Supplementary Questions from Hon. Maryam Omar Said (3 total)
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu na uchakavu wa ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Je, ni lini Serikali itaanzisha ujenzi mpya kwa ajili ya ofisi hizi katika Mkoa huu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mpango wa kujenga ofisi zote za Makao Makuu ya Polisi ngazi ya Mkoa. Kwa hiyo, tumeanza na Kusini Pemba, hatua itakayofuata ni Kaskazini Pemba ili Mikoa yote iweze kupata vituo vya Polisi vyenye ngazi ya Mkoa kwa maana ya Daraja A. Kwa hiyo, uwe na subira katika miaka miwili ijayo kituo hicho pia kitakuwa kimejengwa.
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha vifungashio mbadala ya mifuko hii ya plastiki inapatikana kwa wingi hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nataka Mheshimiwa Maryam afahamu kwamba kuna vifungashio, lakini pia kuna mifuko ambayo imependekezwa na hiyo ndiyo ambayo haichafui mazingira. Sasa, vifungashio vitaongezeka kwanza kwa mujibu wa sheria kwa sababu viko vifungashio ambavyo vimeruhusiwa kisheria na viko vifungashio ambavyo vipo vinasambaa huko ambavyo havijaruhusiwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ili kifungashio kiwe kisheria, kwanza kiwe kina nembo ya kampuni husika, maana yake tukione hiki ni Chilo Company ili hata ikitokea kifungashio kimeenea tunajua tumfuate nani ambaye amesambaza vifungashio hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kikubwa ni kwamba tutaendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii, hasa wenye viwanda, watengeneze vifungashio ambavyo vimeruhusiwa ili viweze kuwa vingi na tuondoe kabisa vifungashio ambavyo haviko kisheria katika jamii. (Makofi)
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha inaviongezea nguvu vikundi vinavyojishughulisha na upandaji miti kandokando ya bahari ili kurudisha uoto wa asili?
NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa ya baadhi ya watu kukata miti iliyopo pembezoni mwa kandokando ya Bahari hasa miti ya mikoko na mwisho wa siku wanaharibu mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, zipo jitihada ambazo tumezifanya; kwanza, tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, ili kuwaeleza umuhimu wa uwepo wa mikoko. Sasa hivi kumekuwa kuna changamoto kubwa, maji ya bahari kuingia kwenye makazi, kuingia kwenye vipando vya wananchi visivyostahimili maji ya chumvi. Hii yote ni kwa sababu, mikoko imekatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kuendelea kutoa mikoko bure ili iendelee kupandwa kwenye yale maeneo ya bahari, lakini zaidi kuendelea kutoa miradi. Pia, miongoni mwa miradi inayotolewa katika Ofisi ya Makamu wa Rais ni pamoja na upandaji wa miti pembezoni mwa bahari, hasa miche ya mikoko. Nakushukuru.