Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dorothy George Kilave (46 total)

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji kwa sababu Jimbo letu la Temeke maji yamefika karibu kila kata. Tatizo letu kubwa ni kwamba bomba lile kubwa limepita katika barabara kubwa lakini kuvuta maji kwenda ndani ya nyumba zetu ambapo miundombinu siyo mizuri sana kwenye Kata za Buza na Kilakala na nyumba ziko mbali. Niombe Wizara ya Maji tunapoomba kuvutiwa maji ndani ya nyumba zetu, fedha ile ambayo tunatakiwa kuilipa kidogo ni kubwa, sasa mfikirie tuweze kuvuta kwa nusu ya bei halafu muendelee kutudai ndani ya malipo ya kila mwezi kama vile tunavyofanya luku ili tuweze kuona kila mmoja sasa anapata maji ndani ya nyumba yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU SPIKA: Hilo ni ombi, nadhani utakuwa umeliandika Mheshimiwa Waziri.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini naomba sasa niseme kwamba sasa ni miaka karibu saba tangu mmelitwaa hili eneo.

Je, haiwezekani kwamba mtachukua tena miaka saba kwa ajili ya kulirekebisha na kuweka mpango huo? Niombe basi kama nilivyosema kwamba wananchi wa Temeke tunatamani kujenga shule za sekondari na msingi kwa sababu tunazaliana sana na maeneo mijini sasa hivi hakuna. Niseme tu kwamba tuombe sasa Wizara yako itupe eneo hili ili sisi katika miaka hii ambayo tumeambiwa tujenge shule za sekondari pamoja na msingi basi tuyapate kwa sababu naona mtakwenda tena miaka saba ijayo katika kutengeneza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali yetu sasa ina mpango gani wa kumalizia fidia kwa wananchi wa maeneo ya jirani karibu na pale ambapo mmetwaa lile eneo lakini yapo maeneo Shimo la Udongo ambapo mlitakiwa kuyatwaa lakini bado hamjalipa fidia. Naomba maswali yangu haya mawili tuweze kujibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nomba kujibu maswali mawili ya ziada ya Mheshimiwa Dorothy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie hatutachukua miaka saba tena. La pili ni kwamba eneo lile ni karibu kabisa na Bandari ya Dar es Salaam na sisi kama Taifa tumekuwa mara nyingi tukijadiliana namna gani kuifanya bandari yetu kuwa effective na efficient na ili iweze kuhudumia waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa. Itakuwa ni makosa ya kimkakati tukiligeuza eneo ambalo halizidi mita 500 au 1,000 kuligeuza kuwa eneo la shule. Nataka tu nimshauri yeye na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Meya wake wa zamani yumo ndani ya Bunge hili ujenzi wa sekondari sio lazima tujenge kwenda…, tuna uwezo wa kujenga maghorofa kwa hiyo nawashauri Manispaa ya Temeke mjenge shule kwa mfumo wa maghorofa na ninyi mna mapato mengi kuliko Manispaa nyingi katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kuhusu fidia katika eneo lile tumebaki nadhani kaya kama mbili au tatu ambazo hazijamaliziwa fidia katika eneo la Kurasini na wale wananchi hawakuwa tayari, lakini wako katika hatua za mwisho kumalizana nao na watalipwa haki yao. Mpango wa Serikali katika lile eneo, eneo la ukubwa wa ekari 20 tunajenga The First Agricultural One Stop Centre ili mazo yetu ya kilimo hasa ya mbogamboga na matunda yaweze kusafiri kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya sasa yanavyotumika kupitia bandari za nchi zinazotuzunguka.

Kwa hiyo, tunawaombeni sana watu wa Temeke mtuunge mkono kufikia azma hii ili eneo lile liweze kutusaidia kutatua changamoto ya usafirishaji wa mazao na kugeuza kuwa ni export hub eneo lile. Nashukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nawapongeza kwa jinsi ambavyo wameweza kutujengea vituo vya afya viwili; cha Buza pamoja na Malawi na vyote vimemalizika katika Halmashauri yetu ya Temeke. Sasa nauliza:-

Je, vifaa tiba vitaingia lini; kwa sababu sasa ni muda mrefu hatujapata vifaa hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya vikiwemo vya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke vimekamilika na kuna changamoto ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao tutakwenda kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha vituo hivi vya afya vinapelekewa vifaa tiba. Katika swali langu la msingi nimesema, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 26 zimeshatolewa tayari; na shilingi bilioni 15 vifaa tiba vimeshapelekwa kwenye vituo vya afya vilivyojengwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili; na shilingi bilioni 11 zipo katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kupeleka vifaa tiba katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vituo vya Afya hivi vya Temeke vilijengwa awamu ya tatu na awamu ya nne, kwa hiyo, vitakuwa katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/ 2022. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo litaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami siko mbali sana. Madhara yaliyopo katika Jimbo la Mbagala ni sawa sawa na Jimbo langu la Temeke.

Nimeona hapa Shule nyingi za Sekondari zimeenda kujengwa Mbagala, lakini Temeke bado tuna kiu; kama nilivyosema siku zote, Temeke tunazaliana sana na sasa tuna watoto wengi wa Darasa la Kwanza. Tutakapofika mbali, naamini kabisa sekondari hizi zilizopo haziwezi kutosha hasa kule Vituka, Tandika, Kurasini, Mtoni, Temeke 14, kote tunatamani sekondari hizi ziwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kwamba kama atakwenda naye Mbagala, basi twende pamoja na Temeke tufike. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge naye kwamba tutakavyopanga safari ya Pamoja, Mbunge wa Mbagala pamoja na Mbunge wa Temeke tutakwenda. Niliainisha Kata za Mbunge wa Mbagala na wewe tutakwenda wote katika maeneo ya Vituka, Tandika, Kurasini, Temeke 14, kuhakikisha tunafanya kazi ya wananchi. Nanyi wote mnafahamu, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuondoa tatizo la Madarasa nchi nzima, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itaweza kutuongezea transformer nyingine kwenye Jimbo la Temeke kwani tuna mahitaji ya megawatt 117, lakini sasa hivi tunatumia megawatt 32. Je, tutapata lini transformer hii nyingine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Jimbo la Temeke pamoja na Mbagala na Mkuranga tumelazimika kuongeza vituo vitatu katika kila wilaya kwa ajili ya kuongeza transformer za megawatt 48 kila mahali, kwa hiyo Temeke, Mbagala pamoja na Mkuranga tunaongezea transformer ya megawatt 48 kila eneo. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Temeke, hasa Jimbo la Temeke, naomba kuuliza: Je, ni lini sasa umeme utakamilika kwenye Jimbo letu la Temeke? Kwani hata kabla ya mgawo tulikuwa hatupati umeme; na sasa pia hatupati umeme kwa masaa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Temeke wanataka kujua; je, ni lini sasa kutakuwa na ukamilifu wa umeme kwenye Jimbo letu la Temeke? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa kuna outage kadhaa ndani ya Jimbo la Temeke. Sababu ya kukatika kwa umeme mojawapo ilikuwa inasababishwa na ujenzi wa barabara ya BRT ambapo tumekuwa tuna schedule ya kukata umeme katika siku ya Jumanne na Alhamisi kwa ajili ya kupisha uhamishaji wa nguzo kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hii. Pia zoezi hilo limekuwa likiendana pamoja na kuhamisha ile miundombinu ya umeme kuipitisha chini ya ile barabara na kuweza kuweka mazingira mazuri ambayo yatakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linakwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya umeme katika Jimbo la Temeke na mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kujenga vituo vya kupoozea umeme na kuviongeza nguvu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi ujao kama nilivyojibu juzi, kwamba tutakuwa tumeweka vizuri mazingira ya umeme kwenye Mkoa wetu wa Dar es Salaam na katika maeneo mengine kwa kurekebisha miundombinu mbalimbali. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba niongeze maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefanya jitihada kuweza kuleta Walimu, lakini utaona kwamba, asilimia 71 ni kubwa sana kwa jimbo letu la Temeke au Wilaya nzima ya Temeke. Sasa je, Serikali haioni kwamba, inaweza kufanya jitihada za ziada ili kuweza kupata vibali kwa halmashauri zetu kuweza kuajiri Walimu kwa mikataba, hao wa sayansi ili tuone kwamba, elimu sasa inaendelea mpaka hapo Wizara itakapokuwa imepata namna ya kuweza kuajiri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuhusiana na vifaa katika sekondari zetu, je, bado haionekani ya kwamba, tunaweza tukapata vibali hivyo tukaweza kununua vifaa hivi kwa ajili ya maabara zetu, badala ya kusubiria wadau na sisi tuna fedha katika manispaa zetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali imeendelea kufanya jitihada za makusudi, ili kupunguza pengo la upungufu wa Walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari, lakini mikataba ya ajira kwa watumishi wa umma; tayari Serikali ilishaandaa modal ya mikataba kwa halmashauri zetu kuajiri watumishi kwa mkataba kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.

Kwa hiyo, kibali kilishatolewa na watumishi wote wa sekta ya afya, sekta ya elimu na wengine ambao halmashauri kwa uwezo wa mapato ya ndani wana uwezo wa kuwalipa mishahara kwa mikataba, kibali kilishatolewa na tunatia shime kwamba, waendelee kutumia fedha za mapato ya ndani kuajiri watumishi kwa ajili ya kupunguza pengo la upungufu wa watumishi hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa vya sayansi kwa shule za sekondari, nalo linafanana na jibu langu la kwanza kwamba, mapato ya ndani ni sehemu ya fedha za Serikali kwa hiyo, kazi yake ni pamoja na kutatua changamoto zikiwemo za upungufu wa vifaa vya sayansi katika shule zetu. Kwa hiyo, lazima halmashauri zitenge fedha hizo ili kupunguza mapengo ya vifaa hivyo. Nakushukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu mimi ni, kule Temeke Kata ya Sandali, kuna jengo kubwa sana ambalo mmelijenga la zimamoto, lakini mpaka sasa halijamaliziwa wala hakuna vifaa vyovyote ambavyo vimeingizwa kwa ajili ya zimamoto.

Je, ni lini sasa vifaa hivi pamoja na jingo lile litamalizika kwa ajili ye Serikali yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nalifahamu amelizungumzia suala hilo la eneo la Mchicha majuzi, tutalipa kipaumbele kwa interest ya watu wa Dar es Salaam, uchumi wao na shughuli nyingi za kiviwanda zinazotekelezwa ili kuwawezesha Fire kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nina swali dogo la nyongeza kuhusiana na barabara inayotoka Mbagala kuelekea Temeke kutokea Kilungule - Mbagala kupitia Buza Kwa Mpalange; ni lini sasa itakamilisha ile lami? Kwa sababu wananchi wanapiga kelele sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zetu nyingi za TANROADS na TARURA zinaingiliana. Lakini nitumie tu nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuzijenga barabara zote kwa kiwango cha lami na kwa kuwa barabara zimeshaanza kujengwa, tunamhakikishia kwamba Serikali itazikamilisha hizo barabara, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itarekebisha au kupunguza bei ya huduma ya upasuaji hasa ya uzazi katika hospitali za rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha inatoa huduma ambazo zinaendana na gharama kwa maana ya kupunguza gharama za matibabu na hasa eneo la upasuaji. Katika hospitali za Rufaa za Mikoa, bado gharama za upasuaji ni changamoto na tumekubaliana na Wizara ya Afya, pia katika maeneo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Vituo vya Afya na hospitali za Halmashauri, bado gharama za upasuaji ni kubwa. Kwa hiyo, tunapitia lakini baada ya muda tutatoa gharama ambazo zitakuwa zinafikika kirahisi kwa wananchi wetu. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ili kuepusha hii migogoro: Je, ni lini sasa Serikali itaweza kwenda kuweka mipaka halisi ya ile sehemu ili tuendelee na shule kwa sababu mgogoro huu umekuwa ukijirudia mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nawaagiza Halmashauri ya Temeke kwamba baada ya rufaa hii kwisha, mara moja waanze mchakato wa kuweka mipaka halisi ili watu wasiende kuvamia hilo eneo. Kwa hiyo, mchakato uanze mara moja kuanzia sasa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana swali langu dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na magari mengi ambayo mmeyatuma yatakuja kwa awamu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha za kutengeneza magari yaliyopo ambayo ni mengi tunayaona yapo katika vituo vingi vya Polisi ni mabovu. Sasa ni wakati mzuri labda muweze kutenga fedha ili tuweze kutengeneza haya yaliyopo tukisubiri hayo mageni, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja yake ni ya msingi lakini nimhakikishie kwamba tumekuwa tukifanya hivyo na hata ndani ya Jeshi la Polisi tuna kitengo maalum kwa ajili ya matengenezo ya magari ya Polisi yale ambayo yanaweza kutengenezeka tunafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tunafikiria kuja na mpango mwingine ambao utasaidia sana kuweza kutatua changamoto ya ubovu wa magari, nadhani wakati tutakapokuja kuwasilisha bajeti yetu hapa tutakuwa na nafasi pana zaidi ya kuweza kufafanua, lakini nimpongeze kwa wazo lake ni zuri na tunaendelea kulifanyia kazi na tutazidi kuliboresha zaidi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu, ni lini sasa kituo cha afya kinachoitwa Malawi kilichopo Yombo Vituka kitapata maji? Tumepata vifaa vizuri sana vya ndani ya hospitali lakini maji tunayotumia ni ya visima, leo na tuko mjini.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoa huduma ya maji katika maeneo kama ya hospitali, shule ni moja ya vipaumbele vyetu.

Kwa hiyo maeneo haya ambayo bado yanatumia maji ya visima tunatoa kipaumbele na tutahakikisha kwenye kituo cha afya tutapeleka maji safi na salama bombani kwa lengo la kuona kwamba wanaendelea kuishi kwenye karne ya mama Samia kwa sababu Serikali ya Mama Samia imeweza kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya maji.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali, ni lini sasa barabara inayotoka Chang’ombe kupitia DUCE mpaka Mgulani mtamalizia, kwa sababu sasa hivi malori ni mengi sana ambayo yanapeleka vifaa viwandani na njia haipitiki sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, labda tu nichukue nafasi hii kumuhimiza mkandarisi lakini pia na Meneja wa TANROADS kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilishwa haraka. Mheshimiwa Mbunge kama kutakuwa na changamoto ya ziada naomba tuonane nae ili tuweze kutatua hiyo changamoto kama ipo kwa upande usimamizi ama kwa mkandarasi mwenyewe. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na yote hayo utaona kwamba Hospitali ya Temeke sasa hivi ni hospitali ya Kimkoa. Kwa nini, sasa basi isiwe muhimu kituo hiki cha afya cha Malawi kipandishwe nakuwa Hospitali ya Temeke kwa sababu ile ya Temeke ni ya Kimkoa sasa hivi?

Swali la pili; Je, ni lini sasa Serikali itatutengea fedha ili tuweze kujenga mochwari katika kituo hiki cha Malawi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dorothy Kilave kwa namna ambavyo anawasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Temeke, nimhakikishie kwamba katika utaratibu ambao Serikali inaendelea kuufanya kila Halmashauri lazima iwe na hospitali ya Halmashauri, ni kweli kwamba hospitali ya Temeke ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa hiyo taratibu zitafanyika kufanya tathmini ya kituo cha afya cha Malawi kama eneo linatosheleza ili miuondombinu iongezwe ili baadaye iweze kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Halmashauri ya Temeke.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na jengo la mochwari tumeelekeza Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ianze kutenga fedha kwenye mapato ya ndani, ili ijenge jengo la kuhifadhia maiti na huduma hiyo iweze kuwa bora kwa wananchi wa Temeke.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, siko mbali sana na swali alilouliza mtu wa Mbagala kwa sababu kata ulizozitaja ndiyo mtandao huo huo wa Kata ya Buza, Makangarawe, Sandali na Vituka. Tunaomba na sisi maji haya yaweze kusambazwa kule kwetu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba niseme nimepopkea, maji yatafika.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nilitaka kujua ni mpango upi wa kupunguza kabisa gharama hasa za mama mjamzito anapojifungua kwa operesheni, ambapo Temeke tunalipa laki mbili kwa operesheni na Vituo vya Afya ni shilingi laki moja; je, mpango huo ukoje wa kupunguza kabisa gharama hii?

Swali la pili; je, kuna mkakakti gani wa kufanya ili sasa Serikali itoe vifaa vile ambavyo akina mama tunapokwenda kujifungua tunaambiwa tununue pamba viwembe vile na kadhalika.

Je, Serikali ina mpango mkakati gani sasa wa kuweka vile vifaa ndani ya hospitali zote ili tusiweze kununua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala haya kwa ukaribu kwenye Jimbo lake. Niseme tu kwamba suala ni la kisera kwamba mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano hawatakiwi kulipishwa. Ninaomba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa tuweze kushirikiana pamoja kusimamia hili takwa la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es salaam kwa kweli nilitembea kwenye baadhi ya vituo vya afya na hospitali za Wilaya nilichogundua ni kwamba, unaweza ukakuta Kituo cha Afya kinapata wagonjwa wengi kuliko hata baadhi ya hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, wakati mwingine mgao wanaoupata MSD unakuwa mdogo kiasi kwamba wanaishiwa mapema kulingana na idadi ya watu, hata kwa mwaka ni zaidi ya 160,000 watoto wanazaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Kwamba mgao wanaoupata MSD ni mdogo ukilinganisha na idadi ya watu, kwa hiyo tutakwenda sisi kama MSD kufanya kuhakikisha inatolewa mgao wa dawa na vifaa kulingana na idadi ya watu na siyo kuangalia kituo, aidha ni kituo cha afya au na ku-generalize.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu mkakati ndiyo huo, kwamba tukiweza kwa Dar es Salaam ambapo unakuta kituo cha afya kinapata wagonjwa kuliko hata baadhi ya Hospitali za Wilaya sehemu nyingine, tukienda kuwapa vifaa kulingana na idadi ya wagonjwa badala ya kuangalia ni status gani hospitali inayo, maana yake hawatakuwa tena na huo upungufu na pale MSD zimenunuliwa kit za kutosha kwa ajili ya akina mama kujifungua. Hivyo hilo tatizo litaenda kuisha, nafikiri shida kwako ni idadi ya watu kwa hiyo kinachopelekwa kinakuwa kidogo sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, mimi nina swali moja tu; kuna upotevu mkubwa sana wa maji Mkoa wa Dar es Salaam hasa kwenye Jimbo la Temeke, nadhani mabomba yale ni chakavu na ya siku nyingi.

Je, mna mkakati gani sasa wa kubadilisha yale mabomba kuweka mabomba mapya ili tusipate taabu ya maji tena?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Ni kweli moja ya changamoto kubwa juu ya miradi ni upotevu wa maji na tumetoa maelekezo mahususi juu ya kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga miundombinu mipya ili kuhakikisha upotevu huu unakuwa katika standard.

Kwa hiyo, nataka nimhakikishie na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na DAWASA katika kuhakikisha tunakarabati na kujenga miundombinu mipya ili upotevu huu usiendelee na wananchi wahakikishe wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Sambamba na nyumba za Walimu Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga ofisi za Walimu au kukarabati ofisi zilizopo kwa ajili ya Walimu na kuweka samani zake ndani ya ofisi hizi, hasa katika Jimbo letu la Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama tulivyojibu kwenye upande wa nyumba za Walimu sasa hivi moja ya mkakati wetu mkubwa ni kuhakikisha kila tunapokenga madarasa tunaweka na ofisi za Walimu, kwa hiyo huo ndio mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba walimu wanakuwa na maeneo mazuri ya kukaa ambayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku. Hivyo, hilo lipo na limezingatiwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza: Je, ni lini sasa Serikali itamaliza ujenzi wa barabara ya Chang’ombe inayoanzia mataa ya Chang’ombe kuelekea barabara ya Kilwa; ukilinganisha kwamba, sasa hivi kuna foleni kubwa sana na ile barabara ni kubwa na hasa ukizingatia wananchi wengi wanapita; na hasa kipindi ambacho kuna michezo kwenye uwanja ule wa Taifa, hasa Simba na Yanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Chang’ombe kwenda Kilwa ni sehemu ya barabara za BRT Awamu ya Pili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, naye atakuwa shahidi kwamba kasi imeongezeka sana. Tuna uhakika, kwa mujibu wa kazi anavyoendelea mkandarasi huyu, barabara hii itakamilishwa kama tulivyokubaliananaye kwenye mkataba, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa mtaweza kufunga transformer mliyokuwa mmeahidi tangu Desemba ili kupunguza adha ya kukatikatika umeme kwenye Jimbo la Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, transformer iliyotakiwa kuwekwa katika eneo la Temeke ipo katika mchakato wa manunuzi kwa sababu tayari pesa ilishatengwa na uamuzi ulishafanyika, hivyo katika miezi miwili au mitatu inayokuja tunaamini taratibu za manunuzi zitakuwa zimekamilika na transformer itafungwa kwa ajili ya kuongeza uwezo wa umeme katika maeneo hayo kuweza kuwahudumia wananchi wote.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kwamba Mahakama imetupilia mbali suala hili, lakini je, hamuoni sasa iko haja ya Serikali na wananchi tukaweza kukaa pamoja tukapata uelewa wa pamoja ili wajue kwamba kweli walilipwa?

Swali la pili; je, yale maegesho ni lini sasa pataanza kujengwa maana bado pako wazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy Kilave Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kukaa na wananchi hawa katika kujenga uelewa wa pamoja ili kuondoa sintofahamu ya baadhi ya wanaodai kufikiri kwamba hawajalipwa. Kwa hiyo nikuhakikishie kwamba tutapanga utaratibu wa kwenda kuonana na wadai hao ili tuweze kuwapa uelewa wa pamoja wajue kwamba tayari walikwisha lipwa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kujua lini ujenzi unaanza, naomba hili tulichukue kama Serikali tukalifanyie kazi tuweze kuona lini ujenzi huu unaanza, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa Serikali itajenga mortuary katika Kituo cha Malawi kilichopo Yombo Vituka Jimboni Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatvyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uwezo wa mapato ya ndani ya Manispaa ya Temeke, naelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuweka kipaumbele cha kujenga jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya cha Yombo Vituka, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara inayotoka Buza kwenda kuunganisha jimbo la Ukonga pamoja na Temeke?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kusaidiana na wenzetu wa TAMISEMI tutahakikisha kwamba hiyo barabara tunaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Uko ujenzi unaoendelea na TBA kule Temeke, tunaita Temeke quarter.

Je, Serikali mna mkakati gani wa kuwapatia nyumba wale ambao walikuwa wakiishi pale kabla ya ujenzi huu unao endelea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Temeke Mwisho na Temeke quarter kuna mradi unaendelea na mradi huu tutajenga majengo takribani saba ya ghorofa yatakayo kuwa na uwezo wa kubeba familia 1,008 na kwa maana hiyo sasa wale wote ambao watakuwa ni waathirika wa maeneo

hayo pia TBA tutaona ni namna gani ya kuwafanya hawa waishi katika maeneo hayo.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilikuwa kwenye swali hilo hilo. Mlihakikisha kwamba Halmashauri zetu zinanunua dawa kutoka kwenye hicho kiwanda, lakini naona NBS walipojenga hiki kiwanda ilikuwa ni makusudi maalum kabisa kwamba fedha hizi zirudi ndani ya shirika lile.

Je, sasa hamuoni ipo haja Serikali itoe mamlaka zaidi ili tuweze kununua dawa kutoka kwenye Manispaa zetu kutoka kwenye hiki kiwanda ili kiwanda hiki kiendelee kujiendesha kwa sababu sasa hivi naona kama kiwanda chenyewe hakipo tena? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, ukiona tumeomba shilingi bilioni 129.1 kwa maana tunaomba fedha maalumu kutoka Wizara ya Fedha, hiki ni kikao ambacho Waziri Mkuu mwenyewe amekisimamia na ameki-push ili haya mambo yatokee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, alikaa mwenyewe kikao na kuelekeza tulifanye hili na pia kwa maana ya ushauri wenu pia uandikwe waraka kuhakikisha kwenye CCHP za halmashauri inawekwa bajeti kwa ajili hiyo. Tukifanya hayo yote tutaenda kufakinikiwa.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, Serikali haioni uko umuhimu sasa wa kuweka majina ndani ya data base waliojitolea na wanaoendelea kujitolea ili wawe wa kwanza kuajiriwa wakati huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, hali ilivyo kwa sasa na miongozo iliyotolewa na Serikali inahifadhi majina ya watu wote wanaoshiriki michakato mbalimbali inayohusu ajira ndani ya database.

Mheshimiwa Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba database tuliyonayo sasa inaishi kwa mwaka mmoja, baada ya mwaka mmoja ili turuhusu watu wengine nao waweze kuingia, lakini wazo analolisema ni moja ya mabadiliko makubwa ambayo yanakuja kuletwa na huu mchakato ambao sasa unafanyika wa mabadiliko ya Sheria ya Utumishi, pia sera mbalimbali zilizopo ili kuweza kuweka mahitaji yote ya ajira katika chombo kimoja lakini mwongozo mmoja ambao utaweza kutoa nafasi kwa Watanzania wote. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini je, sasa Serikali haioni ipo haja ya visima vile ambavyo vilichukuliwa na DAWASA ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam viweze kurudishwa mikononi mwa wananchi, kwa sababu tangu vilipochukuliwa mpaka sasa hakuna marekebsho yoyote na ndiyo maana tunakosa maji mahali pengine kwa sababu visima vilikuwa ni vingi lakini DAWASA hawavifanyii kazi. Hivyo virudishwe kwa wananchi ili maji yaendelee kupatikana kulingana na hizi asilimia 30 mlizosema mpaka sasa yanapatikana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili je, lini Serikali sasa mtarekebisha au mtaweka mabomba, kwani yaliyopo ni chakavu a ya zamani sana ambapo sasa hivi yanatitirisha maji tu na ni upotevu tu wa maji kwa Serikali lakini sasa tuombe muweze kuyarekebisha na wananchi tuendelee kupata maji safi katika mabomba ya majumbani? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawilii ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, visima vilivyochukuliwa kurudishwa kwa wananachi, visima hivi vilichukuliwa kwa sababu za kiufundi. Sasa hivi namna ambavyo kwa mfano Wizara ya Afya inaweza kumiliki hospitali zake, nasi Wizara ya Maji tunahitaji kumiliki vyanzo hivi vya maji vyote ili viwe chini ya uangalizi wa wataalam wetu. Kwa hiyo, cha kufanya hapa hatutavirudisha kwa wananchi bali tutaongeza nguvu kuhakikisha visima hivi vinakwenda kutumika na kuongeza usambazaji wa maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubadili mabomba chakavu tayari hili lipo kwenye mkakati wa mwaka huu wa fedha 2023/2024 utaona Mheshimiwa Mbunge kazi huko namna ambavyo vijana wanachakarika. Nimpongeze sana CEO wa DAWASA ameingia kwa kasi na watendaji wake wote wanafanya kazi kwa kasi. Wiki iliyopita nimefanya ziara pamoja na DAWASA maeneo haya yote ninayozungumzia Mheshimiwa Kilave, nimeweza kuyapitia.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu la kwanza; kwa kuwa fedha za ujenzi zilitengwa tangu 2023/2024 na kwa kuwa eneo hakuna;

Je, ni kwa nini hizo fedha zisitumike sasa kufidia eneo la kujenga stendi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kutokana na umuhimu wa stendi hiyo juu ya Serikali pamoja na wananchi wa Temeke;

Je, haioni sasa kuna umuhimu wa kuwa na sababu ya kuipa fedha za miradi ya mikakati Halmashauri yetu ya Temeke ili kuendeleza ujenzi huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chaurembo; la kwanza, hili la mwaka wa fedha 2024/2025 hii ni fedha ambayo wameitenga. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, fedha hii bilioni mbili imetengwa katika mwaka wa fedha tunaoenda kuanza, yaani July mwaka 2023/2024 sasa ni maamuzi yao wenyewe kupitia kikao chao cha finance na maamuzi ya halmashauri, kama wataweza kufanya fidia kutokana na fedha hii wanaweza wakalipa ili wa-secure ili lile eneo liwe ni la kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali la pili, umuhimu wa Serikali kuipa fedha, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Tunatambua kwamba ni jambo la muhimu sana kuwa na maeneo ya miradi ya kimkakati hapa nchini ili kuziwezesha halmashauri zetu kuongeza uwezo wa kipato. Tutawapatia fedha wakiandika andiko na kulileta Ofisi ya Rais TAMISEMI na kisha sisi kulichakata na kulipeleka katika Wizara ya Fedha ambapo ndio wanaotoa fedha hizi. Kwa hiyo niwaatoe hofu wana Temeke na wana Mbagala kwamba pale tutakapo pokea andiko lao basi tutatenga fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa stendi hii.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi nina swali moja.

Je, Serikali hamuoni umuhimu wa kumaliza utengenezaji wa umeme katika Jimbo la Temeke hasa Jimbo la Mjini, ukizingatia kuna wakati umeme unakatika kwenye viwanja hasa katika mechi hizi za Kimataifa, ni lini sasa mtarekebisha umeme huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave ni la msingi kabisa. Tunayo nia ya dhati kama Serikali kumaliza tatizo la kukatika umeme Tanzania nzima. Tunashukuru kwamba juzi mmepitisha bajeti ya Wizara ya Nishati yenye fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha tunaondokana na tatizo hili. Tuwahakikishie litakwisha kupitia mradi wetu wa gridi imara tutaendelea kuimarisha maeneo mengi ambayo yana changamoto kubwa ya ukatikaji wa umeme ikiwemo Jimbo la Temeke. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je ni lini Serikali sasa itamaliza nyumba za askari eneo la Barracks Kilwa Road ndani ya Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Vituo vyote vya Polisi ikiwa vya Wilaya ikiwa vya Mikoa itahakikisha kwamba vinakamilika, lengo na madhumuni wananchi wajue sasa wapi wanakwenda kupeleka changamoto zao, kwa sababu tumegundua bado kuna baaadhi ya maeneo yakiwemo wilaya na maeneo mengine bado hayajapata Vituo vya Polisi. Kwa hiyo nimwambie tu Mheshimiwa kwamba tutahakikisha kwamba Kituo cha Polisi kinakuja na fedha zitakapopatikana, tutahakikisha kwamba tunampa kipaumbele kwa ajili ya kupata hicho Kituo cha Polisi.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini je, haioni iko haja ya kufanya nguvu zaidi kwa ajili ya shule hizi za sekondari ambazo ni kongwe hasa katika Jimbo langu la Temeke, Shule ya Kibasila?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali haioni iko haja ya kuongeza pia nguvu katika shule ambazo zilianza kujenga ofisi hizi lakini mpaka sasa hazijaendelezwa mfano kwangu, shule inaitwa Ally Hassan Mwinyi ambayo ni jina kubwa sana. Je, ni lini sasa Serikali itaweza kumalizia ofisi hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dororth Kilave, Mbunge wa Temeke, kwanza kuhusu kuongeza jitihada ya Serikali kwa ajili ya kukarabati na kujenga shule hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge na wana-Temeke kwa ujumla kwamba, Serikali hivi karibuni imepeleka shilingi milioni 700 katika Shule ya Sekondari Kibasila kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na madarasa, likiwemo jengo la utawala katika shule ile. Kwa hiyo, ni jitihada kubwa za Serikali hii ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya shule za sekondari na shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali la pili kuhusu shule zilizoanza ujenzi wa majengo haya ya utawala zenyewe, ikiwemo shule ya Ali Hassan Mwinyi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge na kuona ni namna gani Serikali inaweka jitihada kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo hili la utawala katika shule hii yenye jina la Rais wetu wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Dkt. Ali Hassan Mwinyi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana swali langu ni dogo tu kusiana kama lililokuwa Mbagala. Iko barabara inayopita ndani ya Jimbo la Temeke, sawa sawa na sambamba na Reli ya TAZARA ambayo nayo katika mvua hizi imeharibika sana.

Je, Serikali mtatusaidiaje changamoto ya TAZARA pamoja na Manispaa yetu ili waturuhusu hata kuitengeneza tu kwa changarawe au hata kuweka lami kidogo kwa sababu ni Barabara ambayo inatumika sana kwa wananchi wa Temeke.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii alimradi inapita kandokando mwa reli kuna sheria ambazo zinalinda ile mipaka ya reli inakopita. Hivyo tutakaa na wenzetu wa TAZARA kuona ni namna gani wataruhusu ipitike kwa muda kwa sababu haitoweza kutengenezewa miundombinu kama ya zege na lami kwa muda ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi na TAZARA wakiridhia basi tutaona ni namna gani Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam anaweza akatengea fedha kwa ajili ya kuweza kuweka changarawe.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana swali langu ni dogo tu kusiana kama lililokuwa Mbagala. Iko barabara inayopita ndani ya Jimbo la Temeke, sawa sawa na sambamba na Reli ya TAZARA ambayo nayo katika mvua hizi imeharibika sana.

Je, Serikali mtatusaidiaje changamoto ya TAZARA pamoja na Manispaa yetu ili waturuhusu hata kuitengeneza tu kwa changarawe au hata kuweka lami kidogo kwa sababu ni Barabara ambayo inatumika sana kwa wananchi wa Temeke.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii alimradi inapita kandokando mwa reli kuna sheria ambazo zinalinda ile mipaka ya reli inakopita. Hivyo tutakaa na wenzetu wa TAZARA kuona ni namna gani wataruhusu ipitike kwa muda kwa sababu haitoweza kutengenezewa miundombinu kama ya zege na lami kwa muda ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi na TAZARA wakiridhia basi tutaona ni namna gani Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam anaweza akatengea fedha kwa ajili ya kuweza kuweka changarawe.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, mimi leo nauliza je, ni lini sasa mtatupa jibu la uhakika la kutokukatika-katika umeme kwenye Jimbo letu la Temeke? Kwa sababu, mwaka 2021 hapa mlituambia mwezi wa Disemba umeme utakuwa sawasawa, mwaka 2022 mwezi Aprili utakuwa sawasawa, sasa ni mwaka 2023, je, ni lini? Tunaomba jibu la uhakika umeme kutokukatika-katika Temeke.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sababu za kukatika umeme kwenye maeneo mbalimbali zinatofautiana. Wako ambao umeme unakatika kwa sababu miundombinu yao imepita kwenye maeneo ya mapori na inasongwa sana na miti. Wako wenye maeneo mengine umeme unakatika sana kwa sababu wako kwenye maeneo yenye radi na mvua kali kwa hiyo, zile radi zinaathiri vile vifaa.

Mheshimiwa Spika, yako maeneo mengine kama ya mjini ambako miundombinu imezidiwa na matumizi ya wananchi, lakini pia yako mambo mengine shughuli za kibinadamu za kugonga nguzo kwa magari na vitu kama hivyo vinavyosababisha matatizo hayo yatokee.

Nimuahidi Mheshimiwa Kilave kwamba kwenye mradi wetu wa Gridi Imara kwanza tunaongeza uwezo wa mitambo yetu wa kupeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali, na yeye ni shahidi kwamba kwenye maeneo ya Temeke tumeanza kupitisha miundombinu chini kwa maana ya underground ili tupunguze zile habari za malori na magari mengine kugonga zile nguzo.

Mheshimiwa Spika, sasa mradi huu wa Gridi Imara pamoja na miradi mingine ambayo tunayo ambayo tayari umeshaona inatekelezwa tunatarajia itakapokamilika katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili ijayo maeneo mengi sana matatizo ya kukatika kwa umeme yatakuwa yamekwisha, lakini yapo matatizo mengine madogo madogo ya transfoma imezidiwa kwa sababu wakazi wameongezeka kama maeneo ya Kariakoo na vitu kama hivyo, tunavifanyia kazi kwa kadri vinavyotokea. Tunaomba tuendelee kushirikiana kupeana taarifa pale changamoto zinapotokea ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, swali langu ni dogo sana lakini la uhakika. Je, ni lini Serikali itakipandisha hadhi Kituo cha Polisi cha Tandika ambacho tunatumia kata kama tano kwenda pale na sasa unaona kama kuna uhalifu mkubwa sana upande ule. Je, ni lini sasa mtakipandisha hadhi hata kipate class B ili tuweze kuona kwamba kazi nzuri inafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia masuala ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam mara kadhaa amenisumbua kidogo kuhusu hata njia inayokwenda Mbagala kupitia eneo la polisi na tumeshakubaliana ile njia itafunguliwa Mheshimiwa Mbunge lakini kuhusu ili la kupandisha hadhi kwa kupitia Bunge lako Tukufu namuelekeza Kamishna Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Uongozi wa Polisi wa Mikoa ya Kipolisi Dar es Salaam kufuatilia, kupima na kufanya tathimini ya mahitaji ya kupandisha hadhi kituo hiki kama sababu alizozisema Mheshimiwa Mbunge zipo basi waone uwezekano wa kukipandisha ili kikidhi mahitaji ya eneo la Tandika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali moja nyumba za bara pale Kilwa Road. Kuna maghorofa yalitangulia kujengwa sasa sijui ndio yameishia pale pale na wale wengine bado wako kwenye zile nyumba ambazo Kilwa Road Barax. Maghorofa yale yamejengwa vizuri lakini katikati pana nafasi sijui ndio mwisho pale maana yake zile nyumba sasa ni ndogo sana na zinavuja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Dorothy Kilave wa Temeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kota za Askari kule Temeke Kilwa Road unaendelea na kama pana dosari zozote ambazo zimeoneshwa na Mbunge kama maeneo mengine yanavuja tutamwelekeza IGP ili kumsimamia mkandarasi aweze kusimamia mjenzi ahakikishe kwamba viwango vilivyowekwa vinazingatiwa ili kuondoa hizi dosari ambazo zimeonekana.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Zahanati za Tandika pamoja na Mibulani zitaanza kufanya kazi kwa sababu majengo yako tayari na kila kitu na yameanza kupata ufa, tusiipoteze Serikali fedha zile. Je, ni lini zitaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vituo vyote vilivyokamilika vinatakiwa vianze kutoa huduma mapema iwezekanavyo na natoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuhakikisha zahanati au vituo hivi vya Tandika na Mibulani vinasajiliwa haraka iwezekanavyo na vinaanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyotarajiwa.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na majanga makubwa ya Mkoa wa Dar es Salaam hasa kuunguliwa kwa masoko.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza magari ya zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kweli kwamba Jiji la Dar es Salaam linaongoza katika majanga haya ambayo tumejiridhisha kwamba mengine ni uzembe, lakini mengine ni miundombinu ambayo husababisha athari za moto. Kwa kuzingatia hilo ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu tayari tuna magari matatu yaliyokuwa yanatengenezwa na kiwanda chetu cha NYUMBU yatagawiwa kwenye mikoa yenye changamoto kubwa likiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mwaka ujao tunayo bajeti ya zaidi ya Euro milioni 4.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya magari na maeneo yote yenye changamoto yatagawiwa vifaa hivyo.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa kuwa Jimbo letu la Temeke limepata kilometa 53.10; je, huoni haja ya Serikali kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia mapema ili kweli Julai hii hizo barabara zianze kujengwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lako la msingi umenijibu kwamba kuna kata ambazo tayari zimeshafanyiwa ukarabati na barabara hizo zinatumika. Niombe kusema kwamba katika Kata ya Chang’ombe, Sambali, Keko, Azimio, Temeke 14 na Miburani sijapata kuona hizo barabara.

Je, uko tayari kuandamana na mimi twende tukazione hizo barabara katika jibu lako la msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mapendekezo hayo yameshapelekwa na yapo Wizara ya Fedha, na mazungumzo yanaendelea, ni imani yangu kwamba haya mazungumzo yataisha kama ambavyo tulikubaliana mwezi wa saba ili sasa huu mradi wa kwa Halmashauri ya Temeke na Jiji la Dar es Salaam uweze kufanya kazi. Nimhakikishie niko tayari tunaweza tukaongoza na yeye siku ya Jumamosi, weekend hii kwenda kuziona barabara hizo.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea fedha za kujenga chumba cha maiti na jengo la emergence katika Kituo cha Malawi katika Kata ya Vituka ukizingia sasa Temeke hospitali ni ya kimkoa na si kituo tena.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba huduma zote za msingi zinapatikana katika maeneo ya vituo vya huduma ikiwemo majengo haya ya mortuary na majengo ya dharura. Ndiyo maana mwaka 2022 majengo ya dharura zaidi ya 80 yamejengwa, majengo ya ICU yamejengwa.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutafanya tathimini ya majengo hayo tujue gharama zake lakini pia tuone mapato ya ndani yatachangia kiasi gani na Serikali kuu itachangia kiasi gani. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, kwa kuniona. Naomba kuuliza swali. Je, ratiba ya mgawo wa umeme katika Jimbo letu la Temeke umekuwa ni wa muda mrefu sana na ratiba yake haifuatilii kadiri ya ratiba zinavyokuja kwamba, umeme utakatika kuanzia muda fulani mpaka muda fulani, sasa umekuwa ni wa muda mrefu sana. Kuanzia jana mpaka leo saa hizi Temeke hatuna umeme, je, una tamko gani Waziri, ili kule Temeke waweze kutuletea umeme kulingana na mgawo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, kidogo tumetengemaa kwenye suala la upatikanaji wa umeme, na kwa Mkoa wa Dar es Salaam tunafahamu maeneo mengi kwa sasahivi yanaweza yakapitisha hata siku mbili mpaka tatu bila kukatika kwa umeme. Kwa hili ambalo ambalo ameniambia Mheshimiwa Mbunge inaonekana ni suala ambalo ni specific, yaani ni mahususi. Naomba nilifuatilie, Mheshimiwa Mbunge, nikitoka hapa na nitakupatia majibu, ahsante. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Je, ni lini sasa Serikali mtaendeleza kujenga nyumba za askari pale Kilwa Road Barracks? Kwa sababu majengo mengine yamejengwa lakini mengine bado hayajaendelezwa. Naomba kujua sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tunatambua uchakavu wa baadhi ya majengo ya Makazi Jeshi la Polisi pale Kilwa Barracks. Ni mpango wa Serikali kama ambavyo tumeanza kujenga zile flats ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziona, dhamira ya Serikali ni kuendelea hatua kwa hatua kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, umesikia ikielezwa hapa kwamba tumefanya Dar es Salaam lakini maeneo mengine bado yanalia. Katika hali ya kutaka ku-balance kadri tutakavyofikiwa basi Dar es Salaam tutaiendeleza kadhalika pia.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam miundombinu yake ya maji ni ya muda mrefu sana, kwa sababu tulipata maji muda mrefu kabla ya Mikoa yote. Sasa hivi miundombinu ile ni mibovu na inamwaga maji mengi hasa katika Jimbo letu la Temeke.

Je, Serikali mna mkakati gani wa kuelekeza tena upya miundombinu ya maji katika Mkoa wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dorothy Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna baadhi ya maeneo ya Temeke yana changamoto ya mabomba kupasuka kwa uchakavu na maji sasa yamekuwa mengi kwa sababu ni miradi mikubwa iliyotekelezwa na DAWASA, hivyo nipende kukutoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeanza utekelezaji nimeshafuatilia hili maeneo ya Tandika, Tandale maeneo ya Wailess na Temeke penyewe tayari wameanza kubadilisha yale mabomba yaliyochakaa.

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo bado maji yanaendelea kuvuja tunaendelea kufanyia kazi na kadri tutakavyopata fedha tunakuja kukamilisha maeneo yote ambayo maji yanavuja. Hili siyo tu kwa Temeke Waheshimiwa Wabunge niseme Mikoa yote, Majimbo yote tumetoa maelekezo kuhakikisha maeneo ambayo maji sasa yamekuwa ni mengi na mabomba yamechakaa yanashindwa kuhimili presha ya maji haya, tunakuja kufanyia ukarabati.(Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Gereza la Keko lipo katikati ya makazi ya watu katika Jimbo la Temeke na linaleta migogoro sana kwa baadhi ya nyumba ambazo zinazunguka gereza hilo.

Je, nini mkakati wa Serikali kulihamisha gereza lile kutoka Keko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Gereza la Keko kama lilivyo kwa sasa Dar es Salaam limezungukwa sana na wananchi na tunatambua hizo changamoto anazozisema. Kwa wakati huu ambapo bado Wilaya ya Temeke halijapata eneo lingine la kulihamishia gereza hilo na hivyo kuliingiza kwenye mpango wetu wa ujenzi wa gereza jipya. Niwaombe wananchi Jeshi la Magereza ni sehemu ya chombo cha wananchi kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kikatiba hayo ya kuhifadhi wenzetu wanao tuhumiwa na kuhifadhiwa kule kwa makosa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba waishi nao kwa mahusiano mema kabla hatua ya kulihamisha gereza hilo kuliweka eneo la mbali kabisa na makazi ya wananchi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni ipi kauli ya Serikali kuhusiana na wananchi wanaoishi katika nyumba za Keko Flats ambao ni takriban miaka saba sasa waliambiwa kuna mwekezaji na wamekataliwa kulipa kodi hawapeleki National Housing, wako katika dilemma. Sasa sijui majibu ya Serikali yakoje, mwekezaji yupo au waendelee kukaa bila kulipa kodi, Je wakija kuwaambia waanze kulipa watadaiwa kuazia hiyo miaka saba iliyopita? Naomba majibu ya Serikali.
SPIKA: Naona maswali yako yamekuwa mengi, uliza moja kati ya hayo.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ni upi mkakati wa Serikali kuhusiana na wananchi wanaoishi katika eneo lile la Keko National Housing.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Kilave ni jirani yangu swali hili nitawasiliana na uongozi wa National Housing na nitampa majibu kwa haraka sana kwa sababu linahitaji details na nitampa majibu yake leo hii.