Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Usonge Hamad (19 total)

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naitwa Juma Usonge.

Mheshimiwa Spika,Mkoa wa Kaskazini Unguja ni mkoa ambao unaongoza kwa shughuli za kitalii kwa Zanzibar, lakini pia population ya watu ni kubwa sana. Naiomba sana Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri; wamejipangaje Wizara hii ili kuhakikisha Mkoa wa Kaskazini Unguja unakuwa na idadi kubwa ya Vituo vya Polisi, ingawa sasa hivi kuna Vituo vitano tu vya Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tumefanya tathmini ili tuweze kuona uchakavu wa vituo vilivyopo kwa madhumuni ya kuvifanyia ukarabati. Kwa hiyo baada ya kumaliza zoezi hilo, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tutaona maeneo mengine yanayohitaji kuimarishwa ulinzi ili tuweze kuona namna ya kuviongezea nguvu. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana Serikali kwa commitment ya kutaka kukijenga Kituo hicho cha Lungalunga. Sasa naomba niulize swali langu la nyongeza.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atapanga ziara ya kuja kutembelea kwenye eneo hilo ili wananchi wale wawe na matumaini makubwa kwamba kweli Serikali ina commitment ya kutaka kujenga kituo hiki cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ujenzi wa kituo hicho haujafanyika, nampa ahadi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kutembelea eneo hilo tukiwa pamoja naye ili kuweza kujiridhisha kwamba kazi itafanyika. Nashukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar kila siku kila tukija hapa kwenye kikao suala hili linaibuka. Mpaka muda huu nazungumza, mimi Jimbo langu la Chaani sijapokea kwa ukamilifu fedha hizi za Mfuko wa Jimbo. Tumekuwa tukilalamika kila session ya Bunge, bado Serikali hatujaona kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kutatua changamoto hizi ambazo tena tunakubaliana nazo sisi Wabunge kupitia upande wa Zanzibar. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge, Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiri kwamba bado kuna changamoto kwenye Mfuko wa Jimbo pamoja na kuboreshwa kwa hizi sheria. Changamoto kubwa tuseme ipo kwenye Mabaraza ya Miji na kwenye Halmashauri. Tulichokipanga baada ya Bunge hili, twende tukakae na viongozi wote wa Mabaraza ya Miji na Wakurugenzi wa Halmashauri wote Zanzibar ili tuwaeleze umuhimu wa fedha hizi kufika kwa wakati kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutekeleza miradi yao.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka, 2013 Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kilipata majanga ya kuungua kwa moto na hadi kufikia tarehe 29 Machi, kituo hicho tayari kimekamilika kwa asilimia 95. Je, ni ipi kauli ya Serikali ili kukamilisha asilimia hizi tano ili kituo kile cha polisi kiweze kufanya kazi vizuri kama inavyotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Usonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ikiwa wananchi wamejitahidi kukamilisha kituo kwa kiwango cha asilimia 95, nachukua dhima ya kuwasiliana na wenzetu wa Jeshi la Polisi kupitia Mfuko wao wa Tunzo na Tozo kukamilisha asilimia tano zilizobaki ili kituo hicho kiweze kukamilishwa. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa Vijiji ambavyo vipo hatarini kutoweka kwa miamba hii ya matumbawe ni Kijiji cha Pwani Mchangani ambacho kipo katika Jimbo langu la Chaani.

Je, ni lini Serikali itachukua hatua za haraka ili sasa kunusuru Matumbawe yale yasiharibike lakini pia yasitoweke kutokana na shughuli za kibinadamu ambazo zinaendelea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Juma Usonge Mbunge wa Jimbo la Chaani Kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nae nimshukuru na nimpongeze kwamba ni mmoja wa miongoni mwa Mabalozi wetu wazuri wa mazingira hasa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo juhudi mbalimbali ambazo tumepanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Kijiji cha Pwani Mchangani kinaendelea kuwa salama hasa katika suala zima la uhifadhi wa mazingira. Moja ni kupitia taaluma lakini yapo matumbawe ambayo tumeshayaandaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kuyaweka angalau sasa vile viumbe ambavyo vimo kwenye bahari viweze kuishi katika mazingira ambayo wanaweza waka-survive ili waweze kuhifadhi mazingira zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Wilaya ya Kaskazini B - Unguja ni miongoni mwa wilaya ambazo zimekosekana ofisi hiyo ya NIDA; je, ni lini Serikali itawahakikishia wananchi wa Wilaya ya Kaskazini B kuwajengea kituo hicho cha Ofisi ya NIDA? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua uwepo wa changamoto za ofisi maeneo mbali mbali ikiwemo wilaya aliyoitaja ya Kaskazini B, Unguja. Ni ahadi yetu tutaendelea kujenga hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Kama muda ungeruhusu, ningeweza kusoma hizo ofisi 31 ambazo zitapata fedha, lakini niko tayari kuzi-share na Waheshimiwa Wabunge wajue lakini kadri tunavyopata fedha, kila kusipokuwa na ofisi tutajenga ofisi hizo. Nashukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana namimi kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tumekuwa tukishauri sana hususan sisi Wabunge ambao tunatokea mwambao wa Pwani kuhusiana na bei ndogo ya mwani.

Je, Serikali haioni haja sasa kufungamanisha mfumo huu wa ununuzi wa mwani na mfumo wa stakabadhi ghalani ili kupunguza utitiri wa wanunuzi ambao wamejipangia bei ndogo na kumuumiza mkulima wa mwani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimeeleza, mkakati wetu ni pamoja na kujenga maghala. Hili la kujenga maghala ni kuelekea katika kile alichokishauri Mheshimiwa Mbunge, ya kwamba tunaweza pale mbele kwenda katika mfumo wa kuliingiza zao la mwani katika stakabadhi ghalani. Tukijenga maghala na tukaongeza uzalishaji tutafanikiwa kufika katika hatua ile aliyoishauri Mheshimiwa Juma.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile Mheshimiwa Waziri amekiri kabisa kwamba katika miradi hiyo kuna changamoto ya ucheleweshwaji; naiomba sana Serikali, kama itaridhia.

Kwa nini kwa mwaka wa fedha huu isikamilishe miradi hii kwa kutumia fedha za ndani badala ya kusubiria fedha za wahisani, ambapo hadi leo hii ni muda wa miaka mitano miradi ile haijakamilika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami kwenda kuiona miradi hiyo inayotelelezwa kwenye wilaya mbili ilivyosimama na bado hatma ya kukamilika miradi hiyo haijulikani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi hii ambayo inatekelezwa Zanzibar, takribani ukiangalia miradi yote; ile ya EBARR na hii ya LDFS ni miradi ambayo kwanza fedha zake zipo, lakini ni miradi ambayo ukiiangalia muda wake wa kukamilika bado yaani haujafika, kwa sababu miradi hii ukamilikaji wake ni mpaka 2024.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Usonge kwamba pamoja na kwamba miradi hii ina fedha za wahisani, lakini pia kuna fedha ambazo zinatoka kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinakwenda kukamilisha miradi hii. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa asiwe na hofu.

Mheshimiwa Spika, suala la kufatana naye kwenda kukagua miradi hii, nimwambie tu kwamba niko tayari, kama ambavyo nimeshaanza mara ya kwanza, tutakwenda naye kukagua miradi hii na kuona ukamilifu wake na namna ambavyo inanufaisha wananchi. Nakushukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ukweli uliokuwepo, Shirika la Nyumba la Bara halitumi fedha kupitia Shirika la Nyumba la Zanzibar hadi muda huu.

a) Je, kuna ushirikiano gani sasa ya kuliwezesha shirika la Nyumba la Zanzibar kwa kulipatia fedha kwa ajili ya kuwajengea watumishi wa bara?

b) Je, kuna mkakati gani wa ushirikiano kati ya ZBA pamoja na TBA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyo kwisha kusema, ni kwamba nyumba za Zanzibar kwa watumishi wa umma zinajengwa chini ya Wakala wa Majengo wa Zanzibar lakini wana ushirikiano wa karibu sana kati ya ZBA pmoja na wakala wa majengo Tanzania Bara. Ushirikiano huo ni pamoja na kwamba Wakala wa Majengo Zanzibar wamekuja mara kadhaa huku Bara kujifunza namna ambavyo TBA wameweza kuendesha miradi mbalimbali happa nchini ikwemo miradi ya Dar es Salaam Magomeni quarter hapa Dodoma pamoja na mji wa kiserikali.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa swali lake la pili ni kwa kiwango gani TBA iipatie fedha ZBA. ZBA fedha zake zinatengwa kwenye Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi kule Zanzaibar. Na kwa mwaka wa fedha ujao, kwa maelezo ya ZBA ni kwamba wametenga takribani kiasi cha shilingi bilioni 56 ili kujenga nyumba takriban 400 zitakazo jengwa kwa Zanzibar nzima kwa maana ya Unguja na Pemba, na walau kila Wilaya watagusa kupitia mradi huu.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa hii. Kwa kweli vijana wetu wa skauti wametapakaa takribani nchi nzima; Bara na Visiwani. Kama Mheshimiwa Waziri alivyokiri kwamba wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali. Je, Serikali haioni haja sasa kutenga mfuko maalum wa kibajeti kupitia Wilaya, Mkoa na Kitaifa zaidi ili wawe na uhakika wa fedha zao kwa ajili ya kuendesha programu zao pamoja na kufanya kazi zao kiujumla? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge ambalo limefanana pia na jibu langu la msingi, na hata swali alilouliza Mheshimiwa Asha kwenye suala la kibajeti, kwamba tayari wao wana sheria ambayo inaanzisha na inatoa taratibu ikiwa ni pamoja na masuala ya kifedha, lakini kwa sababu pia ni eneo ambao linaonekana pengine lina upungufu, tutauangalia na Serikali na kuweza kuona pale panapopelea tuweze kuwasaidia zaidi na kutengeneza mifumo ambayo itawasaidia kuweza kuratibu na kutekeleza majukumu yao kama ambavyo jinsi tunawatarajia, ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa vile Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Muungano na Mazingira ndiyo ambayo inashughulika na masuala ya kuratibu na kushughulika na mabadiliko ya tabianchi. Nilitaka kujua je, mnatumia utaratibu gani wa kupokea miradi yote ambayo inatoka Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa kushughulika na haya mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ni kwamba kwanza tunaandaa maandiko ambayo yanalenga kwenye mradi husika. Kinachofuata sasa ni kufanya tathmini na utafiti wa kujua mradi ulioombwa na baadaye mradi huo unaanza utekelezwaji kama miradi iliyotekelezwa huko Zanzibar.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi ambao unatekelezwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ya Unguja kwa upande wa Zanzibar, mradi huo wa EBA ambao umedhaminiwa kupitia Mfuko huo ambao Mheshimiwa Waziri umetamka mradi wa EBA lakini mradi huo utekelezaji wake ilikuwa ni 2018 mpaka 2022, ukomo wa mradi huo tayari umeshakamilika.

Je, Wizara yako ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba mradi ule ambao tayari uko kule Wilaya ya Kaskazini Unguja kwenye Vijiji vya Matemwe na Shehia ya Mbuyutende unakamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najibu swali la Mheshimiwa Usonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Watanzania kwamba azma ya Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba inatatua changamoto zote zinazokabili wananchi hasa changamoto zinazokabili kwenye upande wa mabadiliko ya tabianchi. Azma nyingine kubwa ni kuhakikisha kwamba miradi yote iliyokwishaanzishwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwa inasimamiwa na fedha kutoka nje, tutahakikisha kwamba miradi hii inakamilika ili sasa iweze kunufaisha wananchi na wananchi waweze kunufaika na hiyo miradi na mambo mengine yaende. Nakushukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia matumaini hususan kwenye Balozi zetu. Ila tukumbuke kwamba tuna takribani zaidi ya miaka 30 sasa tokea mwani huu uletwe hapa kwetu Tanzania ambayo ni nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha mwani mwingi, lakini bado hatujaona jitihada kubwa za kuhakikisha mwani utambulika nchini na kuwa na thamani kwa wakulima wetu: Je, ni upi mpango wa Serikali sasa wa kushirikiana na taasisi ya sayansi na teknolojia iliyokuwepo Dar es Salaam pamoja na ile taasisi ya Zanzibar ambayo inashughulika na masuala ya mwani ili kuhakikisha mwani unakuwa na thamani nzuri na unatambulika? Hilo swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wizara imejipangaje sasa ili kutoa elimu kwa wakulima wetu ili wafahamu faida zinazopatikana kwenye huo mwani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu zao la mwani. Zao la mwani ni moja ya mazao ya kimakakati katika Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi ambayo yanatokana na mazao ya bahari. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni pamoja na kuzitumia hizi taasisi ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge hapa kwa maana ya COSTECH pamoja na ZSF iliyoko upande wa Zanzibar. Malengo haya tutaendelea kuyasisitiza kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha sasa huu mwani unakuwa maarufu siyo kwa Tanzania peke yake, ni mpaka nchi za pembezoni ili kuongeza biashara kubwa na pato la Taifa kwa ujumla kwa pande zote mbili; Tanzania Bara pamoja na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, hilo ndiyo mpango wetu wa sasa kuhakikisha kwamba tunaongeza engagement ya watu katika zao hili la mwani ikiwemo vijana, akina mama pamoja na wanaume ambao watahitaji kuingia katika zao hili. Kwa hiyo, tutatoa elimu na tutaongeza wataalam kwa ajili ya kusaidia zao la mwani. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya utekelezaji wa CSR kupitia Halmashauri. Kwa ushauri wangu, je, Wizara sasa haioni haja ya kuja na sheria na kanuni kabisa ambazo zitawa-guide watu wa hifadhi pamoja na wanaofanya shughuli za kiutalii zaidi ili lile suala la CSR liwe suala la kisheria kabisa? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake tunauchukua na tutakwenda kuufanyia kazi. Nashukuru.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipatia fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Kwa vile zao hili la Mwani zaidi ya asilimia 80 ndiyo tunategemea mauzo ya nje, lakini zaidi ya asilimia 20 ndiyo inabakia kwa ajili ya kulichakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zinabaki ndani ya nchi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu hasa kwa wale wakulima wetu ndani ya nchi kuweze kutengeneza bidhaa ambazo zitakuwa na soko pia zitakuwa na quality pia zitakuwa zinauzika ndani ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamad kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani kama nilivyokwisha kueleza kwenye jibu la msingi. Kwanza Mwani wetu mwingi unakaushwa katika michanga, Mheshimiwa Hamad na Wabunge wa kutoka katika Mikoa hii ya huku Pwani inayolima Mwani wanaweza kuwa ni mashahidi wangu. Ndiyo maana tumejielekeza katika kuhakikisha kwamba tunapata kitu kilicho na ubora kwa kwenda kupeleka mashine za kukausha huu Mwani ili kusudi twende katika hatua inayofuata sasa ya kuongeza thamani kutengeneza sabuni, shampoos, bidhaa za chakula kwa ajili ya kuongeza hii thamani. Kama haitoshi, mbele zaidi tunataka tuanze kufanya extraction.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ngoja ngoja kwa sababu muda wa kujibu swali ni mfupi, anataka kujua mpango wa elimu kwa hao wakulima wa Mwani.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, shukrani sana. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi elimu tayari ilishatolewa na tunaendelea kutoa. Kwa hivyo, tutaendelea na mpango wa utoaji wa elimu katika vikundi vyote tunawaunganisha wakulima wa Mwani ili kuweza kuwa rahisi kwa kazi yetu ya utoaji wa elimu katika Mwambao mzima wa Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kuwa utaratibu wa kutoa msamaha kwa wazee umekuwa na mlolongo mrefu, lakini wazee hao wanakatishwa tamaa wanapopata hizo huduma.

Je, ni ipi kauli ya Serikali ya kupunguza mlolongo huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, toka Bunge hili kuanza tumekuwa tumesikia sana hizi kauli za kusema kwamba inakuja Bima ya Afya kwa Wote.

Je, ni nili hasa Serikali italeta Muswada wa Bima ya Bure kwa Wote? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja la kwanza; suala la ukiritimba kwenye msamaha kwa wazee na kuwahudumia wazee. Kwanza nitumie fursa hii kutoa agizo kwa Waganga wote Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya kwamba suala la tiba kwa wazee siyo tu kwamba ni bure lakini vilevile wanatakiwa wawe na dirisha lao. Kwa hiyo, hatutegemei tena kusikia haya malalamiko ya kwamba wazee wanapata mlolongo mrefu wa kupata tiba. Lakini Waganga Wakuu wa Wilaya wahakikishe vilevile wazee wamepata vile vitambulisho vyao.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwamba ni lini sasa Muswada huu utakamilika, Mheshimiwa Mbunge hili nisije nikalidanganya Bunge ninachoomba tutalishughulikia na mapema sana tunaweza tukaja kukuambia ni nini kitakachofanyika kabla Bunge hili halijaisha. Lakini kwa sasa ukinipa tarehe specific inaihusu organ mbalimbali za Serikali ili hilo liweze kuja hapa Bungeni, naomba nilifuatilie kwa uhakika zaidi. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bidhaa ambazo tayari za mifugo hususan ng’ombe pamoja na mbuzi kwa Zanzibar ni adimu sana, lakini pia bei yake inakuwa ni ghali sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba kufuta, lakini pia kupunguza kodi zote zile ambazo zinakuwa-charged pale bandarini kwa upande wa Tanga pamoja na Kitumbwi, bandari ya Tanga ili sasa kumpunguzia Mtanzania wa Zanzibar gharama nafuu bidhaa ile ya ng’ombe kama wa Bara?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; je, ni lini hasa Mheshimiwa Waziri utapanga safari ya kwenda bandarini kwenda kushuhudia namna Watanzania wanavyolazimishwa kulipa kodi maeneo ya bandarini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juma Usonge Hamad kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la usafirishaji wa nyama za mbuzi, ng’ombe na wanyama wengine ni kweli kwamba kupeleka Zanzibar ni nyama adimu hazipatikani sana, lazima tunavusha kutoka bara kwenda kule. Lakini suala la ufuataji wa kodi na tozo naomba hili tulichukue tulifanyie mchakato kwa sababu ni suala la kisheria.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu kwenda kutembelea ili kuona hali halisi naomba niambatane mimi na yeye mara tu Bunge hili litakapomalizika tuende tukatembelee katika sehemu husika. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichokuwepo pale Mchangani kwenye Jimbo langu la Chaani ambacho kwa takribani 80% kimeshatengenezwa na wawekezaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana kwa ujenzi wa kituo ambacho kimefika 80% na ninamhakikishia Serikali kwa kazi hiyo nzuri iliyofanywa na wananchi, 20% iliyobaki tutamalizia katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Swali langu ni kwamba, je, ni lini mtaweka commitment ya kwenda kwenye Kijiji cha Kandwi ili kujionea hasa mazingira ambayo wananchi wangu wa Kandwi wanakosa huduma ya mawasiliano ukilinganisha na maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Juma kwa ufuatiliaji mzuri, lakini naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tayari timu yetu imefika kwenye Jimbo lake eneo hili la Kandwi na tayari wameweza kuona changamoto ambayo ipo, hasa ni miembe mingi ambayo ipo katika lile eneo. Hata hivyo, kama Wizara, tayari tunafanyia kazi na kuhakikisha kwamba mapema iwezekanavyo tunakuja kuhakikisha maeneo haya ya Kandwi yanapata mawasiliano ya uhakika Mheshimiwa Juma.