Primary Questions from Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel (20 total)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa maji kwenye Vijiji vya Engutukoiti, Losineni, Juu, Losineni kati, Oldonyawasi, Lemanda, Lemengrass, Oldonyosambu, Likurat, Olkeejulbendet, Lenigjape, Olkokula, Lemanyati, Lenjani, Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni na Kata za Kimyak, Sambasha Tarakwa, Oloirien, Kiranyi, Likidingla, Sokon II, Olturito, Bangata, Mlanganini, Nduruma, Bwawani, Oljoro na Lahni Musa, Kisango, Mwandet Wilayani Arumeru?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lemburis Saputi Mollel, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli vijiji hivi vilikuwa na changamoto ya huduma ya maji, lakini kuanzia mwezi Disemba, 2020, Vijiji vya Lengijave, Olkokola, Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni vimeanza kupata huduma ya maji kutoka kwenye mradi uliofadhiliwa na Shirika la Uingereza la DFID kupitia Shirika la Water Aid Tanzania. Aidha, Vijiji vingine vya Oldonyosambu, Oldonyowasi, Lemanda, Losinani Kati na Juu na Ilkuroti vinatarajiwa kupata huduma ya maji kutoka kwenye mradi huu kupitia upanuzi unaofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Jiji la Arusha kutoka kwenye tanki la maji lililopo kijiji cha Lengijave, lenye ukubwa wa mita za ujazo 450. Kijiji cha Lemanyata kina huduma ya maji kupitia Mradi wa Olkokola – Mwandeti.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/ 2021, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.13 kwa Wilaya ya Arumeru kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa Mradi wa Maji wa zamani wa Nduruma – Mlangarini na kukarabati Mtandao wa Bomba unaopeleka maji Vijiji vya Themi ya Simba, Kigongoni na Samaria na ukarabati wa Mradi wa Manyire – Maurani – Majimoto utakaonufaisha Vijiji vya Maurani, Manyire na Maji moto kuwa na maji ya uhakika na Miradi ya Likamba na Oloitushura & Nengungu.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali ya Wilaya ya Olturumet katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwa kuipatia jengo la OPD, Wodi ya kulaza Wagonjwa, Jengo la X-Ray na mashine ya X-Ray ili Hospitali hiyo iweze kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemberis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Olturumet Arusha, ambazo zinahitaji ukarabati na upanuzi wa miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Ukarabati wa Hospitali kongwe 43 nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa Hospitali 21 za Halmashauri nchini. Mpango huo utaendelea kutekelezwa kwa awamu hadi ukarabati na upanuzi wa hospitali kongwe zote nchini utakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge Noah kuwa Hospitali ya Wilaya ya Olturumet Arusha ni miongoni mwa hospitali ambazo zitafanyiwa ukarabati na upanuzi.
MHE. NOAH L.S. MOLLEL aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia ya kupisha njia kubwa ya umeme wananchi wa Vijiji vya Lengijape, Ilkurot na Olkejulenderit katika Jimbo la Arumeru Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme TANESCO inaendelea kukamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga. Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imeshalipa fidia kwa wananchi wote jumla ya shilingi bilioni 52.67 zikiwa ni fidia kwa wananchi 4,526 katika mikoa yote mitatu iliyoguswa na mradi huu wakiwemo wananchi wa Vijiji vya Lengijape, llkurot na Olkejulenderit katika Jimbo la Arumeru Magharibi. Aidha, Serikali kupitia TANESCO imeshalipa fidia kwa taasisi zilizopo katika vijiji vyote vya Wilaya za Singida Vijijini, Hanang, Babati na Longido.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya ulipaji wa fidia shilingi bilioni 314.675 kwa maeneo ya taasisi na vijiji 38 katika Wilaya za Monduli, Arumeru na Manispaa ya Sindida yanaendelea na maeneo ya vijiji na taasisi hizo yatalipwa fidia kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri husika ifikapo mwezi Juni, 2021.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mianzini, Sambasha, Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Ole Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aliagiza barabara ya Mianzini – Sambasha – Ngaramtoni hadi Hospitali ya Selari yenye urefu wa kilometa 18 kupandishwa hadhi ili isimamiwe na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na aliagiza ijengwe kwa kiwango cha lami. Awali barabara hii ilikuwa inasimamiwa na Halmashauri za Arusha DC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ilifanya usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami pamoja na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kazi ambayo ilikamilika mwaka 2019. Zabuni za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kilometa zote 18 zimetangazwa tarehe 17 Mei, 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami zitaanza mara baada ya tathmini ya zabuni kukamilika na mkandarasi kupatikana. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 jumla ya shilingi bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya mradi huu. Ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa Barabara ya Redio Habari Maalum kwenda Hospitali ya Wilaya ya Olturumet kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Redio Habari Maalum hadi Hospitali ya Wilaya ya Olturumet iliyopo Arumeru Magharibi yenye urefu wa kilomita 2.5 ni miongoni mwa miradi nchini ambayo ni ahadi za Rais. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabra hiyo kwa kiwango cha lami, na itatoa kipaumbele cha ujenzi pindi fedha za ujenzi zitakapopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuifanyia matengenezo barabara hii kila mwaka wa fedha ili kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka. Katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 na 2020/2021 Serikali imetoa shilingi milioni 37.7 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 56.75 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Redio Habari Maalum hadi Hospitali ya Wilaya ya Olturumet.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itayachukua Mashamba Pori yasiyoendelezwa kwa Shughuli iliyokusudiwa yakiwepo Mashamba ya Aghakan, Lucy Estate na Gomba Estate na kuyagawa kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada waliyofanya wenzangu naomba kabla sijajibu swali nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunichagua mimi na mwenzangu Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula kuwa katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; ahadi yangu kwake na kwa viongozi wote wa juu yetu ni kwamba hatutowaangusha tutafanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kwa ruhusa yako nijibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, hatua za ubatilishaji wa milki nchini hutekelezwa ikiwa mmiliki wa shamba au kiwanja amekiuka masharti ya umiliki yaliyoainishwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, Shamba la Agakhan kwa sasa lipo ndani ya eneo la mpangomji ambalo limeingizwa kwenye Mpango Kabambe wa uendelezaji wa Jiji la Arusha. Kwa kuzingatia mpango huo, eneo la shamba hilo limepangwa kuendelezwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu, eneo la biashara na makazi. Mmiliki wa eneo hilo alipaswa kuendeleza kwa kuzingatia mpango huo. Kutokana na kubadilika kwa mpango wa matumizi ya eneo hilo, Serikali ipo katika mazungumzo na mmiliki ili kuona namna bora ya kutekeleza mpango huo.
Mheshimiwa Spika, shamba la Gomba Estate ni miongoni mwa mashamba ambayo wamiliki walichukua mikopo na kushindwa kurejesha kwa hiyo shamba hilo kwa sasa lipo chini ya uangalizi wa taasisi ya benki ya Standard Chartered na Shirika la NSSSF. Ili kutatua changamoto ya urejeshaji wa mkopo, Serikali kwa kushirikiana na wamiliki na taasisi tajwa imeanza zoezi la kupanga, kupima ardhi husika ili kupata viwanja vitakavyouzwa ili mkakati wa kurejesha mkopo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu shamba la Lucy Estate, miliki ya shamba husika ilibatilishwa mwaka 1999 kutokana na kukiukwa kwa masharti ya umiliki. Hata hivyo, mmiliki wa shamba hakukubaliana na hatua hiyo na hivyo alifungua shauri Na. 50/2015 katika Mahakama Kuu ya Arusha dhidi ya Serikali kupinga ufutaji huo. Baada ya majadiliano ya kisheria, ilikubaliwa kwamba aliyekuwa mmiliki alipwe fidia ya maendelezo yaliyokuwepo. Hivyo, Serikali inaandaa mpango wa matumizi wa shamba hilo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na sehemu ya shamba husika itatumika kupata fedha kwa ajili ya fidia.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani juu ya mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji na hayatumiki kuzalisha mali na ajira nchini?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa yapo mashamba makubwa nchini ambayo yamegawiwa kwa wawekezaji ambapo baadhi ya mashamba hayo yanatumika kwa uzalishaji mali na ajira na mengine hayatumiki kama ilivyokusudiwa. Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine imeanza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji kwa kufanya ukaguzi na kuainisha changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni kufanya majadiliano na wawekezaji waliobainika kuwa na changamoto ili kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji. Kwa mashamba ambayo yametelekezwa, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti ya uwekezaji ikiwemo kuyarudisha na kuyapangia matumizi upya kwa manufaa ya umma.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kutoa chakula cha bei nafuu kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi kutokana na athari za ukame?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kutoa chakula na kukiuza chini ya bei ya soko. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2023 kiasi cha mahindi tani 24,975.152 zimepelekwa na kuuzwa katika Halmashauri 60 nchini katika vituo vya mauzo 116. Halmashauri ya Arumeru, kituo cha mauzo kimefunguliwa eneo la Kikatiti na jumla ya tani 6.28 zimeshauzwa kwa Wananchi.
MHE. NOAH L. SAPUTU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wagonjwa wa Nje, Jengo X-Ray, Jengo la Watoto na Jengo la Utawala katika Hospitali ya Wilaya Olturumet Halmashauri ya Arusha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais- TAMISEMI mwezi Aprili, 2021 ilipokea maombi maalum ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Hospitali ya Olturumet ambayo miundombinu yake imechakaa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 16.55 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe 19 nchini. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali Kongwe nchini ambapo Hospitali ya Olturumet itapewa kipaumbele.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo ili kuongeza uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kupunguza gharama za upatikanaji wa mbolea na pembejeo nyingine kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mazao ya kilimo. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa ruzuku ya mbolea, mbegu bora kwa mazao ya alizeti, miche ya chikichi, parachichi, chai na kahawa pamoja na viuatilifu vya mazao ya korosho, pamba na viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mimea ikiwemo viwavijeshi, inzi, panya, kweleakwelea na nzige.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Aprili, 2023 jumla ya tani 349,922 za mbolea zimenunuliwa na wakulima 799,937 kwa bei ya ruzuku. Vilevile, Serikali imetoa jumla ya lita 48,033 za viuatilifu vya kudhibiti viwavijeshi, ekapaki 1,823,688 za viuatilifu vya pamba, tani 15,015.03 na lita 2,684,470.5 za viuatilifu vya zao la korosho, tani 1,004 za mbegu bora za alizeti na miche bora 61,486,981 ya mazao mbalimbali kwa utaratibu wa ruzuku. Aidha, utaratibu wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima utaendelea kufanyika kulingana na bajeti ya Serikali. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini huduma ya Mawasiliano ya Simu itapelekwa Kata za Bwawani, Oldonyowas, Laroi, Mwandet, Oljoro na Oldonyosambu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Saputu, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ili kubaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata za Bwawani, Oldonyowas, Laroi, Mwandet, Oljoro na Oldonyosambu zilizopo Jimbo la Arumeru Magharibi, tathmini hii itasaidia kufahamu ukubwa wa tatizo na mahitaji halisi ili hatimaye yaweze kuingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha na kutangazwa katika zabuni zijazo, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza
Je, lini Serikali itafanya ukarabati wa mnada wa ng'ombe na mbuzi wa Olokii?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya mifugo hapa nchini kwa kujenga na kukarabati minada ya mifugo ya awali, minada ya upili na minada ya mipakani. Kwa sasa kuna jumla ya minada 504 ya awali, 17 ya upili na 12 ya mpakani. Mnada wa Olokii (Themi) ni moja ya minada ya upili ambao upo chini ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 na Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imejenga na kukarabati minada 12 katika maeneo mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itafanya usanifu wa miundombinu ya mnada wa Olokii (Themi) ili uweze kuingizwa katika Mpango wa Bajeti wa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Arusha – Mirongoine – Simanjiro – Terati hadi Kongwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Arusha – Mirongoine – Simanjiro – Kongwa inajulikana kwa jina la Arusha – Kibaya – Kongwa yenye urefu wa kilometa 453. Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction plus Finance (EPC + F). Hadi sasa Mkandarasi amekwishapatikana na mkataba wa ujenzi utasainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023. Ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Mji Mdogo wa Ngaramtoni?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Polisi haina eneo lililotengwa na Halmashauri kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi na nyumba za makazi ya Askari. Tunazo taarifa kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni inaendelea na mchakato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru kupata eneo na kutenga kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za taasisi za umma ikiwemo Kituo cha Polisi na nyumba za makazi ya Askari. Pindi eneo hilo litakapopatikana Wizara itatenga fedha za ujenzi wa kituo na nyumba za makazi ya Askari kupitia Jeshi la Polisi, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga mradi wa maji wa vijiji tisa vya Kata za Oldonyosambu na Oldonyowas?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa maji wa Oldonyosambu kwa ajili ya kuhudumia vijiji tisa vya kata za Oldonyosambu na Oldonyowas. Utekelezaji wa mradi huo unahusisha ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 47.8, ujenzi wa matanki matatu yenye ujazo wa lita 575,000, ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji na booster stations mbili. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022 na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji katika kata hizo.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Eneo la Oldonyosambu kuna viteule viwili vya Jeshi ambavyo ni Kiteule cha Kikosi cha Oljoro na Kiteule cha Kikosi cha Rada. Katika maeneo hayo mawili, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hatujapokea taarifa ya kuwepo kwa maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kuna malalamiko yoyote kuhusu maeneo ya wananchi kuchukuliwa na Jeshi, Wizara ipo tayari kupeleka wataalam katika eneo hili ili kushughulikia malalamiko hayo.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza kujenga Mahakama Kata ya Bwawani katika Jimbo la Arumeru Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Mahakama za Mwanzo. Kwa sasa tunazo Mahakama 960 nchi nzima, baadhi zikiwa na majengo chakavu na ya zamani, hivyo yanahitaji kufanyiwa ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Bwawani kwa sasa wanapata huduma za Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo ya Nduruma ambayo kwa sasa inafanya kazi kwa kutembelewa. Mahakama hii ya Nduruma ipo umbali wa kilomita 15 kutoka Bwawani na inasajili wastani wa mashauri 120 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa kuzingatia umuhimu, katika mwaka wa fedha 2023/2024 tunajenga Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai katika Jimbo la Arumeru. Aidha, ujenzi wa Mahakama ya Bwawani utazingatiwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kulingana na mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. NOAH L. SAPUTU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itazuia kupaki magari ya Serikali sehemu za starehe baada ya saa za kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Waraka wa Rais Na. 1 wa Mwaka 1998 kuhusu Hatua za Kubana Matumizi ya Serikali, ilielekezwa kuwa Magari yote ya Serikali yanatakiwa kuwa yameegeshwa sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo ifikapo saa 12.00 jioni bila kukosa. Vinginevyo, kiwepo kibali rasmi kinachoruhusu Gari la Serikali kuwepo barabarani baada ya saa 12.00 jioni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Serikali kupitia Kanuni Na. 21 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, imezuia Watumishi wa Umma kutumia Magari ya Serikali kwa matumizi binafsi. Hivyo, mtumishi anayekwenda kinyume na maelekezo hayo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa hii naomba kuwakumbusha Maafisa Masuuli wote kusimamia maelekezo hayo. Ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi kukamilisha miradi ya maji mikubwa na midogo nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kupitia bajeti ya 2024/2025 jumla ya miradi 1,095 inatarajiwa kutekelezwa vijijini na miradi 247 mijini. Miradi hiyo inatekelezwa ili kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha miradi ya maji yote mikubwa na midogo iliyopangwa kutekelezwa na inayoendelea na utekelezaji nchini inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. Mkakati mahsusi wa Serikali ni kuhakikisha inapeleka fedha zinazohitajika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati sanjari na kusimamia utekelezaji wake.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza:-
Je, lini minara itajengwa vijiji vya Kata ya Bwawani na Vijiji vya Nengung’u, Oloitushula, Olchorovus, Engutukoit, Losinoni Juu na Losinoni Kati?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekamilisha utekelezaji wa ujenzi wa minara mitano ya kufikisha mawasiliano ya simu katika Kata za Oljoro, Olmotonyi na Oldonyosambu zilizopo Wilayani Arumeru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia UCSAF itafanya tathmini katika Vijiji vya Kata ya Bwawani na Vijiji vya Nengung’u, Engutukoit, Losinoni Juu na Losinoni Kati ili kubaini mahitaji halisi ya huduma za mawasiliano katika kata hizo na kuweka mkakati wa namna bora ya kufikisha huduma za mawasiliano hitajika.