maana ya research miaka 20 kama hamjaweza ku-meet vile vigezo vya kila Wilaya kuwa na mabaraza ina maana tume-fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe baadae Mheshimiwa Waziri hili suala mlitolee tamko na sio suala gumu. Tuna mfumo mzuri wa mahakama yetu kuanzia Baraza la Kata, Mahakama ya Mwanzo mpaka juu hata hayo mabaraza yakiendelea kuwepo, lakini yaingie kwenye mkondo wa kimahakama hii itasaidia wananchi waweze kupata haki na kuepuka kufata haki kule mbali ambako sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini Mheshimiwa Rais aliyewaweka pale, Mheshimiwa Waziri, Rais anakutegemea umsaidie katika kuleta mabadiliko katika Wizara hii ya Ardhi. Mabadiliko yenyewe ni haya ambayo inatakiwa wananchi waone haki inatendeka kwa sababu sio tu haki itendeke, lakini haki ionekane ikitendeka.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, wananchi wanakutegemea, wanakuangalia unavyoweza kuwatoa katika dhiki hii ya mabaraza haya. Tume ya Kurekebisha Sheria inatakiwa iyaone haya kwa sababu ni kazi yao kuleta sheria ambazo hazina tija na zimepitwa na wakati. Sheria ya Ardhi irekebishwe, Sheria hii ya Mabaraza irekebishwe na sheria zingine ambazo ni kandamizi na hazileti tija na mwelekeo mzuri kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, yeye aliyetupa uwezo kwa siku ya leo kuwepo katika Bunge hili kutekeleza majukumu yetu ya Kibunge. La pili, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo anafanya kazi yake vizuri ya kuliongoza Taifa letu ili kuhakikisha hatma na matumaini ya wananchi wa Tanzania yanafikiwa katika nyanja na sekta mbalimbali. Nisiache kupongeza Wizara nzima ikiongozwa na Waziri wetu na wataalamu wake wote wanaoshughulika na masuala ya Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu moja kwa moja na changamoto zinazokabili Wizara hii ikiwemo Mahakama. Kwanza suala la ufinyu wa bajeti katika Mahakama na Wizara kwa ujumla, hasa Mahakama. Pale ambapo chombo kama Mahakama kinakosa uwezo wa kufanya shughuli zake za kutoa huduma na utoaji wa haki katika nchi ina maana kwamba suala la utawala bora halipo sawa. Kwa hiyo kitendo chochote cha kujaribu kuinyong’onyeza Mahakama kwa kutoipa bajeti yake kihalisia na jinsi ilivyopitishwa na Bunge na jinsi walivyokusudia, hiyo inamaanisha kwamba ni kudhoofisha utoaji wa haki na kukiuka misingi ya haki za kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka kuiasa Serikali katika kutoa fedha kwa ajili ya kuipa Mahakama itoe OC kikamilifu ili iwezeshe Mahakama kutekeleza majukumu yake. Itoe pia suala la kuiwezesha Mahakama katika kuhakikisha kwamba imefika katika maeneo ya huduma. Hata hiyo Tume ya Haki za Binadamu kama kweli ukiweza kuunda chombo ambacho hukiwezi kukihudumia au kukipa fedha, basi ina maana gani? Haina maana ya kuwepo, sasa kama Serikali inataka kutuambia hiko chombo hakina maana, basi Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie kwamba kwa nini hiyo Tume ya Haki za Binadamu haipewi fedha zake na kama ina uhalali wa kuwepo kwa mujibu wa Katiba kwa sababu ipo kwenye Katiba kwa nini hamuipi fedha? Ni suala ambalo Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kama Serikali atujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la OC lazima Mahakama ipewe, lakini siyo hilo tu pia suala la ukarabati wa Mahakama na ujenzi wa Mahakama. Tunashukuru kwa sababu Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa sana katika suala la ukarabati wa Mahakama, lakini pia suala la ujenzi wa Mahakama mpya, tunaipongeza Serikali sana katika sehemu hiyo na tunampongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa ujumla ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba ili mtu aweze kuona kwamba haki inaweza ikapatikana na ikatendeka ni pale tu ambapo anafika katika eneo la utoaji wa haki akaona eneo hilo linafaa, anaburudika kwa sababu ni eneo safi, ni eneo ambalo linaonesha kabisa kwamba kuna tafsiri na taswira ya yeye kupata haki zake za msingi. Sasa anapofika katika eneo ambalo ni la utoaji haki na yakawa ni maeneo ambayo ni mabovu, ni machakavu, anaona hivi hapa kweli nitapata haki yangu au ndiyo nimekuja kuangamia. Kwa hiyo, hili nalo ni suala ambalo lazima Serikali ilione kwa mapana yake, kwamba lazima Mahakama zote zile za zamani zikarabatiwe na maeneo mengine ambayo yanahitaji Mahakama yaweze kupata hizo Mahakama, ikiwemo katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi katika Kata ya Bwawani ambayo nilikwishaitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la upungufu wa watumishi. Suala la upungufu wa watumishi kwa maana ya Majaji, naona Mheshimiwa Rais, anajitahidi sana kuteua Majaji mara kwa mara, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini katika kada hii ya Mahakimu naona kama bado kuna changamoto. Pia, Mahakama ipewe uhuru wa kuajiri yenyewe kwa sababu yenyewe ndiyo inajua inahitaji watu kiasi gani na watu ambao wana-professional kiasi gani katika uzoefu wa kutoa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo pia cha kutoipa Mahakama uhuru ni kuikiuka ile Ibara ya 4(i) ya Katiba ambayo imezungumzia kuhusu suala la separation of power ambayo ndiyo tunapata masuala ya executive, legislative na Judiciary. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Serikali yenyewe inashindwa kutoa uhuru kwa Mahakama kwamba iajiri ina maana bado inaingilia (interference) ya Mhimili mwingine, inaonesha kwamba hatuheshimu misingi ya haki za kibinadamu. Pale unapogusa sheria yoyote ambayo inataka kuzuia haki yoyote una maana unakiuka haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye marekebisho ya sheria mbalimbali, maana ya kuwepo kwa sheria ni kuweka sheria ili iweze kusaidia Taifa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kadhalika, sasa kama kuna sheria ambazo zimepitwa na wakati lakini bado tunaendelea kuziangalia hatuzirekebishi ina maana kwamba, hapa ndipo ambapo pia tunaendelea kukiuka haki za binadamu na kurudisha uchumi wetu nyuma na kuwafanya wananchi wasiweze kuona Serikali kweli ina nia njema ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria kama Sheria ya Rushwa, The Prevention and Combating Corruption Act, Cap 329 na marekebisho yake ya mwaka 2022. Sheria hii bado haiipi TAKUKURU uwezo wa kupambana na rushwa kikamilifu. Nikisema hivi waliosoma hiyo sheria na hata AG anaweza kukubaliana na mimi kwamba, tunahitajika kufanya marekebisho makubwa sana kwenye hiyo sheria ili kuiwezesha TAKUKURU kuwa na uwezo mkubwa na kuiimarisha ili kuwa na adhabu ambazo zinaendana na suala lenyewe la rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo chochote cha kuhujumu mali ya umma si suala la kufumbia macho, ni suala la sisi wote kukazia macho ili tuweze kujenga uchumi ambao Serikali ikikusanya kodi yake pasiwepo na panya yeyote ambaye anaingiza mikono yake kwa sababu ya udhaifu wa sheria, pia kutokuwepo kwa maadili. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ije kuirekebisha sheria hii kwa sababu haipo sawa, imepungua nguvu zake kwa mujibu wa jinsi ambavyo tutaitazama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la marekebisho ya sheria mbalimbali kama nilivyosema, sheria za kurekebisha ni nyingi, lakini najaribu kutaja haya ambayo nimeona yapo hapa. Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1979, kwanza nasikitika sana, Mahakama imetoa hukumu kwamba sheria hii irekebishwe na ikatoa na muda specific, lakini mpaka leo Serikali imekuwa na kigugumizi, ina maana Serikali haitaki kusikia Mahakama imesema kama Mhimili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya wananchi kule nje wanaona kwamba, kumbe Serikali yenyewe kwa sababu ni Serikali inaweza kukataa kutekeleza sheria au kutekeleza hukumu ya Mahakama, ni kwa nini? Nadhani Mheshimiwa Waziri akija hapa katika ku-windup atueleze ni kwa nini Serikali haitaki kuhitimisha jambo la kutekeleza hukumu ya Mahakama ya kurekebisha Sheria ya Ndoa kuhusiana na umri wa kuolewa watoto wa kike? Kwa nini na matatizo hayo bado yanaendelea mpaka leo? (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa mzungumzaji kwamba, kuna sheria zinazohusu wanadamu, pia zina maadili ya kidini na maadili mengine ya kibinadamu na utamaduni wao katika nchi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mollel.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei, mtoa taarifa labda angesoma sheria na kuunganisha pia Sheria za Dini ya Kikristo, Sheria ya Kiislamu, hakuna sheria inayosema kwamba mtoto wa umri wa miaka 16 au 13 aolewe. Kwa hiyo, naomba mzungumzaji asipotoshe Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hiyo ni kengele ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sheria hiyo naomba irekebishwe na Mheshimiwa Waziri atuambie kwa nini Serikali haitaki kurekebisha sheria hii au inakataa uamuzi wa Mahakama ambapo Mahakama ambayo ndiyo chombo pekee kichopewa uwezo wa kutafsiri sheria na kutoa haki katika Taifa hili, otherwise tuambiwe kuna namna nyingine ambayo tunaweza tukapata haki kwa kupitia chombo kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kusema Sheria ya Wanyamapori. Sheria ya Wanyamapori imekuwa na yenyewe ni sheria kandamizi, wanyamapori wana thamani zaidi kuliko binadamu. Binadamu anapouawa fidia anayopewa sijui ni shilingi 500,000, sijui 1,000,000 lakini mnyama akiuawa au akikutwa mtu na ngozi ina maana atapigwa faini ya uhaini ya kuua mnyama ambayo atatozwa faini labda mamilioni ya shilingi au akafungwa hata maisha, hapa binadamu haangaliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria nayo ni ya kuitazama ili fidia ya raia nayo iongezeke kwa kiwango ambacho hakiwezi kumlipa binadamu, lakini kitoe matumaini kwamba, angalau binadamu nao wameonekana ni watu. Kwa hiyo, sheria hii nayo inatakiwa kurekebishwa kwa sababu haitendi haki kwa wananchi wa Tanzania, tunaona wanyama wana thamani zaidi ya binadamu au Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mabaraza ya Ardhi kwa maana ya Land Disputes Act. Cap. 216 na marekebisho ya 2019 na yenyewe inatakiwa irekebishwe. Mabaraza haya hayatoi haki kwa wananchi wa Tanzania. Mabaraza haya yenyewe katika mikoa, unaweza kukuta kwa mfano, Mkoa wa Arusha, Mabaraza ya Ardhi yapo mawili katika wilaya saba, sasa haki inapatikana wapi hapo na migogoro ya ardhi ni mingi? Naomba sheria hii irekebishe Mabaraza yote ya Ardhi yapitishwe kwenye mkondo wa Kimahakama, kwa sababu itatusaidia sana kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata haki na kuepukana na mambo ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya, kesi inapigwa kwa mara moja miezi sita. Mtu anakaa miezi sita ndiyo aende kwenye kesi au mwaka mzima ndiyo aende kwenye kesi. Sasa hiyo ni kesi au ni kitu gani? Hiyo ni kudhulumu na ni kwamba, sisi kwa upande wa Sheria tunasema the right delayed is the right denied kwamba, haki iliyochelewa kutolewa ni sawa na haki iliyonyimwa. Sasa sidhani kama Serikali inakusudia kufanya hivyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili hiyo…

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia dakika moja kidogo tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili, utachukua muda wa mwingine.

Tunaendelea na Mheshimiwa Dkt. Chaya, ajiandae Mheshimiwa Kilumbe. (Makofi)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhili nisipompongeza sana Waziri na timu yake nzima kwa maana ya Naibu wake pamoja na Wizara yake kwa ujumla ikiongozwa na Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kusema kwamba katika usambazaji wa nishati kwa maana ya umeme Tanzania kwa kweli tumepiga hatua kubwa sana. Ukipita kwenye mapori na maeneo mbalimbali ukiona jinsi ambavyo nguzo zinapita utaona jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi kwa kiwango kikubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani ya usambazaji wa umeme bado tunaendelea kusema tunakwenda kusonga mbele na kuikumbusha Serikali kuendelea kumalizia maeneo ambayo bado. Katika usambazaji wa umeme wakandarasi ambao walikuwa wamepewa kazi hii wengine wamekuwa siyo wazuri sana, siyo wote lakini siyo wazuri sana. Hivyo, Wizara ni vizuri ikaangalia kwa makini sana wakandarasi hawa ambao wamekuwa hawafanyi kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi mkandarasi aliyepewa kazi pale amechimba mashimo kwenye maeneo mengine hajaweka nguzo, amesimamisha nguzo hajaweka waya, maeneo mengine hayajakamilisha miradi kwenye vijiji na na kadhalika. Uchimbaji wa mashimo umewafanya wananchi, ng’ombe na mbuzi kuvunjika miguu. Naomba Wizara chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Kalemani (mchapakazi) afike kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi ili kuweka msukumo katika usambazaji wa umeme kwenye Kata za Bwawani, Nduruma, Kisongo, Musa, Mwandeti, Lingijale, Lemanyata, Kimyaq, Sambasha, Ikiding’a, Oljuroto, Tarakwa, Oturumet, Matebesi, Naroi na Oljoro. (Makofi)

Mheshimiwa Sjpika, kama unavyofahamu Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo ambalo limeweka Jiji la Arusha katikati, kwa hiyo sisi tumezunguka Jiji la Arusha kama yai, wananchi wale wanahamu sana ya umeme. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Kalemani aweze kutembelea na kuweka msukumo wa usambazaji wa umeme kwenye jimbo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la bei ya nguzo. Suala hili limekuwa kizungumkuti kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuwa akijitahidi sana kutumia nguvu kubwa kueleza kwenye mihadhara mbalimbali kwamba usambazaji ni shilingi 27,000 lakini jambo hili TANESCO wanapolitelekeza linakuwa kinyume chake. Sasa inawezekana tunailaumu TANESCO lakini kuna nini huko ndani? Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kufafanua zaidi kupitia waraka maalumu, kama ameandika sijui, lakini kama hajaandika atoe waraka TANESCO kwa maana ya TANESCO mikoa yote Tanzania, umeme wa REA ni shilingi 27,000, je, miradi ya TANESCO yenyewe ni shilingi ngapi, ni shilingi 177,000 au kuna tofauti ili mwisho wa siku wananchi waweze kuelewa gharama hii ya shilingi 27,000 na shilingi 177,000. Suala hili ni kizungumkuti katika utekelezaji, Waziri anatamka lakini utekelezaji unakuwa mgumu labda kuna kitu ndani. Hilo nalo Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia na kulitolea ufafanuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, suala la upandaji wa gesi. Ujio wa gesi umepunguza sana uharibifu wa mazingira na huko vijijini gesi hizi ndogondogo kwa mfano hii ya kilo sita imepanda kutoka shilingi 16,000 hadi shilingi 20,000. Sasa hali hiyo inaenda kutusababishia uharibifu wa mazingira, wananchi watarudi tena kwenye kukata miti na kuharibu mazingira. Naomba pia hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa nini gesi ile ya kilo sita ipande kutoka shilingi 16,000 mpaka shilingi 20,000? Hili nalo ni jambo ambalo Wizara inatakiwa iliangalie kwa makini kwa sababu gesi imesaidia sana katika kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kukatikakatika kwa umeme. Kumekuwepo na tatizo la kukatika kwa umeme, hatukatai kwa sababu mitambo ni mitambo tu lakini pale ambapo umeme unakatika ghafla basi tunaomba Wizara isimamie TANESCO iweze kutoa taarifa kwa wananchi kwamba umeme umekatika kwa muda huu na tunategemea uwake kwa muda fulani au siku tatu au nne. Kukaa kimya au kutowaeleza wananchi umeme umekatika kwa sababu gani na ni kwa nini inaleta wasiwasi na hofu na kurudisha pia maendeleo nyuma. Kuna watu umeme ukikatika dakika moja tu wanapata hasara kubwa sana katika kuendesha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, umeme ni nishati ambayo inahitajika sana kwa Watanzania kwa ajili ya kuleta maendeleo tena maendeleo endelevu. Kwa hiyo, niombe kukatika kwa umeme tuwape taarifa wananchi ili waweze kukaa tayari kujua kwamba kuna nini na baadaye watapata kwa wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi pia na mimi ya kuchangia Protocol au Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na kuwepo asubuhi ya leo katika Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ina historia ndefu kidogo ambayo imetoka mbali. Ilianzishwa na Waasisi waliotangulia mbele ya haki na sisi leo tunaendelea kuiboresha zaidi kama ambavyo tumepata fursa hii siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mwaka 1917 ikiwa na nchi mbili ya Kenya na Uganda. Baadae mwaka 1927 Tanzania ilijiunga katika Jumuiya hiyo ikiwa na jina jingine kwa maana ya Tanganyika. Lakini Jumuiya hii ilikuja tena kuanzishwa rasmi kwa hizo nchi tatu ikitambulika kama Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967 ambapo baadae iliendelea kushamiri na kunawiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1977 Jumuiya hii iliweza kuanguka. Sababu za kuanguka kwa jumuiya hii zilikuwa ni nchi wanachama ikiwemo Kenya kudai sehemu kubwa ya maamuzi. Pia jambo lingine la pili ilikuwa ni nchi ya Uganda kwa maana ya Dikteta Idd Amin kuvamia Tanzania, kuchukia kuona kama Tanzania inaingilia uhuru wa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na historia hiyo yote, jumuiya hii tena ilianzishwa mwaka 1999 baada ya Wakuu wa Nchi kukaa na kuona kwamba kuna haja tena ya kuendelea kunyanyua jumuiya hii. Jumuiya hii iliendelea kwa wananchi wake kushirikiana kwa nchi tatu na baadaye nchi nyingine mbalimbali ziliongeza kama Burundi, Rwanda mpaka baadaye na Kongo juzi imejiunga. Hayo yote yanafanya jumuiya hii iweze kusaidia wananchi wake kuingia katika nchi yoyote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kufanya biashara, kazi, na pia ule ushirikiano wa kindugu, kisiasa kijamii na kiuchumi nao umeendelea kushika kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba jumuiya hii inaendelea kusonga mbele, Wakuu wa Nchi tarehe 2/3/2004 waliweza kusaini Itifaki ya Soko la Pamoja, lakini pia tarehe 30/11/2013 ilisaniwa pia Itifaki ya Sarafu ya Pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naendelea kusema hivyo? Ni kuonesha kwamba sisi leo kuletewa itifaki kuisaini, siyo kwamba ni jambo la kwanza, bali hasa katika itifaki hii tumechelewa kufanya hivyo. Nadhani ni kwa sababu Tanzania ni nchi makini, ambayo watu wake wanafanya utafiti wa kina katika masuala mbalimbali, ndiyo maana tumechelewa kwa kiwango hicho, lakini bado tuko kwenye jumuiya na tumekuwa ndio wabeba jumuiya kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunatakiwa kuongezea Jumuiya ya Afrika Mashariki nguvu kwa maana ya mamlaka? Tunatakiwa kufanya hivyo kwa sababu kwanza mkataba wenyewe unatutaka kufanya hivyo. Katika kifungu cha 27 kifungu kidogo cha (2) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa ruhusa yako naomba kunukuu: “the Court shall have such other origina,l appellate, human rights and other jurisdiction as will be determined by the Council at a suitable subsequent date. To this end, the partner states shall conclude a protocol to operationalize the extended jurisdiction.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifungu hicho tunapewa mamlaka hayo ya kuweza kuongezea Mahakama hii mamlaka ili iweze kuamua haki kwa wanachama wote kwa maana ya nchi wanachama, kwa wananchi wetu; na kwa maana nyingine kwamba lazima wawekezaji wetu waweze kuamini nchi yetu kwamba imesaini mkataba kikamilifu katika kuhakikisha kwamba tunapata wawekezaji wengi zaidi na wananchi wetu wanaweza kupata haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, kabla ya hapo, suala la migogoro ya biashara ilikuwa inafanywa na nchi wanachama kwa maana ya Mahakama za ndani ya nchi wanachama. Sasa suala hili wakati mwingine linaleta changamoto kwa sababu inakuwa ni mgogoro wa maslahi (conflict of interest) katika Mahakama za ndani. Labda tuna kesi Uganda na nchi nyingine au mwananchi wetu wa Tanzania, obviously tutaanza kufikiri kwamba kama yule mtu wa Uganda atapewa haki, ina maana tutasema Mahamaka ya Uganda imetuonea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuridhia itifaki hii ni faida kubwa sana kwetu kama nchi na wananchi wetu pale ambako tutakuwa na mashauri ambayo yanafanyiwa maamuzi. Kwa sababu tukienda mbali zaidi, utakuta shauri ambalo limefanyika Uganda linaweza likatolewa maamuzi tofauti, baadaye ikija Tanzania maamuzi tofauti, ikienda Rwanda maamuzi tofauti. Kwa hiyo, kama tutaiongezea Mahakama hii ya Afrika Mashariki suala la mamlaka kamili, itakuwa inatoa maamuzi ambayo ni moja tu katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kulikuwepo pia na wasiwasi ndani ya nchi yetu kwa maana ya wananchi wa Tanzania kwamba sisi kuridhia itifaki hizi inaweza kuchukuwa ardhi yetu. Hiyo ilikuwa ni mitizamo ya wananchi wetu wa Tanzania, lakini tunahakikishiwa ndani ya itifaki katika Ibara ile ya 15 ya Soko la Pamoja kwamba ardhi haitahusika katika itifaki hii ambayo inaridhiwa na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaondoa kabisa wasiwasi kwa Watanzania kwamba ardhi itakuwa ni miongoni mwa maamuzi. Ardhi itabaki katika kuamuliwa na Mahakama za ndani za Tanzania, kama ambavyo imesemwa ndani ya itifaki yenyewe. Kwa hiyo, wasiwasi huo kwa wananchi wetu na Bunge lako Tukufu tuondokana nalo kabisa kwa sababu haitakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuridhia itifaki hii ni kubwa sana na ninaamini kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataridhia. Kwa sababu tukiridhia, wananchi wetu watakuwa na uhuru wa kuingia katika nchi yoyote kwenye Jamhuri hizi za Afrika Mashariki, kuingia na kutoka na kufanya biashara mbalimbali, watakuwa na uhuru wa kufanya kazi kama ambavyo hata sasa wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watakuwa na uhuru wa kupata huduma mbalimbali katika Jamhuri hizo za nchi za Afrika Mashariki, kuwekeza mitaji mbalimbali. Kama walivyosema, tutakapokuwa tumesaini itifaki hii, wawekezaji wetu watakuwa na imani kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania na katika nchi za Afrika Mashariki kwa sababu sasa wana kitu ambacho wanaamini kwamba Mahakama ya Afrika Mashariki itatoa haki kwa pande zote bila upendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasisitiza kwamba tukumbuke kwamba Wimbo wa Jumuiya wa Afrika Mashariki ni kielelezo dhahiri shahiri, inatueleza kwamba tuilinde Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Maudhui ya wimbo huo yanaeleza kabisa kwamba tuna wajibu mkubwa wa kulinda Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupitisha itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapitishe itifaki hii bila wasiwasi wala tashwishi kwa sababu sisi Kamati tumepitisha na tumechambua kwa kina, na tumeuliza maswali kadha wa kadha ili kujiridhisha kwamba tuna maslahi gani ndani ya itifaki hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri wake wote wanaomsaidia, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii na Manaibu pia kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia kwa kuanza na TAMISEMI. TAMISEMI ambayo ndiyo Wizara tunayoichangia na kwenda kuanza na TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri sana katika kipindi hiki ambacho imepewa fedha baada ya sisi Wabunge kusema sana katika Bunge hili. Kumekuwa na changamoto, tumepewa fedha shilingi bilioni 1.5 iliyotolewa na Mheshimiwa Rais na tulitangaziwa kwenye Bunge hili. Hata hivyo, naweza kusema wakandarasi ambao wamepewa kazi katika kipindi hiki hasa kwenye jimbo langu kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa sababu imekuwa ikileta matatizo makubwa kwa wananchi kwa sababu tangu mwaka jana fedha zipo kwenye akaunti wakandarasi wamepewa kazi, wakandarasi ni dhaifu, hawafanyi kazi, matokeo yake wananchi wanalalamika usiku na mchana. Hapa ninapozungumza wananchi wa Kata ya Kihutu wameandamana ambao tumewaambia kwenye mikutano kwamba barabara inatengenezwa toka mwaka jana, wanasema, Mheshimiwa Rais utusaidie Mkandarasi hayupo kazi, wanaona sisi ni waongo, hatufanyi kazi, tunawadanganya kwenye mikutano ya hadhara, wakati Serikali imeshatoa fedha, lakini udhaifu wa wakandarasi. Naomba TARURA waliangalie jambo hili kwa sababu wanatudhalilisha. Fedha za UVIKO zimekuja juzi tu miradi ilishatekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu ya usimamizi mzuri. TARURA wanafanya kazi nzuri lakini wakandarasi wanawaangusha, hawafanyi kazi na sisi wanatudhalilisha.

Mheshimiwa Spika, naomba pia katika mgao wa fedha za TARURA kwa majimbo tuangalie kwa sababu kuna majimbo ambayo ni magumu sana kama Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Jimbo langu la Arumeru Magharibi lina makorongo, barabara zake zote ni mbovu, kwa hiyo naomba katika mgao watuangalie kwa jicho la huruma kwa sababu wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi na majimbo mengine makubwa, kwa kweli wanahitaji fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara zinatengenezwa. Barabara katika Jimbo langu ni kilometa 685 za changarawe. Sasa kwa fedha ambazo tunazipata ni kidogo sana kwa hiyo naomba mtuangalie.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye ahadi za Rais ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa katika Jimbo la Arumeru Magharibi na katika majimbo mengine yote. Naomba ahadi hizi ambazo zinatolewa na Mheshimiwa Rais ziangaliwe sana kwa makini na Waheshimiwa Mawaziri katika kuingiiza kwenye mipango yao. Kwa sababu mwisho wa siku Taasisi ya Rais inaonekana kwamba haiheshimiwi na wananchi pale inapotoa tamko kwamba itatekeleza jambo fulani, kwa mfano, Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo langu ameahidi ukarabati na marekebisho makubwa kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo yeye ameizindua, kwamba itaongezewa majengo, itawekwa na kila kitu lakini tangu Serikali ianze kugawa fedha za Hospitali za Wilaya, Hospitali hiyo ya Wilaya ya Oturumeti Arusha DC haijawahi kupata hata shilingi moja kutoka Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho aniambie ni lini atapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha hospitali hiyo. Vinginevyo nitashika mshahara wake kwa sababu wale wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi nao wana haki katika mgao wa fedha za hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kujenga barabara kilomita tatu katika hospitali hiyohiyo, Rais ametoa ahadi hiyo hadi leo hakuna namna ambayo kuna namna ambayo wanatekeleza ahadi hiyo ya Rais. Siyo kwangu tu na kwa majimbo mengine yote, lazima sasa wafike mahali Mawaziri wote ahadi za viongozi wetu ambao wanazitoa kwa kuwajengea heshima na hasa Taasisi ya Rais ambaye ndiye msemaji wa mwisho katika Taifa hili na ndiyo tumaini la wananchi anaposema jambo lazima zitekelezwe. Kwa hiyo naomba ahadi za Rais ziwekwe kwenye kitabu maalum kitakachoonyeshwa kila Bunge kwamba zinatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna zahanati ambazo hazijakamilika mmetuma milioni 50, lakini bado tunaomba TAMISEMI warudie tena kutoa fedha kwa ajili ya zahanati hizo na vifaa tiba pia.

Mheshimiwa Spika, posho za Madiwani na Wenyeviti wa Vitongoji; hawa watu wanafanya kazi kubwa sana kwenye majimbo yetu na kwenye halmashauri zetu. Wao ndiyo wanasimamia miradi yote, wao ndiyo wanasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini kwa mshangao mkubwa tunasema tunawapa posho. Ifike mahali sasa Madiwani hawa wapewe mshahara kama watu wengine, wanafanya kazi kubwa. Kuna zile shilingi 350,000 ambazo wamesema wametoa shilingi 100,000 kwa ajili ya kuwapa watendaji, hizi fedha nazo waziweke kwa ajili ya Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji waweze kupata posho. Serikali sasa iangalie Madiwani kwa sababu wanateseka, hawana uwezo wa kuwasimamia watu wanaolipwa shilingi 700,000 au shilingi 800,000 na wao wanapata mshahara lakini wao wanafanya kazi kama wanafanya bure, halafu tunawatumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda kuingia kwenye eneo la chakula mashuleni. Tunasema watoto wafaulu, ni mtoto yupi anaweza kukaa kuanzia asubuhi hajala chochote lakini unategemea afanye vizuri au amsikilize Mwalimu? Naomba eneo hili TAMISEMI waliangalie na watoe waraka maalum na unaoelekeza namna ya watoto kupata chakula shuleni kwa lazima, kwa sababu ndiyo tunatengeneza Taifa la watoto ambao wanakuwa na kwashiorkor, kwa sababu haiwezekani mtoto kukaa kuanzia asubuhi bila kula chakula alafu tunaona ni jambo la kawaida.

Mheshimiwa Spika, suala la mfumuko wa bei. Kule vijijini kwa sasa hizi hali ya vyakula, vitunguu, nyanya, chumvi, mafuta ya kula, hali ni tete. Kwa hiyo naomba waende waangalie Serikali watoe namna kwamba kuna wafanyabiashara baadhi ambao wanapandisha bei eti tu kwa sababu wamesikia mafuta yamepanda. Naomba Serikali ifanye uchunguzi ili iwape wananchi maelezo na matumaini ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, suala la bajeti hii kutekelezwa. Lazima bajeti hii itekelezwe bila kuwepo na wizi, rushwa, ufisadi na ujanja ujanja. Bajeti ikitekelezwa bila rushwa tutatekeleza vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kila mmoja achukie rushwa, wizi na ufisadi ili mwisho wa siku Taifa hili lipone. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. NOAH L. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Taarifa ya Kamati zote mbili ya Katiba na Sheria na Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kama tujuavyo Bunge lako limepewa mamlaka chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 64 na Ibara ya 97 yenyewe ndiyo imepewa mamlaka katika kuhakiisha kwamba sheria inatungwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba hakuna chombo kingine chochote chenye mamlaka labda Bunge ikasimu madaraka haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo imekuwa ikifanyika vyema na Bunge lako na Kamati pia tumeendelea kufanya kazi nzuri ya kuchambua miswada mbalimbali ambayo imekuwa ikiletwa na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kupata sheria nzuri, Sheria ambayo inakuwa ni ya matumaini, sheria ambayo inaweza kujenga uchumi na mambo ambayo yanaleta matumaini kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia katika jambo lolote tulipokuwa kwenye mjadala mbalimbali kuna sheria ambazo zimepitwa na wakati, ambayo sasa kama tunataka kujenga uchumi lazima tutizame sheria zetu, kama tunataka kuhakikisha wananchi wetu wanapata nafuu ya maisha kwa maeneo mbalimbali lazima tuangalie sheria zetu, kwa mfano kama tunataka kuhakikisha kwamba mali za Serikali zipo salama lazima tuendelee tena kuangalia sheria hii ya manunuzi (Public Procurement Act) sasa inatakiwa irekebishwe kwa sababu imekuwa kama ndiyo yenye kutoa mwanya wa wale wahalifu wa wizi na masuala ambayo hayafai katika ubadhirifu wa mali za umma. Sheria hii inatoa mwanya mkubwa sana, lakini sheria hii imeendelea kuchelewesha miradi mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ni kwa nini hatutaki kuirekebisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kutokutaka kurekebisha simaanishi kwamba katika utaratibu wa kutunga sheria tunajua kwamba lazima Serikali ilete muswada kwenye Kamati na baadae tuje kwenye Bunge, sasa hii ni changamoto kubwa kwa sababu Serikali lazima ione kwamba hiyo sheria imekuwa na mapungufu makubwa; kwa nini hatutaki kurekebisha au tunataka kuendelea kuwalea hawa wezi, hawa wanaoweka mwanya wa ujambazi, hawa ambao wanataka kutafuna fedha ambazo zinatafutwa na Mheshimiwa Rais usiku na mchana? Hii siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sheria hizo zinatakiwa zirekebishwe, lakini pia hata Sheria ya TAKUKURU bado na yenyewe ina madhaifu makubwa, watu wenye kesi za kuku sijui na kesi ndogo ndogo za kupigana ndiyo wanaoshughulikiwa zaidi kuliko wale ma-giants wanaofanya ufisadi. (Makofi)

Kwa hiyo, lazima sheria hizi ziangaliwe kama kweli tuko seriously katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inataka kusonga mbele kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mheshimiwa Rais, amekuwa akijitahidi sana ku-harmonize mambo mengi sasa na sisi wasaidizi wake tujitahidi kuhakikisha kwamba tunakwenda kwa spirit hiyo hiyo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria pia ambayo inatakiwa irekebishwe sheria iliyoanzisha TEMESA. Hii nayo ni kidonda ndugu kwenye halmashauri zetu, sheria ile inasema gari ikatengenezwe TEMESA, lakini halmashauri inalazimishwa wakishapeleka gari pale wao TEMESA wanapeleka kwenye garage za uchochoroni. Sasa gharama inakuwa kubwa kuliko hata halmashauri ingetengeneza, hii nayo ni changamoto kubwa ambayo lazima Serikali ifike mahali iweze kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la utunzi wa sheria kwa lugha ya Kiswahili. Tumepitisha sheria hapa tukasema ile sheria imeeleza bayana kwamba katika mjadala lazima katika maamuzi yetu au utungaji wa sheria lazima sheria iwe kuna Kiswahili na Kiingereza ili iweze kusaidia wananchi wetu waweze kupata haki zao na waweze kuelewa hasa tukizingatia kwamba Tanzania sisi siyo kisiwa, sisi ni miongoni mwa nchi za Commonwealth ambayo tunatumia precedent za Jumuiya ya Madola na kama unavyojua kuna maneno mengine kwenye sheria ambayo hata Kiingereza haina, maneno kama mandamus, certiorari, obiter dictum na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ngumu sana kwa hiyo tunataka tuombe Serikali ifike mahali ituletee na tumeshauri kama Kamati, tunapoletewa miswada uje muswada wa Kiingereza na Kiswahili kwa sababu kama jinsi ambavyo ilikuwa intention ya Bunge wakati wa kutunga ile sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona nisiache suala la Marekebisho ya Sheria ya Ndoa, nataka niiulize Serikali; nini chanzo cha kurekebisha sheria hiyo? Kwa nini tunataka kwenda kuangalia sheria nzima ya ndoa kama ndiyo ni mbaya zaidi? Mahakama imetoa hukumu mwaka 2016 kwamba vifungu namba 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa inakiuka Katiba, sasa kama Mahakama imetoa Serikali ikakata rufaa mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa Tanzania ikakataa; sasa Serikali imeenda tena zaidi inataka tena kuchukua maoni kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wadau wamefungua kesi ya kutokukubali maoni hayo yachukuliwe; sasa je, Serikali haioni katika kukataa kutekeleza uamuzi wa Mahakama yenyewe inakosa uhalali wa kuweza kuendelea kusimamia sheria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali inataka kuangalia sheria nzima ya ndoa kama ni mbaya badala ya kuangalia vifungu viwili ambayo Mahakama imesema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kusababisha mgogoro pasipo na sababu, hii siyo sawa, lazima muangalie vifungu viwili tu ambayo Mahakama ndiyo imesema. (MakofI)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu wa bajeti ya TAMISEMI. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikushukuru wewe kwa jinsi unavyoongoza Bunge letu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anapambana katika kuhakikisha kwamba, Taifa letu linasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, nisiache kumshukuru Mkuu wangu wa Mkoa, Ndugu yetu Mongela, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwa uaminifu na uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe niseme mambo yafuatayo ambayo kwa kweli, bajeti hii ni bajeti nzuri ambayo tumewasilishiwa na Waziri wetu Mheshimiwa Kairuki. Lakini nisiache kusema kwamba, miundombinu ya Jimbo la Arumeru Magharibi hali sio nzuri kwa sababu mafuriko yamelikumba jimbo hilo na wananchi wanateseka sana sasa kwa kukosa barabara ya kupitia.

Mheshimiwa Spika, TARURA inafanya kazi nzuri ambayo hakuna mtu anayepinga na Bunge hili linaendelea kuipongeza TARURA, lakini barabara yangu katika Jimbo la Arumeru Magharibi kuna barabara ya Hospitali ya Oturmeti na yenyewe haipitiki. Barabara ya Loning’o kwenda Mringa imekatika daraja. Barabara kutoka Mnadani kwenda Hospitali ya Oturmeti imekatika, hivyo naiomba sana Wizara kupitia Waziri wetu aone namna gani tunapata fedha za dharura kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, maeneo haya yaliyokatika yanaweza kutengenezwa mara moja kwa sababu, wananchi wanateseka.

Mheshimiwa Spika, lakini ningeomba TARURA iongezewe fedha kwa sababu, katika Jimbo la Arumeru Magharibi tuna barabara nyingi ambazo sasa hazipitiki kutokana na mvua hizi. Barabara ya Sanawari – Oldonyosambu hali ni mbaya, Barabara ya Malalua – Nduruma – Bwawani hali sio nzuri, Silent Inn – Freedom sio nzuri, Barabara ya Kisongo – Musa sio nzuri, madaraja yanakatika. Barabara ya Kigarai – Likamba hali sio nzuri, Barabara ya Lemanyata – Orkokola Kituo cha Afya sio nzuri, Barabara ya Kilima Moto – Mwande – Kingalaoni sio nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri, ujue Jimbo la Arumeru Magharibi lina kata 27, vijiji 86, vitongoji 268. Tuangalie kwa jicho la huruma Jimbo la Arumeru Magharibi kwa sababu wananchi wanateseka kutokana na maeneo ya maporomoko ya maji na barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mgawo wa fedha tuione Arumeru kama ni sehemu na yenyewe ya kupata fedha za kutosha. Na niombe TARURA iongezewe pesa kwa sababu, pamoja na kufanya kazi nzuri TARURA isipoongezewa fedha haya yote tunayoyasema hayawezi kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la ajira, sisi Wabunge hapa tulipo na hapa nilipo nina message zaidi ya mia mbili, mia tatu, vijana wanasema tutafutieni ajira kwa sababu, bila connection, kama hakuna connection ina maana hatupati ajira. Jambo ambalo sio sawa kwa sababu, Serikali haitoi ajira kwa connection, Serikali inatoa ajira kwa usawa kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kusema basi, ajira hizi zigawanywe kwa mikoa na badae hata kwenye mikoa zigawanywe kwenye Wilaya, ili tuweze kupata usawa katika kugawa ajira hizi, ili kuondoa hii sintofahamu ya vijana wetu ambao kwa kweli, wanaendelea kuzungumzia kuhusu suala la connection, jambo ambalo halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la posho ya Madiwani na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji. Kama Serikali imeweza kuchukua suala la Madiwani ikalipa hiyo posho ya mwezi, zile fedha ambazo zilikuwa zinalipwa na halmashauri kwa nini isiunganishwe hapo ikawasaidia Madiwani, ikajumlishwa ikawasaidia hawa Madiwani? Ikawa ni sehemu kabisa ya kuhakikisha kwamba, wanapata mshahara? Kwa sababu, kama tunavyopeleka billions of money kwenye Halmashauri kwenda kumsimamia mkurugenzi anayelipwa labda milioni nne au milioni kadhaa, yeye analipwa posho, hatuoni kwamba, tunapoteza fedha nyingi kwa sababu ya usimamizi mbovu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana hili suala la sehemu ya Madiwani iangaliwe, lakini pia Wenyeviti angalau na wao waangaliwe. Wenyeviti wa vitongoji na vijiji waangaliwe kwa sababu, wanafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la umaliziaji wa maboma. Wananchi wamejenga maboma mengi ya zahanati na vituo vya afya na hata madarasa. Ningeomba sana hili eneo liangaliwe kwa sababu, ni eneo muhimu kwamba, tukiwavunja wananchi nguvu kwa sababu, wanachangia na hatimaye wasione nguvu ya Serikali ikimalizia hizo zahanati za kutoa huduma kwa kweli, itakuwa ni kuwavunja moyo na kazi hiyo haitakuwa imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na umaliziaji wa maboma kumekuwepo na shida kubwa sana katika suala la vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya n ahata hospitali ya Wilaya. Hospitali ya Wilaya ya Oturmet tangu Serikali imeanza kugawa migao ya fedha kwa ajili ya Hospitali za Wilaya hospitali hiyo haijawahi kupata hata shilingi kumi ya mgawo wa Serikali kwa ajili ya kupanua hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hospitali hiyo imepandishwa hadhi na Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Kikwete mwaka 2012, lakini haijawahi kupata hata senti. Nimekuwa nikiimba kwenye Bunge hili, labda sasa nifike mahali na mimi niimbe kimasai, labda nikiimba kimasai “laleiyo” ndio mtajua kwamba, hospitali hiyo inahitaji msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii sio nzuri kwa sababu, tunapoona maeneo mengine yanapata fedha zaidi ya bilioni tatu, bilioni nne, lakini hata shilingi milioni 500 hospitali ya Wilaya haijapata, si sawa. Naweza kufika mahali nikasema siwezi kusema ni ubaguzi, lakini naweza kusema Serikali imesahau hospitali hiyo, ni kwa nini? Mheshimiwa Waziri naomba sana hospitali hiyo, ukifika pale huwezi kusema ni hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimeona umewasha kipaza sauti. Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya lakini nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa uzima kuwepo katika Bunge hili.

Nikushukuru na wewe kwa jinsi ambavyo unaendelea kuendesha Bunge lako kwa umakini na umahiri mkubwa sana. Niendelee kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaongoza Taifa letu, lakini kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaendelea kupata afya njema kwa kutoa vifaa tiba, kujenga majengo, zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na hata za mikoa na kuleta vifaa tiba mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki ametuheshimisha sana sisi Wabunge, kwa sababu ametuletea miradi mikubwa mpaka ukiwa jimboni unakosa uelekee upande upi katika kukagua miradi. Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Pamoja na pongezi zote nilizozitoa kwa Wizara ya Afya kwa maana ya Waziri wetu Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri wake pamoja, Katibu MKuu na Naibu Makatibu Wakuu na Wizara nzima kwa ujumla na Madaktari wote hapa nchini lakini bado tunasema barabara ndefu haikosi kona. Kwa hiyo, katika yale ambayo tunayo kama Wabunge na hasa mimi kama Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kuna mambo ambayo pia napenda tujaribu kushauri ili basi mwisho wa siku hili gurudumu liweze kusonga mbele sisi kwa pamoja kwa maana ya kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Serikali katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi tumejengewa vituo vya afya karibu vitatu. Tumejengewa zahanati nyingi kumalizia nguvu za wananchi, bado zingine hazijaisha, lakini kwa kweli hizo ni shukrani ambazo naweza kusimama katika Bunge hili na kujivunia kwamba natoa shukurani nyingi sana sana kwa Serikali yetu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema barabara ndefu haikosi kona. Kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi kulikuwa na hospitali ambayo naiongelea kila siku katika Bunge hili ya wilaya. Imepandishwa hadhi toka 2012 na Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Hospitali hii ilipandishwa hadhi, Rais aliahidi pia kwamba lami kilometa 2.8 iwekwe lakini pia majengo yaongezwe, hospitali hiyo haina jengo la wagonjwa wa nje kwa maana ya OPD, hospitali hiyo haina X- Ray, hospitali hiyo haina jengo la mochwari. Hospitali hiyo haina chochote na tangu Serikali ianze kuboresha hospitali za wilaya, kwa kweli sisi hasa katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi hatukuweza kubahatika kupata hizo fedha za kwa ajili ya kuhakikisha hospitali hiyo inakaa katika mkao sasa wa kuitwa hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liko katika Wizara mbili kwa maana ya TAMISEMI na vile vile katika Wizara ya Afya kwa maana ya upande wa vifaa tiba. Nalizungumzia kwa ujumla wake ili Mheshimiwa Waziri wetu wa Afya aweze kuona namna gani atahakikisha tunapata x-ray, lakini pia tunapata na vifaa tiba vingine vyote ambavyo vinatakiwa katika hospitali hiyo. Upande wa majengo, TAMISEMI nao wataona jinsi ambavyo wataboresha hospitali ile kwa sababu sasa umefika wakati muafaka hata katika bajeti nimeona wameiangalia hospitali hiyo na nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kutoa huduma kwa wazee na watoto; suala hili la kuhudumia wazee wetu halijakaa vizuri kabisa. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Ummy na Dkt. Mollel, ni Wabunge wenzetu, hiki kilio nadhani na wao wanakipata mara kwa mara. Wazee wetu wanakwenda pale hospitalini, wanaandikiwa barua wanakuwa labda na hiyo sijui ndio vitambulisho wanapewa halmashauri, lakini wanapoenda pale wanaambiwa dawa zenu hazipo.

Mheshimiwa Spika, wale wazee wanateseka, kwa kweli wazee wetu wanateseka. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali kama itawezekana na naomba iwezekane kwa sababu wale wazee wametumika Taifa hili kwa umri wao wote huo ambao mmeuona na sisi sote siku moja tutakuwa wazee na hapa tunaelekea kuwa wazee sasa. Kwa hiyo tunahitajika kuhakikisha kwamba tunaanzisha msingi wa kuendelea kuwatunza wazee wetu.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara iangalie namna ya kuwasaidia wazee. Aidha, wawape kabisa CHF moja kwa moja ili ijulikane kwamba wakienda pale, basi Serikali ndio inatoa hiyo ruzuku kwa wazee. Hebu tulione hili kwa kweli kwa sababu linaumiza na linatesa sana wazee wetu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la upungufu wa watumishi. Kuna upungufu wa watumishi katika zahanati zetu, hospitali zetu za wilaya na na kadhalika. Kwa hiyo, naomba waliendelee kuliangalia suala hili pamoja na kuishukuru Serikali kwamba imetangaza ajira hizi za juzi, lakini bado upungufu ni mkubwa sana katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la ununuzi wa madawa na vifaa tiba. Katika sehemu hii inatakiwa sana Mheshimiwa Waziri wakae waangalie namna ya kuhakikisha kwamba watakuja na strategy mpya kwa sababu, kwa mfano, juzi katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi, Halmashauri ya Arusha DC, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba tangu Mwezi wa Tisa mwaka jana. Mshitiri anasema kila siku hakuna vifaa, hakuna vifaa mpaka juzi mwezi Machi ndio vifaa vimekuja kupatikana, can you imagine? Ina maana hiyo variation lazima bei zinapanda, kuna vitu ambavyo vitakuwa havijanunuliwa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili eneo la Mshitiri na kuimarisha MSD, hebu wakae vizuri waangalie kwa umakini na umahiri zaidi, kwa sababu kwa kweli tutatesa wananchi wetu na hata ukizingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika ukurasa wa 138 imeeleza kinaga ubaga na dhahiri shahiri kwamba, naomba kunukuu; “Kuimarisha Mfumo wa Mshitiri ili kuhakikisha kuwa bidhaa za afya zinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu katika ngazi zote za huduma”. Hiyo ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika suala la upungufu wa magari katika Halmashauri yetu ya Arusha DC, Jimbo la Arumeru Magharibi. Tunaomba Serikali itakapokuwa imekamilisha ugawaji wa ambulance, Jimbo la Arumeru Magharibi tuna zahanati nyingi, tuna vituo vya afya vingi, jiografia yake imekaa katika mazingira ambayo kwa kweli ni changamoto sana. Kwa hiyo naomba sana watukumbuke katika kupata gari la wagonjwa. Hasa gari mbili tukipata angalau itakuwa imetusaidia sana na imetufaa sana kuwaokoa wale wananchi katika kuhakikisha wanapata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; suala la maadili kwa Madaktari wetu, lakini kabla sijasema maadili, niombe Wizara pia muangalie namna ya kuwawezesha Madaktari na Wauguzi katika mishahara yao, posho zao na mambo yote yanayowahusu. Naomba sana waangalie hili kwa sababu yawezekana pia katika changamoto tunazozisema inawezekana na yenyewe ikawa ni changamoto kubwa. Kwa sababu mtu anapochoka hata hapati overtime, hapati chochote anajitoa, ana-toil lakini mwisho wa siku hapati stahiki yake ambayo anastahili. Kwa hiyo naomba sana tuangalie Madaktari wetu, wanaoshika roho zetu, wanaoshika afya ya Taifa hili, ili waweze kupata stahiki zao kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa muda naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo ndiyo inafanya Taifa letu liwe na mwanga kila saa.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa jinsi ambavyo unaongoza Bunge letu na niseme tu kwa moyo wa dhati kwamba wewe ni Spika ambaye nimeona na nadhani kwa sababu ya taaluma yako ya sheria ndio maana unatuongoza vizuri katika Bunge hili. Kwa kweli Mungu akubariki sana. Lakini nikutakie kila la kheri katika safari yako ya shughuli iliyoko mbele yako. Mungu akutangulie na naamini utashinda kwa sababu una uwezo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme pia nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaongoza Taifa letu na kusimamia kila Nyanja ya Taifa letu kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, lakini nitakuwa mwizi wa fadhila nisipompongeza pia Mheshimiwa Waziri, Ndugu yangu Makamba pamoja na wasaidizi wake Naibu Waziri pamoja na Wizara nzima kwa ujumla wataalamu ambao wanamsaidia. Kwa kweli mnachapa kazi na mnajitahidi pamoja na changamoto nyingi ambazo mnakabiliana nazo. Mwenyezi Mungu aendelee kuwatia nguvu ili muendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais akatekeleze majukumu haya na wananchi waendelee kumwamini, na In Shaa Allah Mungu akijalia aendelee kuongoza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza mimi niseme tu kwamba bajeti hii nimefarijika na ninaipongeza kwa sababu moja tu; nikiangalia jinsi ambavyo bajeti hii ni ya shilingi trilioni tatu na bilioni karibu 48 na point juu; lakini ukiangalia Wizara imekuja na kwamba ujenzi wa miundombinu ni asilimia 97.1. Hiyo tu peke yake mimi ilinifanya nione kwamba hawa watu wako committed, kwamba kweli wanataka kupunguza changamoto za wananchi. Matumizi ya kawaida ni asilimia 2.9 tu. Hapo peke yake imenionesha kwamba kwa kweli Wizara hii iko kwenye mazingira ambayo ya kujisikia kwamba ingetaka kuondoa matatizo yote ya umeme katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tujuavyo, changamoto zinakuwepo tu kwa sababu ya resources tulizonazo, kwamba hazitoshi. Na kwa sababu hazitoshi ndiyo maana sasa unaona tunaendelea kuzungumza katika Bunge hili kuiomba Serikali sasa ione ni jinsi gani inaweza kuhakikisha kwamba changamoto zilizopo za upatikanaji wa umeme katika maeneo yetu, katika vijiji, kata na vitongoji viweze kuwepo umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi; mimi nina kata 27, vijiji 86, vitongoji 268. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kusema kwamba atatupatia vitongoji 15 kwa kila Jimbo; lakini katika vitongoji mia mbili karibu 68 ukitoa vitongoji, 15 hebu fikiri kwamba hali itakuwaje huko kwenye jimbo? Kwa hiyo bado tunaiomba Serikali ione ni jinsi gani itahakikisha kwamba inatupunguzia adha hii sisi Wabunge kwa sababu tunapokuwa majimboni, tunapokuwa kwenye ziara mbalimbali changamoto kubwa wananchi wanatudai umeme na wanasema mbona umeme hakuna? Tunajaribu kwaambia Serikali imeanza mchakato wa kuhakikisha kwamba kila kijiji inapata umeme halafu tutakuja kwenye kitongoji. Sasa katika bajeti hii vitongoji 15 bado tunaona kidogo Serikali ingeangalia, na hasa Wizara ingeangalia namna ambayo itatufikisha.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi katika vitongoji vingi, ambavyo siwezi kuvitaja, lakini kata ambazo mpaka sasa vitongoji vyake havina umeme ni vya Bwawani, Oljoro, Nduruma, Musa, Mwandeti, Oldonyo Sambu kwa maana ya Kata ya Otoroto, Mlangarini, Sambasha, Oldonyo Sambu, Oldonyouwas, Lengijabe, Lemanyaka, Kimnyak. Vitongoji vya hiyo kata hizi zote ambazo nimezitaja bado havina umeme; na wananchi wetu katika kata hizo nilizozitaja hawako mbalimbali, kwa maana hawako scattered, wako karibu karibu kabisa; kwa hiyo wanahitaji umeme kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na unajua umeme ni sehemu kubwa sana ya maendeleo. Kama ni kuchaji simu, uchomeleaji, kusaga mahindi, na kufanya mambo mengi basi wananchi wanategemea kupata huduma ya umeme ili mwisho wa siku basi waendelee kufurahia huduma kutoka kwenye Serikali yao. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo moja gumu mno, na ugumu wake miundombinu yake jinsi ilivyokaa ramani yake imekaa vibaya, na hivyo niombe sana kwa kweli ujaribu kutusaidia kwa sababu wananchi wanahitaji umeme.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna suala la uimarishaji wa TANESCO. TANESCO inahitaji kuimarishwa. Niwapongeze Wizara kwa sababu mmefanya mabadiliko makubwa hivi karibuni katika hiki kipindi cha mwaka mmoja, naona kama kuna mabadiliko makubwa ndani ya TANESCO kiasi fulani lakini bado mnahitaji kufanya kazi kubwa kurekebisha TANESCO; lakini pia TANESCO isaidiwe kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ukiachilia madai makubwa, yale ambayo yametajwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nikiangalia mfano taasisi za Serikali. Taasisi za Serikali hazilipi bili za umeme, ni kwa nini? Ukisoma ripoti ya Kamati, taasisi za Serikali tu peke yake inadaiwa zaidi ya bilioni 334, hazilipi. Naomba hili nalo liangaliwe, TANESCO ipewe nguvu. TANESCO bado haina nguvu kwa upande wa madeni makubwa, lakini pia Serikali na taasisi za Serikali zinavyotumia umeme hailipi ina maana gani? Kwa hiyo naomba kama taasisi hizi kwenye bajeti zao zimeweka ulipaji wa bili ya umeme kwa nini wasilipe? Mheshimiwa Waziri TANESCO wasaidiwe wawakatie umeme. Wakiwakatia nafikiri watashtuka na watalipa bili. Hii siyo sawa, tutakuwa tunawaonea TANESCO lakini hatuwasaidii.

Mheshimiwa Spika, Namshukuru sana Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Arusha kwa sababu anajitahidi sana. Ukimpigia simu saa yoyote maskini ya Mungu anapokea, ana-deal na mambo makubwa makubwa magumu. Kwa kweli nampongeza sana na ninashukuru sana kwa sababu ni mtu msikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la uunganishaji wa umeme. Uunganishaji wa umeme bado hatuelewi vizuri kama Wabunge na hata Watanzania hawaelewi; kwamba, ni wapi ambapo ni shilingi 27,000, ni wapi ambapo labda inatozwa nguzo moja shilingi laki tatu karibu na 60, ni wapi inakuwa sijui ngapi? Hili nalo Mheshimiwa Waziri inabidi Wizara iliangalie sana na itoe kabisa schedule ambayo nchi nzima itajulikana. Kama maeneo yametofautiana basi iwekwe vizuri. Kuna wananchi unakuta nguzo imefika mpaka kwake, Serikali imefikisha nguzo pale lakini insahindwa kuvuta umeme kwa sababu ya gharama kubwa. Kwa hiyo hebu tuangalie ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu hawa waweze kuendelea kufurahia matunda ya nchi yao na hasa kuhakikisha kwamba siku zijazo Chama cha Mapinduzi kinaendelea kung’ara ndani ya nchi yetu na kuendelea kutawala vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu ya mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametupa uzima kuwepo katika ukumbi huu siku ya leo, kuendelea kujadili bajeti ya Taifa letu kwa maana ya hatma ya wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akijishughulisha kwa hali na mali kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma mbalimbali katika afya, elimu, barabara, maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiache kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa kazi nzuri na njema ambayo ameendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais, Naibu wake pamoja na Wizara nzima Watumishi wa Wizara ya Fedha ambao wanahakikisha kwamba anafanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba huduma inapatikana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kumpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo kwenye bajeti hii amehakikisha kwanza watoto wanaokwenda katika vyuo vya kati sasa wanakwenda kusoma kwa kupata mikopo. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwetu Wabunge kwa sababu kila mtoto analia kwamba tunaomba ada. Mheshimiwa Mbunge naomba ada, kwa hiyo hii kwa kweli tunampongeza Mheshimiwa Rais, tunakupongeza na Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu mmefikiria jambo la msingi sana kwa Watanzania ambao wana familia maskini. Pia mmeenda kuondoa ada kabisa kwenye vyuo vingine hivi vya technical, kwa kweli mmefanya jambo la maana na jambo la muhimu kwa Watanzania na mnapaswa kushukuriwa, Mheshimiwa Rais anapaswa kushukuriwa na Mheshimiwa Mwigulu na timu yako nzima mnapaswa kushukuriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msamaha huu utaenda kuondoa vilio vya Watanzania walio wengi ambao hawakuwa na uwezo kwa ajili ya kupata elimu ya vyuo vikuu hasa vyuo vya kati na itaenda sasa kuleta faraja katika familia ambazo walikuwa wanafikiri kusoma haiwezekani, leo watakwenda kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu Mheshimiwa Waziri kwamba basi bajeti hii itakapoanza kutekelezwa katika kipengele hiki cha kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi hawa, tuweke utaratibu ambao hatutasikia tena kwamba huyu kapata, huyu kakosa maadam tu ana vigezo na amekidhi vigezo vyote na amechaguliwa kwenda kwenye chuo husika. Basi ile azma ya Rais wetu na Serikali yetu chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ikaendelee kutimia na wananchi waendelee kufurahia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niingie kwenye suala la miundombinu. Kama tunavyojua TARURA tumeiongezea fedha. Mimi kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi hivi karibuni kama alivyoeleza huko awali, nimekubwa na mafuriko makubwa sana ambayo yameharibu miundombinu ya barabara, imeharibu madaraja na hata kupelekea kabisa wananchi hawawezi kwenda hospitalini hawawezi kupata huduma za jamii, kwa sababu hali siyo nzuri kwa miundombinu kuharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumeomba fedha za dharura kwa madaraja kama manne. Daraja la Sekei kwa maana ya Kiutu - Naurei, daraja ambalo tumepata zaidi ya milioni 400 kwa fedha za dharura, daraja la Loning’o - Ilboru kwenda Kiranyi tumepata milioni 200 karibu na 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kuna madaraja matatu sasa ambayo wananchi hawapiti kabisa. Daraja la TPRI - Likamba kwenda Musa kwenda kutokea Jeshini Monduli. Kwa kweli hali siyo nzuri, hilo daraja halipitiki tena, hali ni mbaya. Vile vile daraja la kwenda Hospitali ya Oturmeti, maeneo yameharibika sana kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile barabara ya Mnadani – Mwandeti, Mnadani – Mindo kwenda Hospitali hali ni mbaya. Naomba sana Mheshimiwa Mwigulu kwa kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alishaongea na wewe, utusaidie hizo fedha za dharura kwa sababu, kwa kweli hali kule ni mbaya. Nami kurudi jimboni bila kunisaidia hilo, utakuwa umeniumiza, umewaumiza wale wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi hasa kwa upande wa huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mifumo. Katika Halmashauri zetu Tanzania kumekuwa na changamoto kubwa sana inapofika mwezi wa sita, mifumo yote inafungwa. Mifumo mwezi wa Sita haifanyi kazi, mwezi wa Saba haifanyi kazi, mpaka mwezi wa Nane. Hii nayo ni changamoto kubwa. Kwa sababu, inakwamisha utoaji wa huduma kwenye Halmashauri, inakwamisha utekelezaji wa shughuli za miradi mbalimbali, inakwama kwa sababu mifumo imefungwa. Zaidi ya hapo, mifumo hii ingesaidia wananchi kuendelea kulipa kodi ndani ya Halmashauri na pia kulipa kodi kwenye Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo Wizara ya Fedha iliangalie kwa makini na mapana namna ambavyo litaweza kupunguza kadhia hii ya wananchi kulipa kodi kwa sababu, bila kulipa kodi ina maana uchumi utakuwa umedorora kwa wananchi na Taifa. Kwa hiyo, naomba sana hili nalo liangaliwe kwa makini ili basi wananchi wasione kero katika kulipa kodi na utoaji wa huduma mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupitisha bajeti hii, bajeti hii ikipitishwa tunategemea Serikali na yenyewe inahakikisha inasimamia mapato hayo, ukusanyaji na matumizi. Kila mwaka kumekuwa kukitokea taarifa ambazo CAG anakuja hapa anatuambia umefanyika ubadhirifu hapa, umefanyika ubadhirifu kwenye taasisi fulani, umefanyika ubadhirifu kwenye Wizara fulani, hii haipendezi. Ni kwa nini sasa Serikali isiweke mkakati? Pamoja na kwamba, kuna mechanism kwa maana ya vyombo mbalimbali vinavyozuia suala hili la watu kujiunga na kufanya mbinu ya kujipatia fedha zisizo halali katika miradi mbalimbali na kuanzisha masuala ya rushwa, wizi, ufisadi na mambo mengine kama hayo, kwa nini Serikali isione haja ya kuondoa jambo hili kabisa la CAG kuja kila mwaka na maajabu na maajabu na masikitiko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitisha bajeti hii, lakini Serikali ina mzigo mkubwa. Mheshimiwa mwigulu ana mzigo mkubwa wa kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba masuala haya ya rushwa na ufisadi katika miradi mbalimbali inatoweka kabisa. Tufurahie taarifa ya CAG inapotolewa, basi tuone CAG anasema mambo madogo madogo ambayo hayaleti karaha na hayawezi kumuudhi Rais, hayawezi kumuudhi mtu yeyote na Watanzania wanafurahia Serikali yao kwa sababu, inasimamia mapato ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu hatua kuchukuliwa kwa wale ambao wanahusika. Kama kweli mtu kabainika kwa mujibu wa sheria na taratibu, basi wahusika wachukuliwe hatua. Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wachukue hatua, sio mpaka wasubiri labda Mheshimiwa Waziri au Mheshimiwa Rais ndio aongee, labda ndiyo ionekane, hapana. Kuna watu wanaomsaidia Mheshimiwa Rais, kuna watu ambao wanamsaidia Waziri, kwa nini wasichukue hatua? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya. Pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa suala la mbolea. Mbolea ya Tanzania imekuwa ni changamoto sana kwa wakulima wetu kwa sababu imekwenda juu sana. Jinsi ambavyo mbolea imepanda ukiangalia mwaka jana, mfano kwenye Mkoa wa Arusha, 2021 Sulphate Amonia ilikuwa ni Sh.45,000 kwa mfuko wenye kilo 50, lakini mwaka huu ni laki Sh.145,000. Hili ni ongezeko kubwa sana. Ukiangalia 2021 Urea ilikuwa Sh.65,000, mwaka huu 2022 ni laki Sh.150,000. Ukiangalia mbolea ya kupandia DAP ni Sh.75,000 mwaka jana, lakini mwaka huu ni laki Sh.165,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni janga kwa wakulima wa Tanzania kwa sababu hawana uwezo wa kufikia kiwango hicho cha mbolea kupanda. Ukiangalia wale wananchi wangu wa Kata za Ikiding’a ambao wanatumia mbolea Sambasha, Olomontoni, Soko Ntu, Nimnyaki na Oldonyosambu hawana uwezo ya kununua mbolea kwa gharama kubwa hivyo. Tunaishauri Serikali kwamba lazima ifike mahali iweke ruzuku ya kutosha kwenye mbolea ili wakulima wale wadogowadogo na hata wale wa kati waweze kumudu mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mbegu, nalo ni changamoto. Kumekuwepo na mbegu feki zinazoingizwa nchini na Mawakala, mbegu ambazo hazina tija, imekuwa kama ni kilio wale wakulima wanaponunua mbegu, wakidhani wananunua mbegu bora, wanaona ni bora wangerudi kwenye zile mbegu zao za zamani, kwa sababu umekuwa ni utapeli, watu wanachukuwa rangi, wanaweka kwenye mahindi, hivyo wakulima wanaona kama ni mbegu bora lakini kumbe ni mbegu feki. Hili nalo tunaishauri Wizara iangalie suala la mbegu hasa kwa kuwaangalia watu wanaouza mbegu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la madawa ya kunyunyuzia mimea, kwa maana ya mazao, nalo hili ni janga kwa sababu wakati mwingine madawa yananunuliwa, lakini hayana uwezo wa kuuuwa wadudu katika mazao. Kwa hiyo hili nalo naomba Wizara iliangalie na Mheshimiwa Bashe sina wasiwasi naye na Naibu wake kwamba kazi hii wanaiweza na wanaiweza kwa dhamira ya dhati, niwaombe sana kwamba kazi hii kubwa waliyekabidhiwa na Mheshimiwa Rais waweze kuifanya kwa uaminifu na uadilifu ili mwisho wa siku wapate karama yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba mwaka huu katika maeneo mengi hasa ukanda wa Kaskazini kuna upungufu wa chakula kwa sababu mvua ni kidogo. Kwa hiyo, naomba pia Wizara ilione hili na kulichukua kuwe na tahadhiri ya kwamba kutakuwepo na suala la upungufu wa chakula katika Ukanda wa Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila jambo wakati ule wa Serikali zingine zilizopita za kwetu kulikuwa na slogan mbalimbali, Siasa ni Kilimo, Kilimo ni Uti wa Mgongo. Haya yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunahamasisha jamii na Serikali kwa ujumla kujihusisha na kilimo ili kuleta tija ndani ya Taifa letu. ninaomba Serikali yetu kama mnavyojua sehemu kubwa ya Watanzania wanapata ajira kupitia kilimo, kama tunasema tunaongeza ajira Mheshimiwa Bashe na Naibu wako mnayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata ajira kwenye kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukitumia mashamba makubwa ya kilimo na mkayafuatilia kwa makini mashamba yote yanayojihusisha na kilimo na masuala ya umwagiliaji tutaongeza suala la ajira kwa vijana wetu na wengine wote kwa ajili ya kuinua uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mpaka shamba liwe pori ndiyo muweze kufuatilia, fuatilieni mashamba ya kilimo hata kabla hayajawa mapori, mwisho wa siku wale wanatelekeza mashamba na wamekopa kwenye benki mbalimbali, wakishakopa wakidhani wanaendeleza hayo mashamba lakini mwisho wa siku wanatelekeza yanakuwa ni mapori, ndiyo Serikali tunakuja kushtuka sasa tunasema uzalishaji wa maeneo hayo umekufa. Kwa hiyo, nayasema haya nikiamini kwamba Waziri na Serikali kwa ujumla itaona kwamba inafuatilia mashamba yote ya kilimo ili kuleta tija kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti Kuu hii ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu moja kwa moja kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake nzima kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo ni bajeti ya Watanzania wote itakayowasaidia katika sekta mbalimbali katika maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa sababu ya kuondoa ada kwa kidato cha tano na kidato cha sita tunaomba tena Serikali iangalie tena mbele zaidi kusaidia katika Vyuo vya Kati kwa sababu kuna watoto ambao bado wakienda katika vyuo hivyo hawana uwezo wa kulipa ada katika Vyuo vya Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita katika masuala makuu mawili, jambo la kwanza ni suala la makusanyo ya Serikali na rushwa, jambo la pili ni matumizi ya Serikali katika vyombo vya umma pamoja na mashirika yote ya umma na rushwa, hayo ndiyo mambo yangu mawili ambayo nitayazungumzia kwa ufupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukusanyaji wa mapato kumekuwepo na masuala ya watu kula njama ya kufanya rushwa, ufisadi, wizi na hujuma mbalimbali katika kukusanya mapato ya Serikali. Kumekuwepo na baadhi ya watumishi wachache ambao kazi yao kubwa ni kuchonga dili ili waweze kuhakikisha kwamba wanajipatia fedha za aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria ile ya PPRA ambayo ni Sheria ya Manunuzi ya Umma kumekuwepo na tabia ya watu kukubaliana kwenye mikataba mbalimbali kwamba fanya hivi nitakufanyia hivi, hasa katika maeneo ya makadirio yanayofanywa na Maafisa mbalimbali wa Serikali hasa katika eneo la TRA hasa katika tender mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hiyo, kama watu hawa wachache ambao hawana nia nzuri na Taifa letu wakiachiwa kuendekeza masuala ya wizi na ufisadi katika mikataba mbalimbali ya Serikali na manunuzi ya umma, bajeti hii ambayo tunaipigia kelele hapa ili ikalete tija kwenye barabara, kwenye elimu kwenye uletaji wa madawa hospitalini na kwenye maji hatutafikia malengo hayo kwa sababu watu hawa wamejikita wanasubiria tu hapa tukishapitisha wanasema, hewala! tumeshaupata tukapate kula na kunywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alipokuwa anasoma hotuba yake hapa nilimuona kama ni mtu mwadilifu sana kwa sababu alijaribu kujikita sana kupinga masuala ya rushwa; kwamba atashughulika na rushwa na wanarushwa. Mwenyezi Mungu akubaliki Mheshimiwa Waziri kama nia yako ni hiyo, na kweli naamini nia yako ni hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana pia kwamba wakusanyaji wa kodi hasa katika TRA hasa kuanzia ngazi ya mikoa ngazi ya wilaya wapewe mikataba kila mwaka katika kukusanya kodi kwa sababu ndio watakaoweza kuleta tija. Kama tukimpa kwa mwaka mmoja atakuwa anaangalia bajeti yetu, kwamba alitakiwa kukusanya shilingi ngapi kwa mwaka huo, na ameyafikia malengo hayo, na kama hajafikia ni kwa sababu gani. Hapo ndipo Wizara na Serikali itakuwa inatathimini, kwamba mtumishi huyu kweli alifanya kazi kwa uwaminifu na uadilifu. Vilevile tutapunguza rushwa na mambo yanayofanana na hayo katika kuhakikisha kwamba watu hao wamikoa na wilaya wanapewa mikataba ya kukusanya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naungana na Wizara pale ambapo mtumishi atakuwa amefanya hujuma na akabainika kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu kwamba amefanya ufisadi na wizi asiendelee na huo mshahara aliokuwa nao kwa sababu ameshindwa ku- maintained status quo ya kuendelea kuwa na huo mshahara. Hatuwezi kuwa na huruma na watu ambao hawana huruma na akina mama na watoto wanaoteseka bila huduma. Waondolewe hiyo mishahara ili mwingine akiona asirudie kufanya ufisadi na wizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika masuala ya matumizi. Kwenye suala la fedha za umma katika ununuzi katika matumizi ya ununuzi wa umma na mambo mbalimbali pamekuwepo pia na mchezo mbaya sana katika taasisi zote za umma. Hapo utagundua kwamba kila mwaka CAG anapoleta ripoti yake hapa Bungeni kumekuwepo na taarifa za wizi, ufisadi na mambo mengine yote machafu ya ubadhilifu katika miradi mbalimbali ya umma. Kwanini hatutaki kusema kwamba watu hawa ifike mwisho, tuseme basi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuna nia ya kuondoa rushwa katika masuala ya miradi ya maendeleo naamini ripoti ya CAG imekuwa kila mwaka ikitupa taarifa nzuri ya kutuonesha hali ya maendeleo katika nchi yetu dhidi ya watu wanaoujumu bajeti katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hao wamekuwa wakishirikiana kabisa na mawakala na makandarasi kusema nipunguziwe bei fulani nitakupa kitu fulani; hata katika tender zile za ununuzi wa bidhaa za Serikali. Naomba hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa makini sana kwa sababu hapa ndipo Serikali inaposhindwa kutekeleza miradi yake. Kwa sababu, kwa mfano unakuta labda mradi ni milioni 50 lakini watu watapelekea huo mradi lutafika milioni 100. Mtu anakuwa na kampuni tatu. Kampuni ya kwanza itasema milioni 90 nyingine itasema milioni 95, nyingine itasema milioni 100, obviously kutokana na ile sheria atachukua mtu wa milioni 90 lakini uhalisia wa mradi ulikuwa ni milioni 50; hiyo ni hasara kubwa kwa Serikali ingetekelezwa zaidi ya miradi miwili. hapo napo lazima tuangalie na tuamue kwa moyo wa dhati na moyo wa kizalendo kwa sababu ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, katika kuyafanya haya niliyoyasema lazima tuangalie sheria zetu hasa Sheria hii ya Manunuzi lazima irekebishwe haraka iwezekanavyo ili iweze kuleta tija katika utekelezaji na utoaji tender mbalimbali za Serikali. Kwa sababu sheria hii imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo, naweza kusema hivyo. Haiwezekani mtu unaenda kusema the lowest bidder na highest bidder ndiyo utachukua the lowest bidder ilhali bado sheria hiyo imetoa mwanya mkubwa kuhakikisha kwamba mtu anaweza akafanya jambo hapo katikati na akaiba fedha nyingi tu kwa kutumia sheria hiyo. Naomba tuangalie hiyo na turekebishe haraka iwezekanavyo tuendane na bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, si sheria hiyo tu, pia utaona Sheria ya TAKUKURU (Prevention and Combating Corruption Act, 2007); hii sheria nayo inatakiwa iangaliwe. Kutoka mwaka 1980 mpaka 1990 ilikuwa imeonekana sheria hii imeshindwa kuleta tija, ikaunda tume ya Warioba mwaka 1996 ndiyo iliyokuja kuleta sasa hii ambayo ipo hapa sasa. Naomba sasa pia iangaliwe na irekebishwe. Makosa yote yaliyopo kwenye sheria hii ya kuzuia rushwa yapelekwe yawe ya uhujumu uchumi. Kwa sababu watu wanaoiba dawa za hospitalini, fedha za barabara si ni wauaji? Ni zaidi ya yule mhujumu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utaona jinsi Waziri Mkuu alivyokuwa analalamika MSD; dawa moja milioni 17 inaenda mpaka milioni 100 hawa si wauwaji wanaoua watu hospitalini. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia muswada huu. Lakini na mimi niungane na wenzangu kutoa pole sana kwa familia ya ndugu yetu ambaye ametangulia mbele ya haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakwenda moja kwa moja kujielekeza kwenye kuunga mkono muswada huu wa kuweka Kiswahili kitumike kwenye sheria zetu na sababu yenyewe ni kwamba ili lugha yoyote iweze kuwa na uhalali, lazima watumiaji wake wawe ni kwa kiwango kikubwa katika sehemu husika.

Kwa minajili hiyo, Kiswahili Tanzania kinazungumzwa na zaidi ya wazungumzaji asilimia karibu 90; asilimia 10 iliyobaki ndiyo inazungumza hiyo lugha nyingine ya kigeni. Kwa hiyo tayari imeshajihalalisha kwamba Kiswahili ni halali kitumike Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ufanisi wake, kama tutazungumza lugha ya kigeni na ufanisi wake hauwezi kukaa vizuri miongoni mwa jamii tunayoiongoza, tutakuwa hatujatenda haki.

Lakini pia haki za binadamu zinatutaka pia tuhakikishe wananchi wetu wanapata haki za binadamu dhidi ya mazungumzo, kwa sababu unapozungumza lugha usiyoijua inakuwa ni utata na hatimaye unaathirika. Kwa hiyo, hayo ni mambo ambayo tunatakiwa tuyaangalie…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, muda wetu umetubana sana, hii itakuwa ni taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Salome Makamba, sekunde 30.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba sheria ilivyo sasa hivi kabla hatujabadilisha kwenye muswada huu inasema lugha ya Mahakama ni Kiswahili na Kiingereza au vyote viwili.

Kwa hiyo hakuna sehemu inayosema lugha ya Mahakama ni Kiingereza, ni attitude za watu wetu wanao- practice sheria ndio wanaotumia Kiingereza peke yake. Kwa hiyo, nadhani tunatakiwa tubadilishe mtazamo wa watu wanaofanya kazi za sheria kuliko kusema kwamba Kiswahili hakitumiki.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana; Mheshimiwa Noah Mollel, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa hiyo na siipokei kwa sababu pia mtoa taarifa ni tabia zao za kutokuwa na heshima, kwa hiyo nadhani sipokei taarifa hiyo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Noah Mollel, hilo neno la kutokuwa na heshima liondoe halafu umalizie mchango wako.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee, hizi hofu kwanza kabisa za kusema kwamba Tanzania tunakwenda kuji-isolate siyo kweli kwa sababu Tanzania kama Tanzania lazima tuwe na haki ya kumiliki lugha yetu, hiyo ndiyo sifa yetu, ndiyo itatutangaza duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama wenzangu walivyosema, Hong Kong kwa mfano, wananchi walipopiga kelele Serikali ilikuja na muswada wakasema tunahitaji Kichina kiwekwe kwenye sheria zetu. Mwaka 1995 Jaji wa Kwanza wa Kichina alitoa hukumu ya Kichina.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tarehe 11 Machi, 1996 Mahakama zote nchini China zilitoa hukumu kwa lugha ya Kichina kuanzia makosa yote ya jinai na madai, kwa nini sisi Tanzania tunakuwa na hofu? Kazi hii ya kutumia Kiswahili ilianza muda mrefu. Mwaka 2001 kulikuwa na shauri ambalo lilitolewa la Hamisi Rajab Dibagula dhidi ya Jamhuri, 2001 na lilizungumzwa kwa Kiswahili. Kwa nini tunakuwa na hofu? Pia sheria hii ilibainisha wazi kwamba pale ambapo haki inatakiwa kutendeka, parties kwa maana ya pande mbili zitaamua zitumie lugha gani, sasa tunataka nini? Tunataka kuenzi vya wageni, vya wakoloni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2021
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Muswada huu ulioko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nikupongeze pia wewe kwa jinsi ambavyo umechaguliwa kwa kura nyingi kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Muswada huu ambao umewasilishwa na Serikali kwenye Bunge lako Tukufu ni Muswada ambao kwa kweli, kwa maeneo kadhaa, kama wenzangu walivyochangia, unaleta matumaini makubwa na hasa kwa Watanzania ambao wamekuwa wakiteseka sana katika kipindi wanapoachiwa. Kama tunavyojua kwamba, msingi wa Bunge hili linaongozwa na Katiba na ndio maana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeamua kuleta marekebisho ya sheria mbalimbali katika Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, nitajikita sana katika eneo hili la kuachiwa kwa washtakiwa mbele ya Mahakama pale ambapo DPP ameweka nolle prosequi kwamba, hana nia ya kuendelea tena na kesi iliyoko mbele ya Mahakama. Eneo hili limekuwa na changamoto kubwa sana pale ambapo washtakiwa wanaachiwa kwa nolle prosequi. Kumekuwepo na mtafaruku mkubwa mahakamani pale ambapo mshtakiwa anaachiwa na anapotoka mlangoni anashikwa tena shati, kaptula, inakuwa kama mahakamani ni huzuni.

Mheshimiwa Spika, hapa Mahakama wakati ule ilikuwa inakosa pia heshima mbele ya macho ya Watanzania kwa sababu, ya mshtakiwa kuachiwa muda huohuo na kukamatwa muda huohuo. Mshtakiwa wakati mwingine anatamani kubaki pale mbele ya Hakimu au Jaji, ili asitoke nje kwa sababu, akitoka nje atakamatwa tena na kurudishwa rumande, lakini sasa Mheshimiwa Spika utaona jinsi gani ambavyo Serikali kwa kweli, tunaipongeza sana kwa sababu imekuja na tiba ya kuwasaidia Watanzania hasa wanyonge ambao wamekuwa wakiteseka.

Mheshimiwa Spika, msingi wa marekebisho haya inatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 59(b) ambayo inaelezea kuwepo kwa Ofisi ya DPP, lakini pia msingi mkubwa ni katika Ibara ya 59B(5) ambayo inaelezea kwamba, mamlaka ya DPP. Mkurugenzi wa Mashtaka atatekeleza mamlaka yake kama ilivyoelezwa katika sheria yote iliyotungwa na au itakayotungwa na Bunge. Kwa hiyo, utaona kwamba, kama DPP atatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hii iliyowekwa basi, ina maana kwamba, Watanzania walio wengi watapata haki zao.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo ukiangalia katika sheria za wenzetu, kama Kenya, kwenye Katiba yao wameweka katika Ibara ya 157(8), wameweka kwamba DPP hataweka nolle prosequi bila kutoa sababu za kufanya hivyo, kwamba kwa nini anaacha shauri hilo, utaona jinsi gani wenzetu ambavyo wameenda mbali zaidi. Kwa hiyo na sisi kwa sheria hii inatusaidia kuonesha kwamba, tunaingia katika hizi nchi za Commonwealth, kwa maana ya nchi zilizotawaliwa na Mwingereza, tuwe katika msingi ambao ni wa utawala bora na kuhakikisha kwamba, wananchi wetu wanakuwa na furaha wanapokuwa mahakamani kwamba, haki itatendeka.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, wenzetu wameenda mbali zaidi, Mahakama pia imekuwa na uwezo wa kuamua kwamba, nolle prosequi lazima itolewe sababu. Kwa mfano, kwenye kesi ya Enock Wekesa and Michael Wata, Mahakama ilisema hivi na nanukuu, “the principle state council entered nolle prosequi and the court dismiss it for lack of reason behind entry.”

Mheshimiwa Spika, milolongo hii yote katika utoaji wa haki ina mambo mengi hasa pale ambapo mshtakiwa anahitaji kupata haki mbele ya Mahakama. Kama Bunge lako Tukufu likipitisha muswada huu kutakuwa na manufaa makubwa sana katika eneo hili kwamba, itakuwa imesaidia Serikali kukuza utawala bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu, lakini pia kuondoa matumizi mabaya ya Kifungu hicho cha 91 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, lakini pia haki kwa washtakiwa itakuwa imetolewa kiuhakika na kuwaondolea wasiwasi washtakiwa pale wanapokuwa mbele ya Hakimu au mbele ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo pia, itaijengea Mahakama heshima pale ambapo inafanya maamuzi na maamuzi hayo yakaheshimiwa katika viunga vya Mahakama badala ya mshtakiwa kukamatwa tena katika viunga vya Mahakama na kuidhalilisha Mahakama. Tunaipongeza sana Serikali kwa sababu, imeona jambo hilo na nina hakika itaendelea kufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuna suala pia la kuisaidia Serikali kupunguza bajeti kubwa ya kuhudumia wafungwa magerezani. Huu Muswada nao katika sehemu hiyo utasaidia Serikali kupunguza gharama hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho katika hilo, Serikali itapunguza msongamano magerezani. Walio wengi wanaoteseka ni wale ambao hawana uwezo.

Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge lako Tukufu liunge Muswada huu mkono, nami nauunga mkono Muswada huu. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, 2022
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Muswada huu wa Maafa. Katika Kamati yetu ya Katiba na Sheria tumejadiliana masuala mbalimbali kwa kutazama sheria hii ambayo ni muhimu na nyeti kwa wananchi wetu kwa maana ya Taifa letu katika kuzuia maafa. Mambo ambayo yaliibuka zaidi ambayo tulikuwa kwenye mjadala mrefu na mpana zaidi ilikuwa ni suala la jina la Muswada.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipoleta Muswada huu tulikuwa tumejadiliana kwa kina sana kwamba kwa nini Muswada huu uitwe Sheria ya Usimamizi wa Maafa? Tukawa tunajaribu kujadiliana kwamba kwa nini sheria hii isiitwe Sheria ya Kuzuia Majanga na Kukabiliana na Maafa?

Mheshimiwa Spika, baadaye tulikaa vizuri sana na Serikali na kueleweshana vizuri na tukaona kwamba kutokana na uandishi wa sheria, jina sahihi na muhimu kuwa ni iwe ni Sheria ya Usimamizi wa Maafa. Mambo haya yote kwenye Kamati yetu tulikuwa tumeona kwamba msingi wa sheria hii ni kuhakikisha kwamba ni kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali pale ambapo panatokea maafa.

Mheshimiwa Spika, mambo mengine haya yote ambayo tumejadiliana kwenye Kamati yetu ni kuhusu pia ukubwa wa Kamati kama Waheshimiwa Wabunge wanavyozungumza hapa. Tuliliona hili na tukazungumza kwa kirefu sana na tunashukuru Serikali kwa sababu wamekuja na wakaeleza vizuri na wamerekebisha ukubwa wa kamati, hivyo imekuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, pia tulipokuwa tumejadiliana kuhusu ukubwa wa kamati, haimaanishi kwamba maafa yakitokea sasa ndio lazima hizi kamati zikae ili hilo jambo likashughulikiwe, hapana. Serikali ilitoa maelezo mazuri sana kwamba maafa yanapotokea kunakuwepo na timu ya haraka sana kushughulikia masuala ya maafa. Kwa hiyo niwaondoe Waheshimiwa Wabunge wasiwasi kwamba haimaanishi kwamba kamati zote zikae, halafu ndio maafa yakashughulikiwe wakati watu labda wanakufa, nyumba zinaungua, lazima mambo mengi yatakuwa yanachukuliwa kuhakikisha kwamba jambo lenyewe linakabiliwa ili wananchi waendelee kuwa salama na mali zao.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kuna majanga ambayo ni ya asili na majanga ambayo yanasababishwa na binadamu. Majanga kama ya volcano na ukame ni mambo ambayo yanakuja automatically sisi hatuyaelewi, lakini kuna mambo mengine ambayo yanaweza kusababishwa na binadamu. Kwa hiyo tukasema kwamba kwa mfano, Serikali ihakikishe kwamba inapokabiliana na maafa au kujiandaa kama ambavyo nimekwishatangulia kusema, Serikali imeweka mipango na mifumo kwenye sheria hii kuhakikisha kwamba maafa yanapotokea kunakuwepo na mkakati mahususi wa kushughulikia maafa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, katika Kamati yetu pia tulijadiliana masuala ambayo wenzangu walishasema kwamba uchukuaji wa mali. Serikali ilikuja na kifungu hiki lakini tunashukuru tena Serikali kwa mara nyingine kwa sababu baada ya mjadala mrefu kwenye Kamati yetu tulisema hili linakwenda kinyume na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 24(1) kwamba uchukuaji wa mali za wananchi kwa maana Waziri awe na uwezo wa kuchukua mali…

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Noah Lemburis kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza mzungumzaji kaka yangu pale akifafanua kuhusu majukumu ya Kamati za Maafa. Napenda kumpa taarifa kwamba ibara ya 20 ya Muswada inaeleza majukumu nikiacha zile kamati zingine nakutolea tu mfano wa kamati moja, majukumu ya kamati za maafa itakuwa ni kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa na huduma za dharura katika eneo husika kama itakavyoelekezwa na Kamati ya Utekelezaji ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa. Kwa hiyo namna taarifa kwamba kuna bureaucracy, hakuna kamati ya dharura nyingine itakayotengenezwa kamati ndizo hizi na zitakazoshughulika na suala la maafa. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Noah Lemburis unapokea taarifa hiyo?

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nimeshirikia sana kwenye mjadala huu na ulikuwa ni mjadala mkali sana, lakini nataka niseme taarifa yake siipokei kwa jinsi alivyoelewa.

Mheshimiwa Spika, iko hivi, kwanza tukumbuke sio mara ya kwanza Tanzania kushughulikia maafa kwa sababu kwa mfano tu juzi Nzige walipovamia Tanzania hakuna kamati yoyote iliyokaa, ni Serikali yenyewe ilishughulikia, imetafuta ndege, imefanya mambo mbalimbali na baadaye wakaweza kudhibiti hawa nzige. Kwa hiyo nataka nimwondoe wasiwasi kwamba haimaanishi kuwepo kwa kamati hizi sasa ndio nyumba inaungua mpaka kamati ikae, hapana au mafuriko inachukua watu halafu ndio kamati zikae, hapana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea kusema kwamba suala la uchukuaji wa mali za wananchi, Waziri au Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya tuliona ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo sisi kama kamati tuliweza kuishauri Serikali na kuishukuru Serikali kwa sababu imeondoa kifungu hicho na sasa hakuna mali ya mwananchi yeyote wa Tanzania itakayochukuliwa na Waziri, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Sheria hii ina manufaa makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania. Kwa mfano, wajibu wa Serikali kwa sheria ni kuhakikisha kwamba imeweka mifumo mizuri ya kukabiliana na maafa na kuzuia maafa mengine ambayo yanaweza kuzuiwa kama yale ya binadamu. Pia kuweka vitendea kazi kwenye maeneo mbalimbali ambayo inatakiwa kwa ajili ya kujiandaa kuzuia maafa. Sheria hii pia inakwenda kuipa Serikali mamlaka ya ujenzi wa kuhakikisha kwamba inajenga miundombinu kwenye maeneo mbalimbali. Kwa mfano, kwenye maeneo ambayo mafuriko yanaweza yakaingia au labda kuhakikisha kwamba majengo yote ya Serikali yana vizimia moto na kadhalika. Vile vile usimamizi wa ujenzi wa majengo imara ili maghorofa yasije yakaanguka, pia suala la kuhakikisha kwamba mifumo mizima kwenye nyumba zote ambazo kuna vitu vingi ambavyo vinaweza vikaleta vihatarishi, iko vizuri.

Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge lako liweze kupitisha sheria hii kwa sababu ni kwa manufaa ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama tunavyojua, tunapotunga sheria tunatunga kwa sababu ya kuhakikiisha kwamba ina manufaa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2022
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.3 ya Mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea kuchangia, madhumuni na nia ya kurekebisha Sheria mbalimbali au kutengeneza Sheria mpya ni kwa sababu ya maendeleo ya kijamii, kielimu, biashara, kisiasa na maendeleo ya taifa kiteknolojia.

Mheshimiwa Spika, kwa madhumuni hayo taifa lolote ambalo linategemea kuwa na taifa bora ni lazima liangalie sheria zake na kuzirekebisha ili ziweze kuendana na hali halisi katika jamii husika, kwa maana ya sisi Watanzania kwenye nchi yetu na kufuata misingi ya autawala bora wa sheria (rule of law).

Mheshimiwa Spika, baada ya kutanguliza maelezo hayo, kwamba kwa nini tunarekebisha Sheria sasa niende kuchangia Muswada wenyewe ambao umewasilishwa mbele yako na mbele ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, kamati imejadili kwa mapama na marefu katika maeneo ya Sheria mbalimbali ambayo zimetajwa na zilikuwa takribani sheria karibu sita.

Mheshimiwa Spika, tulianza na Sheria ya Mali Kale Sura Namba 333. Sheria hiyo ilikuwa inabadilishwa maeneo kadhaa ili iweze kuendana na Sheria ya Makumbusho ya Taifa, kwa maana ya Bodi ya Taifa iweze kushughulikia majukumu ambayo yalikuwa yanashughullikiwa na wadhamini.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilikubaliana na marekebisho ya Serikali kwa sababu yameendana na hali halisi na yamekidhi matakwa ya Sheria ya Makumbusho ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilileta marekebisho ya Sheria ya Ibara ya 14 kuongeza kifungu kipya cha 17A. Kifungu hiki ni kwa ajili ya kuangalia faini mbalimbali zinazoweza kutozwa kwenye taasisi mbalimbali na watu ambao wanatunza mali kale. Kwa hiyo katika misingi hiyo, kama Kamati tuliangalia Tanzania kama nchi ambayo ina makabila zaidi ya 122, kwa hiyo wananchi wetu kwa maana ya kutunza mali kale watakuwa na mambo mbalimbali wanayotunza kwa ajili ya kulinda mali zao, mila na desturi. Lakini baadaye tukaona kwamba tukiweka faine kubwa italeta shida katika kutunza mali kale kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini baadaye Serikali iliweza kutuletea sababu ambayo tumeona ni sababu muhimu kwa sababu kumekuwepo na uharibifu wa mali kale; na kama tujuavyo mali kale ikishaharibiwa kuirudisha inakuwa ni changamoto kwa sababu ni non-renewable resources. Haiwezekani pale ambapo mali kale imeharibiwa, kwa sababu kuna maeneo mengi ambayo majengo ya mali kale yamebomolewa na wananchi na baadhi ya watu ambao hawana nia njema ya kutunza mali kale; ambayo baadaye inakuwa ni changamoto katiaka kuurudisha.

Mheshimiwa spika, lakini pia tuliangalia kwenye Ibara ya 18 kwenye Marekebisho ya kifungu cha 27, adhabu hiyo ilikuwa iwe ni Shilingi milioni tano mpaka milioni Ishirini, kwa sababu ambazo nimeshazitaja, au kifungo cha mwaka mmoja hadi miaka mitano. Serikali ilitoa sababu mbalimbali ambazo tuliona kwa kweli ni kwa sababu ya kuhakikisha kwamba mali kale zetu zinakuwa salama na zinaendelea kudumu hadi vizazi vijavyo. hivyo hatukuwa na sababu ya kuendelea kukataa pendekezo hili na moja kwa moja Kama Kamati tulikubaliana jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria nyingine ambayo tuliingalia ilikuwa ni Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha Sura Namba 342. Katika Sheria hii, marekebisho yake ilikuwa ni kuangalia mitaji ya benki ili kuendana na matakwa ya Sheria za Kimataifa za Benki ya Dunia na kadhalika ili kuangalia ku-regulate masuala yetu ya kiuchumi ndani na nje ya nchi; ambayo kwa mwanzo ilikuwa bilioni tano kwa ajili ya mitaji ya benki. Sasa tulipendekeza kuwa Bilioni kumi na tano. Lakini pia kutatengenezwa Sheria ndogo (regulation) ambayo itaweka utaratibu wa kuona mitaji kulingana na hali halisi ya uchumi kwa wakati huo.

Mheshimiwa Spika, suala hilo linasaidia sana benki zetu kuwa imara na kuimarika ili kuwa na uwezo wa kujiendesha na kutoa mikopo kikamilifu na kujenga imani kwa wananchi kutumia benki hizo.

Mheshimiwa Spika, Sheria nyingine ni Sheria ya Masoko na Mitaji Sura namba 79. Sheria hii ilikuwa inarekebishwa Ibara ya 26 kwa kuongeza kifungu kipya kidogo cha 134, ambayo inaweka adhabu ya wale ambao wanashughulika na masuala ya mitaji. Kamati hatukuwa na ubishi kwa sababu mambo yote katika kifungu hiki tumekubaliana na adhabu iliyokuwa imewekwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Sheria ya Madini Sura namba 123, ililetwa kwa ajili ya marekebisho kwa kurekebisha Ibara ya 29 kifungu cha 15(1) kuweka kifungu cha 15(3). Ilikuja hoja, kwamba Waziri awe na mamlaka ya kutwaa maeneo pale ambapo yalikuwa hayatumiki kuyarudisha Serikalini. Kulikuwa na mjadala mrefu katika Kamati yetu na tukaishauri Serikali kwamba eneo hilo la madini lirudishwe tu Serikalini pale ambapo hakutakuwa na mtu aliyewasilisha maombi ya zabuni katika eneo hilo. Kama kutakuwa na maombi ya zabuni basi Waziri hawezi kuruhusiwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hili nalo Serikali imelikubali, na kwakweli tunaishukuru Serikali kwa sababu imekuwa ikikubali mambo kadhaa ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, marekebisho mengine yalikuwa ni madogomadogo ya kusahihisha maneno katika Ibara 33 na Ibara ya 34, ambayo ilirekebisha pia kifungu cha 149 kinachohusu makosa yanayohusiana na local content. Ambayo Serikali ilitoa maelezo kwamba kama tutashindwa kusimamia maeneo ya local content italeta shida sana kwa sababu itawanyima fursa mbalimbali wananchi wetu kushiriki katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya tuliona ni muhimu sana katika kukubaliana na Serikali ili iweze kuleta tija katika uchimbaji wa madini na uchenjuaji wa madini kwenye taifa letu. Hasa ukizingatia kwamba kumekuwepo na suala la ubadhirifu na wizi katika migodi na maeneo kama hayo. Sheria hii iweze kusaidia kupunguza na kuondoa changamoto hizo za ujanja ujanja ambao unaweza ukawepo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, Sheria nyingine illikuwa ni Sheria ya Makumbusho ya Taifa Sura Na. 281, ambayo ilikuwa inaelezea masuala mbalimbali, ikiwemo suala la muundo wa wajumbe katika Sheria hiyo. Kama tunavyofahamu, kwa upande wa muundo wa wajumbe tulikuwa tunashauri kwamba lazima uendane kama vile ilivyo kwenye zile Sheria za Mabaraza ya Ardhi. Sheria ya Mabaraza inaeleza wazi kwamba, lazima pawepo na asilimia kadhaa ya wanawake ili kuwawezesha kufanya maamuzi ambayo yanakuwa sawa wakati wa kutekeleza majukumu hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.