Primary Questions from Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda (12 total)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa bandari kavu inayojengwa Katosho Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bandari Kavu ya Katosho Kigoma ni kituo kilichosanifiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya kuhudumia tani laki tano (500,000) kwa mwaka ili kusaidia kampuni za usafirishaji kuhifadhi makasha kwa muda kabla na baada ya kusafirishwa ndani au nje ya nchi kupitia Bandari ya Kigoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa upitishaji wa shehena katika bandari ya Kigoma umekuwa ukiongezeka kutoka wastani wa tani 180,000 hadi 200,000 kwa mwaka. Hata hivyo, ongezeko hili la upitishaji wa shehena katika bandari hiyo ni chini ya asilimia 50 ya uwezo uliosanifiwa wa kupitisha tani 700,000 kwa mwaka katika bandari hiyo na hivyo kuifanya bandari Kavu ya Katosho Kigoma kutokuwa na matumizi ya kuweza kusaidia bandari ya Kigoma kwa kuwa bado haijaelemewa katika kuhudumia shehena iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, TPA imekwishalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma yenye ukubwa wa hekta 69 na kazi ya ujenzi wa uzio kwa eneo lote la bandari hiyo imekamilika. Usanifu wa ujenzi wa sakafu ngumu na majengo ya huduma umekamilika na tutaanza kuijenga kwa awamu kuendana na ongezeko la upitishaji wa shehena kuanzia mwaka ujao wa fedha (2022/ 2023). Aidha, uendelezaji wa Bandari Kavu ya Katosho Kigoma upo katika Mpango Kabambe wa TPA kwa mwaka 2009 hadi 2028.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
(a) Je, nini matokeo ya Utafiti wa mafuta uliofanyika katika Ziwa Tanganyika zaidi ya miaka mitatu iliyopita?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuvuna mafuta hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, lenye sehemu
(a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika umegawanywa katika vitalu viwili; Kaskazini na Kusini. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016, TPDC ilikusanya taarifa za uvutano wa usumaku zenye jumla ya urefu wa kilomita 24,027 za mstari katika kitalu cha Ziwa Tanganyika Kaskazini. Tathmini ya taarifa hizo pamoja na taarifa za kijiolojia na kijiofizikia zilizopatikana katika eneo la mradi zimewezesha kugundua na kutenga maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa mashapo ya kuhifadhi rasilimali (petroleum).
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo Nchini (TPDC) kwa kushirikiana na Mwekezaji kutoka Kampuni ya Beach Petroleum ilifanya utafiti wa mafuta katika kitalu cha Ziwa Tanganyika Kusini kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2017. Taarifa za utafiti huo ziliwezesha kubaini miamba yenye uwezekano wa kuhifadhi mafuta. Hata hivyo, changamoto za uchimbaji kisima katika Ziwa Tanganyika zilizomkabili Mwekezaji alishindwa kusafirisha vifaa vya kuchoronga kutokana na kina kirefu cha maji katika Ziwa Tanganyika na upatikanaji wa fedha zilisababisha Mwekezaji kushindwa kuendelea na utafiti na hivyo kulazimika kurudisha kitalu kwa Serikali mnamo mwaka 2017 kwa kuzingatia sheria zetu za mafuta na gesi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa viashiria vizuri vya mafuta katika vitalu vya Ziwa Tanganyika, mpaka sasa Serikali haijagundua mafuta wala gesi katika eneo hilo. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 TPDC inatarajia kuendelea kufanya tathmini ya kina ya takwimu za usumaku kwa Kitalu cha Ziwa Tanganyika Kaskazini. Takwimu hizi zitatumika kutengeneza mpango wa kukusanya takwimu za mitetemo kwa ajili ya kuainisha na kuhakiki uwepo wa mashapo ya kuhifadhi mafuta na gesi. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaendelea na matengenezo ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma uliosimama kwa muda wa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kazi ya matengenezo ya Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma yatafanyika kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, matengenezo yalisimama kwa sababu Mfadhili alichelewa kutoa idhini ya kumpata Mkandarasi atakakayetekeleza kazi hizo. Kwa sasa, idhini (No Objection) imeshatolewa.
Mheshimiwa Spika, mfadhili wa mradi huu ameshatoa fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu. Kwa sasa rasimu ya Mkataba imepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya mapitio.
Meshimiwa Spika, mara baada ya taratibu za vetting kukamilika na Mkataba kusainiwa, utekelezaji wa kazi za matengenezo ya upanuzi wa mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma utaanza. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kuboresha usafiri wa reli ya Kigoma-Dar es Salaam ambao unafanya safari mara mbili kwa wiki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shaban Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) linafanya safari mbili kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na hii ni kutokana na uhaba wa mabehewa ya abiria. Ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa, Shirika lilianza taratibu za kukarabati mabehewa 37 ambapo mwezi Juni, 2021 ulisainiwa mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa hayo. Vipuri hivyo vinatarajiwa kuingia nchini mwishoni mwa mwezi Aprili, kwa maana ya mwaka 2022 na mara vitakapowasili kazi ya ukarabati itaanza. Kazi hiyo ya ukarabati inatarajiwa kufanyika kwa muda wa miezi nane hadi Desemba, 2022 kupitia mafundi wetu wa ndani.
Aidha, Shirika limesaini Mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya ya abiria 22. Mabehewa hayo yanatarajiwa kuingia nchini mwezi Septemba, 2022.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Kilumbe Shaban Ng’enda pamoja na wananchi wa Kigoma kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria. Baada ya utekelezaji wa kazi hizo, idadi ya safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma zitaongezeka kutoka safari mbili hadi nne kwa wiki.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, nini matokeo ya utafiti wa mafuta uliofanyika katika Ziwa Tanganyika na lini mafuta yataanza kuchimbwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma, Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika umegawanyika katika vitalu viwili ambavyo ni Kitalu cha Kaskazini na Kusini. Kitalu cha Kaskazini kina ukubwa wa kilomita za mraba 9,430 ambapo mwaka 2015/2016, TPDC iliweza kukusanya, kuchakata na kutafsiri taarifa za uvutano wa sumaku ili kugundua maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa mashapo ya kuhifadhi mafuta. Kitalu cha Kusini kina ukubwa wa kilomita za mraba 7,163 ambapo TPDC kwa kushirikiana na Mwekezaji - Kampuni ya Beach Petroleum waliweza kukusanya, kuchakata na kutafsiri taarifa za uvutano wa sumaku ili kubaini maeneo yenye uvutano na uwezekano wa kuhifadhi mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo kwa viashiria vizuri vya uwepo wa mafuta katika vitalu vya Ziwa Tanganyika, matokeo ya mwisho kuhusu uwepo wa mafuta katika Ziwa hilo bado hayajapatikana kwa kuwa kazi ya utafiti bado inaendelea. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali haijazikarabati Meli za MV Liemba, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zimesimama kufanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kukarabati meli za MV. Liemba, MV Mwongozo na MV Sangara ili kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji katika Ziwa Tanganyika. Ili kufikia azima hiyo, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inaendelea na ukarabati wa Meli ya MV Sangara ambapo kwa sasa kazi hiyo imefikia asilimia 90.7 na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia MSCL ilikamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV Liemba tarehe 5 Machi, 2023 na kwa sasa MSCL inaendelea kufanya majadiliano na mkandarasi kabla ya kusaini mkataba. Mkataba wa ukarabati wa meli hiyo unatarajiwa kusainiwa Juni, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuhusu Meli ya MV Mwongozo ambayo ilisimamishwa kutokana na changamoto ya msawazo (stability), MSCL inakamilisha taratibu za kumwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili kufanya tathmini ya kina na kuishauri Serikali ipasavyo. Mhandisi Mshauri anatarajiwa kuanza kazi hii mwezi Juni na kukamilisha mwezi Novemba, 2023. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza:-
Je, hatua zipi zimechukuliwa kuhusu Itifaki ya Forodha kati ya Tanzania na DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, DRC imeshawasilisha hati ya kukubali kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha (Instrument of Ratification) kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, DRC inaendelea na mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria zake za ndani ili ianze kutumia Sheria ya Pamoja ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilisha mchakato huo, DRC itafanya vikao na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukubaliana kuhusu utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa utekelezaji (road map) ili kujua lini itaanza utekelezaji wa Itifaki ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ili kiwe Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na kiweze kutoa taaluma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea na jitihada za kukiendeleza Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kuwa Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tayari andiko kwa maana ya dhana concept note kuhusiana na ushirikiano huo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (NMTC) na kuwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ahsante
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ili kiwe Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na kiweze kutoa taaluma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea na jitihada za kukiendeleza Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kuwa Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tayari andiko kwa maana ya dhana concept note kuhusiana na ushirikiano huo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (NMTC) na kuwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza:-
Je, maombi mangapi ya usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini yamewasilishwa tangu 2016 na hazijapatiwa usajili na sababu za kutosajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi Septemba, 2023, jumla ya maombi ya Usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini 1,858 yalipokelewa katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Kati ya maombi yaliyopokelewa, Taasisi na Madhehebu ya Dini 419 yamesajiliwa, maombi manne yamekataliwa na maombi 1,435 yapo katika hatua mbalimbali za usajili. Sababu zinazosababisha baadhi ya Taasisi na Madhehebu ya Dini kuchukua muda mrefu kusajiliwa au kotosajiliwa ni pamoja na baadhi ya Taasisi na Madhehebu ya Dini kukosa vigezo vya kusajiliwa, kubadili anwani za Posta au Makao Makuu ya Taasisi bila kutoa taarifa na hivyo kukosekana kwa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baadhi ya Taasisi na Madhehebu kukosa maeneo stahiki ya kuendeshea shughuli zao na kuingia katika migogoro ya ndani, migogoro na jamii inayozunguka taasisi hizo au Mamlaka za Serikali zilizopo katika maeneo hayo au kukabiliwa na kesi katika mamlaka za utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, inaendelea kushughulikia maombi ya Usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini na kutoa usajili kwa wakati kwa taasisi zenye sifa stahiki na kuhakikisha kuwa Serikali haisajili taasisi na Madhehebu ya Dini ambayo yanaweza kuleta madhara kwa jamii au kuhamasisha vitendo ambavyo ni kinyume cha mila, desturi, utamaduni na maadili ya Kitanzania, nashukuru.
MHE. KILUMBE S. NG`ENDA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ukarabati wa Reli ya Kati kwa kuwa miundombinu yake ni chakavu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TRC inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya njia ya reli iliyopo ambapo hadi sasa imekamilisha ukarabati wa njia ya reli kipande cha Dar es Salaam – Isaka ya Kilometa 970 kupitia mradi wa Tanzania Intermodal Rail Project (TIRP). Halikadhalika, TRC imesaini mkataba wa ukarabati wa njia ya reli ya kati kwa kipande cha Tabora – Kigoma yenye urefu ya kilometa 411 tarehe 23 Juni, 2023 na Kaliua – Mpanda ya kilometa 210 tarehe 26 Novemba, 2022. Kazi ya ukarabati inaendelea, na kwa upande wa Tabora – Kigoma ya kilometa 411 inatarajia kukamilika baada ya miezi 54 na Kaliua – Mpanda inatarajia kukamilika mwezi Mei, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo TRC imesaini mkataba wa ununuzi wa malighafi za ukarabati wa reli (mataruma na vifungio) kwa ajili ya ukarabati wa njia ya reli ya Kaskazini ikijumuisha kipande cha Ruvu – Mruazi Junction.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, nini sababu ya ucheleweshaji wa maombi ya usajili wa taasisi za kidini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kupewa usajili wa kudumu, taasisi na madhehebu ya dini huwekwa katika kipindi cha matazamio ili kubaini kama taasisi au dhehebu husika lina dosari yoyote kwa jamii. Hata hivyo, zipo sababu nyingine ambazo huweza kupelekea baadhi ya taasisi na madhehebu ya dini kuchukua muda mrefu kusajiliwa ambazo ni pamoja na kushindwa kutekeleza maelekezo yanayohusu usajili yanayotolewa na Ofisi ya Msajili kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia ofisi ya Msajili wa Jumuiya inaendelea kushughulikia maombi ya usajili wa taasisi na madhehebu ya dini na kutoa usajili kwa wakati kwa taasisi zenye sifa stahiki, ahsante.