Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Daniel Baran Sillo (38 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Polisi katika Kata za Berege na Ng’hambi Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Berege imetenga eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 1011.5 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata. Ujenzi wa kituo hicho umeshaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Kata 647 vitakavyojengwa nchi nzima kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kata ya Ng’hambi bado haijatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Ng’hambi na kata nyingine zisizokuwa na Vituo vya Polisi vya Kata, ahsante. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMED K.n.y. MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa makosa ya kimtandao (cyber crime) ili yasitokee nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, uhalifu wa makosa ya mtandaoni unasimamiwa na Sheria Na. 14 ya Mwaka 2015 na ndiyo Sheria inayodhibiti makosa haya. Sheria inaelekeza matumizi sahihi ya mtandao na imeainisha adhabu kwa makosa ya matumizi mabaya ya mtandao. Serikali katika kuimarisha udhibiti wa makosa ya mtandaoni imeanzisha mkakati wa Taifa wa udhibiti wa usalama mtandaoni wa kuanzia mwaka 2022 – 2027.

Mheshimiwa Spika, mkakati huu utawatumia wataalam mbalimbali katika kuratibu ugunduzi, kuzuia, kukataza, kufanya uchunguzi wa majibu na kuandaa mashitaka ya uhalifu. Pia, kuimarisha mazingira ya matumizi ya mtandao na kuboresha sheria iliyopo, kulinda huduma muhimu za habari, kuendeleza ujuzi kwa wafanyakazi na usalama mtandaoni, kutoa elimu kwa wadau na kuweka ushirikiano wa Serikali, wafanyabiashara na watu binafsi ili kudhibiti matukio ya uhalifu mtandaoni, ahsante.
MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Nyumba za Askari wa Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imekamilisha taratibu za kufunga mikataba ili kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi sanjari na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Uhamiaji Wilaya Micheweni. Gharama ya utekelezaji wa mradi huu ni kiasi cha shilingi 2,695,937,724.80, ikijumuisha gharama za mkandarasi kiasi cha shilingi 2,549,937,724.80 na mshauri elekezi kiasi cha shilingi 146,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilisha taratibu za ununuzi, tayari Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi 1,250,000,000 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu. Aidha, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake, ahsante sana.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, lini vyombo vya usafiri vilivyosajiliwa Zanzibar vitatambuliwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo katika hatua ya Marekebisho ya kifungu cha nane cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, ambacho kinazungumzia usajili wa vyombo vya moto hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mapendekezo haya yatawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nduguti kwa kuwa ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Nduguti ni Kituo cha Wilaya ya Mkalama kilichoanza kujengwa mnamo mwaka 2015 na kukamilika mwaka 2023 na kuzinduliwa na kwa sasa kinahudumia wananchi wa Mkalama, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali wa kuipatia gari la Zimamoto Wilaya ya Liwale ili kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha na kuliboresha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha taratibu zote za mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani milioni 100 kutoka Taasisi ya Abu Dhabi Export Credit Agency iliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya kupata vitendea kazi mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa magari 150 ya zimamoto na uokoaji yatakayosambazwa kwa nchi nzima, ikiwemo Wilaya ya Liwale.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya kuboresha Sheria za Jeshi la Magereza ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Magereza sura 58 iliyorejewa mwaka 2002 ili ziweze kuendana na wakati, ambapo kwa sasa upo katika hatua ya kukusanya maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Muswada wa sheria hii utawasilishwa Bungeni mara tu baada ya taratibu kukamilika, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya kuboresha Sheria za Jeshi la Magereza ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inaendelea na mchakato wa maboresho ya Sheria ya Magereza sura 58 iliyorejewa mwaka 2002 ili ziweze kuendana na wakati, ambapo kwa sasa upo katika hatua ya kukusanya maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Muswada wa sheria hii utawasilishwa Bungeni mara tu baada ya taratibu kukamilika, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Polisi Tarafa ya Igurubi - Igunga utakamilika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Igurubi ulianza mwaka 2018 kwa kushirikisha nguvu za wananchi na ulisimama mwaka 2020 baada ya kukosa fedha. Tathmini kwa ajili ya kumaliza ujenzi ili kuunga mkono jitihada za wananchi imeshafanyika ambapo kiasi cha fedha shilingi 53,000,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi ya Polisi ya Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilolo na uko kwenye hatua ya umaliziaji. Mnamo tarehe 7 Februari, 2024 Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 400, kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa wananchi wanaochukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo Mwaka 2022, Kifungu cha 258 na 265, ni kosa Kisheria kuchukua mali ya mtu mwingine bila idhini ya mwenye mali ama kuwa na dai la haki. Hivyo, kitendo cha kuchukua mafuta baada ya magari ya kubeba mafuta kupata ajali, bila kuruhusiwa na mwenye mali, ni kutenda kosa la wizi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kuwachukulia hatua za Kisheria wahalifu wote waliokamatwa kwa kosa hilo na kuwafikisha Mahakamani. Ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini Serikali itahamisha Gereza la Kihesa Mgagao ili kubadili matumizi kama yalivyo maeneo mengine yaliyokuwa Makambi ya Wakimbizi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza itaanza kuchukua hatua za awali zikiwemo za kupima upya eneo la Magereza kwa kutenganisha eneo kwa ajili ya shule ya sekondari na gereza la Mgagao, ambapo majengo yanayotumika kama gereza yatabaki kutumika kama shule ya sekondari na gereza litajengwa katika sehemu nyingine itakayotengwa. Aidha, Serikali itatenga fedha baada ya kumaliza kupima kwa ajili ya ujenzi wa Gereza la Mgagao, ili kupisha majengo yaliyokuwa makambi ya wakimbizi. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kudhibiti wimbi la Wahamiaji haramu katika Mipaka ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali katika kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu katika mipaka ya nchi ni kuimarisha doria na misako katika maeneo ya mipaka, kufanya kaguzi kwenye vizuizi mbalimbali katika barabara kuu zinazounganisha mikoa kwa mikoa, kuendesha operesheni za kuwabaini wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria, kuimarisha Mfumo wa Kielektroniki wa Mipaka (e-border) ambao unasaidia kudhibiti wageni wasio na sifa kabla hawajaingia nchini na tunaendelea kufanya vikao vya kimataifa, kikanda na ujirani mwema, kwa lengo la kupanga mipango ya pamoja ya kudhibiti uhamiaji haramu na matukio mengine ya kihalifu yanayovuka mipaka, ahsante.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -

Je, sababu gani zinazosababisha Wananchi ambao wamepatiwa Visa kwenda nje ya nchi kutosafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwaruhusu wananchi kwenda nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali baada ya kukamilisha taratibu zote za kuondoka nchini. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakizuiliwa kuondoka nchini kutokana na sababu kadha wa kadha ikiwemo sababu za kiusalama kutokana na mazuio yanayowekwa na taasisi za kiusalama, kuwa na Visa isiyo halali, kuwepo viashiria vya uhusika katika usafirishaji haramu wa binadamu hasa watoto wadogo na wanawake, kwa wale wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Kazi na Ajira na mwisho ni kutokufuatwa kwa taratibu za kusafiri nje ya nchi kwa watumishi wa umma, ahsante.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka magari Vituo vya Polisi Kisaki na Mvuha ili kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji na kulinda raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Kisaki kina gari moja PT 4770 Ashok Leyland na Kituo cha Polisi cha Mvuha hakina gari kwa sasa na kinahudumiwa na Kituo Kikuu cha Wilaya pamoja na Kisaki. Katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imenunua magari 122 kwa ajili ya Wakuu wa Polisi wa Wilaya na magari hayo yanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa. Katika mgao wa magari hayo Wilaya ya Morogoro imetengewa gari ambalo pia litatumika kudhibiti uhalifu maeneo ya Tarafa ya Mvuha. Serikali itaendelea kutenga fedha toka kwenye bajeti yake kila mwaka kwa ajili ya kununulia vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwemo magari ili kudhibiti uhalifu. Ahsante.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati nyumba za makazi ya Polisi zilizopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 100,000,000 kutoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa ajili ya kufanya ukarabati nyumba ya makazi ya Askari Polisi ya familia 12. Aidha, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba nane za makazi ya kuishi familia 32 za askari Polisi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 416,000,000 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ukarabati zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali na Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Je, polisi kujigeuza kuwa Mahakama siyo kuvunja sheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Majukumu ya Jeshi la Polisi yameainishwa kwenye Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Na. 322 kifungu cha 5, inayoeleza ni kulinda amani, kudumisha sheria, amri na utulivu, kuzuia na kugundua uhalifu, kukamata na kuwalinda watuhumiwa na kulinda mali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa matakwa ya sheria, Jeshi la Polisi hupokea malalamiko, hufanya uchunguzi na upelelezi, hukamata wahalifu na kisha jalada la kesi hupelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua ya kwenda Mahakamani. Hivyo, Jeshi la Polisi halifanyi kazi za Mahakama isipokuwa hushirikiana na Mahakama katika kutekeleza matakwa ya kisheria kama kusimamia amri za Mahakama. Nashukuru.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, ni nchi ngapi ambazo wananchi wake lazima wapate VISA rejea kuingia nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 Rejeo la Mwaka 2016, ikisomwa pamoja na Kanuni za Uhamiaji za VISA za mwaka 2016 pamoja na marekebisho yake, Jedwali la Nne la Kanuni hizo limeorodhesha nchi ambazo raia wake wanapaswa kupata idhini ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (Visa Rejea) pindi wanapotaka kuja nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni hizo, kwa sasa ni nchi 27 ndizo wananchi wake wanapaswa kufuata utaratibu wa VISA Rejea kabla ya kuja nchini, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -

Je, nini sababu ya ucheleweshaji wa maombi ya usajili wa taasisi za kidini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kupewa usajili wa kudumu, taasisi na madhehebu ya dini huwekwa katika kipindi cha matazamio ili kubaini kama taasisi au dhehebu husika lina dosari yoyote kwa jamii. Hata hivyo, zipo sababu nyingine ambazo huweza kupelekea baadhi ya taasisi na madhehebu ya dini kuchukua muda mrefu kusajiliwa ambazo ni pamoja na kushindwa kutekeleza maelekezo yanayohusu usajili yanayotolewa na Ofisi ya Msajili kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia ofisi ya Msajili wa Jumuiya inaendelea kushughulikia maombi ya usajili wa taasisi na madhehebu ya dini na kutoa usajili kwa wakati kwa taasisi zenye sifa stahiki, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Vituo vya Polisi vilivyoanza kujengwa Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa una Vituo vya Polisi vya Kata vinavyojengwa kwa kutumia nguvu za wananchi, ambavyo ni Kate, Kambo, Milepa, Ilemba na Kirando. Tathmini kwa ajili ya kumalizia ujenzi imefanyika na kiasi cha fedha shilingi 311,000,000/= kinahitajika.

Mheshimiwa Spika, ili kuunga mkono jitihada za wananchi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeviingiza vituo hivyo kwenye mpango wa kumaliza ujenzi wa maboma 77 ya Vituo vya Polisi vya Kata kuanzia mwaka wa fedha wa Bajeti ya Serikali 2024/2025.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka magari Vituo vya Polisi Kisaki na Mvuha ili kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji na kulinda raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Kisaki kina gari moja PT 4770 Ashok Leyland na Kituo cha Polisi cha Mvuha hakina gari kwa sasa na kinahudumiwa na Kituo Kikuu cha Wilaya pamoja na Kisaki. Katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imenunua magari 122 kwa ajili ya Wakuu wa Polisi wa Wilaya na magari hayo yanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa. Katika mgao wa magari hayo Wilaya ya Morogoro imetengewa gari ambalo pia litatumika kudhibiti uhalifu maeneo ya Tarafa ya Mvuha. Serikali itaendelea kutenga fedha toka kwenye bajeti yake kila mwaka kwa ajili ya kununulia vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwemo magari ili kudhibiti uhalifu. Ahsante.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati nyumba za makazi ya Polisi zilizopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 100,000,000 kutoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwa ajili ya kufanya ukarabati nyumba ya makazi ya Askari Polisi ya familia 12. Aidha, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba nane za makazi ya kuishi familia 32 za askari Polisi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 416,000,000 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ukarabati zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali na Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipatia vitendea kazi kama magari, majengo na shajara Wilaya ya Kipolisi ya Mlandizi, Jimbo la Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa spika, Serikali inatambua uhaba wa majengo ya ofisi, vitendea kazi na nyumba za makazi ya askari katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi. Tathmini kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za uchunguzi wa kisayansi, intelijensia na upelelezi imeshakamilika na fedha kiasi cha shilingi 82,000,000 zinahitajika. Pia, kiasi cha fedha shilingi 232,590,000 zinahitajika, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba mbili za makazi ya askari za familia sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zote hizo kiasi cha jumla ya shilingi 314,590,000 zimetengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2024/2025. Kwa sasa kituo cha Polisi Mlandizi kina gari moja na pikipiki mbili, pindi magari 122 yaliyoagizwa na Serikali, kwa ajili ya Wakuu wa Polisi wa Wilaya yatakapowasili, Kituo cha Polisi Mlandizi pia, kitapatiwa gari. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti wahalifu wanaovamia wavuvi wakiwa ziwani na kuwanyang’anya mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa spika, wajibu wa Serikali ni kulinda maisha ya watu na mali zao. Katika kudhibiti uhalifu wanaofanyiwa wavuvi wakiwa ziwani, Serikali kupitia Jeshi la Polisi kikosi cha wanamaji hufanya doria kwa kutumia boti na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limewashirikisha wavuvi na vikundi vya Ulinzi na utunzaji wa mazingira ya fukwe kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kudhibiti na kupata…

SPIKA: Mheshimiwa sogea huku ili mnapozungumza mtumie sauti kidogo. Simama, sogea pale alipo ama Mheshimiwa Waziri aje aketi nawe hapo, itarahisisha kidogo.

Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze upya.

Mheshimiwa spika, wajibu wa Serikali ni kulinda maisha ya watu na mali zao. Katika kudhibiti uhalifu wanaofanyiwa wavuvi wakiwa ziwani, Serikali kupitia Jeshi la Polisi kikosi cha wanamaji hufanya doria kwa kutumia boti na kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limewashirikisha wavuvi na vikundi vya Ulinzi na utunzaji wa mazingira ya fukwe kuanzisha vikundi vya Ulinzi shirikishi ili kudhibiti na kupata taarifa za wahalifu wa ziwani. Serikali katika kuhakikisha matukio ya uhalifu unaovuka mipaka ziwani haufanyiki, imeweka utaratibu wa kufanya mikutano ya ujirani mwema kwa mikoa jirani ya nchi zinazotumia ziwa ili kudhibiti uhalifu huo na kupambana na vikundi vya uhalifu, ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -

Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Gereza la Rusumo na Wananchi wa Kijiji cha Rusumo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa spika, Gereza kilimo Rusumo lipo Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera lenye ukubwa wa ekari 9,442.9. Gereza hilo limepimwa na kupata Hati Na.5548 katika mwaka 2023.

Mheshiwa spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inatambua changamoto ya uhitaji wa ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Rusumo na kilichopo ni wananchi kudai majira ya nukta za upimaji ya Gereza Rusumo uliofanywa na Halmashauri ya Wilaya Ngara uliopitiliza hadi kwenye barabara na maeneo ya Hifadhi ya Mto Kagera. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeendelea kuchukua hatua mbalimbali vikiwemo vikao vya ujirani mwema na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kushughulikia changamoto hiyo, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -

Je, lini Muswada wa Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi utaletwa Bungeni kwa kuwa kampuni binafsi za ulinzi zilianzishwa bila sheria wala kanuni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI ajliibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria inayosimamia kampuni binafsi za ulinzi. Maoni ya wadau wa pande zote mbili za Muungano yamepokelewa na yanafanyiwa kazi kwa kina na mara yatakapokamilishwa muswada wa sheria utawasilishwa Bungeni, ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Jimbo la Kilindi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishatenga fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilindi kutoka kwenye bajeti ya Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Kiasi cha fedha shilingi milioni 800 zitatumika katika kukamilisha ujenzi huo. Maandalizi ya ujenzi yanaendelea na kiasi cha fedha shilingi milioni 400 zimekwishakutolewa, ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi pamoja na kukarabati zilizopo mkoani Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mbeya una mahitaji ya nyumba za makazi ya kuishi Askari Polisi 1,045 na nyumba zilizopo ni 186 na ni chakavu. Tathmini kwa ajili ya kubaini uchakavu na kuzifanyia ukarabati nyumba hizo zilizopo imefanyika na kiasi cha fedha shilingi 3,523,078,000 kinahitajika. Aidha, kiasi cha fedha shilingi 51,760,000,000 zinahitajika kujengea nyumba za makazi ya Askari ili kukidhi mahitaji ya mkoa. Serikali itaanza kutenga fedha kiasi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. MWATUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuongeza kasi ya ujenzi wa Vituo vya Polisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga Vituo vya Polisi nchi nzima ili kutoa huduma ya ulinzi kwa wananchi. Utekelezaji wa mpango wa ujenzi unategemea fedha zinazotengwa kutoka kwenye bajeti ya Serikali kila mwaka, toka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo pamoja na michango ya kujitolea ya wananchi na wadau mbalimbali. Hadi sasa Serikali imeshajenga vituo vya Polisi Daraja A, B na C 487 na vituo vidogo vya Kata/Shehia 667 nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza kasi ya ujenzi wa Vituo vya Polisi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga kituo cha Polisi Kijiji cha Ashengai Kata ya Karansi – Siha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Karansi imeshatenga eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,023 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ambacho kitajengwa kwenye Kijiji cha Ashengai. Ujenzi wa kituo hicho umeshaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa vituo vya Polisi vya Kata vitakavyojengwa kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ahsante.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, lini Jeshi la Zimamoto Halmashauri ya Mji Korogwe litapatiwa Gari la Zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, Serikali imeshakamilisha taratibu zote za mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani milioni 100 kutoka Taasisi ya ADEX iliyopo Umoja wa Nchi za Kiarabu, kwa ajili ya kupata vitendea kazi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa magari 150 ya Zimamoto na Uokoaji pamoja na vifaa kwa nchi nzima ikiwemo pia Wilaya ya Korogwe, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS K.n.y. MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la makazi ya askari Kituo cha Polisi Mkokotoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeshatenga eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,500 ambalo litatumika kujengwa maghorofa sita yatakayoishi jumla ya familia 24 za askari polisi. Fedha kwa ajili ya ujenzi huo zinatarajiwa kuanza kutengwa kwenye bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kubadilisha sheria ya mwendo wa magari kutoka kilometa 80 hadi kufikia kilometa 100 kwa saa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya Mwaka 1973 iliyorejewa Mwaka 2002, Kifungu cha 51(8) inayoelekeza matumizi ya mwendokasi wa kilomita 50 kwa saa na mwendokasi wa kilomita 80 kwa saa, bado ni sahihi ukizingatia aina ya barabara tulizonazo nchini kwa sasa. Aidha, Wakala wa Ujenzi wa Barabara wakiboresha barabara na madereva wakielimishwa ipasavyo kuheshimu sheria za usalama barabarani, maboresho ya sheria yanaweza kufanyika na kufikia kilomita 100 kwa saa. Ahsante.
MHE. KHAMIS YUSSUF MUSSA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati Kituo cha Polisi Ng’ambo, Kwahani kwa kuwa ni chakavu na cha muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Ng’ambo – Kwahani ni kituo cha Daraja B na jengo lake ni la siku nyingi na ni chakavu. Tathmini kwa ajili ya kufanya ukarabati imefanyika na kiasi cha fedha shilingi 109,582,820 kinahitajika. Fedha hizo zinatarajia kutengwa toka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Mdabulo Mufindi wanaojenga Kituo cha Polisi kwa nguvu zao wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeshafanya tathmini kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la Kituo cha Polisi Mdabulo ili kuunga mkono nguvu za wananchi ambao umefikia kwenye hatua ya lenta na kiasi cha fedha shilingi 56,000,000 kinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa toka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Raia wa Kigeni hawashiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 na kanuni zake za mwaka 2024, raia wa Tanzania ndio wenye haki ya kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kwa kupiga kura au kuchaguliwa kuwa Viongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusimamia vipindi vyote wakati wa uchaguzi, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya uraia kwa watendaji (waandikishaji na wasimamizi wa uchaguzi) ili kuhakikisha raia wa Tanzania wenye sifa ndio wanaoshiriki katika chaguzi na sio raia wa kigeni. Aidha, inapobainika kwamba kuna mtu anadiriki kujiandikisha ama kutafuta fursa ya kugombea na zipo taarifa au tuhuma, kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi, mhusika huyo huwekewa pingamizi na ikithibitika mtu huyo huchukuliwa hatua za kisheria ikiwepo kuondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura sanjari na kufikishwa Mahakamani, ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia ya shilingi 236,000,000 kwa wananchi wanaopisha ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua madai ya Shilingi 235,271,532.30 kama fidia ya wananchi 31 wa Kijiji cha Busengwa, Kata ya Kharuma, kwa ajili ya kupisha eneo la ujenzi wa Gereza la Wilaya Nyang’hwale. Madai haya hayakuingizwa kwenye Mpango wa Bajeti wa mwaka 2024/2025 kutokana na kutokamilika kwa daftari la orodha ya wanufaika kwa wakati na badala yake fedha hiyo itaingizwa katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi husika kama mapendekezo ya taarifa ya Mthamini Mteule yalivyowasilishwa, ahsante sana.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kuwapa Vitambulisho vya Taifa wafungwa pamoja na mahabusu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kusajili na kutambua watu waliopo katika makundi maalum ikiwemo wafungwa na mahabusu ni kupitia maombi maalum kutoka kwa Wakuu wa Gereza katika wilaya husika. Uratibu wa usajili wa makundi hayo unafanywa na NIDA kupitia Wakuu wa Magereza na Maafisa Usajili wa Wilaya husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wafungwa na mahabusu wamekwisha kusajiliwa walipokuwa uraiani kabla ya vifungo vyao, Serikali kupitia NIDA ipo tayari kufanya usajili na utambuzi kwa watu wote waliokidhi vigezo ikiwemo wafungwa na mahabusu kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza. Ahsante.