Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka (11 total)

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kwanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia Maazimio yote mawili yaliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu Afrika na dunia nzima imeshuhudia upendo usio na mfano ulioonyeshwa na Watanzania walipojitokeza kumsindikiza, kumuenzi na kumuombea Hayati mpendwa wetu Dkt. John Pombe Joseph magufuli. Upendo waliouonesha Watanzania katika maeneo ulikopitishwa mwili wa Mheshimiwa Dkt. John Pomba Joseph Magufuli na maombi na dua yaliyofanyika nchi nzima katika maeneo ambapo mwili wa mpendwa wetu haukuweza kufika ni ushahidi tosha kwamba Watanzania walikuwa na imani kubwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano alifanikiwa kujijengea uhalali wake mara alipochaguliwa na Watanzania kuwa Rais wa nchi yetu. Rais hayati Mzee Benjamin William Mkapa aliwahi kusema: “Kazi ya uongozi ni kuonyesha njia na watu wanakufuata si kwa sababu wanakuogopa ila kwa sababu wanakuamini na imani ya kweli haitokani na maneno bali matendo”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matendo ya hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yalimjengea heshima, imani ya Watanzania kumfuata. Kazi aliyoifanya kwa miaka mitano akisaidiana na Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan amekijengea chama chetu na Taifa letu uhalali wa kuendelea kuheshimika Barani Afrika na duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi nyote ni mashahidi na Watanzania ni mashahidi kwamba ukiacha kufanya maombolezo tuliyofanya kwa kujitokeza kila mmoja wetu lakini siku ya kumuaga Afrika ilileta Rais wapatao 16 na Mabalozi wasiopungua 51 waliotoka kote duniani. Pia nchi zote dunia ambazo hazikuweza kuleta Mabalozi na Rais walituma salamu kwa Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kufuatia kuondoka kwa shujaa wa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba maisha ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli siyo tu yaliwagusa Watanzania yaligusa Afrika na dunia yote. Kinachosikitisha ni kwamba wakati mataifa haya yakitupa pole na kuomboleza pamoja nasi bado kuna Watanzania wenye passport za Tanzania wanaobeza kazi iliyofanywa na hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kazi yetu ni kuendelea kuwaombea msamaha kwa Mungu awafunulie ili siku moja waweze kuijua kweli na warudi kuungana nasi katika kuweka Utanzania mbele hata kama kwa sasa wanalishwa na hao wenye nia ovu na Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii tena kueleza bayana kwamba tunamuenzi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri aliyofanya na tunampongeza mama Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti cha kuendelea kuongoza Taifa letu. Wote wawili hawa wamepata uongozi bila ya kuwa na makundi, bila kutoa hata shilingi. Dkt. John Pomba Joseph Magufuli alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa bila kuhonga hata shilingi moja naye alimteua mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na hatimaye wakaongoza jahazi la nchi yetu kwa muda wa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya miaka hiyo mitano mmeshuhudia kiwango cha kura ambacho CCM imeweza kupata katika uchaguzi wa mwaka 2020. Huu ni ushahidi tosha kwamba tulitekeleza Ilani ya Uchaguzi chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Mgufuli na mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tu uhalali wa uongozi wowote na hasa kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama cha Mapinduzi wa mwaka 1981, ibara ya 107 unatokana na uongozi huo kuendelea kuwa tetezi wa kuaminika kwa maslahi ya makundi au kundi lililokuwa kubwa katika nchi yetu. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba kijiti kinapokabidhiwa kwa mama Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kiongozi kutoka kwenye ngazi za msingi hadi ngazi ya Taifa ya chama chetu na ameongoza Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano na hatimaye Makamu wa Rais, tuna uhakika kabisa nchi yetu ipo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme la mwisho kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nina hakika kabisa miaka hii iliyobaki katika ungwe hii ya miaka mitano itakuwa ndiyo miaka mitano ya kwanza ya mama Suluhu Hassan na miaka mitano mingine itakuwa miaka ya ungwe yake ya pili kwa mujibu wa Katiba yetu. Hili tujiandae kifikra na kimtazamo kwa watu ambao walikuwa wanafikiri 2025 uongozi utabadilika. Ni zamu yao, sisi Bara tuliongoza miaka 23 ya Mwalimu, tukaongoza miaka 25 tena mingine siyo dhambi…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo dhambi sasa kwa Mzanzibar mmoja aliyejipambanua na mwenye sifa kuendelea kuwa Rais katika miaka hii iliyobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi ya kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu kwa viwango ambavyo kila mtu anakiri na kazi yetu ni kuendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, ampe afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwa kura zote na Bunge hili la Jamhuri ya Muungano kuwa Spika wa Bunge letu. Hakika Mbeya imetupa mtu, hakika Magufuli alimwona mtu makini, hakika aliyekuteua kuingia kwenye Bunge la Katiba aliona mbali na leo Watanzania watashuhudia uwezo wako katika kipindi cha uongozi wako. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nisiwe mwizi wa fadhila, niwapongeze Wabunge ambao wamepata dhamana ya kuaminiwa na Rais kwa nafasi mbalimbali; nampongeza Mheshimiwa Shangai kwa kuchaguliwa na wananchi wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu sasa kwanza kwa kuwashukuru waliowasilisha taarifa za Kamati zote mbili, lakini nianze na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Mtakumbuka tumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi au watumiaji wa ardhi na Hifadhi zetu za Taifa kwa muda mrefu; na Rais wa Awamu ya Tano aliunda Kamati ya Makatibu Wakuu na Mawaziri na baada ya kazi kukamilika, alisema maamuzi yatatolewa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema kazi inaendelea, alitekeleza uamuzi huo kwa kufanya uamuzi wa haraka na kwa muda mfupi sana aliweka historia ya kuwatuma Mawaziri wapatao nane kuzunguka nchi nzima kutoa maamuzi ya Serikali ya kilio cha muda mrefu cha wananchi wa maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Mawaziri hawa wanane wakiongozwa na Mheshimiwa Lukuvi, wakati huo akiwa Waziri wa Ardhi, walifika Jimbo la Simanjiro kutokana na mgogoro uliokuwepo kati ya Kijiji cha Kimotoro kwa upande mmoja na Pori la Mkungunero Game Reserve kwa upande mwingine; na pia kushughulikia mgogoro uliokuwepo kwa Vijiji vya Wilaya ya Kiteto kwa maana ya Erikiushi, Bwawani na Katikati, lakini kushughulikia pia mgogoro ulioko kati ya Mkungunero na Jimbo la Kondoa Vijijini la Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na maamuzi yale yalitangazwa na wananchi walipata faraja na hakika walimsifu sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kinachoshangaza mpaka sasa, baada ya maamuzi na maelekezo ya Rais ambayo yalikuja kutamkwa na Mawaziri, watendaji na wataalam walioambiwa wafanye kazi hiyo, mpaka sasa wameshindwa kukamilisha kazi hiyo kwa sababu wanazozijua wao wenyewe. Ombi langu kwa Waziri Mkuu na kwa Serikali, wale waliotumwa kufanya kazi hiyo wakamilishe haraka ili wananchi…

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Venant.

T A A R I F A

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, mchangiaji anaongea vizuri sana juu ya Mawaziri hawa, lakini nataka nimpe taarifa kwamba kweli walitumia fedha nyingi kuzunguka kuja kutatua migogoro hii, lakini cha ajabu wataalam waliachiwa hili jukumu la kusaidia kutatua migogoro hii, wenyewe wanasema wanahitaji maelekezo kutoka kwa wahusika kwa barua. Kwa hiyo nampa taarifa kuwa Serikali sasa ipeleke maelekezo kwa barua ili sasa migogoro hii iweze kwisha.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka.

MHE. CHRISTOPHER O. SENDEKA: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa yake na ninaungana naye kuiomba Serikali ifuatilie kazi ambayo watendaji walipewa ya kuhakikisha kwamba wanamaliza mgogoro huu ili ahadi ya Rais iweze kuwa ni ya kweli kama alivyoahidi mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa katika suala ambalo ninaliomba Bunge hili lijipe muda wa kuungana na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kupata muda wa kulitafakari, nalo ni suala la mgogoro uliopo katika maeneo mawili ya Wilaya ya Ngorongoro. Kwanza Tarafa ya Ngorongoro yenye kilometa za mraba 8,000 eneo ambalo kuna maisha mseto kati ya wanyamapori, binadamu na mifugo inayofugwa na binadamu ambayo imeanza mwaka 1959.

Mheshimiwa Spika, mgogoro mwingine ni katika eneo la kilometa 1,500 za Tarafa za Loliondo ambayo inatakiwa ifanywe kuwa ama Game Reserve au Game Control Area. Jambo hili ni vizuri sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likaelewa, likapata muda wakati Serikali inafanya tathmini, Bunge lako likapeleka Kamati ya kuyajua mambo haya. Kwa sababu upotoshaji unaoendelea kufanywa na baadhi ya vyombo vya habari na upotoshaji unaofanywa na social media hakika hauwatendei haki wananchi wa Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba ninukuu maneno haya ya gazeti la Jamhuri la tarehe 1 mpaka 7 Februari, linasema hivi: “Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla wake ni za Watanzania. Hivyo sote tuna wajibu wa kuona ikiendelea kuwepo ili iwe na manufaa kwa Watanzania na walimwengu wote. Haiwezekani kabila moja katika nchi likatae kutii mipango ya Serikali hasa ikizingatiwa kuwa kinachofanywa na dola kina manufaa makubwa kwa Umma na kwa nchi.” (Narudia), “haiwezekani kabila moja likatae kutii.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, lugha hii siyo njema hata kidogo. Haiwezekani! Unaposema haiwezekani kabila moja; wanaosemwa hapa, walioko Loliondo na Ngorongoro ni kabila moja linaloitwa Wamasai. Wamasai hawa wamekuwa waungwana kwa uhifadhi. Kama kuna kabila lililoonesha uhifadhi bora na kuweza kuishi na wanyama katika eneo moja bila kuwadhuru ni Tarafa ya Ngorongoro katika Wilaya ya Ngorongoro ambalo wengi wa wananchi wanaoishi hapo ni Wamasai.

Mheshimiwa Spika, wananchi hao hao walitoa ardhi yote ya Serengeti, Tarangire, Ngorongoro na Lake Manyara. Leo unapozungumza kilometa za mraba 1,500 ambayo Mheshimiwa Waziri Pinda aliundia Tume na baada ya Tume yeye mwenyewe alikwenda; CCM iliunda Tume iliyoongozwa na Dkt. Mwigulu Nchemba, nami nilikuwa Mjumbe wake tukaleta taarifa. Waziri Mkuu wakati huo Mheshimiwa Mizengo Pinda akaenda Loliondo akatoa tamko la Serikali, juu ya msimamo wa Serikali kuhusu eneo la Loliondo na msimamo wa Serikali kuhusu eneo la Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, Wakati huo huo Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, baada ya kelele kuendelea alisema hivi akiwa kwenye matibabu; na haya ni maneno yake naomba ninukuu kwa ruhusa yako. Haya ilikuwa ni tarehe 23 Novemba, 2014.

Mheshimiwa Spika, nami naomba ninukuu kwa sababu aliandika kwenye twitter yake kwa Kiingereza: “There has never been, nor will there ever be, any plan by the government of Tanzania to evict the Maasai people from their ancentral land.” Mwisho wa kunukuu. Haya ni maneno ya Rais wa Awamu ya Nne. Baada ya kelele za waandishi wa habari kutumia social media na kutumia magazeti yao kutuma ujumbe usio mzuri kwenye ulimwengu mzima.

Mheshimiwa Spika, hata leo naungana na Kamati, wanaposema mfumo wa matumizi bora ya ardhi, usimamizi hafifu ndiyo unapelekea tishio hili lililoko Ngorongoro. Nataka nikwambie, magazeti haya ambayo nilikuwa nakukuu ambayo ni mengi, ninayo hapa, yalikuwa ni matokeo ya semina iliyofanywa na Dkt. Fredy Manongi, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro kwa kuwaita Wahariri wa Habari ili watoe picha wanayoitaka wao na huku wanasahau kwamba hata log yao Mamlaka ya Ngorongoro ina kichwa cha Faru, ina picha ya ng’ombe hapa, kuonyesha kwamba Ngorongoro ni kwa ajili ya wafugaji wa uhifadhi. Hata hivyo, anasahau section 6 ya sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Ngorongoro inasema hivi, naomba ninukuu tena ili hawa wenzetu waelewe kwamba walioko Ngorongoro hawako kwa ajali. Inasema hivi: -

“The functions of the authority shall be to conserve and develop the natural resources of the conservation area;” ya pili, anazungumza: “to promote the tourism; na ya tatu: “to safeguard and promote the interest of Maasai citizens of the United Republic.” Hayo ndiyo malengo makuu matatu.

Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapo kwa sababu ujumbe wenyewe umefika, lakini kwa kukuomba na wewe utupe muda, isaidie Kamati hiyo iende Ngorongoro, ikae na wananchi wa Loliondo na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro. Serikali nayo iunde Tume yake, tutekeleze maelekezo ya Mheshimiwa Rais, amewaambia wasaidizi wake, nendeni mkakae na viongozi wa mila…

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka, dakika moja, malizia.

MHE. CHRISTOPHER O. SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa dakika moja.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwamba viongozi wa Serikali wakakae na viongozi wa Ngorongoro, wakae na viongozi wa mila wa Ngorongoro ili watafute ufumbuzi wa namna ya kuendelezwa kwa ufugaji na uhifadhi katika eneo la Ngorongoro. Ninachoomba Serikali isimamie maelekezo ya Rais kama alivyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuichangia hoja hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii ya kwanza kabisa kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja za Kamati hizi mbili za Kudumu za Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuiendeleza nchi yetu. Hakika ustawi wa nchi yetu sasa uko kwenye mikono salama, kutokana na jitihada anazozifanya Rais katika kujenga umoja wa kitaifa, kulinda muungano wetu, kutafuta uwezo kutoka nje na uwezo wa ndani ili kuleta ustawi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi Mheshimiwa Rais ameendelea kusaidia nchi yetu kuongozwa katika misingi ya kidemokrasia, misingi ya haki inayojali utu wa binadamu na ndio maana Mheshimiwa Rais amekataza watu wengine kufikishwa mahakamani, bila kesi zao kukamilika au upelelezi kukamilika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwapongeza Wenyeviti wote wawili wa Kamati zote za kudumu kwa taarifa zao nzuri pamoja na Wabunge wanaounda Kamati hizo zote mbili wamefanya kazi nzuri na taarifa zao zote ni nzuri na nitamke bayana kwamba ninaziunga mkono taarifa zote mbili za Kamati hizo mbili za kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee na hata pamoja na malalamiko mengi ambayo yametoka katika ukumbi huu leo asubuhi, kulalamikia baadhi ya maeneo ambayo mambo hayaendi vizuri na hasa baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zimepewa mamlaka ya kutunga sheria hizi ndogo na kwa bahati mbaya wakawa wanatunga sheria ambazo kimsingi zinakinzana na sheria za Bunge na hata wakati mwingine kupingana au kukinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Feleshi, kwa kiwango kikubwa tangu ameingia katika ofisi hiyo, kwa kweli naona utulivu mkubwa na ushirikiano wake mkubwa sana wa kuishauri Serikali ipasavyo. (Makofi)

Sisi wengine tunaojua rekodi yake akiwa DPP, akiwa Jaji na hatimaye Jaji Kiongozi tunaamini kabisa ofisi hiyo iko salama na nampongeza yeye pamoja na DPP wa sasa. DPP wa sasa anafanya kazi nzuri na nina hakika haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza katika Bunge hili la leo zitarekebishwa na viongozi wetu hawa wawili ambao wanaongoza taasisi hizo muhimu sana. Pia kwa namna ya pekee nawapongeza pia Mawaziri wa Wizara hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze sasa katika baadhi ya maeneo ambayo ni ya maana sana na ni ya msingi pia katika hoja za Kamati zilizowasilisha leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya baadhi ya mambo ambayo hayajakaa vizuri na hasa katika maeneo yale ambayo yanahusiana na dhamana tuliopewa Kikatiba kwamba Bunge lako tukufu lina mamlaka ya kutunga sheria, lakini bahati mbaya sana kwa jinsi ilivyo tena hizi sheria ndogo ndogo wakati mwingine zinatungwa na kutumika kabla hazijaingia katika Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Waheshimiwa Wabunge kwamba ipo haja ya kubadilisha sheria na kulitizama jambo hilo upya ili sheria hizi ambazo zimegeuka kuwa kero kwa wananchi ziwe zimepitia katika Bunge lako tukufu. Bunge lako tukufu halina nafasi ya kulalamika wala Serikali haina nafasi ya kulalamika. Mimi siamini katika kiongozi anayepewa dhamana au mamlaka yoyote inayopewa dhamana badala ya kukalia kile kiti walichopewa na kujaa, unakaa upande mmoja kama una jipu. Ni vizuri siku zote unapopewa dhamana ukajaa katika kiti chako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Bunge lako tukufu halina nafasi ya kulalamika kwa sababu kwanza linaongozwa na Spika mahiri, makini, mwanasheria aliyebobea, kiongozi madhubuti na ni kijana ambaye bado akili yake iko vizuri zaidi. Pia ana Wenyeviti wasaidizi na Naibu Spika wa viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hivi kwa sababu mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali ni ya kwetu kwa mujibu wa Katiba. Lakini Ibara ya 151(1) inaweka tafsiri bayana ya mamlaka ya nchi kwamba ni pamoja na Serikali na Bunge sisi tumetajwa bayana, Mahakama haikutajwa kinagaubaga katika Ibara ya 151 katika tafsiri ya mamlaka ya nchi. Kwa hiyo, sisi ni mamlaka ya nchi pamoja na executive. Sisi katika Ibara ya 63 tumepewa mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali ikiwa sisi ndio chombo kikuu kwa mujibu wa Katiba kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siamini katika Bunge ambalo linaona kuna tatizo pale mbele, tunashauri kupitia Kamati za Kudumu za Bunge, tunashauri kapitia Bunge, bado zipo taasisi na maafisa wa umma ambao wanaelekezwa kubadili sheria zinazokinzana na sheria za Bunge, wanaelekezwa kubadilisha sheria zinazokinzana na Katiba ambazo ni batili moja kwa moja kwa mujibu wa Katiba bado wanaendelea kunyamaza na kupuuza maelekezo ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kabisa kwamba siku 30 zilizotolewa na siku 60 zilizopendekezwa na Kamati tutaziheshimu na kuziunga mkono kupitisha maazimio hayo leo na baada ya hizo siku 60 ninaamini kabisa na wale waliopewa siku 30 watarekebisha madhaifu yaliyoonekana na Kamati zetu mbili za kudumu ambazo zimeshughulikia na hasa Kamati inayoshughulikia sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba Bunge hili ni Bunge madhubuti na kwa kweli halipaswi kulalamika. Miaka ya 1990 Bunge hili hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokuwa imekuja na hoja ya Tanganyika ya G55 ambayo ilikuwa ni kinyume na sera za CCM, kinyume na Article of Union, lakini bado ndani ya muda mfupi wana-CCM walisimama na Wabunge walisimama wakakataa na Mkutano Mkuu wa Chimwaga ulikataa, lakini baadaye wakarudi tena na kuleta hoja hiyo kutokana na hasira walizokuwa nazo na kutaka kutuingiza katika muundo wa Serikali tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema hasira zenu zisielekezwe kwenye kutuundia jambo linalokinzana na sera, jambo linalokinzana na Article of Union ambayo ndio msingi wa Muungano wa nchi zetu mbili na Mwalimu alitumia maneno haya yafuatayo na mimi naomba niyanukuu katika kitabu cha Mwalimu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania na hili nalisema kwa taasisi hii na nalisema kwa taasisi zingine zote naomba kunukuu; “Kukubali kufanywa vikaragosi vya viongozi ni dalili ya woga, si dalili ya heshima na woga na heshima ni vitu viwili mbalimbali. Maadili mema hayatudai tuwaogope viongozi wetu na viongozi makini hupenda kupata heshima ya wananchi wenzao, lakini hawapendi kuogopwa. Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta. Viongozi halisi hawapendi kuishiriki, kujenga mazoea ya kutii viongozi hata katika mambo haramu ni dalili ya woga ni kukaribisha udikteta.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayatumia maneno haya kwa sababu sifurahii kuona Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likilalamika juu ya maamuzi ambayo mlikwishayafanya. Ningependa tutoke na maazimio kwamba wale walioagizwa wayafanye tuwajue ni akina nani walipaswa kusimamia katika sekta hizo na Bunge hili lielezwe ni nani hao wanaokaidi.

Kwa hiyo, sisi tuko hapa kwa niaba ya wananchi tuchukue hatua, kama hatuna mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya Waziri mmoja mmoja, dhidi ya mtendaji mmoja mmoja, tuchukue hatua kwa wale ambao tuna mamlaka nao ili wawasimamie hao ambao wamepewa dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Edward Olelekaita, Mbunge wa Kiteto alibainisha juu ya dhahama wanazozipata wafugaji sasa kutokana na tafsiri ambazo hazijakaa vizuri. Nchi yetu au Bunge letu lipitie Sheria Namba 5 ya Uhifadhi ya Wanyamapori ya mwaka 2009 na marekebisho mengine ya mwaka 2022, yapo maeneo ambayo kwa mujibu wa sheria iliyokuwepo hayakuwa yanatajwa kama ni maeneo ya uhifadhi, lakini kwa sheria ya sasa ni maeneo yaliyohifadhiwa, ni ardhi ya hifadhi. Lakini unakuja kuhifadhi wakati tayari kuna binadamu walioko pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tukae pamoja kwa sababu ulindaji, uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za nchi ni jukumu la kila raia wa nchi hii, ni jukumu la kila Mbunge aliyeko katika ukumbi huu, ni jukumu la kila kiongozi. Tukae ili pale ambapo ardhi za vijiji ambazo sasa mnataka kufanya kwa Wildlife Migratory Route, Wildlife Dispersal Area, Breeding Areas mnataka kufanya kuwa Game Controlled Area, katika maeneo ambayo yako kwenye ardhi za vijiji hakuna namna unaweza kuichukua ardhi ya kijiji ambayo imekataliwa na sheria ukaifanya kuwa Game Controlled Area.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiacha hii kwa sababu yako mazungumzo na malalamiko niliyowasilisha nikiamini nitakaa na viongozi wenzangu tuyafikie mwisho, lakini kikubwa ninachosema hamuwezi kuendelea kutoza ng’ombe faini ya shilingi 100,000 badala ya ku-compound kama sheria inavyosema katika kifungu cha Sheria ya TANAPA (National Parks) kifungu cha 20A imeweka bayana kabisa juu ya ku- compound lile kosa na kwa yule muhusika ndio anayepigwa faini, ng’ombe hawezi kupigwa faini, anapigwa mmiliki wa ng’ombe.

Kwa hiyo. rai yangu ni vizuri tukazingatia ushauri uliotolewa na Wabunge ili kuepusha adha hii ya kuwatoza wananchi ada zisizokuwa na sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi sote ni mashahidi juu ya hukumu ya Mheshimiwa Elenina ambaye alimaliza kesi yake mwaka 2018 na akashinda, yule mfugaji ambaye amefilisiwa na mnamwona kwenye mitandao ambaye ameshinda kesi yake Mahakama Kuu. Bado DPP aliweza kung’ang’ania wale ng’ombe kwamba akate rufaa abaki na ng’ombe. Jaji wa Mahakama Kuu Jaji Kalombola alikataa na baada ya kukataa bado walikaidi na wale ng’ombe wamekufa na yule mfugaji alikuja kupewa ng’ombe 90 kati ya ng’ombe 265 ambao walikaa nao kwa muda wa miaka mitatu. Ng’ombe 265 wakizaa kila mwaka kwa miaka mitatu ni ng’ombe wangapi?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, nakushukuru kwa kunipa nafasi hiyo, na kwa kweli naishauri Serikali iendelee kuwa sikivu katika eneo hilo, nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi ya kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuungana na Wabunge wenzangu katika azimio hili muhimu sana ambalo Bunge hili limeiamua katika siku yetu ya leo ya mkutano huu.

Mheshimiwa Spika, Waswahili wanasema, “chanda chema, huvishwa pete.” Nachukua nafasi hii kuwapongeza waliowaza na kuleta pendekezo hili la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanyia nchi yetu Afrika na dunia katika muda mfupi wa uongozi wake.

Mheshimiwa Spika, natoa azimio la kumpongeza Rais kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kuimarisha demokrasia nchini. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita anafanya haya tukijua dhahiri kwamba amesimama katika mabega ya mafanikio makubwa ya waliomtangulia kuanzia Baba wa Taifa hadi Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maana ya awamu zote zilizomtangulia.

Mheshimiwa Spika, awamu zilizotangulia ziliweka rekodi ya Tanzania katika hali ya juu sana katika suala zima la demokrasia na diplomasia. Hakuna asiyejua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia; na hakuna asiyejua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Asha Rose Migiro akiiwakilisha nchi hii na kuwa mwanamke wa kwanza na Mtanzania wa kwanza kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kazi nzuri inayofanywa na mwanadiplomasia namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendeleza kazi nzuri iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili na ameifanya kwa kasi ambayo hakuna mfano wake. Katika muda mfupi wa kazi aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameimarisha demokrasia, demokrasia ambayo inazingatia misingi ya utu, misingi ya usawa, misingi ya haki katika nchi hii, bara hili na hata alipokwenda kuhutubia Umoja wa Mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amethibitisha hayo alipozungukia mataifa ya jirani kuweka mahusiano mema kati ya Tanzania na nchi zinazotuzunguka, yeye mwenyewe kwa kutembelea mataifa hayo. Leo Tanzania katika nchi zinazituzunguka, watu wanatuzungumza vizuri.

Mheshimiwa Spika, Rais pia kwa kujua diplomasia ya kimataifa inahitaji wawakilishi wa nchi wenye weledi na uelewa mkubwa, amehakikisha kwamba anawateua mabalozi ambao wana ufahamu juu ya sera, juu ya mipango ya nchi yetu, juu ya fursa zilizoko duniani, na hii imewezesha mabalozi hao kutekeleza na kuendeleza kazi nzuri aliyoianzisha katika filamu yake ya Royal Tour na tumeshuhudia wawekezaji wengi wakija katika nchi yetu, tumeshuhudia pia wafanyabiashara wetu wakiungana na dunia nzima katika tasnia ya biashara. Waswahili wanasema, “Ukiona vyaelea, ujue vimeundwa.” Haya yamefanikiwa kutokana na kazi nzuri aliyoianzisha, siyo mwingine bali ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania na hasa tukiongozwa na Bunge lako Tukufu na wewe mwenyewe kutuongoza, tuna kila sababu ya kusimama kifua mbele na kwa hakika kutoa matamko ya dhahiri ya kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ameirudisha Tanzania mahali tulikokuwa tunaijua huko, na ndiyo maana hata katika kipindi hiki ambacho dunia imetikisika kutokana na tatizo la Uviko, Tanzania tumeendelea kuwa na uwezo wa kuendeleza miradi ya kimkakati, tumeendelea kuwa na uwezo wa kuweza kujenga shule zetu, zahanati zetu katika sekta zote; barabara na miundombiu mbalimbali. Hii ni matokeo ya kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, haya anayafanya kwa kuzingatia mahitaji ya pande zote za Muungano; na kwa sababu yeye mwenyewe ni mtu wa haki, Waswahili wanasema, “Haki na usawa vinaposhamiri katika jamii yoyote, undugu hujengeka na maovu hujitenga.” Ukiona hilo la maridhiano leo linaloendelea, limetufanya tuwe wamoja na wenzetu wa vyama vingine vya siasa.

Mheshimiwa Spika, na haya anayoyafanya kwa kuzingatia mahitaji ya pande zote za Muungano na kwa sababu yeye mwenyewe ni mtu wa haki, na waswahili wanasema haki na usawa vinaposhamiri katika jamii yoyote undugu hujengeka na maovu hujitenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiona hili la maridhiano leo jinsi linavyoendelea limetufanya tuwe wamoja na wenzetu wa vyama vingine vya siasa. Na hii haishangazi kwa sababu

Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni tunda la CCM, chama kinachoamini kwamba, binadamu wote ni sawa, chama kinachotambua kwamba, kila mtu anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, chama kinachoamini katika misingi ya ujamaa na utu na ujamaa maana yake ni misingi ya utu, haki na usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni tuda halisi la CCM. Kwa kweli, ni tunda la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni tunda la hayati Abeid Amani Karume, ni tunda la Mzee Mwinyi, ni tunda la Hayati Benjamin Mkapa, ni tunda la Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ni tunda la Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ni tunda la CCM na ni tunda la Tanzania. Hii ni tunu ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamzungumzia mtu ambaye ameweka bayana kwamba, sauti yake na uwezo aliopewa na Mungu na nafasi aliyopewa ya kuwa Rais wa nchi yetu hapendi kumfokea wala kumkemea mtu, yeye mwenyewe anasema na tunamuona kutoka usoni. Matendo yake, kama ulivyoona juzi akipokea Ripoti ya CAG, katika mambo ya hovyo uliona uso wake; kwa mara ya kwanza ametoa maneno mazito kwa sababu amelazimika, ameona kuna watu hawatembeinae, hawatembei katika mapito ya njia anayoionesha. Wanafisadi uchumi wa nchi hii wakati yeye anahangaika halali kutafuta fedha kwa ajili ya ustawi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wachache wameamua kutumia fursa walizopewa katika uhujumu wa uchumi wa nchi. Katika jambo hili la msingi mama hakuweza kuficha sura yake ya ndani, ililazimika atoe kauli ambayo inawafanya wale wengine wote ambao wamepewa dhamana na Dkt. Samia Suluhu Hassan wajue kwamba, mama hafanyi masihara katika kuleta ustawi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndio maana natumia nafasi hii kuwataka wale ambao wamepewa dhamana na Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya tamko lake alipopokea Ripoti ya CAG na Ripoti ya TAKUKURU wachukue hatua kumsaidia Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa adhabu ambayo Watanzania wataiona. Hasira ya Mama Samia haiwezi kwenda bure, Bunge lako Tukufu lazima katika siku zinazokuja kwenye mkutano huu tutoe msimamo ambao utahakikisha kwamba, Hasira ya mama kwa wale waliofisadi uchumi wa nchi hii wanachukuliwa hatua bila kutizama sura zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muoneeni huruma, amekwenda Marekani amemleta Makamu wa Rais, amekwenda Falme za Kiarabu ameleta maendeleo, amekwenda Ufaransa ameleta maendeleo katika nchi yetu. Leo watu wachache tu waliopewa dhamana wanatumia nafasi hiyo kujineemesha wenyewe halafu bado mpaka leo imeshaisha wiki tangu ripoti imetajwa hatujasikia wakubwa wanachukuliwa hatua; tunataka wachukuliwe hatua, hatuwezi kumuunga mkono Rais kwa maneno, lazima tumuunge mkono Rais kwa vitendo. Na kama hamtachukua hatua tukiwa kwenye Bunge hili tutakuja na hoja nyingine dhidi ya wale ambao wamekabidhiwa dhamana na Rais ya kuwashughulikia hawa ambao bado hawajashughulikiwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alisema uhuru bila demokrasia ni udikteta, lakini demokrasia bila nidhamu ni fujo. Uhuru bila demokrasia ni udikteta na ndio maana mama amesema hataki kwamba, uhuru wetu ugeuke kuwa ni udikteta kwa watu wengine, amehakikisha kwamba, haki inashamiri katika nchi, misingi ya utu inasimamiwa, heshima ya mtu inathaminiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunasema pamoja na uhuru tuliopewa, lakini Mwalimu anasema uhuru bila demokrasia ni udikteta, lakini demokrasia bila ya nidhamu ni fujo; sasa

tutumie nafasi yetu ya uhuru tuliopewa kuhakikisha pia kwamba, hatufanyi fujo kwa kutumia uhuru huo bila mipaka, tujiongoze wenyewe ili tujenge Taifa ambalo lina ustawi, umoja na mshikamano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona umekaa mkao wa kuniashiria, lakini nitoe rai tu kwetu Watanzania wote na vyama ambavyo tunavyo vya siasa; kwanza nawapongeza viongozi wa vyama vya upinzani kwa kuendelea kufanya maridhiano na Rais wetu, kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania mbele. Sasa tumeanza vizuri, tumalize vizuri, tusiachane njiani, hii nchi inahitaji umoja na kila mtu na kila mmoja aweke tofali, nchi hii iendelee kusonga.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja hii. Na Mungu aibariki Tanzania, Mungu ambariki Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi ya kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya siku ya leo. Pia, nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa jinsi ambavyo unaliongoza Bunge letu Tukufu. Siku zote nimekuwa shahidi na Watanzania wamekuwa mashahidi juu ya uwezo wako na umakini wako katika kuliongoza Bunge letu Tukufu. Siku zote ukikaa hapo linapokuja jambo gumu, taaluma yako, uzoefu wako na umakini wako linakuwa ni jawabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana tu peke yake umeendelea kuonesha hivyo tulipokuwa tunapitisha Muswada wa Finance Bill. Katika Kifungu kile ulilazimika kuwaimamisha baadhi ya Wabunge waliokuwa kwenye Kamati ile kulikuwa na jambo dogo lakini kulikuwa na athari kubwa, lakini wewe mwenyewe uliliona kwa jicho lako na ukatufanya wote tulione. Nakupongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakika watu wa Mbeya wanaendelea kuona na kwa kweli ninahakika kelele zile hazitamnyima Tembo kunywa maji na mambo yatakaa vizuri tu, nichukue nafasi hii sasa kurudi kwenye hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Spika, ni kweli usiofichika kwamba hatua ya leo ya kuleta pendekezo na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Comrade Mohamed Mchengerwa na Wasaidizi wake wote, baada ya maamuzi ya Mheshimiwa Rais, kwanza, nichukue nafasi hii kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uamuzi huu wa busara. Mimi nitamke bayana kwamba maazimio yote mawili ninayaunga mkono kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kulinda, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za nchi ni jukumu la kila raia kwa mujibu wa Katiba, lakini suala la kumaliza migogoro kati ya Hifadhi za Taifa, maeneo yaliyohifadhiwa au maeneo yanayopzunguka hifadhi zetu za Taifa kwa kweli Wizara yako inayo dhamana hiyo na nafasi kubwa ya kusaidia katika kumaliza migogoro hiyo. Leo umeonesha kwa vitendo kwamba yale uliyosema wakati wa ziara zako ulipokuwa unatembelea Hifadhi za Taifa kwamba utahakikisha kero hizi zinashughulikiwa, leo umeshughulikia mpaka umeweza kumpelekea Mheshimiwa Rais na kwa mamlaka aliyonayo Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa sheria ameridhia kupunguzwa kwa hifadhi hizi mbili na moja kubadilishwa matumizi kutoka Hifadhi ya Taifa Kwenda TFS, hatua hii ni ya kimapinduzi na hatua hii ni faraja sana kwa wapiga kura wetu na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, nichukue nafasi hii sasa kumpongeza mwenye mamlaka mwenyewe aliyeridhia hifadhi hizi mbili, moja iweze kumegwa na nyingine iweze kubadilishwa kutoka katika hadhi ya Hifadhi za Taifa na kwenda kuwa chini ya TFS naye si mwingine ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninampongeza sana jinsi alivyowajali wapiga kura wake na Watanzania na ni jambo lake la kawaida, mimi nataka niseme wazi kwamba GN Na. 28 ya mwaka 2008, Kamati imethibitisha na wewe mwenyewe umethibitsha kwamba kwa kweli ushirikishwaji haukutosha, ndiyo maana wananchi walikuwa wanalalamika sana katika maeneo hayo ambayo GN Na. 28 iliweza kuondoa baadhi ya maeneo ya wakulima, wafugaji na kuyaingiza maeneo hayo katika Hifadhi ya Taifa bila ushirikishwaji wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni rai yangu tu kwamba sasa mmefanya maamuzi ya hekima, maamuzi haya yamefanyika baada ya ziara yako Mheshimiwa Waziri lakini pia baada ya ziara ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Ninataka nichukue nafasi hii kuipongeza Kamati, kukupongeza wewe na msaidizi wako Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Mtendaji Mkuu wa TANAPA na Mtendaji Mkuu wa TFS.

Mheshimiwa Spika, niseme bayana kwamba, kama tukifanya hivi katika maeneo mengine kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi wetu katika kuinua na kushughulikia masuala yao ya kiuchumi tutakuwa tunafanya maamuzi ya kushughulikia ustawi wa watu wetu. Ni dhahiri basi kwamba haya yaliyofanyika Ruaha, yaliyofanyika Kigosi yakiendelea pia kufanyika Kanda ya Kaskazini mwa nchi yetu itasaidia sana kupunguza migogoro iliyoko huko.

Mheshimiwa Spika, nieleze bayana kwamba Mheshimiwa Waziri nina imani nae kubwa sana, ninaimani kwa sababu anatoa muda wa kusikiliza Wabunge, na mimi amenisikiliza katika suala la migogoro tuliyonayo katika eneo lile, ninaamini busara uliyoitumia baada ya kwenda kule Ruaha, ninakuomba na nikualike rasmi uje Kanda ya Kaskazini kwa maana ya Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Arusha, ndipo mtakapoweza kujua kwamba changamoto kubwa waliyonayo wafugaji katika Wilaya za wafugaji na hata migogoro ambayo inatokana na mchakato unaoendelea wa timu inayofanya tathmini ya maeneo yenye rasilimali za wanyamapori katika mapori ya maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, hali hii imeleta taharuki kubwa sana kwa sababu tumetoa kama wafugaji maeneo ya hifadhi mnazozijua, haibishaniwi kwamba tumetoa mchango mkubwa Serengeti, Tarangire, Lake Manyara, Ngorongoro na tumetoa mchango mkubwa Mkungunero lakini bado mpaka leo katika ardhi ambayo iko kwenye nyanda kame, ardhi ambayo haitoshelezi malisho ya mifugo iliyoko leo, bado kuna mawazo na watu wanaopita katika kuangalia maeneo ambayo tumeyatenga kwa ajili ya malisho ya mifugo, ambapo tunapotenga maeneo ya mifugo ndiyo hayo hayo ambayo wanyama wetu ambao ni rasilimali za nchi wanapopata malisho kwa muda kabla hawajarudi katika Hifadhi za Taifa, mapori tengefu na mapori ya akiba.

Mheshimiwa Spika, kinachoshangaza sasa zoezi linaloendelea ambalo linajumuisha Wizara kadhaa linachukua sura sasa ya kutaka kuanzisha hifadhi nyingine katika eneo la Olokisale Game Controlled Area, eneo lote la Simanjiro Game Controlled Area, eneo lote la Southern Ruvu Masai Game-Controlled Area, eneo la Lake Natron Game Controlled Area, eneo la Longido Game Controlled Area.

Mheshimiwa Spika, nikueleze athari inayojitokeza ni hii, ni dhahiri kwamba maeneo niliyoyataja yanaifanya Simanjiro kwa ujumla kuwa ni eneo ambalo awali kulingana na Sheria ya Fauna Conservation ordnance ya Mwaka 1951 ilikuwa ni Wilaya nzima za Masai zilikuwa chini ya game-controlled area. Sasa kama maeneo yale tumeshayatoa kwenye hifadhi hizo na tumebaki na maeneo madogo ya malisho ambayo hayatutoshelezi leo, Mheshimiwa Waziri, nachukua nafasi hii kukualika naomba uje tutembee na wewe kijiji kwa kijiji, eneo kwa eneo ujue umaskini ulioingia huko umasaini katika Wilaya za wafugaji hao kutokana na maeneo kutowatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Kanda yetu ya Kaskazini mwa Wilaya ya Simanjiro na Ukanda wa Mashariki, mvua iliyopita mwaka huu haijanesha katika ukanda huo, maana yake mifugo yote ya Simanjiro iko katika Kata mbili za Loiborsiret na zingine zimevuka mpaka kuingia Kata ya Makame na Ndedo katika Wilaya Kiteto.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea leo ni kutaka tena kuchukua maeneo yale na kuyageuza kuwa Hifadhi au Game reserve au Game Controlled Area. Ninataka niiombe Serikali yangu sikivu ya CCM kwamba jambo hili naomba mliache. Liacheni maana maamuzi yenu haya ya juu yasiyo shirikishi, yana athari kubwa katika ngazi za msingi, ngazi zetu za Majimbo, Kata, Vijiji na Mitaa. Tunaomba sana tushirikishane.

Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji unaotakiwa kwa mujibu wa sheria, kushirikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ardhi za vijiji ni mikutano mikuu ya vijiji, Halmashauri za Vijiji na Halmashauri za Wilaya ziweze kutoa maoni yao juu ya namna bora ya kutoka pale. Ninaimani sana na Mheshimiwa Mchengerwa, ninaomba ufike uione hali halisi, usiletewe na wataalam usije ukauziwa mbuzi kwenye gunia.

Mheshimiwa Spika, juzi liliendelea zoezi moja lililokuwa Kimotoro Kata ya Kimotoro katika Wilaya ya Simanjiro na kijiji kilichopo Wilaya ya Kiteto katika eneo linalopakana na Mkungunero Game Reserve, kinachoshangaza Mawaziri Nane wakiongozwa na Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, walifika katika maeneo hayo na kueleza maeneo ambayo Serikali imeridhia kuyarudisha kwa wananchi. Kilichokuja kutekelezwa katika uhalisia wake siyo kile ambacho kilitangazwa na Mheshimiwa Lukuvi.

Mheshimiwa Spika, kinachoogopesha kuliko yote kwa sababu mpaka wa Simanjiro na Kondoa ndiyo mpaka wa Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Dodoma, kilichokuja kujitokeza katika tafsiri iliyokuwa inafanywa pale, kimsingi hata mtu aliyeishia darasa la saba anajua kabisa kwamba kilichofanyika hapa siyo sahihi, ninaomba Waziri mkae na Makongoro Nyerere awasaidie. Makongoro Nyerere alikuwa sahihi katika suala la mpaka wa Dodoma na Manyara kwa maana ya mpaka wa Wilaya ya Kondoa na mpaka wa Wilaya ya Simanjiro.

Mheshimiwa Spika, ile GN iko bayana hauhitaji kwenda kwenye darasa kubwa sana ili kujua, unaambiwa tu wazi kwamba, unatoka katika Mlima uliotajwa kwenye GN hiyo ya kuanzisha Wilaya ya Masai ambayo ndiyo GN ya kuanzisha Wilaya ya Kondoa, inaweka bayana kabisa na ninaomba ninukuu na ninatangaza tu point moja ambayo ndiyo inaleta mgogoro na ndiyo GN ilipo, inasema wazi kwamba, “… South - South East to a point four Miles, West South West of Mikuyuni Mikunga ….”

Mheshimiwa Spika, Mikuyuni Mikunga ndiyo beacon tunayogombania na wenzetu ambayo inahamisha leo nusu ya Kitongoji cha Kijiji cha Kimotoro kwenda Wilaya ya Kondoa. Badala ya kwenda hiyo Magharibi mile Nne ambayo Mlima uko hapa nilipo, kisima kipo hapo alipokaa Waziri wa Nchi, unatarajia Four Miles West South West ya alipokaa Mheshimiwa Jafo ndiyo inafanya kuwa kile kisima kinachotamkwa. West south west Four miles, kama hapo ulipo maana yake unakwenda kulia lakini wao wanakwenda kule alikokaa Mheshimiwa Waziri wa Madini.

Mheshimiwa Spika, sasa unajiuliza hapa nilipo ndiyo mlima ulipo unaambiwa nenda west south west four miles kutoka kwenye kisima hicho ambako ndiko aliko Mheshimiwa Jafo, badala ya kunyooka kwenda kutafuta point upande wa Magharibi, unakwenda kutafuta point upande wa Mashariki na kuweka jiwe, kwa maana hiyo, unahamisha mpaka wa Mkoa badala ya kwenda magharibi ambayo inaingia TANAPA ndani ya eneo la Tarangire unalazimisha kwenda mashariki ambapo unaathiri Kijiji kizima cha Kimotoro kuihamishia Wilaya ya Kondoa.

Mheshimiwa Spika, sasa GN hii ni yam waka 1961 GN Na. 65…

SPIKA: Mheshimiwa, dakika moja malizia mchango wako muda umekwisha.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba tu uniongeze dakika moja ikikupendeza.

SPIKA: Mheshimiwa, ndiyo hiyo niliyokuongeza.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru Mkuu.

Mheshimiwa Spika, maana yangu ni nini? Kiacheni kitongoji cha Arkasupai kilichopo pale Kimotoro katika Wilaya ya Simanjiro kwa sababu GN yenyewe inawataka wabaki pale. Ninaomba Mawaziri mje wenyewe mshuhudie tafsiri potofu iliyotolewa hapo. Hatuna taabu hata ikitamkwa kwamba mpaka ndiyo huu lakini Rais anahitaji eneo hili kwa ajili ya hifadhi. Sisi ni wahifadhi lakini zaidi Mheshimiwa Waziri nikualike tuangalie njia za mapito ya wanyama uone jinsi sisi tulivyo wahifadhi wazuri. Angalia eneo la Natron linaathiri mno Longido, angalia lile eneo lingine la GN zile GSA za Simanjiro tusaidie ili tutoke pale.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikiwa ninaimani kabisa kwamba Mheshimiwa Mchengerwa atatupatia muda wake wa ziada basi ninaomba niunge mkono hoja katika mapendekezo haya yote mawili na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutubeba katika barabara yetu kubwa ya kihistoria. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuliongoza Taifa hili na hatua aliyokwisha lifikisha Taifa hili kwa mwaka mmoja ni hatua kubwa sana ambayo kila mtu ni lazima aiunge mkono.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee pia nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha Daktari Mwigulu, kuanzia hotuba yake ya Mpango na hotuba yake pia ya Bajeti, Mheshimiwa Waziri ninakutakia kila lililo jema kwa sababu mipango bora ya sasa ndiyo itakayoamua kesho iliyo njema ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye hoja ambayo ningetaka nigusie na maeneo ambayo nimeyachagua kuyazungumza. Nianze kwa kuyanukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo, ukurasa wa Tisa naomba kunukuu kwa ruhusa yako. ‘‘…..kama tunataka maisha yetu yawe na amani na raha na kama tunataka kufanikiwa katika shabaha zetu na kuinua maisha yetu, basi lazima tuwe na uhuru pamoja na utii. Maana uhuru bila utii ni wazimu na utii bila uhuru ni utumwa’’. Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba tena nifanye nukuu ya pili ili niendelee na ninaifanya katika imani za mwanachama wa CCM, nataja imani ya kwanza na imani ya pili, inasema… ‘‘binadamu wote ni sawa na ya pili ninasema kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake’’. Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, jamii ninayotokana nayo, jamii ya Wafugaji au jamii ya Wamasai katika kipindi hiki wanapita katika taharuki na huzuni kubwa kutokana na maamuzi ya Serikali yanayoendelea katika eneo la Ngorongoro, eneo la Loliondo na sasa tamko la Waziri wa Maliasili na Utalii juu ya nia yake ya kutangaza kupandisha hadhi baadhi ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba.

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuuu maneno ya Waziri wa Maliasili na Utalii katika hotuba yake aliyoitoa Tarehe Tatu yanasema hivi …. ‘‘eneo la Idara ya Wanyamapori; Mheshimiwa Spika, Wizara inatarajia kupandisha hadhi mapori tengefu ya Lake Natron, Kilombero, Loliondo, Lolkisale, Longido, Muhuwesi, Umba River, Mto wa Mbu, Simanjiro, Ruvu Masai, Ruvu Same na Kalimawe, misitu ya Litumbandyosi na Gesimazoa kuwa mapori ya akiba. mwisho wa kunukuuu.

Mheshimiwa Spika, suala la mapori tengefu kupandishwa hadhi, kwa maana maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ameyatamka katika Wilaya ya Simanjiro maana yake Simanjiro kwa ujumla wake sasa inatarajiwa kupandishwa hadhi kwenda kuwa pori la akiba, maana Simanjiro kwa asilimia 100 ni pori la akiba kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 1951 ya Fauna Conservation Ordinance Sura ya 302. Mapori yale yalipotangazwa Simanjiro yote na niseme the whole of Masai land wakati wa Masai District Council karibu yote ukiacha maeneo ya National Parks ni game controlled areas.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Fauna Conservation ilikuja kubadilishwa na Sheria ya Uhifadhi ya mwaka 1974, na Sheria ya 1974 ya uhifadhi ilifutwa na Sheria Na. 5 ya Mwaka 2009. Sheria zote Mbili nilizozitaja za mwanzo Fauna Conservation Ordinance na Sheria ya Uhifadhi ya mwaka 1974 hayakufanya maeneo ya Game Controlled Areas au maeneo ya mapori tengefu kuwa maeneo yanayokataza malisho makazi na vijiji kuanzishwa ndani ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, sheria mpya ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 iliyafanya mapori tengefu kuwa na hadhi ambayo shughuli za binadamu haziruhusiwi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa maana hiyo Waziri alitakiwa kwa mujibu wa sheria hiyo na hasa Kifungu cha 16(1) ilimtaka Waziri kutamka na kutangaza katika gazeti la Serikali eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa pori tengefu, lakini sheria hiyohiyo Na. 16 Kifungu Kidogo cha (4) ilimpa Waziri huyo muda wa kuchukua zoezi hili la kuyapitia mapori hayo tengefu yote ambayo yako 49.

Mheshimiwa Spika, Kifungu hicho cha 16 cha Sheria ya Warrant Conservation Act, ikamkataza Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii kuingiza eneo lolote la ardhi ya Kijiji katika eneo hilo la pori tengefu. Kwa maana hiyo ni kwamba hakuna ardhi ya kijiji ambayo kwa mujibu wa sheria itageuzwa kuingizwa katika ardhi ya pori tengefu, na kwa maana hiyo shughuli zinazoendelea katika Tarafa ya Loliondo na Sale ya kuchukuwa ardhi vijiji vya Kata Saba, Nane za Tarafa ya Loliondo na Sale na kuunda pori tengefu la Loliondo katika sura ya sheria niliyoitaja, ni zoezi batili na linastahili kukemewa na mtu yoyote anayeyatakia mema Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, ninasema hayo kwa kutaja vifungu hivyo vya sheria vinavyokataza kuchukua ardhi ya Kijiji na kuifanya kuingia katika pori tengefu, lakini wakati Loliondo yakiendelea na ya Ngorongoro yakiendelea Waziri mwenye dhamana kana kwamba haoni jeraha hilo kwa jamii ya wafugaji, anatangaza sasa kuifanya Simanjiro kwa ujumla wake kuwa pori la akiba ndiyo kusudio lake, kwa maana ya mapori tengefu aliyoyataja. Kwa lugha nyingine anatangaza Wilaya nzima ya Longido kwa kuchukuwa Natron game controlled area na Longido game controlled area, sasa Longido yote kwa asilimia 100 kwa nia ya Mheshimiwa Waziri Pindi Chana sasa itatarajiwa kuwa pori la akiba na sijui wananchi wale wanaenda wapi. Kana kwamba hiyo haitoshi eneo la Ngorongoro lililokuwa limebaki katika Tarafa ya Sale na Loliondo nalo linamegwa katika sura hii.

Mheshimiwa Spika, ukiondoa eneo la Km 8,300 za Tarafa ya Ngorongoro eneo linalobaki kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro ni Km. za mraba sizizozidi 2007 kwa watu wapatao zaidi ya 180,000. Jambo hili kwa vigezo vyovyote vile haiwezi kukubalika, ushauri wangu kwa Serikali yangu Chama cha Mapinduzi, ni kukaa na wananchi katika eneo la Loliondo, na kuwashirikisha kama ambavyo barua ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda ilivyoelekeza alivyokuwa amemuandikia Mkuu wa Mkoa wakati huo wa Mkoa wa Arusha kwamba wananchi washirikishwe kwa sababu sheria haziruhusu kulichukuwa eneo hili na kulifanya kuwa Pori Tengefu.

Mheshimiwa Spika, kugeuza ardhi za Wilaya hizo zote za Masai maana wamasai wana Wilaya hizo nne ndiyo ambalo ndiyo wako majority leo kuyageuza yote kuwa mapori ya akiba yanatwisha mzigo wa kujiuliza dhamira yake ni nini?

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mary Masanja.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa ambae ametoka kuzungumza sasa kwamba hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii iligusia maeneo ambayo hayatahusisha maeneo ya vijiji vya wananchi, kwa hiyo maeneo yanayoenda kupandishwa hadhi, kutoka mapori tengefu kwenda mapori ya akiba ni maeneo potential tu kwa ajili ya uhifadhi na hayana wananchi ndani yake. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka unapokea taarifa hiyo?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie wala siIpokea maana wala haina hadhi ya taarifa, kwa sababu akisoma section 16 sub-section (5).

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naam!

SPIKA: Kanuni unazifahamu vizuri, unapokea taarifa au unaikataa unaendelea na mchango wako.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, ninakataa siIpokei, kwa sababu ukweli unabaki hivi kwamba alichokitangaza Waziri ni kupandisha mapori ya akiba yaliyoanzishwa na Fauna Conservation Ordinance kuwa game reserve, wakati yeye mwenyewe anajua kabisa kwamba pori, game reserve inaanzishwa na Rais kwa mujibu wa Kifungu cha 14, anamuuzia Rais Mbuzi kwenye gunia kwa sababu yeye mwenyewe hana mapori tengefu hajayaanzisha, kwa mujibu wa Sheria hiyo Na. 16 (1). hujaanzisha kitu halafu unamwambia Rais aanzishe pori la akiba na unafanya hivyo katika Wilaya Nne kamili. Kwa kweli nia hiyo siyo ni njema na Wizara hiyo mnapaswa mjitafakari, muangalie na mpitie maamuzi yenu, lazima yajenge haiba nzuri kwa nchi yetu, yajenge haiba nzuri kwa raia waliotuchagua yajenge haiba nzuri ya nchi yetu katika uso wa dunia.

Mheshimiwa Spika, nataka nirudie kusema….

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka nakulindia muda wako Makatibu mtazame hapo.

Mheshimiwa Naibu Waziri, hii taarifa uliyoitoa kwamba maeneo yale yanayopandishwa hadhi hayana wananchi, Mbunge anasema hayo maeneo yana wananchi, sasa hebu fafanua vizuri hapo, kwa sababu upotoshaji upo kona gani kwenye hoja hii. Hayo maeneo yanayo wananchi au hayana wananchi ili kama hayana wananchi mchango wa Mheshimiwa Ole-Sendeka nitakuwa na mazungumzo nao huo mchango wake kama maeneo hayana wananchi.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nirudie tena ili muongeaji asikie vizuri. Haya maeneo ni maeneo ambayo yalikuwa ni mapori tengefu Game Controlled Areas. Maeneo haya yanapokuwa na hadhi nzuri na haya maeneo kwa asilimia kubwa yanawawekezaji tayari, hivi ninavyoongea kuna wawekezaji ndani yake, kuna wawindaji wa kitalii nakadhalika. Tunapoona yana sifa ya kuhifadhiwa ili wananchi wasiendelee kuwasongelea tumeyapandisha hadhi. Game controlled area inapanda kuwa game reserve, game reserve inapoongezeka kuwa sifa tunapeleka kwenye National Park. Sasa tumeona haya maeneo yana hadhi ya kupanda kutoka kwenye Game Controlled Areas kwenda kwenye game reserve na hayana wananchi.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie hili aelewe vizuri, amesema kwamba asilimia 100 ni maeneo ya wananchi, na hii kauli niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanapotumia maeneo eti ardhi yetu, Tanzania ardhi ya Umma, siyo ya mtu mmoja. Tunawagawa wananchi tunaposema kwamba haya ni maeneo ya kwangu, haya ni maeneo ya nani!

Mheshimiwa Spika, tunapoona haya maeneo hayana watu tumeyahifadhi vizuri na yamekuwa na sifa nzuri, tunayapandisha hadhi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni asilimia 100 haya maeneo hawamo wananchi ndani yake. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka nimekusikiliza kwa makini sana, ukizungumzia hizo sheria, ukivitaja na vifungu. Maelezo niliyomtaka atoe ya ziada Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambayo wananchi ndiyo maneno kama haya yanayozungumzwa, kwamba wananchi watahamishwa hayo maeneo yote wanayoishi huko ndiyo yanayoleta taharuki! Kwa mchango wako Mheshimiwa Ole-Sendeka unaashiria kwamba wananchi wote wa Simanjiro asilimia 100 watatakiwa kutoka huko kwa agizo la Mheshimiwa Waziri. Hebu fafanua hapo ili mimi nijue upotoshaji upo sehemu gani.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, mapori tengefu hayo ambayo Waziri anayazungumza kwanza ili uyajue ni mapori tengefu ambayo yalishafutwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 na yakamwelekeza Waziri hivi….

SPIKA: Kwa kuwa sheria unayo hapo nisomee Mheshimiwa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba nikusomee.

SPIKA: Nisomee.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, for the purposes, nakusomea section 16 subsection (5). …. ‘‘for purposes of subsection (4), the Minister shall ensure that no land falling under the village land is included in the game controlled areas. Lakini….

SPIKA: Nisomee subsection four.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, ngoja nirudi sasa exactly, ngoja nikuanzishie na hiyo subsection (4), safi sana nakushukuru sana. Ninaanza na one ili tuenda four.

SPIKA: Soma four, tutaenda kwa mtiririko huo mpaka tutafika sehemu nzuri wala usiwe na wasiwasi soma subsection four.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, subsection four, The Minister shall, within twelve months after coming into operation of this Act and after consultation with the relevant authorities, review the list of game-controlled areas for the purposes of ascertaining potentiality justifying continuation of control of any of such area.

Mheshimiwa Spika, sasa subsection (1)...

SPIKA: Sawa ngoja umeshanisomea hiyo 16 ngapi ngapi na nimekusikiliza, sasa hebu nisomee kwenye hiyo hiyo sheria kifungu kilichofuta, kwa sababu umesema hiyo sheria imefuta hayo maeneo, hebu nisomee hicho kifungu kilichofuta, nakupa muda nisomee kifungu kilichofuta.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, kifungu cha 16 nilichokusomea kwamba Waziri atayapitia mapori hayo tengefu na ku…

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka kupitia ni sawasawa na kufuta?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, ndio nilikuwa nataka nikusomee, twende moja turudi nne, twende tano ili wewe Mwanasheria utusaidie.

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka sheria huwa inasomwa namna ulivyoanza, wakakuambia subject to subsection (4). Kwa hiyo, kabla hujamaliza kile unakwenda kwenye kifungu kidogo cha (4) ambayo umeshanisomea. Sasa katika kifungu kidogo cha (1) mpaka (4) kuna mahali wanasema wamefuta, kwa sababu ile kifungu kidogo cha (1) uliyonisomea na (4) uliyonisomea, hakuna mahali niliposikia yamefutwa. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, sitaki kubishana na wewe katika angle ya sheria.

SPIKA: Kwenye hoja hii mimi ndiyo niliyekupa ruhusa kwa sababu nazungumza nawe..

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Ili nielewe upotoshaji upo wapi?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, kweli ni hivi kabla sheria hii ili utusaidie wote, maeneo ya Game Controlled Area ilikuwa ni ardhi ambayo ni ardhi za vijiji kwa wakati huo. Kwa hiyo...

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka sheria unayo wewe mwenyewe, nimekwambia usome wewe mwenyewe na mimi nakusikiliza, sasa nakupa nafasi hebu soma hicho kifungu kidogo cha (1) mpaka (4) labda nitasikia mahali uliposema pamefutwa hebu soma.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba kwenye section 16 (1); subject to section 4(2) of the Land Act, the Minister may, after consultation of the relevant local authorities, and by order in the Gazette, declare any area of land in Tanzania to be a Game Controlled Area.

Baada ya mamlaka hayo ya kutamka na kutangaza…

SPIKA: Nisomee umalize ili tuwe tunasikilizana, soma moja mpaka nne kama ulivyosema na mimi nakusikiliza kwa makini sana. Soma sheria yako uliyonayo, usiongezee maneno kwa sababu nitahisi pengine umeanza kutafsiri. Wewe nisomee ili mimi na wewe twende ngazi kwa ngazi.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE – SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nilishakusomea kifungu kinachoanzisha Game Controlled Area na ambacho ni kifungu cha 16(1), nimeshakusomea kifungu hicho cha …

SPIKA: Umesema nikupe nafasi unisomee kifungu cha 16(1) mpaka (4) ndio nitaelewa, si ndio umesema hivyo?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, sawa kwa hiyo nirudie.

SPIKA: Nisomee pengine nitasikia neno la kufuta ili nimshike sasa Naibu Waziri kwamba yeye ndio anayezusha.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, naomba nirejee kwenye wapi ambapo nimenukuu kwamba sheria moja inapoanzishwa inafuta nyingine, naomba nimnukuu barua iliyoandikwa na Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda.

SPIKA: Naomba unisomee Sheria kifungu cha 16(1) mpaka (4).

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, sawa niende kwenye (4), niende kifungu 16(4).

SPIKA: Kifungu kidogo cha (2) umeshasoma tayari?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, no hapa...

SPIKA: Nisome (1) mpaka (4), mimi ninakurahisishia ili nikuelewe, nakulinda na Naibu Waziri naye namlinda.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nilinukuu kwenye sheria na nikawa nakusomea kwa hiyo (2) haikuwa na uhusiano na hoja yangu, kwa hiyo ambazo nimezitaja ndizo zilikuwa na uhusiano na hoja yangu.

SPIKA: Kama hivyo ndivyo, maelekezo yako marefu niliyoyasikiliza, kifungu cha 16(1) na 16(4) ulivyonisomea, hakuna mahali panaeleza kwamba hayo mapori tengefu yaliwahi kufutwa. Hakuna na kwa maelezo aliyoyatoa ya ziada Mheshimiwa Naibu Waziri hakuna mahali ambapo maelekezo ya Waziri mwenye sekta yanasema watu wa Simanjiro na pori tengefu wanaondoka, hakuna. (Makofi)

Sasa haya maneneo ya kwamba maeneo yote ambayo wanakaa Wamasai katika Wilaya nne zote wanaondoka, yametoka wapi?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, hapo ndiyo mahali ningeomba wote wanisikilize. Kabla ya sheria hii tunayozungumza namba tano, maeneo yaliyokuwa yanaitwa mapori tengefu ni maeneo ambayo shughuli za binadamu zilikuwa zinaruhusiwa na zilikuwa zinahifadhiwa kwa mujibu wa sheria hizo mbili nilizozitaja ya mwaka 1974 na ile ya mwaka 1951. Ilipokuja sheria hii ndiyo ikapandisha pori tengefu kupewa hadhi sasa ya kuwa ya miongoni mwa reserved lands ambazo shughuli za binadamu haziruhusiwi. Ili hilo liwezekane ilikuwa lazima mapori hayo yapitiwe kama ilivyosema section (4) halafu mwishoni yatangazwe na Waziri mwenye dhamana baada ya kufanya consultation na local authorities.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo...

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka unanipa wakati mgumu sana, kwa nini unajua? Sheria uliyosoma hapo imetumia neno may, mimi nikakusikiliza kwa sababu wewe unajua sheria, mimi pia ni Mwanasheria. Umesoma mwenyewe hapo, hakuna mahali palipofuta, hilo ni la kwanza, maana ulianza kwa kusema kwamba sheria ilifuta hujasema ni wapi sheria ilifuata, moja.

La pili, umesema maeneo yote wanayokaa Wamasai maeneo ambayo ni mapori tengefu, Wamasai wanaondoka kwa sababu maeneo hayo yamepandishwa hadhi. Mheshimiwa Naibu Waziri pale ametoa ufafanuzi kwamba si kweli maeneo yanayopandishwa hadhi wananchi huko hawapo. Kwa hiyo hapo wewe ukiambiwa kwamba unazikosea kanuni zetu, ukiambiwa wewe Mheshimiwa Ole-Sendeka unazikosea kanuni zetu, kwa nini? Kwa sababu umesema jambo ambalo halipo, kwa sababu la sivyo wote ninyi, jamani mimi ndiyo shughuli yangu hapa ya kusimamia kanuni.

Mheshimiwa Ole-Sendeka tukiendelea kwa mtindo huo, nitataka uniletee ushahidi na Mheshimiwa Waziri ataleta na yeye wa kwake, halafu mimi nitafanya maamuzi kama unashikilia huo msimamo wako. Nilitaka nikurahisishie ili kama huna uhakika na hicho unachokisema tuliachie hapo, kama unao uhakika nitataka wewe uniletee ushahidi na Waziri aniletee ushahidi na si ushahidi ule ambao umeusema hapa Mheshimiwa, kwa nini? Kwa sababu hapa nimekuongoza vizuri, hiyo sheria inachosema, nitakapokutaka ulete ushahidi siyo ushahidi wa hivyo vifungu vya sheria kwa sababu hivyo vinakukaba wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Ole-Sendeka nakupa hiyo nafasi.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu hapa nazungumza habari ya tafsiri ya sheria na mimi siyo bingwa kwenye eneo hilo, naomba niondoe hoja hiyo katika sura hii. (Makofi)

SPIKA: Sasa Katibu alikuwa amekutunzia muda wako kama nilivyoahidi, kwa hiyo sasa endelea na mchango wako. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE–SENDEKA: Mheshimiwa Spika, katika barua ya Waziri Mkuu naomba nifanye nukuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda alisema hivi, nanukuu: “Mwaka 1974, Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori ilianzishwa na kufutwa Sheria ya awali ya Fauna Conservation, Sura ya 302. Chini ya sheria hizo mbili masuala ya malisho na makazi hayakukatazwa katika maeneo ya pori tengefu ikiwa ni pamoja na Pori Tengefu la Loliondo. Sheria hiyo ya Hifadhi ya Wanyamapori iliendelea kutumika hadi mwaka 2009 ambapo sheria mpya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya The Wildlife Conservation ya mwaka 2009 ilianzishwa na kufuta ile ya awali ya mwaka 1974.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni barua ya Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda alipomuandikia Mkuu wa Mkoa baada ya kuchambua hali ya mgogoro wa Loliondo na haya ndiyo maneno ambayo nimeyanukuu.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho, baada ya Waziri Mkuu kupokea maoni ya wananchi wa Loliondo alikuja na uamuzi huu. Kwanza amebainisha kwamba maoni ya wananchi kwa ujumla yanataka eneo hilo kumilikiwa na wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia kuhifadhi kwa taratibu zao za kimila na desturi za jadi, lakini mwisho kabisa Waziri Mkuu alitambua hali iliyokuwepo ya wananchi kutokushirikishwa awali katika uamuzi huo.

Mheshimiwa Spika, ninalotaka kuishauri Serikali kwa sasa ni kwamba ikitaka kwenda kuanzisha mapori tengefu kwa sababu ni matakwa ya sheria kushirikisha wananchi, hakuna mwananchi wa Simanjiro aliyeshirikishwa kuanzishwa kwa pori tengefu, kinachotakiwa sasa ni waje watushirikishe ili wapate pori tengefu ambalo watamshawishi Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kifungu cha 14 alipandishe hadhi kuwa pori la akiba. Hiyo ndiyo hoja yetu ya msingi ambayo tunazungumza na hicho ndiyo kilio cha wafugaji katika maeneo hayo niliyoyataja ambayo yameathiriwa na mapori tengefu hayo niliyoyataja.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na hoja nyingine moja ya uagizaji wa mafuta kwa njia ya bulk procurement. Ni jambo la busara sana kama tunataka kupunguza gharama za mafuta na kuondoa mzigo kwa wananchi, tuyaachie makampuni yote yenye nia ya kuleta mafuta nchini, kazi yetu iwe kuangalia usafi na ubora wa mafuta pale yanapoingizwa badala ya kuwa na makampuni sita au nane. Hii itasaidia kuhakikisha kwamba tunapunguza ugumu wa maisha na jambo hili halina sababu kuendelea kufichwa, tuendee tuweke uwazi kwa kuwakaribisha watu wote wenye uwezo wa kuleta mafuta.

Mheshimiwa Spika, nimwombe pia Waziri mwenye dhamana ya Nishati ya kupitia suala la vinasaba katika mafuta ambapo Wizara ilikuwa imeipatia kampuni moja uwezo wa kutosha shilingi saba kwa kila lita ya mafuta na iliingizwa kwenye pricing template ya mafuta na kampuni hiyo siyo kampuni nyingine ni kampuni ambayo imefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 ya GFI ikishirikiana SICPA SA ambayo ilikuwa ime-tender bei mara mbili zaidi ya washindani wenzake ambao walikuwa wameomba katika zabuni hiyo. Nakusudia baadaye kuleta hoja katika Bunge lijalo ili mambo haya yaweze kuwa wazi na kuweza kunusuru katika nchi yetu katika mzigo huu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, maana naona umeshika microphone.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi ya kwanza kukushukuru wewe mwenye kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye eneo linalonihusu la madini ya vito. Lakini kabla ya kufika huko niseme, waswahili wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, kwa muda mfupi niliokaa kwenye Bunge hili baada ya kurudi juzi Waziri Biteko amefika katika eneo la Mererani kama mara tatu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nilimnong’onezea juu ya kero zinazowakabili wachimbani wa madini ya vito aina ya Tanzanite pale Mererani. Kwa wale wasiofahamu wachimbaji wapatao kati ya 8,000 au 10,000 wanaingia na kutoka katika eneo la machimbo ya Mererani; 8000 – 10000 kwa siku. Nilimuomba Mheshimiwa Waziri asaidie kujenga shade ambayo ingeweza kusaidia wachimbaji wale kujikinga wakati wa mvua na wakati wa jua. Mheshimiwa Biteko alichukua uamuzi palepale na kutoa maelekezo na tatizo hilo sasa linakaribia kufika ukingoni maana jengo hilo linajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimuomba Mheshimiwa Waziri aweke utaratibu rafiki unaoweza kuwasaidia wachimbaji wadogo na hasa wale wakipato cha chini kuweza kumudu kuendesha biashara katika eneo la uzio wa Mererani, nilipata majibu positive na alitoa maelekezo ambayo ni rafiki na wachimbaji walimpongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimuomba sana Mheshimiwa Waziri aliondoshe janga lililokuwa mbele yetu kitendo cha… natafuta lugha ya staha; kitendo cha fedheha cha ukaguzi usio na staha, wanaofanyiwa wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mererani ambapo watu wapato 20 au 15 wa rika mbalimbali wanapotoka kwenye uchimbaji wakifika kwenye gate kuna vyumba viwili vya ukaguzi, kimoja cha wanawake na kimoja cha wanaume. Wanaume zaidi ya 20 au 15 kwa wakati mwingine; wanawekwa kwenye chumba hicho na kuvuliwa nguo zote, zote; na katika chumba cha wanawake vivyo hivyo, wanaingia kwenye chumba hicho bila kujali rika, bila kujali nini wanavuliwa nguo zao zote na wanaambiwa waruke kichura kidogo kitendo ambacho ni cha aibu. Haitarajiwi kwa Taifa kama letu ambalo linatambua na kuthamini misingi ya utu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini cha kustaajabisha zaidi, Mheshimiwa Waziri alitoa kauli mbele ya wachimbaji wadogo na mbele yangu kwamba jambo hili likome sasa na ukaguzi wa staha ufanyike. Alisema hivyo katika ziara yake ya kwanza, akarudia mbele ya Kamati ya Madini, baada yake siku iliyofuata ikaja Kamati inayoshughulika na masuala ya Ulinzi na Waziri wa Ulinzi ambaye ndiye anayeshughulikia mambo ya ulinzi wa madini pale getini.

Mheshimiwa Spika, ninapata mashaka, kwasababu Serikali haikuongea lugha moja, Wizara hizi mbili hazikuongea lugha moja na juzi tumefanya kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati kwa pamoja kujadili masuala ya Mererani. Kinachoshangaza hata baada ya ombi langu mbele ya Kamati hizo mbili ya Nishati la Kamati ya Ulinzi; hata jana na leo asubuhi ukaguzi unaoendelea ni ule ule, walichotofautisha ni kwamba wamiliki wa migodi na mameneja wa migodi wamepewa mlango wao wa kutokea na kwamba hawavuliwi nguo hao. Lakini wale maelfu wengine waliobaki wanaendelea na kitendo hicho cha fedheha.

Mheshimiwa Spika, waislam wanasema; “ukiliona jambo ovu liondoshe, kama huwezi kuliondosha lishtakie kwa mwenye uwezo kuliondosha na asipoliondosha endelea kulinyooshea kidole mpaka atakapopita mtu wa kuliondosha.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ovu, ni jambo ambao halijarajiwi litendeke hasa na Serikali ya chama changu Serikali ya CCM. Ninataka maelezo ya Mheshimiwa Waziri leo, kauli ya Serikali itolewe na kwasababu kuna kujikanganya kati ya Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Madini. Waziri wa Madini yupo clear kwenye jambo hili, Waziri wa Ulinzi anapata kigugumizi, Waziri Mkuu atoe kauli juu ya jambo hili, kama Tanzania tumefika mahali ambapo Watanzania wanavuliwa nguo hadharani na kukaguliwa na watoto ambao wanaweza kuwazaa…

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka nilitaka tu kukuhakikishia kwamba Waziri wa Ulinzi yupo.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana napokea maelekezo yako mkuu.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka ni kwamba atoe kauli yeye vinginevyo ushauri wangu utakuwa ni vizuri kila mtu aonje fedheha hii. Tulikataa wakati wa Azimio la Arusha tukasema tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotupelekea tuonewe, tunyanyaswe na tupuuzwe, sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi yatakayotupelekea tusionewe tena, tusipuuzwe tena, tusinyonywe tena. Azimio la Arusha mwaka 1967 na tukaweka kwenye utangulizi wa Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tamko letu ni la mwaka 1967, kama mnadhani kitendo hiki ni kizuri na mnadhani watendewe watu wa Mererani onesheni demo, ninyi ambao mmepewa dhamana Mawaziri na Makatibu Wakuu tafuteni chumba cha wanaume peke yenu, bila kujali….(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka, hiyo hairuhusiwa Bungeni kuwashauri Mawaziri waende wakaruke kichura. Aaah dakika zako zimekwisha Mheshimiwa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi ya kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi ya kukutana siku ya leo. Nichukue nafasi hii kukupongeza wewe kwa heshima kubwa uliyolijengea Taifa hili, Bunge hili na Afrika kwa kuchaguliwa kwako kuwa Spika wa Umoja wa Mabunge yote Duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natamani kama ningepata nafasi ya kusimama kwenye Jukwaa la Mji wa Mbeya kuwaambia watu wa Mbeya kwamba mmeipa Tanzania zawadi njema kabisa, mmeipa Afrika zawadi, mmeipa dunia zawadi ya kiongozi kijana, makini na msomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado nitasema hivi ndani ya Bunge, nitasema popote nitakapokwenda kwa sababu maandiko matakatifu yananiambia Yesu Kristo alisema; “Atakayenionea haya mbele za watu na mimi nitamuonea haya mbele za Baba yangu.”

Mheshimiwa Spika, unazo sifa mdogo wangu na bosi wangu, endelea Mungu atakubariki, huu ni mwanzo tu wa mchango wako katika ulimwengu tunaoukanyaga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu pia nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Biteko kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kwa nafasi ya kuwa Naibu Waziri Mkuu. Kwa namna ya pekee naungana na Wabunge wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi njema anayolifanyia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mashaka juu ya dhamira njema aliyokuwanayo Mheshimiwa Rais kwa nchi, hii amejitoa kwa hali na mali, ametafuta fedha kwa kukusanya kodi ya wananchi, ametafuta fedha za wafadhili za misaada na mikopo ili kuhakikisha kwamba ustawi wa nchi unapatikana. Nataka niseme wazi, sina mashaka kwamba mafanikio haya ya Mama Samia yana mkono wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri waliopo, Makatibu Wakuu pamoja na Makamu wa Rais anayemsadia, lakini yana mkono pia wa Bunge hili lilosimamia fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu na naanza kuwakumbusha vijana na Taifa hili juu ya maneno ya aina ya viongozi wanaopaswa kukabidhiwa dhamana za kutumikia umma katika Serikali na taasisi zingine zilizoko chini ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa 81 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukurasa wa 103 na ukurusa wa 104 inasema hivi naomba ninukuu: “Kwa hiyo hata katika hali ya demokrasia na ujamaa wakati wote ni muhimu kwa chama na umma kuwa na hakika na anayekabidhiwa madaraka haya ya Serikali maana yakiangukia katika mikono ya wapinga mapinduzi, madaraka hayo yanaweza kutumika dhidi ya maslahi ya umma wenyewe, hivyo chama kuongoza maana yake ni kuhakikisha pia kuwa madaraka muhimu ya Serikali na ya Mashirika ya Umma wanakabidhiwa watu ambao pamoja na uwezo wa kitaaluma…” naomba sana nikazie hapa; “pamoja na uwezo wa kitaaluma ni wenye msimamo wa kizalendo, waaminifu kwa chama na wakulima na wafanyakazi wa Tanzania.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mashaka kwamba Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ndugu yetu Kichere inathibitisha pasipo shaka juu ya matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma kwa muda mrefu sana. Sasa kosa liko wapi? Kosa lipo katika upangaji wa safu ya watendaji na viongozi katika Serikali hii yetu. Naomba kusema hakuna namna unaweza kutenganisha uongozi na maadili, kwa sababu maadili ni sifa ya uongozi, lakini siku hizi mkiangalia leo, mkipitia Ripoti ya CAG ya 2021/2022 na mkaenda 2020/2021 na mkaenda 2019/2020 hakuna shaka kwamba waliohusika katika miaka yote hiyo bado ni watumishi walioko katika Ofisi za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu nakusudia kuleta marekebisho hapa ya kuliomba Bunge hili liliridhie na kukuomba wewe uridhie tuunde Kamati Teule ya kuchunguza, kwa sababu tumekuwa tunapokea Ripoti ya CAG, inakuja Bungeni, tunafanya maazimio, sasa baada ya maazimio tunaishia wapi? Lazima tuangalie namna bora ya kufuatilia utekelezaji wa Maazimio ya Bunge na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wale ambao wamefanya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namna pekee ni kwa kuunda Kamati Teule ya Bunge itakayokwenda kuangalia ukaguzi wa miaka mitatu, waliotusababishia dosari hizo, wamechukuliwa hatua gani, bado wapo maofisini au wameondolewa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukifanya hivi tutakuwa tumekusaidia wewe, tumeisaidia nchi kuhakikisha kwamba Bunge linatimiza wajibu wa Bunge makini ambalo litaacha rekodi ya kuhakikisha kwamba fedha za walipa kodi zinafika maeneo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, haivumiliki, haivumiliki kwamba wanafanya maamuzi kama haya KADCO, Bunge lifanye maamuzi, Baraza la Mawaziri linafanya maamuzi, halafu tumelipa na fedha za kununua hisa, bado wanashindwa kukabidhi shughuli za KADCO kwa TAA, kuikabidhi kwa Serikali, tulimlipa nani fedha hizo? Tulifanya uamuzi huo, wewe unayekaidi wewe ni nani wa kukaidi maamuzi ya Bunge na maamuzi ya Baraza la Mawaziri? Naungana wa Wabunge kusema kuna haja ya kuchunguza na kujua ukweli juu ya jambo hilo kwamba nani anajificha hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme wazi tatizo tulilonalo na ukinzani ambao tunao na wenzetu waliopo kwenye front bench ni vizuri Mawaziri wakajua, viongozi makini hawawezi kuishia kwenye dilemma. Wote, tumekula kiapo kwamba rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, cheo ni dhamana, nisitumie cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu. Ziko kwenye ahadi ya mwanachama wa chama chetu na hii ndiyo inatujengea uhalali kwamba chama hiki kimeendelea kuwa mtetezi wa kuaminika wa maslahi ya wakulima na wafanyakazi pamoja na madaraka yao ya uwajibikaji wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alizungumzia shida ya dilemma ya viongozi wasiokuwa madhubuti kwenye kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania anasema hivi: “Kifo cha maji kushoto, kulia kifo cha moto, kukubali, kukataa kila moja ni balaa, kote huko hatarini, hujui ufanye nini?” Ninyi mko kwenye dilemma na mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viongozi wako kwenye hatari ya kufanya maamuzi, wanakumbuka ahadi yao ya CCM? Wanakumbuka maamuzi ya Bunge? Wanakumbuka wajibu na hasira ya Rais, dhidi ya Ripoti ya CAG? Kinachonitatanisha kwa nini hawafanani na uso wa Mama Samia siku anapokea Ripoti ya CAG? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningekuwa Waziri, ningelikuwa Waziri miezi sita hii, hakuna ambaye angebaki aliyetuhumiwa kwenye ufisadi, kwenye Wizara yangu. Hata hivyo, nataka niwaambie wako watu wamefanya ufisadi kuanzia kwenye IPTL na leo wako Serikalini, pamoja na Maazimio ya Bunge, wako watu na nataka kusema ni leo tu nanyamaza, kesho kutwa katika mjadala mwingine nitataja nani wako nyuma ya IPTL, nitataja nani wako nyuma ya ufisadi wa Standard Gauge Railway ambayo manunuzi ya lot one imetugharimu hasara ya zaidi ya trilioni 1.45. Hizo fedha tungegawawi Majimboni, tungegawiwa Majimboni, Zanzibar…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka, dakika moja malizia.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, tungegawiwa Majimboni maana yake hata Zanzibar kwa mgao wa kanuni ile ile, wangepata zaidi ya bilioni karibu mia tatu, mia tatu na sisi tungepata katika Majimbo yetu zinazotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakusudia kuleta marekebisho haya, nimeshayaweka mezani ili tufike mahali tutafute dawa na nitaomba Bunge hili liniunge mkono ili tuweze kuunda Kamati Teule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nitakuwa sijavunja Kanuni chini ya Kanuni ya 139 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2023, baada ya CAG kuchunguza habari hizi na kuzileta, nataka kutoa hoja na naomba niungwe mkono kama Kanuni zinaruhusu kwa sababu nimeshaweka kwenye meza, nimempa Katibu wa Bunge kuundwa kwa Kamati Teule ya kuchunguza ufisadi huu na kuweza kutusaidia Bunge hili tuweze kutoka, hii itatenda haki kwa sababu Mawaziri watakuwa hawajaonewa kwa sababu watapata haki ya kujieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge itakayoshughulikia mambo haya. Naomba mniunge mkono kabla sijavunja Kanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, siko nayo hii hoja hapa mbele, siko nayo na yeye amewaambia kwamba amekabidhi. Kwa hiyo, pengine wanatazama utaratibu mzuri wa kuitumia, siko nayo hapa mbele. Kwa hivyo siwezi kusema kama imeungwa mkono ama kwa namna gani. (Kicheko)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii. Vilevile nikushukuru pia wewe mwenyewe binafsi kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuchangia mpango wa maendeleo pamoja na bajeti ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukushukuru na kukupongeza kwa kuendelea kuliwakilisha Jimbo lako la Ilala vizuri, kwa sababu unakumbuka mpaka jana ndipo suluhu ya wafanyabiashara wa Kariakoo ilipopatikana. Mchango wako ulikuwa mkubwa sana wa kuifanya Serikali kuelewa tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara wa Kariakoo; ninakupongeza sana kwa jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatumia nafasi hii kumshukuru sana Dkt. Tulia Ackson kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuliongoza na kuliwakilisha Bunge hili, pamoja na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki wakati wa msiba wa ndugu yetu Dkt. Mulozi Sedoyeka ambao ulitokea katika Mkoa wetu wa Manyara. Dkt. Tulia Ackson aliongoza Wabunge wengi sana kuja kutushika mkono. Ukiacha hilo aliweza kuja na chifu wa kabila lao kutoka Mbeya na kutuletea rambirambi ya kumshika mkono mume wa marehemu, Mheshimiwa Profesa Eliamani Sedoyeka. Kitendo hiki kwa kweli kilitufariji watu wa Manyara; na ninapenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Manyara kumshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu niwaombe wananchi wa Mbeya waendelee kumsaidia sana na kumuunga mkono Mheshimiwa Spika ambaye ni lulu ya nchi yetu kwa nafasi yake kama Spika lakini ni zawadi waliyoitoa kwa dunia kama Rais wa Mabunge ya Dunia. Hakika Mbeya imetutendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka nijielekeze kuchangia baadhi ya mambo madogo sana na machache ya jimbo langu ambayo yanatokana na masuala ya uharibifu wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kabla sijafanya hivyo nataka nitumie nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Naibu Mawaziri wao wawili pamoja na watendaji wa Wizara hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kutuandalia taarifa hii ambayo ni nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tumeathirika kutokana na janga la EL-Nino ambapo miundombinu ya barabara zetu imeharibika. Hata hivyo, niseme bayana kabisa kwamba Jimbo letu la Simanjiro limeathirika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo kata nyingi ambazo kwa sasa barabara zake hazipitiki. Pamoja na jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kujenga tuta la Msitu wa Tembo na miundombinu katika Kata za Msitu wa Tembo, Kata ya Ngorika, Loiborsoit, Ruvu Remit pamoja na Darala la Gunge, ukanda wote huo umeathirika kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa bonde la maji linalohudumia maeneo ya Kata ya Shambalai, Endiamutu, Mererani na Kata ya Naisinyai ni vizuri wakashirikiana na Serikali pamoja na TAMISEMI na Wizara zinazohusika na wadau wanaohusika kuhakikisha kwamba maji yanarudi kwenye mkondo wake, kwa sababu maji yameacha mkondo wake na kuleta athari kubwa kwenye mazao ya wakulima pamoja na athari kubwa ya kuharibu miundombinu katika ukanda huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ilani ya uchaguzi tunazo barabara kubwa tatu ambazo ilani ya uchaguzi ilitoa ahadi kwamba ingeweza kutekeleza. Hii ni Barabara ya kutoka Arusha – Losinyai – Komolo – Terrat – Naberera – Namalulu – Orkesumet kulekea Ndido kwenda Kiteto kuja hadi Kongwa. Hii ni barabara ndefu ambayo ilipangiwa fedha kupitia EPC + Finance. Ni rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wahusika wote wahakikishe hiyo fedha inapatikana ili hiyo barabara ya EPC + Finance iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilani ya uchaguzi pia iliahidi kujenga barabara inayotoka Mererani – Landanai – Langai kuja Orkesumet na barabara inayotoka Babati kupitia Galapo kuja kuingia Kimotorok – Roiborsiret – Narakawo kuja Sukuro na kuelekea makao makuu ya Wilaya ya Simajiro na branch inayokwenda mpaka Kiteto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hakuna barabara kati ya hizi ambayo imepata fedha ya kujengwa. Rai yangu kwa Wizara ya Fedha na kwa Waziri Mkuu wa nchi yetu, ni vizuri barabara hizi zinapogawanywa, na hasa barabara za lami kila eneo lionje na kupata kilometa chache. Kama bado mnao urasimu mkubwa kwenye barabara hii ya EPC + Finance au hamjakamilisha uwezo wa kuwezesha barabara hii kuanza, ni ushauri wangu kwa Serikali yangu sikivu ya CCM, anzeni hata barabara moja kwa kutupatia kilometa hata 20 kwa mwaka inayoweza kutusaidia ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Simanjiro na majimbo ya wafugaji nao wanapata barabara nzuri ambazo wanazihitaji katika kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuishauri Serikali yangu sikivu ya CCM kuangalia suala zima la kuwezesha ujenzi wa shule za bweni katika maeneo ambayo jiografia inaweka mazingira magumu zaidi. Shule zetu za Kata tumejenga kwa nguvu za wananchi; hata hivyo ni dhahiri kwamba umbali kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine ni mkubwa zaidi. Kwa hiyo, nilitaka kuiomba Serikali ione uwezekano wa kuwa na affirmative plan, affirmative action katika maeneo ambayo ni magumu ili Serikali iweze kutenga fedha za ujenzi wa mabweni kwa sababu wananchi wamejenga zile hostel na hivyo Serikali iunge mkono jitihada za wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuendelea kuikumbusha Serikali yetu sikivu ya CCM, leo sina haja ya kugusia masuala ya mapori, tumekwishakuzungumza na Waziri na tuliomba Serikali itoe kauli katika suala linalohusiana na mapori tengefu, na kwa hiyo leo sina sababu ya kugusia hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala ambalo Mheshimiwa Rais amelizungumzia juzi alipokuwa anazungumza na baadhi ya watumishi aliowateua katika ile Tume ya Haki Jinai, kuhusiana na malengo ya Serikali yetu au misingi tunayoitaka katika nchi yetu; kwamba ni kuongoza katika misingi ya uhuru, haki, usawa na kuthamini misingi ya utu. Nitumie nafasi hii kumwomba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati suala la Ngorongoro. Tulikwishakubaliana kuwa wananchi wa Ngorongoro waliopo tayari kuhama waweze kuhama kwa hiari yao kama ambavyo Serikali ilitoa kauli; na tunaunga mkono jitihada za wale waliohama kwa hiari yao. Hili ni vizuri likaeleweka bayana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niseme wazi. Ni vizuri Serikali ikaondoa vikwazo vinavyokwaza maisha ya wananchi wa Ngorongoro. Pale ambapo unayo shule kama ya Ngorongoro Girls iliyopo katika Kata ya Lailole ambayo miundombinu yake ya maji inahitaji pump ya ku-pump maji kutoka mtoni kuleta pale shuleni na fedha zipo, ziko pia fedha za kujenga bweni katika Shule hiyo ya Ngorongoro Girls lakini mpaka leo fedha hizo hazijatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya shule zimebomoka vyoo, kuta za madarasa na hakuna fedha zinazopelekwa kwenye maeneo hayo. Ni dhahiri kwamba vitendo hivi vinakwenda kinyume na misingi tuliyojiwekea kama Taifa (Misingi ya haki, utu na kuthamini kwa kweli heshima na utu wa watu wanaoishi katika maeneo hayo).

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kuishauri Serikali ya CCM ikiongozwa na mtendaji anayeongoza kwa niaba ya Rais, Waziri Mkuu wasaidie kuwezesha miundombinu hiyo ili kuondoa fedheha na aibu ya kuonekana kwamba Serikali ya CCM inawawekea vikwazo vya kimaisha wananchi wake kwa kushinikiza watu kuondoka Ngorongoro. Itaharibu zoezi zima la watu kuondoka kwa hiari. Ni vizuri watu waondoke kwa hiari, wasiwekewe vikwazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna vyoo vimebomoka vijengwe, kama kuna madarasa yaliyobomoka yajengwe, pump ya maji msilazimishe watoto wa kike wa Ngorongoro Girls waende kilometa nzima kwenda kuchota maji kwenye mto ambao wanyama nao pia wanakwenda pale na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Olesendeka.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama muda umekwisha naunga mkono bajeti na mpango wa maendeleo, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kwanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuja leo nilikuwa nauguza Muhimbili, lakini nikaona Wizara hii isinipite kwa sababu wananchi wa Simanjiro walinituma niseme maneno, nitakayoyasema. La kwanza, ni kuridhika kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kwa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba mradi mkubwa wa maji ambao sijui naweza kusema sijui ni mradi wa kielelezo, wa kimkakati ambao ulibuniwa na Hayati Edward Moringe Sokoine mwaka 1974 alipokuwa akimkaribisha Hayati Rashid Mfaume Kawawa kuzindua Wilaya ya Kiteto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa mmoja wa vijana chipukizi waliokuwepo wakati wilaya ile ilipokuwa inazinduliwa. Hayati Edward Moringe Sokoine alisema pamoja na kwamba Kiteto hakuna maji pale Kibaya ambalo tatizo liko mpaka leo, Makao Makuu ya Wilaya yatajengwa Orkesumet na tutachukua maji kutoka Mto Ruvu, kilometa 45 mpaka 50 kuleta Makao Makuu ya Wilaya ya sasa ya Simanjiro ambayo ni Orkesumet. Mradi huu umetekelezwa na uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo na umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana ya maji, Mheshimiwa Juma Aweso, wananchi wanamshukuru, wanampongeza kwa kazi nzuri kubwa aliyotufanyia. Wanampongeza kwa sababu yeye mwenyewe kwa kipindi cha Uwaziri wake, mimi nikiwa Mbunge katika kipindi hiki, amekuja pale zaidi ya mara sita, akihakikisha kwamba ule mradi unakamilika. Mara zote alipofika tuliona mabadiliko makubwa ya kukidhi kiu ya wananchi wa Jimbo la Simanjiro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba kazi inayofanywa na Mheshimiwa Waziri Aweso ni kazi ya kupigiwa mfano, ni kijana mnyenyekevu, kijana muadilifu, kijana mchapakazi na ni kijana anayejishusha. Natamani viongozi wote wa CCM tungeiga mfano wa Mheshimiwa Juma Aweso ambaye hanyanyui mabega, siku zote yuko down. Nalisema hili kwa sababu si sifa njema sana kwa kiongozi kwamba Mungu amekupa madaraka ukiwa na umri mdogo, lakini unasahau kwamba wewe una umri mdogo hata kama una madaraka makubwa, lakini Mheshimiwa Aweso anajua nafasi yake katika jamii hasa akiwakuta waliomzidi umri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Rais amempa Naibu Waziri mzuri, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, anafanya kazi nzuri sana kwa kushirikana naye. Katibu Mkuu wa kupigiwa mfano, dada yangu Nadhifa Kemikimba, tangu amekulia kwenye Wizara ya Maji, nilimjua akiwa Mkurugenzi, nikamjua akiwa Naibu Katibu Mkuu amekuja kuwa Katibu Mkuu. Leo Wizara ile imekamatwa na viongozi ambao kwa kweli wanajua wajibu wao, wanawajibika vizuri na ni viongozi waadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema leo kwamba, moja kati ya sifa ya kiongozi ni uadilifu na ndio maana huwezi kutenganisha uongozi wa umma na maadili kwa sababu sifa mojawapo ya kiongozi ni uadilifu. Kwa mafanikio haya tunayoyaona yanatokana na kazi nzuri ya uadilifu wa wale waliopewa dhamana katika Wizara husika. Kwa hiyo, nataka niwashukuru kwa mradi huo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mkubwa pia wa pili ambao ni wa Mji wa Arusha ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Mji wa Arusha chini ya Engineer Rujomba pamoja na Mwenyekiti wake Dkt. Masika na Mheshimiwa Balozi Ole- Njoolay. Mradi ule Mheshimiwa Rais alielekeza maji yale yaletwe Mererani, yapelekwe kwenye Kata ya Endiamtu, yapelekwe kwenye maeneo mengine yanayozunguka Mji wa Mererani ambayo ni Kata ya Shambarai, Kata ya Naisinyai na Kata ya Oljoro Namba 5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake. Nimesema nawapongeza na ndio hasa furaha yangu iliyopo leo na mengine nitaomba tu kwa unyenyekevu. Maelekezo ya Rais kupeleka maji katika maeneo haya niliyoyataja ni kwa sababu maji yaliyoko pale yana fluoride kubwa na yanapelekea watoto kupinda miguu na wengine meno kuoza, ukiwaona unaona meno ya watu ni mekundu na siyo hapo tu na Kata ya Msitu wa Tembo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kuwa na maji ambayo watu wetu wanapinda miguu katika kizazi hiki siyo sifa njema kwa Serikali ambayo Rais wake anatafuta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya watu. Kwa hiyo niendelee kumwomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yake watupie macho yao tena katika maeneo haya. Siyo kwamba sitambui miradi aliyonisaidia ambayo Wizara yake chini ya RUWASA, nampongeza sana Meneja wangu wa RUWASA wa Mkoa, Ndugu yangu Walter Kirita na Ndugu yangu Johanes Engineer wa RUWASA, Simanjiro ambaye kwa kweli nasema amekaa akikaimu nafasi ile kwa muda mrefu na amefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ningeomba sana amfikirie, apitie tena muda aliokaimu na kazi nzuri aliyoifanya ikimpendeza amthibitishe, amefanya kazi nzuri Johanes, kazi ambayo ni ya mfano. Hakuna Diwani leo ambaye hamsifu kwenye halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekumbuka miradi ambayo Serikali ya Mama Samia imetusaidia sana. Wananchi wa Terrat wana furaha kwa sababu ya Mama Samia, wananchi wa Engonongoi wana furaha kwa sababu ya Mama Samia, wananchi wa Endonyongijape, Naberera, Okutu na Lemeshuko wana matumaini kwamba katika bajeti inayokuja watapelekewa maji. Wananchi wa Losoito na Naiborndet katika bajeti ya mwaka huu watapelekewa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwa upande wa, nilikuwa napitia Fungu namba 49 upande wa randama katika ukurasa wa 56 kwamba moja kati ya kazi atakazofanya ni pamoja na ujenzi wa mabwawa ya maji ya ukubwa wa kati hususani katika maeneo makame. Nataka niseme Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika nyanda kame na wote wanajua na Waziri juzi ameshuhudia alipokuja na Kamati. Nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Maji walifika, walishangaa walivyofika katika yale maeneo wakasema, kabla ya mradi huu wa Mama Samia wa kupeleka maji Orkesumet, watu hawa walikuwa wanaishije?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika nyanda kame na ninyi nyote mnajua na wewe mwenyewe juzi umeshuhudia ulipokuja na Kamati nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Maji walifika, walishangaa walivyofika katika yale maeneo wakasema kabla ya mradi huu wa Mama Samia wa kupeleka maji Orkesumet, watu hawa walikuwa wanaishije?

Nikawaambia mmeona tu sehemu ndogo ya sehemu ya Wilaya ya Simanjiro ipo haja ya wakati mnagawa rasilimali hizi za nchi muangalie mazingira na jiografia ya maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachimba mpaka mita 200 chini hatupati maji ardhini, tupo katika nyanda kame, Simanjiro iko kwenye nyanda kame, Longido ipo kwenye nyanda kame, Monduli ipo kwenye nyanda kame. Watu wanapeleka maji kwa matrekta kilometa 50 kilometa 20, 30 ni jambo la kawaida kwenda kutafuta maji kilometa 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka leo Lerumo ambako leo ndiyo inapelekwa maji katika bajeti ya mwaka huu ni kilometa 30 kwenda Rovuremit lakini wananchi wa Lerumo leo Mkandarasi amepatikana na kazi imekwishaanza na hii kazi ni ya Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri wake ni wewe Juma Aweso. Nawapongezeni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upo mradi….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ole-Sendeka.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ooh, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hiyo, hauwezi kuniongezea hata dakika hivi au ndiyo muda umeenda?

MWENYEKITI: Malizia dakika moja.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ngoja nimalizie, ahsante nashukuru. Niombe basi ule mradi wa Mirerani, Endiyamtu, Shambarai, Olgora Namba Tano na Isinyai ukamilishwe na wenzetu wa Mamlaka ya Maji wa Mji wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mpango wetu wa Taifa kwa maendeleo pamoja na Mwongozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi hii ya leo na nichukue nafasi hii ya pili kukushukuru wewe kwa jinsi unavyoendelea kuliongoza Bunge letu, kwa namna ya pekee nitakuwa mwizi wa fadhila katika kipindi hiki ambapo dunia inakabiliwa na misukosuko mikubwa ya kiuchumi inayotokana na athari za janga la UVIKO-19 na yanayotokana na vita vya Mataifa makubwa kama Urusi na Ukraine, lakini nchi yetu imeendelea na uchumi wake umeendelea kuwa stahimilivu chini ya Uongozi wa Jemedari Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae amekuwa ni tulizo na Faraja kwa Watanzania kutokana na mipango mizuri ya kiuchumi anayoiweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa jinsi anavyomsaidia Mheshimiwa Rais katika suala zima, siyo tu la kuweka mipango, lakini kukusanya kodi ambayo leo tunaona fahari, hata leo tutakapotoka kuhitimisha kikao hiki, tutakwenda kupokea magari ambayo ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa kazi nzuri waliyoifanya baada ya kupokea kilio changu cha wananchi wa Kata ya Kitwai katika Wilaya ya Simanjiro ambapo walinielekeza kukutana na Mawaziri wa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maji pamoja na uratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango uliowekwa na Mawaziri hawa kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu, hivi sasa ni faraja kwa wananchi wa Kitwai na nitakwenda Simanjiro kifua mbele nikijua kabisa tunakwenda kuweka mpango shirikishi utakaotekeleza malengo na maombi ya Serikali katika eneo lile na utakaojali maslahi na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yetu ya Kitwai B.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yangu pia kwamba siwezi kukaa tena, baada ya kazi nzuri iliyofanyika hivi karibuni ya kusainiwa kwa mikataba ya zaidi ya kilometa 2,000 za EPC+ Finance, kazi ambayo ni mfumo mpya uliobuniwa chini ya Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Prof. Mbarawa akisaidiwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADs na Kitengo cha EPC+ Finance, Eng. Kitahinda na baadaye maeneo yetu ya Mkoa wa Manyara ikiwemo Wilaya ya Simanjiro, Wilaya ya Arusha kwa Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Kiteto na baadhi ya maeneo mengine ikiwemo Kongwa kwa Mheshimiwa Ndugai ambapo tutapata barabara ya kilometa 453.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpongeze sana Waziri wa Miundombinu wa wakati huo pamoja na Waziri wa Fedha ambao wamefanya kazi hiyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niazime maneno machache ya Prof. Kitila Alexander Mkumbo aliyoyatumia katika ukurasa wa tisa aliyokuwa anazungumza akisema hivi: “Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia usuli huo, ninapendekeza kuwa shabaha kuu ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo Mwaka 2024/2025 na miaka ijayo, iwe ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi ambao ni jumuishi na unaopunguza umaskini, unaozalisha ajira kwa wingi, unaotengeneza utajiri na unaochochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kama tukijipanga vizuri katika kuendeleza kujenga uchumi wetu kwa namna jumuishi na kushughulisha na umaskini wa watu wetu kwa kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ya mazao yanayotokana na ufugaji, thamani ya mazao yanayotokana na kilimo, thamani ya mazao yanayotokana na uvuvi, thamani ya mazao yanayotokana na misitu na madini, nina hakika uchumi wetu unaomgusa mwananchi wa kawaida utaweza kukua na kila mmoja ataona faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mantiki hiyo, rai yangu ni kwamba, ni vizuri tukawa na maendeleo jumuishi kwa nchi nzima. Tunapofikiria juu ya maendeleo ya nchi ni lazima tuangalie na baadhi ya jamii nyingine ambazo historia na jiografia imewaweka mahali pabaya na hasa ukizingatia kwamba kesho kutwa kwa maana ya mapema mwakani au katikati ya mwaka tutakaa na kupitisha bajeti ya 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua, mara nyingi tunapopitisha bajeti, tunazungumza habari ya asilimia 65 ya ajira za watumishi ambayo inalipa mishahara ya watumishi, uendeshaji wa Serikali na asilimia 35 ya maendeleo. Nataka niseme wazi jambo hili lieleweke vizuri, kwamba zipo jamii katika nchi hii ambao hawako katika mfumo wa ajira rasmi za Serikali kutokana na historia, kuchelewa kupata elimu, lakini wote leo wamesoma na hawamo kwenye mfumo wa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza, Serikali ije na mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba hakuna jamii inayobaki nje ya uzio wa ajira rasmi ya umma ili kuhakikisha kwamba nchi nzima tunaitendea haki. Kutokufanya hivyo, jamii nyingine unaziacha zikiwa nje kabisa, hawapo kwenye utumishi wa umma na hili sio jambo zuri katika umoja na mshikamano wa Taifa letu kama ambavyo sote tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni rai yangu kwamba tunapofikiria jiografia katika maeneo mengine kama ya kwetu ambapo umbali kati ya kijiji na kijiji ni kati ya kilometa 40 mpaka 70 na shule za kata tunazo, hakuna mwanafunzi anayeweza kutembea kilometa 50 kwenda huko, ni lazima shule zile zote zingekuwa ni za hostel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni Serikali ilikuwa imetenga fedha kwa ajili ya kusaidia shule hizo za bweni za msingi na sekondari, lakini sasa hivi imepunguza fedha hizo. Nataka niwaambie kwa kupunguza fedha hizo kwa upande wa Wizara ya TAMISEMI, mnatuingiza katika hali mbaya zaidi ya maendeleo ya watoto wetu katika shule hizo za sekondari na msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naiomba Serikali yangu sikivu na hasa Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI, mwone uwezekano wa kukamilisha mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuliahidiwa mabwawa yapatayo manne katika Wilaya ya Simanjiro lakini mabwawa mawili ambayo ni Kopokyoo na Anaryoo katika Kata ya Comoro na Kijiji cha Naruchugin na hiyo ya Kopokyoo iko katika Kijiji cha Lerumo Kata ya Ruremit. Tuliahidiwa kwamba mabwawa haya yangeweza kujengwa, lakini sasa ni mwaka wa tatu fedha hazitoki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningefurahi sana kama Wizara ya Mheshimiwa Mwigulu Nchemba itashirikiana na Wizara ya Mifugo ili fedha zile za mabwawa hayo mawili yaweze kutoka hata kabla ya yale mengine mawili ambayo hayajaweza kuwekwa kwenye bajeti ya miaka iliyopita. Ni ombi langu kwa Waziri mwenye dhamana ili hali hiyo iweze kushughulikiwa na mifugo yetu iweze kupata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofikiria maisha ya wafugaji kutoka ufugaji uliozoeleka kwenda katika ufugaji wa kisasa wenye nyama nyingi na maziwa mengi, pia tunazungumzia haja ya kuweka miundombinu rafiki kwa maana ya kupata maji, kwa maana ya kupata majosho, pia kwa maana ya kupata mbegu bora za Sahiwal, Friesian, Jersey, Ayrshire na Simmentals ambazo zitasaidia wafugaji hawa kufanya mapinduzi ya kuwa na ng’ombe wa kisasa wenye tija kubwa zaidi lakini miundombinu lazima irekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika eneo hilo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Mhandisi Stella Martin Manyanya, atafuatiwa na Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima na watoa hoja wajiandae.

Mheshimiwa Ole-Sendeka, umeshazima kisemeo?

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazima muda mrefu sana, mtafuteni aliyejisahau.