Contributions by Hon. Samweli Xaday Hhayuma (37 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima. Pia nikishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi na Wanahanang kuniwezesha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nitumie nafasi hii kuishukuru familia yangu kwa jinsi wanavyoniunga mkono katika kufanikisha majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kukupongeza wewe na Mheshimiwa Spika kwa jinsi mnavyotuongoza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ikiongozwa na Jemedari, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwa muda wa miaka mitano iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ameeleza mambo mengi ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Nitajikita kwenye maeneo matatu kwa sababu ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya maji, kwamba kwenye eneo la vijijini kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa maji kwa asilimia 47 mpaka asilimia 70.1 na mjini asilimia 74 mpaka asilimia 84; hayo ni mafanikio makubwa sana. Mheshimiwa Rais pia alibainisha kwamba wakati wa kampeni kulikuwa na malalamiko mengi kwenye eneo la maji.
Niombe Wizara ya Maji wawasimamie kwa karibu wataalam wetu ili miradi mingi ya maji ikamilike. Wenzangu waliotangulia waliiongelea, wengine walifikia hatua ya kusema miradi mingine isianzishwe lakini mimi nasema kwamba usimamizi uimarishwe ili miradi hii iweze kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano wa Mradi mmoja wa maji Katesh, mradi huu ni wa muda mrefu lakini mpaka sasa bado haujakamilika. Ukienda Mji wa Katesh watu wanatembea na mikokoteni mjini haipendezi sana. Tunaomba ule mradi ukakamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Mradi wa Maji wa Lambo ambao ulitakiwa ukamilike mwezi Mei, 2020, lakini mpaka sasa umefanyika asilimia 45 tu. Wananchi wanasubiri maji na ndiyo malalamiko mengi ambayo tunayapata kwa wananchi wetu. Naomba huo mradi uweze kukamilishwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba Wizara inafanya kazi nzuri na kubwa. Mheshimiwa Waziri Aweso na Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer MaryPrisca, wanafanya kazi kubwa sana. Kuthibitisha hilo, toka Uhuru, Kata ya Gehandu imekuwa ikilia maji, kwa sasa kisima kimechimbwa, maji yamepatikana mengi. Wameshafanya pump testing. Ninachoomba, usanifu ukamilike haraka ili mradi uweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo eneo la kilimo. Mheshimiwa Rais alibainisha wazi kabisa kwamba nchi yetu ina upungufu mkubwa wa ngano ya chakula na akamwelekeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo atakayemteua kwamba hiyo ndiyo iwe kazi yake ya kwanza. Nampongeza sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Profesa Mkenda na Naibu Waziri Mheshimiwa Bashe kwa kazi waliyoanza nayo. Wamekuja Hanang, tumetembea nao kwenye mashamba ya NAFCO, mashamba ya ngano ambapo Hanang ndiyo ilikuwa inaongoza kuzalisha ngano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaahidi wananchi wale wakusanye ngano, kwa sasa zimeshakusanywa zaidi ya tani 480, zile ngazo zikanunuliwe ili wananchi wapate fedha za kurudi mashambani ili tuweze kuzalisha ngano zaidi. Pia tuliwaahidi wananchi wale mbegu; na sasa ni wakati wa msimu wa kupanda, tunaomba zile mbegu zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la NAFCO yale mashamba yalikuwa ya mwekezaji kabla. Maeneo yale mengi yamebinafsishwa kwa wawekezaji wengine ambao uwezo wao ni mdogo. Naomba sana Wizara ya kilimo ifanye tathmini ya kina ya wale wawekezaji ambao wako kwenye lile eneo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa tupate wawekezaji au Wanahanang wenye uwezo tuweze kutumia yale mashamba na wazalishe kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naomba niishie hapo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwani kuna siku mimi na Mheshimiwa Flatei tulimuelezea kuhusu barabara ya Karatu - Mbulu – Haydom - Katesh jinsi ilivyo na umuhimu wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Alikuwa msikivu hatimaye akamtuma Naibu Waziri kutembelea barabara hii lakini nikiri kwamba Mheshimiwa Waziri bado hajajitikisa vya kutosha kwa sababu kwenye bajeti hii sijaona chochote ambacho kimetengwa kwa ajili ya barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imeahidiwa muda mrefu toka 2005 mpaka wakati wa bajeti ya 2021, Mbunge aliyenitangulia Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu aliomba hapa Bungeni akakumbushwa na Mheshimiwa Mavunde kwamba kwa sasa jua limezama, ni barabara imeahidiwa muda mrefu. Kwa sababu ya umuhimu wake barabara hii inaunganisha Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Hanang lakini hapo katika kuna mashamba makubwa ya ngano. Tunaaagiza ngano kiasi kikubwa sana nje ya nchi, tunatumia fedha za kigeni, tukiwekeza kwenye barabara hii wananchi watazalisha na ngano ya kutosha itapatikana kutoka kwenye Jimbo langu la Hanang. Tutaokoa zile fedha tunazozitumia kununua ngano nje ya nchi lakini pia itarahisisha huduma kwa wananchi wanaotegemea Hospitali ya Rufaa ya Haydom. Mheshimiwa Waziri kwenye barabara hii tumesema sana, barabara imeahidiwa muda mrefu, naomba ujiguse ili barabara hii ianze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna barabara yetu kutoka Naangwa – Gisambalang – Kondoa, ile barabara haipitiki kabisa wakati wa mvua. Kuna daraja la Muguri B limeondolewa na mafuriko ya 2019/2020 ili mvua kubwa. Tumeambiwa kwamba sasa kuna zoezi la usanifu ili kujenga daraja jipya, lile ni suala la dharura, wananchi ambao wanategemea barabara ile kwa shughuli zao zaidi ya laki tatu, mvua zikinyesha hakuna chochote kinachofanyika maana yake uchumi wa wananchi unakwama na Serikali inakosa mapato. Hilo naona mlione kama ni suala la dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna barabara yetu ya kutoka Dareda - Bashinet - Lukumandar – Secheda - Basonesh – Hilbadauh, upande wa Singida barabara hii iko chini ya TANROADS na inatengenezwa vizuri. Wananchi wa upande wa Manyara wanajiuliza sisi tumekosa nini upande huu kwa nini barabara isijengwe vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Hotuba au Bajeti ya Waziri Mkuu. Nianze kama wenzangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini Makamu wa Rais Dkt. Philip Isidor Mpango na Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo inafanyika katika kutekeleza maendeleo ya nchi yetu na ushahidi unaonekana kwamba kazi kubwa inafanyika katika utekelezaji wa miradi mikubwa; hasa mradi wa reli ambako maeneo mbalimbali kazi kubwa tunaiona ikifanyika, lakini Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambako umeshafikia asilimia 83 na ni mategemeo kwamba baada ya mradi huo kukamilika Watanzania wataisahau shida ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu pia inapiga hatua kubwa chini ya usimamizi mahiri wa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kazi kubwa inafanyika kwenye eneo la elimu, kwenye umeme usiseme lakini miundombinu tunaenda nayo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa niaba ya Wananchi wa Hanang’ kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa miradi mingi ya maendeleo ambayo imeelekezwa ndani ya Jimbo la Hanang’. Kwenye upande wa barabara tulikuwa na changamoto kubwa hasa upande wa TARURA, bajeti yetu ilikuwa milioni 800 na hamsini na kitu tu, lakini mpaka sasa tuna barabara nyingi ambazo tumefungua. Nitaje barabara chache tu ambazo wananchi sasa hivi wanafurahia matunda ya Daktari Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na barabara yetu mbovu kabisa ambayo iliyokuwa inatusumbua barabara ya Masqaroda - Lambo – Masakta kwa sasa wananchi wanateleza maendeleo yanaenda sawa sawa. Tulikuwa na barabara mpya nayo imefunguliwa kuunganisha Kata za Bassodesh na Mulbadaw tumefungua barabara mpya kuunganisha Hilbadaw na Mwanga hicho ni kijiji ambako kilikuwa na changamoto kubwa na tuliwaahidi wakati wa uchaguzi, utekelezaji unaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa maji, kazi kubwa pia imefanyika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Tulikuwa na changamoto kubwa ya maji, nilivyoanza kuja tu hapa Bungeni nilianza kulia kwa Mji wa Katesh, mji mkubwa, maji tunateka kwa mikokoteni ya punda, lakini kwa sasa Wanakatesh wanapata maji ya kutosheleza. Naamini kuna maeneo ya kuboresha ambako tutaendelea kuboresha lakini Mradi mkubwa wa Maji kutoka Mogitu, Gehandu, mradi wa zaidi ya bilioni sita karibu umefika asilimia 80 ya utekelezaji wake ambako utaenda kutekelezwa ndani ya bajeti hii inayokuja. Ni kazi kubwa ambayo imefanyika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Tumechimbiwa visima zaidi ya 40 ndani ya Jimbo langu la Hanang’.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na miradi mbalimbali ambayo ilikuwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji nayo imeendelea kukamilika. Tunashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kweli ametuwezesha na changamoto ya maji inaendelea kupungua ndani ya Jimbo la Hanang’. Tunalo ombi kwenye visima ambavyo tumechimbiwa visima 24 lakini tunaenda kuchimbiwa visima 16, vile visima ambavyo tayari vimeshachimbwa tunaomba maji yale yasambazwe kwa wananchi. Bajeti tunayotengewa kwa sasa kwa visima hivyo hatuwezi kusambaza kwa wakati, tunaomba tuongezewe fedha ili tuweze kusambaza kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba kwenye bajeti hizi zinazokuja tutapeleka maji Gawal, tutapeleka maji Gehandu, tutapeleka maji Mureru lakini Gijetamuhog ambako hawajawahi kupata maji nao wataenda kupata maji, lakini Mureru nao wataenda kupata maji. Tunaomba kasi hio iongezeke ili maeneo yote yaweze kupata maji, changamoto ya maji iweze kuondoka. Kwa visima vile 16 naomba maeneo ya Dajameda na Wandela yapewe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, tulitarajia wakati fulani Waziri Mkuu kututembelea kwenye Jimbo letu la Hanang’ akiwa Mgeni Rasmi akamtuma Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Daktari Mwigulu Nchemba. Alipofika pale mbele ya Wanahanang’ nilimwomba kwa sababu amebeba pochi ya Mama aifungue aiangalie barabara yetu ya Mogitu – Haydom na yeye kwa kuwa ni mtoto wetu, jirani yetu, aliahidi kwamba pochi ya Mama ataifungua, mpaka sasa sioni dalili ya hiyo barabara kuanza. Naomba hiyo pochi ifunguke barabara ya Mogitu – Haydom ianze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile barabara inategemewa na wananchi wa Hanang’. Ukanda ule wa juu ndio unakolimwa ngano nyingi na nchi yetu ina changamoto kubwa ya upatikanaji wa ngano, lakini ukanda ule ndiko kunapolimwa shahiri na mazao mbalimbali, ni ardhi ya kilimo, vitunguu tunalima mpaka tunasafirisha katika nchi mbalimbali. Tunaomba tusaidiwe hii barabara ni barabara ya kimkakati. Barabara ambayo itasaidia wananchi wetu pia kupata huduma za afya. Kwa maana ya kurahisisha kuunganisha usafiri kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Hanang’ na Wilaya ya Mbulu hasa Hospitali ya Haydom.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hii barabara kwenye bajeti hii isikose fedha. Jana niliuliza swali la nyongeza hapa kwamba barabara hii itaanza lini, nikaambiwa upembuzi na nini kwamba swali hilo lilishajibiwa, tunachotaka sisi Wanahanang’ na Wanambulu tuone barabara inajengwa na hatimaye barabara inapitika ili kurahisha usafiri kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawahi kuongelea suala la ugonjwa wa malaria kwenye Bunge hili. Ni ugonjwa ambao unaongoza katika kupoteza maisha ya watu wetu lakini tuna kiwanda kimejengwa cha viua wadudu ambacho kitatokomeza viluwiluwi vya mbu. Mbu ni kero katika makazi yetu katika maeneo yetu, tuna kiwanda ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka. Kiwanda hiki kimejengwa toka mwaka 2016. Kiko nchini mwetu mpaka sasa sisi tunahangaika na malaria, tunapoteza watu wetu kwa sababu ya malaria, lakini kiwanda tunacho, hakina soko, ilivyofanyika feasibility study wateja wakubwa walikuwa ni Wizara ya Afya kwa sababu ya kudhibiti malaria, lakini TAMISEMI kwa sababu nao wanashughulika na suala la afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi ninavyoongea kiwanda hicho kimeweza tu kuzalisha lita 916,747 kwa miaka yote ambayo imefanya kazi toka mwaka 2016, lakini tunaendelea kupoteza watu. Kiwanda hicho kinaendelea kufanya kazi kwa hasara, kiwanda cha kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kuna sababu ya sisi akili zetu kuanza kufanya kazi. Kiwanda ni cha kwetu tumekitengeneza, kinapata hasara hakina soko, lakini sisi tunaugua, tunakufa kwa ajili ya malaria. Hii haikubaliki, kila Ripoti ya Wizara ya Afya utaambiwa tu kwamba ugonjwa unaongoza kuua watu Tanzania ni malaria. Tunao mfano Zanzibar, wenzetu malaria wamepunguza kwa asilimia kubwa sana, lakini Tanzania Bara mpaka sasa malaria bado ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kinaendeshwa kwa hasara, tuchukue hatua sasa, Mheshimwa Waziri Mkuu tunaomba awasimamie hawa watu wake. Wizara ya Afya, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sababu, Viwanda na Biashara wanayo dawa, Wizara ya Afya wanapaswa kununua dawa ili kudhibiti malaria, lakini hilo halifanyiki. Tunaomba eneo hilo lisimamiwe vizuri. TAMISEMI kwenye halmashauri zetu wasimamie kuhakikisha kwamba tunadhibiti mbu wanaoambukiza malaria kwa sababu dawa tunayo hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ingekuwa ni teknolojia tunayotafuta kwa mbali tungekuwa tunahangaika kila siku tunarudia jambo hilo hilo hatusogei, tuchukue hatua sasa tusogee kwenye eneo hilo. Niseme tu, kama changamoto yetu ni kwamba tukiwa na taasisi ikawa ya umma umma hivi watu hawaoni hizi fursa na kuunganisha mazingira yaliyopo ili kuhakikisha kwamba tunachukua hatua na tufanye kazi kwa ufanisi. Tuangalie watu tunaowaweka kwenye maeneo hayo. Taasisi zetu zimekuwa zinajisahau kufanya kazi Kiserikaliserikali, wakati kuna taasisi kama zenyewe zinafanya kazi za binafsi, zinafanya kazi vizuri. Tuchukue hatua tuweke watu ambao tutawawekea vigezo hasa tuangalie performance base za wale ambao tunawapa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani una kiwanda kimesimama, wateja wapo, hakuna kinachoendelea na hii imekuwa kila sehemu kwenye nchi yetu. Ukiangalia TTCL wenzao kina Vodacom kina Tigo na wengineo wanaenda vizuri na unawasikia matangazo kila sehemu, TTCL anza kutafuta vocha utazunguka mji mzima, kupata vocha ni shida. Tuangalie kama kweli bado tunahitaji kuwa na taasisi zinazofanya biashara kwenye nchi yetu ambazo zinamilikiwa na Serikali. Tukishafanya tathmini hiyo, kama kweli tunahitaji, tuweke watu ambao wanaweza kufanya kazi ya uzalishaji wakashindana sokoni, wakaleta tija. Kama hilo haliwezekani tuwezeshe sekta binafsi iendeshe hivi vitu, sisi tuvisimane. Vile ambavyo vina maslahi ya umma tuweke usimamizi uwe imara zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu udhaifu umekuwa mwingi katika maeneo mengi. Nikirudi kwenye NDC…
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, wamekopesha matrekta kwa wakulima…
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Hhayuma kwamba ukitaka kutafuta vocha ya TTCL ukiwa kule kijijini ni mpaka utafute namna ya kuweka M-pesa vinginevyo vocha hakuna. Minara ipo kila kitu lakini vocha ni tatizo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Samweli, endelea.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa naipokea na naomba nisisitize tu kama Serikali kwenye taasisi zile ambazo zinafanya biashara inamaanisha biashara basi waweke watu ambao kweli watasimamia biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kuongelea suala la NDC wamekopesha matrekta ya URSUS kwa wakulima. Kilichofanyika tu matrekta yale yamekabidhiwa kwa wakulima, walitakiwa wawe na kipindi cha warrant, walitakiwa watembelee na kufanya services, lakini toka wamekabidhi wameyatupa huko. Wanachofanya kwa juhudi kwa sasa hivi, mara ya wapite kupitia TAKUKURU, kupitia kwa nani kuwakamata wakulima hawa. Wenyewe hawajatekeleza wajibu wao wa kibiashara, lakini wanataka haki, haki yeyote inapaswa kwenda na wajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, utangulizi; kabla ya kuanza mchango wango nimshukuru Mwenyezi Mungu anayetuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yetu ya kuwawakilisha wananchi wetu kwenye Bunge hili tukufu. Pia nimpongeze Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kuendelea kuisimamia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025 inatekelezwa kikamilifu kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, aidha nikiri kuwa kazi kubwa imefanyika toka tulipomaliza uchaguzi wa mwaka 2020. Wananchi wanaendelea kuwa na matumaini makubwa kwa Serikali yao chini ya usimamizi mahari wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utawala; Jimbo la Hanang lina kata 33 na vijiji 96, makao makuu yake yapo Mji Mdogo wa Katesh. Kwa kuwa maeneo mengi ya Jimbo la Hanang ni ya kilimo na ufugaji unakuta kuna maeneo ambayo ni makubwa jambo linalosababisha ugumu wa kutoka makazi ya wananchi na maeneo ya huduma. Ili kuboresha huduma kwa wananchi ninashauri yafuatayo yafanyike: -
(i) Kuundwa kwa mamlaka kamili ya Mji wa Katesh badala ya kuendelea kuwa chini ya mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh kwani Mji wa Katesh unakua kwa kasi na unahitaji usimamiwe vizuri ili kuharakisha zaidi maendeleo na kustawisha biashara na shughuli zingine za kiuchumi ndani ya mji.
(ii) Kugawanywa kwa kata ambazo ukubwa wake unatatiza upatikanaji wa huduma kwa wananchi hasa Kata za Measkron, Lalaji, Laghanga na kuifanya Kijiji cha Mureru ambacho ni kikubwa sana kuwa kata.
(iii) Kuundwa kwa vijiji vipya vya Nyasande, Merekwa, Marega, Gidagong na Nanyami.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maslahi ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji; viongozi wa kuchaguliwa yaani Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wanafanya kazi kubwa kwenye maeneo yao na muda wao mwingi unatumika kwenye kuhudumia wananchi kwenye maeneo yao. Kwa sasa Madiwani wanapata posho ambayo ni ndogo sana ila Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji hawapati chochote hivyo ninashauri yafuatayo yafanyike; kwanza kwa kuwa posho wanayopewa Madiwani ni ndogo sana ukilinganisha na majukumu waliyonayo, waongezewe posho.
Pia Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji watengezewe utaratibu wa kupata posho ili kufidia muda wao unaotumika kwenye shughuli za kusimamia maendeleo. Fedha za kuwalipa posho inaweza kupatikana kwa kurasimisha makusanyo yanayopatikana kwenye usimamizi wa mikataba inayofanyika ngazi za vijiji, mitaa na vitongoji kama vile kuuziana mashamba, viwanja na kukodi shamba, nyumba pia kurudisha kwa wakati sehemu ya mapato inayokusanywa na halmashaji vijijini na mitaani.
Mheshimiwa Spika, viongozi hawa wa kuchaguliwa wakishirikishwa na kutumika vizuri wataisaidi Serikali kwenye makusanyo ya kodi na mapato mengine na kuondoa ufujaji wa mapato ya Serikali inayostahili kukusanywa kw mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maslahi ya watumishi; kumekuwa na usumbufu mkubwa kwa watumishi kufuatilia stahiki zao ikiwepo kupandishwa madaraja, hii inaathiri kwa kiasi kikubwa sana utendaji wa watumishi husika na kuwakosesha wananchi wetu huduma walizostahili. Wapo watumishi wengi ambao hawajapandishwa madaraja kwa wakati na hakuna uwazi kwenye eneo hili ambayo ingewaepusha watumishi ufuatiliaji usiokuwa na uhakika wa lini watafanikiwa hivyo kuathiri utendaji wao.
Pia watumishi wanaoelekea kustaafu mafao na taarifa zao ziandaliwe mapema ili kupunguza shida wanazopata watumishi wanapostaafu ikiwepo kuangalia upya suala la kikokotoo kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kwani kumekuwa na malalamiko makubwa ambayo nitachangia zaidi wakati wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, suala la uhaba wa watumishi; ili kupeleka huduma kwa wananchi kwa kiwango kinachostahili ni muhimu kuwa na watumishi wa kutosha na wenye weledi. Jimbo langu la Hanang lina upungufu mkubwa wa watumishi hasa walimu wa shule za msingi na sekondari, manesi, tatibu, wataalam wa maabara za shule za sekondari na afya pia hatuna mtaalam hata mmoja wa vifaatiba.
Mheshimiwa Spika, watendaji wa kata na vijiji ambao ni muhimu sana katika usimamizi wa shughuli za maendeleo kwenye ngazi ya vijiji na kata nako kuna upungufu mkubwa, mfano katika jimbo langu la Hanang tuna upungufu wa watengaji 37 kati ya 96 wanaohitajika na watendaji wa kata wapo 25 wakati mahitaji ni 33. Hali hii ya upungufu wa watumishi inaathiri kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo ya wananchi wetu.
Ninaiomba sana Serikali ifuatilie na kutatua changamoto kubwa ya ufungufu wa watumishi iliyopo Wilayani Hanang. Aidha, kwa kuhitimisha eneo hili la watumishi, Serikali itupatie Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri au imthibitishe Bwana Ibrahim Mbogo anayekaimu sasa kwani toka Bi. Jenifer Omolo ateuliwe kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango nafasi hiyo imekuwa ikikaimiwa na inaathiri utendaji wa Halmashauri yetu ya Hanang.
Mheshimiwa Spika, miradi ya maendeleo na mgawanyo rasilimali; kwa niaba ya wananchi wa Hanang ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi mikubwa inayotekelezwa maeneo mbalimbali nchini na hapa chini nitataja miradi inayotekelezwa kwenye jimbo langu hasa eneo la afya, elimu na miundombinu; stendi mpya ya kisasa Mji wa Katesh; ufunguzi wa barabara mpya Masqaroda-Ngalda – Lambo - Masakta, Mogitu - Gendabi, Mulbadaw- Basodesh, Hilbadaw - Mwanga, Garawja - Gijetamog, Dawar- Ziwa Chumvi, Waama – Diloda - Mureru, barabara za Mji wa Katesh iliwepo barabara za lami; madarasa ya shule shikizi, shule za msingi na sekondari; na ujenzi wa vituo vya afya Mogitu, Hilbadaw, Bassotu, Gisambalag na zahanati mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo makubwa yaliyofanyika kama nilivyotaja hapo juu, mimi ninaamini mambo makubwa zaidi yangeweza kufanyika iwapo mgawanyo wa rasilimili ungefanyika kwa kuzingatia ukubwa wa majimbo na mahitaji halisi ya maeneo husika. Mfano jimbo langu ina kata 33 na vijiji 96 kama nilivyoeleza hapo awali bado inapata mgao mdogo wa rasilimali ukilinganisha ukubwa wake.
Mheshimiwa Spika, ninaomba sana wakati Wizara ipanga fedha za kupeleka kwenye maeneo yetu iangalie mahitaji halisi ya maeneo husika. Wananchi wamekuwa wakijitolea kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo mpaka sasa kuna maboma mengi ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, zahanati ambazo hazijakamilishwa kwa muda mrefu hii inaathiri moyo wa wananchi kuchangia shughuli za maendeleo mfano Zahanati ya Dang'ayda ambayo iliwekwa jiwe la msingi mwaka 2012 na maeneo kama hayo yapo mengi kwenye jimbo langu.
Baada ya maelezo haya Wizara izingatie yafuatayo; kuongeza fedha za TARURA ili kujenga kilometa 10 za lami Mji wa Katesh, kujenga madaraja ya Siro, Mto Basodesh inayounganisha Gijetamog na Basodesh, Mwanga na Sasemwega, Mara na Endasak, Mbuga Sanjaya inayounganisha Kata ya Simbay na Hidet, daraja la kuunganisha Hidet na Gidahababiye, Murumba na Ghambesh, Qalosendo na Merekwa; kuendelea kuimarisha na kukarabati barabara zilizofunguliwa; pia kuendelea kufungua barabara za kuunganisha vijiji na makao makuu ya kata.
Mheshimiwa Spika, pia kuihamisha barabara ya Bashnet – Luqmanda - Basodesh Hilbadaw - Zinga toka TARURA kwenda TANROADS kwani barabara hii kwa upande wa Singida ipo TANROADS pia sehemu ya Bashnet - Dareda ipo TANROADS hii ni barabara inaunganisha mkoa wa Manyara na Singida
Mheshimiwa Spika, kujengewa angalau zahanati tano kwa mwaka ili kuendana na mahitaji makubwa ya zahanati kwenye wilaya yetu na kuharakisha ujenzi wa vituo vya afya vya Endasak, Balangdalalu, Hidet, Nangwa, Masqaroda na kufanya tathmini kwenye kata zote ili kuboresha miundombinu ya huduma za afya kama Serikali ilivyoahidi kwa Dirma, Laghanga na Getanuwas.
Pia kukamilisha nyumba za walimu, madarasa, mabweni na zahanati ambayo maboma yake yalijengwa kwa nguvu za wananchi kwa mpango wa dharura na kuanzisha mkakati mahususi wa ujenzi wa mabweni kwenye shule za kata ambazo wanafunzi wanalazimika kupangisha vyumba mitaani (mageto) ambayo kwa Hanang ni karibu shule zote ili kuwaokoa watoto wetu na changamoto ya malezi kwa kukaa maeneo yasiyokuwa na usimamizi ikizingatiwa vijana wanaosoma sekondari bado ni wadogo.
Mheshimiwa Spika, pia shule za sekondari za kata za Ishponga, Gendabi, Dawar na Jorodom zijengwe haraka ili kuwaondoelea adha wanayopata watoto wa maeneo tajwa ya kufuata elimu kata za jirani na kwa shida kubwa.
Mheshimiwa Spika, nihitimishe mchango wangu kwa kumshukuru Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kuanza kufanyia kazi maombi tuliyowasilisha wakati tulipokutana na Wabunge wengine wa Mkoa wa Manyara kwani fedha tayari zimeshatoka kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe ya Gendabi, ujenzi wa shule mpya ya Dillinghang, fedha za ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo Basotu, Dajameda, Diloda na Gawolol.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Mpango wa Tatu wa Taifa.
Niseme tu kwenye maelekezo yako umeni-preempt, nilitaka niongelee eneo la elimu. Wadau wengi wamezungumzia suala la mitaala yetu ya elimu kwamba tuna sababu ya kuangalia kama kweli elimu ambayo tunaenda nayo inaendana na mazingira yetu halisia. Tumesema sana lakini ukiangalia kwenye vyuo vyetu tafiti nyingi zinafanyika lakini haziendi kutatua changamoto za wananchi. Maana yake wakati mwingine juhudi kubwa zinafanyika kwenye taasisi zetu za elimu lakini yale yanayopikwa kule hayajafiki kwa walaji ambao ni wananchi katika kutatua changamoto zao kwenye upande wa kilimo, mifugo na masuala mengine ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ufike sasa wakati elimu ile tunayoifundisha isiwe inaowatoa wanafunzi au watu wetu kwenye maisha yao yale ya kawaida, bali iende kuimarisha maisha ya watu yale ya kawaida. Twende tukawasaidie wafugaji wafuge kisasa, hatimaye wapate tija. Siyo kama mtoto akienda shule…
MWENYEKITI: Upande huu kuna kelele sana, naomba tumsikilize Mheshimiwa.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Sio tukipeleka watoto wetu shule, tunawatenganisha na zile shughuli za asili ambazo tumekuwa tukizifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati nasoma shule ya msingi tulikuwa na Afisa wa Kilimo, alikuwa anafundisha kwa vitendo kwa wanafunzi na kwa wanakijiji, naye alikuwa anashika jembe la mkono, alikuwa anashika plau la kuvuta na ng’ombe na katika mazingira yaleyale ambayo watu wapo tuangalie elimu yetu kama inatuelekeza upande huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kwenye Vyuo vyetu vya VETA mambo tunayofundisha ni yaleyale ya kila siku; je, tunaangalia mabadiliko ya maisha ya sasa? Je, tuna-address yale mambo ya msingi ambayo yatatuletea tija? Ukiangalia nchi yetu ina mifugo wengi, tunalima sana, lakini hapo tija inakosekana kwa sababu hatupeleki sayansi kwenye maeneo husika ili tuzalishe kwa tija ili hatimaye tunavyoongea Tanzania ya viwanda tubadilike kutoka kwenye kilimo, tuzalishe tupate mazao ya viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinatumia ardhi, ardhi haiongezeki, Watanzania tunaongezeka. Baada ya muda kama elimu haiwezi kutusaidia waangalie ni namna gani baada ya muda kwa sababu ardhi tuliyonayo haiongezeki lakini sisi tunaongezeka. Kama haiwezi kututoa kwenye eneo hilo kuhakikisha kwamba elimu yetu inatatua changamoto za msingi na mabadiliko ya kila wakati jinsi tunavyoongezeka na ardhi haiongezeki tukatatua hiyo changamoto ya msingi kwamba baadaye tutakuwa hatuna ardhi ya kutosha, hatuna maeneo ya kufuga mifugo, hatuna maeneo ya kulima. Je, elimu yetu itatutoaje kwenye changamoto hiyo? Lazima tujielekeze huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee suala la ufugaji, hasa eneo la usindikaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo. Tuna mifugo mingi sana lakini ukiangalia malori barabarani ukiona yamebeba mifugo, mingi tunasafirisha nchi za jirani. Tunasafirisha nyama, ngozi na mazao mengine. Hatuwezi kupata tija bila kuliangalia hilo eneo kwa makini. Ni lazima tujiwekeze kwenye kuboresha mifugo yetu. Tujiwekeze kwenye kuhakikisha kwamba tunakuwa na machinjio kwenye maeneo yale ambayo kuna mifugo wengi. Hatimaye tu- process vizuri tukatafute masoko nje badala ya kusafirisha mifugo ambayo iko hai. Hiyo inatupotezea na tunapoteza fedha nyingi kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo suala la miundombinu; hii imeongelewa sana. Hakuna namna tunaweza kupata maendeleo bila kuboresha eneo la miundombinu. Kazi kubwa imefanyika lakini bado tunayo kazi kubwa ya kuifanya. Lazima tutoke hapa tukiwa na jawabu. Kwa sababu ukiwa umelima, una mifugo, bila kuwa na uhakika wa kusafirisha na huduma nyingine za kijamii zinakuwa ni changamoto kubwa. Maeneo mengi barabara kwa sasa hazipitiki kwa sababu ya mvua. Lile suala la TARURA kutokuwa na bajeti ya kutosha, hilo eneo bila kuli-address hatuwezi kutoka, lazima tuje na jawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yametolewa mapendekezo mengi. Tuache kwenda kama kawaida, lazima tuje na ubunifu kuhakikisha kwamba kwenye eneo hili tunapata fedha za kutosha na siyo kuchukua kwenye upande wa TANROADS. Nao wana majukumu makubwa ambayo ni ya msingi, hivyo, tuje na njia mbadala ya kupata fedha ilituboreshe TARURA ipate fedha za kutosha ili hatimaye watu wapate huduma za usafiri ulio…
MWENYEKITI: Sasa hapa tulipo Mheshimiwa Engineer ni mahali ambapo utuambie sasa tuzipataje hizo fedha? Yaani utoe mapendekezo.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, lazima tuwekeze kwenye maeneo yetu mkakati. Yameongelewa, eneo la upimaji wa ardhi ambalo nalo nataka niongelee ardhi peke yake, ni sleeping giant ambaye hatujavuna chochote kutoka huko. Ukiangalia kwenye eneo hilo hilo la upande wa ardhi, biashara za upangishaji wa nyumba hazijasimamiwa vizuri. Maeneo hayo kuna mapato ambayo yangeweza kupatikana kuhakikisha kwamba tunapata fedha za kutosha. Tuangalie namna ya kuhakikisha kila tulichonacho tunaweza kukitumia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipima ardhi yote kila mtu akalipa kodi tukahakikisha kwamba biashara zote zinazofanyika za ardhi; za kuuza ardhi, za kupangisha nyumba na nyumba zote zikalipa kodi ile stahiki, tukisimamia maeneo hayo tunapata mapato ya kutosha.
Tuangalie namna ya kuhakikisha kwamba tunapata fedha ili tuwekeze kwenye miundombinu ili hatimaye tuweze kufanya shughuli za uzalishaji kwa urahisi. Miundombinu inayopitika kwa urahisi ndiyo itakayotutoa kwenye mkwamo tulionao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi maeneo mengi wananchi wanakwama kwenda hospitali, wananchi wanakwama kufanya shughuli za kimaendeleo kwa sababu barabara zimekatika na hii kila wakati inakula uchumi wa nchi, lazima tuje na jawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee kidogo eneo la umeme; kazi kubwa imefanyika, vimebaki vijiji vichache. Hata hivyo, ukiangalia kuna baadhi ya maeneo umeme umepita juu, kiasi kwamba wananchi wale wakishushiwa gharama sidhani kama ni kubwa sana, itatusaidia katika kuchochea uchumi kwa kujenga viwanda vidogo na vya kati ili wananchi waweze kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti yetu Kuu. Kwa kuanza naomba nitambue kazi kubwa ambayo inafanyika. Si haba kupandisha pato la Taifa kutoka bilioni 69.9 mwaka 2021 kwenda bilioni 89.4 dola za Kimarekani ni kazi kubwa sana na matumaini ya kwamba bajeti yetu au pato letu la Taifa litaendelea kukua kwa asilimia 5.2, ni kazi kubwa imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya kilimo imeongezwa kutoka bilioni 294 mpaka kufikia bilioni 970.8 mwaka 2023/2024. Hapo tunajihakikishia kwamba tutapata pembejeo, viuatilifu vya kutosha, zana za kilimo lakini wakulima wetu wataendelea kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa afya tumejenga vyumba 111 vya huduma za dharura na pale Hanang sisi tumepata chuma kimoja ambacho kinakaribia kukamilika, vyumba vya wagonjwa mahututi 70 navyo vinakwenda kujengwa, navyo vinaenda kukamilika, nyumba za watumishi wa afya 150 zimejengwa na sisi Hanang tumepata nyumba moja na tumeipeleka pale Zahanati ya Gidagharibu pale Kata ya Simbay. Hii ni kazi kubwa imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepeleka vifaatiba katika maeneo mbalimbali. Hanang tumepata x–ray ya kisasa katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini, lakini vifaa kama CT-Scan zaidi ya 30 zimepelekwa, MRI na vifaa vingine. Hanang tunatarajia kupata ambulance mbili, ni kazi kubwa imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya nishati, miradi mikubwa inaendelea. Bwawa la Mwalimu Nyerere linaendelea kukamilika, lakini na miradi mingine inaendelea kukamilika ili kujihakikishia kwamba gridi yetu inakuwa na umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika kwa upande wa TARURA, barabara nyingi zimejengwa. Tumejenga kilometa 798.1 za lami, lakini kilometa elfu 23.2 hizo za changarawe pamoja na madaraja kadhaa. Mpango wa kutengeneza P4R kwenye upande wa ujenzi wa barabara, hii itatusaidia sana. Ndio maana unasikia Wabunge hapa wanasifia kazi nzuri inayofanyika na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wengine wanasema tumpe maua yake, naunga mkono maua yake apewe kwa kazi nzuri inayofanyika na sisi kwenye majimbo yetu kila sehemu amegusa, ni kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kukumbusha kwenye eneo la TARURA, tunayo majimbo tofauti. Kwenye Jimbo la Hanang kwa sensa ya sasa hivi tuna watu 367,391, kaya ziko karibu 70,000. Vilevile tuna majimbo mengine madogo ambayo hata watu 100,000 hawafiki, kupewa mgao sawasawa sio sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye upande wa nishati hilo pia limefanyika, kwamba kila Jimbo lipewe vitongoji 15 kwa mwaka huu wa fedha. Hilo sio sawa kwa sababu haitaleta tija, tumefanya sensa tumetumia fedha. Hii sensa itumike na wataalam ili hatimaye mgawanyo wa rasilimali uende sawia kwenye majimbo yetu, maendeleo yaende sawa sawa kwenye majimbo yetu. Idadi ya watu izingatiwe ndio maana tumeingia gharama, jiografia ya maeneo yetu izingatiwe ili hatimaye maendeleo yaende sawasawa kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewekeza sana kwenye sekta ya kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anafanya kazi kubwa sana na timu yake. Nampongeza sana rafiki yangu Mheshimiwa Bashe. Hata hivyo, nimhakikishie tumeanza kuingia mashambani mwezi wa 11, kila mtu amepambana kwa namna yake, wengine wamepata na wengine wamekosa. Sasa hivi tuna changamoto na leo hii mimi niko hapa Bungeni kule kwangu wamekaa kikao, maelekezo ni kwamba ukitaka kusafirisha gunia moja la mahindi kwenda Babati, kwenda Arusha mpaka upate kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, hii inatoka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wameenda mashambani kipindi kile Serikali hatukuiona. Sasa hivi tumevuna, tumehangaika wenyewe mbona control zinakuwa nyingi? Kwa nini Serikali isiwe proactive inakuwa reactive? Sisi tunachotaka tukiingia mashambani, Wizara tumeweka fedha za kutosha, wachochee uzalishaji. Wasiende kudhibiti baada ya watu kuwa wamesota mashambani, wao wanazuia sijui watu wasiuze, sijui wasifanyeje. Hii si kazi ya Serikali, Serikali itusaidie tuzalishe zaidi na itusaidie kuweka mifumo mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa inajulikana kwamba kuanzia mwezi Machi hadi sasa tutavuna. Kwa nini mipango hai isiwepo kabla hata muda huu haujafika? Tusiwakwamishe wakulima. Sisi wana Hanang na Watanzania wengi wako kama wana Hanang wanategemea yale wanayopata mashambani, wanategemea mifugo yao kupeleka watoto shule, ni kipindi cha shule kufunguliwa. Sasa hivi biashara ya mazao haieleweki, mifugo tumeuza wakati tunakwenda mashambani. Sasa, unategemea watoto watarudije shule? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itusaidie wakati tunakwenda mashambani, watusaidie mbolea na vitu vingine ili angalau wakati huo tukishazalisha watutengenezee na masoko. Vile vile, kwenye eneo la masoko iwe streamline tuijue, suala la masoko yanakuwa Wizara ya Kilimo au Viwanda na Biashara ili mwishoni sasa tum–task Waziri wa Kilimo kwenye suala la uzalishaji ili upande wa viwana na biashara wahangaike kututafutia masoko. Watusaidie kwenye eneo hili mambo haya yanawachanganya wananchi wetu na hii haikai sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujawahi kumwona Mkuu wa Wilaya wakati tunakwenda mashambani na hatutarajii kumwona Mkuu wa Wilaya sasa hivi wala kwenda kuomba kibali kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo suala la miundombinu. Pia kwenye eneo hili, kazi kubwa yamefanyika. Nikisoma kwenye upande wa uchukuzi, reli hesabu zinasomeka vizuri, lakini napata changamoto kubwa kwenye upande wa barabara. Mwaka 2022 kwenye bajeti kama hii, nilipata nafasi ya kukaa na Waziri wa Ujenzi, tukachorachora Barabara, lakini mpaka sasa sioni kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Kondoa inayokwenda Gisambalang inayotokea Nangwa tulichorachora na Mheshimiwa Waziri mwaka 2022, lakini hakuna kinachoendelea. Vilevile barabara ya Katesh – Haydom, mara zote nimeambiwa hapa Bungeni ni sehemu ya barabara inayotoka Karatu – Mbulu – Haydom – Mto Sibiti – Lalago mpaka Maswa. Juzi wamekwenda kusaini mkataba hata mwaliko Mbunge wa Jimbo la Hanang sikupata na tuna tawi letu hilo ambalo kila mwaka tunaambiwa ni sehemu ya barabara hiyo. Je, yale niliyokuwa naambiwa hapa nilikuwa nadanganywa au wananchi wa Hanang wanadanganywa au Mbunge nilikuwa nadanganywa? Naomba ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alikuwa pale Katesh, babu zake nilivyosema hiyo barabara, nikawambia unabeba pochi ya Mama na yeye ni mtoto mwaminifu wa mama, hiyo pochi ambembeleze mama aifungue kidogo hiyo barabara ijengwe. Wana-Hanang ni wale waliopiga makofi Waziri akatikisa kichwa, lakini mpaka leo hakuna kitu alichoweka pale, hakuna kinachoeleweka. Sasa sisi tufanye nini? Kwenye bajeti hii nikisema naunga mkono bajeti, narudi Hanang wananipokeaje? Tusemezane tu ukweli si aliwambia mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Kampeni amesimama Bassotu, Katesh, Gehandu, tumeongea barabara hiyo hiyo. Tukirudi nyuma Dkt. Magufuli alifanya hivyo hivyo. Tukirudi nyuma Dkt. Jakaya Kikwete naye alifanya hivyo hivyo, mimi nikirudi sasa hivi naenda kuwaambia nini? Tuelezane tu ukweli, barabara hii tumeisema sana na si mimi wa kwanza kuisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 Dkt. Mary Nagu alisimama hapa Bungeni akidai barabara hiyo…
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Hhayuma kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Miraji Mtaturu.
TAARIFA
MHE. MIRAJI J. MTATURU Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji mtani wetu ambaye ametuita sisi babu zake kwamba, unapoambiwa barabara ni kiungo maana yake barabara kuu itakamilika feeder road itajengwa. Kwa hiyo, maana yake ndiyo hiyo tafsiri halisi ya barabara ambayo inaungiwa pale. Ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Hhayuma, unapokea taarifa?
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namheshimu sana mjukuu wangu lakini naomba asitumie muda wangu na naomba tu unilindie muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara hii limesemwa mara nyingi kwamba ni feeder road na maneno yamekuwa ni mengi. Sisi tunachotaka barabara hiyo ijengwe na wala hatutaki maneno mengine na ili nijiridhishe kwamba kwenye bajeti hii tuko pamoja nipate maelezo ya kina na wala sina lingine zaidi ya hilo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako ndio umekwishayoyoma hivyo. Malizia sentesi yako.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi na naamini Mheshimiwa Waziri atakuwa na maelezo ya kina ili tukubaliane bajeti hii ni ya kwetu au ya kwake?
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na jioni ya leo naanza kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruzuku uhai, afya njema na nguvu ili niweze kuchangia kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Hanang.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba tarehe 3 Desemba, 2023 Jimbo la Hanang tulipata changamoto kubwa sana ya maporomoko ya Mlima Hanang na kwenye hayo maporomoko madhara mengi yalitokea. Narudia tena kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo ilifanyika. Mji wa Hanang ambao ni Makao Makuu ya Wilaya pale Katesh palijaa tope ambalo kwa kweli tungetakiwa tutoe sisi wenyewe ingetuchukua labda miaka mitatu ili tuweze kulimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa angalau wananchi wanapita kwa sababu Serikali yetu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya usimamizi makini wa Dkt. Samia Suluhu Hassan waliacha kila kitu ili kuhakikisha kwamba wanatusaidia na kwa sasa mambo mengi yanaenda sawasawa. Mambo mengi yalifanyika ili angalau zile huduma za msingi ziweze kurudi kwenye hali ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kipindi kile kila mtu alikuwa amechanganyikiwa. Tumepoteza ndugu zetu 89, wengi waliathirika lakini na biashara za watu ziliathirika. Miundombinu mingi ambayo tulikuwa tumeitengeneza kwa gharama kubwa yote ilienda na yale maporomoko. Tunasema tunaishukuru sana Serikali kwa nguvu ambayo iliitoa, tulishinda usiku na mchana na Mheshimiwa Jenista Mhagama na timu nzima ya Serikali, tunasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingi zimekwishafanyika. Madhara yale ni makubwa sana, ukiangalia kwa miundombinu ambayo iliathirika, kwa maana ya barabara, mpaka sasa Barabara ya kutoka Endasak – Gitting – Gendabi - Dawar hiyo haipitiki kabisa. Ukishuka upande wa mjini barabara zote za mjini maeneo mengine ni maporomoko makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha tulizoziomba kwa upande wa barabara. Upande wa miundombinu ya maji, mlima Hanang ndicho chanzo kikuu cha maji kwa Wilaya ya Hanang. Tuna kata karibu saba, tunaanza Kata yenyewe ya Gendabi, Kata ya Dawar, Gitting, Measkron, unakuja Kata ya Nangwa. Ukija kwenye mamlaka yote ya mji, Kata ya Katesh, Kata ya Ganana, Kata ya Dumbeta na Kata ya Jorodom wote hao miundombinu ya maji iliathirika, tulijaribu kurudishia kwa kipindi kile kwa dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatamani na sisi turudi kwenye hali ya kawaida ya maendeleo ambayo tuliyatamani na ile Hanang ambayo ni ya maziwa na asali ili tuweze kuirudia. Kuna fedha ambazo tuliziomba, tunaomba zile fedha zitoke kwa wakati ili miundombinu hiyo yote iweze kurudishwa kwenye hali yake ya kawaida ili Hanang iweze kwenda sawasawa na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, fedha kwenye upande wa maji na upande wa miundombinu ya barabara zitoke kwa wakati ili kazi ile iweze kukamilika na sisi tuweze kurudi kwenye hali ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kipindi kile kuna biashara ambazo ziliathirika moja kwa moja kwa sababu lilipigwa eneo la soko ambalo lilikuwa linategemewa na wananchi wote wa Mji wa Katesh. Kwa sasa tunaishukuru sana Serikali, imejenga soko kwa ajili ya kurudishia. Hata hivyo lile soko liko pembeni kidogo ilhali wananchi wameshazoea kuishi mazingira ya mjini. Kuna changamoto ya kukubali yale mazingira kwamba sasa tukitoka kule nani atatufuata, kwa sababu utaratibu wa binadamu pale ambapo umezoea kila siku kwenda ndiyo akili yako muda wote iko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ukitembea Mji wa Katesh kila sehemu kila mtu ametegesha sehemu ya kushikilia na wale wafanyabiashara wengi waliathirika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Jenista Mhagama. Tuliwaita watu wa benki na taasisi za mikopo, tukaongea nao ili waangalie namna ambavyo wanaweza kuangalia kupata unafuu kwa wale wafanyabiashara kwa sababu athari zile ni kubwa na biashara nyingine zilikuwa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuangalia namna ya kusaidia zile biashara zilizoathirika moja kwa moja. Tuwalee wale ili waweze kurudi kwenye hali yao ya kawaida, wale wanahitaji kulelewa. Tunafahamu kazi kubwa imefanyika, tunaomba, kwa sababu kweli changamoto ilikuwa ni kubwa, lakini ukiangalia biashara 713 zilizoathirika moja kwa moja kila mtu alikuwa na hali tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wale ambao wanaweza kujimudu baada ya kuwaombea zile nafuu ambazo tuliziomba na wakazipata, lakini kuna wale ambao hawana namna, hawa tuendelee kuwalea, tuendelee kuwawezesha ili kuhakikisha kwamba wanarudi kwenye hali yao ya kawaida ya maisha. Naomba kwenye eneo hili tuendelee kushirikiana, kuhakikisha kwamba wale wananchi wanaweza kurudi kwenye hali yao ya maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kati ya sehemu kubwa ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu inaifanyia kazi, ni kuwawezesha wananchi kwa kuhakikisha kwamba wanapata au wanachochea uchumi wa wananchi. Tumekuwa na utaratibu wetu wa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri zetu, ile 4:4:2. Kwa maana ya kwamba vijana wanapata asilimia nne (4), akinamama wanapata asilimia nne (4) na walemavu asilimia mbili (2). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hiyo ilitolewa kwa kipindi kirefu, lakini wananchi wengi walinufaika na walikuwa wakiitegemea. Ni kweli changamoto zilijitokeza kwamba fedha zile zilikuwa hazirudi. Tunachoomba sasa ile mikopo iliyosimama maana yake shughuli nyingi za wananchi za kiuchumi zilisimama. Ungefanyika utaratibu wa haraka kuhakikisha kwamba zile fedha zinaanza kutoka tena ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kawaida ambazo wamezoea, za kilimo, biashara, uvuvi na ufugaji. Tukiendelea kushikilia hizo fedha maana yake tumeshikilia uchumi wa wananchi, tumeshikilia uchumi wa nchi yetu. Hizo fedha zianze kutoka mapema inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuangalia mahitaji makubwa ya kupeleka ile elimu ya vitendo kwa wananchi wetu Serikali iliridhia vyuo vya ufundi vijengwe kwenye maeneo mbalimbali ndani ya wilaya yetu. Kulikuwa na ujenzi wa vyuo vya ufundi kila wilaya. Ukipita pale Hanang ambako tulichagua eneo la Nangwa kwa ujenzi wa chuo cha ufundi, ukipita unasikitika kwa jinsi unavyoenda kwa kasi ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iwe inatoa fedha kwa wakati ili ujenzi ukamilike kwa vyuo vile ambavyo tumevilenga ili hatimaye tupate wataalam tunaowahitaji kwenye maeneo yetu. Imekuwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hakuna hata sehemu moja kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi ambao unafanyika, nikitolea mfano eneo la Nangwa ambao haukufika hata hatua ya lintel.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kwenye eneo hili iweke fedha za kutosha ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati. Ili hatimaye watoto wa Kitanzania wapate ujuzi unaohitajika kwenye eneo la kilimo, uvuvi, mifugo na hatimaye waweze kupambana na mazingira waliyonayo kutumia elimu ambayo itatokana na vyuo vyetu vya ufundi ili kutibu tatizo ambalo lipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya wafugaji yalianzisha shule maalum za watoto wa wafugaji. Kwa Jimbo la Hanang sisi tulikuwa na shule mbili maalum kwa ajili ya watoto wa wafugaji. Tulikuwa na shule ya Gendabi na shule ya Bassodesh ambazo zote ni shule za msingi za bweni. Shule hizi zilikuwa zinasaidia kwa sababu maisha yetu ya ufugaji kwa sasa bado hatujayaboresha kiasi cha kwamba tunaweza kutulia sehemu moja na watoto wetu wakapata elimu inayostahiki, tumekuwa na maisha ya kuhamahama. Ili kutibu tatizo hilo la wazazi kuhamahama, watoto walikuwa wanawekwa bweni ili wapate elimu kwa wakati bila kubughudhiwa na tabia ile ya kifugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali chini ya usimamizi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumepata ukarabati mzuri kwenye Shule Maalum ya watoto wa kifugaji ya Gendabi ambako angalau pakikamilishwa kabisa yale mazingira yangekuwa sawasawa. Ukienda Bassodesh kwa sasa hali ni tete, mabweni yamebomoka, madarasa yamebomoka na ile shule ni ya miaka mingi, wamesoma watu ambao mpaka sasa wameshastaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tutengewe fedha ili kuhakikisha yale maeneo maalum tuliyoyatengea na yale ya uangalizi yaweze kupata fedha na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanatengenezwa vizuri ili watoto ambao wana changamoto ya kupata elimu nao wapate elimu inayopaswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa kutoa salamu kwa ndugu zangu wa Wizara ya Ujenzi. Kumekuwa na taratibu hizi za EPC+ F, taratibu hizi za design and build lakini taratibu hizi barabara zingine unaanza ule upembuzi wa awali na usanifu wa kina. Barabara ya Haydom- Mogitu imekuwa ya muda mrefu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea hivi hatutaelewana, barabara hii inapaswa kujengwa ni ahadi ya Marais watatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kuniona na kunipa nafasi hii awali ya yote nichukue nafasi hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na tunaendelea na shughuli zetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti yake. Lakini niipongeze kazi nzuri inayofanywa na Serikali yangu, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, ukiangalia kazi iliyofanywa na Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwanga tunauona, miradi ni mingi imetekelezwa na Awamu ya Sita sera yetu kazi inaendelea, maana yake tunaenda kukamilisha miradi ile yote. Na sisi tuna Imani na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwamba, tutaenda kwa kasi zaidi kwani alikuwepo kwenye maandalizi yote na ile awamu ya tano kazi walifanya vizuri pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye eneo la ajira. Hasa suala la ajira kwa vijana, vijana wetu wengi wamemaliza shule wako mtaani hawana kazi na tumekuwa na mjadala mkubwa kwenye eneo la elimu, kama elimu yetu kweli inaendana na mazingira ya kwetu.
Mheshimiwa Spika, lakini, vijana wengi kuanzia wale ambao hawajakanyaga darasani na wengine wana masters wanafanya kazi ya bodaboda. Ninachoomba Serikali yangu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi kundi hili limekuwa kubwa, lina watu wa aina mbalimbali tujielekeze. Ile mifuko ya maendeleo ya vijana iangalie kundi hili muhimu na vijana hawa wa bodaboda ambao ni kundi kubwa kwa sasa, tuwatengenezee utaratibu maalum wa kuwatoa kwenye kazi ile ya bodaboda na hatimaye nao wapate uchumi kupitia kazi wanayoifanya.
Mheshimiwa Spika, tuwajenge ili waielewe kwamba kazi ya bodaboda ni sehemu ya ajira, lakini wanahitaji kuendelezwa kutoka hapo. Kwenye zile asilimia 4 za vijana zilizoko kwenye halmashauri, tuwaangalie hao ambao tayari wameshaanza kujishughulisha. Fungu lile la mfuko wa vijana ambao uko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, tuangalie hili kundi ambalo limeshaanza kujishughulisha, ili hatimaye waweze kupata shughuli zilizo imara ambazo zinaweza zikawaingizia kipato. Kwani kwa sasa, kundi lile linaonekana kama kundi la watu ambao hawana nidhamu kihivyo katika uendeshaji wa shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, hawafuati sheria, wakati mwingine nao wana hasira na jamii nyingine. Ukiona kijana wa bodaboda ukimgusa tu, wanakusanyika utafikiri ni vita kwasababu, watu wamekosa amani. Sasa, tutengeneze mfumo ambao unaweza kuwatoa kwenye kazi ile wanayoifanya. Kazi ya bodaboda ukiifanya miaka miwili kifua hakifai kwasababu, wanavyoendesha hawafuati sheria. Hawachukui tahadhari, hawajilindi na pia wanakimbizana na polisi sana. Sasa badala ya kukimbizana na vijana hao tuwatengenezee utaratibu mahsusi wa namna ya kuwafundisha kufata sheria na zile shughuli zao ziweze kutambulika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema suala la vijana hasa na kwa eneo la kuwawezesha lakini pia tunalo eneo la ardhi. Ardhi imekuwa changamoto kubwa na sababu kubwa ni kwamba, ardhi tuliyonayo haiongezeki na sisi tunaongezeka. Na ukiangalia wengi ambao wana ardhi zilizo kubwa yawezekana ni wazee wetu ambao hawakwenda shule sana, au wakati mwingine hawajapata bahati na hizo ardhi wamepata kwa njia zile za asili. Sasa hivi watu wanaohitaji ardhi kidogo wameanza kuwa na elimu elimu kwasababu, ardhi yetu haijapimwa yote kumekuwa na dhuluma sana kwenye eneo la ardhi. Ninachoomba Serikali yangu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi tujielekeze kwenye eneo la ardhi. Tuhakikishe watu tunawamilikisha ardhi zao kwa mujibu wa sheria, ili kuondoa migogoro mingi iliyojaa kwenye ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye ofisi za Wabunge nina uhakika wenzangu pia mnapata tatizo kama mimi, kuna malalamiko mengi ya wazee wetu kudhulumiwa ardhi zao. Na ukifuatilia, mzee utakuta hana nyaraka atakuambia mwaka sabini na ngapi aligawiwa ardhi hiyo, sasa mtu amechukua na kwasababu anajua jua kidogo taratibu, inakuwa ngumu sasa kubatilisha kwamba hajaipata kisheria. Na ardhi ni chanzo kizuri cha mapato, tukiipima ni imani yangu malalamiko ambayo tunayo kwenye upande wa TARURA tutapata fedha hapa. Kwani watu wataanza kulipa kodi za ardhi. Ninachoomba eneo hili tuliangalie kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kidogo eneo la miundombinu kwasababu ni changamoto ya kila sehemu. Tumeongea sana namna ya kupata fedha ili angalau TARURA iweze…
SPIKA: Ahsante sana
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa kuwatumikia Watanzania.
Pia niwapongeze Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Maryprisca Mahundi, Naibu Waziri wa Maji, Katibu Mkuu pamoja na watumishi wote wa makao makuu ya Wizara ya Maji pamoja na RUWASA kwani wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Spika, kipekee niwapongeze Engineer Walter, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara na Engineer Idd Msuya - Mkurugenzi Mtendaji wa BAWASA, wanafanya kazi nzuri sana. Naomba sana watumishi hawa waendelee kutusaidia ili kukamilisha miradi inayoendelea.
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia fedha kwa ajili ya maji ya mji wa Katesh wa shillingi 2,300,000,000 ambapo mabomba yameanza kupokelewa ili kusambaza maji, pia mradi wa maji Gehandu na visima 24 ambavyo vinaendelea kuchimbwa kwa fedha za mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukurani nilizotoa hapo juu Wilaya ya Hanang ni kubwa, ina kata 33, vijijini 96 na maeneo mengi hayana maji, naomba mtuangalie kwa jicho la kipekee kwa kukamilisha miradi inayoendelea ya Ziwa Bassotu (mradi wa vijijini 12), mradi wa Gehandu; pia miradi mpya ifanyiwe usanifu kwenye chanzo cha Mto Duru- Masakta, maji ya Bwawa Bassotughang iliyopo kijiji cha Bassotughang, kata ya Hidet ili yatumike kwa matumizi ya binadamu na mifugo.
Mheshimiwa Spika, mimi ninaimani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri na timu yake, ila atusaidie Wilaya ya Hanang kwani Meneja wa Wilaya tuliyenaye kweli hafanyi vizuri na Mheshimiwa Waziri alipokuwa Kongwa alitamka kumfukuza kazi na analalamikiwa sana kwa kufanya kazi chini ya kiwango. Hivyo ili meneja huyu asiharibu kazi nzuri inayofanywa na Serikali apangiwe majukumu mengine atakayomudu vizuri.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango wangu huu naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na jioni ya leo naanza kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruzuku uhai, afya njema na nguvu ili niweze kuchangia kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Hanang.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba tarehe 3 Desemba, 2023 Jimbo la Hanang tulipata changamoto kubwa sana ya maporomoko ya Mlima Hanang na kwenye hayo maporomoko madhara mengi yalitokea. Narudia tena kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo ilifanyika. Mji wa Hanang ambao ni Makao Makuu ya Wilaya pale Katesh palijaa tope ambalo kwa kweli tungetakiwa tutoe sisi wenyewe ingetuchukua labda miaka mitatu ili tuweze kulimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa angalau wananchi wanapita kwa sababu Serikali yetu sikivu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya usimamizi makini wa Dkt. Samia Suluhu Hassan waliacha kila kitu ili kuhakikisha kwamba wanatusaidia na kwa sasa mambo mengi yanaenda sawasawa. Mambo mengi yalifanyika ili angalau zile huduma za msingi ziweze kurudi kwenye hali ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kipindi kile kila mtu alikuwa amechanganyikiwa. Tumepoteza ndugu zetu 89, wengi waliathirika lakini na biashara za watu ziliathirika. Miundombinu mingi ambayo tulikuwa tumeitengeneza kwa gharama kubwa yote ilienda na yale maporomoko. Tunasema tunaishukuru sana Serikali kwa nguvu ambayo iliitoa, tulishinda usiku na mchana na Mheshimiwa Jenista Mhagama na timu nzima ya Serikali, tunasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingi zimekwishafanyika. Madhara yale ni makubwa sana, ukiangalia kwa miundombinu ambayo iliathirika, kwa maana ya barabara, mpaka sasa Barabara ya kutoka Endasak – Gitting – Gendabi - Dawar hiyo haipitiki kabisa. Ukishuka upande wa mjini barabara zote za mjini maeneo mengine ni maporomoko makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha tulizoziomba kwa upande wa barabara. Upande wa miundombinu ya maji, mlima Hanang ndicho chanzo kikuu cha maji kwa Wilaya ya Hanang. Tuna kata karibu saba, tunaanza Kata yenyewe ya Gendabi, Kata ya Dawar, Gitting, Measkron, unakuja Kata ya Nangwa. Ukija kwenye mamlaka yote ya mji, Kata ya Katesh, Kata ya Ganana, Kata ya Dumbeta na Kata ya Jorodom wote hao miundombinu ya maji iliathirika, tulijaribu kurudishia kwa kipindi kile kwa dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatamani na sisi turudi kwenye hali ya kawaida ya maendeleo ambayo tuliyatamani na ile Hanang ambayo ni ya maziwa na asali ili tuweze kuirudia. Kuna fedha ambazo tuliziomba, tunaomba zile fedha zitoke kwa wakati ili miundombinu hiyo yote iweze kurudishwa kwenye hali yake ya kawaida ili Hanang iweze kwenda sawasawa na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, fedha kwenye upande wa maji na upande wa miundombinu ya barabara zitoke kwa wakati ili kazi ile iweze kukamilika na sisi tuweze kurudi kwenye hali ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kipindi kile kuna biashara ambazo ziliathirika moja kwa moja kwa sababu lilipigwa eneo la soko ambalo lilikuwa linategemewa na wananchi wote wa Mji wa Katesh. Kwa sasa tunaishukuru sana Serikali, imejenga soko kwa ajili ya kurudishia. Hata hivyo lile soko liko pembeni kidogo ilhali wananchi wameshazoea kuishi mazingira ya mjini. Kuna changamoto ya kukubali yale mazingira kwamba sasa tukitoka kule nani atatufuata, kwa sababu utaratibu wa binadamu pale ambapo umezoea kila siku kwenda ndiyo akili yako muda wote iko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ukitembea Mji wa Katesh kila sehemu kila mtu ametegesha sehemu ya kushikilia na wale wafanyabiashara wengi waliathirika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Jenista Mhagama. Tuliwaita watu wa benki na taasisi za mikopo, tukaongea nao ili waangalie namna ambavyo wanaweza kuangalia kupata unafuu kwa wale wafanyabiashara kwa sababu athari zile ni kubwa na biashara nyingine zilikuwa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuangalia namna ya kusaidia zile biashara zilizoathirika moja kwa moja. Tuwalee wale ili waweze kurudi kwenye hali yao ya kawaida, wale wanahitaji kulelewa. Tunafahamu kazi kubwa imefanyika, tunaomba, kwa sababu kweli changamoto ilikuwa ni kubwa, lakini ukiangalia biashara 713 zilizoathirika moja kwa moja kila mtu alikuwa na hali tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wale ambao wanaweza kujimudu baada ya kuwaombea zile nafuu ambazo tuliziomba na wakazipata, lakini kuna wale ambao hawana namna, hawa tuendelee kuwalea, tuendelee kuwawezesha ili kuhakikisha kwamba wanarudi kwenye hali yao ya kawaida ya maisha. Naomba kwenye eneo hili tuendelee kushirikiana, kuhakikisha kwamba wale wananchi wanaweza kurudi kwenye hali yao ya maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kati ya sehemu kubwa ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu inaifanyia kazi, ni kuwawezesha wananchi kwa kuhakikisha kwamba wanapata au wanachochea uchumi wa wananchi. Tumekuwa na utaratibu wetu wa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba kupitia mapato ya ndani ya halmashauri zetu, ile 4:4:2. Kwa maana ya kwamba vijana wanapata asilimia nne (4), akinamama wanapata asilimia nne (4) na walemavu asilimia mbili (2). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hiyo ilitolewa kwa kipindi kirefu, lakini wananchi wengi walinufaika na walikuwa wakiitegemea. Ni kweli changamoto zilijitokeza kwamba fedha zile zilikuwa hazirudi. Tunachoomba sasa ile mikopo iliyosimama maana yake shughuli nyingi za wananchi za kiuchumi zilisimama. Ungefanyika utaratibu wa haraka kuhakikisha kwamba zile fedha zinaanza kutoka tena ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kawaida ambazo wamezoea, za kilimo, biashara, uvuvi na ufugaji. Tukiendelea kushikilia hizo fedha maana yake tumeshikilia uchumi wa wananchi, tumeshikilia uchumi wa nchi yetu. Hizo fedha zianze kutoka mapema inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuangalia mahitaji makubwa ya kupeleka ile elimu ya vitendo kwa wananchi wetu Serikali iliridhia vyuo vya ufundi vijengwe kwenye maeneo mbalimbali ndani ya wilaya yetu. Kulikuwa na ujenzi wa vyuo vya ufundi kila wilaya. Ukipita pale Hanang ambako tulichagua eneo la Nangwa kwa ujenzi wa chuo cha ufundi, ukipita unasikitika kwa jinsi unavyoenda kwa kasi ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iwe inatoa fedha kwa wakati ili ujenzi ukamilike kwa vyuo vile ambavyo tumevilenga ili hatimaye tupate wataalam tunaowahitaji kwenye maeneo yetu. Imekuwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hakuna hata sehemu moja kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi ambao unafanyika, nikitolea mfano eneo la Nangwa ambao haukufika hata hatua ya lintel.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kwenye eneo hili iweke fedha za kutosha ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati. Ili hatimaye watoto wa Kitanzania wapate ujuzi unaohitajika kwenye eneo la kilimo, uvuvi, mifugo na hatimaye waweze kupambana na mazingira waliyonayo kutumia elimu ambayo itatokana na vyuo vyetu vya ufundi ili kutibu tatizo ambalo lipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya wafugaji yalianzisha shule maalum za watoto wa wafugaji. Kwa Jimbo la Hanang sisi tulikuwa na shule mbili maalum kwa ajili ya watoto wa wafugaji. Tulikuwa na shule ya Gendabi na shule ya Bassodesh ambazo zote ni shule za msingi za bweni. Shule hizi zilikuwa zinasaidia kwa sababu maisha yetu ya ufugaji kwa sasa bado hatujayaboresha kiasi cha kwamba tunaweza kutulia sehemu moja na watoto wetu wakapata elimu inayostahiki, tumekuwa na maisha ya kuhamahama. Ili kutibu tatizo hilo la wazazi kuhamahama, watoto walikuwa wanawekwa bweni ili wapate elimu kwa wakati bila kubughudhiwa na tabia ile ya kifugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali chini ya usimamizi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumepata ukarabati mzuri kwenye Shule Maalum ya watoto wa kifugaji ya Gendabi ambako angalau pakikamilishwa kabisa yale mazingira yangekuwa sawasawa. Ukienda Bassodesh kwa sasa hali ni tete, mabweni yamebomoka, madarasa yamebomoka na ile shule ni ya miaka mingi, wamesoma watu ambao mpaka sasa wameshastaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tutengewe fedha ili kuhakikisha yale maeneo maalum tuliyoyatengea na yale ya uangalizi yaweze kupata fedha na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanatengenezwa vizuri ili watoto ambao wana changamoto ya kupata elimu nao wapate elimu inayopaswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa kutoa salamu kwa ndugu zangu wa Wizara ya Ujenzi. Kumekuwa na taratibu hizi za EPC+ F, taratibu hizi za design and build lakini taratibu hizi barabara zingine unaanza ule upembuzi wa awali na usanifu wa kina. Barabara ya Haydom- Mogitu imekuwa ya muda mrefu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea hivi hatutaelewana, barabara hii inapaswa kujengwa ni ahadi ya Marais watatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nichukue nafasi hii, kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuaminiwa. Pia niipongeze wizara nzima kwa kazi nzuri inayofanyika.
Mheshimiwa Spika, niongelee maeneo mawili, eneo la kwanza ni eneo la Vitambulisho vya Taifa. Hili suala limesemwa sana jimboni kwangu, wazee wananiuliza hivi tumechukuliwa alama za vidole, ilikuwa ni maonyesho tu, hivi vitambulisho mbona haviji? Kweli hivyo vitambulisho ni muhimu sana kwa ajili ya watu kufanya shughuli zao na kwa ajili ya kujitambulisha katika maeneo mbalimbali. Ukienda kwa watendaji kuomba barua, siku hizi katika maeneo mengine hizo barua za watendaji hazitambuliki, vitambulisho vile ni muhimu kwa watu kupata huduma na kufanya shughuli za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nijielekeze upande wa huduma hasa za Jeshi la Polisi. Nawapongeza kwa kazi nzuri inayofanyika, kazi ya kuhakikisha kwamba usalama na ulinzi wa raia na mali zao. Vijana wetu wanajituma sana na sisi ambao tunafanya siasa huwa tunatembea usiku na njiani tunaona jinsi wanavyopigwa na baridi, wanavumilia. Ninachoomba, ili wafanye kazi kwa moyo Wabunge wenzangu wamesema sana, tuangalie maslahi yao, wawe na furaha na kazi wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye maslahi hasa na kwenye vifaa ambavyo wanavitumia kwa ajili ya kutenda kazi; magari na service za magari, kwa sababu wakati mwingine wanakuwa watumwa kwa viongozi wengine, Polisi katika Halmalshari hawana mafuta wanakwenda kuomba kwa Mkurugenzi. Wakati mwingine wana kazi ya kwenda kufanya au kwenda kukamata, mhalifu, yule aliyelalamika analazimika kuombwa mafuta. Sasa hapo haki inakuwa ngumu kutendeka. Naomba tuwatendee haki tuwape vitendea kazi ili wafanye kazi zao vizuri.
Mheshimiwa Spika, eneo linguine ni eneo la ulinzi shirikishi, Polisi Jamii. Hii inakwenda wakati mwingine inafifia, naomba eneo hilo tulikazie ili angalau sasa wananchi wakishiriki usalama unakuwa mzuri zaidi. Namie niombe ulinzi shirikishi au Polisi Jamii itanuliwe kidogo ifike kwenye upande wa kutekeleza Sheria hizi za Usalama Barabarani hasa inayowagusa vijana wetu wa bodaboda, ambao wengi wao wanaendesha vyombo vile bila mafunzo yaliyokamilika. Kumekuwa na utamaduni sasa kwa sababu anajua kabisa ana makosa, akisimamishwa hasimami anakimbia. Sasa Polisi wanachukua hatua za ziada za namna ya kuhakikisha wanaweza kuwakamata, wakati mwingine wanawachapa fimbo. Sasa ukifanya hivyo maana yake unahatarisha maisha ya yule anayeendesha, lakini na watumiaji wengine wa barabara.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza ajali ambazo zinaweza kuzuilika, naomba katika eneo hili, polisi jamii tuwatengenezee utaratibu mzuri, kwa sababu wana vikundi vyao vile vikundi tuviimarishe ili washirikiane vizuri na Jeshi la Polisi. Kwenye jimbo langu ukienda kimya kimya kama hawajui gari vijana wanaanza kukimbia, maana yake kidogo kuna ile sintofahamu, hilo eneo tukikaa nao, tukalirekebisha angalau tutawasaidia hao vijana kufanya shughuli zao kwa kufuata taratibu na sheria za nchi. Badala ya kuweka nguvu nyingi katika kuwakamata, wakiwa na vitambulisho vya uraia wanafahamika wote wanatoka maeneo gani, wana-register nzuri kwenye eneo lile, inakuwa rahisi kumfuata hata baada ya kuwa umeshajua kuwa kuna kijana huyo amekimbia. Unamfuta kwenye eneo ambalo anaishi hakuna sababu ya kukimbizana.
Mheshimiwa Spika, tuliongea sana na eneo pia la faini wanayopigwa vijana wa bodaboda, pikipiki zile sio zao, kwa siku mapato labda shilingi elfu nane, lakini akipatikana na kosa elfu thelathini. Anaanza kukimbizana na ndugu zake, hii kweli inawaumiza vijana, hatuwajengei uwezo wa kujikwamua kiuchumi. Tutafute namna ya kuwawezesha ili watekeleze sheria na wafanye shughuli zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapa kwa sababu najua kuna limitation ya muda, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayofanyika kwenye sekta ya maji. Kwenye Wilaya ya Hanang inategemewa miradi mikubwa ambayo inaenda kutatua kero kubwa ya maji kwa wana-Hanang.
Mheshimiwa Spika, miradi ya maji Hanang; Wilaya ya Hanang ina Mradi wa Mogitu - Gehandu, Gawlolo, Mureru, Ziwa Bassotu, Bwawa la Bassotughang, Basodesh, Gijetamhog, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh na vijiji vingine ambavyo jumla zimechimbwa visima 24 na utaratibu unafanyika wa kuchimba visima vingine 16 ili jumla tutakuwa na visima 40 ndani ya miaka mitatu. Wana-Hanang wanaendelea kusubiri kwa hamu kukamilika kwa miradi hii ili maji yawafikee wananchi.
Mheshimiwa Spika, maombi mahsusi; Bwawa la Gidahababiye ambalo usanifu wake umekamilika muda mrefu tupate fedha ya kuujenga, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana, pia mnaweza kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili litumike kwa ajili ya umwagiliaji.
Kuhusu miradi inayoendelea ikamilike kwa wakati hasa Mamlaka ya Mji wa Katesh ambayo ili mradi ukamilike inahitajika tu 570,000,000 ukizingatia mpaka sasa tumeshatumia zaidi shilingi bilioni tano kwenye mradi huu.
Mheshimiwa Spika, kasi ya ujenzi wa mradi wa Ziwa Bassotu ni ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji, tuendelee kutenga fedha za kutosha ili uweze kukamilika; na tupate gari ili kurahisisha utendaji kazi kwa RUWASA ndani ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kwa kunipa nafasi awali ya yote nichukuwe nafasi hii kwa falsafa ile ile kwamba mnyonge mnyongeni lakini haki mpatieni. Niipongeze sana Wizara ya Maji kwa kazi nzuri inayofanyika, nikupongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa timu yako yote kwa kazi nzuri inayofanyika kwenye sekta ya maji.
Mheshimiwa Spika, lakini pia niwapongeze kwa kazi ambayo kwa kweli mnaifanya kwa uvumilivu mkubwa mara zote nikikufuata wizarani unanipa nafasi ya kunisikiliza na tunajadiliana majadiliano ambayo kwa kweli yanaonyesha dira kwamba wana Hanang wanaenda kupata maji maeneo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nichukuwe nafasi hii kushukuru kwa bajeti hii kuonyesha maeneo ambayo kwa kweli yalikuwa na matatizo ya maji muda mrefu, kwamba mmetutengea fedha za utafiti wa kupata vyanzo vya maji kijiji cha Mberu, Diloda, Bassodesh, Sasemwega, Mwanga, Lalaji, Wakhama, Masaqa, na ukichukua eneo la Mberu kipindi kirefu wananchi wanaamka saa tisa wanarudi nyumbani saa sita mchana shughuli zingine zote zinasimama wanafuata maji.
Mheshimiwa Spika, lakini zaidi sana mradi wa maji Gehandu eneo lile lilikuwa na changamoto ya muda mrefu tulijadiliana kwa kina na Mheshimiwa Waziri, kisima kimeshachimbwa usanifu umefanyika, lakini kwenye maandiko hapa naona unakwenda Gehandu Ming’enyi na Mugucha nilishaongea na wataalamu kwamba ule mradi kwasababu maji ni mengi tutanuwe kidogo uwende Milongori, uende kijiji cha Gidabwanja, uwende kwenye kitongoji cha Mwanina na kitongoji Marega kwasababu ni maeneo yako karibu na kwenye mteremko ni rahisi kupeleka maji.
Mheshimiwa Spika, lakini pia pale Lalaji tumejenga shule ya sekondari ya kisasa sana na tuna kituo kizuri cha afya na mmeweka angalau mpango wa kupeleka maji na eneo lile halikuwa na maji muda mrefu sana eneo hili nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia na pia tuna mpango huo wa kutanua mtandao wa maji kwenye Kata za Dirima, Lalaji, Mberu pamoja na Hideti. Ni kazi kumbwa naamini kwamba maeneo haya kidogo yatajaribu kupunguza changamoto ya maji ambayo tulikuwa nayo.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na juhudi zote zinazofanyika ninaomba Mheshimiwa Waziri eneo la usimamizi wa utekelezaji wa miradi ili eneo liangaliwe kwa ukaribu, kuna wakati nilishawahi kusema hapa Bungeni tafadhali wasongelee karibu wataalamu wako ili angalau watekeleze miradi hii kwa ufanishi, jana baadhi ya Wabunge walichangia kwamba miradi mingi inatekelezwa kwa njia ya force account, ni wazo nzuri kama tuna rasilimali watu ya kutosha na naamini kwamba ni njia ambayo iko tuseme inathamani ya fedha kwa kazi kutekelezwa tuangalie je, kweli tunao huo uwezo je, hatucheleweshi miradi kwa kufuata hiyo njia lakini pia tuangalie tukiwatumia wakandarasi kwa njia ambazo zimeshauriwa, kwamba wakandarasi wengine inawezekana hawana mitaji tuangalie namna ya ku-manage ili tuhakikishe kwamba miradi inatekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, lakini pia jinsi tunavyozisimamia mamlaka zetu za maji sitaki sana niwe mlalamishi kwenye eneo hilo, lakini kwenye maandiko ya wizara umesema kwa kiwango kikubwa maendeleo ya jamii yoyote inategemea uwepo wa maji ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa. Sasa ukiangalia mji wetu wa Kateshi pale umejengwa mradi wa maji wa bilioni 2.5, mradi ule hauleti tija yoyote kwasababu mradi umekamilika kwa maana na umekabidhiwa kwa mamlaka ya maji, lakini uendeshwaji wa Mamlaka ya Maji kwa kipindi kirefu hakuna board, ukifuatilia ni board ni kazi ya mtu mmoja.
Mheshimiwa Spika, naomba zile mamlaka zisimamiwe vizuri lakini pale ambapo hakuna ufanisi, zile mamlaka wakati mwingine zinatuongezea gharama ukiangalia Dar es Salaam na Pwani inasimamiwa na DAWASA na gharama za maji ni nafuu. Huku kwetu unit inaenda mpaka 2,500 tuangalie eneo hili la mamlaka za maji zinaleta gharama kubwa kwa watumiaji wa mwisho. Ninaomba sana eneo hili lisimamiwe vizuri ili kuhakikisha kwamba tunapata tija ambayo tunaitarajia.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa kumalizia miradi ya maji jaribu kuongea ndani ya Serikali na watu wa Nishati ili pale ambapo kisima kinaenda kuchimbwa nao umeme uende ili maji yanapopatikana maji yale yaweze kusambazwa kwa watu ili yaweze kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache ninashukuru ninaunga mkono hoja ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa leo nianze mchango wangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza miradi mikubwa iliyopo kwenye sekta ya nishati. Nikitaja michache ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - JNHPP MW 2115 ambao sasa upo 60%; Mradi wa Gesi Mtwara na Miradi ya REA Awamu ya tatu Mzunguko wa Pili ambao vijijini vyote nchini vitapata umeme, pia tunaenda kuanza umeme jazilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ikitekelezwa kikamilifu tutakuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji yetu ya sasa na kuwa na ziada itakayotusaidia kwenye uchumi wa viwanda. Utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ukikamilika utasaidia sana uchumi wa wananchi wetu kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali iharakishe utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta hii ya nishati ili kuchochea maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla. Kwa sasa mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili utekelezaji upo chini ya 20% na kwenye Jimbo langu la Hanang kati ya vijiji 42 hakuna hata kimoja ambacho umeme umewashwa na mkataba bado miezi sita tu. Wananchi wangu wa Hanang wanasubiri mradi huu kwa hamu kubwa, naomba Wizara iwabane wakandarasi ili utekelezaji ufanyike kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Hanang ni kati ya maeneo katika nchi hii ambapo umeme unakatika sana, kwa wastani tunapata umeme kwa 50% kwa sababu ya ukatikaji wa mara kwa mara. Niliiomba Wizara ya Nishati itusaidie kutatua kero hii kwa kujengwa kwa kituo cha kupooza umeme Hanang ili isaidie Wilaya yetu ya Hanang na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Byabato akijibu swali langu la msingi hapa Bungeni aliahidi kuwa kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 watatenga shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kujenga kituo cha kupooza umeme eneo la Mogitu-Hanang lakini kwenye bajeti hili halionekani. Naomba sana ahadi hii iliyotolewa hapa Bungeni itekelezwe ili isionekane Wanahanang wamedanganywa kupitia Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri toka amepewa jukumu la kuiongoza Wizara ya Ardhi, Wizara ya Ardhi imekuwa na utulivu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya nitaongelea mambo kama matatu kama muda utaniruhusu. La kwanza ni suala la upimaji wa ardhi ambao wenzangu pia wameongelea kwa kina kwenye eneo hili, hasa kwa maeneo yetu ya vijijini unakuta miji yetu inaanza kuwa vijiji baadaye inaanza kuwa miji na kwenye maeneo hayo unakuta watu wamepimiwa maeneo makubwa kiasi cha ekari moja. Wanapoanza sasa kwenye kuzipima, unaambiwa kwamba ikipimwa ekari moja kuwa eneo la makazi inakuwa ni ngumu, mpaka ugawe maeneo kadhaa ili viwanja viweze kutambulika kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba tu, wananchi hao wapewe elimu ya kutosha wakati wa upimaji huu ili waweze kuelewa na kweli wananchi wetu wa vijijini wana changamoto kubwa ya hofu ya Maafisa wanaotoka wilayani. Washirikishwe vizuri, waelezwe wanapata manufaa gani baada ya kufanya upimaji huo? Unaambiwa kwamba ukipima eneo moja, ni kiasi fulani cha fedha, lakini viwanja vile vinavyoongezeka gharama pia inaongezeka. Sasa wananchi wanapaswa kuelezwa kwamba gharama zile zinapoongezeka, wao wanapata manufaa gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine kwa sababu ya uhaba wa wataalam, Wizara imekuja na ubunifu ambao ni mzuri sana wa kushirikisha kampuni binafsi. Hizi kampuni binafsi zina mtazamo wa kunufaika. Sasa ukiangalia mahitaji ya wananchi wa vijijini; hawana fedha. Tuangalie namna ya kuwezesha ili hawa wananchi waweze kupimiwa ardhi yao bila gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyowahi kuchangia kwenye Bunge hili, eneo la ardhi tukipima ardhi yote kwa kasi, tunaweza kupata mapato kwenye eneo la ardhi. Ninaomba sana Wizara iwekeze kwenye eneo la kupeleka wataalamu wa kutosha wa ardhi kwenye wilaya zetu. Wapeleke pia na vifaa vya kutosha. Kuna changamoto kubwa ya kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu mkubwa wa wataalam hasa baada ya kuanzishwa kwenye Ofisi hizi za Kanda, Ofisi za Mikoa; za mikoa zimewezeshwa vizuri na kama Mheshimiwa Nape alivyosema, wilaya nazo ziwezeshwe ili ardhi iweze kupimwa. Hii itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara. Wataalam wapewe vifaa kwa sababu kwa sasa hivi vifaa viko mikoani. Ili tuweze kupata huduma, maana yake tuzunguke kwenye wilaya zote za mkoa, mpaka afanye booking sisi huku kuna migogoro vijiji na vijiji kwenda kuitatua, ni kalenda ndefu. Mtusaidie tupate vifaa vya kutosha vya upimaji wa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia eneo la Mabaraza ya Ardhi, wenzangu wameongelea sana, nami nikazie hapo. Kwenye Mabaraza ya Ardhi yale ya Kata, tujaribu kuona namna ya kuyaboresha, yana changamoto kubwa ya kiutendaji kwa sababu hayawezeshwi vizuri. Mabaraza haya pia wale wanaofanya maamuzi wanapaswa wapewe elimu nzuri ili angalau waamue kwa mujibu wa taratibu na sheria. Kwenye taratibu hizi za kuamua kesi kwenye Mabaraza ya Kata, linapofika suala la kwenda kutembelea eneo, hapo sasa zinaanza dalili ya kuanza kupata changamoto, kwa sababu unatakiwa kila upande uchangie kiasi ili waweze kufika kwenye site. Maana yake yule ambaye ana nguvu, ndiye atakayeangaliwa na yule ambaye hana uwezo, maana yake hataweza kuchangia hizo gharama za kwenda kwenye site. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili eneo tuliangalie vizuri namna ya kuratibu haya mabaraza kwa sababu wakiamua, ndiyo maamuzi yao; kama kuna rufaa, yanaenda kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Ukija kwenye Baraza la Ardhi, Mabaraza haya ya Wilaya ambayo yako chini ya Wizara yako Mheshimiwa Waziri, hapa tuna changamoto kubwa, Wabunge wengi wanalalamika kwenye maeneo yao, hakuna Mabaraza ya Ardhi. Mfano tu mimi Jimbo langu la Hanang; Wilaya ya Hanang hatuna Baraza la Ardhi, tunategemea Baraza la Ardhi la Babati, nalo kwa muda mrefu halina Mwenyekiti. Jinsi Wilaya ya Hanang ilivyo, kuna wananchi wanatoka kilometa zaidi ya 100 kufika tu Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Katesh Mjini ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, kilometa 70 mpaka Babati. Ukienda babati unakuta Mwenyekiti hayupo, wala udhuru huo haujatolewa kabla. Yawezekana ni siku ambapo kesi hiyo inatakiwa itolewe Ushahidi, anakuja na watu wanne au watano ambao ni mashahidi, kilometa zaidi ya 170. Gharama za kuwaleta hao watu, nauli tu ni zaidi ya shilingi 75,000/=. Anafika na watu hao anaambiwa kesi imeahirishwa kwa sababu Mwenyekiti hayupo. Baada ya hapo, itaahirishwa tena na wala hataambiwa kwamba Mwenyekiti atapatikana wakati gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni usumbufu mkubwa kwa wananchi, tuwe na Baraza la Ardhi la Wilaya ya Hanang. Tulishatoa majengo, tupate Mwenyekiti na lile baraza lianzishwe ili kuondoa kero ambayo tunaipata kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kidogo kwenye haya mashamba makubwa ambayo tumewapa wawekezaji. Sisi tuna mashamba tumempa mwekezaji ambayo zamani yalikuwa ya NAFCO, yalilimwa na tulikuwa tunapata ngano yakutosha. Baada ya kuwa yule mwekezaji wa awali amejitoa kwenye kilimo cha ngano, mashamba yale tukampa mwekezaji mpya. Ni zaidi ya miaka 12 sasa hivi hakuna chochote kinachoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameenda ameona na Wizara ya Kilimo imesema kwamba wameshajadiliana naye, wamekubaliana ndani ya mwaka mmoja, kama hatakuwa na chochote anachokifanya basi yale mashamba yaweze kutwaliwa, yarudi Serikalini na tuangalie namna ya kuwapatia watu wengine ambao watazalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati tutakapokuja atusaidie kwenye eneo hili. Imekuwa kwa mwaka huu amelima ekari 3,000 kati ya ekari ya 47,000. Sasa hii ni kama hujuma tu kwa sababu hatuzalishi, sisi Halmashauri hatupati chochote, wananchi wetu hawapati chochote. Tunaomba ukishaileta hili utusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ninaamini, Mheshimiwa Waziri atakuwa na majibu ya kina juu ya taabu hii wanayopata wananchi wangu kwenye eneo la Mabaraza la Ardhi. Kama sitapata ufafanuzi wa kina, nafakiri tumeshajaribu kuongea hili suala kwa sababu ni kero kubwa kwa wananchi wangu, nitamshikia shilingi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nitumie nafasi hii awali ya yote kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ya usikivu wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani bajeti hii kwa sehemu kubwa imechukua mawazo yetu sisi Wabunge wakati tunachangia Mpango wa Taifa wa 2021/2022 - 2025/2026. Yote ambayo yameletwa mbele yetu ni yale ambayo sisi tumeyaweka Mezani. Bajeti hii ni ya kwetu sisi Wabunge wa Bunge hili la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, mtani wangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu wake na wataalam wote kwa jinsi walivyochakata yale mawazo yetu tuliyoyaweka kitaalam na kuakisi mahitaji halisi ya Watanzania kwa wakati huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulilalamikia sana eneo la fedha ndogo inayopelekwa TARURA ili iweze kuhudumia barabara zetu za vijijini. Eneo hilo limeangaliwa vizuri sana. Tulikuwa tunalia vyanzo vingine vipatikane ili tupate fedha zaidi; hilo limeangaliwa, lakini zaidi sana tumepewa shilingi milioni 500 kwa kila jimbo. Huu ni usikivu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelia sana eneo la maji. Wakati wa kampeni sisi Hanang hatukuwa na ajenda nyingine; ajenda ya kwanza kwetu sisi ilikuwa maji, ya pili ilikuwa maji na ya tatu ilikuwa maji. Eneo hilo nalo limeangaliwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa tuna changamoto bado zipo, naamini nalo litakwenda kukamilishwa vizuri kwani wapo watu wataalam, wabunifu ambao wanaipenda kazi yao na wanaifanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la umeme; wakati tunajinadi ili tupate kura tulikuwa tunafanya reference ya jinsi umeme ulivyokwenda vijijini kupitia REA, lakini kabla ya bajeti ya Nishati kusomwa tulipewa jinsi wakandarasi watakavyokwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya REA kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwenye eneo hili, kwamba ni nyeti zaidi, bado kuna maeneo mengi hatuna umeme. Tunatarajia kukusanya fedha kwenye eneo la kodi za nyumba, kwenye LUKU na hasa kuwapelekea watu wengi zaidi, wapate umeme ili tupate kodi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ambao tumepelekewa wa nyumba 20 na kuendelea kwenye vijiji vyetu hautatusaidia sana kukusanya kodi za kutosha kwenye kodi za nyumba. Tupeleke umeme kwa watu wengi zaidi ili tupate kodi zaidi kwenye nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hilo pia nashauri sana tuwashirikishe na viongozi wa chini ili tuwaangalie watu tunaowachaji ni watu halisi ambao wanapaswa kulipa kodi. Inaweza ikatokea kwamba tunapeleka kodi kwenye nyumba na nyumba zina wapangaji. Nao ndio wameanza kulalamika kwenye mitandao ya kijamii, kwamba wao hawamiliki nyumba lakini wanapelekewa kodi. Eneo hilo tuwashirikishe viongozi wa chini kwa sababu Serikali ipo mpaka chini. Tuwatambue wale Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji, tuwatambue na wenzetu walioko kwenye Kata ili tuwashirikishe vizuri wanaofahamu maeneo hayo vizuri ili tukusanye kodi bila kuleta kelele kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanahanang ni wakulima na wafugaji. Naishukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita, eneo la kilimo imeliangalia vizuri sana. Sisi tunategemea kilimo cha ngano na kilimo cha alizeti; maeneo haya yote yameangaliwa vizuri. Naomba mwendo huo twende nao ili angalau wananchi wetu waendelee kunufaika, tupate manufaa kwenye kilimo tunachokilima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea sana wakati wa nyuma kuhusu mwekezaji ambaye tunaye kwenye shamba lile lililokuwa la NAFCO zamani, kwamba tupate mwekezaji ambaye yuko makini; naona juhudi zinaonekana, kazi zinafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mifugo wafugaji wanachohitaji, mifugo yao tuwasaidie kitaaluma. Tuboreshe mifugo, tujenge majosho na malambo, tupeleke chanjo na dawa za uhakika ili hatimaye waweze kufuga kisasa na tupate tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa mara nyingi sana; maeneo kwa sasa yamekuwa finyu, Serikali iache kufuga. Serikali iache kuchunga ng’ombe. Kazi ya kuchunga watuachie sisi ambao tuna uzoefu wa kuchunga. Yale maeneo, Ranchi za Serikali zile wapewe watu ambao wana asili ya ufugaji, watu wenye nia ya kufuga, ili tupate tija ya kutosha kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba niongelee kidogo eneo la utafiti. Mara zote tumekuwa tukisema kama hujafanya utafiti huna haki ya kusema. Sisi tuna mashirika yetu; TIRDO, TEMDO na CAMARTEC. Ili haya mashirika yaweze kutusaidia, Kamati imesema fedha ambazo wametengewa, bilioni 3.5, ni kidogo sana na ni kweli ni kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutawekeza kwenye utafiti maana yake tutategemea fedha za wafadhili na mfadhili akileta fedha zake maana yake atataka yale anayoyataka yeye ndiyo yasemwe. Serikali iamue sasa kuwekeza kwenye eneo la utafiti ili utafiti utakaofanyika uwe kwa manufaa yetu sisi na uweze kutusaidia katika kutatua changamoto tulizonazo sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na eneo la ardhi. Kwenye eneo la ardhi tumekuwa tukiongea suala la kupima ardhi yote ya Tanzania ili angalau tuweze kupata mapato kwenye ardhi, lakini unakuta kuna ardhi maeneo mengine tumeyapima tumemilikisha watu. Baada ya kumilikisha ardhi ile utakuta ina kodi zaidi ya miaka 10, 15 haijawahi kulipiwa. Ina malimbikizo kibao, mtu yule akitaka kuuza ardhi ile hawezi kuuza kwa sababu tayari ina madeni ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tuangalie eneo hilo; je, yale madeni ambayo tunayo katika ile ardhi tuyatafutie namna, ama kufuta yale madeni ili tuanze upya, tuwape watu wapya ambao wako serious na kuendeleza yale maeneo ambayo tumewapatia watu. Au vinginevyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako mzuri.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia, kwenye mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Awali ya yote niungane na wenzangu ambao wametangulia kwenye kumshukuru na kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa fedha ambazo ametupatia kwenye maeneo yetu hasa kwenye eneo la elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha vizuri Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2022/2023. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nakupongeza wewe na Mheshimiwa Spika kwa jinsi ambavyo mnatuongoza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wenzangu ambao nafanya nao kazi kwenye Wilaya yangu ya Hanang kwa ushirikiano ambao wananipatia. Ushirikiano wao ndiyo uliowezesha Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kuongoza Kitaifa kwenye makusanyo ya mapato. Hii imewezekana tu kwa sababu viongozi tumeshirikiana kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi, Waheshimiwa Madiwani na viongozi wengine, pamoja na watendaji wa Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Wana- Hanang kwa jinsi ambavyo wanatuwezesha sisi kutekeleza majukumu yetu vizuri, sana sana wanaotuunga mkono kwenye ukarabati wa Hospitali ya Wilaya Tumaini, ambako tuna bajeti ya zaidi ya shilingi milioni 200 na mpaka sasa karibu bajeti yote imepatikana ya kukarabati Hospitali ya Wilaya. Ninawashukuru sana kwa jinsi ambavyo wamejitoa, ninaamini Serikali itatuunga mkono; kuna upungufu wa majengo pale, tutapata yale majengo ambayo yanapungua ili angalau, huduma za afya ziweze kutolewa vizuri kwenye Hospitali yetu ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie kwenye Mpango huu. Tumesema mara nyingi kwamba kilimo ni uti wa mgongo na tumesema na hata kwenye Mpango imeandikwa kwamba, asilimia zaidi ya 66 ya wananchi, wanategemea ajira zao kwenye kilimo, lakini ukienda kwenye maeneo ya vijijini ni zaidi ya asilimia 90 watu wanategemea kilimo na ndio wengi wapo huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, bila kuwekeza kwenye kilimo hatutapiga hatua. Tumekuwa na dhana na matamko mbalimbali kwenye eneo la kilimo. Tumekuwa na Kilimo Kwanza na matamko mengine kama hayo. Sekta hiyo inaajiri watu wengi. Ukiangalia wananchi au vijana wengi, wanaokimbia vijijini kwenda mijini, ni kwa sababu kilimo hakina tija. Ili tupate tija kwenye kilimo, ni lazima tuweke fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tupate wataalam watakaosaidia wakulima wetu kulima kisasa ili tupate tija kwenye kilimo. Tupate wataalam wa mifugo ambao watasaidia wafugaji ili angalau ufugaji upate tija. Bila kuwekeza kwenye kilimo kimkakati, bila kukiangalia kilimo na tukawa tunaweka fedha kidogo kidogo, hatutakwenda kokote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mambo mengi tunayoyafanya, tutakuwa tunaangalia sehemu ambazo zinaajiri chini ya asilimia 30 ya Watanzania. Kilimo chetu kina changamoto nyingi; kilimo kinategemea mvua. Ni lazima tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tumeongea na tumeahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutatafuta mbegu, pembejeo, viuatilifu vya bei nafuu, lakini hali kwa sasa ni mbaya kwa wakulima wetu, lazima tuangalie eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunayo mashamba makubwa kwenye nchi yetu ambayo mengine tumeyabinafsisha. Tunayo sababu ya kuangalia ufanisi wa hayo mashamba ili hatimaye pia hayo mashamba ambayo tumewapa wawekezaji ambao inawezekana hawana nia au hawana uwezo wa kuwekeza; tufanye tathmini ya kina, mashamba yale ambayo tunaona hayana tija kabisa, tuyatwae ili kuyapangia matumizi mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tuwekeze kwenye suala la kufanya uchakataji wa mazao yanayozalishwa na wakulima wetu, ikiwepo kwenye upande wa kilimo na upande wa ufugaji ambako ndiko kuna wananchi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu Mpango ambao tunaenda nao, lazima tuangalie sana eneo la miundombinu ya barabara za vijijini, kwani kule wakulima wakilima, mazao yale lazima yasafirishwe na kuwe na usafiri wa uhakika. Kuna maeneo mengine kwenye nchi yetu na hasa Jimbo langu la Hanang, mvua zikinyesha safari ndiyo imeishia hapo. Hakuna kwenda kupata huduma za kiafya, hakuna shughuli za kimaendeleo inayoendelea, mazao ya kilimo hayasafirishwi na tunatakiwa lazima tuwekeze kwenye eneo hilo. Tuwekeze kwenye uchakataji ambao hatimaye pia tutaleta ajira za kutosha kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiboresha kilimo bila kuboresha miundombinu hakuna kitu chochote cha maana ambacho tutakifanya. Lazima tuhakikishe kwamba tunaboresha upande wa bandari, tuboreshe viwanja vyetu vya ndege. Kwa mfano, Mkoa mzima wa Manyara pamoja na ukubwa wake wote, hauna hata kiwanja kimoja cha ndege. Ipo kwenye Mpango muda mrefu; Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Manyara. Itakuwa rahisi watu kufanya shughuli zao kama kweli kuna usafiri wa ndege unaofikika kwa urahisi Mkoani Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna barabara yetu ambayo inaenda kwenye mashamba yenye uzalishaji mkubwa wa ngano. Barabara ya kutoka Mogitu kwenda Haydom, kule tunazalisha ngano ya kutosha; shayiri pamoja na ngano ya chakula. Ile barabara ikitengenezwa itawafungulia wananchi fursa kubwa sana ya kusafirisha mazao yao na kupata tija kwenye eneo la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 wakati tukiwa kwenye Mpango na kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alisema yale ambayo tunaweza kuzalisha ndani ya nchi, tuzalishe na tuondoe nakisi hasa kwenye ngano ya chakula lakini na mazao mengine ambayo tunaweza kuyazalisha nchini kwa wingi, tusiagize nje ya nchi. Kwa mantiki hiyo, uwekezaji ule ambao ulifanywa kwenye ngano ya chakula, shayiri mwaka 2020, bei ilikuwa ya uhakika na wananchi waliingia mikataba ya Kilimo cha Shayiri. Mwaka huu kidogo inasuasua. Wizara ya Kilimo iangalie eneo hili ili angalau wananchi wapate mikataba ya kulima shayiri na ngano ya chakula na uzalishaji uwe wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nipongeze kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye sekta ya elimu na afya. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametembelea Mkoa wetu wa Manyara hasa Wilaya yetu ya Hanang, amehimiza wananchi na wananchi wamechangamka, wameelewa Serikali yao inachapa kazi kweli kweli na kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo la usambazaji wa dawa ambayo inafanywa na MSD. Kweli kuna changamoto kubwa kwenye maeneo na vituo vyetu vya afya kuna uhaba mkubwa wa dawa. Ninachoshauri, Serikali iangalie namna ya muundo mzima wa MSD. Tukiiacha MSD kwenye utaratibu huu wa kawaida wakati, wengine mtu akiamka anaweza akanunua akapelekwa kwenye maduka, lakini MSD inapita kwenye mchakato wa manunuzi. Tuangalie namna muundo mwenyewe wa MSD ulivyokaa na namna ambavyo watatekeleza taratibu za manunuzi ya dawa kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ifanyike tathimini ya kina ya wadau wa MSD kwenye ule mnyororo wa usambazaji wa dawa. Ifanyike tathmini ya kina: Je, ni kweli kwamba wale wadau wote sio washindani wa MSD ambao wakati mwingine wako kwenye vituo vyetu na wao ni wafanyabiashara? Kwa sababu wanataka kufanya biashara, wanasababisha kwa makusudi dawa zisifike kwa wakati kwenye vituo ili zile dawa zilizoko kwenye maduka yao ziweze kuuzwa? Kwa hiyo, tathmini ya kina hiyo ifanyike ili tujue nani ambaye wakati mwingine anakwamisha dawa hizi kufika kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mamalaka ya Dawa na Vifaatiba; kwenye eneo la kufuatilia ufanisi na ubora wa vifaa vile vikubwa, hasa vinavyotumika kwenye uchunguzi na tiba; Serikali imewekeza sana faida nyingi kwenye eneo hilo. Hivyo vifaa vikinunuliwa tuvifuatilie ufanisi wake. Hata hivyo ili vifaa hivyo vifanye kazi vizuri, vinahitaji matangenezo kinga (prevent maintenance).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe kwamba tunawaajiri wataalam wa kutosha wa kufanya hiyo kazi ya matengenezo ya vifaa tiba, lakini tuhakikishe kwamba tunawashirikisha kwenye hatua za awali zile za kufanya manunuzi kwa maana ya kufanya uchaguzi wa teknolojia sahihi, lakini kufanya uchambuzi wa kina wa teknolojia wa vifaa tiba na hatimaye tuwashirikishe kwenye hatua ya uhamishaji wa teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwashirikishe vizuri hao wataalam. Sasa tunao wataalam wa kutosha wa vifaatiba, lakini Serikalini bado wataalam hao hawapo. Ninaishauri Serikali watoe ajira kwa wataalam kwa wataalam wa vifaa tiba. Tunavyo vifaa vingi kwenye sehemu zetu na vifaa vingi havifanyi kazi na sehemu kubwa ukiangalia, hatuna wataalam wa kuviangalia hivyo vifaa. Serikali iwekeze kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwekeze kwenye eneo la mafunzo ya wataalam wa vifaatiba. Walipo, ngazi ya mwisho ni Shahada. Tuwekeze kwenye Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu ili tafiti zifanyike hapa nchini tuanze kutengeneza vifaatiba vyetu wenyewe na hatimaye tuanze kujitegemea kama nchi badala ya kutegemea vifaa vingi tunavyoviagiza kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuongeza fedha kwenye Sekta ya Kilimo kutoka wastani wa bilioni 294 mwaka wa fedha 2021/20221 mpaka bilioni 1,248.96 mwaka wa fedha 2024/2025. Ongezeko hili ni kubwa na inaenda kuimarisha na kupata mafanikio kwenye maeneo yafuatayo:-
(i) Kuchangia kwenye pato la Taifa kwa zaidi ya 26.2% ya sasa;
(ii) Kuendelea kutoa ajira ya uhakika kwa Watanzania kwani Sekta ya Kilimo inaajiri zaidi ya 65.6% ya Watanzania;
(iii) Kuchangia zaidi ya 65% ya sasa ya malighafi ya viwandani ikiwepo eneo la vinywaji vinavyotengezwa kwa kutumia shairi; na
(iv) Kuzalisha ziada ya chakula ambayo tutauza nje ya nchi ili itupatie fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, fedha zilizoongezwa zitawezesha kilimo cha uhakika kwa umwagiliaji, nimshukuru sana Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kupokea na kufanyia kazi sehemu ya maombi yangu niliyowasilisha Wizarani kwa Skimu ya Umwagiliaji ya Endagaw kuendelea kuimarishwa, lakini kufanyika kwa usanifu wa Skimu ya Endasiwold ikiwepo kuchimbwa kwa visima maeneo ya Getasam, Balangdalalu, Laghanga na Qutesh.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iendelee kusimamia kilimo cha ngano na shayiri kwa kuhakikisha isitolewe kibali cha kuingiza nchini ngano na shayiri kabla ya kuhakikisha kuwa watumiaji wa ngano na shayiri wameshiriki kikamilifu katika hatua za kusaidia wazalishaji wa ngano na shayiri na kununua baada ya kuzalishwa. Haiingii akilini vitu ambavyo tunaweza kuzalisha hapa nchini tuendelee kuagiza toka nje ya nchi. Serikali ije na mkakati wa kina wa uzalishaji wa ngano na shayiri ili kupunguza utegemezi wa mazao haya nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, mbegu za shayiri ni kizungumkuti, mwaka huu mbegu walizopewa wakulima hazikuota na imekuwa kilio kikubwa kwa wakulima wangu wa Hanang. Jambo la mbegu ya shayiri nimeshaifikisha Wizarani, naomba ufuatiliaji wa kina ufanyike na wakulima walioathirika wafidiwe ipasavyo na kampuni iliyoleta mbegu ambazo hazina kiwango.
Mheshimiwa Spika, naomba kumkumbusha Waziri kuhusu ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Gidahababieg, Skimu ya Umwagiliaji Bwawa la Bassotughang na kuona namna ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji Ziwa Bassotu.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote mimi nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tarehe 23 alitutembelea sisi Wana-Hanang’ na alikuwa kwetu mpaka tarehe 26 akijaribu kuhamasisha maendeleo ndani ya Mkoa wa Manyara. Akiwa kule alileta salamu za Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdori Mpango. Hakuja hivi hivi, alikuja kueleza zile neema ambazo zimekuja kwenye mkoa wetu na kwenye Wilaya yetu, ya madarasa kwenye shule shikizi pamoja na shule za sekondari, kwenye sekta ya afya pamoja na sekta ya maji.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alipokuwa Hanang’ aliwaahidi Wana-Hanang’ mambo kadhaa. Ninachoomba tu mimi nilivyosimama hapa salamu zile za shukurani za Wana-Hanang’ lakini kukumbusha tuu mambo machache kati ya yale ambayo Wanahanang walimuomba.
Mheshimiwa Spika, Hanang’ ni Wilaya kongwe; Mji wa Katesh ni Mji wa muda mrefu lakini changamoto kubwa ni ya maji. Tunashukuru tangu tumeanza na watu wa BAWASA wanafanya kazi nzuri sana; kabla tulikuwa tulikuwa na KAWASA. Hata hivyo wanayo changamoto, fedha za mabomba zilizoahidiwa hazijafika; bado fedha za kutekeleza ule mradi hazijafika. Tunaomba sana hizo fedha zitolewe kwa wakati ili Mji wa Katesh uweze kupata maji ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Maji wa Gehandu ulioahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni. Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan alisema kwamba yeye akisema inatekelezwa na kweli imetekelezwa. Mkataba wa bilioni 2.8 umeshasainiwa. Tunachoomba; mwaka huu maji ni changamoto kubwa, mvua ni chache wananchi wa Gehandu wako milimani. Ili wapate nafuu huu mradi uliosainiwa wakandarasi waende kwenye site kwa wakati ili waweze kuwasaidia wananchi hao wasipate changamoto kubwa ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna mradi mkubwa wa maji kutoka katika Ziwa Basutu. Kwenye eneo hili, niwapongeze na kuwashukuru sana wadau wa maendeleo wa Water Aids walitoa milioni 500. Serikali kupitia fedha hizi tulizozikopa kupitia World Bank milioni 550 zimeenda pale, lakini kabla zilienda milioni 70; ni mradi wa bilioni 12 kwa vijiji zaidi ya 9. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali yangu iuangalie mradi huu kwa jicho la kipekee. Lakini na hao wadau wanaotusaidia waweke nguvu zaidi ili tuhakikishe kwamba wananchi wale ambao bado hawajafikiwa wawe wamefikiwa.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mji wa Katesh wakati ule wa kampeni tuliwaahidi kilometa 10 za lami. Nilimuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alivyokuja kwenye jimbo letu, kwamba, kwenye bajeti hii tunayoenda 2022/2023 atupe angalau, au atupiganie kupata kilomita nne za lami ili tupunguze ile 10 aliyoahidi mama tukiwa tunaelekea kwenye 25 wakati wa kuomba kura, Wanahanang tumewaahidi lami kidogo kidogo kwa kipindi kirefu. Tukiwapa nne halafu tukaanza kidogo kidogo, kama tukienda na mbili mbili tutakuwa tumeenda zaidi. Ukifikia asilimia 70 utakuwa umefaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachoomba sana, kwenye eneo hili ni kwamba, tupate hizo kilometa nne kwenye bajeti hii ya 2022/2023 ili tuendelee na hizi ahadi ambazo zimetolewa tangu mwaka 2010 ili zianze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna barabara yetu ya Katesh - Masutu - Haydom. Ukifika Mlima Chavda pale changarawe ile inatereza, tunamwaga ngano nyingi sana pale. Tusaidiwe kwenye eneo hilo, barabara ile iwekwe lami, ni kilometa 70 tu.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana Mheshimiwa Flatei alitaka kupiga sarakasi kwenye eneo hili. Ninaomba tusifike kwenye hatua ya kupiga sarakasi, kazi hii ifanyike kwa sababu ni ahadi ambayo imetolewa wakati wa uchaguzi na tumeihaidi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna barabara ya Nangwa – Gisambalang – Kondoa. Kwa sasa barabara ile imekatika kabisa, mvua ikishanyesha haipitiki kabisa. Hakuna shughuli inayoendelea kwenye kata zaidi ya sita. Barabara hiyo ndiyo inayounganisha Wilaya ya Hanang na Wilaya ya Kondoa. Tunazo Kata za Gisambalang, Dirma, Simbay, Sirop, Kata ya Wareta pamoja na Kata yenyewe ya Nangwa. Kote huko wananchi wangeweza kupita katikati tu hapo ambapo ni kilomita kama 50, lakini wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 200 kufanya shughuli zao za kiuchumi. Tunaomba Serikali itusaidie kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, katika barabara hiyo daraja limeondolewa na mafuriko ya mvua ya 2019/2020. Tuliamini lingekuwa ni suala la dharura, lakini mpaka sasa Daraja la Munguri B halijatengenezwa. Ukitaka kupita pale mvua ikinyesha uombe Mungu upite. Tumekuwa tukipata changamoto kubwa kwaajili ya eneo hilo, tunaomba tupate usaidizi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nisemee kidogo uchumi wa Wilaya ya Hanang’. Sisi tunategemea kilimo na ufugaji. Kwenye eneo la mifugo kwa kipindi kirefu tulikuwa na malambo ambayo yamejengwa kwa ajili ya kusaidia kunyweshea mifugo, ikiwa ni pamoja na changamoto nyingine ya malisho. Malambo yale yaliyojengwa mengi ni ya muda mrefu, yamechakaa, ni ya tangu mwaka 1980. Serikali iangalie namna ya kukarabati na kujenga.
Mheshimiwa Spika, tunalo Lambo la Gidahababieg ambalo Serikali kwa kipindi kirefu imeahidi kwamba lile lambo litaboreshwa kwa sababu mkondo ule una maji mengi. Kwamba watajenga bwawa kubwa ambalo pamoja na mifugo kupata maji, vilevile litasaidia wananchi kufanya umwagiliaji. Tunachoomba kwenye eneo hilo Serikali sasa itupie jicho la ziada.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotoba yake, ukurasa wa 24, amesisitiza sana suala la kilimo. Kwamba kilimo chetu ili kiende tunahitaji mbolea, mbegu za kisasa pamoja na viuatilifu. Ninachoomba kwenye eneo hili, tuwasaidie wananchi wa Hanang’.
Mheshimiwa Spika, kwenye hotoba ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge hili la 12 alisema tuna nakisi ya tani laki nane mpaka milioni moja za ngano; na Hanang’ ilikuwa maarufu sana kwenye kilimo cha ngano. Tuliangalie eneo hili ili tuboreshe kilimo cha ngano, tuache kuagiza ngano kutoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na mashamba yale ya NAFCO. Mashamba yale mpaka sasa kwenye yale maeneo ambayo yamemilikishwa kwa wananchi, wakulima wakilima wanapata kati ya gunia nane mpaka 12. Sasa, tunazo ekali zaidi ya 42,000 tumemmilikisha mwekezaji. Mwekezaji huyu yeye akijitahidi sana yeye anapata kati ya gunia tano mpaka sita. Mwekezaji huyo, si wananchi wa kawaida ambao hawatumii mbolea, wananchi wa kawaida ambao wanalima kwa njia za kawaida za asili. Sasa naomba tufanye tathmini ya kina kwenye eneo hilo. Je, mwekezaji huyu bado tunahitaji kuwa naye?
Mheshimiwa Spika, kwa hekari 43,000, kwa hesabu za kawaida ambazo mimi nimezifanya, yeye akilima kwa namna ambayo analima kwa sasa, tunapata kati ya gunia 219,800 mpaka 263,000. Lakini wangepewa wananchi wa kawaida wa Hanang’ wangeweza kuzalisha kati ya 351,000 mpaka 439,000, wananchi wa kawaida ambao hawatumii mbolea, ambao wanatumia kilimo chao cha asili. Ukienda kwenye vyama vya ushirika ambao wanapata misaada mbalimbali kutoka maeneo kadhaa ikiwepo benki yetu ya kilimo wanaweza kuzalisha kati ya gunia 527,000 mpaka 659,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kazi ya kufanya kwenye eneo hilo. Ninachoomba ndugu zetu wa Wizara ya Kilimo, hao wenzetu ambao wamepewa haya mashamba, wapewe shamba moja tu kati ya mashamba yale ambayo wamepewa, yale mengine wapewe wananchi hao wa kawaida ili waweze kulima kwa namna ambavyo wanaona au vinginevyo wapewe vyama vya ushirika ili tuzalishe kwa tija na ili waweze kusaidia Wilaya ya Hanang’ kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushuruku sana. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wetu wa Taifa wa Mwaka 2023/2024. Kwenye wasilisho ambalo Mheshimiwa Waziri amelifanya ameainisha sekta ambazo zinafanya vizuri. Kati ya sekta tano ambazo zinafanya kazi vizuri ameongelea suala la Sekta za Maji, Fedha na Bima, Uchimbaji wa Madini na Mawe na Sekta ya Huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye sekta zetu za msingi za uzalishaji hapa hazipo. Ukigusa kwenye upande ambao unatusumbua kwenye suala la mfumuko wa bei inayoongoza ni sehemu ya vyakula na viinywaji, ni asilimia 7.8. inamaanisha nini? Vyakula hivi vingi tunaweza kulima wenyewe. Kwa mwaka uliopita haukuwa mzuri kwa sababu tunategemea mvua za Mwenyezi Mungu. Mheshimiwa Kwagirwa aliongelea kidogo suala la kujaribu kwenda kupunguza tension ya gharama za maisha ya wananchi wetu huko vijijini kwa vyakula ambavyo viko kwenye maghala yetu ili vipelekwe kwa wananchi ili kupunguza mfumuko wa bei kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza ni muhimu sana kwa sababu kama mfumuko ni mkubwa kiasi hiki inaathiri uchumi wetu, Serikali ichukue hatua sasa bila kuchelewa. Kilimo kinachangia asilimia 26 kwenye pato la Taifa, lakini imeajiri zaidi ya Watanzania asilimia 65, ni watu wengi. Ili tuweze kulikwamua Taifa hili lazima eneo hilo tuliangalie kwa umakini mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka Shilingi bilioni 954. Naamini kwamba changamoto hii ya ukuaji wa uchumi na intervention hii itakayofanyika katika kilimo itaenda kutusaidia. Tunamwamini Mheshimiwa Bashe kwa umahiri wake na hatua anazozichukua. Kwa sasa tunaenda kwenye msimu wa kilimo, wakulima wengi wanalia kwenye suala la pembejeo, masuala ya mbegu bora, naomba eneo hili tulisimamie vizuri. Wale wataalam wetu wa kilimo watoke maofisini sasa waende wakakae na wakulima kuona namna ya kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa tuliyonayo ni mbegu, natoa mfano kwetu Hanang tunaotegemea sana kilimo cha shayiri na ngano, mpaka sasa haujawekwa utaratibu mzuri wa kupata mbegu bora ya ngano. Hata hivyo, mara nyingi kila msimu unapoanza tunahangaika sana na mbegu ya shayiri ambayo mara nyingi wakulima wetu wamekuwa wakiingia mikataba na makampuni yanayozalisha vinywaji aina ya bia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo hili lisimamiwe vizuri. Fedha zilizowekwa huku ni nyingi hizi fedha zilete tija kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo ili wakulima waweze kuzalisha ni muhimu sana kuwawezesha wakulima kwa mitaji. Benki yetu ya kilimo iweze kuwakopesha wakulima. Kwa sasa wanatoa mikopo lakini masharti bado ni magumu sana. Tumeanzisha Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), nyingi ambazo zimeanzishwa lakini wakitaka kuanzisha mikataba ili waweze kukopa kwenye hizi benki bado kuna kitu wanaita mkataba wa utatu. Lazima kuwe na mkataba baina ya benki, wakulima wenyewe kupitia AMCOS zao na wale ambao watakuja kununua bidhaa hizo baada ya kuzalishwa. Serikali itengeneze mfumo wa hizi AMCOS zetu kuaminika bila kuhitaji nani atanunua bidhaa baada ya hapo, vinginevyo isaidie wakulima hawa kupata masoko ya mazao watakayozalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie eneo la mifugo. Wafugaji kwenye nchi yetu wengi wamekuwa kama wakimbizi, kila sehemu wanawindwa, kila sehemu kuna mwingiliano baina ya wakulima na wafugaji na kila sehemu wanawindwa. Katika kila sehemu wameonekana kama ni watu wakorofi, mtu yeyote bila kumpa elimu iliyostahiki ama kumtengea nafasi stahiki kwenye jamii lazima ataonekana mkorofi kwa sababu ataitafuta nafasi yake kwa namna anavyoona yeye. Ni muhimu sana kwa nchi hii, kuwatengenezea wafugaji utaratibu mahususi ili wafuge na hatimaye tuwape elimu waweze ku-transform mifugo yao kuwa ya kisasa na hatimaye wafuge ufugaji wenye tija kwao…
MHE. ZUBEIRI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ZUBEIRI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nathamini sana mchango wa mchangiaji anayechangia, amegusa sehemu anasema kwamba wafugaji kwenye nchi hii wanaonekana ni wakorofi, lakini sio tu kwamba wanaonekana ni wakorofi, nature ya wafugaji ni wakorofi na wao kuua kwao ni jambo la kawaida.
MWENYEKITI: Hiyo sio taarifa. Endelea na mchango wako. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba niendelee. Nilichokuwa namaanisha wafugaji lazima tuwatengee eneo lao na tutengeneze mazingira, tuna mifugo mingi nchi hii, tuone namna gani inaweza kutuletea tija. Haileti maana yoyote, tuna ng’ombe wengi, mbuzi wengi, kondoo na kuku wengi, lakini bado tuagize nyama kutoka nje. Tuwajengee uwezo tutengeneze namna ya kuchakata mazao yanayotokana na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la ardhi; kilimo na mifugo yote inahitaji ardhi. Nimesema kabla kwenye Bunge hili kwamba ni muhimu ardhi yetu tuipange vizuri ili kila mtu aweze kupata sehemu ambako ataendeshea shughuli zake. Tupate ardhi kwa ajili ya kilimo, mifugo na shughuli nyingine ikiwemo viwanda. Ni muhimu sana kuipanga ardhi yetu vizuri na tutaondoa mwingiliano na migogoro mingine ambayo inajitiokeza kati ya wakulima na wafugaji na jamii nyingine. Tukiipanga ardhi yetu vizuri, tunaweza tukawa kwenye baadhi ya vijiji tukatengeneza ranches ndogondogo sio lazima tuwe na ranches kubwa ili tuweze kuwaweka wakulima wetu vizuri na hatimaye tuwaweke wafugaji vizuri ili shughuli zao ziweze kuleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ardhi tukiitumia vizuri kwenye jamii yetu, mwenye ardhi anamkodisha asiye na ardhi ili alime, mwenye ardhi anamkodisha mfugaji ili aweze kulisha mifugo yake lakini pia kuna ile biashara ya kuuziana viwanja na kuuziana mashamba. Tukiirasimisha ardhi yetu yote, kwenye eneo hilo Serikali inaweza kutengeneza mapato. Tukiihusisha hata Serikali yetu mpaka hata ngazi ya kijiji, zile shughuli zinazofanyika kule tukaona namna ambavyo tunaweza kupata mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana ardhi tukiipanga na kuitumia vizuri italeta tija kubwa kwenye shughuli zetu za ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, niombe kwenye eneo hili kuna ardhi ambayo tayari imeshapangwa, ardhi ambayo imelekezwa kwa ajili ya ranches kwa ajili ya mifugo, vilevile mashamba makubwa ambayo yapo kwa ajili ya kilimo. Maeneo hayo yatumike kimkakati ili yaweze kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa ardhi ambayo iko ndani ya Jimbo langu la Hanang. Ardhi hii tuliwapa wawekezaji zaidi ya ekari 43,000, zaidi ya miaka
18 hatuoni tija sisi kama Wanahanang na Watanzania hawaoni tija yoyote.
Mheshimiwa Spika, maeneo kama haya nchi hii ni mengi, ninachoomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo nimekuwa nikiongea na wewe mara kwa mara nakushukuru kwa ushirikiano unaonipa. Ninachoomba zile kazi ambazo umeshaanza ya kutwaa ardhi ile ambayo haitumiki, kamilisha Ndugu yangu ili Wananchi wa Hanang’ waweze kufaidi ardhi ambayo iko kwenye maeneo yao, lakini ifanywe kwa nchi nzima ili ardhi zetu zilizolala ziweze kutumika kwa ajili ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kwenye upande wa utekelezaji wa miradi, ukuaji wetu wa uchumi inanyoongoza ni sekta ya maji lakini tunayo miradi mingi ya maji. Nashukuru sana Mheshimiwa Rais ametenga fedha kwenye eneo hilo, lakini kuna ucheleweshaji mkubwa wa utekelezaji wa miradi. Ukichelewesha mradi maana yake huduma zile ziliozotarajiwa zinachelewa, maendeleo yaliyotarajiwa kwa wananchi yanachelewa na inawezekana hiyo kazi tumewapa Wakandarasi tukiamini kwamba hiyo kazi wataifanya vizuri, tunaomba eneo hilo lisimamiwe kwa ukaribu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia naunga mkono hoja za Kamati zetu zote mbili za Kudumu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wenzangu wameongea sana suala la upungufu hasa wa walimu na jinsi unavyoathiri ufaulu wa watoto wetu, lakini changamoto hiyo pia ipo kwenye sekta ya afya. Kwamba, tunao upungufu mkubwa kiasi kwamba, huduma zinazotolewa zinaathirika kwa sababu ya upungufu wa watumishi, lakini haya mimi nilitaka tu ni high light.
Mheshimiwa Spika, nitaongea zaidi suala la usimamizi wa rasilimali chache tulizonazo. Una Mwalimu anakaa karibu kilometa 40 kutoka Halmashauri, hapo nimechukua wastani wa kawaida. Anazo stahiki zake ambazo hazina uhakika kila siku anarudi Halmashauri, hivyo hafanyi kazi iliyokusudiwa ya kufundisha wanafunzi. Watumishi wa afya vivyo hivyo, ana stahiki zake Halmashauri atarudi kila siku.
Mheshimiwa Spika, natoa mfano, kwenye suala la kuwapandisha watumishi vyeo. Unaweza ukakuta kwamba, aidha Halmashauri ina watumishi 700 nafasi zinatolewa 400, unampa mtihani Afisa Utumishi je, atachaguaje hao 300 kati ya 700 ambao wote wanastahili? Sasa unakuta kila mtu anafanya lobbying badala ya watu kufanya kazi muda wote wanashinda Halmashauri ili angalao waweze kuangaliwa. Maeneo hayo yapangwe vizuri kwenye suala la kuwasimamia watumishi. Kama Halmashauri ina watumishi 700 ikiwezekana twende kwa phases, Halmashauri ngapi zinapandisha watumishi ili wawe comfortable wafanye kazi.
Mheshimiwa Spika, Serikalini kumekuwa na kuongea suala la kuweza kusawazisha watumishi, kuweka usawa. Kwamba, kuna maeneo mengine watumishi wamekuwa wengi kuliko maeneo mengine, lakini tumeongea sana suala la kuboresha mazingira au wale wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu wapewe posho maalum, badala ya kuhangaika kuangalia sehemu gani kuna watumishi wengi, sehemu gani hakuna watumishi wengi, maeneo ambayo yana hali ngumu wapewe posho maalum ya mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, wanaokaa mijini wanayo maji, wanao umeme, usafiri siyo mgumu sana. Wanaokaa vijijini wanakaa maeneo ambako hakuna umeme, hakuna maji, akitaka kusafiri ni changamoto kubwa, hao wapewe vivutio mahsusi ili waweze kufanya kazi kwa utulivu kwenye maeneo hayo. Ukifanya hivyo wale wa mijini wakiona kuna usawa wa huduma kati ya mijini na wa vijijini hawataona taabu kwa sababu wanapata zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri iliyofanyika kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu, ujenzi wa miundombinu ya afya, lakini ninaomba kwenye kupanga miundombinu hii si lazima kila sehemu tupeleke kituo cha afya kilichokamilika, tunaweza tukaangalia yale mahitaji ya msingi. Mheshimiwa Kakunda ameongea kidogo vitu ambavyo vinahitajika, zipo Kata nchi hii ambazo zimepata zahanati zile za mwanzo, tunaweza tukachagua tukajenga OPD nzuri ikawa na vyumba vile vyote vinavyohitajika, tukaweka huduma ya mama na mtoto wakati huo tukiendelea kutanua kila Kata ipate kituo cha afya. Tunaweza tukajenga kwa awamu wakati huo tukijielekeza kwamba, maeneo mengi yapate hizo huduma kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ule mtazamo wa Serikali wa kwamba, Makao Makuu ya Tarafa lazima kuwe na kituo cha afya cha kisasa, safi kabisa, ili angalao yale ambayo tunayatengeneza kwenye Kata yaweze kupata rufaa na huduma zilizokamilika kwenye ngazi ya Tarafa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninasema hivi, unaweza kukuta kata ambayo kituo cha afya au zahanati imejengwa sasa hivi na ile ambayo ilikuwa nayo kabla tofauti ni kubwa sana. Suala la ramani ameshaliongea Mheshimiwa Kakunda, kwamba ramani tulizokuwa nazo mwanzo na zilizopo sasa ni tofauti kabisa. Zile za zamani hazikidhi, hivyo maeneo yale yakaangaliwe.
Mheshimiwa Spika, tumeongea sana masuala ya udhibiti wa vifaa tiba, dawa chakula na vipodozi. Kwenye chakula kuna vitu vinaitwa, bidhaa ambayo ni dawa au chakula, kwenye vipodozi kuna vipodozi vidogo dawa au Kipodozi tunaita bodyline products zinakosa udhibiti makini kwa sababu zinadhibitiwa na taasisi mbili tofauti. Naomba bidhaa hizi, bidhaa za chakula vipodozi ambavyo vilikuwa vinadhibitiwa na TFDA ambayo kwa sasa tunasema Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba; bidhaa hizi zote zidhibitiwe na taasisi moja ili kuhakikisha zile border line products zinasimamiwa vizuri ili kulinda Afya ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana kwa sababu kwa sasa bidhaa zinazodhibitiwa na TBS, kuna changamoto ya utaalam, lakini wanasimamia bidhaa nyingi hivyo hawatoi umuhimu mkubwa kwenye upande wa chakula na vipodozi.
Mheshimiwa Spika, niseme kidogo kuhusu suala la vipaumbele vya namna ya kuamua mradi gani utekelezwe sehemu gani. Sasa hivi kumekuwa na utamaduni kwamba Wizarani wanasema kuna fedha either ya kujenga shule, ya kujenga Zahanati au ya kujenga jengo la utawala ilhali kwenye maeneo halisia unakuta mahitaji ya Wananchi ni Shule, Mahitaji ya wananchi ni ukarabati wa shule. Ninachoomba ile mipango inavyopangwa ianzie kule chini kwenye ngazi ya vijiji ili kujua mahitaji halisi ya chini. Badala ya tunasema tuna fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya utawala, tunafedha kwa ajili ya kujenga zahanati. Tuangalie mahitaji halisi ya maeneo yetu. Kuna shule imechakaa tujielekeze kwenye kukarabati shule, nyumba za walimu hazipo tujielekeze kujenga nyumba za walimu.
Mheshimiwa Spika, lakini tunachangamoto kubwa sana; tumejenga shule za kata nyingi lakini umbali ni mkubwa kutoka wanako kaa watu. Ili kufika shuleni kwenda na kurudi unatembea zaidi ya Kilometa 40. Sasa tuone namna ya kujielekeza kujenga mabweni kwa ajili ya watoto wetu ili wawe salama na waweze kusoma vizuri. Unakuta wanachoka kabla ya kufika shuleni hawana namna ya kujifunza kwa utulivu, tuwekeze kwenye eneo hilo. Inawezekana fedha ni nyingi lakini tuwashirikishe wadau wa elimu ili kuhakikisha tunatatua changamoto hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mwenyekiti kwa kunipa nafasi. Mimi nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya lakini hasa kwa kuangalia maslahi ya watumishi na kwa kumteuwa Mheshimiwa Waziri kwenye nafasi ya kuwaangalia watumishi wa nchi hii. Watanzania wana imani naye watumishi wana imani naye na uthibitisho ni jinsi alivyopigiwa makofi hapa ndani wakati anaenda kusoma hotuba yake ya bajeti jana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwapongeze na wasaidizi wake Naibu Waziri, na watumishi wengine wizarani kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Vilevile tuipongeze sana Serikali yetu kwa kutoa ajira ya watumishi 32,000, hii itapunguza upungufu wa watumishi kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Tabasamu aliongelea kidogo jambo la mazingira magumu ya watumishi kwenye baadhi ya maeneo yetu. Tuna maeneo nchi hii ukimpeleka mtumishi hakuna nyumba hata za kupanga, acha zile ambazo zimejengwa kwa ajili ya watumishi. Ninachoiomba Serikali yangu maeneo kama hayo watumishi hawa wapewe posho ya mazingira magumu ili watumishi waweze kubaki kwenye maeneo hayo ili wawe tofauti na wale ambao wako mijin. Wakipewa fedha kwa kuangalia mazingira magumu wanayoishi watumishi hawa watabaki kwenye mazingira hayo. Kuwe na tofauti kati ya wanaokaa mjini na wale ambao wanaenda kwenye mazingira ambako hata nyumba za kupanga hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utumishi wa umma kumekuwa na changamoto mtumishi anapoenda kusoma. Kwanza Serikali haisomeshi watumishi wengi kwa sababu ya kibajeti, lakini watumishi hawa wanajilipia ada wenyewe hakisharudi kwenye eneo lake la kazi ile elimu yake aliyopata kutambuliwa kwa wakati inachukuwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wengine utakuta mtu ana nafasi, either Mkuu wa Idara au yawezekana ni Mwalimu Mkuu, akirudi kazini nafasi yake hiyo imeshachukuliwa na mtu mwingine, yeye atakaa benchi na wala hakuna consideration kwamba huyu amesoma. Ile elimu aliyopata badala ya kuhitumia ana kaa miaka mitatu yuko bench au yuko frustrated. Hatutumii watumishi wetu vizuri. Kwahiyo naomba eneo hili tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa sana suala la mafunzo kazini. Kumekuwa na utamaduni tu kwamba walioko ngazi za juu kila siku wanatoa maelekezo. Sasa badala ya kuwa tuwe na utaratibu wakutoa tu maelekezo hasa sekta ya elimu tuwe na utaratibu wa kukaa na hao watumishi kufanya mafunzo kazini ya namna ya kuboresha utendaji wao. Si lazima mafunzo hayo yawe ya gharama kubwa lakini yakatengenezwa mfumo wa angalau hata kwenye ngazi ya kata kila mwaka wanakuwa na mafunzo ya namna gani wanaweza wakaboresha utendaji wao wa kazi ili kuwapa motisha watumishi hao, kwamba wao wanafanya kazi lakini tunawaangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu watumishi wetu wanaoelekea kustaaafu. Unakuta mtumishi amepandishwa daraja lakini mshahara wake haanzi kulipwa kwa wakati, ule ambao ni wa daraja husika. Mtumishi huyo anastaafu tofauti ile haijawahi kulipwa, anaanza kudai sasa mafao yake na anakuta mafao hayo yamepunjwa sana. Mtumishi huyo atahangaika atazunguka kote ili kupata haki yake, nah apo inakuwa ni usumbufu mkubwa na sisi Wabunge tunapata changamoto kubwa sana kwenye eneo hilo. Naomba tuangalie na tutengeneze mifumo ambayo inawezesha kujua kwamba mtumishi huyu baada ya muda fulani atastaafu na hivyo taratibu zake zote ziandaliwe ili anapostaafu mishahara yake yote iwe imekuwa sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na changamoto ya kuwalipa mafao yao kwa wakati. Mtu amezoea kupokea mshahara labda tuseme laki tano kwa mwezi, anastaafu halafu anakuta mwezi wa kwanza hamna kitu, wa pili hamna kitu na hata mwezi wa tatu hamna kitu. Tunawatesha watumishi wetu wanaostaafu. Na hata malipo yale ya kila mwezi baada ya kustaafu hayaanzi kwa wakati. Kwa hiyo hili eneo tuliangalie kwa umakini mkubwa kwasababu tunawatesa watumishi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao watumishi ambao wamestaafu siku za nyuma, posho wanazolipwa au mafao yao ni madogo mno na kazi walizofanya ni sawasawa na watumishi ambao wanastaafu siku za hivi karibuni. Tuwaangalie, kwasababu fedha tunazowapa haziwasaidii kitu chochote kwa hali ya maisha iliyopo sasa. Wale wastaafu wetu ambao wamestaafu siku za nyuma tuwaangalie namna ya kuwaboreshea mafao yao ili nao waweze kuishi kama watu waliotumikia nchi yao kwa uhaminifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na suala hili la uhakiki wa wastaafu. Uhakiki huu utakuwa unafanyika mara nyingi Makoa Makuu ya Mkoa ambako ni mbali. Mtu kwenda kuhakikiwa anaingia gharama kubwa ilhali malipo yenyewe anayolipwa ni kidogo. Kwa namna hii tunawatesa wastaafu wetu, wengine wameshaanza kuwa wazee. Sasa, tuwasaidie kwenye kuwahakiki maeneo karibu na wanakoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi baada ya kusema hayo niendelee kupongeza, watumishi wa Tanzania wanayo matumaini makubwa, na mimi ninaamini Waziri wakati wa Mei Mosi watumishi watacheka ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na pongezi kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Architect Omari Juma Kipanga Naibu Waziri; Katibu Mkuu Ndugu yangu Profesa Eliamani Sedoyeka, Naibu Katibu Mkuu wa Sayansi Ndugu yangu James Mdoe, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika masuala ya elimu mwanamama Profesa Carolyne Nombo na wataalam wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hawa nawapongeza si kwa sababu tu nawapongeza, kwa sababu baada ya Mheshimiwa Rais kutoa tamko kwamba sasa tupitie sera, mitaala kwa sasa wanachakalika wanapambana usiku na mchana kuhakikisha kwamba wanapitia sera yetu ya elimu. Wanapitia mitaala yetu ya elimu ili kuisogeza karibu na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya elimu yetu kutokugusa maisha ya wananchi wa kawaida. Profesa Mashimba wameisema hii kwa kipindi kirefu sana. Kwa hiyo, mtoto akitolewa nyumba akipelekwa kwenye mfumo elimu anarudi ile asilia yake imeondoka lakini wameanza kuifanyia kazi kwa kasi kubwa, nawapongeza sana kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe angalizo kwenye hatua hii ya mapitio ya sera na mitaala ambayo tunaifanya kwa sasa. Nimemsikia mara kadhaa Profesa Mkenda akisema mapito ya sera, mitaala ya elimu ni kazi ambayo imeanza kufanywa na dunia nzima, sisi tulianza mapema. Tunaomba sana tusiburuzwe na dunia sisi tulioanza mapema ile nia yetu ya awali ibaki pale pale ili tufikie elimu yetu iguse mazingira ya kwetu. Tupate elimu inayotatua changamoto tulizonazo kwenye mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yote ambayo yanafanyika dunia sasa ni Kijiji hatuyakatai lakini sisi tusimezwe na changamoto zile ambazo zipo duniani. Tuhakikishe tunatatua changamoto zetu kwanza, tunaboresha elimu yetu, tunahakikisha kwamba tunasogeza elimu tunayoitoa kwa wananchi wetu ili ukimfundisha mtu darasani akienda kwenye mazingira ya kawaida ya kuishi aweze kuitumia elimu ambayo ameipata ili iweze kumsaidia kwenye mazingira anayotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na utaratibu wa kutathmini ufaulu wetu kwa kuangalia yeyote aliyefaulu lakini ukiangalia wanaopata Daraja la Nne, wengi mno kwa nchi hii hasa kwa sasa ambao tunatoka vijijini. Vijana wale wamesoma Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne ukilinganisha na wale ambao hata darasa la kwanza hawajaingia shughuli wanazozifanya zinafanana. Tuangalie elimu tunayotoa, itoe tofauti ya yule aliyekwenda shule na ambaye hajaenda shule ili wale waliokwenda shule wakatoe shule kwa wale ambao hawajaenda shule! Wao wawe kielelezo cha wale ambao hawajapata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaoishi na hao vijana, wanaofuga vijana ambao wamemaliza kidato cha nne na wale ambao hawajaingia hata darasa la kwanza mazingira ni hayo hayo, wanaolima vivyo hivyo, elimu yetu lazima itoe tofauti kati ya watu ambao wamekwenda shule na wawaelimishe wale ambao hawajapata bahati hiyo kwa sababu nafasi siyo nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine tuliyonayo, waliomaliza Kidato cha Nne wamepata Daraja la Nne kwenda Sifuri, zaidi ya asilimia 65 mpaka asilimia 70, kwa sisi vijijini inaweza kuwa 75 mpaka 80! Hao tunawaacha tunawasahau historia yao inafutika baada ya kuwa wamefeli elimu ya sekondari. Kwenye imani zetu zote binadamu akiishi, ikifika siku ya kufa tunaamini kwamba baada ya muda fulani kuna jambo fulani zuri linafuata kwa Mwenyezi Mungu, ambaye hajafanya vizuri either anakwenda Jehanamu. Sisi tukimaliza tu Kidato cha Nne tumefunga hapo, tutengeneze uratatibu wa kusaidia hao vijana ili waje wasaidie Taifa lao. Tutengeneze Vyuo vya Ufundi ambavyo vitawapa ujuzi hao vijana waweze kutoa mchango stahiki kwa Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara Ndugu yangu Sedoyeka wakati Mheshimiwa Rais akiwa Mgeni Rasmi pale Arusha. Kwamba tutatanua Vyuo vya Ufundi mpaka kwenye ngazi angalau ya Tarafa. Mimi hivi ninavyoongea Jimbo la Hanang’ halina hata Chuo cha Ufundi – VETA. Tuweke nguvu kubwa kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimefanya kazi mbalimbali wachina ukiuliza tu taarifa zao mtu mwenye cheti tu ana ujuzi wa kufanya mambo mbalimbali, nchi yetu tuwekeze huko kwenye elimu ya kati! tuweka nguvu kubwa huko. Lakini tuunganishe elimu yetu na mazingira yetu ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri ulikuja mwaka 2020 Disemba pale Hanang’, wakati tukitaka kuboresha kilimo cha ngano, tukakuomba sana wakati huo ukiwa Waziri wa Kilimo, sasa Waziri wa Elimu. Kwamba ule uzalishaji wa Ngano Kituo cha Umahiri kiwe Hanang. Tuunganishe sekta zetu za uzalishaji, kilimo, ufugaji, uvuvi na elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kile Kituo cha Umahiri tukipata Chuo Kikuu kitaendesha Kituo cha Umahiri Hanang’, tukafufua kilimo cha Ngano, tunachangamoto kubwa ya mbegu ya ngano na mbegu za mazao mbalimbali, itatusaidia sana. Tuunganishe elimu yetu na kazi tunazofanya za kilimo, ufugaji na uvuvi na mambo mengine mbalimbali ambayo tunafanya biashara ili elimu itusaidie kututoa sisi kwenye changamoto tulizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo suala la angalau hamasa kwa wale wanaotoa elimu. Upande wa elimu ya msingi imesemwa sana na Profesa Kitila Mkumbo. Elimu ya Sekondari ameisema lakini tukija kwenye upande wa Vyuo Vikuu ninachoomba kila mtu anayefanya vizuri tutambue mchango wake sawa sawa! Kama mtu ameleta jawabu la changamoto either ya kudhibiti upotevu wa maji tuutambue huo mchango. Maprofesa wetu wale Wahadhiri wetu wanaofundisha vyuoni tuwatengenezee utaratibu wa kutambua mchango wanaoutoa kwenye jamii yetu kwa kutatua changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo sawa hata kidogo kama nimeitwa Profesa basi, haki ninazopata na Profesa yoyote ni sawa, kama mimi nimechangia zaidi utambuzi huo ufanyike. Kama mtu ameleta jawabu la suluhu ya kisiasa, kiuchumi na mambo ya kisaikolojia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie sekta hii muhimu ya mifugo na nianze kwanza kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano ambao walikuwa wametupa kwenye Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwa sababu ni Mjumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wenzangu kusema kwamba sekta ya mifugo na uvuvi ni sekta muhimu ya uzalishaji kwenye nchi yetu. Na wenzangu pia wamesema Waziri anapaswa kuonesha wivu na suala la mifugo kama Mawaziri wengine wanavyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalisema hili, mifugo imekuwa ikikamatwa hovyo na wafugaji kutozwa gharama kubwa ambayo wakati mwingine wengine wamefilisiwa. Wengi wamekuwa wakizunguka kwenye corridors za Wizara kwa sababu mifugo wao wametaifishwa, lakini hali ya wafugaji nchi hii ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wamelazimika kuhama sehemu moja kwenda nyingine sababu kubwa ni uhaba wa malisho na maji. Na wanapohama tunawashangaa kwa nini wanahama, lakini nikwambie tu Mheshimiwa Waziri, kwa sisi wafugaji unaporudi nyumbani jioni ng’ombe hawajashiba ni sawasawa na mama ambaye watoto wake wana njaa, wewe hupati usingizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo lazima lichukuliwe kwa uzito mpana kwamba suala la malisho kwa mifugo nchi hii ni suala kubwa na lazima tufanye kazi ya ziada. Nimekusikia ukisema kwamba utahakikisha ranchi zote zitatumika kutengeneza malisho kwa mifugo yetu. Lakini sioni kama kuna muujiza utakaotokea Mheshimiwa Waziri, fedha zilizoongezwa kwenye bajeti hii tunayokwenda kuipitisha ni fedha kidogo mno. Hata utekelezaji wa bajeti ya 2023/2024 fedha zilizotolewa ni kidogo mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiiangalia sekta ya Kilimo, Fungu 99, iko kwenye asilimia kama 49 tu. Na ninaomba nitaje vitu vichache ambavyo vimetekelezwa. Vitu hivi hata kama vikitekelezwa kwenye Jimbo la Hanang pekee hakutaleta mabadiliko yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilivyotekelezwa; ujenzi wa Bwawa la Kimambi lita milioni 95; ujenzi wa Bwawa la Matekwe, lita milioni 102 – na bahati nzuri hili bwawa mimi nimelitembelea na Kamati. Ni bwawa dogo ambalo hata kuhudumia kijiji kimoja cha wafugaji hakitoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekarabati Bwawa pale Mwanga, Itigi lita milioni 54; kisima kirefu kimoja na mabwawa mengine 11. Kwa mwendo huu wa kibajeti na fedha hazitoki zote, kwa hakika kazi inayofanyika ni ndogo sana, haitawasaidia wafugaji wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye Wilaya yangu ya Hanang, kwanza nishukuru tumepata mbegu 8,000 za kuhimirisha mifugo yetu ili tuweze kuiboresha; mpaka sasa tumeweza kuchukua tu mbegu 300. Changamoto kubwa ni sehemu ya kutunzia mbegu hizo ili ziwafikie wafugaji, haipo. Vifaa vilivyopo ni vidogo havitoshelezi hata kidogo; lakini kwa sababu hizi zinaenda kwa wafugaji ambao hiyo taaluma hawajaelimishwa vya kutosha, wanachajiwa shilingi 25,000. Elfu ishirini na tano ni sawa sawa na bei ya mbuzi, kwamba hii ni kumpandisha ng’ombe uuze mbuzi. Kwa wafugaji hii ni gharama kubwa na haiwezekani, kwa sababu hawana elimu hiyo. La muhimu kwanza Serikali iwezeshe mifugo yao ihimirishwe bure ili wengine wakajifunze kule, wakijifunza baadae watakuwa tayari kugharamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa watumishi, tunao watumishi wachache. Wilaya ya Hanang’ yenye kata 33, vijiji 96 tuna watumishi 17 tu na tuna pikipiki mbili tu. Sasa ni namna gani utawafikia wafugaji? Mheshimiwa Waziri lazima achukue hatua ya ziada kuwakaribia wafugaji. Wafugaji wanahangaika sana. Wafugaji wetu wanapaswa kuelimishwa, watu wanaacha ufugaji sasa hivi wengi wanakimbilia kwenye upande wa kilimo, kwa sababu ukienda kwenye kilimo unajua kabisa kwenye hekari moja ukilima unapata magunia mangapi utafaidika kiasi gani, kwenye mifugo hamuwaelezi mambo hayo. Wafugaji wangu wa Gehandu, Mureru na Mulbadaw, wanataka elimu hiyo iwasogelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuwa Naibu Waziri muda mrefu kwenye Wizara hiyo hajatembelea Jimbo la Hanang. Hakuna Waziri aliyekuja jimbo la Hanang’ akaongea na wale wafugaji wakapata ile elimu inayotakiwa. Ninaomba eneo hilo muwakaribie wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nigusie kidogo eneo la uvuvi. Sisi tunategemea ziwa Bassotu kwa ajili ya Uvuvi. Ziwa lile limeanza kujaa mchanga, sasa waangalie namna ya kulikarabati. Zaidi ya hapo kuna mwalo pale Mulbadaw tumeomba muda mrefu lile mwalo lifunguliwe wananchi waweze kufanya shughuri za uvuvi. Ninaomba wakati anasimama hapa awaelekeze watu wake ndani ya Wilaya kwa sababu nimeona wakiyumba yumba bila kufanya kazi hiyo. Wananchi wanasubiri wakafanye kazi maandalizi ya awali yameshafanyika, ule mwalo ukafunguliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna bwawa la Gidahababieg, tathmini imefanyika mara nyingi. Ungana na watu wa idara ya maji, watu wa kilimo pale tujenge bwawa ambalo litawasaidia watu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji lakini litasaidia kwa ajili ya kunyweshea mifugo; na pia pale tunaweza kupata mboga ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama muda wangu unaanza kukimbia. Sekta ya mifugo; Jimbo la Hanang ni jimbo la wafugaji, Hanang wanahitaji kusogelewa. Tunaomba tuone miguu yenu ndani ya Jimbo la Hanang’; hakuna chochote cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanyika kwenye Jimbo la Hanang’ ili wafugaji wangu wale waone Serikali iko nao na inafanya kazi ya kuwahudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kukupongeza wewe kwa jinsi ambavyo unatuongoza vizuri siku ya leo pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri Mavunde, Katibu Mkuu Gerald na watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo tumewapa watu makini ambao tunaamini watatuvusha kwa rasilimali ambayo kwa kweli Mama amewapatia. Changamoto kubwa kwenye upande wa kilimo ni suala la kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu, Waziri kwenye hotuba yake ametueleza vizuri jinsi alivyoweka mkakati mzuri wa kutengeneza maeneo ya umwagiliaji. Mimi niombe tu kwenye eneo hili Jimbo langu la Hanang’ kuna maeneo mengi ambayo tukiweka skimu za umwagiliaji na Hanang’ ardhi yake ina rutuba ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bonde la Duru iko Kata ya Masakta ina maji mengi sana, yale maji hayatumiki weka skimu pale. Tuna Bwawa la Gidahabaiek ambayo inakusanya maji yote ya Mlima Hanang. Wizara ya Maji wamefanya tathmini na usanifu wa kina tayari, shirikiana nao weka skimu ya umwagiliaji eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bonde la Getasam Kata ya Masqaroda eneo zuri sana na ardhi pale ina rutuba sana. Tuna eneo tunaliita Endasak Matindigani skimu inafaa. Tuna Bonde la Nyamura ambako vijiji vitatu vingeweza kunufaika tukiwekeza hapo. Kijiji cha Basutuqang, Hidek na Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Balang’dalalu na Gidabanja pale mpakani maji ni mengi sana, tukiweka skimu pale itasaidia vijiji hivyo viwili. Tuna Bwawa la Endesh litaisaidia Kata nzima ya Ishponga. Tuna ziwa kubwa Ziwa Basutu. Wananchi wanalitumia kwenye kilimo cha umwagiliaji, wakati mwingine wanagombana na Serikali kwa sababu wao wanafanya kienyeji wanahitaji kusaidiwa tutengenenze mfumo wa umwagiliaji wa kisasa ili wale wakulima wa eneo la Basutu waweze kutengeneza tija na hiyo itawezesha wakulima wa Wilaya ya Hanang’ kuzalisha kwa mwaka mara mbili au mara tatu na kwa sababu ardhi ile ina rutuba ya kutosha na tukaboresha eneo la usimamizi tutapata mavuno ya kutosha. Ninaamini umelipokea Mheshimiwa Waziri wewe ni msikivu tunashirikiana vizuri, naamini kwenye eneo hilo hutaniangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye tija. Hatuna muujiza wowote ili tuendeleze kilimo bila kuwekeza kwenye sayansi. Eneo hili lazima tuweke fedha za kutosha kwenye eneo la utafiti. Utafiti wa mbegu, mbolea na viuatilifu ambavyo vinaendana na mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri miaka ya nyuma wakati tunakua unachukua tu mbegu ghalani unaenda kupanda na unavuna. Sasa hivi mbegu tulizonazo ukishatumia mwaka mmoja, mwaka mwingine hamna. Tuna mbegu zetu za asili, tumieni sayansi pale tuone namna ya kuboresha badala ya kwamba tunatengeneza biashara za watu kwenye mbegu, tuone namna ambavyo tunaweza kuwapunguzia wakulima wetu gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kakunda ameongea hapa, mfuko mmoja wa kilo mbili shilingi 12,000 wakati ukivuna tu sisi mahindi hayana bei. Kwa hiyo, eneo hilo tuliangalie kwa makini tufanye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikukumbushe Mheshimiwa Waziri mwaka 2020 Desemba wewe na timu nzima ya Wizara ya Kilimo mlikuja Hanang’. Tulitembea kwenye mashamba ya ngano na hii ilikuwa inaenda kutibu hotuba aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge la 12 kwamba tuna nakisi ya ngano ya karibu tani milioni moja. Hanang’ kihistoria ni wazalishaji wakubwa wa ngano. Nimepitia kwenye hotuba yako ukurasa wa 90 umeelezea masuala ya uzalishaji wa ngano. Mwaka 2017/2018 tani 57,000 lakini mwaka 2021/2022 tani 62,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mashamba makubwa Hanang naomba weka jicho kule, yale mashamba hayatumiki vizuri. Tunalo shamba la Basutu plantation ambalo linasimamiwa na Halmashauri, lile shamba wanakodishwa wananchi fedha zile zinakusanywa na Halmashauri inaisaidia sana halmashauri lakini lile shamba limerudiswa kwako, utakapolipokea naomba usitafute wawekezaji wa nje, Hanang ni wakulima wazuri, kilimo ndiyo maisha yetu. Badala ya kutafuta watu waje wawekeze halafu baadaye uzalishaji uwe hafifu kama sasa hivi wawekezaji tulionao. Nikupe tu taarifa, wawekezaji ambao tunao sasa hivi, wanazalisha wastani wa 0.3 to 0.5 tons kwa eka moja. Wakulima wangu wa kawaida wanazalisha 1.2 mpaka 1.5 kwa eka moja. Sasa utahangaika kutafuta wawekezaji wa nini? Watanzania wapo tayari kufanya kazi. Tuwasaidie wale ambao tayari wanafanya kazi yao, tusije tukaleta watu ambao watakuja kutukwamisha kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu niseme tukiwapa Watanzania hawa wa kawaida ile ardhi ya mashamba makubwa ya sasa hivi, karibu ekari 66,000 tukazalisha kwa wastani wa 1.5 ton, tutapata kwa mwaka mmoja metric ton 99,000. Hiyo ni Hanang’ tu na hayo mashamba makubwa. Nikwambie tu kwa sasa hali ilivyo siyo nzuri, mapori ni mengi. Uliniahidi hapa Bungeni kwamba utatwaa ekari 30,000 tuwarudishie wakulima wazuri wa Hanang’ ili waweze kuzalisha kwa tija. Ninaomba hiyo kazi uifanye wale jamaa zako wanakuja kwako wanakupa na maneno mazuri, hakuna chochote kinachofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyoongea kuna zaidi ya ekari 20,000 ni pori, wananchi wangu wanakodi mashamba. Heka moja kwa wastani wa shilingi 200,000. Mfano mzuri tunalo shamba la Halmashauri ambalo mwananchi amelikodi, eka moja shilingi 165,000 lakini kuna mashamba mabingwa tu wa kuweka mipaka lakini hawalimi. Ninaomba angalia eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna ardhi wananchi wanataka kuzalisha lakini kuna mtu ameshikilia ameweka vigingi kila siku ni kukamata mifugo ya wananchi, ukiigusa tu kidogo anaenda anaharibu mazao yako, sasa tumeleta wawekezaji ili walinde ardhi yetu? Hatuwezi kulinda sisi wenyewe? Tafuta watu ambao watawekeza na Wanahanang’ wako tayari wanataka ardhi ya kulima. Hatuna ardhi ya kulima utusaidie kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie Mheshimiwa Waziri mimi nakuamini sana unafanya kazi nzuri angalia maeneo hayo niliyoyataja. Baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Itifaki hii ya biashara ya huduma ya SADC. Kabla ya kuanza mchango wangu, niungane na baadhi ya Wabunge ambao wamepongeza Wabunge wenzetu ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais kwa nafasi mbalimbali ili kumsaidia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na timu yake nzima akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri ya kuwaunganisha wafanyabiashara wetu. Nimeona mara nyingi akikutana na wafanyabiashara ili kuwaonesha fursa zilizopo na namna ambavyo wanaweza kushirikiana na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmoja kati ya ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais ni aliyekuwa Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile. Ninampongeza sana kwa sababu Mheshimiwa Rais amemuamini. Mwenyekiti wewe ni shahidi, Makamu Mwenyekiti alipowasilisha wasilisho na maoni ya Kamati aliwasilisha vizuri sana na mimi nachukua nafasi hii kumpongeza, ametuwakilisha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nachangia maeneo machache. Itifaki hii ikiridhiwa, soko la huduma litaongezeka kutoka hii ya kwetu ya shilingi milioni 61 kwenda shillingi milioni 360. Hili ni ongezeko kubwa na nasema tu kama Mheshimiwa Shangazi alivyotangulia kusema, sisi kwenye Kamati, tumeichakata, tumeangalia na tumeona kwamba kwa kweli ni fursa ambayo tumechelewa kuichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Tanzania siyo wadhaifu tunapongia kwenye mjumuiko huu wa soko letu kutanuka. Mheshimiwa Shangazi amejaribu kueleza fursa ambayo tunayo na GDP yetu ni kubwa kwa maana ya watu ambao tunaweza kuwa na mashaka nao labda ni Afrika Kusini. Pia ukiangalia kwenye sekta ya huduma naona tupo nafasi nzuri zaidi. Nawashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba hii Itifaki tuiridhie na muhimu sana tujiandae vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya sekta ambayo tunaiangalia ni sekta ya ujenzi. Kwenye sekta hii ya ujenzi fursa zilizopo ndani ya nchi bado tunazitoa kwa wageni. Fursa itaongezeka maana yake yawezekana sisi Watanzania tusinufaike sana. Naiomba Serikali kwenye eneo hili tujaribu kuangalia namna ambavyo tunaweza kuwawezesha wataalam wetu wa ujenzi, makampuni ya ujenzi ili tuweze kupata fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo kwa watu wetu ni mitaji. Kingine ambacho kipo ni namna ambavyo makampuni ya kizawa yanahudumiwa ukilinganisha na wageni. Ukiangalia kwenye tendering process watu wetu wataambiwa kwamba wafanye kazi wa-rise certificate ndiyo wanapata malipo, wakati mwingine malipo hayaendi kwa wakati, kwa mantiki hiyo tuna-drain uchumi wao na tunawachelewesha watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitanua soko hili tuweze kunufaika, lazima tutengeneze mechanism ya kuwasaidia Watanzania kwanza kukamata soko hili la ndani pia kukamata soko hili tunalolitanua la nchi za Kusini mwa Afrika – SADC. Ukienda kwenye benki zetu, mtu ana mkataba wa kufanya kazi hata na Serikali ya Tanzania, mlolongo ni mrefu sana, utaratibu wa kupata mkopo ni mgumu, namna ya kuwawezesha lazima itafutwe ambayo ni rahisi ili hili soko tunalolitanua tunufaike nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye sekta ya fedha kutafuta mikopo, ajenda ya kwanza watakwambia kwamba watakuwa na valuer wao kama wewe una mali ambazo hazihamishiki, wa benki yenyewe. Valuers ninavyohamu huwa wanasajiliwa, valuer ambaye utapewa na benki atafanya assessment ya collateral, baada ya kufanya assessment atakuja na maneno mengi, mtaenda back and forth isiyopungua miezi minne mpaka na kuendelea. Tukienda na mwendo huu kwenye soko hili ambalo tunafungua, pamoja na strengths tulizonazo, hatutawasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kazi yako ni kushamirisha biashara. Kazi kubwa uliyonayo mbele yako ni kukamata hili soko la watu miliono 360, ili tuweze kunufaika kwenye eneo hilo, kaa na Waziri wa Fedha ili kwenye sekta hii ya fedha, vikwazo ambavyo wanapata Watanzania viweze kuondolewa ili tuweze kunufaika na isije ikaonekana kwamba tumepata fursa lakini bado hatuna nafasi ya kuikamata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye eneo la taarifa na Watanzania kujua fursa zilizopo. Kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri lazima ufanye kazi ya ziada, tembea na Watanzania, itazame Tanzania, angalia hali zao, kama unavyokuwa na mahitaji muhimu kwenye pochi yako, panga na hitaji la Watanzania, Serikali imuwezeshe Waziri wa Viwanda na Biashara kuwa na fedha za kufanya hamasa kwa Watanzania, kuwa na namna ya kuyafikia hayo masoko, kufanya maonesho maeneo mbalimbali kwa yale mazuri sisi tuliyonayo ili hatimaye hili soko tuweze kuliteka. Ni fursa kwetu, lazima tuchangamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda na utendaji ule wa kawaida wa Kiserikali, haitatusaidia na tutakwama. Fursa iliyojitokeza lazima tuikamate, ni kweli tumechelewa. Ninachoomba tu, Serikali kwa maana hasa Wizara ya Viwanda na Biashara, jitoe kwenye ule mfumo wa kawaida wa urasimu wa Kiserikaliserikali. Jiweke kama wewe ni sehemu ya sekta binafsi, tembea na sekta binafsi kila sehemu ili hatimaye Watanzania tuweze kunufaika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kwa sasa ukiangalia malalamiko mengi ambayo watu wetu wanayo si makubwa kwenye soko hili la Afrika Mashariki. Moja limeshasemwa kwamba kwenye mipaka ile zile blocks za kuwazuia watu, mfano madereva wa trucks, malalamiko yalikuwa ni mengi. Ninaamini kwa Itifaki hii tukishairidhia, yale malalamiko yote yataondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati tumeona eneo hilo la sera zetu, sheria zetu, kanuni zetu za biashara lazima ziweze kufungua fursa tukimbie, tusitanguliwe na wenzetu. Lingine, kwa sababu Bunge hili ni chombo cha wananchi, niwaombe Watanzania wenzangu hii ni fursa tukimbizane nayo, tuwahi, tukichelewa tutakuta mwana si wa kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunapaswa tulirekebishe kabla hatujaenda mbali sana ni eneo la kodi. Kwa mfano, kwenye malori kwa sababu eneo la usafirishaji ni sehemu ya huduma, sisi Watanzania, mtu akishakuwa na lori mbili anaanza kulipia VAT, gharama zipo nyingi na kila lori ina EFD machine. Sasa tuangalie kama hizi changamoto ambazo tunazo na watu wa malori mara nyingi wamekuwa wakilalamika. Kama kwetu ipo, je, kwa wenzetu ipo hivyohivyo? Kwa sasa ukitembea barabarani utaona lori nyingi sana ambazo zimesajiliwa nchi jirani ndiyo zinazosafirisha mizigo kutoka bandarini kwetu zinaenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, hii changamoto, na wapo Watanzania ambao wameshasajili. Mtu ana lori kumi, lazima atafute jina la mtoto wake, ana Watoto wangapi, akasajili kwa marafiki ili angalau kuweza kumudu gharama. Wanalalamika sana gharama za uendeshaji, kodi ni kubwa. Tuangalie hizi changamoto na maeneo mengine, tukiweza kuyatibu na tukachangamkia, ninaamini fursa hii ni nzuri na itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, niliona nichangie eneo hilo. Nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsnate sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongzea sana Mheshimiwa Waziri wazo lake la kufanya wiki ya nishati hapa Dodoma imetusaidia sana sisi Wabunge. Badala ya kutafuta wa wilaya, mkoa na ngazi ya Taifa wote tunawapata kwa pamoja, kweli wameturahisishia huduma na suluhu zingine tumekuwa tukizipata hapa hapa. nimpongeze sana kwa ubunifu huo, ni vitu vya kuigwa na kuendelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa inafanyika kwenye sekta ya nishati, na naamini kwamba miradi hii ikikamilika kwa wakati, na Mheshimiwa Waziri amechambua vizuri, kwamba tutaongeza upatikanaji wa umeme mpaka kufikia megawatt 5,213.22 na tutakuwa tunaanza kuuza umeme mpaka nje ya nchi. Ninaomba, kwa sababu lengo hili limewekwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024, naomba kasi hii iongezeke ili tupate umeme wa uhakika kwani umeme ndio unaowezesha viwanda kuendelea na Tanzania viwanda haviwezekani bila kuwa na umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipindi kirefu tumekuwa na changamoto mmesikia wenzangu wakisema umeme unakatika. Jimbo la Hanang’ changamoto hiyo ipo, umeme unakatika na haijulikani wakati gani kuna umeme na shughuli zinalala. Sisi ni wakulima, sisi ni wafugaji; kuchakata mazao hayo ya mifugo, mazao yanayotoka mashambani inakuwa ni changamoto kubwa kwa sababu umeme unakatika sana. Tulikuwa tumesahau kipindi cha hapo katikati masuala ya kuhangaika na generator lakini sasa hivi wimbo umekuwa ni huo. Naomba uchukue hatua. Na pale ulitupa kituo cha kupooza umeme ili angalau kupunguza ile line kwa sababu line ikiwa ndefu nayo inachangia umeme kukatika. Pale Mogitu watu wako wamekwisha tembeatembea naomba zoezi lile la kujenga kituo cha kupooza umeme liharakishe.
Mheshimiwa Spika, wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan, anashika nchi vijiji vyangu vyenye umeme vilikuwa 54 tu, kwa sasa viko 73. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo inafanyika ya kuwapatia wananchi umeme. Hata hivyo, bado tuna vijiji 23 naomba mkandarasi ambae yuko site msukume aongeze kasi mradi ule uweze kukamilika na wananchi wapate umeme. Lakini kuna maneo mengine ambapo umeme umegusa tu kama Kijiji cha Getasam nyumba tatu tu ndizo zina umeme. Watu wako waangalie eneo hilo ili utusaidie watu wapate umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna maeneo ambayo yamepata umeme tangu miaka ya 90, watu wameongezeka sana kwenye maeneo hayo. Kata kama ya Gitting maeneo yake mengi yalipata umeme zamani. Sasa hivi tunapeleka umeme kwenye vijiji vipya ambavyo havina umeme lakini wale wa zamani kasi ya TANESCO ni ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, ukienda Nangwa maeneo mengi watu wengi wengi hawana umeme, ukienda Gendabi maeneo ambayo umeme ulipatikana zamani watu wengi hawana umeme, maeneo ya Jorodom maeneo hayo yaangaliwe kwa jicho la kipekee ili watu wapate umeme.
Mheshimiwa Spika, umeme ukifika kwenye eneo unachangamsjha maendeleo na watu wanajenga zaidi. Wakijenga TANESCO waongeze kasi ya kupeleka umeme kwa wananchi. Lakini, kuna changamoto pia, sijui ni TANESCO au wakandarasi wenu ambao mmewathibitisha; wanawambia wananchi wafunge umeme. Kwa mfano Kijiji changu cha Dirma Kata ya Bassotu wananchi asilimia kubwa wamefanya wiring miaka mitatu mpaka sasa umeme umeme haujaenda. Sasa mnapohmasisha wananchi wafanye wiring iende sambamba na miradi ya upelekaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya ya jimboni kwangu; kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri kuhusu matumizi ya gesi; ni kama matumizi ya mpito, na ikifika 50/50 kwa ule mpango wa kutumia clean energy gesi nayo itakuwa phased out. Mmefanya negotiation ya gesi asili imechukua muda mrefu sana. Ongeza kasi kwenye eneo hilo ili gesi hii ya kwetu tuweze kuitumia na tunufaike nayo. Imechukua muda mrefu mnajadiliana mjadala huo haufiki mwisho. Simamia, na tunakuamini; wewe nguvu yako ni kubwa na ubunifu tumeuona weka kasi hapo ili hatimaye tuweze kutumia gesi yetu ya asili iweze kunufaisha taifa letu isije ikawa kama makaa ya mawe, ambako dunia sasa inaacha matumizi ya makaa ya mawe na sisi hata hatujawahi kuyatumia. Hivyo, isije ikatokea kwenye gesi pia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa Bungeni tumejadili sana masuala ya udhibiti vinasaba kwenye mafuta. Huko nyuma kulikuwa na kelele nyingi sana, imeenda TBS sasa hivi kumetulia. Maneno yameanza kuwa mengi kwamba sasa TBS waondolewe kwenye eneo la usimamizi wa vinasaba kwa ajili ya kuhakikisha ubora wa mafuta yetu. nikushauri tu kwamba, jambo lililotulia tusiliamshe tusiingie kwenye migogoro ambayo haina tija. Mamalaka ya TBS ni msimamizi wa ubora kwa bidhaa nyingi kazi kubwa anafanya, maabara zake ni nzuri tuendelee kuwaamini.
Mheshimiwa Spika, nigusie kidogo eneo la Shirika letu la TANESCO. Mheshimiwa Waziri, tupia jicho kule kidogo. Shirika hili lina mkataba wa hali bora ya wafanyakazi na chama cha wafanyakazi; lakini kuna harakati mbalimbali zinazofanyika katika kuboresha shirika. Ni jambo jema kwa sababu ili shirika lolote liweze kuwa na ufanisi ni lazima lijitazame. Hata hivyo, majukumu yote yanayofanyika kila mmoja anataka kujua kesho yake iliyo wazi. Hata wewe Mheshimiwa Waziri unapanga mipango yako na upanga vitu ambavyo vitakutengenezea njia ya kazi. Na watumishi nao wanataka kufahamu haki yao na majukumu yao wanayoyafanya na wajibu wao wanaoutekeleza lakini haki ziwe wazi, kama kuna mabadiliko yoyote washirikishwe ili hatimaye nao wajipange kwa sababu ni watu wana mipango yao, badala ya kuwa na harakati ambazo zinafanyika ambazo haziko wazi kwa chama cha wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, nikuombe tu, baada ya kusema haya ambayo nimesema, Jimbo langu la Hanang’ ni kati ya majimbo makubwa; tuna vijiji 96 na vitongoji 414. Wakati unapopanga mipango yako ya kazi majimbo haya makubwa uyaangalie kwa macho ya kipekee ili hatimaye maendeleo yaweze Kwenda sambamba katika nchi yetu. Uki-concentrate, na kwa mfano suala hili upande TARURA nilishaongelea, kwamba tunagawa rasilimali kijimbo au kiwilaya maeneo mengine ni makubwa na mengine ni madogo. Maeneo haya makubwa yaangaliwe ikiwezekana twende kwa idadi ya watu au kwa hali ya jiografia ya maeneo yanayohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadya ya kusema haya nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mimi nianze kutambua kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikipiga kelele sana Daraja la Munguri B, leo kwenye bajeti nimeona imetengwa shilingi milioni 600 na mwaka jana ilitengewa fedha za kufanya usanifu wa kina. Ninachoomba tu kwenye eneo hilo kwa sababu daraja hilo linategemewa na wananchi wetu wengi kabla mvua hazijanyesha daraja hilo lijengwe ili wananchi wetu sasa waanze kufanya biashara bila usumbufu, kwani wananchi wa Kondoa na wananchi wa Hanang tuna muingiliano mkubwa sana wa kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa kawaida wananchi wetu wakienda kwenye mnada wa Mbicha, mnada wa Mitiyangi, wanalala kulekule mvua zikinyesha. Ninachoomba sana kabla mvua hazijanyesha daraja hilo liwe limejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru kwamba kwenye barabara ya Katesh – Hydom ambayo iko kwenye Ilani, barabara hii iliahidiwa toka mwaka 2010, leo nimeona shilingi milioni 280 imewekwa hapo, ila ni ya muda mrefu, shilingi milioni 280 imewekwa kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina. Tumezoea hapa kwamba, usanifu wa kina unaweza ukafanyika wakati huo huo unajenga. Barabara hiyo inategemewa na wananchi wa Hanang katika usafirishaji wa mazao mbalimbali kama ngano; Hanang imechaguliwa kuwa kitovu cha uzalishaji wa ngano, mashamba mengi yako ukanda wa juu yanategemea barabara hii, wananchi wa Basutu, wanaozunguka Ziwa Basutu, wanalima sana vitunguu. Vitunguu hivi vinasafirishwa maeneo mbalimbali mpaka nje ya nchi, wanaitegemea hii barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mlima Chavda, kila siku mizigo inamwagwa pale, nguvu ya mwananchi amehangaika shambani kwa shida, sehemu kubwa inaangukia pale Chavda. Wakati mnafanya usanifu wa kina ninaomba eneo lile litengenezwe kwa dharura. Tumeshaongea na Naibu Waziri, Waziri nimekudokeza, Makatibu Wakuu mara tatu nimeongea nao kuangalia hili eneo kwa sababu linatukwamisha. Mara zote napambana na Engineer wa Mkoa angalia kokote kule hili eneo ulitengeneze. Ninachoomba wakati mnafanya usanifu wa kina eneo la Mlima Chavda muanze kulijenga kwenye bajeti ya mwaka huu. Muongezeeni Meneja wa Mkoa fedha kwenye eneo la matengenezo ili aweze kutengeneza eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Meneja wetu wa Mkoa Engineer Bashiru anafanya kazi nzuri. Wakati wa mvua barabara zote zilifunga tukampigia kelele, baada ya muda mvua ilivyokatika barabara zote akazinyosha. Anafanya kazi nzuri naomba muwezesheni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe; tunayo barabara inayotoka Hirbado – Basodesh – Seche mpaka Bashnet, barabara hii tuipandishe hadhi iwe chini ya TARURA ili itengenezwe vizuri hali yake ni mbaya sana. Wananchi wakiangalia barabara hii upande wa Singida, ukitoka pale Hirbado kuna Kijiji cha Singa, kuanzia Singa ukienda Mtinku - Ilongero – Singida barabara iko TANROADS na inatengenezwa vizuri, lakini ukija upande huu wa Manyara kuanzia Bashnet – Dareda barabara iko chini ya TANROADS inapitika vizuri, wananchi hapa katikati wanasema sisi wa nchi gani? Kama upande wa Singida iko TANROADS, upande wa Bashnet – Dareda iko TANROADS, kwa nini kipande hiki kisiunganishwe barabara yote ikawa chini ya TANROADS ili itengenezwe vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna muujiza, Wilaya ya Hanang yenye kata 33, vijiji 96 tunatenga fedha ndogo tunayopewa upande wa TARURA ika-cover barabara hizo zote. Hiyo barabara ipandishwe ili itengenezeke vizuri iweze kuwasaidia wananchi kwenye shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uwanja wetu wa ndege wa Mkoa wa Manyara. Mkoa wa Manyara ni kitovu cha utalii, mama amepiga Royal Tour kutangaza utalii wetu, ili sisi tunufaike na utalii lazima uwanja ule utengenezwe ili wananchi waweze kufanya shughuli mbalimbali zinazounganika na utalii ambao tumeutangaza sana kupitia Mama Samia Suluhu Hassan. Mama ameupiga mwingi basi na ninyi upande wa uwanja muupige mwingi ili tuendane. Tarangire pale tunakosa wageni kwa sababu usafiri ni mgumu, Lake Manyara tunakosa wageni kwa sababu usafiri changamoto, mtu mpaka atue KIA ndio anakuja mpaka Lake Manyara, safari ni ndefu. Tufungue ile corridor ya utalii, Mlima Hanang, vivutio kibao, lakini namna ya kufika. Tukifungua ule uwanja utatusadia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo upande wa bei ya usafiri wa anga nchini kwetu. Watu wanajitetea sana kwamba base yetu ya wasafiri ni chache, watu wanaotumia usafiri wa ndege ni wachache, lazima tuje na mkakati wa kuwahamasisha ili watu watumie usafiri wa ndege ili kurahisisha usafirishaji nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi mbalimbali umbali uleule ambao unalipa shilingi laki nne kwa wenzetu laki moja. Fanyeni tathmini ya kina kama ni kodi zimezidi angalieni namna ya kurahisisha upande wa kodi tuangalie sehemu gani gharama zetu zinakuwa kubwa ili hatimaye tuweze kusaidia usafirishaji kwa sabahu kusafiri kwa basi unatumia saa nyingi unapoteza muda mwingi, ukichukua ndege saa chache umefika unafanya shughuli zako, unafanya shughuli nyingi kwa wakati, ndani ya siku moja unaweza kufanya shughuli nyingi. Bila kuboresha sehemu ya usafiri hatutaweza kufanya kitu cha maana. Hilo eneo tuliangalie, tusitafute excuses za kwamba, base ya wasafiri ni ndogo, hiyo haitoshelezi. Tutumie vichwa vyetu tuweze kutanzua eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitambue kazi kubwa sana inayofanyika na Serikali yetu. Miundombinu mbalimbali inayotengenezwa ni kazi kubwa, lakini kama wenzangu walivyochangia lazima twende kimkakati, maeneo yale ambayo yanatufungua kiuchumi tuyatazame kwa kina. Nimeongelea barabara ya Katesh – Hydom, tumesema kilimo cha ngano, ile iwe ndio center ya kuzalisha ngano. Tuna nakisi ya ngano zaidi ya tani milioni moja, tujielekeze huko. Maeneo ambako vitunguu vingi vinalimwa tunasafirisha maeneo mbalimbali tujielekeze huko ili tufungamanishe sekta hizi za miundombinu na sekta ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni tuliwaambia wananchi kwamba, miundombinu ya barabara ni sawasawa na mishipa ya damu. Mshipa wa damu ukiziba hautakuwa na amani, utatafuta daktari popote ili uweze kupata matibabu uweze kurudi kwenye hali ya uzalishaji kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ndio hivyo hivyo, ukiangalia maeneo ambayo barabara imefunguliwa, imewekwa lami maendeleo yanaenda kwa kasi, lakini miundombinu hakuna, hakuna maendeleo. Huwezi kumvutia mwekezaji yoyote ili akawekeze kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya mimi niseme naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa; Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu Pauline; Katibu Mkuu, ndugu yangu Abbas; lakini Naibu Katibu Mkuu, ndugu Yakubu pamoja na watumishi wote ndani ya Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ukiona Serengeti Girls wanafanya vizuri na wanaenda World Cup, ukiona Tembo Warriors wanafanya vizuri, wanaenda world cup na maeneo mengi wasanii wanafanya vizuri hiyo ni kazi kubwa imefanyika.
Mheshimiwa Spika, kama wenzangu walivyotangulia kusema kwamba angalau uhai wa Wizara tumeuona, baada ya Waziri kuchakarika, tumekuwa naye kwenye Kamati, ametuambia sasa anaenda mtaa kwa mtaa, anaenda kijiji kwa kijiji hatimaye kata kwa kata, wilaya kwa wilaya kupeleka salamu za Mama kwenye michezo. Tunamsubiri, hiyo salamu njema ya Mama itufikie.
Mheshimiwa Spika, kipekee nizipongeze sana timu zetu hizi zinazofanya vizuri. Jana nilikuwa miongoni mwa waliokuwa Amani kushuhudia Serengeti Girls wakiicharaza Cameroon, siyo kazi ndogo Cameroon ni timu kubwa, jina lake ni kubwa kwenye mpira lakini vijana wetu wamefanya vizuri sana, nawapongeza sana. Hata hivyo, siku za karibuni pia tumeanza kufanya vizuri hata kwenye riadha. Nalisema hili mahususi, nchi hii ukitafuta medali nyingi, zipo Hanang. Tunayo kumbukumbu nzuri ya mzee wetu Gidamis Shahanga ameleta medali mbili za dhahabu za Commonwealth, lakini kijana wetu mahiri Emmanuel Giniki amevunja rekodi iliyodumu kwa miaka nane ya Warsaw Peace Half Marathon, ni kazi kubwa inafanyika.
Mheshimiwa Spika, nikizungumzia eneo hili, ninachoomba Hanang iangaliwe kipekee kwenye eneo la riadha. Nimeona orodha ya michezo ya kipaumbele, mpira wa miguu, netball, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, mpira wa mikono. Sisi tuanze na riadha kwa Hanang kwa sababu tunayo record ukitafuta medali Tanzania hii Hanang tunaongoza, tunaomba tupewe kipaumbele cha kuangaliwa kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, michezo hii yote ya vipaumbele ambayo imewekwa, ili ifanikiwe naishauri sana Wizara washirikiane na TAMISEMI kuboresha eneo la michezo mashuleni, UMITASHUMTA na UMISSETA. Kazi inafanyika lakini ukienda kwenye shule zetu hakuna vifaa vya michezo. Bila vifaa vya michezo itakuwa ni hadithi kuimba, kwamba tutaibua vipaji, ukienda kwenye shule zetu mipira bado wana matambara shule nyingi. Tusaidiane kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo la wataalam wa michezo, wenzangu wamelisema sana hili. Ukiangalia hakuna motisha yoyote wanayopewa Walimu ambayo wanajihusisha na michezo. Tuwatambue, tuwape motisha, lakini tuwape mafunzo mahusus ili wawafundishe vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amekuja na mpango mzuri wa shule 56 mahususi kwa ajili ya michezo. Mambo ambayo nimeeleza kwa ajili ya Hanang naomba shule ya kwanza ikajengwe Hanang. Wakashirikiane vizuri lakini bila kutatua changamoto ya upatikanaji wa wataalam, upatikanaji wa vifaa, bado changamoto ni kubwa. Wizara waanze na suala la kutatua changamoto ya vifaa na wataalam ili hizo shule sasa zitakapokuja ziweze kuwasaidia na tutengeneze vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia michezo yetu ukitoa kwenye mfumo huu wa shuleni, UMITASHUMTA na UMISSETA. Baada ya hapo, vijana wakienda vijijini wanazagaa tu. Kwa sisi wakulima na wafugaji kuanzia mwezi Aprili mpaka mwezi Desemba hatuna shughuli mahususi, kwa hiyo, vijana wengi wanakaa vijiweni. Lazima tuje na mkakati mahususi wa kuwapelekea michezo kwenye mitaa ni mkakati muhimu sana naomba ukatekelezwe. Waziri aje ili tuwaokoe vijana na changamoto za kukaa vijiweni. Vijana wengi wakienda vijiweni wanafundishana mambo ya ajabu. Ndio unakuta watoto wadogo wamejifunza kunywa pombe utotoni tunapoteza nguvu kazi ya Taifa kwa sababu hatuna shughuli za kuwaweka na kuwatoa kwenye vijiwe. Kwenye vijiwe kuna mambo mengi.
Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa viwanja; kwenye bajeti ya Wizara wana viwanja saba ambavyo wanavikarabati, lakini mahitaji ya viwanja nchi hii ni makubwa sana. Tunachoomba kwenye eneo hili hatusemi Wizara wajenge viwanja kila sehemu, kwa sababu wanao uzoefu kwenye eneo la michezo, watutengenezee mpango ambao halmashauri zetu zitafuata wa PPP ili tuwekeze na viwanja hivyo viweze kujengwa, tuweze kuwaendeleza vijana wetu na tuwe na facilities za kufanya mazoezi, lakini ni sehemu ya kutambua vipaji vya vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaweza kutohoa kutoka kwenye Wizara ya TAMISEMI, wao walielekeza kila halmashauri inayokusanya zaidi ya bilioni tatu ijenge kituo cha afya cha milioni 400. Kwa sababu tunapoenda kwenye kituo cha afya tunaenda kutibu watu, lakini ukiwa na maeneo ya michezo unawakinga watu na maradhi. Sasa tuangalie namna ambavyo tunaweza kutohoa na namna ambavyo tunaweza kutekeleza, tukajaribu kuwekeza kwenye eneo la kuwakinga Watanzania na maradhi wakati huo huo tukiendeleza utaratibu wa kupelekea huduma kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili linawezekana wakiunganisha na mpango mahususi wa PPP na halmashauri zetu ili kuondoa burden kubwa na uhaba wa viwanja tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la utamaduni; ukiangalia sasa Watanzania kama wengi tunaanza kusahau asili zetu. Niombe Wizara ianzishe siku mahususi ambako watu watarudi kwenye tamaduni zao, kutakuwa na michezo mbalimbali, wasukuma watakuwa na mambo yao ya kiutamaduni, lakini Wairaki watakuwa na mambo yao ya kiutamaduni, Wakurya watakuwa na mambo yao ya kiutamaduni pia ndugu zangu Wanyaturu watakuwa na mambo yao ya kiutamaduni. Tuchague siku mahususi ili tuweze kuhamasisha tamaduni zetu. Hiyo itatusaidia sana ili angalau watu tusisahau na tamaduni zetu zisipotee.
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kutoa pongezi kwenye makampuni ambayo yanaweka au wanafadhili kwenye michezo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Nicodemas Maganga. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa tu Mheshimiwa mchangiaji, mchango wake ni mzuri sana, naomba Wizara iuzingatie. Kwa kweli kwenye utamaduni hapo kama kweli Wizara ikipashika vizuri, Wasukuma tunacheza ngoma vizuri sana. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mhandisi Hhayuma. (Kicheko)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nafikiri anaongezea kwenye yale ambayo nimesema, ni mambo ya msingi sana ambayo Mheshimiwa Maganga ameyagusia.
Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusema, wale ambao wanawekeza kwenye michezo, wanaofadhili michezo mbalimbali, wanaofadhili sanaa, tutambue mchango wao. Nasema tu kwa wachache tu, nitaje Azam, Mohamed Enterprises, Sports Pesa, juhudi zao tumeziona. Huko nyuma Serengeti waliwekeza kwenye michezo, lakini Tanzania Breweries pia wamewahi kuwekeza kwenye michezo na wengine ambao wanagusa maeneo hayo. Hao wadau tutambue mchango wao, utatuhamaisha wengi zaidi kwenye eneo la michezo kwa sababu inagusa zaidi upande wa sekta binafsi. Tuweze kuhamasisha wengi ili kwenye sekta ya michezo kuwe na fedha ya kutosha na tuweze kuendeleza vipaji.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kuchangia hoja hii kwa kuanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini nigusie tu kwamba tunayo barabara yetu inayotoka Hydom kuja Katesh. Ile barabara inategemewa sana na wana Hanang na Watanzania. Pia ile barabara ukifika Katesh inaunganisha na Nangwa - Gisambala - Nkondoa ni barabara muhimu sana kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, Hanang ukiacha kuwa wanalima sana mazao mbalimbali ikiwepo ngano na ndiyo kitovu cha uzalishaji wa ngano kwa Taifa hili, lakini pia tuna kiwanda cha cement ambacho kiko kwenye utaratibu wa kuanza, na pia tuna kiwanda cha chumvi ambacho kiko kwenye utaratibu wa kuanza. Kwa hiyo, barabara hizi zikitengenezwa zitatusaidia sana kusafirisha bidhaa hizo muhimu kwa Taifa letu na itakuwa ni hub ya kuilisha Dodoma ambako ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna barabara ambayo inatoka Kibarashi inakuja mpaka Kijungu – Kibaya – Kijoro; barabara hii inakuja mpaka Dalay – Mbicha. Kwenye mpango wa Taifa ambao tumeupitisha hapa Bungeni na bahati nzuri ninao hapa, barabara hii inapita Kondoa, baada ya Kondoa inaenda Singida. Ila kwenye mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta sasa, barabara hii amei-divert, badala ya kupita Kondoa, yeye anataka ipite Chambalo, ipite Chemba baada ya hapo iende kwa Mtoro halafu Singida.
Mheshimiwa Spika, barabara hii inategemewa na watu wengi, barabara hii tumeinadi kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Wana-Hanang nimewaambia, wana Kondoa vijijini wameambiwa wana-Kondoa Mjini wameambiwa, maeneo mbalimbali watu wameambiwa kwamba hii barabara inakuja kutengenezwa.
Mheshimiwa Spika, barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, iko kwenye ukurasa wa 73. Sasa kama iko kwenye Ilani, pia iko kwenye mpango wetu wa miaka mitano 2021/2022 - 2025/2026. Nini kilichotokea hapa katikati hii barabara ikabadilika? Mheshimiwa Waziri mimi niseme wazi, hii barabara inategemewa na watu wengi, na watu wameweka matumaini huko. Hayo mabadiliko mnayoyafanya sasa, watu hatuyatambui, ni mapya, hatuyaelewi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa niaba ya wana-Hanang, wana-Manyara wana-Kondoa tunaomba utupe ufafanuzi, nini kilichotokea? Kwa sababu haipo kwenye mpango, haipo kwenye Ilani, kama itabaki hivi ilivyo ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wewe ni mtani wangu, kwa hapa hatuko pamoja. Hapa hatuko pamoja, naomba hili niliweke wazi kabisa. Hili lirekebishwe. Naamini ni makosa madogo ya kiuchapaji, siyo ya kimpango. Makosa haya ya kiuchapaji yarekebishwe ili yale matumaini ambayo Watanzania wameyaweka hapo yaendelee kubaki kama yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusemea hili suala la barabara, na mara zote napenda kuongea masuala ya barabara, nimefananisha barabara na mishipa ya damu ya mwili wa binadamu, kwa sababu barabara ndizo zinazoboresha uchumi wa maisha ya wananchi. Lazima hapo tupaangalie vizuri.
Mheshimiwa Spika, nichangie kidogo kwenye eneo la ukuaji wa uchumi wa Taifa. Nimejaribu kupitia kwenye hotuba ya Waziri. Ukiangalia, ametupa taarifa, mwaka 2019 chumi za nchi za kusini mwa Afrika zilikua kwa asilimia 3.1, lakini wakati wa Corona mwaka 2000 uchumi ukashuka sana ukuaji wake mpaka -1.7. Baada ya Corona kuondoka mwaka 2021, ukuaji huo ukaboreka ukaenda kwenye 4.5.
Mheshimiwa Spika, kwenye nchi zetu za Afrika Mashariki, ukijaribu kuangalia ukuaji kabla ya Corona mwaka 2019 nchi nyingi sisi tulikuwa 7.0, lakini nyingine zilikuwa 4.8, 9.5, 3.1, 1.8, 0.9. Baada ya Corona kututandika na mambo yakaenda ndivyo sivyo, sisi Tanzania kwa kuwa tulichukua hatua mahususi za kutokufunga shughuli za uzalishaji, za kuhakikisha kila fursa tunayoipata tunaitumia ili kuhakikisha kwamba uchumi wetu haudorori. Tulikua kwa asilimia 4.8, lakini nchi nyingine zote za ukanda wa Afrika Mashariki iliyojitahidi sana ilikuwa kwa 0.6, lakini kuna nyingine zilifanya vibaya kabisa, zilikua kwa -6.6.
Mheshimiwa Spika, baada ya Corona mwaka 2021 nchi nyingi zili-bounce back. Iliyoshindwa sana ilikuja kwenye 0.1 kwenye ukuaji wa uchumi, lakini hiyo kabla ilikuwa na -6.6. Maana yake ni kwamba baada ya Corona yenyewe ule ukuaji wa uchumi wake umeongezeka kwa asilimia 6.7. Sisi tume-bounce back kwa 4.9, ongezeko la asilimia 0.1.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema, ukiangalia sisi baada ya Corona ile gain haijawa kubwa. Wataalam wetu wa uchumi, Mheshimiwa Waziri ukiwaongoza, hapo tunapaswa kufanya kazi ya ziada. Tuangalie ni sehemu gani tunapaswa kuboresha ili tu bounce back kama wenzetu. Kuna nchi ambayo ilikuwa -3.4, lakini baada ya Corona iko 10.9. Maana yake ongezeko lake ni asilimia 14.3. Sisi tunapaswa kujitathmini hapa, sehemu gani tumekosea na nini tukifanye?
Mheshimiwa Spika, nimejaribu kuangalia kwenye suala la ukuaji wa uchumi mwaka 2021, sekta ambayo imeongoza ni sekta ya ujenzi asilimia 13.1. Ni imani yangu kwamba eneo hilo lilifanya vizuri kwa sababu fedha ziliongezwa kwenye eneo la TARURA, shughuli nyingi za uchumi zilifanyika kwenye ujenzi wa miundombinu. Ukiangalia shughuli ambayo Watanzania wengi wanategemea, kilimo imekua kwa asilimia 9.6, lakini ufugaji asilimia 7.1. Ukiangalia ndiyo Watanzania wengi walikoajiriwa.
Mheshimiwa Spika, kwa wastani wa kitaifa, wakulima na wafugaji ni asilimia 65 plus. Kwa sisi wa vijijini ni zaidi ya asilimia 95. Eneo hili tumeongeza bajeti, ni jambo jema, lazima tuangalie namna ya kuhakikisha kwamba inaleta tija ambayo tunaitarajia.
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia maeneo ambayo yamefanya vibaya sana, kuna suala la sayansi, utaalam na ya ufundi. Mheshimiwa Waziri wa Elimu alitueleza kwa kina wakati ana-present bajeti yake na akasema yeye ataweka incentive kwa wale ambao watafanya tafiti zitakazoleta tija na hatimaye atatoa fedha. Naomba kwenye eneo hili, Waziri wa Elimu awezeshwe ili tafiti ziweze kufanyika na hatimaye ugunduzi uweze kufanyika, nchi yetu kwenye eneo hilo tuanze kujitegemea tujitengenezee vitu vyetu na eneo hilo liweze kukua kwa sababu ukuaji wake kwa sasa ni asilimia 0.9. Ila ukiangalia shughuli kubwa ambayo inaajiri Watanzania ni hilo eneo la kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti hii tumependekeza uingizaji wa ngano kutoka nje ya nchi tunapunguza kodi. Kwenye ngano tunapunguza kutoka asilimia 35 kuja asilimia 10. Tufanye maamuzi magumu kama tulivyofanya maamuzi magumu wakati wa Corona, wenzetu wakifunga mipaka sisi tunafanya shughuli, uchumi unaimarika. Tuachane na kupunguza kodi kwenye eneo la shughuli zinazohusiana na kilimo kwa sababu watu wetu wana uwezo wa kulima.
Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi wako vijiweni, wakiamka asubuhi utawaona wanacheza karata, wako kwenye michezo ya bonanza; ile kamari ambayo kila siku mtu anakuwa na shilingi, lakini kila siku inaondoka na bonanza. Twende tukawahamasishe watu waende shambani wakalime, fursa ndiyo hiyo. Badala ya kusema tunapunguza kodi ili tupate mazao zaidi kutoka nje ya nchi, tuna ardhi ya kutosha ya kilimo, hatuna sababu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata kwenye upande wa kilimo cha miwa, miwa mingi inaharibika lakini kwa nini tupunguze kodi kwenye sukari? Tuangalie eneo hilo. Hayo ni maeneo ya msingi sana kwa Watanzania wetu tukawahamasishe wakalime zaidi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nitaunga mkono hoja baada ya kuwa nimepata ufafanuzi wa barabara niliyoisema, ile ambayo haijakaa sawa sawa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Mpango wetu. Kwenye Mpango wakati Mheshimiwa Waziri wa Mipango anawasilisha hotuba yake, kwenye ukurasa wa 20 aliongea kwamba, “Tutaongeza uzalishaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kupitia kilimo, mifugo, uvuvi na madini.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni wazo zuri sana, hii mimi likanisukuma niangalie je, kwenye mpango huu suala la ardhi limeangaliwa kiasi gani? nilivyomsikiliza Waziri wakati anawasilisha sikusikia neo ardhi lakini nikaenda kwenye Mpango nimebahatika kupitia ukurasa wa 100 yote yanayoripotiwa ni ambayo yamekwisha kufanyika kwa sehemu kubwa. Ukiangalia zimetumika shilingi bilioni 17.2 kwa ajili ya upimaji wa vijiji lakini katika kurasimisha na viwanja 118,045 kwa mwaka 2020/2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea tena kwenye kuimarisha mipaka ya kimataifa. Mpaka kati ya Kenya na Tanzania umetumia kwa mwaka 2020/2023 shilingi bilioni 1.75 na ukiangalia mambo yote yaliyogusa ardhi ni yale ambayo yamekwisha kufanyika. Ukisikiliza Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamechangia inaonyesha tunatatizo kubwa sana kwenye eneo la ardhi. Ardhi ya kilimo, ardhi ya mifugo kuna changamoto kubwa, ardhi ambayo tunaihifadhi kwa ajili ya misitu changamoto ni kubwa. Eneo hili ninaamini kwamba kwenye mpango ilipaswa kupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea wananchi wangu wa Kijiji cha Diloda, Kata ya Gidafira wote wamechomewa nyumba zao wakisema kwamba eneo lile ni hifadhi. Sasa tuna Kitongoji tumefanya uchaguzi 2019, tumeweka Mwenyekiti wa Kitongoji na viongozi wote wa Serikali wanaohusika. Kwenye ramani ya vijiji Kitongoji hicho ni sehemu ya Kijiji, unaenda leo Maliasili na Utalii unasema hili ni eneo la msitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi imani yangu ni kwamba tukitibu tatizo la ardhi, maendeleo mengine yanaweza yakawa ni rahisi. Tunaweza kuwa na maeneo ya uhakika ya kilimo, tunaweza kuwa na maeneo ya uhakika ya wafugaji lakini pia hata uvuvi kwa sasa kwa sababu tunataka kuchimba mabwawa, tunaweza kuwa na uhakika na maeneo ya kuchimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Mpango lazima uangalie vizuri eneo la ardhi, lakini kuhusu eneo hili ambalo Wananchi wamechomewa nyumba zao. Ninaomba Serikali i-act haraka kwa sababu wananchi hawa kwa sasa hawana makazi, wananchi hawa nyumba zao zimechomwa na mazao ndani na ambayo ilikuwa ni chakula. Mbegu zao zimechomwa ndani lakini pia mavazi yao kwa sababu walifukuzwa na nyumba zikachomwa watu hao hawana mavazi. Hayo yote ni mambo muhimu katika maisha ya binadamu, watu hawa wamekoseshwa haki zao tena kipindi kigumu kipindi ambacho mvua inanyesha, watoto wadogo wanalala nje, mama wajawazito. Naomba Serikali kwenye eneo hili iliangalie kwa kina na watu hawa waweze kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli ni hifadhi, ukiuliza upande wa Hanang’ upande wa Manyara wao wanasubiri kuweka beacon ya mipaka kwa sababu kuna utata wa mpaka kati ya Singida na Manyara hakuna alama zinazoeleweka, Manyara au Hanang’ hatujawahi kukaa vikao vyovyote kutenga eneo la Hifadhi ya Msitu! Ninaomba eneo hili liweze kushughuliwa haraka ili watu hawa waweze kusaidiwa na wasiendelee kukaa kwenye mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kuchangia kwenye mpango wetu, pamoja na malalamiko haya ya wananchi wangu, nitambue kazi nzuri ambayo imefanyika kwenye eneo la kilimo. Kilimo inaajiri watu zaidi ya asilimia 65 lakini ninafarijika sana ninavyoona kwamba yenyewe ndiyo inayoongoza kwenye Pato la Taifa. Tuendelee kuwekeza, tuendelee kuboresha eneo la kilimo lakini pia tuendelee kuboresha utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo, ili tuboreshe eneo hili kwa sasa ni wakati wa mvua, utaratibu wa upatikanaji wa mbolea lakini mbegu za ruzuku, ili tuweze kupata mbegu bora wakulima wetu waweze kulima ili waweze kuzalisha mazao na waweze kuzalisha kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto baada ya kuvuna. Tumejifunza wakati wa corona umuhimu wa nchi kujitegemea. Kipindi kile cha lock down ukitaka bidhaa za afya kwa sababu nyingi tulikuwa tunaziagiza toka nje, changamoto hata mafuta nazo tulianza kupata changamoto kwa vitu vyote tunavyoingiza nchini. Kuna umuhimu sana wa nchi kuanza kujitegemea. Maana yake ni nini? Bidhaa zile tunazozizalisha ndani ya nchi tuhakikishe kwamba zinakuwa na soko la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi tuna changamoto kubwa ya nakisi ya uzalishaji wa ngano lakini wakulima wakizalisha ngano upatikanaji wa soko ni changamoto kubwa kwa sababu tumeagiza ngano nyingi kutoka nje na kwa hali ya uzalishaji wa nchi yetu bei ya ngano ya nje ni nafuu kuliko ya ngano ya ndani. Changamoto hiyo tunayo kwenye alizeti, tunayo kwenye mazao mengine. Ninachotaka kusema, vile ambavyo vinawezekana kuzalishwa hapa nchini tutoe kipaumbele kwanza, tuwe tumevitumia ili nakisi inayobaki ndiyo tuagize kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mjadala mrefu kwenye suala la zao la ngano. Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe anakumbuka vizuri kwamba wale wanaotumia ngano wanunue ngano yote ya ndani ndiyo wapewe kibali cha kuingiza ngano kutoka nje ya nchi. Ninaomba hilo lifanyike kwenye mazao yote ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanakuwa na uhakika wa soko wa kile wanachokizalisha mashambani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda hata kwenye upande wa nishati. Wabunge wengi wameongelea, tunayo gesi. Gesi hii husikii sana matumizi yake yakitangazwa. Ukiongea namna ya vituo hivi vinavyopatikana vibali yawezekana ni changamoto au vinachukua muda mrefu. Ninachoomba kile ambacho kinaweza kupatikana hapa nchini tuwekeze na tuweke msukumo mkubwa. Tufanye marketing ili gesi iweze kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tuendelee kuagiza mafuta kwa kiasi kikubwa wakati tungeweza kuhamasisha matumizi ya gesi kwenye magari yetu. Tukianza kuna Wabunge wameshasema kwamba magari ya Serikali yawe ya kwanza kwenye suala la gesi. Upatikanaji wa vibali vya kujenga vituo kwa ajili ya gesi urahisishwe na ikiwezekana uwe fast tracked ili gesi hiyo iweze kutumika kwa ufanisi na tuache kuagiza mafuta ili hatimae fedha zile ambazo tungezitumia kwa ajili ya kuagiza nishati nje ya nchi izunguke hapa hapa ndani ili tujitosheleze hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mitambo ya kuzalisha umeme, tuhakikishe mitambo yote ambayo inatumia either diesel tuibadilishe ianze kutumia gesi ili gesi hiyo iweze kutumika na iweze kutusaidia. Ni muhimu sana kuweka huo msukumo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamakaa ya mawe, ni karibuni tumeanza kutumia lakini dunia nzima inafanya harakati ya kuondokana na makaa ya mawe, gesi yenyewe harakati zinafanyika mpaka 2040, 2050 iwe imeondoka sokoni na sisi bado hatujanufaika vya kutosha, lazima tuweke nguvu kubwa kwenye eneo hilo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha?
MWENYEKITI: Malizia dakika moja.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi naomba nihitimishe kwa kusema hivi, suala la ardhi ni suala muhimu, tuweke mkakati mzuri wa matumizi ya ardhi na yale ambayo yanaathiri watu wetu tuchukue hatua sasa. Tuone namna ya kuwashirikisha Wenyeviti wa Vijiji ambao wanakaa karibu na wananchi ili elimu iweze kwenda sawa sawa. Hawa Wenyeviti wa Vijiji wakati mwingine ndiyo wanaosababisha confusion hata kwenye maeneo yetu kwa sababu hawana mishahara kwenye kazi wanayoifanya, tutengeneze mfumo rasmi wa kuwatumia na kuwalipa, hiyo itatusaidia ili kutumia ardhi yetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Pia nimpongeze Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ili asaidiane na Mheshimiwa Engineer Masauni kuwahakikishia Watanzania usalama wao na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani itusaidie kufanya maboresho kwenye Vituo vidogo vya Polisi vya Bassotu, Balangdalalu na Endasak kimiundombinu ipi kupatiwa usafiri ili wafanye kazi zao kwa ufanisi. Wilaya ya Hanang ina kata 33, ninashauri Wizara ya Mambo ya Ndani iige kama walivyofanya wenzao wa TAMISEMI kwa kuwapatia watendaji wa kata usafiri wa pikipiki hivyo askari kata nao wapatiwe pikipiki. Hali hii usafiri pia ni mbaya sana ngazi Wilaya, tunaomba tupatiwe magari wilayani ili kuboresha utendaji kazi wa Jeshi letu la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Hanang ni mbaya sana, hakuna askari wa kutosha, hawana usafiri ba hakuna gari la Zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha atuhakikishie Wana-Hanang kupata watumishi waliowezeshwa vitendea kazi. Tumejifunza wakati wa maporomoko ya udongo, mawe na magogo Mlima Hanang kuwa Idara ya Zimamoto Wilaya ya Hanang ina mapungufu makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niwapongeze sana watumishi wachace tulionao wanavyojitolea na kwa kushirikiana na Wana-Hanang wengine walifanya kazi kubwa kuokoa maisha ya Wana-Hanang wengi kipindi kile cha maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize kupatiwa gari la Zimamoto kwa kuwa Hanang ipo njia kuu ya Arusha kwenda Singida na magari mengine yamekuwa yakiungua yakiwa safarini mfano siku ya Jumapili gari iliyobeba cement iliungua moto wilayani kwetu ikiwa na mifuko 600 na sehemu kubwa wataalamu waliopo wilaya wakabaki kuhangaika kwa kukosa gari la Zimamoto. Hivyo Hanang tupewe kipaumbele kwenye magari ya Zimamoto zinazonunuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kuendelea kutubariki ili kutekeleza majukumu yetu ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayofanyika maeneo mbalimbali mfano mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere ambayo ikikamilika itazalisha megawati 2115, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ununuzi wa meli za uvuvi, fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo ambapo miradi mbalimbali ya umwagiliaji inaendelea kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi sana kwa Wilaya ya Hanang tulipopata maporomoko ya udongo, mawe na magogo toka Mlima Hanang, wakati ule Rais aliacha shughuli zake zote ili kushirikiana na Wanahanang ili kuokoa na kuopoa waathirika wa changamoto ile. Serikali yote na wadau walihamia Hanang kutoa misaada ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa jinsi alivyowasilisha hotuba yake kwa umahiri mkubwa, lakini pia kwa kazi nzuri anayofanya toka alipoteuliwa na Rais kuisimamia TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nimpongeze sana Mheshimiwa Zainab Katimba kwa kuaminiwa na Rais kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange kwa jinsi anavyomsaidia Waziri vizuri. Pongezi zangu pia ziende kwa Katibu Mkuu na wataalam wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kujituma kwao kushughulika na changamoto za Watanzania kwani shughuli wanazozifanya zinagusa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri sana imefanyika kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara za vijijini na mijini ila baada ya mvua kubwa iliyonyesha barabara nyingi zimeharibika mfano kwa wilaya yangu ya Hanang hali ni mbaya sana hasa ukijumlisha na maporo maporomoko ya Mlima Hanang hali inakuwa tete sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyochangia bajeti hii ya barabara ya Endasak – Gitting - Dawar imefunga kabisa huu ni mwezi unaelekea kuwa mwezi wa tano, barabara za Mogitu - Gendabi, Dawar - Ziwa Chumvi, Masakta – Lambo - Masqaroda, Hilbadaw - Dang'aida, Dang'aida - Setchet, Waama - Diloda Mureru, Mureru – Dumbeta - Katesh, Murumba – Balang’dalalu, Getanus - Bassotu Mara - Simbay, Mulbadaw - Bassodesh kwa kutaja kwa uchache maeneo mengi magari hayapiti kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh (Kata za Katesh, Dumbeta, Jorodom na Ganana) hali ni mbaya kabisa mfano tu barabara ya lamay ambayo ina makorongo makubwa yanayohatarisha nyumba zilizoko pembeni ya barabara kuanguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kwenye miundombinu ya sekta ya elimu bado Hanang kuna upungufu mkubwa wa madarasa, nyumba za walimu, madawati, mabweni kwa shule za msingi na sekondari pia maabara kwa shule ya sekondari. Wananchi walihamasishwa kujenga maboma ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni na maabara ili Serikali iweze kuzimalizia na kuunga mkono juhudi za wananchi, maboma hayo mengi yana zaidi ya miaka 12 kitu ambacho kinakatisha tamaa juhudi za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya afya vijiji vingi havina zahanati na kata hazina vituo vya afya. Aidha, zahanati nyingi zilizojengwa makao makuu ya kata zamani zimekuwa chakavu na majengo yake hayakidhi mahitaji ya sasa kutokana na idadi ya watu kuongezeka. Wananchi wetu wanajitahidi sana kujitolea kwenye shughuli za maendeleo, tuendelee kuwaunga mkono ili kukidhi mahitaji yao ya kiafya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yangu ni kuwa Serikali iandae mkakati mahususi na bajeti ili kumalizia maboma yote ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni na zahanati zilizojengwa kwa nguvu za wananchi ili kutowakatisha tamaa na huduma iliyokusudiwa kupatikana kwa wakati.
Pili, fedha zilizoombwa kiasi cha shilingi 2,203,854,000 kwa ajili ya kurudishia miundombinu iliyoathirika na maporomoko ya Mlima Hanang zitolewe mapema ili shughuli za uzalishaji na huduma ziweze kuendelea kawaida.
Tatu, Serikali itoe haraka fedha za matengenezo ya dharura ili kurudishia barabara zote zilizoadhiriwa na mvua kubwa iliyonyesha mwaka huu; nne, Serikali ituletee magari mawili ya wagonjwa kwa kuzingatia ukubwa wa wilaya na wingi wa watu; tano, Serikali iendelee kuajiri walimu, watendaji wa vijiji, wataalamu wa afya, wataalamu wa kilimo na mifugo kwa sababu wilaya ina uhaba mkubwa sana wa wataalamu kwenye sekta za elimu, afya, kilimo, mifugu na utawala; na sita, Serikali iliweka vifaa vya kufuatilia mwenendo wa Mlima Hanang ili wananchi wasiathirike pindi changamoto za maporomoko yanavyojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu ninaunga mkono hoja nikiamini changamoto ya wananchi wangu zimepokelewa na zitaenda kufanyiwa kazi kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye Sekta ya Nishati na nianze mchango wangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Judith Kapinga, Naibu Waziri wa Nishati, nampongeza Katibu Mkuu, Mhandisi Felchesmi Mramba na timu yote ya Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Sekta hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana timu yangu ya mkoa ikiongozwa na Meneja wa Mkoa na timu ya wilaya ikiongozwa na Meneja wa Wilaya, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ndani ya maeneo yao na Meneja wangu wa wilaya kwa ushirikiano mkubwa ambao ananipatia. Pia, naipongea sana ile timu ya Wizara kwa sababu kazi kubwa inayofanyika tunaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na changamoto kubwa ya mgao wa umeme; kazi kubwa imefanyika ambapo wakati mwingine wengine tunaweza tusione sasa hivi kilichofanyika kwa sababu tulisema wakati ule kwamba, changamoto ilikuwa ni maji kwenye maeneo ambayo tulikuwa tunategemea umeme kuzalishwa kwa maji na mvua zinanyesha. Niwahakikishie kwamba kazi kubwa imefanyika kuhakikisha kwamba tatizo la umeme limeondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuthibitisha hilo, umeme kwenye gridi ya Taifa umeongezeka kutoka megawati 1,872.1 Mei, 2023, mpaka megawati 2,138 Machi, 2024. Kazi hii ni kubwa na ukiangalia kwa sasa hata kama kuna malalamiko, lakini yamepungua sana. Kati ya sehemu ambayo tumefanikiwa sana ni kuingiza umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo tunatarajia litazalisha megawati 2,115 ambapo mpaka sasa tumeshaingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani, mwaka jana wakati tunajadili Bajeti ya Nishati niliiomba Wizara hii iangalie maeneo ndani ya Wilaya ya Hanang ambayo yalipata umeme muda mrefu. Hivi ninavyoongea tumeidhinishiwa vitongoji 49 na wakati ule nilitaja eneo la Gitting kama mfano, eneo la Nangwa kama mfano, eneo la Gendabi kama mfano na eneo la Mogitu kama mfano wa maeneo ambayo yalipata umeme muda mrefu na nikasema wananchi wameongezeka sana na maeneo hayo yaangaliwe ili wale ambao wamejenga nyumba zao na wanaishi gizani wapate umeme. Mpaka sasa juhudi zinafanyika kuhakikisha kwamba umeme unaenda kwenye vitongoji vya maeneo hayo ambayo nimetaja. Naishukuru sana Serikali na wakati huo huo vitongoji 15 navyo vikiendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi kwenye eneo la utekelezaji wa miradi; tulipata mkandarasi anaitwa Daniel ili atekeleze mradi wa kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo, kwenye viwanda lakini pia kwenye visima vyetu vya maji. Maeneo ambayo tuliyaainisha wilayani, eneo la Getasam, eneo la Moram, eneo la Mara B, Gijega, Jorodom, eneo la Muungano, eneo la Quaredan na eneo ambalo tunatarajia kuwa na mgodi wa madini ya mwanga, utendaji wake siyo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara imwangalie mkandarasi huyu kwa umakini kuhakikisha kwamba kazi inafanyika, amefanya survey kipindi kirefu akapotea, tunavutana sana na kazi haiendi sawasawa. Naomba huyu aangaliwe ili kuhakikisha kwamba wananchi ile huduma wanayoitarajia waipate kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie eneo la uzalishaji wa umeme kupitia Sekta Binafsi, kwenye taarifa ya Wizara, Sekta Binafsi inazalisha megawati 31.8 pekee. Nchi yetu ina vyanzo mbalimbali vya umeme, tuna umeme chanzo cha makaa ya mawe, chanzo cha umeme jua, joto ardhi tuna upepo na vyanzo vingine. Kusema Sekta Binafsi mpaka sasa inachangia megawati 31.8 pekee, wakati huohuo tukitegemea kwamba Serikali iendelee kuwekeza rasilimali kidogo ambayo tunahitaji kwenye Sekta ya Elimu, rasilimali hiyo hiyo tunahitaji kwenye Sekta ya Afya ili itoe huduma, unaona kabisa kwamba kuna changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 kuja 2012 tulikuwa na changamoto kubwa sana ya mgao wa umeme na ukiangalia hata bajeti ya Wizara kwa sasa kwenye upande wa maendeleo umeshuka karibu 36, maana yake keki tuliyonayo tunaigombania na haitoshi vizuri. Nashauri kwenye eneo hili, Wizara ione namna ya kuishirikisha Sekta Binafsi kwenye uzalishaji wa umeme. Tuzalishe mabilionea wa Tanzania kutoka kwenye Sekta ya Umeme na hii inawezekana. Tuwashirikishe, kama ni sera inasumbua tuangalie namna ya kuibadilisha ili tuone Sekta Binafsi inashiriki na hatimaye tunazalisha umeme wa kutosha, tukiwa na umeme wa kutosha maendeleo ya nchi yetu yataenda kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, wakati tukiwa na hali mbaya ya mgao wa umeme, Jimbo la Hanang tulikuwa na hali mbaya mara mbili. Changamoto kubwa ni kwamba sisi hatuna kituo cha kupooza umeme. Waya ukiguswa tu na ndege umeme umekatika wilaya nzima na hatuna umeme. Tukigawiwa megawati zile chache, maana yake ni wilaya nzima, tukikatiwa wilaya nzima iko gizani, nguzo ikianguka wilaya nzima iko gizani. Changamoto hii niliiwasilisha hapa Bungeni mwaka 2021 na Serikali ikanijibu, kwa ruhusa yako naomba ninukuu majibu ya Serikali; “Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Hanang kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) imeanza taratibu za ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo kidogo (switchyard) cha kilovoti 33 kutoka njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400, inayoendelea kujengwa kutoka Singida hadi Namanga katika Kijiji cha Mogitu, Wilaya ya Hanang.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kituo hicho kitaboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya Hanang na maeneo jirani na ujenzi wake utaanza Julai, 2022 na utakamilika Julai, 2023 na gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 2.6. Fedha hizi zinategemewa kutolewa na Serikali kwa 100%.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyoongea hakuna kilichofanyika, ombi langu tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, wana-Hanang tuna changamoto kubwa na ukisikia tu kila baada ya muda unasikia taarifa ya kukosekana kwa huduma ya umeme na watakwambia sababu ni ukarabati wa hitilafu ambao watasema aidha imetokana na nguzo kuanguka au kitu kingine chochote, baada ya hapo tu itafuata taarifa ya kukosekana kwa huduma ya maji, changamoto ni kubwa, lakini pamoja na changamoto hizi, kwa kuwa nina imani na Mheshimiwa Naibu Waziri ...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer naomba hitimisha.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka na utendaji kazi wake, sina shaka na umahiri wake na sina shaka na upendo wake kwa Wana-Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na bajeti yake, sina changamoto nayo, naamini hili atalishughulikia. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Samweli Xaday Hhayuma.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye Mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa letu 2025/2026. Ninaanza mchango wangu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameturuzuku uhai na hatimaye tunaweza kuchangia yale ambayo tumeyaandaa kwa ajili ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimepitia wasilisho ambalo ameliwasilisha Mheshimiwa Waziri wa Mipango, Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, mawasilisho yote yanaonyesha dalili nzuri ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pato letu la Taifa limeongezeka kutoka shilingi bilioni 141 mwaka 2022 na kwenda kwenye shilingi bilioni 148, mwaka 2023 ambayo ni sawa na ongezeko la 5.1%. Hata hivyo, tuna matamanio ya kwamba uchumi wetu utaendelea kukua kwa 5.4%, mwaka 2024; 5.8%, mwaka 2025; na asilimia 6.1, mwaka 2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni matamanio na mwelekeo mzuri wa uchumi wa nchi yetu na tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri. Pia, watu wote ambao wanamsaidia akiwepo Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika kutafuta maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaanza kuongelea masuala ya uwekezaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam kelele zilikuwa ni nyingi kweli, kwamba tunaenda kupoteza, lakini ripoti ambayo tumeletewa, uwekezaji ambao umefanyika kwenye Bandari ya Dar es Salaam umetupatia mapato na mwelekeo mzuri. Pia, tumepata taarifa kwamba ndani ya miezi mitano tu tumepokea shilingi bilioni 325.3 na haya ni mapato ambayo yanatokana na kodi ya pango na tozo mbalimbali na wharfage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawezesha Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam iendelee kuwekeza kwenye maeneo mengine ili tuweze kuboresha mapato yanayotokana na bandari yetu. Kipindi kile wakati tunaongea kila mtu alikuwa anaona kwamba Bandari ya Dar es Salaam imeuzwa, bandari tumepoteza, lakini sasa tunapata fedha ambazo tunaenda kuwekeza kwenye maeneo mengine. Tutawekeza kwenye elimu, afya, maji kwa mapato ambayo yanatokana na Bandari ya Dar es Salaam. Ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wake wa kwamba ule uwekezaji upokelewe na hatimaye matunda sasa tunayaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanayotokana na Bandari yetu ya Dar es Salaam yameongezeka ndani ya mwezi mmoja kutoka shilingi bilioni 850 na sasa yanaenda shilingi trilioni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ujasiri mkubwa na kazi kubwa na maamuzi mazuri ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya. Tunasema ahsante kwa ujasiri wake, nchi yetu inaenda mbele kwa ujasiri ambao yeye ameufanya na sisi tunamuunga mkono na hatuna cha kumlipa zaidi bali tunasema mitano tena kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya niliyoyasema, niseme tu kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Tanzania, Rais anayewapenda Watanzania na anawajali Watanzania. Ninayasema haya kwa ujasiri mkubwa kwa sababu ni sauti iliyotoka Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tarehe 3 Disemba, 2023, tulipata changamoto kidogo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliacha kila kitu chini. Leo hii ninavyoongea hapa Bungeni wale ambao nyumba zao zilienda na maporomoko, wamejengewa nyumba zao, nyumba 109 zimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiache kuwashukuru wenzetu wa Red Cross, tunaye Rais wa Red Cross hapa ndugu yetu Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Kihenzile, alisimamia kwa karibu sana, kati ya nyumba 109 zilizojengwa, 35 zimejengwa na Red Cross. Tunasema ahsanteni sana na hili limewezekana kwa sababu Mheshimiwa Rais ana upendo na anawajali watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanahanang tunasema tunatambua mchango wa Mheshimiwa Rais kwenye maendeleo, tunamtambua Mheshimiwa Rais kwenye mambo ya kuwajali Watanzania wa kawaida na anajali maisha ya Watanzania. Sisi tunasema, tunavyosema mitano tena na sisi tutalipa fadhila, wakati wa uchaguzi mitano yake itakuwa ya mvua ile ya El-Nino. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mheshimiwa Rais kushika nchi, kazi kubwa imefanyika. Kati ya maeneo ambayo Mwenyezi Mungu amenisaidia kutembelea ni Bwawa la Mwalimu Nyerere kati ya miradi ya kimkakati ambayo tunatekeleza ndani ya nchi yetu. Kwa sasa unasikia kila mtu anasema comfortably, kwamba yeyote yule ambaye tunaingia naye mikataba kwa upande wa nishati hatuna wasiwasi, tunaongea nao tukiwa tumetulia, tukiwa na amani wala hatuna haraka kwa sababu Bwawa la Mwalimu Nyerere linaendelea kutuzalishia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea, mashine zote zenye uwezo wa kuzalisha megawatt 2,115 zipo site, Kamati tumeziona. Mashine nne tayari zinafanya kazi, Bwawa la Mwalimu Nyerere matunda yake tunayaona, wale ambao walikuwa wanakebehi sasa aibu ni ya kwao sisi kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu SGR, uwekezaji unaofanyika kwenye eneo la reli ukipanda unaona uko tofauti kweli kweli. Tanzania ya sasa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Tanzania tofauti na Tanzania ya maendeleo ya kuvutia. Ninaomba tu kwenye eneo la reli, sasa ianze kubeba mizigo, sisi tukizalisha ngano, shayiri, katani, mbaazi na dengu kutoka Hanang ifike Dar es Salaam na hatimaye iende duniani kote kwa haraka kwa kutumia reli yetu ya SGR ili tija iweze kuongezeka kwenye eneo hilo. Tukiendelea kusafirisha abiria tu inawezekana tija isiwe kubwa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia kidogo eneo la kilimo, Kipindi hiki sisi wakulima ndiyo tunaenda shambani. Sisi wana-Hanang ardhi yetu ni nzuri inazalisha ngano, shayiri, mbaazi, dengu, ufuta, giligilani na vitunguu. Wakati huu tunavyosikia kwamba ruzuku inayopelekwa, pamoja na fedha ambazo tuliongeza kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni 1.24 ruzuku tuliyopata ni ya mahindi peke yake na haya mazao mengi ambayo tunazalisha nafikiri haitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nami Hanang, Mheshimiwa Bashe, ananitazama, iangalie kwenye eneo la shayiri, ngano, mbaazi na dengu. Tukipeleka nguvu sasa wakati wakulima wanaandaa mashamba yao, tukaweka mkono tukawasaidia, wakati wa masoko tukaanza kuandaa kuanzia sasa. Tunawaambia Stakabadhi Ghalani, twende tukapeleke sasa elimu ya Stakabadhi Ghalani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Stakabadhi Ghalani ni mfumo mzuri ili wakulima wapate tija zaidi, lakini mfumo ule unahitaji elimu na mifumo iliyo imara ya watu kapata fedha. Lengo la Stakabadhi Ghalani ni kwamba mkulima wakati ambapo kuna changamoto ya bei yeye aweze kupata fedha ili asiuze mazao yake kwa hasara. Sasa tupeleke fedha zifike kwenye vijiji na kata ili watu wapate fedha kwa urahisi. Wenzangu wananiambia kwa nini usitumie ule mfumo wa NFRA wa kununua mazao, kirahisi hivyo? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha muda wako umeisha tafadhali.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaamini Mheshimiwa Bashe amenielewa, nimeongea naye mara nyingi hili atalichukua. Ila, Wanahanang wanataka uende ukaongee nao uwape elimu wewe mwenyewe ili tushirikiane kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu muhimu wa Bima ya Afya kwa Wote. Naomba nianze kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Mollel na watumishi wote wa Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, safari hii haikuwa nyepesi. Nilikuwa kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, tulivutana sana. Niwapongeze watu hawa hawakulala muda mwingi, wamepambana ili kufikisha Muswada huu hapa ambapo umefika. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo inafanyika kwenye sekta ya afya. Mmetoa taarifa kwamba, angalau vifo vya akinamama vimepungua, vifo vya watoto chini ya miaka mitano navyo vimepungua. Naamini haya ni matokeo chanya ya uwekezaji ambayo yamefanyika kwenye sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya, kwa kujenga zahanati, kwa kujenga hospitali za Wilaya, kwa kujenga hospitali za rufaa za mikoa, lakini pia kwa kujenga hospitali za kanda.
Mheshimiwa Spika, niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo imefanyika, hasa ndani ya Wizara, lakini nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, nakumbuka maneno yake wakati alipokuja Hanang, alisema yeye afya ni namba moja, elimu, masuala ya maji. Kweli hili tunaliona kwa maboresho ambayo yanafanyika kwenye sekta ya afya. Nampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo inafanyika, lakini pia, Mheshimiwa Waziri na timu yake niwapongeze sana, tulikuwa na mvutano kwenye maeneo kadhaa; moja ilikuwa yale maeneo ya kufungamanisha, hasa kifungu kile cha 32.
Mheshimiwa Spika, sisi tulikuwa tunasema ukifunga leseni za biashara, tunahimiza watu warasimishe biashara, tunahimiza kuongeza base ya walipa kodi lakini ukibana wewe maana yake ni kwamba hayo yote mengine yameshindikana, ina-contradict na mipango mingine ya nchi lakini mmekubali mmeliona hili.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la leseni. tulisema kwamba, suala la leseni ni suala la ajira kwa vijana wetu, ukisema kwamba unaibana kwenye eneo hili ni lazima mtu awe na bima kwanza, unaongeza gharama ya mtu kupata leseni. Sasa, hayo yote mmeyaona nawapongeza sana kwa akili chanya ya kuwasaidia Watanzania ambao walikuwa na changamoto kwenye eneo la afya.
Mheshimiwa Spika, Muswada huu umechelewa, ulikuwa unahitajika jana siyo leo, nawapongeza kwamba tayari angalau tumepiga hatua. Nafahamu kwa sababu mimi nilitoka sekta ya afya, nimekuja mara nyingi kwenye meza zenu kwa ajili ya kuleta malalamiko na namna ya kuwasaidia wananchi wangu. Wengine waliokwama kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao ambao wako hospitalini wanataka msaada wa matibabu kwa sababu gharama zimekuwa kubwa. Hayo yalikuwa ni mengi lakini mara kadhaa mtu amefariki, watu wanalia nyumbani maiti imeshikiliwa hospitali, tungekuwa na mfumo huu wa Bima ya Afya kwa Wote, hizo changamoto tusingezipitia. Ninaamini huu ni mwarobaini na ni wakati sahihi.
Mheshimiwa Spika, niseme maeneo manne tu ambayo mimi napenda nishauri. Eneo la kwanza, kwenye eneo la elimu kwa umma ambalo ndiyo tumeshauriana kwamba ndiyo namna pekee ambayo tunaweza kuwasajili watu wengi, wajisajili kwa hiari bila kusukumana, bila Polisi, bila kukamatana.
Mheshimiwa Spika, tutumie mifumo ya kawaida ya kijamii, kwa sababu suala la afya ni suala la kijamii. Mtu akipata changamoto jamii inahusika. Kwenye utaratibu wetu wa kawaida wa maisha, maeneo mengi ukitoa mijini kidogo kuna utaratibu tofauti lakini sisi tunaotoka vijiini, kuna wale Wenyeviti wanaoshughulika na masuala ya kijamii sherehe, magonjwa, misiba. Tuwashirikishe wale ili angalau hili jambo la Bima ya Afya kwa Wote, liwe jambo la jamii badala ya kuwa jambo la Serikali. Tukitumia mfumo wetu wa kawaida ule wa elimu kwa umma, tutatumia TV na mifumo mingine, tunashusha kutoka juu kupeleka chini. Hii itakuwa ngumu kwa watu kuipokea. Tuanzie kule kwenye grassroots tupande juu, hii elimu itaenda kwa urahisi. Hilo ni eneo la kwanza ambalo mimi nataka nichangie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la kuwatumia watumishi wetu sawa sawa ili watu waweze kutumia huduma za afya kwenye taasisi za Serikali, vituo vya afya vya Serikali, zahanati na hospitali za Serikali. Tuangalie namna ya kuwatumia wataalam wetu vizuri. Kama wataalam hawa ambao tunao kwenye sekta ya umma ndiyo wanaokwenda kufanya kazi sekta binafsi, tuangalie mechanism kuhakikisha kwamba yale wanayofuata sekta binafsi, wanayapata kwenye sekta ya umma. Kwa sababu, mwishoni aliyehudumiwa kwenye sekta ya umma na anaehudumiwa kwenye sekta binafasi au kwenye hospitali binafsi, wote wana mfumo wa malipo sawa sawa.
Mhehimiwa Spika, kama kule wanaweza, Serikali inashindwa nini? Hebu tuboreshe, tuangalie kama kuna incentives zinazotakiwa, siyo kila wakati tu utaratibu, utaratibu, utaratibu, hii itatukwamisha. Tutafute namna ya kutoa incentives kwa watumishi. Badala ya kwenda kutumia muda wake kwenye sekta au hospitali binafsi, tuangalie namna ambavyo tunaweza kum-accommodate kwenye hospitali ya Serikali akafanya kazi ile. Wale wanaozalisha, kwa maana ya wale ambao ni productive, tuone namna ya kuwapa tuzo (incentives) ili hatimaye huduma za afya ziwe nzuri kwenye sekta ya umma.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la bima za magari, namna ambavyo inaweza ikatibu watu wambao wanapata ajali. Tuna vijana wetu wengi, vijana wa bodaboda wanapata ajali sana kwa sababu ya aina ya vyombo wanavyovitumia. Tunapata ajali za magari na hii niseme tu nakushukuru sana, ulinipa nafasi ya kwenda kujifunza Ghana. Wenzetu wanatumia eneo hili la bima kama chanzo cha mapato ya bima. Kwa sababu, vyombo vya moto ni kweli wanalipia bima, sasa, badala ya mtu amepata ajali unahangaika namna gani anaweza kupata matibabu, wakati huo ambapo tunahangaika hangaika, hebu litumieni hili eneo ili tuhakikishe kwamba, wale amabao wanapata changamoto za ajali, mtu amevunjika badala ya kuhangaika.
Mheshimiwa Spika, natoa mfano wa Jimboni kwangu, kwa sababu ya mifumo tu migumu wanaenda kutibiwa kienyeji, wakati mwingine wanapata hasara kweli kweli, wanaumia. Hebu tutengeneze mfumo ambao utaunganisha bima za vyombo vya moto na hii bima ya afya.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo mimi nataka nichangie jioni hii ya leo, ni upande wa teknolojia. Serikali imewekeza fedha nyingi sana kwenye vifaa na vifaatiba. Sasa, teknolojia hizi nyingi zinatoka nje ya nchi, kwa sababu teknolojia zinatoka nje ya nchi, tunao wataalam ambao tayari tuweshawafundisha nchini lakini si wateknolojia mahsusi. Ili tuboreshe huduma kwenye maeneo yetu hasa sekta za umma, maana yake hospitali zetu, tuone namna ya kuhakikisha kwamba zile technology transfer zinafanyika ipasavyo. Pia kunakuwa na training proper ya vifaa tunavyovinunua kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kuna maboresho mengi sana yamefanyika kwenye upande wa teknolojia-tiba lakini bado haitoshi kwa sababu, kila wakati teknolojia inabadilika. Serikali iweke mpango mahsusi wa manunuzi ya teknolojia lakini wa mafunzo ya wataalam wa vifaa na vifaatiba. Hii itatusaidia kwamba, vifaa tutakavyovinunua vitatumika sawa sawa na hatimaye vitaleta tija ambayo tunaitarajia.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niseme tu Mheshimiwa Waziri, pamoja na pongezi zangu zile za mwanzo, hiki ndicho tulikuwa tunakisubiri. Imefika wakati muafaka, ninaamini changamoto tulizokuwa tunazipata kwenye maeneo yetu kwamba, kwenye upande wa wazee kila mkutano unaokwenda Mheshimiwa Mbunge, bwana hili la wazee halieleweki. Ninaamini tukiwa na bima ya afya kwa wote itaeleweka.
Mheshimiwa Spika, akina mama wajawazito hilo nalo litaeleweka na ninaamini pia, matibabu ya watoto chini ya miaka mitano hili nalo litakaa sawa. Ninachoomba tu Mheshimiwa Waziri, utekelezaji uanze mapema. Tuanze taratibu, hakuna kinachoshindikana. Tukianza ndiyo tutajua sehemu gani ambako kuna mashimo na hatimaye mashimo haya tuyazibe.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana kwa nafasi. Ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)