Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Anyigulile Jumbe (18 total)

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ALLY A. MLAGHILA aliuliza: -

Suluhisho la tatizo la maji katika Wilaya ya Kyela ni kutumia chanzo cha Ziwa Nyasa kama ilivyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.

Je, ni lini sasa mradi huo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la huduma ya maji linaloikabili Wilaya ya Kyela. Katika kuhakikisha wananchi wa Wilaya hiyo wanapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha, Serikali ina mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa muda mfupi Serikali imeendelea na ukarabati wa miradi ambapo baadhi ya miradi iliyokarabatiwa tayari inatoa huduma ya maji ukiwemo mradi wa maji wa Makwale Group ambao unahudumia vijiji viwili vya Ibale na Makwale, Mradi wa maji wa Matema unaohudumia kijiji cha Matema (kitongoji cha Ibungu) na Kijiji cha Ikombe (Kitongoji cha Lyulilo) na mradi wa maji wa Lubaga ulioharibika muda mrefu umekarabatiwa na wananchi wanapata maji kwenye vituo 15 vya kuchotea maji. Aidha, kupitia bajeti ya mwaka 2020/ 2021 Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa Mababu, Kisyosyo, Katumbasongwe, mradi wa Kapapa kwenda kijiji cha Mwaigoga na mradi wa Sinyanga Group.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za muda mrefu, Serikali imepanga kutumia Ziwa Nyasa kama chanzo cha kudumu cha kusambaza maji kwa wananchi waliopo Wilayani Kyela pamoja na maeneo ya jirani. Hadi sasa timu ya kitaifa ya wataalam imefanya upembuzi wa awali kwa kufika Kyela na kubaini eneo la kijiji cha Ikombe kilichopo katika mwambao wa Ziwa Nyasa kuwa linafaa kujengwa chanzo cha maji. Mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA Aliuliza:-

Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa zao la kokoa haujamnufaisha mkulima:-

Je, ni lini sasa mfumo huo utabadilishwa ili kukidhi lengo la ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ni utaratibu unaowezesha biashara kufanyika kwa kutumia bidhaa ambazo zinakuwa zimehifadhiwa katika ghala lililopewa leseni kwa mujibu wa sheria kifungu cha 5(a) cha sheria ya mwaka 2005 na marekebisho ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfumo huu, mmiliki wa bidhaa anapewa stakabadhi ambayo inathibitisha ubora, uzito, idadi ya vifungashio na umiliki mahsusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani kwa zao la kokoa umesaidia kuimarisha bei ya zao la kokoa kutoka wastani wa Sh.3,000 kwa kilo katika msimu wa 2017 hadi kufikia Sh.5,011 katika msimu wa 2019/ 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani umesaidia kuimarisha na kuweza kugundua bei halisi na hivyo kumpa mkulima bei nzuri za zao hilo. Pia mfumo huu umeimarisha upatikanaji wa takwimu za uzalishaji na umesaidia ukusanyaji wa ushuru halali kwa Halmashauri za Kyela, Rungwe na Busokelo unaotokana na zao la kokoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 7,532 ziliuzwa ambapo jumla ya Sh.33,697,643,289.75 zilipatikana na kulipwa kwa wakulima na Sh.1,033,098,535.20 zilipatikana ikiwa ni ushuru kwa Halmashauri zote tatu. Katika msimu 2019/2020 jumla ya tani 9,483 ziliuzwa na wakulima kupata jumla ya Sh.45.721 na Halmashauri kujipatia jumla ya shilingi bilioni 1.367. Hadi kufikia tarehe 21 Januari 2021, jumla ya kokoa zilizouzwa ni tani 7,000 na kiasi cha shilingi bilioni 33 zimelipwa kwa wakulima na Halmashauri ya Rungwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kusimamia ubora wa kokoa kupitia Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na hivyo ubora wa zao la kokoa umeongezeka kwa kuwa katika mfumo huu kokoa inaandaliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na matakwa ya walaji.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itaufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira?

(b) Je, ni lini baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira watalipwa stahiki zao baada ya mgodi huo kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, yenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, mgodi wa makaa ya Mawe wa Kiwira ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2013 kwa lengo la kuuendeleza. STAMICO kwa kushirikiana na TANESCO wanaendelea na mpango wa pamoja wa muda mrefu wa kuanzisha mradi wa kuzalisha umeme zaidi ya megawatt 200 utakaotumia makaa ya mawe yatakayozalishwa katika mgodi huo. Makubaliano ya ushirikiano baina ya STAMICO na TANESCO yako hatua za mwisho kabla ya kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha kusainiwa.

Mheshimiwa Spika, tayari timu ya wataalam wa STAMICO na TANESCO imetembelea eneo la mradi kwa lengo la kutambua mahitaji halisi ya uendelezaji wa mradi huo na STAMICO imeanza kufanya ukarabati wa miundombinu ya mgodi wa chini ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzalishaji mkubwa kwa ajili ya mahitaji ya mitambo ya kuzalisha umeme. Aidha, kutokana na ukubwa wa mradi, Mashirika haya yanaendelea na jitihada za kutafuta fedha na uwekezaji kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kuihusisha Serikali yenyewe kuona uwezekano wa kutengewa sehemu ya bajeti kwa ajili ya uwekezaji huo.

(b) Mheshimiwa Spika, kipindi ambacho mgodi unakabidhiwa kwa STAMICO kulikuwa na malimbikizo ya madeni yanayofikia shilingi bilioni 1.02 ikiwa ni stahiki na mapunjo ya wafanyakazi takriban 893 waliopunguzwa. Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na shirika tayari imehakiki deni hilo kwa mara nyingine mwezi Juni, 2019 na taratibu za ulipwaji wa madeni hayo zinaratibiwa na Hazina. Nakushukuru.
MHE. ALLY A. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Songwe, Kiwira, Mbaka na Lufilyo ili kuongeza uzalishaji wa mpunga na kukuza uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji pamoja na fursa zilizopo katika Bonde la Mto Songwe pamoja na mabonde ya Mito Kiwira, Mbaka na Lufilyo, Serikali ilitekeleza miradi mbalimbali katika mabonde hayo. Katika Wilaya ya Kyela, kupitia Mpango wa Kilimo awamu ya kwanza (ASDP I), Serikali ilijenga Maghala mawili ya kuhifadhia mpunga katika skimu za Makwale na Ngana. Aidha, wakulima walipata mafunzo ya uendeshaji wa skimu, kilimo chenye tija na masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imekamilisha ujenzi wa Skimu ya Mbaka iliyogharimu Sh.358,877,336.48. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na Uchimbaji wa mfereji mkuu mita 1,900; Ujenzi wa tuta la bwawa (formation of embarkment) urefu wa mita 450 na usakafiaji wa mfereji mkuu kwa zege mita 1,355.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina Mpango wa kuendeleza hekta 3,005 za umwagiliaji katika Bonde la Mto Songwe kwa ubia baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Mto Songwe. Aidha, Serikali itaendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuendelea na uendelezaji wa mabonde hayo pamoja na mabonde mengine nchini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya kutoka Katumbasongwe hadi Ileje kilometa 90.7 itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katumbasongwe – Ileje ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 114.51 inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Songwe kupitia Wilaya ya Kyela na Wilaya ya Ileje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Katumbasongwe - Kasumulu – Ngana – Ileje ipo katika taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina taratibu za ujenzi zitaanza. Aidha, Serikali inaendelea kuihudumia barabara hii kwa kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati taratibu za ujenzi wa kiwango cha lami zikiendelea. Katika mwaka wa fedha huu wa 2021/ 22 barabara hii imetengewa Shilingi milioni 141.45 za matengenezo. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahuisha Sera ya Maji ili iendane na wakati kwa kukidhi mahitaji halisi kwani kwa sasa haiendani na viwango vya kimataifa na imepitwa na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Maji ndiyo mwongozo unaotumika katika kutekeleza jukumu la Serikali la kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Lengo la Sera ya Maji ya mwaka 2002, ilikuwa ni kuweka mfumo madhubuti na endelevu wa kuendeleza na kusimamia kikamilifu rasilimali za maji. Kupitia Sera hii, umekuwepo ushirikishwaji wa walengwa wa huduma ya maji katika hatua zote za utekelezaji, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, Serikali ilianza utaratibu wa kuhuisha Sera ya Maji hiyo ambayo imetekelezwa kwa takribani miaka 19 ili iweze kukidhi mahitaji ya Mipango iliyopo ambayo ni; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Awamu ya Tatu 2021 – 2026; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2015 – 2030; na Mageuzi ya Viwanda Awamu Nne (Fourth Industrial Revolution).

Mheshimiwa Spika, matarajio ni kukamilisha hatua zote ifikapo mwezi Juni, 2022 na Sera mpya ya Maji ianze kutumika ikianzia mahitaji halisi na kufikia malengo ya Uchumi wa Kati na Maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba maji yote yaliyopo ardhini yanabaki salama kwa kuwa tone moja la oil (vilainishi) huharibu lita 600 za maji yaliyoko ardhini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghali, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mMwaka 2009 na Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 kwa pamoja zinasisitiza uhifadhi, utunzaji na usimamizi wa vyanzo vya maji. Maji chini ya ardhi ni rasilimali ambayo inalindwa dhidi ya uchafuzi wa aina zote hii ni pamoja na oil. Hii ni kutokana na kuwa maji chini ya ardhi yakishaharibiwa ubora wake ni vigumu na ni gharama kubwa kuyasafisha ili yaweze kutumika kwa shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi za Maji za Mabonde inaendelea na jukumu la kutambua vyanzo vya maji juu ya ardhi na chini ya ardhi, kuweka mipaka na kutangaza katika Gazeti la Serikali ili yalindwe kisheria. Hivyo, maeneo tengefu ambayo yametangazwa ni Saba (7) ambapo Sita (6) ambayo yalitangazwa mwaka 2016 yapo Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa maeneo ya Chokaa, Kidole, Kiswaga, Matundasi A, Matundasi B na Mkola katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya na eneo moja Makutupora Mkoani Dodoma katika Bonde la Wami-Ruvu lilitangazwa mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, vilevile, maeneo Hamsini na Nne (54) katika Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (16), Ziwa Tanganyika (3), Pangani (7), Wami/Ruvu (5) Ruvuma na Pwani ya Kusini (13), Ziwa Nyasa (8) na Ziwa Victoria (1), Bonde la Kati (1) yamewekewa mipaka ili yatangazwe mwaka huu 2022.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utekelezaji wa Mipango ya Uhifadhi wa Vyanzo vya maji, Wizara ya Maji inatekeleza kazi ya kuainisha miamba yenye maji (Aquifer Mapping) katika Mabonde manne ambayo ni Bonde la Kati, Pangani, Wami/Ruvu na Rufiji.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kutathmini maeneo yenye maji chini ya ardhi imekamilika na hatua inayofuata ni kuchimba visima ili kupata takwimu za wingi na ubora wa maji katika maeneo hayo. Baada ya hatua hii, itaandaliwa ramani ili kutangaza maeneo hayo katika Gazeti la Serikali ili yalindwe kisheria na yaweze kutumika kulingana na mahitaji ya shughuli za maendeleo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati wa kukarabati barabara zilizo katika hali mbaya Wilayani Kyela kwani bajeti ya TARURA haitoshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kunusuru barabara ambazo zipo katika hali mbaya sana Wilayani Kyela, Serikali imeweka mikakati ifuatayo: -

(i) Kuzipandisha hadhi barabara za udongo kwenda changarawe (Gravel standard);

(ii) Kuzipandisha hadhi barabara za changarawe kuwa barabara za lami;

(iii) Kuendelea kuongeza fedha kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara, mfano, bajeti ya TARURA Kyela kwa mwaka 2020/2021 ilikuwa Sh.611,136,079.47; mwaka 2021/2022 bajeti ya Kyela ilikuwa ni Sh.2,436,996,341.18; na

(iv) Kuendelea kutoa fedha za dharura kunusuru barabara zilizoathiriwa na mvua, mfano, katika mwaka 2021/2022 zimepelekwa milioni 901.52.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazopelekwa kwa maelekezo maalum ni kwa ajili ya kutatua changamoto za muda mfupi za barababara zilizoathiriwa na mvua ili ziweze kupitika kwa wakati huo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, ni lini Barabara inayounganisha Wilaya ya Kyela na Ludewa kupitia Matema, Ikombe mpaka Liuli itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyingulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara inayounganisha Wilaya ya Kyela na Ludewa yenye urefu wa km 156 inapita kwenye safu ya milima ya Livingistone yenye miteremko mikali na miamba kubwa ya mawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufungua barabara hii kwa awamu kwa kufyeka misutu na kupasua miamba. Azma ya Serikali ni kuifungua barabara yote kuanzia Lupingu (Ludewa/ - Lumbila-Matema (Kyela).
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: -

Je, ni lini umeme wa REA utafika katika Kijiji cha Ikombe – Kyela?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe kitapata huduma ya umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotekelezwa na Mkandarasi M/s ETDCO Ltd. Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Ikombe kutoka Kijiji cha Lyulilo inatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2023 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ambayo ujenzi wake umesimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela inatekeleza ujenzi wa jengo la ghorofa la kutoa huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya wilaya. Utekelezaji wa mradi ulianza Septemba, 2019 chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama ya shilingi bilioni 3.81. Aidha, hadi kufikia Aprili, 2023 Serikali imeshatoa shilingi bilioni 2.75 na ujenzi umefikia asilimia 72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi, na Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Ibanda hadi Itungi Port (kilometa 25) utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira/Itungi Port yenye urefu wa kilometa 32 ulisainiwa rasmi mnamo tarehe 27 Desemba, 2022 na kupewa kibali cha kuanza ujenzi mnamo tarehe 31 Machi, 2023. Kwa sasa Mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na ujenzi wa Kambi za Mkandarasi na Msimamizi wa mradi ikiwa ni pamoja na maandalizi mengine kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, uchimbaji wa madini kando ya mito na maziwa ni chanzo cha upungufu wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kuwa uchimbaji wa madini umegawanyika katika aina kuu mbili, uchimbaji juu ya ardhi na ule wa chini ya ardhi (surface and underground mining) na unafuata Sheria ya Madini, Sura 123 ambayo hairuhusu uchimbaji wa madini katika vyanzo vya mito na maziwa. Endapo shughuli za uchimbaji zitafanyika kando ya mito au maziwa, zitafanyika umbali wa mita 60 kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004.

Mheshimiwa Spika, aidha, kabla ya shughuli za uchimbaji wa madini kufanyika katika eneo husika tathmini ya mazingira hufanyika na kutathmini athari za kimazingira ikiwemo viumbe hai pamoja na vyanzo vya maji. Hivyo, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kwa uchimbaji wa madini na upungufu wa samaki katika mito na maziwa. Ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA aliuliza: -

Je, lini Serikali itahakikisha mfumo wa uuzaji wa zao la Kakao unaomnufaisha mkulima badala ya wafanyabiashara wachache?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kakao huuzwa kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani chini ya utaratibu wa minada inayoratibiwa na vyama vya ushirika. Mfumo huo ulianza kutumika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo bei ya kakao imeendelea kuimarika kulingana na mahitaji ya soko. Wastani wa bei ya kakao kwa kilo kuanzia msimu wa 2018/2019 ilikuwa shilingi 4,611; 2019/2020 ilikuwa shilingi 5,034, mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa shilingi 4,818, mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa shilingi 4,711 na hadi kufikia tarehe 23 Oktoba msimu wa mwaka wa fedha 2023/2024 wastani wa bei ya kakao kwa kilo ni shilingi 8,079.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya uuzaji wa mazao nchini ili kuongeza ushindani na kumnufaisha mkulima.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Umeme (substation) utaanza Kyela?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikari kupitia TANESCO inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa (Gridi Imara). Maandalizi yanaendelea ikiwemo upembuzi yakinifu na tathmini ya athari ya mazingira kwa ajili ya kupata gharama halisi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Wilayani Kyela. Kazi hizi za maandalizi zinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2024/2025 na utekelezaji wa mradi huo utaanza mara baada ya kupatikana kwa fedha.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Madaraja ya Bujonde na Ilondo Mwaya - Kyela utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ujenzi wa Daraja la Bujonde linalounganisha Kata ya Kajunjumele na Bujonde. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imefikia 85% na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Daraja la Ilondo - Mwaya, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kulijenga daraja hili, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-

Je, vikwazo gani vinasababisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela usipandishwe hadhi kuwa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji na umuhimu wa kuanzisha maeneo ya kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, uanzishaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287 na (Mamlaka za Miji), Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela ilianzishwa mwaka 2008. Serikali itakapoanza utekelezaji wa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala itaifanyia tathmini mamlaka hiyo na kuendelea na hatua za kuipandisha hadhi ikiwa itakidhi vigezo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-

Je, mchakato wa kuwalipa waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwira Coal Mine umefikia hatua gani?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, deni la Wafanyakazi wa Kiwira lilitokana na malalamiko ya mapunjo ya mafao kutoka kwa waliokuwa wafanyakazi wa mgodi huo kabla ya ubinafsishaji. Baada ya Chama cha Wafanyakazi Mgodini (TAMICO) kuwasilisha malalamiko ya mapunjo hayo Serikalini, Serikali ilifanya Ukaguzi Maalum kupitia kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba, 2008 na baadaye Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (Internal Audit General) alihakiki madeni hayo, Agosti, 2021.

Uhakiki wa madeni hayo ulibaini madai ya wafanyakazi yalikuwa ni shilingi 1,240,000,000 kwa wafanyakazi 893; na madeni ya wazabuni, wakiwemo watoa huduma ya ulinzi, yalikuwa ni shilingi milioni 496; na kufanya deni lote kuwa jumla ya shilingi 1,520,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uhakiki huo kukamilika, Serikali ililitambua deni hilo na kulipeleka Hazina kwa ajili ya hatua za kuweza kulipwa. Ahsante sana.