Contributions by Hon. Geophrey Mizengo Pinda (12 total)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria ambaye, leo yuko kwenye majukumu mengine, ningependa nami kuupitia na kutoa mchango unaoendana na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ambao walipata nafasi ya kuchangia maeneo mbalimbali. Kwa upande wa sheria Waheshimiwa Wabunge wamechangia maeneo mbalimbali yanayohusu mtazamo wa kurekebisha sheria mbalimbali ili kuendana na wakati tulionao.
Mheshimiwa Spika, na katika hali ya kawaida wengi wa wachangiaji walikuwa wanaonesha kwamba, bado tuna sheria kandamizi ambazo kimsingi Tanzania haina sheria kandamizi. Na hili nalirudia tena na niliwahi kulitoa katika maelezo yangu wakati nikijibu swali, isipokuwa tunazo sheria mbalimbali ambazo zinatakiwa kupitiwa upya kulingana na wakati tunaokwendanao kwa sababu, hizi sheria hatuwezi tukazikosoa tukaziita sheria kandamizi kwasababu, chombo kinachotunga sheria ni Bunge lako tukufu na hivyo haliwezi kubebeshwa mzigo wa kutunga sheria kandamizi kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wako watu walihoji uhalali wa baadhi ya Watanzania wenzetu waliokamatwa na kuwekwa ndani wakati wa uchaguzi, na inaonekana kwamba haki haijafata mkondo wake, lakini hawa ni wahalifu na wahalifu wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Hatuna sababu yoyote kimsingi ya kumuacha mhalifu akitumia kofia ya siasa kutuharibia usalama wa nchi yetu. Kwahiyo hawa tutaendelea kushughulika nao kwasababu wanahitaji kufuata msingi wa sheria ya nchi yetu (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge waliona ni muhimu sana. Kwa mfano marekebisho ya sheria za mashirika ya Umma ambayo yanaonekana yamepitwa na wakati, kimsingi haya ni mapendekezo ambayo Serikali inayachukua kwa ajili ya kwenda kuyapitia na kuona kama kweli hizi sheria zimepitwa na wakati, kama tunavyoendelea sasa kufanya marekebisho mbalimbali ya sheria katika kuboresha mifumo ya sheria ambayo kimsingi ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo yale ambayo yameshauriwa tutayachukua na kuyafanyia kazi ili kuboresha. Na Waheshimiwa Wabunge tujue tu kwamba sheria iliyo bora inayokwenda na wakati ni nguzo imara sana katika kujenga uchumi wa nchi yoyote duniani. Kwahiyo kimsingi niseme kwamba tumepokea yale maeneo yote ambayo yameshauriwa na Waheshimiwa Wabunge, tutayafanyia kazi na chombo hiki hiki kitaletewa kwa ajili ya kupitisha sheria ya marekebisho ili tuweze kwenda na wakati na masuala mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wako Wabunge wengine walizungumzia habari za rushwa. Waheshimiwa Wabunge sisi ndicho chombo ambacho kinaweza kikaondoa rushwa Tanzania. Bahati mbaya sana wakati mwingine sisi wenyewe tukawa hatujanyooka sana katika suala la kuzuia rushwa isiendelee kutendeka nchini.
Mheshimiwa Spika, sisi tukisimama imara sisi ni viongozi wa maeneo madogo madogo sana unaweza ukakuta Halmashauri moja ina Majimbo mawili mpaka matatu lakini sisi huko ndiyo hasa tunakuwa ni chanzo kikubwa sana cha kuji-involve kwenye mikataba ya ovyo ovyo huko kwenye maeneo ya Halmashauri zetu, na wala hatusimamii kuzuia rushwa isitendeke. Lakini linakuja Bungeni sasa linabebwa kama vile kuna mtu mwingine mbadala atakayekwenda kusimamia juu ya kuzuia rushwa zisiendelee.
Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, sisi tuko hapa kusimama kuisemea Serikali lakini sisi vile vile ni wawakilishi wa wananchi, tumetoka huko. Kama ingekuwa Waheshimiwa Mawaziri ni wakuteuliwa tu kutoka kwenye taasisi nyingine labda wangekuwa hawajui miondoko na mienendo iliyopo kwenye maeneo ya majimbo. Lakini ukweli ni kwamba, sisi tukiamua kuondoka kwenye rushwa tukasimama imara kama Waheshimiwa Wabunge, na pale linapotokea jambo la rushwa kwenye Halmashauri yako kwenye Jimbo lako tukakuona umesimama Mbunge unazungumza kwa nguvu zako zote mimi naamini baada ya muda suala la rushwa litakuwa ni hadithi tu.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo haya maboresho ya kusimamia haki ambazo zinasababisha vionjo vya rushwa. Ukweli lazima tushirikiane wote, kwasababu hata kama sheria ikiwepo, hapa iko sheria ya kuzuia rushwa lakini rushwa bado zipo, ni kwasababu miongoni mwetu hatuzisemi hadharani, na matokeo yake tunapokwenda kwenye utekelezaji lawama zinarudi Serikalini na kuonesha kwamba Serikali haisimamii vizuri.
Mheshimiwa Spika, sasa Mbunge wewe ni sehemu ya Serikali; na tusipoteze nafasi kwamba sasa baada ya wananchi kukuchagua wewe ni mtumishi wa Serikali moja kwa moja unadhibiti mambo mbalimbali yanayotokea kwenye halmashauri zetu kwenye maeneo yetu ya kata na ya vijiji. Mimi ningeomba tushirikiane sana kwenye eneo hili. Sheria tu kama sheria hata ingekuwepo ya aina gani bila sisi kuisimamia vizuri bado itakuwa ni kazi bure tu.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kwenye maeneo haya. Tumeweka taasisi kama TAKUKURU tuna vyombo kama Polisi, lakini bila kupewa ushirikiano watu hawa hawawezi kuliondoa hili tatizo. Sisi ndiyo wengi tunaweza tukafanya ambushi ya kuondoa matatizo yote kwenye maeneo yetu na kimsingi tukaondokana na hii kadhia ya masuala ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu demokrasia wengi wamesema. Lakini sielewi, nahisi labda kuna watu wanaamini kwamba Tanzania haina demokrasia;
Mheshimiwa Spika, lakini nikuhakikishie, demokrasia ya Tanzania huwezi kuikuta mahali popote, hata Uingereza wenyewe hawana demokrasia hii. Wanatawaliwa na Mfalme huwezi kupata demokrasia ya kweli, demokrasia inatoka kwenye vyombo ambavyo watu wake wanatumia demokrasia ya kuchagua…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana…
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SEHRIA… sisi tunachagua hapa na tunaendelea vizuri kabisa na maisha yetu na wale wanaodai demokrasia kimsingi ebu wajitafiti wao wenyewe kama wana demokrasia ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii na mimi kuwa sehemu ya wachangiaji wa hoja iliyopo mezani, lakini nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na leo hii tuko mbele ya Bunge lako tukufu kwa ajili ya kupangilia maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa mara ya kwanza kusimama na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kwa jinsi alivyoniamini nahaidi kwenda kufanya kazi ya kuishauri Wizara kwa maana ya Waziri, lakini na kutoa matokeo ambayo ni matarajio ya waliyo wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana sana familia yangu kwa utulivu, kwa sababu muda mwingi siko nayo, waendelee kuwa wavumilivu wakati huu tunapotekeleza majukumu ya kuiendeleza nchi. Niwashukuru wapiga kura wangu kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa mwakilishi wao na baadaye kutokana na hayo ndiyo nikaaminiwa kuwa kwenye nafasi hizi ambazo ni za kiutendaji Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwashukuru Wabunge wote mliopata nafasi ya kutoa michango yenu. Watu karibu 30 na zaidi mmechangia kwa uzito wa hali ya juu masuala yote yaliyowasilishwa ambayo yanaisoma bajeti yetu kwa mwaka huu ambao ni mwaka tarajiwa unaokuja na kimsingi mawazo yote ni ya muhimu sana sisi kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Kamati kwa kuonesha ule uelekeo wa nini ambacho kama Wizara tunatakiwa tulibebe na mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, maoni na mapendekezo na maelekezo ambayo mmetupatia kama Wizara itakuwa ni ajabu sana tukatoka nje ya maoni yenu tukaenda kufanya vitu vingine ambavyo vitakuwa haviendi sambamba na maelekozo ya nchi ambayo ndiyo mwelekeo wa nchi yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ukienda kwenye hili eneo la migogoro, migogoro hii ina sura mpaka tatu; tunayo migogoro ya ndani ambayo hii ni mimi nimeibiwa kiwanja, mimi nimefanya nini, nimecheleweshewa hati nimefanya nini? Hii ni migogoro ambayo iko kwenye eneo la utendaji wa Wizara katika kusimamia watendaji wetu kufanya kazi zao kwa uadilifu na uaminifu na ninashukukuru sana Waheshimiwa Wabunge wengi mmeungana na sisi katika mabadiliko mbalimbali ambayo tumeendelea kuyafanya ndani ya Wizara katika kuimarisha utendaji. Mojawapo ni lile lile la kutambua hata watumishi wetu ambao walikuwa wanafanya kazi moja kwa moja kwenye halmashauri, lakini badaye Serikali iliamua kuwarudisha na kuwa chini ya Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwatoe wasiwasi kwamba kurudi kwao Wizarani bado hakutafisha au kudhoofisha utendaji katika maeneo yote ya Serikali yetu kwa maana ya halmashauri na hii itasaidia sana kuimarisha usimamizi kwa sababu kama mtabaini katika muundo wa utumishi ukitoka ngazi ya Waziri mpaka Kamishna wa Mkoa palikuwa pana gap kubwa sana kwenda kukuta watendaji wetu ambao wako kwenye halmashauri, lakini sasa tunakwenda kuhakikisha kwamba hawa wanarudi kwenye nguvu ya Wizara ili usimamizi wao uwe karibu zaidi ili waweze kuwajibika ipasavyo, hii itatusaidia sana kutoka matokeo, kwa sababu taasisi nyingine zote zilifanya hivyo hata TAMISEMI yenyewe ilitambua kwa mfano Mamlaka kama za TARURA kwa ajili ya kuongeza usimamizi mzuri. Hata sisi Wizara ya Ardhi tunaendelea kutengeneza mpango ambao utaletwa mbele ya Bunge lako tukufu kwa maana ya kutengeneza Kamisheni ya Ardhi ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kusimamia shughuli za ardhi hapa nchini na inaweza ikaleta ufanisi mkubwa sana ambao ndiyo matarajio ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye migogoro; kuna migogoro ambayo ni ya kati kati hapa na migogoro mingi ni kwa muda mfupi niliyokaa Wizara hii migogoro hii ya kati ambayo inasababishwa na mgongano wa kimipaka ndani ya nchi, ndani ya wilaya na wilaya, ndani ya kijiji na kijiji na hii inayohusisha kwa maeneo ya hifadhi tunajaribu kupitia vilevile hata sheria zetu kuziangalia. Kwa sababu utaona kuna kachangamoto kadogo unaweza ukakaona ni kama ni kadogo lakini kanagonganisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zile GN zinazosomwa katika kila maeneo ni mamlaka tatu zimepewa mamlaka ya kutoa GN ambazo ukiliangalia unaweza ukakuta linaleta mgongano ule ambao unasababisha migogoro kwa wananchi wengine, kwa mfano TAMISEMI kwenye kupima vijiji imepewa mamlaka ya kutoa GN, Maliasili imepewa mamlaka ya kutoa GN, Ardhi ambao ndiyo wasimamizi halisi wa ardhi nao wanatoa GN. Sasa mgongano huu lazima tukae, tutakaa katika Wizara hizi ili tuweze kutafsiri nani hasa awe wa mwisho kwenye kuzungumza juu ya matumizi ya ardhi kitu ambacho kitasaidia sana kuondoa hii matatizo makubwa ambayo yanatukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano niwape mfano mdogo tu hapa Wilaya ya..., I mean mgongano uliyopo kati ya Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara eneo moja linaitwa Mkungunero. Mkungunero TAMISEMI ilienda ikatambua vijiji, baadaye Maliasili ikatambua maeneo ya hifadhi, sisi tukaenda tukaweka mpaka wa mkoa; ule Mkoa kimsingi umesoma vijiji vingine ulikata ule vijiji ile alama ya mkoa imeacha vijiji vingine Dodoma, vingine Manyara.
Sasa migongano kama hii tusipo ikalia pamoja tukaiweka vizuri migogoro hii haitaisha, lakini ndani ya migongano hiyo ya kimpaka mingine ipo kwenye wajibu tu wa viongozi wa maeneo, tunaikuza sana sana mpaka ikapelekewa na Mawaziri nane na nini, lakini kwa mtazamo halisi unaona kabisa DC wa eneo anahusika, Mbunge wa eneo anahusika, Mwenyekiti wa Kijiji anahusika, yangeishia kwenye level hiyo wala kusingekuwa na mgongano, lakini kule nimeona kabisa na kubaini kuna baadhi maeneo mengine watu wanakimbiana, hawakai pamoja kuzungumzia matatizo ya wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo gani kati ya mwananchi ambaye amepitiwa na mpaka wa Mkoa analima Mkoa wa Manyara anakaa Mkoa wa Dodoma, kuna tatizo gani huyu mwananchi kuachwa katika muundo huo wa kutumia ile ardhi na badala yake tunaandamana. Mimi niwaombe kwenye eneo hili mamlaka za maeneo zisimame imara kuzungumza mambo haya hadharani, yakija huku Wizara, huku tunafuata sheria, hata tukienda na sheria zetu pale hazitatanzua mgogoro kama ambavyo tungekaa huko katika ustaarabu wetu wa maisha yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti mimi niwaombe ndugu Waheshimiwa Wajumbe na Wabunge wenzangu, tuzungumze, kwenye maeneo haya tuzungumze kwa uwazi kabisa. Tunafanya juhudi mbalimbali na kimsingi lazima muone namna ambavyo Serikali inafanya juhudi za kujaribu kutatua migogoro, lakini migogoro mingi haiwezi kutatuliwa kama viongozi wa maeneo husika wao wenyewe hawawi sehemu ya kumaliza migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lipo hili tatizo la mipaka ya nchi, hilo tunaendelea nalo na Waheshimiwa Wabunge tunaendelea na kutambua mipaka, kuna maeneo mengine bado kuna mvutano kidogo ila yanaenda kumalizika hivi karibuni na nchi nyingine tumeendelea kuzungumza nao kwa ajili ya kunyoosha mapito, kwa sababu Tanzania na majirani zake hatuna mgogoro wowote wa kimahusiano, kwa hiyo, masuala haya yanakwenda vizuri na ni wahakikishie kabisa kwa mfano hili eneo la Mheshimiwa Kitandula kule juu baharini wala asiwe na wasiwasi kwa sababu mazungumzo ya Kenya na Tanzania ni ya karibu mno kuliko hata mataifa mengine kwenye suala la mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la mabaraza; hili suala la mabaraza Waheshimiwa Wabunge mmetoa mawazo kuhusu uimarishwaji wa mabaraza, ni kweli hata sisi tumeliona na tumeunda timu maalum ipitie. Hata hivyo Serikali Kuu jambo hili lilikwenda kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuangaliwa, je, lirudi mahakamani au liendelee kuwa Wizara ya Ardhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa upande wote kwa sababu ni watu ambao tunasubiri maelekezo sisi tumeendelea kujiandaa upande wetu kuimarisha haya mabaraza na mwaka huu wa fedha ambao leo tumewaletea bajeti hapa tunakwenda kwa ajili ile tofauti ya mabaraza 47.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu, ahsante, wale wanao kosekana kwenye halmashauri karibu 47 tunakwenda kuwaajiri mwaka huu wa fedha kwenye zile wilaya ambazo bado hazijapata Wenyeviti, tunaenda kuajiri. Vilevile tuwaombe mshikamano wenu kwamba tunakwenda kuleta wale watendaji lakini tunahitaji maeneo ya kufanyia kazi ambayo kimsingi tunapata msaada kutoka TAMISEMI kwa maana ya maeneo yale ya ofisi za mahakama hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera tumeshaanza kuipitia kwa uzito wa kutosha, hata hili suala la diaspora linakwenda kuisha kwa sababu hatuoni kama tunaweza tukaendelea kuwa na msimamo wa kutokutambua Watanzania wenzetu ambao wakija kujenga nyumba Tanzania hawahami nayo. Wakija kuwekeza Tanzania maana yake wanarudisha nguvu walizozikusanya nje nchini mwao, Serikali imeliona na sasa liko katika hatua za mwisho na hawa Watanzania wenzetu wataenda kunufaika na hii huduma ambayo ni ya kupata ardhi na kuwekeza nchini Tanzania na hii ndiyo mataifa mengi yanafanya kuwatumia watu wao ambao wako nje kwa maendeleo yao hata ukienda Ethiopia pale utakuta wazamiaji wengi ndiyo wanajenga majengo kule ya maana kabisa. (Makofi)
MWENYEKITI: shsante sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia afya na leo tuko hapa mbele yake tukisikiliza mambo mbalimbali. Nianze kwa kuipongeza Kamati kwa maazimio mbalimbali ambayo yamewasilishwa kwetu. Sisi kama Serikali maazimio haya tunayachukua kwa ajili ya kwenda kuyafanyia kazi na kuyachakata kwa namna yoyote ile ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo machache ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge na kwa kweli kwa upande wa Wizara yetu Wabunge wengi wamechangia na sehemu kubwa sana walijikita kwenye hii migogoro ya adhi, fidia lakini pia mpango wa maboresho ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji. Mambo yote haya na ushauri wote walioutoa sisi kama Serikali tunayapokea na tunakwenda kuyachakata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kama Wizara kwenye suala la mabaraza ya ardhi, sasa hivi tunaendelea na mchakato ambao, ili kukamilisha ile idadi ya wilaya tulizonazo ya kuajiri wale wenye viti wa mabaraza. Muda mfupi ujao tunaweza kabisa wilaya zote zikawa zimepata watendaji ambao watakwenda kutusaidia kupunguza hasa umbali kutoka wilaya moja mpaka wilaya nyingine, kwa mfano mtu wa Dodoma hapa tumempa mpaka Kiteto kule unakuta wakati mwingine tunakuwa na limbikizo la kesi ambazo zingetakiwa zitatuliwe kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni imani yangu kwamba wakati ujao tutakapokuwa tunatoa taarifa ya utekelezaji tutakuwa tunawafikisha kwenye kuondoa kiu hii hasa kwenye upande wa mabaraza. Ninaomba mtupe nafasi ili tuweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kubuni na kutekeleza mipango mbalimbali ya kupunguza migogoro ya ardhi naomba niwape comfort Waheshimiwa Wabunge, kwamba Wizara imejipanga na kama Wabunge walivyosema asubuhi, tuna timu mbalimbali zinazotafiti kwa nini kuna migogoro mingi hapa nchini na nini asili yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu unaweza ukaona migogoro hii ina sura kama mpaka tatu hivi. Iko sura ile ambayo ni wananchi wenyewe kugombania maeneo yao kwa mipaka ile isiyotambuliwa. Tunayo mashamba makubwa makubwa ambayo wananchi wanaoonekana wamekaa katika maeneo yale uasili wao ni kwamba wana historia ambazo haziwezi zikabadili uwepo wao pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mashamba makubwa watu walichukuliwa kutoka sehemu mbalimbali kwenda kuongeza nguvu za uzalishaji kwenye yale mashamba. Hili nalo tumelipokea na tunalifanyia kazi kwa haraka ili kuangalia. Case study moja ni Mkoa wa Manyara ambao wananchi wake wengi ambao wanagombana na wale wawekezaji sehemu kubwa sana wana asili ya uwepo wao pale kwa sababu wazazi wao ambao walichukuliwa kutoka maeneo mbalimbali waliletwa na hao wenye mashamba na sasa hivi inaonekana ni tatizo na ni kadhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunafanya nao kazi na nimekutana na wawekezaji wa mashamba makubwa takriban Mkoa mzima wa Manyara. Tumekubaliana na wengi wameanza kukubaliana kwamba okay tatizo the way lilivyo iko haja sasa ya kuangalia upya namna ya kuachia maeneo mengine ambayo hawa Watanzania wanaweza wakaendelea kuyatumia kwa namna yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili suala la mipango ya kutatua migogoro tunaendelea nalo. Tunatengeneza mifumo ambayo baada ya muda kama mlivyosikia kwenye taarifa ya Kamati, tuko zaidi ya asilimia 80 katika kuanza kufanya majaribio ya kutumia TEHAMA katika process nzima ya mtu anapotafuta kiwanja. Kwa sasa hivi bado tunabeba mafaili mkononi, na hiyo imesababisha matatizo mengi sana. Matatizo mengi ya katikati ya miji ambayo tayari imeshapimwa siyo kwamba inahitaji kupimwa upya. Kule ku-move kwa njia ya mkono bila kutumia mitandao hii mara nyingi imesababisha vitu vingi kuwa na mambo ya double allocation bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa dawa inachemka; niwaombe tu Waheshimiwa nadhani mpaka kufikia Bunge linalokuja tutakuwa tunatoa taarifa ya utekelezaji. Wengine mtakuwa mnaona kwenye mitandao yenu kupitia simu zenu jinsi mnavyopewa ripoti ya maeneo ambayo mnayamiliki kihalali. Kwa hiyo, niwaombe tuwe na muda wa kutosha ambao tutakwenda kuleta matokeo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie kwa ufupi sana kuhusu susala la maboresho ya mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji. Waheshimiwa Wabunge niwaambie, mpaka kufikia 2024 hapo tutakuwa tayari tumeshapima vijiji 5,000 na vijiji 5,000 ni karibu nusu ya safari ya vijiji vyote vya Tanzania. Kwa hiyo, naomba tu kwa sababu fedha zile ambazo zimeombwa kutoka kwenye mifuko mbalimbli, tunazo fedha zinazotegemewa kutoka kwenye halmashauri kama mtakumbuka Bunge lililopita na tuna fedha ambazo tunazitenga kwenye bajeti yetu ya kila siku. Kwenye huu mfuko ambao unatokana na mfuko wa World Bank tayari kwa sababu bajeti ya kwanza ilikuwa inasema tutenge bajeti ya shilingi bilioni saba; lakini nataka niwakikishie mpaka sasa tumeshatenga shilingi bilioni 21 katika zoezi hili na tunakwenda kupima vijiji zaidi ya 1,600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea hapa katika tofauti ya utekelezaji; Tume hii iko chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Utendaji kazi wake ni wa pamoja wala siyo kwa kutenganisha. Mradi kama huu wa World Bank una masharti magumu sana katika kutoa fedha yake kuihamisha kuipeleka Tume. Kwa hiyo, hizi shilingi bilioni 21 zinasimamiwa na Wizara yetu chini ya fungu la Wizara lakini watendaji ni wale wanaotoka kwenye tume kwenda kutekeleza yale majukumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ni kweli mnaweza msizione fedha kwenye account za tume lakini tume tunai-facilitate kwa asilimia 100; na mpaka sasa hivi maafisa wengi kutoka kwenye ile tume wako uwandani na wanaendelea na kazi, hatujakwama mahali popote. Kwa hiyo, niwaombe tu kwamba ni mambo ambayo yanatekelezeka kwa utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ongezeko la fedha. Mkopo huu ulikuwa na mambo mengi, na moja ya eneo lake ilikuwa ni kufanya mamboresho kwenye maeneo ya utawala wa Wizara. Niwakikishie Waheshimiwa Wabunge, mikoa yote inaenda kupata majengo kwa ajili ya maafisa wetu. Najua mnajua wanavyohangaika kwenye halmashauri kule, wanavyojibana kwenye vyumba vidogo vidogo. Tunakwenda kujenga ofisi za mikoa yote. Mikataba tayari imeshasainiwa ya kubaini wale wakandarasi. Tunakwenda vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na eneo hili vile vile tunakwenda kuanzisha ofisi za ardhi za wilaya ambazo kwa miaka yote hazijawahi kutokea. Kwa hiyo, kumekuwa na miss communication. Kumekuwa na mtengano wa kimawasiliano kati ya maafisa wetu ambao tumewa-attach kwenye halmashauri ambao wako chini ya Wizara yetu na kamishna wa mkoa; unakuta load ya kamishna wa mkoa ni kubwa. Tunakwenda kuwa na makamishna wasaidizi wa wilaya ili waweze kusimamia zile halmashauri zilizoko chini ya Wizara zao. Hii itatusaidia sana kutusogeza karibu na huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumzia masuala ya mabadiliko ya sheria na sera. Wizara iko kwenye mchakato na sera ilishakwenda mpaka kwenye Baraza la Mawaziri. Sasa Waheshimiwa Wabunge tukae mkao wa kuipokea huku Bungeni kwa ajili ya kuipitia, lakini iko mwishoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliabaini kwamba sera ile ni ya muda mrefu na ina mapungufu. Kwa hiyo, yale mapungufu yote mliyoyaona ninyi na kushauri, ushauri wenu wote tumeuweka kwenye haya mapendekezo ya sera mpya ambayo inakuja. Niwaombe tu kwa ujumla wake. Kwanza napokea shukrani nzote napongezi zote mlizozipeleka kwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yake, na mimi nitamfikishia; lakini pongezi zote zilizotolewa kwa Serikali nzima kwa maana ya Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wake wote tuliopo. Tunashukuru sana kwa hizo shukrani ambazo kweli mnatambua mchango ambao unatolewa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Niwaombe tujipe muda kuhusiana na mambo haya. The way tunavyokwenda tunakwenda katika michakato tofautitofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo ningependa niwambiwa Watanzania wote ardhi ya Tanzania kwa ukubwa wake haina nyongeza nyingine yoyote tulikuwa nayo Mwaka 1953, tukawa nayo Mwaka 1960, tunayo Mwaka 1970 na tunayo 2024, haitaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kupitia hilo sisi Watanzania Mwaka 1950 tulikuwa chini milioni tisa, leo tunapozungumza tuko milioni 61. Hekima ituongoze katika kupitia haya mambo ambayo yanaihusu ardhi. Ongezeko letu ni sababu nyingine ya msingi kabisa ya ongezeko la kusukumana sukumana katika maeneo yetu. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na nawashukuru kwa jinsi ambavyo mnatupa mawazo jinsi ya kukabili ongezeko la watu bila ongezeko la ardhi, ahsante sana Mungu awabariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipitie maeneo machache ambayo Waheshimiwa Wabunge katika mjadala wa leo walijaribu kuibua hoja. Kwa ujumla wake tunawashukuru sana Wabunge wote waliochangia na ninadhani Mheshimiwa Waziri wakati atakapokuwa anahitimisha atatambua kwa majina mchango wa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo langu nitazungumzia hoja mbili; moja, ni msongamano wa mahabusu katika Mahakama zetu ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi ni kweli kwamba kumekuwepo na msongamano wa mahabusu katika Magereza zetu. Hii kwanza ni kutokana na Magereza zetu kutokumudu hiyo namba ya wahalifu wanaopelekwa pale. Hii ni kwa sababu Magereza nyingi nchini zimejengwa muda mrefu sana na nyingi zilijengwa siku za nyuma, hata nchi yetu kabla ya kupata uhuru. Kwa hiyo, utakuta Magereza ilijengwa wakati ambapo Tanzania haina idadi ya Watanzania ambao sasa tuko milioni 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa tu mfano, Gereza la Mpanda pale ambalo lilijengwa 1947 lilikuwa na uwezo wa kuchukua watu chini ya 200, lakini kwa sasa lina watu zaidi ya 800. Magereza kama hii, ziko nyingi hapa nchini na hivyo kusababisha mlundikano wa watu, lakini juhudi mbalimbali zinafanyika na kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Magereza ambayo iko Wizara ya Mambo ya Ndani, sasa hivi kuna program za kujenga Magereza mapya na yale yaliyopo kuyaongezea uwezo ili tuweze kumudu idadi ya wahalifu ambao kila uchwao wanaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitu cha kuongezeka kwa wahalifu hatuwezi kukikwepa kwa sababu idadi yenyewe ya Watanzania ni kubwa na ukubwa huu unasababisha misukumano ya hapa na pale ambayo inasababisha kwenda kwenye vyombo vya utoaji haki; na wakati wa taratibu zile za kusubiri kukamilisha eneo hili la utoaji haki, basi yule aliyetuhumiwa anakuwa amehifadhiwa mahali ambapo vilevile kwake ni salama kwa upande mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Wabunge wote tushirikiane kwa sababu tunatoka kwenye maeneo hayo tuone namna nzuri ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu ili wasiendelee kuingia kwenye makosa ambayo hawakuyatarajia, kusudi pamoja na mambo mengine tuendelee sasa kupunguza uhalifu nchini. Kwa sasa katika juhudi za kupunguza msongamano, tuna vyombo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, chombo cha kwanza ambacho kinatusaidia sana kupunguza msongamano ni pamoja na Mheshimiwa Rais kutoa msamaha kwa wale ambao vifungo vyao vinaonekana kufikia mwisho na kimsingi huko kumekuwa na idadi kubwa ya wafungwa ambao wanapata msamaha wa Rais. Vilevile kwa kupitia Mahakama, kujaribu kuziondoa kesi ambazo hazina mashiko. Vilevile tuna mfumo wa plea bargaining ambapo DPP kwa mamlaka aliyopewa amekuwa akijaribu sana kupunguza idadi ya wale mahabusu wetu ambao wengine wanasubiri kesi huko Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la kubambikiwa kesi. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamesema kumekuwa na utaratibu wa kubambikiwa kesi kwa wananchi. Napenda kusema tu kwamba Serikali yetu tukufu kupitia chombo chake cha utoaji wa haki hakina utaratibu wa kumbambikia mtu kesi. Hizi kesi mara nyingi kama kuna sura ya kubambikiwa, wanaanzana huko walikoanzia safari ya kuchokozana, lakini huwezi kukamatwa kwa kesi ya wizi wa kuku, ukafika Mahakamani ukaambiwa unashitakiwa kwa kosa la kuiba ng’ombe, haiwezekani. Kwa Serikali yangu hiki kitu hakipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye eneo hili la ubambikizwaji kesi, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, ushirikiano ni kitu muhimu sana. Tushirikiane kwenye mazingira, kwa sababu unaposema kubambikiwa kesi, inahitaji ushahidi wa kutosha kuonesha kwamba kweli mtuhumiwa au mlalamikiwa kabambikiwa kesi. Kwa sababu, mbambikiaji, yule anayefanya zoezi la kumbambikia kesi ni mhalifu kama wahalifu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukipata taarifa za mapema, maana yake huyo aliyehusika kubambika kesi atatueleza nia yake, naye anatakiwa kwenye vyombo vya sheria ili tukamwelewe vizuri, kwa nini aliweka nia ya kubambika kesi? Kama ni sehemu ya watumishi wetu wa Serikali, tunachukua hatua za haraka sana, kwa sababu kwanza huko ni kuidhalilisha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kubambika kesi lina uwezo wa kumalizika katika maeneo ya ngazi ya chini sana. Tukipata ushahidi wa kutosha kwamba, kweli katika mazingira yaliyo wazi au kulingana na mazingira yake inaonekana kuna watumishi wamejihusisha na kuwabambikia kesi wananchi wetu, kama nilivyosema mwanzo, hatua kali sana zinachukuliwa dhidi yao. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwenye ngazi ya Mahakama, sisi tuna Kamati ya Maadili ya Mikoa ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kwenye wilaya hali kadhalika. Sasa mambo haya yanapotokea katika ngazi hizo, tukiwa na uhakika sisi Wabunge, tupeleke haya maelezo kwa Wakuu wa Mikoa ili kama ni Hakimu amehusishwa na jambo hili, basi kamati zile zipitie kupitia ile Kamati ya Maadili, ili tuweze kumbaini na baadaye hatua za kisheria dhidi yake ziweze kuchukuliwa. Kama ni Idara ya Polisi, nako huko vilevile. Tunapopata Ushahidi inasaidia kwa sababu, jambo la kubambikia linahitaji ukaribu sana katika suala la kulithibitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ile tu kwamba wamebambikiwa kwa maelezo ya mlalamikaji anapokuja kwako, inawezekana likawa na ukweli au lisiwe na ukweli. Hivyo, basi nawaomba tuwe na ushirikiano wa karibu sana. Mahakama ndiyo sehemu ambayo haki zote zinatolewa kwa kuzingatia sheria ambazo sisi Waheshimiwa Wabunge tumekaa hapa na tunazitunga ili ziende zikatumike vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyaeleza haya mawili kwenye maeneo yangu sasa niache nafasi kwa Mheshimiwa Waziri ambaye kwa kweli, ndiye alikuwa mtoa hoja, aweze kutusaidia kukamilisha hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende ku-declare interest yangu hapa, mimi nimezaliwa jeshini, ni mwanajeshi niliyefanya kazi jeshini miaka 33; kati ya hiyo miaka 13 nilikuwa nimewekwa attachment Wizara ya Mambo ya Nje, kwa hiyo….(Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pinda, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nakumbuka kumbukumbu zangu ukiwa umekalia kiti hapo ulitupa mwongozo tukisema una-declare interest au maslahi jambo unalozungumzia labda uwe unapata fedha direct. Sasa Mheshimiwa Pinda naomba nikupe taarifa kwamba kukaa kambini sio kwamba una maslahi, wengi tumekaa kambini.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, mtoa hoja hajaelewa ninachokisema, kwa hiyo naomba nimuhurumie tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema kwamba mimi ni uzao wa jeshi na nimetumika jeshini miaka 33 na hivyo basi ninaposimama kama Naibu Waziri wa Katiba na Sheria najisikia raha sana kwa sababu nimetokea kwenye chombo hiki ambacho leo kimewasilisha bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya kuchangia; kwanza niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna ya pekee jinsi ambavyo mmechangia, mmetoa mawazo makubwa sana, nadhani Wizara ya Ulinzi mwakani tutakaa mkao mzuri ili kuandaa bajeti inayolingana na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge kwa sababu mmegusa maisha ya wanajeshi kwa karibu sana na hili ni jambo muhimu sana kwa sababu wakati mwingine tungekuwa tunashuhudia tu nashika shilingi, lakini kumbe nimebaini kwamba mnajua umuhimu wa hiki chombo ambacho ni chombo muhimu sana hasa kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba katika kufikia uchumi wa kati, jeshi limechangia sana kwa sababu bila utulivu tumeshuhudia nchi nyingi zinakimbia kimbia, hakuna muda wa kuzalisha. Hivyo basi niwaombe mkawe mabalozi huko ambako vikosi vyetu vya jeshi vipo karibu na wananchi, mjaribu kutusaidia kuelimisha wananchi kuelewa umuhimu wa hivi vikosi vya jeshi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hakuna Kikosi cha Jeshi kinachowekwa bila mpango maalum wa umuhimu katika ulinzi wa nchi. Kwa hiyo utaona maeneo mengi ambayo vikosi hivi vipo vina malengo maalum katika kulinda mipaka ya nchi yetu na kuwalinda wananchi wake ambao tunalala na kuamka salama bila hata kuchomwa na sindano na maadui zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya jeshi; makambi na vikosi vya jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) vinaundwa kulingana na sheria ya ulinzi ya Taifa Na. 24 ya mwaka 1966 ambayo imefanyiwa marekebisho na kuwa Sura ya 192 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mwaka 1966 hadi 1979 Serikali imetenga maeneo mengi na makubwa mbalimbali mbali na miji na vijiji kwa matumizi ya jeshi. Miaka ya hivi karibuni kumezuka migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo kadhaa ya jeshi, kwa sababu mbalimbali zikiwemo maeneo ya jeshi kutopimwa kuchelewa kulipa fidia mapungufu ya sheria za ardhi kupanuka miji midogo kuwa miji mikubwa wananchi wasio wahaminifu kuvamia maeneo ya jeshi. Hata hivyo Wizara inachukuwa hatua mbalimbali kutatua migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na kupima maeneo yake kufanya uthamini na kufanya vikao vya usuluhishi na wadau wa migogoro husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo tayari upimaji umefanyika na ramani zake kusajiliwa. Wizara inafanya jitihada za kuandaa hati miliki, hadi sasa Wizara ya Ulinzi imeweza kupima maeneo yake yapatayo 121 kati ya 203; maeneo matatu tayari hati miliki zimepatikana na maeneo 62 yapo katika mipango ya kuomba kuandaliwa kwa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021 imeweza kulipa fidia kwa maeneo kumi yakiwepo Kigongo Ferry na Ilemela shilingi 6,824,544,927; Nyagungulu na Burihahela shilingi 3,534,295,165.58; Mwanza Mlangalini na Mashono huko Arusha shilingi 1,548,490,247.88. Kwa upande wa Kilwa ni shilingi 624,236,405 Makoko ni shilingi 1,109,841,249 na Nyabange Musoma shilingi 203,646,661 na Airport Chato, Geita ni shilingi 972,218,036.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara inatarajia kulipa maeneo yafuatayo Nyamisangula Bugosi na Kanyambi - Tarime shilingi 1,631,984,692.76; Kaboya - Muleba shilingi 4,440,346,998.25; Kikombo - Dodoma shilingi 2,261,604,837.45; Mitwero - Lindi shilingi 187,888,88 na Duluti - Arusha shilingi 4,694,000,000 idadi ya maeneo yaliyotarajiwa kulipwa fidia kwa mwaka wa fedha 2021/2022 yataongezeza kutokana na timu ya wataalam walioko uwandani hivi sasa wakifanyia upimaji na uthamini kwa sababu timu hiyo ipo Mikoa ya Lindi na Mtwara wakiendelea kutekeleza majukumu ya upimaji na thamani yake. (Makofi)
Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo niombe tu kwenu mjaribu kuwapelekea wananchi wawe watulivu kwenye maeneo yale ambayo bado hatua za uthamini zinaendelea, lakini Serikali inaendelea kupunguza ulipwaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kilimo kwa upande wa JKT; katika kuhakikisha kwamba JKT inajitosheleza kwa chakula, umeandaliwa mpango mkakati 2019/2020 - 2024/2025 ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya mkakati huu ambayo yamefanyika ni pamoja na kuandaa andiko la mkakati, upimaji wa ukubwa wa mashamba na afya ya udongo katika maeneo ya vikosi, upatikanaji wa pembejeo na kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba. Aidha, kwa kuanzia JKT imeanza ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Shamba la Chita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutekeleza mkakati huu JKT imeingia makubaliano na Wizara ya Kilimo katika maeneo ya utaalam na teknolojia ya kilimo, mafunzo ya utaalam, mbinu za uzalishaji bora wa mazao, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, masoko ya mazao na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo makuu ya mkakati huu ni kuongeza uzalishaji wa mazao ili kujitosheleza kwa chakula na kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia sekta ya kilimo na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio ya Jeshi la Kujenga Taifa ifikapo mwaka 2024/2025 ni kuhakikisha linaongeza maeneo ya kilimo kutoka ekari 14,200 zinazolimwa sasa hadi kufikia ekari zaidi ya 28,000 sanjari na kuongeza eneo la umwagiliaji katika shamba la Chita kutoka ekari 2,500 zinazojengwa kwa sasa hadi kufikia ekari 12,000 ifikapo 2024/ 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo basi, mimi naamini wazi kwamba hata baada ya muda huu vijana watapata nafasi ya kujiajiri kwa sababu sasa hivi ni kweli vijana wetu wanapoambiwa wanakwenda JKT wazo la pili walilonalo ambalo wanaondoka nalo ni kupata ajira. Lakini ukweli ni kwamba JKT inakwenda kuwajengea uwezo wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa naamini wazi kabisa kwamba tukihamasika hata sisi Wabunge kuwatumia wale vijana waliomaliza JKT kuwaweka katika makundi ya uzalishaji kwenye maeneo yetu, watakuwa na tija ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, nipende tu kusema hayo, lakini naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha tukae hapa leo na kulijadili jambo hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Kamati kwa kutoa mwelekeo ambao mawazo yao ni chanya sana katika kukubaliana na wazo la kuridhia Itifaki ya Kuwaongezea Majukumu Mahakama yetu ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa mawazo yao wametoa msukumo kwamba jambo hili kwanza lilichelewa, na ni kweli kabisa kwamba lilichelewa kwa sababu wale waliokuja na wazo la kuanzisha chombo hiki walikuwa na maana yake. Nasi kama Tanzania katika ile Mihimili mitatu ya nchi kubwa zilizoanzisha Jumuiya hii nasi ni mmojawao. Kwa hiyo, nadhani lilikuwa linasubiri wakati na sasa wakati umefika, nami nikubaliane na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia, kuwashawishi Wabunge wote mliopo katika ukumbi huu kuiridhia hii Itifaki ya kuwaongezea majukumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, actually siyo kuwaongezea majukumu ile Mahakama ni kutufungulia milango sisi Watanzania, kwa sababu kuchelewa kote huku kunaweza kukawa kumesababisha vitu vingi sana ambavyo watu wetu wameshindwa kunufaika kwa wakati juu ya matumizi ya Mahakama hii. Kwa sababu wakati mwingine unaweza ukapata hofu ya kitu chenye msaada kwako mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wengi sana wanafanya biashara na hizi nchi, lakini inapotokea migogoro unaona kabisa uhitaji wa chombo cha marekebisho ya migogoro ile ni mkubwa kuliko wakati wowote ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini wazi tunapokwenda kuridhia Itifaki hii ya kuwaongeza Majukumu hii Mahakama ya Afrika Mashariki, itatusaidia sana, hasa katika haya maeneo matatu ambayo yanatufanya tuwe pamoja zaidi. Kuendelea kutoridhia kutasababisha tubaki nyuma sana kwa sababu huwezi kukaa nje ya competition halafu ukasema na wewe ni mmojawapo. Ni lazima tuingie huko ndani tuendelee kunufaika na uwepo wa vyombo hivi, kimsingi kama tulikuwa na mashaka yalishaondolewa na waliokuwa watungulizi wetu, wameonesha kwamba ardhi iendelee kubaki chini ya milki za Serikali husika. Kwa hiyo, hatuna mashaka makubwa sana ambayo unasema hapa hili ndilo linaloweza likasababisha tusi-ratify haya makubaliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mazingira ya kawaida ninashukuru sana mapokeo ya Waheshimiwa Wabunge kwa sababu katika wale wachangiaji, pamoja na kwamba walikuwa kama Sita tu, lakini unaona ile message walioiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu, ni message nzito sana ya kushawishi ili wananchi wetu waende wakanufaike na hizo opportunities zinazotokana na haya masoko huria, matumizi ya shilingi moja na ile free movement ya vitu katika ukanda wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaamini wazi kwamba ikiridhiwa hii inakwenda kufungua miliango. Kwa sababu tukisharidhia tukamalizika katika Jumuiya yetu hii, maana yake vitu vingine ambavyo havijafanyika, kwa mfano kuwa na hiyo one currency haiwezi kwenda kuanza mchakato wa aina yoyote mpaka turidhie sisi wote wanachama ili tukaunde mawazo mapya, kwamba, okay, kutoka hapa sasa hela gani tunaweza tukai- formulate pale iweze kutembea katika huu muungano wetu wa jumuiya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nchi kama zile za Eurozone unaona wanatumia Euro, siyo hela ya nchi moja katika zile. Na advantage ni kubwa sana kwa sababu biashara inakuwa miongoni mwa wanachama, haikui kwa mtu mmoja mmoja. Kwa hiyo, unaona faida ambayo tunategemea itakwenda kupatikana huko ni kubwa sana. Hivyo basi, mimi nisiwe msemaji sana kwa sababu hakuna ambacho unaweza ukasema unajibu hoja ambazo labda zinataka ufafanuzi. Katika watoa hoja, wote wamekubaliana na wazo la kuridhia mkataba huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kwanza naunga mkono hoja, vilevile nimalize kwa kusema twendeni kwenye maendeleo ya kweli kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kweli kama alivyotangulia kuzungumza Mheshimiwa Ndejembi hapa, Wizara ya Ardhi ni kiungo kati ya Wizara zile za Kimkakati katika kutatua migogoro mbalimbali hapa nchini. Katika mazingira ya kawaida Serikali iliona umuhimu wa kuwa na Timu Maalum ya Mawaziri Nane kupita katika maeneo yote ya migogoro nchini na ilitoa miongozo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, yale maeneo machache ambayo yamebaki, tunaendelea kuhangaika nayo kwa ajili ya kutatua ile migogoro. Niwape tu comfort wananchi kwamba wawe watulivu katika kipindi hiki cha kutatua hii migogoro ambayo kimsingi inakwenda kumalizika hasa kwenye hii mipaka ya hifadhi na wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya kawaida yale maoni yote ambayo nimesikia kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge yanayohusu hii migogoro ni maelekezo kimsingi tunayapokea kwa mikono miwili na tutatoa ushirikiano mkubwa sana kwa sababu maeneo mengi Wabunge wanasema hatushirikishwi, hatushirikishwi. Tunapokwenda uwandani hatuwapi taarifa lakini ukweli wana majukumu mengi sana ambayo wakati mwingine yanawatenga na zile shughuli za kiutendaji. Hata hivyo, ahadi tunayoitoa Wizara ya Ardhi…
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Pinda, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwijage.
TAARIFA
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Pinda. Jukumu muhimu la Mbunge ni maslahi ya wananchi, hakuna kazi yoyote ninayoweza kupewa na mtu yeyote zaidi ya kazi ya wapigakura wangu. Wawe wanatujulisha. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine mnakuwa hapa Dodoma na Kamati zenu zimepewa na Spika, mnashindwa kwenda majimboni Serikali inapokuwa inakwenda huko. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba sio kila Mbunge anakuwa sehemu ambayo Waziri yupo. Waziri anakwenda anafanya kazi yake, lakini hoja ya Msingi ni Mbunge kutaarifiwa ili hata yeye asipokuwepo awepo mwakilishi wake aweze kumpa mrejesho. Hata hivyo, hakuna uhalisia wa kufikiri kwamba kila Waziri anapokwenda kwenye ziara Mbunge atakuwepo, hakuna huo uhalisia. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hiyo malizia mchango wako.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana huko ndiko nilikuwa naelekea. Nataka tu kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, wakati wote wa zoezi hili tutawarifu Waheshimiwa Wabunge na watuwie radhi kama huko nyuma walikuwa hawaarifiwi. Nia yetu ni kuongeza mshikamano katika kutatua migogoro ambayo inatukabili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo kwa kweli tumwachie mtoa hoja ili aweze kwenda kufanya majumusiho ya mwisho kabisa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata uhai na leo hii kupata nafasi ya kuwasilisha bajeti ya Wizara kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali yaliyopangwa katika mwaka wa fedha ujao. Nitakuwa na eneo dogo la kuzungumzia, ni maboresho mbalimbali ambayo tunaendelea kuyafanya kama Wizara kwenye maeneo mbalimbali hasa ujenzi wa miundombinu kama Mahakama, kuimarisha ofisi za watendaji wetu kama ofisi ya DPP na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kimsingi kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kwanza wametoa kama appreciation kwa Wizara katika kutekeleza wajibu wake na wamekiri kabisa kwamba wanaona kazi zinazofanywa na Wizara yetu. Nawashukuru sana sana kwa eneo hili na kadri uwezo wa kifedha utakavyoendelea tutaendelea kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kuboresha miundombinu ambayo kimsingi maboresho yoyote ya miundombinu yanasababisha utoaji wa haki usiokuwa na mashaka.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama, tunao mkakati wa mpaka ifikapo mwaka 2025 kwa nchi nzima, tutakuwa tumeweka miundombinu mizuri sana. Mahakama zile ambazo ni mahakama jumuishi ambazo zipo kwenye level kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufaa kwa sasa zipo sita, lakini mpango ujao tunategemea kuweka karibu mahakama tisa nyingine zenye sura ile.
Mheshimiwa Spika, vile vile katika ngazi za Wilaya hadi kufikia mwaka 2025, tunategemea Wilaya zote nchini zitakuwa na majengo mapya kwa zile wilaya ambazo hazina majengo kabisa tutakuwa tumekamilisha kabisa uwekaji wa miundombinu ya mahakama.
Kwa upande wa Mahakama zile za Mwanzo mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba mpaka ifikapo mwaka 2025, Makao Makuu yote ya Tarafa kwa nchi nzima, tutakwenda kuweka mahakama mahali ambapo huduma hii haijafika. Kwa hiyo haya ni makubwa ambayo tunakwenda nayo.
Mheshimiwa Spika, vile vile upande wa DPP kweli kuna uhaba mkubwa kama Waheshimiwa Wabunge walivyoliona na kwa kadri fedha zitakapopatikana tunataka kukimbiza ujenzi wa ofisi kwa sababu ofisi hii itakapoimarika, ni uhakika wa kutosha kwamba na Mahakama ule ufanisi utaonekana kwa uwazi mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa, kwa sababu Mahakama haiwezi kukamilisha shughuli bila ushirikiano na DPP na vyombo vingine.
Mheshimiwa Spika, vile vile upande wa Wakili Mkuu wa Serikali naye kumuimarishia ofisi ili aweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Kwa hiyo jambo la kuimarisha miundombinu ni jambo muhimu sana na sisi tunapokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge wote na maboresho yataendelea kulingana na jinsi ambavyo tunaendelea kupata fedha au vitendea kazi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, lipo eneo lingine ambalo limeguswa na Waheshimiwa Wabunge hapa ni marekebisho ya sheria mbalimbali. Kuna Mheshimiwa ameeleza kwamba tupitie sheria mbalimbali hasa za vyama hivi kuangalia jinsi ambavyo wanaweka usawa wa kijinsia haya yote tunayapokea kwa sababu ni lazima yachakatwe.
Mheshimiwa Spika, ni wito tu kwa vyama na vyenyewe kwa sababu sheria yenyewe imetoa uhuru mkubwa sana, ni utekelezaji tu na usimamizi wa vyama vyenyewe binafsi kwenye utekelezaji wao, kwa sababu ukiangalia Chama cha Mapinduzi hakina uhaba wa akinamama katika ngazi mbalimbali za uongozi. Kwa hiyo unaweza ukaona labda ni mapungufu tu katika baadhi ya vyama ambavyo vinatakiwa vifungue milango kwa akinamama kupata ile haki sawa, hakuna mahali ambapo sheria imewanyima haki ya kugawana madaraka katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, hivyo niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na tumepokea maelekezo yao na tutakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kwa sehemu kubwa sana nitachangia kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria.
Kwanza, napenda kuunga mkono hoja lakini nipongeze Kamati zote mbili ambazo zimetoa wasilisho lake leo, na maalumu kwa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa hoja mbalimbali ambazo zimetolewa mapendekezo na maazimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Katiba na Sheria inaungana kwa ujumla wake juu ya mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hii ya Utawala Katiba na Sheria na hasa kwenye maeneo yafuatayo; moja, majengo ya Mahakama ya Mwanzo yaboreshwe kwa kufanyiwa ukarabati. Tunapokea ushauri. Vilevile, tunataka tu kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo ni ya miaka mingi sana. Mengi yamejengwa kati ya miaka ya 1950 – 1960. Mengine yamerithiwa. Mahakama hizi zote, hasa zile za majengo yasiyokarabatika, haya tunakwenda kubadili na kuyajenga majengo mapya na kasi ya ujenzi ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili lililotolewa kama ushauri kwa Serikali, Serikali ijenge majengo ya Mahakama za Mwanzo kwenye maeneo ambayo hayana Mahakama za Mwanzo. Zoezi linaendelea. Tayari Mahakama za Mwanzo zipatazo karibia 60 zilishafanyiwa kazi, na kwa kipindi hiki cha fedha 2024/2025, zinakwenda kujengwa Mahakama za Mwanzo 32 katika maeneo mbalimbli hapa nchini. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao hayajafikiwa na majengo mapya, majengo yanakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu katika eneo hili ni matumizi ya TEHAMA. Napenda tu kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge, Mahakama yetu ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa sana kwenye eneo la TEHAMA. Mtakubaliana nami, kwamba katika maeneo yote ya Mahakama ambazo zinaanzia ngazi ya wilaya kupanda juu mpaka kwenye Mahakama Jumuishi, Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria imepita kwenye majengo ambayo sasa yako kwenye TEHAMA ya kisasa kabisa. Tuwaahidi tu kwamba, kwenye Mahakama hizi za Mwanzo kadiri zinavyoendelea kufanyiwa marekebisho makubwa ya ujenzi, TEHAMA inaenda kuchukua nafasi yake kwa sababu, karibu Mahakama zote nchini hilo ndilo lengo lake la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye eneo lingine ambalo Kamati imetoa maazimia yake, ni eneo ambalo imeshauri kutumia wale wanasheria wa halmashauri hapa nchini. Ushauri wao umepokelewa ingawa utapitiwa upya kwa sababu, yule mwanasheria wa halmashauri ni mwawakilishi wa AG kama ilivyo kwa sisi hapa Bungeni. Kwa hiyo, tunakwenda kupitia yale maeneo ambayo kimsingi yasije yakaleta usumbufu kwa wananchi kwa sababu hawa wanatakiwa kuwa neutral wakati watu wawili wanapogombana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na tunashukuru sana na tunaunga mkono hoja. (Makofi
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii nami kama Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nipate nafasi ya kuchangia kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote, kwanza ndugu zangu ambao ni Wawakilishi wa Wananchi, kama kuna eneo ambalo tulikuwa tumeliacha likiendelea kutawaliwa ni hili la utoaji haki. Kwa sababu mwanzo wa matumizi ya Kiingereza katika utoaji haki ulianzia kwa Wakoloni. Nchi yetu imepata uhuru kamili na sasa tuna miaka ya kutosha kabisa katika uhuru wetu. Kwa hiyo, utaona namna ambayo kuchelewa kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji haki ilikuwa ni kuendelea kukandamizana katika maeneo ya maisha yetu ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itambulike tu kwamba sheria ndiyo msingi wa maisha. Sheria ni makubaliano ya jamii kuishi katika mfumo fulani na kuuheshimu. Sasa huwezi kuleta zile sheria na miundo hiyo kwa lugha ambayo wewe mwenyewe huijui. Waingereza walileta lugha hii kwa sababu ndiyo walikuwa wanatutawala. Sasa hata baada ya kutawaliwa, tuendelee tu kusimama kwenye eneo lao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kusema ni nini? Kiswahili kinaheshimika sana kote duniani na mtakublaiana nami kwamba kwa sasa hivi Mataifa mengi sana yamefungua TV za Kiswahili. Ukienda Ujerumani, Korea, Japan, BBC wote hawa wanatuenzi Watanzania ambao hatujajitambua thamani yetu. Sisi tunathaminika sana duniani, lakini sisi wenyewe hatujajithamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ufike na kila jambo linahitaji uthubutu. Mheshimiwa Rais asingekuwa mthubutu tungeendelea kuimba wimbo wa kuhamia Dodoma hata miaka 500 ingepita bila kufika hapa Dodoma. Sasa ifike wakati, tunataka kubadilisha miundo ya maisha yetu ili wananchi wetu ambao ndiyo wanufaika wakubwa waweze kunufaika na lugha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingi sana nimeshuhudia akina dada, akiwa mjamzito Tanzania anataka kwenda kuzalia Ulaya ili aandikishe uraia wa Ulaya. Sasa sijui ni mawazo tu ambayo mtu anakuwa nayo ya kuathirika kisaikolojia, lakini ukweli Tanzania yetu ni Tanzania ya Kiswahili. Kwa hiyo, sheria zetu zikibadilika zitawasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi migogoro ni mingi. Hapa nina judgment zilizotolewa kwenye Mahakama karibia sijui copy ngapi, wananchi hawajui namna ya kuzitafsiri, wanatafuta Mkalimani awatafsirie. Acha hao Waingereza watafute mtafsiri wa Kiswahili, siyo kazi yetu sisi tulio wengi kutafuta watafsiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini wazi mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ambayo yamelenga katika kukubaliana na wazo la Wizara, ni vizuri mkayapa nguvu ili muweze kufika mahali tuweze kukubaliana na hii hoja iliyowasilishwa na Wizara ili tuweze kufikia muafaka wa lugha ya Taifa kutumika mahali popote pale kwa ujasiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuniona, dakika saba hazitafika kwa kweli. Kwa sababu mtoa hoja atakuja kutoa maelezo yote. Nilitaka nirekebishe usemi fulani ambao usije ukanukuliwa vibaya.
Mheshimiwa Spika, hakuna sheria ambayo ilishakuwa sheria halafu ikakatwa. Serikali inachofanya ni kupeleka mapendekezo kwenye Kamati, na Kamati inapopitia yale yanayokuja hapa sasa hayana sura ya Serikali yana sura ya Kamati ya Bunge ambayo imechakata na sasa inaleta kwa ajili ya ridhaa ya Waheshimiwa Wabunge; na sasa Wabunge ndio Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Kwa hiyo hapa napo tunapata ule mchakato na mapendekezo then tunafikia kwenye muafaka wa kuitunga ile sheria ambayo inapelekwa kwa ajili ya kusainiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka tu nirekebishe hilo, kwa sababu wananchi wasije wakafikiri kwamba kuna sheria ambayo inatungwa na Serikali halafu inapelekwa Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya aina yoyote. Kwa hiyo yale mapendekezo yanapita kwenye vyombo ambavyo kimojawapo ni Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, inapitia mawazo ya Serikali juu ya kutunga ile sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nilisemee tu hilo, lakini vinginevyo niwapongeze wajumbe wote ambao wametoa mawazo yao. Na kimsingi kwa sehemu kubwa sana nimeona mengi ni yale ambayo vilevile kamati imependekeza yafanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kwanza kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali ambayo ni ya kulijenga Taifa jipya. Nimesikiliza michango yote ya Waheshimiwa kutoka mwanzo mpaka msemaji wa mwisho, wote wameunga hoja mabadiliko ya hii sheria ambayo imekuja kurekebisha sheria mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kwa niaba ya Wizara na kwa niaba ya Waziri kuwashukuru sana kwa mshikamano ambao tumeupata toka wakati tumeanza haya mawazo ya kufanya mabadiliko kwenye hizi sheria na daima sheria zinapofanyiwa marekebisho, zinakuwa zimeangaliwa kutokana na matokeo ya matumizi yake kule kwenye maeneo ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hizi sheria zote ambazo sasa tunakwenda kuzipitisha leo, ninaamini zitaisaidia nchi hii sasa kwa wakati tulionao huu kwenda kwa kasi ya ajabu. Ni kweli kulikuwa na masumbuko mengi sana kwenye hizi Mahakama zetu, hasa kwenye maeneo ambayo kimsingi yalilenga katika suala zima la upelelezi; yaani upelelezi unakaa muda mrefu, watu wanasumbuka na kadhalika. Haya yote yanayokuja hapa, mnaona kabisa kwamba yanakwenda kutatua tatizo la watu kulundikana magerezani na hili litakwenda kujenga sura mpya ya utoaji haki kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda tu kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia kutoka maeneo mbalimbali na kwa kweli tutayazingatia baadhi ya mambo ambayo kidogo mmetoa maoni na kadhalika, na pia sheria yenyewe kimsingi mmeikubali na Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli niliona nisimwachie tu AG akatoa majumuisho bila na mimi kwa niaba ya Wizara kuyasemea haya na kuwashukuru sana kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, nami naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)