Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Daniel Baran Sillo (92 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, utaratibu wa kuwa na Polisi Kata kila kata umesaidia kupunguza uhalifu katika maeneo mengi. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya Polisi Kata angalau kufikia wawili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni nini mkakati wa Serikali kuwapatia vitendea kazi Polisi Kata, kwa mfano pikipiki, ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Malima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali imeendelea kuajiri Askari wa Jeshi la Polisi, na jinsi bajeti itakavyoruhusu. basi tutaendelea kuajiri askari wa kutosha na hatimaye kuwafikisha walau wapatikane wawili kwenye kila kata kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mahitaji ya pikipiki kwa nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ni pikipiki 4,434 na kwa awamu ya kwanza tayari Serikali imeshasambaza pikipiki 105 kwa maana ya pikipiki 95 upande wa Tanzania Bara na pikipiki 10 kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi bajeti itakavyoruhusu, tutaendelea kununua pikipiki kwa awamu ili kuhakikisha zinafika kwenye kata zetu, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi wetu. Ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina ushauri mdogo tu kwa Serikali. Kwa vile haya makosa ya uhalifu mitandaoni yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, ninaishauri Serikali ijaribu kukiwezesha Kitengo hiki cha Cyber, ili kiwe na mfumo mzuri wa kufanya kazi zake kwa wepesi pamoja na kujaribu kurekebisha baadhi ya sheria ambazo zimekuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri na tutaufanyia kazi, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama shida iliyopo Micheweni Wilaya ya Rungwe pia ina tatizo kama hilo la wafanyakazi wa uhamiaji kutokuwa na makazi ya kudumu ya wafanyakazi wale. Ni lini Serikali itapeleka fedha ili kuwasaidia Askari wale na siyo tu wa Uhamiaji, hata Askari Polisi kwani nyumba zao zimechakaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Askari wake wote wa Uhamiaji na Askari wote wanakaa makazi yaliyo bora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jinsi fedha itakavyopatikana, tutatenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi kwa ajili ya askari wa Wilaya ya Rungwe, ahsante sana.
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchakavu wa nyumba za Polisi zilizopo Finya, Basra maeneo ya Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, nia ya dhati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Askari wake wote; Askari wa Uhamiaji na Askari Polisi, wote wanakaa kwenye makazi ambayo ni bora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jinsi fedha zinavyopatikana, tutatenga fedha awamu kwa awamu kuhakikisha Wilaya ya Wete pia inapata ukarabati wa nyumba za Askari wetu.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kazi gani zimefanyika kwenye shilingi 1,250,000,000 ambazo Serikali imepeleka kwenye Wilaya ya Micheweni kama jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri linavyosema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu, pengine Mheshimiwa Mbunge hajasikia vizuri, ni kwamba katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 baada ya kusaini mkataba huu sasa, itaanza kazi ya ujenzi wa nyumba za makazi za askari hawa wa Uhamiaji. Kwa hiyo, kiasi hicho kilichotengwa cha shilingi 1,250,000,000 kitaanza utekelezaji wake mara baada ya kusaini mkataba.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu hili sasa naliuliza kwa mara ya tatu na Serikali inaahidi, lakini hakuna kinachofanyika. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba, wananchi wamefanya kila juhudi kuweza kujenga boma na limefikia kwenye lintel, lakini tayari kuna maboma sita pale kwa ajili ya Askari: Je, ni lini watakamilisha kazi hii ili kituo kile kianze kufanya kazi na tayari kuna nyumba sita ambazo zina Askari, lakini wanakwenda mbali na kituo hakijaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza wananchi wa Jimbo la Ilemela kwa kazi kubwa walioifanya ya ujenzi wa maboma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ambayo wananchi walishaianza, Serikali inaunga mkono na nitapata fursa ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hicho niweze kuzungumza naye kuona namna bora ya kumalizia maboma haya ambayo tayari wananchi wameshayajenga.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu hatuna kabisa nyumba za Askari; Askari Polisi pamoja na Askari wa Uhamiaji. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Minza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba askari wetu wote wanakaa kwenye makazi bora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kwenye mwaka huu wa fedha, kama Mkoa wa Simiyu hauna kituo kabisa, basi tuangalie kwenye mwaka wa fedha unaokuja ili kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Polisi pamoja na Uhamiaji. Nakushukuru sana.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria hii ili kuweza kufanya vyombo vya usafiri kutambulika hapa Tanzania Bara umeonekana umechukua muda mrefu sana, sasa ni kwa nini Serikali haioni haja ya kuweka mwongozo maalumu kipindi hiki wakati tunasubiria mabadiliko ya sheria hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bakar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zipo katika mazungumzo, naomba tuwe na subira na utaratibu uliopo kwa sasa uendelee kutumika. Pale mazungumzo yatakapokamilika, basi marekebisho yatafanyika ili kuhakikisha kwamba vyombo vinasajiliwa kwa pamoja.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba sasa kituo kimeanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo Kidogo cha Polisi cha Ilunda wanafanya kazi zao kwenye kibweni kidogo cha vyumba viwili, Kituo Kidogo cha Polisi Ibaga, wanafanya kazi kwenye Ofisi ya Kijiji, Kituo Kidogo cha Polisi Mwangeza wanafanya kwenye Ofisi ya Kata. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo hivi vidogo ili wenye ofisi zao waendelee na kazi zao kwa sababu wanalalamika sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, polisi wetu ukienda kusikilizwa kesi wanaandika kwenye vikaratasi vya ajabu ajabu tena wanageuza kuangalia mahali ambapo hakuna maandishi. Ni lini Serikali itaanza kusikiliza mambo yetu kwa kutumia TEHAMA ili kuokoa kazi ambazo polisi wetu wanahangaika nazo sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri wa vituo vya polisi kama alivyotaja. Ni maagizo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa vituo vya polisi vya kata nchi nzima na Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeanza mkakati wa kujenga vituo vya afya vya kata nchi nzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge vituo vyako vitatu ulivyovitaja vilivyoko Wilaya ya Mkalama vitaingia kwenye mpango tayari kwa kujengwa katika utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la matumizi ya TEHAMA, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imekwishaanza matumizi ya TEHAMA kwa Jeshi la Polisi na mwezi uliopita tulizindua hapa Kituo cha Polisi cha Mtumba ambacho tayari kinatumia TEHAMA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia jambo hili litafika Mkoa wa Singida hadi Wilaya ya Mkalama kama ambavyo ameuliza, ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilianzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika mpaka sasa bado ujenzi hatujapata nguvu yoyote kutoka Serikalini na Serikali iliahidi kutupatia fedha za kuendeleza huo ujenzi.

Je, ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze wananchi wa jimbo lake kwa kazi waliyoifanya ya kujenga kituo cha polisi mpaka hatua hiyo waliyofikia. Nimhakikishie kwamba Serikali itaunga mkono wananchi hawa na itatoa fedha ili kumalizia Kituo cha Polisi cha Tanganyika.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya ujenzi wa kituo cha polisi katika Kata ya Mchinga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema nia ya Serikali ni kuhakikisha vituo vya polisi vyote vinakamilika na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo chake cha Mchinga tutazungumza naye ili tuone namna ya kukikamilisha ili kupata huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi wake.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Bassotu, Wilaya ya Hanang umekuwa ni wa muda mrefu sana. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Bassotu kimetengewa fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuweza kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi wa Bassotu na Wilaya ya Hanang kwa ujumla.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ya kutujengea vituo vya polisi, lakini Kituo cha Polisi Chang’ombe ni cha Kimkoa wa Kipolisi Dar es Salaam. Je, Serikali mna mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi cha Tandika ndani ya Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea maombi ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Tandika kama alivyosema na tuweke kwenye mpango na kutengewa fedha ili tuweze kujenga kituo cha polisi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi wa Temeke.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona, wananchi wa Kata ya Kasharunga katika Kijiji cha Kasharunga katika Wilaya ya Muleba wamejenga Kituo Kidogo cha Polisi na kimekamilika. Ni lini Serikali itafungua kituo hicho kwa kupeleka askari ili wananchi waweze kupata huduma waliyoihitaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa Rwamlaza, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo na nimhakikishie kwamba tuko tayari kwenda kufungua wakati wowote hata baada ya Bunge la Bajeti na tutaleta askari tayari kwa kutoa huduma katika eneo hilo.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi, Mbarali, Kyela, Chunya na Mbeya DC, askari polisi hawana nyumba za kuishi, wao wanaishi uraiani yaani wamepanga. Je, ni lini Serikali itawajengea nyumba askari polisi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Suma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga nyumba za polisi katika maeneo mbalimbali kwa awamu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika maeneo ambayo ameyataja katika Wilaya ya Chunya, Mbarali na maeneo mengine tutatenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za polisi katika maeneo hayo.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Kata ya Mkiwa tumeanza ujenzi wa Kituo Kidogo cha Polisi ambacho ni kituo cha kimkakati. Mimi kama Mbunge nimechangia shilingi milioni tano kutoka katika mfuko wa jimbo na wananchi wameji-organize na wadau. Ni lini Serikali itatuunga mkono ili kumalizia kituo hicho kwa ajili ya usalama wa wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtaturu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga shiliongi bilioni 3.8 kwa ajili ya kumalizia maboma yote 77 yaliyojengwa na wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baadaye tuonane pengine kituo chake alichokitaja kiko kwenye maboma haya 77 ili tuweze kukimalizia katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni upi mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha kisasa katika Mji wa Tunduma ili kiendane na mahitaji hasa ukizingatia ni lango kuu la SADC?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana population kubwa, lakini pia yana maeneo makubwa ya biashara kama Tunduma, yanakuwa na vituo vya polisi vya uhakika ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge eneo hilo pia tumelichukua, tulipange kwenye mpango, ili tuweze kujenga kituo cha polisi cha kisasa kama ambavyo ameomba Mheshimiwa Mbunge.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri, Kata ya Masumbwe tayari tuna eneo la kituo cha polisi, lakini pia mimi kama Mbunge kule Lulembela nimetoa shilingi milioni tatu, Gilorwanguru nimetoa mifuko 100 kwenye kituo cha polisi. Je, ni lini Serikali Kuu mtatupa support Mbogwe kuweza kukamilisha vituo hivi vya polisi vilivyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye baadhi ya majibu ni kwamba Serikali imetenga fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kumalizia maboma yote ambayo wananchi wameshaanza kujenga, yapo maboma 77. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuonane baadae pengine kituo chako pia kama kipo kwenye vile 77 kitatengewa fedha ili kumalizia kazi kubwa waliyofanya wananchi wa Mbogwe, ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale pamoja na kwamba haina Kituo cha Polisi cha Wilaya chenye hadhi, lakini kuna uhitaji mkubwa sana wenye Tarafa ya Kibutuka, Lilombe na Kimambi na ni ahadi ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema Serikali imepanga kujenga vituo vya polisi vya kata kwa awamu. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pia kata zake alizotaja naamini zipo kwenye mpango, kwa hiyo, tutazitengea fedha ili ziweze kujengwa na wananchi wapate ulinzi na usalama wa mali zao, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Kyerwa ni Wilaya mpya lakini mpaka sasa hakuna kituo cha polisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa vituo vya kata, kama nilivyosema Serikali inaendelea kujenga vituo vya wilaya kwa kupitia Mfuko wa Tozo na Tuzo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Wilaya ya Kyerwa ni moja kati ya wilaya za kimkakati kwa hiyo, tutajenga kituo cha polisi katika wilaya hiyo, ahsante sana.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichokuwepo pale Mchangani kwenye Jimbo langu la Chaani ambacho kwa takribani 80% kimeshatengenezwa na wawekezaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Usonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana kwa ujenzi wa kituo ambacho kimefika 80% na ninamhakikishia Serikali kwa kazi hiyo nzuri iliyofanywa na wananchi, 20% iliyobaki tutamalizia katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika Kata ya Bukumbi wananchi na Mbunge tumejenga kituo kizuri cha afya. Lini Serikali itapeleka magari au pikipiki, kwa ajili ya usafiri wa hawa askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani alikuwa anaulizia swali kituo cha polisi na siyo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mpaka sasa imetoa pikipiki 105 kwa ajili ya vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini na kwa jinsi ya upatikanaji wa fedha, Serikali itatoa pikipiki kwa ajili ya kuhudumia vituo vya kata, kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge Maige.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kijiji cha Pujini kilichopo Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba ni kijiji ambacho kina matukio ya uhalifu siku hadi siku, je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Mwinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, Serikali ina mkakati wa kujenga vituo vya kata nchi nzima, nadhani takribani kata 4,434 zimebaki. Kama nilivyosema, vinajengwa kwa awamu, havijengwi mara moja, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kituo alichotaja kitawekwa kwenye mpango ili kiweze kutengewa fedha kwa miaka inayokuja na kujengewa kituo cha polisi katika eneo lake, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiuliza Serikali, kituo cha polisi kilichopo Kata ya Kashai kimepewa chumba kimoja katika Ofisi ya Kata na tukizingatia kwamba Kata ya Kashai ndani ya Jimbo la Bukoba Mjini ina wakazi zaidi ya 33,000. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Kashai? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Kata ya Kashai ina wananchi wengi, kama alivyotamka Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo namhakikishia kwamba kwa kuwa ina wananchi wengi na pia kunakuwa na hatari ya kuwa na wizi au matukio mbalimbali. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kata yake aliyoitaja ya Kashai na yenyewe tumeichukua na tutaiingiza kwenye mpango kwa ajili ya kujengewa Kituo cha Polisi, ahsante sana.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Karanga, viongozi pamoja na wananchi wamejenga kituo kizuri sana cha polisi, lakini bado hakijakamilika na mimi nimewasaidia tofali 2,000. Je, Waziri yuko tayari kuja kukitembelea na ku-allocate bajeti ya kumalizia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa aliyofanya ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kata aliyoitaja ya Karanga. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge niko tayari kwenda kwenye kituo hicho kukikagua na kukitengea fedha, kwa ajili ya kumalizia kazi kubwa waliyoifanya wananchi wa Karanga, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi hili la Zimamoto ni la muhimu sana na limekuwa likifanya kazi kubwa sana, hasa kwenye Mkoa wetu wa Lindi, ikiwemo kudhibiti na kupambana na mafuriko yanayoendelea katika Mkoa wa Lindi. Hata hivyo, jeshi hili hawana Ofisi nzuri za kufanyia kazi.
MWENYEKITI: Swali la nyongeza Mheshimiwa Francis.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati Ofisi za Zimamoto zilizopo katika Wilaya za Mkoa wa Lindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watumishi wa Ofisi za Zimamoto wamekuwa hawana nyumba za kuishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea nyumba za kuishi katika Mkoa wa Lindi?
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Francis Ndulane kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linalohusiana na ukarabati wa ofisi, kadiri Serikali itakavyopata fedha itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi za Zimamoto na Uokoaji katika maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba za makazi ya Askari, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba kadri Serikali itakavyopata fedha itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari wetu wa zimamoto na askari wengine hapa nchini, ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la wanufaika wa msamaha wa Parole, kwamba wakishafika uraiani wanatengwa na jamii na kuonekana bado ni wahalifu, jambo linalowafanya kufanya tena uhalifu na kurudi Magerezani.

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa Njau.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ili marekebisho ya sheria yaweze kugusa jamii na jamii iweze kuelewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wapo watoto wanaozaliwa Magerezani wakiwemo na mama zao ambao watoto wale sio watuhumiwa, lakini watoto hawa hawapati haki za msingi kwa mujibu wa Katiba kama elimu na vitu vinginevyo.

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho haya ya sheria yatagusa vipi watoto hawa wanaozaliwa Magerezani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Felista Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa jamii nzima ili kuhakikisha kwamba wenzetu wanaotoka magerezani basi wasitengwe tena ili waendelee kuwa raia wema na kutimiza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu watoto wanaozaliwa Magerezani, amedai wanakosa haki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria hii itakapofanyiwa marekebisho itapata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile jamii nzima, viongozi wa dini pamoja na Maafisa wa Magereza pamoja na Wizara nyingine za kisekta ili kuhakikisha kwamba tunatunga sheria mahususi kwa ajili ya ku-cover watoto wetu wanaozaliwa katika Magereza. Ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa kuamua kukamilisha kituo hiki ambacho kiko Tarafa ya Igurubi kitakachozihudumia Kata za Kinungu, Igurubi, Mwaitunduru, Mwamashiga, Kinig’inila, Mwamashimba na Mwamakona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nauliza kwamba, kwa kuwa Serikali yetu imeamua inapojenga vituo inatoa na vitendea kazi, je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na kituo hiki kitakapokamilika, watatupatia vitendea kazi kwa ajili ya doria ?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali imeshatoa pikipiki kama 105 kama vitendea kazi nchi nzima na bado tuna mpango wa kutoa pikipiki kwa awamu ili kuhakikisha kwamba kata zote ambazo tunajenga ofisi za Polisi pia zinapata pikipiki ili kurahisisha utendaji kazi, ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa Ofisi hiyo kwa sababu, zaidi ya miaka 12 tumekuwa tukifuatilia ujenzi wa Ofisi ya Polisi, Kilolo. Nina maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, askari karibu wote wa Wilaya ya Kilolo wamekuwa wakiishi uraiani kwa bei tofauti tofauti za pango: Je, ni lini sasa Serikali itakuwa na Mpango wa kuwajengea makazi askari hao, ili kuondoa changamoto hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, Vituo vya Polisi vya Mtitu, Ruaha Mbuyuni, Nyalumbu na Boma la Ng’ombe ni vituo vinavyohitaji ukarabati mkubwa: Je, ni lini Serikali itatenga Bajeti ili viweze kukarabatiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunatambua uhaba wa Nyumba za Makazi ya Askari katika maeneo mbalimbali, ikiwepo Wilaya ya Kilolo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatenga fedha kwa jinsi ya upataikanaji wake, kwa ajili ya kujenga Nyumba za Askari wetu wa Wilaya ya Kilolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la ukarabati wa Vituo vya Polisi alivyovitaja, namhakikishia kwamba vitaingia kwenye mpango. Hata hivyo, naagiza Jeshi la Polisi kufanya tathmini ili kujua kiasi cha fedha kinachotakiwa ili tuweze kufanya ukarabati wa vituo hivyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali. Ofisi ya OCD Wilaya ya Kishapu imejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo, ukiwepo Mgodi wa Mwadui, mpaka kufikia katika hatua ya upauaji. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri alifika na kuahidi kwamba, watahakikisha wanatoa shilingi milioni 271, kwa ajili ya kukamilisha mradi huo...

NAIBU SPIKA: Uliza swali.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: ...Mradi huo wa Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza wananchi wa jimbo lake kwa kazi kubwa walioifanya ya kujenga Kituo cha Polisi hadi hatua ya linter. Pia, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatenga fedha kama alivyoahidi Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ajili ya kumalizia kituo hicho kilichojengwa kwa nguvu za wananchi, ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi ilipatikana mwaka 2002, lakini toka mwaka 2015 nimeingia hapa Bungeni, nimekuwa nikiomba Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Wilaya ya Kilindi ni Wilaya kubwa na ni kweli haina kituo cha Polisi cha Wilaya. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatenga fedha kwa mwaka wa fedha unaokuja 2025/2026, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilindi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Lengatei, Magungu na Chekanao wameshaanzisha Vituo vya Polisi. Lini Serikali itawasaidia kumalizia vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Lekaita, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa wananchi wameshaanza kazi nzuri ya ujenzi wa Vituo vya Polisi kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. Serikali yetu kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inamalizia Vituo vya Polisi ambavyo ni maboma 77 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na ujenzi wa vituo vipya 12. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa vituo vyako pia viko kwenye mpango kwa ajili ya kumaliziwa.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Vituo vingi vya Polisi nchini vimechakaa na vingine havitamaniki kabisa. Ningependa kufahamu, nini mkakati wa Serikali wa pamoja kuhakikisha vituo hivyo vinakarabatiwa, kwa maana ya nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lambert, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba, kuna Vituo vingi vya Polisi ambavyo ni chakavu na ni vya muda mrefu. Hata hivyo, katika hali ya kawaida huwezi kujenga vyote kwa pamoja. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kila awamu tutatenga fedha kwenye bajeti ili kuhakikisha tunavikarabati awamu kwa awamu na mwisho wa siku tutavimaliza vyote.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Licha ya hatua hizo ambazo Serikali imekuwa ikichukua, lakini matukio haya yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na yamekuwa yakileta madhara makubwa. Ni upi mkakati wa Serikali wa kuchukua hatua kali zaidi kwenye matukio ambayo yanasababishwa inapotokea ajali na watu wanachukua mafuta na baadaye yanaleta madhara makubwa kwenye Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni la Watanzania wote. Naomba nitoe kwa jamii nzima ya Watanzania, Viongozi wa Dini pamoja na wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, tunaendelea kutoa elimu kwa familia zetu, ili kuhakikisha kwamba, inapotokea ajali si jambo jema kukimbilia kwenda kuiba badala ya kwenda kusaidia. Kwa hiyo, natoa wito kwa jamii nzima tushirikiane kuhakikisha kwamba, jambo hili linakomeshwa mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nakuhakikishia Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote ambao wanaiba mafuta haya inapotokea ajali. Ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana kwa swali letu hili la leo. Je, ni kwa nini sasa hilo eneo Serikali isilikabidhi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kiwe chanzo kizuri sana cha mapato na kuleta tija kwa wananchi wa eneo hilo ambao mara nyingi sana hata barabara zao hazipitiki wakati wa mvua?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana nami twende mpaka Kilolo katika hilo eneo la kambi hiyo ili akajionee uhalisia wa maombi yangu ambayo yamekuwa ya muda mrefu ili wananchi waweze kupata moto kwa majibu mazuri ambayo umewapatia siku ya leo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali la kwanza ni kwamba kwa sasa mpango wa Serikali ni kuhakikisha inapima eneo hili na kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule pamoja na Gereza la Mgagao. Pia Mheshimiwa Mbunge ameleta mapendekezo na sisi kama Serikali tunayachukua tukayachakate tuone kama eneo hili litafaa kwa ajili ya kuhamia kwenye Wizara nyingine.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, kwenda eneo hilo alilotaja, mimi niko tayari, baada ya Bunge tutaongozana naye kwenda kwenye eneo hilo na kuliangalia. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wahamiaji haramu bado wamekuwa wakionekana wanaingia nchini na wanapopatikana wanapelekwa katika Magereza yetu ambako wanaongeza gharama za bajeti katika Magereza yetu: Je, Serikali haioni haja ya kuwarejesha kwao mara tu wanapowakamata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Othman, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli wapo wahamiaji haramu ambao wanapokamatwa hurejeshwa kwenye nchi zao, lakini wapo ambao wakati tunafanya mawasiliano na nchi zao, huwekwa Magerezani na wapo wanaofungwa kutokana na aina ya makosa waliyoyatenda, ahsante sana.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha umakini katika kutoa haki ya msingi kwenye Visa ambazo zinatolewa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Serikali ipo makini sana katika eneo hilo, itaendelea kuwa makini na ninawaomba wale wote wanaoomba Visa kwa ajili ya kusafiri nje ya nchi, wazingatie sheria na taratibu za nchi yetu na wasijihusushe na vitendo ambavyo vitawazuia kutokusafiri nje ya nchi, ahsante
MHE. INNOCENT E. KALEGORIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, nini kauli ya Serikali katika hili suala la gari ambalo limetengewa Wilaya ya Morogoro ambalo Mheshimiwa Waziri anasema kwamba litatumika katika kutoa huduma katika Tarafa ya Mvuha. Nataka nipate commitment ya Serikali kumwelekeza OCD wa Morogoro gari hilo litakapokuwa limefika liende katika Kituo cha Tarafa ya Mvuha ili liweze kuhudumia Tarafa nne ambazo ni Ngerengere, Matombo, Mkuyuni na Mvuha yenyewe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Morogoro Vijijini imetenga kiasi cha shilingi milioni mia tatu ambazo zimejenga jengo la Kituo cha Polisi chenye hadhi ya wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha jengo hili ambalo linahitaji shilingi milioni mia moja?
NAIBI WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, magari tuliyoyaagiza kwa sasa ni magari ya Ma-OCD ambao wapo kwenye Wilaya za Kipolisi, kwa hiyo gari hili litakalokuja litahudumia Wilaya nzima ya Morogoro kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jengo ambalo limejengwa na wananchi, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa aliyofanya ya kujenga jengo la Polisi. Nimhakikishie kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo wananchi wameyajenga kwa nguvu zao. Ahsante sana.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri lakini bado kuna mahitaji makubwa ya kupata makazi ya kudumu katika maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ili kuondosha usumbufu. Swali la kwanza; ningependa kujua, je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuandaa makazi kwa askari wetu hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza maeneo ya makazi katika Wilaya ya Wete ili kuondosha askari wetu kupanga nyumba za mitaani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asya Sharif, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, kwamba kuna mahitaji makubwa ya makazi, ni kweli na sisi kama Serikali tunatambua kuwa kuna mahitaji makubwa ya makazi ya askari wetu. Tunatenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga makazi ya askari wetu ili wafanye kazi ya kulinda wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la maeneo ya makazi, Serikali itafanya tathmini katika maeneo yote ya Pemba na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari yatatengewa bajeti katika miaka inayokuja ya fedha, 2025/2026 na miaka inayoendelea. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni nini sasa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inakabiliana na wahamiaji haramu ambao kimsingi wamekuwa wakihatarisha sana usalama wa nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari tuna nchi 27 ambazo zinatumia VISA Rejea, je, Serikali imeweka mfumo gani wa kuhuisha VISA Rejea kwa sababu kuna kipindi tunaona nchi zinaongezeka na nyingine zinapungua? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya Serikali; kwanza iko misako lakini pia iko doria ambayo inafanywa na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha kwamba raia au wahamiaji haramu hawaingii nchini. Pia, ipo kauli mbiu kwamba; ‘Mjue Jirani Yako,’ hii imesaidia sana kuwatambua wahamiaji haramu ambao wanaingia hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, kwanza VISA Rejea inatokana na changamoto ya raia wa nchi hizo ambazo nimezitaja nchi 27 lakini pia jukumu hili hufanywa na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya Muungano pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuhakikisha kwamba wanatambua viashiria hatarishi kwa wahamiaji haramu hapa nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua kwa nini sasa Serikali haitoi muda maalumu wa kufanya uchunguzi wa taasisi hizo wakati wa maombi na badala yake kuacha inakwenda mpaka miaka mitano wameomba?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali inafaidika nini na hizi taasisi ambazo zipo zinafanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 zinahitaji usajili, kurasimisha tu lakini Serikali inashindwa kufanya hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza, tumeweka miaka miwili hadi mitano ili kuhakikisha kwamba kwanza tunazichunguza vizuri taasisi na hii inatokana na unyeti wa taasisi za dini. Lazima tujiridhishe kwamba taasisi zinafanya majukumu ambayo yameorodheshwa kwenye katiba zao na siyo nje ya utaratibu ambao umewekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jambo la pili, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba taasisi hizi zote za dini zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi na hii ni katika kulinda usalama wa nchi yetu. Ziko sababu ambazo zinapelekea baadhi ya taasisi kukaa muda mrefu bila kusajiliwa, kama alivyosema miaka 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ambazo ziko ndani ya Wizara, kwa sasa kuna taasisi zisizozidi tano ambazo zimekaa muda mrefu. Hii inatokana na kwamba taasisi hizo zinahamahama ofisi. Mara zimesajili kwa kupitia taasisi nyingine wakati zinasubiri usajili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, jukumu kubwa hasa ni kuhakikisha taasisi hizi zinafuata Katiba na sheria za nchi yetu lakini pia kuzingatia usalama wa raia na nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kumalizia maboma hayo yaliyojengwa na wananchi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Sumbawanga Mjini Kituo cha Polisi ni cha tangu enzi za mkoloni, ni kidogo na hakina hewa kabisa, wala hadhi ya mkoa. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Sumbawanga Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wilaya ya Kalambo haina Kituo cha Polisi kabisa na inaazima majengo kutoka CCM na shahidi wangu ni Mbunge mwenye Jimbo, kaka yangu Mheshimiwa Kandege, amekuwa akilalamika siku nyingi hapa kuwa hana Kituo cha Polisi Wilaya ya Kalambo. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Kalambo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bupe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Kituo cha Polisi cha Sumbawanga pale mjini ni cha zamani kama alivyosema na kimechakaa na Serikali tumeshafanya tathmini. Kinahitajika ni kiasi cha fedha shilingi 1,200,000,000. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 tumetenga shilingi milioni 400 tayari kwa kuanza ujenzi wa Kituo cha Daraja A pale Sumbawanga Mjini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, kwa ukosefu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kalambo, hilo nimelichukua na tutaliingiza kwenye mpango kwa ajili ya kukijenga katika mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa.

Mheshimiwa Spika, nini mkakati wa Serikali wa kujenga Kituo kidogo cha Polisi katika eneo la Kizota - Mbuyuni ambako kumekuwa kuna matukio ya uhalifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani tayari ina mpango wa kujenga Vituo vya Polisi kwa awamu. Awamu ya kwanza ambayo inaanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025 vituo 12, na kumaliza mabomba 76 kama alivyosema. Pia, ipo awamu ya pili ambayo itajenga Vituo vya Polisi mbalimbali ikiwemo na kata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitaangalia kwenye mpango wetu wa 2024/2025 kama Kituo cha Kizota kipo, kama hakipo nitakiweka kwenye mpango kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja wa 2025/2026.
MHE. INNOCENT E. KALEGORIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, nini kauli ya Serikali katika hili suala la gari ambalo limetengewa Wilaya ya Morogoro ambalo Mheshimiwa Waziri anasema kwamba litatumika katika kutoa huduma katika Tarafa ya Mvuha. Nataka nipate commitment ya Serikali kumwelekeza OCD wa Morogoro gari hilo litakapokuwa limefika liende katika Kituo cha Tarafa ya Mvuha ili liweze kuhudumia Tarafa nne ambazo ni Ngerengere, Matombo, Mkuyuni na Mvuha yenyewe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Morogoro Vijijini imetenga kiasi cha shilingi milioni mia tatu ambazo zimejenga jengo la Kituo cha Polisi chenye hadhi ya wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha jengo hili ambalo linahitaji shilingi milioni mia moja?
NAIBI WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, magari tuliyoyaagiza kwa sasa ni magari ya Ma-OCD ambao wapo kwenye Wilaya za Kipolisi, kwa hiyo gari hili litakalokuja litahudumia Wilaya nzima ya Morogoro kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jengo ambalo limejengwa na wananchi, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa aliyofanya ya kujenga jengo la Polisi. Nimhakikishie kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo wananchi wameyajenga kwa nguvu zao. Ahsante sana.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri lakini bado kuna mahitaji makubwa ya kupata makazi ya kudumu katika maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ili kuondosha usumbufu. Swali la kwanza; ningependa kujua, je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuandaa makazi kwa askari wetu hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza maeneo ya makazi katika Wilaya ya Wete ili kuondosha askari wetu kupanga nyumba za mitaani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asya Sharif, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, kwamba kuna mahitaji makubwa ya makazi, ni kweli na sisi kama Serikali tunatambua kuwa kuna mahitaji makubwa ya makazi ya askari wetu. Tunatenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga makazi ya askari wetu ili wafanye kazi ya kulinda wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la maeneo ya makazi, Serikali itafanya tathmini katika maeneo yote ya Pemba na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari yatatengewa bajeti katika miaka inayokuja ya fedha, 2025/2026 na miaka inayoendelea. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa masikitiko makubwa hili swali ninalirudia leo karibu mara ya pili au ya tatu sasa na majibu ya Serikali ni haya. Sasa, naomba nijue kutoka kwa Serikali kwamba, nini tamko la uhakika kabisa kwamba, pesa hizi zitafika na kuweza kutekeleza au kuondoa changamoto hizo ambazo nimezieleza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Pale, hili gari ambalo wanalitaja ni moja, kwa ufupi jamani, lile ni lori la mizigo kwa hiyo, ni kazi sana askari kufanya doria kwenye maeneo ambayo yanaendelea na ujenzi kule Kwala, kwenye kongani ya viwanda ya Morden Park Industries na maeneo mengine ya Jimbo la Kihaba Vijijini. Sasa nataka nijue, haya magari ambayo yameahidiwa ni lini yanafika na ni wapi wanayakabidhi, ili niweze kushuhudia yakitolewa na wananchi wakipata huduma katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tamko la uhakika ni, ili kudhihirisha kwamba, tumechukua hatua kwanza tulifanya tathmini ya mahitaji ya majengo hayo ambapo, kama nilivyosema, hatua ya pili ni kutenga fedha kwenye bajeti hii ya Mwaka wa Fedha unaokuja wa 2024/2025. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa, tumeshachukua hatua kufanya tathmini, tumetenga bajeti, naomba nimtoe wasiwasi kwamba, sasa tunaenda kutekeleza miradi hii, kama ambavyo tumeainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu magari; namhakikishia Mheshimiwa Mbunge tayari tumeshaagiza magari 122, kwa ajili ya ma-OCD wote nchi nzima. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wa Kibaha gari mtalipata, kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Mlandizi, kama ambavyo umeomba. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wilaya ya Tanganyika haina Gari la Polisi. Ni lini mtapeleka gari kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tayari Serikali imeshaagiza magari 122. Kwanza tulishatoa magari 71 kwa ma-OCD hapa nchini na sasa hivi wakati wowote magari 122 yanaingia, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kila OCD katika nchi hii anapata gari, kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwenye haya magari ambayo unasema umeyaagiza au yameagizwa, kwa Wilaya ya Nyang’hwale tumekuwa na uhitaji mkubwa kwa muda mrefu. Naomba kauli ya Serikali kwenye haya magari na Nyang’hwale itapata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Nyang’hwale pia, ni Wilaya. Kwa hiyo, watapata gari, kwa ajili ya kulinda mali zao na raia wetu wawe salama. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya hizi zitakazopata Magari ya Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nchi hii ina Wilaya 139, tumeshagawa magari 71 na tumeagiza mengine 122. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kwamba, Wilaya ya Kilindi ni moja kati ya Wilaya zitakazopata gari, kwa ajili ya wananchi wake. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, lini Serikali itarekebisha majengo na kuweka vitendea kazi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunatambua Mbagala ni eneo ambalo lina wakazi wengi, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Kituo cha Polisi cha Mbagala pia kinapata fedha kwa ajili ya kukarabatiwa ili waweze kutoa huduma kwa wananchi wetu.
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itatatua changamoto za magari, pikipiki na vifaa vingine kwenye Kituo cha Polisi cha Ng’ambo – Unguja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tayari tumeshagawa pikipiki 105 mpaka sasa na tunazigawa kwa awamu. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge pia kituo chako ulichokisema tutaweka kwenye mpango ili tuweze kupata polisi kwa ajili ya kutoa huduma katika eneo lako ulilotaja.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. kumekuwa kuna uhalifu wa wizi wa mifugo kwa maana ya ng’ombe na jambo hili limekuwa likiendeleza na likitia umaskini wananchi ambao ni wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya. Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa lengo na dhumuni la kuanzisha Kanda Maalum Rorya ilikuwa ni kudhibiti wizi wa mifugo kwenye eneo hili na jambo hili limekuwa likiendelea.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupitia upya Kanda Maalum ya Tarime – Rorya kuifumua na kuunda upya ili kuongeza ufanisi wa kudhibiti uhalifu unaoendelea kwenye eneo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa matukio haya mawili wizi wa mifugo na uvamizi wa wavuvi ndani ya ziwa imekuwa ikiendelea na majibu yamekuwa haya haya kwenye majibu ya msingi. Je, Mheshimiwa Waziri hauoni baada ya Bunge hili kuna umuhimu wa mimi na wewe kuongozana ikibidi na IGP, kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kukaa na wadau na wananchi wanaoathirika na matukio haya mawili ili kuona namna ya kudhibiti na kuongeza ufanisi kwenye maeneo haya kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao ndani ya Wilaya ya Rorya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu wizi wa mfugo, katika Wilaya ya Rorya tayari tushaanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi, lakini nimhakikishie kwamba sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani tumeongeza pia Askari wa Polisi wanaohusika na kuzuia wizi wa mifugo katika Mkoa wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza tumeongeza boti za doria na tumeshaagiza boti 10. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge baadhi ya boti zitaenda katika eneo lake la Rorya kwa ajili ya kufanya doria katika Ziwa Victoria, lakini pia niko tayari kuongozana naye baada ya Bunge hili kuhakikisha kwamba tunawasikiliza wananchi na kutatua changamoto hiyo, ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Briefly tu nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pia kwa kutuma vehicle yeye na Ndugu Suzan Kaganda kwenda kutatua changamoto ya leseni Ngara. Nina swali moja la nyongeza

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa matatizo ya majira ya nukta yanayosemwa na Mheshimiwa Naibu Waziri yalitokana na magereza kufanya upimaji bila kuhusisha kijiji wala wananchi wanaohusika maeneo yale na hivyo kuleta matatizo makubwa mpaka kuingilia hifadhi na ardhi nyingine ambayo ipo nje ya nchi (no man’s land).

Ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri ataambatana na mimi twende Rusumo, tukae na wananchi tukatatue matatizo ya ardhi kwenye Kijiji cha Rusumo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mimi niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge la Bajeti tutapanga utaratibu mzuri, twende kwa wananchi tukaisikilize changamoto hii, lakini pia naagiza Jeshi la Magereza kwamba wataalamu wetu watangulie waanze kupima kabisa ili tukifika tumalize mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali na kwamba ninaipongeza sana Serikali kwa kuwa na nia ya kuleta muswada huu hapa Bungeni, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Jeshi la Polisi limeanzisha Kampuni ya Ulinzi Binafsi, wakati huo huo Jeshi la Polisi ndio wasimamizi wa sekta hii ya ulinzi binafsi, kampuni za ulinzi zinaona kwamba suala la Jeshi la Polisi kuanzisha kampuni ya ulinzi litaleta ushindani mbaya kinyume na matakwa ya Tume ya Ushindani.

Je, Serikali inasema nini kuhusu suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya ulinzi iliyoanzishwa na aliyosema ya polisi si ya Jeshi la Polisi ni ya Shirika la Uzalishaji la Polisi, ni shirika ambalo linafanya biashara kama shirika lingine. Kwa hiyo, siyo kampuni ya Jeshi la Polisi per-se, ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwanza kwa dhati ya moyo wangu na kwa niaba ya Wana-Kilindi ninaomba niipongeze Serikali kwa sababu lilikuwa ni jambo la muda mrefu sana, sana, sana. Niombe tu kwamba Serikali au Wizara ya Mambo ya Ndani iharakishe kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Kikunde wamejenga Kituo cha Polisi na kimefikia 99%. Kwa utaratibu ule ule wa ku-support nguvu za wananchi; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutenga kiasi cha fedha ili kuwa-support wananchi wa Kata ya Kikunde?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunapokea pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Polisi cha Kata alichokitaja Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunajenga na kwamba tunamalizia maboma ambayo tayari wananchi wamekwishaonesha juhudi zao za kujenga vituo hivyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo chake hicho pia tutakichukua tukiongeze kwenye mpango ili tukimalizie na ili wananchi wapate huduma ya ulinzi na usalama katika eneo lao, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kujenga au kukarabati kile Kituo cha Kegonga ambacho kilikuwa katika hali mbovu sana, sasa hivi kimekuwa cha kisasa. Sasa ninataka kujua, je, ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi katika Kata ya Susuni ambayo haina kabisa kituo cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapokea pongezi kwa kituo cha kisasa ambacho tayari kimekwishakamilika. Kuhusu Kituo cha Polisi cha Kata ya Susuni, tunajenga hivi vituo vya polisi awamu kwa awamu. Nimhakikishie Mheshimiwa Esther kwamba kituo chake cha Kata ya Susuni kitaingia kwenye mpango na tutakitengea fedha na kitajengwa, kwa sababu nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila kata katika nchi hii inapata kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao, ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya swali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, nyumba za Askari Polisi zilizopo Mbeya Jiji pamoja na Wilaya ya Rungwe zimeonekana kuchakaa. Ni lini Serikali itaenda kukarabati nyumba hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Jeshi la Polisi mtatujengea nyumba za Maaskari kwenye Jimbo la Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo. Ni kweli baadhi ya nyumba za Askari kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge katika Jiji la Mbeya, ni chakavu. Kama alivyosema, timu yetu ya wataalamu ishafanya tathmini tayari na kiasi cha fedha kama nilivyotaja kwenye jibu la msingi kimetengwa. Kwa hiyo, kwenye mwaka wa fedha 2025/2026 tutaanza ukarabati wa nyumba za Askari Polisi katika Jiji la Mbeya na maeneo hayo aliyotaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la pili, kama nilivyosema, Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya tathmini ya upungufu wa nyumba za Askari katika wilaya zote hapa nchini ikiwepo na Jimbo la Momba. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Momba pia litawekwa kwenye Mpango ili kujenga nyumba za Askari Polisi kwenye Jimbo la Momba, ahsante sana.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahanste sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri aliyoyatoa hapo lakini nina maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa baadhi ya maeneo nchini havijafikiwa kujengwa vituo vya polisi, lini Serikali itajenga vituo hivyo? (Makofi)

Swali langu la pili, sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi, vipi kuhusu ujenzi wa nyumba za askari nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa vituo vya polisi ambavyo havijafikiwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye mwaka wa fedha 2024/2025 tunajenga vituo vya polisi 12 na tunamalizia maboma 77 ambayo tayari yamejengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Pia, kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani tunajenga vituo 26 kutoka kwenye bajeti pamoja na Mfuko wa Tuzo na Tozo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali imeendelea kujenga nyumba za askari katika maeneo mbalimbali na itaendelea kutenga fedha na kujenga nyumba awamu kwa awamu na kukamilisha katika maeneo ambayo hayana nyumba za askari. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Kata ya Susuni ni moja kati ya Kata ambazo zipo pembezoni kabisa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, nataka kujua ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi ukizingatia Kata jirani ya Mwema ina vituo viwili vya polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama niliyosema tunajenga vituo vya polisi vya Kata kwa awamu. Kwa mwaka wa fedha huu 2024/2025 tunajenga vituo 12, lakini hii ni kwa awamu ya kwanza, kwa mwaka unaofuata tutajenga vituo 196 na vinakuja vituo 212.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kituo chako kama hakipo kwenye mpango wa mwaka huu tutapanga mwaka wa fedha unaokuja ili kujenga kituo cha Polisi cha Kata ya Susuni kama ambavyo umeomba. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, Halamshauri ya Itigi, Kituo cha Polisi Itigi, Polisi wa Itigi wanakaa kwenye majengo ya Reli na Reli wanajiimarisha pia yamechakaa sana.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kituo cha polisi katika Halmashauri ya Itigi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema tunajenga vituo vya polisi kwa kutumia bajeti ya Serikali, Mfuko wa Tuzo na Tozo lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kituo chake mwaka wa fedha huu hakipo basi tutakitengea fedha kwenye mwaka wa fedha 2025/2026 ili tujenge kituo cha polisi katika eneo lake la Itigi, ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wananchi wa Kiteto, Kata ya Magungu, Kijungu na Lengatei wameshaonesha nia ya kujenga vituo vya polisi. Lini Naibu Waziri utakuwa tayari kutembelea vituo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nipo tayari kwenda Kiteto kutembelea vituo hivyo ambavyo vimeshaanza kujengwa na wananchi, kama nilivyosema maboma yote ambayo wananchi wameshaanzisha, Serikali ipo tayari kumalizia kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Tumetenga shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nitakuja kukutembelea katika eneo lako. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Kata ya Karansi kumekuwa na matukio ya mauaji ya mara kwa mara. Mnamo mwaka 2016 aliuawa baba mmoja katika Kata hiyo na mnamo mwaka 2022 mwanamke mmoja alichinjwa. Je, Serikali inaongea nini au inawaambia nini wananchi wa Karansi, katika kuwasaidia ili kuepukana na matukio mazito kama hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Kata hiyo hiyo kumekuwa na matukio ya uhalifu yakiongezeka sana kutokana na idadi ya wananchi waliopo. Hivi karibuni katika mwezi wa Tatu mwaka huu 2024, na mwezi huu wa Nne yamevunjwa maduka manne ya wafanyabiashara na mali za thamani ya zaidi ya shilingi milioni 48 zimepotea. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kujenga kituo kidogo cha Polisi ili kuwasaidia wananchi katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii taarifa nimeipokea sasa kwamba kuna mauaji yalifanyika katika Kata hiyo, nitafuatilia kujua ni watu gani waliohusika, lakini pia ni hatua gani zilichukuliwa na Serikali kwa mauaji yaliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; Jeshi la Polisi limesambaza Askari Kata ili kushirikiana na wananchi na kuboresha ulinzi shirikishi katika maeneo yote na kuboresha doria ili kudhibiti masuala yote ya uhalifu katika Kata zetu na vijiji vyetu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mbunge awasihi wananchi wa Kata ya Karansi kushirikiana na Askari ili kuboresha doria katika maeneo yote ili Kata hiyo na Kata nyingine ziendelee kuwa salama, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itakamilisha jengo la Kituo cha Polisi Kata ya Mgoma Wilaya ya Ngara ambapo Kata hiyo iko mpakani mwa Burundi na Tanzania kwa ajili ya usalama zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itakamilisha vituo vya Polisi Kata 77 ambavyo tayari viko katika hatua za boma. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo chake alichokitaja pia ni moja katika vituo ambavyo vitakamilishwa, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Polisi kilichopo Kengeja ni chakavu sana. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa sasa hivi tunajenga vituo vya Polisi katika ngazi za Kata na Jimbo la Mbulu Mjini tuna Kata 10 vijijini, lakini hatuna hata kituo kimoja cha Afya cha Kata, je… (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa umeeleweka.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Afya? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Issaay Mbunge wa Mbulu Mjini kwamba, ujenzi wa vituo vya Polisi vya Kata unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vya Polisi vya Wilaya. Nimhakikishie pia kwamba, kadiri tunavyopata fedha basi tutazingatia pia ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Mbulu, ahsante sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hali ya kituo cha afya kule Siha, Kituo cha Polisi... (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya uhitaji wa kituo cha Polisi kule Siha inafanana kabisa na uhitaji wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Lukozi Wilaya ya Lushoto. Ni upi mpango wa Serikali kwenda kujenga kituo cha Polisi katika Kata ya Lukozi? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kujenga Vituo vya Polisi 647 na itaendelea kujenga kadiri ya upatikanaji wa fedha kwa awamu kwa kadiri fedha zinavyopatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika swali la kwanza, imekuwa miaka mitatu sasa tangu nafuatilia gari la Zimamoto kwenye Halmashauri yangu na hadi leo sijapata majibu sahihi. Mji wa Korogwe ni kati ya Miji inayokua kwa kasi sana, majanga ya moto yanatokea na hakuna msaada wowote kwa kuwa hatuna gari la zimamoto.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni basi kubwa la abiria limeungua lote na kuteketea na nyumba ya mwananchi wangu katika Kata ya Majengo imeungua na kuteketea, hatuna msaada. Kwa hiyo, nahitaji commitment ya Serikali ya kweli, ni lini mtatupatia gari la Zimamoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tuna gari letu la Zimamoto ambalo ni chakavu sana, linahitaji matengenezo. Je, Serikali haioni haja ya kulikarabati hili gari la Zimamoto ambalo liko ili tukiwa tunasubiri hayo magari ambayo yanakuja, wakati huo tukiwa tunaokolewa kwa kutumia hili? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Kimea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza natoa pole sana kwa wananchi wa Korogwe waliopatwa na changamoto hii ya moto, lakini namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwamba, Wilaya ya Korogwe ni moja kati ya Wilaya zitakazopata gari la Zimamoto katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, kati ya magari 150 ambayo nimeyasema.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu utengenezaji wa gari ambalo liko kwenye matengenezo, nikitoka hapa nitalifuatilia kuhakikisha gari hili linapatikana ili liendelee kutoa huduma katika Wilaya ya Korogwe, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tunanunua magari 150 ambayo tutayapeleka kwenye mikoa yote ambayo haina magari hayo ikiwemo Mkoa wa Manyara, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inanunua magari 150 kupeleka kwenye Halmashauri zote, je, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama itapata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, katika magari 150, zitapata Halmashauri zote ambazo ni Wilaya zote 139 na Mikoa ambayo pia haina, ikiwemo Halmashauri ya Kahama katika Mkoa wa Shinyanga, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Mbeya kuna baadhi ya Wilaya zina changamoto za gari la Zimamoto, hasa Wilaya ya Chunya, kuna shida sana ya gari la Zimamoto. Je, ni lini mtapeleka gari la Zimamoto katika Wilaya ya Chunya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Fyandomo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, tunatarajia kununua magari 150 na Wilaya ambazo ziko 139. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya aliyoitaja itapata pia gari la Zimamoto na Uokoaji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba Serikali sasa kwa vile tayari imesema itatenga fedha iwaone na iwasaidie kwa dharura kwa kipindi hiki cha mpito wale askari ambao wanaishi mbali na kituo hicho. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, tumeupokea ushauri na ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Jeshi la Polisi tunafanya tathmini kuhakikisha majengo yote ambayo ni chakavu, yanakarabatiwa, lakini tunajenga majengo mapya, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha askari wetu wanakaa katika maeneo ambayo yako salama kwa ajili ya kulinda raia na mali zao. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Maswa ni wilaya kongwe kabisa katika Mkoa wa Simiyu, lakini haina Kituo cha Polisi, je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Maswa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunajenga Vituo vya Polisi vya Kata na Ofisi za Wilaya nchi nzima pamoja na shehia kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Maswa ambayo haina Kituo cha Polisi pia tutaitengea fedha na kujenga Kituo cha Polisi kwa ajili ya usalama wa wananchi wa Maswa na vitongoji vyake, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itajenga nyumba za askari polisi katika Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninajibu swali la Mheshimiwa Minza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua askari wetu wengi hawana nyumba za kuishi, lakini ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunafanya tathmini nchi nzima kuhakikisha kwamba upungufu wa nyumba uko kiasi gani ili tuweze kutenga katika bajeti zetu mwaka hadi mwaka. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Masasi imeendelea kukua, lakini nyumba za polisi zilizopo zimechakaa na ni za muda mrefu. Je, Serikali haioni haja ya kujenga nyumba mpya kwa ajili ya askari polisi wa Wilaya ya Masasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninajibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, timu yetu ya wataalamu inapita nchi nzima kupitia nyumba zetu za askari polisi na kuona jinsi ambavyo zimechakaa ili sasa tupange, tujenge awamu kwa awamu kwa sababu hatuwezi kujenga zote kwa mara moja. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru, wananchi wa Jimbo la Kishapu bado wanahangaika kuhusiana na kituo cha afya cha wilaya. Tumejenga kwa kutumia nguvu za wananchi, Mfuko wa Jimbo pamoja na Mgodi wa Williamson Diamond Limited. Mradi huu unahitaji jumla ya shilingi 175 kwa ajili ya kukamilisha, Mheshimiwa Naibu Waziri aliyepita kipindi kilichopita, alifika katika kituo hicho na akaahidi mwaka huu wa fedha watakamilisha kituo hicho cha wilaya...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninajibu swali la Mheshimiwa Butondo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Serikali imeahidi kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 kuwa inamalizia maboma 77 na imetenga takribani shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge pia boma lake la Kishapu tutaweka kwenye mpango na kumtengea fedha ili kuweza kukamilisha. (Makofi)
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Wilaya ya Nkasi haina kabisa nyumba za askari, jambo ambalo linasababisha usalama hafifu wa familia zao na utendaji hafifu wa kazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza nyumba za askari polisi katika Wilaya ya Nkasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Sigula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu maswali mengi ya nyongeza, Serikali inafanya tathmini kuangalia upungufu wa nyumba za askari katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo na Wilaya ya Nkasi aliyoitaja ili tuweze kutengea bajeti kwenye mpango na kutenga fedha kwa ajili ya nyumba za askari polisi kujengwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba, pamoja na majibu ya Serikali kwa swali langu, lakini miundombinu yetu ya barabara imeimarika sana, hususan barabara kuu. Hizi sheria zilizotunga speed limit ya 50 na 80 kiukweli ni kama zimepitwa na wakati. Sasa hivi tuna magari yanakimbia mpaka speed 280 na yeye kama Naibu Waziri atakuwa shahidi; je, hawaoni sasa uko umuhimu wa lazima wa kubadilisha sheria ya speed 50 kwenda angalau 80 na ile ya 80 kwenda angalau mpaka 100 hadi 120. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vilivyopo sasa hivi vya kilometa 50 kwa saa na 80 kwa saa viliwekwa baada ya kufanya tathmini ya hali ya barabara na kupokea maoni ya wadau mbalimbali na hatimaye zikawekwa kisheria. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafanya tathmini ya hali ya barabara ilivyo nchini na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kabla ya kubadilisha sheria hii ya viwango vya 50 kwenda 80 na 80 kwenda 100. Ahsante sana.
MHE. KHAMIS YUSSUF MUSSA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na yanatuletea faraja kidogo lakini kuna swali moja tu la nyongeza. Je, ni lini mchakato wa ukarabati huo utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Khamis Yussuf Mussa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2025/2026, tumetenga fedha hizo kwa ajili ya kuanza ukarabati wa hilo Jengo la Polisi Kwahani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la Mkoa wa Manyara la Kamanda linaendelea, lakini kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, tumetenga shilingi 800,000,000 kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Je, Serikali wapo tayari kunirudishia fedha zangu za Mfuko wa Jimbo, ambazo nilizitoa kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Liwale na hawataki kukijenga mpaka leo ni miaka mitatu? (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Sawa. Sasa ili nijue swali lako nilielekeze kwa nani fedha za Mfuko wa Jimbo alikabidhiwa nani? Walikabidhiwa Polisi ama bado zipo kwa Mkurugenzi, lakini wewe kwenye vikao vyako uliekeza kijengwe kituo, ili nijue nani ajibu swali lako?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, fedha hizi zilitengwa kwenye bajeti ya 2020/2021, tayari zipo Polisi lakini hawaoneshi nia ya kujenga hicho kituo mpaka leo? (Makofi)

SPIKA: Hapana, zilishatoka fedha kwa Mkurugenzi zikaenda Polisi?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, zipo Polisi.

SPIKA: Aaah! zipo Polisi.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, Polisi wamekubali kupokea na hati ninayo hapa waliyopokelea, lakini hawana nia ya kujenga hicho kituo ni mwaka wa tatu leo. Hizo fedha zirudi kwenye Mfuko wa Jimbo! (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuanzisha kujenga Kituo cha Polisi japo hajamaliza, basi sisi kama Jeshi la Polisi tunamalizia kituo hicho, lakini pia nitaonana naye baadaye tuzungumze jinsi alivyotuma fedha hizo. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Kasharunga, Kata ya Kasharunga katika Wilaya ya Muleba walijenga Kituo chao cha Polisi kwa nguvu za wananchi. Ni kwa nini Serikali haitaki kufungua kituo hiki? Watoe sababu wananchi waelewe. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta kama ifuayavyo:-

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza sana wananchi wa Kijiji cha Kasharunga kwa kujenga Kituo cha Polisi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya Bunge hili tutaenda kufungua kituo hicho kilichojengwa ili kuhudumia wananchi wa maeneo haya. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati Kituo cha Polisi Wilaya ya Micheweni wakati ni mara nyingi wametuahidi, lakini bado mpaka leo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Kombo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kukarabati vituo vyote vya Polisi ambavyo ni chakavu na kujenga vipya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo chake hicho alichokitaja kipo kwenye mpango na tayari tumefanya ukarabati ili wananchi wetu waweze kuhudumiwa kwa maana ya usalama wa raia na mali zao katika eneo lake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninaomba Kata ya Mapanda katika Jimbo la Mufindi Kaskazini ina changamoto kubwa sana ya Kituo cha Polisi. Je, Serikali ipo tayari sasa kutenga fedha ili wananchi wa Mapanda waweze kupata Kituo cha Polisi kizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ninapongeza sana Serikali kwa ujenzi wa Jengo la Polisi la Makao Makuu Wilaya ya Kilolo. Je, nini sasa mpango wa kuwajengea makazi Askari Polisi wa Wilaya ya Kilolo kwa sababu wanaishi mtaani na hawana Kambi ya Polisi wanaishi maisha magumu sana. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja; mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya polisi vya kata nchi nzima pamoja na shehia kwa upande wa Zanzibar, vituo hivi vinajengwa awamu kwa awamu. Kwa kuwa, Kata aliyoitaja ya Mapanda inahitaji Kituo cha Polisi, tutaiweka kwenye mpango ili na chenyewe kitengewe fedha kwa ajili ya kujengwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mkakati wa makazi ya Askari Polisi. Ni kweli maeneo mengi bado kuna changamoto ya makazi ya Askari Polisi, lakini Serikali inaenda kujipanga kwenye mipango yetu ili kuhakikisha kwamba askari wetu wanakaa katika makazi bora kwa ajili ya kuendelea kulinda raia pamoja na mali zao. Kwa hiyo, Wilaya ya Kilolo pia itakuwa ni mojawapo ya Wilaya ambayo tutaweka kwenye mpango kwa ajili ya kujengewa nyumba za makazi ya Askari Polisi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mbunge wa Jimbo la Busokelo na Mkuu wa Wilaya wamejitahidi sana kutafuta fedha za kujenga Kituo cha Polisi Busokelo; je, Serikali wataongeza nguvu lini ili waweze kumalizia kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya pamoja na wananchi hawa waliojitahidi kujenga kituo hicho na tutafanya tathmini kwa fedha zilizobaki ili Serikali pia iweze kuwaunga mkono kwa kazi hiyo nzuri iliyofanywa na wananchi wa Busokelo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nina swali dogo tu la nyongeza; ninaomba kujua lini Kituo cha Polisi katika Tarafa yetu ya Mchinga kitajengwa na hii ni kwa sababu hata Mheshimiwa Jumanne Sagini akiwa Naibu Waziri, alikuja akaangalia na akaona kadhia inayopatikana na hasa kwa askari wetu kuishi katika mazingira ambayo siyo rafiki. Swali langu, ni lini watatuletea fedha tujenge Kituo cha Polisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Tarafa ya Mchinga inahitaji Kituo cha Polisi na tayari Serikali imeshaahidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutatenga fedha kwa ajili ya kujenga Kituo hiki cha Polisi haraka iwezekanavyo kwa sababu wananchi hawa wa Mchinga wamesubiri kwa muda mrefu sana. Ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninashukuru kwa majibu ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; nchi yetu imekuwa na matukio ya wananchi kuchonganishwa hasa Jeshi la Polisi lakini kweli ni kwamba wanaofanya matukio ni watu wengine wakitumia mgongo wa Jeshi la Polisi. Ni ipi kauli yako ya kuhakikisha kwamba unawalinda Askari na kuondoa utapeli unaofanya na watu wabovu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwenye sheria zetu, maandamano na mikutano ni vitu vinaruhusiwa zinapoanza kampeni. Mmejipangaje kuhakikisha kwamba wanasiasa tunalindwa kikamilifu na kuhakikisha tunamaliza mikutano salama na maandamano yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inaongozwa kwa mujibu sheria na taratibu kwa hiyo kama wapo watu ambao wanafanya fujo au kuchonganisha wananchi kwa kutumia Jeshi la Polisi, ninaomba kutoa wito kwa watu hao waache tabia hiyo mara moja na watakaobainika sheria itachukua mkondo wake ikiwepo kufikishwa Mahakamani. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nianze kuipongeza Serikali kwa kutambua fidia ile ya wananchi 31 ya Kijiji cha Busengwa. Swali la kwanza; je, Serikali haioni haja ya kuanza kuandaa michoro ya gereza hilo ili fidia hiyo itakapolipwa ujenzi uanze?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali haioni kufanya ujenzi huo kwa haraka, ili kuokoa gharama za wananchi kufuata huduma hiyo ya magereza kutoka Nyang’hwale kwenda Geita zaidi ya kilometa 130?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuandaa michoro. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, michoro itaandaliwa haraka iwezekanavyo lengo letu ni tuhakikishe kwamba, gereza hili linajengwa haraka, ili kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu ujenzi kuanza haraka. Kama nilivyosema, baada ya kukamilisha michoro hatua inayofuata ni tutatenga fedha kwenye Mwaka 2025/2026, baada ya hapo ni kuanza ujenzi mara moja, ili wananchi wasipate tabu ya kutoka Nyang’hwale kwenda Geita ambako ni umbali mrefu. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Gereza la Wilaya ya Liwale limejengwa Mwaka 1982, lakini wananchi waliopisha ujenzi wa gereza lile mpaka leo hawajapata fidia. Nini Kauli ya Serikali ya kuwapatia fidia wananchi wale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba jambo hili nilichukue na niagize Jeshi la Magereza kwenda kufanya tathmini katika eneo hilo, ili wananchi hawa wapate fidia, kama ambavyo walitoa eneo hilo, kwa ajili ya ujenzi wa magereza. Ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itatoa majibu kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Gereza la Keko kwa sababu, Gereza la Keko wanalalamika ni eneo lao, lakini wananchi wanaozunguka hapo wana vithibitisho maalum kabisa kwamba ni eneo lao. Je, ni lini Serikali itaenda kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna mgogoro huo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaenda.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Kishapu wamechangia jumla ya shilingi milioni 250, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wilaya. Ni lini Serikali itatimiza ahadi iliyoahidi kwa ajili ya kuwachangia ili wakamilishe mradi huo na uweze kufanya kazi? Nakushukuru sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu rudia tena swali lako.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wilaya ya Kishapu wameshapata eneo, kwa ajili ya ujenzi wa magereza na tayari taratibu zote za fidia zimeshafanyika na Serikali ilishaahidi kwamba, itakwenda kutekeleza ujenzi huo kuanzia Mwaka wa Fedha 2024/2025. Je, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa? Ninashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatenga fedha kwenye Mwaka huu wa Fedha 2024/2025. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, as long as tumeshatenga fedha na bado mwaka wa fedha unaendelea, basi tutatekeleza mradi huo kwa ujenzi wa magereza katika jimbo lake. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza, naishukuru Serikali kwa kuwa tayari kwenda kufanya utambuzi kwa kuwa suala la kupata Kitambulisho cha Taifa ni haki ya kila Mtanzania aliyekidhi vigezo. Je, ni lini sasa zoezi hili litaanza kwa kuwa wafungwa waliokaa kwa muda mrefu magereza wakitoka wanapata adha ya kupata huduma? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Vijana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni haki ya msingi kila raia mwenye kigezo kupata Kitambulisho cha Taifa na ndiyo maana jibu la msingi tumesema NIDA ipo tayari kuwasajili wafungwa pamoja na mahabusu waliopo magerezani, lakini lini itaanza? Usajili huo utaanza katika Mwaka wa Fedha 2025/2026. Ahsante sana.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itawapa wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi Vitambulisho vya Taifa ambao wamepewa namba za NIDA tu kwa muda mrefu sasa na hawaelewi hatima ya kupata vitambulisho hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Noah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Mwezi Oktoba, 2023 tumetengeneza vitambulisho vya kutosha na niagize Msajili wa Halmashauri ya Arumeru kuhakikisha kwamba anavipeleka vitambulisho hivi kwa wananchi wote waliosajiliwa katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ahsante. (Makofi)