Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Nashon William Bidyanguze (15 total)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani kuhusu kujenga daraja katika Mto Maragalasi Ilagala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja katika Mto Maragalasi katika eneo la Ilagala liko katika barabara ya Mkoa wa Kigoma (Simbo – Ilagala – Kalya) yenye urefu wa kilometa 235. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 345 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa kutambua umuhimu wa daraja husika kwa wananchi, hususan wa Mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani, baada ya kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali imejipanga kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza na kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini watumishi waliohamishiwa Halmashauri ya Uvinza kutoka Halmashauri ya Kigoma Vijijini watalipwa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya Uvinza ina watumishi 99 wanaostahili kulipwa stahiki za uhamisho kufuatia kuhamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza katika mwaka wa fedha 2013/2014. Kiasi cha shilingi milioni 319.89 kinahitajika ili kulipa madeni hayo ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imezielekeza Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuanza kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kulipa madeni na stahili za watumishi. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki madeni ya watumishi na kuyalipa kwa kadri wa upatikanaji wa fedha.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara tatu za Lukoma – Lubalisi, Kalya – Ubanda na Kalya – Sibwesa zinazounganisha Mkoa wa Kigoma kupitia Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, asante sana; kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 barabara za Lukoma - Lubalisi, Kalya - Ubanda na Kalya - Sibwesa zilitambuliwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kuwekwa kwenye mfumo wa barabara zinazotambuliwa na TARURA (DROMAS). Barabara hizo zitaingizwa kwenye mpango wa matengenezo ya barabara kupitia fedha za matengenezo ya barabara zinazotolewa kwa TARURA katika kila Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wananchi pamoja na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji la Kuendeleza Kilimo – Kigoma (SAKIRP) inaendelea na ujenzi wa madaraja 10 kwa kutumia teknolojia ya mawe kwa gharama ya shilingi milioni 190 ambapo madaraja matatu yamekamilika likiwemo Daraja la Mto Ruega katika barabara ya Kalya – Ubanda lililojengwa kwa shilingi milioni 37 katika mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti zake ili kuzifanyia matengenezo barabara hizo kwa kadiri upatikanaji wa fedha utakavyoendelea kuimarika.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga mnara wa mawasiliano ya simu katika Kata ya Mtego wa Noti ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa kutembelea Kata ya Mtego wa Noti mnamo tarehe 19 Disemba, 2021 na kubaini kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata hiyo.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mtego wa Noti imeainishwa ili kuingizwa katika zabuni ijayo ya kufikisha huduma za mawasiliano ya simu inayotarajiwa kutangazwa katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Aidha, ujenzi wa mnara huo utaanza mara baada ya kupatikana mtoa huduma na hivyo wananchi wa kata hiyo watarajie kupata huduma za mawasiliano ya simu mara baada ya kukamilika ujenzi huo, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Mwekezaji wa Kiwanda cha Saruji katika Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Vieanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhamasisha na kuvutia wawekezaji ikiwemo kwenye sekta ndogo ya saruji. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kimeweza kuvutia mwekezaji (Itracom Fertilizers Company Limited) kujenga kiwanda cha saruji na tayari tumeshampa ekari 47 katika Eneo la Uwekezaji la Kigoma (KiSEZ). Wilaya ya Uvinza pia itanufaika na mwekezaji huyu. Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji zaidi ili kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma ikiwemo Wilaya ya Uvinza. Nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX K.n.y. MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji Kata ya Kazuramimba?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Maji wa Kata ya Kazuramimba ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 90. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu kilometa 3.3, ulazaji wa mabomba ya usambazaji Kilometa 26.7 na ujenzi wa tanki la ukubwa wa lita 470,000. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba, 2022.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga majengo katika Kituo cha Afya Nguruka kilichopandishwa hadhi ya kuwa Hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Nguruka kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma kinahudumia wakazi wapatao 135,546. Kituo kinatoa huduma kwa ngazi ya kituo cha afya kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imekwisha jenga hospitali mpya ambayo imeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, kituo hiki kina uhitaji wa majengo mbalimbali ya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na wodi mbili za kulaza wagonjwa, kliniki ya mama na mtoto, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la kufulia.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 kituo hicho kimetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo itakayowezesha kutoa huduma kwa ngazi ya kituo cha afya. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Simbo - Kalya yenye urefu wa km 234?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Simbo – Kalya yenye urefu wa kilometa 234 kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Lower Malagarasi ambalo lipo katika barabara hii. Kazi za usanifu zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika Novemba, 2023. Baada ya usanifu kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja na kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Simbo hadi Kalya, yenye urefu wa kilometa 234, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Simbo hadi Ilagala?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Simbo – Ilagala – Kalya yenye urefu wa kilometa 234 imeanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Lower Malagarasi ambalo lipo katika barabara hii na kazi zinatarajiwa kukamilika Disemba, 2023. Kuhusu usanifu wa barabara hiyo, Serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Mheshimiwa Mbunge tumemtengea shilingi milioni 100 ili kufanya kazi hiyo.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, lini Serikali itashawishi mabenki kufungua benki nchini Congo DRC katika Miji ya Kalemie na Uvira ili kurahisisha biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo Mei, 2021 Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iliipa Benki ya CRDB kibali cha kufungua kampuni tanzu Lubumbashi, nchini Congo ambapo inatarajia kuanza kutoa huduma za kibenki mara tu itakapopewa leseni na Benki Kuu ya nchi hiyo ya Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkakati wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa mwaka 2023 - 2028 unaonesha kuwa benki hiyo inatarajia kufungua kampuni tanzu zitakazotoa huduma za kibenki kwenye Miji ya Bukavu, Uvira na Kalemie nchini Congo. Hivyo, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa benki za biashara za hapa nchini kuanzisha kampuni tanzu nje ya nchi ili kusambaza huduma za kibenki katika nchi mbalimbali kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya nchi na nchi, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudisha huduma za Mahakama za Mwanzo katika Kata ya Kalya Buhingu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama inaendelea na mipango ya kufanya ujenzi na tayari huduma imerejeshwa kuanzia mwezi Julai, 2022 na mpaka sasa wapo watumishi wanatoa huduma kwa kutumia Ofisi za Kata. Kuanzia mwezi Julai 2022 huduma iliporejea hadi Machi, 2023 jumla ya mashauri 38 yamesajiliwa na kusikilizwa katika Mahakama hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa ujenzi wa Mahakama, tumepanga kujenga Mahakama ya Mwanzo Mgambo mwaka 2024/2025, ambapo ndiyo Makao Makuu ya Tarafa ya Buhingu. Hivyo, tunatajarajia kuwa wananchi wa Kalya watapata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Mgambo. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Uvinza katika eneo la Lugufu baada ya eneo hilo kupimwa na kupata hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza ni moja ya miradi ya Mahakama inayotekelezwa katika kipingi mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia programu ya maboresho ya Mahakama. Mkandarasi wa ujenzi wa Mahakama hii amepatikana ambaye ni Lucas Construction na kukabidhiwa eneo la ujenzi mwezi Oktoba, 2021. Kazi za ujenzi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Julai, 2022.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ahadi ya shilingi milioni 10 za ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kazuramimba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Kazuramimba. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ilitenga shilingi millioni 158 na kuendeleza ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo ujenzi wake upo katika hatua za ukamilishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia vyanzo mbalimbali na kuhakikisha inajenga na kukamilisha vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati kote Nchini kikiwemo kituo cha Afya Kazuramimba, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka fedha kukamilisha mradi wa Maji uliokwama kwa muda mrefu Kijiji cha Nyanganga Kata ya Kazuramimba – Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Maji ya Kijiji cha Nyanganga iliyopo Kata ya Kazuramimba, Wilaya ya Uvinza ilijengwa mwaka 1994 kwa lengo la kuhudumia wananchi 4,378 kwa wakati huo. Kwa sasa mahitaji ya maji katika kijiji hicho yameongezeka na kufikia lita 178,340 kwa siku, kutokana na ongezeko la watu kufikia 8,917 mwaka 2024 sambamba na kuchakaa kwa miundombinu ya maji ya Skimu hiyo iliyodumu kwa takribani miaka 30 sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto hiyo, Serikali itakarabati Skimu ya Nyanganga kupitia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, ili kurejesha ufanisi wake wa kuhudumia wananchi wa kijiji hicho. Kazi zinazotarajiwa kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ukarabati wa tanki lenye ujazo wa lita 150,000, ukarabati wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 3.2 na ukarabati wa vituo 10 vya kuchotea maji. Kazi ya ukarabati wa skimu hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika Oktoba, 2024. (Makofi)