Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Elimu. Nazidi kushauri na kupendekeza Wizara hii kupewa fedha zilizoombwa na kuona uwezekano wa kuiongezea fedha nyingi Zaidi. Hii ni kwa sababu Wizara ya Elimu ni moja ya Wizara pekee zinazoweza kuzifikisha nchi yetu mahali tunapopata. Nasema haya kwa sababu ukiangalia hata katika Dira ya Maendeleo ya Taifa letu ya 2020 – 2025, katika yale malengo makubwa matano tuliyokuwa nayo, malengo yote matatu yanategemea sana elimu ili tuweze kufikia huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeonyesha tunahitaji kutoa zaidi ya ajira milioni nane na hizi ajira kwa hakika zitatokana na uboreshaji mkubwa wa elimu. Pia ni dhahiri kuwa, tafiti nyingi zimefanywa, kwa mfano utafiti mmoja wa ending poverty in India uliofanywa na Profesa Ramanuja umeonesha hakuna nchi yoyote inaweza ikaendelea zaidi ya maendeleo yake katika elimu. Kwa hiyo niombe tutenge fedha nyingi ili kuona tunaweka vizuri katika elimu

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa miaka mitano iliyopita pamoja na Wizara yote kwa ujumla, lakini niombe kuchangia mambo machache kwa ajili ya kuboresha zaidi na kufikia matarajio ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ikawekeze zaidi katika bajeti hii kuona tunapata Walimu wa kutosha. Shule zetu nyingi hazina Walimu wa kutosha, katika jimbo langu la Serengeti ukienda shule nyingi Nagusi, Serengeti, Machochwe na zingine nyingi hazina Walimu wa kutosha. Walimu wengi imeonekana wanaoletwa katika Jimbo la Serengeti, wanahama, wanaobaki ni wachache.

Sasa wakati tunajipanga kujenga nyumba za kuishi pamoja na mazingira kuboreshwa Zaidi, niombe Wizara ishirikiane na Wizara nyingine kuhakikisha kuwa Walimu wanaojitolea ambao wanatoka mazingira yale, tuweze kuwapatia kipaumbele katika ajira na mie niko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Waziri ili kuona kuwa tunawaajiri vijana wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri pia tuwekeze zaidi katika maabara, vitabu na mabweni. Shule yoyote ya sekondari isiyokuwa na vitabu vya kutosha na maabara ni sawa na kujenga bwawa la kuogelea lisilokuwa na maji. Na shule zetu bila kuwa na maabara, bila kuwa na vitabu watoto hawa tusitarajie kuwa na elimu tunayoitaka. Kwa hiyo, niombe fedha nyingi iende kuwekezwa huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuangalie kwasababu ya changamoto ya fedha kutotosheleza, katika jimbo langu na majimbo mengine ambayo wamejenga maboma ya maabara, maktaba pamoja na mabweni ziende kupewa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha mabweni, maabara pamoja na maktaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu shule za Sekondari za Serengeti na Dagusi, Shule ya Msingi Mugumu, Kitunguruma, Machochwe, Kisaka, Ngoremi wameshajenga maboma pamoja na shule nyingine nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende pia kushauri kwamba ili tufikie ajira milioni nane, sasa Wizara iende kuweka kipaumbele kikubwa katika ujenzi wa vyuo vya VETA, VETA zinahitajika sana ili tufikie lengo hili la ajira milioni nane. Kwa hiyo, niwaombe Wizara twende kufanya kazi kubwa. Katika jimbo langu tayari tumetenga maeneo yapo ya kutosha na tupo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kuhusu mitaala, tumelalamika sana, tumezungumza kuhusu elimu na Watanzania wengi wanaona kuna shida. Sasa wakati mwingine sit u kwamba kutoa degrees nyingi ni shida, lakini shida kubwa naiona katika suala la mitaala, mitaala yetu mingi ambayo tunaitumia, hasa ile ya knowledge-based education and training haiwezi kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala ya competence- based education (CBET) pamoja na outcome-based inaweza ikatusaidia. Mitaala hasa inayosimamiwa na NACTE inaweza kufanya vizuri sana. Kwa hiyo niiombe sana Wizara iangalie namna ya kuipa nguvu NACTE kuweza kusimamia mitaala hii. Na process ya utengenezaji wa mitaala, hasa katika situation analysis tuweze kwenda kuwekeza vizuri sana katika eneo hili. (Makofi)

Niishauri pia Serikali kuangalia vizuri suala la uongozi au management ya elimu. Leo ukiona katika shule nyingi walimu wakuu ndio hao sasa wamekuwa manesi, wahasibu, wamekuwa pia kama matron. Sasa kazi hii inawafanya ile core business yao iweze kuwa shifted. Tuombe sasa katika hizi shule tupeleke wahasibu, manesi na watu wa kusaidia shughuli nyingine, wakuu wa shule washughulike na kazi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia shule zetu nyingi sasa na Wizara yetu tunaangalia sana suala la matokeo ya mitihani zaidi ya process ya ufundishaji. Naomba management ya elimu sasa i-focus kwenye process ya ufundishaji.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe sana Wizara iweze kuhakikisha wanazipatia TCU na NACTE nguvu zaidi zitusaidie katika ubora wa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kushukuru na kuwapongeza sana Wizara ya Ujenzi kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya. Niwapongeze sana kwa mara ya kwanza kabisa barabara yetu ya kutoka Nata – Mugumu sasa imeingizwa katika ujenzi kwa kiwango cha lami, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunawashukuru kwa ajili ya kuonesha mpango wa kuanza kujenga barabara ya lami kutokea Tarime kuja Mugumu. Vilevile nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza TANROADS Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuiomba sana Wizara ya Ujenzi kutoa kipaumbele na commitment ya kutosha katika barabara ya Makutano – Nata - Mugumu. Barabara hii ni ya muda mrefu sana, imeanza kulimwa toka mwaka 2013 tayari kulipelekwa pale makampuni ambayo ilikuwa ni joint venture ya makampuni kumi. Ujenzi wake umeanza lakini umeendelea kusuasua sana, sasa hivi ni takribani miaka kumi barabara ile haikamiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia hata pesa ambazo zimekuwa zikiendelea kutolewa bado haituridhishi kama kuna commitment ya kutosha, hakuna priority katika barabara ile. Ukiangalia mwaka 2014/2015 kulitengwa shilingi bilioni 5.6 tu, 2015/2016 kukatengwa shilingi bilioni 2.2, mwaka 2016/2017 kukatengwa shilingi bilioni 12, mwaka 2017/2018 shilingi bilioni 9 na ukiendelea bado bajeti ile imeendelea kupungua kutoka shilingi bilioni 12 mpaka bajeti ya mwaka huu 2021/2022 kumetengwa shilingi bilioni sita tu, barabara ya kilometa 125.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ikumbuke barabara hii ya Makutano – Nata – Mugumu ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha. Barabara hii kwa mujibu wa Mpango na Dira ya Maendeleo ya nchi yetu tulikuwa tumejiwekea kwamba lazima kipaumbele kitolewe kuunganisha barabara zote za mikoa. Sasa barabara hii ya kuunganisha Mkoa wa Mara pamoja na Mkoa wa Arusha bado haijajengwa lakini barabara za mikoa mingine tayari wamejenga. Tunaomba sana Wizara iongeze commitment kubwa ya fedha katika barabara hii ili kuhakikiisha kwamba sasa inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna mkandarasi yuko pale sasa hivi lakini kuna shida ya menejimenti. Mimi nimewatembelea mwezi huu wa tano mwanzoni, pesa imetolewa tofauti na sehemu zingine pale watu wale bado hawajaanza kupambana kuhakikisha kwamba wanajenga barabara ile. Niombe sana Wizara muweze kupita pale na kusimamia mradi ule kwa karibu sana ili uweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile wameanza kuilima lakini bado fidia haijatolewa. Niombe sana Wizara iende kuhakikisha kwamba fidia zinatolewa na watu wale wanaweza kupata nafasi tena ya kuchukua maeneo mengine wafanye kazi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Uwanja wa Ndege wa Serengeti sasa uingizwe katika upembuzi yakinifu. Pia naiomba Wizara hii, kuna barabara ambazo zinapaswa kufanyiwa review tena ziingiwe katika barabara za TANROADS; tayari Wabunge wengi wamelalamika kwamba fedha haitosheleza katika TARURA, sasa ni vema tupeleke barabara nyingine zinazoweza kufaa kutokana na umuhimu wake katika uchumi, ziingizwe katika barabara za TANROADS. Katika Jimbo langu, barabara ya Mesaga – Masinki; barabara ya Mugumu - Mbalibali mpaka Machocho mpaka Nyansurura ni muhimu sasa ziingie kuwa barabara za TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara inayotoka Musoma kwenda makutano ya Nyakanga mpaka Rung’abure, ujenzi wake wa lami unasuasua. Mheshimiwa Waziri tunashindwa kuelewa kuna mpango gani pale? Mbona barabara ile inajengwa kidogo kidogo sana na barabara ile inaunganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Mji wa Musoma ambao ni Makao Makuu ya Mkoa? Tunaomba barabara ile iongezewe fedha ili ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba kuwepo na msukumo mkubwa wa ujenzi wa barabara hizi. Pia namwomba sana Waziri pamoja na Wizara yote kwa ujumla, waangalie sasa uwezekano wa kuzifanyia upembuzi yakinifu barabara mpya ambazo zina umuhimu mkubwa sana kiuchumi ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara inayotoka Nyansurura ikipita Majimoto mpaka Iramba mpaka Sorisimba ni muhimu sasa ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwanza, naipongeza sana Wizara hii ya Kilimo kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ambapo tunaona kwa mwaka jana imechangia zaidi ya asilimia 58 ya ajira katika nchi yetu. Ukiangalia Serikali yetu katika mapato inavyo vyanzo vingi, ikiwemo kutoka katika bandari, madini na utalii lakini tukienda kwa kipato cha mwananchi mmoja mmoja kule vijijini zaidi ya asilimia 95, 98 sehemu zingine wanategemea kilimo peke yake. Leo kilimo kinapoendelea ku-perform poorly maana yake wananchi watakuwa na hali mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, kule tunapotoka Wabunge wote wanafahamu hali za wananchi ni mbaya sana na hakuna initiative ya maana na ya pekee inayoweza kusaidia sana, yenye high potential for poor growth kama kuwekeza katika kilimo. Hata hivyo, trend zinaonesha sasa hivi hasa kwenye Jimbo langu na Majimbo mengine jirani naona kilimo kinaendelea kushuka na kila wakati watu wanaendelea kukata tamaa. Sababu kubwa ni masoko, kwa kweli masoko yanaendelea kuwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoa mfano, katika takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Dunia (FAO) Agosti, 2020 wameonesha Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika kwa kulima tumbaku kwa wingi ambapo Kenya ni ya tisa na South Africa ni ya saba. Hata hivyo, katika uuzaji wa cigarette, Shirika la FAO limeonesha South Africa ni ya kwanza, Kenya ni ya pili na Tanzania ni ya sita. Kwa hiyo, unaona wenzetu wamewekeza sana katika viwanda vya kilimo. Kwa hiyo, lazima Wizara sasa iende kuangalia inavyoweza ku-priotize katika masoko. Motivation kubwa sana ya kilimo kwa wananchi ni masoko tu kuwepo, haya mambo mengine yatakuja. Tukiwa na masoko ya uhakika wananchi watalima sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Wizara waangalie pia katika suala hili zima la kilimo biashara, bado kuna high cost of production katika nchi yetu kwa sababu ya inputs za agriculture zinauzwa kwa bei kubwa. Kwa mfano, mbolea au pembejeo kwa ujumla wake gharama ni kubwa, sasa hatuwezi kushindana katika masoko na wenzetu wakati sisi uzalishaji wetu ni gharama kubwa ukilinganisha na wenzetu. Ukienda nchi zingine zao lilelile katika unit ileile price inakuwa chini ukilinganisha na kwetu kwa sababu inputs cost yake iko chini sana. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iende kuhangaika sana na suala hili.

Mheshimiwa Spika, watu hawashindwi jambo kwa sababu hawana uwezo wakati mwingine watu wanashindwa kwa sababu ya wrong priority. Kwa hiyo, niombe priority kubwa sana katika Wizara hii sasa i-shift kwenda kuwekeza fedha nyingi katika kutafuta masoko, tutafute masoko ndani na nje ya nchi kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana pia Wizara iende kuangalia, wakati mwingine hatufanyi vizuri katika masoko kwa sababu ya unfavorable terms of trade. Ukiangalia wenzetu Kenya katika exportation maeneo mengi kuna free tariffs lakini kwetu bado cost zetu hata katika kusafirisha ni kubwa. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kazi ilifanyika pale Serengeti katika Skimu ya Nyamitita. Leo ukienda pale Nyamitita kumewekwa fedha nyingi na Serikali lakini bado skimu ile ya umwagiliaji haijakamilika niombe Wizara waende kuikamilisha.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo mengine mazuri sana ya umwagiliaji ambapo wananchi wanapambana sana lakini wanafeli kwa sababu hawajapata support ya Serikali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, maeneo kama ya Isenye, Nata, Nyambuleti yanahitaji skimu za umwagiliaji.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote nawapongeza sana Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nawashukuru kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia kila mara tunapokuwa na changamoto, lakini pia nawapongeza wameanza vizuri, kasi yao ni nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia, Dkt. Kijazi kwa kazi nzuri, wananchi wa Serengeti wanatambua kazi yake pia. Nampongeza Mhifadhi Mkuu wa Serengeti National Park, Ndugu yetu Mwishawa anafanya kazi nzuri. Nadhani wote wamesikia hifadhi ile sasa imekuwa ya kwanza mara mbili mfululizo katika kuwa hifadhi bora Afrika, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka siku moja Dkt. Bashiru alishauri Bunge hili ni vizuri likaweka record kuwa limeweza kusaidia ku-transform kilimo. Nishauri pia katika nchi yetu maeneo mawili pekee ambayo tunaweza tuka-compete kiuchumi ni kilimo na utalii tu, kwa sababu tunazo rasilimali nyingi sana katika eneo hili la utalii. Kwa hiyo niombe Serikali kwa safari hii tuwekeze sana katika utalii. Wabunge wenzangu wengi wamechangia kuwa bado performance yetu si nzuri uki-compare na rasilimali tulizonazo, lakini nikiangalia si kwamba kwa sababu Wizara haifanyi kazi, hawatendi kazi, no naangalia ni how much tuna-invest katika sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Wizara sasa ijielekeze core business yake iwe ni biashara ya utalii, siyo kwenye uhifadhi tu na tutoe fedha nyingi tu invest sana katika marketing. Marketing ina mambo mengi sana, ina watu wanaofanya kazi, product zetu, service delivery, miundombinu na vitu vingi sana. Kwa hiyo tujielekeze huko tunaweza tuka-transform sekta hii na kuifanya nchi yetu ifanye vizuri kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ningeomba Wizara hii pamoja na jitihada nzuri wanazozifanya, sasa waongeze kasi kwenye kutatua matatizo au migogoro iliyopo kati ya hifadhi pamoja na wananchi. Simba na tembo wameendelea kuua sana wananchi katika Jimbo langu la Serengeti. Najua jitihada zipo, lakini naomba ziongezwe na niombe sana Wizara hii ni vizuri sasa wale askari wa wanyamapori wa-shift focus yao, pengine wasikae kule ndani ya hifadhi, zamani wananchi walikuwa hawana awareness, sasa hivi hawaendi kuwinda.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa wale askari hata wangewajengea nyumba waishi huku vijijini, wapewe pia magari ili kwamba tembo anapoingia wawe huko, kuwapigia wale watu simu usiku ni ngumu. Sasa hivi ninapoongea ukienda Kata za Issenye, Natta, Nagusi ukienda Ikoma, Machochwe, kule Merenga, watu wanakaa usiku kucha wakilinda tembo wasiingie na wakati huo hawana silaha wala hawana magari. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara, waende sasa wawahamishe wale askari, sasa hivi watu hawawindi, wakae huku ili waweze kutusaidia kufukuza tembo wakati wa usiku.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo la mipaka, kuna vijiji saba mpaka sasa mipaka ile haijawa solved. Niombe sana mipaka ile waende kutatua hili tatizo, ni la muda mrefu na wananchi walifungua kesi, wakashinda. Niombe vile Vijiji vya Mbirikiri, Bonchugu, Sedeco viweze kusaidiwa ili viweze kuondokana na tatizo hili, limekuwa ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala hili la kutaifisha mifugo mbona toka wameendelea kutaifisha bado watu wanaingiza tu. Kwa hiyo unaweza ukaona kuwa, hii sheria haiwezi ku-work, ni vizuri sasa suala hili la uhifadhi tuwashirikishe sana wananchi. Tuwashirikishe kwa kiwango kikubwa, nafikiri tunaweza tukatatua tatizo hili na likaisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, niiombe Wizara hii iangalie namna ya kuongeza namna ya wananchi kufaidika zaidi na utalii. Hapa nishauri eneo moja tu, hizi hoteli za kitalii ni vizuri sasa Wizara itafute namna ya kuboresha sera, zijengwe katika vijiji vya jirani ili wananchi waweze ku-trade kwa urahisi na hoteli hizi, lakini pia uwepo wa hoteli hizi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi itaongeza ile spirit ya kuhifadhi hifadhi zetu pamoja na ku-change ile mind set yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Wizara tuende kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuona tunatengeneza miundombinu mizuri kule ndani ya hifadhi na katika vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi. Leo wananchi wengi ukiwaambia hizi hifadhi zina maana zinaweza kusaidia nchi, hawaoni maana yake. Unamuuliza mwananchi kwa nini aendelee kuingiza ng’ombe ndani? Kwa nini aingie ndani ya pori kuwinda? Yeye anaona akiingia yeye binafsi anapata faida kubwa kuliko faida ambayo anasikia kwamba Taifa linapata, lakini tukimsaidia, akaona shule zinajengwa, barabara zinajengwa, vituo vya afya vinaboreshwa, anaweza kuelewa na akawa mtu namba moja katika kuhifadhi maliasili zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022. Awali ya yote nimpongeze sana mama yetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuijenga nchi yetu na kuwaletea maendeleo watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika moja ya hotuba zake Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 alisema to build this country we have to make many changes. And to change it we must be willing to try what is new. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Wizara ya Fedha wamekuja na mambo mengi mapya bajeti yetu kwa mwaka wa jana kutoka trilioni 34 sasa trilioni 36 hongereni sana. Lakini kuna mabadiliko mengi tumeyaona wamekuja na mapendekezo mengi mazuri na mimi naamiini kama Waingereza wanavyosema where there is a will there is a way. (Makof)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi yetu sisi Wabunge ni kuwachangia kuwaonyesha njia ni kuwashauri nimeona baadhi yetu wakiwa na wasiwasi naamini tunaenda kufanikisha bajeti hii na ninadhani yawezekana tukavuka hata lengo hili endapo Wizara itaenda kuwekeza vizuri katika mambo yafuatayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja Wizara ya Fedha tunaishauri sana nimeona katika bajeti hii bajeti kwa maana ya kiasi gani cha fedha kimetengwa katika research and development bado ni kidogo. Nimejaribu sana kuzisoma nchi za China, nchi za Taiwan, South Korea, nchi za Israel nchi hizi zinaenda kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siri pekee ambayo wameifanya leo ukiangalia China kila mahali tunanunua vitu vyao kila kitu tunanunua China vitu vingi tunanunua China na uchumi wao unapaa sana lakini China kwa miaka 10 iliyopita kila mwaka katika bajeti yao wanatumia zaidi ya dola bilioni 380 katika research and development. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kufanya maajabu katika kuzalisha ajira nyingi kama uwekezaji wetu katika research and development bado ni kidogo. Taiwan, South Korea kila mwaka wanatumia Zaidi ya asilimia tatu ya GDP yao katika utafiti. Nchi ya Israel kila mwaka inatumia Zaidi ya asilimia nne katika research and development leo nchi ya Israel ni nchi ambayo inazalisha ajira nyingi pamoja na makampuni mengi ni ya pili baada ya Marekani na hiii ni kwa sababu ya uwekezaji mkubwa katika research and development.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna vijana wengi wanamaliza vyuo kuna watanzania wengi katika private sector wanahitaji kufanya vizuri lakini ni kwa sababu hatujawekeza sana katika research and development. Tax base yetu bado ndogo naamini tukiwekeza sana katika research and development tukawekeza kwa kiasi kikubwa investment spending yetu ikiwa kubwa katika research and development lazima tax base yetu itaongezeka. Kwa miaka hii na ijayo lazima pato letu litaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili lazima hizi sekta tatu kilimo, viwanda na biashara ya huduma lazima tufanye uwekezaji mkubwa sana investment spending katika sekta hizi tatu itakuwa ni tiketi pekee ya kuiondoa Tanzania katika umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kilimo chetu uwekezaji ni mdogo sana uwekezaji katika kutafuta masoko, uwekezaji katika kuwa-train wakulima, uwekezaji katika mitaji bado ni mdogo tunaiomba sana Wizara iangalie kila namna kupata fedha kwa ajili ya kuwekeza zaidi katika eneo hili la kilimo, viwanda pamoja na biashara ya huduma hasa ile ya utalii, na uwekezaji katika sekta hizi tatu utatutoa katika umaskini kwa sababu kubwa tatu sababu ya kwanza sekta hizi tatu zinaweza kuzalisha ajira nyingi sana na kwa sababu hiyo tutakuwa tumeongeza tax base kubwa sana katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, sekta hizi tatu ndizo sekta zinazoweza kutusaidia kuongeza sana mauzo ya nje. Vilevile tukiwekeza vizuri kwenye sekta hizi tatu itatusaidia kuondoa sana inflation katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Wizara iwekeze sana katika viwanda, tutoe fedha za kutosha sana na tuweke mazingira mazuri na ya kutosha ku-support ukuaji wa viwanda ili tuongeze ajira kwa vijana wengi ambao sasa wamehitimu na wako willing kuweza kuchangia katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sekta ya miundombinu. Miundombinu inayo-support utalii bado. Inasikitisha sana kuna maeneo tuna potential kubwa ya utalii lakini bado miundombinu ya barabara pamoja na ya viwanja vya ndege ni shida. Leo ukienda upande wa Magharibi wa Serengeti watu wengi wanahitaji kuwekeza lakini bado ujenzi wa barabara unasuasua, tunaendelea kupoteza Pato kubwa la Taifa. Kwa hiyo niiombe sana Wizara twende na priorities watu hawashindwi kwa sababu hawana uwezo bali wakati mwingine tunashindwa kwa sababu ya vipaumbele visivyo sahihi. Tukiongeza uwekezaji katika sekta hizi ni lazima tutaongeza tax base yetu. Hivyo ni lazima mapato yetu yata-shoot tunaweza tukafikia huko mbele hata ku-double hii bajeti ya tirioni 36.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais katika hotuba yake Wizara mbalimbali zimeahidi mambo mengi makubwa; na sisi sote tumeona Waheshimiwa Wabunge waki-report changamoto nyingi zilizoko majimboni. Tunaweza kufikia hili kama tutaongeza tax base tukakusanya mapato makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukiangalia sekta ya utalii utangazaji bado ni mdogo, investment yetu katika marketing ya tourism bado ni ndogo. Sasa niwaombe sana Wizara itafute namna ya kuongeza uwekezaji katika matangazo katika vivutio vyetu tulivyonavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuweza kufanikiwa sana katika tourism siyo function ya kuwa na rasilimali nyingi, kwa maana ya vivutio vingi ila ni function ya good marketing, na hii itatokana na uwekezaji mkubwa wa fedha katika eneo hili. Niiombe sana Wizara ya Fedha katika bajeti hii itafute kila namna inavyowezekana, kila mahali tunapoweza kupata fedha tuwekeze sana katika kuendeleza VETA pamoja na elimu ya ufundi nchini, hawa ndio wanaweza wakatusaidia katika kuzalisha ajira nyingi tukaongeza tax base na tukaweza kukusanya fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote naunga mkono hoja ya Kamati zote tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kutafuta fedha na kupeleka fedha nyingi sana za maendeleo katika Halmashauri zetu. Kwa kweli hii ni kazi kubwa sana amefanya na kushirikiana na Serikali. Bado tunaona wako baadhi ya watumishi katika Halmashauri zetu ambao wanaturudisha nyuma kutokana na utendaji wao wenye madhaifu makubwa pamoja na vitendo vinavyotia shaka katika matumizi ya fedha hizi zinazoenda katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mfano, pesa ambayo ilipelekwa katika ujenzi wa Vituo vya Afya karibu nchi nzima Shilingi Milioni 500, sasa hivi ukizunguka katika vituo vingi hivi havijakamilika. Vingi vimebaki tu majengo yako hapo, pia ukiangalia pembeni unakuta baadhi ya majengo utaona kuna vifaa vya ujenzi ambavyo vilikuwa vimenunuliwa vimebaki na hatua hiyo imeshapitwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii sasa inaleta mashaka, wanachi wengi wanafika mahali wanaitilia mashaka Serikali yetu na wanafikia mahali ambapo hawaiamini Serikali yetu. Sasa baadhi madhaifu ambayo yanaonekana katika kazi hizi kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; halmashauri nyingi zimeingia katika ujenzi wa majengo haya pasipokuwepo na quantity surveyors. Kwa hiyo, unaona BOQ nyingi ambazo zinaandaliwa, hazijaandaliwa na quantinty surveyors. Sasa mwisho wa siku jengo linafikia mahali halikamiliki ukiuliza wanasema hatukuwa na quantity surveyors. Sasa je, ni kwanini Serikali isitumie quantinty surveyors ili kuwa na uhakika wa gharama ya kujenga jengo hilo, badala yake tuanjenga na tunafikia mahali ambapo tunakwama na jengo halijakamilika, tunasema pesa hakuna?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunajenga tunafikia mahali vifaa vinabaki ambavyo havihitajiki tena na haviwezi vikatumika tena na ili hali tunasema kwamba hatukuwa na quantity surveyors? Inaigharimu shilingi ngapi hata kuweza ku–outsource quantinty surveyor ili tuweze kufanya kazi kwa uhakika?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia imeonekana kuwa watu wetu wengi wa manunuzi, kwa maana ya wale maafisa wa manunuzi, hawana knowledge ya kutosha katika supply chain management. Hivyo nitoe mapendekezo machache kwa ajili ya kuiomba Serikali iyafanyie kazi mapema ili tuondokane na changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; tunaomba sasa majengo yote yanayojengwa katika halmashauri zetu tusiingie kujenga majengo haya pasipo kuwepo na BOQ ambayo imeandaliwa na quantinty surveyors.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; hawa wataalam ambao wamesomea manunuzi, kila siku zinapoenda mtu anahitaji kuendelea ku-upgrade knowledge yake. Tunaomba hawa watumishi katika halmashauri ambao wanahusika na manunuzi wapatiwe knowledge ya supply chain management. Huwezi kukutana na habari ya material kubaki katika sites kama tutatumia watu wenye knowledge ambayo ni up to date.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini majengo yale ambayo yalijengwa katika halmashauri zetu na pesa zikaonekana hazitoshi yakiwemo majengo ya sekondari na majengo ya vituo vya afya, tunaiomba Serikali, kwa maana ya TAMISEMI, itenge pesa ili kukamilisha majengo yale kwa sababu sasa ni aibu kubwa sana katika maeneo yetu. Wananchi wanalaumu, wananchi wanalalamika na majengo yale yamekaa ilhali pesa nyingi ya Serikali imeenda pale na hakuna kinachoendelea. Naomba sana watu wa TAMISEMI watukumbuke pia katika kazi hii kule Serengeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda kuunga mkono hoja ya bajeti hii, lakini pia nitumie fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Elimu. Wizara hii inafanya kazi kubwa na kwa wale wanaofuatilia kuna mabadiliko makubwa yanaendelea katika utendaji ndani ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa jana nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya Ofisi za Wadhibiti Ubora katika jimbo langu pia na hapa Dodoma. Wanafanya kazi nzuri sana, rai yangu waongezewe vitendea kazi, magari pamoja na fedha za kutosha. Pia nimepata nafasi ya kutembelea mara kadhaa Ofisi ya Kamishna wa Elimu, wanafanya kazi nzuri sana sana, waongezewe kile kinachohitajika kwa maana ya fedha na vitendea kazi vingine wanaweza wakasaidia Taifa hili kufika mahali pazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimpongeze sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa leadership commitment kubwa ambayo ameiweka katika elimu. Nimefanya assessment ndogo kwa haraka, toka Rais wetu ameingia nimeona ameweka sana vipaumbele vikubwa viwili; elimu pamoja na uchumi. Toka Rais ameingia katika hotuba yake alijibainisha wazi anataka kuona mitaala inafanyiwa mabadiliko na akawa ametoa rai mitaala hii i- shift kutoka kuwa knowledge based kuwa competence based. Kwa hiyo hili ni jambo kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wetu katika majimbo tunayotoka karibu kila mtu hapa amesema anahitaji Chuo cha VETA. Kule Serengeti ili wananchi waweze kupongeza juhudi za Rais hizi ambazo zimekuwepo katika ujenzi wa madarasa wanahitaji sasa kuona pia wanafunzi hao wengi wanaomaliza wanaingia na kusoma kozi za ufundi ili waweze kujiajiri.

Kwa hiyo, nimwombe Waziri wa Elimu waendelee kukamilisha mipango ile ambayo wamekuwa nayo ya kuona sasa kuwa Chuo cha VETA kinajengwa katika Jimbo la Serengeti na wananchi wale waweze kupata elimu ya kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Mkoa wa Mara pale Butiama kuna Chuo cha Mwalimu Nyerere, Chuo cha Kilimo cha Mwalimu ambacho kitakuwa na branches moja ya branch itakuwa katika Jimbo la Serengeti. Eneo lile Mheshimiwa Waziri lipo na mpaka leo wananchi kila siku wanauliza mbona hakuna kinachoendelea? Kwa hiyo niwaombe sana ile mipango ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, sasa uingizwe katika utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuishauri wizara hii katika eneo la mitaala. Tumeona sasa kila mmoja wetu anaona hakuna uwezekano wa nchi hii kuendelea kuahidi kwamba kila anayemaliza university ataajiriwa na Serikali, haiwezekani ukienda Amerika na ukienda sehemu yo yote ile haiwezekani. Profesa Golan Hiden alifanya kazi katika nchi ya Kenya na Tanzania, amefanya kazi University of Nairobi na University of Dar es Salaam.

Katika machapisho yake kadhaa, alibainisha tofauti kubwa aliyoiona kwa nini Kenya ilikuwa ikiendelea kwa kasi ukilinganisha na Tanzania, aliona tofauti kubwa ni elimu; lakini bado alibainisha vitu hapa ambavyo ningeiomba Wizara hii ijifunze.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia mitaala, tunaanza kutengeneza mitaala, lakini nikiangalia pale kuna shida kubwa ambayo bado hawajai-address, elimu yetu tumeendelea kukazania mtu tu apate division one, division two, it’s okay watu washinde katika mitihani. Hata hivyo, nina uhakika na tunaona, leo tuna watu wana division one wana first class, lakini hawajiamini, hawawezi kuthubutu, hawawezi kufikiri na kuja na ubunifu. Kwa hiyo, kuna shida kubwa hapa, ni lazima hii mitaala sasa ambayo tuna-focus kuwa nayo lazima tutafute masomo yatakayowajengea vijana wetu uwezo wa kuwa wabunifu, uwezo wa kujiamini, uwezo wa ku-take risk na uwezo wa kufikiri vizuri mahali walipo na mahali pa kazi. Ndio maana sasa umeona sisi hatuwezi kushindana sana, ni kwa sababu vitu hivi vinapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naamini na baadhi ya Walimu wetu wanaotufundisha ujasiriamali ukiwafukuza kwenye kazi hizo hawawezi kufanya chochote. Sasa hii ni kwa sababu hawa ambao wanafundisha mambo haya hata hawaja-practice hawawezi ku-take risk, hawawezi kufikiri kitu kipya, kwa hiyo niombe sana hili lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nichangie katika mikopo. Mikopo inayotolewa katika elimu ya juu, sasa inaendelea kuleta manung’uniko makubwa miongoni mwa wananchi, imeanza kuona baadhi ya watu wanapendelewa, wengine wanapata mikopo na, wengine hawapati. Tumekuwa na vijana wengi mwaka jana hawakupata mikopo. Sasa leo tunaimba kwamba Taifa hili Watanzania waweze kuwa na patriotism. Patriotism haiwezi kuwepo kama mtu anaona Taifa halitendi kitu fulani ambacho anakitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, tuangalie kila inavyowezekana, tuone wapi tunaweza tukapunguza, vijana wote wanaoomba mikopo waweze kupewa. Kule katika elimu ya msingi na sekondari tuangalie vitu vinavyowezekana tukavipunguza ili twende kuwapatia vijana hawa mikopo wote wanaoomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotolewa vingi havioneshi uhalisia na ukweli wa hali ya maisha ya wananchi wetu na sababu za kuweza kuwanyima mikopo. Kwa hiyo, tuombe tuchukue shule ya msingi, vijana wanaaomaliza elimu ya msingi, baadhi wanapobaki hawawezi kufanya kitu chochote. Investment kubwa ya fedha inayopelekwa kwenye elimu ya msingi na sekondari haimpi mtu ujuzi, lakini tunapeleka fedha nyingi sana huko na hawa vijana ambao wanashindwa kusoma, kama leo tumefikiri kwamba Watanzania hawawezi kujilipia elimu ya msingi, tunawezaje kufikiri kwamba Watanzania wanaweza wakajilipia elimu ya University, ambayo ni fedha nyingi sana. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili kwa mwaka huu tuone vijana wetu karibu wote wanapewa mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nzuri ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. Awali ya yote nimshukuru sana Rais kwa namna ya pekee kabisa kwa jinsi ambavyo anapambana kuhakikisha Watanzania wanapata maji. Hii inatokana na a very strong political will aliyonayo pamoja na ubunifu mkubwa alionao katika kutafuta fedha.

Mheshimiwa Spika, pia pale Serengeti tuna watu wa RUWASA wanafanya kazi nzuri sana wakiongozwa na Eng. Mchele. Wameendelea kupambana kila wakati kuhakikisha mambo yanaenda vizuri. Tunao watu wa MUGUWASA, taasisi inayosimamia utoaji wa maji katika mji wa Mugumu, pia wanafanya vizuri sana, na hivi karibuni kulikuwa na shida kubwa ya maji kuchafuka kutokana na tope la mvua nyingi kunyesha bado walifanya vizuri wakasafisha matenki, kwa hiyo wanafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa kwa taasisi hizi mbili ni kwamba taasisi hizi ziongezewe vifaa vya kutendea kazi. Watu wa RUWASA hawana gari za kutosha, wanayo gari moja na imechoka ilhali wana miradi mingi ya kuisimamia. Kwa hiyo niombe sana Wizara, nimeona kwenye bajeti hamjawawekea fedha kwa ajili ya gari, niombe muwafikirie kuwaongezea gari. Lakini pia wanao watumishi wachache. Kwa mfano RUWASA wanaye engineer mmoja tu, engineer Mchele ambaye yeye huyo huyo ndiye Mkuu wa RUWASA katika wilaya nzima. Kwa hiyo mostly anafanya kazi za administration. Kwa hiyo tuongezee watumishi ili waweze kusimamia miradi hii vizuri kwa sababu component ya usimamizi ni ya muhimu sana ili tuweze kuwa na miradi mizuri na inayokamilika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wizara hii ya Maji. Wizara hii mnafanya vizuri sana, tumeona mkisimamia na kutekeleza majukumu yenu kwa umahiri mkubwa. Hii imechangia Wizara hii kuwa na mafanikio makubwa sana. Kipekee sana nimshukuru Rais wetu kwa kutupatia kijana makini mahiri kabisa, rafiki yetu Aweso, anafanyakazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Baraza kuwa limetangazwa Waziri wa kwanza kukutana naye nilikutana na Aweso. Aweso ni mtu mahiri, ni msomi mzuri lakini ni mtu yuko tayari wakati wowote kupokea mawazo ya na maoni ya watu. Ni mtu unayeweza pia ukamkosoa, hana tatizo anasikiliza na anapokea mambo. Kwa hiyo nilizungumza naye na kukosoa jinsi utekelezaji wa mradi wa chujio pale Mugumu ulivyokuwa ukiendelea; na Awezo aliniambia hebu usiwe na wasiwasi hii umetoboa. Kweli baada ya muda mfupi niliona utekelezaji mkubwa fedha imepatikana na mradi ule ukakamilika; kwa hiyo tunashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna jambo moja ambalo katika bajeti iliyopita, hii tunayoenda kukamilisha, ya mwaka 2021/2022; niombe sana Wizara, tuliomba kiasi cha milioni 800 hii ilikuwa kwa ajili ya kuhakikisha mradi huu sasa unapanuka kiasi cha kutosha. Kwa kufanya hivi ingetuwezesha kuondoa utegemezi ambao upo. Kumekuwa na utegemezi sana katika kuendesha ule mradi na kila mara tunawapigia simu umeme unakatwa kwa sababu mradi ule hauwezi kulipa gharama za umeme na zingine na zingine, sasa imekuwa ni shida. Pamoja na kazi hii nzuri ambayo Serikali imefanya ya kutupatia fedha na mradi ule wa chujio kukamilika na expansion ile ambayo Mheshimiwa Aweso ulipokuja mwisho wa mwaka wa jana ukatuongezea milioni 527; expansion ya mradi ule umefanyika kuelekea katika tenki ni nzuri lakini maji mara kwa mara yanakatwa. Sisi tuliamini kwamba kwa kupata hii milioni 800 tutapanua wigo wa mradi ule ili watu wengi wapate maji ili katika multiplier effect tunaweza tukapata fedha nyingi za kuendelea kuendesha ule mradi sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuombe sana katika muda huu uliobaki mtusaidie fedha hizi ili tuweze kukamilisha mradi ule na tuweze kusimama imara na kuendesha huu mradi vizuri. Hii itaondoa manung’uniko ya wananchi ambayo yanakuwepo mara kwa mara hasa huduma ya maji inapokatwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia ni vizuri ikakumbukwa kuwa mradi huu pamoja na kwamba kuna mradi ule wa miji 24, 28 bado ni muhimu kuendelea kupanua mradi huu, ambapo tayari tutakuwa tumeanza kufanya kazi ya sehemu ya mradi ule mkubwa unaokuja. Kwa hiyo tunaomba hili tuweze kutekelezewa.

Mheshimiwa Spika, lakini tunashukuru sana, kuna miradi mingine ambayo imeweza kukamilika katika baadhi ya vijiji kule Robanda kuna miradi mingine Makundusi kule Kebancha na vijiji vingine vingi. Tunaona kuna miradi inaendelea katika vijiji 56. Kwa kweli ni commitment kubwa na fedha hii imetolewa lakini bado pamoja na miradi hii mingi inayoendelea bado kuna zaidi ya vijiji 24 ambavyo bado havina maji kabisa. Kuna vijiji vya Masinki, Magange kuna vijiji vya Nyamihuru kuna ukienda vijiji vya kule Bisalala kuna vijiji vya Robanda ambapo tayari tumepata kisima kimoja lakini bado sehemu ni kubwa sana ambayo inahitaji maji.

Mheshimiwa Spika, bado ukienda Bwitengi na vijiji vingine vingi kama vile Kebosongo vingi sana havina maji. Sasa katika ile 85% ambayo Wizara imekusudia kufikia by 2025 naona Serengeti tunaweza tuka-lag behind, kwa hiyo tuwaombe sana Wizara tuone kila linalowezekana katika bajeti, hii kuona kwamba mmetutengea bilioni nne point something bado kungehitajika fedha nyingi zaidi ya kuongeza maana naona pale kuna vijiji kama vitano ambavyo vimewekewa fedha ambavyo ni Vijiji vya ijiji Ligicha, Nyiberekera Singisi pamoja na Nyamisingisi ambavyo viko jirani ambavyo mngeweza mkavi-connect na hiyo project havina maji bado.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niombe katika bajeti hii mpya 2022/2023 kuna mradi ule wa miji 28. Pale Serengeti tunahitaji mradi ule uweze kuwa mkubwa zaidi. Lile bwawa la Manchila wakati linajengwa lilikuwa kwa ajili ya kutafuta temporary solution ya maji katika mji wa Mugumu ambao ni Makao Makuu ya wilaya. Wakati ule Mugumu ilikuwa ni kijiji ilikuwa na watu wachache sasa watu ni wengi na ule mji bado unaendelea kuwa mkubwa; na hivi karibuni tunaendelea na maandalizi tukishirikiana na Serikali ya wilaya kwenda kwenye project kubwa sana ya Smart City.

Mheshimiwa Spika, project hii inaenda kujenga itahusisha ujenzi wa mahoteli makubwa kwa ajili ya huduma za kitalii tunaenda kujenga miundombinu mikubwa facilities nyingi sana ambazo zinahitaji maji. Maji katika lile bwawa ni lina cover kama ni almost mita cubic milioni 14.2 na wataalamu wanaonesha miaka 15 hadi 20 ijayo litashuka mpaka kufikia mita cubic 6,000,000 sasa hii na mategemeo yetu kwa miaka 10, 20 ijayo tunaweza tukawa tunahitaji zaidi ya mita cubic milioni 30.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna haja sasa huu mradi mkubwa badala ya kutumia bwawa la Manchila sasa mwende kuu-connect na ule mradi mkubwa unaotoka Mugango – Kyabakari – Butiama. Kutoka Butiama mpaka Mji wa Mugumu ni kilomita 90 tu. Tukifanya hivi tutapata maji ya kutosha na maji kwa muda mrefu. Ni vizuri tukafikiria kuwa na solution kuwa na matatizo ya muda mrefu kuliko kila siku ku-invest katika mean solution za muda mfupi, baada ya kusema haya naunga mkono hoja ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nampongeza sana Rais kwa jitihada kubwa anazozifanya za kutafuta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii ya jitihada kubwa za Rais kutafuta fedha kwa nchi yetu kwa ajili ya maendeleo kwa ujumla, nimepata maswali mengi sana, kwa nini sekta ya mifugo inapata fedha kidogo? Nilipoendelea kusoma document yao hii ya bajeti nimeona kuna changamoto kadhaa. Moja, sioni sayansi. Sijaona sayansi kabisa katika document yao. Ukiangalia ni kiasi gani cha fedha kimeelekezwa katika Research and Development, huoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakutana na changamoto kule Ziwa Tanganyika kwamba ghafla tu ziwa lifungwe. Je, kama tulikuwa tumewekeza kiasi cha kutosha katika R & D, leo tusingekutana na changamoto hii. Kama tungekuwa tumewekeza kiasi cha kutosha katika Research and Development tungepata malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya wana ng’ombe milioni 14 peke yake, lakini they are the second largest milk producer katika Afrika kwa ng’ombe milioni 14 tu. Nini walifanya? waliwekeza sana katika research and development. India sasa hivi wanalisha ulimwengu katika maziwa. Asilimia 24 ya maziwa yote duniani yanazalishwa India. Nini India wamefanya? Wamewekeza sana katika research and development. Kwa hiyo, bajeti hii haitoshi kwa sababu hakuna fedha ya kutosha kwenye research and development. Vyuo vyetu vya mifugo pamoja na uvuvi, unaona pesa nyingi ni kwa ajili ya uendeshaji tu, huoni fedha ya kutosha kwenye research. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni biashara katika bajeti hii. Ukiangalia katika ufanyaji wa biashara ya mifugo, Tanzania is highly costly. It is very cost kufanya biashara ya mifugo Tanzania. Nimeona kwa mfano biashara ya exportation ya 5 tons za mutton, nyama ya mbuzi, Tanzania gharama ni kubwa sana, ni zaidi ya Shilingi milioni 10 uki-compare na nchi ya Kenya. Kwa hiyo, ile mikoa ambayo iko pembezoni, wana-opt zaidi kufanya biashara Kenya kuliko Tanzania. Badala yake watu wa mifugo wangejielekeza kuhakikisha kwamba economies of scale inaongezeka kwa maana ya ku-encourage wafanyabiashara wengi kwa Tanzania na ndiyo ingeweza kupunguza ule utitiri wa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wenzetu wa Kenya unaweza ukatumia Shilingi bilioni 15 mpaka 16, wame-cut down zile cost nyingi kwa sababu kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara. Kwa kufanya hivi, nchi yetu pia ingeweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sijaona collection centers za maziwa. Maziwa yetu mengi hayaingii katika mfumo rasmi wa biashara kwa sababu, hakuna milk collection centers. Pale Serengeti tumejaribu kutaka kuweka kiwanda cha maziwa. Utafiti umeonesha, ni lazima mwekezaji atumie pesa nyingi sana kwa sababu bado Serikali haijawekeza kwenye collection centers. Kwa hiyo, tuiombe sana Wizara iende kuwekeza kwenye milk collection centers kwa sababu zitaongezea mapato mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuoni miundombinu ya ufugaji. Sasa hivi kule kwetu wanyama wengi wanaingia kwenye mapori, wanaenda kwenye mapori ya akiba, wanaingia kwenye hifadhi kwa sababu hakuna maji ya kutosha, na hakuna malisho. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii tutengee fedha ya kutosha. Serengeti peke yake tuna zaidi ya ng’ombe 600,000, tunahitaji zaidi ya majosho 30, tunahitaji zaidi ya malambo 25, kwa sababu yaliyopo sasa hayatoshi. Tunakuomba kwa uwekezaji huu, tunaweza tukawa- boost wale wakulima ili waweze kufanya uzalishaji mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado transformation ya income ya mfugaji ni ndogo. Leo ukienda vijijini wanahitaji zaidi fedha ili waweze kuendesha maisha yao, tofauti na huko nyuma. Pamoja na kwamba pesa hii ya mkulima na mfugaji, bado ingeongeza National income pamoja na individual income. Sasa kazi ambayo wenzetu wa Wizara hii wanayo, ni kuhakikisha maziwa na mazao mengine yote ya mifugo wanaweza kuyabadilisha yakaleta fedha na waongeze ubora, lakini sasa unaona hakuna jitihada hizi zikiendelea. Kwa hiyo, tuombe sana Wizara, wenzetu vijijini nao wanahitaji maisha mazuri, wanahitaji kulipia bili za umeme, maji, wanahitaji kusafiri, wanahitaji vocha, wanahitaji simu na haya yanawezekana kama tuta-transform sekta hii ya maziwa na sekta ya mifugo kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika vituo vyetu vya uzalishaji wa ng’ombe, ukienda pale Mabuki unaona kazi inafanyika, lakini vifaa gani wanatumia? Teknolojia gani wanayoitumia? Bado ni very old, haiwezi kufanya watu hawa wakasonga mbele, haiwezi kufanya wazalishaji wa maziwa wakapiga hatua kwa sababu, uzalishaji huu ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona soko la nyama, bado soko letu la nyama limeendelea kuwa na wasiwasi mkubwa duniani kwa sababu hatu-clear information. Ukiangalia kuna baadhi ya magonjwa ambayo yaliwahi kuikumba nchi yetu na mpaka leo hatujawahi kutoa taarifa katika ulimwengu juu ya magonjwa haya kwamba tumepambana nayo. Kwa hiyo, nadhani ukiangalia kwa ujumla huioni concept ya biashara, huoni jinsi gani Wizara hii imejipanga vizuri ku-trade, huoni namna gani inatafuta information ya masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Muhammad Yunus anadai ukienda China peke yake, mtu mmoja anatumia zaidi ya kilo 60 za nyama kwa mwaka. Ukienda Marekani mtu mmoja anatumia zaidi ya kilo 55 za nyama kwa mwaka; haya yote ni masoko. Ukienda Bangladesh kuna masoko makubwa, ukienda India kuna masoko makubwa, ukienda South Africa kuna masoko makubwa. Lakini kwa nini hatuwezi ku-trap masoko haya, ni kwa sababu hatujakaa kibiashara zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana wenzetu wakae kibiashara. Tunaomba wawekeze uwekezaji mkubwa, matokeo makubwa ya kufanya vizuri…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Amsabi, muda wako umekwisha.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru sana sana Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia pale Serengeti. Kwa muda mrefu kabisa barabara zetu zilikuwa ni changamoto, lakini Rais ametoa fedha nyingi, iko barabara sasa inajengwa kutoka Tarime mpaka Serengeti, lakini ipo nyingine kutoka kule Bunda mpaka katika Mji wetu wa Serengeti. Tunamshukuru Rais bado katika miradi mingi katika afya, katika elimu na kadhalika, lakini katika miradi ya maji tumeona akifanya mapinduzi makubwa sana. Katika miaka yake miwili iko miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa, iko Miradi ya Kibanchabancha, Nyiberekera, Rigicha, Gesarya, Motukeri, Nyamitita, Kenyana na Nyamakobiti, iko mingine mingi kwa sababu ya muda siwezi kuitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nishukuru kwa jitihada hizi za Rais za kutafuta fedha, miradi ambayo nimeipendekeza, nimewasilisha pia imeweza kuingizwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024. Upo Mradi wa Nyamisingisi, Nyamihuru, Gantamome, Bwitengi, Nyichoka, Iharara, Kuitete, Iseresere, Mesaga, Masinki, Ketembere, Misarara, Nyansurura, Tamkeri na Manyata, lakini pia viko visima 20 ambavyo vinachimbwa katika sehemu tofauti. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Aweso, Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ya usimamizi na utekelezaji wa shughuli hii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa muda huu mfupi niseme changamoto chache ambazo tunaziona na tunashauri zifanyiwe kazi katika Mradi wetu mkubwa wa Maji katika Mji wa Mugumu pale Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti. Tunamshukuru Rais kipekee, mradi huu ulikuwa umeshindikana katika miji yote 28, lakini Rais kipekee kabisa amepata fedha. Sasa bilioni 11.5 zinazokuja pale Mugumu kwa utekelezaji wa mradi huu naishauri sana Wizara iangalie namna ya kuupitia tena ule mradi. Ule mradi unakutana na changamoto ya scope, una-cover maeneo machache. Wakati mradi huu unakuwa designed miaka iliyopita huko wali-focus population ndogo.

Mheshimiwa Spika, Mji wetu wa Mugumu ulikuwa na watu takribani 30,000 na hata mji ulikuwa hujapanuka kiasi ambacho umepanuka sasa hivi. Sasa Mji wetu wa Mugumu una wakazi 59,348, ukiona ni karibu mara mbili ya ongezeko la watu ambao walikuwepo. Kwa hiyo, tunaomba, kwa mfano specific ukienda Kata ya Matare maji yanafika kwenye Eneo la Senza pale. Ukienda maeneo ya mbele Igina mpaka Shule ya Sekondari Kambarage, kuna zahanati imejengwa kule maji katika mradi huu hayatafika. Kwa hiyo, ombi letu na ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, mradi huu sasa uongezewe ile scope uweze kukutana na watu wengi kulingana na population ya watu ambao imeongezeka katika mji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya pili ni chanzo cha maji; katika chanzo cha maji cha mradi huu wa bilioni 11 iko changamoto kubwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri nilimwandikia barua, nimezungumza naye mara kadhaa na Waziri ameonekana kuwa msikivu. Waziri Aweso namfahamu ni mtu msikivu, ni mtu wa mabadiliko, ni mtu anayeweza kubadilisha vitu na akavifanya kuwa bora zaidi. Mradi huu najua kwa uwezo wako, kwa umahiri wako angekuwa ni yeye ndiyo ameu–design kwa wakati huu angeufanya kuwa wa tofauti, lakini nimwombe sana Mheshimiwa Aweso, bado hatujachelewa. Alituma wataalam baada ya ombi langu wakaja, wakafanya tathmini, kwa maana ya chanzo kile sasa ambacho ni kidogo. Wakati bwawa hili linajengwa lilikuwa na uwezo wa kuwa na maji lita milioni 23, sasa hivi limeweza kupungua mpaka lita milioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati linajengwa lilikuwa ni kwa ajili ya mji ule mdogo ambao ulikuwa bado kijiji, population yake ilikuwa ni around watu 7,000 tu. Sasa population imekuwa kiasi hiki, lakini pia mahitaji yamebadilika kwa maana ya namna ambavyo ule mji sasa unaendelea kubadilika na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, timu ile ilijielekeza sana kumshauri kuhusu kuchukua maji kwenye chanzo cha maji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na wakamwambia kwamba haiwezekani. Ni kweli kwa sababu tayari Mradi wa Mugango – Kiabakari - Butiama ulikuwa umeshafika mbali, lakini bado hawakuwa na option nyingine.

Mheshimiwa Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, watu wa Serengeti tunaona shida hii inaweza ikawa kubwa baadaye na upo ushauri wa wataalam wengi, Profesa James Scott wa University of Yale kule Marekani. Huyu ni Profesa wa Political Economy katika kitabu chake cha Weapons of the Weak, anasema long term solutions is the function of proper planning. Kwa hiyo, sisi katika hali yetu hii, uchumi wetu huu bado tunapambana hivi, tunapaswa kuwa na mpango ambayo ni sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Aweso aangalie, ilipangwa miradi mingi ya muda mfupi kutafuta solution ya muda mfupi mpaka leo tumepoteza fedha nyingi kwa ajili ya Taifa hili. Pale Serengeti ipo miradi ya HESAWA ilijengwa mingi sana, almost kila kijiji leo ukienda vijiji vingi vinaonekana havina maji, kwa sababu vile visima vilikuwa ni temporary solution. Iko pia miradi mingine ya mabwawa mengi katika sehemu mbalimbali za nchi ambazo yote mpaka leo inaonekana siyo kitu, miradi ile imeisha na tumefikiri tena miradi mingine.

Mheshimiwa Spika, unapofikiria long term solution lazima uangalie scope kwa upana kabisa, population ya watu inaongezekaje, mahitaji na vyanzo vyenyewe. Ukiona kama chanzo cha Bwawa la Manchira wakati ule kilikuwa kina vijito takribani nane vilivyokuwa vinaingiza maji. Kutokana na population pressure, wakati ule Serengeti ilikuwa na watu takribani 180,000, sasa kwa sensa ya 2022 tuna watu 340,349, watu wameongezeka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya pressure hii, vyanzo vingi vya maji vilivyokuwa vinapeleka katika bwawa hili vimeharibika. Kutokana pia na mabadiliko ya tabianchi hatupati mvua za kutosha. Kwa hiyo, ni dhahiri chanzo hiki cha maji ya Bwawa la Manchira hakiwezi kuwa cha kudumu ni cha muda mfupi. Kwa hiyo, hatutaki tena baada ya muda mfupi tuliingize Taifa katika shida ya kutafuta namna tena ya kujenga miradi mingine.

Mheshimiwa Spika, leo tumeshuhudia mahali pengi miradi ilijengwa baadae tena wanaacha yale mabomba wanaweka mengine, wanaweka mabomba makubwa. Huu ni uharibifu wa fedha ya Taifa hili. Kwa hiyo, tunamuomba ndiyo maana tumekuja na ushauri mkubwa kabisa kwa Mheshimiwa Waziri lazima tuwe na integrated water systems kwenye nchi. Kama kwenye nchi nzima ni shughuli kubwa basi walau iwe katika regional. Lazima tuwe na mpango ambao ni unganishi na shirikishi wa kupata maji katika Mkoa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Mkoa wa Mara, Mkoa wa Mara leo tungeweza tukawa na vyanzo vikubwa vitatu tu, vikubwa sana. Watu wengi hapa kila wakati wameshauri nchi hii ni vizuri tukawa na mipango ya miaka 50, miaka 60 kwa maana gani? Tunapofikiri kuwa na maji, tusi-focus kuwa na maji ndani ya miaka mitano au 10, tufikirie miaka 50 kwa maana hiyo tunaweza tukajenga mradi mkubwa wa maji kule Mugango ambao unge-fucus population ya watu zaidi ya milioni 10 kwa wakati unaokuja. Sasa leo tutaweka milioni moja, milioni mbili baada ya muda watu wameongezeka, maji yale hayatoshi tena tunaanza upya, tunatafuta fedha upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana Mji wa Mugumu utakapokuja katika ground bricking ceremony ya mradi huu mkubwa wa maji, tunaomba uje na taarifa ambayo wananchi wa Serengeti wanaitamani. Tunatamani kusikia tunao mradi mkubwa wa maji sasa unaanzia kule Rorya - Tarime na unakuja mpaka mji wa Nyamongo. Kutoka Nyamongo mpaka Mugumu ni takribani kilometa 57, ni rahisi sana kuleta maji katika Mji wa Serengeti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo rai yetu ni kwamba ule mradi tunauhitaji…

SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, tunamuomba sasa Mheshimiwa Aweso aweze kufikiria mradi ule uendelee lakini ujengwe katika scope ya kuchukua maji Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wataalam mbalimbali wa elimu na masuala ya maendeleo duniani wamebainisha uhusiano mkubwa wa matatizo mbalimbali katika Taifa yakiwemo ajira na ukosefu wa maendeleo endelevu kuwa na uhusiano mkubwa na elimu duni na pia kuwepo uhusiano mkubwa wa elimu na duni na mitaala duni na uwekezaji mdogo katika elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nampongeza Rais wetu, amezingatia ushauri huu wa wataalamu na sasa tumeona uwekezaji mkubwa kabisa katika elimu. Tunaona mapinduzi na mageuzi makubwa katika mitaala yetu. Kazi hii kubwa ambayo inafanyika, tumeiona na tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kipekee kabisa amesikiliza maoni ya Watanzania. Ni muda mrefu Watanzania walikuja na hoja hii ya uwepo wa mitaala mipya. Kwa mfano, katika aspect hii ya 7:4:2:3 na kuendelea, walikuja na maoni. Jambo hili ilianza muda mrefu, toka miaka ya 1985. Wenzetu Kenya walikuwa na mfumo kama huu, toka mwaka 1964 mpaka 1985. Walipofanya mabadiliko haya, kwao katika aspect hii wakaenda miaka minane, miaka minne, minne; kwetu Tanzania pia hitaji hili lilianza. Sasa kwa muda wote huo, hakukuwahi kuwepo mabadiliko mpaka wakati huu ambapo Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia amekubalia kufanya mabadiliko haya na tunampongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Serengeti tunamshukuru kwa pesa nyingi ambazo tumepata kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA ambacho tayari sasa kinaendelea. Nawapongeza watumishi wote katika Wizara ya Elimu kuanzia ngazi ya Wizara mpaka kule Wilayani. Kipekee kabisa nampongeza Prof. Adolf Mkenda pamoja na msaidizi wake, Naibu Waziri Mheshimiwa Kipanga. Nimeangalia mitaala ile, uwezo wa kutafsiri vision kwenda na kuiweka katika grounds vizuri kiasi kile, sisi tunawapongeza sana, tunawaombeeni kazi iendelee vizuri na muimalize vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri mambo machache, kama manne, katika kuchangia bajeti ya Wizara hii. Moja, fedha ile ya SEQUIP, fedha ya uboreshaji wa elimu ya sekondari, naomba fedha hii ipelekwe kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa shule za ufundi. Nasema hivi kwa sababu, shule hizi za elimu ya jumla, tayari tumekuwa nazo nyingi sana, na tayari sote tunaona shule hizi hazijaweza kutusaidia vizuri. Sasa Serikali inaendelea kujenga shule zile zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Serengeti pia tumepata shule ya Nagusi inajengwa. Shule kama ile tungependekeza ijengwe kuwa shule ya ufundi. Zipo shule nyingine zinazoendelea kujengwa, tungefika mahali ambapo tungehakikisha walau kila wilaya pamoja na uwepo wa chuo cha VETA iwe pia na Shule ya Sekondari ya Ufundi pamoja na Shule za Msingi za Ufundi za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuwa uwepo wa shule hizi za ufundi, zitasaidia sana kwenda kulisaidia Taifa letu kukabiliana na changamoto kubwa hii ya ajira ambayo tunaendelea kukabiliana nayo kwa wakati huu. Kwa hiyo, Wizara ya Elimu ikishirikiana na Wizara ya TAMISEMI, waone sasa ulazima wa kwenda kupeleka fedha zile katika ujenzi wa shule za ufundi. Kwa kufanya hivi, tutaisaidia Wizara ya Elimu kwenda kufanikisha mtaala huu mpya ambao wanakuja nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala huu kwa ujumla wake umejielekeza sana kuhakikisha tunahamia kwenye elimu ya ufundi na elimu ya vitendo kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo naomba sana hilo la kwanza. La pili, iko fedha ambayo tayari Serikali yetu imeomba World Bank na wamefanikiwa na pesa hii ndiyo hii tunaona sasa imeanza kutoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza hotuba za Mawaziri wengi inaonesha kwamba fedha hii itaenda kutumika na itaendelea kutolewa kwa muda wa miaka mitano. Ushauri wangu, fedha hii tungeiomba Serikali ifanye kila linalowezekana itoke haraka na itumike yote mapema, ikiwezekana tuitumie ndani ya miaka miwili ili tuweze kufanya mageuzi makubwa haya ya elimu ambayo sasa yanaendelea kuinjiniwa katika mtaala huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuwa tayari tumechelewa, tayari tuko nyuma, sasa ni vyema tufanye uwekezaji huu mkubwa kwa haraka. Katika uchumi, mradi wowote ukiutekeleza kwa muda mrefu, utaingia gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke tayari Wizara hii ya Elimu inahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa hizi shule mpya. Shule hizi za mtaala huu mpya ambao una–focus zaidi katika ufundi unahitaji vifaa. Tumemsikia Waziri akizungumza habari ya ku–train walimu, tumesikia uhitaji wa kuajiri walimu wengine wapya hii yote itawezekana kama tutaruhusu kwenda kutumia fedha hizi nyingi kwa haraka. Tukienda taratibu, tunaenda taratibu mwaka baada ya mwaka kwa miaka mitano, kuna uwezokano tusifikie tija nzuri ambayo tunaikusudia na hasa ambayo wenzetu katika Wizara ya Elimu wanaendelea kuifanya katika mitaala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi tutaenda kukabiliana pia na ule upungufu mkubwa wa walimu ambao tunauona upo katika shule zetu. Tayari inaoneka shule nyingi wanafunzi ni wengi sana madarasani, wanafunzi wengi wanakaa katika madarasa yetu wakiwa hata hawawezi kufundishwa na walimu wa kutosha. Wakati mwingine ile ratio ya one to fifty, kwenye shule za misingi na ile ratio ya one to forty-five imefika mahali inashindikana. Kwa hiyo, ndiyo maana tunaomba mitaala hii sasa twende kuitekeleza kwa uwepo wa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo hili kama unavyoliona limejengwa mara mbili, kuna ile plan ya Artech’s pamoja physical concession. Sasa wenzetu katika Wizara ya Elimu wanakuja na plan, wamekuja na plan nzuri ya namna watakavyo engineer mabadiliko makubwa ya elimu kwenye nchi yetu. Lakini ile utekelezaji wake, implementation ya mitaala hii bila fedha ya kutosha ya haraka, naona mabadiliko haya yanaenda kushindwa. Kwa hiyo, niombe Serikali, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu waone ulazima wa kupeleka fedha hii haraka na tusisubiri miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niombe sana mitaala ile nimeiona Mheshimiwa Waziri, mnafanya vizuri. Ushauri wangu muangalie, Marx pamoja na Friedrich Engels, katika kitabu chao maarufu kabisa duniani cha Das Kapital wanasema mode of production ita–determine jamii itakuwaje, elimu itakuwaje na mahusiano hata pia yatakuwaje, dini itakuwaje na jamii itakuwaje sasa katika utengenezaji wa mitaala hii ni lazima watengenezaji wa mitaala hii waangalie sana je tunazingatia context ipi katika utengenezaji wa mitaala hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho la ushauri wangu, niombe sana Wizara ya Elimu iangalie sasa ufundishaji bora wa kingereza. Iko shida katika namna ambavyo kingereza kinafundishwa wote ni mashahidi hapa hakuna mtu amewekwa darasani akafundishwa kiswahili lakini kwanini kingereza kinakuwa kigumu cha kueleweka? Ni namna ambavyo kinafundishwa approach imekuwa siyo sahihi. Nimeona mara nyingi mchina, muhindi akijifunza kingereza ambayo siyo lugha yake ya kwanza anaweza kuongea vizuri, lakini sisi waswahili tukijifunza kingereza iko shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Elimu waangalie approach mpya ya kufundisha lugha ya kingereza na mwisho na kabisa niombe Wizara ya Elimu maombi matatu. Moja chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere pale Serengeti eneo lipo, naomba mtukumbuke katika ujenzi wa benchi pia shule ya msingi na ufundi Mgumu tunaomba mtukumbuke, iweze kuboreshwa katika mpango wenu na mwisho tunaomba sekondari mpya ufundi pale Serengeti na ikikupendeza tuijenge katika kijiji cha Mesaga kule Ngolemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsnate sana. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake madhubuti katika nchi yetu ambao umeendelea ku-push maendeleo makubwa katika Taifa letu. Jambo ambalo kila mmoja wetu anashuhudia kila sehemu ya nchi yetu maendeleo yapo na ikijumuisha Jimbo letu la Serengeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri ndugu yetu Mchengerwa, nimesikia habari zako nimeona wakati ukiwa Wizara ile ya Utamaduni na kwa kipekee kabisa nimewahi kuleta kwako habari za kujenga kwa haraka barabara ile ya lami ya kutoka Tarime mpaka Mugumu, kutoka kule makutano mpaka Mugumu kwa ajili ya kuboresha utalii kufikika kwa Serengeti na nimeona jinsi ambavyo umepambana kusaidia na ku–push barabara ile. Kwa hiyo, nakupongeza nimeona kazi yako ni kubwa ni nzuri na nikueleze watanzania tunayo matarajio makaubwa sana juu ya mabadiliko katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara hii ni ya kibiashara, Watanzania tunahitaji fedha nyingi ili tuboreshe nchi yetu kwa hiyo utaenda kutusaidia kuhakikisha nchi sasa inapata fedha nyingikupitia Wizara hii. Tunampongeza pia Naibu wako Mheshimiwa Mary Masanja toka ameingia tumeshirikiana naye sana kila wakati kutatua changamoto mbalimbali kule na amekuwa mstari wa mbele sana katika ku–push ujenzi wa uwanja wa ndege katika Mji wa Mugumu kule Serengeti. Kwa hiyo tunakupongeza sana Naibu Waziri endelea kuchapa kazi pamoja na Waziri wako tuko pamoja na ninyi. Nampongeza pia Dkt. Abas, Katibu Mkuu kwa utendaji mzuri, Naibu Katibu Mkuu Bwana Anderson, Kamishna wa TANAPA ndugu yetu William Mwakilema, Mkuu wa hifadhi ya Serengeti ndugu Msindai wanafanya kazi kubwa nzuri kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani yetu ya Uchaguzi 2025, tulibainisha kuwa tunahitaji kukuza kiwango cha watalii wanaokuja nchini waongezeke mpaka kufikia milioni tano. Ndipo sasa kwa muktadha huu ninayo mambo machache ya kuchangia kwa ajili ya kuona namna gani tunaweza tukafikia hili pamoja na kuboresha uhifadhi. Moja, niombe sana Serikali iende kuhakikisha inaongeza fedha katika utangazaji wa vivutio vyetu na hapa nishauri kabisa ni vyema tuone kuweka mfuko maalum kwa ajili ya promotion ya tourism sites au tourism attractions katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Mheshimiwa Rais alikuja na ubunifu mzuri kabisa wa ile filamu ya Royal Tour baada ya pale hatujaona ubunifu mwingine ukiendelea, hatujaona kazi nyingine kubwa endelevu katika kuitangaza Tanzania kimataifa, lakini tukianglia sana wataalamu wapo na watu wapo weneye uwezo, nia wanayo. Tunadhani tu sasa Serikali iende kuongeza pesa ya kutosha kwa ajili ya kuona kwamba tunaitangaza nchi yetu kwa kiwango kiubwa, ili tupate fedha nyingi. Nimeona azma hii Mheshimiwa Mchengerwa unayo umeisema leo sasa basi tuiombe Serikali ikuongezee fedha za kutosha ili kazi hii ifanyike kwa ubora mkubwa kabisa, tuweze kujipata kipato kikubwa na nchi yetu ipate maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine tuhakikishge vivutio vyetu vinafikika vizuri kwa haraka na kwa gharama nafuu na katika hili nishauri kivutio kikubwa katika nchi yetu ninachokifahamu mimi. Vipo vingine lakini kivutio hiki katika hifadhi ya Serengeti cha crossing ya wale wild beast katika Mara River ni moja na vivutio bora kabisa duniani. Kiko katika vivutio 15 bora, lakini kwa nini hatupati watalii wengi katika eneo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu ni kwa sababu ni mbali sana, hapafikiki inachukua muda mrefu sana watalii kufika kule, magari yanaharibika sana njiani, watalii huchoka sana, wanatumia masaa mengi barabarani, wanakosa comfortability, gharama kubwa ya kufika huko, barabara zinakuwa mbovu muda mwingi, umbali mrefu siyo mzuri kwa usalama wa watalii na hivyo basi wamewahi kufanya tafiti na tumesoma ripoti nyingi za wale mawakala wakubwa wa utalii duniani, wakiwemo Hot Wire, wakimwemo Agoda na wakiwemo Expedia wamesema ili watalii waende katika sehemu fulani kwa ajili ya kutalii, yako mambo yanayo-lead ile decision yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, 42% ni ubora wa kivutio, 20% ni ubora wa huduma za malazi, chakula na usalama, 20% ni kufikika kwa kivutio, ubora wa miundombinu ya barabara na usafirishaji, 18% ni unafuu wa gharama. Sasa basi ukiangalia pamoja na kivutio kizuri, pamoja na uwepo wa vivutio vingi sio sababu ya kutosha watalii kuendela kuja kwa wingi katika nchi yetu. Mfano mzuri tunaona Serengeti na hata nikienda kwa mfano mmoja rahisi tu, ukiangalia kutoka katika viwanja yetu vya ndege mpaka kufika sehemu hii ya kwa Kogatende ambako wanyama wale wanakatiza ule Mto Mara kuingia upande ule wa Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka KIA mpaka Kogatende ni kilomita 610, kutoka uwanja wa ndege wa Arusha mpaka kwa Kogatende ni kilomita 557. Kutoka Mwanza Airport mpaka Kogatende pale Mara River ni kilomita 340. Kutoka Seronera kutoka Musoma, uwanja wa Musoma mpaka pale kwa Kogatende ni kilomita 187, kutoka Seronera central Serengeti mpaka kwa Kogatende ni kilomita 183, lakini kutoka Mji wa Mugumu mpka kwa Kogatende ni kilomita 56 peke yake na hili ndilo eneo ambalo limependekezwa kujenga uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana andika historia, jenga uwanja ule 147,000,000 wataalam wameshauri, tafiti zimefanyika, nikuombe Mheshimiwa Mchengerwa chukua hatua, hii itasaidia watalii kuongezeka, itasaidia kukua kwa uchumi kwa watu wa Mkoa wa Mara hususani Wilaya ya Serengeti ambao sisi tunapakana na hifadhi hii, tunahitaji kuona pia na sisi tunanufaiuka na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawasaidia watalii wengi kupunguza gharama za kuja kwetu, kupunguza umbali huu maana ya ke ni kupunguza gharama. Ni kupunguza kulala vituo vingi na hii itafanya watalii kwa comfortability kubwa tukijenga uwanja ule. Pia tunaenda kuongeza ajira nyingi kwa watu wa Mugumu na Serengeti kwa ujumla, tunaenda kusababisha kuongeza au kuboresha utalii na ule uhifadhi kwa sababu sasa ule utitiri wa vile viwanja vya ndege ndani ya Serengeti vinaenda kupungua. Pia tunaenda kuongeza maeneo ambayo watu wengi wanaweza wakajenga mahoteli ya kitalii katika Mji wa Mugumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuomba sasa wizara hii iende kuangalia namna bora ya kuongeza na kuboresha...

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: …uhifadhi katika hifadhi ya Serengeti kwa kushirikisha sana wananchi ili kupunguza migogoro ya wanayama wanaingia na kuvamia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja nakuomba dakika moja tu nimalizie. Sasa wananchi wengi sana wa Serengeti wamepata shida, wanyama wanaingia kila wakati, Mheshimiwa Mchengerwa nikuombe sana tusaidie kuona kwamba tunawashirikisha wananchi. Kama hatuweki tutumie teknolojia ya fensi, basi twende kuchukua wananchi wengi waweze kuelimishwa, waweze kuelekezwa, mambo ya kukamata wanayama wale ng’ombe na nini na wananchi wanaoingia waelimishwe sana.

MWENYEKITI: Haya ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote nampongeza sana Rais wetu kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya hasa ya kuhakikisha pesa inapatikana kwa ajili ya sekta ya uchukuzi katika nchi yetu. Pia Wizara hii wanaendelea na kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi nawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, ili nchi iendelee ni lazima kila wakati ihakikishe inakuwa na vipaumbele sahihi. Wizara hii kwa takribani miongo mitatu imejikita sana katika kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vya lami, tunapongeza sana jitihada hizi. Lakini jambo ambalo nimeliona kwa kiasi kikubwa vipaumbele kwa maana ya barabara gani ijengwe ni jambo la msingi sana, kwa wakati mwingi huko nyuma tulijikita sana katika kuhakikisha tunajenga barabara pamoja na viwanja vya ndege kwa ajili ya malengo ya kiutawala, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jamii inaweza kukutana. Hii ni jambo zuri lakini nadhani kwa wakati huu ambapo Taifa letu linahitaji kuweza kuendelea kiuchumi tena kwa haraka ni muhimu sana tuende kuzingatia barabara ambazo zinaweza zikatuletea manufaa makubwa kiuchumi tupeleke fedha nyingi huko kwanza.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano wa barabara hii inayotoka Makutano, Sanzate, Nata, Mugumu inaenda mpaka Tarime na kutuunganisha na nchi ya Kenya pia inaenda mpaka Arusha. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kidogo sana, ni zaidi ya miaka 10 barabara hii haikamiliki, lakini ukiangalia barabara hii ina manufaa makubwa sana kiuchumi. Katika hifadhi ya Serengeti ambayo sote tunafahamu inatuingizia fedha nyingi sana, product kubwa sana ya kiutalii inayouza ni ile migration na ku-cross Mara River ambayo iko upande wa Magharibi wa hifadhi ya Serengeti, sasa upande ule hakuna barabara zinazoenda.

Mheshimiwa Spika, ningependa kushauri Wizara itambue hili, tunaweza tukadhani kwamba Serengeti ni maarufu watu watakuja Hapana! hawawezi kuja kama hatujaweka miundombinu mizuri. Kwa hiyo, ninashauri sana lazima Wizara sasa iangalie zile barabara ambazo zinaenda kutusaidia kuingiza fedha nyingi sana hasa barabara hii ni lazima tuzikamilishe kwanza ili pesa ipatikane tuweze kupeleka sehemu zingine na nchi ipate maendeleo.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mrimi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninampa taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, ni kweli barabara hii ni muhimu na imechukua muda mrefu sana, hivyo ni vema sana

SPIKA: Taarifa ya ziada kwa alichokuwa anakizungumza.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya ziada ni kwamba Serikali itoe pesa barabara hii imechukua muda mrefu sana zaidi ya miaka Kumi.

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mrimi.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Bulaya kwa taarifa.

Mheshimiwa Spika, barabara hii sasa ni muhimu ikamilike. Siyo tu kwamba wananchi wa Serengeti wanapata adha na Mkoa wa Mara kwa ujumla, lakini pia tunalikosesha Taifa mapato makubwa sana. Leo kuna barabara kwenye nchi hii ukipita, zaidi ya masaa kumi wanapita tu mbuzi, ng’ombe, mbuzi, ng’ombe, hazina manufaa makubwa sana kiuchumi lakini bado leo tunaona barabara ambazo zingetusaidia sana katika uchumi hazijengwi, hazikamiliki fedha inapelekwa kidogo. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iende kuhakikisha barabara hii sasa inakamilika, tunaiomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia uwanja wa ndege ujengwe katika ule Mji wa Mugumu ili tuweze kupata watalii pale moja kwa moja. Rais amejitahidi, ameitangaza nchi yetu kwa maana ya Royal Tour, ni vizuri uwanja wa ndege ujengwe pale kama wenzetu wa Masai Mara wanavyojenga uwanja kule kwao. Tujue kwamba Masai Mara ni substitute ya Serengeti, kwa hiyo, tukichelewa tutakosa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, pia niikumbushe Wizara hii, huko nyuma kama factor kubwa ilitumika kwamba tunaunganisha barabara zote zinazounganisha Mikoa. Mheshimiwa Rais Kikwete mwaka wa 2021 tukiwa Chato alisema ilibaki barabara ile inayounganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha ambayo ndiyo inayopita hapo na Nata mpaka Mugumu hadi Arusha. Mpaka leo barabara hii haijawahi kukamilika. Kwa hiyo, naomba sana Wizara kama basi factor ni kuunganisha Mikoa yote, Mkoa wa Mara pamoja na Mkoa wa Arusha bado haujaunganishwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho nimalizie kuomba Wizara hii iende kutoa fedha kwa ajili ya kulipa fidia. Ukienda pale wananchi wa Isenye, wananchi wa Nata, Nyichoka na sehemu nyingine barabara hizi ambapo zinapita, mpaka sasa wananchi hawajawahi kulipwa fidia, wanalalamika na barabara ukienda pale Mkandarasi sehemu nyingine amesimama, hajengi, ameruka kwa sababu wananchi hawajalipwa fidia. Kwa hiyo, tunaomba sana wananchi wale wameacha shughuli zao kwenye maeneo yale na wanahitaji walipwe fidia ili waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote nimpongeze sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya ya kutangaza nchi yetu hasa hasa kupitia filamu ya Royal Tour, tunamshukuru sana. Lakini pia niipongeze sana Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo na kipekee kabisa tunawapongeza, pale Serengeti wanaendelea na uratibu wa miradi mikubwa ya kijamii inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani ya KfW. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua Wizara hii ya Maliasili co-business yake ni kuhakikisha wanahifadhi maliasili zetu zote pamoja na kuliwezesha Taifa kupata mapato. Sasa yako mambo kama matatu hivi ningependa kuyachangia ili kuona kuwa wanaweza kufanya kazi hii vizuri.

Jambo la kwanza naishauri Wizara hii sasa iharakishe ujenzi wa uwanja wa ndege wa Serengeti. Uwanja wa ndege wa Serengeti unaweza kutusaidia sana kuongeza uhifadhi, ukienda ndani ya Hifadhi ya Serengeti kuna viwanja vingi sana, kuna utitiri wa viwanja na viwanja vile vinaathiri sana uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna ndege nyingi zinatua, ni makelele mengi, sasa mambo haya huwa yanakwenda taratibu taratibu, yanafukuza wanyama kuna hali ya utulivu kukosekana, wiwanja vimekuwa vingi sana. Sasa sisi katika Halmashauri ya Serengeti tumetenga eneo tayari na ninaishukuru Wizara inaendelea na michakato ya ujenzi wa uwanja. Sasa tunawaomba waongeze kasi ya ujenzi wa uwanja ule na ujenzi wa ule pia utasaidia sana wananchi kuona sasa manufaa makubwa ya uwepo wa Hifadhi ya Serengeti katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna habari ya ushindani wenzetu wa upande ule ambao tuna-share nao ecosystem na wao sasa wanakimbizana, kuona namna ambayo wangefanya wapate watalii wengi sana na watalii hao ni wale wale wanaokuja Serengeti. Sasa niwaombe sana waongeze kasi ya ujenzi wa uwanja huu itatusaidia sana kuongeza mapato kwa sababu pia hata watalii hawa itawapunguzia cost kwa sababu hawatasafiri umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuna mikataba ambayo Wizara ya Maliasili inaingia na mahoteli ambayo yanajengwa katika hifadhi. Mikataba hii tunaomba sana Wizara, Wabunge wengi wamelalamika habari ya CSR haieleweki, habari ya service levy haieleweki katika mahoteli. Lakini ukiangalia kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu ya mikataba. Mikataba hii tungeiomba Wizara inaposainiwa iweze kubainisha kabisa wazi kwamba wahusika watalipa service levy pamoja na CSR katika halmashauri ambazo hoteli hizi zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaiomba sana Wizara izingatie hili leo ni aibu sana unakwenda katika Wilaya kama za Serengeti zenye hifadhi kubwa halmashauri hazina mapato. Kwa nini hazina mapato ya kutosha na mahoteli? Ni kwa sababu hoteli zile, hazioni zinawajibika direct kulipa CSR pamoja na service levy katika halmashauri hizi. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara hii ijitahidi kuhakikisha jambo hili sasa linaondolewa utata. Pale Serengeti tumehangaika muda mrefu tunazo hoteli nyingi ndani ya hifadhi zaidi ya hoteli 200 pamoja na camp sites, lakini malipo yao ya service levy imekuwa ni shida malipo yao ya CSR yamekuwa ni shida, tunaomba sasa kwa mwaka huu unaoanza Wizara hii itusaidie kumaliza tatizo hili. (Makofi)

Jambo lingine la tatu, ningeiomba sana Wizara hii ya Maliasili na Utalii ipitie upya, Wabunge wengi wamelalamika kuhusiana na tembo pamoja na wanyama wakali. Tembo na wanyama wakali wameendelea kuwepo karibu kila mahali. Sasa tunaiomba Wizara kwa sababu uhifadhi umekuwa ni mzuri sana na wanyama wameongezeka na wanyama hawa ndio ambao watalii wanawafuata. Sisi hatuna lengo la kusema wanyama hawa sasa waondolewe wasiwepo, sasa tunaomba tupitie vizuri zile taratibu zetu za uhifadhi. Kuna haja sasa ya kujenga fence ya umeme ambayo haina madhara tunahaja hiyo na ukiangalia wenzetu kule wanafanya. Kuna wakati nimepita Masai Mara nimeona pembeni wao wamejenga fence na hakuna namna ambayo tutazuia wanyama hawa wasiweze kuwadhuru wananchi…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, sasa tutalia hapa tutapiga kelele tutaonekana kwamba hatuna mapenzi mema na hawa wanyama hapana, tunawahitaji.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Amsabi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nampa taarifa Mheshimiwa Amsabi kwamba ni kweli kuna haja ya kuweka fence, lakini fence hiyo ikijengwa isije ikajengwa kuziba mito iliyozunguka wananchi. Kwa hiyo, ijengwe kuelekea mapori ya wanyamapori, sio kule kwa wananchi. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, taarifa imetolewa lakini nilishawakumbusha hapa ndani, sio kazi yako wewe kusema kama Mbunge anachokisema ni halali sio halali; kweli au si kweli labda kama umesimama Kuhusu Utaratibu. Kwa hiyo, huwezi kusema anachokisema ni kweli yeye anajua ni kweli ndio maana kasema.

Mheshimiwa Amsabi, unapokea taarifa hiyo?

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante napokea taarifa hii na nipende kuhimiza sana kwamba kuna maeneo ya vijiji ambavyo sasa ile buffer zone haipo, kwa mfano, kule kwenye Jimbo langu ukianzia Kijiji cha Mbilikili ukienda hapa Bisalala, Tamkeli, Mbalibali, Machochwe mpaka Merenga kule wamemaliza kabisa eneo la buffer zone halipo. Sasa maeneo kama haya ndio ambayo naona kwa sasa ni lazima fence iwekwe, kwa sababu kwa namna yoyote ile wale wanyama hakuna namna ya kuwa-control, lile eneo la kinga halipo tena. Kwa hiyo, katika maeneo kama haya yapewe kipaumbele cha kwanza katika kuangalia kwamba sasa yawekewe buffer zone. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa nini wanyama hawa wanapowaua wananchi na wanapoharibu mazao fidia imekuwa ni changamoto sana. Kwa hiyo, niiombe Wizara hii wanayo taasisi ya TAWA ambayo tunajua kwa utaratibu wao ndio wanaoratibu kutoa fidia kwa wananchi. Lakini pia wapo Maafisa Wanyamapori hawa DGO’s hawa Maafisa Wanyamapori pamoja na TAWA process ile inakwenda kwa taratibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kwa mikakati yake mikubwa ya kukuza utalii nchini. Sisi tunaokaa huko maeneo ambayo watalii wanakuja, tumeona matokeo makubwa sana na kipekee sana Serengeti tunazo shukurani kubwa kwa sababu ujio wa watalii wengi umebadilisha hali ya uchumi wa maeneo yetu, kwa hiyo, tunamshukuru sana sana Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana nimshukuru Waziri wa Wizara hii, Dada yetu Angellah Kairuki pamoja na Naibu wake Waziri wanaendelea kufanya kazi na nzuri. Mara nyingi kiongozi mzuri utamwona wakati wa changamoto. Tunakumbuka wakati ule kulipokuwa na hali ya mvua ikinyesha kwa wingi sana maeneo mengi ya Hifadhi ya Serengeti yalikuwa hayapitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naona waliweka jitihada kubwa sana na ndani ya muda mfupi barabara zilianza kupitika. Kwa hiyo, tunawashuru na kuwapongeza pamoja na menejimenti nzima ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake ikiwepo TANAPA, wanafanyakazi nzuri, tunawashukuru. Tunawaomba waendelee kuongeza kasi kubwa na uboreshaji uwe ni jambo lao na malengo yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na kununua mabomu ambayo yametengenezwa hivi karibuni kwa ajili ya kupambana na tembo. Jambo hili ni jema, lakini mimi nashauri kwamba imefikia wakati sasa jambo hili tuliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili kila wakati tembo wanapongia vijijini wanalaumiwa wao, lakini ni kwa nini? Tembo hao wakishaingia vijijini hawaangaliwi kwa maana ya kurudishwa, hawasimamiwi na watu wa TANAPA, wanaoshuhulika nao ni maafisa wanyamapori wa wilaya ambao wako chini ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila taasisi kwa maana ya Wizara, inapoanzishwa inakuwa na core functions zake. Sasa ukiangalia madhumuni ya Wizara, kazi yake mahususi Wizara ya Maliasili ni kuendeleza utalii na kuhifadhi wanyama wetu, lakini TAMISEMI wao kazi yao kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi, kama vile barabara, elimu, maji na kadhalika. Sasa wao si rahisi sana waka-allocate resources katika kupambana na wanyama hao warudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kule Serengeti kila wakati wanyama wanapoingia kwenye vijiji ukimpigia DGO mafuta hana, imeenda imerudi, huku wanyama wanashambulia mashamba na kadhalika. Sasa kazi hii, ninakumbuka katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri pale Morogoro tukipokea mabomu baridi alisema halmashauri zinunue mabomu haya. Sasa nikiangalia zilitajwa pesa nyingi sana ambazo zinanunua mabomu. Kama wanashindwa kutoa mafuta lita 30 wanawezaje kununua mabomu? Kwa hiyo, jambo hili si rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Wizara irudi, ichukue kazi hii ya kudhibiti wanyamapori iwe ni kazi yake. Watu wa TAMISEMI waachwe washughulike na mambo mengine haya ya kuhudumia watu, vinginevyo basi huyu District Game Officer (DGO) basi arudi kwa watu wa Wizara ya Maliasili na wawezeshwe fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanyama hawa wanapoingia katika maeneo ya wananchi waweze kudhibitiwa haraka na nguvu kubwa iwekwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Serengeti tumepata madhara makubwa sana kwa hawa tembo pamoja na wanyama waharibifu. Tuombe sana Wizara sasa ichukue hatua za kudhibiti. Sawa kuna wakati mwingine tunauliza juu ya kifuta jasho, kifuta machozi na kadhalika, lakini hivi havisadii. Sisi tunahitaji wananchi wetu wabaki salama, tunahitaji mazao yetu yabaki salama, tuvune na kuendelea na shughuli zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo la pili ambalo ningependa kuishauri Wizara hii, tunahitaji kuona utalii unakua nchini na watalii wanaongezeka. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi katika utalii, lakini ukirudi na ukiangalia miundombinu katika kufikia hifadhi zetu bado ni changamoto kubwa na wakati mwingine gharama inakuwa kubwa. Leo gharama ya kuifikia Hifadhi ya Serengeti ni kubwa sana. Utoke KIA uende Arusha utoke Arusha mpaka Ngorongoro, Ngorongoro mpaka Serengeti ulipe geti ya Ngorongoro, uende Serengeti gharama inakuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe ule Uwanja wa Serengeti ujengwe. Uwanja huu umekuwa ni wa miaka mingi ambapo tumekuwa tunazungumza utajengwa, utajengwa. Wakati mwingine wanapatikana mpaka wafadhili, wanapatikana watu wa kuwekeza kutoka private sector, lakini bado tunachelewa kufanya maamuzi. Niombe sana Wizara ya Maliasili na Utalii ichukue hii ajenda hii na ishughulike nayo kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba bado barabara zinazoingia Serengeti ni changamoto, kwa maana ya barabara ya lami, kutokea kule Tarime pamoja na ile ya Sanzate – Nata, tunaomba Wizara iangalie barabara hizi ni za kimkakati kwa ajili ya kukuza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kuhusu WMA, hizi Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ambazo zinamilikiwa na vijiji leo wameanza kukata tamaa na wengine wanatamani sasa zingerudi maeneo yao yale wafanya shughuli zingine kwa sababu pesa zao zimekataliwa huko Hazina. Tunaomba sana Wizara msaidie, tuko pale Serengeti na Ikona WMA, tunaomba pesa zao zije, zimesaidia kiasi kikubwa sana maisha ya wananchi kukuza utalii, I mean conservation iliweza kuwa improved sana kwa sababu ya fedha ile pamoja na kujenga miundombinu mbalimbali katika afya na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe pia liko jambo lingine tunaiomba sana TANAPA iangalie vizuri, pamoja na Wizara hii kwa ujumla. Tunapotoa vibali vya ujenzi wa camps pamoja na lodges ndani ya hizi hifadhi zetu, naona kama ubora wa ujenzi wake si mzuri. Ninashauri Wizara iangalie sasa uwezokano wa kusomesha watu maalumu ambao watasimamia viwango vya ubora wa ujenzi wa hizi camps. Mtalii anakuja anaoneshwa picha imetengezwa kwa namna fulani anaona kwamba it is beautiful ni sehemu nzuri, lakini akifika malazi yale yanakuwa siyo mazuri mno. Sasa sisi tunampa tu mtu eneo jenga camp, jenga lodge, lakini ni la viwango gani vya ubora wake? Bado hatujawa na watu wa kusimamia viwango vya ujenzi wa hizi camps pamoja na lodges. Kwa hiyo matokeo yake mtalii anakuja analala sehemu ambayo ni sub-standard kwa hiyo tunaomba sana Wizara iende kuwekeza katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana maeneo ambayo yanapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vijiji vile hasa upande wa Western Serengeti ambapo hakuna buffer zone tunaomba tujengewe malambo ya kutosha kwa ajili ya mifugo yetu. Tunaishukuru sana Wizara, mpaka sasa hivi yako ambayo yanajengwa lakini tunaomba yaongezeke kwa wingi zaidi ili ng’ombe wale wasiweze kupata shida ambayo wanapata sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna malambo na hata wakati Wizara ikiwasilisha, kwa maana ya Kamati, imesema lazima hivi vijiji pamoja na jamii zinazozunguka hifadhi tuweze kuziangalia, kwa maana ya kuzisaidia. Wame-sacrifice land na kwamba wanapata shida nyingi kwa kuishi pamoja na wanyama, kwa maana ya kupakana. Tuhakikishe kwamba watu hao wanajengewa malambo pamoja na huduma zingine za kijamii ili nao waweze kufaidika moja kwa moja na hifadhi hizi ambazo wanaishi pembeni nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niombe sana sasa Wizara hii kwa kushirikiana na TANAPA, waangalie namna bora ya kuongeza ajira kwa watu ambao wanapakana na hifadhi zetu hasa kwa upande ule wa Serengeti, wananchi wetu pamoja na kuwa na elimu nzuri bado ajira nyingi hazijapatikana kwa vijana wetu hata zile ambazo ni seasonal.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Hitimisha.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)