Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Deogratius John Ndejembi (197 total)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba kuwa wanufaika wa TASAF ni wananchi wenye uwezo badala ya kaya maskini:-

Je, hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nami ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa mema yote ambayo anaendelea kutujalia hadi kufika siku hii ya leo. Pili, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika ofisi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Mpango wa TASAF ni kuzinusuru kaya maskini katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini ulianza rasmi mwaka 2000 hadi 2005; awamu ya pili ilianza mwaka 2005 hadi 2012; na awamu ya tatu, kipindi cha kwanza ilianza kutekelezwa mwaka 2013 hadi Desemba, 2019; na kipindi cha pili cha awamu ya tatu kilianza Februari, 2020 hadi Septemba, 2023 ambapo jumla ya kaya maskini 1,100,000 zimeweza kuandikishwa na wanufaika kunyanyua hali yao ya kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kagera jumla ya kaya maskini 68,915 zimeandikishwa na kuingizwa kwenye Mpango huu wa TASAF. Katika utekelezaji wa kipindi cha kwanza walengwa wamepokea ruzuku kwa takribani miaka mitano. Hali hii imechangia walengwa hawa kuwa na miradi mikubwa ya uzalishaji mali kama mashamba, mifugo na shughuli za ujasiriamali ambazo zimewawezesha wao kuboresha maisha na kujiimarisha kiuchumi. Walengwa kama hao ndio wanalalamikiwa kuwa TASAF inasaidia watu wenye uwezo badala ya kaya maskini. Ukweli ni kwamba kaya hizo ziliingia kwenye mpango zikiwa na hali duni na ziliweza kujikwamua kiuchumi.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya kuongeza watumishi 403 wa afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka ya 2015 hadi 2020, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 14,479 wa kada mbalimbali za afya. Katika Mwaka wa Fedha 2020/ 2021 Serikali inatarajia kuanza kuajiri watumishi 75 wa kada mbalimbali za afya kwenye Wilaya ya Hai kwa ajili ya hospitali ya wilaya moja, vituo vya afya sita na zahanati 28 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. DENNIS L. LONDO Aliuliza: -

(a) Je, ni Watumishi wangapi wamerejeshwa kazini baada ya kuondolewa kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti feki na Wafanyakazi hewa?

(b) Je, ni Watumishi wangapi waliorejeshwa kazini wamelipwa stahiki zao kama mishahara ambayo hawakupata kutokana na kuondolewa kazini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia ofisi yangu imewarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara jumla ya watumishi 4,380 walioondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti vya elimu na watumishi hewa. Idadi hii inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa wapatao 3,114.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwarejesha watumishi tajwa, Serikali pia ilitoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia mwezi Disemba, 2020 ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya Kidato cha Nne au kubainika kughushi vyeti. Pia, mnamo tarehe 07 Mei, 2021 Serikali kupitia ofisi yangu ilitoa maelekezo na utaratibu kwa waajiri kuhusu namna ya kushughulikia hatima za ajira za watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne pamoja na malipo ya stahiki zao. Napenda kuwakumbusha waajiri wote kukamilisha utekelezaji wa maelekezo hayo kwa haraka na kwa usahihi ili watumishi husika waweze kupata haki zao mapema.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kusisitiza kwamba msamaha uliotolewa unawahusu watumishi wale tu walioajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004 bila sifa ya elimu ya Kidato cha Nne lakini baadaye wakajipatia sifa za kuajiriwa na haiwahusu watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi au waliotoa taarifa za uwongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi. Utaratibu wa kushughulikia watumishi waliobainika kughushi vyeti ulishatolewa awali na Serikali na watumishi wote waliobainika kughushi vyeti hawastahili kurudishwa kazini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imelipa madai ya mishahara ya jumla ya shilingi 2,613,978,000 kwa watumishi 1,643 waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa. Uhakiki wa madai yaliyobaki unaendelea na yataendelea kulipwa kwa kadri yanavyohakikiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JANEJELLY J. NTANTE Aliuliza:-

Serikali inawahimiza watumishi kujiendeleza kielimu, lakini baada ya kuhitimu wanapoomba kubadilisha kada huteremshwa vyeo na mishahara:-

Je, Serikali haioni ipo haja ya kuwaacha na mishahara yao ili kujiendeleza isiwe adhabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntante, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeendelea kutoa Miongozo mbalimbali kuhusu namna ya kuwabadilisha kada/kazi watumishi waliojiendeleza kitaaluma. Aidha, Serikali inatambua umuhimu wa watumishi kubadilishwa na kupangiwa kazi kulingana na taaluma zao. Hivyo, kupitia Waraka wa Barua Kumb. Na. C/AC.44/45/01/ A/83 ya tarehe 01 Desemba, 2009, Serikali iliweka utaratibu wa kufuata wakati wa kuwabadilisha kada watumishi waliojiendeleza kitaaluma ambapo kuna aina mbili za kubadilishwa kada bila kuathiri watumishi waliomo katika kada hizo.

(i) Kumbadilisha kazi mtumishi aliyejiendeleza na kupata sifa zinazompandisha hadhi kitaaluma, mfano Afisa Kilimo Msaidizi kuwa Afisa Kilimo. Watumishi wa aina hii hubadilishwa hadhi na kuingizwa katika kada mpya kwa kuzingatia cheo cha kuanzia cha kada mpya. Iwapo vyeo walivyokuwa navyo vilikuwa na mishahara mikubwa kuliko mishahara ya cheo walichopewa baada ya kubadilishwa, huombewa kibali cha kuendelea kulipwa mishahara waliyokuwa wakilipwa kama mishahara binafsi hadi watakapopandishwa vyeo vyenye mshahara mkubwa kuliko mishahara binafsi. Utaratibu huu pia unawahusu watumishi wa kada saidizi ambao taaluma walizo nazo hazina vyuo vinavyotoa Astashahada/Stashahada au Shahada katika fani wanazofanyia kazi mfano Walinzi na Wasaidizi wa Ofisi.

(ii) Aina ya pili ni kuwabadilisha kazi watumishi waliojiendeleza katika fani nyingine tofauti na zile walizoajiriwa nazo kwa lengo la kukidhi matilaba ya kazi (job satisfaction) bila kuzingatia mahitaji ya mwajiri. Hawa hulazimika kubadilishwa kazi na kuingizwa katika cheo na ngazi ya mshahara wa cheo kipya na hawastahili mishahara binafsi kutokana na kulinda ukuu kazini na kuwajengea uzoefu wa kazi mpya ambazo wamezichagua wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu, Serikali inasititiza watumishi wa umma kujiendeleza katika kada walizoajiriwa nazo ili kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na kuwa wabobezi katika fani zao. Aidha, watumishi wa umma wanaaswa kupata ushauri kwa waajiri wao wanapotaka kujiendeleza kwenye fani tofauti na wanazofanyia kazi. Waajiri wanao wajibu wa kutenga nafasi za kuwabadilisha kada wale waliojiendeleza katika fani zao ili kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inatumika ipasavyo. Aidha, waajiri wahakikishe kuwa wanawashauri vizuri watumishi wao kabla ya kubadilishiwa kada/kazi watumishi waliojiendeleza kwenye fani tofauti. Endapo kwa namna yoyote kuna suala ambalo lina mazingira tofauti na haya, mwajiri au mtumishi mwenyewe anaweza kuomba ufafanuzi kutoka katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wowote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Vitendo vya rushwa vimekithiri sana katika mchezo wa soka hapa nchini: -

Je, ni kwa kiasi gani Serikali inakabiliana na kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika sekta ya michezo hususan mchezo wa soka hali inayoathiri maendeleo ya mchezo huu kwa ujumla, lakini pia kuikosesha Serikali mapato.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TAKUKURU imekuwa ikikabiliana na vitendo vya rushwa kwenye mchezo wa soka kwa kufanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya viingilio katika mechi za mpira wa miguu. Matokeo ya uchambuzi huo yaliwezesha kubaini kwamba kuna mianya ya rushwa kwenye eneo hili ambapo baada ya kubana mianya hiyo mapato yaliongezeka hadi kufikia shilingi milioni 206 kwa watu 50,233 waliokata tiketi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mwezi Machi, 2019 ukilinganisha na mapato ya shilingi milioni 122 kwa watu 47,499 waliokata tiketi kwa mechi iliyochezwa Januari, 2019 kwenye uwanja huo.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya michezo nchini, mwaka 2016 TAKUKURU iliunda Timu Maalum ya Uchunguzi kufuatilia na kuchunguza vitendo vya rushwa katika michezo ambapo kesi tatu zimefunguliwa mahakamani na tuhuma saba zinaendelea kuchunguzwa. Aidha, semina zimetolewa kwa makundi mbalimbali ikiwemo Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (TAFCA), Waamuzi na Makamisaa wanaotumika katika michezo ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza pamoja na kufanya vikao na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu (TFF) kuhusu kuweka mikakati ya pamoja kuelimisha umma kupitia soka.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwataka TFF, wasimamizi wa soka na viwanja vya michezo waruhusu na kushirikiana na TAKUKURU kuweka matangazo ya kukemea rushwa kwenye soka na michezo kwa ujumla.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-

Vipo baadhi ya Vijiji vilivyoorodheshwa kwa ajili ya kufikiwa na miradi ya TASAF III Awamu ya Kwanza upande wa Zanzibar lakini bado havijafikiwa na mradi unaelekea mwisho:-

Je, Serikali inasemaje juu ya maeneo ambayo hayajafikiwa na Mradi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) naomba kujibu swali la Mhe. Maida Hammad Abdalla Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa TASAF haujafika mwisho na TASAF itafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba kaya zinazotambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango ni zile kaya maskini sana.

Mheshimiwa Spika, kipindi cha pili cha utekelezaji wa Mradi wa TASAF kimeanza baada ya uzinduzi uliofanyika tarehe 17 Februari, 2020. Zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya za walengwa katika Vijiji/Mitaa/Shehia 5,590 ambazo hazikufikiwa na mpango wakati wa kipindi cha kwanza kimeanza tarehe 19 Aprili mpaka tarehe 6 Mei, 2021 kwa mzunguko wa kwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar jumla ya Shehia 304 tayari zinanufaika na mpango wa TASAF. Hata hivyo, jumla ya Shehia 157 ambazo hazikuwa kwenye mpango zimeshaandikishwa na ifikapo mwezi Julai, 2021 Shehia hizo zitaanza kunufaika na Mpango wa TASAF.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwasisitiza viongozi katika Vijiji/Mitaa na Shehia zote kutoruhusu vitendo vya upendeleo na kuingiza kaya ambazo hazina vigezo kwenye Mpango. Maeneo ambayo yatabainika kuwa na kaya zisizo na vigezo, viongozi watachukuliwa hatua za kinidhamu kwani watakuwa wamehusika kufanya udanganyifu na kuingiza wasiohusika kwenye Mpango. Naomba kuwasilisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukaimu muda mrefu kwa watumishi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekretarieti za Mikoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uwepo wa Watumishi wanaokaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu na uchambuzi uliofanyika unaonesha kuwa, watumishi 1,496 wanakaimu nafasi za uongozi katika Taasisi mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa. Kati ya hao, watumishi 332 wanakaimu nafasi zao wakiwa na vibali halali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi na Watumishi 1,164 wanakaimu nafasi zao bila ya kuwa na vibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi, Aidha, Kati ya watumishi hawa 1,164 ambao wanakaimu nafasi bila vibali vya Katibu Mkuu Utumishi, jumla ya watumishi 543 hawana ºifa za kukaimu nafasi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kutatua changamoto hii, ofisi yangu imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kukusanya taarifa za maafýsa Waandamizi na Wakuu 7,008 katika Utumishi wa Umma wakiwemo watumishi wanaokaimu nafasi hizo ili wafanyiwe upekuzi kwa ajili ya kujaza nafasi wazi za uongozi na zinazokaimiwa kwa muda mrefu.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwapandisha madaraja na stahiki nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutimiza masharti ya ajira kwa watumishi wake ikiwemo kupandisha vyeo Watumishi, ambapo Serikali ilitoa barua Kumb. Na. BC.46/97/03D/59 ya tarehe 28 Aprili, 2021 iliyoruhusu upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Umma kuanzia tarehe 1 Juni, 2021. Hadi kufikia tarehe 1 Septemba, 2021, jumla ya Watumishi wa Umma 174,222 wamepandishwa vyeo na kubadilishiwa mishahara yao.

Aidha, Serikali itaendelea kuboresha maslahi kwa watumishi wa umma kadri bajeti itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadilisha Muundo wa Utumishi wa Maafisa Utumishi/Utawala na Walimu ili waweze kuanza na Daraja E kama ilivyo Kada ya Sheria na nyinginezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinkyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi ya Kada mbalimbali inayotumika sasa katika Utumishi wa Umma iliandaliwa kwa kuzingatia matokeo ya zoezi la Tathmini ya Kazi iliyofanyika kuanzia mwaka 1998 hadi 2000. Aidha, Miundo husika ilianza kutekelezwa mwezi Julai, 2003.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya zoezi la tathmini ya kazi iliyoainisha uzito wa majukumu ya kada mbalimbali katika utumishi wa umma na yaliyotumika kama msingi wa kupanga vianza mshahara kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali wakiwemo Maafisa Utumishi na Utawala ambao wanaanza na ngazi ya mishahara ya TGS D, walimu Daraja C yaani walimu wenye shahada ambao wanaanza na ngazi ya mshahara TGTS D na Maafisa Sheria ambao wanaanza na ngazi ya mshahara ya TGS E.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 hadi 2017 Serikali iliendesha zoezi lingine la tathmini ya Kazi katika Utumishi wa Umma ambalo lililenga kubaini uzito wa majukumu kwa kada mbalimbali. Katika kuoanisha na kuwianisha viwango vya mishahara vya watumishi katika Utumishi wa Umma, Serikali itatumia matokeo ya mapendekezo ya zoezi hilo kupanga vianzia mshahara vya kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Maafisa Utumishi na Utawala na Walimu kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti. Naomba kuwasilisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha kipengele cha “moving expenses” kilichotolewa ili watumishi walipwe fedha za nauli wakati wakisubiri mafao mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Kanuni J(1) na J(8) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2008, kipengele cha moving expenses hakijaondolewa. Hivyo, Serikali imekuwa ikigharamia usafiri yaani nauli kwa watumishi wa umma kwa kuzingatia utaratibu ulioelezwa kwa kuzingatia Kanuni tajwa hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni J(6)(1) ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 Mtumishi wa Umma hulipwa gharama za usafiri yaani nauli, yeye, mwenza wake na watoto au wategemezi wasiozidi wanne wenye umri chini ya miaka 18 pale anapoajiriwa, anapohama au utumishi wake unapokoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya kila mtumishi anapostaafu kulipwa gharama za usafiri kurudi mahala atakapoishi baada ya kustaafu, ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha anatenga fedha za “moving expenses” kwenye bajeti. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwakumbusha na kuwataka waajiri kutenga fedha hizi na kutekeleza wajibu wao. Aidha, nichukue fursa hii kuwataka waajiri wote kuandaa orodha ya watumishi wanaokaribia kustaafu na hivyo kurahisisha kubaini gharama halisi zitakazohitajika kuwasafirisha na kuzitenga kweye bajeti kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kanuni J(8) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 pamoja na Waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2008 kuhusu usafirishaji wa mizigo yaani personal effects ya watumishi wa umma, imeeleza namna ya kusafirisha mizigo ya mtumishi wa umma pale anapohama au utumishi wake unapokoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kulipa gharama za kusafirisha watumishi wa umma, familia zao pamoja na mizigo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, kwa mwaka 2018 hadi 2021 ni walemavu wangapi wenye sifa husika wameajiriwa katika nafasi zilizotolewa na Serikali, na ni sawa na asilimia ngapi ya watu wenye ulemavu wenye sifa hizo nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 Serikali imeajiri watumishi wenye ulemavu wapatao 312 wenye sifa stahiki katika fani mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu zilizopo za wahitimu wenye ulemavu ambao wamejiorodhesha katika kanzidata ya Serikali inaonesha kwamba, kuanzia mmwaka 2018 hadi 2021 wahitimu wenye ulemavu walioajiriwa katika utumishi wa Umma ni asilimia 56 ya wahitimu wenye ulemavu waliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutoa rai na kusisitiza wahitimu wenye ulemavu wenye sifa za elimu na taaluma mbalimbali ambazo zipo ndani ya utumishi wa Umma kuomba kazi pindi zinapotangazwa ili waweze kuajiriwa katika utumishi wa Umma kwani ajira hutolewa kwa usawa na kwa watu wote wenye sifa zinazohitajika katika nafasi husika pamoja na kuzingatia ujumuishaji wa watu wenye ulemavu. Vile vile, nitumie fursa hii kuwakumbusha waajiri wote kuzingatia ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika ajira zote zinazotangazwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wenye sifa wa Shehia ya Njuguni, Majenzi na Chomboni – Micheweni wataunganishwa na TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF iliyoanza rasmi mwezi Januari, 2020 unaendelea katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar kwenye vijiji, mitaa na shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika shehia ya Njuguni, Kaya 352 ziliandikishwa, Shehia ya Majenzi Kaya 312 ziliandikishwa na Shehia ya Chamboni Kaya 584 ziliandikishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kaya ambazo hazikutambuliwa na kuandikishwa kwa sababu mbalimbali katika kipindi hiki cha pili utaratibu umeandaliwa kwenda kwenye vijiji, mitaa na shehia zote kwa maeneo yote ya utekelezaji ili ziweze kuandikishwa na kuingizwa kwenye mpango ikiwa zimekidhi vigezo na sifa stahiki.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -

Je, nini Sababu ya kukosekana uwiano wa jinsia ya kike kwenye nafasi za uteuzi na ajira nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kunakuwepo na uwiano sawa wa kijinsia kwenye nafasi za uteuzi na ajira nchini kwa kuweka mazingatio ya usawa wa kijinsia katika nyaraka zinazosimamia Utumishi wa Umma, ikiwemo Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 inayotaka kila mamlaka ya ajira kuhakikisha uwiano wa kijinsia katika uteuzi na ajira zote. Pia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2019, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2009 pamoja na Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, hatua hizi zimeiwezesha Serikali kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikia uwiano sawa wa kijinsia katika nafasi za Uteuzi na ajira nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa suala hili ni kipaumbele cha Dunia kupitia ajenda 2020/2030 kuhusu Maendeleo Endelevu, Lengo Na. 5 Usawa wa Kijinsia, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameazimia kuhakikisha uwepo wa uwiano sawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali za uteuzi katika kipindi chake cha uongozi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hivyo, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iko katika hatua za mwisho za kutoa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma. Mwongozo huu unatoa maelekezo kwa mamlaka za ajira katika utumishi wa umma kote nchini kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanakuwa na fursa sawa kuanzia katika mchakato wa ajira, upandishaji madaraja, uteuzi, mafunzo, ubadilishanaji pamoja na urithishaji madaraka. Lengo likiwa ni kuondoa vikwazo kwa kujenga uwezo wa ushindani kwa jinsia zote ili kupata sifa stahiki za kushika madaraka na fursa mbalimbali.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani Mbunge anashirikishwa katika miradi inayoibuliwa na wananchi katika Jimbo lake kupitia TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uibuaji wa miradi ya jamii inayochangiwa na TASAF hufanyika kwenye mikutano ya jamii ambayo huendeshwa na wataalam chini ya usimamizi wa viongozi wa maeneo hayo. Mbunge au Mwakilishi wa eneo husika kama anakuwepo wakati zoezi la kuibua miradi likifanyika hazuiwi kushiriki kwa kuwa hakuna mwongozo unaomtaka Mbunge asiwepo wakati wa zoezi la kuibua miradi.

Mheshimiwa Spika, wananchi huibua miradi ambayo inatatua kero walizonazo katika jamii kutokana na kukosekana kwa huduma stahiki. Ikiwa wananchi wote kwenye mkutano wameridhia mradi fulani kutekelezwa, basi moja kwa moja huo unakuwa ni chaguo lao. Lakini kama kuna miradi miwili au mitatu iliyopendekezwa, jamii hupiga kura na mradi utakaopata kura nyingi ndio unapewa kipaumbele cha kuanza kutekelezwa. Jamii ikishaamua mradi wa kutekeleza, timu ya Wataalam hufanya bajeti ya mradi huo na kurudi tena kwa wananchi kukubaliana kuhusu mchango wa jamii kabla bajeti hiyo haijawasilishwa TASAF kwa hatua nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza Wananchi wengi zaidi kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwntumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaendelea katika maeneo ya Mamlaka 186 ikiwa ni Halmashauri 184 za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kipindi hiki, idadi ya walengwa iliyobaki awali ya asilimia 30 ya Vijiji, Mitaa pamoja na Shehia 7,217 ambazo hazikufikiwa katika kipindi cha kwanza imeongezwa. Jumla ya kaya 498,091 zilizokidhi vigezo zimeandikishwa na kuingizwa kwenye mifumo ya taarifa za walengwa. Aidha, Kaya mpya na ambazo zilikuwemo kwenye Mpango, zinafanya jumla ya idadi kuu ya walengwa kuongezeka na kufikia kaya 1,279,325.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni watumishi wangapi wamesimamishwa kazi tangu mwaka 2015 hadi 2022 ambao mashauri yao hayajaisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa nidhamu katika Utumishi wa Umma ni suala muhimu ambalo limeainishwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298; Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003; Taratibu za Uendeshaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2003; Taratibu Bora za Nidhamu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2007 na Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2022, idadi ya watumishi waliosimamishwa kazi katika Taasisi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na Serikali Kuu ambao mashauri yao hayajahitimishwa ni watumishi 836. Watumishi hawa ni miongoni mwa watumishi 1,477 waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma. Mashauri haya yapo katika hatua mbalimbali za mamlaka za nidhamu ambazo ni waajiri mbalimbali na mamlaka za rufaa ambazo ni Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Walimu na Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwakumbusha Waajiri/Mamlaka za Nidhamu kuongeza kasi ya kuhitimisha mashauri ya nidhamu yaliyopo kwa kuzingatia taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali iliamua kujiondoa kwenye mpango wa uendeshaji wa Serikali kwa uwazi wakati silaha kubwa ya kupambana na rushwa ni uwazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi wa Serikali kujitoa OGP haujaathiri uendeshaji wa Serikali kwa uwazi kwa kuzingatia ukweli kwamba Serikali inao utaratibu wa ndani wa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi wakati wote kwa kuwa na vyombo na taasisi zilizokasimiwa majukumu ya kusimamia na kufuatilia Sera ya Uwazi na Uwajibikaji. Mfano, TAKUKURU, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kujiunga na OGP ni hiari kwa nchi mwanachama na vilevile inaweza kujitoa kwa hiari. Kwa msingi huo Serikali iliamua kujitoa kwa hiari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ngazi za kimataifa, Serikali imeendelea kuwa moja ya nchi zilizoridhia mfumo wa kukaguana wa nchi za kiafrika APRM (African Peer Review Mechanism) ambao ulianzishwa mwaka 2003 na Kamati ya Wakuu wa Nchi za Kiafrika.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri wahitimu wa kada ya mazingira waliomaliza katika vyuo vikuu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha wahitimu wa kada ya Mazingira na kada ya Afya ya Mazingira (Environmental Health Officers) wanaajiriwa ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitoa jumla ya vibali vya ajira 223 kwa kada ya Mazingira katika taasisi zipatazo 124 ambapo utekelezaji wa ajira hizo unaendelea. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga nafasi 73 za ajira kwa Wataalam wa Mazingira kwa ajili ya taasisi za Serikali zikiwemo Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hatua za utekelezaji wa ajira hizi zote zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023.

Mheshimwa Spika, jitihada hizi ni endelevu kutokana na umuhimu wa suala la utunzaji wa mazingira ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya nchi na dunia kwa ujumla ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Mpango wa TASAF kwa Zanzibar umenufaisha kaya 216, Unguja Shehia 204 na Pemba Shehia 78 ambapo ni sawa na 70% ya Shehia zote Zanzibar.

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Shehia zote 388 Zanzibar zinanufaika na mpango wa TASAF kwa 100% badala ya 70%?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -

Mgeshimiwa Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoanza utekelezaji mwaka 2013, rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia asilimia 70 ya Vijiji, Mitaa na Shehia ambavyo kwa hesabu ni maeneo 9,960. Kipindi cha kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kilidumu kwa miaka sita na kilikamilika mwezi Desemba 2019. Katika awamu hiyo, idadi ya maeneo ambayo hayakufikiwa ni Vijiji, Mitaa na Shehia 5,590 nchini kote zikiwemo Shehia 388 za Zanzibar (Unguja ikiwa ni Shehia 259 na Pemba Shehia 129).

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kilianza rasmi mwezi Januari, 2020. Sehemu hii ya Pili inatekelezwa katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, kwenye Vijiji, Mitaa na Shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza. Utambuzi na uandikishaji wa walengwa katika maeneo yote 5,590 ambayo hayakufikiwa katika kipindi cha kwanza tayari umeshafanyika.

Mheshimiwa Spika, utambuzi ulitanguliwa na semina za uelimishaji kuhusu TASAF na taratibu zake, vigezo vya walengwa na majukumu ya wadau katika ngazi za jamii, shehia, Halmashauri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Aidha, kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza, taratibu za utambuzi wa walengwa zimeboreshwa ili kutambua kaya zinazokidhi vigezo. Aidha, tathmini ya hali ya walengwa waliodumu kwenye Mpango katika kipindi cha kwanza itafanyika kwa lengo la kubaini wale ambao wameshaimarika kiuchumi ili kusitisha utoaji wa ruzuku kwa kaya hizo. Naomba kuwasilisha.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwasaidia Wananchi wa Mwera ambao hawakuingizwa TASAF na wanaishi chini ya viwango vya umaskini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa katika halmashauri 184 za Tanzania Bara na Unguja na Pemba katika vijiji, mitaa na shehia zote 410 (shehia 259 kwa Unguja na 151 kwa Pemba).

Kundi la kwanza la wanufaika wa TASAF waliingia kwenye Mpango mwaka 2014. Hata hivyo, si maeneo yote yalifanikiwa kuingia katika kipindi hicho. Kundi la pili liliandikishwa na kuanza kupata ruzuku mwaka 2021, ambapo Mwera waliandikishwa walengwa 924. Kundi hili ni la Walengwa ambao hawakuwa wamefikiwa katika kipindi cha kwanza na hivyo kukamilishwa kwa asilimia 100 ya idadi ya mitaa, vijiji na shehia zote nchini kuwa na wanufaika wa TASAF ikiwemo Jimbo la Mwera.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali imetoa kibali cha nafasi 10,003 za ajira kwa Walimu. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imepanga kutoa kibali cha ajira kwa nafasi 30,000 zikiwemo nafasi za Walimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wahitimu waliopo kwenye soko la ajira, ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kuanzia mwaka 2016 hadi Desemba, 2020 jumla ya wahitimu ni 248,379. Idadi hii inajumuisha Walimu wa Astashahada, Stashahada na Shahada na kati ya wahitimu hawa wameajiriwa na Serikali na wengine Sekta Binafsi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa nakala ya Sheria ya Maadili kwa Viongozi nchini ikiwemo Wabunge na Viongozi wengine ili kuepuka kukiuka Sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamisi (VITI MAALUM) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika; Serikali imekuwa ikitoa nakala za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995 kwa Viongozi. Serikali hutoa nakala hizo kupitia mikutano, warsha, semina, makongamano na maonyesho mbalimbali. Kati ya mwaka 2015 hadi 2022 Jumla ya nakala 12,400 za Sheria zilichapishwa na kutolewa kwa Viongozi na wadau wengine. Aidha, nakala tepe (soft copy) ya Sheria imewekwa katika tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz. Hivyo, Viongozi wa Umma wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wanashauriwa kutembelea tovuti na kupata nakala ya Sheria.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya kutoka Kintinku hadi Makanda inayounganisha Mkoa wa Singida na Dodoma itahamishiwa TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya mwaka 2009 kifungu 43(1) na (2) na kifungu 44(1) kupitia Tangazo la Serikali Na. 21 ya tarehe 23 Januari 2009, zimeainisha vigezo na utaratibu wa kuhamisha barabara ili iwe chini ya TANROADS ambapo barabara inaweza kupandishwa au kuteremshwa toka daraja moja kwenda daraja lingine.

Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria na kuzingatia vigezo. Ili barabara iweze kupanda kutoka daraja la barabara ya Wilaya kwenda daraja la barabara ya Mkoa (kusimamiwa na TANROADS) inatakiwa barabara hiyo ijadiliwe kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo, Bodi hiyo kupitia kwa Mwenyekiti itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo na hivyo ipandishwe daraja na kuwa chini ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri utaratibu wa kuhamisha barabara kwenda TANROADS uzingatiwe ikiwemo kwa hii ya Kintinku - Makanda kwenda TANROADS.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaangalia upya mipaka ya kiutawala ikiwemo na Halmashauri ya Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikizingatia suala la maendeleo ya mipaka ya maeneo ya utawala ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mipaka ya maeneo ya utawala kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishaji wa maeneo ya utawala katika mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 huanza na kusudio ambalo hupaswa kujadiliwa katika vikao vya Ngazi ya Halmashauri, Wilaya na Mkoa. Kusudio hilo huwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Katibu Tawala wa Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI bado haijapokea kusudio la kubadili mipaka kutoka Halmashauri ya Mji wa Makambako. Hivyo, endapo kuna uhitaji wa kubadili mipaka, inashauriwa kuanzisha kusudio na kuliwasilisha katika vikao vya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na hatimaye katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni shule ngapi za sekondari zimejengwa katika Mkoa wa Mtwara ambao una zaidi ya kata 50 ambazo hazina shule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari imejenga shule 231 za kata na shule 10 za wasichana za kitaifa katika mikoa 10. Hii ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari.

Mheshimiwa Spika, katika awamu hii ya kwanza Mkoa wa Mtwara umeshajengewa shule 10 za kata katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi na kata ambazo zilikuwa hazina shule.
MHE. DANIEL A. TLEMAI K.n.y. MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -

Je, lini barabara ya Kibaoni – Endala – Endamarik hadi Endabash itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Jimbo la Karatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza matengenezo katika barabara ya Kibaoni – Endala - Endamariek hadi Endabash. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilipeleka shilingi milioni 599.97 kwa ajili ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 40 kwenye barabara hiyo, na ujenzi wake umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 68 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilomita tano katika barabara hiyo na utekelezaji wake unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 213.02 kwa ajili ya kujenga madaraja mawili katika matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa 10 pamoja na matengenezo ya muda maalum yenye urefu wa kilomita mbili katika barabara hiyo.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya Mto Piyaya Kata ya Piyaya na Mto Juhe Kata ya Samunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Madaraja ya Mto Piyaya na Mto Juhe ambayo yana urefu wa zaidi ya mita 80. Aidha, ujenzi wa madaraja hayo unahitaji kuanza na kazi ya usanifu wa kina ikiwemo uchambuzi wa miamba, ili kupata gharama halisi ya ujenzi wake.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Serikali itafanya usanifu wa kina wa madaraja haya, ili kupata gharama halisi ya ujenzi. Vilevile, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za Jimbo la Ngorongoro ikiwemo ujenzi wa madaraja kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha za ukarabati wa Madarasa, Mabweni na Usafiri katika Shule ya Sekondari ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Mji Geita ilitumia fedha za ndani shilingi milioni 50 kukarabati mabweni matatu ya Shule ya Sekondari ya Geita. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, shilingi milioni 20 kutoka fedha za CSR zilitumika kukarabati mabweni mawili, shilingi milioni 100 zilitumika kujenga bweni moja na shilingi milioni 40 zilitumika kujenga madarasa mawili mapya. Vilevile katika mwaka 2022/2023, Serikali imepeleka shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mapya matatu katika shule hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kupeleka fedha za ukarabati kwa shule za kitaifa ikiwemo Shule ya Sekondari ya Geita pamoja na ununuzi wa magari kwa ajili ya shule za mabweni kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya Kwamtoro - Sanzawa hadi Mpendo katika Wilaya ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya marekebisho ya kipande cha Sanzawa – Mpendo chenye urefu wa kilomita 38.2 ambapo shilingi bilioni 2.06 zinahitajika. Serikali imeendelea kuihudumia barabara hiyo ambapo mwaka wa fedha wa 2022/2023 shilingi milioni 48 zimepelekwa kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi yenye urefu wa kilomita Nane kati ya Kwamtoro na Sanzawa katika Vijiji vya Kurio na Moto. Aidha, ukarabati wa box culvert katika Kijiji cha Moto umekamilika. Kwa sasa Mkandarasi anafanya maandalizi ya kuchonga barabara eneo korofi la Kurio lenye urefu wa kilomita Tatu.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, serikali itatenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza kufanya matengenezo kwenye eneo korofi la mawe kati ya Sanzawa na Mpendo lenye urefu wa kilometa 34.2.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za Jimbo la Chemba kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha usafiri na usafirishaji.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watumishi wa afya na elimu katika Jimbo la Igalula ili kuondoa kero wanayoipata wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira ili kukabiliana na upungufu wa watumishi katika kada za afya na elimu unaotokana na kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa na kufariki. Tangu mwaka 2018/2019 hadi 2021/2022, Serikali imeajiri jumla ya walimu 26,598 wakiwemo 16,640 wa shule za msingi na 9,958 wa shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022, watumishi wa kada za afya 7,736 waliajiriwa na kupelekwa kwenye maeneo mbalimbali nchini kulingana na uhitaji uliokuwepo. Mkoa wa Tabora ulipata walimu 565 wakiwemo wa shule za msingi 301 na shule za sekondari 264. Aidha, kwa upande wa kada za afya Serikali ilipeleka kwenye Mkoa wa Tabora jumla ya watumishi 265 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ilipata watumishi wa kada ya afya 50.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari imetangaza nafasi za ajira za walimu na watumishi wa kada ya afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Jumla ya ajira 13,130 kada ya elimu na 8,070 kada ya afya zitatolewa hasa kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu mkubwa.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahuisha mpango wa upanuzi wa Manispaa ya Moshi kutoka kilometa 58 hadi 146 pamoja na kuwa Jiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tarehe 25 novemba, 2015 ilipokea ombi la uendelezaji wa Manispaa ya Moshi kuwa Jiji kwa kuongeza ukubwa wa mipaka ya kiutawala kutoka kilomita za mraba 58 hadi kilomita za mraba 142 kwa kuongeza vijiji kutoka Halmashauri za Wilaya za Moshi na Hai.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Uanzishaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014, kigezo cha ukubwa wa kuanzisha halmashauri ya jiji ni kilometa za mraba 1,000 na Halmashauri ya Wilaya ni kilometa za mraba 5,000.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zinaupungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa Hospitali Kongwe ya Magunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali 19. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali Kongwe kumi na nne (14).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 ikiwepo Hospitali ya Mji wa Korogwe ya Magunga ambayo imetengewa shilingi milioni 900.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza madarasa katika Shule ya Msingi Puma kutokana na kuzidiwa na idadi ya wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa kutokana na utekelezaji wa sera ya elimu bila ada, kumepelekea ongezeko kubwa la wanafunzi na uhitaji wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa. Hatua mbalimbali za kukabiliana na uhitaji wa miundombinu ya shule zinaendelea kufanywa na Serikali katika halmashauri, manispaa na majiji hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule ya Msingi Puma, Katika bajeti ya mwaka 2023/2024 shule hii imetengewa madarasa mawili sambamba na ufunguzi wa shule shikizi Isalanda ambayo itasaidia pia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi Puma.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga shule ya Kidato cha Tano na Sita katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Idi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhitaji wa shule za kidato cha tano na sita kwa maeneo mengi hapa nchini, Shule ya sekondari ya Mchoteka katika jimbo la Tunduru, wazazi pamoja na halmashauri walijenga hosteli mbili ambazo zimekamilika; hostel moja ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshapeleka kiasi cha shilingi milioni 160 kwa ajili ya kuongeza miundombinu mingine ili kukidhi vigezo vya kupandisha hadhi shule. Hata hivyo, shule hii imeombewa usajili wa mkondo walau mmoja wa kidato cha tano.
MHE. FURAHA N. MATONDO K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, mpango wa kutumia majengo ya Sekondari ya Sengerema kuwa Chuo cha Madini na Uvuvi umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Sengerema ni miongoni mwa shule za Sekondari kongwe hapa nchini. Shule hii inachuka wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita kutoka nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapanga kuongeza nafasi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita, kutokana na wanafunzi wanao maliza kidato cha nne kuongezeka sana. Mpango wa kuifanya Shule ya Sekondari Sengerema kuwa Chuo cha Madini na Uvuvi hauwezekani kutokana na uhitaji wa shule hii kwani kubadili matumizi ya shule hii kutaongeza uhaba wa nafasi za wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais TAMISEMI haijashirikishwa kwa namna yoyote kuhusu kubadili matumizi ya shule ya Sekondari Sengerema. Hivyo, tunawaomba wenzetu wa Wizara ya Madini kuja mezani na kujadiliana juu ya jambo hili, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa tuna uhitaji mkubwa wa shule za kidato cha tano na sita. Aidha tunaomba kuwashauri Wizara ya Madini kutafuta eneo na fedha kwa ajili ya kujenga chuo kitakachojihusisha na kada ya madini kuliko kubadili matumizi ya Sekondari hii.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya mkato kati ya Wilaya za Mbarali na Chunya ili kupunguza gharama za usafiri na kukuza biashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa umbali kutoka Wilaya ya Chunya hadi Wilaya ya Mbarali kwa kupitia Wilaya ya Mbeya ni mrefu ukilinganisha na umbali wa kupitia barabara ya mkato kati ya Wilaya ya Chunya na Mbarali. Serikali inatambua changamoto ya kutokuwepo kwa barabara hiyo na kusababisha adha ya mzunguko mrefu kwa wananchi wa wilaya hizo mbili ndani ya mkoa wa Mbeya na kusababisha gharama kubwa kwa wananchi wanaosafiri kati ya wilaya hizo mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa uhitaji wa barabara hiyo ya mkato, Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mbeya kupitia kikao chake cha tarehe 09 Januari, 2023, kilitoa mapendekezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuipandisha hadhi barabara ya Njiapanda – Sangambi – Shoga na kufungua barabara mpya kutoka Shoga Wilaya Chunya hadi Udindilwa katika Wilaya ya Mbarali inayokadiriwa kuwa kilomita 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, aliiagiza Kamati ya Kitaifa ya kupanga barabara katika hadhi stahiki (NRCC) kufika mkoani Mbeya na Kamati hiyo ilifika mnamo tarehe 24 Februari, 2023 na kutembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi ikiwemo barabara ya Njiapanda – Sang’ambi – Shoga na kipande cha Shoga - Udindilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Kamati yaliwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Kama barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. KATANI A. KATANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa sekondari zilizojengwa na wananchi Kata za Mnchimbwe, Kwanyama na Litehu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani Ahmadi Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wananchi katika kuibua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule. Serikali imeendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kumalizia miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka wa Fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kupitia mapato ya ndani ilitoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya umaliziaji wa Shule ya Sekondari ya Kwanyama. Mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali illipeleka shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Litehu kupitia mradi wa SEQUIP na Mwaka wa Fedha 2022/2023, shilingi milioni 250 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mndumbwe. Aidha, Shule za Sekondari katika Kata za Mnchimbwe, Kwanyama na Litehu zimekamilika, zimesajiliwa na tayari zinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za umaliziaji wa maboma ya shule katika halmashauri zote nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza: -

Je, kwa nini hoja za ukaguzi hutokea pale fedha za Mfuko wa Jimbo zinapotumika kwa wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa Sheria Na. 16 ya mwaka 2009 na unaelekeza miradi ya kutekelezwa kupitia Kamati ya Mfuko ambayo Mbunge ni mwenyekiti na afisa mipango wa halmashauri ni katibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo mahususi la kuanzishwa kwa Mfuko huu wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ni kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa katika ngazi ya jamii na kupitishwa kwenye vikao mbalimbali vya kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya halmashauri zimekuwa zikitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kutoa mitaji kwa wananchi, hususan wanawake, watu wenye ulemavu na vijana, hali inayosababisha ugumu wakati wa kufanya ufuatiliaji na tathmini na kusababisha hoja za ukaguzi.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Chikola na Makanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipokea vipaumbele vya ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Sanza, Chikola na Makanda zilizopo katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilipeleka Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati cha Sanza ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kwa OPD na maabara umekamilika. Ujenzi wa awamu ya pili, unaohusisha wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji na laundry upo kati hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya kimkakati nchini ikiwa ni pamoja na kwenye Kata za Chikola na Makanda kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya Geterer na Masieda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na umaliziaji wa maboma ya Vituo vya Afya kote nchini. Serikali itapeleka shilingi milioni 800 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Masieda na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kituo hicho. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Markad.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa Vituo vya Afya ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa Kituo cha Afya Geterer kwa kadri fedha inavyopatikana.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabweni kwenye shule za wasichana wanaosoma masomo ya sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule za bweni. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali imetoa Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa shule 10 maalumu za sekondari za wasichana za masomo ya sayansi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita. Ujenzi huu ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule 26 ambazo kila Mkoa utajengewa shule moja kupitia mradi wa SEQUIP.

Mheshimiwa Spika, mradi huo unahusisha ujenzi wa mabweni tisa katika kila shule na kila bweni litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 120. Aidha, kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Sekta ya Elimu, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati mabweni ili kuongeza nafasi zaidi za wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka kipaumbele cha ujenzi wa mabweni kwa shule za kidato cha tano na sita na kwa wanafunzi wote wa kike na wakiume, kwa kuwa wanafunzi wote wana changamoto.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE K.n.y. MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Km 10 kwa kiwango cha lami Mjini Tunduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mwaka 2020 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 10 kwenye Mji wa Tunduma.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi hiyo umeanza ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya kilometa 2.8 zilijengwa kwa kiwango cha lami na shilingi bilioni 1.39 zilitumika. Aidha, mwaka wa fedha wa 2022/2023 shilingi bilioni 2.3 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 3.7 kwa kiwango cha lami ambapo shilingi bilioni 1.64 zimepokelewa na ujenzi umefikia asilimia 45.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukamilisha ahadi hiyo kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. NJALU D. SILANGA K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi na Soko la kisasa katika Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Makambako ipo kwenye Mradi wa kupendezesha Majiji, Manispaa na Miji (Tanzania Cities Transformation Infrastructures and Competitiveness – TACTIC) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia. Kupitia mradi huo, Mji wa Makambako utajengewa Stendi na Soko la Kisasa.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa Jengo jipya la Utawala katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Hivyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi wa Jengo hilo kupitia fedha za Mapato ya Ndani ya Halmashauri ambapo katika mwaka wa Fedha wa 2022/2023 jumla ya Shilingi milioni 500 zimetengwa.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imekamilisha maandalizi ya nyaraka za ujenzi wa jengo hilo na kuwasilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuidhinishwa ili ujenzi uweze kuanza kwa kuwa Halmashauri hiyo imepanga kutumia mchoro wao badala ya mchoro ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imetenga pia Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo hilo.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Shule za Mtapa, Kanani na Wangutwa Wilayani Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, kupitia mapato ya ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging`ombe ilipeleka shilingi milioni mbili kwa Shule ya Msingi Kanani kwa ajili ya ujenzi wa vyoo. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 75 kwa ajili ya ukarabati katika shule hiyo.

Mheshimiwa Spika, Shule ya Msingi Wangutwa inaendelea kufanyiwa ukarabati kwa kushirikiana na wananchi. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali ilipeleka shilingi milioni 61.6 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa matundu ya vyoo. Vilevile, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, shule hiyo imetengewa shilingi milioni 75 kwa ajili ya kuongeza madarasa matatu.

Mheshimiwa Spika, vilevile, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali ilitoa shilingi milioni 12.5 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Mtapa. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 shule hiyo ilipelekewa shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na Vifaa Tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada za afya. Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 na 2021/2022, watumishi wa kada hiyo 10,462 waliajiriwa kote nchini. Katika ajira hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ilipangiwa watumishi 55 na watumishi 25 walipelekwa kwenye Hospitali ya Halmashuri ya Wilaya ya Ushetu. Aidha, Aprili, 2023, Serikali imetangaza nafasi 8,070 za ajira kwa kada za afya ambapo baadhi ya watumishi hao watapelekwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Hospitali ya Wilaya ya Ushetu ilipelekewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na tayari MSD wameanza kusambaza vifaa tiba kwenye Hospitali za Halmashauri 67 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Ushetu. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Hospitali hiyo imepokea shilingi milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya macho na meno. Vilevile, Hospitali hii imepokea vifaa tiba kwa ajili ya jengo la Kutolea Huduma za Dharura (EMD).
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafunga taa za barabarani eneo la Tunduru Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tunduru ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,200. Kati ya hizo, barabara za tabaka la lami ni kilometa 4.5, barabara zenye tabaka la changarawe ni kilometa 285 na barabara za tabaka la udongo ni kilometa 914.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia TARURA ilifunga taa za barabarani 16 kwa gharama ya shilingi milioni 72 katika barabara ya Bus Stand –Sinabei Guest House, TUDECO – Tunduru Sekondari – Borrow Pit, NMB – Ushirika na Nguzo Sita – Muungano – Camp David. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya taa 20 za barabarani zitafungwa kwa gharama ya shilingi milioni 90 katika barabara ya Isalmic Centre – Amazon – Mkunguni na Bus Stand – Mseto – Mkunguni baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara. Mwaka wa fedha 2023/2024 TARURA imetenga shilingi milioni 270 kwa ajili ya kufunga taa 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini itaendelea kuhudumia miundombinu ya barabara ya Mji wa Tunduru kwa kuweka katika mipango yake ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwemo ufungaji wa taa za barabarani kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Mto Duma Bariadi Mkoani Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Duma ni mto mkubwa unaoanzia Kata za Gibishi kupitia Kata ya Matongo, Mwaubingi na Gilya. Mto huu ni wa msimu ambao hujaa kipindi cha Mvua kutokea Mbuga ya hifadhi ya Serengeti kuelekea Ziwa Victoria na hukauka kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukidhi haja ya kuwa na mawasiliano kwa Wananchi wanaotenganishwa na mto huu, jumla ya madaraja mawili yanahitajika ambapo hadi sasa ni daraja moja limejengwa katika barabara ya Igegu – Matongo - Gibishi. Kwa upande wa barabara ya Gasuma – Gilya, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 50 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa daraja ili kujua gharama halisi za ujenzi wake.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kukomesha vifo na upotevu wa mali kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kilwa, Nachingwea na Liwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Lindi ni miongoni mwa Mikoa ambayo imekuwa na ongezeko kubwa la wafugaji wanaohamia na mifugo yao ikiwemo ng’ombe na mbuzi katika kipindi miaka ya karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi umekumbwa na migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya za Kilwa, Liwale na Nachingwea. Migogoro hii imesababishwa na ongezeko la mifugo iliyopelekea kuongezeka kwa mahitaji ya malisho na maji, ukosefu wa mipango ya matumizi ya ardhi, uuzaji holela wa ardhi na wakulima kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaondoa changamoto ya migogoro ya aridhi kwa kutekeleza yafuatayo: - kutenga maeneo kwa ajili ya mifugo, ujenzi wa miundombinu ya mifugo, kuwezesha upatikanaji wa malisho, uanzishwaji wa ranchi ndogo ndogo, kuweka utaratibu wa uingizwaji wa mifugo katika Mkoa wa Lindi, kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa kwa viongozi ngazi ya Mkoa na Halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatatua migogoro kwa wakati, hii ikiwa pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA K.n.y. MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali 19. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimeshatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali kongwe 14 ikiwemo Hospitali ya Mji wa Handeni iliyotengewa shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 zilizosalia.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia Vituo vya Afya Kizengi, Tura, Lutende na Goweko kwa kujenga OPD na kupeleka vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya katika kata za kimkakati ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali ilitenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Lutende katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Lutende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini ikiwemo ukamilishaji wa Kituo cha Afya Lutende, na Tura, pamoja na ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Goweke na Kizengi.
MHE.SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya Mureru – Diloda – Gorimba – Masusu hadi Waama ili ipitike wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mureru – Diloda – Gorimba – Masusu hadi Waama imegawanyika katika vipande viwili vya Mureru – Waama chenye urefu wa kilometa 34 na Diloda – Gisambalang’ chenye urefu wa kilometa 25.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023, TARURA imefungua kipande cha barabara ya Mureru - Waama kwa kiwango cha tabaka la udongo yenye urefu wa kilomita 34 na ujenzi wa (culvert) yaani vivuko 11 vya maji kwa gharama ya shilingi milioni 284.99. Awali kipande hiki kilikuwa ni njia ya ng’ombe (Pario). Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, shilingi milioni 80 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa culvert, yaani vivuko 16 vya maji katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufunguzi wa kipande cha barabara ya Diloda – Gisambalang’ chenye urefu wa kilometa 25.1 utafanyika kadiri ya upatikanaji wa fedha ambapo kwa sasa kinatumika kama njia ya ng’ombe (pario).
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga shule ya msingi ya watoto wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Halmashauri ya Morogoro ina watoto wenye mahitaji maalum. Hadi sasa halmashauri imeanza kujenga bweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mvuha. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 24, Serikali tayari imekwishapeleka kiasi cha shilingi milioni 100 katika shule hii katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa bweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga na kupeleka fedha katika Halmashauri ya Morogoro kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya mkato kutoka Kigwe B hadi Magiri Uyui ili kuchepusha magari makubwa kupita Tabora Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara ya mkato kutoka Kigwa B mpaka Magiri - Uyui Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo inapitika wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 125 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya muda maalum ya kilomita Saba kwa kuziwekea changarawe na kujenga kalavati moja ili iweze kuendelea kupitika muda wote na kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuifanyia matengenezo na kujengwa kwa kiwango cha lami kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu katika Halmashauri ya Mji Tarime?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime imeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kuondoa msongamano wa wanafunzi pamoja na kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma kwa zamu. Baadhi ya maeneo tayari wananchi wameanza kujenga shule, mfano Kata ya Turwa, Chirya, Kenyamanyori.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jitihada hizo za wananchi, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, hii itasaidia kuongeza madarasa katika shule za msingi na hivyo kuondokana na msangamano wa wanafunzi darasani.
MHE. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaongezea TARURA bajeti ili barabara za ndani ya Jimbo la Kinondoni zijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Jimbo la Kinondoni lilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 2.38 ambazo zilitekeleza matengenezo ya barabara ya jumla kilometa 26 za lami na changarawe na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya kilometa 0.52. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 32 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 1.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Jimbo la Kinondoni lilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 4.87 kwa ajili ya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara zenye jumla ya kilomita 26.52, ambapo matengenezo ya kawaida ni kilomita 24.32 na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa 2.2 ambapo utekelezaji wake unaendelea na umefikia asilimia 70. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 29 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuiongezea fedha TARURA kwa ajili ya kuongeza mtandao wa barabara za lami katika Jimbo la Kinondoni na maeneo mengine kwa kadri ya upatikani wa fedha.
MHE. JOHN M. SALLU aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Afya katika Kata ya Segera, Tarafa ya Mkumbulu kitajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga fedha shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati katika kata 234 kote nchini. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ilipewa shilingi milioni 500 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Sindeni.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Segera katika Tarafa ya Mkumbulu.
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupeleka walimu wa kike katika shule za sekondari na msingi – Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira ili kukabiliana na upungufu wa walimu shuleni unaotokana na walimu kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa, kufariki na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa. Kwa mwaka 2021/2022 Serikali imeajiri jumla ya walimu 26,598 wakiwemo 16,640 wa shule za msingi na 9,958 wa shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ajira zilizotangazwa 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipata Walimu 46 wa kiume na Walimu 49 wa kike kwa shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara kufanya msawazo wa Walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zenye upungufu zaidi kwa kuzingatia jinsia ili kuwa na uwiano wa Walimu wa kike na kiume kwenye shule zetu mbalimbali.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanza kutoa Posho kwa Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kila Halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa kuwalipa posho, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa Fedha za ujenzi wa Vituo vya Afya katika Kata za Mnongodi na Nyundo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya kimkakati kwenye Kata 234 nchini. Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ilitengewa kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitaya. Ujenzi wa Kituo hicho upo hatua za ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata za Kimkakati nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata za Mnongodi na Nyundo.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi Mkoani Mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Mkoa wa Mara ulipata walimu 531 kwa shule za Msingi na Sekondari. Kati yao walimu wa masomo ya sayansi walikuwa 197. Ni dhamira ya Serikali kuendelea kuajiri na kuongeza idadi ya walimu wa sayansi ili kuendana na malengo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari imetenga nafasi za ajira za walimu na watumishi wa kada ya afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo jumla ya nafasi 13,130 ni za kada ya elimu na kipaumbele ni masomo ya sayansi. Waombaji watapangiwa vituo vya kazi kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu mkubwa ukiwemo Mkoa wa Mara.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuboresha Kituo cha Afya Igurusi ili upasuaji uweze kufanyika katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Igurusi kilijengwa mwaka 1966 na kuanza kutoa huduma katika ngazi ya zahanati hadi ilipofika mwaka 2010 kilipopandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya. Aidha, miundombinu ya kituo hiki ni michache na iliyopo ni chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imefanya uchambuzi na kupata vituo vya afya vikongwe 193 nchini kote ambavyo vinahitaji kufanyiwa ukarabati na kuongezewa majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki umefanyika kutambua vituo vya afya vikongwe na Serikali iko kwenye mchakato wa kutafuta fedha ili kuvikarabati vituo hivyo.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini Shule ya Sekondari Mkalapa itatambuliwa kuwa shule ya vipaji vya michezo ya mpira wa wavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea ombi la Mheshimiwa Mbunge la kutambua shule ya Sekondari Mkalapa kuwa shule ya vipaji vya mchezo wa wavu.

Nielekeze wataalam wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kutembelea shule hiyo ili kuona miundombinu iliyopo na namna shughuli za michezo zinazofanyika shuleni hapo ili kuona kama inakidhi vigezo vinavyotakiwa.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari utakamilika kama ilivyokusudiwa katika bajeti ya 2022/2023?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara Sita Halmashauri ya Mji wa Mbulu na tayari mabara hizo zinatumika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ilitenga na kutoa shilingi milioni 30 kupitia mapato ya ndani ili kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya maabara na ujenzi huo upo katika hatua ya umaliziaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya umalizaji wa maabara 11 ambazo hazijakamilika kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Iyula – Ipyana hadi Idunda – Vwawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 10 kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali imechonga kipande cha barabara hiyo chenye urefu wa kilometa 3.5 kilichobakia kutoka Idunda kwenda Kitongoji cha Itete kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Songwe na Mbeya kwa shilingi milioni 10.5.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka mipango ya matengenezo ya barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, kwa nini Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nansio haifanyi kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika inaonesha kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo Nansio bado haijakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zina upungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, mashine ngapi za kukusanya mapato zilibainika kutokuwa hewani na hazikutambulika na Halmashauri mwaka 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 kulikuwa na mashine 14 za kukusanyia mapato (POS) katika halmashauri mbili, mwaka 2019/2020 kulikuwa na mashine 1,469 za kukusanyia mapato (POS) katika halmashauri 54 na mwaka 2020/2021 kulikuwa na mashine 1,355 katika halmashauri 46 ambazo hazikuwa hewani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya maboresho ambapo matumizi ya mashine za kukusanyia mapato kupitia mfumo wa LGRCIS yatakoma ifikapo tarehe 30Juni, 2023 hivyo kuanzia tarehe 1 Julai, 2023 hakutakuwa na POS zitakazokuwa offline zaidi ya saa 24.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasimika taa kwenye barabara za mitaa Mji wa Masasi ili kuongeza usalama, kupunguza uhalifu na kuhamasisha shughuli za biashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa uhitaji wa taa za barabarani katika Halmashauri ya Mji wa Masasi kutokana na kukua kwa shughuli za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa wedha wa 2022/2023, Serikali kupitia TARURA - Wilaya ya Masasi imetenga shilingi milioni 192 kwa ajili ya kusimika taa 48 kwenye barabara za Mji wa Masasi ambazo zitawekwa kwenye barabara za TANESCO - Yatima na Barabara ya Mkapa.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza: -

Je, lini Serikali itapunguza tatizo la upungufu wa walimu katika Shule za Sekondari Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza kupunguza tatizo la upungufu wa Walimu u katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, walimu 50 walipelekwa katika shule zilizopo Babati Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetangaza nafasi 13,390 za ajira kwa walimu ambapo baadhi ya walimu hao watapangiwa katika Shule zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri walimu na kuwapeleka katika shule zote nchini hususan katika maeneo yenye uhitaji kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaipandisha hadhi Zahanati ya Solwa kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalamu katika Zahanati ya Solwa ili kuona kama inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi Mkoa utakapojiridhisha na miundombinu iliyopo, watawasilisha ombi hilo Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya kwa ajili ya hatua za kuipandisha hadhi Zahanati ya Solwa na kuwa Kituo cha Afya.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaowaongezea posho Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliongeza posho za Madiwani ambapo mwaka 2012 posho hizo ziliongezwa kutoka shilingi 120,000 hadi shilingi 250,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipandisha tena posho za Madiwani kupitia waraka wa mwaka 2014 kutoka shilingi 250,000 hadi shilingi 350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40 na shilingi 400,000 kwa Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya ukosefu wa Vituo vya Afya katika Jimbo la Tabora Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Misha. Aidha, ujenzi wa Jengo la OPD na Maabara umekamilika na Kituo hicho tayari kimesajiliwa na kimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje, ujenzi wa Jengo la wazazi, jengo la upasuaji na jengo la OPD lenyewe upo hatua za ukamilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye maeneo ya kimkakati ikiwemo vituo vya afya katika Jimbo la Tabora Mjini.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, lini shule za Sekondari Nyamtukuza, Muhange, Shuhudia, Kasanda na Gwanumpu zitakuwa za kidato cha tano na kidato cha sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Muhange imekaguliwa na wadhibiti ubora wa shule ikaonekana ina mapungufu ya mabweni mawili, mapungufu hayo yakikamilishwa itapandishwa hadhi ya kuwa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, Shule za Nyamtukuza, Shuhidia, Kasanda na Gwanumpu zinaendelea kuongezewa miundombinu ya majengo, ikikamilika zitakaguliwa na wadhibiti ubora wa shule na kuombewa kupandishwa kuwa za Kidato cha Tano na Sita. Hata hivyo, shule moja mpya ya kidato cha tano na sita imesajiliwa ambayo inaitwa Amani Mtendeni.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE K.n.y. MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -

Je, lini Serikali itatangaza Mamlaka ya Mji Mdogo Bagamoyo kuwa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokea mapendekezo ya kupandishwa hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya tathmini ya kina imebainika kuwa, Halmashauri hii bado ina upungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii na mapato yasiyotosheleza kuipandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo kuwa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuboresha miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo na siyo kuanzisha maeneo mapya.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza: -

Je, kiasi gani cha bajeti kimetengwa TARURA miaka mitatu mfululizo kwa ajili ya ukarabati wa barabara Kyerwa na upi ufanisi wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha wa 2020/2021 hadi 2022/2023, Wilaya ya Kyerwa imetengewa jumla ya shilingi bilioni 7.34, ambapo mwaka 2020/2021 shilingi bilioni 1.26 zilitengewa, mwaka 2021/2022 shilingi bilioni 2.89 na shilingi bilioni 3.18 zimetengwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, ufanisi uliopatikana ni kuwa, barabara zenye kiwango cha changarawe zimeongezeka kutoka kilomita
185.46 hadi kilometa 261.71 na barabara za udongo kupungua kutoka kilomita 711.96 hadi kilometa 634.81 na makalvati 95 yamejengwa, ikiwa ni pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilometa 4.2 katika Makao Makuu ya Wilaya na Mji Mdogo wa Biashara wa Nkwenda.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ambayo ujenzi wake umesimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela inatekeleza ujenzi wa jengo la ghorofa la kutoa huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya wilaya. Utekelezaji wa mradi ulianza Septemba, 2019 chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama ya shilingi bilioni 3.81. Aidha, hadi kufikia Aprili, 2023 Serikali imeshatoa shilingi bilioni 2.75 na ujenzi umefikia asilimia 72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi, na Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi wa Kilimanjaro kwa kumalizia ujenzi wa maboma ya zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi bilioni 1.96 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 37 katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.35 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya vitatu na zahanti 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya vituo vya afya na zahanati nchini kote.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa kibali cha ajira za watendaji wa kata na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilikuwa na upungufu wa watendaji wa vijiji 33. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro imeajiri watendaji wa vijiji 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro imeomba kibali cha kuajiri watendaji wa kata saba na watendaji wa vijiji 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendela kuajiri watendaji wa vijiji na kata katika halmashauri zote inchini iliwemo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati majengo ya shule za msingi chakavu Wilayani Masasi yaliyojengwa kati ya mwaka 1905 na 1960?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Cecil Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ina jumla ya shule za msingi 40 ambazo ni kongwe na chakavu. Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imepeleka shilingi milioni 200 katika shule kongwe na chakavu za Liloya na Lusonje kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na tayari yamekamilika. Aidha, shilingi milioni 180 zimepelekwa katika Shule Kongwe ya Luatala kwa ajili ya ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa, na taratibu za ujenzi zimeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule nyingine kongwe za Mkalapa, Rivango, Chikoropola, Mwena na Lulindi Maalum zimetengewa fedha kupitia mradi wa BOOST na utekelezaji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, lini barabara ya Mombo Mzeri itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mombo - Mzeri ina urefu wa jumla ya kilometa 30 inayounganisha barabara kuu ya Segera – Same na Makao Makuu ya Kata ya Magambakwalukonge, Mkalamo na Wilaya ya Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza kufanya Upembuzi yakinifu na Usanifu wa kina katika barabara hii na kazi hii inatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 ili kupata gharama halisi za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA imeendelea kuimarisha barabara hii kwa kiwango cha changarawe pamoja na kujenga vivuko na makalavati ili kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Kituo cha Afya cha Msanda Muungano katika Tarafa ya Mpui?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kukarabati vituo vya afya vikongwe nchini kikiwemo Kituo cha Afya Msanda Muungano kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuongezea miundombinu ili kuviwezesha kutoa huduma muhimu ikiwemo upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Afya ikiwemo kituo cha Msanda Muungano katika Tarafa ya Mpui.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isikae na taasisi za afya za kidini Wilayani Muleba ili kupunguza changamoto zilizopo katika kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Jimbo la Muleba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ina vituo sita vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na mashirika ya kidini. Hospitali tatu za Lubya, Ndolage na Kagondo, Kituo cha Afya kimoja na zahanati mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao utaratibu wa kukaa na hospitali teule za wilaya kupitia bodi ambazo zimejumuisha wataalam wa kutoka ngazi ya mkoa na halmashauri husika. Bodi hizo hukutana kila robo mwaka kwa ajili ya kupitia taarifa za utendaji pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wakutoa huduma.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, lini Barabara ya Majengo – Ruvuma – Subira - Muungano itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza mipango ya ujenzi wa Barabara ya Majengo – Ruvuma - Subira na Muungano kwa kiwango cha lami ambapo katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024, jumla ya shilingi milioni 517.50 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami nyepesi kilomita moja.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu ya maji mashuleni ili kuepusha milipuko ya magonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa shule zote za Msingi na Sekondari zinakuwa na miundombinu ya maji safi na salama pamoja na vifaa vya kunawia mikono vikiwemo ndoo, jaba tiririka na miundombinu iliyojengwa kwa pamoja (mass handwashing facilities). Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia mradi wa usafi na mazingira (SRWSS) imejenga miundombinu bora ya kunawia mikono pamoja na vifaa vya kuhifadhia maji katika shule za msingi 1853.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha usafi mashuleni kupitia vilabu vya uhamasishaji usafi mashuleni (Swash Clubs).
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa ujenzi wa soko la kisasa Tengeru utatekelezwa ili kuongezea mapato na kuboresha huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. John Danielson Pallangyo, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Meru imetenga eneo la Madiira lenye ukubwa wa ekari
15.5 kwa ajili ya ujenzi wa soko litakalokuwa na miundombinu muhimu ya soko ikiwemo huduma za wafanyabiashara wadogo wadogo.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri inaandaa michoro ya soko la Madiira na itakapokamilika itawasilisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI kama mradi wa kimkakati kwa hatua zaidi.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuweka utaratibu kwa wananchi kuwasilisha Hoja Binafsi mbele ya Mabaraza ya Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Halmashauri, Mwananchi wa kawadia hawezi kuwasilisha hoja binafsi katika Vikao vya Baraza la Madiwani kwa kuwa tayari yupo mwakilishi wake katika kikao hicho ambaye ni Diwani wa Kata husika.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza majengo katika Kituo cha Afya cha Matamba Wilayani Makete?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2022 Serikali ilitenga na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vinne vya Ipelele, Kitulo, Bulongwa na Lupalilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati ikiwemo kuongeza majengo ya Kituo cha Afya Matamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete kadri ya fedha zitakavyopatikana.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya kwenye Kata zilizopo pembezoni mwa Tabora Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkakati wa kujenga vituo vya afya katika kata za pembezoni Tabora ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Misha. Aidha, ujenzi wa Jengo la OPD na Maabara umekamilika na kituo hicho tayari kimesajiliwa na kimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje, ujenzi wa jengo la wazazi, jengo la upasuaji upo katika hatua za ukamilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati nchini yakiwemo maeneo ya pembezoni ikijumuisha maeneo ya Jimbo la Tabora Mjini.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabainisha mipaka ya Kata ya Wariku - Bunda Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mipaka kati ya Kata ya Wariku na kata za jirani katika Wilaya za Butiama na Musoma zilianza kutatuliwa kwa njia ya vikao kati ya Mkurugenzi wa Mji wa Bunda na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Musoma na Butiama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya vikao hivyo, wataalam waliweza kuwakutanisha Viongozi wa Mitaa ya Kata ya Wariku na Vijiji vya Kata za Kyanyari (Butiama) na Suguti (Musoma Vijljini) na kutafasiri mpaka huu ardhini na kugundua kuwa sehemu ya Mto Wariku ulimeguka na kuacha njia yake ya asili kutokana na shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwa na suluhu ya kudumu, zitawekwa nguzo ndefu na pana (pillarrs) zinazoweza kuonekana na kila mwananchi. Kazi ya maandalizi ya nguzo hizo inaendelea na itakapokuwa tayari wataalam watarudi uwandani kwa ajili ya kuzisimika.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga vyumba maalum vya kuweka mitambo ya x–ray na ultra sound katika Kituo cha Afya Upuge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018, Serikali ilitenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Upuge kwa kujenga jengo la wazazi, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba ya mtumishi na njia ya kupita wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika vituo vya afya nchini kwa kuendelea kujenga majengo ya kutolea huduma muhimu ikiwemo huduma za mionzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga vyumba maalum vya kuweka mitambo ya X– Ray na Ultra Sound katika Kituo cha Afya Upuge kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga shule ya Bweni ya Wasichana katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Kondoa tayari ina shule moja ya wasichana ya Serikali inayoitwa Kondoa Girls. Shule hii ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 660. Kwa sasa shule ina wanafunzi 572 wa kidato cha tano na sita na Halmashauri imeomba kuongezewa mchepuo wa HGE ili iweze kutumika kwa full capacity.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuongeza shule za bweni za wasichana kulingana na uhitaji na upatikanaji wa fedha.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa majengo yaliyobaki ya Kituo cha Afya Mlimba utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mbili; jengo la upasuaji na nyumba ya mtumishi katika Kituo cha Afya Mlimba. Ujenzi wa majengo hayo umekamilika na kwa sasa kituo kinatoa huduma katika ngazi ya kituo cha afya ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura wa akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki ya Kituo cha Afya Mlimba, kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA K.n.y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati Vituo vya Afya ili kuendana na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango na mikakati madhubuti ya kujenga na kukarabati vituo vya afya nchini ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 jumla ya Shilingi bilioni 118 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 236 katika Kata za kimkakati nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya Afya nchini, kiasi cha Shilingi bilioni 8.75 kimetengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vipya 15 na ukamilishaji wa vituo vya afya vitano. Vituo hivi vya afya vinapaswa kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja Mfuko wa Afya wa Jamii ulioboreshwa (iCHF).
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Bajeti ya TARURA inazingatia mitandao ya Barabara katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la msingi la TARURA ni kuhakikisha kuwa bajeti inayotengwa inaendana na mtandao wa barabara zilizopo katika Halmashauri nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kendelea kutekeleza jukumu hili, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya barabara ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 962.48 kilitengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Kumekuwa na ongezeko la bajeti ambapo shilingi bilioni 2.31 zimetengwa kwa ajili ya kazi za barabara katika Wilaya ya Rungwe.
MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza: -

Je, ni lini Mradi wa DMDP Awamu ya Pili utaanza kwa lengo la kutatua changamoto ya miundombinu Kigamboni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa DMDP Awamu ya Pili kupitia mkopo wa Benki ya Dunia unatarajiwa kuanza mwezi Februari, 2024 na utahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, mifereji ya maji ya mvua pamoja na madaraja. Kwa sasa mradi upo katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu. Hatua hiyo itakapokamilika, ombi la fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo litawasilishwa Benki ya Dunia.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kujenga kilometa moja ya lami nyepesi Mabira Station ili kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara hiyo ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 shilingi milioni 117.14 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa saba za barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, shilingi milioni 83.1 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa nne kwa kiwango cha changarawe na ujenzi umekamilika. Vilevile katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, barabara ya Mabira Station imetengewa shilingi milioni 47.6 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga kilometa moja ya lami nyepesi Mabira Station kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali iliajiri watumishi 7, 736 wa Afya na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilipangiwa watumishi 104 na watumishi saba walipangwa Hospitali ya Halmashuri ya Wilaya ya Meatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2022/2223, Serikali itaajiri watumishi wa kada ya afya 8,070. Aidha, baada ya taratibu za ajira kukamilika watumishi hao watapangwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Meatu.
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mabweni yaliyoanzishwa na wananchi kwa michango yao katika shule za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali iliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 9.21 kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni 461, kati ya hayo mabweni 28 ni kwa ajili ya shule za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mabweni ili kuunga jitihada zilizofanywa na wananchi za kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mabweni kila mwaka kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya mchepuo kwenda Moshi kupitia Chekereni – Kahe – Mabogini - TPC kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 kujengwa kwa kiwango cha lami. Hadi sasa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro imefanya usanifu wa barabara yote kilometa 31.25 ambapo kwa kuanzia makisio ya ujenzi wa kilomita 12 kwa kiwango cha lami yenye jumla ya shilingi bilioni 15 yamewasilishwa TARURA makao makuu kwa hatua zaidi.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara za mitaa za Mkoa wa Dar es Salaam kwa mfumo wa EPC+F kwa vile Mradi wa DMDP haukidhi haja?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa maandalizi ya Mradi wa DMDP Awamu ya Pili. Tayari wataalam washauri watatu wanaendelea na kazi ya usanifu ambapo mkataba wa kazi hiyo utafanyika kwa muda wa miezi sita kuanzia Tarehe 30 Mei, 2023. Mara tu usanifu utakapokamilika, taratibu za ununuzi wa kuwapata wakandarasi zitaanza kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, EPC+F ni mfumo wa ujenzi wa kimkataba ambapo mkandarasi anafanya usanifu, ununuzi, ujenzi na kugharamia kazi za ujenzi (engineering design, procurement, construction and financing). Serikali kupitia TARURA bado haijaanza kutekeleza mfumo huu. Serikali inapokea ushauri na itapitia na kuufanyia kazi.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023, Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP ilitoa shilingi bilioni 1.054 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za Gicheri na Nyagisese zenye miundombinu yote ya madarasa, maabara, jengo la utawala na chumba cha kompyuta. Shule hizo zitakapokamilika zitaongezewa miundombinu ya mabweni ili ziweze kudahili wanafunzi wa kike.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Stendi ya Mabasi yaendayo Mikoa ya Kusini katika eneo la Mbagala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na stendi ya mabasi yaendayo kusini katika eneo la Mbagala. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaendelea na taratibu za kupata eneo la kujenga stendi hiyo katika Kata ya Mbagala. Pindi eneo litakapopatikana ujenzi utaanza.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Vituo vya Afya vya zamani ikiwa ni pamoja na kujenga Chumba cha kuhifadhi Maiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya. Tayari Ofisi ya Rais TAMISEMI, imekwishakusanya orodha ya vituo vya afya vinavyohitaji ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais TAMISEMI, ilipoanza kusimamia mpango maalum wa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya msingi mwezi Oktoba 2023, jumla ya vituo vya afya 379 kati ya vituo vya afya 697 vimekarabatiwa na kuongezewa miundombinu iliyopungua ikiwemo wodi za uzazi, vyumba vya upasuaji na majengo ya kuhifadhia maiti. Jumla ya majengo 117 ya kuhifadhia maiti yamejengwa na kuwekewa majokofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kukarabati vituo vya afya 50 kupitia fedha za Mfuko wa Afya wa Dunia, ili kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa mama mjamzito. Serikali, itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati vituo vya afya ili kuviwezesha kutoa huduma zinazokosekana likiwemo jimbo la Kalenga.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya kujenga Kituo cha Afya Kata ya Kasanga itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasanga kama iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyotembelea Kata ya Kasanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Kasanga kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa stendi ya Wilaya ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kuwa na Stendi ya Mabasi na kwa kuzingatia umuhimu huo tayari imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 22 na tathmini ya gharama za ujenzi wa stendi hiyo ni takribani milioni 643.82.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuanza na kukamilisha stendi hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba inashauriwa kuandaa andiko la mradi huo ili liweze kutumika kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huo kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Pugu - Majohe - Viwege njia nne na Kampala - Bwera - Rada hadi Chuo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikizifanyia matengenezo barabara za Jimbo la Ukonga zikiwemo barabara za njia nne Pugu – Majohe hadi Viwege na Kampala – Bwera – Rada hadi Chuo ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 jumla ya shilingi milioni 701.67 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo yenye urefu wa kilomita 20.7 na kazi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la matumizi katika barabara hizo limesababisha matengenezo yanayofanyika kutokudumu kwa muda mrefu. Hivyo Serikali imeingiza barabara hizi katika mpango wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili, ili barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mradi upo katika hatua za awali za kufanya usanifu.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuubadilisha Mkoa wa Dar es Salaam kwa kujenga barabara za mitaa, mifereji na miundombinu mingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 – 2022/2023 Serikali ilitenga shillingi bilioni 100.06 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara ambapo kilomita 47.77 za lami, kilomita 1,896.966 za matengenezo ya barabara, madaraja na makalvati 70 pamoja na taa za barabara 862. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya shilingi bilioni 48.68 zimetengwa kwa ajili ya kazi ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango uliopo sasa ni wa kuanza utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II), pamoja na maboresho ya Mto Msimbazi na Daraja la Jangwani. Miradi hii itahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara, mifereji ya maji ya mvua pamoja na madaraja.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, lini Mradi wa TACTIC utaanza Singida Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Singida ni miongoni mwa Miji 45 ambayo imepewa kipaumbele cha kupata ufadhili wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji, Manispaa na Majiji ya Tanzania ambao unaitwa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC) Project. Ufadhili huu ni wa Serikali Kuu kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia ambapo unaratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mradi huu unatekelezwa katika Miji ya Tanzania kwa awamu tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ina Miji 15 ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Singida. Serikali inatarajia kutangaza zabuni za kuwatafuta wasanifu (Design Consultants) mwishoni mwa mwezi Mei, 2023 ambapo wasanifu watakapopatikana wataanza kazi ya usanifu mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024 na ujenzi utaanza mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:-

Je, lini barabara ya Hilbadaw – Bashnet itahamishiwa TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya mwaka 2009 Kifungu 43(1) na (2) na kifungu 44(1) kupitia Tangazo la Serikali Na. 21 ya tarehe 23 Januari, 2009, imeainisha vigezo vya utaratibu wa kuhamisha barabara ili iwe chini ya TANROADS ambapo barabara inaweza kupandishwa au kuteremshwa kutoka daraja moja kwenda daraja lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sheria hii, barabara ambayo inakidhi vigezo kutoka daraja la barabara ya Wilaya kwenda daraja la barabara ya Mkoa (kusimamiwa na TANROADS) inatakiwa ijadiliwe kwenye kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa na ikionekana inakidhi vigezo, Bodi hiyo kupitia Mwenyekiti itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara husika, kwamba barabara hiyo imekidhi vigezo na kupandishwa hadhi. Hivyo, nashauri kwamba utaratibu huo uzingatiwe katika kupandisha hadhi barabara ya kutoka Hirbadaw – Bashinet kwenda TANROADS.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali katika kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa walimu ili kuwaongezea morali ya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa kupeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya mafunzo kwa walimu ambapo shilingi bilioni 1.9 zimetumika. Aidha, vitendea kazi kama vile kompyuta, printa, photocopy na projector vimenunuliwa kwa ajili ya walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa vishikwambi kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari ili waendane na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.03 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na taratibu za ununuzi zinaendelea. Vilevile, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.04 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo 252 vya walimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuviimarisha vituo vya Walimu kwa ajili ya wao kukutana na kujengeana uwezo utakaowaimarisha katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji na itaendelea kuboresha maslahi ya Walimu kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga wodi katika Kituo cha Afya Kihangara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya Mbunge wa Jimbo la Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya nchini, Serikali imeanza na uboreshaji wa miundombinu ya Vituo vya Afya, kipaumbele kikiwa ni utoaji wa huduma za dharura na upasuaji ambapo fedha iliyotolewa ilielekezwa kujenga jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kufulia na nyumba ya mtumishi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) inakusudia kuanza ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa kwenye Vituo vya Afya ambavyo vilikwisha pokea fedha za ukarabati na ujenzi jumla ya vituo vya afya 807 vinahitaji kujengewa wodi za kulaza wagonjwa kikiwemo Kituo cha Afya Kihangara.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga madaraja katika Mto Garamoha, Isolo, Nyagokolwa, Mbogo na Mhuze Wilayani Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, TARURA iliajiri Mhandisi Mshauri ambao ni Chuo cha Ufundi Arusha kufanya uchunguzi wa kijiolojia katika Mto Garamoha ambapo kazi hiyo imekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 35. Kwa sasa TARURA inaendelea na usanifu wa daraja hilo kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji wa ujenzi wake.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mto Isolo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 41 kwa ajili ya kujenga daraja la mawe sehemu ya kwanza ya Mto Isolo. Ujenzi wa daraja la pili katika Mto Isolo usanifu wake utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa kutumia wataalam wa ndani wa TARURA.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mto Mbogo, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 40 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya usanifu wa ujenzi wa daraja kwa tekinolojia ya upinde wa mawe lenye ukubwa wa mita 15 ili kupata gharama halisi. Mto Mhuze umetengewa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kijiolojia ili kuwezesha kusanifu kwa daraja hilo.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa madaraja katika Mto Garamoha, Isolo, Mbogo na Mhuze utaendelea baada ya kukamilika kwa usanifu ili kupata gharama halisi za ujenzi.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa daraja la juu katika Mto Mwamanongu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 43 kwa ajili kufanya usanifu wa Daraja la Mto Mwamanongu. Usanifu huo umekamilika na jumla ya shilingi bilioni 7.5 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Serikali itajenga daraja hilo kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhudumia miundombinu ya Wilaya ya Meatu kwa kujenga, kukarabati na kufanya matengenezo ya barabara na madaraja kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -

Je, lini vifaatiba vya Hospitali ya Wilaya ya Buchosa vitanunuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 ilipeleka Bohari Kuu ya Dawa fedha shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa hospitali za halmashauri 67 zilizoanza ujenzi mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Buchosa ambapo kila hospitali ilitengewa shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 Hospitali ya Wilaya ya Buchosa imepokea fedha za ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba shilingi milioni 800 pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 596.

Mheshimiwa Spika, taratibu za kusimika vifaatiba vilivyopokelewa unaendelea kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Buchosa. X–Ray mashine tayari imefungwa tangu mwezi Aprili 2023. Tunsubiri wataalamu wa mionzi kutoka Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania kukagua na kutoa kibali ili utoaji wa huduma uweze kuanza.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA K.n.y. MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kutoa fedha za ujenzi wa vituo vya afya kwa kigezo cha idadi ya tarafa ni kuwanyima wananchi vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kati ya tarafa 570 zilizopo 211 hazikuwa na kituo cha afya hata kimoja, hivyo Serikali ilitoa kipaumbele cha ujenzi wa vituo vya afya kwenye tarafa ambazo hazina kituo cha afya. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilijenga vituo vya afya 234. Kipaumbele cha ujenzi kilizingatia tarafa ambazo kata zake hazikua na kituo cha afya. Aidha, ujenzi wa kituo cha afya ulizingatia kata za kimkakati.
MHE. MINZA S. MJIKA K.n.y. MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Kata ya Ihanu – Mufindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni moja ambapo shilingi milioni 500 ni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mgololo, shilingi milioni 150 ni kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji kwenye Kituo cha Afya Mbalamaziwa na shilingi milioni 350 ujenzi wa Kituo cha Afya Mdabulo. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 562 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la OPD Kituo cha Afya Ihalimba na shilingi milioni 120 ukamilishaji wa jengo la OPD Kituo cha Afya Mapanda.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya kwenye kata za kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Ihanu.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-

Je, kuna mwongozo unaoruhusu watu wenye ulemavu mmoja mmoja kukopeshwa fedha za Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mtu mwenye ulemavu mmoja mmoja kuweza kupata mkopo ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa. Mwaka 2021 Serikali ilitoa mwongozo wa kumwezesha mtu mmoja mmoja kukopa kwa kufanya maboresho ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 za Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, ambapo maboresho hayo yalihusisha kuongeza Kifungu kipya cha 6A(i) na (a) ambacho kwa sasa kinatoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye Ulemavu kukopa kutoka katika mikopo inayotolewa na Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuendelea kutoa elimu juu ya uwepo wa fursa hii kwa watu wenye ulemavu nchini kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, lini Sheria italetwa kupunguza michakato ya utangazaji wa Miradi ya TARURA na fedha kusimamiwa na Mameneja wa Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma imetungwa ili kuweka uwiano mzuri wa haki na ushindani katika Ununuzi wa Umma na hutumika kwa Taasisi zote za Serikali na siyo TARURA pekee. Kwa mujibu wa muundo wa TARURA, fedha zote za miradi na utekelezaji wake umekasimiwa kwa Mameneja wa Wilaya. Malipo yote huandaliwa na Meneja wa Wilaya na kutumwa kwa Meneja wa Mkoa kwa ajili ya uidhinishwaji na ulipwaji kupitia mfumo wa Malipo Serikalini (MUSE). Aidha, Ofisi ya Mkoa kwa kushirikiana na Ofisi ya Meneja wa Wilaya, itaendelea kufanya tathmini kuhakikisha miradi inafanyika kwa kuzingatia thamani ya fedha ili iweze kukidhi uhitaji wake.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-

Je, lini Serikali itawapa ajira za kudumu walimu walioajiriwa tangu mwaka 2002 kwa masharti ya ajira za muda Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2017 – 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua iliidhinishiwa na kuajiri walimu 13 ambao walitimiza sifa za kuajiriwa kwa masharti ya Ajira ya Kudumu na Malipo ya Uzeeni. Aidha, Walimu 29 wameajiriwa kwa masharti ya Ajira za Mkataba kwa kuwa walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 45. Walimu hawa walikuwa ni wakimbizi waliopatiwa uraia wa Tanzania baada ya kupata sifa kwa mujibu wa sheria.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, lini barabara ya Irambo - Nsonyanga ambayo inaunganisha barabara ya Isyonje – Makete hadi Njombe na TANZAM itapandishwa hadhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 09 Januari, 2023, kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Njombe kilifanyika ambapo moja ya barabara zilizopendekezwa kupandishwa hadhi ni Barabara ya Irambo – Nsonyanga yenye urefu wa kilometa 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara Katika Hadhi Stahiki (NRCC) ilifika Mkoani Mbeya tarehe 24 Februari, 2023 na kutembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi ikiwemo barabara ya Irambo – Nsonyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Kamati yamewasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Endapo barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya Mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa Kiwango cha lami barabara ya Getifonga – Mabogini – Kahe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 kuijenga kwa kiwango cha lami ambapo hadi sasa TARURA – Mkoa wa Kilimanjaro wamekamilisha usanifu kwa kiwango cha lami na inahitaji shilingi bilioni 28.59 ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 TARURA imetenga shilingi milioni 158.85 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kwa urefu wa kilomita 12 katika barabara hiyo na kazi imekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilometa 1.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwalo la Shule ya Sekondari Igwachanya Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa Mabwalo katika Shule za Sekondari nchini. Hata hivyo, natoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kuanza kutenga fedha kupitia Mapato ya Ndani kwa ajili ya ujenzi wa bwalo katika Shule ya Sekondari Igwachanya.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwezesha Shule za Kata kuwa pia za Kidato cha Tano na Sita kutokana na kuongezeka kwa ufaulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza shule za Kidato cha Tano na Sita kulingana na uhitaji. Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali ilisajili jumla ya shule 23 ambazo zilikuwa Shule za Kata kuwa Shule za Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza shule za Kidato cha Tano na Sita katika Halmashauri zote nchini kwa kuongeza miundombinu ya mabweni, madarasa mabwalo kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha na uhitaji.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Jengo la OPD katika Kituo cha Afya cha Kintinku ambacho kimeanza kutumika bila kuwa na jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Kintinku. Aidha, majengo matano yalijengwa ikiwa ni pamoja na jengo la Wazazi, jengo la Upasuaji, jengo la Kufulia, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetenga shilingi milioni 20 katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la OPD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu msingi katika vituo vya afya kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Kintiku.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika Kata ya Kwai na Makanya Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 234 kwenye Kata za kimkakati ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo iliyotengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Lunguza HC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu ngazi ya Afya ya Msingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini zikiwemo Kata za Kwai na Makanya.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, lini Shule ya Sekondari Kayuki itafanyiwa ukarabati kama alivyoagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kutekeleza agizo lililotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu la kukarabati Shule ya Sekondari Kayuki zinaendelea ambapo Halmashauri imekamilisha BOQ kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Kayuki na imebainika kuwa shilingi milioni 776 zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya kukarabati shule hiyo unaendelea ambapo ukarabati mdogo kwenye hosteli na jengo la utawala umefanyika kwa shilingi milioni 17.4. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukarabati shule hii kama alivyoelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Ikana – Chitete pamoja na kujenga kwa kiwango cha lami barabara za milimani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.03 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ambapo miamba ilipasuliwa kwenye kipande chenye urefu wa kilometa mbili ambacho kilikuwa na mwinuko mkali uliokuwa unafanya magari yashindwe kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi milioni 460 kwa ajili ya kuweka tabaka la zege la mita 200, ujenzi wa mifereji na kuongeza upana wa barabara kwa kujaza kifusi kwenye eneo la kona kali.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za vijijini zinazopita katika vilima vikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa mbili kwa kiwango cha lami katika Kilima Kikali wa Miyuyu - Ndanda na kazi imekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, shilingi milioni 825 zimetengwa kwa ajili ya kujenga kilomita mbili za lami, kilometa mbili kwa kiwango cha changarawe na kujenga daraja dogo (box culvert) moja katika kilima hicho ambapo kazi hizo zinaendelea kutekelezwa na zimefikia asilimia 52.2 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 jumla ya shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kilometa moja kwa kiwango cha lami katika kilima kikali cha Miyuyu-Ndanda na kiasi cha shilingi milioni 300 kimetengwa kujenga kilometa 0.5 kwa kiwango cha zege kwenye eneo la kilima katika Barabara ya Malatu Juu – Mnauke – Mitahu -Mkululu yenye urefu wa kilometa 16.4.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu na kujenga barabara zenye changamoto ya vilima vikali kwa kiwango cha lami kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha kwa kila mwaka.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaupa hadhi ya Manispaa Mji wa Kibaha ambao ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri huanzishwa au kupandishwa hadhi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014 ambapo umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuanzisha na kupandisha hadhi halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Aprili, 2023 Halmashauri ya Mji Kibaha iliwasilisha ombi la kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Manispaa. Maombi haya yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa kuzingatia vigezo vilivyopo.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kwamagome?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Mji Handeni, ilitengewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati ya Kwamagome na mwaka wa fedha wa 2021/2022 shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kwaluwala katika Kata ya Kwamagome.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatoa jumla ya Bilioni 117 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya ya Msingi kwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga pamoja na wataalam wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI), watafanya tathmini ya kina kuhusu kata hii na mara fedha zitakapopatika Kituo cha Afya katika Kata ya Kwamagome kitajengwa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kupata viwanja vya michezo na kuvilinda kwani baadhi ya shule zimetumia kujenga madarasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Costantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya vigezo vya kuanzishwa shule ni pamoja na uwepo wa viwanja vya michezo. Michezo ni muhimu kwa kuwa husaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kujenga akili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itafuatilia jambo hili na kujiridhisha, endapo kuna shule ambayo imetumia viwanja vya michezo kujenga madarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule pamoja na Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia kanuni na taratibu zote zinazohusu usajili na uendeshaji wa shule ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu iliyopo shuleni kama viwanja vya michezo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mnyamasi ili Barabara ya Kambanga-Ifinsi hadi Bungwe iweze kutumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto wanayopata Wananchi wa Kijiji cha Kambanga-Ifinsi wakati wa kuvuka Mto Mnyamasi na inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Mkataba wa ujenzi umesainiwa tarehe 11 Mei, 2023 na Mkandarasi yupo kwenye hatua ya maandalizi ya kuanza kazi ambayo inatarajiwa kukamilika Februari, 2024.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isiongeze kundi la wanaume kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEM naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290 Kifungu cha 37A ya mwaka 2018 na Kanuni za Usimamizi na Utoaji wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 na Kanuni za Marekebisho za mwaka 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria hii, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa ajili ya kuwezesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba kwa kuzingatia kwamba makundi haya hayawezi kupata mikopo katika taasisi zingine za kifedha kwa sababu ya kukosa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa mikopo hii kwa mujibu wa sheria na kanuni. Aidha, makundi mengine ambayo siyo walengwa wa mikopo hii wanashauriwa kupata mikopo kupitia taasisi zingine za fedha zinazohusika na utoaji wa mikopo. (Makofi)
MHE MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kwa kutengeneza barabara zote mbovu katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutengeneza barabara zenye hali mbaya katika Mkoa wa Simiyu kila mwaka kutokana na bajeti inayotengwa. Barabara zenye hali mbaya zimeendelea kupungua kutoka kilometa 1,512.71 sawa na asilimia 36.32 mwaka 2020/2021 hadi kilometa 1,126.38 sawa na asilimia 27.05 mwaka 2022/2023. Hii ni baada ya ongezeko la bajeti kutoka shilingi bilioni 5.13 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 18.38 kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 17.78 kwa ajili ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini katika Mkoa wa Simiyu kufanya ujenzi na matengenezo ya barabara za jumla ya kilometa 995.21 ambazo zitapunguza barabara zilizo na hali mbaya kutoka asilimia 27.05 hadi asilimia 19 ya mtandao unaohudumiwa na TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuzihudumia barabara za Mkoa wa Simiyu kwa kutenga bajeti kwa ajili wa ujenzi na matengenezo ya barabara hizo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la upungufu wa Walimu wa Shule za Msingi katika maeneo ya Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu Mwaka wa Fedha 2018/2019 hadi mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeajiri jumla ya Walimu 26,598 wakiwemo 16,640 wa Shule za Msingi na 9,958 wa Shule za Sekondari. Kati ya walimu hao, walimu 1,111 walipangiwa kazi Mkoa wa Tabora na kupelekwa kwenye shule mbalimbali. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeajiri na kuwapangia vituo Walimu 13,130 nchini zikiwemo shule za Mkoa wa Tabora. Kati yao 7,801 ni wa shule za msingi na 5,329 wa shule za sekondari.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI K.n.y. MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa huduma ya kifungua kinywa kwa wanafunzi wa shule za msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma ya chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni wakati wa masomo katika kupunguza utoro, kuongeza usikivu na kuboresha afya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa wanafunzi Elimumsingi unaoelezea taratibu za mifumo ya uchangiaji wa huduma ya chakula shuleni. Aidha, Serikali iliwaelekeza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri kusimamia mwongozo wa Lishe wa Mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii, kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuona namna bora ya utekelezaji wa mwongozo wa lishe na kuwawezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Ofisi za kisasa za Walimu katika kila shule nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Miradi ya Kuboresha Elimu ya Msingi (BOOST) na Sekondari (SEQUIP) imeendelea na azma ya kuboresha Sekta ya Elimu Nchini kwa kujenga shule mpya za msingi na sekondari, ambapo hadi sasa shule 231 za sekondari zimeshajengwa na ndani yake kuna majengo ya utawala ambayo ni ofisi za Walimu za kisasa, vivyo hivyo kwa shule za msingi, shule zote mpya ambazo zinaanza kujengwa, hitaji hili limezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa BOOST shule nane za zamani zinakarabatiwa sambamba na uboreshaji wa Ofisi za Walimu. Uboreshaji utaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itatunga Sera ya Ugatuaji wa Madaraka na kutunga sheria ili kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mtaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha maandalizi ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka ambapo wadau mbalimbali wameshirikishwa na kutoa maoni yao. Aidha, Rasimu hiyo imewasilishwa katika ngazi ya maamuzi kwa mapitio na maelekezo zaidi.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Uyui - Tabora katika Kata ya Tura na Wilaya ya Ikungi – Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sekretarieti za Mikoa ya Tabora na Singida imeendelea kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui katika Kata za Tura na Wilaya ya Ikungi. Kamati za Ulinzi na Usalama za pande zote mbili zilikwisha kutana. Kila Mkoa ulipewa majukumu kwa ajili ya kutatua mgogoro huo kwa kufanya yafuatayo:

(i) Wataalam wa Wilaya zote mbili kufika uwandani ili kutafsiri ramani, kufuatilia historia ya eneo, kuandaa kikao cha Majadiliano ya Wataalam na kuandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa kuelezea yaliyobainika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wataalam wa Ardhi wa Wilaya ya Ikungi na Wilaya ya Uyui, wanapitia nyaraka mbalimbali yakiwemo matangazo ya Serikali (GN) yaliyoainisha Mikoa hiyo, ramani na mihtasari mbalimbali iliyohusika kupima Vijiji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani kuhakikisha uwepo wa walimu wa kutosha wa masomo ya hesabu na fizikia katika elimu msingi hadi kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI), alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuajiri walimu wapya wa masomo ya sayansi ili kukabiliana na upungufu uliopo ambapo kwa mwaka 2022/2023, tayari walimu 13,130 wameshapangiwa vituo vya kazi wakiwemo walimu wa masomo ya hesabu na fizikia.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza madaktari na watumishi wa kada nyingine katika Kituo cha Afya Mrijo chenye Daktari na Nesi mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilipata kibali cha ajira na kuajiri Watumishi wa Kada ya Afya 7,340 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipatiwa Watumishi 87. Kati ya hao, Watumishi wawili walipelekwa kwenye Kituo cha Afya Mrijo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeajiri Watumishi wa Kada za Afya 8,000, ambapo Halmashauri ya Wilaya Chemba nayo imepatiwa Watumishi wa Afya ambao watapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ukarabati wa madarasa, nyumba za Walimu na vyoo katika Shule za Msingi, Jimbo la Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu katika Shule za Msingi Nchini na kubaini uwepo wa miundombinu inayohitaji ukarabati mkubwa, ukarabati mdogo, kubomoa na kujenga upya na isiyohitaji ukarabati. Kwa kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 kipaumbele kitakuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na shule mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hali ya uchakavu kwa nyumba za Walimu, ni jukumu la Halmashauri kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika kukarabati nyumba za Walimu zilizopo kwenye maeneo yao na kuzitengea bajeti ili zikarabatiwe. Nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya ukarabati wa nyumba za Walimu na kuchukua hatua stahiki.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Je, nini mpango wa kuajiri waganga, watumishi wa afya na kupeleka vifaatiba kwenye zahanati na vituo vya afya nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira kwa watumishi wa kada ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi uliopo. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, iliajiri watumishi 7,732. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 tayari Serikali imeajiri watumishi 5,319 wa kada za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Kati ya hizo, shilingi bilioni 7.1 ni kwa ajili ya hospitali 71 za Halmashauri, shilingi bilioni 47.7 ni kwa ajili ya vituo vya afya 159 na shilingi bilioni 15 ni kwa ajili ya zahanati 300. Hadi kufikia mwezi Aprili 2023 jumla ya shilingi bilioni 58.85 zilikuwa tayari zimetolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya vifaatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 116.92 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Kata ya Enkikret - Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari imedhamiria kujenga shule za sekondari 26 za bweni za wasichana wanaosoma masomo ya sayansi kidato cha kwanza mpaka cha sita ambapo kila mkoa utajengewa shule moja. Ujenzi wa shule za bweni za wasichana za Mikoa unafanyika kwa awamu. Katika Awamu ya kwanza ya ujenzi Mikoa 10 imenufaika ambapo kiasi cha shilingi bilioni 30 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo na ujenzi upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi wa Shule ya Mkoa wa Arusha utafanyika katika awamu inayofuata hivyo ombi lake lipo kwenye utaratibu wa utekelezaji, wakati wowote fedha zitakapokuwa tayari, zitapelekwa Halmashauri husika kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je lini Serikali itajenga barabara ya mchepuko kutoka barabara ya Tanga - Horohoro - Chongoleani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inachepuka kutoka barabara ya Tanga - Horohoro kuelekea eneo ambalo kutajengwa bohari kubwa (depot) ya kupokelea mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi huu wa bomba la mafuta na ujenzi wa bohari kwa ajili ya upokeaji wa mafuta unaofanywa na Kampuni ya EACOP ambao ndiyo wasimamizi wa mradi huu, waliomba kibali cha kuimarisha barabara ya Chongoleani kwa viwango ambavyo vitaweza kuhimili uzito wa magari na mitambo itakayokuwa inapitishwa katika barabara hii kwa kipindi chote cha ujenzi wa mradi hadi utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kutokana na hali hiyo kwa sasa barabara hii inahudumiwa na EACOP kupitia Mkandarasi walieingia naye mkataba kwa kipindi chote cha mradi.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Mogitu – Dawar hadi Ziwa Chumvi ili kusafirisha chumvi ghafi kwenda kiwandani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang’ kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, shilingi milioni 188.73 zimetumika kwa ajili ya kufungua na kujenga makalavati manne katika barabara ya Dawar – Ziwa Chumvi ambapo awali ilitumika kama njia ya ng’ombe (Pario). Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kwenye eneo la kilometa 6.3 umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 53.34 kwa ajili ya kujenga kipande cha Barabara ya Endasak - Dawar inayoelekea Ziwa Chumvi chenye urefu wa kilometa nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuihudumia Barabara ya Mogitu – Dawar mpaka Ziwa Chumvi kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga barabara ya Ninde, Masokolo hadi Lupata katika Kata ya Kuzumbi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ninde – Masokolo – Lupata yenye urefu wa kilometa 40 inahudumia vijiji vitatu ambavyo ni Ninde, Masokolo na Lupata. Barabara hii ipo mpakani mwa Tanzania na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ni muhimu kwa shughuli za kufuatilia masuala ya kiusalama. Barabara hii haipo kwenye mtandao wa barabara za TARURA. Hivyo, barabara hiyo inahitaji kufunguliwa ili kuunganisha vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafungua barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha usafiri na usafirishaji.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga barabara za lami katika Mji wa Mombo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, TARURA ilitenga jumla ya kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuchonga na kuweka changarawe urefu wa kilometa 2.7, kujenga makalavati tisa, kujenga mifereji yenye urefu wa kilometa 1.9. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuchonga kilometa 2.84 kwa kuweka changarawe, ujenzi wa makalavati 23 na ujenzi wa mifereji urefu wa kilometa 2.46. Utekelezaji wa kazi hizi unaendelea na umefikia asilimia 56. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Mombo Mjini zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mara baada ya kuziimarisha kwa kiwango cha changarawe na ujenzi wa mifereji kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya Matwiga na Mafyeko Jimboni Lupa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 na 2021/2022 Serikali ilitenge kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Isangawana katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati nchini kote ikiwemo ukamilishaji wa vituo vya afya vya Matwiga na Mafyeko katika Halmashauri ya Chunya.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO aliuliza:-

Je, nini hatma ya Barabara ya Zakhiem Mbagala Kuu inayoshindwa kujengwa kwa kuwa bomba la mafuta lipo chini ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kijichi - Mbagala Kuu - Zakhiem ina urefu wa kilometa 5.1. Kati ya kilometa hizo kipande cha mita 600 ni sehemu ya bomba la mafuta la TAZAMA. Baada ya majadiliano ya mara kwa mara kati ya TARURA, TAZAMA na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, TAZAMA waliruhusu mita 200 kuwekewa tabaka la zege na tayari tabaka la zege limewekwa kwa gharama ya shilingi milioni 155.79 kupitia mradi wa DMDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kipande cha mita 400 kilichobaki, TAZAMA wameruhusu kiwekewe tabaka la changarawe pekee na sio kujenga barabara kwa kiwango cha lami au zege.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa sekta ya afya kufikia asilimia 50 ya mahitaji katika Halmashauri ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji makubwa ya watumishi wa afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yaliyosababishwa na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika ngazi ya afya ya Msingi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilipata kibali cha ajira na kuajiri watumishi wa kada ya afya 12,653 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepangiwa watumishi 68.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya kadri Bajeti ya Serikali itavyoruhusu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kupitia Bajeti ya Serikali Kuu?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura Na. 290, kila Halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa malipo ya posho kwa wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 222 kwa ajili ya matumizi mengineyo kwa halmashauri zote nchini. Hivyo Ofisi ya Rais – TAMISEMI inahimiza halmashauri zote nchini kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Mulungu Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kizazi. Aidha wananchi wa Kata ya Kizazi wamejenga jengo la OPD hadi kufikia hatua ya lenta.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini ikiwemo Kituo cha Afya katika Kata ya Mulungu.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuviwezesha Vikundi vya Wanawake vya Ufugaji Mkoani Tanga ili viweze kuongeza tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamilu Zodo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 hadi mwezi Machi, Halmashauri za Mkoa wa Tanga zimetoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.56. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi Bilioni 1.82 zimekopeshwa kwenye vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na biashara ndogondogo pamoja na ufugaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mchanganuo huo hapo juu, vikundi vya Wanawake 102 vyenye wanufaika 875 vinavyojishughulisha na kazi za ufugaji wa mifugo ya aina mbalimbali vimekopeshwa kiasi cha Shilingi Milioni 575 na kuweza kutengeneza ajira zipatazo 253.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya vifaa tiba katika Hospitali za Wilaya zinazojengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali ilitenga shilingi bilioni 7.1 kwa ajili ya vifaa tiba vya kinywa/meno na macho kwa hospitali 71. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 15.5 kwa ajili ya vifaa tiba kwenye hospitali 31 zinazoendelea na ujenzi kila moja imetengewa shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zote nchini ili kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuigawa Shule ya Msingi Mwanhuzi kwa kuwa shule hiyo ina wanafunzi 1,400?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Shule ya Msingi Mwanhuzi ina changamoto ya mlundikano wa wanafunzi. Katika kutatua changamoto hiyo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Mradi wa BOOST imepeleka shilingi milioni 348.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Mwanhuzi. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo, changamoto hii itakuwa imetatuliwa.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vya Afya Misenyi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na hadi kufikia Mei, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zimekwishatumika katika ujenzi wa majengo saba ya Hospitali ya Wilaya ya Misenyi na kiasi cha shilingi milioni 500 kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kimkakati cha Kanyigo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenge bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu msingi katika hospitali na vituo vya afya kote nchini vikiwepo vya Halmamashauri ya Wilaya ya Misenyi.
MHE.SYLIVIA F. SIGULA K.n.y. MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kizazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kizazi.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Halmashauri ya Sikonge itapatiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya Ipole, Kipanga na Usunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Tutuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mipango Madhubuti ya ujenzi wa vituo vya afya vikiwemo vituo vya afya vya Ipole, Kapanga na Usunga ili kuendelea kutoa na kuboresha huduma za afya nchini.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni nyumba ngapi zinahitajika kwa Watumishi wa Umma waliopo Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Mwenyekiti, ni kweli kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za watumishi waliopo vijijini hususan watumishi wa kada ya elimu na afya. Hadi Mei, 2023, idadi ya nyumba za walimu zilizopo vijijini ni 55,097 wakati upungufu ni nyumba 255,097. Aidha, kwa upande wa watumishi wa afya, nyumba za watumishi zilizopo ni 7,818 na upungufu ni nyumba 15,272.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 kupitia Mradi wa SEQUIP, Serikali imekamilisha mchakato wa kujenga nyumba 212. Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na upungufu wa nyumba za watumishi wa kada za elimu na afya hususan waliopo vijijini.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika Kata za Mji wa Tarime kwa kuwa kuna Kituo kimoja tu cha Afya Nkende?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kimkakati cha Ketare katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kujenga jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), Maabara, Jengo la Wazazi, Jengo la upasuaji na Jengo la Kufulia na ujenzi umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya katika Kata za kimkakati kote nchini, zikiwemo Kata za Mji wa Tarime.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -

Je, lini SACCOS 130 za wanawake na vijana zitaanzishwa katika mikoa 16 ikiwemo Kigoma kama ilivyoainishwa katika Ilani ya 2020/2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, ninaomba kujibu swali Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kuanzishwa kwa jumla ya SACCOS 41 kwenye Mikoa 16 zikiwemo SACCOS 03 za Mkoa wa Kigoma. SACCOS hizo ni Kasulu Women SACCOS yenye wanachama 100 ikiwa na mtaji wa milioni 44, Vijana Kidahwe SACCOS yenye wanachama 20 ikiwa na mtaji wa milioni 14, na Amani Wanawake SACCOS yenye wanachama 33 ikiwa na mtaji wa milioni 21.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha Mikoa ikiwemo Mkoa wa Kigoma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuanzisha na kuzisimamia SACCOS kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ili ziendelee kutoa huduma inayokusudiwa.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la ekari 1000 za Shirika la Elimu Kibaha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) aliuliza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Elimu Kibaha lina eneo lenye ukubwa wa hekta 1,358 katika Mji wa Kibaha. Eneo lenye ukubwa wa hekta 675.31 limeendelezwa kwa huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika. Aidha, eneo lenye ukubwa wa hekta 220.1 limetengwa kwa ajili ya upanuzi wa huduma za Shirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lenye ukubwa wa hekta 170.913 limetengwa kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa la kilimo cha umwagiliaji (block farming). Aidha, Shirika limetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 38.84 kwa ajili ya uwekezaji (investment hub) lililopo mkabala na barabara ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lililobaki lenye ukubwa wa hekta 252.837 linatumika kwa ajili ya huduma nyingine za kijamii ikiwemo Makanisa na Misikiti na lina miundombinu ya umeme, maji na limepitiwa na bomba la mafuta (TAZAMA).
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kabla zahanati haijafunguliwa inawekewa vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 15.15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati ambazo zimekamilika ambapo tayari Serikali imekwishatoa fedha shilingi bilioni 12.90.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 18.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati zote zinazoendelea kukamilishwa na itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya zahanati zinazoendelea kukamilishwa kwa kadri fedha zinavyopatikana.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kupandisha hadhi Mji wa Magugu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uanzishaji wa Mamlaka za Miji Midogo hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Mwongozo wa Uanzishaji wa Maeneo ya Utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 ambapo umeanishwa utaratibu na vigezo vinavyopaswa kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, kusudio la kupandisha hadhi Mji wa Magugu lipo katika hatua za upangaji wa Mji ikiwemo uandaaji wa mpango wa jumla na mpango kina ambapo ikikamilika itatangazwa kupitia gazeti la Serikali.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari katika Kata ya Mjimwema Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo ujenzi wa shule mpya unafanyika katika Kata ambazo hazina shule. Katika awamu ya kwanza shule 231 zimejengwa.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi unaendelea ambapo jumla ya shule 1,000 zitajengwa na mchakato wa kupeleka fedha kwa Halmshauri utakapokamilika fedha hizo zitapelekwa. Hivyo, Halmashauri iweke kipaumbele cha ujenzi wa shule hii kwenye mpango wake kwa awamu zijazo katika Kata ambazo hazina shule ikiwemo Kata ya Mjimwema Makambako.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kutenga fedha ili kuweka uwiano sawa kwa bajeti za Halmashauri kwani Halmashauri nyingi haziwezi kujiendesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua utofauti uliopo wa uwezo wa Halmashauri kujiendesha baina ya Halmashauri moja na nyingine kutokana na uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri. Kwa kutambua hilo, Serikali imeziweka Halmashauri kwenye madaraja manne kwa kuzingatia uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato kutokana na fursa za vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye eneo husika la utawala.

Mheshimiwa Spika, ili kuziwezesha Halmashauri zisizo na fursa za kukusanya mapato makubwa kujiendesha na kwa kuzingatia madaraja hayo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-

(i) Kuzipunguzia viwango vya upelekaji wa fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo;

(ii) Kuziondolea mchango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa Barabara;

(iii) Kuzisaidia kulipa stahiki za Viongozi hususan Wakurugenzi na Wakuu wa Idara;

(iv) Kuzisaidia kulipa posho za kila mwezi za Waheshimiwa Madiwani; na

(v) Kuziongezea viwango vya ruzuku ya matumizi ya kawaida na ruzuku ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuziwezesha Halmashauri zenye uwezo mdogo wa ukusanyaji wa mapato ili ziweze kujiendesha.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapandisha hadhi barabara ya Kwinji - Kilindi Asilia hadi Kimbe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kwinji - Kilindi Asilia hadi Kimbe ina urefu wa kilometa 43.7, barabara hii inaanzia Kata ya Msanja, inapita Makao Makuu ya Kata ya Kilindi Asilia na kuunganisha Kata ya Kimbe.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007, Kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya mwaka 2009 kifungu 43(1) na (2) na kifungu 44(1), kupitia Tangazo la Serikali Na. 21 ya tarehe 23 Januari, 2009 imeainisha vigezo vya utaratibu wa kuhamisha barabara ili iwe chini ya TANROADS ambapo barabara inaweza kupandishwa au kuteremshwa kutoka daraja moja kwenda daraja jingine. Mkoa unashauriwa kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha hadhi barabara hiyo kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa ili utaratibu ufuatwe.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mtwango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Sadan. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya na itapeleka fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mtwango pindi fedha zitakapopatikana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, lini Serikali itavigawa Vijiji vya Makangara, Mkomazi, Mkalamo, Mwenga, Kwemasimba, Mkwajuni, Sekioga na Bungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uanzishaji wa maeneo ya utawala hutekelezwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura Na. 287 na Na. 288 pamoja na mwongozo wa uanzishaji wa maeneo ya utawala wa mwaka 2014 ambao umeanisha utaratibu na vigezo vinavyopaswa kufuatwa. Miongoni mwa vigezo hivyo ni uwezo wa Halmashauri kujitegemea katika bajeti ya uendeshaji kutokana na mapato ya ndani, uwezo wa kutoa huduma za kijamii na kiutawala, upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na uwepo wa huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa kipaumbele kuboresha na kukamilisha miundombinu msingi kwenye maeneo yaliyoanzishwa ili yaweze kutoa huduma kwa jamii na baadae kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa kuwa ya Mkoa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mbeya kupitia kikao chake cha tarehe 9 Januari, 2023 kilitoa mapendekezo ya kuipandisha hadhi Barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa kuwa ya Mkoa. Baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, tarehe 24 Februari, 2023, Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara Katika Hadhi Stahiki (NRCC) ilitembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi Mkoani Mbeya ikiwemo Barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa.

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Kamati yamewasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Endapo barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati katika Kituo cha Afya cha Nanyumbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na uchambuzi na mapitio ya vituo chakavu vinavyohitaji ukarabati katika ngazi ya afya ya msingi ili bajeti ya Serikali ikiruhusu vituo hivyo chakavu viweze kufanyiwa ukarabati kikiwepo Kituo cha Afya cha Nanyumbu.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha changarawe barabara ya Mbinga, Kikolo hadi Kihungu ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) ajilibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanyia matengenezo Barabara ya Mbinga – Kikolo - Kihungu yenye urefu wa kilometa 36 ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021, barabara hii ilifanyiwa matengenezo sehemu korofi kwa gharama ya shillingi milioni 150. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, barabara hii imechongwa kwa urefu wa kilometa 30 na kuwekewa changarawe kilometa 14 kwa gharama ya shilingi milioni 247.12.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mlola Wilayani Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji ya kuwa na magari ya wagonjwa kwenye Vituo vya Afya na Hospitali ili kurahisisha huduma za rufaa kwa wagonjwa. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 35.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari 316 ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Spika, magari haya yameanza kupokelewa kwa awamu na yatagawiwa katika Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo itapata magari mawili kwa ajili ya huduma za rufaa za wagonjwa.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka lami walau kilometa 10 za barabara za ndani za Mji wa Katesh ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NGEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang’ kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TARURA imeanza utekelezaji wa ahadi hiyo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 470.61 zimetumika katika ujenzi wa barabara kilometa 1.12 kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, jumla ya kilometa 0.7 zimejengwa kwa kiwango cha lami na shilingi milioni 499.91 zimetumika. Kwa upande wa mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya ya shilingi milioni 941.96 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 1.2 na utekelezaji umefikia asilimia 30.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kulingana na upatikanaji wa fedha ili kukamilisha ahadi hiyo ya kukamilisha ujenzi wa kilomita 10 za barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Kibo – Mgombezi – Bagamoyo na NMB Benki hadi Magunga hospitali zilizo kwenye mradi wa TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Kibo - Mgombezi - Bagamoyo na NMB Benki hadi Hospitali ya Magunga zipo kwenye utekelezaji wa mradi wa TACTIC kundi la pili (Tier 2). Kundi hili linatekelezwa kwenye Miji 15 ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kazi ya usanifu wa miradi ya ujenzi wa barabara kupitia kundi la pili (Tier 2) unaendelea kutekelezwa na Wahandisi Washauri ambapo tayari walisaini mikataba tarehe 15 Disemba, 2023 na itafanyika kwa kipindi cha miezi nane ambapo kitakamilika mwezi Agosti, 2024. Aidha, usanifu wa miradi hiyo utakapokamilika Agosti, 2024 kazi ya kutangaza zabuni itaanza Septemba, 2024.
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga barabara ziendazo maeneo ya mazao ya kimkakati kama chai, kupitia mradi wa Agri-Connect - Lupembe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeainisha barabara zinazopita kwenye maeneo ya mazao ya kimkakati, ikiwemo zao la chai katika Jimbo la Lupembe, ambazo zina urefu wa jumla ya Kilometa 182.5. Kwa Mwaka wa fedha 2023/2024, usanifu wa Barabara ya Ukalawa – Kanikelele – Lupembe yenye urefu wa Kilometa 18.5, upo hatua za mwisho kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na mpango wake wa kutenga bajeti ili kuboresha barabara kwenye maeneo ya mazao ya kimkakati ikiwemo Jimbo la Lupembe. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa mawe Korongo la Starehe ambalo linahatarisha maisha ya wananchi wa Kata ya Nyamisangara, Tarime?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatenga shillingi millioni 280 kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi wa Korongo la Starehe lililopo Mji wa Tarime.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutoa chakula mashuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina wadau mbalimbali wanaounga mkono jitihada za Serikali katika utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni. Baadhi ya wadau hao ni kama vile Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), United Nations Children's Fund (UNICEF), World Vision, Feed the Children, SANKU, GAIN Tanzania, Project Concern International (PCI), CiC, Save the Children.

Mheshimiwa Spika, wadau hao hufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kuzijengea uwezo Kamati za Shule namna ya ushirikishwaji wa wazazi/walezi katika upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni, kutoa elimu ya uongezaji wa virutubisho katika chakula cha wanafunzi shuleni (fortified foods); kuhamasisha upatikanaji wa matumizi ya mazao lishe (biofortified) yakiwemo maharage, mahindi ya njano, kwa ajili ya uji wa wanafunzi; kushirikiana na shule zenye utayari wa kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya chakula kwa kugawa mbegu za mahindi na maharage shuleni; na kuandaa miongozo ya utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni.

Mheshimiwa Spika, mpango upo na unatekelezwa kwa kushirikisha wadau ili kuendelea na mpango wa kutoa chakula.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina utaratibu wa kukusanya takwimu za maboma yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweka mkakati na mpango wa ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Halmashauri ya Mbozi ina maboma mengi ya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Mwaka 2020/2021 kulikuwa na maboma 1,529 yakiwepo madarasa ya shule za msingi 1,513 na sekondari 86. Yaliyopo kwa sasa baada ya Serikali kwa kushirikiana na Wadau na wananchi kuyakamilisha ni ya shule za msingi 1,386 na sekondari 76 ambayo kati ya hayo 64 yamepauliwa. Aidha, maboma yaliyotengewa bajeti kwa kipindi cha 2023/2024 ni 18. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuyapunguza kadri inavyopata fedha.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa maabara ya sayansi katika shule za Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mpango wa kuboresha elimu ya sekondari katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga shilingi bilioni 5.148 kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara ili viweze kusambazwa katika shule za sekondari kote nchini ikiwemo shule za Mkoa wa Katavi. Ununuzi wa vifaa hivyo upo katika hatua za mwisho kulingana na taratibu za manunuzi.

Aidha, katika Mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka vifaa vya Maabara katika Shule za Mbede, Usevya, Mizengo Pinda, Mamba, Chamalendi, Kasansa, Kabungu, Karema, Mpandandogo, Kandamilumba, Mwese, Kapalamsenga na Homera zilizopo kwenye Mkoa wa Katavi.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa shule chakavu za msingi Jimbo la Kibiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza ukarabati wa shule chakavu ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilipeleka shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Kiasi. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali imepeleka shilingi milioni 180 kwa ajili ya kukarabati shule chakavu za msingi katika Jimbo la Kibiti ambapo jumla ya shule nne zitakarabatiwa ambazo ni Pongwe (maradasa matatu yalikarabatiwa), Mchinga (madarasa mawili), Saninga (madarasa mawili) na Misimbo (madarasa mawili).
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaingia ubia na Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) kuwajengea nyumba walimu nchini na kisha kuwakata mishahara yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba kwa ajili ya walimu ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2021 hadi 2023 zimejengwa nyumba 562 zenye uwezo wa kuchukua familia 1,124 kwa thamani ya shilingi 56,325,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni la msingi na linahusisha ujenzi wa nyumba ambazo itabidi Walimu wazilipie kupitia mishahara yao, Serikali itakaa kwanza na walimu ili kulijadili na endapo wataafiki wazo hilo litawasilishwa kwa Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) kwa ajili ya makubaliano.
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali vikiwemo vya ufugaji ambavyo wanawake wamehamasika ili wafuge kwa tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri za Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini, zimekuwa zikitoa mikopo ya uwezeshaji kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani. Mikopo hiyo imekuwa ikitumika kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo ufugaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023, Halmashauri za Mkoa wa Tanga zilitoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya shilingi bilioni 4.569 ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.827 zilikopeshwa kwa vikundi vya wanawake ambapo vikundi 102 vya wanawake vyenye wanufaika 875 vinavyojishughulisha na kazi za ufugaji vimekopeshwa kiasi cha shilingi milioni 575.39.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuviwezesha vikundi mbalimbali kwenye shughuli za uchumi na uzalishaji ikiwemo vikundi vya akina mama ili kutengeneza ajira, kipato na hivyo kupunguza umaskini.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Igurubi iliyopo katika Wilaya ya Igunga kuwa ya kidato cha tano na cha sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya shule zilizopendekezwa katika Tarafa ya Igurubi kuwa shule za A level ni Igurubi Sekondari na Mwamakona Sekondari. Suala lililokwamisha shule ya Igurubi kutosajiliwa ni kutokuwa na miundombinu Kama bweni, bwalo na miundombinu mingine wezeshi. Hivyo shule ikikidhi vigezo kwa mujibu wa miongozo na taratibu, itasajiliwa kuwa ya Kidato cha Tano na Sita.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, mpango wa kuugawa Mkoa wa Morogoro umefikia wapi hasa baada ya kuonekana kuwa na sifa ya kugawanywa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa huduma za kiutawala, kiuchumi, kijamii kupitia ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa katika maeneo ya utawala yaliyopo ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata na Vijiji, endapo kuna ulazima wa kuanzisha maeneo mapya, Serikali itatoa maelekezo muda muafaka utakapofika.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Msambiazi – Lewa – Lusindi hadi kwa Blue kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya kiasi cha shilingi milioni 470 zilitumika kujenga barabara kwa kiwango cha zege mita 824, mifereji urefu wa mita 600, kuchonga na kushindilia barabara urefu wa kilometa 16.5, kujenga madaraja madogo yaani box culverts matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Serikali imetenga jumla ya Shilingi millioni 400 kwa ajili ya kujenga mifereji na barabara kwa kiwango cha zege urefu wa mita 700 na kujenga madaraja madogo yaani box culverts matatu ambapo ujenzi umefikia asilimia 17.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha barabara hii kwa kuijenga kwa kiwango cha zege katika maeneo yote yenye changamoto hasa kwenye miinuko na utelezi kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri Walimu 13,130 ambapo Walimu 20 wa shule za msingi na 55 wa shule za Sekondari walipelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale. Serikali inatambua mahitaji ya Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale na maeneo mengine. Hata hivyo, kila mwaka Serikali inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kuhusu maboma ya majengo ya Nyumba za Walimu na Madarasa yaliyotelekezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathmini ya maboma ya nyumba za walimu ambapo jumla ya maboma 2,527 yamebainishwa. Ili kukamilisha maboma haya, zinahitajika shilingi bilioni 37.905 na kila boma litagharimu shilingi milioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madarasa, jumla ya maboma ya madarasa 10,106 yanayohitaji shilingi bilioni 126.6 yametambuliwa. Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ya nyumba za walimu na madarasa yaliyoanzishwa na wananchi.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, Serikali inafahamu kuna upungufu kiasi gani wa Walimu katika Halmashauri ya Mkalama na ina mpango gani kupunguza pengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2022 Serikali iliajiri Walimu 9,800 nchi nzima na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilipangiwa walimu wa ajira mpya 70, kati ya hao walimu 52 wa shule za msingi na 18 kwa shule za sekondari. Kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri walimu 13,130 na Halmashauri ya Mkalama ilipangiwa Walimu 92, kati yao walimu hao, 65 kwa Shule za Msingi na 27 kwa Shule za Sekondari. Serikali inatambua mahitaji ya walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na maeneo mengine. Hata hivyo, kila mwaka Serikali inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Shule ya Sekondari ya Hagati itapandishwa hadhi kuwa ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipeleka fedha shilingi milioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa bweni. Ujenzi umekamilika na taratibu za usajili wa kidato cha tano unaendelea. Tayari halmashauri imeomba kibali cha kupandisha hadhi ya kuwa kidato cha tano na sita, kwa barua yenye Kumb. Na. MDC/E.80/31/150 ya tarehe 15 Januari, 2024. Hivyo shule inatarajia kuanza rasmi kwa kidato cha tano na sita Julai, 2024.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2021/2022 jumla ya walimu wa Sekondari 7,799 na walimu 8,950 wa msingi waliajiriwa. Aidha, katika mwaka 2022/2023, walimu wa Sekondari 5,329 na walimu 7,801 wa Msingi wameajiriwa na kupangwa moja kwa moja katika shule kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwiano wa idadi ya wanafunzi kwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa walimu hao katika ufundishaji na ujifunzaji bora na kujenga nguvu kazi yenye maadili mema. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kulingana na mahitaji kwa shule zote nchini na uwezo wa kifedha wa Serikali. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Shule ya Sayansi ya Wasichana Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana kwa ajili ya masomo ya sayansi katika Mkoa wa Katavi unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo katika Kata ya Katalala ambapo hadi sasa ujenzi upo asilimia 80. Shule hii imesajiliwa na kuandikisha wanafunzi 100 wa kidato cha kwanza mwaka 2024.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, ni lini wazee wanaostaafu watapata mafao yao kwa wakati?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafao ya pensheni kwa wastaafu yanalipwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo zinaelekeza mifuko kulipa mafao ndani ya siku 60 tangu mwanachama anapostaafu. Kwa sasa, mifuko imeboresha mifumo yao na wastaafu wote wanalipwa mafao yao kwa wakati ndani ya siku 60.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-

Je, wahitimu wangapi wa vyuo wanafanya kazi ya kujitolea na wangapi wameajiriwa na kujiajiri baada ya kujitolea?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianza rasmi kuratibu utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa Wahitimu (internship) mwaka wa fedha 2019/2020. Tangu kuanza utekelezaji wa programu hii, jumla ya wahitimu 21,280 wamenufaika, ambapo wanaume ni 11,281 na wanawake ni 9,999. Miongoni mwa wanufaika hao, jumla ya wahitimu 3,772 wamepata kazi, wanaume wakiwa ni 2,265 na wanawake ni 1,507.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuna wengine wanaajiriwa Serikalini, sekta binafsi na nje ya nchi, lakini kazi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuwaongezea uwezo.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza umri wa Vijana kufikia miaka 40 kutokana na changamoto wanazopitia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, AJIRA, KAZI NA WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 na Mikataba Mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kama vile Mkataba wa Vijana wa Afrika wa Mwaka 2006 (African Youth Chater 2006), Sera ya Vijana ya Afrika Mashariki na Azimio la SADC kuhusu Maendeleo na Uwezeshwaji wa Vijana la Mwaka 2015 (SADC Declaration on Youth Development and Empowerment) inatambua kuwa umri wa kijana kwa Tanzania ni kati ya miaka 15 hadi 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu hizo, Serikali kwa sasa inaona ni muhimu kuendelea na tafsiri hii ya umri kwa vijana kama inavyotambuliwa na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika kukabiliana na ukuaji wa makazi yasiyopangwa, imeendelea kuchukua hatua mbalilmbali ambazo ni pamoja na kuendelea kuandaa Mipango Kabambe (Masterplan) yenye dira ya kusimamia ukuaji wa miji. Aidha, Wizara imeanzisha miradi na programu mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi hapa nchini.