Contributions by Hon. Omar Issa Kombo (7 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hotuba ambayo iko mbele yetu kutoka Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu na kuweza kuchangia, naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa. Vilevile nichukue fursa hii kukishukuru sana Chama changu Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini kuweza kupeperusha bendera katika nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Wingwi katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Wingwi kwa imani yao kwangu. Sambamba na hilo, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wingwi kwa imani yao kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Ofisi yake kwa hotuba nzuri iliyojaa maono ya viongozi wetu pamoja na Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Vilevile nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoanza kuchapa kazi katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Wingwi na kwa niaba ya wananchi wa Pemba hatuna shaka hata kidogo kama Wanzanzibar kwamba Muungano wetu upo kwenye mikono salama chini ya Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili amelidhihirisha siku anamuapisha Mheshimiwa Makamu wa Rais alipomwambia aanze kuzifanyia kazi changamoto za Muungano. Hii ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuuboresha, kuuendeleza, kuuenzi na kuulinda Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli Serikali yetu inafanya jitihada kubwa sana katika kuuenzi na kuulinda Muungano wetu. Kuna mafanikio makubwa ambayo tunayapata sisi Wazanzibar lakini watu wanajitia kuwa hawaoni wala hawasikii wala hawataki kuona mafanikio makubwa ya Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli changamoto 11 zilipatiwa ufumbuzi lakini wanaposimama hawataki kuyasema haya. Changamoto nimeiona, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri Mkuu Serikali iweke utaratibu wa kwenda kwenye vyombo vya habari kueleza mafanikio na yale mambo ambayo yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar ili wananchi waweze kuona na kufahamu na kuelewa waepukane na kupotoshwa. Nasema hili kwa sababu kuna upotoshwaji mkubwa kwamba Serikali haifanyi kitu katika suala la Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niendelee kuipongeza Serikali kwenye mradi mkubwa wa umeme. Nafahamu mradi huu ukikamilika tutaweza kupata huduma hii kwa unafuu mkubwa zaidi. Sasa niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Serikali, kwa vile nchi yetu tuna pande mbili za Muungano; upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara, uandaliwe utaratibu maalum au watueleze ni jinsi gani sisi Wazanzibar tutaweza kufaidika pindi mradi huu utakapokamilika. Licha ya kwamba tunalo Shirika la Umeme kule Zanzibar lakini tunafanya kazi kwa ushirikiano. Niombe wakae meza moja na sisi watuangalie kama wenzao ili tuweze kupata huduma hii itakayokuja katika hali ya unafuu mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Bismillah Rahman Rahim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuchangia nami katika hotuba hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ni muhimu sana kwa maslahi ya wananchi wetu, hususan wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kukushukuru wewe, vile vile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri na baadhi ya watendaji wa Wizara hii. Kwa nini niseme baadhi ya watendaji, nitatoa ufafanuzi mbeleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wakati tunapochangia sekta tatu, lazima tuoneshe hisia za ukaribu zaidi; Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwa sababu sekta hizi zinawagusa asilimia kubwa sana ya Watanzania na hususan wenye kipato cha chini ambapo wengi wa Wabunge tunatoka katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitagusia kwenye Sekta ya Uvuvi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kweli ameanza vizuri. Kwa nini ameanza vizuri, amekuwa tofauti na wale wengine ambao wanawachukulia wavuvi kama maadui zao. Baadhi ya wengine waliopita tuliwaona, walikuwa wanahisi kwamba kutekeleza majukumu yao ni kuwanyanyasa, kuwaadhibu wavuvi wetu, jambo ambalo siyo sahihi. Mheshimiwa Waziri huyu amekuwa msaada mkubwa sana kwa wavuvi wetu, Mheshimiwa Waziri hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hongera hizo, lakini bado kuna changamoto kwenye Sekta hii ya Uvuvi na tunapozungumzia changamoto hizi, ni kwenye suala la kanuni. Kwa kweli kanuni ambazo zimetungwa hivi karibuni haziko rafiki na wala haziwasaidii wavuvi wetu. Kwa mfano, kuna kanuni ambayo inakwenda kuzuia uvuvi wa ring net kwamba uvuvi huu unaharibu mazingira. Nataka kusema kwamba siyo kweli kwamba uvuvi wa ring net unaharibu mazingira. Ila inaonesha kwamba kuna shirinikizo fulani, kuna watu ambao wanajaribu kuwaonea wavuvi kwa kisingizio cha uvuvi haramu au cha kuharibu mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane kwamba shughuli zote za binadamu kwa njia moja ama nyingine zinaharibu mazingira. Tukizungumzia kilimo, kinaharibu mazingira, tukizungumzia uchimbaji madini, unaharibu mazingira, viwanda vinaharibu mazingira, utalii unaharibu mazingira, shughuli zote za binadamu zinaharibu mazingira; lakini hatuwezi kutumia kigezo hiki kuwadhalilisha wananchi. Licha ya kwamba shughuli za binadamu zinaharibu mazingira, lakini lazima maisha ya binadamu yaendelee. Ni lazima binadamu afanye shughuli zake za kujipatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa ufafanuzi atueleze ni lini kanuni hii inakwenda kufanyiwa mabadiliko? Vinginevyo hapa patachimbika kwa sababu wavuvi wetu wanapata dhiki kubwa sana kutokana na kanuni hii. Lazima niseme kwamba tunapotunga kanuni au sheria lazima tuzingatie utekelezaji wa sheria hizo. Hivi unatunga kanuni ya ring net kwamba wavuvi wakavue maji mita 50, wapi na wapi? Ukiangalia wavuvi zana wanazotumia ni duni, au tunataka tupate mayatima wengi na wajane wengi? Kwa sababu mvuvi anapokwenda maji mita 50 ni kutafuta kifo tu, hakuna kingine, kutokana na zana wanazotumia, ni duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukisema labda ring net wafanye uvuvi wa usiku, haiwezekani kwa sababu samaki wengi wanapatikana muda wa mchana, usiku huwezi kumvua samaki kama aina ya jodari, lazima uvue wakati wa mchana. Vilevile wakati wa usiku unapomvua dagaa, mpaka asubuhi tayari ashaharibika; na ukizingatia ring net ndiyo uvuvi ambao unabeba wavuvi wengi. Boti moja ya uvuvi wa ring net wa mchana inachukua wavuvi kati ya 40 mpaka 100, lakini uvuvi wa usiku unachukua wavuvi 10 mwisho wavuvi 15. Hebu tuangalieni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tunapozungumzia Sekta ya Uvuvi, wananchi walio wengi wamejiajiri katika sekta hii. Mfano ulio hai, hebu tuangalieni soko la ferry, umati ambao uko pale; wote wale wanategemea Sekta ya Uvuvi. Nenda Mafia ukaangalie akina mama wanaojiajiri kwenye Sekta ya Uvuvi. Tunaweza kuiangalia Sekta ya Uvuvi kwa kuangalia mchango kwenye pato la Taifa, hii haiko sahihi. Pamoja na mchango ulioko kwenye pato la Taifa lakini Sekta hii ina tija kubwa kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mifano iliyo hai. Nenda katika Soko la Ferry, pale pana akina mama ntilie wanategemea Sekta ya Uvuvi, pana bodaboda wanategemea hii, pana daladala, hata Ferry inayovusha, abiria wengi wanakwenda kwenye Soko la Ferry kutokana na Sekta ya Uvuvi. Hata ukienda Kisiwa cha Mafia, akina mama walio wengi au wananchi walio wengi wa Mafia wanategemea Sekta ya Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujiulize tunapokwenda kuzuia uvuvi wa ring net, tunategemea wananchi wetu waishi katika maisha gani? Lazima tuzingatie. Kanuni hizi, nikwambie ukweli, inaonekana kuna shinikizo fulani. Watendaji wako Mheshimiwa Waziri wa ngazi za juu mara nyingi wanatuambia kwamba umeunda Tume ya kwenda kufanya utafiti, nakupongeza sana lakini katika Tume ikija kufanya utafiti inaonekana kuna vitu vitatu. (a) Tume hii haina elimu ya kutosha juu ya uvuvi huo. (b) kama siyo hivyo, Tume hii haishirikishi wadau ipasavyo; na kama siyo hivyo, Tume hii haielezi ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa ring net hauvui samaki walio chini, wanavua samaki ambao wako juu. Isitoshe, uvuvi wa bahati kuu kama Bahari ya Hindi, hatuwezi kuzungumzia ufugaji wa samaki kama unayefuga samaki kwenye bwawa. Kwa sababu samaki wanatembea masafa ya mbali. Unaweza kufuga samaki Tanzania akaenda kuliwa Kenya. Sasa lazima tuangalie vizuri tunavyozungumzia masuala ya ufugaji wa samaki kwenye bahari kama Bahari ya Hindi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Omar Issa Kombo kwa mchango mzuri.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ingawa muda umekuwa mfupi, tutakutana na Waziri tuongee vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema anayetujalia mpaka sasa hivi tukiwa tuko katika hali ya afya na uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nianze kwa kukupongeza wewe kwa kunipatia fursa ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. Aidha, nichukue fursa hii kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kaka yangu Nchemba pamoja na Naibu Waziri kaka yangu Masauni kwa hotuba nzuri ambayo kwa kweli inawagusa Watanzania wote. Vile vile, nichukue fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ujumla wao kwa namna wanavyoendelea kujitoa kumsaidia mama yetu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassain, kwa kweli Waheshimiwa Mawaziri tunawaambia hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona jinsi mnavyofanya kazi ya kuhakikisha kwamba mnawatumikia Watanzania kwa lengo la kulipeleka mbele Taifa letu, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna anavyoendelea kuwasimamia Mawaziri na kuisimamia Serikali kuhakikisha kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pongezi za pekee nimpongeze sana sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassain, kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio na ufanisi mkubwa kwa kweli Mama huyu ametuheshimisha sana Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nampongeza Mheshimiwa Rais wetu siku tunamuaga mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, pale Jamhuri alituahidi watanzania kwamba hakutoharibika kitu na kwakweli tumeshuhudia hakuna kitu kilichoharibaka wote ni mashahidi tunaona kwamba miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa, hakuna mradi hata mmoja ambao umesimama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile na mpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutumiza matarajio, matamanio ya mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Tunaona reli zinaendelea kujengwa, ndege zinaendelea kununuliwa, vituo vya afya vinajengwa, shule zinaendelea kujengwa, mradi wa umeme unaendelea kutelezwa, tunasema kwa kweli Mama yetu anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii, niwaombe watanzania wenzangu kwa umoja wetu bila kujali tofauti zetu tusimame pamoja kumuunga mkono Rais wetu. Kwani ameonesha nia ya dhati ya kulipeleka mbele Taifa letu, ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia watanzania kwa hiyo tusimame pamoja kumpa support kiongozi wetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba sasa nichangie kwenye bajeti hii, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, bajeti ni bajeti nzuri sana kwa kweli ni bajeti ambayo imegusa maisha ya watanzania na kwakweli ni bajeti ya kwanza watangulizi wetu wanasema hapa, kwamba ni bajeti ambayo imesikiliza vilio vya Wabunge kwa asilimia kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona suala la TARURA Wabunge tulisimama hapa kwa umoja wetu kuzungumzia Sakata la TARURA na kwa kweli TARURA ilikuwa ipo katika hali mbaya, kwa sababu barabara za vijijini zilikuwa zipo katika hali mbaya. Ukizingatia athari mbalimbali zimeelezwa kutokana na ubovu wa barabara za vijijini ikiwemo kina mama kujifungulia njiani, watoto kufariki kutokana na kusombwa na maji kipindi cha mvua, lakini vilevile uzito na kupanda kwa gharama ya kusafirisha mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekisikia kilio hiki na kwenda kuweka fedha kwenye mfuko wa TARURA. Lakini vilevile Mama yetu Samia Suluhu Hassan amesikia kilio hiki kwa kuweka kila jimbo shilingi milioni 500 tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuongoza na kuongeza vianzio vipya vya mapato kwenye suala la mapato ya simu vilevile yanatokana na miala ya simu, lakini vilevile malipo ya line. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na kwenye tozo za mafuta kwa kweli umefanya jambo muhimu sana na umeandika historia na watanzania wataendelea kukumbuka kwa kazi yako kubwa uliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, tunafahamu kwamba Wizara ya Mawasiliano ni wizara ambayo haipo kwenye Muungano, lakini kuna sekta ambazo tuna-share pamoja, mfano Sekta ya Mawasiliano kama Posta, lakini vilevile kama TTCL, Air Tanzania na mambo mengine. Sasa kianzio hiki kipya cha mapato ambacho kinakwenda kukusanya mapato kutokana na line za simu na miamala ya simu, tunafahamu kwamba simu hizi wanaotumia ni watanzania wote wa pande zote mbili upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini miamala ya simu inafanywa na watanzania wote na sisi upande wa Zanzibar wananchi walio wengi mpaka vijijini wanatumia simu, ni watu wachache sana ambao hawamiliki simu. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba ukija uje utueleze kama Wanzibar na sisi mmetufikiria vipi, tunakwenda kufaidika vipi kutokana na fedha hii ambayo itakusanywa kutokana na makusanyo ambayo tunayachangia wote watanzania, tunaombeni sana na sisi kule Zanzibar kusema ukweli hali ni mbaya sana ya barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nije suala la fedha hizi milioni 500 kama tulivyosema kwamba Mama amefanya jambo zuri sana, lakini kiukweli na sisi Zanzibar barabara zetu za vijijini hali ni mbaya sana. Na tunafahamu hatuna shaka Mama yetu atakisikia kilio hiki.
Nichukue fursa hii kwa niaba ya Wabunge wenzangu wa Zanzibar tunamuomba sana Mama yetu, tunamlilia na sisi atuangalie hali zetu za barabara Zanzibar kwakweli ni mbaya, tunamuomba sana atuangalie ili na sisi aweze kutupatia fedha hizi na wala hatuna shaka kutokana na usikivu wake nina imani yangu kwamba atatufikiria. Waswahili wanasema Mama ni Mama na anaye mdharau Mama hukumbwa na laana, hatupo tayari kukumbwa na laana, tunafahamu sana Mama yetu ni msikivu na ataendelea kutusikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kumalizia nigusie Sekta ya Uvuvi mara nyingi tumekuwa tukipiga kelele kuhusu Sekta ya Uvuvi hususani kwenye kanuni zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba hadi sasa bado Serikali haijataka kuliangalia kwa ukaribu sana kuhusiana na changamoto ya kanuni ya uvuvi inayozuia ring net hadi sasa hivi ninavyoongea wavuvi wa Kigamboni na wa Mafia bado hawajapatiwa leseni, wanakaa hivi watu wanafamilia, wanakaa kila wakifika wanapigwa danadana hawapatiwi leseni kisingizio ni kanuni, tuambie, Mheshimiwa Waziri nikuombe au kwa Waziri Mkuu aliingilie kati wavuvi wanapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa ring net uliingia nchini mwaka 1984 mpaka 1985 Serikali iliwapatia kibali na ikauhalalisha uvuvi huu kwamba auharibu mazingira. Lakini kama haitoshi uvuvi wa ring net duniani nchi kama India, China, Norway, Dubai, Finland, Oman zinatumia uvuvi huu na uvuvi huu hata Shirika la Chakula Duniani unautambua uvuvi huu wa ring net kwamba hauharibu mazingira, iweje leo Tanzania tuseme kwamba uvuvi huu unaharibu mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali ituangalie ndugu zetu wanapata tabu wanategemea Sekta ya Uvuvi na Serikali inapiga kelele kwamba wananchi wajiajiri sasa wanapojiajiri tunapokwenda kuwawekea vikwazo tujue tunawasababishia mazingira magumu. Mtu anatoka ameacha watoto nyumbani anakwenda sehemu za Mafia au Kigamboni kufanya shughuli ya uvuvi akifika anazuiwa tuliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana Mwenyekiti kwa kunipatia fursa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Rais. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia mpaka muda huu nikiwa bado nina neema yake ya uhai na afya njema. Vilevile nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yao yote Wizarani kwa kuandaa hotuba nzuri kabisa na kuiwasilisha kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Jemadari Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maendeleo anayoendelea kuifanya katika Taifa letu. Mama ameonesha uwezo mkubwa sana na kwa kweli anastahili pongezi. Tunapompongeza, hatumpongezi kwa bahati mbaya, ni kwa mazuri na makubwa tunayoyaona katika nchi yetu ambayo anaendelea kuyatekeleza mama huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia hotuba hii kwenye taasisi ya TASAF. Nitagusia kidogo tu. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuutekeleza mradi huu kwenye jamii yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali kuendeleza mradi huu. Tunafahamu kwamba mradi huu umeanza awamu kwa awamu, ulianza na Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, wakaja viongozi wengine wakauendeleza. Sasa kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia kukubali kuuendeleza mradi huu, kwa kweli, anastahili pongezi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naipongeza TASAF, imekuwa ikifanya kazi nzuri sana. Pia kuna maeneo naomba niishauri Serikali ili iangalie katika program hii ya TASAF. Kwa mfano, kwenye vigezo vya kuwatambua wanufaika; malalamiko yamekuwa mengi kwa wananchi wetu kwamba, kuna baadhi ya wananchi wana sifa za kuingia kwenye mpango huu, lakini kwa kweli bado wanaendelea kuachwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie vigezo. Kwa mfano, tunapoangalia kigezo cha umasikini, tukiangalia kwamba mtu akipata nyumba tayari eti anaonekana kwamba, sio masikini. Tuangalie hiyo nyumba ameipataje? Kuna mazingira tofauti ya kuipata nyumba. Wakati mwingine mtu anajengewa na wahisani. Hatuwezi kusema kwamba huyu siyo masikini tena. Au wakati mwingine familia ilikuwa na baba, baba amefariki, anapofariki familia hii inarudi katika ukwasi wa maisha. Kwa hiyo, kigezo cha nyumba hakiwezi kutumika kama ni kigezo cha mtu kutoingizwa kwenye Mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tuangalie vilevile ruzuku inayotolewa. Naipongeza TASAF imeandaa program za kutoa ajira za muda. Lengo la ajira hizi ni kuwawezesha wananchi kujimudu katika vile vipindi vigumu. Pia tuangalie: Je, unapokwenda kumlipa mtu Shilingi 3,000/= kwa siku, hivi jamani kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ni njema na malengo ni mema, lakini kulingana na kupanda kwa gharama za tuangalie namna ya kuboresha. Shilingi 3,000 sasa hivi kumpa mtu kwa kweli haiwezi kwenda kumsaidia kama vile ambavyo Mheshimiwa Rais amekusudia kuwasaidia wananchi wake. Kwa hiyo, tuangalie ikiwezekana tuongeze angalau iwe shilingi 5,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile muda wanaoutumia katika hizi ajira za muda. Wanakwenda wanufaika wanaanza saa 01:00 mpaka saa 09:00, analipwa shilingi 3,000, kulingana na ukubwa wa kazi na muda anaoutumia. Muda huo anaoutumia ina maana tayari hapa hatumsaidii. Ni vema tukaweka muda mchache ili aweze kufanya kazi nyingine za kumwingizia kipato. Nadhani hii itakuwa ni njia sahihi ya kuweza kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miradi ambayo tutakwenda kuifanyia kazi, tuwachagulie zile kazi nyepesi. Kama tunavyofahamu kwamba, wanufaika wengi wa TASAF hali zao ni duni, wengi wao ni akina mama. Kwa mfano, katika jimbo langu tunakwenda kutekeleza mradi huu wa ajira za muda kwenye masuala ya zege. Mama unambebesha saruji, wengine wanaangukanayo, ni jambo ambalo kwa kweli Mheshimiwa Waziri, ni lazima tuliangalie kwa kina. Ni vyema tukawatafutia zile kazi nyepesi ambazo wanazimudu, lakini vilevile muda wanaoutumia uwe mchache ili waweze kwenda kufanya shughuli nyingine za kujiingizia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kingine ni suala la vitambulisho vya NIDA. Mara nyingi Wabunge tumekuwa tukipiga kelele kuhusu tatizo la vitambulisho vya NIDA. Tokea Wizara hii iko kwenye Kamati ya USEMI tumekuwa tukishauri mara kwa mara kwamba, Wizara ikutane na Wizara ya Mambo ya Ndani, wakae kwa pamoja waangalie namna ya kutatua au kama haiwezekani basi, kigezo cha kitambulisho cha NIDA kiondolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Masheha, akishathibitishwa na Sheha basi aweze kuingizwa kwenye Mpango, lakini suala la kuweka kitambulisho cha NIDA kama ni kigezo, na huku tayari kuna vikwazo vya kupata hicho kitambulisho cha NIDA, hapa itakuwa hatuwatendei haki wananchi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akutane na Wizara inayohusika ili tuangalie namna ya kutatua changamoto hii ya vitambulisho vya NIDA ili wananchi waweze kupata haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa haraka kulingana na muda, nije kwenye program ya kuendeleza miundombinu ya miradi ya kijamii. Tumeelezwa hapa kwamba kuna miradi 550 tayari iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Naomba kuwe na utaratibu mzuri wa kugawanya miradi hii, kwa sababu kuna baadhi ya Shehia, mfano kwenye jimbo langu Shehia ya Mjini Wingwi, Mapofu, wamepeleka barua za maombi ya miradi kama hii, lakini hadi leo ukiangalia, miradi inapelekwa sehemu moja au sehemu chache, wakati wananchi wanaohitaji miradi hii ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili mkalifanyie kazi. Kwa zile Shehia ambazo tayari wameshapeleka barua zao za maombi basi na huko kuangaliwe namna ya kufanyiwa kazi. Wananchi wote tunahitaji hizi huduma, keki hii ya Taifa tuweze kuifaidi sote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nije kwenye upelekaji kwenye rufaa. Tumeelezwa kwamba, bado kuna malalamiko ya rufaa yanaendelea kufanyiwa kazi na ni muda sasa. Kwenye majimbo yetu wananchi wanakuwa wakitulalamikia kwamba rufaa imekuwa ni muda mrefu, watu wanatolewa bila utaratibu. Hebu niombe hizi rufaa ziende kwa haraka ili kama anastahili kuingizwa kwenye mpango aendelezwe kwenye mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha zaidi ni kwamba kuna wananchi tayari wameshafanya kazi karibu miezi miwili, lakini wanafikia mahali wanaondolewa kwenye mpango na kile walichofanyia kazi bado hawajalipwa. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iende ikafanyie kazi hizi rufaa. Hawa wananchi kama wanastahili kupata hizi haki waendelee kuzipata, lakini kama hawastahili vilevile kuandaliwe utaratibu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vikundi, kutolewa elimu kwa wanufaika. Tumeambiwa kuna vikundi kadhaa vimeundwa, lakini ukifuatilia kwa kweli bado wananchi hawa elimu ya kuibua miradi ni ndogo. Tutumie maafisa wetu wa huduma za jamii, lakini vilevile tutumie wataalam wetu ili waweze kuwasaidia wanufaika hawa waweze kuibua miradi kulingana na mazingira wanayoishi ili mradi huu wa TASAF uweze kukidhi yale malengo ambayo Mheshimiwa Rais ameyakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nishukuru sana, naunga mkono hotuba hii. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia mpaka muda huu nikiwa na afya njema na kunipa kibali cha kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Marais wangu; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuudhihirishia ulimwengu uwezo wake, umahiri wake wa kuliongoza Taifa letu. Watanzania wana matumaini makubwa kwa Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimpongeze sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ally Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya kule Zanzibar. Sasa hivi ukija Zanzibar ni mafuriko ya miradi ya maendeleo. Kila sehemu ni miradi ya maendeleo maskuli yanajengwa kwa wingi sana na vituo vya afya kila sehemu. Kiukweli Mheshimiwa Dkt Hussein Mwinyi kwa upande wake wa Zanzibar na yeye anaupiga mwingi sana. Yote haya ni kutokana na ushirikiano mkubwa ambao anaupata kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli tunawapongeza sana Viongozi wetu hawa Wakuu wa Kitaifa, kazi wanayoifanya ni nzuri sana na inaleta matumaini kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake pamoja na timu yote ya Wizara ya Fedha kwa wasilisho zuri la bajeti, ni bajeti ambayo inakwenda kujibu changamoto za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo sasa nielekee kwenye mchango wangu na nitachangia mambo mawili; suala la kilimo cha mwani, pamoja na suala la uvuvi. Kwa kawaida duniani kote wananchi wanategemea kuendesha maisha yao kutokana au kutegemeana na rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amewajaalia katika Taifa lao, ni vivyo hivyo kwa wananchi wa Tanzania. Kwa upande wa Zanzibar kama tunavyofahamu Zanzibar ni nchi ya visiwa ambavyo eneo lake kubwa imezungukwa na Bahari kuu ya Hindi. Hapa maana yake wananchi hawa wa Zanzibar watategemea bahari kama rasilimali yao. Kwa upande wa Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi hawa inawajengea mazingira mazuri na mazingira wezeshi katika kuhakikisha kwamba wanatumia rasilimali hii ili kuweza kujipatia kipato cha kuendeshea familia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali nitagusia zao la mwani. Kama nilivyosema eneo la ardhi kwa Zanzibar ni dogo sana, hivyo wananchi hawawezi kujishughulisha na shughuli za kilimo kwa vile eneo la ardhi ni dogo, maana yake wananchi hawa wa Zanzibar hususan Pemba wamejiajiri kwenye zao la mwani kama ndivyo zao la mwani. Wananchi wa Pemba au wa Zanzibar wamelichukulia zao la mwani kama ni kilimo mbadala, badala ya kuelekea kwenye ardhi maana yake wanaelekea baharini kulima zao hili na ni zao ambalo kwa sasa limeajiri wananchi wengi. Wananchi hawa ambao wamejikita kwenye kilimo cha mwani ni wananchi wenye kipato cha chini na hususan akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la mwani ni zao ambalo linalimwa na nchi mbalimbali ulimwenguni ikiwemo China, Indonesia pamoja na Philippine. Kuna aina mbili za mwani; kuna cottonii na spinosum farm. Hizi ni aina ambazo zinalimwa ulimwenguni miongoni mwa nchi zinazolima ni kama nilivyozitaja. Mwani unatumika katika matumizi mbalimbali Wabunge wenzangu wengine wameelezea vya kutosha, unatumika kama chakula, madawa, unga, mbolea pamoja hata mapambo ya nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile unatumika kiongozeo cha ladha katika vyakula, kutokana na faida hii tumeona nchi ambazo zinazalisha mwani mfano Indonesia wananchi wake wanapata faida mbalimbali, na wanaendesha familia zao kutokana na kilimo hichi cha Mwani. Kwa mfano, mnamo miaka ya 2015 katika familia moja iliweza kuzalisha takribani tani 70,000 kwa familia moja na kuweza kuingiza kipato wastani wa Dola 15,000 ambayo ni sawa na fedha ya Kitanzania 34,500,000 hiki ni kipato kikubwa sana kwa mwananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuangalie wananchi hawa wa Indonesia katika Kijiji cha Solowesi mwaka 2015 waliweza hadi kufikia familia kupata kipato cha Milioni 34 fedha ya Kitanzania hili ni pato kubwa sana, sasa ni wakati Serikali yetu kuona kwamba inalitilia maanani na kulipa umuhimu zao la mwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameelezea vizuri mikakati ya Uchumi wa Bluu na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri amelielezea katika kitabu chake cha bajeti kwenye ukurasa wa 76 mikakati ya Uchumi wa Bluu, nimuombe Rais wa Zanzibar na Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba katika Sera au mikakati ya uchumi wa bluu kwa upande wa Zanzibar kipaumbele kiwekwe kwenye zao la mwani, kwa sababu ni zao ambalo limebeba wananchi walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar wananchi walio wengi wamejiajiri kwenye zao la mwani, sasa nimuombe sana Mheshimiwa Rais, miongoni mwa vipaumbele katika mikakati ya kulikuza au kukuza sera ya Uchumi wa Bluu iwekwe kwenye zao la mwani, atatusaidia sana Wazanzibar. Nimuombe sana Mheshimiwa Rais na niiombe Serikali zao la mwani wasione kwamba labda ni zao la kiwango cha chini, ni zao ambalo linaweza kuwasaidia sana wananchi na linakwenda kuwakomboa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nilivyoelezea umuhimu wa mwani wakulima wetu wa mwani wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali, miongoni mwa changamoto hizo kwanza inaonekana Serikali bado haijailipa uzito wa kutosha zao la mwani, changamoto ya pili wakulima wetu bado wanalima kienyeji hawana elimu ya kutosha juu ya zao hili, lakini kama haitoshi zao la mwani kwa kawaida linastawi zaidi katika kipindi cha mvua na kipindi cha kiangazi halistawi kutokana na temperature kuwa katika hali ya kiwango cha juu. Kama ndivyo, maana yake katika msimu huu wa mvua ambao zao la mwani linastawi vizuri zaidi, wakulima wanajitahidi kulima lakini changamoto inajitokeza wakati wa ukaushaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu zao la mwani linahitaji jua ili kuweza kukaushwa na kuweza kupelekwa sokoni. Sasa maana yake wananchi wanapolichukua zao la mwani, wanapolitoa baharini na kwenda kulikausha hatimae inanyesha mvua, na kawaida ya mwani unaponyeshewa na mvua, mara moja tu maana yake umepoteza uhalisia wake wote, na hivyo kumtia hasara mkulima. Changamoto nyingine ni suala la bei, mara nyingi wanaonunua mwani ni matajiri au kampuni na hatimaye kampuni hizi au matajiri hawa wanapanga bei ambazo wanazitaka wao, bei ambazo zinamuumiza mkulima, hizi ni changamoto ambazo kwakweli zinasababisha wakulima wetu kupata hasara kubwa na kutoweza kuona ile faida ya kilimo chao cha mwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kama nilivyoelezea wakulima wetu wanaliendesha zao hili bila utaratibu mzuri, bila kutumia utaratibu wa kibiashara, bila kuzingatia kwamba labda…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali sasa itujengee makaushio ili wakulima waweze kukaushia mwani wao katika kipindi cha mvua, vile vile niiombe Serikali…
Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa Mwaka 2023.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi ya kuchangia Miswada hii ya Sheria ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla tumuombee kwa Mungu Mheshimiwa Spika wetu ili Mwenyezi Mungu amjalie aweze kufanikiwa katika safari yake ya kuwania Urais katika Mabunge ya Dunia. Kwa nini ninasema kwamba tumwombee ni kwa sababu pindi Mwenyezi Mungu atakapomjalia kupata nafasi hii anakwenda kulitangaza Taifa letu na anakwenda kutuheshimisha kama Taifa, kwa hiyo tunaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu akujalie ili uweze kufanikiwa katika nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dkt. Samia suluhu Hassan kwa kuleta Muswada huu au kwa kuleta Miswada hii. Miswada hii kwa kweli inakwenda kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge mara nyingi tumekuwa tukizililia hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa nini nampongeza Mheshimiwa Rais kwenye Muswada huu wa Tume ya Mipango kwa kweli unadhihirisha ni kwa jinsi gani Mheshimiwa Rais anaonesha dhamira yake ya kuweza kulipeleka mbele Taifa letu, kwa sababu kama Taifa hatuwezi kusonga mbele bila kuwepo na mipango lakini vilevile utekelezaji na kufanya tathmini juu ya utekelezaji wa mipango hii. Kwa kweli Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana.
Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango. Kama walivyotangulia kuzungumza Wabunge wenzangu hapa kwamba Tume hii ilikuwepo tokea kipindi cha uhuru mwaka 1961 lakini imekuwa ikija katika sura tofauti tofauti. Kwa kweli kuwepo kwa Tume hii ya Mipango au kitendo cha Mheshimiwa Rais kurejesha tena Tume hii ya Mipango maana yake kwanza inakwenda kuipa zaidi Bunge jukumu lake la kuisimamia Serikali katika mipango ya maendeleo, kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 63(3)(c) ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba Bunge miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia mipango ya maendeleo. Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba tulikuwa tulikuwa tukilalamikia kwamba kutokuwepo kwa Tume hii ya Mipango vilevile kulikuwa kunapelekea ufanisi mdogo wa usimamizi na utekelezaji. Kama tunavyokumbuka kwamba kwa sasa upangaji wa mipango na utekelezaji uko kwenye Wizara ya Fedha na kama tunavyokumbuka kwamba jukumu la Wizara ya Fedha na kwenda kuongezea tena mzigo wa upangaji wa mipango wa maendeleo na utekelezaji na usimamizi kwa kweli inapelekea ufanisi mdogo sana wa utekelezaji wa mipango yetu ya nchi. Sasa Serikali inapoleta Sheria hii maana yake sasa tunakwenda kutofautisha mipango, usimamizi pamoja na Wizara ya Fedha, maana yake sasa usimamizi wa mipango yetu na utekelezaji itaweza kwenda kusimamiwa kwa ufanisi mkubwa zaidi tofauti na sasa ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna tafiti mbalimbali zilifanyika mwaka 2022 zilionesha kwamba kutokana na wingi au ukubwa na uzito wa majukumu ya Wizara ya Fedha inapelekea usimamizi wa Tume hii ya Mipango na mipango ya nchi kutokuwa na ufanisii wa juu zaidi. Sasa Serikali inapoleta Sheria hii ya Tume ya Mipango maana yake sasa mipango yetu itakwenda kutekelezeka vilevile pia kufanyika kwa tathmini jinsi gani mipango yetu itakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, jirani yangu hapa Mzee wangu Kakunda ameelezea juu ya ushirikishwaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar. Kama tunavyofahamu kwamba Zanzibar kwa upande wetu na sisi iko Tume ya Mipango ambayo mfumo wake ni sawa na huu ambao unataka kuanzishwa ambapo Mwenyekiti wake anakuwa ni Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, vilevile hata ukiangalia baadhi ya majukumu ya Tume ukiangalia kama vile yanashabiana au yanakwenda kugusa vipengele vya Muungano. Kwa mfano, kwenye Ibara ya 6(2)(g) inasema kwamba miongoni mwa majukumu ya Tume kutoa mwongozo kuhusu uchumi kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa. Tunapozungumzia nchi nyingine na mashirika ya kimataifa maana yake tunakwenda kugusa suala la Muungano, kwa hiyo niombe Serikali kwamba iweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba inaishirikisha Tume ya Mipango ile ya Zanzibar ili tuende pamoja kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kwamba nchi yetu ilivyoingia katika uchumi wa kati mwaka 2020 ilijumuisha pia Zanzibar, kwa hiyo ili kwenda pamoja ni vyema kuwepo kwa ushirikiano wa mara kwa mara kati ya Tume hii ya Tanzania Bara na Tume ile ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, vilevile niendelee kutoa mchango wangu katika suala la Tume hii ya Mipango. Vilevile niseme kwamba matarajio yetu baada ya kupitishwa kwa Sheria hii nini tunatarajia? Kwanza ni Wizara zote za kisekta kuwa na utaratibu wa kupanga kwa pamoja. Tumeona imekuwa ni kawaida kila Wizara inajipangia mipango yake ya maendeleo na hivyo kupelekea gharama kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Leo Mheshimiwa Kairuki au Profesa Mbarawa anajenga barabara kesho Mheshimiwa Juma Aweso anakwenda kukata barabara anapitisha miradi ya maji. Hii inapelekea matumizi mabaya ya fedha za umma. Kuja kwa chombo hiki cha Tume ya Mipango maana yake sasa tutaweza kutumia vizuri rasilimali zetu za Taifa na hivyo kupelekea kasi ya uchumi katika maendeleo na maendeleo endelevu katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kupitishwa au kuundwa kwa Tume hii itakwenda kuongeza ushiriki na ushirikishwaji wa sekta binafsi. Kama tunavyoona kwamba kwa sasa kila sekta inajipangia mipango yake ya maendeleo lakini hata ushiriki na ushirikishwaji wa sekta binafsi unakuwa ni mdogo sana au unakuwa haupo katika hali ya ufanisi zaidi lakini kuwepo kwa Tume ya Mipango maana yake sasa ushirikishwaji na ushiriki wa sekta binafsi utakwenda kuwa mkubwa zaidi na wa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nigusie katika Sheria hii ya Usalama wa Taifa. Niwaombe Wabunge wenzangu kwamba tuzipitishe sheria hizi na lengo la kuletwa Muswada huu wa Sheria ni kwenda kuongeza hali ya usimamizi wa Usalama wa Taifa letu. Kama tunavyoona kwamba chombo hiki ni chombo muhimu sana kwa maslahi ya usalama wa Taifa letu, hivyo inavyokuja Sheria hizi maana yake tunakwenda kuweka Taifa katika hali nzuri zaidi ya kusimamia usalama wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuzipitishe kwa moyo mmoja Sheria hizi kwani zinakwenda kuleta hali ya mabadiliko makubwa katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Yatokanayo na Urekebu wa Sheria wa Mwaka 2023 .
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi ya kuchangia Miswada hii ya Sheria ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla tumuombee kwa Mungu Mheshimiwa Spika wetu ili Mwenyezi Mungu amjalie aweze kufanikiwa katika safari yake ya kuwania Urais katika Mabunge ya Dunia. Kwa nini ninasema kwamba tumwombee ni kwa sababu pindi Mwenyezi Mungu atakapomjalia kupata nafasi hii anakwenda kulitangaza Taifa letu na anakwenda kutuheshimisha kama Taifa, kwa hiyo tunaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu akujalie ili uweze kufanikiwa katika nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dkt. Samia suluhu Hassan kwa kuleta Muswada huu au kwa kuleta Miswada hii. Miswada hii kwa kweli inakwenda kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge mara nyingi tumekuwa tukizililia hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa nini nampongeza Mheshimiwa Rais kwenye Muswada huu wa Tume ya Mipango kwa kweli unadhihirisha ni kwa jinsi gani Mheshimiwa Rais anaonesha dhamira yake ya kuweza kulipeleka mbele Taifa letu, kwa sababu kama Taifa hatuwezi kusonga mbele bila kuwepo na mipango lakini vilevile utekelezaji na kufanya tathmini juu ya utekelezaji wa mipango hii. Kwa kweli Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana.
Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango. Kama walivyotangulia kuzungumza Wabunge wenzangu hapa kwamba Tume hii ilikuwepo tokea kipindi cha uhuru mwaka 1961 lakini imekuwa ikija katika sura tofauti tofauti. Kwa kweli kuwepo kwa Tume hii ya Mipango au kitendo cha Mheshimiwa Rais kurejesha tena Tume hii ya Mipango maana yake kwanza inakwenda kuipa zaidi Bunge jukumu lake la kuisimamia Serikali katika mipango ya maendeleo, kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 63(3)(c) ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba Bunge miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia mipango ya maendeleo. Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba tulikuwa tulikuwa tukilalamikia kwamba kutokuwepo kwa Tume hii ya Mipango vilevile kulikuwa kunapelekea ufanisi mdogo wa usimamizi na utekelezaji. Kama tunavyokumbuka kwamba kwa sasa upangaji wa mipango na utekelezaji uko kwenye Wizara ya Fedha na kama tunavyokumbuka kwamba jukumu la Wizara ya Fedha na kwenda kuongezea tena mzigo wa upangaji wa mipango wa maendeleo na utekelezaji na usimamizi kwa kweli inapelekea ufanisi mdogo sana wa utekelezaji wa mipango yetu ya nchi. Sasa Serikali inapoleta Sheria hii maana yake sasa tunakwenda kutofautisha mipango, usimamizi pamoja na Wizara ya Fedha, maana yake sasa usimamizi wa mipango yetu na utekelezaji itaweza kwenda kusimamiwa kwa ufanisi mkubwa zaidi tofauti na sasa ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna tafiti mbalimbali zilifanyika mwaka 2022 zilionesha kwamba kutokana na wingi au ukubwa na uzito wa majukumu ya Wizara ya Fedha inapelekea usimamizi wa Tume hii ya Mipango na mipango ya nchi kutokuwa na ufanisii wa juu zaidi. Sasa Serikali inapoleta Sheria hii ya Tume ya Mipango maana yake sasa mipango yetu itakwenda kutekelezeka vilevile pia kufanyika kwa tathmini jinsi gani mipango yetu itakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, jirani yangu hapa Mzee wangu Kakunda ameelezea juu ya ushirikishwaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar. Kama tunavyofahamu kwamba Zanzibar kwa upande wetu na sisi iko Tume ya Mipango ambayo mfumo wake ni sawa na huu ambao unataka kuanzishwa ambapo Mwenyekiti wake anakuwa ni Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, vilevile hata ukiangalia baadhi ya majukumu ya Tume ukiangalia kama vile yanashabiana au yanakwenda kugusa vipengele vya Muungano. Kwa mfano, kwenye Ibara ya 6(2)(g) inasema kwamba miongoni mwa majukumu ya Tume kutoa mwongozo kuhusu uchumi kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa. Tunapozungumzia nchi nyingine na mashirika ya kimataifa maana yake tunakwenda kugusa suala la Muungano, kwa hiyo niombe Serikali kwamba iweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba inaishirikisha Tume ya Mipango ile ya Zanzibar ili tuende pamoja kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kwamba nchi yetu ilivyoingia katika uchumi wa kati mwaka 2020 ilijumuisha pia Zanzibar, kwa hiyo ili kwenda pamoja ni vyema kuwepo kwa ushirikiano wa mara kwa mara kati ya Tume hii ya Tanzania Bara na Tume ile ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, vilevile niendelee kutoa mchango wangu katika suala la Tume hii ya Mipango. Vilevile niseme kwamba matarajio yetu baada ya kupitishwa kwa Sheria hii nini tunatarajia? Kwanza ni Wizara zote za kisekta kuwa na utaratibu wa kupanga kwa pamoja. Tumeona imekuwa ni kawaida kila Wizara inajipangia mipango yake ya maendeleo na hivyo kupelekea gharama kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Leo Mheshimiwa Kairuki au Profesa Mbarawa anajenga barabara kesho Mheshimiwa Juma Aweso anakwenda kukata barabara anapitisha miradi ya maji. Hii inapelekea matumizi mabaya ya fedha za umma. Kuja kwa chombo hiki cha Tume ya Mipango maana yake sasa tutaweza kutumia vizuri rasilimali zetu za Taifa na hivyo kupelekea kasi ya uchumi katika maendeleo na maendeleo endelevu katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kupitishwa au kuundwa kwa Tume hii itakwenda kuongeza ushiriki na ushirikishwaji wa sekta binafsi. Kama tunavyoona kwamba kwa sasa kila sekta inajipangia mipango yake ya maendeleo lakini hata ushiriki na ushirikishwaji wa sekta binafsi unakuwa ni mdogo sana au unakuwa haupo katika hali ya ufanisi zaidi lakini kuwepo kwa Tume ya Mipango maana yake sasa ushirikishwaji na ushiriki wa sekta binafsi utakwenda kuwa mkubwa zaidi na wa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nigusie katika Sheria hii ya Usalama wa Taifa. Niwaombe Wabunge wenzangu kwamba tuzipitishe sheria hizi na lengo la kuletwa Muswada huu wa Sheria ni kwenda kuongeza hali ya usimamizi wa Usalama wa Taifa letu. Kama tunavyoona kwamba chombo hiki ni chombo muhimu sana kwa maslahi ya usalama wa Taifa letu, hivyo inavyokuja Sheria hizi maana yake tunakwenda kuweka Taifa katika hali nzuri zaidi ya kusimamia usalama wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuzipitishe kwa moyo mmoja Sheria hizi kwani zinakwenda kuleta hali ya mabadiliko makubwa katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)