Primary Questions from Hon. Juma Usonge Hamad (7 total)
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa Kituo kidogo cha Polisi cha Chaani Lungalunga.?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo kidogo cha Polisi cha Chaani, Lungalunga kilichopo Wilaya ya Kaskazini A ni kituo kilichojengwa kwa kushirikisha jitihada na nguvu za wananchi. Jengo la kituo hiki ni chakavu na haliwezi kufanyiwa ukarabati kwa sababu kuta zake zimeweka nyufa nyingi na kingo za jengo zimebomoka.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar imeshaandaa mchoro na makadirio kwa ajili ya kujenga Kituo kipya cha Daraja C katika eneo hilo. Kiasi cha fedha, shilingi 82,530,960 kinahitajika kwa ajili ya ujenzi huo, na zitaingizwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 kulingana na upatikanaji wa fedha. Nashukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Miradi ya muda mrefu ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi inayotekelezwa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge Hamad Juma, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaratibu miradi miwili kwa Upande wa Zanzibar. Mradi mmoja wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa kwenye Wilaya ya Kaskazini A, Unguja; na Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame Nchini (LDFS) unaotekelezwa katika Wilaya ya Micheweni, Pemba.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, tayari Serikali imechukua hatua za kiutendaji kuwataka waratibu na washughulikiaji wa miradi hii kitaifa kuhakikisha miradi inakamilika kikamilifu na kwa ubora. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ili kusimamamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa upande wa Zanzibar ili miradi hii ikamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kupitia TBA kuwajengea nyumba watumishi wa Serikali ya Muungano kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala, Sura 245 ikisomwa pamoja na Agizo la Uanzishwaji wa Wakala GN. Na. 24 la tarehe 14 Februari, 2003. Moja ya jukumu la msingi la TBA ni kujenga na kukarabati nyumba na majengo ya Serikali kwa ajili ya makazi kwa watumishi wa umma Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, Jukumu la ujenzi wa nyumba kwa watumishi wa Umma kwa upande wa Zanzibar liko chini ya Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA). Hata hivyo, TBA na ZBA wanashirikiana na kushauriana kwenye mambo mbalimbali ya kitaalam na kujengeana uwezo, ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitangaza ndani na nje ya nchi bidhaa zinazotokana na Zao la Mwani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge Hamad Juma, Mbunge wa Jimbo la Chaani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitangaza bidhaa za zao la mwani nchini kupitia maonyesho, warsha na matamasha mbalimbali ikiweno Sherehe za Wakulima Nane Nane, Maonesho ya Biashara za Kimataifa Saba Saba, Sherehe za Siku ya Mvuvi Duniani na Siku ya Chakula Duniani. Pia bidhaa za mwani zinatangazwa katika vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo runinga, redio, magazeti na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Korea Kusini imeandaa Tamasha la Uvuvi Korea na Afrika (Korea African Fisheries Forum) litakalofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 14 hadi 15 Juni, 2023 litakalojumuisha wadau kutoka Korea Kusini na Senegal. Tamasha hili linalenga kutangaza shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji za Afrika ikiwemo zao la mwani na bidhaa zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inaandaa mpango wa kutangaza bidhaa za mwani nje ya nchi kwa kutumia Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali kupitia matamasha, vikao na warsha zitakazofanyika katika nchi hizo.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama kisukari, pressure na shinikizo la damu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Jimbo la Chaani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yana gharama kubwa na yanahitaji tiba wakati wote. Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa ambao wamethibitika hawana uwezo wa kugharamikia matibabu hayo kwa mujibu wa Sheria ya Afya. Hata hivyo, Serikali ipo katika hatua ya mwisho za ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ambao utawezesha wananchi wote kupata huduma za afya katika Vituo vya Afya nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kupunguza kodi, tozo na ushuru wa bidhaa za chakula/mboga kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bidhaa za chakula na mbogamboga halisi zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar hazitozwi kodi, tozo na ushuru wa aina yoyote kwa mujibu wa sheria, lakini bidhaa za chakula kutoka viwandani hutozwa tozo ya uchakataji nyaraka za forodha ya asilimia 0.6 tu kwenye thamani ya mzigo huo. Lengo la tozo hii ni kugharamia huduma ya uchakataji wa nyaraka za forodha na hutozwa kwa wateja wote wanaotumia mfumo wa forodha.
Mheshimiwa Spika, bidhaa za chakula na mbogamboga halisi hazitozwi tozo ya uchakataji wa nyaraka kwa sababu, hazihitaji kufanyiwa mchakato wa nyaraka katika mfumo wa forodha, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, lini Serikali itatuma wataalamu kwenda Kijiji cha Kandwe kilichopo Wilaya ya Kaskazini Unguja ili kutatua changamoto ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano katika pande zote mbili za Muungano kwa kushirikiana na watoa huduma. Kwenye mradi wa kufikisha mawasiliano katika Shehia (Kata) 38 Visiwani Zanzibar uliokamilika mwaka 2022, Kijiji cha Kandwi kilijumuishwa katika mradi huu na Kampuni ya Tigo – Zantel ilipewa jukumu la kufikisha mawasiliano katika Kijiji hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeiagiza UCSAF kufika katika Kijiji cha Kandwi kufika wiki ya kwanza ya mwezi huu Septemba kwa lengo la kufanya tathmini ya kina ili kubaini kama kuna eneo lolote lenye changamoto ya mawasiliano liweze kutatuliwa.