Supplementary Questions from Hon. Charles Muguta Kajege (34 total)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- Kwa kuwa barabara za Bugoma kwenda Mchigondo barabara ya Igundu kwenda Bulomba na barabara ya kutoka Mranda kwenda Mwiliruma hazipitiki kabisa kwa muda mrefu.
Je Serikali iko tayari kutengeneza barabara hizo kwa kutumia hata mfuko wa maafa?
Mheshimiwa Spika, kwa vile kuona ni kuamini yaani seeing is believing je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya kikao hiki tuongozane nae ili akajionee mwenyewe hali ilivyo katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hizi ambazo Mheshimiwa Kajege amezitaja katika Jimbo la Bunda zimeharibika kufuatia mvua nyingi sana ambazo zimeendelea kunyesha kote nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mpango muhususi wa kwenda kuhakikisha barabara hizi ambazo zimeharibiwa na mvua na hazipitiki zinatengenezwa mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kusafirisha lakini na kusafiri katika huduma mbalimbali za kiuchumi, na kijamii. Kwa hiyo, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha katika mpango uliopo tunatoa kipaumbele cha hali ya juu katika barabara hizi zilizopo katika Jimbo la Mwibara.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI tuko tayari wakati wowote kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge na kufuatana nao katika majimbo hayo ili tuendelee kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Kajege kwamba niko tayari baada ya kikao hiki tutapanga tuone ratiba nzuri ya kwenda katika Jimbo lake ili kuendelea kuwahudumia wananchi.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Umuhimu wa barabara ya Mkundi ni sawasawa na barabara ya Mugala kwenda Busambala. Je, ni lini Serikali itafikiria kuijenga barabara hii katika kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mwibara, mdogo wangu Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza eneo hili nalifahamu, mimi natoka katika Mkoa wa Mara na tumeshapata taarifa, Mheshimiwa Mbunge hapa ameulizia ili wananchi wasikie kama analisemea katika Bunge hili Tukufu. Mheshimiwa Mbunge tuliwahi kuzungumza nje ya box, inafanyiwa kazi na asubiri tarehe 17 na 18 atapata majibu sahihi. Kwa hiyo, watu wa Mwibara na Mkoa wa Mara kwa ujumla na mikoa mingine yote tutazifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo walilonalo Ulanga ni sawasawa na tatizo tulilonalo katika Wilaya Bunda hasa katika Jimbo la Mwibara. Je, ni lini Serikali itatusaidia kuondoa tatizo la madawa na vifaatiba katika zahanati zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA ((MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, anachouliza Mheshimiwa Mbunge ni lini Serikali sasa tutasaidia kuondoa tatizo la vifaatiba na dawa katika jimbo lake. Ukiangalia katika bajeti za Serikali kila mwaka tumeendelea kuongeza fedha ili kuhahakisha tunasogeza huduma hizi kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri, sisi wote ni mashuhuda bajeti ya vifaatiba na dawa kwa mfano katika mwaka 2015/2016 nchini ilikuwa ni shilingi bilioni 31, lakini katika mwaka 2021/2022 tunazungumzia bajeti ya dawa na vifaatiba nchi nzima ni shilingi shilingi bilioni 270. Kwa hiyo, niseme tu, tumeongeza bajeti tutaendelea kuongeza na kuboresha ili kuhakikisha tunaliondoa kabisa tatizo hili la huduma ya afya katika maeneo yetu yote nchini. Ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naipongeza Serikali kwa kuanza kufanya malipo hayo. Je, ni lini Serikali itakamilisha malipo ya madai yaliyosalia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhakiki na kupitia madeni yote ambayo maombi yao yameletwa. Mara tu utakapokamilika uhakiki huo, Serikali itaendelea kulipo kwa madeni yote yaliyosalia.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na matatizo ya magari ya kubebea wagonjwa katika vituo vya afya; je, ni lini Serikali itapeleka magari hayo katika Kituo cha Afya cha Kisolya na kile cha Kasuguti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, magari ya wagonjwa yatapeleka kwenye halmashauri zote 184 nchini kote na sasa ni maamuzi ya halmashauri kuona kipaumbele katika halmashauri yao ni kituo kipi cha afya ambacho kina uhitaji zaidi wa gari la wagonjwa.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je lini Serikali itajenga Vituo Vya Afya katika Kata za Igundu, Muhura na Kitengule katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege Mbunge Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge zinahitaji vituo vya afya, na amekwisha leta kama vipaumbele vya jimbo lake. Nimhakikishie, kwamba tumekubaliana na halmashauri, kwamba kwanza waanze kutenga fedha kwa awamu kupitia asilimia arobaini ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya hivyo; lakini pia Serikali itakwenda kuunga mkono nguvu hizo kwa ajili ya kukamilisha vituo vya afya katika maeneo hayo. Ahsante sana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naulizia kuhusiana na eneo la Bunda. Eneo lile limekua ni muhimu sana kwa maisha na uchumi wa wachimbaji wadogo wadogo katika Wilaya yetu ya Bunda.
Je, kwa nini Serikali isiende pale na kulikata lile eneo ili sehemu nyingine ibakie kwa wachimbaji wadogo wadogo.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la rafiki yangu Mheshimiwa Charles, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Madini, kazi yetu ni kusimamia Sera, Sheria na Kanuni. Wawekezaji wa machimbo ya madini wawe wa ndani au wa nje, kazi yetu ni kuwasimamia na inapotokea kwamba eneo lina maslahi mapana ya Kitaifa na wenye eneo wamegoma kabisa kutoa ushirikiano, tunachofanya ni kufuata sheria zilizowekwa za huo utaratibu unaobainishwa katika Kifungu cha 97 cha Sheria yetu ya Madini Sura ya 123, kwa kuangalia suala la fidia, suala la kuhamisha watu na kuwapangia makazi mengine kwa mujibu wa sheria ambayo inashirikisha Wizara ya Ardhi pia, Sheria ya Vijiji au Sheria nyingine inayohusika na masuala ya ardhi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swali moja; kwa vile Vituo vya Polisi vya Kibara, Bulamba na Kisorya vinatumia nyumba za wenyeji kufanyia kazi zake. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kajege kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za ulinzi wa wananchi ikiwemo kuhamasisha wananchi kushiriki kujenga vitu vya Polisi vya Bulamba na Kisorya. Napenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya tathmini ya kiwango cha fedha zinazohitajika kukamilisha vituo hivyo ili viweze kuingizwa katika mpango na bajeti itakayosomwa siku zijazo. Nashukuru.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante Mheshimiwa Spika, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Mkoani Mara mwezi wa Pili mwaka huu, alielekeza kwamba Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda iweze kujengwa. Je, ni lini Serikali itajenga hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege Mbunge wa Jimbo la Mwibara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni maelekezo ya kuyafanyia kazi mapema iwezekanavyo na tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeshaanza kuweka taratibu ili tuanze ujenzi wa hospitali katika Jimbo la Mwibara. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba suala hilo tayari linafanyiwa kazi.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jimbo la Mwibara ni kama limezungukwa na maji, lakini hatuna hata mradi mmoja wa umwagiliaji maji: Je, ni lini Serikali itajenga miradi hiyo katika Kata ya Namuhula, Igundu, Iramba na Kasuguti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Kajege, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni jambo ambalo ameliwasilisha hapa, nami nitaelekeza wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakalitembelee eneo hilo na baada ya hapo waone namna ya kuwasaidia wananchi katika eneo hilo kufanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na program ambayo imeitoa. Ila nina swali moja dogo la nyongeza. Kwa vile wahenga walisema seeing is believing, je, Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili, uko tayari tuongozane, mguu kwa mguu twende tukatembelee hizo shule ambazo nimezitaja ili uone jinsi ambavyo zimechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kwenda na Mheshimiwa Mbunge hata kabla ya Bunge kwisha, ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini zoezi zima la utambuzi katika Jimbo la Mwibara lime – collapse.
Je, ni lini Serikali itafanya tena zoezi hilo upya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mwijage, Mbunge wa Mwibara, samahani kwa kukuchanganya majina nimekuita Mheshimiwa Mwijage badala ya Mheshimiwa Kajege. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika eneo lako la Mwibara nikiri kwamba mimi kama Naibu Waziri sijapata taarifa za kina juu ya wapi tatizo lilitokea na nini kilitokea mpaka zoezi zima likasimama, lakini ninaomba nilichukue hilo jambo na baada ya kumaliza session hii ya maswali na majibu tukutane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujadili kwa kina tuone nini kinafanyika na wapi walikosea ili tuende tukasahihishe tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza tena kwamba ni nia ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanufaika wote wa TASAF tunawafikia na kuwatendea haki katika kupata wanachostahili. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza sikubaliani na majibu ya Serikali kwa sababu kila siku wanajipanga, wanajipanga; wanafanya utafiti, wanafanya utafiti; sikubaliana nayo, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa vile Jimbo la Mwibara linakabiliwa na upungufu wa chakula na mojawapo ya sababu ikiwa ni ukosefu wa skimu za umwagiliaji maji: Je, ni lini Serikali itaanza tena mpango wa kupeleka chakula cha msaada katika Jimbo la Mwibara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali inaendelea kufanya kazi kulingana na mipango kama nilivyosema, katika mwaka wa 2023/2024 kuna fedha nyingi zimetengwa kwa ajili ya skimu za umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na changamoto ya chakula katika Jimbo la Mwibara, utaratibu ni kwamba pale kunapokuwa na uhitaji wa msaada wa chakula katika maeneo husika, naomba viongozi ikiwemo kupitia Mbunge mweze kuandika barua ya maombi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili tuweze kuratibu namna ya kupeleka chakula cha msaada katika maeneo husika ili kufidia au kupunguza nakisi ya chakula na adha kwa wananchi katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na viongozi wengine ili kuandika barua na kupata maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Majengo ya Mahakama ya Mwanzo katika Jimbo la Mwibara yamechakaa kabisa. Je, ni lini Serikali itajenga upya majengo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimetangulia kusema kwamba fedha hizi ambazo tumezipata haziishi kujenga Mahakama za Mwanzo ni pamoja na za Wilaya, lakini tunajenga pia Integrated Justice Centers kwenye Mikoa, kujenga Mahakama Jumuishi kuanzia Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya, Mkoa mpaka ya juu. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mpango huu pia tutakufikia. Ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata ya Igundu na Namura katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga vituo hivi vya afya kadiri ya upatikanaji wa fedha na tutaangalia tena katika mwaka wa fedha unaofuata ili tuweze kuweka kipaumbele fedha hiyo iweze Kwenda. Na kama haipo tutatengea kwenye mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuna wananchi wengi wa Mwibara uliopisha mradi wa barabara kati ya Bulamba na Kisorya imechukua muda mrefu kweli bila kulipwa. Sasa naomba commitment ya Serikali: Ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu wakati najibu muuliza swali la msingi wananchi ambao bado hawafidiwa ni wale ambao wako kilomita I mean wako mita 7.5 kutoka kwenye barabara na ndiyo maana nilisema tunafanya tathimini ya nchi nzima. Wamepewa kazi hiyo wale Mameneja wa Mikoa kuangalia na kufanya tathimini ili tupate gharama halisi ili wakati Serikali inalipa basi iweze kujua gharama halisi ya fidia ambayo inatakiwa kulipwa ikiwa ni pamoja na wananchi wa Mwibara ambao wamepisha barabara hiyo ya Kisorya ya Bulamba, ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha na kuona, maana yake Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya compilation ya ahadi zote za viongozi wetu Wakuu wa Nchi na kuziwasilisha Wizara ya Fedha na kuona namna gani tutapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hizi. Hivyo basi, nimtoe mashaka Mheshimiwa Kajege kwamba baada ya kukaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha na kuona ni namna gani Serikali itapata fedha hizi, tutaanza ujenzi huu wa Hospitali hii.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; tatizo sio tozo peke yake kuna utitiri wa vituo bubu vya ukaguzi wa bidhaa barabarani; je, na hivyo vitaondoka lini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kajege kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ndio inawezekana lakini naomba hili tulichukue tulifanyie utafiti tuone kama zipo changamoto hizo ambazo zinakwamisha harakati za biashara tuweze kuzipunguza ama kuziondoa kabisa.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, tatizo la tembo, mamba na viboko ni kubwa sana katika Jimbo la Mwibara na imefikia kwamba wameuwa mpaka wananchi.
Sasa je, Serikali ina mpango gani au inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba, hilo tatizo linakwisha?
SPIKA: Hao viboko wanavamia mashamba pia? Wanavamia mashamba na wananchi?
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, yes, yaani kwa sababu wanatoka majini kwenda kula vyakula huko nchi kavu.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.
Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.
Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Mji wa Kibara ndiyo makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi hatuna stand ya mabasi. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Kajege kwa kazi nzuri na kubwa anayowafanyia wananchi wa Mwibara, lakini nimuelekeze Mkurugenzi na Halmashauri kwa ujumla kuainisha eneo hili kama ni eneo la kimkakati na kwamba ni mahitaji ya Halmashauri ili kuona uwezekano wa kupata stand katika eneo hilo.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, vituo vya afya vya Kasaunga, Kisorya na Kasuguti bado havina mashine za X-ray; je, ni lini vituo hivi vitapata hizo mashine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa UVIKO-19 Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajilli ya kununua digital X-ray 65 kwa ajili ya halmashauri zetu, lakini kwa sababu tunakwenda kununua kwa utaratibu wa kushirikiana na wenzetu wa UNICEF zinaweza zikafika zaidi ya 80, 90.
Kwa hiyo vituo vingi vile ambavyo vinahitaji X-ray vitapata, lakini kwa maana ya hospitali za wilaya kama kipaumbele na baadaye tutakuja kwenye vituo hivyo na tuta-consider pia vituo vya Mwibara, ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja na nasema ni ombi; kwanza nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo inafanyika katika jimbo langu. Naomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye tuweze kwenda Mwibara ili tukatembelee shule za msingi na zahanati husika.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Muguta Kajenge, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Kajege kwa kazi kubwa anayofanya kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Mwibara lakini tupokee shukrani nyingi na pongezi zake kwa Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na nimuhakikishie kwamba tutaendelea kutekeleza miradi hii kwa mnufaa ya wananchi wa Mwibara, lakini nikuhakikishie kwamba niko tayari tuambatane pamoja baada ya Bunge hili kwenda Mwibara kupita vituo, lakini pia na miradi mingine ya Serikali. Ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa Getere na mimi liko kwangu Mwibara; je, ni lini Serikali itajenga majokofu katika Vituo vya Afya vya Kasaunga, Kisolya, Kasuguti na Isanju?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaelekeza Halmashauri zetu zote kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha majengo ya mochwari, pia kutenga fedha ambazo zinapelekwa kwa ajili ya vifaatiba kwa ajili ya kununua majokofu ya mochwari. Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafuatilia kuona Halmashauri ya Rorya Jimbo la Mwibara pia wanatenga na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma zinazostahili. Ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya kutosha kwa ajili ya Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Charles Kajege Mbunge wa Mwibara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kajege tayari ameshanijulisha changamoto ya mawasiliano katika jimbo lake na tayari maeneo yake nimeshayachukua tutawatuma wataalamu wetu wakafanye tathmini ili tujiridhishe na ukubwa wa tatizo ili tupeleke ufumbuzi wa tatizo kulingana na changamoto iliyoko kule, ninakushukuru sana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa vile mfumo wa TASAF katika Jimbo la Mwibara umekufa, matatizo ni mengi, malalamiko ni mengi; je, ni lini Serikali itafanya upya zoezi la kuwatambua wanufaika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumjulisha Mbunge na pia kulijulisha Bunge lako kwamba mfumo wa TASAF haujafa. Tunazo changamoto katika maeneo mbalimbali ambayo kweli yako matatizo hasa katika eneo la utambuzi na uandikishaji wa wanufaika hao.
Mheshimiwa Spika, nataka nirudie tena kuendelea kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako kwamba kama liko tatizo lolote, ofisi zetu zipo kwa ajili ya kusikiliza na kama taratibu zetu zinavyoeleza, kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri yeyote, basi rufaa zitapelekwa hapo na taratibu kwa ajili ya kutatua matatizo au changamoto zinazotokea yatafanyika.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ukiona mchakato uliopo sasa hivi kufikia uamuzi huo ni mrefu sana. Kwa nini Serikali isiachie jukumu hilo katika level ya juu (Serikali Kuu) ndiyo ifanye maamuzi badala ya vikao vyote hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, utaratibu huu umewekwa kwa sababu kugawa maeneo ya kiutawala pia kuna hitaji ridhaa ya wananchi kutoka katika maeneo husika. Serikali hii sikivu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini hata Serikali zilizopita zinahitaji kuwashirikisha wananchi katika kugawa maeneo yao ya utawala ndiyo maana mfumo huu ni muhimu na vizuri sana utaratibu huu ukafuatwa, ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa Getere na mimi liko kwangu Mwibara; je, ni lini Serikali itajenga majokofu katika Vituo vya Afya vya Kasaunga, Kisolya, Kasuguti na Isanju?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaelekeza Halmashauri zetu zote kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha majengo ya mochwari, pia kutenga fedha ambazo zinapelekwa kwa ajili ya vifaatiba kwa ajili ya kununua majokofu ya mochwari. Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafuatilia kuona Halmashauri ya Rorya Jimbo la Mwibara pia wanatenga na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma zinazostahili. Ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika mgao wa watumishi wa afya ambao umefanyika juzi, nimeona bado katika vituo vyangu vya afya vya Kasaunga, Kisorya na Kasuguti havikupata; je, nini kauli ya Serikali sasa kuhusiana na upungufu huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, labda nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba aliona Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI akisema kuna nafasi zaidi ya 700 ambazo bado hazijapata watu, lakini kwenye Wizara ya Afya kuna nafasi vilevile ambazo zinaweza zikabaki. Watashirikiana Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI kuona, na aje tupange ili tuone ni namna gani inaweza kufanyika ku-fill hizo gap anazozisema. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga maabara na wodi ya kina mama na Watoto katika Kituo cha Afya cha Kasuguti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): -Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa ujenzi wa vituo vya afya ambavyo vina majengo pungufu kwa kadiri ya standard ya vituo vya afya ni mpango ambao unaendelea kutekelezwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuweka mipango kwa ajili ya kutafuta fedha lakini kwa ajili ya kwenda kufanya ujenzi wa majengo hayokatika kituo hiki cha afya, ahsante.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Wilaya ya Bunda, mwaka juzi, 2022, aliagiza hospitali nyingine ya halmashauri ijengwe katika Jimbo la Mwibara. Je, hospitali hiyo itajengwa lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya viongozi wetu wa kitaifa na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele namba moja katika utekelezaji wa shughuli zetu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kajege kwamba, tayari Serikali imeshaweka mpango na itaenda kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kujenga hospitali katika eneo hilo.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ni lini Vituo vya Afya vya Kasiguti na Kisole vitakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, vituo hivyo vya afya ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja sina taarifa kwa nini havijakamilika. Aidha, fedha hazijafika au hazijatumiwa vizuri. Kwa hiyo, naomba nilifuatilie niweze kujua hali halisi ikoje ili Ofisi ya Rais, TAMISEMI iweze kujua hali halisi ikoje ili Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuweze kutoa maelekezo kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Rais Samia mwaka juzi Wilayani Bunda aliagiza hospitali ya halmashauri ijengwe katika Jimbo la Mwibara. Je, ni lini hospitali hiyo itajengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Viongozi Wakuu wa Nchi ikiwemo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kipaumbele kikubwa sana katika utekelezaji wa miradi hii ya Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itakuja kuhakikisha kwamba inatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuna baadhi ya wananchi wa jimbo langu waliopisha ujenzi wa Barabara ya Bunda – Kisorya, bado hawajalipwa. Je, ni lini Serikali itakamilisha malipo yao?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kajege kuhusu fidia ya wananchi wa Barabara ya Bunda – Kisorya. Nimelichukua, tutafanya kila aina ya jitihada ili malipo ambayo tumeya-process kwa ajili ya fidia yaweze kufanyika. Ahsante sana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara ya kutoka Buguma kwenda Mchigondo kimeliwa na maji. Sehemu hiyo imekuwa ni karaha kubwa sana kwa akina mama, watoto na wazee kupita. Nataka Mheshimiwa Waziri aniambie, ni lini tutaongozana naye aende pale, aone tu jinsi akina mama wanavyopita pale wakivuka? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi wa wananchi wake. Kuhusiana na ombi lake mimi na yeye tutakaa tutajadili na tutapanga kwa ajili ya utekelezaji.