MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo pale ambapo Serikali haina eneo la kufanya miradi hiyo hasa hasa miradi kama ya shule, hospitali au kupanua maeneo ya jeshi au uwekezaji, na baada ya kuchukua maeneo hayo hufanyiwa tathmini ili watu waweze kulipwa fidia. Hata hivyo kumekuwa na tatizo la ucheleweshaji wa kulipa fidia na sehemu nyingine kuingia hata mambo yasiyokuwa ya uaminifu katika utekelezaji wa ulipaji wa fidia.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini msimamo wa Serikali katika jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’enda, Mbunge wa Manispaa ya Kigoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa Serikali wa kuchukua maeneo mbalimbali ya ardhi yetu, kwa ajili ya miradi ya maendeleo pale ambapo tunaona tunahitaji kutekeleza mradi maalum kwa maslahi ya Watanzania na kwa hili naomba nianze kueleza umma wa Watanzania kuwa ardhi yetu hii ni ya umma na Mheshimiwa Rais, ndio mdhamini wa ardhi hii. Mheshimiwa Rais anaweza kuchukua ardhi popote kwa maslahi ya umma, kwa lengo la kutekeleza mradi ambao unaweza kusaidia jamii ya eneo hilo kuutumia vizuri. Lakini tunapochukua ardhi hiyo huwa tunafanya tathmini ili kulipa fidia ya mali iliyoko kwenye ardhi, inaweza kuwa labda nyumba au mazao, lazima yafanyiwe tathmini.
Mheshimiwa Spika, ni kweli mara kadhaa Serikali tumekuwa tukichukua maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya miradi ya umma na tunapokuta kuna mali imewekezwa na mtanzania huwa tunalipa fidia.
Sasa suala la ucheleweshaji ni taratibu vigezo kama havijakidhi; moja, wakati tunafanya zoezi la tathmini ni lazima tufahamu nani hasa yuko hapo na amewekeza hiyo na lazima kuwe na viambata vinavyoeleza kwamba huyu ndio mwenye eneo hili na tunampiga na picha, thamani inatambulika hapo hapo na yeye anatambua thamani yake halafu maandalizi ya kulipa fidia yanafanywa.
Mheshimiwa Spika, ucheleweshwaji unakuja kama zoezi hilo halijakamilika au kuna migogoro ya wao kwa wao, wanagombania eneo hilo kwa umiliki, hapo inaweza kuchelewa, na wakati mwingine tathmini na idara inayolipa labda kama ilikuwa inategemea bajeti kunaweza kuwa na- delay, lakini niendelee kuwahakikishia Watanzania ambao wanafikiwa maeneo yao kwa ajili ya tathmini, kwa ajili ya kutumika kwa miradi na tunafanya tathmini kama kunachelewa. Hakuna Mtanzania, hakuna mwananchi ambaye anachukuliwa ardhi na huku akiwa amewekeza, tukafanya tathmini akakosa stahiki yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali itaendelea kusimamia maeneo hayo na kama yako maeneo labda pale Kigoma kuna eneo ambalo tathmini ilishafanyika na bado hatujalipa kutakuwa na moja kati ya haya niliyoyasema; au kuna migogoro, labda idara ilifanya tathmini hiyo na ilikuwa haijajiandaa na kama haijajiandaa tunarudi kwenye sheria yetu ile ya kwamba toka siku ya tathmini mpaka siku ya malipo ikiwa zaidi ya miezi sita lazima ifanyike tathmini tena ili kujua thamani halisi ya wakati huo ili sasa kuwezesha idara, lakini wananchi kujipanga kwa ajili ya kupata fidia yao.
Mheshimiwa Spika, hayo ndio maelezo sahihi ya Serikali ambayo yanatumika wakati wote tunaopohitaji kuchukua eneo na kufanya tathmini na kulipa wananchi. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sera yetu ya viwanda hapa nchini imetuwezesha kupata viwanda vingi sana na kuwafanya Watanzania watumie bidhaa nyingi ambazo zinatengenezwa hapa nchini. Hata hivyo, sera hii bado haijapiga hatua kubwa katika viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi. Tunataka tuone viwanda vya maziwa, vya nyama, tunataka kuona viwanda vya kusindika samaki, dagaa, na viwanda vya kusindika matunda.
Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza viwanda vya kusindika au kuongeza thamani ya mazao ya wakulima? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’enda Kilumbe, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imeendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwawezesha Watanzania wanaojishughulisha kwenye sekta zote zinazozalisha mali na kuongeza uchumi, kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ili mapato yawe makubwa zaidi ikiwemo na sekta ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika, sekta hizi zimekuwa na manufaa makubwa kwa sababu sekta hizi ndiyo zina uwezekano wa kuwa na viwanda vingi kwa sababu zinakuwa na malighafi nyingi, na kwa hiyo, mkakati wa Serikali kuongeza viwanda zaidi ya viwanda tulivyonavyo, ni kuhakikisha kuwa na hili tumeshalifanya la kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ili kuweza kuwavutia wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda, awe Mtanzania au yeyote kutoka nje ya nchi kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, pia tumefungua wigo wa kuhakikisha kuwa, wawekezaji wote wanapokuja nchini tunawahakikishia uwekezaji wao kuwa salama. Kwa hiyo suala la usalama kwa wawekezaji wetu tumelipa nafasi kubwa ili kuwakaribisha walio wengi sana. Hata hivyo, tumeimarisha miundombinu inayowawezesha wafanyabiashara wanaotaka kujenga viwanda kuendesha viwanda vyao na kupata faida, kama vile barabara na Watanzania mnaona barabara zote nchini zimejengwa na zinaendelea kujengwa, reli lakini pia njia ya anga, tumeshanunua na ndege ya kupeleka mazao nje ya nchi. Hii yote ni kuvutia wawekezaji wetu, hata pia ukanda wa bahari na maziwa tumeongeza meli ili kuwezesha kusafirisha bidhaa zao kwa ajili ya kufuata masoko. Uboreshaji wa mazingira haya ya miundombinu unamuwezesha kumpa uhakika muwekezaji kujenga kiwanda popote nchini ili aweze kutumia malighafi tulizonazo aweze kufanya biashara yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tulikuwa tunaangalia wafanyabiashara wengi, wawekezaji wengi wa viwanda wanakwazwa wapi? Tukagundua kwamba tulikuwa na tozo nyingi sana za uwekezaji. Tumepunguza tozo ili kumuwezesha yeye kufanyabiashara na kupata faida na bado mkakati wetu wa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya uwekezaji wetu unafanywa kuvutia wawekezaji hao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe wito tena kwa Watanzania wenye uwezo kujenga viwanda ndani ya nchi, malighafi tunazo kwa sababu Sekta ya Kilimo imepata mabadiliko makubwa, Mifugo nako pia tuna malighafi za kutosha na uvuvi nako pia tumeimarisha uvuvi bora na wa kisasa kwa lengo la kupata malighafi nyingi za kuendesha kwenye viwanda vyetu, lakini pia tunajaribu kuhakikisha kwamba tuna tunasikiliza kero za wawekezaji. Hii inatoa fursa sasa ya Mwekezaji kufanya maamuzi kuja nchini na ndiyo kwa sababu wakati wote tumekuwa na maonyesho ya viwanda, maonyesho ya kilimo ili kuwahakikishia kwamba viwanda vina nafasi vilivyopo na vile ambavyo vinakuja, lakini kwenye maonesho ya mazao kuonesha uwepo wa malighafi hapa nchini. Tunaendelea kufanya haya kwa kutoa wito na kufanya maboresho ya maeneo yote niliyoyatamka ili kukaribisha viwanda zaidi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mpango wetu ambao tunao wa kuwezesha kuongeza viwanda viweze kuleta faida nchini na sisi tunaamini kwamba tukiwa na viwanda kwanza tunatengeneza ajira kwa Watanzania, mbili, tunapata kodi ya hawa wawekezaji wanalipia, tatu tunahakikisha kuwa huduma mbalimbali zinazohitajika viwandani wale majirani wananufaika nazo. Hayo yote ni manufaa ambayo tunayapata na kwa hiyo wito wako uliotokana na swali lako, tutaendelea kuusimamia na kuyasimamia hayo maboresho tunayoyafanya kwa lengo la kuvutia wawekezaji zaidi wa kujenga viwanda hapa nchini. Ahsante sana. (Makofi)