Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omar Ali Omar (10 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia na mimi fursa hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu muumba wa mbingu na ardhi, aliyetuwezesha kusimama hapa na kukaa kitako huku tukiwa na hali ya afya njema wakati wenzetu wengine sasa hivi wako makaburini na wengine wako hoi bin taabani mahospitalini. Tuwaombee dua wote hao wapate nafuu ili tuungane nao katika kujenga Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kwanza kutoa shukrani zangu za dhati…

SPIKA: Mheshimiwa Khatib, vipi walioko mahospitalini wana nafuu?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, vizuri sana.

SPIKA: Aah, basi. Haya endelea Mheshimiwa Omar. (Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana..

Naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Wete, Pemba. Wengi wamezoea kule tuseme kwamba Wazanzibar walio wengi hasa wakiingia kwenye Kisiwa cha Pemba wanasema waja leo warudi leo? Kwa maana ya kwamba hiyo ni jumla ya question mark. Usiende ukarudi, ukienda ubakie.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakishukuru chama change cha ACT - Wazalendo. Kwanza namshukuru sana kiongozi wangu wa chama, Ndugu Zuberi Kabwe pamoja na Mwenyekiti wangu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Ndugu Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

SPIKA: Mheshimiwa Omar, samahani kidogo. Kwani hicho chama bado kipo?(Kicheko/Makofi)

MHE. OMAR ALI OMAR:Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naenda moja kwa moja kwenye hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwenye ukurasa wake wa 14 ambapo alitamka bayana katika hotuba yake ile kwa kusema kwamba katika kipindi hiki cha awamu yake ya tano ya miaka mitano inayofuata atatoa ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuleta maendeleo kwa pande zote za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Rais kwa hatua hiyo na kwa nia yake safi na tayari matunda yake tumeanza kuyaona, kwa sababu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tayari amepanga safu nzuri sana ya kuhakikisha kwamba sasa Zanzibar inafikia uchumi wa kati, kwa sababu ameanza kutumbua majipu. Nafikiri labda yeye kafuata kichogo cha mlezi wake, naukifuata kichogo cha mlezi wako, basi inawezekana wewe ukafanya vizuri zaidi kuliko hata mlezi wako huko nyuma kwa sababu kazi yako itakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia katika hoja hizo, kuangalia zaidi ya changamoto za Muungano. Zamani tulikuwa tunaziita kero, lakini siku moja nilikutana na Mheshimiwa Waziri akasema sasa tusiziite tena kero, tuziite changamoto. Na mimi nakubaliana naye kwamba changamoto hizo, kwa sababu tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Zanzibar, kero zile zinazofika nadhani 21 kama sikosei, tayari kero 11 zimeanza kupatiwa ufumbuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa Mheshimiwa Waziri anayehusika na Muungano akae chini na kutafakari na kutumia juhudi na maarifa na uwezo wake wote kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zimebakia basi zimeondolewa kabisa. Ili kwamba sasa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano tusizungumze tena kero, tuzungumze maendeleo. Baadhi ya kero hizo, ni wafanyabiashara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Endelea.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wa Zanzibar wanapochukua bidhaa zao kutoka Zanzibar na kuzileta Tanzania Bara, wanatozwa kodi mara mbili. Hilo ni tatizo kubwa ambalo ni moja katika vitu ambavyo vinatakiwa vipatiwe ufumbuzi.

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Omar, nakushukuru sana.

MFUNGE FULANI: Aunge mkono hoja. (Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ila ungeniongezea kidogo kwa sababu ulichukua muda wangu kidogo.

SPIKA: Unataka kuunga mkono hoja?

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, nilitaka uniongezee japo dakika moja.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Omar. (Kicheko)

Wiki ijayo tutakuwa na muda mwingi zaidi wa dakika kumi kwenye kujadili Mipango, kwa hiyo, utamalizia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, nipo ahsante sana na mimi kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii nyeti kabisa ya Muungano. Kwanza niwapongeze wote Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, na zaidi nakupongeza zaidi Mheshimiwa Chande kwasababu ni mwenzangu ananijua tunajuana. Tunapiga shamvi pamoja katika maeneo yetu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi nijikite kwenye Wizara hii inayohusiana na mambo ya Muungano kwenye sehemu zaidi ya Elimu ya juu. Kama tunavyojua kwamba Wizara hii ni Wizara nyeti sana katika kujenga mustakabali wa Taifa letu. Kwa bahati nzuri ni mwalimu ninapotokea miaka 22 nimefundisha, na nimeona matokeo mengi ambayo tunapokuja kufanya kazi inayohusiana na mambo ya Muungano zaidi katika Wizara yetu ya Muungano kwenye Sekta ya Elimu kuna vitu ambavyo kidogo vinaleta ukanganyifu kwa sababu ni Wizara ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, maombi yangu, zaidi ni kwenye suala zima linalohusiana na watendaji, watendaji wanaotoka visiwani kuja kwa wenzetu huku bara, kuja kufanya shughuli nzima inayohusiana na shughuli za Muungano zaidi kwenye sekta hii inayohusiana na Elimu ambayo pia ni Wizara ya Muungano. Kwa kweli kwa upeo wangu nimeona kwamba mahusiano yetu yanakuja katika sekta nyingi sana zinazohusiana na Muungano. Nikiangalia katika sekta hii zaidi kwenye suala la upatikanaji wa syllabus ambazo tunakuwa tunakwenda nazo kule visiwani na bara kwa ujumla. Tukiangalia kwenye syllabus zetu tunatakiwa tuwe na ulinganifu.

Mheshimiwa Spika, ulinganifu wetu unatakiwa kwenye syllabus ziwe zinalingana tokea from standard one au darasa la kwanza mpaka darasa la saba alafu tuje tuangalie curriculum yetu iendane sambamba na curriculum ile iliyopo bara ambayo ni ya kuanzia form one mpaka kufika madarasa ya juu zaidi form six.

Sasa hii ina ukanganifu mkubwa ukiangalia kwamba matokeo yanapotolewa wanafunzi wetu wengi wanakuwa wanafeli na wanafeli kwasababu mtaala unaotumika Zanzibar na Mtaala unaotumika huku Tanzania Bara unakuwa ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kuonyesha kwamba wanafunzi wetu wanaonekana kwamba siku zote wanashika nafasi ya mwisho zaidi Zanzibar, unasikia nafasi zile kumi za mwisho zinatoka Zanzibar, hii ni kwasababu kwamba sio kwamba wanafunzi hawana uwezo lakini wanauwezo mkubwa bali mitaala haiendi sambamba kwasababu kitengo kile kinachohusiana na elimu ya juu hakihusiana zaidi na kule Tanzania visiwani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili naomba sasa liangaliwe kwa kina kabisa ili kwamba mitaala yetu iende sambamba, kinachofanyika Tanzania visiwani from standard one hadi standard seven na sawasawa kiendane na bara na visiwani viwe ni vitu vinalingana, huo ndio mchango wangu siku ya leo kwenye suala zima la Muungano. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu- Wataala aliyetupa uhai wa kuimiliki siku ya leo tukawepo katika Bunge hili. Pia niwatakie mfungo mwema kwa wale Waislamu na wenzetu ambao sio Waislamu kwa kutuunga mkono kwa njia moja au nyingine katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kutoa kauli ya Mheshimiwa Marehemu Shaaban Robert; alizungumza katika kitabu chake cha Adili na Nduguze, akasema kwamba haja ikishughulikiwa kwa matendo humalizika upesi na ikishughulikiwa kwa maneno, huchelewa kama sadaka. Kwani tendo hukidhi haja maridhawa kulikoni maneno na mwenye matendo hula uhondo na asiye matendo hula uvundo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa ruhusa yako naomba nitoe kauli moja tu ya mshairi mmoja wa Kiarabu aliyesema kwamba Inna Safina Tajir illa ljabas. Hakika ya Safina haitembei katika nchi kavu. Nina maana ya kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, asiogope, asonge mbele na nina Imani kwamba Tanzania hii itapata maendeleo makubwa chini ya uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba sasa nijikite kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niende moja kwa moja katika ukurasa wa 71 ambao ulikuwa unazungumzia kuhusu cross cutting issues au masuala mtambuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Visiwa vya Zanzibar; Kisiwa cha Pemba ni kisiwa ambacho kina ukubwa wa square kilometer 198 na Zanzibar 1,666. Visiwa hivi vimebarikiwa na neema kubwa; vimebarikiwa na neema ya visiwa vidogo vidogo vilivyozunguka visiwa vikubwa hivi. Ila visiwa hivi vinapotea siku hadi siku. Suala la mazingira katika Visiwa vya Zanzibar ni tete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mnamo mwaka wa 1970 huko, kule Tanga Kisiwa cha Maziwe kilipotea na sasa hivi tunajivunia visiwa vyetu vya Zanzibar; na kauli njema kabisa inayozungumzwa hata na wahiribu wakubwa pale Zanzibar wanasema, “Zanzibar ni njema, atakaye aje.” Hata hivyo ukiangalia visiwa hivi ambavyo tunavinadi kwamba Zanzibar ni njema, atakaye aje, kila siku vinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka maji ya bahari yanakula 5% ya visiwa vile. Kuna maeneo mengine ambayo, bahati nzuri mwaka wa 2019 Mheshimiwa Zungu alifika sehemu moja inaitwa Sipwese Kengeja. Akatembelea katika lile eneo na akaitaka idara inayohusika kufanya upembuzi yakinifu ili kuona athari kubwa ya kimazingira iliyopo katika eneo lile. Kisiwa kimoja tu, ni eneo moja tu hilo ambapo athari yake mpaka sasa hivi tunavyoongea ni kwamba maji ya bahari yanaingia kuzuia kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wanaosoma katika shule, wanaotoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ambao ni vijana wanaotoka Sipwese kwenda eneo lingine la kisiwa wanafunzi wanashindwa kwenda kusoma. Hata Magereza wameyahama maeneo yao, haiwezekani kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa heshima kubwa na taadhima, basi tufanye upembuzi yakinifu katika visiwa hivi vya Unguja na Pemba kuona je, athari ya mazingira iko kwa kiwango gani ili tuvihame visiwa hivi tuweze kuringia Muungano huu wa Zanzibar na Tanganyika? Kwani vikipotea visiwa vya Zanzibar, tayari tutakuwa hatuna tena nchi ya kusema kwamba tuna Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nianze kwa kusema kwamba Waswahili wanasema, kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Pia kuna Mwalimu mmoja wa Kiswahili, Shaaban Robert katika kitabu chake cha Adili na Nduguze, alisema kwamba, haja ikishughulikiwa kwa matendo, humalizika upesi, lakini ikichelewa, huchelewa kama sadaka ikishughulikiwa kwa maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya matendo. Anawaachia watu wakazungumza maneno; na nime-quote speeches zake nyingi anasema kwamba, “kuna watu watatusikia, watatuona kwa matendo yetu lakini walio wengi watatupongeza na walio wachache watasema watabeza.”

Kwa hiyo, sote tuliomo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeziona juhudi za Mama Samia, amezifanya vizuri kabisa, hata kwenye Jimbo langu najisifia kwamba sasa hivi juhudi za Mama Samia naziona. UVIKO-19, kuna majengo ambayo yanajengwa ndani ya Jimbo langu kwa fedha za UVIKO-19. Zimetoka kwa nani? Kwa Mama. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba Mama ana juhudi kubwa kabisa ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano mmoja mkubwa kabisa ambao huo ni kisa maarufu na kinaendelea mpaka leo duniani. Mama Hajra wakati alikuwa anatafuta maji, alikuwa anakwenda Kusini na Kaskazini, Mashariki na Magharibi kutafuta maji; nani aliyekuwa akitafuta maji? Ni mama. Matokeo yake maji yalipatikana. Kwa hiyo, hii ni kuonesha kwamba mapambano ya mama, ni mapambano makubwa na ataendelea kupambana mpaka dakika ya mwisho kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono azimio hili kwa asilimia mia moja. Ni azimio ambalo lina mashiko, lina mwelekeo; na tumpe moyo Mama yetu aweze kutuongoza vizuri, na kila mtu aliyekuwa ana nia mbaya kwetu sisi na kwa Tanzania hii, basi Mungu ndiye anayejua vipi anaweza kumshughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nina ombi maalum kwa Bunge. Kwa vile tuzo aliyopewa mama ni ya kwetu, tutayarishe jambo maalum la kumpokea Mama katika tuzo hii ili tuone sasa kwamba kweli tunamthamini kwa tuzo hii aliyoipata ni ya Watanzania wote. Kwa hiyo, nasema kwamba Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kasema wanawake waende, lakini na wanaume sote twende tukaipokee hiyo tuzo. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa fursa hii ya kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na cabinet yake kwa kutuletea Bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba katika askari ambao wanastahili kupongezwa ni Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa sana nchini kwetu. Lakini Jeshi la Polisi linafanya kazi katika mazingira magumu mno. Jeshi la Polisi toka mwaka wa 2015 hawajapata nyongeza ya mishahara; Jeshi la Polisi halijapata increment; halijapata kupandishwa vyeo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani, hongera sana; huyo ni Mbunge wa ACT – Wazalendo.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, lakini kwa kweli kwa masikitiko makubwa, tena makubwa mno, ukienda hata majengo wanayokaa askari polisi ni majengo ambayo hayastahiki. Kwa mfano Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo natoka mimi, Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba hata nyumba ya kukaa hana. Mpaka sasa hivi tunavyoongea hana nyumba ya kukaa kwasababu ya kwamba nyumba ile imekuwa mbovu kabisa, hawezi kuishi. Kwa hiyo, hii ni kuonesha kwamba Jeshi la Polisi hatujalipa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna nyumba za maafisa ambazo zimejengwa kule Finya, Mkoa wa kaskazini Pemba, mpaka sasa hivi nyumba zile hazijamalizwa. Hata Naibu Waziri aliwahi kufika katika eneo lile na akaona majengo yale hali halisi yalivyo na akashindwa kushughulikia lile suala mpaka leo hii. Kwa hiyo, tunataka sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, je, nyumba ile itamalizwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukitoka maeneo hayo, Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Kaskazini Pemba haikaliki, inavuja kama pakacha. Kwa kweli inasikitisha sana, kuna vyumba ambavyo ndani ya ofisi ile hawafanyi kazi tena askari polisi kwasababu vimekuwa vichakavu na kwasababu ofisi inavuja sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenyewe binafsi tarehe 1 Machi nilifika katika Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba na kujionea kwa macho yangu kwamba lile eneo liko katika hali ya hatari. Jengo liko hatarini, toka mwaka wa 1970 mpaka kaja kalifungua Mheshimiwa Hayati Moringe Sokoine mwaka 1979, jengo lile mpaka leo halijafanyiwa ukarabati wa aina yoyote. Hii ni kuonesha kwamba askari wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, hilo tuliangalie.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama wanavyosema Waswahili, kidonda kikioza sana basi hata nzi hakitaki. Hii ni kuonesha kwamba hata lile jengo lenyewe la polisi, Kamanda wa Polisi hana hata pa kuishi, kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika eneo lingine la askari polisi; Kisiwa cha Pemba kina bandari bubu16. Kutokana na muda itaweza kuzitaja, lakini Pemba ina bandari bubu 16. Kwa hiyo, hizi bandari bubu ndiyo bandari ambazo zinatuhatarishia amani katika Kisiwa cha Zanzibar. Kwasababu kama tunavyojua kwamba mipaka yetu inahitaji kulindwa na askari polisi ni moja katika jamii ambao wanastahiki kulinda mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu hayo makubwa lakini askari polisi hawana vitendea kazi. Mkoa mzima wa Kaskazini Pemba una gari moja tu la Kamanda wa Polisi, magari yote yamelala, kwa sababu ya ukosefu wa vipuri, mafuta na upungufu pia wa askari. Kwa taarifa tu Mheshimiwa Maida alinifilisi kidogo lakini napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Kaskazini pekee una mahitaji ya askari 150 na hii ni kutonana na kwamba kumetokea mambo mengi; askari wameumwa, wengine wamestaafu na wengine wamefukuzwa kazi. Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo ya ukosefu wa askari, bandari hizi bubu ndizo ambazo zinatumika katika kuingiza uharamia wa kila aina ikiwemo madawa ya kulevya. Kule Zanzibar mahakama zetu zina kesi nyingi ambazo zinahusiana na madawa ya kulevya. Hii ni kuonesha kwamba maeneo ambayo yanatumika kupitisha madawa ya kulevya ni bandari bubu na idadi ndogo ya askari ambao tunao katika vituo vya polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha sana Kamanda ana dhamana ya kuwalisha mahabusu badala ya dhamana ile kuwa ya Serikali. Kwa kweli wanapata misaada kutoka kwa wasamaria wema, wenyewe wanawaita wafanyabiashara werevu wanaojua athari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Omar Ali Omar, dakika tano ni chache, lakini nakushukuru sana.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, lakini mngetuongeza tuko wachache. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kunipa fursa hii jioni hii kuweza kuchangia bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu Subhana wataala aliyetuwezesha jioni hii kutupa pumzi zake na nguvu zake tukaweza kubakia katika Bunge hili Tukufu, siyo kwa uwezo wetu siyo kwa ujanja wetu wala siyo rai isipokuwa ni uwezo wake yeye mwenyewe. Katika mchango wangu kwanza nataka nitoe kauli ya ndugu yetu mtunzi maarufu wa Kiswahili Shaaban Robert aliposema kwamba jibu linaposadifu swali shaka huondoka, hii ina maana ya kwamba nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujibu maswali ya Watanzania moja kwa moja kwa matendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili kwa kweli hatuna budi tumpongeze sana na wala asichoke na asonge mbele kwani asie macho haambiwi tazama, katika mchango wangu pia nataka niweze kuangalia kwa ruhusa yako unipe nafasi ndogo niweze kutoa nukuu ya falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa hili la Tanzania. Marehemu mwalimu alisema siku moja katika nukuu yake ‘‘Njia pekee ambayo uongozi unaweza kutunzwa kama uongozi wa watu ni pale ambapo viongozi wanapokuwa na sababu ya kuogopa hukumu kwa watu’’.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana ya kwamba furaha ilitanda katika ukumbi huu wakati Waziri wetu Mama Ummy Waziri wa TAMISEMI alipozitaja Milioni 500 kwenda moja kwa moja kutatua tatizo la barabara zetu za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli furaha ilitujaa katika nyonyo zetu na bado furaha ile tunaendelea kuwa nayo, lakini tulikuwa tunajiuliza sana sana maswali na ndiyo hapa majibu yalipokuja kwenye falsafa ya Mwalimu Nyerere kwamba Hukumu ya watu tunaiogopa, kwamba tunatakiwa tutende mema kwa watu ili kwamba hukumu hiyo isitujie kwetu sote, kutokana na hali hiyo basi tukawa tunajiuliza hizi milioni 500 kwa vile zinatoka Mfuko wa Hazina, na Mfuko wa Hazina ni wa Tanzania tukaona sasa furaha na sisi imeanza kutuingia, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana pamoja na Naibu Waziri kwamba hili litaweza kutatua tatizo la Wazanzibar kwa kiwango kikubwa kwenye barabara zetu ambazo na sisi zinakero kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Tumbatu barabara ni mbaya hazipitiki za vijijini, ukienda Mwera kwa Mheshimiwa Mwinyi nako ni vilevile ukija kwenye Jimbo langu mimi la Wete pia hukumu ni hiyo hiyo, ukienda kwenye Jimbo la Mfenesini nalo linalia, ukienda kwenye Majimbo mengine yote ya Zanzibar yanalia kilio hiki cha barabara ambazo hazipitiki. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakushukuru tena naendelea kukushukuru kwamba mfuko huu wa Hazina nao utakwenda kutibu lile donda tulilonalo kule Zanzibar, kwa heshima kubwa kabisa napenda kukushukuru sana pamoja na Naibu Waziri wako na Waziri wa TAMISEMI kwa kulitoa tangazo kwamba Majimbo yote kwa hiyo mimi ninaichukulia yote ni yote Tanzania ni moja itajibu maswali na swali hili litajibiwa na Watanzania wote, hasa ukilinganisha mfuko ni wa Hazina na Hazina ni ya Watanzani wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nashukuru sana kwa kunipa fursa hii kuweza kuchangia, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika Mpango huu. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea Mpango huu. Kwa kweli utasaidia kujenga Taifa letu lenye uchumi utakaoendelea na kudumu katika nchi yetu na wananchi kupata manufaa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie katika maeneo mawili makubwa; eneo la kwanza nataka nichangie kwenye uvuvi wa bahari kuu na eneo la pili nitajikita kwenye kilimo cha mwani. Kwani katika Mpango huu Mheshimiwa Waziri amezungumza kwa kiwango kikubwa kuhusu habari ya uvuvi wa bahari kuu na ameonesha kwamba, mpango ule wa kupatiwa meli nane zile za uvuvi bado, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuangalia kwa kina sana. Hata hivyo, bado nahisi kwamba, kutokana na mazingira ya uvuvi wa bahari kuu, basi kuna haja katika Mpango huu uelekeze zaidi kwenye hizi meli za uvuvi, basi zisiwe nane badala yake zile meli ziongezeke zaidi na zaidi zielekezwe katika maeneo ambayo yana uvuvi wa bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uvuvi ni sekta moja ambayo inatuwezesha kuishi maisha ya rah ana starehe katika maisha yetu ya kila siku. Hakuna mtu hata mmoja anayeishi bila ya kutegemea minofu ya samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unataka kujua kwamba uvuvi au samaki wana faida kubwa katika maisha ya mwanadamu, twende pale canteen tu ukawaangalie Waheshimiwa wanavyohangaika kushughulika na minofu ya samaki. Hii ni kuonesha kwamba uvuvi wa bahari kuu unaweza kutusaidia kutupatika pato la Taifa, lakini kujenga maisha yetu ya kila siku. Hata tunaweza tukampunguzia Waziri wa Afya wagonjwa wengi ambao anawatibu kwa kila siku kutokana na hali ya afya zao kutokuboreka, lakini zinaboreka kwa sababu ya minofu ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia samaki hawa hawa ndiyo wanaowawezesha wananchi wetu wakaishi wakiwa na afya bora za kuweza kufanyakazi kwenye kilimo, kwenye viwanda na shughuli mbalimbalii tunazozitegemea za maisha yetu ya kila siku. Hii ni kuonyesha kwamba sekta ya uvuvi ni sekta ambayo inahitaji kupewa kipaumbele kama vile tunavyoipa kipaumbele sekta ya kilimo kwa sababu hizi ni sekta pacha kama unataka kuleta maendeleo katika nchi basi lazima sekta ya uvuvi uiangalie kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwenye sekta hii ya uvuvi lakini kwenye kilimo cha mwani, kilimo cha mwani ni kilimo ambacho kinategemewa sana katika Taifa hili kwa sababu mwani wenzetu wanasafirisha tunasafirisha mwani zaidi Zanzibar kwa matani na matani kuupeleka nje kama nchi ya Philippines, Marekani na Wachina wenzetu nchi hizi wanajikita sana kuuchukua mwani wetu kwa sababu mwani wenyewe ni ubora lakini ni mwani ambao unatengeneza vitu vingi sana na vitu vyenye thamani wanatengenezea Madawa, ni chakula pia unasaidia mwani katika mambo mbalimbali katika kukuza uchumi wao mataifa ya nje zaidi ya China na Philippines. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kama ikiwa tunataka tuwatoe wananchi wetu kwenye dimbwi la umaskini kwa vile nchi tumeitangaza ni nchi ya viwanda Tanzania kwa hiyo sasa tuangalie kujenga viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mwani. Kwa sababu kila tukichakata mwani basi mwani unapanda thamani zaidi kulikoni kuuza mwani ambao haujachakatwa. Kwa hiyo, hili tulichukue kama katika mpango wetu tuhakikishe kwamba tunajenga viwanda vidogo vidogo vitakavyoweza kuchakata mwani ambao sasa tutauongezea thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie tu mwani kama utauponda ponda ukawa kama unga basi thamani yake ni tofauti na mwani unaousafirisha ukiwa katika ma-bundle ambao haujachakatwa hii ni kuonyesha kwamba huu mwani unaweza ukatusaidia sana katika kukuza uchumi na kuwapunguzia umaskini wananchi wetu wa Tanzania kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kuzungumza kilimo cha mwani kule Zanzibar mwani ndiyo kilimo ambacho kinategemewa kwa kiwango kikubwa sana ukienda kama Kisiwa cha Pemba kuna sehemu ya Kiui Minungwini, kuna Maziwa ng’ombe, kuna maeneo ya mkoani huku Kangani maeneo mengi tu ambayo yanategemewa kwa ajili ya kuzalisha huu mwani na wananchi kupata faida. Shida ni kwamba wananchi wetu wanalima kilimo cha mwani bila ya kuangaliwa soko ambalo linaweza kuwakuzisha katika kukuza uchumi wao wa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri mazao ya baharini hayahitaji msimu wa kumwagiliwa humwagilii maji, maji ndiyo wenyewe. Kwa hiyo huhitaji kwenda kumwagilia wala huwezi kusema kwamba kuna ukame bahari haina ukame kila siku inakua kwa sababu mabadiliko ya tabia nchi kila siku kina cha bahari kinaongezeka sasa hii ni kuonyesha kwamba ikiwa tutajikita kwenye kilimo hiki cha mwani na kwa kuhakikisha wananchi wetu tunawawezesha ninaimani kwamba tutaweza kufika pahala pakubwa na uchumi wetu utaweza kukua. ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu. Kwanza, sina budi kumshukuru Allah Kareem aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo vyote tukapata uhai huu ambao tumo katika siku ya Jumamosi tukiwa sote tuko wazima.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa na ufahari mkubwa leo nimesimama katika Bunge lako Tukufu ukiwa wewe ndiye Rais wa Mabunge ya Dunia. Kwa kweli nakupongeza sana na nina imani kwamba, Wabunge wote wataunga mkono hili la kukupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwa heshima na taadhima, naomba uniruhusu kidogo nitoe ushairi ambao mtaalam wa Lugha ya Kiswahili kule Zanzibar ndugu yangu Haji Gora aliutoa katika kitabu chake cha kimbunga. Katika kitabu cha kimbunga ndugu yangu Haji Gora alizungumza maneno yafuatayo; katika ushairi wake alisema kwamba: “Chura kakausha mto, maji yakamalizika, Pwani kuliwaka moto, mawimbi yaliyowaka usufi nusu kipeto, rikama likavunjika, nyoyo zikafadhaika.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana ya ushairi huu ni kwamba sote Wabunge tuliomo humu, tumefadhaika sana na Ripoti ya CAG na tumefadhaika kwa sababu ya hali ya upepo wa fedha za walipakodi wa nchi hii zinavyotafunwa, zinatafunwa mkono wa kulia wa kushoto haupati. Zinatiwa kwenye pua ya upande wa mkono wa kulia wa kushoto haupati, matokeo yake hali ya uchumi inadorora na matokeo yake Wananchi wetu wanabaki katika umaskini uliokithiri.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kuhusu Wazabuni na Wakandarasi ambao imezungumzwa katika ripoti zetu hizi tatu kwenye ukurasa wa 44. Taasisi 259 zinadaiwa na Wazabuni, zinadaiwa na Wazabuni ambapo Serikali inadaiwa jumla ya trilioni 4.82 kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana, lakini wazabuni pekee wanadaiwa fedha trilioni 3.40 sawa na asilimia 83, hilo ni deni la wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nina documents ninataka nitaje baadhi ya taasisi za Serikali ambazo zinadaiwa madeni makubwa. Kwa mfano, kuna Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inadaiwa bilioni 60. Wakala wa Ufundi wa Umeme (TEMESA) bilioni 49, Wakala wa Huduma ya Ununuzi wa Serikali (GPSA) inadaiwa bilioni 13. Kwa kweli hicho ni kimbunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, SUMA JKT Kampuni ya Ujenzi inaidai Serikali, wazabuni hao jumla ya bilioni 10. Mfuko wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) bilioni 90. Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) bilioni 41. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Dar es Salaam bilioni 137. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa angalia kimbunga hiki, Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao ndiyo Taasisi Mama inayokusanya mapato inadaiwa bilioni 224, hawa ni wazabuni ambao wanaidai Serikali kwa kipindi kirefu sasa. Sasa nenda basi ukaangalie katika hospitali zetu. Ukienda Benjamin Mkapa, wazabuni hawa wanapima pressure kipimo kinasoma juu moja kwa moja. Ukienda Hospitali ya Mirembe, ambako huko ndipo wagonjwa wanaoshikwa na matatizo ya akili, napo huko wapo wazabuni ambao tayari wameshakwenda kule, kwa sababu akili hazifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake watanzania hawa ndiyo wale ambao sasa hivi waliokuwa sasa hawana uchumi tena, nyumba zao zimepigwa mnada na mabenki, viwanja vyao walivyokuwa navyo vimeuzwa, magari yao waliokuwa wakitembelea waliokuwa wakifanya kazi nayo yamepigwa mnada, matokeo yake ni kwamba hawa wamekuwa masikini. Hii ni kuionesha kwamba Serikali haijawa makini katika kulishughulikia suala la hawa wazabuni.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika hii paper niliyonayo, mpaka Wizara zote zimo humu, Wizara zote zinadaiwa na wazabuni! sasa hii tunakwenda wapi? tunafika wapi ikiwa Serikali inadaiwa namna hii na deni kubwa kama hili, je tunafanyaje? Mawazo yangu mimi, maana yake najua kwamba wasimamizi wa Serikali ni Mawaziri, lakini kuna watendaji wao. Hao watendaji ndio wanastahiki sasa wawajibishwe, kwa sababu hizi fedha nina imani kwamba zinakwenda, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatoa Fedha na anazipeleka, kwa sababu tunampitishia fedha kwenye bajeti lakini matokeo yake fedha hizi zinaliwa na watu wachache.

Mheshimiwa Spika, mawazo yangu mimi, wenznagu wengi walisema kwamba wanyongwe lakini ukinyongwa ndio umeshakufa, utakuwa huonekani wala hupati uchungu, kwanza wezi hawa tuanze kuwakata mkono, wakiona mkono mmoja hawana watajua kwamba kweli waliiba pesa za watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia wafungwe jela wawekewe daftari maalum la uzalishaji, kwamba ikiwa umezalisha kule mali ya 10,000 na ionekane deni letu lile tulilokuwa tunawadai tayari 10,000 imetoka, mpaka muda wao umeisha. La tatu na mwisho, wafilisiwe mali zao hadharani na kila mtanzania ajue kwamba mali hii inafilisiwa kwa sababu ya kuibia Serikali mali ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno hayo mafupi mimi naunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa jioni hii ya kuchangia katika bajeti yetu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka mchango wangu niuelekeze zaidi kwenye lugha ya Kiswahili. Nianze kwa maneno aliyoyazungumza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania. Mwalimu alizungumza kwamba Uhuru wa Tanganyika ulichochewa sana kwa kutumia lugha hii ya Kiswahili. Kwa hiyo, uliharakishwa kutokana na kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, lugha ya Kiswahili ilisaidia sana kupata uhuru wa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1962 lugha ya Kiswahili iliamriwa kwamba ni lugha ya kutumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1964 lugha ya Kiswahili ndiyo ilitangazwa rasmi kwamba ni lugha ya Taifa. Kwa hali hiyo basi, lugha ya Kiswahili ni moja katika lugha ambayo tunatakiwa Watanzania tuienzi, tuitukuze na tuhakikishe kwamba tunaitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi nyingi za Ulaya ikiwemo China, Korea, Uturuki na kadhalika, zimepata maendeleo makubwa kwa sababu ya kutumia lugha zao. Sasa sisi Watanzania bado hatujajikita kutumia Kiswahili kama ni lugha yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza sana tena sana Wizara ya Katiba na Sheria kwamba wameanza angalau kuonesha mwanga kwenye hukumu wanazozitoa kwenye Mahakama. Ila ni jambo la kushangaza, Wizara mama ya Elimu ambayo ina mitaala ya kutosha, ina uwezo wa kubadilisha kuitumia lugha ya Kiswahili katika shule zetu za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili linahuzunisha sana, kwa sababu hata somo la historia jamani! Hata somo la historia ya nchi yetu tunalizungumza kwa lugha ya Kiingereza! Lugha ya Wakoloni ambao wametutawala kwa sababu ya kuitumia lugha yao? Ukitaka mtoto ajisikie katika nchi hii, basi azungumze Kiingereza. Ila ukitaka aonekane kadhalilika, basi azungumze lugha ya Kiswahili. Hii ni kuonesha kwamba lugha yetu ya Kiswahili bado hatujaipa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba lugha hii ndiyo lugha halisi tunayotakiwa kuitunza na kuhakikisha kwamba tunaitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wataalam wengi wamezungumza lugha ya Kiswahili. Kama mtunzi mmoja Ibrahim Hussein, alizungumza katika tamthilia yake ya “Mashetani” kwamba Tanzania tunajiamini kwamba mkoloni katuachia kisu sasa, na kisu kile ndiyo tunachotumia kujikata sisi wenyewe. Siku zote tunaona kwamba lugha ya Kiswahili ndiyo lugha ambayo inaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waingereza hao hao wanasema don’t bite the hand that feeds you. Usiule mkono unaokulisha, ukiula mkono unaokulisha utakulia nini? Naomba sana lugha ya Kiswahili itumike kwamba ni lugha ya Taifa kweli kweli na tuhakikishe kwamba vizazi vyetu tunawarithisha lugha yetu ya Kiswahili kwa kuitumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende kwenye ukurasa wa 75 ambapo Mheshimiwa Waziri wa Fedha alizungumza juu ya mkakati wa uchumi wa bluu. Ni dhahiri kwamba Tanzania tuna watu ambao wanategemea sekta ya uvuvi wasiopungua milioni tano. Watu hawa wote wanategemea sekta ya uvuvi, lakini uvuvi huu unategemea vyombo vinavyohusika kwenda bahari kuu. Ni-quote speech moja ambayo aliitoa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alisema kwamba kipindi cha miaka mitano, mwaka 2020 Novemba 15, alisema maneno haya yafuatayo: Kwamba, kipindi cha miaka mitano sekta ya uvuvi itakuzwa ikiwemo uvuvi wa bahari kuu kwa kununua meli nane zitakazofanya kazi katika ukanda wa Pwani ulioko Zanzibar na Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo haitoshi. Mheshimiwa Waziri katika bajeti iliyopita ya 2021/2022 aliizungumza kwa kinywa kipana kwamba tunanunua meli nane za uvuvi. Naomba atakapokuja Waziri, atueleze, hizi meli nane zilipotea wapi kwenye bajeti hii ikawa haionekani? Hazionekani kabisa, wala hakuzungumza kwamba kutakuwa na meli nane zitakazofanya shughuli za uvuvi. Angalau angesema kwamba tushanunua meli mbili zimebaki sita, lakini hata moja hajaizungumza katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee katika kilimo cha mwani. Mikoa inayozalisha mwani kwa Tanzania Bara haipungui minne; Lindi, Mtwara, Mkoa wa Pwani, Mafia; nadhani ni mikoa hiyo. Kwa Tanzania Visiwani, Zanzibar, karibu mikoa mitatu inazalisha mwani ikiwemo Mkoa wangu wa Kaskazini Pemba.

Mheshimiwa Spika, asilimia 90 ya wanawake wanajishughulisha na kilimo cha mwani. Ni masikitiko makubwa sana kwamba wanawake hawa wanadhalilika mpaka sura zao zimebadilika, nywele zimenyonyoka vichwani kwa kushughulikia kilimo cha mwani. Nadhani hata kiwanda kile cha kutengeneza nywele bandia kinaweza kikajengwa Pemba sasa, kwa sababu nywele hazimo tena kwa kilimo cha mwani. Zimepotea kabisa kwa sababu ya kilimo cha mwani. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini? Ni kwa sababu mwani haujapewa kipaumbele na nchi yetu. Kilimo cha mwani kinasaidia sana kukuza uchumi wa wanawake nchini, lakini changamoto kubwa ni jinsi bei zinazopangwa na mashirika yanayonunua mwani. Mashirika haya yote, hakuna ambalo linawaonea huruma wakulima wa mwani. Maana wananunua kati ya Shilingi 600/= mpaka Shilingi 1,800/=, kiwango kidogo kabisa cha fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake wakae kutafakari na kupanga bei ya mwani kama vile inavyopangwa bei ya korosho, kahawa, karafuu kwa kule Zanzibar na maeneo mengine. Hii itaweza kuwakomboa wanawake wabaki salama kwenye mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo, mwani huu tunauuza sisi kama malighafi. Inakera sana. Tanzania ni nchi ya viwanda, ina uwezo wa kujenga viwanda vidogo vidogo, lakini mpaka sasa hivi hakuna kiwanda hata kimoja kinachochakata mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwani unatusaidia sana kwa kutengeneza mboga mboga, mwani ni chakula, mwani tunatengenezea mafuta, lakini hutoamini rasilimali inayotoka kwenye mwani. Mwani unatengeneza mpaka hii mitambo yetu wanaume tunayoitumia inatokana na kilimo cha mwani. Hii ni kuonesha kwamba mwani kumbe una faida kubwa kwa nchi yetu. (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Omar, hoja ya msingi sana hiyo, dakika moja malizia muda wako umeisha. (Makofi/Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Penye watu wazima wengi hufahamu lugha nzuri. Mitambo ya wanaume mnaijua, na mkifanya mchezo basi wanaume tunaweza tukapoteza mabibi zetu kwa sababu ya mitambo haifanyi kazi kutokana na kwamba hatuutumii mwani vya kutosha. Kwa hiyo, mwani una faida kubwa na tuendelee kuutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi/Vicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwanza sina budi kumshukuru Allah Subhanahu Wa Ta’ala aliyetuwezesha kufika hapa katika Bunge hili jioni hii tukiwa wazima na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kujielekeza kwenye mchango wangu kwa kuanza kuzungumza kuhusu mshairi mmoja ambaye alitunga shairi linasema Jeraha la Moyo. Alisema kwamba:-

“Moyo uliojeruhiwa, mengi huyafikiria,
Hufikia kuzidiwa, zitawalapo hisia,
Unaweza kuamua, lolote kujifanyia,
Ni rahisi kupagawa na kutoka kwenye njia.”

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hivi kwa hisia kali. Nazungumza kwa hisia kali kwa sababu ya kikokotoo. Kikokotoo kama jina lake lilivyo, lakini kwa kweli linawakokotoa wafanyakazi ambao tumewatumia kwa muda mrefu sana. Wafanyakazi wamefanya kazi kwa miaka 30, 35, wengine ni waajiriwa wa Polisi, wengine ni Madaktari, Walimu kama mimi, kwa kweli wako katika hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine sasa hivi tunavyozungumza, kwa sababu ya kikokotoo, wanapumulia mashine, kuna wengine sasa hivi sukari inapanda kiasi cha kwamba, hawana maisha, lakini kuna wengine sasa hivi hawajui maisha yao yatakuwa yako wapi, wamebaki kuwa ombaomba hata chakula hawana, hawana cha kuvaa. Ukiwaangalia, unaweza ukamkuta mwalimu, daktari au mfanyakazi, anavaa kiatu kimoja chekundu kimoja cheupe. Unajiuliza, shida ni nini? Shida ni kikokotoo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, hapa tumefanya kitu kibaya kabisa, ingawa tulipitisha sisi katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna haja ya kuhakikisha kwamba sheria hii inaletwa tena kufanyiwa mabadiliko, tena mabadiliko ambayo yanaweza kusaidia kuhakikisha kwamba wafanyakazi hawa wanaishi katika hali ya raha na starehe. Unashangaa na unajiuliza, hivi kweli Mkurugenzi wa Manispaa au Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye umemtumia miaka 30 ashindwe kuzitunza fedha zake ambazo umempa kiinua mgongo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni fedha yake, kweli ashindwe kuitumia wakati wewe ulikuwa unampa posho, unampa stahiki mbalimbali za wafanyakazi, lakini zile alikuwa anazitunza na anahakikisha kwamba zinafanya kazi vizuri na hakuna ubadhirifu wa aina yeyote. Aje ashindwe kutumia hela ambayo anaiendeshea familia yake? Naomba fedha hizi zirejeshwe kwa wafanyakazi ambao wametumika katika Taifa hili na kuhakikisha kwamba maisha yao na wao yanakuwa katika hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Polisi sasa hivi, ndiyo ambao wanalinda nchi hii. Kwa kweli utawashangaa, nenda kaangalie hali walizonazo Polisi sasa hivi, ni mbaya. Ni wastaafu ambao wamekuwa ombaomba. Leo Kamishna wa Polisi analipwa kiinua mgongo chake shilingi 200,000,000, unampa shilingi milioni 60, kweli hii ni halali? Hii ni haki? Shilingi 140,000,000 unazo wewe mfukoni, unamtunzia nani jamani? Mtu mzima anatunziwa pesa. Ikitokea akifa fedha ndiyo zimepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli ni mtu mzima gani mwenye akili timamu aliye na umri wa miaka 60 bado akili inafanya kazi, halafu unachukua hela unakwenda kumtunzia wewe? Serikali inatunza fedha za wafanyakazi ambao wamestaafu, kwa kweli hili ndiyo tunalolisema ndiyo hilo jeraha la moyo ambalo wafanyakazi wetu wanalo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niondoke hapo. Sasa naenda kwenye suala zima la ajira. Dada yangu Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kazungumza sana kuhusu ajira. Kwa kweli, tunasema kuna upendeleo wa ajira. Kwa nini tunasema hivyo? Kuna vijana wetu ambao wamemaliza chuo, wanatumikia Wizara ya Elimu, kwa mfano, wanajitolea. Vijana hawa hawalali, hawanywi, wanafanya kazi na watoto wetu, matokeo yanakuja mazuri na Tanzania tunajivunia kwamba tuna elimu bora, lakini unashangaa anakaa miaka saba hapati ajira. Halafu anakuja mtu anatoka university, fresh kabisa, leo yeye ndiye anapewa ajira. Huu si ni upendeleo! Upendeleo huu unatupeleka wapi? Kwa kweli hili naomba tuliingilie kati kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ajira 46,000 zitatolewa, naomba Mheshimiwa Waziri uhakikishe kwamba vijana hawa wanaojitolea wanapata ajira ili nao mwaongezee motisha waweze kuona kwamba kweli wanaitumikia nchi yao kwa weledi na uaminifu na pia wanapata stahiki zinazowastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda kwenye Mfuko wa TASAF. Hiki ni kizaazaa, kwa sababu nia ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba anawafanya Watanzania wawe na maisha bora. Kila mmoja aishi maisha ambayo yanamsaidia katika familia yake. Tuna familia zilizo duni kabisa. Familia zetu ziko katika hali mbaya, lakini jambo la kushangaza ni kwamba, utaratibu unaotumika kupata kaya maskini ambazo zinasaidiwa na Mfuko wa TASAF siyo sahihi, umeingiliwa na Masheha kwa kule kwetu Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheha sasa ndiye mwenye say kwamba huyu mpe, huyu usimpe. Kuna watu wako katika hali mbaya zaidi kuliko hawa ambao sasa hivi wanapata fedha kwenye Mfuko wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tena la kushangaza ambalo kwa kweli linakera zaidi ni kwamba, kila siku fedha zinapungua. Kaya maskini inapewa shilingi 70,000, kesho unakuta zile fedha zimekatwa, inalipwa shilingi 30,000. Je, wale vijana waliokuwa wakihudumiwa na hiyo kaya wamekufa? Kuna kigezo gani kinatumika kukata fedha? Ukiuliza, majibu yao wanakwambia, aah, nenda, mambo haya yanatoka Bara bwana, siyo huku Visiwani, yanatoka Bara. Sasa kwa kweli, hili haliko sahihi. Naomba na hili lifanyiwe marekebisho. Ahsante sana. (Makofi)