Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nashon William Bidyanguze (28 total)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini pia naomba nimuulize swali kwamba eneo lile ni eneo ambalo lina watu wengi kwa maana kata sita katika ukanda ya maji na wakati mwingine kivuko kilichopo huwa kinasombwa na maji kupelekea wananchi wale wanaathirika kwa muda mrefu zaidi na eneo lile lina vituo viwili vya afya ambavyo vina ambulance mbili.

Kwa hiyo, naomba Serikali ione namna ya kufanya haraka katika kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Jimbo la Kigoma Kusini katika maeneo yale ya kata sita wanapata ufumbuzi wa jambo hili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Nashon kwa kufuatilia jambo hili la barabara hii ya Ilagala. Niseme tu mimi Mkoa wa Kigoma nimefanyakazi na barabara hii naifahamu sana, ni kweli anachosema na ndiyo maana Serikali imeamua kutengeneza hili daraja ili kuondokana na adha hii.

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea tayari Serikali iko kwenye hatua ya manunuzi ya kufuata Mhandisi Mshauri ambayo inasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kusombwa na vivuko ni kweli kwamba kwenye daraja hili huu mto Maragalasi ni mto wenye zaidi ya kilometa 300 kwahiyo inawezekana kivuko hiki kinapata changamoto kwasababu ya magogo ambayo yanasombwa na mito na ndiyo maana usiku kivuko hiki huwa hakifanyikazi ila tu kinafanyakazi kunapotokea emergency.

Kwa hiyo tutaendelea na utaratibu huo huo lakini tutahakikisha kwamba hiyo barabara hilo daraja linakamilika mara mara fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa NaibU Spika, Waziri haoni kwamba kwa namna moja au nyingine anasababisha watumishi hawa kufanya kazi katika mazingira magumu na hasa muda ni mrefu maana Halmashauri ile imeanzishwa mwaka 2013 na tayari kuna baadhi ya watumishi wamekwishastaafu. Kwa hiyo naomba commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo hili hawa wananchi wapiga kura wangu wanakwenda kulipwa lini fedha hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kusema katika majibu yangu ya msingi kwamba tunatambua madeni ya watumishi wetu katika Halmashauri ya Uvinza na Serikali imeendelea kuweka mipango kwa maana ya kutenga fedha kwenye bajeti ili kuhakikisha kwamba hayo madeni yatakwenda kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni haya yanalipwa kwa kutumia fedha za matumizi mengineyo kwa maana ya OC, lakini pia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Na hivyo tunaendelea kuwaelekeza Wakurugenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwa muktadha huu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza waanze kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa watumishi wale madeni yao kwa awamu ili watumishi wale sasa waweze kufanya kazi kwa kuwa na motisha kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na Serikali pia inaendelea kufanya uhakiki wa madeni hayo na kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunawalipa wale watumishi stahiki zao za yale madeni.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri yaliyotolewa mbele hapa, lakini ninalo swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Kigoma Kusini linao urefu wa barabara hii ya Simbo kwenda Kalya ndio hiyo ambayo inazalisha hizo barabara tatu nilizozisema. Barabara ya Kalya kwenda Sibwesa inatoka nje ya nchi kwa sababu kuna bandari pale Sibwesa, lakini barabara hii pia ya Lubalisi inatoka nje ya mkoa na hii ya Kalya – Ubanda inatoka nje ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iangalie kuweza kuipa kipaumbele barabara hizi kwa sababu zinaufungua mkoa kupitia Halmashauri ya Kigoma Kusini kwa maana ya Jimbo la Kigoma Kusini, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichoomba ni kwamba Serikali tuizingatie ile barabara na mimi nipokee ombi lake kwa sababu tumeshakiri katika jibu letu la msingi kwamba moja hiyo barabara tumeitambua na kuiingiza katika mpango. Awali TARURA wakati inaanzishwa tulikuwa tulikabidhiwa barabara zenye urefu wa kilometa 108,000; kwa hiyo sasa hivi kuna ongezeko la barabara karibu 36,000 mpya.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa barabara hizo ambazo zimetambulika ni pamoja na hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge umeziainisha. Kwa hiyo, kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na tutakavyoendelea kuziweka katika mpango basi barabara hiyo tutaipa kipaumbele katika mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru pia kwa Serikali kutoa majibu mazuri lakini bado naomba niulize swali moja la nyongeza.

Katika Vijiji vya Ilalangulu, Chagu, Katumba na Songambele ni maeneo ambayo yanazungukwa na msitu wa Halmashauri na ambao msitu ule wakati mwingine wananchi wanapata shida ya kutekwa na hivyo kukosa mawasiliano.

Naomba Serikali itoe majibu kwamba ni lini hasa hawa wananchi nao wataweza kupata nafuu ya kupata mawasiliano kwenye vijiji vyao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi na pia kwa maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara 61(j) ni haki ya msingi kwa kila wananchi wanaoishi ndani ya nchi yetu kupata mawasiliano; hivyo tunaamini kabisa kwamba baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha ukubwa wa tatizo tutaenda kuchukua hatua na kuhakikisha kwamba wanafikishiwa mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika maeneo ambayo yako pembezoni na maeneo ambayo ni ya mbuga tunaamini kwamba katika mkataba huu ambao Mheshimiwa Waziri anaenda kuusimamia ili usainiwe maeneo 90 yanaenda kupata utatuzi wa changamoto wa mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara 90. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira kipindi ambacho Serikali itakuwa tayari basi tutahakikisha kwamba mawasiliano katika eneo hilo itakuwa imetatuliwa ahsante sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini pia ninalo swali moja la nyongeza; kwamba, Uvinza ndipo kunapopatikana malighafi ya kutengeneza saruji. Sasa nataka nijue Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba, kiwanda hicho kinajengwa ili wananchi waweze kupata ajira ya muda mfupi, lakini na muda mrefu na ili tuweze kukamata soko la DRC na Burundi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mbunge kwa kufuatilia. Amekuwa anafuatilia sana kuhusiana na ujenzi wa kiwanda katika Wilaya ya Uvinza, lakini mkakati wa Serikali ni kuendelea kuboresha miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji zaidi katika ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi sasa hivi Kigoma itaenda kufunguka kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, anaunganisha gridi ya Taifa ya umeme katika Mkoa huo. Maana yake hii ni miundombinu wezeshi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Kwa hiyo, tunaamini kwa uboreshaji wa miundombinu hii wezeshi, pamoja na barabara tutavutia wawekezaji zaidi ambao watakuja kujenga pia katika Wilaya ya Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kufanya juhudi za makusudi ili kuvutia wawekezaji zaidi ambao watajenga viwanda katika ukanda huo wa ziwa ili kushika soko katika nchi za jirani, kama alivyosema. Nakushukuru sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa kujenga Chuo cha VETA pale Uvinza.

Sasa nauliza; ni lini chuo kile kitafanya kazi ili watoto wa pale waweze kuanza kuingia chuoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna vyuo vyetu 25 vya Wilaya ambavyo tulianza ujenzi wake toka mwaka 2021 na ujenzi ule uko kwenye hatua za mwisho. Hivi sasa tunatengeneza samani au tunasambaza samani pamoja na vifaa vya kufundishia. Ni matarajio yetu katika mwaka ujao, 2023 vyuo hivi 25 vya Wilaya pamoja na vile vinne vya mikoa vitaanza kutoa mafunzo rasmi. Nakushukuru.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi cha Wilaya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Wilaya ya Uvinza ni miongoni mwa wilaya mpya ambazo hazina vituo vya polisi, na kwa hiyo katika mkakati wetu wa kuhakikisha mikoa na wilaya zote ambazo hazina vituo vinajengewa vituo hivyo Uvinza ni eneo mojawapo litakalo zingatiwa katika ujenzi wa vituo vipya vya polisi.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Kata ya Kazuramimba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi yote ambayo ipo kwenye utekelezaji, tunaendelea kwa kasi nzuri sana kuhakikisha inaisha ndani ya wakati. Mheshimiwa Mbunge kama tulivyozungumza, tutasimama kwa pamoja kuhakikisha mradi huu unaisha ndani ya wakati. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri pamoja na kwamba wananchi walitegemea iwe ni hospitali lakini kwa sababu kwa kuwa Halmashauri imeshakuwa na hospitali haiwezekani kupata hospitali nyingine ya Wilaya.

Je, ni lini fedha hizi ambazo zimetengwa zitakwenda kwa ajili ya utekelezaji kwa sababu mwaka wenyewe ndiyo unaelekea mwisho maana Juni ndiyo mwisho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba Mheshimiwa Waziri aweze kuongozana nami kipindi hiki ambacho Bunge linaendelea aweze kwenda kuona kituo chenyewe cha afya ambacho tunakizungumzia kwa sababu kina hali mbaya sana. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Jimbo la Kigoma kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Sera ya Afya kwa sasa Halmashauri moja inakuwa na hospitali moja na ndiyo maana Serikali ilileta fedha imejenga Hospitali ya Halmashauri, kwa hiyo, hiki lazima kiendelee kama kituo cha afya. Fedha hizi zitapelekwa ndani ya mwaka wa fedha huu wa 2022/2023 Serikali inatafuta fedha ili kupeleka fedha kwa ajili ya mpango huo wa kukamilisha kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, niko tayari kuongozana nae na ningeomba uridhie tuongozane baada ya kuahirisha Bunge hili ili tukapate muda wa kutosha, tufanye ziara hiyo na kufanya majukumu hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri ni lini, kwa sababu kivuko hicho ambacho amekizungumza eneo hilo lina giza sana. Je, ni lini ataweka taa kwenye eneo hilo la kivuko?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge naomba nichukue wazo lako na tuangalie uwezekano wa kuweka taa kwenye hilo eneo la kivuko ambalo linaunganisha hizo pande mbili kwa ajili ya kusaidia kufanya kazi muda wa usiku.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hiyo barabara ya Simbo – Kalya, hiyo barabara inaendelea mpaka Wilaya ya Tanganyika ambayo ni Kalya -Lugalaba, Bujombe yenye urefu wa kilometa 37 ambayo inaenda kwenye Wilaya ya Tanganyika katika Mkoa wa Katavi. Ni lini nayo itawekewa fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha changarawe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika barabara hiyo hiyo, iko barabara ambayo ni ya Lukoma hadi Mwese, yenye urefu wa kilometa 47 ambayo nayo inakwenda nayo kwenye Mkoa wa Katavi. Naomba nijue, ni lini nayo itawekewa fedha kwa ajili ya ujenzi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo tunazihudumia sisi zinaishia Kalya, lakini ni kweli pia kwamba, kwa sababu tumeshawekeza eneo la Sibosye, tuna bandari yetu pale, kwa hiyo, tumefungua barabara mpaka Sibosye kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hiyo bandari inafanya kazi, na tutaendelea kwa barabara ambayo inaenda Katavi. Pia kwa upande wa Kigoma tumeshaifungua mpaka mpakani mwa Katavi, na wenzetu wa Katavi pia wameshaanza kutenga fedha kuifungua ili hizo barabara ziweze kuunganishwa ambapo itatumika pia kama barabara ya ulinzi kwa mikoa hiyo miwili ya Katavi na Mkoa wa Kigoma, ahsante.
MHE. NASHONI W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza Serikali. Ni lini itapeleka mawasiliano katika Kijiji cha Songambele, Kalilani, Mkanga pamoja na Chagu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wote. Miradi ya Mawasiliano ambayo tumesaini mwezi wa tano iko katika hatua za awali za utekelezaji wake. Ninaamini kabisa kwamba kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hawajaanza kuona minara ikiwa ina simama katika maeneo yao, wavute subira ili tutakapoanza utekelezaji wake na baadaye minara itakapoanza kuonekana basi tutaweza kubaini maeneo ambayo yatakuwa bado yanahitaji kupelekewa mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Songambele, tayari imeingizwa katika vijiji 2116 ambavyo vinafanyiwa tathmini na tayari Serikali imeshaanza kutafuta fedha ambapo Mheshimiwa Rais alishapata fedha ya kufikisha minara 600 mingine. Ninaamini Mheshimiwa Mbunge, atakuwa mmoja wa wanufaika katika minara hiyo 600, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Daraja la Malagarasi Lower litakuwa na kilometa saba za lami. Je, Serikali haioni haja ya kufanya upembuzi yakinifu haraka wa kipande hiki kidogo cha Simbo - Ilagala chenye kilomita 40? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nashon, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge nimeisikia na Mheshimiwa Mbunge naomba unipe muda ili niweze kufuatilia kipande cha barabara hii ili tuweze kuona lile ambalo linawezekana. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mitandao yote ya barababara ambayo ipo chini ya TANROADS, kwanza zile ambazo hatujafanya upembuzi yakinifu, tunafanya upembuzi yakinifu na kuwa na database ili fedha zinapopatikana tu ujenzi wa barabara hizi unaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua pia mahitaji ni mengi ya barabara kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini naomba Waheshimiwa Wabunge wanipe muda, nitakaa na timu yangu ya Wizara lakini kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Miundombinu ya Bunge, tuangalie mahitaji haya makubwa na majira haya tunayoingia ambayo Waheshimiwa Wabunge wanafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeahidi vingi kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila aina ya jitihada fedha zinapatikana, kazi inaenda vizuri, lakini hata mahitaji ambayo bado tutaangalia namna ya kujipanga tukisaidiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, kaka yangu Kakoso, Makamu Mwenyekiti Mama Anna Kilango, tuangalie resources ambazo zinapatikana ndani ya Serikali. Tufanyaje kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge ili yale ambayo tuliwaahidi wananchi tuweze kuyatekeleza kwa kiasi kikubwa kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpanda – Uvinza – Kasulu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, barabara hii tumeshakamilisha usanifu na itakuwa ndiyo barabara kuu ya kutoka Kusini kwa maana ya Mpanda – Uvinza hadi Kasulu ambayo haizidi kilometa 57.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kweli inatafuta fedha ili iweze kukamilisha hicho kipande ambacho ndiyo kimebaki peke yake katika Mkoa wa Kigoma, barabara kuu ambayo haina lami. Kwa hiyo, tunalifahamu na Serikali imeendelea kutafuta fedha ili kukamilisha kipande hicho kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Kalemie na Uvira ni miji ambayo iko karibu sana na Mikoa ya Kigoma, Katavi na Sumbawanga: Je, Serikali haioni haja ya kufanya haraka kuhakikisha kwamba maeneo haya ya Uvira na Kalemie yamefunguliwa hizo branches za CRDB? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Serikali imeona haja hiyo na ndiyo maana kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, kwamba Benki Kuu ya Tanzania ilishatoa kibali kwa CRDB sasa, lakini tumetoa wito kwa benki nyingine zote nchini ambazo ziko tayari kuwekeza katika miji hiyo ya Congo, basi Serikali imetoa idhini ya kufanya zoezi hilo. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba na mimi niulize swali. Ni lini mawasiliano yatafika Ilolanguru, Chagu, Songambele, Ubanda na Mumbala? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa bado tuna changamoto baadhi ya maeneo katika nchi yetu lakini tunakwenda awamu kwa awamu. Tunapeleka minara 758 vilevile tumefanya tathmini ya vijiji 2116, baada ya hapo tunapeleka minara 600 na baada ya hapo tutapeleka minara 1000. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge aniletee maeneo hayo kwa maandishi ili niyaweke katika mpango wa utekelezaji wa awamu inayokuja, ahsante sana.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami ninalo swali linalofanana na Korogwe. Pale Mji wa Nguruka Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliwaahidi kilometa tano za lami, lakini mpaka sasa zimejengwa mita 250 tu. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga barabara za lami pale Nguruka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon kwenye hii barabara ya Nguruka ambayo ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutakaa kupitia ahadi zote za Viongozi Wakuu, kupitia wakala wetu wa TARURA na kuona ni namna gani tunaweza tukakaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuona tunapataje fedha ya kuanza kutengeneza taratibu kutenga ili kila mwaka angalau kwenye ahadi hizi tuweze kuwa tunapunguza kilometa hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunalifanyia kazi chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Angellah Kairuki, kuhakikisha kwamba tunajua ahadi zote na kuziratibu na kuhakikisha barabara hizi zinajengwa kwa wakati.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nilulize swali la nyongeza. Kwamba Mahakama ya Mwanzo kule Kalya inaendelea ni kweli. Sasa nilikuwa naomba niishauri Serikali kwamba yule Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo kule Kalya basi aje kwenye Makao Makuu ya Tarafa pale Buhingu kabla jengo hilo halijajengwa la Mahakama ili aendelee kuhudumia wananchi kwa masuala ya sheria, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Makao Makuu haya ya Mgambo na Kalya kuna umbali zaidi ya kilomita 100 na wananchi wamekuwa wakipata tabu kufikia huduma hii. Mahakama yetu ya Tanzania inaridhia maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwamba huyo Hakimu aliyeko Kalya aende sasa Mgambo walau tumtafutie Ofisi pale kwa Afisa Tarafa ili huduma, iendelee kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tunalipokea jambo hili na tunalifanyia kazi na huduma itatolewa. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili analotolea majibu kwamba halina hati, lina kituo kidogo cha Polisi cha muda mrefu; na eneo hili halina mgogoro; sasa ni kwanini Serikali isijenge na hiyo hati ikaja kupatikana baadaye kwa sababu hakuna anayelalamikia eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wilaya yangu ni kubwa sana na ni mpya, lakini OCD hana gari ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Nashon kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa masuala ya ulinzi na usalama kwenye jimbo lake. Pia tumtie moyo kwa namna anavyoshirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kigoma na kwa sababu tunafahamu hata hili jengo linalotumika sasa ni lile ambalo Halmashauri imetoa kuiazima Jeshi la Polisi waweze kufanya shughuli zao, kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Bidyanguze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa nijibu swali lako kwamba kama kweli hakuna mgogoro, basi tutamwagiza OCD na RPC wa Mkoa wa Kigoma kufuatilia kwa haraka, kwa sababu maelekezo ya Serikali ni kwamba maeneo yote ya Serikali yapate hati ili kuondoa uwezekano wa migogoro huko mbele. Kwa hiyo, hati itakapokuwa imetoka na kwa sababu hati inatolewa na Halmashauri na mahusiano yenu ni mema, bila shaka wataharakisha kutoa hii hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la gari, tumejibu hapa mara nyingi Mheshimiwa Mbunge, kwamba magari ambayo tunatarajia kuyapata ifikapo Septemba ni zaidi ya 370. Tunatarajia maeneo yenye changamoto kama hili la kwako la Kigoma ambalo liko karibu na maeneo ya mpakani yatazingatiwa kama maeneo ya kipaombele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Simbo – Kalya kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Simbo – Kalya ipo kwenye Ilani na Serikali inaendelea kutafuta fedha lakini kabla ya kuijenga barabara hii Serikali kwanza imeamua ijenge daraja la kudumu la Mto Malagarasi Chini na hatua ya pili itakayofuata itakuwa ni kutafuta fedha kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba kuiuliza Serikali; ni lini kilometa tano zilizoahidiwa na Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano katika Mji wa Nguruka zitajengwa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon Bidyanguze, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa ahadi zote za viongozi tumeshazichukua pale Ofisi ya Rais – TAMISEMI na jukumu letu la sasa ni kuzitafutia fedha ili kuhakikisha kwamba zinaanza kutekelezeka.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini ninalo swali moja la nyongeza. Ni lini Serikali itapeleka Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kalya na ni lini itapeleka Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo pale Buhingu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tutawaepeleka hawa watendaji ambako kuna upungufu katika maeneo yao kwenye kipindi cha bajeti hii ambayo kimsingi ndiyo tunayoijadili sasa. Kwa sababu tuna eneo ambalo tutapata watumishi wapya ambap tutazingatia maeneo ambayo hayana watumishi. Ahsante. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali langu la nyongeza, kwamba kwa kuwa Kituo cha Afya cha Kazuramimba ni kata ya kimkakati. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga majengo mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bidyanguze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshaainisha maeneo yote ya kata za kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwa awamu na mpaka sasa imeshajenga vituo vyake 466 vyenye thamani ya shilingi bilioni 718 na Kituo cha Afya cha Kazuramimba ni miongoni mwa vituo hivyo ambavyo vitatengewa fedha kwa ajili ya majengo mengine, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, naomba kujua ni lini Kijiji cha Chagu, Kalilani, Songambele na Ikuburu watapata mawasiliano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunikumbusha.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza katika Kijiji cha Songambele na vijiji vyote ulivyovitaja Mheshimiwa Nashon tunakuja kuleta minara na kuhakikisha mawasiliano yanakuwa murua.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itajenga daraja katika Mto Malagarasi pale Ilagala? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la Malagarasi Chini najua sasa hivi halipitiki kutokana na maji kujaa. Tumeshakamilisha ama tuko mwishoni kukamilisha usanifu wa daraja hilo. Nataka nimhahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale lilipo tunalihamisha linakwenda juu kwa sababu lipo karibu sana na Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea pengine katika bajeti kwa sababu hatujapitisha, kama usanifu utakuwa umekamilika, basi litakuwa lipo kwenye mipango ya maandalizi ya kuanza kulijenga hilo daraja, ahsante. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba niulize swali kwamba ni lini Mahakama ya Mwanzo ya pale Buhingu itajengwa?

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mhehimiwa Naibu Spika, naomba tu nipokee ombi la Mheshimiwa Mbunge juu ya kujenga hii Mahakama ya Mwanzo kwa sababu kama nilivyosema kwenye majibu ya Waheshimiwa Wabunge kwenye maswali yao ya nyongeza, kipaumbele tulianza na Mahakama Jumuishi ngazi ya mikoa. Tumeingia ngazi ya wilaya kuhakikisha kwamba wilaya zote zinapata Mahakama na sasa tunashuka kwenda kwenye Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu na kwa mazungumzo yetu na wadau wa maendeleo Mahakama ya Mwanzo aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge kule Mkoani Kigoma itazingatiwa, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ipo Miradi ya Maji ya Kijiji cha Mwakizega, Buhingu na Kandaga. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; vipo Vijiji vilichimbiwa visima Basanza, Msebehi na Lemseni. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha sasa kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza sana Mheshimiwa Nashon kwa kazi kubwa ambayo unaifanya kwa wananchi wa Uvinza, mimi ni shahidi kabisa kwamba, tulizunguka kijiji kwa kijiji, Kazuramimba, Uvinza yenyewe na maeneo mengine kujionea hali halisi. Ninamhakikishia Mbunge kwamba, maeneo ya Basanza pamoja na maeneo mengine aliyoyataja, hatua ya kwanza tumechimba visima, hatua ya pili tunapima wingi wa maji na hatua ya tatu sasa tunaanza kufunga mitambo na kuhakikisha kwamba mtandao wa maji unakuwa unapatikana kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ambayo imesimama, Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeshafanya tathmini ya miradi yote nchi nzima ambayo ipo katika hatua mbalimbali, tumeelekeza namna gani ya kwenda kuikamilisha. Kwa hiyo, kuanzia Mwezi wa Kumi mpaka wa Kumi na Mbili kuna baadhi ya miradi itakuwa imeshakamilika katika Mkoa wa Kigoma. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa mmesikia miradi yote ambayo ina changamoto mwezi wa Kumi na Mbili imekwisha. Kama mna maswali ya nyongeza swali hilo msiulize. (Kicheko)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopitiwa kwenye mashamba yao pale Uvinza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, fidia hiyo italipwa. Tayari tumeshapeleka taarifa kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha baada ya kufanya tathmini na tutakapopewa fedha hizo zitalipwa. Ahsante.