Supplementary Questions from Hon. Ravia Idarus Faina (3 total)
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Je, ni lini nyumba za Askari wa Wilaya ya Kusini zitafanyiwa marekebisho kwasababu hali yake ni mbaya sana? Inafikia hatua kwamba baada ya kupigiliwa misumari hizo nyumba zimewekewa vipande vya matofali na mawe; kwa katika kipindi hiki cha mvua ni hali ngumu sana za wale askari. Je lini nyumba hizo zitafanyiwa marekebisho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina Mbunge wa Jimbo la Makunduchi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sikuwa na uhakika sana kama kuna nyumba zimewekwa mawe badala ya kuwekwa bati; lakini kubwa niseme kwamba hata katika bajeti ambayo tuliyonayo mwaka huu tayari ujenzi wa nyumba hizi umezungumzwa na hatua za ujenzi wa nyumba hizi upo mbioni. Na si nyumba hizi tu tayari tuna mpango wa kujenga kituo kikubwa cha Polisi katika Mkoa wa Kusini na nyumba za kukaa maaskari katika Mkoa wa Kusini. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa Mbunge tuendelee kustahimili kidogo. Najua hili linamgusa na linamuuma kwasababu anawaona askari wanavyopata tabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini binafsi nafahamu hili kwasababu huo Mkoa ni wa kwangu. Niseme tu kwamba ninalichukua hili tunakwenda kulifanyia kazi na nyumba za kukaa askari polisi Wilaya ya Kusini hasa Makunduchi zitapatikana Inshallah.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kwenye TFF ukomo wa uongozi ni vipindi vitatu vya miaka minne minne. Lakini, kwenye TOC hakuna ukomo. Je. haoni inazuia uhuru wa watu wengine kugombea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TFF wao wamekwenda vizuri kama alivyosema lakini TOC wanaendelea kufanya marekebisho katika katiba yao. Katiba yao Mwaka 2019 walirekebisha, 2020 msajili aliweza kuipitisha Novemba na katika marekebisho ambayo amefanya sasa, wameweka kipengele cha kwamba, mtu akigombea nafasi ya Urais basi ahudumu kwa term 3 akishahudumu kwa term 3 ya miaka minne minne ya miaka 12, baada ya hapo asirudie kugombea nafasi hiyo bali sasa apande juu aende IOC au kwenye nafasi zingine. Kwa hiyo, wameendelea kuboresha vile vipengele ambavyo vinaminya uhuru wa watu wengine na wengine kuendelea kugombea. Ahsante.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, NIDA walikuwa na mashine mbili za kuzalishia vitambulisho. Wakaomba kuongeza tena na mashine mbili kwa ajili ya kuzalisha vitambulisho vya Taifa. Sasa je, ni kwa nini uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho hivyo umepungua kwa kiasi kikubwa sana na je, hawaoni wametumia fedha za wananchi vibaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Radhia Idarus Faina, Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinazalisha vitambulisho vichache kwa muda mrefu, lakini tukaomba fedha kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukanunua mashine nyingine mbili na mashine hizi zikawa zinazalisha vitambulisho hivi kwa haraka kama ambavyo tofauti na mara ya mwanzo.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyokwambia shughuli za usajili, utambuzi na utoaji wa vitambulisho hivi unaendelea mpaka ilipofika tarehe 12 Oktoba, tulishakuwa na vitambulisho karibu 10,000,000 ambavyo viko tayari na muda wowote vinategemewa kwenda kusambazwa kwa wananchi. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba mashine hizi zinafanya kazi na vitambulisho vitapelekwa kwa wananchi hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia fedha vibaya, hakuna fedha iliyoingia katika akaunti ya NIDA, aidha kwa Serikali au kutoka kwa wafadhili ikatumiwa vibaya. Hivyo nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, fedha zote zilizoingia kwenye akaunti ya NIDA zimetumika accordingly. Nakushukuru. (Makofi)