Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdallah Jafari Chaurembo (11 total)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza kipande cha barabara kutoka Mbagala Zakhem hadi Mbagala Kuu na kipande cha barabara toka Mbande – Kisewe hadi Msongola?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbagala Zakhem – Mbagala Kuu yenye urefu wa kilometa 5.1 ni miongoni mwa barabara ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne alitoa ahadi mwaka 2017/2018. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilijenga kilometa moja ya lami katika barabara hii ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara ya Mbande – Kisewe – Msongola ni sehemu ya barabara ya Chanika – Mbande – Mbagala Rangi Tatu yenye urefu wa kilometa 29.4 inayounganisha barabara ya Kilwa na barabara ya Nyerere. Kati ya kilometa 29.4 kilometa 22.8 zimekwishajengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 6.06 zilizobaki zipo kwenye kiwango cha changarawe. Barabara hii inasimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Msongola mpaka Mbande kilometa 6.06 kwa kiwango cha lami. Ujenzi unaendelea kwa awamu kupitia fedha za maendeleo ambapo kuanzia mwaka 2018/2019 hadi mwaka 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1.05 zimetumika kujenga kilometa moja kwa kiwango cha lami nyepesi. Kazi hiyo imeanza Msongola kuelekea Mbande. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza transfoma ya 100 MVA katika substation ya Mbagala ili kuondoa tatizo la kukatika umeme katika Jimbo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge Wa Mbagala, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mbagala msongo wa kilovoti 132/33 chenye uwezo wa MVA 50 ulikamilika na kuanza kufanya kazi rasmi tarehe 25 Februari 2018, kupitia utekelezaji wa mradi wa TEDAP chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. Baada ya kituo hiki kuanza kufanya kazi, hali ya upatikanaji umeme katika eneo la Mbagala uliimarika ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha kupoza umeme, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa kuboresha vituo vya kupoza umeme vya Kinyerezi na Mbagala kwa kufunga transfoma zenye uwezo wa MVA 50 kwa kila kituo pamoja na kuongeza uwezo wa njia ya kusafirisha umeme ya kilovoti 132 kutoka Kinyerezi hadi Mbagala kupitia Gongo la Mboto. Mradi huu unatarajia kutekelezwa kwa kipindi cha miezi kumi kuanzia Juni, 2021 na kukamilika Aprili, 2022. Gharama ya mradi huu ni takriban Dola za Marekani milioni 9.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huu, kutaboresha hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya Mbagala na maeneo mengine ya jirani yanayopatiwa umeme kutoka katika kituo hicho.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa fedha Halmashauri ya Temeke ili iweze kujenga Shule mpya za kutosha kutokana na Jimbo la Mbagala kuongoza kuwa na wanafunzi wengi wa Shule za Msingi na Sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, katika mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Shilingi milioni 724 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Msingi ya Marten Lumbanga na Shule ya Msingi Dovya. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kupitia mapato yake ya ndani imejenga jengo la ghorofa moja kwa ajili ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Mbagala kwa gharama ya shilingi bilioni 1.056.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imeitengea Halmashauri ya Wilaya ya Temeke shilingi bilioni 1.74 ambapo shilingi bilioni 1.53 zitaelekezwa katika Jimbo la Mbagala kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Chamazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilikamilisha maboma 10 ya madarasa ya Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwa gharama ya Shilingi milioni 137.5. Aidha, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 Serikali imejenga madarasa mapya 25 ya Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kupitia mapato yake ya ndani imejenga vyumba 76 vya madarasa ya Shule za Sekondari kwa gharama ya shilingi bilioni 1.72. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga Shilingi milioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 11 vya madarasa ya Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Shilingi milioni 209 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Shule za Sekondari.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Mbagala Kokoto hadi Kongowe wanaopisha ujenzi wa barabara ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara Ujenzi na Uchukuzi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa lengo la kushughulikia tatizo sugu la msongamano wa magari, hususan katika barabara kuu za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo barabara ya Kilwa kuanzia Mbagala Rangitatu mpaka Kongowe yenye urefu wa kilometa 3.8. Utekelezaji wa mpango huu unahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili kuwa njia nne pamoja na ujenzi wa Daraja la Mzinga.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha ujenzi huo unafanyika bila vikwazo, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha hatua za awali za kupitia jedwali la fidia na kuhakiki mali za wananchi wanaostahili kulipwa fidia. Aidha, zoezi hili liliwahusisha pia viongozi wa Serikali za Mitaa husika ili kuhakikisha wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia wanalipwa stahili zao kwa mujibu wa sheria zilizopo. Hivyo wananchi wa Mbagala eneo la Kokoto hadi Kongowe wanaombwa kuwa wavumilivu wakati zoezi la kuhakiki taarifa za fidia linaendelea. Mara uhakiki utakapokamilika wahusika wote watalipwa fidia kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyarudisha kwenye Halmashauri maeneo yote yasiyoendelezwa na Mashirika ya Umma kwa zaidi ya miaka kumi ili Halmashauri zijenge miundombinu ya huduma za jamii?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, haki ya kumiliki ardhi hutolewa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi. Hivyo zimeweka masharti ya umiliki wa ardhi ikiwa ni kufanya maendelezo ndani ya muda husika, pamoja na hatua za kuchukua endapo kuna ukiukwaji wa masharti hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba baadhi ya Mashirika ya Umma yaliyomilikishwa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, hayajaendeleza ardhi zao. Katika kutatua changamoto hizo, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka za upangaji, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia ardhi iliyomilikishwa na kuachwa bila kuendelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Wizara imeanza kwa kufanya ukaguzi wa maeneo yaliyomilikishwa kwa watu binafsi, wawekezaji wakubwa na Mashirika ya Umma ili kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki yaliyotolewa na hivyo kuanzisha taratibu za ubatilisho. Baada ya kubatilisha miliki za maeneo ambayo hayajaendelezwa, ardhi husika hupangwa na kupimwa upya kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo uwekezaji, miundombinu ya huduma za jamii kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuendelea kufanya ukaguzi wa maeneo yaliyotolewa kwa Mashirika, Makampuni na watu binafsi na kuanzisha utaratibu wa ubatilisho endapo itabainika uwepo wa ukiukwaji wa masharti ya umiliki na kuwasilisha mapendekezo Wizarani kwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya mapunjo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu Mbagala?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa mkono wa pole na siyo fidia, kwa wananchi 12,647 waliothirika na milipuko ya mabomu iliyotokea tarehe 29 Aprili, 2009 katika Kambi ya JWTZ Mbagala. Malipo hayo, yalitolewa kwa awamu sita kuanzia mwaka 2009 hadi 2020. Vile vile, Serikali ilitoa kifuta machozi pamoja na kugharamia huduma za mazishi kwa familia 29 zilizopoteza wapendwa wao kutokana na milipuko hiyo ya mabomu ya Mbagala.

Mheshimiwa Spika, zoezi la kutoa mkono wa pole kwa waathirika lilisitishwa rasmi na Serikali mnamo mwezi Machi, 2020 baada ya walengwa wote waliokusudiwa kujitokeza na kulipwa.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, lini maji yatasambazwa Toangoma, Chamazi, Mianzini, Kilungule, Kiburugwa, Kijichi, Mbagala, Charambe, Kibondemaji na Mbagala Kuu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata za Toangoma, Chamazi Mianzini, Kilungule, Kiburugwa, Kijichi, Mbagala, Charambe, Kibondemaji na Mbagala Kuu zinapata huduma ya majisafi na salama kupitia vyanzo vya maji ya visima virefu na vifupi. Changamoto iliyopo katika kata hizo ni kuwa baadhi ya maeneo hayajafikiwa na mtandao wa maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kutumia vyanzo vya visima vya Kimbiji kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji katika kata hizo. Kwa sasa, taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, kuna mpango gani kujenga mifereji Barabara ya Kigamboni – Kongowe, Mtaa wa Mikwambe, Kata ya Toangoma - Mbagala?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam ipo kwenye hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi wa kufanya ukarabati wa mabega ya Barabara ya Kongowe – Kibada, yenye urefu wa kilometa moja. Ukarabati huo pia utahusisha Ujenzi wa mitaro kwenye baadhi ya maeneo, ikiwemo eneo la Mikwambe yenye urefu wa kilometa mbili, ahsante sana.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Stendi ya Mabasi yaendayo Mikoa ya Kusini katika eneo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na stendi ya mabasi yaendayo kusini katika eneo la Mbagala. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaendelea na taratibu za kupata eneo la kujenga stendi hiyo katika Kata ya Mbagala. Pindi eneo litakapopatikana ujenzi utaanza.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, nini hatma ya Barabara ya Zakhiem Mbagala Kuu inayoshindwa kujengwa kwa kuwa bomba la mafuta lipo chini ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kijichi - Mbagala Kuu - Zakhiem ina urefu wa kilometa 5.1. Kati ya kilometa hizo kipande cha mita 600 ni sehemu ya bomba la mafuta la TAZAMA. Baada ya majadiliano ya mara kwa mara kati ya TARURA, TAZAMA na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, TAZAMA waliruhusu mita 200 kuwekewa tabaka la zege na tayari tabaka la zege limewekwa kwa gharama ya shilingi milioni 155.79 kupitia mradi wa DMDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kipande cha mita 400 kilichobaki, TAZAMA wameruhusu kiwekewe tabaka la changarawe pekee na sio kujenga barabara kwa kiwango cha lami au zege.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, lini Barabara za Tinyango, Machimbo, Kisiwani, Mapemba, Federation, Kwa Mzala na Kwa Masista, Kata ya Chamazi zitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara hizi, ambapo kwa mwaka 2022/2023 barabara ya Machimbo yenye urefu wa kilometa 1.35 ilijengwa kwa zege urefu mita 240 kwa gharama ya shilingi milioni 73.8 na kuwekewa changarawe mita 800 ambapo shilingi milioni 36 zilitumika na mwaka 2024/2025 imepangwa kujengwa kwa zege mita 100 kwa gharama ya shilingi milioni 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2024/2025 barabara zifuatazo ziko kwenye mpango ambapo barabara ya Tinyango (kilometa 1.14) imepangwa kujengwa kwa zege urefu wa mita 500 kwa gharama ya shilingi milioni 350 na barabara ya Transfoma Kwa Mzala (kilometa mbili) itajengwa kwa zege mita 100 sambamba na kufanyiwa matengenezo ya sehemu korofi ambapo shilingi milioni 94 zimetengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara za Molemole Kwa Masista (kilometa 1.28), Federation (kilomita 0.58), Mapemba (kilometa 0.8) na Kisiwani (kilometa 1.0) kwa mwaka 2024/2025 zimepangwa kufanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa kuweka changarawe na kuchongwa ambapo shilingi milioni 300 zitatekeleza kazi hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.