Supplementary Questions from Hon. Ally Anyigulile Jumbe (44 total)
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani umewafanya wananchi na wakulima wa kokoa wasipate pesa papo kwa papo kama ambavyo Serikali leo imejibu; na kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni tofauti kabisa na uhalisia ulioko kule field, je, anachukua hatua gani kwa watu ambao wametoa taarifa ambazo sio sahihi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa zao la kokoa linalimwa na watu kwenye nyumba/kaya zao na siyo mashamba makubwa na wanatumia muda mwingi kukusanya hizo kokoa kidogo kidogo na pesa zinazolipwa zinachukua muda mrefu na kwamba makampuni yanayonunua yanaanza kwanza kukubaliana wao kwa wao pamoja na makato makubwa, je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti haya matatizo yaliyopo kwa wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anaposema taarifa tulizotoa sio sahihi; taarifa tulizotoa ni sahihi, wakulima wamelipwa kutokana na takwimu tulizonazo na uthibitisho tulionao. Kwa hiyo, kama ana kesi maalum ya mkulima ama wakulima ambao hawajalipwa atuletee hiyo kesi na tutaishughulikia kwa wakati na inavyostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kupitia Bunge lako Wabunge wanapoinuka na kusema kwamba, kuna mkulima X hajalipwa na sisi Wizara tunapoomba kwamba, tuleteeni uthibitisho, tunaomba mtuletee uthibitisho, mjadala huu usiishie humu ndani. Mtuletee uthibitisho, ili tuweze ku- resolve tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, taarifa tulizotoa ni sahihi. Hoja iliyoko ya kwamba, mkulima anapovuna, anapokausha, anapopeleka kwenye chama cha msingi mpaka inapoenda kwenye chama kikuu ni vizuri tukaelewa kwamba, cocoa inakusanywa kidogokidogo; mkulima atavuna kilo moja, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa atapeleka kwenye chama cha msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna hoja kwamba, tujadiliane kupunguza muda wa kutoka kwenye chama cha msingi kwenda kwenye mnada, lakini hatuwezi kurudisha mfumo ambao ni maarufu kama njemke ambao wakulima walikuwa wanafuatwa majumbani na wanakusanyiwa cocoa yao na wanapewa bei ndogo na walanguzi hao ndio wanapeleka kwenye mnada, hatutaruhusu huo mfumo. Kama kuna changamoto kwenye mfumo wa malipo, tuujadili huo mfumo wa malipo na kama Waheshimiwa wana maoni watuletee, lakini Wizara sasa hivi tunatengeneza utaratibu wa kuondoa mfumo wa kuhifadhi mazao ya cocoa kwenye maghala binafsi na yatatumika maghala ya Serikali. Tutaanza pia kuuzia katika AMCOS, badala ya kuleta kwenye chama kikuu cha ushirika, ili tuweze kupunguza time kati ya mnada na malipo ya mkulima. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Kyela jengo la mama na mtoto liliungua. Je, ni lini Serikali sasa itamalizia pesa zilizobaki kwa ajili ya jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Kyela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ni moja ya hospitali ambazo nazifahamu sana kwa sababu nimekuwa mganga mkuu wa Kyela kwa zaidi ya miaka tis ana nimekuwa sehemu ya uendelezaji wa miundombinu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Ninafahamu kwamba ni kweli wodi ilipata ajali ya moto na Serikali imesha peleka fedha na kazi za ukarabati wa wodi ile zinaendela.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie kwamba katika Mpango ujao tumetenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha ukarabati wa wodi ile iliyopata ajali ya moto ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba jambo hilo linafanyiwa kazi na mara fedha zitakapopatikana basi ukamilishaji wa wodi ile utafanyika ili tuendelee kutoa huduma kama ambavyo tunatarajia.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; Serikali kama kawaida imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kwenye elimu. Sasa hivi imetokea wanafunzi wanaotoka kidato cha nne wanachaguliwa moja kwa moja kwenda kwenye vyuo.
Sasa nilitaka kuuliza na wengine hawana uwezo kabisa na wazazi wao wameshindwa kuwalipia na utakuta ana division one au two. Sasa nilitaka kuuliza je, Serikali inawasaidiaje hawa vijana ambao wanashindwa uwezo wa kwenda huko vyuoni kwa ajili ya kuwasaidia wafike huko vyuoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jumbe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jumbe anazungumza kwamba wapo wanafunzi ambao wanafaulu lakini nafasi za kujiunga kwenye elimu ya juu zimekuwa ni changamoto na suala kubwa hapa ni kuweza kufanya upanuzi. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jumbe na Wabunge wote kwamba tumesaini sasa mkopo kutoka Benki ya Dunia katika mradi wetu wa HIT ambao zaidi ya dola za Kimarekani milioni 425,000 ambazo zinakwenda kufanya upanuzi mkubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu. Tutakapofanya ukarabati huu tunaamini tutaongeza nafasi za udahili na kuondoa changamoto hii ya wanafunzi wengi ambao wamefaulu vizuri lakini kuachwa kwenye vyuo vyetu. Nafasi hizo zitakapoongezeka tunaamini wanafunzi hawa wote ambao watakaofaulu wataweza kupata nafasi ya kwenda kuingia katika vyuo vyetu, asante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Leo ningekuwa CAG kwa majibu haya ningetoa hati hafifu. Haiwezekani leo tunazungumza mambo ya 2013 wakati aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Mizengo Pinda mwaka tarehe 8 Januari, 2015 alisema kwamba sasa wataanza utaratibu wa kupeleka mgodi huu TANESCO na kupeleka kwa STAMICO, lakini kumekuwa na ahadi hizi nyingi zikiendelea. Wananchi wa Wilaya ya Kyela, Wilaya ya Rungwe na Ileje wanachotaka ni kujua tarehe mahsusi ambayo suala hili linaenda kutekelezeka, la kuanza mgodi hiyo ni. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na matamko mengi ya malipo haya. Tarehe 29 Novemba, 2018 walisema STAMICO sasa imesha-save hela ya Serikali, lakini tarehe 12 Septemba aliyekuwa Naibu Waziri Mheshimiwa Nyongo alisema TRA wanawatafuta hawa TAN Power ambao walisema…
SPIKA: Sasa swali!
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ndiyo naomba nipate tarehe ya kulipwa ili na mimi nikienda Jimboni nikawaambie wananchi kwamba Serikali sasa inalipa pesa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba jambo hili limekuwa ni la muda mrefu kama ambavyo tarehe ya kukabidhiwa mgodi kwenda Serikalini imekuwa ya mwaka 2013, lakini pia tujue kwamba uwekezaji katika mgodi ni uwekezaji unaohitaji fedha. Katika kipindi hiki ni kweli kwamba pia Shirika letu la STAMICO limekuwa likipitia maboresho makubwa ya kulipa uwezo wa kuendelea kufanya shughuli zake. Kwa hiyo, ahadi hizi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu, tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa jinsi ambavyo shirika limeboreshwa na kwa jinsi ambavyo Serikali imejitahidi kuwa inalipa mapunjo hasa ya muda mrefu, hatimaye tumewaelekeza Shirika letu la STAMICO pamoja na TANESCO kwamba hata sisi hatuko tayari kuendelea kuchukua fedheha ya kuambiwa tuna hati chafu, badala yake wafanye jitihada zinazowezekana ili waweze kupata mtaji na hatimaye mgodi wa Kyela uweze kufunguliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mustakabali huo, naendelea kuwaagiza STAMICO pamoja na TANESCO kwamba, wakatafute fedha na ndivyo tulivyoongea kwamba sasa ifikie mahali watafute fedha, kama ni kutenga bajeti, kama ni kwa ushirika na partners wafanye hivyo ili hatimaye jambo hili liweze kufikia mwisho. Nakushukuru sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya dawa yanayojitokeza katika zahanati zetu ni sawa na yanayojitokeza katika Zahanati za Ipinda, Kyela na hata pale mijini. Ni mpaka lini tutasubiri tatizo hili liishe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha; kwanza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba lakini pili, imeendelea kuboresha sana upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vyetu. Ni kweli pamoja na maboresho haya bado kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa katika baadhi ya vituo na halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ambayo Serikali tumeyatoa, kwanza ni kuhakikisha watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanatumia vizuri fedha zitokanazo na uchangiaji wa huduma za afya kwa maana ya cost sharing. Tumejifunza kwamba baadhi ya halmashauri hazitumii vizuri fedha za cost sharing na tumewapa maelekezo kuhakikisha angalau asilimia 50 hadi 60 ya fedha za uchangiaji zinakwenda kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika swali la msingi, Serikali imeendelea kuongeza bajeti na itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kuongeza bajeti na kusimamia matumizi bora ya dawa katika vituo vyetu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kulifanyia kazi suala hilo. Pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu sisi ni Madiwani katika mabaraza yetu kufuatilia kwa karibu matumizi ya dawa katika vituo vyetu na kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha makusanyo yanakuwa bora zaidi.
MHE. ALLY A. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza naomba unipe nafasi pia nikushukuru wewe na Bunge hili tukufu kwa niaba ya Wananchi wa Kyela, pia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha kwamba baadhi ya wananchi wanapata msaada hasa wale walioathirika na mafuriko. Naomba niseme ahsante sana kwa Mama yetu Rais wetu ambaye ndiyo anayeongoza nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kama ifuatavyo; nikweli kuna Scheme ambazo zimetajwa za Ngana na Makwale, hizi skimu zimechukuwa tumito tudogo na tuchache sana ambayo tuna maji machache.
Sasa naomba niulize Serikali je, wanampango gani wa kutumia Mito ya Mbaka, Rufirio na Kiwila, mbali na Songwe ambayo ina maji mengi na ya msimu wote ili kujenga mabwawa makubwa kama ilivyofanyika utafiti na JICA miaka 1969 mpaka 1970 ili pia tupunguze mafuriko?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kyela tunaelekea kupata mwekezaji mzuri ambaye yuko tayari kuendeleza zaidi ya hekari elfu 10 akishirikiana na wananchi, lakini pia yuko tayari kujenga kiwanda kikubwa ambacho kita-process mpunga. Je, Serikali itakuwa tayari kushirikiana na mwekezaji huyo na sisi kwa Pamoja? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la mwekezaji, wala halihitaji majadiliano marefu, kama mwekezaji yupo na serious investors karibu Wizara ya Kilimo tukaenaye, tujadiliane naye tuone anahitaji msaada gani ili tuweze kusaidiana kuweza kufikia adhima ya kuwekeza na haya ni maelekezo ya Serikali wala hatutomsumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mito miwili aliyoitaja nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge; mfano maeneo yete yaliyokubwa na mafuriko sasa hivi kwa maana kuanzia Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya Kyela kwa maana ya Mkoa wa Mbeya na maeneo mengine, wataalamu wetu wa Wizara ya Kilimo wapo sasa hivi wameshakwenda kwa ajili ya kufanya tathimini na ingawa kuna stand ya JICA na zipo stand zingine ambazo zilifanywa katika baadhi ya maeneo kwenye nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wataalamu wa Wizara ya Kilimo wa Tume ya Umwagiliaji wana review stand zote zilizofanywa zamani ili kuangalia namna gani tunaweza kuziboresha na kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wengine wote kwamba maeneo yote potation yatafanyiwa kazi katika kipindi cha miaka hii mitano Inshallah!
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni barabara muhimu sana kwa ulinzi wa nchi yetu hasa kwa upande wa Tanzania na Malawi, pamoja na hayo kuna barabara muhimu sana ambayo kwa uchumi wa Kyela inafaa ijengwe mara moja.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini barabara ya Ibanda – Itungi – Poti itaanza kujengwa rasmi?
Swali la pili, wakati wa ujenzi wa barabara ya Kikusya – Matema kuna madaraja ya chuma yaliyokuwepo kwenye Mto Lufilyo Nambaka yalitolewa. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu ya uhaba wa madaraja na watu wanaotembea kilometa nyingi kufuata daraja lilipo, Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa madaraja yale yarudishwe Kyela ili yapelekwe sehemu zenye uhitaji za Ilondo, Ipande na sehemu za pale Ngorwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ibanda – Itungi – Poti imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami na naamimi tayari maandalizi yako ili iweze kutangazwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Kyela waiamini Serikali na hata akienda kwenye vitabu vyetu vya bajeti tumeonesha fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili haya madaraja ambayo anayasema. Madaraja haya ya chuma ni madaraja ambayo yanatumika kwa ajili ya kutumika pale panapotokea dharura. Kwa hiyo, madaraja anayoyasema ni kweli yalikuwepo lakini yalishapelekwa Katavi kwa ajili ya koa changamoto ambayo ilitokea. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya aende akafanye tathmini halafu tuone kama tutapata madaraja sehemu nyingine tuweze kurejesha mawasiliano ili kuwapunguzia adha wananchi ambao wanakwenda mbali kwa ajili ya kupata huduma ya usafiri. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Swali langu pia lililenga hili ambalo limeulizwa na Mbunge wa Rungwe, lakini pia naomba basi niulize kwamba, kwa kuwa imekuwa ni tabia ya wakandarasi kuruka baadhi ya vitongoji, halafu wanapeleka sehemu ya mbele na vitongoji vingine ambavyo vimekatiwa miti yake havipewi. Je Serikali inasemaje kuhusu hili?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlaghila kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na tumeshaongea naye kuhusu vijiji na vitongoji vilivyorukwa. Naomba pia nitumie nafasi kupitia Bunge lako Tukufu kuwakumbusha tu wakandarasi na tumetoa maelekezo haya mara kwa mara, kwamba mradi wa vijiji ambavyo tunakwenda kuutekeleza sasa ambao pia una miradi ya vitongoji na mitaa, hauzingatii na hautarajii kuruka kitongoji chochote.
Kwa hiyo niwakumbushe wakandarasi kutoruka sio kitongoji tu kutoruka kijiji, kitongoji, kaya na nyumba, haitegemei ni aina gani ya nyumba. Nashukuru.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa sera yetu sasa itachukua muda kuihuisha mpaka mwaka 2022; na kwa kuwa mpaka sasa kuna miradi mingi sana ya maji inaendelea na kwa kuwa pamoja na Sera hii kuna uhitaji wa maji wa kila mwananchi anahitaji kiasi gani kwa siku. Je, miradi inayofuata kwa sasa, Serikali imejipangaje kuhakikisha inakuwa endelevu?
Mheshimiwa Spika, la pili, mradi mmojawapo ambao umeathirika sana kwa Wilaya ya Kyela na hii Sera ya Maji ya watu 250 kuchota kwenye kituo kimoja ni Mradi wa Ngana group. Serikali imejipangaje sasa kuhakikisha mradi huu unafufuliwa na unakuwa katika viwango vya sasa ili kukidhi matarajio ya wana Kyela? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mlaghila, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa miradi ambayo inaendelea sasa hivi ni miradi endelevu na tayari tunajitahidi kuhakikisha kuona kwamba tunapata vifaa vya kufanya uchunguzi kabla ya kuingia kwenye miradi na tumshukuru kabisa kwa kipekee Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia fedha ambazo tumepewa tayari tumeagiza mitambo saba kwa ajili ya kuchunguza maeneo ambayo yatatuletea vyanzo endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa Mradi wa Ngana Group tayari umeshafufuliwa, wiki hii fedha zaidi ya shilingi milioni 500 tunaelekeza huko, ili kuona kwamba shughuli za awali zinaanza kutekelezwa. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa sana, lakini ameendelea kutoa hadithi zile zile. Sasa naomba tujue, ni lini mgodi huu utaanza kuzalisha ile mass production? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Bahati njema yeye mwenyewe katika kipindi kilichopita alitupa hati ya mashaka. Sasa hivi nataka nimwambie hati ile aiondoe kwa sababu tayari uzalishaji umeshaanza.
Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa, itakapofika mwezi Machi mwaka huu 2022 uzalishaji wa mass production wa tani 50,000 kwa mwezi utaanza mara moja.
Mheshimiwa Spika, vile vile underground mining kama nilivyokukwa nikijibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, tayari tumeshaijenga na kiberenge kinapita na uzalishaji unaanza. Ndani ya mwezi huu tunaanza kuzalisha kwenye mradi wa Kiwira tani 5,000.
Mheshimiwa Spika, Block E na yenyewe tumeanza kuanzisha open pit kwa ajili ya kuchimba. Mgodi huu ulisimama kwa muda mrefu toka mwaka 2008. Ni Awamu ya Sita ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa ili mgodi huu uanze na wateja wako wengi, tayari wanapita. Hata barabara ile Mheshimiwa Mbunge alikuwa analalamikia tayari tumeshaijenga. Sasa hivi tunakamilisha lile Daraja la Mwalisi watu waanze kupita pale; na wananchi wa maeneo yale wananufaika na uwepo wa mradi huu. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Mto Kiwira unapita maene mengi sana ya Wilaya ya Kyela ikiwemo Vijiji vya Lema, Mwalisi, mpaka Bujonde. Na kwa kuwa mto huo umelalamikiwa na wananchi wa maeneo hayo kuwa na uchafuzi mkubwa ambapo inafikia hatua mto unanuka na unakuwa na rangi ya damu.
Je, ni lini Serikali itaunda Tume Maalum kufanya utafiti wa nini kinasababisha maji hayo yawe machafu?
Mheshimiwa Spika, mbili, kwa kuwa wananchi wengi wa eneo hilo baada ya kukosa maji ya Ngana wanatumia kwa ajili ya kunywa na kuoga. Je, ni lini Serikali sasa itaanza ujenzi wa mradi wa Ngana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Ally amekuwa mfuatiliaji mzuri, amekuwa anakwenda zaidi ya uhitaji wa kupata maji yakiwa bombani lakini pia amekuwa akizingatia suala la usalama.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na bonde hili maji haya yanapochafuka, Mto Kiwira ni Mto ambao tunautumia kwa miradi mingi, naomba kutumia Bunge lako Tukufu kuagiza Bonde husika lifanye kazi kadri ambavyo inatakiwa kisheria. Vilevile Wizara tutaendelea kusimamia. Tayari Mheshimiwa Waziri amekuwa akitoa maagizo kadhaa kwa Mabonde yote kuhakikisha shughuli za maji kuwa salama yafanye usimamizi unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la lini ujenzi wa Ngana utaanza, kwa furaha kubwa ninapenda kukuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu tayari tumeshatangaza na hivi karibuni kabla yam waka huu wa fedha kuisha tutapata Mkandarasi na lazima kasi zije zianze kwa kasi kwa sababu tunafahamu umuhimu wake kulingana na jiografia ya eneo hilo. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ni lini Mkandarasi wa kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Makwale Wilayani Kyela kutumia Mto Rufilio ataanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, maelekezo ambayo tuliyatoa kwa Wakandarasi wote wale ambao walisaini mikataba wakati wa sherehe ya Nanenane pale Mbeya ni kwamba wanapaswa kuwa site kuanzia tarehe 15. Lakini tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa hoja yake mahsusi, basi tutahakikisha kwamba tunamharakisha Mkandarasi huyo aende kuanza kazi mapema kama ambavyo maelekezo yalitoka Wizarani.
MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni miezi mitatu sasa katika Wilaya ya Kyela, umeme haupatikani mchana. Je, ni lini wananchi wa Kyela watajisikia kwamba nao wana haki ya kupata umeme asubuhi na mchana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba baada ya hapa nikafuatilie ili kufahamu kwa nini Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake kwa miezi mitatu hakupatikani umeme mchana. Ninachofahamu ni kwamba kwa sababu ya upungufu wa umeme kumekuwa na kupungua kwa umeme kwenye baadhi ya maeneo, lakini jambo la kwamba miezi mitatu mchana wote hakuna, hilo ni jambo la kufuatilia, halafu tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kutatua changamoto hiyo.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Swali la kwanza; kwa kuwa Kyela ni sehemu ambayo ina mvua nyingi sana na huwa inakumbwa na mafuriko kwa kipindi kila mwaka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta fedha ambazo zimekosekana kwa muda mrefu kwa maendeleo ya barabara Wilayani Kyela?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa inajulikana barabara haziwezi kudumu kwenye mafuriko hasa hizi za changarawe na udongo. Je, Serikali imewahi kufanya utafiti wa kutafuta namna nyingine ya ujenzi wa barabara kwa mfano, kutumia enzymes katika kitengo chake cha utafiti hapo TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kupeleka fedha kwa ajili ya barabara na nimwondoe shaka tu. Bahati nzuri Serikali sasa hivi imeongeza bajeti yake na sisi tumekuwa tukitekeleza vya kutosha. Kwa hiyo, hilo aondoe shaka kabisa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu tafiti katika maeneo ambayo barabara hazidumu kutokana na mvua nyingi kama ilivyo Kyela, utafiti huo umefanyika na moja ya mipango yetu ni kuja na majibu ambayo yatasaidia barabara za maeneo hayo ziweze kupitika muda wote. Kwa hiyo, Serikali ipo kazini na inafanya hii kazi kwa umakini kabisa ili kuwasaidia wananchi wake.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwenye Mradi wa Songwe River Basin kuna package inayounganisha eneo la umwagiliaji la hekta zaidi ya 3,500 pale Kyela.
Je, Serikali imefikia wapi kuungana na Malawi kuanza kutekeleza mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema muuliza swali, Mheshimiwa Mbunge, amelitaja Bonde la Mto Songwe ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huu. Kazi ambayo Wizara inafanya hivi sasa ni kuhakikisha tunaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu wa haya mambonde yote, lengo letu kubwa ni kuwa na miradi mikubwa ambayo itahusisha miradi ambayo pia Mheshimiwa Mbunge ameitaja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mwaka huu wa fedha tayari tumeshawapa kazi washauri elekezi kwa ajili ya kuanza kazi hii na tunategemea kwamba mabonde yote yale 22 kuanzia Bonde la Ziwa Victoria, Malagarasi, Manonga, Wembele, Bonde la Ruvuma, Bonde la Rufiji, Bonde la Mto Songwe, Ifakara Idete, Kilombero, Mkomazi, haya yote yapo katika mpango na yatakwenda kukata kiu ya wakulima wa Tanzania. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza ni lini uwanja wa Mbeya utaanza kutumika usiku na mchana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea uwekaji wa taa kwa uwanja wa Mbeya ambao ni Songwe airport upo pengine kwenye asilimia 95 uwekaji wa taa, runway imeshakamilika zaidi ya mita 3000, uzio na sasa hivi tunakamilisha pia jengo la kisasa la abiria. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba uwanja huu utaanza kutumika, taa zimeshajengwa na utaanza kupokea ndege usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba uwanja huo unatumika kwa asilimia 100, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, je ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa barabara ya Katumba - Songwe – Kasumuru – Ngana - Ileje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara hiyo ilishatangazwa na tender zimeshafunguliwa, kwa hiyo muda wowote itaanza kujengwa baada ya kumpata mkandarasi, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe, tangu kuumbwa kwa dunia hii hawajawahi kuona gari. Zimebaki kilomita moja na nusu, ili barabara ifunguke mpaka Kijiji cha Ikombe, na mwezi wa kumi tuliambiwa kwamba mkandarasi yuko tayari, amepatikana.
Je, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba mkandarasi mpaka sasa hivi hayuko site?
Mheshimiwa Spika, mbili, barabara ya Ngamanga – Lusungo Matema inaenda moja kwa moja Ikombe, pale kuna daraja la bilioni 4.50 lakini eneo la Ngolwa halina daraja. Je, unaonaje sasa ni wakati sahihi wa kujenga daraja la Ngorwa, ili barabara ipitike kirahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya mheshimiwa Ally Anyingulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi ambao hawajaona gari nimuhakikishie kwamba barabara hiyo tunaifikisha kwenye hicho kijiji ili wananchi hao waweze kuiona gari katika maisha yao.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nichukue nafasi hii kumuagiza Meneja wa Mkoa wa Mbeya, ahakikishe kwamba mkandarasi anarudi site na anafanya kazi ambayo anatakiwa kuifanya. Lakini kuhusu daraja hili ambalo amelisema, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali italijenga hili daraja ili paweze kuwa na mawasiliano ambayo yamekosekana kwa sasa. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ETBICO ni Kampuni ambayo inasambaza umeme Mkoani Mbeya, wanaenda vijijini, kwa mfano Kijiji cha Bukunelo, Kijiji cha Ikama wanasema wamewasha umeme na taarifa Serikalini ni kwamba imewasha umeme, wakati huo wamewasha transformer zinaunguruma na umeme wenyewe kwa wananchi haujafika, je hiyo ni sahihi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Ally Jumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuwasha umeme kwa mwananchi ni kumwashia katika nyumba yake na eneo lake analohitaji umeme. Kwa hiyo, kama wanasema wamewasha kwenye transformer hiyo sio sawa na tutalifuatilia kuhakikisha kwamba umeme unawafikia wananchi kwa sababu ndio wanaouhitaji. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ikombe ni kijiji ambacho kiko pembezoni sana na ni kisiwa ambacho hakifikiwi kirahisi. Leo hii tunapouliza hili swali wananchi wa Ikombe wamewatuma viongozi wao waje washuhudie majibu haya ya Serikali, wako hapa leo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ETDCO ambao wanasambaza umeme wa REA walianza kazi hii Agosti, 2021 na wamefikia vijiji 21 tu na vijiji vilivyobaki ni 14. Na katika vijiji hivyo 14 bado hata nyaya hazijavutwa wala hakujatokea uwezekano wa kupeleka nguzo na mkataba unaisha ndani ya siku kumi zijazo, swali la kwanza: -
Je, sasa Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kushirikiana na TANESCO ili kwa Kyela vijiji hivyo viishe mapema?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni maajabu gani yatatokea kufanikisha ndani ya siku kumi mkataba huu uendelee ufike mpaka watakapofikisha hapo Juni pale Ikombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa spirit ya kutotaja kumuwakilisha Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya muda naomba niendelee.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu mawali ya nyongeza la Mheshimiwa Ally Anyigulile kwa ujumla wake kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna mikataba ambayo muda wake utaisha kabla kazi hazijakamilika, lakini nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata umeme. Na tunachokifanya ni kukabana na wakandarasi wote wanaopeleka miradi yetu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali kuhakikisha wanamaliza kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini sababu nyingine moja inayofanya kazi izidi muda wa mkataba wa awali ni kuongezeka kwa hizo kilometa mbili ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pesa ya nyongeza kwa ajili ya kuongeza scope. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Ally kwamba kama tulivyosema kabla ya mwezi Juni hicho kijiji kitakuwa kimepata umeme na wananchi wataweza kuutumia katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, na kwa mkandarasi ETDCO yupo zaidi ya asilimia 60 na vijiji 14 vilivyobaki vitakamilika katika huu muda ambao tumejipangia kwa spidi mpya ambayo tuko nayo kwa sasa. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa pesa nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa kivuko cha Mwaya – Kajunjumele; je, ni sababu gani zinafanya mpaka sasa hivi kisianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kati ya Mwaya- Kajunjumele tuna kivuko ambacho kilitoka Luhuhu kiko site na tunachosubiri sasa hivi ni kwamba maji yaweze kupungua ili tuweze kurekebisha rampu halafu baada ya hapo kivuko hicho kitaanza kutoa huduma kati ya Mwaya na Kajunjumele, ahsante.
MHE. ALILY A. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Barabara ya Uyole – Kasumulu ina zaidi ya miaka 35 sasa, muda ambao imekwishapita design age yake. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuanza kuiwekea hata layer ya juu badala ya kusubiri ibomoke yote?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa kufuatilia barabara hii na nimhakikishie tu kwamba kwa kuwa hapa Kasumulu ni lango muhimu la kwenda katika Nchi Jirani ya Malawi. Katika bajeti zetu za TANROADS kupitia Mkoa wa Mbeya tumetenga fedha kwa ajili ya kuboresha barabara hii iweze kupitia wakati wote, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia hospitali ambazo ni kielelezo na zipo mpakani ni Hospitali ya Kyela, lakini hospitali hii ni hospitali kongwe sana ambayo kwa sasa hivi haitamaniki na hata ukifanya usafi haioneshi kwamba ni hospitali ambapo watu wanaweza wakatibiwa na kupata faraja.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kuhakikisha majengo haya yanajengwa upya na yanakuwa mapya kwa ajili ya kuwa na manufaa kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ikama ya wafanyakazi walioko katika Wilaya ya Kyela imepungua sana na iko kiwango cha chini kukidhi mahitaji ya magonjwa mengi ambayo yako Kyela.
Je, Serikali haioni haja ya kuongeza wafanyakazi kwa kipindi hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mlaghila Jumbe; la kwanza la fedha kutengwa kwa jili ya ukarabati wa hospitali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kama nilivyokuwa nimeshasema kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imeshatenga fedha zaidi ya bilioni 2.75 ambazo zimekwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela ili kuhakikiusha kwamba inafanyiwa ukarabati; na katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo. Nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni adhma ya Serikali hii ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha inakarabati hospitali kongwe zote nchini, ikiwemo ya Kyela, na tutaendelea kutafuta fedha kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali la pili la ikama ya watumishi. Bunge lako tukufu hili ni mashahidi, Serikali imetangaza ajira zaidi ya 21,300 kwenye sekta ya elimu na sekta ya afya. Ajira hizi zitakapokamilika tutahakikisha vilevile Hospitali ya Kyela inapata wataalamu ambao wanatakiwa kuhudumia Watanzania waliopo Kyela pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ziwa Nyasa ni karibu wiki moja limechafuka na akina mama wajawazito wameshindwa kabisa kuvuka kwenda kupata huduma pale Matema. Je, Waziri yuko tayari sasa kufuatana na mimi kuangalia jinsi gani barabara ya kutoka Matema kwenda Ikombe inavyosuasua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza tutoe pole kwa changamoto ambayo inatokea katika Jimbo la Kyela. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba yupo Mkandarasi ambaye alikuwa anasuasua na tayari tumeshamuagiza Meneja wa Mkoa wa Mbeya amsimamie ili kwanza aweze kukakamilisha eneo ambalo lilikuwa lina changamoto. Mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa tukubaliane tuende tukatembelee ili kuhakikisha kwamba kazi ambayo inafanyika iweze kukamilika. Nipo tayari kufuatana naye.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaiondoa Wilaya ya Kyela kwenye adha ya mawasiliano yake kuingiliwa na Mtandao wa Malawi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunafahamu kwamba mawasiliano ni uchumi, mawasiliano ni usalama na mawasiliano ni huduma ya msingi ya kila Mtanzania. Sasa wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha tunaona ni busara kuwaacha kwanza wananchi wetu waishi katika mazingira ambayo wanaweza kuwasiliana. Pindi fedha zitakapopatikana, ndipo sasa tutakapoenda kuweka miundombinu yetu na kuhakikisha kwamba sasa mitandao ya nchi jirani tunaiondoa ili waweze kutumia mitandao ya nchi yetu, ili waweze kuchangia uchumi ndani ya Taifa letu na vilevile wawe na usalama ambao unajitosheleza katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ina mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba tunakuja na mradi maalum wa borders and special zone kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha ili Watanzania wawe na amani ndani ya nchi yao.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata za Busale, Ibanda na Itope zipo mpakani sana mwa Malawi, na siku zote unapopita kwenye kata hizo mawasiliano yanapokwa na Wamalawi. Hata juzi Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Josephine Keenja, ameshuhudia hoteli zote zilizopo mpakani zilivyokosa wateja kwa kukosa mawasiliano: Je, ni lini sasa Serikali itatuondoa kwenye utumwa huo wa kubaki kama Wamalawi wakati sisi ni Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuwa na Mradi wa Tanzania ya Kidigitali, tulikuwa na mradi wa special zones and boarders. Mradi huu ulikuwa mahususi kwa maeneo ya mipakani, hasa kule ambapo kuna mwingiliano wa mawasiliano na nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba mawasiliano ni uchumi katika maeneo ya mpakani, tunafahamu mawasiliano ni usalama, lakini ni haki ya msingi ya kila Mtanzania kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano. Kwa vile Mheshimiwa Mbunge amesema, basi tutatuma timu yetu tukajiridhishe tena kuona ni maeneo yapi ambayo yamebaki kuwa na changamoto hizo ili tuweze kuchukua hatua, ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzii kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ujenzi wa barabara hii na kwamba sasa imeanza. Sasa, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali imejiridhisha na uwezo wa Mkandarasi huyu mpaka kumpata maana inachoonekana sasa ni kwamba mkandarasi anasuasua sana tangu alipopewa ile site?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wote ambao wamepitiwa na barabara hiyo tangu miaka mitano iliyopita waliambiwa wasiendeleze maeneo yao na mpaka sasa hivi hawajalipwa maeneo yao na bado hawajapewa hata kiasi chochote au karatasi lolote linaloonesha kwamba wanaweza kulipwa kiasi fulani. Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi wanaopitiwa na barabara hii pesa zao za fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kyela kwamba Mkandarasi ambaye amepewa kazi hii ana uwezo wa kutosha ndiyo maana amepewa kazi hiyo. Vile vile, ni mkandarasi ambaye alifanyiwa due diligence kwa maana ya kuangalia uwezo wake wa kifedha kwa maana ya mtaji lakini pia na vifaa vya kufanyia kazi hiyo. Kwa hiyo, tunaamini uwezo huo anao na ataijenga hiyo Barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la fidia. Ni kweli wananchi hawa bado hawajalipwa fidia, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kyela kwamba uthamini ulishakamilika na majedwali ya malipo yalishakamilishwa na tayari Wizara ilishapeleka uthamini kwa maana ya gharama watakazolipwa ambayo ni bilioni 1.734 kwa wananchi wanaostahili kulipwa, hususani wale ambao watapisha ujenzi huu na watalipwa kwa mujibu wa Sheria yetu ambayo tunaituma kwa watu wanaopisha ujenzi wa barabara, ahsante.
MHE. ALLY. A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, mwaka 2018 Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga Barabara ya kutoka Mbambo – Ntaba – Ipinda; je, Serikali imefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema kwamba Kiongozi wa Taifa alishaahidi, atakubaliana nami kwamba barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu wa kina na sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kwamba kufika tarehe 30 Juni, wananchi wa Ikomba watakuwa wamefikishiwa umeme wa REA, leo ninavyoongea hata nguzo zilizokuwepo kule wameziondoa; je, Serikali haioni kwamba haiwatendei haki wananchi wa Ikombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nimuahidi Mheshimiwa Jumbe kwamba, Mradi wa REA III, Round II unatakiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2023. Yale maeneo ambayo bado hayajakamilika na nguzo pengine zimeenda zimepelekwa sehemu nyingine zitarudishwa zitapelekwa hapa, lakini nia ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwezi Disemba, 2023 kila kijiji kimepata umeme na wananchi waweze kupata huduma hiyo, kwa hiyo, ahadi hiyo tutaitekeleza kwa kadri ilivyotolewa.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Bonde la Mto Songwe lina eneo la kilometa za mraba 3,500 kwa ajili ya umwagiliaji.
Je, ni lini Serikali sasa itaanza kutekeleza mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa dam pale kwenye Bonde la Mto Songwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika bajeti yetu ambayo tumeiwasilisha jedwali la kwanza yako mabonde 23 ambayo tunakwenda kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake likiwemo Bonde la Mto Songwe. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya mipango ya Serikali na tumedhamiria mabonde yote kuweza kuyafikia. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini mkandarasi wa kujenga Mradi wa Ngana Group atapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ngana Group taratibu ziko mwishoni. Tunatarajia kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha, mkandarasi atapatikana na kazi ziweze kuendelea.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa leo tumeambiwa tarehe ya utekelezaji wa mradi huo na kwa kuwa kabla ya hapo tuliahidiwa kwamba mwezi wa Tatu mradi huu ungekuwa tayari.
Je, wananchi wa Vijiji hivyo kwenye Wilaya ya Rungwe wategemee kauli gani ya Serikali ya kuhakikisha hili jambo linakamilika kwa uweli baada ya miezi mitatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; Kijiji cha Ikombe Wilayani Kyela kilishafanyiwa uhakiki na kuwekea peg lakini mpaka sasa hivi hakuna dalili zozote za kupelekewa umeme wa REA: Je, ni lini Serikali itapeleka umeme huko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Ally Jumbe kwa niaba ya Mheshimiwa Mwantona, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza ni kweli kwamba tulitarajia kumaliza mradi huu mapema lakini kama mnavyofahamu kulitokea ongezeko na mabadiliko makubwa sana ya bei na hivyo hata baada ya ukamilishaji wa kuangalia upungufu uliokuwa umejitokeza, tumeingia katika negotiation ya kuhakikisha kwamba tunapata fedha halisi ya kuweza kuongeza ili tumalize mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaahidi wananchi wa maeneo hayo kwamba baada ya kukamilisha mchakato wa kukubaliana bei halisi ya ongezeko la vifaa, sasa tupo tayari kwenda kupeleka umeme katika maeneo hayo kwa kurekebisha yale maeneo ambayo yalikuwa yamebakia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili. Katika kijiji hicho ambacho kimesemwa na vijiji vingine vyote ambavyo vipo Tanzania bara kama tulivyosema, vitapelekewa umeme kufikia Desemba mwaka huu kama ahadi ya Mheshimiwa Rais kwenye Ilani ilivyotolewa.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tarehe 10 Agosti, 2021 TANESCO na STAMICO waliasaini makubaliano ya kuzalisha megawati 200 kutoka kwenye Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira; je, mpango huo umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Jumbe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mpango huu bado upo na tunautekeleza kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanyika Aprili, 2018 huko Tennessee Marekani, unaonesha kwamba sehemu zenye machimbo ya makaa ya mawe karibu na mito kuna upungufu wa viumbe wa majini kwa asilimia 53 wakiwemo samaki. Swali la kwanza; je, sisi Serikali yetu imefanya utafiti huo na kuja na majibu haya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi tunaanza kuchimba makaa ya mawe Kiwira Coal Mine na Mto Kiwira na Mto Songwe vimeathirika kwa namna hiyo. Je, ni hatua gani zinazochukuliwa kwa Serikali ili kusiendelee kupatikana kwa athari hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mlaghalila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa taarifa anayosema kwamba kuna tafiti za kidunia zinazothibitisha kwamba uchimbaji wa makaa ya mawe una uhusiano na kupungua kwa samaki katika maziwa na mito; nikiri kwamba sisi hatuna scenario kama hiyo katika Nchi yetu ya Tanzania kwa sababu hatuna uchimbaji katika maeneo ya karibu na mito ambayo ina samaki au maziwa ambayo kuna upungufu uliobainika kwa tafiti za kisayansi.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo la machimbo ya makaa ya mawe lililoko Kiwira na Kabulo tuna Mradi unaoitwa Kiwira-Kabulo Coal Project ambao uko chini ya taasisi yetu ya STAMICO. Katika eneo Kasumulu, Wilaya ya Kyela ilianzishwa site ndogo ya heka mbili kwa ajili ya kuwa selling point ya yale madini kutokana na shida ya barabara ya kutoka Kabulo kwenda Kiwira kuliko na kituo kikubwa cha makaa ya mawe ya STAMICO. Kwa sasa hivi, barabara hiyo ya kilomita saba ilishakamilika na utaratibu wa kuhamisha kile kituo umeshafanyika na kuna tani 1,200 za makaa ya mawe mpaka kufikia mwezi Agosti, 2022 yatakuwa yameondolewa yote, ila tahadhari zote zilichukuliwa.
Mheshimiwa Spika, kwanza; kulingana na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Kifungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto. Site iliyotengwa kule katika mradi huu wa makaa ya mawe kule Kasumulu upo mita 120; lakini kana kwamba hii haitoshi makingamaji ya kuchepusha maji yasielekee mtoni yamejengwa na kuna mashimo makubwa kama mvua itanyesha na maji yakatiririka yakaingia mle yakakaukia humo. Pia kana kwamba hiyo haitoshi, kulingana na Kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, sisi kama Wizara ya Madini tunazingatia sana suala la utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hiyo, Kifungu cha 107(2) cha Sheria ya Madini Na. 123, kinazingatia utunzaji wa mazingira kwamba baada ya ile site kuachiwa tutapenda kuirejesha na kuzungushia fence na kutumika kwa matumizi ya kufundisha wananchi wa eneo la Kyela na Ileje namna ya kutengeneza makaa mbadala ya makaa ya mawe yanaitwa Coal Breakage. Kwa hiyo, hakuna athari ya mazingira na sisi tupo makini. Ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali ndiyo wanaondesha mfumo huu kupitia vyama vya ushirika, na hapo awali kabla ya kuanza mfumo huu bei ya kakao ilikuwa ni shilingi 7,000 kwa kilo tukiuza kwenye kampuni za botanical; na sasa hivi mfumo huu umeingia wizi mkubwa sana ambao unaendelea mpaka sasa. Kwa sasa zao hili halimnufaishi mkulima wa Kyela mpaka Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa comrade Homera amekiri wazi kwamba mfumo huu unawanufaisha watu wachache na hela haionyeshi kwamba inaingia kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu una matatizo sana, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa nini Serikali inaendelea kung’ang’ania mfumo huu ambao haumnufaishi mkulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tarehe 7 mwezi wa nane, mwaka 2022 Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alikiri wazi kwamba mfumo huu utaondoka kwenye zao hili. Je, ni lini sasa Waziri ataenda kuwaambia wananchi wa Kyela kwamba sasa mfumo ambao utamnufaisha mkulima ni huu ambao na wao watakuwa wameujadili naye? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza namuondoa hofu Mheshimiwa Mbunge, na ndiyo maana mnaona katika matumizi ya huu mfumo tunavozungumza sasa bei ya zao la kakao kwa kilo imefika shilingi 8,000 kwa hiyo unaona kuna maendeleo makubwa. Bahati nzuri katika mfumo huu mkulima analipwa ndani ya masaa 48 baada ya mnada kuwa umekamilika; kwa hiyo utaona kuna manufaa mengi kwenye huu mfumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Kilimo kwa sababu tunaendelea kupitia hii mifumo na kuangalia kama kuna changamoto basi tunapokea sehemu ya maoni ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatoa na tutayapitia tuone kama kuna mahali kuna changamoto ili tuweze kuirekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kueleza kwamba, ni lini mfumo huu utaondoka nafikiri baada ya mapitio ya changamoto tujue kama kweli kuna changamoto lakini jukumu letu sisi ni kuboresha na kuhakikisha mfumo huu unawasaidia wakulima nchini, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazofanya kuhakikisha umeme unapatikana. Wananchi wa Kyela wamekuwa ni wavumilivu sana kwa muda mrefu, umeme pamoja na ratiba ya mgao wa umeme, lakini bado kuna hitilafu za umeme ambazo zinatokea mbeya na Rungwe zinawaathiri wananchi wale. Je, Serikali haioni sasa kwamba ni wakati muafaka kuachana na mlolongo mrefu huu wa upembuzi yakinifu na kuleta mambo mengine yanayoathiri uharakishaji wa ujenzi wa kituo hiki cha umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, miaka ya nyuma ya 1990, umeme Kyela ulikuwa unatoka pale Kiwira Coal Mine na wananchi wa Kyela walikuwa wanapata umeme bora kabisa, lakini sasa hivi umeme huo haufanyi kazi na haupo. Kwa kuwa tarehe 10 Agosti, 2021 TANESCO iliingia makubaliano na STAMICO ili wazalishe megawat 200 ambazo zingetokea Kyela moja kwa moja, je, Serikali haioni sasa kwamba ni wakati muafaka wa kuharakisha kuanza kwa mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kadhia wanayopata wananchi wa Jimbo lake la kukatika kwa umeme mara kwa mara. Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinaondoka, lakini hitimisho la muda mrefu ni ujenzi wa kile kituo cha kupoza umeme katika Wilaya ya Kyela. Kama nilivyosema, mradi huu ni sehemu ya mradi wa gridi imara ambapo katika kipindi hiki Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 470 kuhakikisha mradi ule unaweza kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusu kuharakisha na kuachana na mlolongo, hatua hizi zinazofanyika sasa za upembuzi yakinifu, kufanya tathmini ya maeneo ya wananchi ambayo yakichukuliwa watahitajika kufidiwa na mambo kama hayo, ni hatua muhimu sana ili mwisho wa siku tuweze kupata mradi ambao hautakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi kama tulivyosema mradi huu unatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jibu lake la swali la pili ni kweli kwamba pale kuna mradi wa makaa ya mawe unaokusudiwa kujengwa kati ya TANESCO na wenzetu wa STAMICO. Nafurahi kusema kwamba, mwezi uliopita wataalam wa TANESCO na STAMICO wamekaa na kukubaliana kuharakisha mchakato wa ujenzi wa mradi huu katika kupitia upembuzi yakinifu uliofanyika ili kuakisi mahitaji ya sasa. Takribani shilingi milioni 400 zimetengwa kwa ajili ya kuharakisha kazi hiyo. Nimuombe awe na subira tunauhitaji sana mradi huu.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wakati Serikali inaendelea na upembuzi yakinifu, je, ni mkakati gani unafanywa kwa barabara ambazo zinaunganisha madaraja hayo mawili, kati ya Kajunjumele – Mwaya – Lusungo na Matema?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Daraja la Bujonde pia lina kipande cha barabara cha Ibanda – Itungi Port, je, baada ya kumwondoa mkandarasi nini mkakati wa Serikali kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyojenga madaraja ambayo mara nyingi ndiyo kikwazo kikubwa cha kuunganisha eneo na eneo Serikali itazijenga hizo barabara ambazo zinaunganisha haya madaraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu baada ya kumwondoa mkandarasi, kwanza nimwagize Meneja wa Mkoa wa Mbeya kwamba kama kuna changamoto zozote ambazo zinaendelea sasa hivi ahakikishe kwamba anaweka utaratibu wa kuzikarabati hizo barabara wakati Serikali inakamilisha taratibu za kuweza kufanya tathmini na kuona namna ya kusimamisha au kusitisha mkataba na mkandarasi ambaye alikuwa amepewa barabara hii kwa kufuata taratibu zote za mkataba, ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, mamlaka hii ina zaidi ya miaka 16 na leo hapa tunapata majibu ambayo ni too general na hayaoneshi matumaini ya kwamba ni lini sasa mamlaka hii itapandishwa. Nina maswali mawili. Swali la kwanza; madiwani zaidi ya 14 hawana KAMAKA (Kamati za Maendeleo) wanaelea na kumeingia mgogoro wa maslahi ambapo Wenyeviti wa Vitongoji na Madiwani hawawezi kukaa pamoja kirahisi na kufanya maendeleo, je, Serikali inafikiria nini kwenye jambo kama hili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Halmashauri ya Wilaya ya Kyela inaendesha mabaraza mawili kwa wakati mmoja, Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo na Baraza la Halmashauri ya Madiwani pale Kyela. Je, Serikali haioni ni wakati sahihi kuzisaidia pesa halmashauri zilizo katika hali hiyo ili ziweze kuendesha hayo mabaraza mawili kwa wakati mmoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatambua uwepo wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela kwa kipindi cha takribani miaka 16. Kwa kipindi hicho chote mamlaka ile haijawahi kukidhi vigezo vya kuwa halmashauri ya mji ikiwemo idadi ya wananchi, ukubwa wa kijiografia wa eneo husika pamoja na vigezo vingine. Walishawahi kuleta maombi hayo, Serikali ilifanya tathmini na kuwapa maelekezo ya kwenda kufanya maboresho. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba tunahitaji kupata halmashauri ya mji lakini tunasubiri kwanza vigezo viweze kutimia. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, tunaelekeza Wenyeviti na Madiwani wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela na Baraza la Madiwani, waweze kufanya kazi kwa ushirikiano na ni kazi ya Mkurugenzi na Viongozi wote wa Serikali kuhakikisha kwamba wataalam hawa, watendaji hawa na viongozi hawa wa vijiji na kata wanafanya kazi kwa ushirikiano.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na Serikali kupeleka fedha za ziada kwa ajili ya kuendesha Baraza la Mamlaka Mji Mdogo na Baraza la Madiwani. Suala hilo linatokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Kwa hiyo, nisisitize kwamba Halmashauri ya Kyela kupitia mapato ya ndani waendelee kuhudumia pia Mamlaka ya Mji Mdogo mpaka pale mamlaka hiyo itakapopandishwa hadhi au itakapoondolewa kwenye orodha ya Mamlaka za Mji Mdogo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Chunya wanaishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo imefanyika mpaka sasa, lakini wana maswali.
Je, sasa hizi pesa ambazo zimetengwa ni kweli zitawahi ili zipelekwe na hospitali hiyo kuanza kufanya kazi kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hospitali mojawapo katika Mkoa wa Mbeya ambayo ni kongwe sana ni Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Je, ni lini ukarabati wa hospitali hiyo kwa viwango vya kimataifa utaanza kufanyiwa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya. Kama vile ambavyo tayari katika miaka ya nyuma Serikali ilikuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuboresha na kukamilisha miundobinu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya hivyo hivyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetenga fedha na fedha zitafika kwa wakati kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka 15 sasa tangu mchakato huu umeanza na katika mchakato huu kuna wananchi wengine mpaka sasa hivi wameshapoteza maisha. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuharakisha hili zoezi ili hawa wananchi walipwe fedha yao? Wananchi hawa wanatia huruma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Naishukuru sana Serikali kwa kuanzisha kiwanda bora kabisa pale STAMICO ambacho kwa sasa kitatoa makaa ya kupikia kwa kutumia makaa ya mawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha makaa ya mawe na makaa haya ya kupikia ambayo ni bora zaidi yanawafikia wananchi wa Rungwe, Kyela na Ileje? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ally kwa maswali yake mazuri. Ninakiri kwamba, kweli deni hili la wafanyakazi hawa limechukua muda mrefu. Pia sisi kama Wizara, hata kupitia ziara ya Kamati ambayo ilitutembelea miezi michache iliyopita, tulipewa jukumu la kulifuatilia Hazina. Namwahidi kwamba, baada ya kujibu maswali hapa niko tayari kuungana naye tuendelee kufuatilia deni hili ili liweze kulipwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, kuhusu makaa ya mawe ambayo yanachakatwa Kiwira kwa mtambo ambao uliwekwa na Serikali, namjulisha kwamba, kwanza mtambo huo umekamilika na tunavyoongea mzabuni yuko site kwa ajili ya commissioning na uzalishaji wa majaribio umeanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango uliowekwa na Serikali ili kusambaza makaa haya kupitia Shirika letu la STAMICO ni kwamba, wazabuni, wasambazaji (distributers), walikuwa wanatafutwa nchi nzima na mpaka sasa hivi wamepatikana wasambazaji 52. Pia nitumie fursa hii kuwaasa wananchi wa Kyela waunde vikundi, wapeleke maombi ya kuwa mawakala wa kusambaza makaa hayo ambayo yanaitwa Rafiki Briquettes ili waweze kutumia makaa hayo ambayo ni safi na salama na itanusuru misitu yetu na mazingira kuharibiwa na wakata mkaa. Maana yake ni kwamba haya makaa sasa ni mbadala wa kuharibu mazingira. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza tuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuajiri watumishi hasa wa kada ya afya na walimu.
Mheshimiwa Spika, shule nyingi za pembezoni katika Wilaya ya Chunya kwenye kata za Lualaje, Ifumbo, Mafyeko na Kambi Katoto zimekosa walimu pamoja na watumishi wa afya. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuhakikisha inafanya msawazisho ili walimu walioko mijini na walioko kule wafanane?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali itaandaa mpango maalum wa kufanya sensa ya kuhakikisha tunakuwa na takwimu za walimu na watumishi wa afya walio mijini na walio vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsate sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela kwa kazi nzuri na kubwa anayowafanyia wananchi wa Jimbo la Kyela. Nianze kwa kumpa uhakika kwamba, kwanza tunatambua kuna baadhi ya shule zilizoko pembezoni mwa miji au halmashauri zina upungufu mkubwa sana wa watumishi zikiwemo hizo za maeneo ya Kambi Katoto, Mafyeko na maeneo mengine ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshaweka mpango wa kuhakikisha maeneo yale ambayo yana upungufu mkubwa zaidi wa watumishi wanapelekwa na ndiyo maana kwenye mfumo wa ajira wa sasa, ni mfumo kwanza wa kieletroniki pia kila anayeomba ajira analazimika kuomba kwenye maeneo ambayo yameainishwa na ule mfumo automatically unaweka nafasi nyingi zaidi kwenye shule, halmashauri au mikoa ambayo ina upungufu mkubwa zaidi wa watumishi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalifanyia kazi ili tupunguze gap la watumishi katika shule hizo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na kufanya sensa ya walimu walioko mijini na vijijini. Tayari tulishafanya hivyo miaka miwili iliyopita na tunafahamu uwiano wa walimu vijijini na watumishi wa afya vijijini na mijini. Mpango uliopo sasa kwanza ni kuhakikisha kwamba kipaumbele cha ajira kinakwenda kwenye halmashauri za vijijini zaidi. Pili, tunazuia uhamisho kutoka vijijini kwenda mijini kwenye majiji, manispaa ili kuhakikisha kwamba tuna-balance uwepo wa watumishi katika vijiji na katika miji, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera sasa aulize swali lake.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Aprili, 2019, Mheshimiwa Rais aliagiza barabara ya Ipanda – Mbambo kilomita 19 ianze kujengwa mara moja. Je, ni kwa nini Serikali inasitasita na kutokuipa kipaumbele mpaka sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haisitisiti na maagizo ya viongozi wa kitaifa huwa ni maelekezo ambayo lazima Serikali itekeleze. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tunaendelea kutafuta fedha ili kipande hiki cha Ipinda – Mbambo kiweze kujengwa kama alivyokuwa ameagiza Mheshimiwa Rais. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Aprili, 2019, Mheshimiwa Rais aliagiza barabara ya Ipanda – Mbambo kilomita 19 ianze kujengwa mara moja. Je, ni kwa nini Serikali inasitasita na kutokuipa kipaumbele mpaka sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haisitisiti na maagizo ya viongozi wa kitaifa huwa ni maelekezo ambayo lazima Serikali itekeleze. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tunaendelea kutafuta fedha ili kipande hiki cha Ipinda – Mbambo kiweze kujengwa kama alivyokuwa ameagiza Mheshimiwa Rais. Ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni lini Mradi wa Maji wa Lema katika Kata ya Busale wilayani Kyela utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, eneo la Busale – Lema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi 223,000,000 na mradi umefika 67%. Kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika na kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.