Primary Questions from Hon. Dr. Charles Stephen Kimei (19 total)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI Aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwepo na Mwongozo kwa Tour Operators wanaopandisha watalii Mlima Kilimanjaro wanaoajiri Wapagazi, Wapishi na Waongoza Misafara kwa kuwalipa ujira stahiki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kusimama mbele ya Bunge hili. Vile vile namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na chama changu kwa kuniamini na leo hii nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2015 ilitoa Mwongozo kwa Mawakala wa Utalii wa Mlima Kilimanjaro Tour Operators wa kuwalipa ujira stahiki Wapagazi, Wapishi na Waongoza Watalii waliowaajiri kwa ajili ya kuwahudumia watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwongozo huo, Serikali iliagiza kuwa mwongoza watalii alipwe dola za Kimarekani 20 kwa siku, sawa na Sh.40,000 kwa siku, mpishi alipwe dola za Kimarekani 15 sawa na shilingi 30,000 na mpagazi alipwe dola za Kimarekani 10 sawa na Sh.20,000 kwa siku. Wastani wa siku za kupanda mlima hadi kileleni na kushuka ni kuanzia siku 5 hadi 7.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 12 Disemba, 2015, wadau wa utalii wa Mlima Kilimanjaro ambao ni mawakala wa utalii, viongozi wa wawakilishi wa vyama vya waongoza watalii, wapagazi na wapishi walikutana na kusaini mwongozo huo wa malipo ambapo pande zote ziliridhia viwango hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo huu na makubaliano hayo. Katika utekelezaji wa mwongozo, kulijitokeza changamoto ya baadhi ya mawakala wa utalii kutokulipa viwango hivyo na kwa hivyo Serikali iliweka mikakati kadhaa ya kuhakikisha kuwa viwango hivyo vinalipwa kama ilivyoagizwa. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na: -
(i) Kushirikiana na Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kuandaa mikataba ya kisheria ambapo mawakala wa utalii husaini pamoja na waongoza watalii, wapagazi na wapishi wanaoajiriwa kabla ya kuanza kazi. Mkataba huo umeainisha kiwango cha malipo na idadi ya siku atakazofanya kazi na jumla ya malipo anakayostahili kulipwa. Nakala moja ya mkataba huu hukabidhiwa kwenye lango la kupandia mlima, nakala nyingine hupewa waajiriwa (waongoza watalii, wapishi na wapagazi) na nakala moja hubaki kwa wakala wa Utalii.
(ii) Idara ya Kazi imekuwa ikihimiza waajiriwa kutokuanza kazi bila ya kuwa na mikataba. Pia, Idara imekuwa ikifanya ukaguzi wa karibu na wa mara kwa mara katika malango ya hifadhi, ofisi za mawakala wa utalii ili kujiridhisha kuwa utaratibu huo unazingatiwa wakati wote; na
(iii) Changamoto zinazotokana na waajiriwa kutokulipwa kiwango stahiki, kuchelewa kulipwa au kutokulipwa kabisa zimekuwa zikishughulikiwa kwa karibu na Idara ya Kazi na vyama vya waongoza watalii na wapagazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutoa wito kwa waongoza watalii, wapishi na wapagazi kuendelea kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya Taifa. Pia, Serikali inaendelea kutoa wito kwa mawakala wote wa utalii kuhakikisha kuwa wanatoa ujira stahiki kwa wahusika ili waendelee kupata motisha ya utendaji kazi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani kupitia SIDO kutengeneza mashine zitakazosaidia kuchakata mazao ya Wakulima, kama vile mashine ya kutengeneza chips za ndizi, muhogo, sauce za nyama, karoti, pilipilihoho na mbogamboga kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuendeleza viwanda hususan viwanda vidogo sana na viwanda vidogo vinavyolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Serikali imeendelea kulijengea uwezo Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili kubuni na kuendeleza teknolojia mbalimbali kutokana na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lina Vituo vya Uendelezaji Teknolojia (Technology Development Centres) katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Lindi, Iringa, Mbeya na Shinyanga kwa ajili ya kutengeneza mashine za kuchakata na kusindika mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashine hizo ni pamoja na za kutengenza chipsi za ndizi, chipsi za viazi na muhogo, mashine za kukausha mboga mboga na matunda mashine za kusindika nyanya, karoti na mashine kusindika pilipili kwa ajili ya achali kulingana na mahitaji. Aidha, mashine mbalimbali zinazotengenezwa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO zinapatikana katika tovuti ya SIDO na husambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia ofisi za SIDO.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya SIDO kutengeneza mashine hizo pia imekuwa ikitoa mafunzo ya usindikaji wa muhogo, ndizi, nyanya, karoti, pilipili na mbogamboga katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Bei za mashine hizo hutegemea na uwezo wa mashine yenyewe kwa maana ya capacity na pia mahitaji halisi ya mjasiriamali.
Mheshimiwa Naibu Spika, SIDO imeendelea kutafuta teknolojia mbalimbali za kisasa na nafuu ndani na nje ya nchi hii, ambazo zinaweza kutumika kutengeneza mashine kulingana na mahitaji ya wajasiriamali. Vile vile SIDO inasimika mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kutengeneza mashine kwa wingi na huisambaza kwa wajasiriamali kwa gharama nafuu kwenye vituo vya kuendelezea teknolojia katika Mikoa ya Kigoma, Lindi na Shinyanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha hili katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao, Serikali imeweza kuliwezesha SIDO zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya wajasiriamali ikiwemo maendeleo ya teknolojia na ujenzi wa majengo ya viwanda vya wajasiriamali wadogo. Naomba kutoa wito kwa wananchi wenye uhitaji wa mashine za kuchakata na kusindika mazao ya kilimo wakiwemo wananchi wa Jimbo la Vunjo, kuwasiliana au kuwasilisha mahitaji yao kwenye Ofisi zetu za SIDO zilizopo katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge wote kuwahamasisha wajasiriamali kwenye maeneo yetu kutumia fursa zilizopo za uwepo wa vituo vya kuendeleza teknolojia yaani TDC vya SIDO ili kujinufaisha kiuchumi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kusamehe kodi za miaka ya nyuma taasisi za dini 7 zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu usiolenga kupata faida na kuziwekea utaratibu taasisi hizo kuanza kulipa tangu walipojulishwa kutakiwa kulipa kodi?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za kodi, taasisi za dini ambazo zinajiendesha kutokana na sadaka kutoka kwa waumini wao ama misaada inayotolewa na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, hazikatwi na hazitakiwi kulipa kodi ya mapato, isipokuwa taasisi zenye sifa kama hizo husajiliwa na kupewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa madhumuni ya kuziwezesha kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Mapato kama vile kuwasilisha kodi zinazokatwa kutoka kwa watumishi wa taasisi hizo na usajili wa mali mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, aidha, taasisi za dini zinazofanya shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujipatia faida kutokana na shughuli hizo zinatakiwa kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama wafanyabiashara wengine na kulipa kodi ya mapato kulingana na faida inayopatikana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipokea maombi ya kusamehe kodi za miaka ya nyuma kutoka taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za dini. Serikali inaendelea kutathmini maombi hayo ili kuona hatua zinazoweza kuchukuliwa bila kuathiri matakwa ya sheria zilizopo.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali inaweza kuwahakikishia Wananchi wa Moshi Vijijini kuwa barabara za Himo – Kilema, Pofo –Mandaka, Uchira – Kisomachi na Mabogini – Kahe - Chekereni zitawekwa kwenye Bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Pofo –Mandaka – Kilema, Uchira – Kisomachi – Kolarie, Fongagate – Mabogini – Kahe na Chekereni – Kyomu – Kahe zina jumla ya urefu wa kilometa 57.28. Serikali imeendelea kujenga na kukarabati barabara hizi mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilijenga barabara ya Uchira – Kisomachi -Kolarie kipande chenye urefu wa kilometa 1.4 kwa kiwango cha lami kwa shilingi milioni 694, ujenzi wa barabara ya Chekereni – Kyomu - Kahe kipande cha kilometa 11 kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 230.01 na kufanya matengenezo ya barabara za Fongagate – Mabogini - Kahe kipande cha kilometa 3 kwa gharama ya shilingi milioni 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 Serikali inatekeleza kazi za matengenezo ya kawaida katika barabara ya Pofo – Mandaka – Kilema kilometa tisa kwa gharama ya shilingi milioni 13.5, matengenezo ya barabara ya Uchira – Kisomachi – Kolarie kilometa 2.5 kwa gharama ya shilingi milioni 15, matengenezo ya barabara ya Fongagate – Mabogini – Kahe kilometa mbili kwa gharama ya shilingi milioni 60 na matengenezo ya barabara ya Chekereni – Kyomu – Kahe kilomevta 3 kwa gharama ya shilingi milioni 4.5. Matengenezo ya barabara hizi yanaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 33 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Pofo – Mandaka – Kilema kilomita 11, matengenezo ya barabara ya Uchira – Kisomachi – Kolarie kilomita 4 kwa gharama ya shilingi milioni 11 na matengenezo ya barabara ya Fongagate – Mabogini – Kahe kilomita 42.25 kwa gharama ya shilingi milioni 540.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara hizi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Vituo vya Polisi vilivyopo katika Kata za Kilema, Kirua Vunjo, Kahe na Marangu katika Jimbo la Vunjo vinapewa usafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa magari katika vituo vya Polisi vilivyo katika Jimbo la Vunjo ambavyo ni Kilema, Kiruavunjo, Kahe na Marangu kama vyanzo muhimu katika kutendea kazi. Kwa kupitia mkataba wake wa kampuni ya Ashok Leyland ya nchini India, Jeshi la Polisi linategemea kupokea magari 369 na pindi magari hayo yatakapofika kipaumbele kitatolewa kwa vituo vya polisi vyenye uhitaji mkubwa ikiwemo kituo ama vituo vilivyo katika Jimbo la Vunjo. Nakushukuru.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali inaweza kutoa tathmini ya urejeshwaji wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vikundi vya Akinamama, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu katika kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2018/2019, ilitoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 42.06 ambacho kiasi cha shilingi bilioni 12.88 kilirejeshwa sawa na aslimia 3.6; Mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni 40.73 kilitolewa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.65 kilirejeshwa sawa na asilimia 35.96; na katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shillingi bilioni 53.81 kilitolewa ambapo shilingi bilioni 29.85 kilirejeshwa sawa na asilimia 55.47.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshasanifu mfumo wa kieletroniki utakaowezesha usimamizi madhubuti wa mikopo katika usajili wa vikundi, utengaji wa fedha, utoaji wa mikopo, usimamizi wa marejesho na shughuli za vikundi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, mwongozo wa usimamizi wa mikopo hii umeshaandaliwa na upo kwenye hatua za mwisho za uidhinishaji.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuiwezesha TTCL kuunganisha Wateja wengi kwenye Mkongo wa Taifa kwa punguza gharama za kuunganisha?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba, 2021, Wizara iliingia mkataba wa ushirikiano na TANESCO kwa ajili ya matumizi ya pamoja ya miundombinu inayojengwa. Kupitia mkataba huo, miundombinu inayojenjwa kwenye nguzo za TANESCO nchi nzima zinazojumuisha nyaya za mawasiliano zitatumiwa kwa pamoja. Hivyo, kupitia ushirikiano huo, utawezesha TTCL kuunganisha wateja maeneo ya biashara na nyumbani (fiber to X) kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama nafuu kwa kuwa gharama za uwekezaji zitapungua. Aidha, Serikali inaongeza uwezo wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano kutoka kiwango cha 200G hadi 800G. Kuongezeka kwa kiwango hiki kitasaidia kupunguza gharama, hali itakayopelekea kuwaunganisha wateja wengi zaidi.
Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine wa Serikali ni kuondoa Wizarani shughuli zote za mkongo wa Taifa wa mawasiliano na kupeleka TTCL. Suala hili litawezesha TTCL kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kibiashara kwa haraka zaidi inayojumuisha masuala ya kuwaunganisha wateja kwenye mkongo huo. Aidha, Serikali inaongeza kiwango cha internet band width kinachotumiwa na taasisi 312 za Serikali, taasisi za utafiti na elimu ya juu kutoka 2.1G kwenda 20G. Hii itapunguza gharama za internet kwa taasisi hizo pamoja na nyingine zitakazounganishwa.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, wananchi wa Vunjo wamenufaika vipi na Mifuko ya Uwezeshaji ya Wajasiriamali kama NEEC, NEDF, SELFU na TAFF?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko na programu za uwezeshaji zimetoa manufaa makubwa katika kuwezesha mikopo, ajira, kipato kwa wananchi wakiwemo wananchi wa Vunjo. Mifuko na programu za uwezeshaji zimetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 5.68 tangu kuanzishwa kwake. Mathalani katika Jimbo la Vunjo, kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 mfuko wa NEDF umetoa mikopo 11 yenye thamani ya milioni 25.2 na Mfuko wa TAFF umetoa ruzuku yenye thamani ya shilingi milioni 20, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI K. n. y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuingia kwenye biashara ya Gesi Joto (Carbon Trading)?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, biashara ya gesijoto ilianzishwa chini ya Mkataba wa Kyoto unaozibana nchi zilizoendelea kutekeleza miradi ya kupunguza uzalishashaji wa gesijoto (Clean Development Mechanism – CDM) ili kusaidia nchi zinazoendelea kuleta maendeleo endelevu bila kuchafua mazingira.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaingia na inanufaika na biashara ya hewa ukaa, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mwongozo wa Taifa wa Biashara ya Hewa Ukaa kwa mwaka 2016. Tanzania inayo miradi mitatu ya biashara ya gesijoto inayotekelezwa nchini. Hadi sasa jumla ya tani 900,000 za gesijoto zimeshauzwa kupitia miradi ya uzingatiaji wa kupunguza gesijoto inayotekelezwa nchini.
Mheshimiwa Spika, aidha, miradi minne ya biashara ya soko hiari ya gesijoto imeelekezwa nchini tangu mwaka 2009 na jumla ya tani 1,456,600 za gesijoto zimepunguzwa na kuuzwa kupitia utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya mapitio Mwongozo wa Taifa wa Biashara ya Hewa ya Ukaa ili kuwezesha taifa na wananchi wake kushiriki kikamilifu na kunufaika na biashara hii. Aidha, katika kuboresha ushiriki, Wizara ya Maliasili na Utalii inaandaa mwongozo maalum wa usimamizi wa misitu ambayo itashiriki biashara ya gesijto nchini. Ninakushukuru.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiingize gharama za mita za maji kwenye vitabu vyao vya fedha badala ya kuweka pale inapounganishwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na dira za maji na kuwafungia wateja wanaoomba huduma za maji. Kwa kutambua changamoto za uunganishaji wa maji kwa wateja hususani kwenye suala la dira, Serikali imeandaa mwongozo wa ugharamiaji wa maunganisho ya maji vijijini ambao pia utajumuisha suala la dira za maji kuwa ni sehemu ya gharama za Serikali. Mwongozo huo utaanza kutumika mwezi Julai, 2023.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA K.n.y. MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati Vituo vya Afya ili kuendana na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango na mikakati madhubuti ya kujenga na kukarabati vituo vya afya nchini ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 jumla ya Shilingi bilioni 118 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 236 katika Kata za kimkakati nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya Afya nchini, kiasi cha Shilingi bilioni 8.75 kimetengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vipya 15 na ukamilishaji wa vituo vya afya vitano. Vituo hivi vya afya vinapaswa kutoa huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja Mfuko wa Afya wa Jamii ulioboreshwa (iCHF).
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga barabara ya mchepuo kwenda Moshi kupitia Chekereni – Kahe – Mabogini - TPC kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 kujengwa kwa kiwango cha lami. Hadi sasa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro imefanya usanifu wa barabara yote kilometa 31.25 ambapo kwa kuanzia makisio ya ujenzi wa kilomita 12 kwa kiwango cha lami yenye jumla ya shilingi bilioni 15 yamewasilishwa TARURA makao makuu kwa hatua zaidi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mabwawa katika Mito Ghona, Rau na Deu ili kupunguza athari za mafuriko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mito ya Ghona, Rau na Deu inapitisha maji kiasi cha lita 103,310 kwa sekunde (sawa na mita za ujazo 267,940.21 kwa siku) ambapo Mto Rau ni lita 98,000 kwa sekunde, Mto Dehu Lita 3,100 sekunde na Mto Ghona ni lita 2,210 kwa sekunde. Mito hiyo hupeleka maji yake katika Mto Ruvu na hatimaye kufika katika Bwawa la Nyumba ya Mungu. Serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Pangani imeshafanya upembuzi wa awali na kubaini kuwa sehemu ya maji ya mito hiyo haifiki kwa wakati kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na badala yake husambaa na kuacha mkondo wake na kuathiri wananchi kandokando ya mito hiyo ikiwemo Vijiji vya Chekereni na Kileo kupitia Mto Ghona; maeneo ya Majengo, Msaranga, Mabogini, Oria, Ngasini, Mandakamnono yanayoathiriwa na Mto Rau; na Vijiji vya Mongalia, Soko, Ngaseni na Kiterini huathiriwa pia kupitia Mto Deu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ya maji ya mito hiyo kusambaa ni kutokana na kuharibika kwa kingo za mito husika katika maeneo ya tambarare kunakosabisha maji kutoka katika mikondo yake na kusambaa katika maeneo wanayoishi wananchi. Serikali imeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na ufukuaji wa mikondo ya mito katika baadhi ya maeneo korofi ya mito hiyo na kazi ya ufukuaji itaendelea katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mpaka itakapokamilika. Aidha Bonde la Pangani litafanya tathimini kwenye maeneo yanapitiwa na mito hiyo ili kubaini kama kuna uwezekano wa kujenga mabwawa bila kuathiri upatikanaji wa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo linatumika katika shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, lini Serikali italipa fidia kwa maeneo ya Kahe/Chekereni na Njiapanda yaliyochukuliwa na TANROADS mwaka 2013?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 Serikali ilifanya na kukamilisha uthamini kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 146 watakaoathirika na ujenzi wa mradi wa vituo vya ukaguzi wa pamoja wa magari ya mzigo (One Stop Inspection Station) ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.048 kilihitajika kuwalipa waathirika hao lakini hawakulipwa kutokana na Sheria Na. 7 ya Mwaka 2016 ya Uthamini na Usajili.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro, inarudia zoezi la uthamini ulioanza tarehe 10 Mei, 2023 ambapo zoezi hilo lipo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Baada ya zoezi hilo kukamilika waathirika watalipwa fidia zao, ahsante.
MHE. CHARLES S. KIMEI aliuliza;
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko la Kimataifa katika eneo la Lokolova mpakani mwa Tanzania na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 140 katika eneo la Lokolova kwa ajili ya ujenzi wa soko la mpakani. Hatua inayofuata ni kupata hati miliki ya eneo hilo na hatimaye kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya soko hilo, nakushukuru.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, lini Serikali itafanya mapitio ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu,
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Aidha, katika kutatua changamoto hizo, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya mawakala wa utalii yaani waajiri imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kufanya maboresho ya viwango hivyo vya malipo ya ujira.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, Wizara imefanya kikao na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na kujadili kuhusu viwango vya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii.
Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kufanya kikao kazi baina ya wadau hao na waajiri wao kwa lengo la kupendekeza viwango stahiki, ili viweze kuwasilishwa katika Bodi ya Utatu yenye dhamana ya kumshauri Waziri mwenye dhamana ili makubaliano hayo yawe ya kisheria. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika katikati ya Novemba, 2023 kule Arusha.
MHE. DKT.CHARLES S. KIMEI aliuliza: -
Je, lini Serikali itaboresha uwanja wa michezo katika eneo la Polisi Himo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo nia ya dhati kuhakikisha kwamba uboreshaji wa miundombinu ya michezo nchini unafanikiwa ili kukuza ushiriki wa michezo na kuibua vipaji. Katika kufanikisha suala hili, Serikali imekuwa ikiwahimiza wamiliki wa viwanja na wadau mbalimbali wa michezo kushiriki katika kujenga na kuboresha miundombinu ya michezo katika maeneo mbalimbali nchini kama Sera ya michezo inavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali inahimiza wamiliki wa uwanja wa michezo wa Polisi Himo kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi katika kuboresha uwanja huo. Aidha, Wizara ipo tayari kutoa ushauri wa kitaalam kwa wamiliki na wadau wanaokusudia kujenga ama kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kijiji cha Koresa, Kata ya Vunjo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini. Aidha, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi viporo pamoja na ujenzi wa vituo vya afya vipya kwenye maeneo ya kimkakati ikiwemo Kituo cha Afya cha Koresa katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa wananchi wa Kijiji cha Koresa wanapata huduma za afya kwenye Kituo cha Afya cha Himo. Ahsante.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wa Kahe/Chekereni na Njiapanda ambao maeneo yao yalichukuliwa na TANROADS Mwaka 2013? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uthamini wa Mali za Wananchi wa Kahe/Chekereni – Njiapanda (Himo) watakaoathiriwa na mradi huo ulifanyika Mwaka 2013. Hata hivyo, kutokana na muda mrefu kupita bila kulipa fidia hiyo, Serikali imerudia zoezi la uthamini na taarifa ya uthamini imeidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali Tarehe 8 Machi, 2024. Kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha, kwa ajili ya kulipa fidia kwa mali za wananchi watakaoathiriwa na mradi huo. Ahsante.