Primary Questions from Hon. Robert Chacha Maboto (6 total)
MHE. ROBERT C. MABOTO Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano ya ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Bunda kwa kuwa mpaka sasa hauna barabara za lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina barabara za lami zenye urefu wa kilometa 2.22. Barabara hizi ni za Boma kilometa 1.36; Malugu kilometa 0.42; DC kilometa 0.24 na Posta kilometa 0.2. Barabara hizi zilijengwa kufuatia ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Uendelezaji Miundombinu katika Miji (TACTIC) unaotarajiwa kutekelezwa katika Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji 45 ikiwemo Halmashauri ya Bunda Mji. Programu hii itahusisha pia ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Bunda kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyoainishwa na Halmashauri ya Bunda Mji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatekeleza ahadi zote za Rais zilizotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano kama ilivyoahidiwa na Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika hotuba aliyotoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021.
MHE. JAFARI W. CHEGE K.n.y. MHE. ROBERT C. MABOTO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itasambaza maji katika mitaa ya pembezoni kwa Kata za Kabasa, Guta, Kuzungu, Sazira, Nyatwali, Mcharo na Wariku katika Mji wa Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama na endelevu. Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Bunda ni wastani wa asilimia 69.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Guta inapata huduma ya majisafi na salama kupitia mtandao wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda. Aidha, kwa Kata za Kabasa, Sazira, Mcharo, Kunzugu, Wariku na Nyatwali zinapata huduma ya maji kupitia visima thelathini (30) vilivyofungwa pampu za mikono.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye kata hizo, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022, inatekeleza ujenzi wa miradi ya maji katika Kata za Nyatwali, Mcharo na Guta na ujenzi wa miradi hiyo utakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei, 2022. Serikali itaendelea kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Kata za Kabasa, Sazira, Kunzugu na Wariku.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kumaliza mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye leseni ya uchimbaji madini Kata ya Guta – Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mgogoro uliopo unahusisha wamiliki wa mashamba waliojichukulia haki madini (Mineral Rights) bila kufuata sheria kwenye eneo ambalo leseni zilikwishatolewa kwa mwekezaji aitwaye JB & Partners ambaye alipewa leseni ndogo za uchimbaji (PMLs) nane (8). Leseni hizi zimo ndani ya mashamba 21 ya wakazi wa maeneo ya Mtaa wa Stooni, Kata ya Guta Wilaya ya Bunda. Mpango uliopo ili kumaliza mgogoro huo ni kuendelea na majadiliano ili kufikia maridhiano kati ya wamiliki wa mashamba hayo na mwekezaji aliyepewa leseni. Hadi sasa kupitia majadiliano wamiliki wa leseni wamekwishaingia maridhiano na kusaini makubaliano ya uchimbaji kwa ubia na wamiliki wa mashamba 13 kati ya 21 wanaotambulika katika eneo hilo la uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mashamba 13 mgogoro wake ulifika tamati na machimbo kufunguliwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mnamo tarehe 6 Oktoba, 2022 na shughuli za uchimbaji zinaendelea. Wamiliki wa mashamba nane waliobaki waliogoma kufanya majadiliano na walifungua kesi ya ardhi (Land Case No. 12 of 2021) katika Mahakama ya Musoma ambayo inaendelea kusikilizwa. Hata hivyo, wamiliki wa mashamba hayo nane wamepatiwa nafasi nyingine ya majadiliano na katika maeneo yao uchimbaji umesimamishwa hadi pale watakaporidhiana. Endapo watashindwa kuridhiana ndani ya muda uliowekwa kwa mara nyingine basi taratibu nyingine za kisheria zitafuatwa kwa mujibu wa Kifungu cha 97 cha Sheria ya Madini, Sura 123. Ahsante sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Mji Bunda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zipo katika mpango wa kuanza kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha ambapo tayari kiasi cha Shilingi Milioni 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali ikiwemo upimaji wa udongo kwa ajili ya uhimilivu pamoja na tathmini ya athari za mazingira na jamii wakati wa ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itabainisha mipaka ya Kata ya Wariku - Bunda Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mipaka kati ya Kata ya Wariku na kata za jirani katika Wilaya za Butiama na Musoma zilianza kutatuliwa kwa njia ya vikao kati ya Mkurugenzi wa Mji wa Bunda na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Musoma na Butiama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya vikao hivyo, wataalam waliweza kuwakutanisha Viongozi wa Mitaa ya Kata ya Wariku na Vijiji vya Kata za Kyanyari (Butiama) na Suguti (Musoma Vijljini) na kutafasiri mpaka huu ardhini na kugundua kuwa sehemu ya Mto Wariku ulimeguka na kuacha njia yake ya asili kutokana na shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwa na suluhu ya kudumu, zitawekwa nguzo ndefu na pana (pillarrs) zinazoweza kuonekana na kila mwananchi. Kazi ya maandalizi ya nguzo hizo inaendelea na itakapokuwa tayari wataalam watarudi uwandani kwa ajili ya kuzisimika.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza changamoto ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imedhamiria kumaliza kabisa changamoto za uvuvi haramu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kuanzisha chombo maalumu kitakachokuwa na jukumu la kulinda rasilimali za uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi ikiwemo Ziwa Victoria. Chombo hicho kitakuwa na jukumu la kudhibiti uvuvi haramu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) imeanzisha mpango maalum wa mikopo isiyo na riba ya boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake vikiwemo nyavu halali nchi nzima ili kuwawezesha wavuvi kutumia vifaa vinavyokubalika kisheria, kufanya uvuvi wenye tija na kuachana na uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huo, Wizara imeanza kutoa boti hizo ambapo boti za kisasa 55 pamoja na vifaa vyake zimetolewa kwa Kanda ya Ziwa Victoria. Aidha, Serikali imekuja na mpango mahsusi wa kuhamasisha ufugaji samaki kwenye vizimba ambapo kwa kuanzia jumla ya vizimba 222 vimetolewa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa Victoria ili kupunguza nguvu ya uvuvi kwenye maji asilia (fishing effort).
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.